Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 48. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 48.

“Sasa nisikilize Pius. Maadamu uliamua kumpitishia mtoto wako kwenye familia yangu, ataishi kutokana na SISI.” “Huo ni ukorofi na kiburi kisicho na sababu. Kwani mimi kumpa Mina gari nzuri kwa ajili ya matumizi yake ya kila siku, kuna ubaya gani?” Kabla hajajibu Andy, Mina akaenda kumshika mkono Pius pale alipokuwa karibu kwenye kitanda cha mtoto, akamvuta kumtoa nje.

“Mbona unanitoa tu mimi peke yangu wakati tulikuwa tukizungumza na Andy ambaye wakati wote ni mkorofi?” “Na wewe Andy nifuate hapa nje.” Mina akaamuru. Akafuata bila kubisha. Kisha akafunga mlango nyuma yake.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Kwa akili zako wewe, hapa sasahivi, kuna mwenye shida ya gari?” Wakamsikia Mina akimuuliza Pius nje ya mlango. “Mimi ninachozungumzia ni mtakapotoka. Mtoto atapona Mina, usikate tamaa.” Wakamsikia Pius akijibu kwa unyenyekevu. “Ujue Pius wewe unataka kuniudhi bila sababu!” “Ni kutaka kukusaidia!” “Yaani SASAHIVI mtoto wangu akiwa mgonjwa. Sijamuona hata akiwa amefungua macho, nikajua kama ni mzima ua la, ndio unataka kuzungumzia maswala ya gari!?” Akaendelea kabla hajajibu.

“Huyo mtoto amelala hapo nyinyi wote hamumfahamu. Ayvin ni mtoto mzuri sana. Amezaliwa kwenye amani na utulivu. Amekutana na mazingira ya utulivu sana tuliyomuwekea mimi na Ayan. Akakuta akisubiriwa kwa upendo na yeye akaleta furaha katikati yetu. Hajui malumbano, hajui fujo zenu hizi. Hajui huu ubaya huu. Kutwa tupo MWANZO wa TATIZO. Hatusogei popote! Tokea mimba yake, mpaka leo, mambo ni hayohayo!”

“Sasa hivi ni mgonjwa. Tuna taarifa zile za daktari. Hata sijamsika mtoto wangu nikajua yukoje! Kama walichofanya kimesaidia kurudisha furaha yake au la, nyinyi ndio mnaona huu ndio wakati wa kugombania gari? Kweli?!”

“Pius ndio mkorofi.” “Sasa kati yangu mimi na wewe nani ni mkorofi hapa? Wewe ndio umeng’ang’ania kutosamehe.” “Nisamehe kwani ulifanya kwa bahati mbaya au kusudi tu kuniharibia familia? Na mbaya zaidi, umepanga kuharibu zaidi!” “Jambo limeshatokea. Kwa nini…” “Sasa nisikilizeni nyinyi wawili. Zaidi wewe Pius, humu ndani msiingie tena, mpaka mmalizane hapahapa nje. Anayeingia humu ndani, ni amani aliyozoea Ayvin.” “Tafadhali muite jina nililoomba mimi.” “Pius wewe!” Mina akashangaa sana.

“Kwani jina langu lina ugumu gani? Basi muite hata PJ.” “Kwamba WEWE unataka akiamka na maumivu, ajikute na jina jipya, sehemu ngeni, na watu wapya wamemzunguka!?” “Taratibu atazoea.” Pius akamjibu Mina kwa unyenyekevu kabisa bila kubadili msimamo wake.

Unapenyeza jina lako, kwenye familia yangu, makusudi tu. Unaona akiitwa Ayvin, akajichanganya na kaka yake, roho yako haitatulia maana patakuwa na amani! Yaani kukiwa na Pius ndani ya familia ya Andy, kukawa na mchanganyiko ndio raha yako!” “Sasa mchanganyiko utatoka wapi hapo? Maana nataka akue akijitambua mimi ni baba yake na ninampenda. Na yeye si mtoto wa bahati mbaya.” “Wewe umechanganyikiwa Pius.” “Na…” kabla hajajibu Pius, Mina akawahi.

“Sasa nakuonya Pius. Hicho unachotaka kukianzisha sasahivi, kiishie hapahapa nje, usikiingize ndani. Lasivyo nabeba mwanangu, naondoka hapa. Hakika safari hii hamtakaa mkatuona tena. Sasa endelea kuleta ukorofi, ukidhania watoto wanalelewa na magari.”

“Huwezi kuondoka tena Mina?” “Nabaki kwa sababu ipi? Niambie Pius. Nabakia kwa sababu ipi? Mnataka kuja kuchanganya watoto wangu, wajione ni watoto wa ajabu wakati kwangu ni baraka!”

“Sababu ya utulivu, amani na furaha waliyokuwa nayo huko, si mazingira ya kitajiri kama haya yenu, Ayan amejikuta mbali sana kiakili. Anajifunza yeye mwenyewe kusoma. Japokuwa ni mkimya vile, na hajaanza hata shule, ile tu amani ya pale kwetu, mtoto unamfundisha jambo anaelewa kwa haraka sana. Ayan anasoma mpaka kitabu! Hana table ukamuuliza akashindwa. Akiwa kwenye utulivu, muulize namba yeyote, kuanzia table ya kwanza mpaka 12, mwambie azidishe uone jinsi atakavyokujibu.”

“Ayvin na jina lake hilohilo, amejawa na furaha ambayo kila mtu anatamani kuwa naye. Mpaka mama mwenye nyumba akiwa amechoka, anatufuata kwetu anaomba amshike kidogo, acheke naye, ampunguzie stress za maisha. WEWE unataka kunijazia magari, kisha unipotezee amani kwa watoto wangu! Hakika SIKURUHUSU. Endeleeni kugombana hapa nje, mkiingiza tu fujo zenu ndani, ndio MWISHO wenu.” Akaingia ndani na kufunga mlango. Kimya. Ndani na nje.

Kisha, wakamsikia Andy akilalamika kwa uchungu. “Nilipomleta Mina nyumbani kwa mara ya kwanza, wote mlimuona hafai, MKAMKATAA.” “Mimi nilimpenda Mina tokea mwanzo. Uongo Mina?” Wakamsikia mtoto wa Pius akidakia ndani.

Mkamkashifu mpenzi wangu, kwa maneno mengi machafu, mpaka akaondoka. Mlipoona anazaa watoto wa kiume, mkaanza kujisogeza. Akajiongeza mwenyewe kwenda shule, mkajaa kwenye maisha yetu mkinitafuta mimi ubaya ili wewe Pius uwe karibu yake, upenyeze mtoto wako kwa hila.” “Huna shukurani Andy wewe! Ulitelekeza mkeo hapa mjini, ukawa unahangaikia MALI kama wengine sisi hatutaki mali! Tukakusaidia, yaani hii ndio shukurani yako?”

“Na wewe ukajilipa kwa kumzalisha mke wangu kwa HILA!? Ulikuwa wapi siku zile za Mina niliyemtambulisha kwenu, mkamkajeli na kumcheka mkimuona hafai? Si na wewe ulikuwepo, tena ukanyamaza kimya akidhihakiwa na mpaka watoto wadogo kina Paul? Eti gafla unasema unampenda mke wangu! Hakika Mungu aamue kati yetu Pius. Uharibifu huu unaotaka kuendeleza kwenye familia niliyoanzisha mimi na Mina kwa mapenzi tu, bila kutaka viwango vyenu vya watoto wa jinsia fulani na mtu aliyesoma, Mungu atuamue kwa haki. Unajisogeza baada ya kuona vinang’aa!”

“Mimi sikuwahi kumdharau Mina tokea siku ya kwanza. Na kama utakumbuka nilimtetea mpaka mama akataka kunibadilikia, ndio baba akanunua ugomvi. Mimi sijawahi mdharau Mina hata siku moja.” Pius akajitetea.

Mina akachukua mizigo aliyoletewa na Andy na kuingia bafuni. Pakazuka ukimya. Lakini kwa hakika Andy alimkumbusha Mina mbali sana. Enzi zake hajui hata kula kwa kisu na uma! Elimu yake ndogo kabisa, ya chini! Alivyompokea kwa upendo bila kujali tofauti zao za kiuchumi! Akajisikia kupoa kabisa rohoni. Akakumbuka mapenzi ya dhati yasiyo hila wala masharti ya Andy, ya zamani.

~~~~~~~~~~~~~~

Akatoka akiwa amebadilisha nguo akiwa ameshaoga kabisa. Akawakuta wote wapo hapo. Mara daktari wa watoto akaingia. “Huyo hataamka mpaka kesho. Tumefanya makusudi ili apumzike. Kwanza alikuwa na homa, pili sikutaka ajitoneshe vidonda vibichi, kwa hiyo kama mlikuwa mkimsubiria aamke, sio leo. Na msiwe na wasiwasi. Kila maji atakayoongezewa ni yakumpa nguvu na yatakuwa na dawa. Atakuwa sawa.” Akamsogelea. Akamuangalia na kumpima vitu kadhaa.

“Vipi unaonaje?” Pius akauliza. “Kila kitu kipo sawa kabisa. Atakuwa sawa. Na kesho ataamka akiwa na nguvu mpya.” “Akiendelea hivi, inamaana kesho mtaturuhusu?” Mina akauliza. “Kabisa. Hamna sababu ya kuendelea kuwa hapa. Operation aliyofanyiwa mtoto wako ni ya hali ya juu sana. Baada ya muda hata kitundu alichotobolewa ili kuingizwa mashine ya kurekebishia ndani palipo athirika, kovu litapotea kabisa. Mkija kumsimulia baadaye, itamuia ngumu kuamini.”

“Ila kwa kuwa ni mtoto na ndio anaanza kujitegemea mwenyewe, kutambaa, kukaa na mengineyo, ni muhimu kuwa makini naye asijitoneshe.” Akawapa maelezo yakutosha. Pius akauliza maswali yake mpaka akamaliza. “Hataamka kwa usiku huu. Nashauri mkapumzike tu. Hapa yupo kwenye mikono salama. Manesi watapita kila wakati kumuangalia na kumshugulikia.” Wakina Ruhinda wakashukuru, akaondoka.

Bado Mina Kashika Makali.

“Mina binti yangu, nakuandalia chumba chako na wanao kabisa. Mkiruhusiwa tu, ukapumzike.” “Nashukuru sana mama kwa moyo wako wa kila wakati kutaka kunikarimu mimi na wanangu, lakini naona si sawa mimi na wanangu kuishi pale.” “Kwa nini?!” Pius akahamaki. Mina akamtizama, wakaona anapoa.

“Najua nawajibika kujieleza na kwako pamoja na baba, mbali na Andy, kwa nini niliondoka bila ya kuaga.” “Na mimi Mina!” “Basi sababu ni wewe Pius.” Paul akaanza kucheka kimyakimya. “Tafadhali usicheke Paul.” “Sawa baba.” Akatulia.

“Mimi nimefanyaje?!” “Mbali yako wewe mwenyewe, ambaye ni tatizo mpaka sasa, pale si aina ya mazingira nataka wanangu wakulie.” Wote wakashangaa sana. Kwa Mzee Ruhinda kulivyo matawi!

“Unamaanisha nini Mina, binti yangu?” Mzee Ruhinda akauliza taratibu tu. “Najua nyinyi mnauelewa tofauti na wangu juu ya mazingira. Najua kwenu ni mazingira yaliyo staarabika. Lakini mimi nataka kuelea wanangu kwenye mazingira ya amani na utulivu. Sitaki hata mmoja wao ajione ni kama amezaliwa kwenye mazingira ambayo anaingilia ratiba za watu.”

“Yaani mtoto anakua kwenye mazingira akijihisi HATAKIWI, sababu wazazi wote wanaratiba zao muhimu, yeye ni kama anaingilia tu, kisha anajikuta si wa muhimu.” Andy akajua ni yeye. “Au mtoto anazaliwa kwenye mazingira kama hivi Ayvin. Anakuwa kwenye mazingira aliozungukwa na watu na nyadhifa zao. Pesa. Elimu. Walioweza kuongoza watu wengine, lakini wote wameshindwa kutulia, na kujipanga jinsi ya kumlea mtoto wa aina yake!” Hapo kimya.

“Mtoto anakua kwenye mazingira ya kelele. Ugomvi. Kutoelewana. Halafu yeye ambaye hakuchagua kuzaliwa kwenye mazingira hayo, ndio anakua MUHANGA mkubwa. Anakuwa na majina makubwa. Anasoma kwenye mashule yenu hayo. Anavaa kama hivyo nyinyi, lakini anakuwa ni mtoto tuliyemchanganya, anaye nyanyasika kihisia, ndani ni mbovu kuliko anavyoonekana nje akiwa nadhifu! Hivyo mimi SITAKI.”

“Mimi SITALEA watoto wakuja kuongoza watu wengine wa nje, kimataifa wakati wakishindwa kuongoza familia zao au hata ndugu zao.” Bwana walinywea. Maana hapo ni watu wazima na nyadhifa nzito. Ila wanagombana kama waswahili wa kwa Mfuga Mbwa.

“Najiona mimi kama mama nitakuwa nimeshindwa endapo nitawaacha wanangu wanakua kwenye mazingira kama hayo. Siwezi. Sitaki. Na sitafanya hivyo.” Akaendelea akiwa ametulia tu, ila Mina ni msema moyo wake. Wote walimjua.

“Kingine, kikubwa na cha msingi pia kilichonifanya niondoke ni Raza.” Wote wakaelewa kwa upande fulani. “Raza asikutishe Mina.” Pius akadakia akimuhakikishia. “Yeye bado si ni Raza Ruhinda?” Akamuuliza huyo mumewe. Kimya.

“We Pius?” “Ndiyo lakini nishazungumza naye.” “Kwa kumpiga! Hapana Pius. Cha kwanza, na hiki hata mama nilimwambia. Na Andy nilimwambia mwanzoni kabisa alipoonyesha nia ya kutaka kunioa. Nilijieleza ukweli kwake. Akanielewa na nilimuahidi nimebadilika, tukaoana. Maneno aliyokuwa akisambaza Raza, si uongo. Na mama nilimwambia siku ile. Anaweza kuwa anaongeza kwa hasira lakini kwa asilimia fulani, hakuongopa. Mimi nilikuwa mtoto mbaya. Ila mama akanipeleka kuombewa, nikatulia kabisa mpaka nikaja kukutana na Andy. Yakatokea yakutokea. Nikapotea tena lakini Mungu akanirudisha tena kwake. Nimetubu. Mpaka leo Mungu ananisaidia, mambo niliyokuwa nikifanya zamani, ameyaondoa kabisa.”

“Lakini kinacho nishinda kurudi pale si maneno, ila ni heshima yangu kwa Raza. Naona si sawa kwake. Siku ya kwanza kabisa Andy amenileta pale kwenu, mbali na Andy, Raza alinipokea jamani! Sitasahau. Nilifika jikoni sijui chakufanya, lakini yeye alinikarimu mpaka kunipa mchele wa kuchambua. Alipoona nimenyimwa kila kitu chakufanya huku nikichekwa pale kwenu, Raza alinifuata chooni maana nilikuwa nalia peke yangu sitaki Andy anione.”

“Nyinyi hamkujua maana ni kama alijiiba kunifuata. Aliniambia hivi akinituliza, kuwa mwanzo huwa ni mgumu. Mkishanifahamu vizuri, mtanipokea tu. Akasema kabisa, nyinyi ni binadamu wa kawaida tu. Mapungufu ya kawaida mnayo, lakini sitashindwa kuishi na nyinyi. Raza aliniambia kwa upendo kabisa. Halafu akasema katika Ruhinda, nilipatia kuolewa na Andy. Ni mwanaume mwaminifu sana, na anahitaji kujenga familia. Nikitulia, nitakuwa na familia nzuri, kwa sababu ndicho kitu anahitaji Andy kwa wakati huo. Hana dharau na mengine mengi akiwasema nyinyi wote vizuri.” Wote wakashangaa.

“Raza alinifanya nikatulia, ndio nikaenda kucheza na watoto japo bado mliendelea kunisema vibaya, mimi mwenyewe nikiwepo. Nilipanga ninyamaze tu, lakini nilishindwa pale mezani mlipozidisha maneno mabaya ya dharau ya wazi kabisa huku Paul akitucheka mimi na Andy, halafu Andy akashindwa kunitetea. Ndio nikaondoka nikasema Raza amenidanganya, mbona sasa Andy mwenyewe alinyamaza wakati ndugu zake wakitusema vibaya! Lakini wakati huo nilikuwa sijamjua mume wangu vizuri.”

“Ninachotaka kusema ni hivi, namuheshimu sana Raza. Najua yeye kama binadamu anamapungufu yake, ila zaidi ukimwangalia ni sababu analinda kilicho chake. Huwezi hata kumuhukumu. Lakini binafsi, siwezi kuhamia pale kwenu wazazi wangu, aliponikaribisha Raza, halafu yeye ikawa kama nimemfukuza! Hapana.”

“Nakumbuka picha niliyowakuta nayo siku ya kwanza pale kwa wazazi. Umoja ambao na mimi nilipenda niwe mmoja wenu. Lakini mlinikataa. Mlijaa amani na kuelewana kwa aina ya kupendeza na kuvutia mno. Watoto wenu walikuwa na furaha. Wanacheza pamoja kwa amani kila mmoja anajua chakufanya kwenye ile nyumba. Siwezi eti mimi gafla na wanangu tukaingia na kuvuruga! Hapana kwakweli.”

“Raza na watoto wake niliwakuta pale. Alinikaribisha niongezeke, lakini si kuchukua nafasi yake.” “Hutachukua nafasi yake. Tutaweka mazingira ya amani ili wote muwepo, Mina mwanangu.” “Nakuelewa mama. Na ndivyo nilivyotegemea, lakini mimi na wewe hata kama tungependa iwe hivyo, LAKINI Pius ndio mvurugaji.” “Mina!” “Hakika tena. Naomba Poliny akasubirie kwenye gari. Tafadhali.” Wakaona wazo sio baya japo mwenyewe alitaka kubaki. Mzee Ruhinda akamuomba Devi aongozane naye. Wakatoka.

~~~~~~~~~~~~~~

Aliporidhika huyo kipenzi, mtoto mkubwa wa Pius ameondoka, Mina akamgeukia Pius tena. “Wewe ndio mvurugaji MKUBWA Pius. Hutaki amani tokea mwanzo, na baba alikwambia.” Mina akaendelea. “Jamani mimi nataka ndoa yangu. Nampenda mume wangu.” Andy alibaki ameinama tu, lakini angalau alifurahia.

“Hata kama kwenu tunaweza onekana hatujafikia viwango vyenu, lakini ni ndoa yetu mimi na Andy. Tulianza safari yetu ya ndoa tukiwa hatujui ya mbeleni. Kuna kukosea kwingi sababu ya ndoto tulizoingia nazo kwenye ndoa na matarajio yetu. Nafikiri ndio maana nyinyi wazazi mlikuwa tayari kutusaidia kutuona tunaendelea mbele na si kuachana.”

“Katika magumu mengi tuliyokuwa nayo, nakumbuka Andy alipokuwa nje ya nchi masomoni, alinipigia simu akitaka arudi ili awe na mimi. Aliniambia wazi, haoni faida tena ya kila anachohangaikia kama sisi wawili hatupo pamoja. Andy akasema ni bora arudi nchini tuishi kwa kile tulichonacho, aache hata kile cheo kule Dodoma. Mimi nikamtia moyo aendelee tu, nikimwambia nitaendelea kuvumilia mpaka arudi. Tukaweka mipango mingi bila kujua kumbe Ayvin ameshaingia kwenye picha.”

Mkampa maneno mengi Andy wangu, akaja kuniacha. Tukatengana kwa muda lakini mapenzi yakaturudisha pamoja mpaka mtoto akaja kujulikana ni wa Pius. Msimsaidie mume wangu aweze kuishi na mtoto ambaye hakupanga, Pius wewe ndio unaongeza FUJO kila mkoa, kila mahali, kisha ukishamaliza kutukorofisha, unarudi nyumbani kwako kwenye amani, unatuacha sisi wanne. Andy, Ayan, mimi na Ayvin tumefarakana. Andy haoni nafasi yake kwa sababu hakuna anayempa nafasi, kwanza kujua chakufanya na mtoto wa kaka yake katikati ya familia yake.”

“Mnachofanya ni kuongeza mafuta ya taa kwenye moto unaowaka ndani yake na familia yake. Mnaondoa amani kwenye ndoa yangu ambayo hata hatujui tena ni wapi tunasimamia! Wewe Pius kila siku unakuja na njia mpya ya kuharibu, wakati baba alikuonya kabisa. Tena kwa kumsikia akirudiarudia kwako.” Kimya.

“Hakika mimi nilidhania WEWE ndio ungekuwa mstari wa mbele kuleta amani nyumbani kwetu ili Ayvin akue kwenye mazingira mazuri, lakini umekusudia kuharibu.” “Sio kweli.” “Ni kweli kabisa Pius. Na hata leo uliponipigia simu kunitaarifu kuwa Mina amekutafuta, na alijifungua salama ila mtoto ni mgonjwa, wanarudi kwa matibabu. Sikukwambia maneno kama haya aliyoyasema Mina?” Kimya.

Mzee Ruhinda Naye.

“Sema tu Pius. Sikukwambia hikihiki anachokisema hapa Mina?” Kimya. “Jamani, haya anayoongea Mina, nimetoka kumkumbusha Pius, LEO. Kuwa yeye anahatima ya wapi mtoto wake akue. Akileta AMANI kwenye ndoa ya Andy, mtoto wake atalelewa vizuri tu. Maana najua Andy na Mina wanapendana. Na hata tabia ya Mina pia nilimwambia mama yenu. Nilimwambia kama anayosema Raza ni kweli, basi Mina amebadilika sana. Alikaa hapa mjini hana mwanaume, wakati alikuwa akizunguka jijini hapa, na mumewe akamuacha mikononi kwa vijana kama yeye pale IFM, lakini Mina alibaki akimuheshimu mumewe japo Andy alishindwa kurudi nyumbani kabisa.”

“Nikamwambia mama yenu, inawezekana kuna wawili hawa waliloongea na kukubaliana, ndio maana wanakopita japokuwa ni pagumu, lakini hawakati tamaa.” “Wala hapakuwa na maelewano mazuri baba yangu. Mina alikuwa akinivumilia tu. Nilikuwa silali. Nina usingizi na njaa wakati wote. Hata yeye nilikuwa sizungumzi naye vizuri. Ni aliamua kutulia tu na mimi.” Andy akaongeza.

“Sasa kuja kumsikia Pius anaanzisha maswala ya gari hapa!” “Tena kwa fujo kabisa kama vile hilo gari linatakiwa usiku huuhuu!” Mama yake akaongeza. “Kama akaona havitoshi, anataka mtoto mgonjwa aitwe jina lake!” “Asante baba.” “Kweli Pius? Uharaka huo unatoa wapi wewe? Tena Mina akakuuliza kabisa na nilidhania ungefikiria. Mtoto mwenyewe hatujui! Umeshindwa kuweka mazingira ya atufahamu kwanza. Atuzoee. Kuwe na amani. Mina atulie nyumbani. Ajisikie utulivu, ndipo mzungumze maswala kama hayo ambayo si ya msingi!” “Kwangu ni msingi baba.” Akadakia Pius.

“Nyinyi mnaweza msione umuhimu wake, lakini mimi naona umuhimu. Huyu ni mtoto niliyemtafuta kwa mamilioni ya pesa nyingi sana, ila nikitaka apitie kwa Raza, na nyinyi ni mashahidi. Hatukufanikiwa mpaka Raza kutolewa kizazi. Kwani sikuona wanawake wengine wa kuzaa nao? Lakini nilikubali matokeo. Nikatulia. Hata mimi sikuchagua mwanangu apitie kwenye familia ya Andy.” “Hapo ndipo tunapopishana na Pius. Na huna jinsi ya kunibadilisha.” Andy akadakia.

“Pius wewe SI mlevi. Si malaya. Hujui na hujawahi kulala na mwanamke mbali na mkeo. Nakujua. Habari zako zinajulikana mpaka na mawaziri uliowahi kufanya nao kazi! Wabunge wanao kufahamu pia wanajua sifa yako hiyo. Wote wanao kufahamu wanasema linapofika kwenye swala la wanawake, hata kama umeweka pombe kichwani, HUSHAWISHIKI. Leo ulale na mke wangu, useme ni AJALI!” Andy akasikika na uchungu kabisa.

“Ninachotaka kusema, Mungu amenipa huyu mtoto kwa njia zake.” Wote wakashangaa sana. “Sasa sitaki akue katikati ya familia yenu, asijue ni mwanangu.” “Pius wewe?!” “Hakika mama. Katika hilo itabidi wanielewe tu na watafute njia ya kuishi naye hivyohivyo. Hawawezi kumuita mtoto wangu, jina la watoto wao. Eti mwanangu akue akijijua yeye ni mtoto wa Andy, sio wangu! HAPANA. Nimekataa mama. Mwanangu yeyote yule. Wakike na wakiume. Najitahidi WAJUE mimi ni baba yao, na nina wapenda. Ndio maana mnaona hata kwa dada zake sizembei.”

“Mama yao alijaribu kunikorofisha nao, lakini si mnaona wanangu? Wenyewe wanarudi kunitafuta japokuwa sijawahi kukata matumizi kwao. Hata kama wakiwekwa mbali na mimi kwa maneno ya UFITINI, nahakikisha hawaishiwi na wanajua kuwa nawapenda. Na ndio maana kwa ule upendo niliowaonyesha, hakuna mtoto wangu anaweza ishi bila mimi.”

Upendo wangu kwao umefunika hata dhambi hii MOJA niliyofanya. Sasa SIWEZI nikaanzia kwa huyu ambaye nataka aitwe Pius Junior Ruhinda. Katika hilo sina MJADALA Mina. Na sitayumba Andy. Tafuta jinsi ya kuishi na mwanangu, akijua yeye ni mtoto wa Pius, kama nilivyofanya kwa Ayan. Wote walijua WEWE ni baba yake, ila haupo, na NIKAMLEA kwa upendo wote. Nilikusaidia kwa mwanao kwa upendo kabisa, katikati ya watoto wote.” “Ilikuwa ili umpate mama yake.” Andy akamjibu.

Ulimuweka mwanangu karibu ili kumfikia mama yake.” “Najua umekasirika Andy, lakini mkeo hakuwa mwanamke pekee hapa jijini. Sikuwa na sababu ya kulipa garama ya kulea mtoto ili kumpata mama yake kama si upendo kwako. Kwanza nikijua unaanza kujijenga kikazi, huku unafamilia changa na hili hata Mina kama atakumbuka nilimwambia kabisa nikikutetea. Kuwa wewe ndio unaanza kazi, lazima utachukua muda mwingi ili uaminike kazini. Abishe Mina.” Kimya.

“Sikuwa na hila mimi! Eti ili kumpata mwanamke, eti ndio nilee mtoto wake! Wewe vipi Andy?! Au hujui kama unazungumza na mimi?! Ningeweza au nina uwezo wa kupata mwanamke kama Mina, muda na wakati wowote, nikalala naye bila garama ya kulea mtoto wake! Nilisaidia familia yako kwa upendo tu, yaliyotokea ni ajali.”

Huko Upande Wa Pili!

Kipindi hicho cha likizo Shema akajiunga na hiyo timu ya mpira ya miguu aliyotafutiwa na baba yake. Akawa anakwenda kuchukuliwa na dereva na kurudishwa. Lakini Pam akagundua yeye Mill huwa anakuwepo huko na mtoto wake kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa mchezo. Akafanya hivyo kwa mwanae kama anayemtenga na maisha ya pale kwao uswahilini, mpaka tena shule zikawa zinafungua.

~~~~~~~~~~~~~~

Siku ya ijumaa aliporudishwa tu mwanae ikiwa mapema kabla usiku, akamtumia ujumbe. Ndio ilikuwa siku ya mwisho siku ya jumatatu anarudi shule. ‘Mill, pole kwa usumbufu. Nilikuwa naulizia ile nafasi ya nyumba kama nayo bado ipo? Nahisi itampunguzia safari Shema. Atakuwa karibu na shule na mambo yanayo muhusu.’  Baada ya muda akamjibu.

‘Sehemu ya kuishi ipo, ila nimeanza mahusiano. Bado hayajachukua sura nzuri ya kueleweka kumtambulisha kwa Shema. Ndio tupo mwanzoni kabisa. Tafadhali nipe muda mpaka nitakapokuwa tayari kumtambulisha kwa Shema. Sitaki kumchanganya mtoto kwa kitu ambacho sina uhakika nacho. Nikimaanisha sitaki muhamie hapa aje akutane naye nikiwa sina majibu ya kueleweka. Naamini haitachukua muda mrefu.’ Pam alishituka. Akarudia tena na tena kusoma huo ujumbe, akajikuta machozi yakimtoka.

~~~~~~~~~~~~~~

Alienda bafuni akijidai anaoga ilimradi tu apate faragha ya kufikiria bila mwanae. Haikusaidia, machozi yalikuwa yakimtoka Pam asiyejua kulia. Wakati wanalala mwanae akamuhisi analia. Alipomuuliza akamdanganya macho yanamuuma. Kile alichomringia nacho Mill, anapewa na mwengine!

Na hatimaye maneno ya kina mama Batuli YAKATIMIA. Ameingia mwanamke mwingine kwenye maisha ya Mill, hata mwanae kwenda kuishi kwake, pazuri eti ASUBURI! Pam hakuwa akiamini! Mill anavyompenda mwanae, na alishasema pale wanapoishi ni duni, eti leo anamsubirisha sababu ya mwanamke! HOFU ikazidi kumtesa akijua ameshachezea shilingi chooni.

Akajua kwa hakika HATIMA yake na mtoto wake, ameshamuachia mwanamke mwingine. Inamaana angekuwepo yeye mwenyewe kwenye mapenzi na Mill, angeamua wapi awepo. Alilia Pam mpaka  kichwa kikaanza kugonga kama kuna kengele humo ndani. Akameza dawa na kulala. Ajira amenyimwa na pakuishi alipokuwa akibembelezewa pia amewekewa pause.

~~~~~~~~~~~~~~

Siku inayofuata mchana dereva alikuja kumchukua Shema, kupelekwa kwa kinyozi. Akamuacha mama yake kwa shida kwani alikuwa kama mgonjwa kitandani. Aibu, hawezi kutoka nje. Macho yamevimba, majirani zake aliokuwa akiwakumbatia na kumtambia Mill amejitengenezea familia ingine, ndio hao wamemgeuka, wanamsema vibaya sana. Mtaa ukaanza kukosa raha yake.

Shema alifika kwa baba yake amepoa. Alipomuuliza kulikoni akamwambia mama yake mgonjwa wa macho. Yanatoa machozi. Mill akamfanyia mwanae yote. Wakala pamoja. Akapita duka la madawa, akamnunulia dawa ya macho akampa akampe mama yake. “Mwambie kama bado hajapata dawa, ajaribu kutumia hizi, zitamsaidia.” Akamfungashia vyakula alivyojua angependa, Shema akampelekea mama yake.

Pam akashukuru kwamba haihitaji kutoka nje, kupika. Ni kula tu hapohapo ndani na kwenda msalani. Alilala siku mbili yupo kitandani. Wivu. Kila akifikiria Mill na mwanamke mwingine, alizidi kunyong’onyea.

~~~~~~~~~~~~~~

Inaendelea…


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment