“Hiki alichokifanya Mina, kinaweza onekana ni kibaya
sana,..” “Sio kinaweza onekana! Ni hatari Ruhinda! HATARI SANA.
Tusipoangalia hawa wawili wataishia jela!” “Najua mama, unampenda sana
Pius, lakini pengine hii itakuwa njia nzuri sana ya kutuliza hii fujo.
Na mnajua mimi nitasimama
na mke wangu.” “Andy amenipokonya maneno. Mimi nataka kusema, pengine hii njia itasaidia.
Mina hajakosea. Watoto hawa wametushinda mama! Hata ukikataa.”
Mzee Ruhinda akaendelea.
Mzee Ruhinda akakaa sawa. “Niambieni tu, katikati ya
fujo yote hii, moto
mkali unaowaka na moshi
wake kuenea kwa kila anayetufahamu, au hata wasio tufahamu, eti leo
Paulina anaona ni sawa kwenda kuongeza mafuta katikati yake! Kweli?” “Kulikuwa
na ulazima gani Paulina!?” “Wala usipoteze muda kumuuliza huyo, mama. Paulina
ni mfitini. Hawezi kuona watu wanapatana au sehemu kuna amani,
roho yake ikatulia.” Paul akaongeza.
“Au Pius. Niambie ni mara ngapi nimezungumza na wewe
juu ya hili jambo?” Mzee Ruhinda akaendelea. “Ukijua kabisa, tokea mwanzo wa
hili jambo ni hatari kwa kila mtu. Huyu binti amejirudia rudia kwa kukusihi
sana. Tokea mwanzo alisema wazi kabisa, wema wako kwake, ndio ulizidi ubaya uliomtendea, ndio maana ameacha kama
ilivyo. Haya, ukaona watu ni wajinga,
ukaenda kuanzisha fujo huko. Na usiseme ni Andy, maana wewe ndio baba wa
mtoto, ulitakiwa kujifanya mjinga
katika kila jambo, ili tu hiki anachokifanya Mina, wewe ndio uwe umekifanya!
Kutengeneza mazingira mazuri kwa mtoto wenu!”
“Lakini hebu fikiria FUJO ulizokuwa ukiendesha, hata
katikati ya mtoto aliyekuwa mgonjwa! Mama yake, hata sisi wenyewe tukikusihi
utulie, lakini wapi! Leo mtoto mdogo huyu anawaita wote HAMNA ADABU kwa wazazi
wenu! Kweli?!”
“Nyinyi watu wazima mnakosa uelewa kwa jambo kama
hili mpaka kushitakiwa?!” “Baba naomba niseme jambo moja tu kabla
sijaondoka hapa. Maana lasivyo tutachelewa ndege.” Andy akaingilia.
“Jamani! Zaidi mama. Kuweni makini sana kuanzia
hapa. Huu upendo aliowatangazia Mina, msije mkauharibu. Zaidi
kwenu nyinyi wazazi.” “Unamaanisha nini?” Mama yake akauliza.
“Ukumbuke hiki alichokifanya Mina, ndicho
Paulina na mimi ndicho tulichomfanyia YEYE. Sidhani kama mlishakaa naye
na kuonyesha ni jambo baya tulilomfanyia, japo amekuwa
akilirudiarudia sana mbele yetu.” “Na mimi nimegundua amekuwa akirudiarudia
sana.” “Sawasawa Paul. Na hakuna kati yenu aliye zungumzia hilo
hata mara moja.” Wote kimya.
“Sasa kwa kuwa hamkuonyesha kuwa ni kitu
kibaya kilimpata yeye au tulimfanyia sisi tokea mwanzo, nashauri
msije muhukumu yeye kwa hili. Maana kwa ninavyomjua Mina,
akishahisi mnamuhukumu kwa kitendo kilekile mlichombariki nacho Paulina
na mimi, jueni mmempoteza. Na mkimpoteza Mina, mmepoteza wajukuu
wawili. Na mjue fika, historia itajirudia.” Wote wakamtizama.
“Nimekusudia kujenga kwangu. Kwa nguvu
zote nilizowekeza kazini, nitarudisha kwangu, alipo Mina na watoto
wangu tena bila kuzembea. Sasa basi, atakapokuwa amesimamia Mina,
mjue na MIMI nitasimamia hapohapo. Japo najua kwa upande wangu hamtajali
kwa kuwa mmeshazoea kuishi bila mimi. Ila nimeona niliweke hili wazi. Nitasimama
na Mina.” Akaweka kituo akiwatizama. Kimya.
Akaendelea. “Baba na mama, naomba niwaage. Nikamsaidie
Mina ili tutoke hapa kwa utulivu.” “Naona na mimi nitawasindikiza ili nikaagane
na wajukuu huko uwanja wa ndege.” “Nashukuru baba.” Andy akaondoka.
“Na Pius, nakuonya. Najua siku hizi
hunisikilizi, …” “Nakusikiliza baba!” “Basi usimpige tena Paulina.
Umenisikia?” Kimya. “Naondoka hapa, huku nyuma usije mpiga.” “Na mimi naomba
niongozane na nyinyi ili nikamuage mwanangu.” “Tafadhali zungumza nao kwanza. Usitibue mambo zaidi. Umesikia Pius?” Kimya.
“Hakika mtaishia jela. Umesikia Paulina?” Kimya. “Kama
hii video kama hivi ilivyo, endapo ikifika mbele ya jaji yeyote yule, halafu
ikajulikana uliyafanya haya ukijua unamfanyia mama mjamzito,
HAKUNA wakili atakutoa kwenye hii kesi.” Kimya. Mzee Ruhinda akasimama.
“Kinachokushinda kujishusha kwa Andy ni nini
Pius, wewe?!” “Sasa mimi nimefanyaje mama?!” “Hivi unajua kwa lugha rahisi ni umempoteza
Mina na mtoto wako?” “Mimi na Mina…” “Bro! Hakika upo kwenye denial. Unapingana na UKWELI wa waziwazi kabisa! Wewe
unafikiri Mina atakuja kutengana tena na Andy?!” Paul akauliza kwa
kushangaa sana.
“Jamani, hawa wawili wamekusudia. Na kama
mnadhania nawatania, jueni historia INAJIRUDIA. Mlipomkataa Mina wakati ule,
Andy alimtoa hapa nchini, akaenda kumuoa nje ya nchi bila nyinyi.
Sasa kaka, ukiendeleza hiyo tabia, jua mtoto wako, baba atakayemfahamu
ni Andy.” “Haiwezekani!” Pius akakanusha kwa kujiamini. Paul akamtizama na
kuamua kusimama.
“Jamani usiku mwema. Acha na mimi nikaangalie yangu.
Kama Mina alivyosema, watoto wa Ruhinda, mmeshindikana. Ila mjue MTAVUNA
tu.” Paul akaondoka.
“Kabla sijaondoka hapa, Paulina na mume wako naomba
muondoke. Sitaki niwaache hapa msababishe matatizo mengine humu ndani.” Wakaondoka,
ndipo mzee Ruhinda naye akapandisha chumbani kwake.
~~~~~~~~~~~~~~
Akamgeukia mwanae kipenzi. “Hutaondoka hapa
kwenda uwanja wa ndege, bila ya kuomba ruhusa kwa Andy.” “Mama!” “Hakika Pius. Usitake
kunifanya nitembee humo barabarani nimechanganyikiwa, kwa kufungwa kwako
jela. Tafadhali Pius. Na kama unaona haupo tayari kuzungumza naye, basi subiri
hizo siku zako za kwenda kumuona mtoto zikifika ndipo uende. Usitoe mguu hapa kutufuata
nyuma bila kuzungumza na Andy kwanza.”
“Nilipokuwa nikimlelea mwanae mbona haku…” “Sikuwahi kukudharau
wala kukudhalilisha wakati ukisaidia familia yangu, ila kukushukuru kila
wakati Pius. Na nafsi yako nishahidi hata kama unakataa sasahivi mbele
ya watu.” Kumbe Andy alikuwa akipita kutoka chumba kimoja kwenda kingine,
akawasikia.
Hatimaye Bubu Kasema.
Akashuka mpaka ngazi ya mwisho akawa akiwaona pale
alipokaa mama yake na Pius. “Nilikuwa nikizungumza na wewe Pius kuliko
mtu mwingine yeyote kwenye hii familia au hata Mina mwenyewe. Nilipokuwa nikishindwa
kuja nyumbani nilikuwa nikikupa sababu ni kwa nini nimeshindwa, tena kwa
heshima! Ukawa ukinitia moyo na kusema utazungumza na mke wangu. Nikakuamini
naye, kwa vile ulivyo JIFANYA kusimama katikati yangu na yeye.”
“Leo unanibadilikia mbele ya mke wangu, kujipa umaarufu
ambao hukuwa nao! Unanitusi juu ya malezi kwa mwanangu huku ukijua
kilichokuwa kikiendelea kwenye ajira yangu na wewe kunitia moyo
ukiniambia mwanzo ni mgumu, nipambane tu!”
Ndio wote wakajua kumbe Pius alikuwa akiwasiliana na mdogo wake!
“Sikuwahi kukuvunjia heshima Pius. Nilikusikiliza,
nikiheshimu mawazo yako nikitambua kufanikiwa kwako kwenye ajira. Halafu
unakuja kunigeuka kinyama
hivi, kana kwamba hukujua kilichokuwa kikiendelea!”
“Wewe ndio mtu wa kwanza kukwambia juu ya
kupewa kwangu ile fulsa ya kwenda kusoma nje ya nchi. Nilikushirikisha WEWE
hata kabla ya mke wangu. Unakumbuka ushauri wako kwangu?” Mina alishituka
sana huko alikokuwa akisikiliza. Kwamba Pius alijua mumewe amepata
nafasi ya kwenda masomoni na kumtia moyo aende! Akazidi kujilaumu
akijiona mjinga kuangukia mikononi kwa Pius kiurahisi vile.
“Unanitia moyo nipambane bila kuchoka
ili viongozi wangu waniamini, kumbe ni janja ya kunitenga na familia
yangu, ili ujinufaishe wewe na kujipatia sifa kwa wazazi kisha
kuja kunigeuka VIBAYA kwa kiasi hiki! Unanitangaza ubaya ili Mina
anichukie, akuone wewe ni wa maana kuliko mimi!”
“Unajirudia rudia sana juu ya kulea mtoto
wangu. Kama kweli ulifanya kwa wema, kwa nini leo KUniSIMANGIA wema
wako? Wazi unaonekana ulifanya kwa HILA! Hakuna mtu humu ndani
anamkumbushia mwenzie jambo jema alilofanya kwa mwenzie, wewe umekuwa wa
kwanza Pius. Au useme ni mimi tu, wengine kuwafanyii hivyo!”
“Lakini pia, hukuwa mtu pekee
uliyetusaidia mimi na Mina kukaa na mtoto wetu. Hata kama wazazi wanakutetea
kuwa ulifanya kwa wema na kujituma, mbona wengine wasirudi kutunyanyasa kama wewe?
Nimezungumza na Ron ambaye nilimuumiza zaidi kwa sababu nilimuacha
dada yake vibaya sana. Na yeye alikaa na Ayan akitusaidia na wakati
mwingine kumlazimu kuwa naye mpaka ofisini kwake. Akiwa na hasira na
mimi nimezungumza naye. Lakini hata mara moja hajawi kunitukania
au kuninyanyasia kunisaidia mwanangu. Wewe imekua kero, wimbo
na FIMBO ya kutuchapia
mimi na mke wangu! Wema huo UNAOSIFIWA na wazazi kuwa umenifanyia, ni wema gani huo unao UMIZA ndoa yangu kwa kiasi hiki
ambacho umekusudia kutuangamiza kabisa?”
“Wema huu unautangaza
na kujivuna nao kila mahali, mbele ya kila mtu, kwa kujirudiarudia!
Kweli?! Kwa kumsaidia Mina kipindi hicho ndio unaona una haki ya kuongoza
familia yako na yangu, bila kufikiria, na mimi mwenyewe nikiwepo?
Kwamba wewe unataka kuwa baba mwenye nyumba yako na yangu! Uwe kiongozi wa Mina na Raza! Watoto
wako na wangu! Halafu mimi niwe wapi, na niwe nani, nikifanya nini!?
Watu wote tukufuate wewe kama kiongozi mpaka wa ndoa ZETU kwa
sababu unazo pesa na umeweza
kumsaidia Mina? Kweli Pius?”
“Umemng’ang’ania mke wangu bila aibu
wala nidhamu, ukijigamba unampenda. MKE WANGU! WA NDOA TAKATIFU! Kweli
Pius? Nidhamu ya wapi hiyo? Ni hizo pesa au kwa sababu unaona
mama yupo upande wako ndio unaona una nguvu ya kufanya chochote kwenye hii familia?” “Mimi
sijasema nipo upande wa Piu.” Hapo akamtibua zaidi Andy.
“Acha kunifanya mimi ni mjinga wakupitiliza mama. Ni mara ngapi umemkemea
Pius ki ukweli kwa anayofanya kama si umechukua makosa yake
ukanipa mimi, ukisema mimi ndiye NIMEMSABABISHA kukosea?” Akamuuliza kwa ukali kabisa.
“Andy ume…” “Hapana mama. Pius ANABAKA mke wangu, UNANILAUMU
mimi! Au umesahau maneno yako tulipokuwa Dodoma nyumbani kwangu?” Mama
Ruhinda akashindwa kujibu.
“Kwa nini Paul asilale na Mina na yeye alikiri
wazi Mina anatamanisha lakini ilikuwa bora akutafute wewe uende
naye kwangu kumsaidia Mina, au kumchukua mtoto akakae naye
kwingine asije jiingiza vishawishini. Kilichomshinda huyo mwanao mpendwa
mtukufu, ni nini mpaka kuingia CHUMBANI KWANGU, KUVUA NGUO na KULALA
NA MKE WANGU, tena kwenye KITANDA CHA NDOA YANGU takatifu!?”
“Halafu bila huruma wala kunifikiria,
eti wewe mama uliyetuzaa sisi wote, eti unakuja KUNIKEMEA mimi
kuwa KOSA ni LANGU, NIMEMSABABISHA alale na mke wangu! Kweli?!”
Mzee Ruhinda akatoka chumbani.
“Andy! Tafadhali naomba utulie.” “HAPANA baba. Mmenidhalilisha
vyakutosha. Kwamba huyu Pius yeye hakosei, na akikosea basi amekoseshwa!
AMELALA na mke wangu, kwenye kitanda changu cha ndoa! NDOA TAKATIFU, niliyohangaikia
mimi mpaka Nairobi, mkiwa mmemkataa Mina, nikahangaika mpaka
nimemfikisha Mina kanisani. Pius ANABAKA mke wangu, nyinyi hamuoni hilo
ni kosa, mnakuja KUNISEMA nyumbani kwangu! Mbele ya mke
wangu na mtoto, MKIMSIFIA yeye! Mnashindwa kuwa wanafiki kwangu hata katika JANGA zito kama hili lililonipata
jamani! Hakika nilinyamaza kimya, nikishangaa na kujiuliza, ni katika
lipi mtakuja simama na mimi?! Na pia nilinyamaza kwa kuwa sikujua
upande aliopo Mina kwa wakati ule.”
“Ningejua kama japokuwa ulimrubuni mke wangu
kwa mengi ikiwepo mapesa mengi ili kumgeuza moyo lakini bado Mina ananitaka mimi, kwa HAKIKA siku
ile pale nyumbani, nyinyi watatu, msingeondoka na mke wangu. Mlinifunga
macho na mdomo. Mkafanikiwa kuweka hukumu moyoni mwangu, MSINISAIDIE mke
wangu ABAKI na mimi mumewe, mkabakia kunitupia mimi lawama, kisha
kuondoka na mke wangu na mtoto wangu, halafu nyinyi mnaojiona
mnabusara, na wajuaji, pia mlishindwa kumtuliza Mina, mkidhania
Mina anatulizwa na mali.”
“Mkaja kumuweka hapa kwenu, kwenye nyumba hii nzuri ya
thamani ambayo milango ni miwili tu inayotumika na kijana wenu huyu mtukufu mwenye mapesa mengi akiwa mtaa wa pili tu hapo, na
bado mlishindwa kumtuliza Mina. Halafu eti mlivyo wa ajabu, Mina ameondoka
mikononi kwenu, bado mkanitupia mimi LAWAMA kwa kuondoka kwake!”
“Sikusema kitu, nikakubali yote kwa sababu nayajua mahusiano
yenu na yangu. Shida yangu ilikuwa Mina na mtoto wangu mliokuwa mkiwaharibu
akili mkiwaambia mimi sifai, ili na wao wanitizame kwa jicho lenu.
Lakini baba, mama na Pius, Mungu ameniangalia huzuni yangu na upweke
wangu. Amenipa mke anayenipenda, na kunijali mimi kama Andy na jumla
yangu yote. KAMWE Mina hataniangalia kwa jicho lenu, japokuwa Pius unahangaika
sana kumpandikizia Mina CHUKI dhidi yangu.”
“Kwa Mina na kijana wangu UMEKOSA. Subiria mke wa
Paul, mjinga mkubwa wewe. Malaya usiye na maadili wala aibu
kwa jamii. Mchafu wa kupitiliza ila unashindwa kwa sababu mkeo amekufunga.” “Mama, unamsikia
Andy?” “Wewe ni malaya Pius. Mchafu. Na leo ndio nimejua SI kwa
sababu wewe ni mwadilifu ndio maana hulali huko nje, ni kwa
sababu huna huo uwezo kama sisi wengine ambao nguvu tunazo ila tunathamini
viapo vyetu vya ndoa.”
“Mkeo amejisahau kukufunga kwa Mina akijua
huwezi fanya uchafu wako kwa shemeji yako, akidhani unatambua hata miiko
ya jamii, ndipo ukapata mwanya. Kumbe wewe ni mnyama zaidi ya mnyama
wa porini. HUNA maadili wala
miiko! Huna adabu Pius na wewe ni MCHAFU
wakupitiliza. Na nafikiri Raza alikujua tokea mwanzo, kuwa wewe ni kunguru
usiyefugiga ndipo akatumia njia ya kukulogwa.”
“Sasa NAKUONYA Pius. Mbele ya wazazi wako, wanao kusifia.
Mimi sitakuloga kama mkeo. ILA ukijichanganya tu, mimi mwenyewe
naenda KUKUSHITAKI kwa kumbaka mke wangu.” Wote wakashituka.
“Si wewe mtakatifu
sana, wazazi wanakuona mfalme wa
hii familia, wanakubembeleza kama yai, ukikosa, umekoseshwa?
Kokote unataka utawale kwa kiburi, hata hospitalini kwa mtoto
aliye mgonjwa, ukijua mama yake hajala wala kupumzika, unatuendesha
wote, ukikazana uonekane wewe ndio wewe! Sasa endeleza kiburi chako,
uone nitakachokufanya. Na kama unafikiri nakutania, au nakutisha tu, NIKUSIKIE UNAMSOGELEA MKE WANGU hata kwa ujumbe
wa salamu, ndipo utanijua mimi ni nani.”
“Undugu na mimi kwenu si ni mzigo? Mnanitusi mpaka nyumbani kwangu, mbele ya mke
wangu na mtoto, mnaniona sifai, na mnanichafua kwa familia yangu?
Sasa jichanganye kama hujawaacha wazazi wako na kilio huku
mtaani, wakati wewe upo JELA.”
“Msogelee Mina kwa kisingizio cha mtoto asiye
na hatia. Nitakutia ADABU uliyoshindwa kufundishwa hapa
nyumbani.” Mina akatoka na kumfuata taratibu mpaka alipokuwa amesimama,
akasimama nyuma yake.
“Maana nilikuja kwa wazazi kwa heshima, nikitoa malalamiko
yangu juu ya hili lakini WAMENIPUUZA, na kunipa mimi kosa
lako. Sasa utaona jinsi sheria itakavyo kushugulikia. Kule ambako hakuna
kina Ruhinda, ila haki tu. Tuone na wao watasema nini juu ya ubakaji
wako, kwa mke wangu. Wewe si unayo pesa na nikiburi? Sasa tutakuona
jeuri yako na pesa vitakapo kufikisha.” Alipoweka tu kituo, akamgusa kwa
upendo.
“Mama na Ron wameshafika kutuchukua kutupeleka uwanja
wa ndege, nimewaambia wasiingie.” Andy akamgeukia mkewe. “Usikasirike Andy!”
Wakamsikia akimbembeleza mumewe kwa upendo na sauti ya yake ya kitoto. Andy
akajaribu kutulia.
“Twende nyumbani kwetu. Halafu kuna kitu kizuri,
nitakwambia.” Jinsi alivyoongea mpaka Andy akacheka kidogo. Utafikiri anaye mdanganyishia mtoto mdogo! “Nini?” “Ni siri Andy! Twende
tusichelewe.” “Samahani Mina.” “Pius anatakiwa kuambiwa. Sio mtu mzuri.
Hata mimi nimemuona ananinyanyasia kwa misaada yake aliyokuwa akinipa.
Twende kwetu, Andy. Tutakuwa sawa, usikasirike. Mimi na Ayan tunakupenda
wewe na tunataka uwe na sisi hapa. Twende tusichelewe.”
“Sikujua kama uliomba usafiri kwa Ron. Mimi nilitaka
kuwasindikiza.” Mzee Ruhinda akaingilia. “Sikujua taarifa za kuwashitaki
watoto wenu mtazichukuliaje baba. Ndio nikamuomba msaada Ron mwenye gari kubwa.
Ila sio sababu ya kutotusindikiza kama bado unanafasi. Nakupandishia
wajukuu zako WOTE kwenye gari. Tena Ayvin ameamka. Anakazi ya kucheka tu
hapo chumbani, ameshiba. Unakaa nao nyuma. Mimi au Andy tunakuendesha, halafu
kina Ron watatufuata kwa nyuma, si ndio Andy?” “Ndio tutoke sasahivi. Tunaanza
kuchelewa.”
“Ila wewe hapo Pius hakuna kuja. Subiria siku
zako za kumuona mtoto zifike ndio uje. Wewe hapo mkorofi. Sisi hatutaki fujo
na matusi mbele ya mama na Ron. Haya mambo mabaya, tunayaacha
hapahapa ndani, nyumbani kwenu. Usitufuate nyuma.” Mina akaweka msisitizo.
Pius na mama yake walibaki kama mabubu. Mzee Ruhinda peke yake ndiye
aliyefanikiwa kuwasindikiza hiyo familia ya Andy.
Pande Ya Pili
Baada ya kuweka
ombi lake kwa Mill kutotaka Brenda asifike kwake, na msimamo wa kutohamia
nyumbani kwake, akamuacha Mill amesimama nje kama sanamu, hata kuondoka anashindwa.
Akarudi ndani na kukuta hali ya tofauti. Kina mama Pili wakampokea kwa
kuchangamka.
“Nasikia shoga unahama!
Tuachie basi hata ukumbusho!” “Chumba chote kama kitakavyobakia nimemuahidi
kumuachia kaka Mgoshi.” “Kweli shoga unatuacha hivihivi!” “Hali yangu kama
mlivyokuwa mkisema. Mlalahoi, ila maringo ya baba Shema.
Nawaachia nini?” Akawafanyia kusudi kuwaambia alijua wanamsema
vibaya.
“Wanakupa maneno
ya kutuchonganisha mama Shema. Sie tumetoka mbali!” “Kwa kuwasikia mimi
mwenyewe! Lakini mie sitaki kesi. Nataka kusema sina kitu chamaana chakuwapa.
Hata kaka Mgoshi mwenywe anakuja kuchambua, atakachoona kitamfaa, ndio
atachukua, vingine vyote atanisaidia kutupa.” “Basi akishamaliza yeye
kuchagua, ndio naomba na sisi tupite.” “Hamna neno.” Akaingia chumbani kwake.
“Hamna chakula
mama!” Akaongea kama hajala cha jioni hiyo! “Nakutengenezea tambi sasahivi.
Subiri kidogo tu.” Akamchemshia tambi, akamuwekea na sukari akampa na chai.
Akala, akajitupa kitandani ndio ikawa kwa heri. Akaanza kukoroma, Pam
akaendelea kufungasha. Akiwaza.
Siku
ya Kuhama Pam na Mwanae na
Kwa MARA YA
KWANZA Birthday Ya Shema.
Kesho yake kwenye
majira ya saa tatu na nusu asubuhi akaanza kuja dereva na vitu. Vinywaji vingi
tu. Sahani, na baadhi ya vyakula. “Ameniambia uniambie ni wapi pakuweka.” “Mimi
sikujua kama anataka mambo makubwa hivi! Nilijua analeta keki tu, akakate
na wenzie wale, tuondoke. Hii ni shuguli kabisa, halafu mimi sina hata
meza yakuwekea!” Gari kwa nyuma ilijaa vitu, Pam mwenyewe akachoka.
Akampigia Mill. “Nashukuru kwa
vitu,…” “Lakini nimezidisha?” Akamalizia kwa swali
akicheka. “Sikujua kama ndio unataka kitu kikubwa hivi!” “Hivi unajua tokea
asubuhi nilikuwa huko kwenu kuzungumza na Mwenyekiti wa mtaa wenu?” “Mill!”
“Mtoto wa peke yake huyo, halafu ndio birthday yake ya kwanza! Siwezi
nikafanya jambo dogo. Nishaomba kibali hapo kwenye uwanja, wanapochezea
mpira yeye na wenzie. Nimepata meza. Wanakuja kuweka hapo, na vyakula vingine
vinakuja muda si mrefu. Hutakuwa na kazi kubwa ila kusimamia tu.”
“Bibi yake wa hapa, ndiye anayenisaidia
kuandaa. Mama Colins. Wanakuja na familia yake. Ila sikujua kama Kamila
anakaribishwa ua la. Nimemuomba nizungumze na wewe kwanza. Au tatizo ni
Brenda tu?” Akachomekea kusudi. “Kwa ukubwa huu,
hata yeye akija, watu hawatajua. Wakaribishe tu wote.” Akazidi kumchanganya kwa kumuonyesha hajali tena. Mill akazidi
kupoa.
“Sikukusudia kuja na Brenda tokea
mwanzo, Pam! Nisingefanya hivyo kwa kukushitukiza. Nakuheshimu sana.”
“Nashukuru.” Wakatulia.
“Nakuja muda si mrefu, nimekaribia.”
“Basi utanikuta nikikusubiria pale uwanjani.” “Ujue kuna mechi.
Nimemwambia mwanao anayependa kunionea,
leo nakuja na timu yangu na refa wa kueleweka. Sitaki
anipangie watu wake.” “Ndio maana anahangaika!” “Nimemwambia atafute
timu yake, hata akitaka kukodi mcheza ligi za Ulaya, leo lazima nimfunge.” Pam alikuwa akicheka hana mbavu.
“Masikini mwanangu! Ndio maana
anahangaika!” “Akome uonezi.
Tunakuja. Na usiwe na wasiwasi nimejipanga kila kitu. Njoo kuwa mtizamaji na
kusaidia kupanga.” “Sawa. Nashukuru Mill. Asante kwa yote.” “Ni mwanangu pia
Pam! Najua naweza kuwa nilikuumiza juu ya kuhama kwenu, samahani.
Nia ilikuwa njema. Najali, najali kupita utakavyo fikiria.”
“Hamna neno Mill. Na najua kama unamjali Shema. Naona, na nakushukuru
sana. Karibuni.” Mill akaishiwa maneno, akaona amuage tu.
~~~~~~~~~~~~~~
Kufika saa sita, pakawa pamechangamka
kwelikweli. Wakubwa kwa wadogo wakawa wapo uwanjani. Walivuta watu hapo uswahilini
kupita kiasi. Maana Mill alikuja na watu na wadhifa zao ila wote wamevaa jezi.
Mpaka mzee Komba alikuwepo, daktari mzima na jezi ya kucheza mpira! Colins na
shemeji yake, mchumba wa Connie nao walikuwa kwenye jezi. Alihakikisha
anatafuta kweli timu ya kutoshea. Na Shema naye akatafuta watoto wa Kitaa,
wanao ucheza mpira tokea wanaanza kutembea.
~~~~~~~~~~~~~~
“Sasa msione ni watoto
wadogo, bwana watoto wanacheza hao! Hapa tukazeni msuli.” Mill
akawa anahamasisha timu yake wakati na Shema naye akihamasisha wenzie
hapo uwanjani. Maji ya kunywa yalikuwa ni mengi na soda kibao. Mashabiki kibao.
Hao waliokuwa wakicheza kwenye timu ya Mill walikuja na wake zao au wapenzi na
marafiki zao na viti maalumu vya kukaa mpirani, wao wakajiwekea miavuli.
Refa akapuliza
kipenga, mpira ukaanza. Walicheza hapo kama wanagombania kombe la dunia.
Wazee hao waliokuwa hawajashika mpira miaka zaidi ya umri wa hao watoto, walikimbizwa
mpaka wakachoka. Wake zao walikuwa wakicheka mpaka machozi.
Shema na timu
yake walikuwa uwanja wa nyumbani, wakapata washangiliaji wengi sana.
Alikuwa na furaha huyo mtoto mpaka baba yake aliona pesa liyomwaga hapo inastahili.
Lakini waliwafunga hao wazee 3-1.
Akakata keki
wakimuimbia wote. Akamlisha mama yake kwanza, kisha baba yake na hao
kina Komba kama ndugu upande wa baba. Pam akashangaa anawaita bibi na babu kwa
ukaribu kabisa! Akajua alishapelekwa huko. Akajituliza.
Wakati wakinywa
na kula, Kamila akamsogelea Pam. “Nashukuru kuniruhusu kuja.” Pam akamwangalia,
akashindwa chakumjibu kwa muda ila akasema tu, “Karibu.” Kisha akaondoka
kabisa hapo alipofuatwa na Kamila na kwenda upande mwingine kabisa kama
aliyekuwa akijitenga.
Mill aliona
maana macho yake wakati wote
yalikuwa kwa Pam mpaka Colins akaanza kumcheka. “Nini wewe?” “Mzee hupepesi
macho!?” Ndio Mill akajishitukia. “Hamna bwana!” Akajibaraguza kidogo ila
akajikuta macho yanarudi kwake hata
katikati ya wenzie na mazungumzo ya kuchekesha, basi yeye alibakia macho kwa
Pam muda wote ndio maana aliweza ona
kilichoendelea kati ya Pam na Kamila.
~~~~~~~~~~~~~~
Alipomuona ameondoka
pale alipofuatwa na Kamila, akamfuata. “Vipi?” “Kuna mtu amefika nyumbani,
nataka nikamkabidhi vitu ninavyobakiza ili kubakie kutupu, nisafishe,
tukimaliza hapa tuondoke kukiwa mapema, niwahi kwenye duka lile lenye vifaa vya
Shema.” “Pam, nakuulizia WEWE. Upo sawa?” Akainama na kushindwa
kuzungumza.
“Usiwe na
wasiwasi, hapa tunamalizia muda si mrefu. Nina watu wa kukusaidia
kuhama. Tutawahi tu. Naomba usiondoke na kuacha wageni hapa. Shema hawezi tulia akiona unaondoka. Na yeye ataondoka
na kupoteza maana nzima ya watu wote hawa walioacha shuguli zao
na kuja kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.” Pam akatulia.
Mara Shema
akawasogelea, shida ilikuwa mama yake. “Unaona lakini nakunywa maji?”
Mill akacheka. “Na umalize hiyo chupa, sio ukazane na soda tu.” Mama yake
akamuwekea msisitizo. “Sasa mbona na wewe huli, mama!?” “Nishamaliza
chakula changu.” Mill akawa akiwaangalia. “Nikuongezee kingine ili baadaye usisikie
njaa?” “Nimeshiba Shema mwanangu. Asante. Wewe nenda kafurahie na
wenzio.” “Na wewe utanisubiria?” Mill akamwangalia Pam kama kumkumbusha alichomwambia.
“Siondoki mpaka mwisho, tushukuru wageni kwanza, wakishaondoka, ndio na sisi
tunakuwa wa mwisho kuondoka.” Akafurahi huyo, na ndio akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Haikuchukua muda
mrefu. Watu wa hapo mtaani mpaka mtaa wa jirani waliitana. Wakashambulia
vyakula vyote na maji pamoja na vinywaji mpaka wakamaliza. Walioleta
vyakula wakakusanya vitu vyao, na hizo sahani za disposable walizolia
watu vyakula, wakakusanya takataka zote ndipo wakaondoka wakiacha hapo pasafi.
Kila familia
walio alikwa na Mill ni kama ilikuja na cooler box zao. Wakamwaga barafu
maana vinywaji viliisha. Wakakunja viti vyao na miamvuli. Wakarudisha kwenye
magari yao.
Hao marafiki wa
karibu wa Mill, wakajikusanya tena pembeni peke yao, wakamuimbia tena
huyo Shema akicheka kweli! Kwanza alikuwa amewafunga. Anajisifia hapo,
akiwaambia hawajui mpira. Vikajaa vicheko hapo. Wakampa zawadi zake,
watu wa mtaani wakiangalia kwa pembeni maana walijitenga kufanya chao
cha tofauti. Kisha na wao wakaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Akabakia Mill na
magari mengine mawili. Wakarudi kwa Pam. Gari moja wakapakia vitu vyote vya Pam
na mwanae. Jingine akawaambia wawafuate nyuma. Pam akaaga wapangaji wenzie, wakatoka
ili waondoke na gari la Mill.
~~~~~~~~~~~~~~
Akamuona
anaingia mlango wa nyuma. “Kwa nini hukai mbele!?” “Hapa panatosha.
Asante.” Mill akabaki akimwangalia. “Naheshimu mali na vitu vya
watu Mill! Natambua nafasi yangu. Unataka nijizoeze kwenye viti vya
watu, akija kuwepo mwenyewe, itabidi tena uniambie mimi nikae
nyuma, kumpisha mmiliki? Si bora nikae hukuhuku nitakapobakia kuruhusiwa
kukaa.” Mill akajua Brenda ameshakuwa tatizo litakalosumbua.
Akanyamaza na
kuondoa gari maana Shema alishakaa sawa kusikiliza akimwangalia kwa makini.
Akaona asije muharibia siku yake, akatulia. Gari ya pili ikaanza
kuwafuata mpaka kwenye hilo duka. Shema alishasinzia garini. Mill akaacha gari
ikiwaka, akamfuata Pam. “Nashauri ununue na vitu vya chumbani kwako.” “Taratibu.
Hivyo vingine nitanunua wakati mwingine.” “Leo lipo gari hapo nje na vitu vipo
humo ndani dukani. Naomba tumalize Pam.” Akajua yeye ndio atalipia.
Akaanza kuchagua vitu na yeye akimsaidia mpaka wakamaliza.
Mill alihangaika
siku hiyo mpaka Pam akamuonea huruma. Kuanzia kupandisha mpaka kushusha kwenye
hiyo nyumba wanayo hamia, na kuingiza ndani akimsaidia kupanga kila kitu.
Madereva waliondoka baada ya kulipwa, akabaki yeye akisaidiana na Pam. Hapakuwa
na tv wala friji. Mill aliliona hilo. Akaendelea kumsaidia kufunga
vitanda, kuweka makabati na kumuhamishia Shema vitu vyake chumbani kwake.
“Yaani huyu,
kuanzia leo, anaanza kulala chumbani kwake na awe anafunga mlango akiwa
anavua nguo.” Pam alicheka tu. “Mfundishe bwana Pam! Ujue ameshakuwa mkubwa!” “Taratibu,
ataelewa. Mazingira yatamsaidia. Mpe muda. Muone anavyo koroma pale
chini! Hapo hajui hata alipo! Akiamka hapo, njaa.” “Basi acha nitoke
nikanunue chakula, niwaletee, ndio nirudi kwangu nikaoge. Nimeloa jasho mpaka najionea
kinyaa!” “Pole na asante. Naona leo ningecheza ngoma za kisambaa hapa
mimi mwenyewe na hivi vitu, mpaka kupambazuke. Nisingemaliza leo.” “Karibu.”
Akatoka.
Akaenda
kuwaletea chakula. “Si mtakuwa sawa?” “Kabisa. Wewe nenda kapumzike tu. Hata
mimi naoga, akiamka huyu akaoga, akala na kulala, na mimi nitalala. Mengine
nitamalizia kesho.” “Basi nitawaona kesho. Usipatwe tamaa yakuendelea. Pumzika
kweli, kesho nitakuja kukusaidia, tumalizie.” Akaaga na kuondoka.
Siku ya Pili
Ugenini.
Siku ya jumapili
kwenye mida ya saa nne, Mill akawa ameshawasili. “Nimekuamsha?” “Usijali. Karibu
ndani. Jana nilisahau kukupa funguo zako.” “Wewe usiyeniamini hata na
kiti cha gari, leo unataka kunipa funguo za nyumba!” Pam akajua maneno
ya jana bado anayo moyoni. Akanyamaza. “Eti Pam?” “Njoo upumzike ndani kwangu.
Hatuna makochi.” Akabaki amesimama.
“Njoo ndani.
Shema bado amelala.” Akatangulia ndani. Bado alikuwa na nguo za kulalia ila
alijifunika khanga juu. Akamsikia akimfuata. “Jinyooshe hapo kitandani wakati
naandaa kifungua kinywa.” “Kama ni kwa ajili yangu mimi nilishaamka muda mrefu
sana. Hapa nasubiria cha mchana.” “Basi jinyooshe hapo kitandani wakati
unamsubiria Shema aamke.”
“Hivi vitu
vimependezea chumba! Sema unakosa taarifa za habari Pam! Mmekosana wapi
na tv?” “Nitanunua. Pale palikuwa padogo sana, hapakuwa na nafasi.”
~~~~~~~~~~~~~~
“Naomba nikuombe
kitu Pam. Ila usinichukie.” Pam akakunja uso. “Mike amefariki, ni
kama ameniachia Kamila. Tafadhali naomba umsamehe.” “Hata
nikisema nimemsamehe au sijamsamehe, mimi ni nani kwamba kuna huo
ulazima? Ni mtu wako wewe! Mimi alinifukuza kwake. Sijarudi
tena huko. Kuniona ni kama hivyo kukiwa na jambo la Shema,
ambaye ni mtu pekee anayetuunganisha mimi na wewe. Na ni matukio machache
sana tunaweza jikuta tupo sehemu moja, na yeye kutaka kuwepo ili kukufurahisha
wewe.”
“Haya, birthday
ya Shema ni mpaka mwakani tena. Muhula wa mwisho wa shule Mungu
akisaidia Shema akafaulu tena, zawadi wanapewa mwishoni mwa mwaka. Na
Mungu akisaidia kama atakuwepo kwa ajili yako, kama hivi jana, sitambughudhi,
sitamuingilia. Tatizo lipo wapi?”
“Natamani
Shema awe nao karibu.” Mill akaongeza kwa tahadhari. “Kwa nini, wakati alimkataa!
Anafanya yote hayo na kujidai ukaribu kwa ajili yako WEWE.
Mimi si mkeo! Na wala si Brenda useme kwamba kwenye mambo yenu
mengine tutakutana. Kukutana, tena ikilazimu, kwa kutaka kukufurahisha
WEWE ni mara mbili kwa mwaka! AKIJIDAI anataka kuhudhuria ya mwanangu! Sasa
mimi kwake nina faida gani?” Mill akapoa kidogo.
“Kwangu wewe
unafaida Pam! Na yeye ni kama mdogo niliyeachiwa na Mike. Sina ndugu wengi na
wewe unajua. Amefanyika kama shangazi yake Shema.” “Kama yeye ni kama
shangazi yake Shema, kwangu ni nani? Au kuna ulazima gani wa haya
mazungumzo Mill, kama si kutaka kuniumiza tu?” “Sio nia yangu.”
“Ndio NIA yako.
Kwamba yeye unaona ni wa muhimu sana, na kile alichonifanyia ni SAWA!”
Akawa ameshabadilika. “Kama kweli yeye alikuwa muungwana na anashida
na mimi si angenitafuta muda wote! Alijua ni mjamzito. Alijua sina
kazi. Nilifukuzwa, na mke mwenzie alinifunga jela nikiwa mjamzito.
Namba yangu ya simu alikuwa nayo na sikubadili mimi mpaka nilipokuja uza simu,
tena ni miaka ambayo hali ilikuwa mbaya haswa. Nina mtoto, sina kodi. Yeye
alikuwa na hali nzuri. Alishindwa nini hata kunitafuta na
kunijulia hali, leo ANAKUONA wewe ndio anajirudisha kwangu!?”
“Hivi unajua
mateso niliyopata nikiwa mjamzito, nafungwa jela na wewe sijui upo wapi? Nahangaika,
yeye akijua kila kitu, ANAFICHA ukweli kwa sababu zake binafsi? Kweli
hata Mike ashindwe kumwambia, leo uje hapa uanze KUMTETEA?” Mill
akasimama.
“Samahani Pam.
Samahani mpenzi wangu. Sikukusudia kukuumiza. Samahani. Tafadhali naomba
yaishe. Basi.” “Mimi sio mpenzi wako Mill! Tafadhali usije sahau kuwa UMENIKATAA,
na upo na mwanamke mwingine. Na nafikiri ndio maana unajichanganya. Huo undugu
unaotaka uwepo, ni kati yake na Brenda wifi yake, sio mimi.”
“Subiri kwanza
Pam, aliyemkataa mwenzie ni nani kati yetu!? Sema ukweli mpenzi wa
Mungu.” “Hatukuwa wote Milimani nikakueleza kwa mapana mahali nilipo na Mgaya
na nikakuomba unipe muda?” Mill akakunja ndita.
“Lakini Arusha…”
“Kwamba gafla wewe ulisahau mazungumzo yote yale kwa siku moja tu!?
Nikiwa nilikwambia nilitambulishwa na Mgaya mpaka kwao. Tulikuwa
kwenye hatua mpaka kukaribia ndoa, mimi ndio nilikuwa nikisita
sababu ya Shema! Na nikakwambia kabisa, ni kama nilishajua tokea zamani,
ni nini natakiwa kufanya. Wewe mwenyewe ukaniambia unaomba nichukue hatua
kwa haraka. Tumekubaliana vizuri, unanigeuka KIKATILI kabisa bila kunifikiria!”
“Pam!” Akataka kumshika, akakwepa.
“Wewe niambie ni
kwamba ulisahau ua ulikusudia tu kurudi kwenye maisha yangu na
kuendelea kunitesa?” “Nilijua umenikataa Pam! Nilikuuliza…” “Wewe unaniuliza
maswali ya KUNIDHALILISHA halafu nimeshindwa kukujibu, badala
unifikirie, unaniadhibu! Hukuwahi kunipenda Mill.” Shema akaingia. Wote
kimya.
“Baba hakupendi!
Kwa nini?!” Hilo ndilo aliingia nalo. Wote wakabaki kimya. “Amefanya nini?!” Akamgeukia
baba yake. “Ni kutoelewana kidogo tu!” “Ndio maana humpendi?” Pam
akatoka kwenda bafuni. Mill akabaki hajui amjibu nini!
“Ungemuuliza
akuelezee, kama hujaelewa, kuliko kumchukia!” Shema akamlaumu kwa wazi
kabisa. “Sijamchukia mama yako, Shema! Haya yalikuwa mazungumzo tu. Tunawekana
sawa.” “Mama yangu hajafurahia. Ukimuona hivyo ujue hajafurahia
kabisa. Ungemuuliza tu, angekuelezea. Mimi mama yangu ananipenda.
Hataki nikasirike wala nilie. Ananipenda. Halafu ananijali.
Na mimi nampenda. Huwa ndio maana simbishii. Akiniambia jambo,
hata kama sitaki, nambembeleza mpaka anakubali. Ananiruhusu, na kwenda
kucheza mpira bila kumkasirisha.”
“Nikijisahau
kurudi, akikasirika, namuomba msamaha. Nambembeleza mpaka
ananisamehe. Halafu nikirudi nyumbani namfanyia kitu kizuri, anakuwa hakasiriki
tena. Mama yangu sio mtu mbaya. Usimchukie.” “Shema, simchukuii
mama yako hata kidogo. Nikinyume na hivyo unavyodhania.” Akamwangalia kwa
kutoridhika, akatoka kumfuata mama yake bafuni.
~~~~~~~~~~~~~~
Akamsikia akimrubuni
mama yake. “Nikupikie chai?” Akaanza akiwa amesimama nje ya mlango wa bafuni. Akamsikia
Pam akicheka. “Mikate yako nakupakia mimi blueband, halafu nakupa kabisa
mkononi. Nakutengenezea chai ya kisambaa kama ya bibi. Inakua inanukia
mtaa mzima! Watu wote wanaanza kusema yeye Shema anampenda SANA mama
yake.”
“Unanidanganya
tu hapo. Ukiweka sufuria tu jikoni unaanza kuniambia, ‘niangalizie, narudi
sasahivi’, sikuoni tena!” “Lakini si huwa narudi kuangalia?” “Chai inapikwa
kwa masaa mangapi kama si unakua unanianzishiaga kazi, halafu unaniachia
mwenyewe?” “Leo siendi mpirani mpaka chai iive. Unakunywa, naosha vyombo kabisa.
Leo mimi ndio nakutunza.” Pam akacheka akiguna.
“Uanze kwa kutandika
kitanda chako huko ulikolala, ndio utakuwa umeanza kunitunza.” “Haya.
Halafu niokote nguo zote au nyingine unamalizia wewe wakati mimi…” “Hakuna
Shema. Tulia ndani. Wewe safisha chumba chako bwana. Tulizungumza nini?” “Basi
mama. Nasafisha chumba changu. Patakuwa pasafi kama kwako.” “Hapo ndio utakuwa unanipenda
sana na unanitunza.” “Haya.” Pakatulia.
~~~~~~~~~~~~~~
Mill akabaki
akiwaza mpaka Pam akarudi chumbani. “Maji yanatoka mengi au ni ya kujipaka tu?”
“Yanatosha.” Pam akajibu akijipaka lotion. Akatulia ila akahamisha macho kwenye
simu ili kumpa uhuru wa kuvaa. Akafanya yake mpaka akamaliza. Akamuona anatoka.
Akamfuata kwa haraka.
“Utoke huko, ukaoge.”
Akatoka. “Njaa inauma mama! Nikianguka bafuni je?” “Shema!” “Kweli.
Nimezidiwa.” “Wewe hutaki kuoga bwana!” Akaanza kucheka. “Nikila ndio naweza
kuoga.” “Sasa ile chai uliyoniahidi iko wapi?” Mama yake akamuuliza, akaanza
kucheka kisha akamwambia. “Sasa wewe anza kuweka sufuria jikoni, nakuja.” “Huna
lolote. Nenda kaoge.”
“Tunaweza kwenda
kula wote mahali.” Mill akajipenyeza kwa kujikomba. “Mimi nitabakia
hapa. Nenda na Shema” Pam akajibu bila ya kumuangalia. “Mimi nataka kubakia
na mama yangu.” Shema akawahi kwa haraka akikataa. Mill akajua pashatibuka.
“Nenda kaoge Shema. Ukitoka utakuta chai tayari.” Shema akaondoka na kuacha
wazazi wake hapo hata hawaangaliani.
~~~~~~~~~~~~~~
Love At First Sight!
Inaendelea.
0 Comments:
Post a Comment