Siri ya mtoto, ajuaye
Mama, na DNA siku hizi. Kumbe ukimya wa Mill ulikuwa na mengi. Majibu
yalitoka kama alivyodhania. Watoto wote hawakuwa wake. Lakini aliondoka
nchini Marekani akiwa amekabidhiwa kisheria kuwa ni wake kihalali,
kwamba Kisha hawezi KUWACHUKUA. Alipopata tu majibu akamtafuta
mwanasheria wake. Akamueleza ilivyo.
“Nitafanyaje na watoto nimekabidhiwa na
mahakama?” “Wewe ulitaka nini?” Mwanasheria wake
akamuuliza. “Si sawa hawa watoto kulelewa na mtu baki! Wanahaki ya kulelewa na
wazazi wao!” “Basi hiyo ni rahisi sana. Cha kwanza, Kisha alikudanganya.
Na wakati ukidai hao watoto ulijua ni wako. Huo mkataba
mpaka hapo ni haramu. Si halali. Nitafungua kesi. Ila itabidi urudi nao
huku, vifanyike vipimo upya, kisha kumshitaki Kisha.” Mill akafikiria.
“Nafikiri tufanye hatua kwa hatua.
Nisingependa tena kesi. Vipimo vya huko vitakapo kamilika, ndipo
tumtafute Kisha tuone anasema nini. Akianza ukorofi wake, ndipo nitamshitaki
kwa hakika maana alijua kabisa alichokuwa akikifanya. Na kinachoniuma
zaidi ni kutumia watoto kujinufaisha. Ni ukatili wa namna gani
huo?! Ni mwanadamu gani eti anakubali watoto wake walelewe na mtu mwingine,
tena kwenye Bara jingine kabisa!” “Kwake wewe si mtu baki, Mr Mgini. Unaweza
usiwe umewazaa lakini wakawa ni watoto uliolea. Na najua anajua jinsi unavyo wapenda.
Nina uhakika kwa jinsi ulivyo wahangaikia hao watoto na kupoteza kila
kitu kwa ajili yao, kama wangekua ni watoto wa kawaida, nina uhakika
usingewarudisha.” Mill akabaki kimya maana ni kweli.
Huyo mwanasheria
ametembea naye kwa muda mrefu sana kwenye hiyo ndoa yake. Anawafahamu hao wote
watano ndani na nje. Mill, Kisha, Trey, Miles na Mia. Hawawezi hata
kujificha kwake. Wakazungumza mengi, Mill ikamlazimu kuondoka nchini kwa
haraka.
~~~~~~~~~~~~~~
Huku kwa Pam
yeye hana habari, anajua bado Mill amezira. Ila mkono ulikuwa ukiendelea
vizuri. Siku anapata ajali akienda shuleni kwa mwanae alicha mazingira ya kazi
akijua anaweza fukuzwa maana ni kama alilazimishia baada ya kukataliwa.
Sasa alipopata
ajali, alipokwenda kupeleka vipimo vya hospitalini na kumuonyesha bosi
wake kumuaminisha kama kweli ameumia na ameambiwa hataweza tumia huo
mkono kwa miezi mitatu, hawezi kunyanyua vitu vizito, wala bosi wake hakutaka
kupoteza muda. Akamwambia ataangalia akipona kama kutakuwa na nafasi yake,
maana siku hiyohiyo anatafuta mtu wa kuziba pengo. Pam akaondoka hapo
akijua hiyo kazi nayo imeisha.
Kwa hiyo
alikuwepo tu nyumbani na akajua ni mpaka apone kabisa ndipo itambidi kuanza
kutafuta kazi kwingine. Akaonelea kipindi hicho ndio muda muafaka na yeye
kurudi kusalimia kijijini kwao, kabla hajarudi mjini kutafuta tena kazi. Hata
hivyo Shema alikuwa amefunga shule. Ilikuwa ni kawaida yake kwenda kumuona mama
yake.
~~~~~~~~~~~~~~
Siku hiyo mchana
wakati dereva alipoleta matumizi akamuomba mama Shema wazungumze. Wakatoka nje
kabisa kwenye gari. “Nimetumwa na bro. Anauliza kama anaweza kuja jioni? Ni muhimu,
ila kama kuna wageni wako wengine, anaomba muda ambao hautakuwa na muingiliano.
Na ameahidi hatakuchukulia muda mrefu.” Pam akashangaa sana moyoni mwake
ila akamjibu amwambie yeye atakuwepo.
Mjumbe hauwawi
akarudisha jibu, lakini Pam akaelewa kwamba ndio hataki amkute pale Mgaya. “Kwamba
anadhania kwangu ni dangulo!” Akajilalamisha lakini akimsubiria kwa hamu
haswa.
~~~~~~~~~~~~~~
Jioni Mill
akawasili hapo anapoegeshaga gari akiwa anajishauri kama aingie au atume mtu,
akamuona Shema dirishani kwake. Akashusha kioo. Akamsalimia baba yake na
kupanda garini. Alikuwa mchafu, jasho linamtoka haswa. Mill akacheka. “Hivi
unakumbuka kunywa maji lakini?” “Nakunywa. Wakati mwingine mama anamtuma mtu
aniite, nirudi nyumbani halafu ananipa maji.” “Kwa hiyo wewe mpira ni kuanzia
asubuhi mpaka jioni?” “Hivi nilikuwa katikati ya mechi mama akanilazimisha
kurudi.” Mill akabaki akicheka akimtizama.
“Naenda kwa
mama.” “Mwambie nipo hapa nje, naomba atoke tuzungumze.” Shema akashuka garini
kwa haraka kuingia ndani kumuita mama yake. Pam akashangaa kwamba amegoma
kuingia ndani! Lakini akatoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Akasimama
dirishani. Akashusha kioo maana bado gari ilikuwa ikiwaka ili apate upepo.
Akashusha kioo pale aliposimama. “Unaendeleaje?” “Vizuri tu. Na wewe pamoja na
watoto?” “Sisi wazima. Kama hutajali, naomba upande kwenye gari, nina
mazungumzo ya msingi kidogo na sitakuchukulia muda mrefu.” Akaguna na
kupanda.
“Hivi unajua
hapa kwangu si dangulo, Mill? Useme kwamba huwa naingiza wanaume unaohofia
utakutana nao!” “Nishakutana na mmoja, inatosha. Hata hivyo sikutegemea
tofauti Pam. Wewe bado ni mdogo na ni mzuri tu. Tokea mwanzo nakuacha nilijifariji
kuwa ungeumia kuwa nimepotea, lakini nilijua ungeendelea na maisha kama hivi.
Nasikitika njia zangu nilizochukua zimekuwa ndefu na si sahihi, lakini
sikuwa na nia ya kukuumiza. Naomba unisamehe ila nashukuru
Mungu ameweza kukurudishia niliyokupokonya.” Akaendelea.
“Mwanaume
unayemuamini kuliko mimi, na marafiki wa kweli si wadanganyifu
kama mimi.” Pam alishikwa na kitu, akashindwa kujibu. Alinyamaza kimya.
“Hii ni bahasha.
Ndani kuna nyaraka za muhimu SANA. Tafadhali zitunze. Mimi naondoka tena
nchini.” Pam alishituka, hakutegemea. “Natarajia kurudi
nitakapokamilisha mambo yanayonipeleka huko. Ila miezi miwili ikipita sijarudi,
tafadhali fungua na usome kwa makini. Humo ndani kuna maelekezo
ambayo nina uhakika kwa akili yako, hutachanganyikiwa. Nimejitahidi
kuweka maelezo kwa lugha nyepesi sana. Sijui kama umenielewa?” Pam alibaki kama
amepigwa na ganzi.
“Tafadhali
naomba uulize swali ili nisikuache njia panda. Maswala ya mtoto na
shule, vipo sawa. Ada ni kama ulivyosikia. Italipwa mpaka amalize pale.
Na ninavyomuona Shema, wataendelea kumlipia tu mpaka amalize grades zote
pale. Na pia kama hatabadilika, nina uhakika watamsomesha na chuo.”
“Gari iliyokuwa
ikiwaletea matumizi, ni yenu. Kadi za gari zipo humo ndani. Upo huru
kumuacha yuleyule akawa dereva au ukatafuta dereva mwingine. Lakini kuanzia
kesho utaletewa gari. Najua kuhama ulikataa. Lakini usafiri nafikiri ni
muhimu. Au nakosea?” “Nashukuru japo na sisi tutaenda kijijini.” “Ulipanga
kwenda lini na utataka kukaa huko kwa muda gani?” Akatulia.
“Kama ni mambo
ambayo labda haupo tayari kunishirikisha, labda niseme si kwa kutaka kukuingilia.
Nilikuwa na ushauri. Sijui naruhusiwa?” “Huniingilii Mill! Nilikuwa
nikijaribu kufikiria!”
“Ile kazi nilifukuzwa.
Nimeambiwa ameshapata mtu wa kuziba nafasi yangu.” “Pole.” “Yote maisha tu.
Najua nitapata ingine ila nataka kufuatisha ushauri wa yule daktari.
Kuupa muda mkono, upone kabisa. Naona nitaenda kuusubiria kwa mama
wakati nikisubiria na shule ya Shema kufungua. Kwa hiyo nitakuwa huko
muda wote mpaka labda siku chache kabla ya shule yake kufunguliwa. Sasa
nitafanyaje na hilo gari?”
“Unataka
kuondoka lini?” “Kesho kutwa ili kesho ninunue vitu muhimu.” “Basi mtumie
huyohuyo dereva. Kesho akuzungushe ufanye manunuzi yako. Aje kesho kutwa tena
kuwapeleka kituo cha mabasi. Mkirudi, mnamtaarifu atakuja kuwapokea.
Gari nitamwambia aache nyumbani kwangu mpaka mtakapo rudi. Au unaonaje?” “Sawa.
Nashukuru.” “Karibu.” Wakatulia kidogo. Akaendelea.
“Naondoka,
lakini sitaki kupoteza mawasiliano na Shema. Nimekuja na simu ili tuwasiliane
kipindi ambacho sipo ili tusikuingilie na simu yako.” Pam
akamwangalia, akaona anyamaze tu. “Nikirudi nitaichukua. Lakini
kama msimamo wako ni uleule, hutaki awe na simu, basi nisaidie hata
namba ya simu ya bibi yake, niwasiliane naye kwa kupitia bibi yake, mama
Eric.” “Wewe mpe tu. Ila kama utarudi, tafadhali uichukue. Sitaki
awe na simu sasahivi.” “Sawa.” Akatoa simu na kumkabidhi.
Pam akashangaa
sana. “Kwamba ndio unampa Shema hii simu mpya na ya ghali hivi!?” “Wewe
ulitegemea ningempa simu gani!?” “Hata iliyotumika!” “Na nani?” Hapo
akakwama. “Kwamba mwanangu ndio yeye atumie vitu walivyochoka watu
wengine! Sasa anafaida gani ya kuwa na baba!” “Mmmh!” Pam akaendelea
kushangaa. “Nimemnunulia na kijipochi chake chakufunga mkononi akiwa anacheza
ili isimkere na asipoteze kwa kuiacha chini.” Akamuonyesha jinsi ya kuifunga.
Ilikuwa na mikanda mizuri sana ya kufunga juu kabisa ya mkono. Pam akabaki
akishangaa.
“Binafsi sina la
nyongeza. Mengi nimejieleza humo kwenye hiyo bahasha niliyo kukabidhi. Ila nina
ombi Pam. Tafadhali nisikilize na ulizingatie.” Pam akamwangalia.
“Shema ni mtoto
wangu wa kwanza. Nimekosa maisha yake ya nyuma, lakini nimekusudia ya
mbeleni nisikose. Kwa garama yeyote ile, sitamtelekeza. Na
nakushukuru sana kwa nafasi unayonipa kuwa naye, japo siridhiki.
Haya maisha mnayoishi hapa, ni WEWE umechagua. Na pengine mimi nimechangia
kwa asilimia kubwa sana. Lakini nakusihi Pam, mwanangu asiendelee kuishi maisha
ya kimasikini, wakati mimi ninayo pesa.”
“Chakula kisiwe
cha kuhesabu. Kama utakuwa umeangalia akaunti yake, utagundua
inayo pesa nyingi tu. Na hata kama utaamua kuolewa na huyo Mgaya, naomba mtoto
wangu asiishi kwa uwezo wako na mumeo, ila uwezo WANGU.”
“Mill, umekuza jambo la dokta Mgaya…” “Sio dokta.” Akakanusha kwa jazba.
Wivu tu.
“Sawa. Lakini
ndivyo anavyofahamika hapa. Lakini..” “Ndivyo alivyojitambulisha na
kwangu, mbele yako na hukukanusha. Nimemkuta akikuhudumia ndani ya chumba
chako, kitandani, wala si eneo analofanyia yeye kazi,
kuashiria ni kweli mpo na mahusiano. Hilo si tatizo, ila tatizo
ni mtoto WANGU.”
“Mimi sina
mambo ya wanawake. Sina wasiwasi akiwa kwangu. Najua umeniambia nina laana.
Nimerithi kutoka kwa baba yangu, lakini Pam, nimekusudia
kubadilika hata kabla hujaja kwenye maisha yangu. Chumba tulicho lala mimi na wewe,
pale kwa Mike, hapakuwahi kuingia mwanamke, hata daktari, isipokuwa wewe.”
Pam akaangalia pembeni.
“Nimekusudia kubadilika.
Japo njia yangu imekuwa na vikwazo na sijabahatika, lakini sikati tamaa.
Naamini siku moja na mimi naweza kupata atakayenipokea kama nilivyo.
Ila kwa sasa ukweli najitahidi. Nikiwa na Shema, najitahidi kuzungumza naye na
kumuelewesha nilikopita na kukosea. Mfano mzuri wa kuiga. Nafanya kwa
maneno na vitendo. Naomba na wewe jitahidi.”
“Kutaneni
sehemu ingine. Mambo yenu yatakapokuwa yamekamilika, na yeye mpeleke kwa
wazazi kama ulivyonipeleka mimi, na Shema ajue hilo. Ajifunze. Mkioana
ndio angalau amuone ndani lakini si kabla. Maana na mimi
ananiona nipo. Naingia palepale mnakoishi na mwanangu, ambapo Mgaya naye
anaingia na kuwa huru mpaka kitandani! Tunakuwa tunamchanganya! Hata
kama unataka ajifunze kwa kina baba Pili unao waamini kuliko mimi,
halafu anaona maisha mengine tunayoishi, sidhani kama utafanikiwa sana. Ni hilo
tu. Na samahani kama nimevuka mipaka.” Yaani mpaka hapo yeye Pam ndio malaya!
Akanyamaza hakujibu. Alikabwa na kitu kooni, alishindwa kuzungumza kabisa.
Kwanza swala la
Mill kuondoka tena nchini lilisha mchanganya. Leo anaaga kama
anaacha wosia! Akabaki ametulia kitini akifikiria. Na yeye Mill akatulia
kabisa. Akawa kama amekumbuka kitu. “Wewe unaondoka lini?” “Tunaondoka siku
mbili kuanzia sasa.” “Kwamba unaondoka na watoto kabisa?!” “Ndiyo.” Pam
akatulia akijua ndio kwa heri, kuja kuonana ni majaliwa.
“Unampango wa
kuja kurudi tena Tanzania, Mill?” Akauliza kwa wasiwasi. “Namuomba Mungu
anisaidie nije nirudi salama. Naogopa nisije nikasema kitu ikawa kama
mara ya mwisho nilipokuaga. Ila jua nia ya kurudi ipo. Sitaki Shema akue
bila mimi. Hata kama hatutakuwa tukiishi nyumba moja, ila angalau ajue nipo na
namjali. Mengine ni matokeo tu.” Pam akatulia.
“Kama hakuna
jingine, basi nisikuchukulie muda wako zaidi. Ni hayo tu, nilitaka
kuzungumza na wewe. Unafikiri Shema atakuwa tayari nitoke naye kidogo au ndio
mpira umechanganya? Nataka nimuage.” “Akijua unasafiri anaweza kukubali kuacha
mpira ili muagane. Acha nimuite. Nimemlazimisha atulie kidogo, ale na
kunywa maji ndio arudi mpirani.” “Basi nitashukuru. Ila na pia akionekana ni
lazima sana kurudi kucheza, usimlazimishe. Naweza tenga muda kesho jioni
nikaja kumuaga kabla hamjaondoka. Si ni sawa?
“Mill, hapa
kwangu hakuna wanaume wanao ingia. Tafadhali naomba uelewe.
Siku ile ulimkuta humo ndani kwa sababu nilikuwa na kizunguzungu. Nakiri
mazingira pengine yanaweza yakawa hayakueleweka, lakini si kwamba ni
kawaida yake kuingia mle ndani. Siwezi fanya hivyo na Shema yupo! Mimi si malaya, Mill! Na wala si mjinga.”
“Sijasema hivyo, ila nakutahadharisha tu. Mapenzi yanaweza kukolea,
ukaona kila kitu kipo sawa na kina wezekana. Na pia tafadhali usimuamini
kupita kiasi. Shema bado mdogo na anakuhitaji.”
“Kwamba
unachoniambia hapa niwe nafanya ngono na kinga?!” “Mimi nakusihi
kuwa tu makini, ndio hilo tu. Sitaki kukuudhi, hilo ni ombi.
Maana unaweza nikataa mimi ukidhania mimi ni mchafu sana kama
baba yangu au babu yangu kama ulivyosema, ukadhania huko kwa
Mgaya ni salama kwa sababu yeye yupo karibu yako. Ndio naomba kuwa makini.”
Pam akashuka bila ya kujibu.
Mara akaona
kikundi cha watoto wanaingia ndani kwao wakimuita Shema. Akajua kumtoa hapo ni kumsumbua.
Akampigia honi Pam, akageuka. Akamfanyia ishara ya kumuita. Akarudi. “Naona umuache
tu. Nitamfuata kesho kumuaga.” “Sawa.” Pam akaondoka.
Kwa Mina.
Mina alipoteza fahamu kwa muda wa kutosha. Baada ya
muda akasikia kwa mbali kelele, kisha akapotea tena. Akasikia akiitwa tena na
tena, lakini safari hii hapakuwa na kelele. Kulitulia. “Mina! Mina!” Huku
wakimtingisha. “Pius!” “Mimi ni dokta Kwayu! Unajisikiaje?” Mina akatulia
kidogo. “Unaweza kufungua macho yote?” Akajitahidi akafungua.
“Kichwa kinauma sana.” “Unakumbuka una watoto
wangapi?” Mina akafikiria. “Wawili. Ayan na Ayvin.” Akajibu taratibu. “Naomba
ufikirie vizuri.” Mina akanyamaza. Wakamuona analia.
“Naomba usilie Mina. Pole.” “Hayakuhusu Pius.”
“Yananihusu, Mina ni..” “Naomba utoke. Hapa hakuna mtoto wako.”
Mina akasikia tena Andy na Pius wakibishana. “Naombeni wote msubiri
hapo nje. Tafadhali sana.” Daktari akataka watoke. Wakaendelea.
“Kwanza wewe ndiye uliyempiga!” Akasikia sauti ya Pius
akimshutumu Andy. “Pius nakutahadharisha wewe!” “Utanifanya nini?
Roho yako ni mbaya Andy. Na ukisababisha chochote kitokee kwa mtoto
wangu nita..” “Utanifanya nini?” Akauliza Andy kwa jeuri. Mina akafungua macho.
Lakini likafunguka moja. Akawatizama. Wote walikuwa wameumia.
“Muongo mkubwa wewe Pius. Upo hapa kwa ajili ya
mke wangu wala si mtoto peke yake.” “Ndiyo. Nipo hapa kwa ajili
ya Mina na mtoto wangu. Nani amekwambia ninapinga hilo!?
Wewe vipi Andy!?” Wakaanza tena hapo hapo chumbani. Mina akagundua humo ndani
ya chumba yupo na nesi pamoja na daktari. Akajitahidi, akakaa.
“Naomba utulie Mina.” “Acha kumgusa mke wangu.” Andy
akamsukuma Pius aliyemuwahi Mina. “Naomba mimi
niondoke niwapishe jamani! Hivi sitaweza.” Mina akaanza kulia.
“Naombeni mtulie, ili tujue hali yake! Huyu ni mama mjamzito. Mmempiga mpaka mmemuumiza
jicho. Sijui ni kwa kiasi gani mmemdhuru! Ameanguka mpaka sakafuni!” “Andy
ndiye aliyempiga.” Akadakia Pius.
“Sawa. Lakini naomba nafasi nimuangalie. Maana hata
huyo mtoto huko tumboni hatujui ameathirika kwa namna gani!” “Hakika
Andy nitaku...” “Acha kunitisha Pius. Ilikuwa bahati mbaya! Nilitaka nikupige wewe.”
“Hivi wewe, unamtaka huyu mtoto kwa kiasi gani?” Akauliza
nesi, mama mtumzima kidogo. “SANA.” Akajibu Pius. “Basi anza kutoka wewe ili
mkeo ahudumi..” “Sio mke wake. Ni mke wangu MIMI.” “Haya, na wewe uliyempiga
mkeo mbele ya umati, ndio uanze kutoka,
ili daktari aangalie madhara uliyosababisha kwa mkeo.” Nesi akaongea kwa msisitizo. “Siwezi kumuacha tena Pius na
mke wangu. Yeye ndio atoke kwanza.” “Na mimi siwezi
kukuacha wewe na Mina humu ndani. Umebeba chuki sana kwa Mina, hutashindwa
kumdhuru mtoto wangu. Sikuamini!” Pius naye akagoma kutoka.
Wakaanza tena.
Mina akasimama. Akavuta pochi yake iliyokuwa mkononi
kwa Andy. Akataka kutoka, wote wakaanza kumfuata. “Sitaki mtu anifuate.
Tafadhali sana Pius na Andy. SITAKI. Nyinyi wote si salama kwangu wala mtoto
wangu. Narudia, naomba wote MSINIFUATE.”
“Ila, kila mmoja kwa wakati wake, kuanzia sasa hivi, lazima
afikirie kwanza jinsi atakavyoweza kuishi na mimi pamoja na
Ayvin. Ukishapata jibu ndipo unitafute.” “Mimi nakufuata Mina kwa sababu
najua jinsi yakuishi na..” “Nisikilize Pius. Tafadhali nisikilize.” Mina
akamtuliza, jicho likimuuma haswa.
“Wewe si unanipenda?” “Sana Mina.” “Hamuwezi
kunifanyia hivyo mbele yangu! Huko ni kunidhalilisha.” “Naomba Andy
utulie. Tafadhali sana.” Mina akawa mkali na yeye. “Basi kama unanipenda
kwa kiasi hicho, na kumpenda Ayvin kweli, tafadhali pata muda wakujifikiria.
Fikiria mazingira atakayokulia Ayvin, kama nilivyokwambia mwanzoni kabisa
tulipofika tu hapa.” “Nimef..” “Unakaribia kuniudhi Pius!” Mina
akamtahadharisha.
“Nakusikiliza Mina.” “Hivi mnavyofanya ndivyo
unavyotaka mtoto aje akute haya mazingira?” “Namshangaa sana Pius.” “Tafadhali
sana Andy, nyamaza. Nilikupa dhamana yakuendesha familia yetu, naona umeshindwa.
Umejawa na hasira, mpaka umeniumiza. Hasira zako zimeisha sasa? Maana ni
kama ulikuwa ukitafuta jinsi ya kuniadhibu, leo umepata.” “Ilikuwa
bahati mbaya Mina! Pius..” “Naomba nyamaza na ujiangalie nafsi YAKO
kabla hujamnyooshea kidole mwingine. Nyinyi wote wawili. Mmekuwa kama
watoto bwana! Mtakuja kuniulia watoto wangu bure! Nipambane na nyinyi,
na nguvu ya nje pia!” “Mimi nakulinda Mina.” “Wewe unamlinda kwa lipi Pius?
Acha unafiki ili wewe ndio uonekane mzuri!”
Wakaanza tena. Mina akaondoka
katikati ya malumbano yao.
Alichofanya Mina, alitoka tu hapo na kukimbilia ofisi
ya jirani akajificha chini ya meza, akatulia. Akasikia wanatoka wakikimbia
kulia na kushoto huku bado wakigombana. Akajua lazima watakimbilia nje ya
hospitali ili kumuwahi. Palipotulia, kama baada ya dakika 20 hivi, ndipo
akatoka chini ya meza mwenye ofisi akimshangaa.
~~~~~~~~~~~~~~
“Naomba niitie dokta Kwayu. Alitakiwa kuniona muda
mfupi uliopita, mwambie Mina Ruhinda.” Mina akakaa, yule mtu akapiga simu,
kweli dokta akarudi akiwa na mshangao. “Najua unafahamiana na Pius, tafadhali
nitibu bila kumwambia kwa sasa ili angalau nipumzike kwa leo.
Sijisikii vizuri.” “Naona na jicho limezidi kuwa jekundu.” Akaanza kumpima pressure, haikuwa mbaya. Hilo likamfurahisha Mina.
“Wanakutafuta sana.” “Nisaidie sehemu ya
kupumzika tu kwa leo, mpaka baba mkwe wangu aje. Hapa hakuna
kitakachofanyika kama hawa wawili watakuwa pamoja. Na ninajisikia kuchoka.”
Yule daktari aliposikia mzee Ruhinda mwenyewe atafika hapo, akaona jambo la
msingi kujulikana yeye ndiye aliyetoa msaada. Akaandika kuwa alazwe, ili
kuangaliwa zaidi. Na kweli vipimo vikaanza.
Kwa Raza.
Rafiki wa Raza, akaona video ya Pius na Andy wakipigana,
Mina akitajwa. Na yeye akamtumia Raza shoga yake. Raza akaangalia,
hakuelewa vizuri lakini akawa ameingiwa hofu. Akamtumia hiyo video Paulina wifi yake anayejua hawezi kujizuia kwenye
mambo ya watu. Alipoona ameifungua tu, akampigia lakini Paulina cha umbea hakupokea.
Kumbe Paulina ameshituka sana, haraka akampigia simu
baba yake. “Wanao wanauana Dodoma.” Mzee
Ruhinda akawa hajaelewa, hapo hapo Paulina na yeye akamtumia hiyo video baba
yake, mama yao alikuwa karibu, akampokonya simu mumewe aone yeye maana alikuwa
akiwasikiliza Paulina na baba yake.
Paulina akawapigia wote wawili baada ya kukadiria
muda. Akajua baba yake ameshaona. “Sasa kwa kifupi mzee
Ruhinda, vijana wako wapo mtandaoni. Wanampigania Mina, na yeye mwenyewe
Mina, wamempiga, ameanguka na amezimia. Video hiyo niliyokutumia nimetumiwa na
Raza. Ananipigia mpaka sasa hivi, sijapokea.” “Mungu wangu!” Akasikika mama Ruhinda.
“We Ruhinda si nilikwambia mimi?” “Pius aliniahidi
hatafanya fujo. Ningejuaje kama wataishia kupigana huko!? Mimi nilikuwa
na shuguli zangu leo, sikuwa tayari kwenda Dodoma!” Mzee Ruhinda akajibu lakini
akiwa ameishiwa nguvu kama anayetafakari chakufanya kwa haraka.
“Sasa ndio uende. Maana mwishowe watauana kweli.” “Wewe mama mpe baba hiyo video ajionee mwenyewe. Wote wanatema
damu. Aibu tupu hii jamani! Na sijui Raza mtamwambia nini!” “Hilo sio la
sasa hivi, inabidi kumtafuta kwanza Mina.” Akajibu Mzee Ruhinda.
“Sasa mama wewe mtafute Pius. Akikusikia
wewe, atatulia.” “Mimi nashauri tuongozane tu mama Pius.” “Ujue huyu
Pius anatafuta matatizo jamani! Ni nini anakuwa kama amechanganyikiwa!”
“Wewe mama nenda huko huko, hii ni aibu ya mwaka.” Paulina akasisitiza.
“Mungu wangu Raza ananipigia na mimi! Namwambia nini
mimi huyu mtoto!” Mara video kama
aliyowatumia Paulina ikaingia kutoka kwa Raza, safari hii kwenye simu ya
mama Ruhinda. “Amenitumia na mimi!” “Amechanganyikiwa,
anataka majibu.” “Naona twende wote Dodoma.” Mama Ruhinda akasikika kama
aliyekwisha ingiwa hofu. “Sio kwa kukimbia sasa! Wewe pokea simu. Mwambie
unaelekea Dodoma, ukirudi mtazungumza. Acha nitafute tiketi za kuondoka leo.”
Mzee Ruhinda akajitoa kwenye conference call
kati yake, Paulina na mkewe.
Kwa Mina.
Mina alilala mpaka jioni, ndipo akaamka. Akaamua
kumpigia simu mama Ruhinda. Alipomkosa, akampigia simu mzee Ruhinda. “Tunakutafuta mama, tunakaribia kuchanganyikiwa.”
“Poleni baba. Lakini hali sio nzuri. Nilirudi hospitalini, kichwa kinauma na
jicho nalo lilivilia damu, limeanza kujaa.” “Hapa ndio tumefika Dodoma.
Tumekuja kukuona. Kwahiyo...” “Tafadhali usiwaambie kina Andy, baba.
Nakuomba sana. Wanafanya fujo zisizoisha. Wameniumiza mimi, lakini
nashukuru Mungu vipimo kwa mtoto anaonekana yupo salama. Naomba nipumzike kwa
leo tu, kesho ndipo nitajua chakufanya.” Mina akabembeleza.
“Kwa hiyo hutaki wajue hata ulipo?” Mzee Ruhinda akauliza. “Tafadhali
nisaidie baba yangu, angalau nipumzike kwa leo tu.” “Basi kwa kuwa watu wote
wanawasiwasi, nitawaambia upo hospitalini, na umeomba muda. Ukiwa tayari
utawatafuta.” “Sidhani kama wataelewa baba!”
Mina akatilia mashaka na kuanza kulia. “Mama yao
amezungumza nao sana. Naona wameelewa, wametulia. Tutazungumza
zaidi nikifika hapo. Hatutakawia.” “Nashukuru baba.” Mina akamuelekeza
alipolazwa, wakaelewa na kuagana.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakati mzee Ruhinda akizungumza na Mina, mama Ruhinda
alikuwa akigombesha wanae hao wakiume. Raza naye alikuwa ameshapaniki
hakuna anayepokea simu yake, hakuna anayempa majibu yakueleweka. Akamtumia na mumewe
hiyo video kisha akampigia. “Sasa hivi sipo kwenye
wakati wakuzungumza wala kubishana na wewe Raza. Tutazungumza baadaye.”
Hapo Pius alikuwa kwenye kumtafuta Mina.
“Umeangalia hiyo video niliyokutumia
lakini?” “Nilishatumiwa na watu zaidi ya wawili, wewe sio wa kwanza. Naomba
nikuage.” “Hivi unajua ni kwa kiasi gani umenivua nguo hapa mjini wewe Pius!
Kumbe wewe ndio..” “Nisikilize Raza. Nimekwambia sina muda sasa
hivi wakugombana na wewe. Nipo kwenye wakati mgumu kuliko AIBU yako. Naomba nikuage kwa sasa, tutazungumza
utakaponiona nyumbani.” “Yaani unasafiri bila..” Pius akamkatia simu, ndipo Raza akampigia tena mama
yake mkwe.
~~~~~~~~~~~~~~
Raza akapiga simu tena na tena safari hii akiwa na megi.
Kutukanwa na mumewe, kukatiwa simu bila maelezo ya
kueleweka, kumdhalilisha, na kufichwa na wakwe pia. Alipiga mpaka
mama Ruhinda ikabidi apokee.
“Mimi ndio nimekuwa mtu wakupata habari nzito
kama hizo mitandaoni kweli! Kwa ubaya gani huo ambao mmeshindwa
kuniambia nyinyi kama wazazi wangu! Mnajua jambo kubwa hivyo mnanificha!
Mina anazaa na mume wangu nyinyi mnanyamaza!” “Ni vile upo kwenye mshituko Raza mwanangu na unahasira.
Lakini..” “Halafu Pius ananikatia
simu, ananiambia hana muda wakunisikiliza! Paulina naye hataki
kupokea simu zangu! Lakini hata mfanye nini, hata kama mnanichukia mimi,
mkumbuke mimi ni mke halali wa Pius. Tena wa kanisani kabisa. Nimezaa
naye watoto wawili. Ten...” Raza aliendelea kuongea, mama Ruhinda
akisikiliza.
Mwishoe akaweka ‘mute’ kwenye
simu yake ili asiwasikie wao, wakati yeye akiendelea kuongea bila kunyamaza
huku akilia kwa uchungu sana.
~~~~~~~~~~~~~~
Mama Ruhinda
akaweka simu pembeni Raza akiendelea, akamgeukia mumewe. “Huyo alikuwa nani?”
“Mina. Yupo hospitalini ameomba nisiwaambie Andy na Pius.” “Afadhali, wajinga
kabisa!” Mama Ruhinda akawa ameshachoka na kuchukia kabisa.
“Nimemuomba Mina niwaambie ila wasiende, wamuache
atulie kwanza.” “Wewe ungewaacha wahangaike usiku kucha mpaka kesho au
hata siku tatu baadaye. Hawana akili kabisa! Huyu Pius mkewe bado anaongea hapa
kwenye simu. Analia na kulaumu kila mtu! Pius kamkatia simu na haonekaniki
kujali.” “Sasa kabla hajaaribu na huko nyumbani kwake, ni heri kumtuliza
Pius, ili aweze kuzungumza na mkewe.” Mama Ruhinda akarudi kwenye simu akakuta
bado Raza anahesabu jinsi anavyopuuzwa kwenye hiyo familia. Mama
Ruhinda akashindwa hata kupenyeza neno. Akabaki kimya na kuendelea
kumsikiliza.
~~~~~~~~~~~~~~
Mzee Ruhinda akawapigia vijana wake. “Sasa naomba mnisikilize kwa makini.” Akaanza baada
yakuwapata wote kwenye simu na kuwaunganisha. “Mina ametutafuta
mimi na mama yenu.” “Yuko wapi!?” Andy akauliza wa kwanza. “Naomba unisikilize Andy. Inaonekana huyu binti umemjeruhi
sana. Ameomba muda wa kujitibu na kupumzika, atawatafuta.” “Lini?” Akadakia
Pius na kuendelea. “Na mtoto wangu je, baba? Yupo
salama? Maana Andy alimpiga vibaya sana, akaanguka vibaya sana. Hajadhurika?”
“Kama hayo uliyajua Pius, kwa nini kwenda kuanza kupigana mbele yake akiwa
mjamzito?” Mzee Ruhinda akauliza.
“Ni Andy huyo baba! Sio..” “Acha kujitetea
Pius. Nilimkuta huyu Pius ameshika tumbo la mke wangu! Ulitaka
nikufanye nini?” “Mimi nilikuwa nashika mtoto wangu sio Mina! Roho yako mbaya
wewe Andy.” “Wewe unamtaka Mina sio...” “Mimi nakujua Andy wewe, roho yako
mbaya huwezi...” Wakaanza tena kubishana
hapo kwenye simu baba yao akiwasikiliza.
“Sasa hayo ndiyo yanayomfanya Mina ajione hayupo
salama akiwa na nyinyi.”
Mzee Ruhinda akawakatisha. Wakatulia.
“Pius, naomba mtafute mkeo mzungumze na
urudi nyumbani.” “Siwezi kurudi nyumbani bila ya kumuona Mina, baba. Hapo Raza atanisamehe.
Shida yote hiyo itakuwa bure kabisa! Nawezaje kwenda kulala nikiwa sijui
hali ya mwanangu?” “Sasa Mina hataki kukuona.” “Mimi niambie alipo, najua Mina
atataka kuniona mimi. Tatizo ni Andy.” “Pius jiangalie wewe!” Andy akamuonya.
“Kumbe nani aliyempiga Mina?
Ulitukuta tumetulia, ukaanza fujo. Kama wewe unahasira sana, mwache Mina uone kama sijamtunza vizuri kuliko wewe.”
“Pius! Tafadhali tafuta amani.” “Anataka kumuua mtoto wangu kwa makusudi
baba! Sitamruhusu.” “Nitawatafuta kuwataarifu hali ya Mina.” “Baba!” Mzee
Ruhinda akakata simu na kumgeukia mkewe.
~~~~~~~~~~~~~~
“Naomba umuage Raza, tuzungumze.” “Sasa
nitamuagaje wakati bado anaongea na kulia?” “Wewe muage, mwambie utampigia
baadaye. Usisubiri jibu. Hawezi kumaliza leo, yupo kwenye mshituko
huyo.” “Na kweli.” Mama Ruhinda akajaribu kuaga zaidi ya mara mbili akashindwa,
ikabidi aseme tu, “Nitakupigia baadaye.” Kisha
akakata wakiwa garini wanapelekwa hospitalini alipo Mina.
~~~~~~~~~~~~~~
Walimkuta Mina amelala, upande mmoja mweusi kama mkaa
kabisa na Mina ni mweupe haswa kwa hiyo palitisha. Na kweli palianza
kujaa. Mama Ruhinda akashika mdomo. “Mungu wangu, watakuja kumuua huyu
mtoto!” Akanong’ona mama Ruhinda akiwa na mshangao. “Tumuamshe au tumuache?”
“Subiri kwanza Ruhinda.” Mama Ruhinda akampiga picha akiwa vilevile amelala. Ndipo
wakamuamsha.
Alipofungua macho lile jicho lilikuwa kama limevilia
damu kwa ndani hata mboni ya jicho ni nyekundu. Mama Ruhinda akaweka mikono
kichwani. “Mungu wangu Ruhinda!” “Naomba tulia. Utaongeza hofu.” Ruhinda
akamtuliza mkewe na kumgeukia Mina. “Vipi mama?” “Kichwa ndio kinauma, lakini
wamenipa dawa za usingizi ndio zinanilevya. Na pressure inaanza kupanda sasahivi. Maana mwanzo waliponipima
ilikuwa nzuri, sasahivi wameangalia tena, inapanda.”
“Pole Mina mwanangu. Au ni mawazo?” “Nahisi nimeingiwa
hofu, mama. Hali sio nzuri.” “Pole sana. Naamini tutapata ufumbuzi.
Jaribu kulala. Sisi tutatoka kwenda kukununulia chakula, kisha tutarudi.”
“Asante. Naomba msije kuwaambia kina Andy, ili angalau leo nipumzike.
Hata mama na Ron msiwaambie kitu chochote. Tafadhali wazazi wangu.
Tuache tu kwanza.” Hilo wakashukuru Mungu maana walijua mama yake akiongezeka
hapo, akimuona hivyo alivyo, inaweza kuwa mbaya zaidi.
“Sawa kabisa.
Naona umewaza kama mtu mzima kabisa. Tunashukuru Mina. Ili patulie
kwanza. Patatulia tu. Tupo na wewe.” Wakamfariji ndipo wakamuacha, akarudi
kulala.
Walichofanya nikumletea chakula usiku huo,
wakahakikisha amekula vizuri. “Naomba mpitie nyumbani mkahakikishe Ayan
anapewa maziwa yakutosha, baba. Na kesho asubuhi kabla hamjarudi hapa awe
amepewa chakula na mumuache akiwa na maziwa. Naamini kesho nitatoka tu,
nitakuwa naye.” “Usiwe na wasiwasi. Pumzika tu. Tumemwambia Andy atutayarishie
chumba. Tumeamua kulala hapohapo nyumbani kwake.” “Nashukuru mama yangu.” Ndipo
wakaagana na kuondoka kuelekea nyumbani kwa Andy.
~~~~~~~~~~~~~~
Usiku Mina yeye alilala kama nusu mfu kwa madawa ya
usingizi, lakini nyumbani kwake na Andy walilala panakaribia kupambazuka kwa
kikao kirefu sana mpaka mama Ruhinda akapandisha pressure. Pius hakujali swala jingine lolote hata ndoa
yake isipokuwa huyo mtoto aliyekuwepo tumboni kwa Mina. Utafikiri
alishakaa kwenye ndoa kwa miaka mingi bila mtoto ndio Mina amempatia
mtoto!
Andy naye hataki ukaribu wake Pius na mkewe.
Ndipo ugomvi ukaanza upyaa. Wakaanza kupigana tena mbele ya
wazazi wao.
~~~~~~~~~~~~~~
Pius Kaonjeshwa
Asali, Anataka Kujenga
Mzinga Kama Kina Afidhi,
Mozee Na Omar. Na Andy Naye Ndio Ameshituka kukiwa kushakuchwa, Anakaba Mpaka Kona.
Inaendelea…
0 Comments:
Post a Comment