Siku moja kabla
ya safari. Mida ya saa nne dereva akawa ameshawasili. Shema alikuwa anakuja
kuchukuliwa na baba yake mida ya mchana. Alikuwa anamuacha hapo akimsubiria
baba yake. Dereva akagonga na kuingia ndani.
“Nimeambiwa
nikukabidhi na hii bahasha. Nitakuwa hapo nje nikisubiria. Utakapokuwa tayari,
utanikuta hapo nje.” Pam akapokea. Alipotoka tu akafungua akijua ni pesa. “Sasa
pesa yote hii ya nini!” Akashangaa. Mara mama Batuli akagonga.
“Tunaweza
kuzungumza?” “Karibu japo natoka.” “Sitakuweka.” Akaingia na kukaa kabisa. “Kaa
nikwambie kitu.” Pam akakaa akiwa amekunja uso. “Hili tulikuwa tukiliongea na
mama Pili. Nikasema nitakwambia.” Pam kimya akimsikiliza.
“Pam wewe ni
mdogo na ni mzuri mdogo wangu. Ila umeshazalishwa na baba Shema. Matunzo
unayoyapata sasahivi, ni kwa sababu hana anayemshika mkono. Akija
pata mwanamke mwenye roho mbaya, hata kama nia ya kumtunza
mwanae ipo, mwanamke akamkoleza vizuri, mengi unaweza usiyaone
kwa wingi huu.”
“Ukishikwa
mdogo wangu, shikamana. Makosa yanaweza tokea, lakini kama mwenzio
amejirudi, samehe. Najua mpo kwenye mahusiano na Mgaya. Wewe unataka
ukaanze upya? Baba Shema lishakuwa jini likujuwalo. Halikuli
likakwisha. Endeleza hapohapo.” Kimya.
“Watu wa baya Pam wewe! Eza pata mwanamke
akampeleka kwa wataalamu, wakamfunga akili huyo, asikae akakukumbuka
tena. Lakini ukikaa mwenyewe jikoni, unayo jeuri ya kupakua
utakavyo! Ni hilo tu. Akili kumkichwa. Mjini hapa!” Alizungumza na
lafudhi yake laini ya pwani. Akaondoka bila ya kujibiwa, ila akamuacha ametulia
akifikiria.
~~~~~~~~~~~~~~
Alishampa Mill
maneno machungu kwa hasira. Mill ameyatunza moyoni na yeye ni
kama hataki tena. Anajirudije kwa Mill anayeondoka
nchini!? Akawaza na kuamua kuyaacha tu. Akaondoka kwenda kufanya manunuzi,
kijana akimsaidia kama aliyeambiwa ahakikishe asinyanyue kitu.
Alinunua vyakula
vya kutosha ili huyo mtoto wa Mill asiende shinda njaa huko kwao kama mwenyewe
Mill alivyosema. Akanunua zawadi mpaka kwa babu yake! Pesa si ipo! Yale
mahitaji ya muhimu aliyojua kwao wanahitaji lakini hakuwa na uwezo, safari hiyo
alifanya. Kuja kumaliza, gari nyuma imejaa. Anapangaje kwenye masanduku
kusafirisha kwa basi! Akawa amekwama.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakati wanarudi
ilishakuwa jioni kama ya saa 10 hivi. Foleni na manunuzi mengi wakajikuta
wanafika Tandika mida hiyo. Akakuta gari ya Mill imeegeshwa pembeni kidogo ya
nyumba. Akajua yupo hapo anamsubiria. Akashuka garini, akaenda kwenye gari
yake.
“Shema yuko
wapi?” “Tumerudi hapa, nimekuta kundi la watoto wakimsubiria. Ameingia ndani
kubadili nguo, ameondoka muda si mrefu.” “Yaani Shema na mpira jamani!
Hachoki!” “Na wanampenda kweli wenzie! Wakimuona ndio kama siku imeanza.”
Akacheka na kutulia.
“Nashukuru kwa
msaada wa pesa.” “Umepata kila kitu?” “Naona nimezidisha pia. Walikuwa na
mahitaji huko nyumbani, ila uwezo ndio sikuwa nao. Nikawa nawaambia wanipe
muda. Leo nimejibana mpaka nimewapatia kila mmoja mahitaji yake.
Nashukuru, ila ujue naenda kuwaambia ni zawadi kutoka kwako.” “Haina maana
Pam!” “Kwangu inamaana Mill! Unanijali mimi na Shema. Asante.”
Mill akamwangalia kama hajamuelewa sawasawa. Kama aliyejirudi vile!
Pam akashindwa
azungumze nini tena, ila kuaga. “Acha nikuache ukaendelee na shuguli zako.”
Akabadili mazungumzo akiaga. “Nina wazo. Ila kuwa huru kukataa
kama vitaingiliana na mipango yenu.” “Mill! Sina mpango na Mgaya! Na
siendeshi maisha yangu kwa kupitia yeye! Ni uhusiano wa kawaida tu.
Lakini si kama napanga naye mambo!” “Ingekuwa mimi nisingechukulia
kawaida. Mtu anayekufaa kipindi cha ugonjwa! Uliyemchagua
kuwa karibu yako kipindi cha uhitaji wako na yeye akatoa muda
wake kwa ajili yako! Sidhani kama ni mahusiano ya kawaida.” Wivu tu.
“Lakini tuyaache
hayo. Hayanihusu tena.” “Unamaanisha nini!?” “Mimi mbaya! Nina laana
ya kwetu! Nipo kama baba yangu! Nataka kukufanya mama Kenny!
Nakuona mjinga! Kweli kuna unalotaka kulisikia tena kutoka kwangu?”
Pam akashindwa hata kumtizama, akainama hapo dirishani alipokuwa amekaa Mill.
“Huyu dereva ni
mzuri sana. Mtu mzima na ametulia. Naweza kumuomba awasindikize mpaka
nyumbani Lushoto, kisha kurudi kuja kuwachukua. Itasaidia kuwa na safari
tulivu. Unaonaje?” “Nitashukuru.” Alijibu akiwa bado ameinama.
“Basi kesho mida
ya saa moja asubuhi nitamwambia awe ameshafika, asaidie kumalizia kupandisha
mizigo kwenye gari, muondoke.” “Asante. Nashukuru.” Akabaki ameinama. Mill
anaona tu kichwa. Wakatulia kidogo, akaona aage. “Usiku mwema. Na mkisafiri
muwe nasafari njema.” “Na nyinyi. Mwambie Shema anipigie mkiwa njiani. Na
nitakuwa nikiwasiliana na dereva pia kumkumbusha awe makini huko
barabarani.” “Sawa. Asante.” Pam akaondoka bila hata kumwangalia.
Barua Kwa Mill.
Maneno anayo
rudiarudia Mill aliyomwambia akajua yamemuumiza sana. Na kadiri
alivyokuwa akiyarudia kwake akayasikia machungu hata masikioni kwake
yeye mwenyewe. Kumtafuta kwa simu, aibu. Alishamkatalia namba. Sasahivi
amempa mtoto wake simu, anawasiliana na mtoto wake, hana tena shida na
kumtafuta. Na maneno ya mama Batuli akajua yanaweza kuja tokea. Akamwandikia
barua ili dereva akirudi aje ampe.
‘Mill, ni mengi yametokea katikati
yetu. Nasikitika umerudi umekutana na Pam aliyejeruhiwa nafsi. Imejaa uchungu
na kusalitiwa. Lakini sio sababu ya kukurushia maneno mabaya. Nimekosa,
naomba unisamehe. Nisamehe kukufananisha na baba yako pamoja na
babu yako.’
‘Huna laana, ila mimi nahisi
ndiye mwenye laana kama mama yangu. Imekuwa ngumu kwetu kubahatika kama
wanawake wengine. Tafadhali naomba nisamehe. Sitarudia kusema hivyo.
Naamini Mungu atakusaidia kama unavyoomba kuja kuwa mume mzuri, kwani nimekuona
jinsi ulivyo baba mzuri kwa Shema. Nashukuru. Asante.’
‘Swala la Mgaya nalo pia naomba unisamehe
kwa mazingira uliyoyakuta siku ile. Nilishazungumza naye, na
nimemuweka sawa. Ameelewa. Kwa hiyo ile hali haitajirudia tena.
Tafadhali naomba unisamehe. Kwangu si dangulo. Na mimi
namuheshimu sana Shema. Sijawahi fanya lolote la kumfedhehesha
mwanangu.’
‘Naomba msamaha kwa yote niliyokuumiza.
Nakuahidi kubadili maneno yangu ili yasiendelee kukuumiza.
Samahani na asante kwa yote unayotufanyia mimi na Shema. Asante. Nakutakia kila
la kheri kwenye maisha yako. Pam.’
Akaifunga vizuri
na kuiweka. Mama Pili akaingia kumsaidia kufungasha, kisha akaja mama Batuli.
Vicheko na mengi yakaendelea mpaka wakamaliza. Pam amekaa tu anawaelekeza.
Akawashukuru kila mmoja akaenda kulala.
Safari ya
Lushoto.
Saa moja kamili dereva akawagongea. “Na baba
Shema yupo nje. Na yeye amesema amekuja kuwaaga.” Shema alivyosikia tu hivyo,
akatoka kwa haraka. Alipendeza huyo! Maana baba yake alimpeleka tena kwenda
kunyoa. Mama yake alimuamsha siku hiyo alfajiri. Akaoga na kumpa track suite
nyeusi alinunuliwa na baba yake na sneakers nyeusi zenye nyekundu
kidogo. Akapendeza, ungejua ni mtoto wa Mill.
Pam akamkabidhi
yule dereva vitu vyote kisha akatoka na kufunga mlango wake. Akakuta shoga zake
wameshaamka wametoka kumuaga. “Utafikiri mwali! Umependeza sana mama Shema.”
“Najitahidi kumtia moyo mama yangu. Akiniona, afurahi.” Wakataniana hapo
kisha kuagana nao, ndipo wakatoka wakimsindikiza. Na wenyewe wakashangaa
kumuona baba Shema hapo nje.
“Sasa huyu Shema
anapanda gari gani?” Wakawa wanaulizana wakitamania maisha hayo mapya ya
wenzao. “Anasalimia tu.” Mill akashuka garini alipowaona. Yeye Pam alivaa gauni
zuri, ila refu juu mpaka chini. Japokuwa mwili uliisha, lakini lilimkaa mpaka mate
yakamtoka Mill. Nywele alishasukwa rasta ndogondogo na mama Pili. Siku hiyo
hakufunga kitambaa. Na hivi alisikia Mill yupo nje, akaziachia kusudi kumrusha
roho. Akaweka na hereni na lipstick nyekundu. Bwana Pam alipendeza! Ungejua
kuna neema.
“Umependeza sana
Pam!” Mill kama kawaida yake, hajiwezi kwa huyo mrembo. Na kwa asili
alipenda vitu nadhifu. Sasa siku hiyo Pam akajiweka sawa mpaka akakubali.
Yaani tangia wanakutana baada ya kurudi nchini, siku hiyo ndio anamsifia mbele
ya wenzie.
“Asante. Lakini usingedamka
mapema hivi! Ungepumzika tu.” “Naona bora hivi nikishawaona mmepanda
kwenye gari, nitaridhika. Umembembea huyu masweta yakumtosha?”
“Nimebeba, na nishampa dereva amuwekee moja kwenye gari. Atakua sawa.”
“Mnakwenda nyumbani, hakuna haraka. Tafadhali msisitize huyu, asije pata
tamaa ya kuwahi kufika ili ageuze kwa haraka.” “Nimesikia. Na nitakuwa makini.
Mbona tutafika tu salama, wala usiwe na wasiwasi.” Akajibu huyo dereva.
Akaenda kumtoa
Shema garini. “Usiache kunipigia. Kila baada ya masaa…” “Mawili.” Akamalizia
Shema akicheka. “Kumbe maagizo yote anayo!” Mama yake akasikia. “Nakumbuka kila
kitu. Asante baba. Na wewe usafiri salama. Ningekuwepo ningekusindikiza.”
Mill akacheka. “Tutapanga safari nyingine, tutakwenda wote. Na wewe
ukapaone huko.” Akafurahi Shema. Baba yake akamkumbatia kwa muda na
kumsindikiza garini.
“Funga mkanda
wakati nakuona. Na huo mkanda usitoke hapo mpaka gari iwe imesimama, unashuka.”
Pam akashangaa kuna mito na blangeti kabisa. “Hivi vyote ni vya humuhumu?”
“Nimewanunulia ili mpate pakujiegemezea, mlale mkichoka.” “Nashukuru kujali
Mill. Asante.” Shoga zake wakamuaga wakishangaa kwa kuchungulia mpaka
ndani ya gari.
Akamsogelea
Mill. “Hii ni barua yako.” Mill akamwangalia machoni na kuipokea akimuuliza.
“Ndio talaka yangu rasmi?” “Utaisoma na nina maanisha kila neno.”
“Sawa.” Akaiweka mfukoni. Kisha akampa mkono wala si kumkumbatia. Kiroho
kikamuuma kidogo Pam, ila akampa na yeye mkono. “Muwe na safari nje, na
mapumziko mema. Gari itakuwepo tu nyumbani. Ukihitaji kurudi, mpigie, atakuja
kuwafuata.” “Nitafanya hivyo. Asante.” Pam na mwanae wakaondoka. Safari hii kwa
heshima si kama safari nyingine.
~~~~~~~~~~~~~~
Picha ya Pam
vile walivyoagana ikawa ikimsumbua. Ukweli Mill alimpenda sana Pam.
Akakumbuka ile barua. Alipofika tu kwake hata ndani hakuingia. Akaanza kuisoma
garini. Akarudia tena na tena. Hakupata dawa ya kile, kinachomsumbua
rohoni.
“Inamaana hawa
wawili wapo na mahusiano halisi!” Wivu ukazidi
kumsumbua. Mgaya na Pam! Akazidi kuumia kwa wivu. Akabaki akiwaza garini. Shema
akampigia. “Umefika salama nyumbani?” Akajisikia
kufarijika, mwanae kumjali. “Nimefika salama. Na nyinyi?” “Tupo salama. Nataka
kulala, ndio mama ameniambia nikupigie kwanza kabla sijalala, nijue kama
umefika salama.” Akacheka aliposema ukweli.
“Haya nashukuru. Wewe lala. Utanipigia
ukiamka. Na mwambie mama asante kwa kujali.” Angalau Pam
akafurahia hilo ila kujiuliza kama alisoma barua yake. Wawili hao wakageuka wa
miaka ya 90. Kwa wote kushindwa kujishusha. Pam aliombwa simu akakataa,
baadaye akajuta, ila kushindwa kumpa tena. Mill naye alinyimwa
mara moja, jeuri hataki kubabaishwa. Ila Pam anamtaka.
~~~~~~~~~~~~~~
Pam na mwanae
wakafikishwa kijijini salama. Dereva aliposhusha vitu vyao vyote, yeye akageuza
kurudi Dar. Huku nyuma Mill anawaza kurudi Marekani, kukaa muda wote huo,
akisubiria majibu ya DNA, kisha tarehe ya mahakama! “Nitarudi Pam akiwa
ameshaolewa, mwanangu alelewe na Mgaya.” Akaendelea kuwaza akikusanya vitu
vya hao watoto akiwa hana uhakika kama atarudi nao au la. Kisheria walikuwa
wake wakiwa wameandikishana mpaka mahakamani.
Lakini
Mwanasheria alimpa moyo kwamba huo mkataba utakuwa void kwa sababu
aliingia akijua watoto ni wake. Pam alishakataa kuwa mama Kenny.
Inamaana hataki kuja kuwa mama wa hao watoto. Akazidi kuwaza Mill huku
akijiandaa na safari.
Pam hakuwa
akijua hapo anapopita Mill. Kubambikiziwa watoto wasio wake, na hata hao
watoto hawakuwa wakijua linalowasubiria mbeleni au kwa nini wanarudi
Marekani. Walijua ni kutembea tu. Jeuri, wanaishi na Mill akiwatetemekea,
wasijue kama Mill amefika mwisho.
Kwa Mina.
Kitumbua Kishaingia Mchanga.
Mina akajua kwa hakika kitumbua kimeshaingia mchanga. Taratibu bila kutoa sauti, akarudi juu kwenye chumba
alichokaribishwa. Akaingia bafuni akihema. Akaanza kufikiria kwa haraka. “Hapa hapatakalika tena.” Akawaza Mina.
“Si sawa kwa Raza wala watoto wake.
Itakua mimi nachukua nafasi yao hapa.” Mina akaendelea kuwaza akajisikia
uchungu sana na kuanza kulia. Alilia sana akijutia maisha machafu aliyoishi
zamani.
“Hakuna
atakayeniamini tena, na utabiri wa wengi umetimia. Kweli nishachanganya wanaume
na ndoa imeshindikana!” Akalia Mina
akijilaumu sana. Mwishoe akasikia mlango wa chumbani unagongwa taratibu kama
mtu anayetaka kujaribisha kama yupo macho au amelala asimsumbue.
~~~~~~~~~~~~~~
Akaosha uso kwa haraka na kutoka. Akafungua mlango.
“Nilijua umelala! Nimekuletea chakula.” “Nilikuwa chooni mama. Ingia tu.” “Hili
jicho ni lakuangaliwa tena na daktari wa macho. Sijalipenda linavyoendelea.”
“Na linauma pia.” Mama Ruhinda akaliangalia tena. “Sio zuri kwakweli.” Akamfuta
na tissue.
“Kula ulale. Tutazungumza. Kama twende kwa daktari leo
au kesho.” “Lakini mama, naona mimi niondoke
tu hapa.” Mama Ruhinda akashituka sana. “Kwa nini, na uende wapi!?”
“Sikuwa nimefikiria
vizuri. Si sawa kwa Raza na watoto wake. Hapa ni nyumbani kwao. Kwa mimi kuwepo hapa ni kama nitawanyima uhuru. Mimi ninapo
sehemu ya kuishi pamoja na watoto wangu, kwa muda mpaka wote tutakapojua
chakufanya. Tafadhali mama yangu. Acha mimi niondoke ili kuleta amani. Ndoa yangu imeharibika, sitaki na ya Pius iharibike.”
“Nisikilize Mina, najua kuna uliyosikia, umeumia.
Lakini ndoa ya huyo Pius ipo hivyohivyo tokea zamani. Inabadilika vijimambo tu. Wewe sie utahayesababisha
lolote, na Raza si muondokaji kwa Pius. Hata iweje, ile ndoa si yakuvunjika.
Atatulia tu.” Mama Ruhinda akamtuliza.
“Raza anapenda kuhamisha
maneno na kila mtu anamjua, ndio maana hata mumewe hakutaka kumsikiliza.”
“Lakini mama, kwa asilimia fulani alichozungumza Raza, hakukosea. Yupo sahihi.” Mama Ruhinda akashituka zaidi. Akidhani
mtoto si wa Pius.
“Unamaanisha nini!?” “Kabla sijaolewa na Andy, ilibidi
kumwambia historia yangu ya nyuma. Sikuwa nimetulia
mama yangu. Nilikuwa mtoto mbaya,
ndio maana nikashindwa hata kusoma.
Lakini mama, nilitulia kabisa. Nikabadilika
na tokea niwe na Andy, sijawahi kuwa
na mahusiano na mwanaume yeyote yule, na Mungu wangu ni shahidi.” Akamuona mama Ruhinda amehema
kwa nguvu.
“Ni maisha ya zamani
mama yangu.” “Nisikilize Mina. Naomba utulie. Kama ni maisha ya zamani, na
mumeo alijua na bado akakuamini
kiasi cha kukuacha hapa mjini, inamaana alijiridhisha na tabia zako za
sasa. Naomba utulie hapa. Kwanza
hapa utakuwa na uangalizi mzuri, na wanao wapo kwenye mji wao. Ninachotaka
kukwambia ni kuwa, haitakuwa rahisi hata kidogo. Na ninajua kwa sehemu
unamfahamu Raza. Si ndio?” “Kwa kumsikia tu.” “Basi kama ulikuwa ukiomba, omba
haswa. Huwa hajui kutania, na huwa
hakubali hata iweje Pius akawa na mwanamke mwingine.”
Mina akawa ameelewa kwa kiasi ila akataka uhakika.
“Nitakuja kukwambia habari za Raza na huyo Pius, acha
niende nikamwangalie Ruhinda nijue anahali gani. Lakini usiondoke hapa hata iweje. Tulia tuli, jiuguze, uhudumiwe vizuri.
Ruhinda si mnafiki. Akikupenda, amekupenda. Yeye ameruhusu uwe hapa, ujue atasimama
na wewe kwa kuwa anakupenda. Tulia kabisa, na uwe na msimamo.”
Mina akanyamaza akiwa hajaridhika kabisa moyoni. Bado akaona kuwepo pale
si SAWA.
~~~~~~~~~~~~~~
Akakumbuka jinsi Poliny alivyomfukuza baba yake. Na
alijua huyo binti si kipenzi cha Pius tu, hata babu yake alimpenda sana. Alikuwa binti aliyetulia, haiba nzuri na hapo kwa
babu yake alipapenda sana. Akakumbuka maisha aliyowakuta nayo hapo kabla
hajaolewa. Kupika pamoja japo wote wanao wafanyakazi. Lakini mlo wa jumapili
walifanya kama kijidesturi chao wao wanawake kupikia waume zao na familia, siku
hiyo! Umoja waliokuwa nao. Utulivu wa aina yake! Akajua utabiri wa watu utazidi kutimia kuwa
huwa akiingia mahali, lazima avuruge.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakati kila mmoja anataka kwenda kulala, ili waimalize
hiyo siku ndefu, mama Ruhinda akaingia chumbani
kwa Mina kumuangalia. Hakumkuta vizuri. Kichwa bado kilikuwa kikimuuma japo
alishampa dawa ya maumivu. Akaamua kumpima pressure, akaikuta ipo juu sana. Akaingiwa na wasiwasi,
akajaribu kumtuliza kwa hili na lile baada ya kumpa dawa ya usingizi, akamuomba
alale kabisa na kesho yake ndipo waende hospitalini kwa ajili ya hiyo pressure na jicho. Akamuacha ili alale.
Lakini alishindwa kulala usiku huo kwa
mawazo. Alimwangalia mwanae jinsi alivyolala pale kitandani na yule wa
tumboni, akabaki akiwaza.
Akakumbuka ushauri mgumu
aliopewa na mama yake siku aliporudishwa
na Andy akiwa ni mjauzito. Asisumbue
watu, akaanze kambi yake na wanae wa
baba tofautitofauti! Akaona huo ndio
wakati mwafaka wa kuutendea kazi.
Maamuzi Magumu.
Alikaa akiwaza mpaka kama kwenye saa tano usiku bila
ya kupata usingizi ila kukubaliana na wazo lake. Nyumba ilishatulia.
Wazee hao hulala mapema, kwa hiyo walishalala. Akaenda getini na kuomba mlinzi
amtafutie taksii na kumwambia isubiri hapohapo nje, wasiingie ndani, wasije
kuamsha watu. Akaanza kutoa vitu vyake na mwanae taratibu tena kwa kunyata
akitumia mlango wa jikoni. Jumba hilo ni la gorofa, vyumba vya kulala vipo juu.
Mlinzi akamsaidia kupandisha kila kitu garini. Akambeba na mwanae, Mina akaondoka
hapo bila wenye nyumba kujua.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kila mtu Maji yamemfika
shingoni. Itakuaje?
-
Mill atafanikiwa kushinda kesi na kumrudishia Kisha watoto wake?
-
Mgaya yupo pichani, ameshakuwa kizuizi kati yao. Watafanyaje?
-
Kwa Mina na wanae? Huku ametahadharishwa juu ya Raza kuwa ajipange
haswa, hakubali mwanamke mwingine kwa Pius. Ki vipi!? Japo Pius anaonekana
kummudu, Ila kwa aliyoyasikia, Raza si wakuchezea.
-
Je, Kwa Pius anayemtaka huyo mtoto? Aje asikie Mina ameondoka na
mwanae hajulikani alipo!
-
Kwa Andy je?
Usikose Muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment