Pius
hakuridhika. “Mmemzidishia madawa nini?” “Hata kidogo. Alikuwa kwenye
dozi sahihi kabisa. Huu ni uchovu tu. Yupo sawa.” Daktari akaendelea
kumuhakikishia baba mtu huku akiendelea kumuamsha. “Sasa kama mlihakikisha kila
kitu kipo kwa kipimo sahihi, mbona haamki na mlisema ataamka!?” “Naomba
tulia bwana, Pius! Unataka kuzidisha wasiwasi hapa, umchanganye daktari,
ashindwe hata kufikiria jinsi ya kumsaidia mtoto.” Mina akamwambia kwa ukali
kidogo.
“Ni sawa nikimtoa hapo kitandani?” “Kabisa.” Akamtoa
kitandani na kwenda kukaa naye kwenye kochi. Akaanza kumuombea kimya
kimya huku akimnyoosha vizuri taratibu. Mwishoe akafungua macho. “Muone!
Ulalaji gani huo bwana! Unataka kumtia mama wasiwasi!” Akaanza kucheka kichovu.
“Mchekaji huyo! Mpaka kule theater walikuwa wakicheka anavyocheka na madawa ya
usingizi.” “Ndivyo alivyo. Mwanangu hana neno. Nawashukuru sanaaa. Tena sana.
Kazi yenu njema, na Mungu awabariki kunirudishia mtoto anayecheka hivi
na si kilio.” Angalau Mina akabadili ile hali ya wasiwasi na lawama
aliyoanzisha Pius.
“Nigeuzie na
mimi, Mina.” Bibi yake akaomba akimsogelea. “Haya, msalimie bibi, na
Ruhinda mwenyewe, babu.” Akawa na kazi ya kucheka ila wazi alionekana
amejawa usingizi. “Naomba nimshike kidogo.” Mzee Ruhinda akasogea kabisa
karibu ili kumpokea. Mina akampa.
Akawa anamwangalia. “Haya meno mawili anayatangaza
kweli! Sijui kwa kuwa yanampendeza!” “Nakwambia dada yake alikuwa akimwambia ataibwa!”
Bibi yake akacheka. “Umezaa mtoto mzuri sana Mina. Vijana wako wote
hawana neno na mtu. Hata Ayan alikuwa mtoto mtulivu sana.” “Asante mama.
Namshukuru Mungu.” “Ayan ndio alikuwa si mlizi kabisa.” Babu mtu
akaongeza. “Huyo adui yake njaa na hayo mamumivu.” Mina
akaongeza akimwangalia.
“Basi tukupishe anyonye kabla hajaanza kulia.
Sitaki alie wakati bado ana vidonda.” Pius akatoa wazo lakini
hata Mina hakumwangalia kama ambaye hakumsikia. Ila mzee Ruhinda
akamkabidhi mtoto. “Acha haya mazungumzo na daktari tukayamalizie nje wakati
mtoto anakula.” Wakajua ndio anatoka. Mkewe akamfuata nyuma, Pius na
daktari wakatoka. Mina akaanza kunyonyesha akiwasikiliza huko nje zaidi maswali
anayojibu huyo daktari. Ila akajua wanaruhusiwa.
~~~~~~~~~~~~~~
Mtoto alinyonya mpaka Mina akaishiwa na yeye Ayvin
akamaliza na kuanza kucheka. “Wagonjwa huwa hawali hivi Ayvin wewe! Mpaka ukomboleze
sahani ndio unamaliza!” Mama Ruhinda akaingia. “Ayvin mchekaji! Sasa hapo
amefurahia nini?” “Kushiba! Anapenda kula huyu, naona amemzidi kaka
yake. Angalau Ayan alikuwa anakubakisha na maziwa. Huyu! Haachi mpaka amalize
yote ndio anatulia.” “Maziwa yote?” “Yote mama. Na ni kama anajua. Anafanya
kusubiria umbadilishie.” Wakacheka.
Akasikia mzee Ruhinda anaagana na Pius kuwa anakwenda
kulipia. Kisha akaingia ndani. “Nipe na mimi nimshike!” “Ruhinda kwa wajukuu!
Wewe si umetoka kumshika hapa sasahivi!” “Bora hawa hawanipi pressure kama baba zao.” Akamchukua kutoka kwa mkewe na kurudi
naye kukaa.
Mina Na
Mapinduzi.
Mina akaona azungumze nao. “Najua kuna sehemu Andy aliwachosha.
Lakini wazazi wangu, Andy ananipenda. Alishanieleza ilivyokuwa, binafsi
nimeamua kumsamehe mume wangu na kuendelea na ndoa yangu. Mimi napenda
ndoa yangu, sitaki iishie njiani.” “Umefanya vizuri Mina. Hakuna
ndoa isiyo na matatizo, ni kuvumiliana tu.” Mzee Ruhinda
akaafiki. “Na urahisi unakuja pale nyie wawili mnapoamua kuendelea. Mimi
nakupongeza Mina. Usiondoke na kwenda kulea watoto peke yako.”
“Lakini lazima kufanya mabadiliko mama.” Mina akaongeza na kufikiria
kidogo.
Kisha akaendelea. “Jamani, Andy ni mwanadamu
kama sisi tu. Nia anayo, lakini bila sisi sote kumsaidia, huyu mtoto wa
Pius anaweza geuka kuwa tatizo wakati Ayvin ni baraka. Najua
nyinyi mnafanya kwa nafasi yenu wazazi wangu, na hakika nawashukuru.
Najua mnamajukumu mengi, ila mpo na sisi kila mahali katika kila hali.
Lakini na mimi lazima nifanye kitu. Lazima kumuonyesha Andy, ya kale yamepita
kabisa.”
“Huu mtindo wa ndugu zake kumsema hovyo
mbele za watu na kwangu! Tena kwa kurudiarudia kila wakati, sidhani
kama ni sawa.” “Si sawa Mina.” “Eti mama jamani! Mtu mzima amekiri
kosa. Ameomba msamaha, jambo haliishi!” Mina akaanza kulia.
“Usilie Mina.” “Sipendi jinsi wanavyo mdhalilisha
mume wangu! Si sawa mama. Si sawa
kabisa. Na Pius haonekani kubadilika.” “Mina, binti yangu,
nimezungumza sana na Pius. Sana.” “Nashukuru baba,
lakini nafikiri na mimi lazima nifanye kitu ili kukomesha hii hali.”
“Tulia uniambie vile unavyofikiria kufanya.” Mama Ruhinda akamtuliza.
“Pius anataka kuniharibia
kwangu, wakati kwake ameshapajenga msingi imara, kiasi ya kwamba,
anauhakika Raza hawezi muacha hata akifanya nini. Huo ni msingi
alioweka kwenye ndoa yake. Sisi huko bado hatujafika. Ndoa yetu inashikiliwa
na mapenzi tu. Ndio maana nirahisi kuyumba, ila tunarudiana
sababu ya mapenzi. Lazima na mimi nijenge kwangu mama. Na siwezi
jenga kwangu kama endapo Pius akiwa katikati yetu. Lazima nimuhakikishie
mimi ni mke wa Andy. Japokuwa nimezaa naye, lakini kwangu
ni kwa Andy.”
“Atakuja kuwalalamikia kwa mengi, lakini naomba
mnisaidie tu mjue nia ni nzuri. Sitaruhusu mawasiliano
kati yangu na yeye.” “Hapo atachanganyikiwa.” Mama yake akawaza kwa
sauti. “Siwezi mama. Lasivyo Andy ataishia kuumia tu.”
“Utafanyaje juu ya mtoto wake?” “Nitahakikisha anarudisha HESHIMA kwa
Andy. Na atambue kama mtoto wake anatunzwa nyumbani kwetu, chini
ya Andy. Chochote anachotaka kwa Ayvin, apitie kwa Andy sio
mimi moja kwa moja. Au unasemaje baba?” Mzee Ruhinda akatulia akifikiria.
“Labda kumjulia mtoto hali tu.” “Hapana mama Pius.
Mimi nahisi Mina yupo sahihi, kuvunja hili daraja kati yao kwa muda, mpaka mahusiano ya ushemeji
yarudi. Inaweza ikawa ngumu mwanzoni, lakini nafikiri hii itakuwa njia pekee yakuponya familia nzima ya Ruhinda.” “Asante
baba.” Mama Ruhinda hapo akanyamaza. Pius kipenzi chake.
“Nakuahidi ni kwa muda tu mama. Na wewe nakuruhusu uwe
kati yetu. Andy anashugulikia uhamisho turudi huku Dar. Ila popote tulipo,
milango yetu ipo wazi kwa yeyote anayetaka kuona mtoto. Hata Pius akitaka kuja kumchukua
mtoto na kukaa naye kidogo, ruksa. Na hili nitazungumza na Andy, ila si
kwa kupitia mimi. Hata kama itakuwa wewe mama, kisha mnaweka
mipango na Andy, muda anaotaka kuja kuona mtoto wake, au hata kumchukua.”
“Kuwepo na utaratibu na taarifa maalumu sio mambo yaende kienyeji
enyeji.” “Asante baba. Na haya naomba na wewe mama uzungumze naye, maana mimi
sitazungumza tena na Pius. Ameniumiza sana. Na namuona ni mbinafsi
kupita kiasi.”
“Naomba usimchukie, tafadhali Mina. Na yeye
yupo katikati, hajui chakufanya na hili.” “Hapana mama. Anafanya makusudi
na sitamruhusu hata kidogo. Mtu huyuhuyu asifiwe KOTE kuwa anahekima,
aje ashindwe kumuheshimu mume wangu! Anamtusi mbele
ya watu na kwangu bila kujali! Tena si mara moja! Kwa kurudiarudia
bila huruma! Hapana mama. Lazima katika hilo ajifunze kwa garama
yeyote ile. Tena nashauri umshauri iwe kwa haraka, lasivyo yeye
ndio ataishia kuwa muhanga wala sitakubali iwe Andy au Ayvin.”
Wakajua amekasirika. Pius akaingia, Mina akaingia bafuni. Hakutaka hata kuwepo
hapo.
~~~~~~~~~~~~~~
“Kwema?” Akauliza Pius alipomuona Mina ameondoka kwa
hasira. “Umeshakamilisha huko?” “Kila kitu kipo tayari.” Mina aliposikia tu
hivyo, hapohapo akampigia simu Andy. “Nimekuamsha?”
“Hapana. Nipo njiani narudi huko.” “Mbona hata hujapumzika muda mrefu?” “Nipo
sawa. Nitapumzika mkitoka hospitalini. Na kabla hujauliza, nimekuta Ayan
amelala. Dada yake aliniambia ndio amerudi kulala tena wakati naingia, sikutaka
kumuamsha.” “Afadhali. Naona na sisi tumeruhusiwa.”
“Basi
nisubiri nakuja.” “Asante Andy.” “Acha kushukuru kama nakusaidia
bwana!” “Hapana. Nashukuru kuacha mambo yako na kuwa na sisi huku!”
“Ni wajibu wangu. Najua unaweza ukadhania sijui au nilikupuuza
Mina, lakini natambua ni wajibu wangu, nilikosea tu, au nilipitiliza.”
“Nakusubiri Andy.” Wakaagana na kutoka.
Mina Ambadilikia
Vibaya Sana Pius.
“Tunaweza kuongozana wote. Gari yangu nimeweka mpaka
kiti chake huyu.” “Mimi namsubiria Andy. Nyinyi mnaweza kutangulia tu.” Mina
akajibu na kumsogelea mtoto. “Acha nimbadilishe baba. Mkiondoka naye awe
msafi.” “Nipe mimi nguo zake nikusaidie kuvaa wakati ukila tena.” Bibi yake
akamuwahi, Pius akabaki amekunja uso.
“Kwamba hutaondoka hapa mpaka Andy aje?”
Kimya, Mina hakumjibu. “Akipata simu zake za kikazi zitakazomlazimu
kushugulikia kwanza! Inamaana sisi wote tutabaki hapa tukimsubiria
yeye?!” Mina hakumjibu.
“Nafikiri alichosema, ni YEYE atamsubiria mumewe. Mtoto huyu anaandaliwa. Akiwa tayari upo
huru kutangulia naye na bibi yake, yeye atafuata na mumewe.”
“Huyu mtoto kula yake ni kunyonya kutoka kwa mama yake tu baba! Akichelewa
sababu ya kumsubiria mtu ambaye hana uhakika…” “Huyo mtu asiye na
uhakika ni mume WANGU, na
ndiye atakayekuwa akimlea Ayvin. Itakusaidia kama utalielewa hilo
kwa haraka, Pius. Acha dharau za kijinga.” Alishituka Pius, wote hawakutegemea.
Mina alizungumza kwa jazba na hasira kali. Wote kimya.
Pius aliondoka bila ya kuongeza neno. Pakazuka ukimya
hapo, kila mmoja akageuka kuwa bubu. Mpaka Andy alipoingia. Wala hakuchelewa.
Walipishana na Pius kama dakika nne tu hivi.
Mwenye Mke.
Mina akasimama na kumsogelea. “Vipi?” “Sisi tupo
tayari.” “Naona na Ayvin ameshapendeza!” “Hapo ni rafiki wa kila mtu, ameshiba.”
“Na ni mchekaji huyo!” Bibi yake akaongeza. “Ukikaa naye huyu, kama una pressure hata ya uzee inapona.” Ruhinda akafanya wacheke. Andy
akamsogelea pale alipokuwa ameshikwa na baba yake.
“Baba hii damu ni yako, haina ubishi, lakini safari
hii Mina amekupokonya kidogo.” “Karangi kidogo kamenigomea.
Utajua ni mtoto wa Mina. Lakini mpaka viganja nilivyowarithisha nyinyi
wote na yeye amechukua.” “Ruhinda! Unakazi ya kumwangalia humalizi!” “Kwa
sababu mwenyewe amechangamka. Anataka kushika miwani yangu.” “Na pia anaonekana
yeye anamwili si kama kina Ruhinda wangu, wakavu! Unanyonyesha mpaka mgongo unauma, lakini watoto wamekaukiana, utafikiri wamekosa lishe! Utajua wanakua kwa
kurefuka tu!” Mama Ruhinda akalalamika.
“Mama wewe ulinyonyesha kwa muda gani?” “Mimi
vilinishinda sio kama wewe hivyo. Kazi na hao! Sikuweza. Mapema sana
niliwachanganyia na maziwa mengine. Kunyonyesha nikiwa nao na maziwa ya chupa
nilipokuwa nakuwa kazini. Kujibu swali lako, niliendelea kunyonyesha nafikiri
mpaka miezi 8 hivi. Paul ndiye alinyonya nafikiri mpaka miaka miwili, baba yake
akanikataza akasema atakuwa mjinga.” Wakacheka.
“Alikuwa akimfuata mama yake mpaka chooni bwana!
Nikajua ataharibika.” “Ila Paul mpaka leo yupo karibu na wewe
mama.” “Na hata asiponiona, lazima atanipigia kila siku. Tofauti yake na Pius yeye ni anione.
Nikiwa nchini, na nipo Dar, na yeye yupo hapa, atanifuata hata kazini
mchana, anisalimie hata kwa dakika. Na hata nikiwa nje ya nchi, lazima
kila siku anisikie.” “Na hao ndio waliobahatika kuwa karibu na wewe.
Mimi mlinitupa mbali na nyinyi.” Andy akaongea akisikika na uchungu.
“Hatukukutupa Andy. Na hili nilishakwambia.
Ulionyesha ukaribu sana na alta. Kutumika kanisani hata
siku za katikati za juma. Ulipenda kuwa kanisani mpaka yule askofu aliniomba
kama ungeenda kwenye shule yao ukue karibu yao ujue kama upadri ndio
ulikuwa wito wako au la. Nilikuuliza, ukakubali.” “Nilikuwa mtoto baba! Na mimi ningependa kukua nyumbani kama
wengine. Lakini si kuwekwa mbali na familia kwa miaka yote! Japokuwa
naweza nikaonekana mimi ni baba mbaya, lakini siwezi
mfanyia hivyo mtoto wangu.” Wazazi hao kimya.
“Mimi nipo tayari Andy.” Mina akazungumza naye kwa upendo.
“Mtoto utampakata?” “Anaondoka na bibi yake pamoja na Pius. Ana kiti
chake cha gari. Sisi tutangulie nimuwahi Ayan.” Andy akawa kama hajaridhika.
“Huyu mtoto ananyonya tu, Mina. Halafu ametulia
hivyo sababu pengine bado anadawa za kupunguza maumivu na ameshiba. Sidhani
kama ni sawa ukimuacha hivyo tukiwa hatujui hapo njiani mpaka
nyumbani tutakutana na nini. Foleni, na mengine yanayoweza kutuzuia
barabarani tukachelewa kukutana. Ayan ni mkubwa, atavumilia kwa muda,
ukifika tutampakata huyu, aendelee kukunusa mpaka achoke.” Mina akacheka.
“Au ameacha kukunusa?” “Yupo hivyohivyo mwanao.
Tena ndio vinazidi. Akiweka chupa yake
mdomoni, akininusa ndio anasikia raha mpaka usingizi. Na hapo hataki hata dada
yake amguse mpaka alale kabisa ndio amtoe hapo, amuweke kitandani kwake.” “Mina,
mpaka leo?!” “Mpaka leo mama, na urefu wake wote ule. Yupo hivyohivyo.” “Ndio
maana asipokuona analia.” Babu yake akaongeza na kuendelea. “Hakuwa
hivyo Ayan!” “Naona anavyozidi kukua ndio anazidi kuelewa.” “Nitawafuata
kwa nyuma. Usiwe na wasiwasi. Sawa?” Andy akamwambia mkewe. Mina akakubali bila
shida.
~~~~~~~~~~~~~~
Mara Pius akaingia. “Naomba kuwa muungwana kwenye
maamuzi yako Andy. Unavyomshauri Mina, kumbuka na wewe ni baba. Hivyo
unavyo mpelekesha kwa faida yako ili tu kunikomoa, ujue unamuadhibu
malaika wa Mungu asiye na hatia. Huyu mtoto bado ananyonya na anamtegemea
mama yake. Huna kiti chake kwenye gari yako. Mimi nilikinunua hata kabla
hajafika hapa Dar, ili aweze kusafirishwa kwa usalama. Wewe sijakuona na
kiti hata cha mtoto wako mwenyewe!” Akaendelea kwa jazba.
“Leo unataka tu kumchukua mtoto wangu,
kwa usalama upi? Kama…” “Tafadhali nyamaza Pius.” Mama yake akamuwahi.
“Hapana mama. Huyu Andy anatakiwa kuambiwa mama! Hasira
zisizoisha, zitakuja kumdhuru mtu asiye na hatia. Chochote kikitokea
hapo barabarani, atamlaumu nani? Au ataishia kusema tu ‘samahani’ halafu basi!” “Jamani, mimi nitasubiria kwenye
gari. Mina, nitaarifu mkiwa mnaondoka.” “Hata kama unanidhara…” Andy hakumjibu,
akatoka na kufunga mlango kabisa.
“Umepatwa nini Pius wewe?!” Mina akamchukua mtoto wake
na pochi akawa anatoka. “Acha tukupokee mizigo mingine mama.” “Mimi nipo sawa
tu baba. Asante.” Akatoka na kuwaacha hapo ndani.
Upande Wa Pili
Kesho yake siku
ya jumamosi ambayo hafanyi kazi, na yeye akataka kwenda kuona anakocheza Shema.
Dereva akawachukua wote na kutoka nao mpaka kwenye kituo wanachofanyia mazoezi.
Wakati wanashushwa, na Mill naye akawa anashushwa na mrembo yuleyule aliyemuona
naye jana kule ofisini. Bwana Mill alikuwa amependeza ki weekend! Msafi
halafu amejipangilia juu mpaka chini.
Mrembo akaondoka
bila hata kuwasalimia, Mill akawasogelea. Akamsalimia Pam na kumgeukia mwanae.
“Leo uliniambia huji baba!” “Nimepata muda kidogo, nikaona nije hata kwa huo
muda mfupi tu. Nikuone mwanzoni japo nitawahi kutoka. Umekula vizuri
lakini?” “Nilikula na nina maji ya kunywa.” “Nenda, usichelewe.” Mtoto mwenyewe
kama baba yake na anavyojua kumvalisha vizuri! Ungependa
kumuangalia. Akamuaga mama yake na kukimbilia kwa wenzie.
“Samahani
nilikuja bila kuuliza kama ni sawa.” Mill akamgeukia kama ambaye hakuwa na
habari naye. “Hamna tatizo kabisa.” Mapigo ya moyo ya Pam yakaanza kwenda kasi
vile tu alivyo mtizama. “Kuna sehemu nzuri tu ya kukaa. Kuna kivuli.
Twende nikuonyeshe ili ukija siku nyingine ujue pakukaa.” Akamfuata nyuma
kimyakimya mpaka wakafika. Wakakaa. Ni kwenye ngazi tu ila wanawaona wanavyo
cheza.
“Shema anapendeka
kirahisi! Na hapa napo ameshatengeneza marafiki. Na kocha wake naye
anamsifia sana.” “Ameniambia anapafurahia.” Pam akajibu taratibu na
kutulia. Akapotea kabisa mawazoni wala asijue kama mpira umeanza. Akamsikia
Mill akishangilia na wazazi wengine ndipo akarudisha mawazo hapo. Shema alijaliwa
kipaji. Alijua kucheza mpira wa miguu na aliupenda.
Mpira ukaendelea
mpaka muda wa mapumziko. Shema na timu yake wakaingia sehemu, wakiongozwa na
kocha wao. Mill akamgeukia akamkuta ameinama kama anawaza kitu. Akamwangalia
akawa kama anataka kumuuliza kitu, akasita. Pam akamtizama akakuta
akimwangalia. “Umemuona Shema lakini?” “Nimemuona.” “Kweli au ulikuwa ukiwaza
yako? Mwanangu mpira anaujua kwelikweli!” Pam akacheka vile
alivyozungumza kishabiki.
“Najua nilikushukuru
kwa kazi. Lakini ninaanza kutafuta sehemu nyingine ya kuishi. Naona kwa muda
anao lala huyu, ni mdogo kwa sababu tunapoishi na shuleni kwao ni mbali.
Nikisogea maeneo ya kule Kinondoni nilipokuwa nikiishi zamani, itapunguza
safari zake za asubuhi na jioni.” “Na mashoga zako wale uliokuwa hutaki
kuwaacha?” Akamuuliza kama kwa kumsuta. Pam akainama bila ya kumjibu. Bwana Pam
huyu ni mpole!
“Eti Pam?
Huogopi tena kuwapoteza?” “Shema ndio wa kudumu. Wengine wanakuja
na kupita. Sitaki yeye ndio aendelee kulipa garama ya hofu yangu ya kesho.”
Mill akamtizama, na kunyamaza. Hakuongeza neno mpaka Pam akaumia. Maana
alitegemea pengine angekaribishwa tena kwake au kumwambia angemsaidia
kutafuta pakuishi, lakini hakuongeza. Akanyamaza tu.
Waliporudi kina
Shema kucheza tena, karibu na mwisho simu ya Mill ikaanza kuita. Akapokea na
kusikika kwa mbali sauti ya kike. “Nashukuru. Nakuja sasahivi, hata
wenyewe wanamalizia.” Akarudisha simu mfukoni. Kisha akaitoa tena
kama aliyekumbuka kitu. Akamuona anampiga picha kadhaa mwanae. Akamuga. “Jioni
njema.” “Asante na wewe.” Akasimama.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakati anaondoka
hapo, BILA kutarajia Pam akajikuta anasimama na kumuita. Mill akageuka. Akamkimbilia.
Akawa ametulia akimwangalia. “Nilikwenda kupima UKIMWI.” Mill akabaki
akimtizama kama ambaye HAKUTEGEMEA hilo!
Midomo ikaanza kutetemeka na mikono ikitoa jasho.
“Hiyo ni mara ya
kwanza. Nilirudi tena kama majuma mawili yamepita, kupima tena. Majibu
yote ninayo hapa kwenye pochi. Sijaathirika.” Mill akabaki
akimtizama. Pam akajihisi amefanya KITUKO.
Hata yeye
alifanya bila kupanga wala kufikiria. Pengine wivu! Au kummiss
Mill! Au kuona ameshachezea shilingi chooni! Akabaki ameinama. Alipoona
hakuna jibu, akamwangalia akakuta na yeye ametulia tu, akaondoka kurudi
walipokuwa wamekaa. Mill na yeye akaondoka zake bila ya kujibu.
~~~~~~~~~~~~~~
Pam alijisikia vibaya,
na kujuta kwa alichokifanya. Akajihisi kujidhalilisha
mpaka MWISHO. Alirudi kukaa
pale akiwa amepoa, mpaka mwanae anamaliza kucheza akamkuta amepoa. “Baba
ameniambia aliondoka. Amenitumia picha nilizokuwa na cheza na video zake.”
Shema akawa akimwambia mama yake wakielekea garini macho kwenye simu akiangalia
video alizotumiwa vile alivyokuwa akicheza. Akajua kumbe alishawasiliana
na mwanae. Pam akatulia hapo garini kimya mpaka waliposhushwa nyumbani.
Jumatatu.
Jumatatu kazini
kama kawaida. Alipoona Mill hamfuatilizi tena, akili akahamisha kazini
akijua ameshakosa la mapenzi, aendelee na yake. Maana hapo kazini
bado hakuwa amemtambulisha kama ni mzazi
mwenzie. Alimchukulia kama mfanyazi wa kawaida kabisa tena hata hakuwa
akimfuata kuzungumzia lolote juu ya Shema. Na ikitokea kama wanakutana
mapokezi, inakuwa salamu tu. Hakuzungumzia tena maswala yale ya
kupima kwake UKWIMWI, hata kwa ujumbe! Pam akaona amuache kabisa.
Juma la pili
likaisha hata hakupishana naye popote japo ofisi si kubwa. Hakurudi tena
mpirani. Juma la tatu akiwa tena mapokezi anatoka siku hiyo ya ijumaa, akamuona
yule mrembo akiingia ofisini kwa Mill. Akajua amemfuata tena, wakafunge juma
pamoja.
Usafiri
ulipokuja, akaondoka kwenda benki moyo ukimuuma. Lakini angalau alishaanza kuzoea chakufanya hapo
kazini na kufahamiana na watu wa benki. Akawa mwepesi kwenye kazi zake. Akawa
wa kuaminiwa na mapesa mengi tu. Naye anafanya bila shida.
~~~~~~~~~~~~~~
Akiwa anarudi
kutoka benki, Fatma mrembo wa mapokezi akamwambia bosi amemuita ofisini kwake
mara atakaporudi tu. Mapigo ya moyo yakaanza kwenda kasi. Akarudisha karatasi
ofisini na kwenda moja kwa moja. Akagonga, akamsikia akimkaribisha.
“Vipi kazi?”
“Naendelea vizuri.” Akajibu kwa kifupi ila akamuona kama anawasiwasi. “Karibu
ukae.” Akakaa kama mtoto wa shule ya msingi mbele ya meza ya mwalimu mkuu!
Akajiweka sawa mpaka akatulia, Mill akimsubiria. Alipomuona ametulia ndipo
akaanza.
“Ulifanikiwa
kupata sehemu nyingine yakuhamia na mtoto?” “Nimeambiwa kuna sehemu mbili.
Kesho ndio nataka nikapaone mara dereva atakapokuja kumchukua Shema.” “Ni
wapi?” “Mmmh!” Akafikiria kidogo. “Au ni siri hamtaki mimi nijue?”
Akajua anaamisha na Mgaya.
“Sipo tena na
Mgaya, Mill! Nilishamalizana naye! Sema nafikiria. Maana sehemu ya
kwanza, ni Kinondoni, ila Makaburini. Mwenye nyumba anataka pesa kubwa, ndio nasita.
Sehemu ya pili ni Mwananyamala karibu na hospitali. Kidogo hapo sio bei mbaya.
Lakini nitakwenda kupaona ndio nifanye maamuzi mazuri.” “Kama ukipenda sehemu
moja wapo, ungependa kuhamia lini?” “Haraka iwezekanavyo. Sina sababu ya
kuendelea kuishi kule huku mwanangu anahangaika na foleni.” Akamuona
kama anayefikiria kidogo.
“Nenda kaangalie
chaguzi zako zote mbili. Kisha uje upaangalie na kwangu. Palinganishe
na hizo sehemu zako kisha fanya maamuzi.” Pam akabakia akifikiria
hajui kama ndio habari njema au la. Maana alisema akiwekana sawa na huyo
mwanamke, ndio atawakaribisha kwake. Inamaana ukaribisho huo ni kama hana
chake tena kwa mazazi mwenzie. Akapotelea mawazoni hapo mbele ya Mill.
“Au kwangu umeshapasusa?”
Akanyanyua kichwa na kumtizama. “Hapana. Ila mara ya mwisho kwako ni kama
kulionekana pana ugumu. Sitaki kukuingilia Mill. Hapa
ulipotufikisha na Shema, tunaweza ishi popote, na pazuri bila
kuingilia maisha yako.” “Hapana. Nilipo sasahivi ni pazuri ndio maana
nina wakaribisha. Kama utapenda na ukaona panawafaa, karibuni.” “Sawa.”
Akajibu na kusimama. Kisha akakumbuka ni bosi wake. Akarudi kukaa kwa haraka.
“Mimi nimeshamaliza.” Ndio akasimama.
“Halafu unajua
kuna sehemu ya kula hapahapa? Huwa na mimi wakati mwingine huwa nakwenda kula huko.
Wanavyakula vizuri.” “Nimesikia.” Akajibu tu hivyo, nakuondoka akiwaza.
~~~~~~~~~~~~~~
“Siwezi ishi
nyumba ndogo nikijua nyumba kubwa Mill anaishi na mwanamke mwingine. Waje wazae
na kuanzisha familia, mimi nipo hapo kama wegazi!” Akawaza Pam siku nzima mpaka kwake. Mwishoe akaajiambia anayo shida,
lakini kwa Mill HAPANA.
~~~~~~~~~~~~~~
Kesho yake
akashangaa dereva anamaagizo ya kumshusha mtoto mpirani kisha kumzungusha na
yeye kwenye kusaka nyumba. Hilo akalifurahia wala hakujivunga.
Wakatoka na
mwanae na kumshusha mpirani. Akazunguka kwenye hizo nyumba mbili, akaishia
kupenda ya Kinondoni Makaburini. Ilikuwa ni kinyumba kidogo cha uwani
kinajitegemea na kigeti kidogo cha kutumia wao japo imeunganishwa ndani ya ukuta
mkubwa, ambao mbele kuna geti kubwa la kuingilia magari. Na yenyewe ipo ndani
ya huo uzio. Vyumba viwili sebule na jiko.
Akaadhimia kuhamia hapo. Akazungumza na mwenye nyumba, wakakubaliana alipe kodi ya
miezi sita kwanza, wakaandikishiana mkataba. Pam akapachangamkia. Pesa
ya mwanae ipo, akalipa bila ya kuchelewa. Akakabidhiwa funguo, moyo ukatulia.
~~~~~~~~~~~~~~
Ndipo akarudi
garini. “Ameniambia baada ya kumchukua mtoto, niwapeleke na kwake mkaangalie.”
“Naona huko hatutakwenda. Hapa nimepapenda. Kwanza karibu na barabarani.
Rahisi kufika kazini. Patatutosha tu.” Wakaenda kumchukua mtoto, njiani
akamtumia ujumbe.
‘Mill, nashukuru kwa kutukaribisha
kwako. Lakini naona nimeshapata pakutufaa mimi na Shema. Tutahamia Kinondoni.
Nikishapaweka sawa, tutakukaribisha na wewe upafahamu anapoishi mwanao. Jioni
njema.’ Mill alipopata huo ujumbe, HAKUTEGEMEA.
Ilikuwa kama kibao
cha usoni. Alijua Pam angekimbilia kwake. Na yeye hiyo siku
IKAHARIBIKA kabisa. Akashindwa hata kujibu ujumbe, Pam yeye akajua yupo na
mwanamke wake. Akajituliza.
~~~~~~~~~~~~~~
Alipofika tu
kwake mwanae akataka kwenda kuonyesha wenzie huko mtaani picha na video
alizochukuliwa na baba yake akicheza mpira. “Sasa sio uchelewe kurudi Shema.
Unakumbuka baba yako amekukataza kuzurula usiku.” “Sikai sana mama!
Naenda tu kuwasalimia.” “Na ulikumbuke hilo unapoona mpira, na wenzio wakicheza.
Nikikufuata huko!” “Hata kama nacheza ni kidogo tu.” “Basi hakuna kwenda.”
“Kidogo tu mama! Sasa unataka nikudanganye kuwa sichezi halafu
nicheze kwa sirisiri!” Pam akamtizama asimmalize.
“Mimi sitaki
kukudanganya mama yangu mzuri mzuri.” Akaanza kumlaghai mama yake.
“Huchoki Shema mwanangu wewe! Siku nzima ulikuwa mpirani!” “Nataka niwe nao
kidogo tu, halafu narudi. Nikichelewa wewe usikasirike, nifuate kwa
amani kabisa, halafu tunarudi wote nakusimulia stori.” “Shema!” “Mimi mtoto
mzuri mama!” Akampooza mama yake kwa maneno mazuri mpaka Pam akalainika,
akamruhusu.
~~~~~~~~~~~~~~
Akaona aende
ndani akazungumze na mwenye nyuma. Akamkuta na mkewe, “Kwema mama Shema?”
“Kwema. Nimekuja kuwaaga. Nahama.” Wakashituka. “Mbona bila notice!
Si unavunja mkataba?” “Haiwezekani!” Jazba ikawapanda. Pam akawatuliza. “Wala msijali.
Nawalipa miezi iliyobakia ya mkataba wangu, na ndio hapa natoa na
notice. Si sawa?” Pesa ipo na kodi ya
hapo haikuwa kubwa, hata hakutetemeka. Walishajua baba Shema anayo pesa. Jeuri.
“Kesho nikirudisha
funguo, tutamalizana kabisa. Nawashukuru kwa kufanyika familia kwangu na
Shema.” Hawakutegemea. Akajishusha japokuwa alijua walishaanza kumsema.
Wivu. Lakini hakusita kutoa shukurani zake. “Kuna kipindi mlifanyika
ndugu niliowahitaji. Mkawa wazazi hata kwa Shema. Asanteni sana.”
Akashukuru na kuondoka akiwa amewafunga midomo kabisa. Walitegemea aondoke kwa
jeuri, lakini ndio akawa amejishusha hivyo.
Kutingishiana
Viberiti.
Alipoingia tu
ndani kwake, akaanza kufungasha. Hakuwa na vitu vingi na hakutaka kubeba hivyo
vitu vya ndani kwake. Kwanza vilishakuwa vya zamani karibu umri wa mwanae!
Kisha anakohamia maji yanatoka mpaka bafuni. Sio yakuoga kwa ndoo. Vikorokoro
vingi akakusudia kuviacha.
Nyingi zilikuwa
nguo zake na mwanae. Akajikuta amepotelea mawazoni. Amekaa kwenye kiti. Muda
unazidi kwenda, hana habari. Mara akasikia sauti ya Mill akisalimia nje! Pam alishituka
mpaka akafa ganzi. Hakika hakutegemea kumsikia tena hapo mtaani kwao.
“Yupo ndani, muda tu.” Akamsikia akiambiwa na mama Batuli.
Akagonga mara
moja na kuingia. Akamkuta Pam amekaa ameshikilia nguo. “Mzima!? Mbona
umenyong’onyea?” “Mzima tu. Nikupokee?” “Nitaweka tu hapa. Ni nguo za Shema,
safi.” Pam akashangaa. Maana hizo nguo huletwa jumapili na dereva zikiwa
zimefuliwa. Huzichukua siku za jumamosi
anapomrudisha mazoezini. Pam huzikusanya za juma zima, zinakwenda kufuliwa
kwenye mashine huko kwa baba yake ili tu kumpunguzia kazi Pam. Ila akashangaa
yeye ndio amezileta.
“Sikuzitegemea
leo! Maana amezichukua le,..” Akaona anaanza kuongea sana kwa kubabaika
na haina maana tena. “Nashukuru.” “Karibu.” Akakaa. “Hongera kwa kupata sehemu
nzuri. Nimeambiwa ni pazuri.” “Nashukuru.” Pam akabaki ameinama akifikiria
baada ya kumjibu.
“Unampango wa
kuhama saa ngapi?” “Sina vitu vingi. Kuna kaka yangu hapo mbele, gengeni,
nimempa vitu karibu vyote vya humu ndani. Atakuja kuvichukua kwenye saa
nne. Nikimaliza kusafisha, ndio tutaondoka.” “Sasa mtakwenda kuishi vipi kule
bila vitu?” “Nitaanza chumba cha Shema kwanza. Kikikamilika ndio vingine
nitanunua taratibu. Hivi vya hapa vimechoka, siwezi kuhamisha hapa. Ni
vya miaka mingi sana.” Mill akaanza kuangaza macho.
“Na kweli hakuna
chakubeba hapa.” Akaafikiana naye. “Kesho anaweza kulala kwangu. Chumba chake
kipo tayari kabisa na anakipenda.” “Ameniambia. Na kunionyesha picha
zake mpaka kitanda. Ila sitaki akuingilie. Mpaka kesho jioni nitakuwa
nimekamilisha chumba chake. Kuna mahali nitakwenda kuchukua kila kitu. Nilipita
jana. Nikachagua vitu vyake, nimewaambia nitakwenda kuvibeba kesho mchana.”
Mill akamwangalia na kutulia.
“Kesho ni birthday
yake Shema. Huwa unafanya nini?” Pam ndio akakumbuka. “Sina nifanyalo Mill.”
“Kwamba hata keki hukati!?” “Kwanza huwa hata sikumbuki! Ndio kama hivi
wewe unanikumbusha. Sina utamaduni huo. Yeye mwenyewe kwanza hata hajui
kama kuna kitu anatakiwa kufanyiwa. Sijawahi mfanyia chochote.” Mill
akafikiria.
“Ni sawa kabla
hamjaondoka nikamletea keki na vinywaji akala na wenzie?” “Atafurahi sana. Tena
itakuwa njia nzuri ya kuwaaga.” “Kwanza yuko wapi?” Pam akababaika.
“Usiniambie umemuacha kwenda kucheza tena, usiku huu, Pam!” “Amenibembeleza,
akisema anaenda kuonyesha wenzie picha na video ulizomtumia. Ila
nakwenda kumfuata.” “Giza limeshaingia! Si sawa Pam! Na hili nilikuomba
maalumu. Asiwe nje mpaka giza limkute huko!” “Samahani.” Pam akasimama.
“Wewe endelea
tu. Acha mimi nimfuate.” “Utajuaje sasa alipo?” “Nime pin simu yake. Ni
rahisi kumfuatilia.” Akasimama. Pam akamuwahi akijua amekasirika. Kila akija
hapo anakutana na kitu asichopenda. Akaona ajishushe. “Samahani Mill.
Niliona aagane na wenzie.” Akatilisha huruma. Mill akamwangalia akitoa macho
kwenye simu akitaka kujua mwanae alipo kupitia simu yake aliyounganisha
na yake. “Usijali. Acha nimfuate. Nitarudi naye muda si mrefu.” Akatoka
akimfutilia kwenye simu.
~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya muda
akamsikia akiongea huko nje kama anayemsimulia baba yake kitu kutokana na mechi
ya siku hiyo. Amechangamka kwelikweli wakiingia. “Sasa hapo usikae Shema.
Pitiliza kuoga.” “Hata nisile kwanza?!” Akamuuliza baba yake. “Hapana Shema.
Unanuka jasho na umejaa michanga.” Akaanza kucheka huku akivua nguo hapohapo
mbele yao, Mill akashangaa sana. Pam akamuona anavyoshangaa.
Akaenda
kumuwekea maji bafuni akamuita kwenda kuoga. Akaondoka hapo na taulo kafunga
kiunoni. “Pam! Hivi huyu Shema hajui kama ameshakuwa mkubwa!?” Pam akaanza
kucheka. “Anavua nguo mbele yako, hana hata wasiwasi?!” “Wala hana wazo la
pili! Nakwambia akili yake ni ya kitoto, ni huo urefu tu.” Mill akatingisha
kichwa kwa masikitiko. “Huyu kweli anahitaji chumba chake aisee.” Baba yake
akaafiki.
“Kesho nitakuja
mapema. Nitaleta hiyo keki, vyakula kidogo na vinywaji. Tukimaliza nitawasaidia
kuhama.” “Nashukuru Mill, asante.” Aliporudi mwanae, akamuaga na kumwambia
mipango ya kesho yake. Akafurahi huyo!
“Nitaenda kuita
rafiki zangu wote. Nitawaambia wakija ndio tunakula pamoja halafu tunaagana
nao.” Akaweka mipango hapo akifurahia, Mill akashangaa vile alivyo mtoto
mrahisi. Wala hakulalamika kuhama na kuacha rafiki zake. Yeye chochote
anachoambiwa anakubali tu. Akaaga. “Naomba tuzungumze kidogo hapo nje,
Mill.” “Bila shaka.” Wakatoka.
“Niliambiwa
mlinunua chakula kabla hamjarudi nyumbani!” “Alishakula huyu, ila najua atataka
kula tena. Nitampikia kabla hajalala, hawezi kulala bila kula tena.” Wakatoka
mpaka nje.
~~~~~~~~~~~~~~
Mill akamgeukia
aliporidhika wapo peke yao. Pam akaanza kutetemeka kidogo. Mill si mzazi
mwenzie tu, ni bosi wake pia. “Ni nini?” “Nilipopenda kile chumba na kuona
wengi wanakihitaji, nilifanya maamuzi ya haraka bila kukushirikisha.
Nimetumia pesa ya kwenye akaunti ya Shema.” Mill akabaki akimwangalia. Pam
akameza mate. “Ila nakuahidi nitairudishia taratibu kila nikilipwa
mshahara.” “Hiyo ndio ilikuwa kazi ya hiyo pesa, Pam. Ikusaidie kumlea
Shema kwenye mazingira mazuri.”
“Kwanza
nakupongeza kwa kuchukua hatua ngumu uliyokuwa ukisita kufanya. Najua
pengine unaacha maisha ya kueleweka na watu wako kwa sasa,
sababu ya Shema. Katika hilo nakushukuru. Ila nimeshangaa kwa nini
hujakupa na kwangu nafasi hata kupaangalia! Ni sehemu nzuri ambayo
ungeishi bila garama, na ni karibu na shuleni kwa kina Shema. Asingesumbuka
na foleni na ungetunza pesa yako.” Pam hakumjibu. Akanyamaza.
“Labda nikuulize
ni kwa nini?” “Nilifikiria Mill. Nataka mazingira ya kudumu na ya
kueleweka kwa Shema. Najua nakwenda kupanga. Lakini kwa yale mazingira
na kwa jinsi mwenye nyumba alivyo, nahisi patakuwa ni nyumbani kwa
kudumu kwa Shema kama hapa palivyofanyika. Sio leo yupo kwako, kesho ikitokea havijafaa
na mwanamke huyu, ukianza na mwengine inamlazimu kujitenga na kwako
mpaka kieleweke na mwanamke mpya. Hivyo naona si sawa kwa
Shema, Mill.” Mill aliishiwa nguvu, akabaki kama amepigwa shoti ya umeme.
Hakutegemea kama Pam angechukulia hivyo. Nia ilikuwa ni kumrusha tu
roho.
“Najua naweza nisifikie
viwango vya wanawake zako, na kumkuta Mgaya siku ile kulikupa picha
mbaya. Lakini Mill, Shema ni mwanangu na ni kila kitu changu.
Katika kila jambo ni yeye KWANZA ndio wengine. Isingekuwa Shema, ungekuta pengine nilishaolewa.
Lakini kwangu hakuna mwanadamu anakuja KABLA ya Shema. Na hata Mgaya siku ile ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kufika
ndani kwangu ninapoishi na Shema. Kwanza nilishajua hajampokea mwanangu.
Nilishajua moyoni hawezi kuwa mume, kwa hiyo sikutaka kumsogeza sehemu pekee
ambayo kwa Shema ndio nyumbani na kila kitu chake.”
“Nilipo mimi,
ni Shema KWANZA hata kama patanigarimu mimi. Kwa hiyo hata kama sehemu inasikika
ni nzuri na ingenisaidia mimi, ni bora nifanye kazi kwa bidii, nimpatie
mwanangu sehemu yenye uhakika. Sio kubabaisha.” “Kwangu sio pakubabaisha
Pam!” “Lakini WANAWAKE zako ndio wanatangulia
kabla ya mwanangu Mill! Hilo HAPANA kwakweli. Nina shida, sikatai,
lakini linapofika swala la mwanangu, tena akiwa na UHITAJI, SIWEZI nikampa mtu mwingine kipaumbele.”
“Na mimi nampa
Shema kipaumbele.” “Mimi sijui kwa upande wako Mill. Siwezi kukusemea.
Ila najua nilikutafuta nikikuomba pakuishi mimi na mtoto. Hapa
mazingira yamenibadilikia si kama zamani. Wivu kwa majirani umeongezeka.
Maneno na lawama kwamba nina roho mbaya, nimeshindwa kumpatia
kazi ya udereva baba Batuli.” Ndio Mill akakumbuka.
“Aaahh! Aisee
nimesahau kabisa.” “Imekua mbaya sana. Yule mama anashindwa hata
kuzungumza na mimi! Undugu wote umeisha kabisa. Maneno machungu.”
“Samahani Pam. Sikukusudia kukuharibia na hapa. Nilisahau kabisa maswala
ya udereva wa yule baba. Kwa nini hukunikumbusha?” “Tuliacha kuzungumza kabisa
Mill! Na wewe ukawa ukinisaidia mwanangu, kweli ningeanza na matatizo
ya majirani pia?” Mill akatulia.
“Pakuishi
kwenyewe ulinikatalia!” “Sikukukatalia Pam! Nilikuomba usubiri kidogo na
nilikupa sababu.” “Nilikuelewa, na mimi ndio maana nakupa sababu ya kutokaa
kwenye mazingira YASIYO na UHAKIKA kwa Shema. Sitaki mwanangu ayumbishwe.
Leo yupo hapa, kesho kule, hakuna sababu yakumfanyia hivyo. Kwanza SITAKI
kufanya hivyo. Lazima mmoja wetu alipe garama kwa ajili yake. Mimi nimejitolea
Mill. Na usifikiri nakulaumu! Nakushukuru sana. Ila siwezi kukuacha
ulipe garama zote peke yako. Unafanya vyakutosha. Acha mambo mengine
nikusaidie.” Mill alipoa huyo! Hakutegemea.
Pam alimng’ata
na kumpuliza kwa heshima tu bila ugomvi. “Naomba nikuombe jambo moja tu.
Ila sina nia ya kukukwaza.” Mill akarudisha macho kwake maana alipotelea
mawazoni akiangalia pembeni. “Hapa mtaani nimeshaingia doa.
Maneno yanayoendelea ni ULIACHA kuonekana hapa sababu ya kunifumania na
Mgaya. Najua kwako umeshaweka vizuri, upo tayari kumtambulisha au
kumsogeza Shema kwa Brenda.” Mill hakutegemea. Hakujua hata kama
anamjua. Mill akashangaa sana.
“Niliambiwa jina
lake na Fatma.” Mill hakujibu. “Nakuomba sana. Nakusihi. Kesho usije ukaja
naye hapa.” Mill akashituka. “Mnaweza kumchukua mkasherehekea
naye sehemu nyingine, lakini HAPA, naomba nitunzie heshima
yangu.” “Unawezaje kufikiria hivyo Pam?!” “Lisingekuwa jambo baya, maana najua
hata mpirani kwa Shema umeanza kuingia naye, lakini hapa, nimeshaharibu
Mill. Acha niondoke na heshima ndogo niliyobakia nayo.”
“Mpirani kwa
Shema aliingia na kukaa, lakini hata Shema hakukutana naye! Kabla
ya mpira kuisha na Shema kutoka nilimuomba aende kunisubiria
kwenye gari! Huyo anayekupa habari zangu, hakupi kamili!” “Sitaki
kukuudhi Mill. Ni ombi tu. Naomba usije na Brenda hapa. Ni hilo
tu. Usiku mwema.” Akasubiria kidogo, nakuondoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Inaendelea….
0 Comments:
Post a Comment