Asubuhi.
Mzee Ruhinda aliwakatalia kabisa Andy na Pius wasiongozane
nao hospitalini, wabaki. Na mama yao akawaonyesha tena ile picha aliyompiga
Mina usiku uliopita kama kuwakumbusha madhara waliyomuachia Mina.
Wakatulia. Walifika hapo hospitalini, jicho la Mina lilikuwa limevimba haswa
mpaka wakashangaa. Hakuwa akiweza kufungua tena. Lilijaa mpaka shavu lilivimba.
“Mungu wangu!”
Akasikika mama Ruhinda. Ikabidi mzee Ruhinda kuzungumza na daktari,
akamwambia asubuhi hiyo Mina ameamka pressure ipo
nzuri kabisa ni hilo jicho tu, nalo alimwambia walipe muda litakuja kurudia
hali yake. Daktari akawatia moyo.
“Naomba niwaombe kitu wazazi wangu.” Mina akaanza
taratibu wakiwa wanasubiria kuruhusiwa. “Karibu Mina, mama.” “Kwa sasa kama
mnavyoona, hali sio nzuri. Naomba kama itawezekana, nije niishi
kwenu kwa muda mpaka hii hali itakapotulia.” Akaona wanaangaliana.
“Lakini kama haitakuwa sawa, nitakwenda kuishi
kwangu mpaka nitakapojifungua.” “Hapana. Naona mawazo yako yamekuwa kama ya
mama yako hapa. Alifikiria hivyo hivyo.” Angalau Mina akalifurahia hilo.
“Lakini lazima nikazungumze na Andy. Nitaondoka na Ayan.” Hapo wakapoa. Wakaona
wamuachie yeye mwenyewe.
~~~~~~~~~~~~~~
Walifika nyumbani kwa Andy wakamkuta na Pius yupo.
Mina akashangaa, akajua lazima atakuwa ameambiwa na wazazi wake awepo
hapo. Lakini hakuwa hata na hali ya kulifikiria hilo. Akaingia na kwenda kukaa
moja kwa moja. Wote wakashituka sana kumuona vile. Alivimba uso, zaidi upande
ule wa jicho lililoumia. Usingeweza kumtambua Mina vile alivyo. Alitisha sura
na kuogopesha kumtizama.
“Pole
sana Mina.” Andy akamsogelea akataka kumshika, Mina akasogea kama kumkwepa.
Wote wakaona. “Sikukusudia kukuumiza Mina! Samahani sana.” “Ulitafuta
njia yakumlipa kisasi. Acha uongo.” “Tafadhali Pius, nyamaza.”
“Sitaki amdanganye Mina, baba. Andy ni hatari. Amebeba chuki
kwa Mina, anaweza kumdhuru yeye na mtoto wangu. Mwangalieni alivyo Mina
sasa hivi. Halafu niambieni ni kwa jinsi gani mwanangu atapona kwenye
mikono yake huyu! Kuweni wakweli na mniambie. Andy amejawa chuki,
hawezi kujisaidia.” “Nakuonya Pius wewe!” “Utanipiga tena?” Pius akamuuliza
Andy.
Mina akasimama kuelekea chumbani kwa mtoto wake.
“Mina!” “Naona niondoke kwa muda Andy.” Andy naye akasimama na kumfuata
nyuma. “Mbona nimekuomba msamaha!” Mina akasimama na kumgeukia wakiwa wamefika
koridoni karibu na kuingia chumbani. Watu wa sebuleni hawawaoni lakini wanaweza
kusikia.
“Mina?” “Sio hivyo tu Andy. Hii hali ni ngumu,
mimi nakuelewa na wala sikulaumu. Nimeishi na wewe nimeona jinsi
inavyokuwia ngumu Andy. Najua nia unayo,
lakini uhalisia nao unakuvuta nyuma.” “Nakupenda Mina!” “Hilo nalijua.
Najua unanipenda sana, mimi kama Mina. Lakini mambo yamebadilika
Andy, tuwe tu wakweli. Sio kama zamani. Unaogopa hata kunikumbatia
kama zamani ulivyokuwa ukitaka nilale mikononi mwako kipindi chote hata
nilipokuwa mjamzito wa Ayan.” Mina akaendelea taratibu.
“Sasa sijui tatizo ni Ayvin au mimi kwa ujumla wake! Sijui..”
“Nakup...” “Naomba nisubiri nimalize Andy. Umekuwa ukirusha ngumi na maneno
makali kila wakati. Umejawa hasira huwezi, kujisaidia. Na huniamini
tena Andy!” “Nakuamini.” Andy akajitetea.
“Hapana Andy. Tafadhali naomba nisikilize.
Ugomvi wa jana umetokana na kile alichokifanya Pius, kwa kuwa wewe umeshindwa
kabisa. Na umekataa hata kujaribu!” “Hunitendei haki Mina! Nimemkuta
Pius akikushika.” Mina akashangaa.
“Kuwa mkweli Andy na tafadhali fikiria kabla hujajibu.
Kama kweli mimi nilikuwa na nia mbaya, ningekuomba kweli unisindikize
kliniki ili tuwe pamoja? Fikiria tu Andy. Nilikuomba kabisa nikitaka
tuwe wote, lakini ulikataa mwenyewe ukaniambia upo na kazi nyingi
kazini, na muda ni mbaya!” Mina akaendelea tu taratibu. “Na ndio kisingizio
chake kila siku, KAZI.” Pius
akadakia, wakajua wanasikilizwa. “Pius nyamaza.” Baba yao akasikika na sauti ya
kuonya.
“Nakuomba pata muda wakufikiria Andy. Hii kitu sio
rahisi kama tulivyodhani. Ayvin atakuwa kwenye maisha yangu daima. Sina
jinsi yakumkimbia au kumuacha. Hawezi kulelewa na Pius,
kwa hiyo nilazima awe kwangu. Pata muda wakufikiria kwa kina,
bila mimi kuwepo na kuamsha hasira kila ukiniona na tumbo langu.
Usifanye haraka na sitalaumu kwa maamuzi yeyote utakayoyachukua.
Utanijulisha, na ninakuahidi, sitakudai hata shilingi moja.” “Unanifanyia hivyo
kwa kuwa unajua unaye Pius!” Andy akalalamika kwa kuumia.
“Husemi kweli Andy! Mara ya kwanza
ulinifukuza kwako kwa kunitaliki nikiwa mgonjwa bila hata pesa ya kwenda
kumuona daktari! Mbona nilikutafuta kwa ajili ya mwanangu tu na wala si mali?
Unafikiri sikuwa nikijua kuwa nilikuwa na haki yakudai mali kwa kuwa
nilikuwa mke wako halali kwa miaka takribani minne! Lakini nilijiambia Mungu hataniacha.
Kama anavyosema Pius, mimi sijui kwa nini Mungu ameruhusu mimba ya Ayvin
itungwe. Sijui! Ila ninachojua mimi ni mama yake, na ninawajibika kwake kama
kwa Ayan.” Mina akaendelea.
“Nitaondoka na Ayan pia.” “Mina!” Andy akashangaa. “Huwezi
kumlea Ayan, Andy! Wewe ni shahidi. Huna huo muda. Hujawahi kuwa
nao, na sidhani hata kama unao mpango wa kutenga muda kwa ajili
ya mambo ya familia, Andy. Unakuwa kama unalazimishia tu! Nafikiri hata
jana ulikuja hospitalini kwenye kliniki yangu si kwa ajili yangu, ila kufumania.
Ukijua Pius yupo.” “Sio kweli Mina!” Andy akabisha.
“Mimi sitaki kubishana na wewe Andy. Nakuheshimu
mume wangu. Lakini utagundua ninachosema ni kweli. Na ndio maana ulipofika pale
ulikuja ukiwa umejawa na hasira. Na kwa haraka sana bila hata salamu, ukatafuta
kosa. Ukanilaumu mimi kwanza na kuanza kurusha ngumi bila kujali aliyekuwepo mbele yako ni nani.” “Hapana
Mina! Labda umetafasiri vibaya!” Akajaribu kujitetea Andy.
“Sasa ile hasira uliyokuja nayo na kuanza kumpiga
Pius, ilikuwa ni ya nini Andy?” “Alikuwa amekushika Mina! Kweli ulitaka mimi
nifurahie tu?” “Wewe ulifikiri ni nini kinaendelea pale mbele ya watu, tena hadharani
kama si tayari moyo wako umeshachafuka juu yangu mimi na mtoto niliyebeba!
Au niambie ukweli tu Andy, utakuwa na amani uje utukute mimi na Pius tu peke
yetu tumekaa tu sehemu hivi?” Kimya.
“Najua ni ngumu na ndio maana kwa heshima yako Andy,
na kwa kuwa nakupenda, nimeomba
nikakae kwa wazazi kwa muda hata mpaka nitakapojifungua.” “Mina!” “Sina jinsi
Andy! Mtakuja kuniua, niache watoto wangu bure! Acha kila mmoja wetu ajipange
kwa upya. Ukija kunitafuta uwe umeamua kweli kuishi na Ayvin kama
vile Ayan.” Wakamsikia Pius akicheka.
“Pius wewe, ujue unanitafuta Pius!” “Mimi
nimefanya nini mama yangu!?” “Unachocheka hapo nini?!” “Mina anamtaka Andy awe baba
kwa PJ wakati alishindwa kuwa baba hata kwa Ayan mwanae!” “Pius unakokwenda
huko wewe utaharibu kabisa!” “Basi Mina, mama. Nimeongea tu nikikuhurumia
wewe. Usitegemee kitu ambacho wazi unajua hutaweza kukipata.
Sitaki uje uumie.” Pius akajaribu kumtahadharisha kwa upendo.
“Kwa hiyo yeye Pius ndiye anayeruhusiwa kuwa karibu
na wewe?” “Hapana Andy. Na yeye lazima apate muda wakujifikiria
ni jinsi gani ataishi na mimi akijua mimi ni mke wako, kama
utaamua uwe na mimi. Lazima jukumu
la kuandaa mazingira mazuri kwa mtoto wake liwe kwa Pius mwenyewe.
Hawezi akaendelea kukukejeli wewe na kukujibu vile atakavyoweza
na kupigana na wewe huku mtoto wake anakutizama wewe kama baba!
Hilo haliwezekani.”
“Kama anataka mahusiano na mtoto, nilazima
ajifunze kuwa baba, na garama pekee ninayotaka ailipe kwa Ayvin, iwe kukuheshimu na kukukubali wewe kwa namna yeyote ile ulivyo. Unaweza ukabaki
kwenye maisha ya Ayvin kama baba atakayekuwa akikuona kila siku, KAMA narudia
tena KAMA TUTAKUWA WOTE. Tusipokuwa wote kwenye ndoa, basi mimi na Pius,
tukisaidiwa na wazazi, tutajipanga upya.” Pakazuka ukimya mkubwa sana.
“Yaani Mina, mama, hapo nakupongeza. Umeamua
vizuri sana. Na naona wote umewagusa
pabaya.” “Wala si pabaya mama.” Pius akabisha. “Mbona umepoa kama kweli ni
rahisi kumuheshimu Andy na kukubali masharti yote Mina anayokupa?”
“Kwa kuwa Andy mwenyewe hajui hata kuwa baba kwa mwanae, mama! Atawezaje
kuwa mfano wa kuigwa kwa mwanangu?” “Ndio sasa umeambiwa utamkosa
mtoto.” “Mimi na Mina hatujawahi kushindwana.” Mina akarudi pale
sebuleni.
“Hutafika kuonana na mimi, kama baba na mama hawapo
nyumbani Pius. Ili kumfanya Andy arudishe imani na wewe. Kuanzia
leo, tafadhali anza kufikiria jinsi ya kumuheshimu Andy. Vile alivyo,
ukijua ndiye atakayempa mwanao sehemu ya kuishi kama nitakuwa
naye. Na wakati nyinyi wote mnajifikiria na kujipanga upya, jua
ili kuniona mimi ni mpaka uzungumze na baba pamoja au na mama kwanza.
Wakiwepo nyumbani, ndipo uje. Lasivyo itakuwa ni kutoniheshimu,
na hapo utaniudhi. Nitaondoka na watoto wote, niende nikawawekee nyinyi
wote restrain order msiwe karibu na wanangu kwa kuwa mtawadhuru
kama mlivyonifanyia mimi jana.”
“Na ushahidi wa picha jinsi nilivyoumia kumbe
kuna mtu alijiiba na kunipiga picha pale hospitalini, nesi aliyenisaidia
asubuhi hii ameniambia, nasikia upo mtandaoni. Kila mtu ameona jinsi mlivyokuwa
mkipigana, wakati mimi na mtoto tukiwa katikati yenu, wala hamkujali
hilo. Mkaniumiza. Sitapata shida kuwawekea nyinyi wote wawili restrain
order.” Wote wakashituka
wasiamini kama Mina anayajua hayo yote. Wakapoa haswa.
“Niliwapa dhamana, nikiwaheshimu lakini
naona mmeshindwa. Mmeishia kunidhuru na kubishana kusiko
isha. Sasa ili wote muwe na mahusiano na watoto wenu, naomba nikaishi
kwa wazazi kwa muda wakati nikijipanga na wote tukifikiria
chakufanya sasa na baada ya mtoto kuzaliwa.”
“Majibu yangu kutoka kwa Andy na wewe Pius
nitayapata kwa vile mtakavyofanya kuanzia sasa. Nawaahidi, sitafanya
chochote bila kuwataarifu. Kama nikiwa naondoka kwa wazazi na kwenda
kuanza maisha yangu, nitatafuta ushauri wa kisheria, wote mtawasiliana
na huyo mwanasheria.” Pakawa kimya zaidi.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakamuona mzee Ruhinda akicheka taratibu. Mina
akasimama na kuelekea chumbani, akampita Andy pale alipokuwa amesimama.
“Niliwaambia mimi! Tulieni ili mpange mambo kama watu wazima! Mmeona mambo yenu ya kitoto jinsi yalipowafikisha?
Mmejiharibia sifa bila sababu!” “Mimi ninayo sababu baba. Pius amempa
mimba mke wangu.” “Sasa kwa fujo mnazozifanya hizo, imebadilisha nini?” Akauliza mama Ruhinda.
“Umeharibu sana Andy. Tena nilikwambia unayo
nafasi nzuri yakuongoza haya mambo utakavyo, kwa sababu Mina alikuamini
wewe. Ona ulipomfikisha huyu binti! Wote mmekuwa kama watoto wadogo! Wote mnakosa nafasi ya kuwa na watoto wenu!”
“Ni kwa muda tu baba, naamini akipona atatulia.” “Nafikiri katika vitu
ambavyo unatakiwa ujifunze Andy, kwa kipindi hichi ni juu ya mahusiano.”
Akaanza mama Ruhinda.
“Acha nikwambie ukweli tu, pengine itakusaidia.
Umeshindwa vikubwa mno. Tupo hapa sasa hivi, katika hili
sababu yako WEWE Andy.” “Unampendelea Pius, mama. Kwa nini hum..” “Nisikilize
kwanza Andy, kisha uwamue lolote utakalo. Useme nampendelea Pius
au la, sitajali tena. Mimi ni mama yako, na nina jukumu la kukufundisha.
Umekosea kwa Mina mara ya kwanza, ukapewa nafasi ya pili, UKAHARIBU kwa
kumsikiliza Paulina, lakini napo ukifikiria kwa makini ni kwa kuwa HUJUI mahusiano
Andy.” Mama Ruhinda akaendelea.
“Ukapewa dhamana nyingine na Mina, akakutanguliza
huyu binti katika hili. Mbele ya kila mtu, Mina akakutangaza wewe
ndio utakuwa kiongozi wa haya yote. Nishamsikia baba yako akizungumza na wewe
kwenye simu, akikwambia ukitulia utaweza kuongoza hili jambo
vizuri sana. Lakini hebu angalia hapa tulipo, jinsi ulivyoshindwa
vibaya na kudhalilisha kila mtu mwenye jina la Ruhinda! Wote tupo
kama uchi huko mtandaoni.”
“Usingekuwa kumtelekeza Mina, wala huyu mwenzio
tamaa isingemwingia.” Mama Ruhinda akawa mkali kabisa. “Wewe unaacha
mkeo analishwa, anauguzwa na kutunzwa na mwanaume
mwingine! Eti wewe unazunguka kila mahali sababu ya kazi! Ulitegemea
nini Andy? Tena ushukuru Mina alitulia, angekuwa malaya huyo, angekuua kwa maradhi kwa kubadili wanaume! Sasa badala utulie
na kujirudi, unapigana kila mahali, na sijui kama hiyo kazi bado utakuwa
nayo endapo viongozi wako wataona hiyo video.” Andy kimya.
“Huko unakojificha Andy, lazima utoke na
ukubali kuwajibika kwa kuwa uliamua mwenyewe kuanzisha familia.
Wote sisi tunazo kazi, lakini mbona bado tunakumbuka majumbani
kwetu? Pius huyo ni shahidi. Ana kazi kubwa sana, lakini ameweza
kumudu FAMILIA MBILI! Yake na yako.” “Na bado nyumbani
amekuwa tegemezi.” Mzee Ruhinda akaongeza.
“Haya, umemsikia baba yako! Hutamuita Pius, au kumtuma
popote na chochote, akashindwa. Japokuwa wote mnasema nampendelea
Pius, haya, umemsikia na baba yako? Ndiye mtoto anayepita nyumbani kutuona mara
kwa mara na kutujulia hali kwa simu kila siku. Anajua habari zote za nyumbani.
Sasa jiulize yeye anawezaje, tena bila kuchoka au kubadilika,
na kazi nzito aliyo nayo! Na bado anazo biashara zake, halafu wewe
mwenye kazi moja tu, huna hata biashara, mke mmoja, mtoto mmoja
tu, unashindweje!?” Siku hiyo mama Ruhinda akawa amekusudia, bila
kumuogopa tena.
“Na kama
alivyokwambia mkeo, mtafute baada ya kujifikiria. Ukishindwa,
SEMA. Tena sema haraka uache kupotezea watu muda! Wewe sio wakwanza kushindwa na mambo
ya familia na wala hutakuwa wa mwisho. Sema mapema watu wajue moja.
Twende Ruhinda tukajiandae, turudi kwetu.” Mama Ruhinda akasimama na kwenda
kwenye chumba walicholala usiku huo, Mzee Ruhinda naye akafuata. Pakawa kimya.
Kuruka Moto, Kakanyaga Majivu.
Mina aliondoka kwake na Judy pia ili akamsaidie kazi
nyumbani kwa wakweze. Walifika mida ya
jioni. Hata hawakujua Pius aliondokaje pale Dodoma, lakini mzee Ruhinda alimkataza
kuongozana nao. Wakaondoka yeye, mkewe, Mina, Ayan na Judy. Moja kwa
moja mama Ruhinda akampeleka Mina chumbani.
“Judy atalala na mwenzie.” “Nashukuru mama, labda
nilale na Ayan chumba hiki. Asiwe peke yake.” “Sawa kabisa. Ila ujue vyumba
vipo vingi tu, ukitaka tunaweza kumtayarishia chumba chake.” “Nashukuru mama
yangu. Lakini acha nilale naye tu.” “Basi pumzika, chakula kikiwa tayari
nitakuletea.” Mama Ruhinda akatoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakati anapitiwa na usingizi baada ya kumeza dawa ya
maumivu akasikia kilio sebuleni kama mtu aliyefiwa. Mina akashituka sana,
akatoka chumbani. Kadiri alipokuwa akishuka ngazi kutoka chumbani kuelekea
sebuleni, akagundua ni sauti ya Raza. Mina akasimama kusikiliza.
“Nafikiri pata
muda na Pius, atakueleza vizuri.” “Pius ananidharau baba! Tangia anikatie simu
jana, hapokei simu zangu. Hajarudi nyumbani na wala hajanipigia mpaka sasa!”
“Ni kweli tulikuwa naye Dodoma, nafikiri leo atakuwa nyumbani.” Mzee Ruhinda
akajaribu kumtuliza kwa kuzungumza naye taratibu.
“Kwa hiyo nyinyi wazazi mpo na mume
wangu, na baba wa watoto ambao hawana hatia kuzaliwa wakike, mnamuuza
mtoto wenu kwa mwanamke mwingine!?”
“Najua upo kwenye mshituko Raza, lakini angalia usivuke
mipaka.” Akazungumza mama Ruhinda kwa
kumtahadharisha.
“Najua hamnipendi na mnanilaumu kwa kumzalia Pius watoto wa kike, lakini mkumbuke mwenye uwezo wa
kutoa mtoto wa kiume ni mwanaume wala si mwanamke. Nyinyi mmesoma, mnawezaje kunilaumu mimi na si mtoto wenu!” Raza akaendelea kulalamika huku akilia.
Mama Ruhinda akachukua simu na kumpigia Pius. “Uko wapi?” “Njiani naelekea nyumbani.” Pius akajibu. “Pitia hapa nyumbani haraka.” “Kuna nini tena!?” Pius
akauliza. “Wewe husikii sauti ya mkeo bwana! Hebu njoo
hapa.” Mina akabaki akitetemeka amesimama kwenye ngazi za
kushukia.
“Namjua Mina
ndani na nje. Nimepata leo habari zake zote kutoka kwa mtoto wa mama yake
mkubwa! Mina ni malaya na...” “Raza! Raza!” Mzee Ruhinda akamuita
haraka. “Tafadhali sana.” “Mimi nawaambia ukweli
ili mumjue Mina. Mina ni...” “Najua upo kwenye mshituko, kuwa mwangalifu
sana, haswa kwenye kipindi hiki.” “Mina ndivyo
alivyo hivyo. Yupo kama na jini fulani lakuvuta watu upande
wake, Pius na Andy sio wakwanza.” Mara
Pius akaingia kama aliyekuwa akipita hapo nje nyumbani kwao, hakuwa mbali. Bado
mkewe alikuwa akiongea.
“Huyu Mina alishatembea na mtu na
rafiki yake kipenzi. Akatembea na bosi wao pia. Mina ni malaya asiyeweza kujisaidia.” “Unaongea nini hapa kwa wazazi wangu Raza!? Umechanganyikiwa wewe!?” Pius akashituka
sana kusikia maneno anayoongea mkewe wakati akiingia ndani.
“Nakuokoa Pius, usifikiri wewe ndio
mwanaume wa kwanza kwa Mina.” “Hujui ni
nini unaongea hata kidogo. Nyamaza na usimame haraka kabla HUJAJUTA, vibaya
sana!” “Kwa nini nijute wakati mimi naongea tu?” “Unanijua jinsi
ninavyochukia maneno ya uzushi. Na nilikuonya usifike kwa wazazi
wangu na maneno ya uzushi.” “Huu sio uzushi
Pius, ni ukweli kabisa kutoka kwa ndugu yake Mina, wa damu! Mina
alichowafanyia wewe na Andy sio kigeni. Ni mchezo..” “SIMAMA Raza!” Pius
akaamrisha.
“Pius!” “Kabla hujaniudhi zaidi,
kwanza funga mdomo wako, na utoke
hapa ndani kimyakimya.” Mina akamsikia Pius ambaye hajawahi kumsikia kabla. Anaunguruma
kama simba. Akabaki amesimama kwenye ngazi, miguu ikitetemeka. Raza
akabaki amekaa kochini akilia.
“RAZA!” Pius akaita kwa ukali mpaka Mina akakaa kwenye
ngazi. Raza akasimama kwa haraka. “Mimi ni mkeo
Pius na nina haki.” “Haki yako unaipoteza kwa kuja hapa na kumwaga sumu. Hujui chochote kinachoendelea, unazunguka kutafuta habari za Mina na kuja hapa na kuanza kuongea
kama mwehu!” “Nitajua vipi wakati wewe na wazazi
wako mnanificha? Ulishindwa vipi
kuniambia ukweli?” “Jana uliponitumia ile video na kunipigia simu,
nilikwambia nini?” Raza kimya.
“Nakuuliza wewe? Nilikwambia nini?” “Sasa kwa nini mpaka leo hujanitafuta na jana hukulala
nyumbani!?” “Wewe mara ya mwisho kuzungumza na mimi nilikwambia
nini? Mbona unakataa kujibu?” Kimya. “Sikukwambia nipo Dodoma, nipo kwenye
wakati mgumu sana, ila nikirudi nyumbani tutazungumza?
Sikukwambia hivyo wewe?” “Kwa hiyo ni sawa mimi
kujua mambo mtandaoni?”
“Na
kama wewe na wazazi wako mnanilaumu
mimi kuzaa watoto wa kike, nawashauri mjifikirie kwa upya. Kosa ni lako. Na kama unafikiri mtoto
aliyembemba Mina ni wako, unajidanganya.
Unaambiwa Mina hana uwezo wa kukaa
na mwanaume mmoja. Kama alikudanganya kipindi mumewe amemtelekeza, ukadhani upo naye wewe tu, basi ujue mlikuwa wanaume
wengi tu.” Mina alisikia sauti kubwa kama
mtu amechapwa kofi. Alishituka mpaka akajishika tumbo.
Raza alilia kama amepasuliwa. “Toka Raza.” “Unanifukuza
mimi mkeo, unamuacha malaya huyo
ndani!” “Nitakuumiza Raza, toka.” “Na
nyinyi wazazi mpo hapa mnaacha nadhalilika
mimi sababu ya malaya huyo! Mnadhani atawaletea mtoto wa kiume mwingine!
Kama amewaambia ana mimba ya mtoto wa kiume ili mumpende, basi
mjue Mina ni tapeli. Na kwa kuwa
mmekubali nifukuzwe hapa, basi mjue na watoto wangu hawatakaa wakakanyaga hapa.” “Ona unavyo
jidhalilisha! Nani amekwambia watoto wangu huwa wanakuja hapa kwa sababu
wewe unafika hapa?” Pius akaenda kumvuta na kumtoa nje, Raza akilia. Pakatulia
kimya. Wakasikia magari nje yanaondoka. Mzee Ruhinda na mkewe wakabakia hapo
kama wamepigwa ganzi.
~~~~~~~~~~~~~~
Kila Mahali Moto & Sintofahamu
Ya Hali Ya Juu.
Baba Wa Watoto Wote
Wamekuja Juu Wanamtaka Mina Aliyebeba Suluhu Ya
Watoto Wao.
Ndio Raza Na Andy Wanakumbuka
Shuka, Kushakuchwa.
Maji Yashamwagika.
Ayvin YUPO Mzima
Wa Afya Njema, Tumboni Kwa Mama Yake Na ANAKUJA. Ready Or Not, Ayvin Muda Wake Utakapowadia Atakuja Tu Kwenye Ulimwengu Huohuo
Wa Wazazi Wake Na Wanao Wazunguka.
Kuna Garama
Ya Kulipa Ambayo Pesa Na Elimu Yao Vinashindwa Kuwasaidia.
Nini
Kitaendelea?
0 Comments:
Post a Comment