Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 36. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 36.

Juma zima hakumsikia wala kumuona Mill. Siku ya jumamosi jioni Pam akapokea mgeni anayemuulizia mama Shema. Alikuwa akipika chapati. “Unataka nini?” Akamuuliza kwa jeuri akijua wazi ametumwa na Mill. “Nina mizigo yenu hapa.” Akatulia akifikiria kama apokee au la! Wote kimya. Walimjua Pam alivyo jeuri. Na hataki kuingiliwa. Wote kimya wakisubiria kujua uamuzi wake.

“Nani amekutuma?” Akimjua mtumaji kabisa, ila akauliza. “Baba Shema na ameomba usome barua yake.” Akanyamaza. “Niweke wapi?” Akauliza kwa makini kama aliyeonywa. “Shema, mpokee uweke ndani.” “Bora shoga, nilijua ungekataa!” Ndio kila mtu akaanza kuongea lake.

Akaweka mpaka akamliza. “Amesema funguo za gari nikuachie hapa. Halafu uniambie asubuhi nije niwafuate saa ngapi.” Alishituka Pam, hakutegemea. Akamgeukia vizuri. “Amesema nini?!” “Ni usafiri kwa ajili yako na mtoto.” Pam akafikiria. “Mrudishie gari yake. Mwambie sina shida.” Bwana walishangaa pale, mpaka mletaji mwenyewe. “Haya, potea.” Akamuwekea msisitizo. Akaondoka.

Ujumbe Mzito Kwa Pam.

Alipoingia ndani akakuta amenunua vyakula vya humo ndani kibao! Akaoga wakati analala, akafungua hiyo bahasha yenye barua. Akakuta kadi ya benki, imeandikwa jina la mwanae. Akaanza kusoma.

‘Pam mke wangu!’ Hapo akafyonza kabisa. “Huyu ananitania huyu.” Akawaza moyoni akiwa amejawa hasira. ‘Najua nimekuumiza na huwezi kuniamini kwa chochote. Lakini Shema ni mtu wa mwisho kabisa nataka kumuumiza. Nimekosa sana, na nakusudia nisirudie kosa mpenzi. Katika jitihada za kukuleta kule nilipokuwa, nchini Marekani, ndio nikajikuta nimeangukia kwa Kisha. Mimba zote alizoshika, ni kama alinitega tu. Ulichokiona huko Insta, alikulenga WEWE moja kwa moja kwa sababu mwanzoni kabisa alinitongoza, tukiwa chuoni, nilimkataa na kumwambia nina mke nyumbani, anaitwa Pam.’

‘Nilipokwama jinsi ya kukuleta kule, ikabidi kumrudia yeye na kumuomba kama anaweza kunisaidia ndoa ya kumlipa ili mimi nipate uraia wa Marekani kupitia yeye, kisha nikutafutie na wewe Green card. Tuweze kuishi pamoja.’

‘Ikabidi kufunga ndoa yakueleweka na picha nzuri  kabisa ili kuaminisha Uhamiaji kuwa ilikuwa ndoa ya kweli. Hakika nilifilisika Pam. Alikuwa akinidai pesa mchana na usiku. Nilikuwa nikifanya kazi bila kupumzika. Kila nilipokuwa nikitaka kukata tamaa, nilikuwa nakukumbuka wewe mpenzi. Ilibidi nijitoe ili tuje kuwa pamoja.

Kwa hakika tulifanikiwa upande wa harusi hiyo ya maigizo. Na Mungu ni shahidi, hata pale ulipotuona kwenye harusi, nilikuwa nikimlipa Kisha.’

‘Najua unaweza usiniamini tena, lakini Pam, nilifika sehemu nilikwama kabisa. Njia zote za kukuleta kule tuwe pamoja zilifunga, akabakia Kisha TU. Na najua nilitakiwa kukwambia, ila tokea mwanzo kwa kuwa ilikuwa ni biashara, nikaona nisikutie wasiwasi wa wivu wa bure juu yake. Nikiamini baada ya muda, nitaachana naye, sisi tuendelee na yetu.’

‘Ili kuaminika, kwa sababu hii njia hata wao wamarekani wanajua wageni wengi hutumia kudanganya ili kujipatia uraia, ilibidi niwe makini, sisi tuanzie mbali. Sio kukurupuka tu kwenye ndoa na kugundulika kirahisi. Angalau kuonekane kulikuwa na mahusiano kabla ya hiyo ndoa. Kukusanya USHAHIDI wa kutosha ili wakija kutuita kwenye usahili tusionekane ni matapeli na kuingia matatizoni.”

“Ilibidi kumuhamishia Kisha pale nilipokuwa nikiishi ili tuonekane tuliishi pamoja, au kulikuwa na mahusiano ya kweli kabla ya hiyo ndoa. Tupeleke ushahidi wa kutumia address moja na bills zenye majina yetu sisi wote wawili hata tunapotokea kwenye mahojiano baada ya ndoa, tuonekane tuna HISTORIA ya muda mrefu, ya kweli, sio kudanganya. LAKINI Pam, hakika nilikoma, nitakuja kukusimulia, siku utakapo nifungulia moyo wako tena.’

‘Turudi kwenye swala la Kisha. Tukafanikiwa kwenye hatua ya kwanza. Mambo mengi yakaanza kuchukua picha yetu sisi kama wapenzi. Majina yetu wote mawili yalifanikiwa kuingia kwenye systems za nchini, tukionekana tunaishi pamoja kama wapenzi. Ndipo sasa nikaanza taratibu za kufunga ndoa, ili sasa ijulikane kama ni mke wangu, ndio niombe rasmi au nianze hatua ya kubadili uraia wangu.’

‘Nikiwa nimeshampanga Kisha, nimelipia ukumbi na garama zote za harusi ambazo ni kubwa sana, halafu nilibeba peke yangu. Ilibidi kumuomba Mike na Kamila na wao wahudhurie ili ionekane kama ni ndoa ya kweli kabisa. Yaani ionekane mpaka nimeleta ndugu kutoka nyumbani kuhudhuria harusi hiyo. Nilifanya taratibu za wazi kabisa, kuwaalika wao kwa kuwaandikia kabisa barua ya mwaliko wa harusi yetu. Yote hayo ni ili kuaminisha Uhamiaji kuwa si ndoa ya uongo.”

Pia nilishaalika jamaa niliokuwa nikiwafahamu wa kutokea kulekule nchini Marekani, kuhudhuria hiyo harusi, ilimradi tu kupata USHAHIDI wa kutosha wa picha kuwaridhisha wamarekani waone ni ndoa ya kweli. Na ukumbuke hapo na yeye nilikuwa nimemlipa pesa nyingi sana.’

Alinimaliza yule mwanamke, sina jinsi nikakwambia ukaelewa. Madai ya kila siku yasiyoisha. Nilifika sehemu sikuwa na pesa kabisa kwa ajili yake. Na akijua wewe upo na tupo kwenye mahusiano si ya uchumba, nilimwambia wewe ni mke uliye na baraka za marehemu baba yangu, maana alikuachia na wewe watoto wake.’ Hapo Pam akaanza kupoa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akakumbuka siku za mwisho za uhai wa mzee Mgini, akiwa hospitalini alimwambia mzigo wa familia yake anamuachia Mill ambaye ndio yeye. Akamsihi amsaidie Mill kusogeza ndugu zake sehemu watakayoweza kujitegemea. Hasira na uchungu vilimfanya asahau, akabakia kumtukania baba yake na ndugu zake. Akapoa kabisa. Akarudi kusoma.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

‘Usiku wa kuamkia asubuhi ya kufunga hiyo ndoa ya maigizo ambayo tayari ilishakuwa imenigharimu kiasi cha kunifilisi, Kisha akanibadilikia. Nilirudi nyumbani jioni hiyo tayari kwa ndoa ya kesho yake, maana sikuwa nikiishi hapo na yeye, japo ilikuwa ni kwangu. Aliniambia hatakwenda huko kwenye kufunga ndoa mpaka nilale naye. Yaani nifanye naye mapenzi. Na aliniambia nikikataa,  hataendelea na mchakato mzima na kunitisha kunishitaki kwenye vyombo vya usalama vya Marekani. Kwamba nilimlipa pesa ili anisaidie makaratasi. Hilo ni kosa kubwa sana kwa huku, Pam. Nisingebaki salama.’

‘Halafu ningerudije nyumbani, sina kitu! Na baba hayupo! Na hapo tulikuwa tumeshaalika watu kuhudhuria harusi hiyo kama nilivyokwambia awali. Mike na Kamila walikuwa wameshatua nchini, wapo hotelini tayari kwa harusi siku inayofuata. Nyumbani kwa kina Kisha nao walikuwa miongoni mwa hao wageni waalikwa, na wenyewe walishakuwa wakiitizamia siku hiyo kwa hamu, wakijua binti yao anaolewa ndoa ya kweli. Kwamba mabadiliko yeyote yale, ingebidi wajue ukweli na mimi kuangamia vibaya zaidi, na bado wageni wengine waalikwa waliokuwa tayari kwa shuguli nzima.”

“Sikuwa na jinsi mpenzi. Nilikuwa na hali mbaya, nikajikuta nimekwama, nisingekuwa na maelezo ya kueleweka ya kwa nini naahirisha harusi iliyokwisha nigarimu kwa kiasi hicho, halafu pengine kuja kuishia tena jela nikiwa sijapata kitu! Akiwa ananiita mimi ni mbinafsi, kwamba ananisaidia lakini mimi nakataa kumsaidia, huko kulala naye, ilinibidi kulala naye tu.”

‘Kesho yake akafanya vizuri sana huko mahakamani, ndoa ikafungwa, kisha kwenye sherehe hiyo ya harusi, mpaka kwenye hiyo honeymoon ya maigizo ambayo hakuomba tena penzi. Huko alitulia kabisa ila kutoa ushirikiano mzuri sana wa picha mpaka nikafanikiwa kukusanya ushahidi mzuri sana.’

‘Nikiwa na hukumu ya kukusaliti, baada tu ya hiyo fungate ya maigizo na kupata picha zangu, niliondoka kabisa pale tulipokuwa tukiishi naye, nikaenda kujifungia kwenye sehemu ninayofanya kazi. Kuishi kwa shida, nakula vyakula vya wagonjwa, nikimtunza yeye kwa gharama kubwa sana.’

‘Sikurudi kwake mpaka baada ya mwezi. Siku niliyozungumza na wewe kwa mara ya mwisho, nikakwambia ninarudi nyumbani. Nimechoka sana. Lakini nikioga na kupumzika kidogo, nitataka kusikia sauti yako. Lakini ndiyo siku iliyobadili maisha yangu mpaka leo.’

‘Nilifika nyumbani nikakuta Kisha akinisubiria na mama yake. Ukumbuke hata kwao ilikuwa ni siri. Walijua ni ndoa ya kweli. Aliyekuwa akijua ukweli ni Mike, Kamila pamoja na yeye mwenyewe Kisha.’

‘Kisha akiwa na mama yake, eti akaniambia ni mjamzito. Siku ile tulipolala pamoja kwamba ameshika mimba! Nilikuwa nahali mbaya Pam! Mungu anajua. Niliingiwa na hofu, sikuwa na lugha ya kukwambia ukaelewa. Nikaamua kujificha na JANGA langu.’

‘Ulichoona huko Istagram, sio wewe pekee uliamini. Hata wale wamarekani tulifanikiwa vizuri sana kuwaaminisha. Hatukupata shida kabisa siku tumeitwa kwenye usahili. Kwanza ukumbuke tayari nilikuwa na ushahidi wa wazi kabisa wa ndoa yetu, iliyopo mitandaoni na tayari Kisha alikuwa mjamzito.”

“Nilipewa Green card ya miaka miwili. Kwamba baada ya miaka miwili, kama bado tupo PAMOJA na hatujaachana, ndipo ningepewa ya miaka 10 ambapo sasa hapo, ndani ya muda huo ningeweza kubadili, kutoka kwenye Green Card na kuweza kupata uraia. Na kwa NJIA ya ndoa, hiyo niliyotumia mimi, ni rahisi sana. Nikimaanisha ni njia ya haraka endapo ukifanikiwa kuitumia vizuri na kufanikiwa kuwaaminisha. Ilimradi tu, wasijue kama mmedanganya.’

Sitakudanganya mpenzi. Kiuchumi nilifanikiwa sana. SANA. Nilijijenga sana kule. Na huku nyumbani pia namshukuru Mungu niliwekeza, na nikaweka vyanzo vya pesa vinavyonisaidia mpaka sasa. Lakini Pam, Mungu aliniadhibu kuliko hivyo unavyoniadhibu wewe. Nililipa kwa machozi.’

‘Nilijikuta nimekwama kwenye ndoa ya vitisho kila siku. Hapakuwa na amani hata siku moja. Chochote ulichokiona huko mtandaoni alikokuwa akipost Kisha ulikuwa umekusudiwa wewe mpenzi, na Uhamiaji wa Marekani. Kwa upande wako, alikufanyia makusudi ilimradi tu kuniumiza mimi na kuhakikisha sirudi tena kwako. Na Uhamiaji ili kuendelea kurekebisha mpaka kupata uraia.’

‘Ili nisikuchoshe, ndoa ile Mungu unayemshangaa namuombaje, ndiye aliyenisaidia mama. Ilibidi kumgeukia nikiwa nimekata tamaa, nikimuomba anitoe. Nikiwa na hofu ya kurudia kosa la baba, siwezi kimbia watoto wangu, nisijue kumbe huku yupo tayari Shema, watu wakinishauri niondoke kwa yule mwanamke, lakini nilishindwa kuondoka na kuachana naye tukiwa tayari na watoto wawili. Nilikwama kabisa. Ndipo nikajisalimisha kwa Mungu.’

‘Nilikuwa nikifunga ila sijui niombe nini. Maana nina watoto, na ndoa ya hila. Mungu mwenye rehema akaishia kunitoa kwenye ile ndoa kupitia JELA alikokuwa amenishitaki Kisha kwa kosa baya sana. Pengine nisingetoka mpaka leo.’ Pam akashituka sana.

‘Nilikaa huko rumande kwa muda mpaka mwanasheria alipoweza msoma Kisha na kugundua shida ni zile mali, na hataki hata watoto. Nilipo mkubalia kumpa mali zote na kuchukua watoto, ndipo akafuta kesi, na mimi kutoka kifungoni, nikiwa nimepoteza kila kitu huko nchini Marekani. Kasoro uwekezaji niliokuwa nikifanya kwa siri mtandaoni, asijue. Nilimuachia mali yote ndipo nikafanikiwa kupata talaka yangu, nakuondoka na watoto wangu.’

‘Ndivyo ilivyokuwa. Huna adhabu utakayonipa ambayo Kisha hajanipa Pam. Alikuwa akinitusi mpaka watoto wangu wanashindwa kuniheshimu kabisa.’ Pam akajisikia vibaya. ‘Hawa watoto hawawezi kuzungumza na mimi kama hivyo Shema anavyozungumza na mimi, kwa jinsi wanavyonidharau kwa aina ya maisha mabaya niliyokuwa nikiishi na Kisha, mama yao.

‘Kwa hiyo kama ni adhabu mpenzi, Mungu wako amekusaidia kukulipia. Nimelipa kwa machungu ambayo hutawahi hata kufikiria kama niliweza pitia. Sijawahi kulala usingizi ule tuliokuwa tukilala mimi na wewe kwa miaka yote 10, miezi miwili na siku 5 mpaka sasa.’

‘Sitakuficha Pam, nina watoto wenye tabia mbaya sana. SANA. Lakini Shema ni mwanangu. Nitamficha wapi? Kilichotokea juzi, najua ni kosa langu lakushindwa kulea, lakini niliwaacha kwa dakika chache nikiwa naandaa popcorn wale pale sebuleni alipokuwa Mia na Shema. Miles alikuwa chumbani. Kumbe huku nyuma Mia alienda kuchukua kitabu cha hesabu cha Miles, ili amuonyeshe Shema vitu wanavyofundishwa huko shuleni.’

‘Mia alichukua bila kumuomba Miles, akampa Shema. Sasa wakati Shema anasoma ndio Miles akamkuta, mimi nikiwa jikoni. Mia ni muongeaji kama mama yake na mwepesi sana kudanganya. Kwa haraka sana akadanganya kwamba yeye alimuona Shema ameingia chumbani kwa Miles na kuchukua kitabu chake. Miles akampokonya na kumpiga na game controller.’

‘Nakuapia kwa Mungu, Pam, nilichomwambia Shema nikiwa sijui stori nzima, ila kuambiwa na Miles ameiba kitabu chake, nilimwambia, ‘siku nyingine ni vizuri aombe’. Sasa wakati nakwenda kuchukua sanduku la huduma ya kwanza nimsaidie kabla sijampeleka hospitalini, huku nyuma ndio akaondoka.’

‘Nisamehe mpenzi kama kuna jinsi nilitakiwa kufanya, nikakosea. Nampenda Shema, na sina sababu ya kurudi kwako kama si kiapo tulichoapiana na wewe mpaka kifo. Nakutambua wewe kama mke wangu, na HAITABADILIKA. Shema ni damu yangu, siwezi mnyanyasa. Tafadhali nihurumie mpenzi. Na kama bado moyo wako haupo tayari na mimi, naelewa kabisa. Ila naomba Shema asome kama tulivyokubaliana.’

‘Naomba tuendelee kama tulivyokubaliana. Hiyo ni kadi, inayo pesa yote atakayohitajika shuleni. Ameshapata nafasi, tena wamekubali kumpokea bila mtihani. Ila wamesema watampa muda. Wakiona anapata shida, ndipo watazungumza na sisi jinsi ya kumsaidia ili aendelee vizuri. Usafiri upo tayari. Kwa upande wangu nimekamilisha. Utakapokuwa tayari kwenda benki, nenda na hiyo kadi na vitambulisho vyako, watakuongeza wewe kama msimamizi. Wanazo taarifa zako zote kasoro vitambulisho.’

‘Nakupenda Pam! Nakupenda sana mpenzi wangu. Sina sababu ya kurudi kwako kama si kukusudia kufanya bora kuliko baba yangu. Na nikikutambua wewe kama mke wangu. Naamini utanielewa, na kukubali kuweka tofauti zetu pembeni, ili tusimuathiri Shema. Pale watamuendeleza kipaji chake cha mpira, atakua bora sana. Ni hilo tu mama.’ Pam akahema kwa nguvu. Zilikuwa barua zilizoandikwa kwa mkono. Mbele na nyuma. Akabaki akifikiria na kupitiwa na usingizi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Lilipita juma jingine tena, kimya. Pam akaanza sasa kuhaha rohoni. Mill hamuoni wala yule kijana aliyetumwa hizo barua na vyakula. Akaanza kupooza rohoni. Mtoto ameachiwa, alichokitaka kimekua. Mill hajarudisha sura yake. Akapotea akiwa amehakikisha amejua kilichokuwa kikiendelea huko ugaibuni. Pam ubinadamu ukamrudia.

Andy na familia yake kwa Kina Ruhinda tena.

Ilikuwa mida ya saa 10 jioni wakati taksii ikiwaingiza Andy na familia yake, Msasani nyumbani kwa wazazi wake. Alishawapigia simu na kuuliza kama wapo nyumbani. Baba yake akamwambia wote wapo. Hakusema kama anakwenda na Mina. Walishafika hotelini, wakaacha mizigo yao yote ndipo alipoambiwa wote wanamsubiri yeye, ndipo wakatoka. Walishushwa karibu na mlango, Andy akawafungulia mlango, Mina na mwanae wakapita na kusimama pembeni kama wanao msubiria yeye ndio aingie ndani kwanza.

Akapita Andy, wakashangaa Mina na mwanae nao wanaingia. Pakazuka ukimya wa namna yake. Alikuwa Paulina na mume wake. Pius na wazazi wao. Raza hakuwepo.

“Njoo ukae hapa Mina.” Andy akavunja ukimya. “Shikamooni.” Mina akasalimia na kwenda kukaa na tumbo lake. “Marahaba Mina, mama. Unaendeleaje?” “Naendelea vizuri kabisa.” “Uliacha kutapika?” Mzee Ruhinda akaendeleza mazungumzo na Mina. “Kwa asilimia kubwa, baba. Sasa hivi ni mara chache sana. Si ndio Andy?” Mina akamrushia swali Andy, akajisikia vizuri.

“Mpaka ale kitu ambacho hakipendi. Au kupikwe samaki.” Kila mtu akajua wamerudi kuishi pamoja. “Basi ndio vitu vya kuepuka hivyo. Mwenye hamu na samaki akamlie hotelini.” Akaongeza mzee Ruhinda, Mina akacheka taratibu. Andy alipita na kwenda kumfungia Ayan chumbani na chupa ya maziwa. Akamwashia tv na kumwambia asitoke mpaka aende akamchukue. Ayan akakubali.

Andy akatoka. Akakaa pembeni ya Mina. “Nashukuru kwa kukubali kufika hapa.” Andy akaanza. “Baba na mama, Pius ALIMLEVYA mke wangu, akambaka. Na ndiye aliyempa mimba.” “Mina sio mke wako, Andy. Usisahau hilo.” Pius akadakia akiwa AMETULIA kabisa. Watu wote wakawa wameduaa. Wakashangaa sana.

“Pius!” Mama yake akashituka na mshangao kama aanguke. “Hapana mama. Anaongea hapa yeye kama nani? Kilichotokea ni kati yangu mimi na Mina. Hayamuhusu.” “Lakini kipindi hicho alikuwa ni mke wa mwenzio, Pius!” Mzee Ruhinda akaongeza kwa kuumia sana, asiamini kama Pius kijana anayemuamini SANA, anaweza fanya hivyo. 

“Na mimi nililewa baba. Nikajikuta nimefanya hivyo. Nikashindwa kusema kwa haraka sababu ya mshituko. Na ndio maana mimi sijamtelekeza Mina. Muulizeni. Andy alimfukuza, mimi nikaenda kumchukua na kumpeleka hospitalini akatibiwa. Namtunza Mina mpaka leo. Na nilikuwa natafuta wakati mwafaka wa kukiri kwake na kumuomba msamaha, ndipo nije kwenu niwaambie nyinyi. Nilifanya kosa, na nikakubali kuwajibika. Mimi sijamtupa Mina!” “Si nilikwambia Andy?” Mina akaongea kwa kulalamika kinyonge na tumbo lake.

Andy akasimama na kumpiga ngumi kaka yake pale alipokuwa amekaa. “Ulijua wazi Mina hanywi pombe, kwa nini ulienda kununua champagne yenye kileo na kumnywesha mpenzi wangu kama hukukusudia KUMBAKA?” Andy akamshindilia ngumi nyingine kaka yake. Pius akasimama, zikaanza kupigwa. Ndugu hao, kaka wasomi na nyadhifa za juu kwenye jamii, wakaanza kupigana hapo kama mabondia mbele ya wazazi wao, kila mtu akishangaa.

Walipoona wanazidi kuharibu pale na kuumizana, ikabidi Devi asimame na baba yake asimame wasaidiane kuwaamulia, maana walikuwa wakirushiana ngumi za haswa. Walitenganishwa lakini wakarudiana tena. Mina akasimama. “Sasa kama mnaendelea kupigana, mimi naenda kumchukua mtoto wangu, naondoka. Nyinyi endeleeni kupigana mpaka muuane au kumuua mama na baba kwa pressure.” Wakaachina.

“Subiri kwanza Mina.” “Naomba usiongee na mimi Pius. Umenikosea sana. Umenitendea ubaya, ukaacha ninadhalilika! Umesababisha nikaachika.” “Come on Mina! Ndoa yenyewe kila mtu alijua ilishaisha.” Andy akamrushia ngumi, Pius akaikwepa huku akicheka.

“Nakushangaa hasira za nini Andy! Mina si mkeo na mapenzi yote yalishaisha kabisa tokea zamani sana, kila mtu aliliona hilo. Ulimtelekeza hapa mjini, na hukuwa ukijali! Mimi ndio nilikuwa nikimtunza yeye na mtoto wako wakati ulikuwa hapahapa nchini!” “Sijawahi kuacha kumpenda Mina. Na wewe ulitumia udhaifu wangu kuzaa na mke wangu. Hukuwa umelewa Pius. Ulifanya makusudi. Sababu ya tamaa zako kwa Mina. Ulishindwaje kujizuia Pius!?” Andy akauliza kwa kuumia lakini Pius hakumjibu. Akamgeukia Mina.

“Mina, nilikusudia kabla mtoto hajazaliwa tulizungumzie hilo ila ukaniblock kila mahali, nikashindwa kukupata kwa simu. Nilikufuata mpaka Iringa kujaribu kufuatilia sehemu ulizokuwa ukiniambia ulipata sehemu ya kuishi pia sikufanikiwa. Hangaika yote hiyo ni kukiri kosa na kuomba msamaha.” “Sio kwangu kwanza Pius. Anza kwa Andy, akikusamehe Andy...” “Mina!? Huyu Andy si alikutelekeza wewe aka..” “Kilichokuwa kikiendelea kati yangu na Andy, hakikuwa kikikuhusu Pius. Acha kuhalalisha kosa lako kwa kumdhalilisha hapa Andy. Unazidi kuharibu.” Pakawa kama watu wamepigwa na butwaa tena.

“Kaa chini Pius, maana naona wewe unataka kuharibu na usiwahi hata kuwa na mahusiano na huyu mtoto.” “No way Mina! Mimi namtunza mtoto wangu na wewe kwa ukaribu sana. Nimekutunza Mina, hata kabla hujabeba mtoto wangu.” “Mimi mpaka nakuhisi vibaya Pius! Nahisi ule msaada wako ilikuwa ni njia ya kunivutia. Ulipoona sijaelekea kwenye mapenzi bado nakuheshimu kama shemeji ndipo ukanibaka.” “Ninachotaka usije kuwahi kusahau Mina, ni kuwa, mimi nakupenda sana na ninakujali.” Andy akaruka kutaka kumfikia kaka yake, Pius naye akakimbia upande wa pili.

“Pius, umechanganyikiwa wewe!?” Paulina akashangaa sana. “Wala sijachanganyikiwa. Mlitaka nidanganye ndipo mjisikie vizuri? Naongea ukweli wangu. Nampenda sana Mina.” “Baba, unamsikia lakini Pius!?” Andy akamsemelea kana kwamba mzee Ruhinda hakusikia. “Umepatwa na nini Pius!?” Baba yake akamuuliza kwa kumshangaa sana.

 “Juu ya kumpenda Mina au kumpa mimba?” Akauliza Pius bila wasiwasi, wote wakabaki wameshangaa. “Mbona lakini mnashangaa kama nimefanya jambo la ajabu sana!? Sasa hivi Mina si mke wa Andy, kilicho cha ajabu ni kipi? Wote mnanijua mimi sio muhuni. Miaka yote nimekuwa na Raza tu, hamshangai kwa nini iwe kwa Mina? Ni kwa kuwa nampenda.” Pius akaongea bila wasiwasi.

“Ujue Pius una wazimu wewe!?” Paulina akamshangaa kaka yake. “Wazimu ni mimi nimependa au wewe unayepita kwenye majumba ya watu na kuharibu? Aliyesaidia kuvunja ndoa ya Andy na Mina ni nani kama sio wewe? Unaingilia mambo ya watu hata huyajui, lakini unataka wewe ndio uwe kimbelembele!” Pius akaendelea kwa ukali kabisa.

“Mina alikuja siku ile akawa muwazi kabisa. Hana hata taarifa kama ni mjamzito! Mtu mwenye akili timamu si angetulia, na kumsaidia? Umempiga na kumvunjia ndoa yake. Sasa hivi ndio unaniita mimi wazimu! Mnafiki mkubwa wewe Paulina. Mbaya kuliko shetani. Umejua Andy hana uwezo wa kuwa mume, ndipo hapo na wewe ukaweza kuingia na kuharibu.” “Sikuvunja ndoa ya Andy mimi.” Paulina akaruka.

“Paulina wewe!” Andy akashangaa sana. “Mimi nilikushauri chakufanya, sikukulazimisha umuache mkeo, Andy! Yalikushinda wewe mwenyewe, tokea mwanzo.” Pius akaanza kucheka. “Mmeona sasa? Mnarudi kulekule mliko nishangaa mimi. Mimi mkweli na sikutaka kuzunguka. Wewe Andy ndoa ilishakushinda muda tu, sababu ya kushindwa kubalance mambo. Ukalemea upande mmoja kama ambaye hukuwa na mke wala watoto! Paulina alikusaidia tu kuhitimisha kihalali. Lakini ubaya wa Paulina, kila mtu anaujua. Muulize mama yake huyo hapo.” “Msiniingize kwenye mambo yenu.” Mama Ruhinda akakataa kabisa, tena kwa haraka bado akionekana na mshituko.

“Unakataa tu mama. Lakini wote tunamjua Paulina ni mbeya na mchonganishi. Alianza kwenye ndoa yangu mimi. Akawa anamsema Raza vibaya, nikamkanya na vibao vya usoni. Akaja kunisemea hapa kwa baba akiwa analia. Na wewe ulikuwepo. Najua mnakumbuka. Akavumilia akashindwa, akahamia kwa Raza kunishitakia mimi. Raza alipoona unataka kumtoa kwenye pesa zangu, maana mimi nilimwambia Raza, akiendelea kukusikiliza wewe Paulina, anaondoka pale kwangu bila kitu. Raza akaanza kukukwepa. Ndipo ukajirudi. Bisha kama ni uongo?” “Uongo.” Pius akamkazia macho.

“Sasa kwa kuwa najua huwezi kunyamaza, hata hili utamwambia Raza. Nakutuma nenda kamwambie kama ilivyo. Ila ONGEZA hivi, chochote kitakachompata Mina na mtoto wangu, ajue ndicho kitakachoipata ndoa yake. Aombe na akaloge kwa waganga zake, wote hawa, Mina na mwanangu waishi ili na yeye ndoa yake iishi.” Pius aliongea bila wasiwasi na kushangaza kila mtu mpaka hata Mina mwenyewe kwamba haogopi hata kwa mkewe!

Akamsogelea Mina. “Nataka mahusiano yangu na wewe yasiharibike, Mina. Na nipo tayari kumlea mtoto wangu. Na ninataka anitambue mimi kama baba yake. Niambie unataka nifanye nini.” “Cha kwanza Pius na Andy kama mnataka kuzungumza kaeni chini wote mtulie. Kama hamtaki mimi naondoka zangu na wanangu. Mnakuwa kama watoto bwana!” Wote wakakaa.

“Weka msisitizo kwa Andy. Yeye ndio anataka fujo.” Pius aliongea huku akicheka tu. “Tafadhali acha dhihaka kwa mwenzio Pius!” “Kwani mimi nimefanya nini baba!?” “Mbona halipo lakuchekesha hapa?!” Mzee Ruhinda akauliza kwa ukali, Pius akanyamaza. “Hiyo ni dharau ya hali ya juu Pius! Umenifedhehesha sana mimi kama baba yako na mtu niliyekuamini na Mina.” “Naomba baba usijilaumu. Haya ni makosa yangu mimi mwenyewe.”  “Nitaacha vipi kujilaumu wakati na mimi nilihusika kuwa nikikutuma kwenda kumsaidia Mina!” “Haya ni makosa yangu baba. Ni mimi.” Hapo Pius akatulia, kidogo akaonekana anazingatia. Pakatulia kila mtu akiwaza lake kama walio kwenye mshituko mkali sana. 

“Naomba tumsikilize na Mina. Karibu mama.” Mzee Ruhinda akavunja ukimya. “Asante baba. Mimi nilitaka kumwambia Pius, ajue sijamshitaki polisi ni kwa sababu ya wema wake kwangu. Japo hata huo wema naanza kuutilia mashaka, lakini...” “Naomba kosa moja lisikufanye...” “Tafadhali nyamaza Pius. Kwa hakika umeharibu na kuniumiza sana.” “Sawa baba.” Pius akanyamaza.

“Endelea mama.” Mzee Ruhinda akataka Mina aendelee. “Andy ameniacha sababu yake! Hata kama kulikuwa na mapungufu kwa Andy, lakini bado alikuwa mume wangu na nilikuwa nampenda Andy wangu. Alishakiri makosa yake na kuamua tuanze upya.” Mina akajifuta machozi.

“Na niwaambie kweli tu, mwezi mmoja kabla ya kurudi kwa Andy, alishakuwa tayari kuacha kila kitu, ili aje awe na mimi na Ayan. Alishakubali kurudi atafute kazi ingine ili awe na mimi. Ndio nikamtia moyo, nikamwambia nimesamehe yote, tukakubaliana tuanze upya. Lakini Pius umenipokonya ndoa, wakati wewe bado upo kwenye ndoa yako!” Mina akaendelea taratibu tu akilia.

Amemfedhehesha Andy vibaya sana. Kila mtu aliyejua mimi nimeshika mimba nje ya ndoa atakuwa amemuona Andy ni hovyo. Ameoa mke wa ajabu!” “Unakwenda mbali Mina.” “Sio mbali Pius. Hata hapa pia, umemsema vibaya Andy wakati ni baba wa mtoto wangu. Sitakusamehe kwa hilo. Ukitaka amani na mimi na uwe na mahusiano na huyu mtoto, muombe msamaha Andy, tena wakumaanisha.” Pakazuka ukimya, Pius akainama.

“Cha pili Pius, umesababisha nilifukuzwa nyumbani. Mama anajua mimi ni mtoto mbaya, nimemsaliti Andy, akanifukuza. Sina mawasiliano na mama pamoja na Ron. Sasa, Andy akishakusamehe, mkaweka mambo sawa na Andy, nataka uende na kwa mama na Ron. Uwaeleze ukweli usafishe jina langu kwa mama. Wengine sijali. Ila mama yangu, Ron na Andy. Ukishapatana na hao, ndipo unitafute sasa tuzungumze maswala ya mtoto. Mimi nimemaliza.” Pakazuka ukimya lakini Mina alimfurahisha sana Andy, hapakuwa na mfano. Alimrejeshea heshima aliyokuwa amepoteza hapo kwao.

“Umesikia Pius?” “Nafikiria baba.” Pius akajibu. “Basi twende zetu Andy. Ukimaliza kufikiria utamtafuta Andy.” Mina akasimama. “Subiri kwanza Mina.” Mina akamwangalia. “Nitajuaje kama nikienda hawatanifunga?” “Hutajua mpaka utakapofika pale. Mimi sina hayo majibu Pius.” Pius akabaki akimwangalia.

“Huna haraka. Na sikulazimishi kwa lolote. Siku utakayokuwa tayari kufanya hayo, fanya. Ukiona ni ujinga, pia ni sawa. Endelea kunyamaza kama ulivyofanya mpaka tukakufuata hapa na kutukejeli mimi na Andy.” “Sijakukejeli Mina!”

“Usinifanye mimi mtoto mdogo Pius. Huwezi kumcheka Andy mbele yangu, tena kwa kitendo cha kinyama ulichonifanyia mimi nikiwa mkewe, halafu utegemee mimi niwe sawa! Kivipi? Kwa lipi lakunifanya umcheke Andy, halafu kuwe sawa! Wewe ni mbaya na unadharau mbaya sana. Labda ni kwa vile ulivyoyajua mahusiano yetu kwa undani kati yangu mimi na Andy, ndio ukaona sisi ni watu wakutudharau tu. Au labda ni mimi ndiye unanidharau.” “Sikudharau Mina!” Pius akajitetea tena kwa kumbembeleza Mina. Akionyesha wazi hataki kukosana hata kidogo na Mina, lakini si mtu mwingine.

“Ni dharau na uonevu wa hali ya juu Pius. Mwenzio Andy kabla yakunigusa, alikwenda nyumbani. Akazungumza na mama pamoja na Ron. Akafanya taratibu zote, ndipo akanioa. Andy aliniheshimu, hakunigusa mpaka ndoa. Pius wewe umenidharau mimi na mama yangu. Sasa sijui kwa kuwa umetuona hatuna hali kama zenu! Sijui!” “Usiseme hivyo Mina! Nilikosea.” Mina akakunja uso wa mshangao.

“Tuwe wawazi tu. Hivi mimi ningekuwa ni kama Paulina huyu dada yako. Mzee Ruhinda na mama Ruhinda ni wazazi wangu, mimi. Nikalelewa kwa hali kama hii ya Paulina. Nina wazazi wote wenye uwezo na wanafahamika kwa nyadhifa za juu hapa nchini, kama kina Ruhinda. Ungenifanyia ulichonifanyia kweli Pius?” Kimya. Kila mtu akabaki kimya.

“Twende Andy.” Andy akasimama na kwenda kumchukua mtoto wake. “Lakini katika yote Mina, naomba uamini nakupenda. Najua lilifanyika kosa tokea mwanzo sababu ya pombe na kwa kuwa nakupenda SANA. Lakini sio dharau kwako wala kwa mama yako. Na mimi si muhuni. Kila mtu ni shahidi yangu. Wananijua.” “Pius wewe mwanangu umerukwa na akili!” “Nampenda Mina, mama. Si heri nimwambie tu ukweli, ajue.” Kila mtu akabaki amemkodolea macho Pius kama wameona muujiza wa fimbo kugeuka nyoka.

Mina akatoka bila hata kujibu. Andy akarudi na mtoto wake, akakuta Mina alishaondoka pale. Wakaondoka. Lakini Andy alijisikia vizuri sana kwa heshima aliyopewa na Mina. Ni kama alimtetea na kutaka Pius asimpuuze hata kidogo.

~~~~~~~~~~~~~~

Mahusino yapi yatapona, yepi yataharibika?

Na mahusiano hayo yatakuje na watoto wa wanaume wawili, tena NDUGU waliokwisha umizana? Halafu wote WANAMPENDA mwanamke mmoja?

Pius anamtaka mwanae na Mina.

Andy anamtaka mkewe.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment