Maji yamezidi unga, bado Mina alikuwa njia panda asubuhi hiyo ya saa nne akiwa
bado yupo chumba cha daktari, ameshindwa kufanya maamuzi ya huyo
mtoto, kufanyiwa upasuaji. Akakumbuka fujo aliyoacha nyuma, hakuona
atakayempa ushauri wa haraka bila kufikiwa baba wa mtoto mwenyewe. “Hata
nikimpigia mzee Ruhinda, ataishia kuzungumza na Pius mwenyewe kwanza ndipo
anirudie.”
Akaendelea kuwaza. “Andy na mtoto wa Pius!” Akazidi
kusita kila alipokumbuka jinsi walivyoachana na mumewe, na vile Andy walipofika
na kaka yake. “Hata yeye atataka kumshirikisha Pius kwanza kabla hajafanya maamuzi
ya mtoto wa Pius mwenyewe asije laumiwa baadaye. Kwanza hata sijui kama bado
anatutaka mimi na mtoto wa Pius!” Akawa anaendelea kuwaza hapohapo mbele ya
daktari akiwa bado anahofu ya ajabu. “Bora niokoe muda.” Daktari
akamuona anachukua simu na kupiga. Ikaita kama mara tatu hivi, upande wa pili
akaitika.
“Mimi Mina.” Akajitambulisha. Kimya asijue mshituko uliompata. “Pius?” “Nimekutafuta Mina! Mpaka nimechanganyikiwa.
Nipo kama mwehu! Mpaka leo asubuhi pia nilikuwa nahangaika kukutafuta! Upo
mzima?” Akauliza kisha akaongeza. “Ulifanikiwa
kujifungua salama?” “Ayvin anaumwa, ndio
maana nimekupigia.” “Ni nini tena?” Mina
akaanza kilio.
“Usilie niambie.” “Mtoto alikuwa mzima
kabisa. Akaanza kulia sana, halali. Nimemleta hapa hospitalini tokea
asubuhi ndio hatimae daktari amesema ana henia, wanataka kumfanyia upasuji.
Ndio nikasema nikwambie kabla hawajaanza kumkatakata.” “Sasa hivi anaendeleaje?” “Analia kila wakati mpaka amepata homa! Hanyonyi vizuri
tokea juzi. Analia tu. Yaani sasahivi ndio amepitiwa na usingizi. Amelala, tupo
hapa chumba cha daktari.” “Naomba kuzungumza na
daktari.” Mina akampa simu daktari.
Pius akazungumza naye kwa kifupi ila akajua walipo.
“Anataka kuzungumza na wewe.” Daktari akamrudishia simu. “Nashukuru kwa hatua uliyochukua, lakini tafadhali hapo wasimguse
kabisa mwanangu.” “Sasa nitafanyaje?!” “Kodi gari. Sogea mpaka Mtwara.
Nakutumia tiketi ya ndege, yako na ya watoto.” “Mimi nina msichana wa kazi
anayenisaidia watoto. Siwezi muacha. Kwanza bado mdogo, mama yake amenikabidhi.”
“Basi na yeye namkatia ticketi. Lakini Mina, lazima muondoke sasahivi ili
muwahi ndege, huyo mtoto atibiwe LEO. Yaani wewe ukiwa safarini, mimi nafanya taratibu
za madaktari huku ili mkifika tu, moja kwa moja twende hospitalini.
Usiogope, kila kitu kitakuwa sawa.” “Asante Pius.” Akamalizia taratibu
za hapo hospitalini huku akiwa amepiga simu kwa mama mwenye nyumba wake amsaidie
kuandaa safari.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mina anafika kwake, wapo tayari, wanamsubiria
kuondoka. Akawachukua mpaka Mtwara. Akamlipa huyo mama mwenye nyumba wake, pesa
yakutosha haswa, kama shukurani kubwa kwa mengi
aliyomfanyia kwa upendo. Maana na hapo napo alijitolea kumuendesha mpaka Mtwara
kumuwahisha uwanja wa ndege.
Hawakuwa wamechelewa sana. Wakaondoka na ndege ya
mwisho kutoka Mtwara kurudi Dar. Yaani safari ya Lindi mpaka Mtwara ikawa ndefu
kuliko ndege ya kuwatoa Mtwara mpaka Dar iliyochukua lisaa na dakika kumi tu,
wakati ya Lindi mpaka Mtwara ilikuwa lisaa na dakika 45.
Jijini Dar.
Alitoka uwanja wa ndege na wanae pamoja na msichana wa
kazi akakuta wanasubiriwa! Mpaka akatamani arudi ndani. Uzuri mtoto
alikuwa akilia. Pius akamuwahi na kumpokea mwanae, akaondoka naye
kabisa hapo akisikika akimbembeleza. “Pole Ayvin. Pole sana.” Akashika kazi ya
kubembeleza, Mina akamshika mkono Ayan na kumsogeza karibu yake hajui pakuanzia
na hao alio watoroka.
“Pole na kuuguza, mama.” Alikuwa mzee Ruhinda.
“Shikamooni.” Akasalimia. “Marahaba Mina mwanangu. Pole kwa kila kitu. Kujifungua
na kulea mwenyewe.” Alikuwa mama Ruhinda. “Asante. Ila Ayvin ndio
anaumwa, mama. Analala kidogo, anaamka na kilio. Hivi hapo homa imerudi.
Tulipokuwa hospitalini Pius aliwaambia wamuongezee dawa ya maumivu, naona
inaisha mwilini. Hali vizuri.” “Atapona tu. Hivi anasubiriwa huko hospitalini.”
“Asanteni na samahanini kwa kuwa…” Akasita na kunyamaza. Akamsogeza Ayan
karibu kama kujibaraguza
tu akimwangalia mwanae.
“Ayan njoo unisalimie.” Alikuwa Andy. Moyo wa Mina ukapasuka kama kulikoanguka chuma sakafuni. Mwanae akawa kama anasita.
Akazidi kujisogeza kwa mama yake. Mina akamwangalia. “Nenda kamsalimie dad.”
Ndio akaenda baada ya mama yake kumuhimiza.
“Wote mna afya nzuri. Hongera kulea,
Mina. Kumbe mwenyewe unayaweza bila msaada!” Akacheka kwa aibu. “Na umependeza
kweli! Uzazi umekupenda.” “Naombeni tuondoke jamani. Huyu anahoma kali,
inamaana ana maumivu makali.” Pius alirudi na mtoto aliyekuwa akiendelea
kulia.
Sababu ya mtoto kulia na ile hali pale akawa kama amechanganyikiwa
pale. Akajikuta anamfuata mtoto anayelia na kupanda kwenye gari, Ayan hayupo,
Ayvin analia, baba yake ndio anaendesha na mtoto mkubwa wa Pius, Poliny, yupo
pembeni. Akajua wamepatana na baba yake.
“Simuoni Ayan!” Mina akazungumza akimbembeleza mtoto.
“Atakuwa na Andy.” “Tafadhali naomba mpigie, nihakikishe Pius. Sina amani.”
Pius akampigia Andy. “Mina anataka kuzungumza na
wewe.” Akampa simu. “Samahani Andy, unaye
Ayan?” “Ninaye hapa na dada yake.” “Nashukuru. Naomba mwambie dada ampe maziwa
yake. Yapo kwenye thermos. Atakuwa na njaa. Alilala njia nzima
kutoka nyumbani mpaka hapa. Halafu akifika nyumbani amtengenezee chakula.
Asimuache hivyo mpaka nyumbani. Atateseka na njaa.” “Sawa. Nitahakikisha.
Nakushukuru Mina. Anaonekana na afya nzuri!” “Asante. Tutaongea zaidi baadaye.” Akamrudishia simu Pius.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Mina, una roho ya umama wewe! Unamtoto
anayelia maumivu na bado unamkumbuka kaka yake!” “Ayan ni mkimya
sana. Unaweza msahau chakula, na akanyamaza tu. Lakini huyu!
Mpaka majirani watajua kama humo ndani kuna njaa! Atalia kama kuna hatari
ya kifo, mpaka majirani wanamjua. Ukishasikia tu, ‘Mina, humo ndani kwako
hapaliwi leo?’ Ujue ni Ayvin ashasikika mpaka nje. Na kama ukitoka ukamuacha
amelala, kokote uliko ukishapata simu ukasikia, ‘kwako kuna njaa,’ ujue ni yeye ameamka, akajisikia tumbo lipo
tupu.”
Binti wa Pius akacheka sana akimwangalia baba yake.
“Sasa unacheka nini wewe?” Baba yake akamuuliza kama anayejua anachocheka. “Mimi
najua alikorithi huyu Ayvin. Pale ndani mpaka wasichana wa kazi wanajua.
Chakula kiwe kinamsubiria dad, sio yeye akisubirie. Hapo hapatakuwa
na amani. Muone dad mkimya hivyohivyo. Ila asiumwe na njaa. Bwana nyumba inakua ndogo, na hakuna
mtakalozungumza mpaka aone chakula mbele yake.”
“Basi ndio huyu. Kunakuwa kama kuna kipimo huko
tumboni kwake. Kikipungua tu, amani inapotea. Na nimchekaji huyo!
Mpaka nje mtamsikia akicheka. Ila njaa ikianza tu, basi. Hana urafiki.” “Sasa
kwa nini msubirie mpaka apatwe njaa? Kwa nini asiwe anakuta chakula kila
wakati?” “Bado ananyonya, na amekataa chupa kabisa. Nilijaribu kuwa
namkamulia, nikamuanzishia na chupa. Akishatia mdomoni, akakutana na plastiki
anatema, anaanza kulia. Na hatatulia mpaka umpe nyonyo.” “Kwamba bado
ananyonya tu mpaka leo!?” Dada yake akashangaa.
“Mimi nanyonyeshaga wanangu miezi sita bila
kuwapa kitu chochote ila maziwa yangu tu. Akishafikisha miezi sita kamili ndio
naanza kumuongezea vyakula laini taratibu. Miezi nane anakula kabisa.” “Unajuhudi
Mina, huchoki?” “Ndio umama, halafu naona kama wanakua vizuri kama Ayan. Hakuwa
mtoto mgonjwa mgonjwa ndio maana huyu aliniogopesha alivyoanza kuumwa.
Alikuwa mzima kabisa, hana ugonjwa hata wa mafua!” Wakawa wanaongea hapo nyuma,
Mina na mtoto mkubwa wa Pius. Poliny.
Hospitalini
Wakafika hospitalini wakakuta kweli wanasubiriwa.
Mpaka Paul mtoto wa mwisho wa Ruhinda alikuwepo hapo hospitalini akimsubiria.
“Pole sana Mina.” “Asante.” Akaishia kumjibu tu hivyo asijue pole hiyo ni ya nini kwa Paul aliyekuwa hayupo nchini
wakati hekaheka za kaka zake zikiendelea. “Kwamba shule ndio imeisha au?”
Akajiuliza ila alikuwa na mengi kichwani, akaangalia yake.
Baada ya muda mfupi kina Ruhinda wengine na mume wa
Paulina naye akawa ameshafika hapo. Wamejaa, Mina hajui kama wamemjalia
yeye au huyo mtoto aliyeondoka na mimba yake. Asijue ni mengi ya uzushi,
yanaendelea. Kila mtu alitaka kushuhudia, na kuthibitisha kama kweli
mtoto ni wa Pius!
Akaanzishiwa
vipimo vya harakaharaka na kumpa dawa ya kutuliza maumivu, akalala. Pius
alikuwa amembeba muda wote akimwangalia kama aliyeokota lulu!
Kwenye majira ya saa mbili, akawa anaingizwa chumba
cha upasuaji. “Naomba hata dakika moja tu, niombe naye kabla
hamjamuingiza huko.” Mina akawahi na kushangaza kila mtu. Ikabidi wote
watulie. Akainama kwenye kitanda cha mtoto wake aliyekuwa amelala. Akaanza
kuomba ila kimyakimya. Akaomba kisha akamaliza. Aliposema Amina kwa sauti ya kusikika kidogo, na wengine
wote mpaka mzee Ruhinda akasema Amen.
“Afadhali umekumbuka kuomba Mina. Wote naona tumechanganyikiwa.”
Akaongeza mama Ruhinda wakimwangalia Ayvin. Ndipo akaingizwa chumba cha
upasuaji.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akamsogelea Pius. “Nisaidie tena simu, nizungumze na
Andy.” Akamnong’oneza ila wote wakasikia. Pius akapiga na Andy akapokea bila
kuchelewa, akamkabidhi simu. “Nimemchelewa kaka
mkubwa?” “Naona alikuwa akiogeshwa. Hivi nilikuwa nasubiri amalize, nimuage,
nije huko.” “Naomba kuzungumza naye. Niwekee video.” Akasogea pembeni.
Akamsikia akitembea kama anayewafuata. “Mama anataka
kuzungumza na wewe.” Akampa na kumuona. “Umekula
vizuri?” Akamuuliza kwa upendo. Akakubali. “Maziwa?”
Akanyamaza. Akamuuliza tena, akamuona na yeye anamwangalia dada yake. “Nipe dada nizungumze naye.” Akampa. “Mbona kaka hana maziwa?” “Tulikutana na foleni njiani,
amemaliza yote, naona alikuwa na njaa.” “Sasa kwa nini usimuombee hapo maziwa?
Hawezi kulala vizuri.” Kila mtu akawa anasikiliza japo alikuwa pembeni.
“Hapa ugenini dada, sijapazoea.” “Naomba
kuzungumza na baba yake.” “Nimesikia Mina. Naenda kuangalia kama kuna maziwa,
lasivyo itabidi nikanunue.” “Maziwa yapo.
Mwambie dada ampe. Yapo kwenye friji. Tukiwa tunarudi tutanunua mengine.”
Akageuka, alikuwa mama Ruhinda. “Asante mama na samahani kwa kuwaharibia
bajeti. Lakini Ayan bila maziwa, hapapambazuki vizuri.” “Bado mpenzi
wa maziwa tu?” “Naona ndio vinazidi!” Akamjibu mzee Ruhinda na kurudi
kwa Andy.
“Andy?” “Nimesikia. Wakati wanampa haya,
nitaenda kutafuta mengine ili na kina mama wasiishiwe na kesho akute mengine.”
“Nakushukuru. Basi naomba nimuage kabla hujaondoka.” Akamrudishia simu.
“Watakupa maziwa. Sawa?” “Unarudi saa
ngapi?” Wakamsikia
akimuuliza mama yake. “Ayvin
akipata tu nafuu, narudi naye. Usiwe na wasiwasi. Sikuachi. Sawa?” Akakubali. “Haya, funga macho
tuombe. Leo si unaomba wewe?” “Nimuombee na Ayvin?” “Utafanya vizuri.”
Wote wakatulia. Akaomba kwa kifupi akimuombea mdogo wake mpaka msichana wao wa
kazi. Akamaliza.
“Asante Ayan na nitamwambia Ayvin kwamba
umemuombea.” “Atapona haraka?” “Kwa maombi hayo! Lazima atapona tu. Kunywa
maziwa, ulale.” “Lakini utarudi kunichukua na mimi tuwe wote na Ayvin.”
“Sikuachi Ayan. Mtoto akipata tu nafuu, nakuja kukufuata. Usiogope. Sawa?” Akakubali lakini wazi akionyesha mashaka, lakini
ikabidi amuage tu, na kukata. Kila mtu akakutana na Mina wa tofauti.
~~~~~~~~~~~~~~
Akamrudishia simu Pius. “Asante.” “Karibu. Upo sawa?
Hata chakula wewe mwenyewe umekula?” Akakumbuka jali ya Pius. “Nimeshindwa!
Nina hofu tokea jana hata maji hayapiti kooni. Acha nipate muda nimuombee
mwanangu.” “Subiri kwanza Mina! Wewe unanyonyesha halafu huli!?” “Hanyonyi! Ndio
kitu kinanitia wasiwasi hata dokta kule nilimwambia. Ayvin ni mlaji
haswa, na mchekaji akiwa ameshiba. Kitendo cha kukataa kula
halafu analia tu, siwezi kufikiria. Halafu mwanangu hajawahi ugua hata
mafua! Leo wanaenda kumkatakata!”
Pius akakwama.
“Usiangalie kwa njia hiyo, mama.” Akamsikia
mzee Ruhinda, akageuka. “Huko alipo jua wanamsaidia kurudia hali yake. Kisu ndio njia ya kumfanya arudi kwenye hali yake.
Na nakuhakikishia yupo kwenye mikono salama sana. Na watamuwekea
maji ya kumpa nguvu. Atapona kwa haraka sana. Usiogope.” “Asante baba.
Acha tu nimuombee japo kidogo labda na mimi nitatulia. Sijui kwa
nini, nimeingiwa na hofu kweli!” “Ni roho ya umama hiyo. Pole sana, Mina
mwanangu. Atapona tu.” “Asante mama.” Akaenda kutafuta sehemu ya peke yake,
pembeni kabisa, akaanza kuomba kimyakimya bila hata kutoa maneno, akiwa
amejiinamia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya muda daktari aliyekuwa akimfanyia upasuaji
akatoka. Wote wakamsogelea. “Kila kitu kimekwenda salama?” Pius akawa wa kwanza
kuuliza. “Safi kabisa na…” “Subiri kwanza. Ngoja nimuite mama yake akusikie.
Maana ana wasiwasi sana.” “Lakini niliwaambia msiwe na wasiwasi
ni procedure ya muda mfupi na sahihi.” “Hayo hawezi sadiki
mpaka kwa vitendo. Acha tu aitwe.” Mzee Ruhinda akaingilia. Pius akaenda
kumuita pale alipokuwa amejiinamia.
Akasogea. Akawaelezea kwa kifupi. “Na kama tulivyozungumza,
ili asirudie maumivu kwa mara ya pili, tumemfanyia na tohara kabisa.”
“Ni Pius huyo anayetaka mambo yote, kwa wakati mmoja, wakati mtoto mgonjwa!
Sasa si atakuwa na maumivu makali?” “Hata kidogo. Kila kitu kimeenda sawa. Tumemuweka
kwenye usingizi kwa muda, ili asijitoneshe.” “Sasa yuko wapi?” “Wanamalizia,
wamtoe.” Hapo Mina akavurugwa.
“Kina nani tena wanammalizia wakati wewe ndio tumekuamini
naye? Hao wanao mmalizia wakiharibu!?” Wakajua ni hali ya umama na kutoelewa.
“Ni utaratibu wa kawaida Mina! Huyu kazi yake imeshaisha. Lazima apishe
wataalamu wengine wafanye huduma nyingine kwa Ayvin.” Paul daktari wa familia
akajaribu kumuelewesha. “Kwanza hapo palipobakia hakuna kuharibika tena.
Yupo kwenye mikono salama.” Akazungumza na tabasamu kubwa tu kumfariji, haikusaidia.
Mina mashozi mpaka kifuani. “Mimi
sijazungumza na mtu mwingine akanielewesha na kumuelewa mtoto wangu kama
wewe. Hawajamshika mtoto wangu kwa upendo kama wewe kabla
hawajamuingiza humo ndani. Wamekutana naye tu humo ndani, hawamjui na hawaelewi
ni nini kinaendelea. Wataanza…” “Nakuomba, rudi tu ndani. Tafadhali
dokta Patel. Labda ukitoka naye, utatuliza hii hali.” Mzee Ruhinda akamsihi
kwa heshima sana. Huyo daktari wa kichotara
akakubali kwa heshima ya hao kina Ruhinda, akarudi japokuwa ni kweli kazi yake
ilishaisha.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya muda kweli wakatoka naye akiwa anasukumwa na
manesi, amelala. “Alivyo hivyo, isikutishe. Daktari wa watoto ameshauri
aongezewe dawa ya usingizi ili atulie. Lakini tulishamuamsha ndani baada ya
kumaliza kila kitu. Na nimchekaji sana.” “Hapo nimekuamini. Ayvin
ni mchekaji kwa kila mtu. Na inamaana maumivu yamepungua.” Mina akadakia
akionekana amefurahia.
“Asante sanaaa. Nashukuru.” “Nitapita baadaye
kuwaona. Ila daktari wa watoto atakuja kuzungumza na wewe. Lakini watamuweka
kwa uangalizi angalau mpaka kesho ndipo tutawaruhusu.” Akaondoka na wao
wakarudishwa chumba cha kupumzika upande wa watoto.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Walipomuweka tu kitandani wote wakamzunguka
akiwa amelala. “Ruhinda una damu kali! Damu
yako haipotei kabisa! Japokuwa huyu ana rangi tofauti, lakini hajifichi
kabisa kama ni Ruhinda!” Akaongea mama Ruhinda wote wakimtizama hapo kitandani
kama wapo kwenye kivutio cha
wanyama! Kila mtu yupo kuthibitisha maneno yaliyozagaa juu ya
Mina aliyeondoka na huo ujauzito.
Raza aliwahakikishia kuwa alikimbia
baada ya kuona atakamatwa uongo, mtoto si wa Pius. Na shutuma nyingine
nyingi tu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mzee Ruhinda wazi alikuwa na furaha sana. “Na
anaonekana na afya nzuri kweli!” “Mlaji huyo! Na hana neno na yeyote labda awe na njaa, hapo haelewani
na yeyote mpaka mimi nimshike. Mchekaji haswa. Yaani huwa
akipitiliza usingizi, mimi na Ayan tunaenda msubiria pembeni ya kitanda
aamke aanze kucheka. Na akifungua tu macho, akituona mimi na Ayan, anaanza kucheka
haswa. Analeta furaha huyu, mpaka raha.” Mina akamsifia mwanae.
“Ni kama tu baba yake. Pius alikuwa hivyohivyo, mtoto asiye
na shida.” “Sasa nani aliyekuwa na shida?” Paulina akauliza na kufanya
waanze kucheka. “Kuna waliokuwa wakitaka kuwa mikononi wakati wote.
Hawawekeki chini.” “Labda Paul.” “Mimi nilishaambiwa nilikuwa mtoto ninayependa
kujitegemea.” Paul akajiwahi. “Huyo ni Andy. Alijua kujitegemea
mapema sana.” Mzee Ruhinda akarekebisha kwa haraka sana na kufanya
wacheke tena.
“Inamaana waliobaki hapo ni Paulina na Paul.” Mumewe
Paulina akaongeza. “Sasa mwenye ufahamu atambue. Ambaye hapendi
kuwekwa chini mpaka leo ni nani, na ambaye yupo na mama mpaka kesho,
basi ndiye huyohuyo.” “Paul unanitafuta wewe!” “Kwani mimi nimemtaja mtu jina?”
Vile ambavyo wazazi wao hawakukanusha tena wakajua ni yeye Paulina.
Wakazidi kucheka.
Andy Kwa Mkewe.
Wakati wakiendelea kuzungumza Andy akaingia. Moyo wa Mina
ukajawa furaha, wote wakamuona anamsogelea mumewe. Angalau Andy
akajisikia umuhimu. Wote wakawageukia. “Poleni.” “Asante. Naona kila
kitu kimeenda sawa. Wamempa dawa ya usingizi ili alale asijitoneshe.”
“Pole kuuguza na kulea.” Akaendelea kuzungumza na mkewe taratibu wakiwa
pembeni.
“Hatukuwa na matatizo mpaka majuzi alipoanza
kulia mfululizo na hataki kula. Vinginevyo wote ni watoto warahisi
kulea.” “Acha nimuone. Amefungua hata macho?” Akasogea, wakampisha kama kumpa
nafasi wasiamini kwa hatua kubwa anayotaka kuchukua! Hata Mina alifurahi
kumuona anataka kumuona Ayvin.
“Hapana. Wamempa dawa ya usingizi ili apumzike.
Hata hivyo anaonekana alilia sana. Mpaka homa!” Baba yake akajibu macho kwa
mwanae. “Aisee mmefanana! Hajachukua rangi kali ya baba,
aliyotupa sisi wote kasoro wewe Pius.” Pius akacheka wote wakimwangalia huyo
mtoto. “Na naona yeye atakuwa na mwili
sio kama miili yenu hiyo mikavu
mtafikiri hamlishwi!” “Watoto wanabadilika mama! Anaweza kuja kurudi
kwetu tu.” Paul akadakia.
“Na anakula huyu! Mkianza kulishana
mpaka mgongo unauma. Na haachii mpaka amalize maziwa yote.” “Ndivyo
wakina Ruhinda walivyo. Sasa mimi huo mchezo kama wako nilikuwa sifanyi. Kwanza sikuwa na maziwa mengi hivyo
yakuwatosha. Miezi mitatu tu, ziwa peke yake. Matenity leave yakiisha, nikiwa narudi kazini, week moja kabla nilikuwa nawaanzishia maziwa ya chupa.”
“Hivyo niliweza kwa Ayan wangu, hakuwa na neno. Huyu, hataki
kabisa. Akishajua umemuwekea plastiki mdomoni, ndio hasira
zinaongezeka. Atalia hapo kama amekatwa!” “Basi atakuwa kama baba.”
“Wewe mbona umenikazania mabaya yote ni mimi?” “Muulize bibi. Dad
anasahani yake, kijiko, uma na kisu maalumu vya kulia. Visibadilishwe.”
“Na sehemu anayokaa wakati akila, iwe hiyohiyo.” Mama Ruhinda akaongeza. “Na ni
kwenye kila nyumba, iwe hivyohivyo mpaka tushamzoea Pius. Kila nyumba
anaachiwa kiti chake kama baba!”
“Basi kazi itakuwepo!” Mina akaongeza. “Wala si
kazi. Ni mambo ya kawaida tu. Na yeye atafika hatua ataelewa anatakiwa
kutumia chupa. Au kula vyakula vingine. Taratibu si kumuharakisha.
Atazoea tu.” Pius akaongeza wote macho kwa mtoto.
“Umemuacha Ayan amelala?” “Anawasiwasi huyo!
Sijui kama atalala kwa haraka.” “Alipewa maziwa?” “Alipewa, lakini nayo ikawa
kama hana raha nayo! Kila wakati anauliza kama utarudi kwenda kumchukua.”
Mina akatulia na kurudisha macho kwa Ayvin. Wakatulia.
~~~~~~~~~~~~~~
“Nimekuletea chakula ule. Msichana wako ameniambia
hujala tokea majuzi.” “Asante kunifikiria Andy. Yaani sasahivi ndio nasikia njaa baada ya kumuona Ayvin ametulia.” Wote wakajisuta,
walikuwa naye huyo mama mtoto hakuna aliyekuwa akimfikiria chakula mawazo yao
yote kwa mtoto japo alishasema alishindwa kuweka chochote mdomoni.
“Basi, kaa ule.
Nimekuletea na nguo za kubadili ukioga. Msichana wako amenipa.” “Nahisi
wewe umetumwa na Mungu wangu. Asante Andy, mume wangu.” Andy alitamani kurukaruka kwa furaha. Pius wivu.
Wengine kimya.
“Naona acha nioge kwanza, maana tokea asubuhi
nilipotoka nyumbani sijatulia, na taskii yenyewe niliyokuwa nimepanda asubuhi
mpaka nilishindwa kuweka pochi chini, ilikuwa chafu! Nilibaki nimepakata
mtoto na pochi zangu.” “Pole.” Andy akaonekana kujali kweli.
“Itabidi uwe na gari yako. Ninunue
haraka iwezekanavyo.” Hapo AKAMTIBUA Andy.
“Umnunulie wewe kama nani?!” Chumba kizima kikataharuki jinsi alivyouliza. “Mimi kama Pius na baba
yake Ayvin ambaye hilo jina nilishaomba lisiitwe hivyo aitwe Pius
Junior Ruhinda. Lakini wewe…” “Nisikilize Pius. Mina ni mke wangu na
anayo gari ambayo mimi nilishamnunulia.” “Mwanangu ataishi kwa uwezo
wangu sio kwa uwezo wako Andy. Hawezi kuendesha gari ya miaka
ambayo hata mtoto wangu hakuwa amezaliwa! Kwa nini haswa?” “Mmeanza!
Nyinyi wawili mmeanza.” “Hayakuhusu Paulina.” Wote wawili
wakamchangia kwa pamoja. Wazazi wao kimya. Mina akabaki ameduaa.
Kuliko Ungua Mpini.
Ilimuia ngumu
kwa Pam kupata usingizi lakini mwishoe akalala mpaka pakapambazuka
kabisa. Kimya. Mill hata hakuwagongea. Pam alioga akajitengeneza vizuri mpaka
saa nne, kimya. Mwanae bado akawa anakoroma tu. Ikabidi ajitulize akijua fika
Mill ameamka. Shuguli zake hufanya asubuhi na mapema.
Kwenye saa tano
hivi ndipo Shema akaamka. Akaoga na kuvaa ndipo yeye akaenda kumgongea baba
yake. Na kweli alimkuta alishavaa. “Njaa inauma baba!” “Nilikuwa
nikiwasubiria nyinyi. Kama mama yako yupo tayari mwambie tutoke tukale.” Shema
akatoka kwa haraka wakati baba yake akimalizia kufunga kompyuta zake.
Pam akaenda
kumgongea na kuingia. “Nilijua bado umelala!” Akajizungumzisha. “Mimi nilazima
niamke mapema. Hapa nimeshaenda mazoezini, nishafanya na kazi zangu, sasahivi
nipo huru kwa siku nzima.” Ndipo akamgeukia. “Umependeza Pam.” “Asante.
Na wewe unaonekana msafi!” Akasimama. Ukweli alivutia, halafu akawa ananukia
vizuri. Ila akawa kama amebadilika kidogo si kama alivyokuwa jana yake.
Shema akarudi.
“Nimeshabadili viatu, mama.” “Basi twendeni.” Wakazunguka hiyo siku sehemu
ambazo alijua wazi zimemgarimu mno. Ukweli akawa ametulia kwa Pam
tofauti kabisa na jana yake. Mazungumzo mengi yalikuwa kati yake na mwanae.
Mpaka siku ikaisha. Walirudi hotelini usiku wakiwa wamechoka.
~~~~~~~~~~~~~~
“Nashauri tuwahi
kulala ili kesho tuwahi kuamka kwa safari ya mbugani.” Hayo anawaambia
wakiwa kwenye lifti. Akawasindikiza mpaka mlangoni, hata ndani hakuingia,
walipoingia tu ndani na yeye akaingia chumbani kwake kwa mlango wa nje wala sio
ule wa ndani unao ingiliana nao. Pam akajua amembadilikia.
Kimya. Akaoga
yeye na mwanae na kulala. Kimya mpaka tena kesho yake. Pam alitegesha alamu ya
kumuamsha, akajitayarisha yeye ndipo
akamuamsha na mwanae, alipomaliza ndipo akamtuma akamgongee baba yake. Akakuta
yupo tayari mpaka na masanduku. Wakatoka na kupata gari ya kuwapeleka mbugani.
Ilikuwa bado mapema tu. Wakawa na muda mzuri huko mbugani ndipo safari ya
kurudi Dar siku inayofuata ikaanza.
Safari yakurudi
Dar.
Safari hii
kurudi Dar haikuwa imejaa furaha kama walivyokuwa wakielekea Arusha.
Walisimama kila walipotaka kula na kujisaidia, vinginevyo aliendelea kukanyaga
mafuta mpaka nyumbani kwao. “Kesho nitamtuma dereva aje amfuate huyu, akakate
nywele. Zimeanza kutisha.” “Sawa.” Akawasaidia mizigo mpaka ndani na kuondoka
bila ya kukaa wala kuzungumzia swala la kuhama. Pam naye akaona atulie.
~~~~~~~~~~~~~~
Juma likaisha, kimya.
Hakuna kuulizwa lolote juu ya kuhama wala kazi. Na akawa
akimtuma tu dereva kumchukua Shema na kumrudisha mpaka shule ikafunguliwa. Hakumuona
wala kumsikia Mill. Ila alijua anazungumza na mwanae.
Safari hii
dereva ndiye aliyekuwa akimfuata Shema kumpeleka shule, na kumrudisha. Mwezi ukaisha,
KIMYA. Yeye hajamtafuta, na Mill hajamtafuta. Ila Shema alikuwa
akimwambia kama huwa baba yake anamfuata shuleni mida ya chakula cha
mchana na kula naye kisha anaondoka.
Pam akabaki njia
panda. Hakuna mawasiliano kati yao, ila anatunza mtoto wake vizuri tu.
Na pale kwake hakuonekana tena tokea alipowashusha siku alipowarudisha toka
safari. Wasiwasi ukamzidi Pam. Ila akajikaza.
~~~~~~~~~~~~~~
Miezi 3 ikapita,
hajamuona wala kuwasiliana. Akazidi kummiss ila hajui anajirudije.
Alipoona muda aliombiwa wa kumpumzisha mkono umeisha akaanza kutafuta kazi.
Alihangaika Pam mpaka akachoka, kazi hapati.
Usiku huo
akaamua kumtumia ujumbe. ‘Samahani kukusumbua Mill. Nakujulia hali na pia kuulizia ile nafasi
ya kazi kama bado ipo? Mkono ulishapona na ninaweza fanya kazi.’ Akatuma huo ujumbe. Akaona umefika. Ila hata haukusomwa.
Kesho yake
kwenye majira ya saa nne asubuhi akapata majibu. ‘Huku kwema kabisa. Nilipoona
kimya, nikajua huhitaji tena. Nikatafuta mtu wa kuijaza ile
nafasi. Nilikuwa na uhitaji ambao sikuweza kuendelea kusubiri zaidi.’ Pam alipoa, mpaka akasikia baridi mwili mzima. Akarudia ujumbe tena na
tena ukawa umeishia hapo. Mwanae alikuwa shuleni.
Akafikiria kwa
haraka, akamrudishia mwingine. ‘Nina shida sana na kazi Mill. Ikitokea unasikia
nafasi popote au kwako kukifunguka tena nafasi utakayodhania naweza fanya,
tafadhali nikumbuke.’ Mill akasoma akajua inamaana ametafuta
kwingi amekwama na amefika mwisho. Pam si wakujishusha. Ni
jeuri. Na alimjua. Akamjibu kwa kifupi tu. ‘Sawa.’ Ukaishia hapo.
~~~~~~~~~~~~~~
Mwezi mwingine
tena ukaisha kimya. Minong’ono uswahilini ikazidi, kuwa ameachwa.
Wakasahau yote, ikawa sasa eti alipokutwa Mgaya chumbani kwake, eti ni kufumaniwa.
Baba Shema hamtaki tena, anatunza tu mwanae. Pale alipokuwa akiishi
pakaanza kuwa pachungu. Kina mama Pili wanamsema mpaka kwa
majirani kwamba walimuonya, lakini amefanya kichwa ngumu mpaka akaachwa.
Pam akanyong’onyea haswa.
Muda huohuo
na Shema naye akawa anafunga shule kwa mapumziko
mafupi. Akarudi na bahasha. “Baba amesema usome, ukiafikiana nayo,
nimjibu.” Akafurahia akijua ni kazi. Akafungua kwa haraka akagundua ni kuhusu
huyo Shema. Amemtafutia kikundi cha mpira wa miguu anataka ajiunge.
Alipoa Pam, asiamini. Safari hii akaamua kujishusha.
Akamtumia
ujumbe. ‘Nafikiri hii timu ya mpira itamsaidia na kumuongezea
ujuzi zaidi. Nashukuru kumfikiria. Na muda na wakati wowote anapohitajika
kwenda, nitajitahidi awe tayari.’ Baada ya muda
majibu yakarudi kwa kifupi. ‘Sawa.’ Pam akazidi kuumia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Aliyoyakimbia Ndio Anakutana Nayo Siku Ya Kwanza Mtoto Akiwa Mgonjwa Hata Hajafungua Macho Baada Ya
Upasuaji.
Ila HISIA Kwa Mumewe Bado Zipo
Wala Si Za Kulazimisha, Na Andy Bado ANAMPENDA sana na anaonekana KUMUHITAJI mkewe.
Ila Bado Pius Yupo Kwenye Picha, HAKWEPEKI Tena, Maana Na Ayvin naye Yupo.
Mill&Pam Bado Wanahangaika Kurudi Mwanzo.
Wivu, Kujihami, Hofu
Ya Kuumizana TENA, Jeuri, Kila Mmoja Ameshika Pakali Japo Penzi Lipo,
Lakini Uharibifu Ulishatokea. Ni Kama Washapoteza Dira.
Ni nini
Kitaendelea kwa wote Love At First time?
0 Comments:
Post a Comment