Alipofika nchini
Marekani tu, baada ya mapumziko ya siku mbili akakutana na mwanasheria wake.
“Nina wazo ambalo naomba tujaribu. Mtafute mwanasheria wa Kisha. Muombe kikao
na sisi, ila mwambie lazima Kisha awepo. Mimi nitazungumza na Kisha. Kwa sehemu
fulani najua udhaifu wake, tunaweza kuutumia.”
“Kisha bila kumtisha
hawezi kutulia na kukusikiliza.” “Wewe usiwe na wasiwasi kwa sababu katika hili
nina uhakika alikuwa akijua analofanya. Sio bahati mbaya. Sitaki kukaa
sana huku. Natakiwa nyumbani kwa haraka. Vinginevyo tukifuata taratibu za
kawaida, nitajikuta nakaa huku muda mrefu.” “Basi nashauri angalau ufanye
vipimo hata vya huku. Vyenye uhakika kabla hujazungumza naye.”
Akafikiria, akaona hana la kupoteza.
Safari hii
alikwenda na hao watoto hospitalini kabisa. Wakafanyiwa vipimo. Aliambiwa
itachukua majuma matatu. Akatulia lakini akiendelea kuwasiliana na Shema kwa
shida kwa sababu ya network huko kijijini kwa kina Pam. Akajitahidi
mwanzoni na hivi mida inatofautiana, Tanzania walikuwa mbele kwa masaa nane!
Mwishoe mawasiliano yakakata kabisa. Pam akajua ndio ameshakutana na wakimarekani
tena, habari yake imeisha. Akapoa akijutia hili na lile.
Mill
Apoteza Yote Aliyohangaikia Nchini Marekani.
Baada ya majuma
matatu kwenda la nne majibu yakatoka kama ya Tanzania. Watoto hao wawili hawakuwa
wa Mill. “Sasa mtafute mwanasheria wake. Mwambie ni muhimu tukutane
kabla sijawafungulia mashitaka.” Mwanasheria wa Mill akafanya hivyo.
Kisha kusikia kuna mashitaka, akakubali kukutana kwa haraka sana,
hakujua anataka kumshitaki kwa lipi tena. Maana wawili hao walishindana
kwa kushitakiana.
Mwanzoni ilikuwa
ni Kisha akimtishia kwamba atamsema kwa Uhamiaji kuwa alimlipa pesa ili
ampe uraia, lakini baadaye Mill akafikiria na kumgeuzia na yeye
kibao kuwa atamshitaki kwa kumuomba RUSHWA ampe uraia. Na
ushahidi ni pesa alizokuwa akimpa na kupokea. Katika hilo Kisha akatulia.
Mill&Kisha
Siku wanakutana
Mill alihakikisha anakuja na wale watoto na mizigo yao yote ili ikitokea tu
Kisha anakubali amkabidhi watoto wake hapohapo. Ila chakushangaza wakati
wanajipanga kumtisha, Kisha alizungumza bila shida kuwa, “Itakuwa ni
watoto wa Trey tu. Maana tulikuwa na mahusiano ya muda mrefu sana, kabla
hajanitapeli na kukimbia.” Mill akaumia sana. “Kwamba wakati upo na mimi
pia ulikuwa na Trey!?” “Hatukuwahi kuachana!” Alijibu Kisha bila
wasiwasi maana ni kweli ilikuwa ni ndoa ya mkataba.
Mill hakutaka
mengi. Akamkabidhi kila kitu cha hao watoto. “Ila huwezi kurudi
kinyumenyume na kudai mali ulizokuwa umeniachia. Maana tulikabidhiana
kwa mkataba. Wewe mwenyewe uling’ang’ania watoto. Sikukulazimisha.
Na hata hivyo ni kama tuliuza kila kitu.” “Kwamba na ile nyumba pia
umeuza, Kisha!?” “Wewe ulitegemea niendeshe nyumba kama ile kwa pesa
gani!?” Mill hakutaka kumjibu. Kwa asilimia fulani alitegemea, hakuwa na
uwezo wa kiakili ya kumiliki mali zote hizo. Alijua tu ni shindikizo
kutoka kwa Trey. Na alijua wazi, nia ya Trey ni badaye kuja kumtapeli
kama hivyo. Wakafanya makubaliano na kuandikishana tena.
Akaondoka hapo akiwa kama ametua MZIGO. Ila hangaika yote nchini Marekani
ikawa imeishia kwa Kisha. Mali karibia asilimia 80 alizokuwa
amehangaikia nchini Marekani na kulipa garama kubwa sana mpaka
mahusiano yake na watu wake wa karibu akiwemo Pam, viliishia kupotelea
kwa Kisha. Na watoto walio mgharimu pia wakaishia kwa
Kisha. Aliondoka hapo akijua ndio amebakiwa na Shema tu.
Mtakuja.
Akarudi nchini
na kuanza kuweka nyumba yake kama mseja sasa. Alihakikisha vile vitu vya
wale watoto vyote, haachi hata karatasi yao. Akasafisha na kupaka rangi ya
nyumba nzima, maana vyumbani mwao aliwapakia rangi zile walizotaka wao,
wale watoto. Ilimradi tu kuwapa mazingira mazuri watulie, lakini hakuna walichothamini.
Kukabadilishwa mpaka mashuka, vikabaki vyumba vilivyo safi ila vitupu kabisa
ndipo akatulia.
Alifanya shuguli
zake. Akaweka mambo yake sawa ofisini ndipo akajiandaa na safari ya Mlalo,
Lushoto, alipo Pam na kijana wake. Akajifungasha kweli. Vyakula na
zawadi za wakwe alizowanunulia pia kutoka nchini Marekani, pamoja na vitu vya
Shema. Mapigo ya ukweli na nguo za michezo. Safari hii hakumsahau Pam.
Ila yeye na mwanae aliwabea vitu baadhi vingine akaacha kwake.
Mapenzi!
Aliondoka mida
ya mchana tu. Hakuwa na haraka na wala hakuwataarifu kama atakwenda.
Alishamuuliza yule dereva aliyewapeleka. Akamkumbusha njia vizuri. Akaenda moja
kwa moja mpaka alipofika kijijini kwao ndipo akaulizia nyumbani kwa mzee
Shelukindo. Ilikuwa rahisi maana alishafika huko alipokwenda kulipa mahari
na kufanyiwa hiyo harusi ya kimila.
Ilikuwa majira
ya saa mbili usiku wakati Mill akibisha hodi hapo kwao. Walikwisha kula
mapema tu, wakabaki wakizungumza sebuleni, Pam amepakata kichwa cha mwanae
anasinzia. Babu yake Pam ndiye aliyekwenda kufungua.
Kwanza
hakuamini. “Ni mimi Mill, mume wa Pam.” Alishituka Pam, hakutegemea!
Mwili mzima ulikufa ganzi. Akabaki kama ametolewa kwenye barafu. Shema
akashituka usingizini na kukimbilia mlangoni. “Baba!” “Sasa wewe utamuangusha
babu yako, vipi wewe!” Bibi yake akamwambia Shema aliyempita babu yake hapo
mlangoni. Na yeye alimuita babu kama mama yake.
Akakaribishwa
ndani, Pam akabaki amekaa vilevile amekufa ganzi. Hata hakusogea wala
kuzungumza. Yeye na mwanae walikuwa wamekaa tu chini kwenye mkeka.
Pakachangamka
hapo. Maana taarifa za kurudi kwake nchini na kuwa anawatunza
hao, zilitangulia hata kabla mwenyewe hajafika. Ikawa kama ameingia mungu
mtu! Akasalimia wote kwa kuwapa mkono, kisha akaenda pale alipokaa Pam. Alimjua
anavyokuwa. Mbaya wa kuagana na kumpokea. Hapo tayari machozi
yalikuwa yakimtoka.
Akaenda kumbusu
pale apendako Pam, kusudi tu. Chini ya shavu, kwenye shingo. Ili
kupafikia hapo, basi uso wake huenea vizuri kwa Pam na kumsikia hapo shingoni.
Sasa akimbusu ndio hummaliza kabisa. Akamuona machozi yakimtoka.
“Nimerudi mama.” “Nilijua umetusahau!” Pam akalalamika
akilia. “Nawezaje?! Network ilikuwa ikisumbua. Hatupatani
na Shema. Mwishoe nikaona namchosha tu. Kwanza mida haikuwa ikiendana!
Nikahisi usumbufu tu. Nampotezea muda wake. Pole.” Akamfuta kabisa machozi hapo
mbele ya wakweze. Akajisikia vizuri huyo! Alijua keshaachwa.
“Pole na wewe
kwa safari. Umekula?” “Nilinunua nyama choma nyingi, na ndizi za kukaanga
anazopenda Shema na za kuchoma. Vipo kwenye gari. Ukiniongezea nyanya na tango,
hapo utanikamilishia.” “Kuoga kwanza au kula kwanza?” “Kabla ya kushusha mizigo
ndipo nile kisha kuoga, halafu kulala,
naomba kuzungumza na wazazi kwanza.” Pakatulia kabisa kumpa nafasi
yakumsikiliza.
“Niombe radhi
wazazi wangu kwa kilichotokea kati yangu na Pam. Nakumbuka kuanza vizuri
nikisindikizwa na baba yangu mzazi. Lakini katika juhudi za kumleta Pam kule
nchini Marekani, ndipo mambo yalipo haribika.” Akawasimulia kwa kifupi
jinsi ilivyokuwa. “Na kwa hakika sikujua kama nilimuacha Pam akiwa mjamzito.”
Hapo napo akajieleza. “Nilikosea tangia mwanzo, nimekosa, naomba mnisamehe
wazazi wangu. Najua hata nikitoa sababu nzuri za namna gani, hazitabadilisha
nilichokifanya kwa Pam na kuwafedhehesha hata nyinyi wazazi wangu.”
Hapo akajinyenyekeza karibu apige goti.
“Mnisamehe. Najua
nilimtelekeza vibaya sana. Tafadhali wazazi wangu, mnisamehe.” Wazee
wenyewe hawakuwa hata na neno. Babu yake Pam ndio kabisa. Kwake ilikuwa kama MUUJIZA. Binti yake alitelekezwa akiwa
ameolewa ndoa kama hiyo ya mjukuu wake na kanisani kabisa. Akarudishwa
hapo na watoto wawili, mume hajawahi kurudi tena! Sembuse huyo mjukuu!
Amemzalisha na ameshajua anamtunza mtoto wake kwa garama kubwa hivyo! Mzee
Shelukindo akasamehe kabisa na kumshukuru kwa yote anayoyafanya. Mill
akasimama kabisa na kuwapa mkono hao
wazee kila mmoja kisha kuendelea.
“Kipekee
nikushuru mama kusimama na Pam tokea ni mjamzito. Najua ilikuwa fedheha
kubwa lakini ulimbeba yeye na mtoto kwa kadiri ya uwezo wako, bila kumtelekeza!
Leo Shema anao msingi mzuri wa kielimu ni kwa sababu ya msingi ulioweka wewe,
kwake tokea mdogo kabisa! Na anakutambua kuwa wewe ndio chanzo cha
kufanya kwake vizuri shuleni japo imekugarimu kusimama na hawa
wawili. Umepoteza heshima kwa wengine kwa sababu ya kusimama kwenye
nafasi yangu! Nakushukuru na hakika nitakuenzi mama yangu, daima.
Asante sana. Tena sana.” “Karibu sana. Na tunashukuru kwa kurudi.
Maana ungeweza potea na wala tusijue ulipo. Karibu tena. Na ujisikie upo
nyumbani.” Akasimama na kumpa tena mkono.
“Maadamu mmenisamehe
na kunikaribisha tena, sasa naweza shusha mizigo yangu, nikaribie
rasmi.” Pakachangamka hapo. Maana zawadi zilizokuwa zimeletwa, nyumba ilijaa uhai.
Kila mtu alijazwa zawadi zaidi mama Eric, kama kumshukuru na kumuomba
msamaha. Vyakula pia ni kama alijazilizia tena palipokuwa kumepungua pale Pam alileta.
Pakajaa shamrashamra kila mtu akihangaika pakuweka. Nyumba yenyewe
haikuwa imechoka. Kawaida ya kijijini. Ya bati na vyumba vinne, alijenga mjomba
wake Pam. Na hivi huwa anakujaga likizo na mkewe na watoto, walipaweka aghueni
pakijijini.
“Hii hali ya
hewa huku, mnaweza nifukuza.” “Kweli baba! Na vumbi hili!” Akauliza mama
Eric kwa heshima. “Kabisa mama. Joto ni adui yangu mkubwa na wa kwanza.
Ila ukiniweka sehemu kama hii, naweza hata kufikiria jambo,
likafanyika.” Shema alishakula, lakini hapo akaanza kula tena. Nyama ya kuchoma
tena! Alianza upya. Wakaendelea kula wakati Pam akimwandalia chumba.
~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya yote
akapelekwa bafuni, ni nje tu. Akaoga bila shida Pam akimsubiria nje. “Angalia
usije anguka humo ndani!” “Maji mazuri hayo! Nayafurahia.” “Ningekuwekea ndoo
mbili?” Mill akacheka na kujibu, “inatosha kwa leo.”
Baada ya yote
akamsaidia kurudi chumbani kwake, akataka kutoka. “Mbona unanikimbia tena!?”
“Nakupisha uvae.” Mill akamwangalia kwa kumsuta. Pam akarudi na kukaa ila akawa
hamwangalii.
“Vipi Shema huku
kijijini? Ashapata wenyeji?” “Mmmh! Hana ugeni wowote huyo! Washamzoea.
Huwa namleta huku mara kwa mara. Na ugonjwa wake huo wa mpira, hajaacha.
Anakusanya watoto, kuna uwanja kule mbele karibu na shule, basi huko ndiko anakoshinda.”
“Na huku pia!?”
“Hutamuweza Shema. Na hivi sasahivi ana ile mipira yake uliyo mnunulia,
asubuhi wanakuja kumuulizia. Au wale wakubwa wakitoka shule, pia wanataka
kucheza naye. Siku za jumamosi ndio hutamuona hapa mpaka umfuate na umgombeshe,
ndio atarudi kula kama anakimbizwa. Akitoka hapo hutamuona tena mpaka
jioni! Maji ya kunywa ni ya kumpelekea hukohuko!” Mill akawa anacheka.
“Pakulala?”
“Nalala naye. Hajiwezi. Usingizi bila kuniona hapo kitandani, halali.”
“Itabidi aanze kujifunza kulala peke yake Pam! Huyu mtoto ni mkubwa
sana.” “Halafu nitapata wapi hicho chumba chakumuweka peke yake?” “Maisha
lazima yatabadilika. Hamtabakia hivyo wakati wote. Tutazungumza
zaidi.” “Nashukuru kwa kuzungumza na wazee. Na asante kwa zawadi zote. Zote.
Kuanzia zangu, Shema, mama, bibi na babu. Babu amefurahia mashati huyo! Saa
ndio hataki hata kutoa mkononi.” Mill akacheka akifikiria.
“Na asante
pia kwa kuja.” “Karibu.” Akamuona ni kama ana kitu ila hawezi
kukisema. “Kuna nini?” “Tutazungumza vizuri kesho. Si tunaweza toka kidogo? Si
lazima sehemu maalumu! Hata huko milimani kwenye hayo maji. Nasikia huku
kunasifika kwa mitiririko ya maji. Ndio twende huko.” “Sawa.” Shema
akaingia na vitu alivyoletewa na baba yake. Akachangamka hapo, maneno mengi,
Pam akimwangalia tu alivyochangamka.
“Kesho
tunakwenda kucheza wote baba.” “Shema na mpira! Husubiri hata apumzike?”
“Aliniambia lazima atachukua likizo, halafu tutapata muda. Sasa
huku yupo mbali na nyumbani. Hana kazi. Tukacheze tu. Sasahivi nina
viatu vipya na ameniletea mipira mingine miwili.” “Naona ungemalizia vile viatu
vyeusi huku kwenye udongo mwekundu, vingine uache mpaka tukirudi mjini.” “Sasa mtoto wako
mwenyewe huyo miguu inakua mchana na usiku. Mpaka arudi mjini vitakuwa havimtoshi
tena.” Shema kusikia hivyo, akafurahia sana. Miguu hiyo ilishazoea viatu
chakavu, leo kubadilisha viatu atakavyo!
~~~~~~~~~~~~~~
Asubuhi Pam,
mama yake na bibi yake waliamka kuandaa kifungua kinywa cha nguvu kama chakula
cha mchana. Kilikuwa kikinukia, ungejua kwao kuna neema. Wakaandaa meza
akaenda kumuangalia Mill.
“Kumbe
ulishaamka!” “Nipo mtandaoni nasoma habari za uchumi. Napitia kujua leo soko la
dunia likoje. Stock ipo na thamani gani na mengine mengi.” “Maji yakuoga
yapo tayari.” “Acha nikacheze kwanza huo mpira, kulipa deni, ndio nije
kuoga. Ila nitataka kusafisha kinywa na uso.” “Una vitu vizuri! Chumba kizima
kinanukia!” “Ni vilevile ulivyoniacha navyo. Sijabadilisha.” “Nimeona na mimi
umenikumbushia enzi! Umeniletea kama vya mwanzoni. Nashukuru.” “Pam kwa shukurani!
Ulishashukuru jana, zaidi ya nitakavyokumbuka! Unafurahia
mapumziko yako lakini?’
“Sana. Nikiwa
hivi, huku na mama! Nadeka.” Mill akacheka. “Hajui umeshakua, na
una mtoto anayekuzidi mpaka urefu?” “Naona mimi na Shema wote tunadekezwa.
Njoo uoshe uso upate kifungua kinywa.” “Mbona simsikii Shema?” “Huyo mpaka saa
nne kwenda saa tano. Analala kama aliyekufa. Sasahivi si muda wake. Na
namuacha makusudi ili huo mwili upumzike, maana najua akimka tu, mpira.”
“Njoo nione mkono.” Mill bado alikuwa amejilaza na kujifunika ndani ya
chandarua.
Akakifunga
vizuri, Pam akasogea. “Naona nje kumepona kabisa. Labda huko ndani kama
alivyoniambia dokta. Nje kunaweza funga, lakini ndani kukachelewa. Ndio
nachukulia taratibu.” “Kaa hapa tuone.” Akimuonyeshea pembeni ya kitanda.
Akakaa taratibu.
Mill
akajinyanyua kutoka kwenye mto na kumvuta mkono. Jinsi alivyomshika akimpapasa
ili kutizama huo mkono, mwili mzima wa Pam ulikuwa ukisisimkwa mpaka
akahisi anamfanyia makusudi! Alimpapasa kama alivyokuwa akimfanyia
kitandani. Pam akashindwa kuvumilia, akasimama kwa haraka.
“Si unaona
unavyoendelea vizuri?” Mill akacheka taratibu kama kwa masikitiko akitoka
kitandani. Jamaa alikuwa amesimama wima mpaka Pam akabaki
ameduaa. Akaona bora atoke. Mill kawakwa tamaa kwa kumshika tu, na yeye kabadilika
hisia kwa kushikwa tu mkono! “Acha nikuandalie maji.” Akawa kama anakimbia
hapo chumbani.
Mungu Asiyechunguzika & Asiyetaka Msaada Anapofanya Yake
Muda wake wa kujifungua ulipofika, hakujua. Maana
alianza maumivu ya kawaida tu jioni akiwa na mwanae nje, ndani ya geti. Ayan anazunguka na baiskeli, yeye
amekaa akimwangalia. Vile mwanae alivyokuwa akifurahia, akaona asimkatili, akapuuzia yale maumivu. Ni kama yakaisha, asiwe na
habari ni uchungu. Yakawa ni maumivu ya kuja na kuondoka.
Usiku wa saa sita wamelala, ndio vikazidi.
Ikabidi ampigie simu mama mwenye nyumba wake. Naye kwa kuwa alishajua ni
mjamzito wa kujifungua wakati wowote na yupo peke yake na watoto tu, akiwepo
Ayan na huyo msichana wa kazi naye mdogo tu, hakuchelewa.
Kufika, hali ya Mina ni mbaya, mtoto anachungulia
kabisa. “Mina, kichwa cha mwanao nakiona kabisa! Kwa nini umechelewa?”
“Sikujua kama ni uchungu anti! Nisaidie nijifungue tu hapahapa nisije ua
mwanagu.” Ni mama mtu mzima anafahamiana na watu. Hapohapo akampigia simu nesi
anayemfahamu. Akawa akimuelekeza chakufanya na yeye akakimbilia hapo.
Wakamsadia Mina.
Yule mtoto aliyekuwa akisubiriwa na wakunga
WAMAANA. Walioandaliwa kwa pesa nyingi, baba yake akitaka uzembe wowote usitokee
siku ya KUZALIWA kwake, akazaliwa nyumbani. Tena akizalishwa na mama
mfanyabiashara tu, hana elimu yeyote ya unesi na kuja kumaliziwa na nesi
wa kawaida tu.
Ila wakashangaa
Mina hataki kwenda hospitalini.
“Kwani mimi na mtoto ni wagonjwa?” “Hapana Mina! Ila unatakiwa kwenda kuangaliwa!
Kuandikishwa tarehe na jina la mtoto!” Hicho ndio alikuwa akikwepa,
wao wasijue. “Nitakwenda lakini sio
leo, anti. Acha nipumzike.” Wakamsaidia usafi na uji wa mzazi. Na kwa
kuwa aling’ang’ania kutokwenda, wakaona wamuache tu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kumbe Mina akili kichwani. Alijua akienda tu
hospitalini kwa haraka, na kumuandikisha huyo mtoto, kina Ruhinda wanao fahamiana
na kila mtu, kila sehemu, wanaweza pata taarifa kwa urahisi, wakampata,
na yeye hakuwa tayari kurudi Dar. Maisha na wanae yakaendelea bila shida.
Hakuna Marefu Yasiyokuwa Na Ncha.
Watoto wake wakaendelea kukua na yeye ametulia. Mina
akang’aa kwa uzazi usio na stress.
Anafanya anachotaka na wanae, hana shida pesa si ipo! Akaendelea hivyo mpaka
Ayvin alipofikisha miezi karibia 6 ndipo akambadilikia vibaya sana.
Akaanza kulia mfululizo. Siku na hiyo alilia
usiku mpaka panapambazuka! Mina hajalala anabembeleza tu. Asubuhi akawa
ameshikwa homa ndipo ikabidi kumpeleka hospitalini. Baada ya vipimo vya muda
akagundulika ana henia, anatakiwa kufanyiwa UPASUAJI ili kumtibu.
Hofu
ikamuingia Mina kupita kiasi. Mtoto wa Pius aliyekuwa akimpigania na fujo zote
zile! Hajawahi kumuona hata mara moja! Iweje MAKOSA yatokee
chumba cha upasuaji, mtoto afe hajamuona baba yake wala Pius
mwenyewe hajamuona mwanae! Akabaki amekwama. Anafanya nini kwenye hiyo
hali! Akabaki akiwaza mbele ya daktari aliyekuwa akimpa maelekezo na mtoto bado
akiwa analia, anatakiwa kutoa maamuzi ili mtoto atibiwe.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ni Nini Afanye Mina Katikati Ya Hali
Hiyo?
Katika Wote Aliowaacha Nyuma, Nani Ampigie Simu Kwanza Kueleza
Ugonjwa wa Ayvin?
Au Afanye Maamuzi Magumu Kumuingiza
Mtoto Chumba Cha Upasujia, Tena Huko Hospitali Ya Wilaya, Halafu Mengine Yaje Yajijibu Baadaye?
Inaendelea....
0 Comments:
Post a Comment