Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 52. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 52.

Akaelekea moja kwa moja alipo Andy. Alipomuona anakuja na mtoto, akatoka garini alishakuwa amezama mawazoni. Akamkumbatia mkewe na mtoto akiwa analia. “Nisikilize Mina, tulia kabisa nikwambie kitu.” Akamsaidia kumfuta machozi akampokea na pochi kubwa ya mtoto.

“Kuna mahali nilifika na mimi nikawa sijui chakufanya kwa sababu nimeshaharibu sana machoni kwa kila mtu, na wewe ukawa umeondoka nikiwa nimekujeruhi vibaya sana. Ilikuwa ni lawama, juu ya lawama.” “Pole Andy! Ila sikuondoka kwa sababu yako!” “Ninachotaka kukwambia nilifika mahali nilikuwa sijui chakufanya kabisa na mimi ndio mtuhumiwa mkubwa, lakini ikabakia palepale, mke wangu ana mtoto wa kaka yangu. Nilikuwa sijui chakufanya.”

“Kuna mtu akaniambia, hata Ayan ni roho ambayo nimepewa dhamana tu. Inapita kwenye mikono yetu kwa muda fulani, ataondoka kuwa na hatima yake. Wajibu wetu kwao ni kwa miaka michache sana, kuwasaidia kufikia hatima yao.” Mina akajua anamzungumzia baba yake, yule askofu aliyemlea huko Nairobi.

“Akaniambia nifanye kana kwamba nafanya kwa Bwana. Nitimize wajibu wangu, kisha kuwaacha wote waende zao. Si unasikia jinsi inavyosikika rahisi?” Mina akatingisha kichwa kukubali. “Lakini je, ni rahisi?” “Mimi nishaanza kujuta kurudi na kumtafuta.” “Lakini huwezi jua kurudi kwako kulivyo faraja kwa wazazi. Unaposikia baba ni mgonjwa, ni kweli aliumia sana kuondoka kwako na watoto, tena mkiwa nyumbani kwake!” “Andy!” “Oooh! Ilikuwa mbaya sana. Iliwauma mno. Na wao wakabaki wakijilaumu kuwa walishindwa kuwa msaada kwako. Na bado mama yako alikuwa akitulaumu sana.” Mina akazidi kuumia.

“Kwa hiyo uwepo wako hapa na hao watoto ni faraja kwa kila mtu. Kusudia kubaki kwa faida ya wengi. Itakua rahisi? Hata kidogo. Lakini naamini baadaye kila mmoja wetu atapata nafasi yake kwenye maisha ya kila mmoja wetu na patatulia tu. Mwanzo ni mgumu, itabidi sisi kama wazazi wa karibu wa hawa watoto kulipa garama kubwa ili kutuliza familia nzima. Tulia.” “Tunaondoka lini?” Mina akauliza.

“Nilikuwa nikifikiria na kuomba ushauri wa kidaktari, nafikiri tumpe mtoto mpaka siku ya kesho. Akishinda vizuri, jioni turudi kwetu.” Mina akavuta pumzi kwa nguvu nakutulia. “Acha nikupokee mtoto. Na usiogope. Kila kitu kitakuwa sawa. Tujipe muda.” Kabla hajampokea mtoto, Pius akawa amefika hapo.

“Nitatoa kiti chake, niwape.” Akaongea akiwa amepoa kabisa kama si yeye! Wakajua mama Ruhinda ashazungumza naye. “Hamna haja. Acha tu kibakie kwako. Mina ataondoka na nyinyi.” Mina hata hakujibu, akaondoka hapo kuelekea kwenye gari la Pius. Andy akamfuata na mkoba wa mtoto.

Kwenye gari akawepo mama Ruhinda, Ayvin, Mina na huyo Pius. Mzee Ruhinda akaondoka na gari yake, na Andy vilevile. Safari ya kwa wazazi ikaanza.

~~~~~~~~~~~~~

Walifika nyumbani, Mina akawaachia Ayvin hapo sebuleni na kuanza kumtafuta Ayan. Akamkuta amekaa jikoni na dada yake akipika, yeye ametulia kimya kama mkiwa. Alifurahi kumuona mama yake huyo! Hakuamini. Akamkumbatia na kuongozana naye chumbani. Wakatulia huko, hakurudi tena sebuleni.

Baada ya muda mfupi tu kuingia chumbani, Andy akawafuata. “Vipi huyo?” Mina akamchungulia mwanae. “Nimekuta amenyongea! Ila mzima. Njoo tukae wote.” Andy akaenda kukaa.

~~~~~~~~~~~~~

“Kesho kabla ya kuondoka, naomba niende na watoto kwa mama.” “Unataka nikusindikize?” “Hapana. Kuna mambo nataka kuzungumza naye, naona tutahitaji muda wa peke yetu. Ila naomba niongezee heshima, Andy mume wangu. Mpigie wewe kumtaarifu kwamba kesho nitakwenda na watoto. Asubuhi mapema tu kwa sababu tunatarajia kurudi Dodoma.”

“Naomba wewe ndio umtaarifu kurudi kwetu na mwambie unatuchukua mimi na watoto. Itaniongezea heshima.” Andy hakuwa akiamini. “Sio wewe tu Mina! Na mimi pia. Hujui unachokifanya kwangu. Nilishapoteza heshima kabisa. Kila mtu alikuwa akinilaumu kwa kuondoka kwako na kuona sijui mahusiano.” “Pole Andy. Na samahani mume wangu. Nimekuingiza kwenye fedheha. Ila naamini ulichosema, tutakuwa sawa.” “Kabisa.”

“Nashukuru, basi itabidi kuwaaga wazazi usiku huu ili wakiamka na kutukosa, wasiingiwe na wasiwasi na nitawaambia nishakuomba wewe ruhusa, umekubali niende na watoto kabla hatujaondoka.” “Sasa usije badili mawazo huko, ukaondoka moja kwa moja!” “Siwezi Andy. Niliondoka nilikuwa sina kimbilio. Sasahivi wewe ndio utakuwa kimbilio langu, usije tu nigeuka.” “Siwezi Mina.” Wakaendelea kuzungumza hapo wakicheka yao, mpaka walipokuja kugongewa na mama Ruhinda.

~~~~~~~~~~~~~~

“Ingia tu mama.” “Naona kaka mdogo ameanza kujilamba na kuhangaika.” “Ukiona hivyo njaa imemuanza. Ikifikia sehemu fulani hivi huko tumboni kwake, wala hutauliza, wote mtajua ni njaa tu. Nipe ale.” “Na huyo kaka yake?” “Ameshalala. Nilimuacha hapa makusudi. Nilikuwa na hamu naye! Acha Andy amtoe mdogo wake ale.”

“Sasa maziwa yenyewe yapo?” “Nimetoka kunywa supu sasahivi, dada yake ameniletea, nasikia yamejaa.” “Afadhali. Akimaliza nitakuja kumchukua tukakae naye. Au unaona alale?” “Wewe mama fanya naye utakacho. Sina neno. Ilimradi ale tu. Akishashiba huyu, popote ukimuweka atalala tu.” “Basi nitarudi.” Akatoka, akaanza kunyonyesha, Andy ameinama anaangalia simu yake.

Akamaliza na kumbadilisha kabisa. “Amelala hana habari na alipo.” “Sasa utafanyaje? Unamlaza au utampa mama?” “Acha tu tuwape. Bado wanahamu nao.” “Basi mimi nitampeleka.” Andy akamchukua vizuri, na kumuweka kifuani mpaka Mina akafurahi, ndio akaondoka naye akiwa amemshika kwa upendo! Mina akaanza kumshukuru Mungu huku akifikiria zaidi jinsi ya KUMSAIDIA mumewe ili aweze kumudu hiyo hali.

~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya muda Mina akashuka. Akawakuta hapo sebuleni, Pius amejiegemeza, na kuweka mtoto wake kifuani, Ayvin amelala, hana habari. “Baba na mama, nimekuja kuwaaga. Kesho asubuhi na mapema, nitakwenda kumuona mama kabla ya safari ya Dodoma. Nawaambia mapema ili msije amka mkanikosa mimi na watoto mkapatwa na wasiwasi.” “Kwamba unaondoka na watoto wote?!” Akahamaki Pius. Mina akatulia bila ya kumjibu.

“Utarudi saa ngapi, maana nataka muda na mtoto kabla hamjaondoka.” “Nimeshamuomba ruhusa Andy, amekubali niende na watoto. Lakini kama wewe unataka kubaki hapa na Ayvin, nitakuacha naye na maziwa kwenye chupa.” “Si umesema hataki chupa?” “Anakaribia miezi sita, sio vibaya akaanza kujifunza. Vinginevyo, itabidi niende naye, unisubiri mpaka nitakapo rudi.” Mina akamjibu taratibu tu.

Kisha akamgeukia mzee Ruhinda. “Kwa hiyo ni hivyo baba na mama.” “Utarudi Mina, mwanangu?” “Lazima mama. Niliondoka kwa sababu nilikosa kimbilio mama yangu. Lakini sasahivi ninaye Andy ambaye nilidhani hawezi tena, au atashindwa kuishi na sisi, lakini mume wangu ametupokea sisi wote, mama. Sina sababu ya kuondoka tena. Na najua niliwaumiza wazazi wangu, naomba radhi, na nawaahidi sitarudia tena.” Walifurahi hao wazazi wawili!

“Au nikusindikize?” Mama Ruhinda akajaribu. “Nimemuomba Andy niende peke yangu ili tukawekane sawa na mama. Tunahitaji kuzungumza kwa kirefu na nimuache ameelewa.” “Sasa kama ni mazungumzo marefu, utarudi hapa saa ngapi? Na si kwamba nakufunga wewe, nataka kupata muda na mwanangu.” “Basi ukija kesho, utamkuta hapa na mama.” Akaanza kubabaika tena yeye mwenyewe, wote kimya wakimwangalia.

Mina akasimama akitaka kuondoka. “Sasa mbona unaondoka hatujamaliza!?” “Una uchaguzi mmoja tu, na nishakupa. Siwezi kujirudiarudia. Sema kama unabaki na mtoto au nimchukue mimi. Maana swala la mimi kwenda au kutokwenda si uwamuzi wako, Pius. Mume wangu ameshaniruhusu.” Mina akabaki akimtizama.

“Unataka mwanzo wangu na mwanangu uwe wa mapambano? Yaani mimi ndio nianze kumlazimishia kitu asichokipenda?” “Kama nitakuwa nimekuelewa, umeamua mimi ndio niondoke naye. Kwa hiyo utapata taarifa tutakapo kuwa tumerudi.” Akatulia kidogo, alipomuona hajibu akaondoka. Wote kimya.

Mama ni Mama Tu.

          Kesho yake asubuhi Mina aliondoka hapo na watoto wake pamoja na msichana wa kazi. “Nitakuwa nikikupigia Andy, usiwe na wasiwasi. Na sitachelewa kurudi.” “Na mtoto akianza maumivu pia nijulishe, tumrudishe hospitalini.” “Sawa. Japo naamini atakuwa sawa.” Mina akaondoka na kumuacha mumewe roho juu juu hana uhakika kama atarudi au la. Aliondoka na gari ya mama Ruhinda akiwa amepewa kiti cha Ayvin na baba yake.

~~~~~~~~~~~~~~

          Ilipofika mida ya mchana akampigia Andy. “Kuna mambo nafanya kabla hatujaenda kutulia Dodoma. Naomba nivumilie. Tuondoke usiku.” “Kwema? Mbona unasikika haupo sawa?” “Sipo sawa Andy. Ila nitakuja kukwambia kila kitu. Kwa sasa naomba niombee kikao cha familia kwa baba, kabla hatujaondoka. Mwambie naomba Pius, Paulina wasikose kwenye hicho kikao.”

“Ni nini Mina?” “Nipo katikati ya watu wananisubiria. Nimeomba kukupigia tu ili kukutoa wasiwasi. Nitakueleza kila kitu baadaye. Usiwe nawasiwasi. Nakupenda Andy.” “Nashukuru kwa kunipigia. Nilishaanza kuwa na wasiwasi.” “Siwezi badilika. Baadaye.” Wakaagana.

Ukila Na Kipofu, Usimshike Mkono.

          Ndilo KOSA walilofanya kina Ruhinda. Waliletewa kipofu na Andy, wakala naye wakimshika mkono. Sasa anakula nao sahani moja, tena sambamba bila ya kuwabakiza. Kwenye majira ya saa 11 jioni ndipo Mina akawa akiingia hapo kwa wakweze.

Andy akasimama kwenda kumpokea mtoto. “Samahani nimechelewa.” “Usijali. Pole. Unaonekana umechoka!” “Nimechoka Andy! Tutafanikiwa kuondoka leo?” “Pumzika kwanza na unipe hali ya mtoto.” “Tokea nilivyokujibu saa zile kwa ujumbe, hali yake haijabadilika. Yupo vilevile.” “Afadhali.” Walikuwa wamesimama kwa kuingilia ndani, wa sebuleni wanawasikia.

“Naona huyo akalale Andy. Ayan yeye nilimuacha kwa mama, nasikia alilala. Yupo sawa.” “Basi wakati mdogo wake analala, yeye aogeshwe. Tutaondoka na ndege ya mwisho kabisa.” “Asante Andy.”  Ndipo wakaingia.

Mina alionekana amechoka. “Pole Mina. Kwema?” Mama Ruhinda akamuwahi. “Si kwema mama. Nilikuwa mbiombio siku nzima. Shikamooni.” Aliwakuta wote hapo sebuleni bila watoto wao na Raza. Ila Paulina alikuwepo na mumewe. Paul, Pius, mzee Ruhinda pia alikuwepo. Ayan naye akasalimia na kumsogelea babu yake. “Nimekuletea zawadi.” Mzee Ruhinda akacheka. “Ila umpe na bibi.” “Nilijua umenisahau Ayan!” Akacheka. “Babu atakugawia. Aliniletea anko Ron mbili. Nikala nusu. Nusu nampa dad, halafu moja nimewabakizia nyinyi mgawane.” Ilikuwa chokleti. “Asante kutukumbuka Ayan. Kumbe wewe ndio kaka mzuri hivyo! Unajali familia!” Akacheka tu akimlisha baba yake aliyekuwa amembeba Ayvin, hiyo nusu, alikuwa ameifunga vizuri akionekana kweli alikusudia ifike hapo. “Asante Ayan.” Baba yake akamshukuru. “Bibi mzima?” “Amewasalimia. Amesema niwaambie asante sanaaaaaaa. Bila mwisho.” Wakacheka.

“Haya, Ayan nenda kaoge.” Akaondoka. “Badala ya kumlaza PJ naomba nimpakate mimi kabla hamjaondoka naye.” Andy akaenda kumkabidhi kaka yake. “Kula hata kidogo ndio uje uzungumze.” “Nimeshindwa Andy. Naona pengine tukizungumza ndio nitatulia.” Andy akamtizama, akajua kweli kuna kitu kimemvuruga sana. “Pole.” “Asante.” Akamshika mkono kumuongoza kwenye kochi akae pembeni yake, kisha yeye akanyanyuka na kuondoka hapo.

~~~~~~~~~~~~~~

“Vipi hali ya mama huko?” “Afya yake anaendelea vizuri. Anawasamilia.” Kisha akatulia, wote kimya. Andy akamletea kikombe cha maziwa. “Naomba kunywa haya maziwa. Unaonekana umechoka Mina.” “Asante Andy.” “Moto, kuwa mwangalifu.” Akaanza kuyanywa. Kila mtu kimya.

“Yamalize kwanza. Usiyaache. Hakuna haraka. Wote tupo hapa kukusikiliza.” Wakamsikia Andy akimbembeleza mkewe. Mina akamaliza. “Asante.” “Karibu. Sasahivi unaweza kuzungumza.” Wote wakamwangalia Mina.

Kipofu Aliyeshikwa Mkono.

“Baba na mama, najua mmezungumza na kila mmoja wetu hapa jinsi ya kuishi pamoja. Inawezekana mimi nimekua mgeni kwenu, sijajua jinsi mnavyoishi, na pengine hivi ndivyo mnavyoishi. Lakini mimi hivi naona sitaweza ishi hivi na wanangu. Na kuondoka tena sitaondoka, maana naona namtesa mume wangu na kuwapunja watoto wangu nafasi ya kuwa na nyinyi.” Wote kimya.

“Sasa kwa kuwa nimewaona nyinyi ni WASOMI. Mnafanya mambo yenu KISHERIA kama alivyofanya Paulina KWANGU, na mimi nimeona nimuige.” Wote wakashituka. Akafungua pochi, alikuwa na kabrasha lilionekana safi kabisa.

“Naomba nianze na Pius, na usiniingilie mpaka nitakapo maliza. Ukiwa hujaridhika na chochote nitakachokwambia ambacho kimeandikwa hapa, unachaguzi mbili. Kuonana na mwanasheria wangu.” Walishituka zaidi, hawakutegemea. “Mina?! Ndio tumefika huko?” “Wewe ndio umenifikisha huko Pius. Nimesikia ukionywa na baba zaidi ya mara moja. Tena kwa kurudiarudia. Unamtukana mume wangu mbele za watu. Hata mama ambaye tulidhani utamsikiliza, humsikilizi.” “Kwa…” “Nimekuomba usiniingilie Pius.”

Nishashitaki kila kitu.” “Haah!” Wote wakahamaki. “Yaani hapa, kila kitu kipo kwa maandishi kwa mwanasheria wangu ila KWA SASA, yako hatujafikisha polisi. Kila kitu, kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Na ushahidi wote upo kwa huyo mwanasheria. Utakapoona chochote hapa hujakipenda au  hujakubaliana nacho, usitukane yeyote yule. Ndio inakuja chaguzi yako ya pili kama ukishindwa kuzungumza na mwanasheria wangu, basi nenda kashitaki popote kisheria. Vinginevyo wasiliana na huyu dada,  ambaye ndio mwanasheria wangu, namba zake za simu zipo hapa. Uchaguzi ni wako.”

“Cha kwanza na cha muhimu kutoka kwangu. Nakuonya, usiwahi kurudia kumtukana Andy mbele yangu kwa kuwa ni mume wangu na watoto wangu wanamtizama yeye kama kiongozi wa familia. Kama kwako hafai, ni wewe. Lakini wale ambao Mungu ameona wanamstahili yeye, ndio hao amewapitishia kwake. Tunza heshima yetu. Unao watoto wako na mke wako, waongoze vile unavyotaka wewe, ILA sisi, mimi na watoto nitakao zaa nikiwa mke wa Andy, tutaongozwa na Andy.”

“PJ ni..” “Nilikuomba usiniingilie.” Wote kimya. Mina akaendelea. “Nakuja cha pili, mimi Mina, kama mama yake, nimekataa rasmi huyo mtoto kuitwa jina lako kwenye familia YETU.” “Haiwe…” “Unaniingilia Pius. Na hiyo tabia yako mimi sina muda nayo. Huwezi kunisikiliza, twende mbele ya vyombo vya sheria.” Kimya.

“Jamani, ninapo waambia nimeandikisha kila kitu kwa huyu mwanasheria, ni nimeandika KILA KITU. Kuanzia mimba ya huyu Ayvin kutungwa, na yooote yanayoendelea mpaka sasa tulipo kaa hapa.” “Sasa huko si ni kumfunga Pius?!” Mama Ruhinda akalalamika.

Utanisamehe mama, na baba pia. Lakini watoto WENU wamenifikisha hapa. Na watamuua mama yangu, siwezi kuwaacha hivihivi. Najua kwako mama unawasiwasi na upande wa watoto wako, na mimi pia nina wasiwasi na watoto wangu.”

“Watoto wako wananiharibia kwangu. Na wao ndio wamenifikisha hapa mama. Utanisamehe. Ila ukitulia, utagundua ninachofanya mimi hakifiii hata nusu ya wanachofanya wanao, kwangu. Uzuri au ubaya, ushahidi wangu haukuwa shida kuupata. Palepale kwenye ofisi ya huyo mwanasheria, wakanisaidia kuupata huo ushahidi. Mambo yangu, au maisha yangu mimi, yapo wazi mtandaoni. Yaani palepale kwenye ofisi ya mwanasheria, wao wenyewe wameweza kutoa video zangu mpaka hospitalini.” Kimya.

“Pius, mwanzoni kama unakumbuka, nilikukubalia mtoto aitwe PJ, lakini Pius nimekuangalia, nimeona utasumbua sana, na wewe ni muharibifu. Sitakuruhusu uniharibie mazingira ya wanangu na ndio maana nimeweka mambo yote kisheria. Mtoto ataitwa Ayvin Ruhinda. Ukiwa naye utamuita vile utakavyo. Ila kwetu sisi na kwenye VYETI vyote atabakia kuitwa Ayvin Ruhinda.” Mina akaendelea.

“Una siku mbili tu za kuja kumuona mtoto. Ijumaa na jumamosi. Tafadhali usifike kwetu siku ya jumapili, ni siku yetu. Nimeichagua hiyo kwa sababu kwenye mazungumzo nimegundua ndiyo siku Andy hahitajiki kazini kabisa. Sasa basi, katika siku hizo mbili, ijumaa na jumamosi, tafadhali toa taarifa, usitokee tu.”

“Sasa kwa kuwa umeshindwa kumuheshimu Andy, basi waambie wazazi siku utakayofika kumuona Ayvin. Karibuni sana atazoea chupa, hata ukija kumchukua na kwenda naye unapotaka wewe, ruksa. Ila kwa sasa, nilazima usiku awe analala nyumbani. Hujaridhika na hilo, nenda kashitaki popote unapotaka wewe. Ila sio hapa, tena sasahivi.” Walipoa hapo, hakuna aliyeamini.

“Lakini ikitokea upo safarini, siku zinabadilika, wasiliana kama nilivyokwambia ilimradi tu upate muda na Ayvin kwa juma, hatutakuwa wakatili eti kusema tutasimamia hapohapo siku ya ijumaa na jumamosi tu, hapana. Ila ni lazima kuwa na utaratibu.”

“Ayvin atakapokuwa mkubwa, tutapanga zaidi. Na nimefanya hivi makusudi ili kwangu kuwe na amani, kama kwako. Na wote mkitulia mtagundua na mimi nafanya kama alivyofanya Paulina kwangu. Kuniwahi kisheria, ila mimi si sababu ya MALI kama yeye. Binafsi nataka wanangu wakue kwa utulivu na ndoa yangu ISIHARIBIWE.”

“Hizi hapa ni nyaraka zako. Upo huru kusoma au kutosoma. Upo huru kufuata kilichoandikwa hapa au la. Ila kama ungekuwa ukisikiliza ushauri wa mtu, mimi ningeshauri usome, ili usikiuke chochote kile. Kwa sababu, sitarudia tena aina hii ya vikao na wewe ukitugomba mimi na Andy kama watoto wadogo huku ukirudiarudia kutudhalilisha kwa dhambi zetu za nyuma. Leo ndio mwisho Pius.”

“Utakapoweza kurudi kumuheshimu Andy, utazungumza naye na kupanga zaidi. Ila kuanzia sasa, hutawasiliana na mimi moja kwa moja. Mtoto akiwa mgonjwa kama hutakuwa naye, utapata taarifa. Umeshauriwa kumfungulia akaunti yake, umuwekee yeye pesa. Sio mimi tena. Andy amekataa. Na naona tufanye hivyo. Unaweza wewe kufungua hiyo akaunti, au mimi nitafungua na kupewa taarifa zote.” Kimya.

Wifi

“Baba na mama. Nazidi kuomba radhi na kurudia, watoto wenu WAMENIFIKISHA hapa. Na Paulina huyu ndiye amenifanya nifikirie chakufanya na kuomba ushauri wa kisheria.”

“Nilifika kwa mama, sikukuta taarifa nzuri. Ikabidi sasa kwenda Ustawi wa Jamii. Huko nako nikakuta wanataarifa zangu na video zangu. Huyo niliyemkuta hapo ndio akanishauri vizuri na ndiye aliyenipeleka kwa huyu sasa mwanasheria anaitwa Sonia Tambo. Baba yaje alikuwa Judge mkuu wa Tanzania. Sijui kama mnamfahamu?” “Mimi namfahamu sana.” Mzee Ruhinda akadakia.

“Basi huyo mama wa Ustawi wa Jamii, ndiye aliyenipeleka kwake. Akaniambia Sonia anatetea sana wanawake wanaoonewa au kukandamizwa. Zaidi anasimama na wanawake wahitaji. Akasema kwa sababu ametoka kwenye familia iliyofanikiwa sana, maana bibi yake pia alikuwa mkuu wa Usalama wa Taifa. Anao uwezo mkubwa sana kwenye kesi zake maana anapata ushahidi kiuharaka.” “Hata Tambo mwenyewe alitumika sana kama Waziri kabla ya kifo chake. Alikuwa muadilifu sana.” Mzee Ruhinda akaongeza.

“Endelea Mina.” “Asante baba. Nilikuja kuamini. Yaani yule dada nimefika ofisini kwake, ndani ya lisaa, akaita video ambayo sikuwa hata najua kama naweza pata, akapata.”

“Turudi kwa mama kwanza. Umesema ulikuta hali si nzuri. Ni nini Mina binti yangu? Samahani lakini.” “Paulina na mwenzie Raza, baba.” “Mimi nimefanyaje?!” “Yaani baba, huyu Ayvin si mnadhania amekuja jana tu watu hawamfahamu, lakini sivyo! Jana ileile mwanangu akiwa mgonjwa, Paulina alishampiga picha, yeye na kaka yake na kumtumia Raza na watoto wa mama mkubwa.” Walishituka pale, Pius nusura atupe mtoto, amvamie.

Haiwezekani Mina! Sio kweli!” Mama Ruhinda alikuwa kwenye mshituko, ameshikilia moyo. “Huyo hapo Paulina, AKATAE.” Ulitokea ugomvi hapo, Andy kimya akimwangalia dada yake. Pius alimuita dada yao kina Ayan na kutaka amchukue mtoto. Alipochukuliwa tu akamvamia Paulina, mumewe akamuwahi na kusimama naye.

“Acha Pius. Tafadhali usimpige.” “Wewe unaona alichofanya ni sawa?” “Sasa itasaidia nini ukimpiga? Tulia aisee.” Mumewe akamtuliza shemeji yake. “Mnapaniki nini? Kwani ilikuwa siri?! Wewe vipi Pius?” Paulina aliongea bila wasiwasi.

“Naomba mimi nimalize tuondoke na mume wangu. Mtaendelea wenyewe baadaye. Pius tulia. Maana ni hayahaya niliyosema. Mazingira yenu haya, hayafai kwa wanangu.” Ndio wakatulia.

“Yaani baba!” Mina akamgeukia mzee Ruhinda aliyekuwa kama amepigwa shoti ya umeme. “Nimemkuta mama yangu anasononeka na hofu. Kusononeka sababu ya kukutana na mjukuu mpya kwenye picha, pili VITISHO vya Raza ndio vinamuogopesha zaidi.” “Raza amesema nini?” Pius akauliza, lakini Mina akaendelea akimpuuza.

“Nimemkuta hajala tokea mtoto wa mama mkubwa na mama mkubwa wamfuate nyumbani. Yaani wamemwambia mama, japokuwa yalikuwa ni maswala ya umbea, lakini sisi ni ndugu, imebidi kumfuata mama kumwambia LAZIMA afanye kitu. Ila wao walimshauri na yeye aende kwa waganga amuwahi Raza, ndio mama akawakatalia akasema yeye mganga wake Yesu. Atamlilia, mpaka amlindie wajukuu zake ambao hawana hatia.”

“Maana Raza nasikia analalamika anasema, nilipokuja kwenye maisha yenu eti nikagundua Pius mwenye mali nyingi hana mtoto wa kiume, eti ndio nikafanya ushirikina mpaka kumbembea mimba mumewe ambaye alishamfunga huyo mumewe.” “Unamaanisha nini?” Andy akauliza.

Mina akasita. “Sema tu usiogope. Weka wazi tu ili wote tuyajue.” “Samahani wazazi wangu. Naweza nikawa naongea neno baya, ila kama alivyosema Andy, acha niseme tu.” “Tushavuka huko Mina binti yangu. Naona hakuna anayetaka sitara hapa. Wameamua kuanika mambo hadharani, wewe tuambie kinachoendelea.” Wazi mzee Ruhinda alionekena upande wa Mina bila kujificha.

“Eti Raza anasema Pius hana uwezo wa kulala na mwanamke yeyote yule hata kama akitaka, amemfunga nguvu. Sasa eti kwangu amewezaje wakati yeye alishamfunga! Eti mimi natumia waganga wenye nguvu lakini atanishinda tu.”

“Na amesema atanilipiza kisasi kibaya sana kwa kuzaa na mumewe. Maana anasema eti nia yangu ni ili Ayvin arithi mali ZOTE za Pius sio binti zake. Amesema yeye hakubali.” Wote wakaingiwa hofu, Pius alikuwa amebadilika!  

“Anasema ameshahangaika sana na Pius tokea zamani, hawezi ruhusu mwanangu aje achukue haki yake na wanae.” “Raza hajawahi hangaika na mimi. Amenikuta na mali zangu na nyingine nimepata wakati yeye akijua kutapanya tu!” “Sasa mimi hayo siyajui ila jumbe zake zote za malalamishi na vitisho wamempa mama, na mimi nikaenda kumuonyesha zote mwanasheria wangu, binafsi akaona ni hatari, anaweza kweli kumuua Ayan au Ayvin mtoto asiye na hatia, akaona twende polisi.”

“Tumemfungulia kesi polisi. Hivi atamtafuta Raza, amuonyeshe na kumwambia kesi yake ishaandikishwa polisi ila sijamshitaki. Chochote kikimpata mtoto wangu hata mmoja, na mimi, hata kama ni baada ya miaka 30 kuanzia sasa, atakamatwa yeye.” “Mungu wangu?!” “Sina jinsi mama. Watakuja niulia wanangu wasio na hatia!” “Sio wewe Mina!” Mama Ruhinda akamjibu lakini wazi akionekana na mshituko mkali sana.

“Na Paulina, wewe ni mbaya wa kupitiliza.” “Nimefanya nini mimi?! Kwani mtoto alikuwa siri?” “Jumbe zako zote ninazo, na zimetunzwa. Wewe ni MCHONGANISHI. Unawasha moto, halafu una kazi ya kumwagilizia petrol kila unapoona panaanza kupoa, kisha unajiweka pembeni. Upo pale hospitalini watu tunajua upo kwa ajili ya ugonjwa, kumbe ili kusambaza maneno. Utamuua mama yangu kwa pressure.” “Kama ni mgonjwa ni yeye tu, mimi hainihusu.” Paulina akajibu kwa jeuri kama asiyejali.

“Basi nimeamua kukuwekea kikomo Paulina. Bwana kuna watu wana UWEZO wa mambo hapa nchini, sijawahi ona! Nilipomueleza Sonia juu yako, na JEURI yako, mpaka ulichonifanyia siku ile hospitalini ulipojua ni mjamzito wa Ayvin, palepale akaomba atumie video kutoka kwenye kamera/cctv za hospitalini. Bwana umeletwa kama ulivyo!” Wote wakazidi kushangaa.

“Ninayo hapa kwenye simu.” “Naomba kuona Mina. Pole.” “Ni mbaya Andy! Yaani ukiangalia hivi kwenye video ndio utajua ubaya wa dada yako kwangu. Alinisukuma vibaya na kunipiga zaidi ya mara moja, kasoro ya ofisini kwa daktari tu, ndio hapakuwa na kamera. Ila Sonia amesema tukihitaji, hata huyo daktari ataitwa mahakamani na atatoa ushahidi kwa lazima hata kama anafahamiana na nyinyi kina Ruhinda.”

“Sonia amenihakikishia kwa asilimia ZOTE, kuwa siku hiyo huyo daktari atakapohitajika mahakamani, atasimama na kueleza ukweli wote wa kile kilichotokea kwenye kile chumba wakati amenipa taarifa za ujauzito wa Ayvin.” “Kwamba umemshitaki?” Mumewe akauliza.

“Afadhali umeuliza ili usikilize kwa makini, uje umkumbushe mke wako. Mungu amewageuza mioyo ya watoto wa ndugu zangu kwa ajabu, sijui kwa nini, wote wamejirudi kwa mama. Wamesema washaona hii familia yenu ni hatarishi.” “Wao wenyewe ndio wanatutafuta.” “Hujanisikiliza Paulina. Jumbe zako na za Raza kwa ndugu zangu zote zimekamatwa na ZIPO. Mmewaanza nyinyi wenyewe, na wanasema mnalia wivu. Sasa NAKUONYA Paulina.” Hapo Mina akawa mkali.

“Wewe ni mbaya. Ukianza tena chokochoko zako, ujue umejishitaki rasmi na kuomba kesi yako ianzishwe. Popote utakapozagaza maneno yeyote yale juu yangu na wanangu, ujue umelianzisha. Na sitakuacha Paulina. Nyinyi watoto wabaya. Hamsikilizi wazazi wenu, na hata nyinyi wenyewe hamsikilizani. Mnatakiana MABAYA. Na hata sasahivi usinijibu. Nilikuheshimu, lakini umeshindwa kujiheshimu.”

“Umeweka uadui kati ya mwanangu na Raza, wala hukumpa nafasi Pius amtambulishe Ayvin kwa mkewe, umekimbilia wewe kumchafua mwanangu, asiye na hatia, kwa Raza. Unamchukia mwanangu tokea yupo tumboni. Na hata hilo nimeandikisha. Nilipokuwa mjamzito, ulianza kunivamia hospitalini kwa kunipiga. Na siku nilipokuja hapa kwa wazazi, kumuona Ayan, nikiwa Andy ameniacha na ujauzito wa Ayvin, pia ulinivamia kwa maneno, tena nikakuomba kabisa tuheshimiane, lakini umeshindwa. Sasa ukirudia maneno yako ya uchonganishi juu yangu na wanangu, tunaanza kesi ya kunipiga nikiwa mjamzito. Ushahidi upo. Sitakuacha.” “Hapo jueni baba na mama, huyu ataishia JELA tu. Paulina hajui kunyamaza. Mbea wa kupitiliza. Unalaana wewe!?” “Shika adabu yako Paul. Mimi sina laana.”

“Kinacho kusumbuaga wewe ni nini?!” Paul akaendelea kumuhoji kwa hasira. “Mimi sioni kosa kumtambulisha huyo mtoto kwa Raza.” “Wewe kama nani?! Kama si uchonganishi tu.” Pius akamuuliza kwa hasira zaidi na kumpiga kofi la nguvu la kushitukiza. Kabla hajarudia kumpiga la pili mumewe Paulina akamuwahi tena shemeji yake, kumshika mkono. “Acha Pius.”

“Kwanza hilo pia ni kosa. Umepiga picha wanangu kwa siri, na kusambaza kwa ubaya bila idhini yangu. Hilo ni shitaka, na Sonia amekuandalia vizuri sana. Na namshukuru Mungu na yeye amesoma na ana uwezo kama nyinyi. Anasema anapendaga kushugulika na familia kama hizi zenu, zenye kiburi cha pesa na mamlaka. Nakushauri ujiandae.” Kimya.

“Na mwambie mwenzio Raza mniache. Mnamtafuta Mina aliyekuwa amekosa na Mungu alishanisamehe. Kwa nini nyinyi mnahangaika na dhambi zangu za nyuma, hamtulii, wakati hata Mungu mwenyewe ashasema hazikumbuki tena? Mume wangu mwenyewe ameshanisamehe na alinipokea akiwa ananijua wala sikujificha kwa Andy wangu. Nyinyi mnahangaika na mimi kama nyinyi ni malaika vile, huwa hamkosi? Wakati Raza mwenyewe mchafu kunuka. Wala hajatulia.” Wote wakashituka mpaka mumewe.

“Kama ni mahusiano, Raza ameapa ashaachana na yule mwanaume. Acha..” “Kwamba wewe ulijua kama Raza ana mwanaume nje?!” “Wewe si ulinipiga ukasema hutaki nikuletee maneno kwenye ndoa yako? Sasa unacho paniki hapa ni nini?” Pius akakwama, Paulina akaendela.

“Mimi niliposikia, nikamfuata Raza mwenyewe, maana wewe umesema hutaki maneno ya umbea. Tena nilimfuata na ushahidi kabisa asikatae. Maana aliyekuwa akitembea naye, mkewe ndiye aliyenitafuta, akisema nimuonye wifi yangu, amezidi, ana muharibia kwake. Anakaa na mumewe mpaka usiku mwingi, harudi nyumbani.” Paulina asiyeweza zuia maneno, na hivi Pius ametoka kumchapa kofi, akaona amwage mboga hadharani baada ya Mina kumwaga ugali. Tena kusudi kumkomoa kaka yake akimuanika mkewe.

Akanionyesha jumbe zao. Kati ya mumewe na Raza. Nikazichukua mpaka kwa Raza. Nikamwambia mkewe yule mwanaume anampa onyo asitishe kwa haraka mahusiano ya kimapenzi na mumewe, lasivyo anamfuata mzee Ruhinda mwenyewe maana mumewe, yaani huyu Pius amesikia hapokei simu usizozijua na hapatikaniki kwa urahisi. Ndio Raza akanisihi sana nisiseme na anaachana na yule mwanaume.” Palizuka ukimya hapo. Mina akashukuru Mungu amepata wakuthibitisha maneno yake sio kwamba ni alimshitaki Raza kwa ufitini tu, ni kweli. Maana na yeye aliropoka kwa hasira tu, hakutegemea kuyaongea ya Raza hapo.

Akaendelea. “Nyinyi wote wawili hamna utakatifu wowote ule. Acheni kuhangaika na mimi, maana mimi sihangaiki na yenu. Niliyofanya, niliyafanya zamani, nimetubu, na Mungu amenisamehe. Niliingia kwenye ndoa, nikatulia na Andy. Achaneni na mimi. Sasa nikusikie tena.” Hapo Mina akaongea naye kwa ukali kabisa bila nidhamu aliyokuwa akimpa zamani ila kila mtu kimya. Yalitibuka ambayo hakuna kati yao aliyetegemea.

Kwa Wazazi.

Akawageukiwa wazazi. “Baba na mama, najua nimewaumiza. Ila sikuwa na jinsi. Watoto wenu wabaya. Watanifanya mimi ndio wa kukimbia, naacha ndoa yangu, wao wakisha nikorofisha, wanarudi kwenye ndoa zao. Wanatuacha mimi na Andy wangu tunafarakana. Safari hii mimi sitaondoka kwa mume wangu. Napenda ndoa yangu. Nataka kubaki na Andy. Watoto wenu hawatanikimbiza tena. Tumekubaliana na Andy kuanza upya.”

“Pius akianza kumkumbusha tu mambo mabaya ya zamani, nampigia simu Sonia. Namwambia anavuruga amani kwenye mazingira ya anapoishi mtoto wake, basi Sonia amesema hata hizo siku mbili alizopewa, atapokonywa na kuanza kuchunguzwa kwa upya ndipo kuamuliwe kama ataweza kuwa na sisi kwenye malezi ya mtoto au la!”“Mina!” Pius akashangaa kwa kulalamika.

“Wala hapana ugumu hapo. Ni wewe uwe na adabu, ili uwe na mwanao. Basi. Mengine kati ya Mina na mumewe, ndio unaambiwa kisheria, maana kwa kupitia sisi umeshindwa kukubali. Unaambiwa hayakuhusu. Kilichotokea nyuma, ni kati ya Andy na mkewe. Wewe angalia ya mwanao. Sasa hapo ugumu uko wapi?!” Mzee Ruhinda akamuuliza kwa ukali.

“Ila nyinyi nawapenda baba. Mama na baba msione nimewalipa ubaya wakati nyinyi mnapenda wajukuu zenu na mmesimama na mimi. Hapana. Wajukuu zenu wapo, kwa Andy. Muda na wakati wowote, nimezungumza na Andy, mnakaribishwa kuwaona. Baba, hata kama una hamu nao, na huna muda wa kuja kule, niombee kwa Andy, mimi mwenyewe nitakuletea wajukuu zako ukae nao hata kwa masaa machache tu. Mimi sitawatenga na wajukuu zenu. Ni hayo tu wazazi wangu. Mimi naenda kuandaa wanangu, tuondoke.” Kimya.

~~~~~~~~~~~~~~

“Mimi naomba kukuuliza Paulina, kwa hiki ninachokuona ukifanya kwa Mina. Kuanzia hospitalini alipogundulika ni mjamzito, ukampiga kikatili hivi mpaka jana unasambaza watoto wetu kwa ubaya, sema tu ukweli, nia yako ni nini?” “Wala sikuwa na nia mbaya. Nil..” “Jamani, mkiona hii video, unaweza sema alikuwa akipiga mwizi!” “Na ndivyo nilivyojua, ameiba nje ya ndoa!” “Kweli Paulina wewe hujutii hata kidogo!?” Baba yake akauliza akimshangaa sana binti yake.

“Si ndio maana ameshitakiwa? Sasa jichanganye uone kama hujaishia jela, na shule yako yote hiyo, itaishia gerezani. Ukaongee umbea huko.” “Unafiki tu wewe Paul. Unashindwa…” “Jamani hii video inasikitisha, ni ngumu hata kuangalia mara ya pili.” “Naomba na mimi kuona Andy.” “Na mimi.” “Acheni niwatumie kwenye kundi la familia. Japokuwa unajitetea Paulina, nafikiri ulichotakiwa kufanya nikuomba msamaha.” Andy akaongea akituma hiyo video.

“Muache tu Andy. Lakini hakika nakuonya Paulina. Wewe ni mbaya na hatarishi sana. Umetibua mazingira ya amani ya wanangu, ila jua mimi sijali kwa kuwa sina shida na pesa ya kaka zako, unayo hangaika nayo. Jua nitalinda watoto wangu kama simba. Nikikusikia tu tena, hakika utawapisha. Wewe si ulidhania mimi ndio nitatizo na nitakupisha, basi jua wewe ndio utapisha wanangu. Hutasababisha Raza aue wanangu.” “Na wala hataua hata mmoja.” Pius akadakia.

“Wewe unayeishi naye nyumba moja wala hujui vitisho anavyosambaza juu ya mwanangu, leo unauhakika gani kama kweli hatamuondoa mwanangu?” “Unazo jumbe zenyewe nione?” “Wewe umeniudhi na kuniumiza sana Pius, siwezi kukuonyesha. Kaangalie kwenye simu ya mkeo au ukitulia na kuona Andy anafaa kuzungumza naye kwa heshima, muombe yeye. Lakini mimi nimekukasirikia Pius.”

“Wewe ni mbinafsi na huna adabu kwa watu. Sikujua kama upo hivyo! Nilikuwa nakuona ni mtu mzuri lakini na wewe unahatarisha mazingira ya mwanangu, kwa kuweka chuki kati yake na Andy.” “Mina!?” “Niambie tofauti yako wewe na hiki alichokifanya dada yako, Paulina ni kipi!? Ameweka UADUI kati ya Ayvin na Raza, na wewe unahangaika kuweka uadui kati ya Ayvin na Andy. Hakuna tofauti na sikuruhusu.”

“Wewe unapenda binti zako na kuwatunza kwa garama kubwa sana, KIMALI. Lakini mimi nalinda vijana wangu ili wakue kwa AMANI. Hamtanitoa tena kwa Andy na hamtasumbua wanangu.” Akataka kuondoka.

~~~~~~~~~~~~~~

“Mina, nakuomba msamaha.” Mina akageuka. “Unaomba msamaha kwa sababu nimekushitaki, wala humaanishi msamaha wako.” “Hakika nimekosa.” “Mara moja hii! Wakati ulikuwa mkorofi muda si mrefu?” “Hapana. Nimejifikiria, nimegundua upo sahihi, nimekosa.” “Basi endelea kujifikiria zaidi, utagundua uliyemkosea zaidi ni Andy, anayekwenda kukulelea mtoto wako. Ukiweza kumuomba yeye msamaha, na kuweka naye amani, ndio urudi kwangu. Usinifanye mimi mjinga.” Akaondoka. Kukazuka ukimya.

~~~~~~~~~~~~~~

Kipofu Kashikwa Mkono, anakula nao sambamba.

Wamemfundisha Mina Kwa Vitendo, Ndio Na Yeye Amefanya Kama Wao.

Walimuanza, Ndio Kawamaliza.

 Na Shule yake ambayo ni kama Nusu yao, ANGALAU amejaribu KUWEKA KIKOMO KWA WASOMI HAO WASIO SIKIA HATA LA WAZAZI WAO.

Patamu Hapo!

Ya Raza nayo Hadharani.

Ni nini kitaendelea?

Usipitwe.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment