![]() |
Kwa Mina.
Akatoka hapo na kwenda chumbani kwa Mina. Akamkuta
amelala. “Mina!” Mina akaamka. “Vipi?” “Nakuomba ufikirie na ukumbuke.” “Juu ya
nini!?” Mina akakaa kwa shida kidogo. “Uliniambia hukuwahi kwenda
nyumbani kwa rafiki zako wala kuwakaribisha pale nyumbani hata siku moja. Una
uhakika? Naomba ufikirie kwanza kabla hujajibu.” “Katika hilo sihitaji kukumbuka
Andy. Nina uhakika.”
“Okay. Je, kukutana nao sehemu wakakupa kinywaji
chochote, hata maji?” Mina akafikiria. “Labda kula nao palepale chuoni. Na
tunakuwa wengi Andy! Sio kwamba nakuwa peke yangu. Kikundi.” “Kwa hiyo hukuwa
karibu na kijana yeyote yule?” Mina akafikiria.
“Kama wawili hivi, lakini tulikuwa nao palepale chuoni
hata kukutana nao kwenye kundi la kujisomea nilikuja kushindwa hata kabla wewe
hujaondoka nchini. Nilikuwa nikikosa muda Andy! Mara nyingi walikuwa wao
wanakutana siku za weekend na
usiku mara mbili kwa juma.” “Na hukuwahi kufika huko?” “Hapana. Nilitaka,
lakini nilishindwa.” Mina akajibu kwa uhakika.
“Kwa hiyo unao uhakika hapakuwahi kuwa na
mazingira mkawa nao hao rafiki wawili?” “Nina uhakika Andy.” Andy akatulia
kidogo.
“Kwani vipi?” “Wewe sio mlevi Mina. Hunywi
kabisa. Haiitaji mtu kutumia nguvu nyingi kukulevya na kukufanyia
mambo mabaya na akakuacha ukiwa umelewa. Na hata pombe ikikuishia usikumbuke.”
Mina akaanza kufikiria. “Sijawahi..” Gafla akamuona amesita. Halafu kama
aliyeshituka SANA, kisha akajibaraguza.
“Sijawahi kudhania hivyo.” Andy akajua amebadilisha
alichotaka kusema. “Sasa hivi, hapo, umenidanganya.” “Bee!” Mina
akajidai kama hajaelewa.
“Mina?” “Juu ya nini?” “Hicho ulichokumbuka na kutaka
kunificha sasa hivi. Nani aliwahi kukupa pombe hata kwa kuonja?”
“Mimi?” Mina akauliza na kusimama. “Nakwenda chooni.” Akaelekea chooni. Andy
akamuona kama ameingiwa na hofu kubwa. Mina akawa kama
amefunguliwa macho kwa haraka sana.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati analala alimuomba Mungu amfunulie ajue
ni kwa jinsi gani ameshika hiyo mimba. Andy amemsaidia kumvuta
kumbukumbu. Akakumbuka ni Pius pekee ndiye kwa mara ya kwanza alikunywa akiwa naye na kulewa sana. Kesho yake hakukumbuka
na hakumwambia kilichotokea.
Mina akaanza kulia sana huku amefunga mdomo
ametoa macho asijue alikuwa akila na kunywa na baba mtoto
wake! Akakumbuka jinsi Pius
alivyokuwa akimfuatilia kwa karibu hata kutaka kujua jinsia ya
mtoto! Mahela aliyokuwa akimtumia! Upendo wa kumjali na kutaka
kujua mtoto anaendeleaje kila wakati! Mina akaumia sana. Anamwambia nini
Andy? KIPI na KUACHA kipi? Ameshalala na Pius! Akaona heri asimtaje.
Akaosha uso, akatoka akiwa ametulia asijue hata macho yanaonekana.
Mambo Hadharani.
Alimkuta Andy ametulia kimya ameinama. Akanyanyua uso
alipomsogelea. “Ni lini na wapi ulipokunywa pombe na Pius?”
Mina alishituka akakaribia kukaa chini. Kimya. “Mlikuwa na mahusiano
naye?” “Ya kama shemeji mpaka uliponifukuza kwako, na mama naye akanifukuza
ndipo nikaenda hotelini, akanipigia kunijulia hali. Akanikuta natapika sana,
ndipo akanipeleka hospitalini. Akakaa na mimi mpaka dripu niliyowekewa ikaisha,
akanirudisha hotelini. Akanihudumia, nikapata nafuu ndipo nikamuaga kuwa
lazima nikaanze maisha yakujitegemea kwa ajili yangu na mtoto.” Mina akaenda
kukaa pembeni ya Andy pale pale kitandani.
“Tuliagana lakini akiwa ameniambia muda na wakati
wowote hata nikitaka mtu wa kuzungumza naye nimpigie. Au ushauri.
Nikitaka kitu, nimuombe yeye. Hapo alishakuwa na akaunti yangu ya
benki.” “Aliipata wakati gani?” “Wakati bado mimi ni mke wako. Alisema atakuwa
akiniwekea hapo pesa za matumizi yangu na Ayan ikitokea kama wewe umetingwa,
hujatutumia pesa.”
“Maana kuna siku alinipigia simu kutaka kunijulia
hali, wewe ukiwa huku. Akaniuliza mbona nimekuwa kimya. Nikamwambia sina pesa
ya simu kwa wakati huo, nakusubiria wewe, unitumie pesa za matumizi ya week, niliishiwa mapema, nilinunua vitu vya mtoto ambavyo
havikuwa kwenye bajeti ya pesa uliyokuwa umenitumia. Halafu kuna wakati
mwingine alitaka anisaidie kukaa na mtoto, nikafanye shopping ya nyumbani. Nikamwambia asije kesho yake maana bado
hujatuma pesa, sina hela. Ndipo akaniomba namba ya akaunti
kuwa na yeye atakuwa akiweka pesa humo ili nisiwe napata shida.”
“Kwa hiyo akawa akikuwekea pesa hata kipindi tupo wote?!”
“Kwa kweli katika hilo sitadanganya Andy. Pius alikuwa hataki anisikie
napata shida wakati wowote ule. Alijitoa kwangu kwa namna ya ajabu
sana. Na alikuwa akiweka pesa nzuri sana. Mambo mengi ya pale nyumbani kwa mama
niliyafanya kwa pesa aliyokuwa akiniwekea Pius. Sikuwahi
kuishiwa wala kukopa tena, kuanzia wakati ule mpaka uliponifukuza kwako.
Kwa asilimia 100, nilikuwa nikitunzwa na Pius hata kule uliponikuta
nikiishi, Iringa.” Andy akainama. Akatulia. Mina naye akatulia.
“Na ni lini alikupa pombe?” Andy akauliza akionyesha
wazi kuishiwa nguvu. Macho yalishakuwa mekundu haswa. “Unakumbuka tulikuwa hatuwasiliani
kabisa wakati ulipoenda Uswiz?” Andy akabaki kimya akimtizama. “Kipindi kile
Pius ndio akawa karibu sana na sisi. Zaidi. Akinisaidia mambo yote
ya pale nyumbani na mtoto. Sasa nilipopata matokeo yangu kuwa nimefaulu, mtu wa
kwanza kumfikiria ilikuwa wewe. Nikijiambia wewe ndio ulikuwa mtu sahihi
wakufurahia mafanikio yangu. Ndio maana nikakupigia kukwambia.” Mina
akaendelea.
“Nilipomaliza kuzungumza na wewe, bila maelewano sikukwambia
hata kama nilitegua mguu. Hata hivyo nilijua usingejali, Andy. Maana
hata ulipokuwa upo huku Tanzania nilikuwa nikiumwa huna hata habari!
Hujali. Anyway, nikawa nimekaa tu
kwenye kochi, mguu unauma, siwezi hata kutembea. Ikabidi
kumwambia yeye kuwa nina maumivu ya mguu, siwezi hata kukanyaga. Hapo
hapo akaja na kunipeleka hospitalini. Nikawa nimemwambia pia kuwa
nimefaulu akasema lazima tusherehekee.” Mina akatulia kidogo.
“Hospitalini wakanifanyia vipimo, mguu ukawa
haujavunjika. Ni kuteguka tu. Ukawa pia umeshajaa, umevimba na unauma sana.
Wakaniandikia dawa kali za maumivu pia. Pius akanichukua tena mimi na Ayan, tukaenda kununua dawa na chakula. Akasema lazima
tusherehekee. Akanunua na champagne na wine.” Mina akajifuta machozi,
tayari Andy akawa yupo kwenye mahesabu makali.
Muda huo mpaka Mina kugundulika mjamzito. “Tulifika nyumbani. Akanisaidia kumuogesha Ayan baada ya
kumlisha, akamuweka kitandani wakati na mimi nilishakula na kuoga, nikajilaza
kitandani. Alipomalizana na mtoto akagonga kule chumbani, akaniambia nisilale
lazima tusherehekee. Nikamwambia nilidhani itakuwa wakati mwingine kwa
kuwa amechoka. Kunipeleka hospitalini, kukaa na mimi mpaka matibabu, kununua
dawa, kuturudisha nyumbani na kuanza kumuhudumia Ayan, nikajua atakuwa
amechoka.” Mina akajifuta tena machozi kama ambaye na yeye alishamjua
moja kwa moja.
“Basi, akaniambia hiyo siku ndio ya
habari njema, lazima tusherehekee. Champagne ikawa kali. Akasema nisiogope.
Ninywe tu. Nakumbuka akaniambia tugonge, halafu ninywe yote bila kufikiria ule
uchungu. Nikafanya hivyo. Nikaona nimeweza, halafu sio chungu kama
nilivyodhania. Akaniambia sasa tunywe ile wine. Ni tamu. Na kweli ilikuwa tamu kama
juisi. Kumbukumbu nafikiri zinaniishia kwenye glasi ya tatu. Vile alivyokuwa
akiniambia ninywe kama maji, nisisikilizie.”
“Kesho yake nakumbuka niliamka kichwa
kizito sana. Lakini msafi vile vile kama nilivyotoka bafuni jana yake na mguu
ule ulioteguka ukawa upo vizuri tu, juu ya mto. Akaja asubuhi na mapema.
Nikamuuliza jana kulitokea nini, mbona sikumbuki chochote,
akacheka. Nikahisi niliharibu kwa kuwa sikuwahi kunywa pombe, ile
ilikuwa mara yangu ya kwanza. Nikaingiwa hofu, nikajiambia labda
nililewa sana, nikajisahau. Akaniambia nisiwe na wasiwasi, uzuri
nilikuwa na yeye. Hakunipa maelezo marefu na mimi nikawa nimeingiwa hofu ya
pengine nilitamka jambo baya au nilimsimulia mambo mabaya au hata kufanya jambo
baya! Nikaona iishe hivyo tu, nimuulize zaidi.” Mina akajifuta tena machozi.
“Ndio akawa amempigia simu mama kumwambia nimeumia
mguu, nahitaji msaada. Ndio mama akaniletea Mamu. Lakini sasa kuanzia hapo wote
wakawa kama wamepeana zamu kuja pale kuniangalia hakuwa tena peke yake.
Wakati mwingine akija akawa anamkuta baba na wengineo. Na wewe ukawa kama
umetengeneza. Unajali. Ukarudisha simu za mara kwa mara, tena
ukitaka kuniona! Ikawa sasa nakosa muda wakumtafuta tena.”
“Hata alikuwa akinipigia nakuwa labda
nipo na wewe kwenye simu. Ndipo nikagundulika na ujauzito. Mkanifukuza,
yeye akarudi kwenye picha tena, ndio akaanza kunitunza sasa kwa asilimia
zote, mpaka leo.” Pakazuka ukimya. Wote
wakawa wamemjua baba wa mtoto.
Andy akabaki ameinama. Mina analia. Akajipandisha kwenye kitanda, akajilaza.
Akamuona Andy anatoa simu. Ulikuwa usiku sana.
Kwa wazazi.
Akampigia simu baba yake. “Kwema!?
Mbona usiku sana!?” “Samahani baba. Kesho utakuwepo nyumbani wewe na mama?”
Andy akauliza. “Hata kama nikutoka, ni hapahapa mjini.
Ninauhakika hata mama yako hatasafiri. Ulitaka nini?” “Nina mazungumzo na wewe,
mama, Paulina na Pius.” “Saa ngapi?” Baba yake akauliza. “Nategemea kuwa hapo mida ya jioni.” “Basi nitawauliza
wenzako. Ila hata kama wao watashindwa, mimi na mama yako tutakuwepo. Karibu
sana.” “Ni muhimu wawepo baba.” “Basi
nitazungumza nao.” Andy akakata.
~~~~~~~~~~~~~~
“Unataka
kufanya nini Andy?!” “Lazima kuzungumza na Pius mbele ya wazazi wajue alichokifanya.”
Mina akanyamaza. “Au wewe ulikuwa ukifikiria nini?” “Hata sioni maana Andy! Kwa sasa haileti maana tena. Heri
ningekuwa mkeo! Sasa hivi unaongea juu yangu, wewe kama nani?
Halafu ni ndugu yako. Huwezi kumshitaki popote. Hata mimi sitamshitaki
popote. Namuacha tu.” Andy hakuridhika.
“Lakini lazima ajue, ninajua.” “Halafu
kitatokea nini Andy? Itasaidia nini? Pius hakuwahi kuniacha hata
mara moja! Ni ukiri tu wa alilonifanyia. Lakini kila nikimfikiria
sasa hivi, ni kama mtu aliyekuwa akiniandaa kuja kumsamehe au
akiniambia anawajibika na alichokifanya kwa maneno na vitendo.
Wakati watu wote mmenitupa, yeye
alibaki na mimi.”
“Ulinifukuza nyumbani ukanirudisha kwa mama na
kuniacha nikiwa mgonjwa, bila hata shilingi! Mama
akijua umeniacha bila hata pesa, naye akanitukana sana na kunifukuza
bila hata kujali wapi nakwenda. Pius alinitafuta na kuhakikisha natibiwa.
Silali nje, na silali na njaa.” Mina akaendelea.
“Wewe na mama yangu mzazi hamkujua
nilipo wala ninaendeleaje, lakini sio Pius. Yule mtu amehangaika na mimi
mpaka natamani kama ingekuwa vinginevyo sio kufanya mapenzi na mimi bila
ufahamu wangu, tena nikiwa mke wako. Halafu pia asiniambie,
aache naaibika! Natamani ingekuwa ni mtu mwingine sio Pius. Sisemi kuwa wema
wake unazidi ubaya alionitendea, lakini hakunikimbia kama nyinyi.
Na angeweza Andy. Nani angejua?”
Andy alipandwa na hasira, akashindwa hata kuzungumza.
“Nipende, nisipende, na yeye atakuwa
kama wewe. Tumezaa naye.” “Naomba usiseme hivyo Mina! Mimi nilikuwa mume
wako.” “Wewe nishahidi Andy, ulifika sehemu ukawa mume tuliyekuwa tumeandikishana
tu kanisani, yeye ndio ananitunza. Na nafikiri ndio maana haikukusumbua
kunifukuza kwako mikono mitupu na usijali nilipo wala ninaendeleaje,
kwa kule ulipokuwa umefika na mimi Andy. Mapenzi yaliisha kabisa,
nikabaki kama mfanyakazi wako tu, nikikutumikia.”
“Ukinituma huku na kule. Mara kwenda kuwalipa mafundi,
kununua hiki na kufanya kile. Na ukanifukuza bila hata marupurupu wakati
nilikutumikia bila kuiba! Haikukusumbua Andy. Lakini sio Pius.”
“Pius alihakikisha siishiwi nilipokuwa mkeo
na pia uliponiacha. Alikuwa ananiwekea pesa benki mara kwa mara. Hivi
ninavyokwambia Andy, nina mamilioni ya pesa, amekuwa akinipa Pius. Sina uhitaji
na chochote jinsi anavyoweka pesa. Na ni vile nimeamua mimi nisimtafute tena,
lakini Pius alikuwa hawezi kulala bila hata kujua nimeshindaje au
asubuhi kujua kama niliamka salama. Jana nimeangalia salio benki,
japokuwa hatuwasiliani, lakini Pius ameweka tena pesa. Sasa, sasa hivi naelewa
ni kwa nini anahangaika hivyo.”
“Wewe nishahidi Andy. Watu WANAWAPA mimba
wanawake, wanakimbia nakuja kudai watoto baadaye sana. Au hata kukataa
watoto wao! Alishindwa vipi Pius? Huyu dada hapa, Judy, amekimbiwa
na mume aliyezaa naye watoto watatu, lakini Pius amebaki kulea mimba ambayo ni yeye
peke yake ndiye anayejua ni YAKE, wakati hata mimi mwenyewe sijui!” Andy
akasimama na kuondoka pale kwa hasira.
~~~~~~~~~~~~~~
Asubuhi Mina akaamshwa na sinia la chakula. Akakaa.
“Andy!” “Amka ule. Nataka twende Dar.” “Kufanya nini?” Mina akauliza. “Lazima
tuwekane sawa Mina. Pius ametumia udhaifu wangu kuvunja ndoa
yangu. Lazima wazazi wajue.” “Mimi sitaki kesi Andy!” “Kwa hiyo wewe
unataka yaishe hivi hivi!? Na yanaishaje?”
“Niliamua muda mrefu sana. Tokea mama amenifukuza
na yeye nyumbani kwake, kuwa hii mimba nitazaa na mtoto nitalea.
Japo sikuwa namjua baba yake, niliamua nitalea tu. Ni WANGU. Sina uwezo wakumfukuza.
Jana usiku ndio nimemjua baba yake, sitaki kukurupuka, sitaki kesi
mbele ya familia yako. Haitanisaidia mimi wala mtoto wangu.” Mina akatoka pale
kitandani kwenda kuosha uso.
“Mbona kama wewe hizi habari hazijakushitua
Mina!?” Akashitukia Andy amemsimamia hapo maliwatoni. “Habari zipi zinishitue?
Hii mimba nilikuwa nayo tokea miezi 6 na siku kadhaa iliyopita? Pius nilikuwa
naye karibu, akinitunza kama mume kwa takribani miaka
mitatu sasa. Hajawahi kuniacha, atakachokwenda kusema ni ‘samahani’.
Akijitahidi, atadanganya labda na yeye siku ile ALILEWA, shetani akampitia. Ataomba msamaha wa dhati. Atabaki kuwa kaka
kwako na baba wa mtoto wangu ambaye anamtunza. Sasa natakiwa
kufanya nini mimi!?” Kimya. Mina
akainamia sinki na kuendelea kuosha uso.
Akatoka kurudi chumbani. Andy anamfuata nyuma. “Basi nisindikize
mimi kuzungumza na wazazi.” “Na kwenda kwenu mimi kama nani, Andy? Mimi si
mkeo! Mimi sio Ruhinda tena. Au umesahau mara ya mwisho nilipokwenda
kwenu dada yako alivyonitukana?” “Nilimkataza na nilizungumza naye tena
mbele ya familia yote ya Ruhinda. Nikamuonya kuwa asithubutu hata kukugusa
tena au kukuongelesha vibaya. Na nilimwambia sitamsamehe, mpaka
akuombe msamaha.” Mina akakaa kwenye kochi, Andy akamsogezea chakula.
“Na kwa taarifa yako tu Mina, mimi sikukutafuta
kwa kuwa nilijua unaishi na mwanaume aliyekupa mimba. Sikutaka kujiumiza
zaidi. Nilijua umeshindwa kunisamehe, japo nilipokuwa Uswiz nilijieleza
na kukuomba msamaha sana. Mwanzoni ulionyesha ni kama hutaweza
kunisamehe. Mwishoni nakaribia kurudi ndipo ukanirudia vizuri sana.
Nikawa na nguvu hata yakumaliza mafunzo. Narudi, naambiwa ni mjamzito! Moja kwa
moja nikajua ndio sababu hukuwa ukitaka kuzungumza na mimi kwa kuwa ulishaanza mahusiano
mengine.”
“Mimi ni binadamu Mina, nilikosea jinsi ya
kukuacha bila kujali utaishije. Lakini naomba na wewe unifikirie, kama mimi
ningekuwa mchoyo wa kiasi hicho, ningekuwa nikikupa kadi zangu karibu zote
za benki na namba za siri? Wewe mwenyewe ndio ulikuwa ukisema unaogopa
kuchukua bila kuniomba. Au umesahau hilo?” Mina akanyamaza.
“Mina?” “Sasa kwa nini ulinifukuza nikiwa
mgonjwa na bila kunijali? Mambo ya zamani nilishasamehe Andy, na
nilikwambia nimesamehe na wewe ukaniahidi ukirudi nitaona mabadiliko.
Hiyo sitazungumzia. Yameisha. Lakini kwa nini uliniacha kikatili vile?”
“Hasira Mina. Ni hasira kutaka uende huko kwa huyo mwanaume hivyo hivyo
ukateseke mpaka unikumbuke.” Mina akacheka kwa kushangaa.
“Andy wewe!?” “Nakwambia ukweli kile kilichokuwa
kikiendelea kwenye moyo uliokuwa umeumia na kujua umenisaliti! Hata
wewe ungekuwa mimi ungeumia Mina. MIMBA!” Mina akanyamaza akaendelea
kula. “Ila nimefurahi kama unakumbuka kukuomba kwangu msamaha. Nashukuru.
Nilijua bado unahasira na mambo ya nyuma!” “Ulivyokuwa umenibembeleza
vile!” Wakacheka.
“Nilisamehe Andy. Na nikwambie ukweli tu, nimekusifu
kitendo chakuweza kumudu kunichukua na kuishi na mimi nikiwa na
mimba isiyo yako! Nakushukuru. Najua ni ngumu.” Akamuona Andy
anatoka huku akicheka. Mina akaendelea kula.
Akamuona anarudi na kabrasha. Akakaa pembeni
yake. “Unakumbuka hii?” Akamkabidhi Mina. Akaanza kusoma. “Si ndio talaka
yangu uliyoniambia niweke saini!?” “Basi sikuipeleka popote. Ilibaki
hapahapa.” Mina akamwangalia na kuendelea kula. “Kisheria wewe bado ni mke
wangu Mina. Hata ofisini bado unajulikana kama wewe ni mke
wangu. Haya makaratasi yanabaki hivi hivi mpaka ningeyapeleka kwa
mwanasheria, yakafanyiwa kazi. Tukiamua mimi na wewe tunaweza kuyachana
tu, tukaendelea kama kawaida. Na ahadi zangu za Uswiz zile
nilizokuahidi, zitabaki vile vile.” Mina kimya
kwa muda akifikiria.
“Mina?” “Ulitaka twende Dar saa ngapi?” “Tuondoke
dakika 45 kuanzia sasa. Halafu tunaweza rudi hata kesho.” “Ila sitamuacha
Ayan.” “Mina! Siku moja tu!” “Hapana Andy, huyo sitamuachia mtu.
Judy mwenyewe nilishamuona anamshangaa vile anavyokunywa maziwa mengi.
Acha tu nikiwa na uhai, niwe naye mpaka atakapoweza kujitetea. Ayan ni mpole
sana.” Mina akafikiria kidogo.
“Mimi nitajilipia nauli yangu na Ayan. Na
nitalipia chumba cha hotelini. Wewe jilipie nauli yako. Lakini sitamuacha
Ayan. Naenda naye.” Andy akatoka. Mina akala kwa haraka, akaanza kujitayarisha
kwa safari.
~~~~~~~~~~~~~~
Familia ya Ruhinda Na janga la ndugu wa tumbo
moja wote kuzaa na mwanammke mmoja!
Nini Kitaendelea kwa ndugu hao?
Mill na Pam Nao?
0 Comments:
Post a Comment