Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 40. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 40.

Huko alikokuwa kwenye ulimwengu wa usingizi, Pam akasikia mwanae akilia huku duniani, akarudi kwa haraka, akafungua macho na kukaa akionekana ana maumivu na bado na madawa ya usingizi. “Njoo baba mzazi. Ni nini?” “Nataka twende wote nyumbani.” Akazidi kulia. “Nimepitiwa tu na usingizi. Njoo, usiogope. Usilie mimi nipo sawa, na tunarudi wote nyumbani.” Akaenda kukaa kitandani kwa mama yake. Pam akaanza kumfuta machozi kama toto dogo.

“Njaa inauma?” Akatingisha kichwa kukubali. “Sijala mchana.” “Kwa nini tena!?” “Watu wachokozi.” Pam akawa hajaelewa. Ila Mill na Colins wakahisi ni pengine na hiyo siku Miles na wenzie walimfanyia fujo bwaloni akashindwa kula. Mill akazidi kuumia ila kuogopa. Maana akajua Pam akijua, huo ni moto mwingine.

Akaendelea kumfuta machozi na mkono wa shoto. “Tunatoka hapa sasahivi, nitaenda kukutengenezea ugali na nini tena?” Akawa ashasahau hana mkono mmoja, akawa anamtania mwanae, acheke. “Umeumia mkono mama!” “Wewe niambie unataka ugali na nini au ni yaleyale mambo yetu?” Shema akacheka akikubali. “Basi mama Pili au Batuli watakurekebishia. Nawapigia simu sasahivi, nawaambia nakuja na baba mzazi, mzee Shelukindo mwenyewe, ananjaa ya kufa mtu. Wote wanaijua dawa yako. Ukifika tu nyumbani unakuta washakuwekea.  Tena leo ugali mboga tatu!” “Ndio zawadi ya kufaulu?” Akauliza akicheka. “Kumbe! Leo wote watajua mzee Shelukindo amefanya vizuri. Mboga tatu, peke yako! Au unasemaje?” Akacheka akionyesha kuridhika.

“Muone! Muoga wa njaa wewe!” Akamsugua mwanae kidogo na kuangalia, akamuona Mill na Colins. “Nashukuru Mill. Asante sana kwa matibabu. Lakini acha sisi tuondoke hapa. Huyu akale, apumzike.” “Basi ngoja nikamuite daktari azungumze naye kabla hajatoka.” “Nashukuru Colins.” Mill akamshukuru. Daktari aliingia hapo kwa haraka. Akapewa dawa za kukausha kidonda, na za maumivu, akaruhusiwa.

~~~~~~~~~~~~~~

Njiani alikaa kiti cha nyuma na mtoto wake akiwa ameshika dawa zote, akajiegemeza na kurudi kulala asijue alipo mpaka aliposikia gari limesimama, akafungua macho akidhania wamefika. “Nisubirini nikawachukulie chakula. Shema ananjaa sana. Hawezi subiri na kuna foleni.” “Asante.” Akarudi kulala.

Akahisi amerudi na mtu wa kumsafisha mikono. Akafungua tena macho. “Na wewe unataka kula sasahivi?” “Hapana. Mwache tu huyo ale. Ila sasa kuwa makini Shema! Sio tena kumwaga mwaga kwenye gari ya watu!” “Simwagi mama. Nitakua makini nisichafue.” “Haya sema asante.” Akamshukuru aliyemnawisha. Akapewa chakula na baba yake, maji akamuwekea kwenye sehemu ya kushikilia chupa au vikombe. Akaweka chakula kingine mbele, safari ikaendelea.

~~~~~~~~~~~~~~

Alilala Pam, mpaka wanafika. Shema akashusha kila kitu, yeye amelala. “Pam!” Akasikia Mill akimuita. Akafungua macho. “Naomba nikuuguze.” Akawa hajaelewa, akajaribu kufikiria alipo akagundua gari imesimama. Akakaa na kumuona Mill amekaa kiti cha mbele amemgeukia nyuma.

“Unamaanisha nini?!” “Mkono ulioumia ni wa kulia. Una mtoto anayekutegemea kwa kila kitu. Kuanzia kula yake, kufua na mengine mengi. Anaanza likizo, inamaa kuanzia kesho yupo nyumbani atakuhitaji kuanzia asubuhi mpaka usiku akilala, halafu bado wewe mwenyewe.”

“Kama ulivyomsikia daktari, madawa waliyokupa yatakupa kizunguzungu. Hutaweza kufanya mambo yako kwa muda mpaka upone.” Pam akabaki akimsikiliza.

“Lakini pale kwangu nina mashine za…” “Subiri kwanza Mill. Kwamba msaada huo unaouzungumzia ni mimi na Shema tuhamie kwenu?!” “Ile nyumba ni kubwa Pam! Kuna vyumba vya kutosha. Yupo mtu anakuja kusaidia kazi kuanzia asubuhi na kuondoka jioni au usiku. Ni vile utakavyomwambia. Kuna mashine za kufulia na…” “Nashukuru sana. Lakini hapana, Mill.”

“Sababu ya mimi kuishi hapa uswahilini, chumba cha uwani kwenye joto, ni wale wapangaji pale. Hapa mjini nimejitengenezea familia ingine, baada ya watu wangu wa karibu wa mwanzoni na ndugu, KUNISUSA. Hawa wapangaji si wakamilifu, lakini sina wasiwasi na hayo yote unayoyasema wewe. Watagawana kazi zangu zote mpaka nipone. Na huyo Shema atalishwa chochote watoto wao watakachokula hata kama ni ugali na mchicha, watampa mpaka mimi nipone.”

“Safari hii hutanitoa katikati ya watu wangu, na kwenda nitekeleza kwa watu wako walio wabaguzi na roho mbaya. Wema wao ni wakikuona WEWE tu, ambaye uwepo wako hautabiriki! Ukiwepo na mimi kwa muda ule ndio wanakuwa WANAFIKI kwangu. Mimi si mjinga wa kiasi hicho Mill. Nilifanya kosa mara ya kwanza, sirudii kosa tena. Mbaya zaidi safari hii nikiwa na Shema! Hapana Mill. Nitamuhangaisha sana Shema endapo sasahivi nikianza kuyumba. Sina huo mwanya. Sisi tutakuwa sawa tu.” Akawa kama amekumbuka kitu.

