Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 49. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 49.

Mina akaona hakuna kumaliza. Akasimama na kuchukua chakula alicholetewa na Andy, akarudi kukaa karibu na mumewe, na kuanza kufungua. “Umekula na wewe?” Akamuuliza mumewe kwa kujali. “Wewe kunywa tu hiyo supu kwanza. Nitaenda kununua nyama choma, tuje tule wote.” Mina akacheka. “Nini sasa?” Andy akamuuliza. “Mwenzio nilikuwa nakula kiuzazi. Yule anti, mama mwenye nyumba niliyekuwa nimepanga kwake, hakuwa akitaka kabisa nile vitu kama hivyo. Anasema vitamuumiza mtoto tumbo. Sijala nyama choma muda mrefu, naona umri wake Ayvin. Nina hamu nayo kweli! Bora ulete tu, tule wote.”

“Sasa kama uliambiwa vitamuumiza mtoto tumbo, kwa nini unakula Mina, wakati mtoto anakutegemea wewe tu?” Pius akaingilia. Mina akamwangalia maana walikuwa wakizungumza wao wawili. “Tafadhali jikaze umalize. Zaidi kipindi hiki mgonjwa. Hutataka akiwa na vidonda hivi, halafu  aanze tena na maumivu ya tumbo! Tafadhali Mina. Na kama navuka mipaka hata kwako Andy, naomba mnisamehe. Utakuja kula hizo nyama, mpaka uchoke. Vumilia tu umsogeze.” Hakuna aliyeingilia.

“Basi wakati nyinyi bado mpo, acha mimi nikaoge, nibadili nguo. Nikila nitakuja kulala hapa na Mina, maana Pius hatalala hapa na mke wangu.” Andy akasimama kabisa. “Tafadhali baba, usiondeke kabla sijarudi.” “Sawa.” “Sasa wewe unahisi ni nini kitatokea nikibaki hapa na Mina?” Andy hakumjibu. Akamgeukia mkewe. “Ice cream si sawa?” “Hayo ni maziwa tu. Mletee na yeye ajipongeze.” Mina akacheka aliposema hivyo mama Ruhinda.

“Asante mama yangu. Lakini si umeelewa sababu yangu ya kutokuja nyumbani? Mimi sitaki nikuudhi mama.” “Sana tu. Tena naona unahekima kuliko wote hawa. Ila nakusihi Mina, usiondoke tena mama. Wajukuu watamu mama! Najua mazingira ya hapa si mazuri,`lakini naomba tutafute jinsi yakufanya muishi hapa na sisi.”

“Binafsi nikuombe radhi Mina. Kucheka kule kiukweli sikuwa nikikucheka wewe wala bro, hapa.” “Ulikuwa ukimcheka nani?” Paulina akauliza kwa haraka. “Nikisema ndio mtakasirika kabisa, bora ninyamaze tu. Na Paulina acha uchochezi.” “Wote tunajua uliyekuwa ukimcheka ni mama na mkwe aliyekuwa ameletewa.” Paul akamtizama mama yake.

