Asubuhi ya saa 11, Andy akawa amewasili na yeye hapo
nyumbani kwao. Mzee Ruhinda akamfungulia na kumkaribisha. “Vipi Mina?” “Mama
yenu alimpa dawa akamuacha amelala ila anawasiwasi sana na lile jicho. Sio zuri
kabisa na pressure ilipanda sana.
Tunafikiria leo kumrudisha hospitalini.” Akabaki amesimama akifikiria.
“Nenda kapumzike. Unaonekana hujalala.” “Sikukusudia kumuumiza
Mina, baba!” Baba yake akabaki akimwangalia. “Na simchukii mtoto aliye
beba.” “Nafikiri unaongea kitu sahihi lakini kwa mtu asiye
sahihi.” “Nataka na wewe ujue!” “Itasaidia nini!?” “Nataka ujue tu.”
“Acha nikwambie ukweli mgumu Andy.” Wakakaa ila alizungumza kwa sauti ya chini
kama asiyetaka kusumbua waliolala.
“Nazungumza hili si kupuuza kilichokupata! Au kudharau
maumivu yako! Hapana. Ila nataka kukwambia jambo ambalo najua mama yako
alikwambia na dada yako. Ila mimi nitazungumza kwa upande wa hiki
ulichotaka nikijue.”
“Wakati Pius anatunza familia yako, tokea mtoto wako
ni mdogo kabisa, hakuwahi kumwambia mtu kama anampenda
Ayan au Mina. Kwa hakika, mwanzo alianza kama Pius, jukumu la kaka kwenye hii
familia, mpaka ungemuhurumia jinsi alivyokuwa akihangaika na mwanao, ili
tu kuwasaidia wewe na Mina ambaye bila sisi kuingilia kati, ile shule ingemshinda.
Pius alihangaika na Ayan kama mtoto wake huku mazingira ya nyumbani
kwake hayaruhusu kabisa, wewe unamjua Raza.”
“Mtoto wako alipokuwa hapa, tena bila mama yake kuwepo
au mimi na mama yako, alikuwa akijua ameachwa hapa na msichana wa kazi, basi
hata mida ya mchana atatoka kazi na kuja hapa anashinda naye na kucheza,
ilimradi tu Ayan asikue bila aina ya baba. Alimpenda Ayan kama wake! Mchana na usiku, kwa uzima
na maradhi, alisaidia familia yako nafikiri huko ndiko shetani alipomjaribu.
Huko sitataka kwenda.”
“Lakini ninachotaka kukwambia ni hivi, tafadhali
sana, MATENDO yako yazungumze bila maneno. Ni hilo tu.” Andy
akabaki ameinama, macho mekundu. “Nenda kapumzike. Tutazungumza baadaye.”
Akanyanyuka na kupandisha ngazi akielekea chumba alichoambiwa amelala Mina na
mtoto wake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kufungua mlango, patupu. Na utupu ule ni kama
mtu amekimbia. Baadhi ya nguo zilikuwa zimezagaa mpaka sakafuni.
Akakimbilia chooni. Hakuwepo Mina wala Ayan. Akakimbilia chumbani kwa
wazazi. Akagonga na kuuliza hata kabla hajakaribishwa. “Mina na mwanangu wamekuaga
wanakwenda wapi?” Swali hilo akawa anamuuliza mama yake. “Umeangalia chumbani?
Watakua bado wamelala.”
Akatoka hapo akikimbia ikabidi baba yake amfuate
nyuma, mpaka getini kwa walinzi ambako alipita bila salamu. Alifunguliwa geti
na kuingia kama chooni. “Mlimuona mke wangu na mtoto wakitoka hapa?” “Usiku
aliniomba nikamtafutie taksii. Ikaja nikamsaidia kubeba mizigo. Alionekana
mgonjwa, yupo dhaifu na anatumia jicho moja. Ila nikihakikisha yupo
salama na mtoto.” Andy akajikuta akilia hawezi kumlaumu huyo mlinzi
kwani alifanya kwa sehemu yake na anaonyesha alifanya zaidi kumsaidia. Mina si
mtoto na hakuonekana ameruka ukuta, ametokea mlangoni kufika hapo getini akiwa
na mwanae na mizigo yake. Si kosa la mlinzi. Hawawezi kumlaumu. Historia ya
Mina mtoro ikamjia Andy.
“Ilikuwa saa ngapi?” Mzee Ruhinda akauliza. “Kwenye
saa tano usiku hivi kwenda saa sita.” “Unamjua mwenye taksii?” “Hapana.
Nilibahatisha tu, alikuwa akipita.” Mzee akarudi ndani akikimbia.
Kila Mtu Ana Mwisho Wake.
Naye Andy akamfuata bila kujua anakimbilia wapi. “Naomba
mpigie simu mama Roni kujua kama Mina yuko huko.” Akashituka mama Ruhinda ila
akapiga simu.”
“Samahani nakusumbua alfajiri hii.” “Hamna
shida. Kwema?” “Nataka kujua kama Mina yuko huko?” “Ashawatoroka?” Akauliza bila wasiwasi, ikamfanya mama Ruhinda atulie
kidogo na kuuliza. “Wewe unajua alipo?” “Mimi nilijua
tu, hizo fujo za kwenu huko, hawezi kukaa. Namjua Mina. Na
akiamua kuondoka, hamtampata mpaka aamue kurudi mwenyewe.” “Sasa
atafanyaje na ni mgonjwa, mjamzito na ana mtoto mdogo?” “Hayo umeyakumbuka kwa kuchelewa
sana mama Ruhinda.” Wote kimya wakisikiliza.
Ticha akaanza kutoa somo. “Nilimwambia
Roni, kama angekuwepo macho sasahivi angekwambia. Nilikuwa nikimuhesabia masaa.
Na hata hivyo amejikaza, kwamba kuna
alipokuwa ameweka tumaini, ameona na hapo halipo ndio maana ameondoka.
Hizo fujo zenu, Mina haziwezi.
Na hivi ana wanae wote, hapo mtafute mahali, msubiri, na kumuombea.
Hata mtume jeshi, Mina akikuponyoka, humpati ng’o. Anaweza akawa anaishi
chini ya pua yako na usimpate.” Wote kimya
wakisikiliza.
“Hata hivyo, muacheni apumzike.”
“Mbona unazungumza hivyo, mama Roni?!” “Waswahili tuna usemi wetu unasema hivi,
ukimchunguza sana bata, hutakaa ukamla. Mina alitulia na kujirudi
haswa. Vijana wenu wakaanza kumchanganga hapo. Halafu binti zenu wanazunguka
kwa watoto wa dada zangu kusaka habari mbaya za Mina.” “Ni mke wa
Pius, tena ni sababu ya hasira tu.” “Basi una mambo mengi ya ndani kwako,
yanakupita.” Mama Ruhinda akakunja sura
na kumuangalia mumewe. Akaendelea.
“Si huyo mke mwenzie tu, hata wifi
yake huyo Paulina anahangaika na Mina! Tena yeye anatafuta mpaka
mganga wake. Eti kwamba mwanangu mshirikina, anawaloga. Nikanyamaza tu, nikiwaangalia, ila nilikuwa nikiwahesabia
siku zenu.”
“Mama Ruhinda, 40 yenu imefika. Sasa hemeni. Mlicho kuwa
mkikichokonoa, mmekipata.”
“Tutamtafuta tu, na tutampata.” Akajibu kwa uhakika. “Sawa.”
Na yeye mama Roni wala hakutaka kumbishia. Akamkubalia kiurahisi tu. “Najua ni mchanganyiko wa hapa katikati lakini patatulia.”
“Kwako kunabadilika majina tu mama Ruhinda, lakini michanganyiko haiishi. Mlimkataa akiwa
hajaolewa. Mkasema hajasoma, na katoka kwenye familia duni. Haya, kijana wako akahangaika
wee, akamtoa hapa kwangu mnapopaona
ni duni, lakini alikuwa ametulia, akampeleka kwenye mafleti pale katikati ya jiji, kisha akamtelekeza baada ya kumzalisha.” Akaendelea. Andy macho mekundi, hajiwezi.
“Mina akahangaika wee. Analea mtoto wenu,
huku anasoma shule ngumu zinazofanana na nyinyi wasomi. Akawa
hajulikani kama ameolewa au kaachika. Kijana wenu mara yupo mkoa
huu, mara nchi hii. Mkaona havinogi,
mkambebesha mtoto wa pili. Mkampiga mwanangu, ndio sasa, eti
Andy aliyekuwa busy sana, gafla eti ndio akapata muda wa kurudi na kunirudishia
mwanangu kama mzigo! Asimrudishe akiwa mzima, akaja kumtupa hapa
mtoto wangu, anatapika, hajiwezi.”
“Tena akamuacha kama hawara tu,
aliyekuwa amekutana naye barabarani wakati na nyumba alikuwa akisaidia ujenzi.
Mkatumia ujinga wake. Mkamsainisha makaratasi asije wadai mali. Mkambwaga hapa, sikuwaona nyinyi wala mjukuu
tuliyekuwa tukisaidia na sisi kulea wakati baba yake akiwa busy na anayoyajua yeye. Mkadharau hata
juhudi ya Ron ambaye na yeye alikuwa na kazi kama ya Andy tu, lakini
yeye aliweza kumlea Ayan bila kulalamika tena mpaka ofisini
alikuwa naye. Ila mkaondoka na mjukuu pia mkatunyima hata kuja kusalimia.”
“Mkatupokonya mjukuu, na Mina mkamfukuza
kama paka mwizi. Na
yeye hakuwa na mengi, akaenda kutulia kimya. Halafu mlivyo majasiri
nyinyi, na mwanae aliyekuwa akihangaika naye, akitangatanga naye
hapa mjini kama kuku mwenye kifaranga asiye na banda, wakati baba yake
anakula UJANA, pia MKAMPOKONYA. Sikusema kitu, nikawaacha tu.”
“Mkaenda kumtoa alikokuwa ametulia,
mkamrudisha kwenu, mkaanza kumfanyia tena fujo. Amejaa mitandaoni, ndugu na wanao mfahamu
wote wanatucheka, wanasema utabiri
wao umetimia. Mina malaya, kashachanganya ndugu.”
“Mkaona na safari hii msimuache
mzima, mumuweke kilema chakudumu,
ndio aondoke kwenu. Na picha zake akiwa ameumizwa yupo hospitalini, pia zipo
mtandaoni, kila mtu anaona na kujua, kasoro mimi mama yake mnayenidharau,
mlishindwa hata kuniambia kwamba mwanangu yu mgonjwa, amelazwa. Mkaona mniweke
pembeni, nyinyi ndio muendelee na mtoto niliyehangaika naye.” Walishituka hao kina
Ruhinda, hawakujua kama kuna mtu alimpiga picha Mina akiwa hospitalini maana
alilala usiku mmoja tu, tena chumba cha kulipia cha peke yake! Hawakujua kama
watu walijua kama alilazwa akiwa ameumizwa.
“Mina
anapendwa sana hapa kwetu, hajafukuzwa.” “Basi hiyo njia yenu
mnayotumia kuonyesha huo upendo wenu kwa Mina, imemuacha UCHI,
hadharani. Tena si yeye tu. Mimi na kaka yake wote ni kama mmetuvua nguo kwenye ukoo na jamii nzima
inayotufahamu.”
“Andy alimtoa kwangu akiwa ametulia. Mwanangu amejirudi, akaenda kumchanganya. Sasa, sasahivi ndio
unasemaje tena!?” Mama Ruhinda hoi. Kila
mtu hapo anamsikiliza huyo mama, Ticha, tena anaongea taratibu kama aliyekuwa akiwasubiria.
“Sikukupigia kukuudhi mama Roni. Samahani.” Akamsikia akicheka kwa kuguna. “Bora ungekuwa umeniudhi. Hilo mbona si tatizo? Wewe
na hiyo familia yako, mnabaki na amani, mtarudisha umoja wenu, lakini
mimi masikini, utajiri wangu ni wanangu.
Sina mali, sina mume, mmeniingilia
kwangu na kunipokonya kitu kimoja tu nilichokuwa nimeshikilia kwa maombi
ya mchana na usiku, nikimlilia Mungu.”
“Mmesambaratisha kwangu, sasa mtulie. Mwambie Paulina na mwenzie Raza,
mimi mganga wangu Yesu. Wasinitafute huko kwa wachawi na washirikina. Sijaloga
mtu, wala sijawahi kumpeleka Mina kwa mganga aloge yeyote kati yenu. Ila
namlilia Mungu wangu. Naamini ipo siku atanijibu
tu. Sina chenu, mwanangu kaondoka kwenu,
naomba waambie familia yako, inatosha.
Washatuvuruga hapa vya kutosha. Washatuchafua kwa ndugu zangu,
INATOSHA. Sasa BASI. Furahieni huo utajiri wenu kwa amani.” Simu ikakatwa. Sebule nzima ikapoa kama wamepigwa
kibao cha uso.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakamuona mzee anapiga simu. “Naomba
uje hapa nyumbani, sasahivi.” Simu ikakatwa. Akapiga tena ya pili.
Akatoa maagizo hayohayo. Kisha akaanza kuondoka. “Akija Pius na Paulina naomba muwaambie
wasubiri, nakwenda kuoga nitoe hizi nguo za kulalia.” Mzee akapandisha ngazi na
kupotelea chumbani. Akabaki Andy na mama yake, kimya kama msibani.
Akatulia kwa muda akamgeukia mama yake. “Kwani
kilitokea nini tena?! Mbona kama Mina alikubali kuja kuishi hapa!” “Hilo
swali uje kuliuliza wote tukiwepo hapa. Subiri.” Na yeye akaondoka. Akabakia
Andy peke yake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya muda akaanza kuingia Pius. “Baba amesema
tumsubirie hapa.” Akamaliza hivyo na kurudi kuinama. Mara Paulina naye
akaingia. “Kwema?” “Mzee amesema tumsubirie.” Pius ndio akajibu. Wakakaa ila
Paulina akaanza kuita. “Mama Ruhinda?” “Tunakuja sasahivi.” Wakasikia akijibu.
Kimya.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya muda mzee akashuka akionekana msafi. Akakaa
kwenye kochi lake akamsubiria mpaka mkewe akaja. “Safari hii nimewaita nyinyi
watatu tu, watoto wangu mliopo hapa. Nataka kuzungumza na nyinyi, ila sitaki
UGOMVI hapa ndani kwangu. Nikimalizana na nyinyi, mnaruhusiwa kwenda popote
mkaanze kupigana tena.” Mzee akaanza.
“Baada ya kuja na Mina hapa nyumbani jana, alikusudia
kuishi hapa. Ninavyofikiria, sijazungumza naye, ila nafikiri maneno
ya Raza, yalimuingia.” “Wala si kufikiri, Ruhinda. Alizungumza na mimi kabisa, akasema amemsikiliza
Raza, yupo sahihi. Sio sawa kuishi hapa kwa sababu ni kama nyumbani
kwa kina Raza na wanae pia.” “Raza alisema nini?” “Atakusimulia kaka
yako, mkitoka hapa na kwenda mtakapochagua kwenda kuzungumza na kupigana.
Ruhinda endelea.”
“Kwa hiyo ndio tumepata uhakika, sababu ya kuondoka
kwa Mina na mtoto ndio hiyo.” “Eti nini!?” Pius akashituka sana. “Mina ameondoka
usiku na Ayan, hajulikani alipo.” “Bora kutulie.” Akaongea Paulina bila hofu
na kushangaza wote.
“Umesemaje Paulina!?” Baba yake akamuuliza kwa kushangaa
sana ndio kama akili ikamrudia Paulina. “Nazungumzia kwa muda huu kama kuwapa
nafasi hawa, kufikiria chakufanya na mchanganyiko huo wa watoto kwa
mwanamke mmoja.” “Umechanganyikiwa wewe Paulina!” “Wewe na mwenzio
ndio mmechanganyikiwa wala si mimi. Mmejaa mtandaoni, wanaume wazima
hamna aibu!” Akaongea kama jambo la kawaida kabisa.
“Paulina, wale watoto ni wajukuu ZANGU mimi!
Kwako wanaweza wasiwahi kuleta maana, lakini si kwangu. Umesikia
Paulina?” Mzee akauliza kwa ukali haswa. “Ile ni damu yangu mimi. Nianze na wewe maana tuna ujumbe wako kutoka
kwa mama Roni. Paulina, wewe umechangia kwa asilimia za kutosha kumfikisha
Mina alipo. Na usijibu.” Paulina akanyamaza.
“Ulikuwa ukimtafuta nini uchawi mke wa kaka
yako?” “Mimi sijamtafuta Mina uchawi.” “Hukwenda kwa ndugu wa Mina kutaka kujua
habari zake?” “Wao ndio walinitafuta wakitaka kujua huku anaendeleaje!
Na hiki kilichotokea pia walikitabiri kabla. Wakasema atatuchanganya,
mpaka tujisahau tulipokuwa tumesimamia kabla hajaingia kwenye maisha yetu.
Kama waliongopa, tujiangalie tulipo leo, na yeye yuko wapi.” Akaendelea
Paulina na yeye bila jazba.
“Kwa maneno yao wala si yangu, walisema Mina ana majini…”
“Nyamaza Paulina.” Pius akamkatisha. “Nyamaza kabisa na nisikusikie
unarudia kusema tena.” “Wewe vipi Pius?! Sio maneno yangu, ni ya ndugu zake.”
“Na ibakie hivyo. Na nakuonya Paulina na sitarudia kukuonya tena.
Nitakupiga mpaka nikuumize, kama unadhani nakutania, rudia tena.” Pius akawa
mkali kama yeye ndio Andy.
“Koma kusaka habari za Mina, na koma
kupokea habari zake. Wakikuletea, zikimbie kama ukoma. Unanielewa
Paulina? Hayajawahi kukuhusu na hayakuhusu. Maana hata Ayan alipokuwa na
mama yake hapa akisoma, hukuhusika kwa karibu kwa lolote zaidi ya kusambaza
chuki ya maneno. Nakuonya, kama nilivyomuonya Raza. Kaa
mbali na Mina. Kwa maneno na vitendo. Sitarudia tena kukupa hili onyo.
Kama huna neno zuri la kuzungumza juu yake, ikitokea anatajwa na wewe upo hiyo
sehemu, nyamaza.” Akamgeukia baba yake.
“Samahani baba. Mina yuko wapi?” “Ametoroka.” Mama
yake akamjibu yeye. “Wakati mkeo anatukana hapa chini, kumbe alikuwa akisikiliza
huko juu. Akaniambia hataweza kuishi hapa, si sawa. Nikajaribu
kuzungumza naye, nikadhani ameelewa. Jicho lilikuwa linatisha na pressure ikapanda gafla, ikawa juu sana. Nikampa dawa na
kumwambia alale ili leo tumpeleke hospitalini. Ndio usiku huohuo akaita taksii
akaondoka na mwanae.” Pius akaanza kulia mpaka akawashangaza. Alilia. Akalia
sana.
“Ni mkosi gani huu jamani! Imekua kama mfalme Daudi na adhabu aliyopewa
na Mungu alipomuua Uria, akazaa na mkewe! Mwanangu anakwenda kufa hivihivi!
Bora Mungu angeniadhibu kivingine lakini si kumgusa kijana wangu jamani!” “Sasa huo uchuro.” “Umemuona
Mina, mama? Mina hana nguvu ya kuzaa, nakulea akiwa kwenye hali ile! Alitakiwa
mapumziko kabisa kabla ya shuguli ya kujifungua!”
“Nisikilize Pius. Tupo hapa tulipo kwa sababu yenu
nyinyi wote watatu. Sisi tumekuja kuingilia, tukiwa tumeshachelewa.
Kama kweli uliyajua hayo yanayo kuliza juu ya mtoto wako, ungetafuta
amani!” “Ni Andy, baba. Andy ana…”
“Hutanizungusha kwa maneno ya lawama.
Nilikuwa nimekaa hapahapa nikizungumza na wewe ukiwa unakwenda Dodoma.
Sikukusihi uende ukatafute amani?” Wakashangaa
Andy ameinama kimya. Hajachangia wala kukana!
“Eti Pius?” “Mimi nilikwenda kwa amani, Andy aka..”
“Jamani, mama Roni na nyinyi wote mpo sahihi. Mimi ndio chanzo cha matatizo
yote. Kweli nilimtoa Mina kwao kwa ahadi ya kumtunza, lakini…” Akasita.
“Mimi ndio nimekosea.
Wote tupo hapa tulipo, kama mama alivyosema, kwa sababu yangu MIMI. Leo mtu kama Paulina anaweza kunitusi mimi na mke wangu, kiurahisi
kabisa, ni kwa sababu mimi mwenyewe nimeweka mazingira ya kudharaulika. Nimempoteza
Mina aliyekuwa tayari ametulia,
anataka tu ndoa na mimi. Katika yote niliyomfanyia, Mina alinisamehe na
alikuwa tayari tuendelee. Lakini nimekosa mke na mtoto wangu, sababu...” Akaona
abadili alichokuwa akizungumza. Akamgeukia kaka yake.
“Pius umenikosea sana. Sana. Lakini
najua sasahivi haisaidii tena.” Akanyamaza kidogo, kisha akaendelea. “Sijui
nitampata vipi Mina, lakini nitamtafuta
bila kukata tamaa.” “Tafadhali popote utakapomsikia hata kwa fununua na mimi
naomba unitaarifu Andy. Tafadhali sana. Mtoto aliyebeba Mina si takataka, na hana hatia. Nililea mtoto wako bila kuchoka na si kwa
ajili ya Mina, ila nilithamini ile ya kujua sisi wote hata tukiondoka,
Ayana atabaki kubeba ukoo.” İkamgusa sana mzee Ruhinda na mkewe.
“Nilimpenda Ayana na kumlinda,
nikiiangalia kesho yetu sisi sote. Mungu ni shahidi, na naomba alikumbuke
hili hata huko mwanangu alipo. Hakika sikufanya kwa hila, ila upendo
usio na hila hata kidogo. Nilimpenda Ayan. Ninachokuomba ni na wewe kumbuka
fadhila. Ukisikia fununu au Mina akikutafuta, tafadhali nijulishe.” “Nitafanya
hivyo.” Wote wakashangaa, Andy akasimama.
“Kama mtaniruhusu, naomba nipumzike kidogo, ndio
niondoke.” Akaongea akimtizama baba yake. “Kwa namna hiyo, hapo hamna shida
Andy. Ninachotaka ni amani. Ila mjue mmenipokonya wajukuu, waendeleza
ukoo wangu. Roho inaniuma, najutia mengi sana.” “Tutawapata
Ruhinda. Usikate tamaa.” “Acha na mimi nikaanze kufuatilia taksii iliyomtoa
hapa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kazi ya kumsaka Mina ikaanza kwa kasi kubwa mno. Pius
alikuwa kama amechanganyikiwa. Alitumia pesa akitafuta hata fununu tu
kujua alipo, bila mafanikio. Walimsaka Mina mpaka wakanyanyua
mikono.
Andy alikuwa na hukumu, akajifungia Dodoma. Ikawa
kazi, mazoezini. Wanaume hao wakabakiwa na kazi ya kuweka pesa kwenye akaunti
ya Mina. Andy kwa matunzo ya mtoto ila Pius ndio alikuwa nusunusu. Hakuwa na
uhakika kama huyo mtoto atazaliwa. Mina aliondoka mgonjwa. Pressure ilikuwa juu, hatari ya kupoteza mtoto! Alikuwa dhaifu
na jicho linalotisha hata kutizamika.
Huku Kwa Mina.
Kumbe huku kwa Mina alitoka pale, akaomba apelekwe
kituo kikuu cha mabasi akitaka kutoka jijini kwa haraka sana kabla
hapaja pambazuka na kina Ruhinda kumuwahi. Alifika pale akiwa ndani ya
hiyo taksii, wakata tiketi
wakaanza kukimbilia taksii aliyopanda na mwanae, wakitaka kumuuzia tiketi. Kila
mkoa waliotaja, ulisikika wazi sana,
akajua lazima watampata tu. Aliposikia wakiuza tiketi ya kwenda Lindi,
mkoa ambao hata hakuwahi kuufikiria, akafurahi sana. Akachukua tiketi
yake. Basi lilikuwa likiondoka alfajiri sana. Akaamua kwenda kusubiria kwenye
basi na mwanae. Hakuchukua muda, baada ya kumuweka mwanae sawa, na yeye akalala
mpaka asubuhi mwanae alipotaka kutumia choo.
Akamsafi kabisa ndipo safari ya Lindi ikaanza. Alipofika
Lindi, bado akaona yupo hadharani,
wanaweza kumpata. Akachukua pesa ya kutosha akaamua kwenda Nachingwea kabisa. Maamuzi hayo anafanya kwa kusikiliza hisia zake na vile anavyohisi watafutaji wake
wangefanya kumtafuta. Akajua huko hata hawatapawazia. Safari ya Nachingwea ikaanza. Bado yupo na mwanae
na tumbo lake. Alipofika huko akaangalia mazingira, akaridhika. 803034
Akafanya kama alivyofanya alipokimbilia Iringa.
Akatafuta nyumba ya kulala wageni akatulia hapo kwanza kujiuguza mpaka apone
kabisa, zaidi jicho. Na akajua kwa kuwa na Ayan tu pale, hata pressure itatulia. Pili aliona hapo ni sehemu nzuri
itakayomsaidia kusoma mazingira. Ili kujua ni wapi aishi na hao watoto
wake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akatulia hapo na mwanae kwa juma zima. Kula, kulala.
Bila dawa za ziada mbali na alizofika nazo hapo, jicho lenyewe likapona.
Akajisikia na nguvu akajua hata pressure imejirekebisha. Ayan
yeye hana neno na mtu. Bora maziwa na mama yake awepo. Basi. Mina akapata utulivu
na kufurahia kutoroka kwake. Pesa ipo na alikuwa na uhakika lazima
Pius atamtunza tu. Alimtunza akiwa na mtoto wa Andy, akajua itakua zaidi
akiwa na mtoto wake. Hakuwa na wasiwasi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Taratibu akaanza kutafuta msichana wa kazi na nyumba ya
kupanga. Alijua kwa hakika hataendelea kuishi huko, ila alitaka akae hata
akitoka huko kurudi Dar ambako ndiko alijiambia angerudi kuishi huko na wanae
maana hakuwa na uhakika tena na ndoa yake, iwe angalau Ayvin anaweza kutembea.
Hana mshauri, linalopita kichwani kwake basi ndio hilohilo, kazi ikabaki
pakuishi mpaka akapapata.
Mwenye nyumba alikuwa mama mfanyabiashara. Ana
maduka hapo mjini akitoa vitu jijini Dar. Kwa hiyo akampangisha nyumba ilikuwa
ndogo tu ila nzuri na inajitegemea japo inapakana na mwenye nyumba. Na pakawa
na uwanja mkubwa tu aliosakafia kuzunguka nyumba zote, kisha hizo nyumba zikawa
ndani ya ukuta na geti zuri tu. Pazuri na ilionekana bado ni nyumba mpya. Na
hivi pesa ipo, akalipia ya mwaka mzima bila kujifikiria mara mbili na kuzidi kumfurahisha
huyo mama.
Akamtafutia na msichana wa kazi kabisa, basi maisha ya
Mina yakazidi kukaa sawa. Hanaga mawazo mazito. Hapo alishasamehe kila mtu,
akaacha wanao mchukia, hakutaka hata kujisumbua kuwafikiria. Akaanza
kuongeza mwili. Furaha na mwanae. Akitaka vitu, anamuagiza mama mwenye nyumba
wake, akienda Dar, anamletea. Mina na mwanae wakawa wa kula kulala. Wana kila
kitu wanachokitaka. Mtoto msafi muda wote na nguo za maana. Amani tele.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ni Nini Kitaendelea?
0 Comments:
Post a Comment