“Kwanza wanao hawampendi Shema wangu! Kweli unataka mwanangu aache marafiki zake hapa mtaani, aende akaishi kwa kunyanyasika eti sababu ya A/c na mashine za kufulia nguo!” “Hapana. Hiyo sio sababu ya msingi. Sababu ya msingi ni kuishi na wazazi wake pamoja.” “Nilikwambia hutanifanya mimi mama Kenny, Mill! Hapana.” “Na nilikwambia wewe si mama Kenny, na hautakaa kuwa mama Kenny. Nakupenda Pam. Na wewe ni mwanamke niliyekufikisha mbali kuliko hata baba alivyomfikisha mama Kenny. Mbona hilo unashindwa kutambua?” Akatulia.

“Nimekueleza ilivyokuwa. Kweli umeshindwa kunielewa kabisa?” “Nimekuelewa kwa kile ulichosema. Lakini haimaanishi eti na safari hii nikiwa na mtoto, nikurupuke tu na kufanya kama unavyotaka! Hapana Mill! Nashukuru kwa nia yakutaka kutusaidia, lakini mimi na Shema tuna maisha yetu. Tuna furaha  na amani na kidogo tulicho nacho. Amefunga shule, nashukuru kumsogeza mpaka hapa. Angalau utapata muda wa shuguli zako. Tutawasiliana shule zitakapokuwa zinakaribia kufungua, tujipange tena kwa upya kama bado utakuwepo.” Akafikiria kidogo kabla ya kushuka na kuongeza.

“Hakika natamani angalau ungekuwa umeniamini kama Mike na Kamila. Na kunishirikisha kilichokuwa kikiendelea Mill. Uliniacha kikatili sana. Kweli leo unarudi na kudhania kwa meneno yaleyale yaliyonidanganya mwanzoni ndio kweli niamini tena! Kweli Mill!? Hata mimi nisingempenda mtu wa namna hiyo. Kwamba ni mjinga wa kupitiliza! Unampeleka kama doli tu! Hapana Mill! Hakika endelea tu.”

“Unataka kuniambia wewe Pam, ungeamini nipo nchi ya ugenini, mbali, halafu eti nikwambie NAOA sababu ya kutengeneza uraia huko. Halafu eti huyo mwanamke ambaye nimemuoa, nina ISHI naye nyumba moja! Halafu nikwambie hakuna kitakachoendelea. Kweli ungesema ‘sawa’ kabisa? Kuwa mkweli.”

“Nakwambia hivi, bora ungenipa sababu ingine yeyote ile ya kutoendelea kuwasiliana na mimi, kuliko kufungia simu zangu, na usijue ninavyoendelea kabisa! Kwa miaka yote hiyo! Kweli Mill?! Halafu urudi eti kila kitu kiwe kama ulivyoniacha kikatili? Unadhani na mimi sikuendelea na maisha yangu, eti nilikuwa nimekaa tu?”

“Kwamba ulishakuwa na mwanaume mwingine?!” “Nashukuru kwa msaada unaotaka kutupa. Lakini HAPANA.” Akakusanya shuka alilokuwa amejifunika la hospitalini, akataka kufungua mlango kwa mkono wa shoto. Mill akamuwahi, akamsaidia kushuka. Maana gari yake ilikuwa kubwa, ndefu. Akashuka. Akamsindikiza mpaka ndani. Kila mtu akimpa pole mpaka aliowakuta nje.

“Nini tena?!” Akauliza mama Batuli. “Ajali ya pikipiki. Ila nitakuwa sawa tu. Acha nikalale. Nina madawa ya usingizi huko mwilini, kila kitu kinazunguka. Na huyu amefunga shule leo. Ikifika saa 12:30 jioni naomba nirudishie ndani. Aoge, atulie ndani.” “Chakula?” “Hapo alipo ameshiba na baba yake amemnunulia cha usiku. Yupo sawa.” “Na wewe?” “Nikiamka kama nina njaa, nitakwambia. Ila sasahivi nataka kitanda tu.”  “Basi kwenye saa moja nitakuja kukutoa, japo ujimwagie maji.” “Sawa, nashukuru.” Akaingia ndani alipokuwa ametangulia Mill akisikiliza. Kweli wenyewe waliwezana hapo ndani.

~~~~~~~~~~~~~~

“Nenda kapumzike Mill. Mimi nalala.” “Kwa hiyo una mwanaume mwingine?” Pam akashangaa, asiamini. “Kweli Mill hilo ndilo ulilobaki nalo?” “Ndiyo. Ni yule daktari wa pale dispensary?” Pam akakunja uso. “Niambie nijue moja.” Akampita pale alipokuwa amekaa, akaanza kujaribu kubadili nguo.

“Naomba utoke nibadili nguo, nilale.” “Acha nikusaidie.” “Hapana. Asante.” Mill akaanza kucheka. “Kwamba unaona nitafaidi sana?” “Ndiyo. Haya toka Mill. Nenda kwa wanao. Hapa huna chakufanya. Mimi nalala.” “Utavuaje nguo Pam, kama si ubishi tu!?” “Nina mama Batuli na mama Pili. Wote  wapo. Ondoka bwana Mill!” Akasimama na kumzunguka nyuma. Akamfungua zipu ya gauni. Pam akatulia.

“Unataka kuvaa nini?” “Nivutie khanga hapo kabatini.” Akafungua kabati, lililokuwa upande vyombo, tena duni tu, upande nguo. Akamuhurumia hayo maisha, ila hakuwa na jinsi ya kufanya. Akachagua khanga. Akamtoa gauni. “Sidiria?” “Nitatoa mwenyewe bwana Mill, ni nini?!” Akamfungua hiyo sidiria kwa nyuma. “Haya toa.” Akatoa. Akamfunga hiyo khanga akiwa amesimama nyuma yake. Akapanda kitandani. “Asante.”

“Nguo zenu chafu zipo wapi?” “Nilifua zote, jana usiku.” “Basi nikusanyie zikifika za kufua, nitakuja kuchukua.” “Wewe unataka kujitia shuguli isiyo na lazima. Sisi tutakuwa sawa. Huu muda utumie kufanya mambo yako mengine!” Akakaa pale kitandani. Akamuona kama anayewaza kitu, halafu akasita kukisema. Akaondoka akiwa ameacha chakula na mazingira mazuri hapo.

Kimeumana. Msingi Mpya Unagoma kujengeka.

Matofali hayapangiki.

Kesho yake mida ya saa nne akawa amewasili. Akagonga na kukaribishwa. “Ingia, pako wazi.” Akaingia na mizigo yake. Akakuta Pam amejilaza kitandani kuna mtu amemshika mkono, amekaa pembeni ya kitanda. Ikamshitua sana.

“Ni nini kinaendelea!?” “Ndio hakuna hata salamu?” “Pam?” “Wala hakuna la ajabu hapa. Huyu ni daktari, na ni rafiki yangu. Amekuja kunisaidia, gozi imejaa damu. Nimeomba anisaidie kunibadili.”

“Daktari gani anakuhudumia amekaa kwenye kitanda unacholalia na mwanangu?!” Huyo daktari akamwangalia. “Naomba toka hapo kitandani. Wewe ushaona wapi madaktari eti wanatibu na kukaa kabisa kwenye kitanda cha mgonjwa! Kwanza wewe huo udaktari umesomea wapi?” “Mill!?” “Mbona swali la kawaida tu? Udaktari umesomea wapi?” “Kibaha.” Mill akakunja uso.

“Kibaha kuna chuo cha madaktari?!” Kabla hajajibu akaongeza. “Kwanza naomba simama hapo ulipokaa. Hicho kitanda analalia na kijana wangu. Huwezi kukaa hapo.” “Ni nini Mill, jamani?!” “Tafadhali simama.” Akasimama.

“Halafu hicho chuo cha Kibaha, kinachotoa madaktari wa aina yako ni chuo gani hicho, mbona mimi sijawahi kukisikia?” “Sio daktari kama daktari, ni Medical assistance.” “Oooh! Sasa mbona unadanganya kama wewe ni daktari wakati..” “Mill tafadhali!” Pam akamuonya, na kumfanya aanze kucheka.

Bwana alicheka Mill! Mpaka kero. “Ujue akiondoka huyu utafunga wewe hiki kidonda!” “Kabisa. Kwanza anajipa cheo kisicho chake! Madaktari wanasoma miaka zaidi ya sita. Yeye amekaa darasani miaka miwili tu, ndio anataka kupanda mpaka vitandani kwa watu! Ndio maana umenishangaza na elimu yako!” “Sijapanda kitandani!” Hapo akamtibua Mill. Akambadilikia kabisa.

“Sijakukuta umekaa kitandani au unataka kuniita mimi muongo?” Akampandishia na sura ya ukali kabisa hamna cheko tena. “Unadanganya watu wewe…” “Mill unapandisha hasira, bila sababu wakati amekuja kunisaidia.” “Basi SITAKI akusadie. Kama msaada wake ndio huo mpaka apande vitandani kwa wagonjwa ndio asaidie, SITAKI Pam. Heshima ya wapi hiyo!? Yaani kitanda hikihiki analalia mwanangu na yeye pia anakalia! Hapana Pam.”

“Sasa si ameshanyanyuka, hasira za nini?” “Sasa kwa nini akae?” “Mill, huyu si adui. Ni mtu mzuri sana na huwa anatusaidia sana.” Asijue anazidi kumtibua Mill. WIVU, akijua ndiye yuleyule aliyesikia kina mama Pili wakisema anampenda sana Pam. “Msaada wake ndio wa kupanda mpaka vitandani?! Kwani hawezi saidia kama wauguzi wengine!?” Akazidi kupandisha na kumgeukia na yeye.

“Ndio maana umenitia sana mashaka na huo udaktari wako!” “Lakini si kwamba nipo tu hapa kama muuguzi. Tuna mahusiano ya karibu na mama Shema.” Hapo ndipo na yeye alipoharibu zaidi.

Pam alitamani kupaa. “Kwamba nini?! Unamahusiano na mke wa mtu?” “Pam hajaolewa na mimi nina nia nzuri naye.” “Nia yako nzuri na mke wa mtu?! Kama ungeenda kwao, ungejua kama Pam alishaolewa. Unazunguka huku mtaani ukiparamia vitanda vya watu, na kujipa vyeo visivyo vyako kwa makusudi ili kudanganya wake za watu! Sasa hapa nisikuone tena. Pam ni mke wangu mimi kihalali. Nikimaanisha mpaka nimelipa mahali na kumuoa kabisa. Na kikubwa cha msingi nina mtoto naye. Sijamvizia barabarani, na kumdanganya kama wewe. TOKA.” Pam akabaki akimwangalia Mill.

“Mimi hapa nimemfuata, mama Shema. Huwezi kunifukuza.” Na yeye akaweka ngumu. “Hivi unajua Mill wewe unajaza watu hapo nje bila sababu? Ni nini lakini?!” “Nikuulize wewe Pam, na huyo daktari wako!” “Mgaya, naomba uondoke. Tuta…” “Na hakuna kuwasiliana tena. Haya toka kabla ya mwanangu kukukuta hapa ndani na kumchanganya kijana wangu. TOKA. Na leo ndio iwe mwisho wako kukanyaga anapoishi kijana wangu. Adabu ya wapi hiyo?! Toka.” Akatoka kimyakimya. Ukweli alionekana ni mstaarabu.

“Umefurahi sasa?” “Kipi chakunifurahisha hapa?! Mimi nakuomba nikakuuguze, unakataa kwa kunipa sababu za kuniumiza, kumbe sababu ya kweli ni mpuuzi huyu, anayejiita daktari wakati amekimbia shule?” “Hili gozi lilijaa damu. Nafikiri nililala vibaya. Bado dawa zinanipa kizunguzungu. Mama Pili alipokuja kuniletea chai ndio akaniona hivi, akaenda kunisaidi kumuita ili aje anisaidie kubadilisha.”

“Ndio akaona apande kabisa kitandani ili akutibu vizuri?” “Mill umekasirika. Tafadhali tulia.” “Unanikatalia mimi nisikuuguze, najilaumu kwa mengi, silali. Halafu nakuja huku namkuta yeye ndio anakuuguza!” “Haniuguzi! Amekuja kunisaidia tu. Mbona hilo hutaki kulielewa? Karibu ukae.” Akabaki amesimama.

“Umekula?” Pam akamuuliza kama kumtuliza, lakini hakujibu. “Shema alikuwa akikuchorea vitu vya kukupa ukija. Ametoka hapa muda si mrefu.” Mara Shema akaingia anatokwa jasho kwelikweli. “Shikamoo baba.” “Mapema hii ushafikisha siku nusu! Sasa unamsaidia mama yako saa ngapi?” “Nishaosha vyombo alivyonywea chai. Nimemsaidia mama Pili kusafisha uwani ndio akaniruhusu nikacheze.” 

“Sasa wenzio si wapo shule, unacheza na nani?” “Dula ndio rafiki yangu, tunachezaga naye. Sema yeye haendagi shule. Anaaga kwao anaenda shule. Akifika huku anabadili nguo, tunacheza mpira mpaka muda wakutoka shule ukifika ndio anakwenda kwao.” Mill akashangaa sana.

“Pam!” “Na nirafiki yake kweli! Maana Dula mzuri sana kwa mpira wa miguu. Sasa huyu ndio anayempenda ili wacheze naye.” “Na swala la shule?” “Baba yake katandika naona mpaka kachoka. Hataki shule kabisa. Yeye anataka kucheza mpira tu, mwenyewe anasema atakuja chezea ligi za Ulaya.” “Nimekuandikia barua, baba.” Ndio Mill akaonekana kutulia na kucheka.

“Ni barua au mchoro?” “Barua na nikakuchorea picha. Nikupe sasahivi au baadaye? Nimekuja nikikimbia, wamenifuata kule wakasema umekuja. Sijataka uondoke bila ya barua yangu.” “Nipe tu sasahivi, asante.” Akamtolea na kumkabidhi. “Ni ya asante.” Mill akawa anacheka akionyesha wazi amefurahia. Akakaa kabisa na kuanza kusoma. Shema akatoka tena kwenda kucheza.

“Ulivyofurahia! Mpaka uso unaonyesha!” “Ndio mtoto pekee mwenye shukurani na ninachomfanyia. Umesikia jana alivyonitambua mbele za watu lakini?” Pam akacheka. “Halafu eti mjinga mmoja anakuja tu anajiita dokta, anataka aje kuwa baba yake!” “Hakuna anayetaka kukupindua kwa Shema! Tafadhali tulia. Kwanza mwanao mwenyewe hata ufanyaje, mmefanana kupita maelezo!” “Lakini ndio hao wanao tutenganisha! Mimi naomba kukuuguza, unanikatalia sababu ya mpuuzi huyu! Unanitajia kina mama Pili ambao siwaoni humu, namuona yeye tu amejaa mpaka kitandani!” “Hivi ujue hata hujanijulia hali?” “Najiona sina maana! Ameshaitwa mwenye maana, mimi tena wa nini?” “Mill umekasirika bila sababu!”

“Kweli huoni sababu hapa?!” “Sasa si ameshaondoka! Tafadhali rudisha mawazo hapa.” “Siwezi. Maana naona yeye ndio umempa uthamani kuliko mimi! Unataka nifanye nini Pam ili ujue hata Kisha nilifanya kwa ajili yako WEWE? Nimelipa garama kubwa sana ilimradi tu, TUWE PAMOJA. Mara ngapi mimi mwenyewe nilikuhangaikia uje Marekani, ili tuwe wote lakini ikashindikana?! Nilikubali kulipa garama kwa ajili yetu, lakini huoni! Nifanyaje?”

“Mbona habari za mkono huzitaki, unalalamikia mtu ambaye ameshaondoka?” “Hujataka nijue! Uliyemuona ni wa muhimu, ndiye uliyemtafuta asubuhi na mapema, mimi unaniona kero! Basi Pam. Acha nikuache na maisha yako. Ila nataka kujua, bado utahitaji kurudi kule kubadilisha gozi au ndio umeshapata mtu wa kukusaidia, nikuache?”

“Maadamu nina dawa zote, acha tu nisafishe hapa.” Mill akamwangalia na kusimama. “Naamini ukitumia dawa vizuri, kitakauka haraka. Nitakuwa nikimtuma dereva aje achukue nguo chafu na kuleta mahitaji. Kukiwa na uhitaji, tafadhali tuwasiliane kwa njia yeyote utakayochagua wewe. Ila naomba niwe napata muda na Shema tafadhali. Nitakuwa nikimtuma dereva aje kumchukua. Tafadhali mpe na muda unaotaka awe anarudishwa.”

“Kama hakuna jingine, acha mimi niondoke, nikuache na hayo mahusiano yako na dokta Mgaya.” “Mill umekasirika. Lakini ukitulia, utagundua hakuna baya lililokuwa likiendelea hapa, isipokuwa kupatiwa msaada.” “Msaada wake yeye, ambao wangu umekataa! Sasa nina faida gani hapa kama si kero tu?” Pam akanyamaza, Mill akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~

Na kweli hakutania. Hakurudi hapo tena! Akawa akimtuma dereva kuleta matumizi na siku anazomtaka Shema, basi anamtuma anakwenda kumchukua. Pam naye jeuri, hakujali. Siku zikazidi kwenda, akijiuguza na kusaidiwa na aliotaka yeye, ila pesa ikawa inatumwa ya kutosha tu. Pam akawa na pesa, ugonjwa ukawa rahisi. Anaagiza tu.

Mwezi ukaisha hajamuona Mill, akaanza kuwa na hamu naye. Anahangaika rohoni ila jeuri. Mwanae akirudi kutoka kwa baba yake atadodosa kwa hili na lile mpaka ajue hali yake. Ila Mill mwenyewe hamtafuti japo alishapata namba yake.

Kuishi Na Uhalisia Halisi.

Baada ya mapumziko ya kisiwani Zanzibar, kuanzia siku ya jumamosi mpaka jumatano, familia hiyo ya Andy walirudi nyumbani bila huyo Ayvin kuzungumziwa kabisa. Mina akabaki nalo rohoni, asijue ndio hiyo ndoa itaendeleaje! Na waliporudi tu, siku ya alhamisi Andy akaanza kazi.

Alirudi nyumbani kutoka kazini, jioni mapema tu. “Naona Pius amempata daktari anayetaka uhamie huko. Baba amenipigia simu. Amenipa jina na namba yake ya simu. Ameshaweka na apointment ya kesho saa sita mchana.” “Sawa.” Mina akakubali akiwa hajui anatakiwa aongeze nini, maana alikumbuka ni kama Andy alimkubalia Pius.

Akainama pale alipokuwa amekaa mtoto wake sakafuni kabisa akichezea magari, pembeni ya mtoto wake. Akaanza kushindana naye akiwa Mina amejilaza hapohapo sakafuni.

“Vipi kazini lakini?” Mina akapenyeza hilo swali katikati ya michezo ya Andy na mwanae. “Nzuri. Na inaonekana hiyo kesho Pius mwenyewe atakuwepo. Baba amesema ameomba awepo ili kuangalia maendeleo ya mtoto wake.” Andy akaongeza, huku akiendelea kucheza na mtoto wake bila kumtizama Mina. Ila akajua hilo la kuwepo Pius, ndilo linamkera zaidi. Hakuonekana na furaha hata kidogo, ni kama alijikaza tu. Mina naye akabaki kama amepigwa na bumbuwazi hajui aongeze nini! Akafikiria hapo akasimama kwenda jikoni.

Usiku wakati wanalala, Mina akaona ajaribu. “Tutakuwa wote huko kliniki kesho?” “Kesho ni siku ya kazi Mina! Na ni saa sita mchana katikati ya kazi!” “Kweli ni muda mbaya.” Mina akaongeza kwa kunyongea, akikumbuka vile mwenzie Pius alivyokuwa akiacha kazi zake na kukimbizana na mtoto wake, Ayan, mahospitalini. Lakini akaona anyamaze tu. Hapakuwa na mapenzi usiku huo. Wakalala tu.

Kliniki Dodoma.

Ilipofika saa tano kamili asubuhi, Mina akamtumia ujumbe Andy. ‘Ndio naelekea kliniki. Nawahi kidogo ili kupata nafasi yakujaza fomu kwa sababu ni mara yangu ya kwanza. Hata hivyo sipafahamu. Sijui kutakuwa na umbali gani, na sijui watakuwa na taratibu gani! Sitaki kuchelewa.’ Akamtumia ujumbe huo Andy, akapiga.

Mina akapokea. “Vipi lakini?” “Nipo tu sawa. Nimemuomba Kashinde anitafutie taksii ya dereva anayepafahamu hapo hospitalini, ili nisipate shida ya kufika. Nitakwenda na Ayan.” “Sidhani kama ni sawa kwenda na Ayan. Hujui itachukua muda gani, hujui mazingira ya hapo yatakuaje. Hatutaki akacheze huko, achukue magonjwa.” “Ni wazo zuri. Basi nitamuacha.” Mina akakubali huku akiumia, hajui atamwambia nini Ayan ambaye alishamuandaa kwa safari.

Wazazi Wa Ayvin Pamoja Kliniki.

Alifika hapo hospitalini saa tano na nusu baada ya kubembelezana na Ayan mpaka kufanikiwa kumuacha. Mina akaumia sana kumuacha Ayan, lakini hakutaka kumuudhi Andy. Akaelekea mapokezi akiwa amepoa sana usoni, akamkuta Pius akimsubiria hapo. “Vipi wewe na mtoto? Mnaendeleaje?” “Namshukuru Mungu, hatujambo.” Akajibu taratibu tu.

“Pole na safari.” Mina akaongea kwa kujali, angalau Pius akajisikia vizuri, japo hakuchangamkiwa. “Asante. Upo sawa lakini?” “Mimi nipo sawa kabisa.” Akajibu. Pius akamtizama kidogo kama kutomsadiki.

“Nilishazungumza na madaktari wote. Nilimuomba yule wa Iringa azungumze na huyu mtakayeanza kumuona sasa, ampe maendeleo yenu yote. Amtumie kila kitu, kwa hiyo hautakuwa kama mnaanza upya.” “Nashukuru.” Pius akatulia kidogo. “Niliweka appointment ya Ultrasound pia. Naomba leo tumwangalie mtoto. Kama hautakuwa na haraka.” “Haina shida. Halafu nimempa jina.” Mina akatoa tabasamu kidogo na kumshika mtoto wake kwa kujishika tumbo.

“Jina gani?” “Ayvin.” Akamuona amepoa gafla. Hakuongea lolote katika hilo ila akauliza upande wa kliniki, wakaelekezwa, wakaondoka hapo mapokezi, Pius akiwa amepoa. Mina akamuhurumia. Ni Pius, mwanaume aliyejawa upendo na alimjali sana Mina. Hata kama kulikuwa na hila, lakini Mina alitambua kujaliwa naye bila kuchoka! Na alijua wazi, wote watamuacha, lakini si Pius. Wakatafuta sehemu ya peke yao kama waliojitenga, wakakaa hapo wakisubiria. Pius alishajaza kila kitu, wakabakiwa na muda mwingi tu.

“Tutamwita hivyo ili kupunguza hii hali ambayo tayari ipo Pius. Na ili Ayvin asionekane kama ni tatizo. Lakini kwenye vyeti vyakuzaliwa tutamwandika Ayvin Pius Junior Ruhinda.” Hapo akamuona Pius ameridhika. “Hata ukiwa naye ukitaka kumuita Pius Junior sitajali, lakini nakuomba Pius, kwa sasa tumuite hivyo. Ukishindwa, angalau mwite PJ, ili kuwe na amani tafadhali.”

“Maana hata tufanye nini, huyu mtoto hawezi kulelewa na mimi peke yangu au wewe peke yako. Wewe unayo familia yako na mimi nina yangu. Sisi kama wazazi wake Ayvin tunawajibika kumfanya akue kwenye mazingira mazuri ambayo hatajiona yeye ni tatizo. Naomba katika hili uwe upande wangu Pius.” Mina aliongea naye taratibu tu, akashangaa Pius amekubali bila shida.

“Hapo nimekuelewa na nimefurahi. Angalau jina langu lipo. Ni mwanangu huyo Mina! Hata iweje, ni mtoto wangu.” Mina akabaki akijisugua mikono taratibu. Wakatulia. “Nikuulize kitu Pius?” “Uliza tu.” “Utawaambia nini familia yako? Zaidi yule binti yako mkubwa anayekupenda na kukuheshimu kiasi cha kutamka wazi anakupenda wewe kuliko Raza mama yake. Utawaambia nini!?”

“Nikwambie tu ukweli, hali sio nzuri Mina. Lakini nimekusudia kuwajibika.” Mina akamwangalia. “Nimeanza na Poliny, bado Raza. Ilibidi kuzungumza naye yeye kwanza. Nilimfuata chuo, nikaomba tuzungumze. Imemshitua sana. Na ameomba muda.” “Muda wa nini!?” Mina akashindwa kuelewa. Akamuona Pius ameinama akifikiria. “Pius?” “Kwamba nisimtafute mpaka atakaponitafuta yeye.” Mina akaumia sana. 

“Hiyo ilikuwa lini?” “Naomba wewe usijali juu ya upande wangu Mina. Fikiria swala la mtoto, na afya yako tu. Mengine yatajijibu kadiri siku zinavyokwenda.” Mina alijua mahusiano ya Pius na Poliny binti yake mkubwa. Alijivunia baba yake huyo binti, ungejua anampenda, halafu wakafanana utafikiri alitakiwa azaliwe wakiume.

“Mara ya mwisho kuzungumza naye ilikuwa lini?” “Mina!” “Nataka tu kujua Pius!” “Itakusaidia nini? Mbona kama unayo mengi tayari! Sitaki...” “Wewe niambie tu.” Mina akasisitiza, Pius akabaki akimtizama. “Pius?” “Ni mwezi sasa. Hajarudi nyumbani. Na nafikiri hajamwambia hata mama yake, lakini Raza hajapatwa na wasiwasi, kwa kuwa huwa hawapatani. Mara ya mwisho kuondoka pale nyumbani waligombana sana na mama yake. Kwa hiyo Raza anajua bado amekasirika.” Mina akanyamaza.

~~~~~~~~~~~~~~

Alimuhurumia Poliny. Maana pia alimpenda sana Mina. Walipishana kama miaka 4 tu, kwa hiyo wakati mwingine Mina alipokuwa akienda kwao, akimkuta alikuwa akimchukua na kwenda naye saluni kutengeneza nywele au kucha. Alikuwa akimwambia siri zake na yeye ndiye aliyekuwa akimwambia mambo mengi ya mama yake. Na ndipo Mina alipomfahamu Raza kwa undani kupitia mtoto wake ila hakuwahi kumsema kokote. Mina akajua hatamuamini tena, atajua amemzunguka mama yake. Akanyamaza akifikiria.

Ya Sirini Mwangani.

“Kwani ilikuaje Pius?!” Mina akavunja ukimya. Pius akamwangalia kama asiyeelewa swali. “Ulikusudia kuzaa na mimi au ilikuaje?!” “Yaani wewe hukumbuki kabisa ule usiku!?” Pius akauliza kama ambaye hasadiki kidogo. “Sikumbuki Pius!” “Hata kidogo!? Kwamba haikujii kama ndoto hivi au mawazo fulani hivi!?”  “Nimejaribu kufikiria, hakika sikumbuki. Ilikuaje?” “Naona tuyaache tu Mina. Mimi nimekubali kuwajibika, naomba hiyo itoshe.” Hilo halikukaa sawa kwa Mina, inamaana kuna kitu.

“Nataka kujua Pius! Sitaki wewe ndio ubakiwe na kumbukumbu ya ushikwaji mimba wa Ayvin, halafu mimi nibakiwe kuwa alikuwa wa bahati mbaya!” “Nakuhakikishia hakuwa wa bahati mbaya Mina.” Mina akakunja uso.

“Ninachotaka ujue, ni kuwa, PJ hakuwa mtoto wa bahati mbaya. Ndio maana hicho kipengele nimekubali mimi fedheha ili wasimuathiri mwanangu kwa maneno mabaya, akajijua ni wa bahati mbaya. Hapana. Haikuwa ajali na wala sikukubaka. Tulikuwa na wakati mzuri sana Mina. Sana. Natamani ukumbuke hata kidogo. Ukumbuke maneno uliyoniambia mimi. Ukumbuke ule wakati, pengine utajisikia kile ninachojisikia kwa PJ. HAKUWA wa bahati mbaya hata kidogo.” Mina akabaki akimtizama kwa hofu. Pius akamgeukia Mina vizuri.

Nakuhakikishia tulikuwa na wakati mzuri kuliko nyakati zote unazokumbuka kuwa na mimi, Mina.” Mina akazidi kuogopa, akainama kwa hofu na aibu. “Kwanza uliniomba kwa machozi, ukitaka nikuguse kidogo.” Mina akashituka sana. Akamwangalia Pius. “Kinachoniuma ni kitendo cha wewe kutokukumbuka MANENO yako kwangu. Inaniuma mno. Mpaka najilaumu nikijiambia pengine hukumaanisha kabisa. Ile ilikuwa pombe tu. Lakini najirudi, najifariji, najiambia, mara nyingi pombe huwa haimfanyi mtu adanganye ila kumtoa UKWELI uliopo ndani.” Mina akaanza kusikia mpaka baridi ya hofu.

“Uliniambia unanipenda, Mina. Ukataka kunishukuru. Na ukasema ni jambo ulilokuwa ukilitamani sana kunifanyia kwa muda mrefu, sema ulikuwa ukiniogopa kwa vile ambavyo sikuwa nikikuonyesha nia ya mapenzi.” Mina akafunga macho kwa hofu akitamani iwe yupo usingizini, anaota.

“ULINIOMBA nikuguse tu, angalau unishukuru kwa upendo ambao nimekuwa nikikuonyesha. Uliniambia upo mpweke, wakati mwingine unatamani mtu wa kukufikiria wewe kama Mina, na hisia zako. ULINIOMBA nikukumbatie kama nitashindwa kufanya na wewe mapenzi.” Mina aliumia sana.

“Nilikuwa nimelewa Pius! Ungelielewa hilo!” “Kwa hiyo hukumaanisha chochote?” Mina akamshangaa sana asimuelewe. Yaani yeye kwake hilo halikuwa tatizo ila hisia zake kwake! “Kwa hiyo maneno yote ya kuwa unanipenda na kunijali, ile ilikuwa pombe tu?” Mina alikuwa ameshavurugwa. Kumbe yeye ndio alichangia! Akapoa kabisa akijifikiria mara yake ya kuzwa kukubali kunywa pombe kulivyoharibu hiyo familia. Akabaki akijilaumu sana. Akatamani ile siku irudi, afanye tofauti kwenye mengi! Akabaki majutoni, akiwa amejiinamia.

 “Eti Mina?” Kimya. “Anyway, na mimi mwanzoni nikajikaza, nikijua ni pombe, ikiisha utakuja kunilaumu sana. Nikakusudia kukutuliza, mpaka kesho yake ukiwa hujalewa, tuzungumze na kukubaliana kwa kuwa mimi ni kweli nakupenda Mina. Nakupenda kama wewe Mina, na wala si shemeji. Na hilo nimejitahidi kukwambia na nimewaambia hata wazazi wako na wangu.” Mina akashituka sana na kumtizama.

“Najua hakuna anayeelewa sasa hivi kwa kuwa Andy amerudi kwenye picha, ila najua unajua kutoka moyoni, kuwa ninakupenda Mina. Na wewe ndiye shahidi wangu wa kwanza na ndiye ninayejali kama unaamini hilo.” Mina akashangaa sana.

"Pius, mimi mke wa mdogo wako!" "Sasa hivi ndio amerudi Mina!" "Lakini hata iweje, Andy ni mume wangu!" “Na yeye ndio sasahivi amelikumbuka hilo! Lakini mimi nina mapenzi ya dhati kwako Mina. Hata iweje, hakuna hali wala mtu namtanguliza kabla yako. Ndio maana kila kitu huwa kinakuwa kikisimama ninaposikia upo matatizoni, kuhakikisha hujikuti peke yako. Nakupenda na ninakuja." Mina alibaki akimshangaa Pius na kushindwa kumuelewa.

"Anyway, tuyaache hayo maana najua sasahivi hata nikikwambia hutanielewa tena. Turudi kwa unachotaka kujua. Usiku ule nilipokusudia kukuacha mpaka kesho yake, ulivua nguo Mina, ukabakiwa na nguo ya ndani tu. Hapo ndipo nilipozidiwa. Ukaniuliza kama nakuruhusu uvue nguo ya ndani.” Pius akatulia kidogo.

“Wewe Mina unajijua jinsi ulivyo mzuri. Ulipiga magoti mbele yangu ukiwa uchi kabisa, na chupi tu!  Unanililia ukitaka nifanye mapenzi na wewe, umekuwa mpweke na unanipenda! Hakika nilishindwa Mina. Ukumbuke hapo hata mimi nilishakuwa karibu na wewe kwa muda mrefu, ule upendo niliodhani ni wa kishemeji, ukawa dhahiri kabisa kuwa ni penzi halisi kwako. Nakupenda kwa hakika, na nikawa nimeshakutamani kimapenzi.”

“Tulianza mapenzi ambayo hakuna jinsi nikakwambia ukaelewa. Ila jua tulipata wakati mzuri SANA. Ulinifurahia Mina, sijawahi kupata mwanamke akanifurahia kama wewe, tena kwa kunisifu. Tulifanya mapenzi bila kuchoka, tena ukinishukuru kabisa, na kuniambia umefurahi nimekupa kitu ulichokuwa ukikihitaji kwa muda mrefu.” Mina alishindwa hata kumtizama Pius.

“Na sikudanganyi Mina.” “Naomba unisamehe Pius. Nisamehe kukuingiza vishawishini. Hakika nilikosea. Sijui nilipatwa na nini! Nafikiri pombe ilinizidia, nikafanya pengine jambo ambalo NILISHAUONYA moyo na akili kutofanya. Pengine ni kweli nilikutamani, lakini NILISHAJIONYA. Pombe ikanifanya kutekeleza. Naomba unisamehe Pius. Nimekuingiza matatizoni! Nimeingiza familia kwenye matatizo. Kumbe mimi ndiye mwenye makosa!” Mina aliongea kwa kuumia sana, akiwa amejawa aibu na majuto.

“Hakika nilazima nifanye kitu kwenye maisha yangu. Kweli mama yangu hata na watu hawajakosea. Nimebeba mbegu ya uharibufu ndani yangu na mimi mwenyewe nasababisha..." Hapo akamshitua Pius. "Tafadhali naomba usiseme hivyo Mina na usilie, unamuadhibu PJ sasahivi. Hisia zozote mbaya sasahivi kwako, anazipata moja kwa moja. Ndio maana unaona sitaki wewe ulaumiwe kwa lolote na yeyote ila mimi. Mimi nitabeba kila lawama na shutuma zote, wewe naomba nibebee tu huyo mtoto awe salama. Tafadhali Mina."

"Nakuhitaji sasahivi ili huyo mtoto azaliwe na furaha." "Nimeharibu sana Pius. Mimi nimuharibifu. Siwezi kuepuka kujilaumi. Mimi ni chanzo cha haya matatizo yote wala si wewe." "Huna uharibifu uliobeba ila tulikosa. Kama wengine WOTE wanavyokosea, ila kosa letu limezaa tunda linaloonekana kwa wazi. Wengine wamebahatika dhambi zao zinafichika"

Pius akakaa sawa. "Naomba ujue, PJ ni mtoto niliyemuomba kwa Mungu, nashangaa ni kwa nini aruhusu apitie kwako! Nimekubali kila kitu, shutuma ZOTE, kwa sababu kwangu si wewe wala PJ mmekuwa wa bahati mbaya. Ni kweli nakupenda Mina. Na namuhitaji sana PJ." 

“Huyo PJ nilimtaka mimi na Raza. Tukamtafuta SANA. Kwa kila namna, kwa garama ya mapesa mengi mno mpaka Raza akatolewa kizazi, Nikakata tamaa kabisa! Lakini nashangaa amekuja kupitia kwako! Niliwaambia wazazi kabisa. Mimi sio wa kwanza kufanya nilichofanya. Au si mwanandoa wa kwanza kufanya mapenzi nje ya ndoa! Lakini kwani ni wote wanaoshika mimba!”

 “Na wote tunaamini watoto wanatoka kwa Mungu si shetani. Sasa kwa nini PJ aruhusiwe kuja kwa njia hiyo? Hakuna anayejua, ila ninachojua Mungu amenikumbuka katika umri huu, nimempata PJ, basi. Katika yote, nitakuwa na mtoto wangu kwa kadiri nitakavyojaliwaKwa Raza nililipa garama kubwa sana ya pesa bila mafanikio. Kwako NITALIPA garama ya shutuma, fedheha, na NITAMLINDA PJ  kwa kadiri ya uwezo wangu bila kuzembea. Nampenda na kumuhitaji sana PJ, na kwamwe usikufuru kwa kusema umebeba uharibifu. PJ ni majibu ya maombi yangu hata kama kwa wengine ni kosa, ila kwangu ni mtoto wangu ninayempenda sana.” Pius akamuona Mina ametulia kabisa, anajishika tumbo kama aliyepotea hapo kimawazo hasikilizi tena.

Cha Mtu Mavi.

“Anacheza?” Pius akauliza. Mina akacheka kidogo. “Umejuaje!?” “Nimekuona ulivyobadilika na mawazo yote ukayahamishia kwake.” “Anacheza. Naona amekusikia ukimwambia unampenda.” Pius akajisikia vizuri. “Naruhusiwa kumshika?” Mina akasita. “Naogopa Pius! Sidhani kama ni sawa tena.” “Unafikiri nini kitatokea hapa?!” Mina akanyamaza akibaki akifikiria. 

“Mina! Mpaka mtoto wangu ataacha kucheza! Amejua kama baba yake nipo hapa, anataka nimsalimie. Ni mwanangu huyo Mina. Hata ufanyaje, hakuna mwanaume atampenda huyo mtoto kama mimi. Tafadhali acha tu nimguse ahisi upendo wangu. Na nakuhakikishia namshika mtoto wangu tu, tena kwa heshima kabisa.” “Naomba kweli usiende mbali Pius. Iwe tu hapa juu ya tumbo.” Pius akacheka kwa masikitiko. 

“Acha kujihami wewe!” “Mimi nakujua Pius.” “Hata kama nina uchu jamani, hivi unajua na mimi ni mtu mkubwa sana hapa nchini! Siwezi kufanya mambo ya ajabu hadharani. Nina wadhifa wakulinda.” Mina akamtizama na kumruhusu.

Ile anaweka tu mkono amegusa tumbo la Mina, Pius anafurahia, mwenye mke akatokea. Wote wakabaki wameduaa. Pius mkono tumboni kwa Mina, macho kwa Andy kama Mina. 

“Unafanya nini Mina?!” “Naomba usimlaumu Mina. Mimi nimeomba kumshika mtoto baada yaku..” Ngumi. “Sizungumzi na wewe Pius.” Andy akamrushia kaka yake ngumi ya pili, Pius akaidaka na kusimama nayo.

“Wewe vipi Andy!?” “Usiwahi kuniuliza ujinga huo! Hujui unachokifanya kwenye familia yangu?” Ikarushwa ngumi nyingine, Mina akiwa amekaa ameshangaa.

“Una roho ya ajabu sana Andy! Unashindwa vipi kumpokea mtoto asiye na hatia, wakati mimi nilikulelea mtoto wako karibu miaka 3 yote!” “Si kwa sababu ulitaka kuwa karibu na mama yake! Watoto wangapi wapo huko mitaani hawana baba wala mama, umeshindwa kuwa karibu nao, ukaja kumganda mwanangu mpaka akakutambua wewe kama baba, kumbe ni sababu ya mama yake!” “Huna shukurani mjinga wewe Andy.” Pius naye akarusha ngumi. Andy naye akarudisha.

“Unaona uchungu mimi kumshika mwanangu! Roho yako mbaya Andy.” “Ndivyo alivyokusemelea Mina kuwa nimeshindwa...” “Acha kumuingiza Mina katika upumbavu wako. Kwanza wewe ndio umemfikisha Mina hapo alipo. Nashangaa ni kwa nini umeshindwa kukubali kuwajibika.”  Ngumi tena. Andy naye akarudisha.

“Kwa lipi?!” “Ungekuwa umetulia nyumbani, Mina asingekuwa hapo, mjinga wewe! Umeshindwa kujifunza kwa hili na hutakaa ukajifunza daima.” Wakarushiana ngumi mfululizo, wakitukanana. Wakaanza kukusanya watu.

Andy akatema damu. “Huwezi kumnyanyasa Mina mbele yangu.” “Mina ni MKE wangu, MIMI. Sijamnyanyasa, acha kujitafutia umaarufu wa bure.” Ikarushwa ngumi ingine, Pius akachanika juu ya jicho, damu zikaanza kumwagika. Mina akasimama kwa haraka ili awaamulie maana wengine walitaka kujua kulikoni.

Mina alipowasogelea ili awaachanishe wasiendelee kujidhalilisha hapo na kutoa siri za familia, nje. Maana walishachukuliwa video vyakutosha. Ili kuwaamulia akaingia katikati yao na kujaribu kuwapishanisha, hakujua ngumi ilipotokea, ikatua juu ya jicho lake la kulia, akaona giza, akaanguka na tumbo lake mzimamzima mpaka chini na KUPOTEZA fahamu. Akazima kama mshumaa.

~~~~~~~~~~~~~~

Baba Watoto Wa Mina Wanakaribia Kutoana Roho Wao Wenyewe Na Wamemdhuru Mina Mwenyewe.

Itakuaje Kwa Mina Aliyeanguka Na Kupoteza Fahamu Akiwa Na Mtoto Wa Pekee Wa Kiume Wa Pius, Tumboni?

Hatima Yao Hao Wote mpaka Mill & Pam Ni Nini?

Usikose Muendelezo Wa Sintofahamu Hii kwa hawa Love At First Time.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment