Akasikia Mill
akisalimia nje. Alifurahia moyoni, hakuamini. “Washaingia
kulala.” Akasikia akiambiwa na mama Pili aliyekuwa akimalizia usafi hapo uwani
na yeye aingie nyumba kubwa anakoishi na familia yake, alale. Aliposikia mlango
wao ukigongwa Shema akamwangalia mama yake wakiwa wamelala pamoja.
“Kamfungulie.” Akashuka na kumfungulia baba yake.
Akamsalimia na
kumkaribisha ndani. “Unaendeleaje?” “Vizuri.” “Pole sana Shema. Pole sana.
Naomba kuona ulipoumia.” Akamwangalia mama yake huku akisita. “Naona tu.” Mill
akamsihi kwa upendo. “Ila mimi sio mwizi. Alinipa Mia. Sikujichukulia
tu. Kwanza hata chumbani kwake sikuingia. Watoto wako wamedanganya.
Wamesema uongo.” Mill akaumia na kumuhurumia.
“Najua wewe si muongo
wala si mwizi, Shema. Ilibidi baadaye kumbana Mia, akaniambia ukweli.
Lakini pia sikukutilia mashaka. Nilizungumza vile sio kukushutumu au
kukuhisi vibaya, ni kuweka tu utaratibu wa pale. Na pia kama niliongea vibaya,
naomba unisamehe.” Mpaka Pam akajisikia vibaya.
Mill mtu mzima
na uwezo wake, anajishusha mpaka huruma! Shema akarudi kitandani kwa mama yake.
Akalala. Mill akabaki ameinama pale alipokuwa amekaa, Pam akatoka kitandani na
kwenda kukaa mbele ya kitanda.
Akamwangalia.
“Anaendeleaje?” “Wamemtoa nyuzi. Kumebaki hapo palipovilia damu, ila kidonda
kimepona.” “Samahani sana Pam. Tafadhali nisamehe. Lakini jua siwezi
kuacha mtu yeyote yule akamnyanyasa Shema. Sithubutu! Na yeye ni
mwanangu na ninampenda. Na nimezungumza nao sana.”
“Lakini naomba
huko usimrudishe. Tafadhali sana. Huyu mtoto yupo sawa kabisa hapa.
Usione unawajibika kumuweka kwenye hayo mazingira yenu ya hali ya juu,
ya kitajiri. Mwanangu yupo sawa. Mmemtia hofu, anaogopa kabisa kuwasogelea!
Hapana Mill.” “Naelewa. Lakini swala la shule? Maana nilitaka nije
kumchukua kesho nimpeleke shule. Angalau aendelee na wenzake. Hawajafika mbali.
Mihula yao ya shule si kama shule za hapa. Wao ni kama wanaanza.
Nimezungumza nao, hajachelewa.” “Sawa.” Mill hakuamini.
“Kwamba upo
tayari anaanze kesho?” Akauliza kwa kutaka uhakika. “Si ndivyo
unavyotaka?” Ikabidi Pam na yeye aulize. “Kabisa. Kila kitu kipo tayari kasoro
yeye na sare zake. Tena akifika wakimjaribisha, wanaweza kumpa siku hiyohiyo.”
“Unataka saa ngapi awe tayari? Naweza hata kumsogeza.” “Hapana. Nitamfuata. Saa
12 kamili asubuhi awe tayari.” “Sawa.” Mill akatulia kidogo akawa kama anasita
kusema kitu.
Pam akamgundua.
“Umefanya nini tena?” “Sio kitu kibaya.” “Sasa mbona unasita kusema?”
“Katika majina ya Shema nimeongeza na langu.” Pam akapigwa na butwaa. “Na
usikasirike. Kama hutaki, tusigombane, nitalitoa. Ila nimemuandikisha
kwa jina la Shema Shelukindo Mgini.” “Kwamba la
ukoo wetu ndio liwe la katikati lako ndio liwe la mwisho?!” “Ndiyo.” Akamuona
kama anayetaka kulipuka, akawa kama amejionya. Akatulia.
“Ila kama unaona
ni sawa mtoto wangu MIMI, aitwe jina la BABU yako WEWE, sio langu, mimi sitabisha. Nitaenda
kulifuta kesho. Nimuache aitwe vile unavyotaka wewe.” “Hakika unanijaribu
kupita uwezo wangu!” “Basi Pam. Basi. Kesho nitaenda kufuta langu.”
Akajilalamisha makusudi.
“Na uhakikishe
anaitwa majina yote matatu. Sio Shelukindo lifupishwe liwe ‘S’ aishie
kuitwa Shema S Mgini!” “Sithubitu.”
Alifurahi huyo na kuondoka haraka bila ya kuongeza jingine, asije haribu. Ila
akashangaa vile Pam alivyo tulia siku ile. Akajua amesoma barua zake.
Kutoka Uswaz
Mpaka Internatinal School.
Alifika hapo saa
12 kamili asubuhi. Pam alishamwandaa mwanae. Alikuwa msafi na alishatolewa pop.
Baba yake akamchukua, Pam akawahi daladala na chapati zake kuelekea kazini.
Aliweka juhudi
na mwanae, mpaka Pam alikuwa akimuhurumia. Alfajiri anakuwa amewasili hapo na
kumrudisha jioni kwa wakati. Akafanya hivyo kama mwezi mzima.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jioni moja wakati amemrudisha mtoto, Pam
akatoka na kumfuata garini na kumuuliza. “Kwani yule dereva aliishia wapi?”
“Alinimbia ulimfukuza. Nikajua hutaki mtu mwingine amchukue
Shema.” “Wewe tuma dereva ili uwe huru na kazi zako.” Akamuona anafikiria.
“Ingenisaidia.
Lakini, huu muda ninaokuwa naye njiani, nahisi unamsaidia sana Shema.
Kumbuka ametoka kwenye masomo karibu yote ni kiswahili, lakini sasahivi masomo
yote ni English. Sasa alipogundua na mimi nilisoma kiswahili na najua
English, kuna maswali ananiuliza tukiwa njiani. Nahisi anakuwa akiyaandika kila
akikwama, ambayo ni yale madogo madogo nafikiri hawezi muuliza
mwalimu, akamuelewa. Sijui kama unanielewa?” Pam akawa bado anataka
kujua zaidi. Akaendelea.
“Namuhisi
anaakili sana, halafu ni msomaji. Hata jinsi anavyouliza, utagundua ni
mtu mwenye uelewa wa juu. Au anaufahamu na anachokizungumzia. Kwa hiyo
kila akiwa anasoma, akikutana na kitu kikamtatiza, nahisi anaandika.
Nikiwa naye njiani anaomba nimtafarisie. Au kumuelezea zaidi.”
“Kwa mfano mdogo
tu, upande wa hesabu anajua kigao kidogo cha shirika. Hesabu ni
zilezile, lakini sasahivi anakutana na hesabu anazozijua, lakini wanamwambia
kwa lugha nyingine kwamba atafute low denominator. Basi ndio ananiuliza
kama ni vilevile au ni tofauti.”
“Aaah! Masikini mwanangu! Ndio maana amepoa,
michezo amepunguza! Kutwa yupo ndani anaandika, wenzie wapo mlangoni
wanamsubiria hamalizi! Utawaonea huruma! Nikimuuliza, ananiambia anamalizia.
Wakati mwingine usiku anaomba tusizime taa, ili asome, analala ameshika kitabu!
Sijamuona akisoma hivi tangu anaanza shule, mdogo. Amezaliwa na ile akili akifundishwa
darasani, ujue ndio kimekaa. Harudii kusoma tena. Sasa kumuona
anajisomea mpaka muda wa mpira hamna, nikahisi amepata kibako
yake. Kumbe ni lugha!”
“Ila kwa jinsi
ninavyomuona na hiyo juhudi, anahitaji muda mfupi sana, atakaa sawa tu.
Lugha ndio kwa sasa ni kikwazo. Hajaweza pia kuzungumza na
wenzie. Walimu wake wameniambia bado hajaweza pata rafiki. Maana pale ni watoto
wa mabalozi, na wafanyakazi wa kigeni waliopo hapa nchini kwa shuguli maalumu.
Na waafrica wachache ambao ni kweli hawajui kiswahili. Amejikuta amekwama
peke yake.”
“Masikini
mwanangu!” “Hapana Pam. Namuona hajakata tamaa. Na mimi sitaki
kumuonyesha ni tatizo. Nimewasisitiza walimu wake wamchukulie taratibu sana ili
asipaniki na kukata tamaa. Kwa upande mmoja bila marafiki
itamsaidia kupunguza destruction, atajiangalia mwenyewe na kufanya mambo
kwa haraka na vizuri.”
“Wanasema muda
mwingi kwa kuwa yupo peke yake, anakuwa anasoma. Na wanasema kwa kuwa anapenda
kusoma na anatabia nzuri, walimu wengi wanajisogeza kwake kumsaidia.
Akishaweza kuweka lugha kwenye anachokifahamu, atawakimbiza wale watoto
wakizungu pale, mpaka watamjua Mgini kwa kumtamka kama wazawa wa hapa.”
“Unavyojisifia! Ndio maana umeweka jina lako mwisho na kutoa la babu
yangu. Mbaya wewe!” Mill akacheka sana.
“Acha nimsaidie
kidogo. Nabanwa kwenye majukumu yangu mengine, na dereva angenisaidia sana tu,
lakini nimeona ni mtoto mwenye muelekeo, halafu ananihitaji si
kama wale ndugu zake, acha nimtie moyo. Nikishamuona amekaa sawa, ndio
nitamtafutia dereva. Ila acha sasahivi niwe naye mwenyewe. Apate smooth
transition.”
“Naomba uelewe nakushukuru
Mill. Kutoka kwenye moyo wangu, pokea shukurani zangu. Asante kwa kuwekeza kwa
mwanangu, nakushukuru sana. Asante.” “Pam, ni mtoto wangu pia!” “Mtoto
wa kukutana naye barabarani ndio umuhangaikie hivi! Sisi tulikuwa
watoto wa ndani ya ndoa na pia tuliachwa, sembuse Shema wangu
huyu! ASANTE.” “Shema si mtoto wa barabarani. Huyu mtoto amezaliwa ndani
ya penzi zito la agano lenye baraka za wazazi wetu.” Pam
akaondoka kabisa hapo dirishani alipokuwa amesimama kwenye gari lake. Akaingia
ndani bila ya kujibu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mill akakazana
na huyo mtoto, yeye mwenyewe bila kuweka mtu. Ndani ya miezi mitatu kweli
matokea yakaanza kuonekana. Akaanza kuburuza watu darasani kiasi cha kushangaza
wote. Yale masomo waliyokuwa wakifeli wengine, yeye anaweza pata asilimia 100
au akifeli ni 98, halafu anayemfuata anaweza akapata hata asilimia 45 au chini
zaidi. Akaanza kuwa gumzo hapo shuleni.
Kila mwalimu
akamjua. Na kwakuwa hakulelewa mazingira ya watoto wa wakishua/kitajiri ya
kulemazwa, akawa na adabu za kitanzania kabisa hapo shuleni, halafu kwa
wote. Akazidi kuwavutia walimu wake ila wanafunzi wenzie kumuona mjinga
au mshamba.
Mtoto
aliyelelewa kwenye nyumba ya kupanga uswahilini, mama watatu, wote wapo
naye na watoto wa mtaani wakiishi kijamaa, basi pale shuleni akajulikana kwa kujali
watu wote bila kubagua.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Siku ya mwisho
kabla ya kufunga shule, walipanga kutambua watoto waliofanya vizuri na kuwapa
zawadi. Sasa kabla ya hiyo siku kufika, jioni moja ambayo anamshusha Shema, Pam
alifanya kama mazoea, lazima amfuate Mill garini aulizie maendeleo ya mwanae.
Maana huwa hashuki garini, akimshusha tu, anaondoka.
Mara nyingi Pam
husubiria kabisa nje. Akiona tu gari, anasimama karibu. Mwanae atasalimia na
kuingia ndani kuwahi chakula, yeye anabaki kuuliza kwa kifupi. “Nimepewa barua maalumu
ya mualiko pale shuleni kwao hawa. Katika watoto wanaofanya
vizuri shuleni kwao, na yeye yupo. Watawatambua mbele ya shule
nzima na wazazi. Wametuambia tunaweza kualika watu wa karibu. Ni muhimu
Pam. Na ni kitu kikubwa. Naomba ujitahidi uwepo.”
“Na mimi ameniletea hiyo barua. Lakini kumbuka
nimeajiriwa. Ikitokea yule mama ananipa ruhusa, nitakuja. Kesho nikifika
tu, nitamuomba ruhusa. Sasa inategemea na kichwa chake vile alivyoamka. Hatabiriki.
Ila nikishindwa, tafadhali nichukulie video na picha nyingi nimuone.” “Tafadhali
naomba uhudhurie Pam.” “Nitajitahidi. Sina chaguzi Mill! Hii kazi ndio inategemewa
mpaka na mama yangu mzazi kule kijijini! Hana msaada mwingine ila mimi
tu. Siwezi ipuuza au kukosea. Nikikwama mimi, jua na wao
kule kijijini wamekwama.” “Naelewa.” Akafikiria na kuona aulize.
“Mbona kama Eric
ana kazi nzuri sana?” “Mmmh! Hafikiki. Na mkewe alishakuwa muwazi kabisa
kuwa na wao wana majukumu mazito. Wanasomesha watoto wao kwenye
shule za garama na kujijenga. Ni kama mkewe ndiye anayeshikilia pesa
yote. Mbaya zaidi, niliposhika hii mimba ya Shema na mama kuja huku kunisaidia,
aisee ni kama nilimponza. Eti amemsusa mama, kwamba ananiendekeza.
Alitakiwa kuniacha, nijifunze peke yangu. Ila mama ananiambia nisijali.
Amepata tu sababu. Hakuwa mtoaji tokea amepata mke. Kwa hiyo Eric
si wakumtegemea kabisa. Nisipomtumia mama pesa, ujue ndio amekwama.”
“Ndio na bibi na
babu?!” “Mjomba anajitahidi kwakweli. Na mkewe ni msaidiaji japo mlalamishi
sana. Japokuwa nilikuwa nikiishi kwao, nilipokuwa nikienda kijijini,
shangazi alikuwa haachi kunipa vitu nipeleke kwa wakwe zake. Hana
roho mbaya, ni ubinadamu wa kawaida tu. Ila sasa sitaki mama akae pale aombe
wazazi wake mpaka pesa ya sabuni yake yakuogea! Au akiugua ndio tena ategemee
wazazi ambao kwanza ni wazee, pili na wenyewe wanamtegemea mjomba! Naona
sio sawa.”
“Unajitahidi
Pam! Unajitahidi sana.” “Hivyohivyo, sio nyingi ila tunasogea.” “Binafsi
najivunia Pam wangu.” Pam akacheka kinyonge na kuondoka hapo garini. Ila
angalau waliweza zungumza. Angalau hilo likamfariji Mill!
Maji Yamezidi
Unga kwa Mill na watoto wa Marekani.
Ila ukweli furaha
ya Mill ilikuwa ni pale anapokuwa na Shema. Mengine yote ilikuwa vurugu. Watoto
aliokuja nao nchini alijikaza mpaka maji yakafika shingoni. Hawabadiliki
na jeuri inazidi. Hawana shukurani na yeye hata kidogo. Walimdharau kama
walivyoona mama yao akifanya. Wakaibua maswali mengi sana kwa Mill. Kadiri akiwalinganisha
na Shema mtoto aliyekutana naye muda mfupi, ni kama usiku na mchana.
Kadiri
alivyokuwa akiwaangalia na kuwatafakari, mahesabu yakaanza kutolipa.
Kwa kuwa hapo hospitalini kwa kina Komba aliweka mashine za kisasa. Nzuri sana
zilizokuwa zikimuingizia pesa nzuri, maana zilikuwa chache nchini kwa hiyo watu
walitoka sehemu mbalimbali kufuata vipimo kwenye kitengo chake. Akawa na ofisi
yake nzuri tu na wafanyakazi baadhi chini yake. Basi hapo akaweka kituo
akifanya na mambo yake ya stocks mtandaoni. Kuuza na kununua hisa,
kitega uchumi alichojifunza na kufanya kwa miaka mingi sana na ndiko alikojilundikizia
pesa.
Alijua ni mida
gani aingie sokoni auze na kununua hisa. Wakati gani hisa/stocks
ziko vibaya, ashikilie asiuze, au kipindi gani anunue nyingi. Amefanya hivyo
kwa miaka mingi tokea tu alipofika nchini Marekani mpaka akawa mtaalamu. Haishi
sehemu bila kuwa hewani. Mtandao kwake ni masaa 24.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Colins
akamtembelea upande zilizopo kazi zake hapohapo hospitalini. “Mbona kama haupo
sawa?” “Kuna kitu nataka kufanya, lakini nahisi ni hofu tu. Nimejaribu kukipuuzia
muda mrefu, naona kinazidi kunipigia kelele. Siwezi kulala,
siwezi kufikiria.” Colins akakaa vizuri.
“Unataka
kukizungumzia?” Akafikiria, akawa kama anasita. “Hivi ndivyo vipindi namkumbuka
sana Mike. Ndio alikuwa kama jalala langu. Namtupia kila kitu.
Huzuni zote na furaha zote alijua kuzibeba! Hakika wamenikatili aisee! Kumtoa
Mike duniani!” “Pole sana Mill. Lakini
na mimi nipo.” “Sitaki kukuchosha na maisha yangu! Nahisi nimejivuruga
sana.” “Unamzungumzia Pam?” “Nianze mimi mwenyewe.” Akajiweka sawa.
“Nisikilize tu
nikwambie kitu.” Akamsimulia mkasa wa mara ya kwanza kulala na Kisha. “Yaani
Colins, ilikuwa ni kama nilazima NILALE naye usiku ule na si vinginevyo.
Na zikawa siku kamili zimetimia za mtu kujua kama alishika mimba, akanivaa
akiwa na mama yake kuwa ameshika hiyo mimba. Kumbuka huyu mtu hatukuwa hata
tukitumia chumba kimoja na haikuwahi kubadilika.”
“Miles akazaliwa
siku zikiwa hazijatimia tokea nilale na mama yake na kushika hiyo
mimba. Tena nakuja kupata taarifa za kujifungua kwake masaa
machache baadaye.” “Haiwezekani!” “Kabisa. Na ukumbuke wanawake wa kule wanavyokuwa
kwenye swala la kujifungua.” “Lazima uwepo.” “Ewahh! Sasa
sikiliza juu ya Mia.”
“Hapakuwahi kuwa
na amani aisee pale kwetu. Ila tukawa tukilea mtoto nyumba moja, vyumba
tofauti tofauti. Akaanza kuwa mwema mpaka nikashangaa! Ubishi akaacha
kabisa, hataki nikasirike. Akafanya kama majuma mawili mpaka kufikia siku ya Anniversary
yetu. Akaomba tusafiri sisi tu na mtoto. Sasa kwa kuwa kulikuwa na amani, na
bado sijapata uraia, tupo kwenye ndoa ya maigizo, namtegemea yeye baada ya hiyo miaka miwili nirudi
naye Uhamiaji anitetee kama bado mimi ni mumewe, ndio nipewe sasa
Green Card ya miaka 10, alipo nibembeleza, nikajiambia sio
wazo baya. Tutapata hata picha za ushahidi. Nikakubali, sikutaka
kumtibua.”
“Tulipofika huko
akawa mwema, mke kwelikweli. Na mimi si muhuni Colins. Sijui kuwa
na wanawake hovyo na hapo ukumbuke bado moyoni nilikuwa na Pam. Ila
nikalala naye tena kwa mara ya pili.” “Subiri kwanza Mill.”
“Kwamba sio
kwamba mlikuwa mkifanya mapenzi mara kwa mara?” “Nakwambia ni mara ya kwanza aliponigomea
kwenda kufunga hiyo ndoa na siku hiyo. Kwa sababu ilikuwa ni ndoa ya
MKATABA kabisa. Namlipa kama mfanyakazi. Sasa siku inayofuata baada ya
kulala naye kwa hiyo mara ya pili, yaani sasahivi ndio natulia, nafikiria
na kugundua ni kama alinitafutia sababu kabisa.”
“Aliamka kama mbogo,
tena hukohuko tulikokuwa mapumzikoni. Tulirudi nyumbani hatusemeshani kabisa.
Na ndani ya majuma manne akasema tena ameshika mimba ya Mia. Hakika sikuamini.
Ila sasa kukataa siwezi. Maana na safari hii alifanya kama mwanzo ila
zaidi. Aliniambia taarifa za huo ujauzito wa Mia, akiwa na mama yake
pamoja na anti zake. Niliwakuta wakisherehekea hapo tulipokuwa tukiishi,
ndio wakaniambia wanasherehekea ameshika mimba.”
“Akaanza kliniki
ambazo nyingi hanikaribishi.” “Mmmh!” “Umeona hapo? Wanawake wa kule
kwenda kliniki ni lazima uwepo, usipokuwepo ni kosa la talaka
kabisa.” “Najua!” “Basi yeye akawa ananiambia nisiache kazi kwa ajili hiyo. Mpaka
wakati mwingine nilikuwa nikimlazimisha na mimi kuwepo kwenye hizo kliniki ambazo
anafanyiwa ultrasound ili angalau na mimi nione mtoto. Napo ikawa kama
kuna kukwepwa fulani hivi mpaka nikaona nimuache tu. Ila hapo katikati
akaanza kusema kuna complication, daktari anamwambia hadhani kama mtoto
atatimiza miezi tisa. Kufupisha habari, naye Mia akazaliwa kwa staili hiyohiyo
kama kaka yake. Amepatwa uchungu, sikuambiwa, nimekuja
ambiwa ashajifungua. Nikanyamaza kwa sababu nilijua hata hivyo haikuwa
ndoa, tupo kimkataba.”
“Sasa kadiri
ninavyomuangalia Shema na hawa, nazidi kuwa na wasiwasi Colins! Hawa
watoto ni wangu kweli!?” “Mbona rahisi sana. Wapime!” “Naogopa jibu
ambalo nishalihisi ndilo.” “Huna chakupoteza. Ukijua ukweli
utapata uhuru wa kuchagua kama kuwatunza ukijua si wako, au kuwarudisha
kwa wazazi wao.” Mill akatulia akifikiria mwishoe akaona liwalo na liwe.
Maamuzi Magumu.
Kujua Mbivu
& Mbichi.
Akatoka muda huohuo kurudi kwake. Akachukua miswaki ya hao watoto na baadhi ya nywele walizoacha kwenye vyanuo vyao, na kurudi navyo hapo hospitalini. Wakasaidiana na Colins, wakamuachia mtu wa maabara afanye vipimo. Maana hata damu hazikuwa zikifanana na hao watoto wawili, Mia na Miles. Ilikuwa ni vipimo vinatakavyochukua majuma matatu mpaka mwezi. Akabaki akisubiria kwa hamu ili ajue moja. Ila hakumshirikisha hata Pam juu ya wasiwasi wake juu ya hao watoto japo na yeye aliongeza wasiwasi pale aliposema ametapeliwa. Akalinyamazia hilo. Ikabakia siri yake yeye na Colins akisubiria hayo majibu.
Siku Ya Zawadi,
Yazua Janga kwa Pam
Siku hiyo
ilianza kama kawaida tu. “Naomba usikose mama. Nataka uwepo wakati napewa
zawadi, ndio nitafurahi.” “Acha nikaombe ruhusa kwanza. Nitaona. Ila
nitajitahidi.” Mill akaja kumchukua mwanae, wakaondoka. Kama kawaida naye Pam
akachukua daladala, akaelekea kazini. Jambo la kwanza akamuomba bosi wake
ruhusa, akamkatalia. “Yaani uache kazi hapa sababu mwanao anaenda pewa zawadi!
Ujinga gani huo? Kama hutaki kazi, basi.” Akakwama.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Huku kwa Mill
yeye kumbe alilifanya jambo kuwa zito. Alishaalika familia ya Komba wote
akisisitiza ni muhimu kwake kwa ajili ya Pam atambue jinsi wao
walivyo wamuhimu kwake. Kwamba Dokta Komba aliacha shuguli zake muhimu,
akaenda kuhudhuria. Colins na Kamila pia walitoka kazini wakaenda huko
shuleni kwa watoto wa Mill. Mama Colins yeye ndio hata kazini hakwenda, na wote
walimnunulia zawadi huyo Shema.
Muda wa saa nne
na nusu, shuguli ikaanza. Wazazi wote na wageni wao pamoja na wanafunzi
wakakusanyika ukumbini. Mkuu wa shule akaeleza dhumuni kubwa la kuwa hapo.
Akaweka uzito haswa. Mpaka kila mtu akaona umuhimu wa kuwa pale.
Wakaanza kutaja
madarasa ya juu mpaka darasa la nne la kina Shema. Wanafunzi wenyewe waliokuwa
wakipewa zawadi ni wachache sana kulinganisha na idadi ya wanafunzi wote
wa hiyo shule. Ila Mill akamuona mwanae amekuwa mwekundu, macho yapo
mlangoni, kuingilia hapo ukumbini.
Mtu wa kwanza
kutajwa kwenye hilo darasa la nne akawa yeye Shema Shelukindo Mgini.
Baba yake akaona hasimami, macho yapo nje. Watu wakapiga makofi mpaka
wakaacha, Shema hasimami. Akaitwa tena. Hakusimama. Alikuwa
amekaa katikati ya Colins na baba yake, ndugu zake upande mwingine wa baba yao,
wapo kwenye simu zao wanachezea game wala hawana habari na walipo na
kinachoondelea.
Mill
akamwangalia. “Pengine mama yako amekosa ruhusa. Nenda nitamchukulia video,
ataona.” Akabaki ameinama. Jina lake likaitwa tena. Mill akasihi,
akasimama na kwenda kupokea. Hajafika katikati ya ukumbi kurudi
alipokuwa amekaa, akaitwa tena kwa soma jingine kwamba amefaulu kwa
kiwango cha juu sana. Akarudi akapokea tena zawadi. Kabla
hajafika tena katikati, akasikia tena jina lake. Watu wakaanza kushangilia
sasa mpaka kusimama. Maana walikuwa wakieleza uzito wa somo, kiwango
alichofika mpokea zawadi, ndipo anatajwa jina.
Mara Shema akaangua
kilio. Watu wakashangaa. Ikabidi Mill aende kumchukua maana alibaki
amesimama katikati ya ukumbi. Hataki kurudi kuchukua zawadi, hawezi
kurudi tena kukaa. Analia kwa kwikwi kabisa. Mill akaenda
kumkumbatia na kurudi naye pale mbele ya walimu.
“Samahanini.
Alitaka mama yake awepo, ila ametingwa kwenye kazi. Nakwenda kumpigia simu
nijue alipofikia. Kama mnaweza, naomba zawadi zake ziwekwe mwisho.
Wakakubali kuahirisha kwa muda. Ndipo akatoka na mwanae sasa kwenda kumtafuta
Pam.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Namba ya Pam hana,
mwanae analia kwelikweli. Ikabidi amtulize amuombe namba ya mama yake,
akampigia. Colins naye akatoka na wengine wakafuata kwenye familia ya Komba.
“Vipi?” “Hawezi kupokea zawadi bila mama yake.” Baada ya muda akapokea kukiwa
na kelele kama yupo kwenye pikipiki.
“Tafadhali naomba niambie upo njiani,
Pam. Shema ameshindwa kupokea zawadi bila wewe.” “Nilikataliwa ruhusa,
hivi nimelazimishia. Nimechukua pikipiki nakuja.” “Naomba uzungumze
naye, atulie.” “Nipe.” Mtoto alikuwa akilia huyo, akashindwa
hata kuzungumza na mama yake, ila akamrudishia simu baba yake.
“Huyo hawezi kutulia mpaka anione.
Na hapa naweza kuongea na unanisikia sababu nipo kwenye foleni tumesimama,
ikiruhusiwa sitaweza. Ila nipo njiani nakuja.” Akakata. “Mama
yako anakuja, Shema. Naomba turudi ndani.” Wakarudi akiwa analia taratibu.
Ikabidi watoe
nusu saa ya vinywaji na vitu vidogo vya kujitafuna, wakisema itaendelea baada
ya muda. Wanafunzi wengine wakiwepo kina Mill wakatoka nje ya ukumbi, wengine
wakabaki ndani wakizungumza na wazazi wao hapo ndani wakiulizana kulikoni kwa
huyo mwanafunzi bora! Wakabaki hapo nje kimya wakimsubiria Pam.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya kama
dakika 10 hivi Mill akamuona Pam katikati ya watu akiwatafuta, kama aliyekuwa
akikimbia. Nywele kama amemwagiwa mchanga! Chafu. Yeye mwenyewe kama aliyeanguka!
Amefunika mkono. Mill akamuita akimfuata.
“Vipi, kwema?
Mbona upo hivyo?” “Mimi nipo sawa. Yuko wapi?” “Mwanao amegoma kupokea
zawadi zote. Na bado analia.” “Yuko wapi?” Mill akaongoza njia mpaka akamuona
mwanae. Akamsogelea Shema. “Pole nimechelewa. Nionyeshe zawadi.” “Anazo baba.” “Nyamaza, usilie. Nimekuja tupokee hizo zawadi. Pole.” Akaendelea
kumbembeleza mwanae taratibu asijue hata waliopo pembeni yao, maana watu
walikuwa wengi. Yeye akili akaweka kwa mwanae tu, kumtuliza. Mill
akamkabidhi mama yake hizo zawadi alizokuwa amepewa na kuondoka kumuwahi mkuu
wa shule kumtaarifu kwamba mama Shema amefika.
Kwa Mara
Nyingine Tena, Pam Akutana Na Kamila
Wakaitwa tena
watu wote ndani. Watu kuangalia huyo mama aliyekuwa akisubiriwa! Ni mchafu
huwezi sema alikuwa kwenye kazi ya maana! “Mbona kama una mamumivu mama?”
Wakamsikia akimuuliza mama yake. “Nipo sawa. Usiwe na wasiwasi. Jua najivunia
sana wewe baba mzazi. Nimefurahi mimi! Leo nitacheza mdumange
mpaka kuchwe.” Mill na wengine wak awa wanawasikiliza wakiingia ndani.
Wakamsikia Shema akicheka huyo, kama siye yeye aliyekuwa akilia.
“Unanichezea
mimi mdumange?” “Nakwambia mpaka kuchwe. Na zawadi zote hizi!” “Nyingine bado
mama! Ninazo nyingi.” “Basi twende. Tukusanye zote. Halafu..” “Unaweka
kitandani kwanza, halafu ucheze sana?” Akamuuliza mama yake akicheka.
Wakawa wanazungumza wao wawili wakiingia ndani.
“Mambo Pam?”
Kamila akamsalimia. Pam akageuka na kukunja uso. “Umezungumza na mimi?!” Jinsi
alivyomuuliza, kidogo ikasikika sio vizuri, akafanya wote wawaangalie.
“Nimekusalimia.” Kamila akajibu na tabasamu. “Unanisalimia mimi?! LEO
ndio unanijua?” Akafanya kabisa kusimama, wote wakasimama.
“Huna haja ya
kuwa mnafiki Kamila. Mimi si kitu hata kwa huyo
Mill kama UNAFANYA kwa ajili yake.”
“Pam!” Mill akamtuliza, kina Komba wote wakasimama. “Nilikufuata kwako
Kamila. Nikiwa na tumbo la Shema, NIMETOKA jela. Njaa inaniuma,
nina kiu, UKAKATAA hata nisifunguliwe geti! Mlinzi wako akakwambia
kabisa, ‘Mama, huyu mama ni mjamzito, amekaukiwa kabisa, labda umfungulie
angalau umpe hata maji ya kunywa, anaweza kuanguka.’ Unakumbuka jibu
lako?” Kimya.
“Kwa taarifa
yako nilikuwa nikisikiliza mazungumzo yako na yule mlinzi wako, ulimjibu
kwa kumfoka kabisa maana alikuomba kwa mara ya pili unifungulie,
baada ya mara ya kwanza pia kumkatalia. Ukamwambia aniambie NIONDOKE, haupo.”
Wote wakashangaa. “Nikamrudia tena yule mlinzi, nikamwambia shida yangu ni
kumuulizia tu Mill. Nina wasiwasi, sijamsikia, akuulize kama
unajua kama Mill yupo salama? Unakumbuka Kamila?” Jabza ikawa imeshampanda Pam,
Kamila kimya.
“Kwa mara ingine
tena, ulimfoka yule mlinzi. Ukamwambia NIONDOKE pale, aniambie hampo,
wakati nikikusikia ndani! Ulishindwa hata kunipa maji ya
kunywa, mlinzi wako akikusihi unisaidie, nimekaukia na nina mimba!
Ukabaki gorofani kwenu pale, ukitoa amri nifukuzwe. Eti leo
unaniulizaje?” Kimya.
“Acha unafiki
Kamila. Na wala usijisumbue. Mimi ni Pam yuleyule uliyenifukuza kwako, sijabadilika.
Sikuwa na maana siku ile, na LEO sina maana. Nimekuja hapa kwa ajili ya
mwanangu, sitakubugudhi, na wewe usinibughudhi. Mungu wako atashugulika
na wewe, wala si mimi. Twenda Shema mwanangu.”
“Kwamba Kamila
wewe ulijua kama Pam ni mjamzito, ulishindwa kuniambia!?” “Sikutaka kuingia
katikati yenu Mill!” Pam akaondoka na mwanae, akawaacha. “Kwamba hata usinigusie,
halafu ukanipa nafasi ya kuchagua?! Kweli Kamila? Miaka yote hiyo
tupo pamoja!” Kimya. “Mike alijua swala la ujauzito wa Pam?”
“Sikumwambia.” Mill alishangaa, akashindwa kuelewa, ila akagundua watu
wanazidi kuwapita kuingia ndani. “Nashauri haya mambo tuzungumze baadaye Mill.
Tumalize hili la Shema kwanza.” Mzee Komba akashauri, wakaingia ndani.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Shuguli ikaanza
tena. Mkuu wa shule akaomba radhi na kueleza UMUHIMU wa kusubiri, ndipo
wakaelewa. Walisema ni kwa mara ya kwanza kupata mwanafunzi kama Shema.
Kutoka chini sana, na kuweka juhudi ya namna ile. Alieleza jinsi
alivyofunga mwaka kwa kupata alama zote 100 mpaka kushangaza waalimu
wote. Watu walipiga makofi mpaka kusimama kabisa.
Baba yake akamkumbatia
na kumbusu kichwani, Pam asiamini! Walishangilia ukumbi mzima kasoro
ndugu zake hao wawili. Miles na Mia, walibaki wameinamia simu zao kama hawapo
hapo.
Ndipo sasa
akaitwa kuanza kupokea zawadi. Ilibidi tu asimame palepale. Maana kila somo
alipata 100. Utii na nidhamu kwa walimu, YEYE, Shema Shelukindo Mgini. Usafi.
YEYE. Utulivu mpaka darasani, YEYE. Mtoto alipewa zawadi huyo, mpaka
akalemewa. Akakimbia akiwa amebeba, anacheka, mpaka kwa mama yake.
Akamkabidhi zote akicheka na kurudi tena mbele.
Akakabidhiwa
vitu vyake na kupewa mkono. Ndipo sasa ikatangazwa zawadi KUBWA. Akapewa
schoolarship, asilimia 100. Kwamba huyo Shema atasoma hapo bure
kwa miaka yote mpaka amalize grade 7. Na wakatangaza kumrusha
darasa moja maana walishampa mitihani ya kidato cha tano, akafaulu vizuri tu.
Pam alishangaa! Kwamba mwanae akiwa na umri wa miaka 9, anakwenda 10
anakwenda darasa la sita! Alifurahi sana.
Akatoka hapo na
kumkimbilia baba yake, akampa vyeti vyote. Maana kila zawadi aliyokuwa
akipewa, alipewa na cheti/certificate yake. “Asante baba.” Hakika Mill alifurahi
sana. Akaitwa aongee, akawa anacheka. Alivyo mzuri wakaanza kumpigia makofi,
akaenda.
“Mimi nililelewa
na bibi na mama yangu yule pale. Mama alipokuwa akienda kazini,
ananiacha na bibi yangu, na bibi yangu hawezi kutembea, ni mlemavu, kwahiyo
nikawa nashinda naye tu ndani, ananifundisha hesabu na kusoma. Halafu
mama na yeye akawa ananifundisha kusoma pia. Nikaanza kusoma tokea mdogo sana.”
“Bibi
alipoondoka, mama alipokuwa akienda kazini, akawa akiniacha kwa rafiki yake ana
shule ya chekechea na mimi nikawa nasoma nao. Ila nikawa tayari najua
kila kitu anachowafundisha wale watoto. Akamuomba mama anipeleke shule nikiwa
mdogo. Walimu wakanipokea, nikaweza kuanza shule nikiwa na umri wa miaka minne
tu nikaanza la kwanza.” Watu wakampigia makofi.
“Baba yangu
alipokuja, akanihamishia kwenye hii shule. Mwanzoni nikawa naogopa. Lugha
sijui. Lakini baba akawa ananifundisha vitu vile ambavyo sijui jinsi ya
kuuliza kwa english hapa shule, wakanielewa. Nikawa kila nikisoma,
naandika maswali yangu, nikipata tu muda na baba, namuuliza ananielewesha.”
“Baba yangu amenisadia
SANA. Isingekuwa yeye najua nisingeweza hii shule. Kuna vitu nisingeweza
elewa kwa haraka bila yeye. Kila siku za shule alfajiri ananifuata
kwa mama, na ananirudisha yeye mwenyewe jioni. Bila kuchoka. Na njiani
anazungumza na mimi, na kunielekeza mambo mengi. Yeye ndiye aliyenitoa hofu
akiniamini nitaweza, huku akiniongoza taratibu, mpaka nimeweza kuweka
mengi niliyokuwa nikiyajua kwa lugha ya kiswahili na kujifunza
hapa kwa upya kwa lugha hii ya kingereza na kuelewa kwa haraka.
Yote hayo ni baba yangu.”
“Na mama
aliniambia inamgarimu SANA pesa na muda wake ambao kwake ni
muhimu sana. Anaacha mambo yake muhimu, anakua akiniendesha yeye
mwenyewe, wala sio dereva ili anisaidie njiani pia. Tangia naanza
hii shule mpaka leo asubuhi, baba hajaacha kuniendesha kuhakikisha
nawahi shuleni na narudi nyumbani salama. ASANTE baba.” Watu wakapiga sana
makofi mpaka kusimama huku wakimwangalia Mill. Kwamba ni makofi yake.
“Halafu hapa
nimekutana na walimu wazuri sana. Kila mwalimu yupo tayari kunisaidia
ndio nikawa nawatumia. Halafu wakawa wananitia moyo, hata
wanafunzi wengine walipokuwa wakinicheka siwezi lugha, wao wakawa
wananitia moyo. Nawashukuru…” Akawataja walimu wake wote
na kuondoka kurudi kwa mama yake. Watu wakapiga sana makofi.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati mkuu wa
shule anafunga kwa neno la mwisho, Shema akamwangalia mama yake. “Mama,
mtandio umeloa damu!” Akajikuta anaongea kwa sauti ya wasiwasi. “Usiwe na
wasiwasi.” Mill akawa anasikia. Ikabidi kuamwangalia. “Ni nini Pam!?
Mbona mpaka jasho linakutoka jingi kama upo kwenye maumivu makali?” “Nipo sawa
tu.” Akajifuta na mkono mwingine wazi akionekana na maumivu.
Shuguli ikaisha,
watu wakawa wanatoka. Wale watoto wa Mill walikuwa kama hakuna
kilichotokea kwa kaka yao au hawakujua walipo. Walipoambiwa wasimame
walisimama na kuendelea na simu zao. Wakisimama, macho wanahamisha
kwenye simu, kimya.
Walipotoka
dereva wa wale watoto alikuwa ameshafika. Mill akawagutusha, wanae wakaondoka
hapo na kupanda kwenye gari na kuondoka bila kumsemesha mtu wala
kumpa hongera kaka yao au hata kumtambua kama yupo, ni kama
hakuwepo pale.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Pam
akajiangalizia, akaamua kumuaga Mill anayemfahamu na kumshukuru kwa
yote. “Hakika Mungu akubariki Mill. Asante kwa yote unayomfanyia Shema.
Nashukuru sana.” Kina Komba walikuwa pembeni, wakijingalizia
yote. Mill katikati ya hiyo familia iliyochanganyika. Watoto wa wanawake
wawili tofauti tofauti, na huyo Pam. “Usihesabu Pam! Shema ni mtoto
wangu.” “Hata hivyo. Nakushukuru. Asante. Yote haya yamewezekana sababu yako.
Muda na pesa. Shema hajakosea. Wewe ndio umemfanya afike hapa na kuweza
yote haya. Nakushukuru.” Mill akajisikia vizuri. Angalau mwanamke huyu wa ndoa
ya kimila, alijawa shukurani, si kama Kisha, mke wa ndoa
ya mahamani, na wanae.
“Karibu Pam.”
“Basi acha leo mimi nimrudishe Shema nyumbani, ili na wewe angalau leo
ukafanye shuguli zako. Mchana mwema.” Bila kugeuka nyuma, akaanza
kuondoka na mwanae wakitoka nje ya geti wakatafute usafiri. Kina Komba
walishatoa pongezi zao, Pam akiwa pembeni tu anamsubiria mwanae, kimya.
Walipomaliza ndio akaondoka naye.
Ila Mill alibaki
akiwaangalia vile wanavyoondoka pale wao tu wakitembea kwa miguu, Pam
yupo hovyo, mchafu, amejawa vumbi halafu kama yupo na maumivu, wakati
wengine wote magari ya maana na ya kifahari yakiwasubiria! Akashindwa.
Akawakimbilia
Pam na mwanae bila hata kusema kitu kwa hao wageni wake kina Komba. “Acha
niwasogeze Pam.” “Usijali. Sisi tutakuwa sawa. Na wewe pata muda leo, ufanye
mambo yako kwa utulivu.” “Upo na maumivu Pam. Ni nini? Na usiniambie si kitu,
maana naona kabisa damu.” “Ni nini mama!?” “Wakati nakuja huku, tulipata ajali
na pikipiki. Nitakuwa sawa. Usiwe na wasiwasi. Twende.” “Kwa nini unakataa
nisiwapeleke?!” “Unayofanya kwa huyu, yanatosha, Mill! Achana na
mimi. Baadaye.” Akamgeukia Shema. “Twende.” Wakataka kuondoka.
Mill akamuwahi
tena. “Pam, kuna hospitali niliyompeleka na Shema, wale ulio waona pale ni
wamiliki, na watu wangu wa karibu sana. Na nimewekeza baadhi ya mashine zangu
pale. Ukienda pale, watakuangalia kwa haraka. Tafadhali
usirudi na mtoto nyumbani ukiwa na maumivu, ukaugua mkiwa peke yenu.
Mimi sina majukumu mazito ya kushindwa kutoa muda wangu sasahivi.
Tafadhali twende.” “Mkono unauma! Unauma sana.” Akajikuta
anajisalimisha. “Basi twende hospitalini.” Safari ya hospitalini kwa kina Komba
ikaanza.
Pam na Ajali.
Kwa hakika Pam
alikuwa ameumia haswa. Kumbe mkono ulipasuka, akafunga na shati la
mwenye pikipiki na ndio kujifunika mtandio. Alizuia kuvuja kwa damu kwa
kufunga hilo shati, hasemi, ameng’ata meno mpaka shuguli ilipoisha. Mbaya
ilikuwa ni mkono wa kulia.
“Mill, ni mbaya
aisee!” Colins akamfuata baada ya kutoka chumba alichokuwepo Pam akiangaliwa na
daktari. “Naombeni mumsadie, asiondoke hivyo alivyo.” “Lakini unajua inabidi
aingizwe chumba cha upasuaji kabisa? Amepasuka kuzunguka mkono mzima!
Nyama za ndani kukaribia mfupa mkubwa zinaonekana kabisa! Na amepoteza damu
nyingi.” “Mimi aina yangu ya damu ni O, kama atahitajika damu, nitampa yangu.”
Ikabidi akimbizwe theater, chumba cha upasuaji.
Alishonwa na
kurudishwa kwenye chumba cha kupumzikia. Alimkuta Mill na Shema wakimsubiria.
“Vipi?” “Nashukuru, asante.” “Najua Pam! Ila nataka kujua unaendeleaje
maumivu?” “Nahisi wamenipa dawa inayonifanya nisikie nafuu kubwa.”
“Pumzika basi.” “Hapana Mill. Inatosha. Acha sisi tuondoke.” “Unaweza
kupumzika hapa kwa leo, nitamchukua Shema.” Alishituka Pam kama anaombwa
roho.
“Hapana
Mill! Nisaidie kuturudisha nyumbani, tutakuwa sawa tu.” Hapo anazungumza
ana madawa ya usingizi kibao. Akapitiwa usingizi hata kabla hajajibiwa. Mill
akabaki njia panda. Huyo mrudishwa nyumbani na mtoto, yupo hoi.
Shema akabaki akimwangalia mama yake kwa wasiwasi.
Colins akaingia.
“Vipi?” “Anasema maumivu yamepungua ila naona analemewa na usingizi.”
“Nashauri umuache apumzike hapa kwa leo.” “Ndivyo ninavyotamani, lakini
mwenyewe hataki. Anataka nimrudishe nyumbani.” “Atafanyaje na mtoto?!
Huo mkono hataweza kuutumia kwa muda mrefu aisee! Vinginevyo atajikuta anajitonesha
kila wakati. Ameshonwa karibu sana na kiwiko!” Mill akabaki akifikiria.
“Najua shida
yake ni Shema.” Akawaza kwa sauti na kumgeukia Shema. “Kwa leo twende ukalale
nyumbani uta…” Mtoto alishituka huyo mpaka Colins akashangaa. Akasimama pale
alipokuwa amekaaa akaanza kusogelea kitanda cha mama yake.
“Shema! Na mimi nitakuwepo,
nitakupa chumba chako.” “Watoto WAKO hawanipendi. Yule wa kiume, Miles,
amewaambia darasani kwao mimi ni mwizi, nilikuja kwenu, nikaingia
chumbani kwake nikamuibia. Rafiki zake wote hawaniiti Shema,
wamenipa jina la mwizi. Wakiniona popote wananiita mwizi na kunicheka.
Na yule mtoto wako wakike, mdogo, Mia, amewaambia rafiki zake nilikuja
kwenu nikawa sijui kutumia vyoo vyenu, nikajinyea, rafiki zake wananiita
pop face. Hata wakinikuta sehemu na rafiki zake wananiita pop face.”
“Wakati mwingine Miles na rafiki
zake wananizomea bwaloni, siwezi kula naenda kukaa chooni. Sitaki
kwenda kwenu, nabaki na mama.” Akaanza kulia. Nusura Mill
kutokwa na machozi. Mpaka Colins alibadilika rangi.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Mill Anafanyaje na aina hiyo
ya watoto tofautitafauti.
Je, watoto wa Kisha ni Wake?
Usikose Kujua majibu ya DNA, na HATUA atakayochukua baada ya hapo.
Aidha wawe wake au la, atafanyaje kukuza watoto hao wa aina mbili TOFAUTI, pamoja?
Pam anamtaka, lakini
Pam alishakataa kuwa mama Kenny. Na Pam hajui kinachoendelea kwa mwanae
akiwa shuleni.
Je, Shema atamshirikisha mama
yake juu ya mateso ya ndugu zake wanapokuwa shuleni? Pam atafanyaje?
Nini Kitaendelea kwa Love
at first sight kwa
Pam&Mill?
Inaendelea…..
0 Comments:
Post a Comment