Ushabiki tu! Haya uliyekuwa ukinicheka ni mimi, lakini aliyeumia ni Mina. Umepata faida gani? Maana mimi nilishamuomba msamaha. Mimi na Mina hatuna tatizo. Si ndiyo Mina mwanangu?” Mina akacheka. “Mimi na wewe tushapita kwingi mama yangu, mpaka nimesahau ubaya wote kama ulikuwepo! Naona nakuamini wewe kuliko hata mama yangu mzazi.” “Andy, nenda nizungumze na Mina.” “Baba usiondoke bila mimi kurudi.” “Usiwe na wasiwasi.” Akatoka.

~~~~~~~~~~~~~~

“Mina, mtafute mama yako. Anawasiwasi sana.” “Si kwa mazingira haya anayoyaweka Pius. Mimi namjua mama yangu. Hawezi. Andy ataelewa ninacho zungumzia. Mama yangu hii fujo ni kumchanganya, kisha kunichanganya na mimi mwenyewe na kushindwa kufikiria kabisa.”

“Mama amehangaika sana na mimi. Sana, kuliko nitakavyo kwambia. Nishamfedhehesha kupita kiasi. Tokea anaachwa na baba mpaka nakaribia kuolewa na Andy, mimi nilikuwa ni mzigo mzito sana kwa mama yangu.” “Kama unalijua hilo, ndio iwe sababu ya kumtafuta ili ajue unaendelea salama.” “Siendelei salama, mama yangu. Na yeye si mjinga, sina jinsi ya kumdanganya.”

Picha ya mama baada ya yote, kwangu mimi, ilikuwa si niishie hivi hata kidogo. Kuolewa na Andy ilikuwa ni muujiza kwake, muujiza mkubwa sana. Kisha kumpata Ayan, ndio mama aliweza kurudisha sura kwa ndugu zake, akazungumza jambo kwa kujiamini. Siku nimeachwa na Andy. Amenirudisha nyumbani akimwambia mama ananiacha kwa ujauzito ambao si wake, mama hakujisumbua hata kuniuliza ilikuaje.”

“Alifanya kama Paulina huyu. Moja kwa moja akajua nimerudia tabia mbaya, asubuhi na mapema nikiwa natapika na yeye akanifukuza kwake.” “Mina!” “Hakika mama. Alinifukuza kwa maneno machungu mno. Kumbuka hapo nilikuwa nimeachwa sina pesa, na mtoto niliyekuwa nikihangaika naye nimenyang’anywa. Natapika sina hata nguvu, ila masanduku aliyonifungasha nayo Andy. Na alisema nisiache kwake hata mswaki!”

“Niliondoka pale siwezi hata kuangalia sababu ya kutokula, natapika mfululizo na siwezi kunywa hata maji! Nahisi isingekuwa Pius, ningefia kwenye ile nyumba ya kulala wageni peke yangu.” Wakamwangalia Pius.

“Alinipigia simu, hata kuzungumza nilikuwa siwezi. Akaja kunichukua, na kunibeba mpaka hospitalini ndio nikapoteza fahamu, nikaja kuzinduka nina dripu. Ndio maana hata wakati mwingine nikitaka kumchukia sana, najirudi.” “Mimi sio mtu mbaya. Sema sitaki mwanangu akue kinyonge.” “Tafuta amani Pius.” “Sawa mama, lakini sitatafuta amani wakiwa wanataka kumkandamiza mwanangu. Hapana.”

“Sasa nani atakaye mkandamiza mwanao? Kwanza ni hivyo hujakutana naye Ayvin mwenyewe. Hakandamiziki. Amejawa amani na mleta furaha kwa kila anaye mzunguka. Nilikuwa nikimfikiria Andy kwa vile alivyokuwa, nikimlinganisha na Ayan anavyoishi naye huyo. Na ukimya wake wote, ilikuwa akimka yeye kabla ya Ayvin anasononeka. Kila wakati anaenda kumchungulia ili aamke achangamshe nyumba. Sasa wewe utapokonya hiyo nafasi ya Andy na kuweka uadui kati yao, hata asimfurahie mtoto mzuri kama huyu.”

“Hiyo siyo nia yangu.” “Tafadhali baba, nisaidie kumuuliza Pius, NIA yake yeye haswa ni nini? Na anafikiria nini kwa maisha ya Ayvin sasahivi?” “Wala sio lazima baba aniulize. Nia yangu kwa mwanangu ni nzuri, na nataka mwanangu ajue mimi ni baba yake na ninampenda.”

“Wewe baba unaona kwa sasahivi huyo mtoto anahitaji kweli gari, kama si kutaka kumuharibia mazingira ya kuishi huyo mtoto anayetaka ajue anampenda?” “Na kabla hujajibu kwa haraka Pius, tafadhali fikiria haya maswali maana ni muhimu sana.” “Sitaki mtoto wangu akue kwa shida wakati mimi nina pesa! Hapana jamani.”

“Wewe unavyofikiria, huyo mtoto wako atakuja kukumbuka aina ya gari unayomnunulia sasahivi au mazingira yaliyomkuza ndio yatamfanya aje awe mtu mzuri ambaye wala hutahitaji kuwekeza mapesa kwake kama sisi tulivyofanya kwenu?” “Asante mama. Na muulize…” “Kwa nini unatuma watu wazungumze na mimi wakati tunaweza zungumza sisi wenyewe?” Pius akamuuliza kwa kulalamika.

“Kwa sababu mimi sikukujua kama upo hivyo Pius!” “Nipoje?” “Mbinafsi.” “Mina!” “Hakika tena. Wewe ni mbinafsi Pius. Unajifikiria wewe mwenyewe tu. Vile unavyotaka mambo yawe, unataka yabakie hivyo ilivyo bila kumfikiria yeyote yule hata huyo mtoto unayesema unataka aishi kitajiri kulingana na pesa yako. Humfikirii yeye. Hunifikirii mimi, wala hutaki kumuelewa Andy!” “Andy ndio ameshindwa kukubaliana na….” “Tafadhali jipe muda wa kufikiria Pius.” Mzee Ruhinda akamkatisha, Mina akaendelea.

“Jamani, Andy si mkamilifu na mimi si mkamilifu. Lakini ni mume wangu. Tupo na ndoa takatifu na tumekubaliana kuendelea mpaka kifo. Hilo ni agano aliniomba Andy kabla ya ndoa. Haamini kwenye talaka kabisa. Haamini kwenye kuachana. Yakatokea yakutokea akapata ushabiki mpaka akaandika talaka, lakini Andy alishindwa kabisa kuendelea na ile talaka.” “Haiwezekani Mina!” “Kweli mama. Alikuja nirudishia yale makaratasi vilevile. Kisheria nilibaki kuwa mkewe, japo alinirudisha nyumbani.”

“Lakini hata kabla ya kuniambia yote hayo. Akijua mimi ni mjamzito, mimba hajui ni ya nani, alikuja kule Iringa na kunichukua. Tena kwa kulazimishia kabisa akitaka niondoke naye, nikaishi naye Dodoma, mpaka mimi nikawa namshangaa! Tumbo kubwa kabisa, sijampa hata maelezo juu ya ujauzito wenyewe, maana na mimi mwenyewe nilikuwa sijui.”

Alinirudisha kwenye maisha yake na mtoto wetu, akiniachia niendeshe nyumba yake ile ya Dodoma vile nitakavyo. Na hapo bado alikuwa hajui mimba ni ya nani ila yupo tayari kuendelea vile ilivyo. Ila nafikiri ni kwakuwa alipata muda wa peke yake wa kufikiria na kuamua. Sasa wewe Pius, unataka kila kitu kiendelee kwa haraka, kwa muda wako wewe, na vile unavyotaka WEWE! Umezaa na mkewe. Huonyeshi hata kama ni ajali imepata familia nzima, zaidi yeye mwenyewe Andy. Unataka mambo yaendelee kama kawaida! Kweli jamani!?”

“Ingekuwa ni Paul au Andy amezaa na Raza, kweli Pius ungesema tu sawa, yaishe?” Kimya. “Ni ngumu jamani, tafadhalini naombeni mumuelewe Andy wangu. Ni ngumu. Na mbaya zaidi Pius amekusudia kuharibu kabisa na si kutengeneza. Naombeni wengine zaidi wazazi, mumchukulie Andy taratibu. Anajitahidi kwa kadiri ya uwezo wake.” “Sisi tunamuelewa, Mina binti yangu. Ndio maana unatuona tupo hapa.” Mzee Ruhinda akaingilia.

“Na hivi ninavyozungumza na Pius, ndivyo ninavyozungumza na Andy ila nafikiri yeye Andy amekua msikivu zaidi kuliko Pius.” “Baba!” “Ni kweli Pius. Nilichozungumza na wewe leo, ndivyo nilivyozungumza na Andy. Amefika mjini, kimya. Wote tulimkuta pale uwanja wa ndege ametulia kabisa akisubiria familia yake. Aliyemuanza mwenzie pale uwanjani ni nani kama sio wewe Pius?” “Na kweli! Na Andy alinyamaza kabisa. Hakukujibu. Umepatwa na nini Pius?” Mama yake akaingilia na kumuuliza kwa ukali. Mina hakujua kilichoendelea hapo uwanjani kabla hajafika.

“Na usifikiri nilizungumza na huyu mtoto wako kwa kifupi! Nilimueleza kabisa. Andy anaomba AMANI, ili aipate familia yake. Na alisema wazi kabisa, mazingira ya utulivu atakayoyakuta Mina, yatamfanya atulie na watoto kuliko kwenda kuishi maisha ya kimasikini.” Mina akaumia sana. “Sikukwambia hivyo Pius?” Kimya. “Nilimwambia. Tena nikamuongezea mazungumzo niliyozungumza na Andy kabla ya hapo, kuwa mdogo wake anasema alikuwa akihangaika japo alikosea jinsi ya kufikia lengo, akaishia Mina kulipa garama, lakini alitaka afike sehemu Mina na watoto wake waishi vizuri.”

“Andy anasema alikuwa halali, akihangaika kuwafurahisha mabosi wake, wamkabidhi cheo alicho nacho, akiamini atakuja kutulia na mkewe. Andy alilia kwangu akisema amekuja vipata VYOTE, lakini hana Mina, hana kijana wake. Kulikuwa na nafasi ya kurudi Dar, alisema alishindwa kurudi na kuja kuishi kwenye ile nyumba waliyojenga na Mina, sababu ya hukumu. Ameamua kubaki Dodoma. Akawa analalamika kabisa anasema anauhakika huko mkewe na mtoto wake walipo, hawaishi kama wanavyostahili, na yeye ndio anajilaumu.”

“Yote hayo nilikwambia Pius, na nikakusihi, hayahaya anayokuomba Mina. Huyu mtoto anakuwa kama anarudia maneno yangu kwa Pius. Mpe muda Andy, msaidie akae sawa na familia yake, ili Ayvin aje aishi vizuri.” “Kwani inawawia vigumu vipi kumuita mwanangu jina langu?” Walishangaa hapo, hata mama yake hakuamini. Mina akaona hawafiki popote, akapasha chakula akaendelea kula.

“Ni jina tu jamani! Kwani mnaona ugumu gani?” Mzee Ruhinda alinyamaza kabisa akajisogeza kwenye kiti, akakaa vizuri. Wakajua amemaliza. “Wewe umeamua kuvuruga hii familia Pius.” “Kwani mimi nimefanya fujo gani hapa? Kinacho washinda kumuita mwanangu jina lake ni nini?” “Huyu Pius anafikiria mtoto analelewa na pesa tu. Kwamba akitoa pesa nyingi, ndio mwanae atakua vizuri.” “Kwani kuna ubaya gani wa pesa kwenye maisha yake?!”

“Mtoe basi hapo mpeleke benki akakulie zilipo pesa zako. Pesa si muhimu? Mpeleke akalelewe benki kwenye mamilioni yako. Wamnyonyeshe huko, wamuuguze, halafu wewe uwe unaenda kumuangalia tu kama salio.” “Umekasirika Mina. Na mimi sitaki kukuudhi.” “Najua lengo lako ni kuharibu Pius. Wewe si mjinga wa kiasi hiki chakutufanya sisi WOTE, tujirudierudie na kushindwa kuelewa.”

Paul.

“Hapo naungana mkono na Mina.” Paul akaingilia. “Kabla hajarudi Andy, acha mimi niseme vile nilivyowaangalia nyinyi.” Paul akaendelea. “Utanisamehe bro, ila hii ni kutaka kuwasaidia mama na baba, wakuache kabisa. Maana kile wanachotamani kukiona kwako kinatokea, wewe umekusudia kwa makusudi kabisa, kutowapa. Na kama Mina unaacha kumtafuta mama yako mpaka mambo hapa yakae vizuri, jua unamuadhibu mama yako bure.”

“Mama anapokwambia mtafute mama yako, ni kwa ile hali tuliyomkuta nayo. Niliporudi nchini, japokuwa nasikia mama yako ni kama hakutaka kabisa familia yetu tena baada ya wewe kuondoka, lakini mama akaniomba nimsindikize angalau akamjulie hali. Tulimkuta ni kama mgonjwa. Ila kwa sababu mimi ni daktari, nilijua ni msongo wa mawazo. Mama alizungumza naye sana, mimi nikiwasikiliza. Mama yako yupo tayari kukupokea vile ulivyo na hii familia yetu.”

“Ana majuto makubwa sana. Alituelezea hatua kwa hatua na mpaka ni kwa nini wewe umekosa imani naye, yeye kama MAMA. Alitueleza vile ilivyokuwa hata siku ya harusi yenu. Alivyokufanya siku uliporudishwa. Alijilaumu kushindwa kusimama nawewe kama mama, ila hakutuambia kama alikufukuza. Alijionyesha na majuto makubwa sana. Na hajui chakufanya. Alikuwa akimwambia mama, ingekuwa si kuharibu kwake, ungekimbilia kwake. Yaani nyumbani. Lakini yeye amekuondolea mazingira ya pale kwake kama ni nyumbani kwenu na wewe. Hilo anajutia Mina. Nakushauri, pata muda fikiria na ujirudi kwa mama yako.” Paul akaendelea.

“Mimi nimezungumza sana na Andy. Msamaha niliokuomba wewe Mina, ndio nilimuomba Andy. Sikukusudia kuwacheka. Nilikuwa nikimcheka mama, na utaratibu wa pale nyumbani. Kabla mama hujakasirika, acha nimwambie ukweli Mina, maana na yeye sasahivi ni mama na anafamilia, ndipo nitakuja kuwaambia juu ya Pius. Ili wote mtulie.”

“Kila mzazi anakuwa na ndoto juu ya watoto wake. Mimi najua nimefikia ndoto za wazazi wangu isipokuwa kwenye maswala ya kuoa tu.” “Sasa kwa nini huoi na wewe kama si …” “Mama, utanitoa kwenye pointi!” “Mwache amalize. Tushajua huyu si muoji, basi.” Baba yake akataka aendelee. Paul akacheka na kuendelea.

“Wewe Mina, vile ulivyokuja kwetu, na vile wazazi walivyokuwa wametulea sisi, hawakutarajia kabisa Andy alete msichana wa namna yako! Samahani Mina. Na si kwa kukudharau, ila ni kule tulikokuzwa, mazingira yetu ambayo najua unayajua, na aina ya watu wanao tuzunguka. Haijawahi pita akilini kwa wazazi kwa kijana wao kuja kukutana na msichana ambaye hakuwa amesoma kabisa. Si kiuwezo. Hapana. Elimu na aina hiyo ya ustaarabu. Si hata na wewe mwenyewe ulisema mwanzoni kabisa, tuna ustaarabu wetu?” Mina akanyamaza.

“Ninachokwambia ni hivi, tatizo haukuwa wewe kama Mina. Tatizo ni yale malengo yao kwetu. Siku ile ulikutana na mama aliyeshitushwa tu. Ila si kwamba tulikudharau. Na mimi nilikuwa nikicheka japo nilikosea, kwamba wamepambanishwa! Wanasema mapenzi ni maua, huota popote. Huwezi mpangia mtu ampende nani. Yaliyobaki wewe unayajua na kina mama wakajifunza kwa machungu, pale walipomlazimishia Andy aende kwa mwanamke waliyefikiri anafaa. Wenyewe walishindwa.”

“Kama alivyokwambia Raza, si uliona mwenyewe baadaye jinsi walivyokufungulia mikono na kukumbatia?” Mina akacheka taratibu. “Mzee Ruhinda si wa kuahirisha safari zake eti alee mtoto!” “Hata wake wakuwazaa alikuwa hafanyi hivyo.” “Sasa hapo mama Pius unazidisha.” “Kweli baba. Kwani uadui wa Paulina na Mina ulianzia wapi kama si wivu.”

“Paul jiangalie wewe!” “Acha kunitisha, utanifanya nini? Huo ndio ukweli. Chuki yako kwa Mina hata kutaka kumtoa Mina kwenye familia ukimshawishi mumewe amuache, ukikimbilia hospitalini kumpima mimba, huku wakweze wametulia kimya ilikuwa ni kuthibitisha ubaya wake, ATOKE, akupishe kwa baba. Bisha.”

“Wewe ni mnafiki.” “Sina ninachonufaika hapa ila kuwaweka huru kwa ukweli ili kila mtu ajue moja, hivi vikao vyenu visivyoisha, na kumpandisha pressure baba, kuishe. Mtamuua mzee bure!” “Pole baba, kumbe unaumwa!?” “Uzee tu Mina binti yangu.” “Hauna uzee wowote wa kuanzwa na pressure sasahivi wakati upo na afya nzuri. Ni msongo wa mawazo. Na usipo angalia, hawa wanao wawili hawa, watakuua baba.” Akimaanisha Paulina na Pius.

“Paul jiangalie wewe!” “Paul kuwa na kiasi.” “Hapana bro. Wewe umekusudia kuharibu na ni kwa MAKUSUDI.” Paul akawa mkali kabisa.

“Baba, Pius anampenda SANA Mina.” “Kwani hilo ni siri?” “Hapana Pius, nasikia umesema hilo. Lakini ambacho baba hajui na ni ukweli ambao hata ukipinga, utabakia ukweli, shida yako ni hawa wawili WATENGANE, abakie Mina BILA Andy, wewe uendelee naye.” “HAIWEZEKANI!” Mama Ruhinda akahamaki kama aliyefunguliwa macho gafla, mzee akamtizama Pius.

“Baba, acha kunitizama hivyo! Paul amechanganyikiwa.” “Si ubishe? Wewe jiulize baba. Atakayenufaika na kuvunjika kwa ndoa ya Andy na Mina, mbali na Paulina ambaye yeye ni mchonganishi tu na wivu, ni nani kama si PIUS?” Paulina akamrushia funguo za gari mdogo wake, akakwepa.

“Tafadhali tulia Paulina. Maana ni kweli wewe ndiye uliyehangaikia karatasi za talaka za ndoa yao hao mpaka kumlazimisha Andy asaini. Na usinijibu maana unajua ni kweli.” “Asante baba. Sasa nia ya kijana wako huyu, kama alivyosema Mina, maana wote tunamjua Pius si mjinga. Wakati wote, Pius ni mleta AMANI. Kukiwa na tatizo kama mzee hayupo au hata mzee akiwepo, ataitwa kuongeza nguvu ya amani. Pius hana tatizo la kuelewa. Wote mnamjua. Hafanyi jambo kwa hasara na ndio maana amefanikiwa sana kila alipoamua kuwekeza muda wake.”

“Sio kama hata mmoja wetu hapa. Anajua kufikiria mbele. Anajua kuweka faida ya kila jambo na hasara zake, ndipo anachukua hatua kwenye kila jambo kwenye maisha yake. Na ndio siri kubwa ya mafanio yake kutuzidi sisi sote. Na najua baba anajua maana nilishamsikia akilisema hili.”

“Sasa basi, nina uhakika kabisa. Hata kabla hajapanda kitandani na kulala na Mina, alishapiga mahesabu yote haya. Akaona siku mpaka za leo. Akimjua Andy ni mtu wa uchungu mwingi. Aina ya familia yetu na atakachokifanya. Nina UHAKIKA ameshajua mpaka kesho ya leo, ndipo akalala na Mina.”

“Pius hajakurupuka jamani! Na hili nilimwambia Andy. Yeye mwenyewe Andy alifungua mlango wa kumfanya mpaka Pius ampende hivi Mina, kiasi hata chakuwa tayari kumchukua Mina kama mkewe. Bisha, bro.” “Sina muda wa kubishana na wewe.” “Si umeona baba? Pius anampenda Mina ile yakupitiliza. Na kwa mara ya kwanza, hawezi jisaidia ndio maana yupo tayari kubeba yote ili tu, ampate Mina. Yaani Andy akijichanganya tu na kumuacha huyu mtoto, ndio furaha ya Pius. ALEE mtoto wake na Mina tu. Andy asiwepo kwenye picha.”

“Umechanganyikiwa Paul?” “Kwani uongo bro? Sijui ya nyuma, yakukubali kujidhalilisha mpaka mitandaoni, wewe na nyadhifa zako, lakini kwa LEO tu. Nakuona unafanya MAKUSUDI kabisa, KUHARIBU. Kuanzia uwanja wa ndege, ulikusudia kumuharibu Andy akili ili akija mkewe, amkute AMETIBUKA. Kusudi tu. Hapa kwenyewe unahangaika, kuwatibua bila sababu.”

“Unapenda sana kuongea Paul.” “Kwa sababu unajua ni kweli. Huyo mtoto wako unajua wazi hana rikodi yeyote ile serikali wala hospitalini. Umeletewa mpaka mikononi mwako na ukweli UNAuJUA. Kinachokushinda kufanya hiki unachokitaka hapa kihalali, kisheria ni nini, UNAKAZANA kupoteza amani kwa mama ambaye unajua ananyonyesha, hajala, alikuwa akiuguza mtoto aliyekuwa akilia muda wote?” Kimya macho kwa mwanae.

Ila Paul akawa amemfungua macho kila mtu zaidi Mina. “Najua unajua bro. Ila unafanya KUSUDI tu.” “Na kweli! Maana kama shida ni jina la mtoto, si angeenda kumuandikisha jina analotaka yeye. Akatengeneza vyeti vya kuzaliwa hata vitambulisho anavyotaka yeye, kwa majina anayotaka yeye, na kuleta akisema ndio majina ya mtoto!” “Umeona baba? Sasa wewe unafikiri haya yeye Pius hajui kama si kwamba anafanya tu kusudi KUWAVURUGA hawa wawili?” Mina aliumia sana, ila aliendelea kula.

“Na mkewe?” Paulina akauliza. “Kwani Pius anashida na Raza? Raza ndiye anayeshikilia ile ndoa. Na Pius anajua wazi, Raza hawezi muacha hata akimwambia anaoa mke wa pili. Atapiga kelele na uchawi, lakini si muondokaji.” “Na bora umejiingiza kwa Yesu na kuwa muombaji, Mina mwanangu.” Mama Ruhinda akazungumza hivyo tu.

“Mimi natoka. Namrudisha Poliny chuo. Kukitokea chochote, tafadhali unijulishe Mina. Nitarudi hapa asubuhi na mapema.” Hakuna aliyemjibu Pius. Akainama kumbusu mwanae akamwangalia Mina. “Jaribu kupata muda wa kupumzika, kipindi hiki mtoto akiwa amelala. Huwezi jua akiamka atakuaje? Sawa?” “Sawa.” “Na acha mawazo ya kutaka kuondoka. Nakuahidi kila kitu kitakuwa sawa. Tulia ulee watoto kwenye mazingira yakueleweka. Kila kitu kitakuwa sawa.”

Akamgeukia Paul. “Acha kueneza sumu na kumjaza Mina ujinga. Namtegemea kulea huyu mtoto. Kama huwezi kuleta amani hapa, ondoka. Nisikuone karibu ya mtoto wangu. Umenielewa Paul?” Hapo akawa mkali kabisa. “Kama wewe una hekima sana kwenye mambo, mbona hatukuoni ukaanzisha familia na kuiongoza kwa hiyo hekima yako? Umejawa maneno maneno tu ya uchonganishi! Nani amekukaribisha hapa?” “Paul ni mmoja wa hii familia Pius. Acha kumkaripia.” “Hapana mama. Anachotaka ni kuchonganisha si kuleta amani.” “Unataka yeye alete amani wakati wewe ndio unaharibu?” Mama yake akamjia juu.

“Leta amani hapa uone kama kuna atakaye haribu.” “Naomba Paul, aondoke mama.” Paul akaanza kucheka. “Ukimfukuza Paul ujue umenifukuza na mimi.” “Mama?!” “Unafikiri nilimuokota huyu? Acha kujifanya umechanganyikiwa.” Pius akaondoka kwa hasira.

“Na Pius.” Akasikia akiwa ameshatoka. Akarudi. “Zingatia mawasiliano kwa Mina. Kama mumewe alivyoomba, ukitaka kitu kwa Mina, wasiliana naye. Ukishindwa, mwambie mama yako.” “Sikukubaliana na hilo baba. Na sioni sababu. Yaani mimi kutaka kujua hali ya mwanangu ni mpaka nimuulize mama ua yeye, wakati mama yake ndio yupo karibu?! Hapana baba!”

Mnamwadhibu mwanangu bila sababu! Mwambie Andy nimekataa. Sitafanya hivyo. Hata mahakamani nitaenda. Acheni kunifanya mimi ndio mbaya wakati aliondoka kwake, nikamlelea mtoto wake mchana na usiku yeye akishindwa hata kupiga simu! Leo eti gafla nimuamini kwamba atakuwa na mawasiliano juu ya mtoto wangu wakati wakwakwe alimshindwa! HAPANA baba. Mwambie nikitaka hali ya mwanangu nitamtafuta mama yake. Akitaka awe na Mina kila wakati ili awe analinda mazungumzo yetu. Msinichezee akili.” Akaondoka kwa hasira.

Huko Upande Wa Pili.

Shema akarudi tena shule. Safari hii ratiba ikawa shule na mpirani. Akawa anaondoka asubuhi kurudi usiku. Ameshakula, ni kuoga na kulala. Upweke ukaongezeka kwa Pam. Maisha yakaendelea, kimya, hamsikii Mill kwa la kheri wala kwa salamu! Na yeye akatulia.

Nafasi Ingine

Baada ya mwezi tena kupita kwenye majira ya saa nne asubuhi akapata ujumbe kutoka kwa Mill. ‘Sijui kama naruhusiwa mawasiliano kwa mida gani, lakini ni maswala ya kazi. Kama bado unatafuta kazi, wasiliana na namba hii.’ Akamrushia namba. ‘Asante. Nashukuru Mill. Muda gani mzuri wa kumpigia?’ ‘Anatafuta kujaza hiyo nafasi kwa haraka. Nashauri usivute.’ ‘Asante. Nampigia sasahivi.’ Hakumjibu.

~~~~~~~~~~~~~~

Akapiga bila ya kuchelewa. Akapokea sauti ya kiume. Akajitambulisha na kumwambia amepewa namba yake na Mr. Mgini. Kwake akamtambulisha kikazi, sio kwa jina la Mill. Akaonekana kuelewa kwa haraka na kama aliyekuwa kitarajia simu yake. Akamuhoji maswali ya msingi tu na kumuuliza yupo tayari kuanza kazi lini. Pam akasema baada ya siku mbili. Akitaka kujiandaa maana ni kazi ya kiofisi.

Ilifanana kama aliyokuwa ameambiwa na Mill mwanzoni. Na ni kama kazi aliyokuwa akifanya kwa Sandra, ila si mikopo. Kushugulika na maswala ya benki, akimsaidia muhasibu. Alifurahi Pam, hakuamini.

~~~~~~~~~~~~~~

Akaenda kujisafi haswa, kusudi ili kumrudisha Pam wa viwango. Na hivi alishaletewa na Mill mapigo ya ukweli! Hakutaka kujikosea. Alitengeneza nywele vizuri na kuongezea kununua baadhi ya nguo za kiofisi. Pam alishafanya ofisi za warembo, alijua wapi pakupata nguo zakueleweka za kiofisi. Na hivi bado Mill alikuwa akiweka pesa benki, hakujipunja. Uzuri viatu vya maana Mill alishamletea, alijua lazima enzi zitarudi tu.

 Akaona awe muungwana. Siku kabla yakuanza kazi akamtumia ujumbe. ‘Nashukuru, ile kazi nilipata. Naianza kesho. Asante.’ ‘Karibu. Na kama utahitaji usafiri, unaweza kumtumia dereva wa Shema. Vinginevyo kila la kheri.’ Alifurahia Pam, mpaka akajikuta akirukaruka kwa shangwe na kumjibu. ‘Nitashukuru. Akija kumchukua Shema, na mimi nitaomba lifti.’ Hakujibiwa. Akasubiria majibu mpaka akachoka na kunyong’onyea. Hakujibiwa.

Light, at the end of tunel.

Hakumwambia mtu kama anaanza kazi maana mahusiano ni kama yalishaharibika na wapangaji wenzie. Mama Batuli alishakuwa akimtangaza ana roho mbaya, alishindwa kumuombea kazi mumewe kwa baba Shema, ndio maana na yeye Mungu amemnyima. Ushoga ukaisha kabisa hapo ndani, wakasahau mazuri yote waliyokwisha fanyiana. Akawa amebakia peke yake tu. Akajiapia mshahara wa kwanza, anahama hapo. Ila hakumwambia mtu.

~~~~~~~~~~~~~~

Hatimaye nuru ingine tena ikaangaza. Alitoka hapo alfajiri na mwanae. Bwana alipendeza kama aliyekuwa amepania! Kuanzia juu mpaka chini, kiatu cha juu. Na mguu wake ukapendeza maana alivaa gauni fupi mpaka kwenye magoti. Dereva alifika na maelezo kuwa amfikishe Shema shule kwanza kisha ampeleke na yeye kazini. Akajua Mill alishashugulikia hilo. Ila wasiwasi wa kuwahi kazini ndio ukamuingia.

Walipofika kituo cha Sayansi, akamuomba amshushe achukue daladala ya kazini kwake. Hakumbishia sana japo alimwambia wasingechelewa. Pam akalazimishia akiwa na hofu ya kutoharibu kazi mpya.

Daladala ilimshusha nje ya geti la hospitalini, akajitambulisha getini na kuulizia zilipo ofisi zao. Akaonyweshwa. Akatembea mpaka huko. Ikawa imetimia saa mbili kamili na yeye yupo mapokezi.

Lilikuwa eneo dogo lakini safi sana. Ofisi nadhifu mno tofauti kabisa na kwa Sandra. Mambo yaliendeshwa kitaalamu. Akaitiwa huyo muhasibu. Akiwa anasubiria hapo mapokezi, akatokea mwanaume amevaa shati jeupe na tai. Alionekana na neema. Akamtambulisha kwa mrembo pale mapokezi, Fatma, kuwa na yeye atakua mfanyakazi wa hapo, ndipo akamkaribisha ofisini.

Akampa utambulisho na kumzungusha sehemu ya biashara. Akahisi ni kama kile alichoambiwa na Mill anamiliki hapo nchini lakini bado hakuwa ameonana na Mill mwenyewe, akajiambia atulie, pengine vinafanana. Akampeleka sehemu wanazo fanyia vipimo, wanapopokea pesa au malipo na kuandikiwa risiti maana kote huko alitakiwa yeye ndio awe anapita kukusanya malipo na kopi za risiti. Kumpelekea muhasibu. Kufunga mahesabu, kisha anapewa yeye kupeleka benki. Haikuwa ngumu.

“Ningekupeleka kwa bosi, lakini leo yupo busy kidogo.” Hilo halikuwa tatizo kwa Pam, shida ilikuwa kazi wala si bosi wao. Akaanza kuelekezwa chakufanya. Hapakuwa na kitu kigumu alichoona kingemshinda. Mida ya mchana walizoea huyo muhasibu na wengine wawili kutoka kwenda kula kwenye mgahawa wa hapohapo hospitalini. Lakini Pam alipokaribishwa, akakataa kiuungwana.

Jioni wakati anatoka akakutana na dereva wa Shema nje akimsubiria. “Anakaribia kumaliza mazoezi. Nakufuata wewe, kisha namfuata na yeye, nawarudisha nyumbani.” Alishukuru Pam, maana hakujua angerudije nyumbani na foleni hizo. Wakaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~

Kesho yake akafanya vilevile, alishukia kituo cha Sayansi na kuchukua daladala ya kumpeleka kazini. Alimkuta Mill amesimama mapokezi. Amevaa kiofisi. Bwana Mill alipendeza, mpaka Pam akababaika. Alikuwa kwenye simu hapo mapokezi. Akasimama kusubiria mpaka alipomaliza kuzungumza, ilisikika ni simu ya kikazi maana alikuwa akizungumza kwenye simu ya mezani, akionekana amepewa na huyo mrembo wa hapo mapokezi, Fatma.

Kama apige goti kumsalimia. “Vipi umeonaje siku ya kwanza?” “Bado najifunza na kuelewa kazi yenyewe.” Akamuona ni Pam aliyenyong’onyea na amepungua mwili si kama alivyoachana naye wakitokea Arusha. Akagundua hapo hajamsifia kama amependeza. Kabla hajaongeza kingine, muhasibu, ambaye ndio Pam anafanya kazi naye, alijitambulisha kwake kwa jina moja tu, Mbise, akatoka akionekana anamazungumzo naye. Akamwambia waelekee ofisini kwake. Ndio akajua ni kweli. Yeye ndiye anayemiliki hapo.

Akapoa na kuelekea ofisini kwao. Maana Mill aliondoka bila hata kuaga, na hapo aliheshimika kama mmiliki wala si bosi tu. Alishaona hapo mambo yanaendeshwa kitaalamu wala si kiswahili. Sekretari mwenyewe, huyo Fatma, alikuwa msafi haswa na amependeza. Anazungumza lugha zote mbili, kiswahili fasaha na kingereza bila kona ndefu.

Akaenda kutulia ofisini kwao akifanya kazi. Siku hiyo mida ya saa tano wakatoka kwenda benki kutambulishwa kama mmoja wa wafanyakazi wa hapo ili akifika wawe wanamsaidia kwa haraka asiwe anasimama kwenye foleni. Na hapo walipelekwa na gari ya ofisi. Nzuri sana. Safi. Akajua ni mambo ya Mill tu, kupenda vizuri.

~~~~~~~~~~~~~~

Akaendelea na kazi mpaka siku ya tano ambayo ni ijumaa wakati anakwenda benki akakutana na Mill akitoka na mrembo wa nguvu! Pam mwenyewe alimkubali. Msichana alikuwa mzuri, halafu alijijulia. Yeye hakuwa mweupe kama Pam, maji ya kunde inayokwenda rangi nzuri nyeusi. Ila umbile kama la Pam! Na alijua vile Mill anavyopenda wanawake wenye maumbile ya kibantu! Wenye minofu sehemu zao. Akajua wazi ndiye huyo mwanamke wake. Wote walijikuta mapokezi.

Pam akitaka Fatma amuitie dereva, na Mill naye alikuwa akiaga kwa Fatma huyohuyo akimalizia maelezo akisema siku hiyo hatarudi, ndio amemaliza. Ilikuwa saa tano asubuhi. Pam akajiweka pembeni AKIUMIA. “Inamaana anakwenda kupumzika na mwanamke wake!” Pam akawaza AKISONONEKA. “Ila nao wamezidisha. Mapema hivi!” Akajilalamisha moyoni ila akakumbuka mapenzi ya Mill. Mkiwa naye kitandani, huwezi jua kama masaa yanakwenda. Akaenda kukaa kwenye makochi akisubiria gari, akapotelea mawazoni.

Alisikia kiitwa kuwa dereva amefika. Wala Mill na mrembo wake hawakuwepo pale. Kwamba walishaondoka, hata hakumsemesha wala kumtambulisha kwa huyo msichana! “Ameshindwa hata kusema mimi ni mzazi mwenzie!” Pam AKAUMIA sana. Siku ikawa imeshamuendea vibaya.

~~~~~~~~~~~~~~

Inaendelea…


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment