![]() |
Nani amempa mimba Mina? Akarudi hapo akakumbuka maneno
ya Paul. Akawa kama amepata jibu alilokuwa akilikataa nafsini
kwake na kupingana nalo akiomba Mungu isiwe hivyo. Akatetea kwa
hili na lile.
Mtoto Wa
Ujanani Aibua Maswali Kwa Baba Yake.
Alimkuta Shema
anamsubiria. Ameshavaa, amependeza. Msafi. Amevaa nguo mpyaa zote
alizomnunulia. “Nilijua huji tena!” Akamwambia alipompokea. “Nilipitia kazini
kwa mama yako ndio nimekuja hapa. Naona upo tayari, twende.” Wakatoka kila mtu
hapo mtaani akimsifia Shema alivyopendeza na vitu vyake vipya. Basi Shema yeye
hana moja, anacheka tu.
Moja kwa moja
kwa kinyozi. Wale vinyozi ambao Shema hajawahi hata hisi anaweza ingia huko.
Wakamchonga mtoto wa Mill, akaanza kufanania na pesa za baba yake.
Alishaongea na Colins amsaidie kumtafutia daktari atakayeangalia huo mkono
tena. Gozi lilikuwa chafu sana, alitaka abadilishwe.
Akafika
hospitalini. Akakuta Colins na Kamila wanawasubiria. Shema akasalimia kwa
heshima huyo! Lakini wakabaki wanamshangaa huyo mtoto. “Aisee umefanana na na
huyu mtoto! Kama ni mimba ulikuwa uliikataa, hapa ungeumbuka!”
Mill akacheka akikumbuka maneno ya kule uswahilini kwa kina Pam.
“Hafanani kabisa
na Mia wala Miles! Utafikiri si watoto wa baba mmoja!” Collins akaongeza
akiendelea kushangaa bila hila asijue anazidi kugongelea msumari kwenye
wazo aliloanzisha Pam kichwani kwa Mill mpaka moyoni kwake.
Mill
akamwangalia mwanae akacheka akifikiria mengi. “Sasa huyu sina muda naye mrefu.
Hili gozi chafu sana aisee. Nimeambiwa muda uliobakia ni majuma mawili tu
atolewe, nataka kujua kama anaweza kutolewa hili akawekewa jingine, na pili
nataka kumuanzishia faili lake hapa la afya yake. Afanyiwe annual checkup,
iwepo rikodi ya aina yake ya damu. Kama kuna kilichopungua huko mwilini mwake,
nijue, ili kiongezwe. Nataka na physical checkup maana ni mcheza
mpira wa miguu. Afanyiwe kila kitu, ila kwa haraka tafadhali.” Colins
akamsaidia akafanyiwa huduma kwa haraka huku Mill akiangalia saa asije pitisha
muda.
Mpaka kuja
kumalizana na mambo ya hospitalini. X-ray na kufungwa tena, muda ukawa
umeshaenda. Akampeleka tu kula, akaanza kupambana na foleni kurudi Tandika kwa
Pam lakini akiwa ameibua maswali mengi sana.
Shema alikuwa na
aina ya damu, ‘O’ kama baba yake kabisa. Majibu ya DNA yalikuwa hayajatoka,
japo aliomba vipimo vyote ili viwekwe kwenye faili lake la hospitalini.
Hakutilia mashaka kabisa kama Shema ni mwanae. Bila DNA, huyo mtoto
alifanana sana na baba yake.
“Hawa watoto
wengine mbona kama hatufanani na hata damu yao ni ‘B’!” Akajiuliza na kujirudi. “Pengine Kisha ni ‘B’! Lakini ndio
wasifanane na mimi hata urefu jamani! Unaweza kuta Pam yupo sahihi. Japo
aliongea kwa hasira. Isije kuwa nilibambikiziwa!” Akaendelea kuwaza
akikimbizana na foleni.
“Ukute ndio
maana damu zetu zimeshindwa kuendana kabisa na hawa watoto!” Akaendelea kuwaza ugumu anao pambana nao akiwa anawalea hapo.
Mwishoe akaamua
kuacha kufikiria hilo akihofia matokeo. “Huku kufungwa na kuwaacha na Kisha
pamoja na Trey ndio kumewaharibu tu. Na pengine Kisha ana damu kali, watoto
wamechukua kwake.” Akajifariji na kutulia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alifika pale saa
12 kasoro. Akamkuta Pam amejilaza ndani. Mwanae akaenda kumuamsha. “Ona
nilivyopendeza!” Pam akacheka na kukaa. “Umekua msafi! Umependeza kila mahali!”
“Asante mama.” “Basi naomba ukacheze na miguu, Shema mwanangu! Mkono huo msafi,
utunze ili tupunguze kukunana usiku. Walikuosha kabla hawajakufunga
tena?” “Wamenisugua vizuri na kunikausha. Wakanipaka kama mafuta, wameniambia
itanisaidia kupunguza kuwasha. Ndio wakanifunga tena.”
“Wamesema
unaonekana umeunga, ila daktari ameonelea amalize muda wake.” Mill akaingilia
kwa kujihami. “Nakushukuru. Asante sana. Amekua msafi! Na nywele pia
amependeza. Asante.” Akagundua likifika swala la mwanae, anatulia na anajawa shukurani.
Watoto wakawa
wamejaa mlangoni, wanamuita Shema atoke. “Sasa sio upotee, nianze kazi ya
kukutafuta!” “Siendi mbali. Leo nataka nisijichafue, ili kanisani wanione
msafi.” “Na ulikumbuke hilo, unapokwenda huko nje, halafu ukaona mpira.
Sio ushawishike.” “Siwezi. Na hata nikicheza…” “Nilijua tu.” “Sijichafui
mama! Nacheza kwa miguu kama ulivyoniambia.” Mill akacheka akimwangalia mwanae.
“Basi badili
nguo vaa..” “Nataka wanione na nguo mpya, mama!” “Wewe unataka ukazitie madoa,
mimi nishike kazi ya kufua tu!” “Naenda kuwaonyesha, halafu
narudi kubadili za kuchezea.” “Naomba ukumbuke Shema! Maana wewe
ukiona mpira tu, akili inapotea kabisa.” “Sipotei mama. Nitarudi.”
Akatoka.
“Nimewaletea
zawadi ya pipi.” Akamsikia akiwaambia wenzie. “Na mimi Shema?” Kila mmoja akawa
anamuuliza huyo Shema. “Nimemuomba baba aninunulie mfuko mkubwa, nikamwambia
nina marafiki wengi. Wote mtapata.” Wakamsikia akiongea huko nje.
“Basi kuja
kurudi humu ndani tena ni usiku au mpaka nikamtafute! Atapita kila
nyumba kwenda kugawa hizo pipi, kisha mpira. Shema bwana!” “Lakini Pam,
huyu mtoto umemlea vizuri aisee! Kila unapokwenda naye,
mpaka raha! Kila mtu anamsifia! Halafu nafikiri ana damu ya kupendwa
tu.” Pam akanyamaza akiwa amekaa tu kitandani.
Mill&Pam
Mkakati wa Shema.
“Ulikuwa
umelala?” Akamuuliza kwa kujali. “Nimetoka kupika chapati za biashara, nikaona
nipumzike.” “Hazijabaki na mimi nichukue?” Pam akabaki akimwangalia. “Wewe
mfanyabiashara gani unachagua wateja?!” “Wa uzunguni nyinyi mnakula vya
uswahilini vinavyopikwa na mkaa?” “Hakika nataka chapati. Kama unazo za
ziada nipe na mimi.” Pam akacheka taratibu na kunyamaza.
“Huwa unamuuzia
nani?” “Pale kwenye ule mgahawa karibu na kazini. Na kwenye lile eneo
linalopakana na pale ninapofanya kazi, wanalouza matairi na kutengeneza magari.
Wale wanaume wote pale wanategemea vitafunwa kutoka kwangu. Nawatengenezea
chapati na maandazi. Ila mgahawani wanachukua chapati. Leo kama hivi nikipika
ni chache za hapahapa mtaani. Si haba! Zinasaidia. Na ni wazo la mama.
Alinikuta sina kazi, halafu tumbo kubwa, siwezi ajiriwa.”
“Akanifundisha
hiyo biashara. Tukawa tunapika naye, napeleka kwenye
mahoteli mpaka
nikajifungua. Akanisaidia kukaa na mtoto, nikaanza kazi. Yeye anakaa na
mtoto na kupika. Nikitoka kazini tunamalizia. Nasambaza jioni au asubuhi.
Tunapata pesa. Shema alipofikisha miaka minne nafikiri, ndio akaondoka kurudi
kumsaidia na bibi kijijini, babu alikuwa mgonjwa.”
“Ndio nikaona
nalemewa. Kazini na malezi ya mtoto.
Nikampa mama Batuli hoteli moja, na mama Pili hoteli ingine. Mimi
nikabakiwa na za huko upande wa kazini. Jumapili nikiwa siendi kazini, napumzika
mpaka jioni ndio naanza kupika vya kupeleka kazini siku za jumatatu. Kwa hiyo
napika jumapili, jumatano na ijumaa wakati mwingine jumamosi. Inategemea. Si haba!
Inanisaidia kutusogeza.” “Hongera Pam. Na pole kwa matatizo.” Hakumjibu
akatoka kitandani.
“Kabla
sijaondoka, nimefikiria. Nakusihi Pam, kubali mtoto wangu akapate elimu
bora, si bora elimu. Tafadhali Pam. Na kukuhakikishia kwamba nimekusudia,
maana umesema huamini chochote
nitakachokwambia.” “Hata kidogo.” Akaweka msisitizo. “Sawa. Na mimi nakubaliana
na wewe. Hata mimi nisingeamini tena. Ila kumbuka ulisema hatasoma shule
ambayo huna uwezo wa kumlipia wewe.”
“Huko kwenye
mashule yenu ya kizungu, sitaweza mimi.” “Basi, mimi nitafanya hivi,
jumatatu, nakwenda huko shuleni. Watanipa jumla ya pesa yote watakayokuwa
wakitaka kwa mwaka. Nitakuletea kule ofisini. Ukitoka, tunakwenda wote benki.
Naiweka pesa hiyo kwa miaka yote mitatu iliyobaki kumaliza darasa la saba. Ya
kumalizia mwaka huu nalipa kabisa.” Hapo Pam akakaa.
“Na hiyo akaunti
inakua ya jina lake, lakini wewe unaisimamia. Unaonaje wazo langu.”
“Usafiri wa kumtoa huku kwetu uswahilini kumpeleka shule? Na kuhama
hapa, HAKUPO kwenye mjadala.”
“Nimekuelewa.
Ila jua utamtesa mtoto.” “Atafanyaje na yeye kajaliwa baba wa namna
yako? Ingekuwa chaguzi yangu na si ujinga wangu tokea siku ya
kwanza na kuku..” “Naomba huko usirudi Pam. Ukipandisha hasira, hutaki
tena kunisikiliza. Hatua kwa hatua. Kwa swala la kwanza la shule, si mpaka hapo
umekubali?” “Hapo sawa. Nakuuliza usafiri wa kueleweka. Maana wewe una mwanzo,
mwisho huna. Tutaanza vizuri hapa, kisha uje uniache na mwanangu
ana nguo za shule, hajui jinsi ya kufika huko shuleni kwenyewe, halafu wewe hupatikaniki,
upo Ulaya huko!” “Ni Marekani.” “Unanitania Mill!?” Akaanza kucheka.
“Nilikuwa naweka
sawa hoja yako. Ulaya na Marekani ni tofauti kabisa. Kwanza ukiangalia
hata kwenye ramani ni mbalimbali sana.” “Kweli huu ndio muda wakutaka kunifundisha
mimi jografia ya ulimwengu, kweli?” Mill akacheka. “Basi mama Shema. Maana siku
hizi nasikia unaitwa mama Shema, sio Pam tena.” “Pam ulimuua muda mrefu
sana. Naomba ongea maswala ya msingi.” “Sawa mama. Turudi kwenye
swala la usafiri.”
Akajiweka sawa.
“Gari ya mara ya mwisho uliyokuwa nayo uliipenda au unataka aina nyingine?” Pam
akabaki akimtizama. “Nina maana yangu kukuuliza Pam!” “Unachokifanya hapa, ni kutaka
kunitibua.” “Basi. Kazi ya kuanzia leo mpaka kesho natafuta dereva wake
Shema. Jumatatu, nakuletea gari. Tutakuwa tunaliacha pale CCM.
Wameniambia watu hulaza magari yao usiku, malipo kidogo. Asubuhi huyo dereva
anawahi, anakwenda kuchukua gari, anampeleka Shema shule. Anaacha gari
shuleni. Anarudi kwenda kumchukua jioni akitoka shule. Alipo Shema, ndio
hilo gari litakuwepo.” “Haaa!” Wakasikia nje wakihamaki. Wote
wakaangalia dirishani. Wakajua wanawasikiliza.
Wakatulia
kidogo. “Unaonaje hilo wazo langu?” Akauliza kwa sauti ya chini. “Hapo sawa.”
“Yess!” Akashangilia kwa sauti ya chini. “Basi jumatatu nakuja kumchukua Shema
tunakwenda naye ….” “Umeanza!” “Nisikilize. Acha kuondoka.”
“Nikimuombea
nafasi ya darasa la nne, akiwa mtoto wa umri wake, miaka 9, lazima watataka kumpima.
Kujua kweli anastahili hilo darasa au arudishwe kuwa darasa moja la watoto wa
mri wake. Maana yule mdogo wake ni kama mwaka wanalingana lakini kwa kuwa yeye
alikwenda kawaida kama watoto wengine yupo 3rd grade. Kama darasa la
tatu anakotakiwa kuwepo Shema.” Pam akamtizama kama ammeze.
“Nimeshakosea
Pam, mpenzi wangu. Nitafanyaje? Siwezi kukimbia, siwezi telekeza
damu yangu.” “Kama baba yako!” “Sawa mama! Ila naona bora mimi
kuliko wengine hawajali watoto wanao zaa nje. Kwa hiyo jumatatu nije
kumchukua?” “Saa ngapi? Maana mimi nakwenda kazini alfajiri. Saa moja natakiwa
niwe nishafika maeneo ya kule. Nisambaze chapati ndio kazini. Na yule ni wakumsaidia
kuoga lasivyo anajilowesha gozi.” “Nikikuomba uwe naye ili nikija kumchukua na
wewe nikuone, si ni sawa?” “Acha kunipaka mafuta kwa mgongo wa chupa!”
Mill akacheka.
“Wewe nenda
naye, nitakuja kumchukua niende naye shule kwenye mida kama ya saa nne. Saa
nane wakati unatoka kazini, nakuja kukuchukua twende benki.” “Sitakaa nikikusubiria
popote. Kamwe sirudii huo ujinga. Niambie ni benki gani unataka tukutane.
Tumalizane, tuachane palepale kila mtu ashike lake. Usitake kunifanya mimi
mtoto mdogo.” “Kwamba unachofikiria, ni kwamba nina tiketi tayari ya
kuondoka hapa nchini, na jumatatu naweza kuondoka nikakuacha ukinisubiria?”
“Unataka nikujibu hilo swali, kweli?” “Hapana.” Mill akakataa kwa haraka. Pam
akasimama.
“Pam!”
Akamgeukia. “Nikikuomba ukatengeneze nywele, nitakukera?” Pam akamtizama na
kuendelea na shuguli zake palepale ndani. “Leo upo tu nyumbani na kesho. Pesa
sasahivi unayo. Kwa nini usiende ukatengeneza nywele kama zamani?” “Pam wa
zamani alikuwa akifanya kazi ofisini. Huyu sasahivi ni mama Shema, anauza
maziwa. Lazima kufunga nywele. Ni sheria ya kiafya. Bila hivyo
unapigwa fine. Huko unakokwenda sasahivi ndio unakaribia kunikera.
Kwanza ondoka. Tushamalizana mambo ya mtoto, huna jingine. Nenda
unipishe nifanye mambo yangu.” “Nilikubebea chakula tulichokula mchana. Mambo
yako matupu humo.” “Asante.” Kwa shukurani tu, alijaliwa.
“Ombi la mwisho.”
“Wewe unataka kuharibu!” “Jambo zuri.” “Nini?” “Kesho naomba nije
nimchukue Shema…” “Ishia hapohapo. Naona unataka kufanya mazoea sasa.” “Ni
jambo la kheri. Nataka akakutane na ndugu zake.” Hapo Pam akageuka.
“Unasema nini?!”
“Nampeleka nyumbani Pam. Kwao.” “Nilikuonya Mill wewe!” “Basi Pam.”
“Nilipo mimi ndipo nyumbani kwa Shema.” “Sawa, sawa. Acha nitengeneze.
Nataka afahamiane na wadogo zake.” “Yaani ukiongea hivyo unazidi kunikera.”
“Basi na wenzie.
Kumbuka kuanzia jumatatu au niseme jumanne, hawa watu wote watakuwa wakisoma
shule moja. Kweli unataka wakakutane shuleni kama watu baki?” Akatulia
kidogo akifikiria. “Nakuahidi hatachelewa. Nakuja kumchukua tukitoka
kanisani halafu…” “Na wewe unasali?! Makubwa! Unamuomba Mungu gani?” Mill
akaamua asijibu, aendelee.
“Tunakwenda kula
chakula cha mchana, halafu nyumbani, jioni namrudisha. Na tutacheza mpira pale
kwangu. Nina uwanja mkubwa tu. Leo hatukucheza sababu muda ulionipa ni mfupi.”
“Na kesho arudi muda kama wa leo. Sasa umcheleweshe.” “Si umeona leo
nimekuwa mwaminifu, nimemrudisha kwa wakati?” “Ulikumbuke hilo kesho.
Maana ukichelewa, sitakumbuka kuwahi kwa leo.” Akavuta pumzi kwa nguvu na
kuzishusha kama aliyetua mzigo.
“Nina ombi
jingine, ila hilo nalitunza mpaka jumatatu. Nahisi nikilileta sasahivi, naweza
nikaharibu.” “Sasa kwa nini ulilete hilo ombi kama unajua kabisa ni la kukera?”
“Ni lazima tutafikia tu muafaka. Nishakuona wewe kwenye mambo ya msingi tunaelewana.”
“Haya, jioni njema. Naona muda wako wa kukaa hapa umeisha.” Mill akacheka na
kuondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Alipotoka tu,
majirani zake wote mlangoni. “Mimi ndio nimewahi, mama Batuli!” “Sasa
kwani baba Pili alishaendesha wapi gari, kama si tamaa tu?” Pam akawa
hajaelewa. “Nakuomba muombee baba Batuli hiyo kazi ya kumuendesha Shema.
Tafadhali shoga.” Pam akabaki amepigwa na butwaa hapo mlangoni.
“Mimi niliwahi
tokea baba Shema yupo ndani!” “Sasa acha niwaambie. Huyu mwanaume hayupo na mambo
ya juujuu. Kama kweli kuna anayetaka hiyo kazi, ataitisha leseni ya
kuendesha. Ataipeleka ikakaguliwe, na atataka huyo mtu amuendeshe
yeye kwanza. Ndivyo alivyo Mill. Hafanyi mambo ya kienyeji.” “Mimi
leseni ninayo mama Shema.” Akadakia baba Batuli mwenyewe.
“Na nina uzoefu
wakuendesha mabosi wa Wizara ya Afya. Sema walinipunguza kazi.” “Na wewe
baba Pili?” “Naona hapo mimi nitakwama. Leseni ilishapotea zaidi ya
miaka 10. Naona hiyo riziki ni ya baba Batuli.” “Basi mimi nitazungumza
naye akija kesho. Ila hakikisha unayo kweli leseni. Atataka kuiona na kuifuatilia
kujua ulikuwa ukiendesha vipi! Ulishapata ajali au la.” “Mama Shema!”
“Hakika sikudanganyi. Hana njia za mikato. Utamsikia mwenyewe.”
“Ila bwana dume
lile unalo!” Akasifia mama Batuli. Pam akamwangalia hakutaka kuongeza neno.
“Ngoja mimi nikamtafute Shema. Maana najua kuja kurudi hapa ni usiku!”
“Na hivi ana viatu vipya!” Mama Pili akamfanya Pam acheke. “Mwanangu kipofu
kaona mwezi! Utafikiri apae!” “Kaniambia alilala navyo jana usiku.” “Wewe
acha tu!” “Naomba mimi vile vya zamani, mama Pam. Mwanao navaliana naye
kabisa.” Baba Pili akaomba.
“Wala usijali.
Acha nikamuwahi kabla hajajichafua huko alipo. Baba yake msafi sana.
Hapo kambadilisha gozi sababu kaliona chafu. Sasa mtoto mwenyewe
anacheza mpira wa miguu na mikono! Jasho litamtoka.” Wote
wakacheka, Pam akatoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Pam aliwahi
ibada mapema, kwenye majira ya saa tano anarudi akitembea na mwanae, akaona
gari ya Mill akajua anawasubiria. Shema akakimbilia mpaka dirishani. Mill
alipomuona, akashuka garini. Akamsalimia Pam na mwanae. “Mimi naomba hata ndani
nisiingie. Kuna mahali tunakutana kwa chakula cha mchana. Wengine
wameshatangulia, wananisubiria mimi na Shema tu.” “Nirudishie mwanangu
kama ulivyomchukua. Sio arudi hapa mnyonge.” “Pam!” “Kumbe! Maana
unaweza kwenda kumkutanisha na watu wa hali za juu, ukamfedhehesha.
Sasa arudi hapa amenyongea, jua ndio mwisho wa kwenda kumnyanyasa
mwanangu.” Mill akaona asiongeze.
“Ushapata
dereva?” “Bado. Kwanini?” “Baba Batuli alikuwa…” “Hapana Pam. Mimi mambo
ya ujamaa, halafu uje uniletee matatizo, hapana kwakweli.”
“Alikuwa dereva anaendesha magari ya Wizara ya Afya.” “Una uhakika?” Pam
akanyamaza.
“Pam? Maana ujue
itabidi aniletee uthibitisho. Na nitataka kuona leseni.” “Nimemwambia,
amekubali.” “Sawa. Nitazungumza naye nikirudi. Panda kwenye gari Shema,
twende.” Shema akapanda kwa haraka. “Umependeza sana Shema. Halafu msafi!”
Akamsikia akimsifia mwanae. Ila alimjua Mill anapenda vitu vizuri.
“Humu ndani kuna
baridi sana.” Pam akamsikia mwanae. Akadakia. “Sasa sio arudi anakohoa
huyo!” “Napunguza mama. Wewe hutaki kuongozana na sisi?” Ikawa kama amemfukuza
Pam, akaanza kuondoka. Mill akaanza kucheka. “Umependeza Pam, mke wa ujana
wangu.” Hata hakugeuka, akaingia ndani. Akaondoa gari.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kwenye majira ya
saa 10 hivi, amejilaza akipepewa na feni. Joto haswa ndani, anasubiria papoe
nje, akaanze kupika chapati, akaona Shema anaingia na nundu kubwa pembeni ya
jicho. Na hivi ni mtoto mweupe, ule uvimbe ulikuwa mwekundu haswa.
Pam alishituka,
nusura roho imtoke. “Njoo hapa. Umefanyaje?” Shema akaanza kulia. “Mtoto wake
wakiume amenipiga na game.” Pam aliumia
sana. “Kwa nini?!” “Anasema nimemuibia kitabu chake. Na baba yake ameamini.” “Yuko wapi huyo baba yake?!” “Sijui! Mimi nimeondoka kwao,
nikarudi nyumbani.” “Kwamba umekuja hapa bila yeye?!” Shema
akazidi kulia. “Na hapa juu pamechanika. Twende dispensari.” Akatoka na mwanae
amemshika mkono akimtuliza.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Huku nyuma Mill
akafika kama aliyekuwa akikimbia. Akakutana na majirani wamekaa pale uwani.
Baba Pili akamuwahi. “Mimi nashauri kwa leo, ukae mbali. Mtaa mzima huu wanamjua
mama Shema. Hakuna anayegusa mwanae. Ashapigana na kijana mmoja
pale baoni, sababu ya kumgusa mwanae. Ngumi zilizopigwa pale, mpaka leo
wanasimulia.”
“Mama Shema alimpiga
yule kijana, kama kapigwa na bondika. Waulize pale baoni
watakukusimulia. Huyo Shema haguswi.” “Wala hatukanwi.” Akadakia
mama Pili. “Ukimtukana tu mwanae, akisikia, anakufuata mpaka kwako na hutamtuliza
kwa maneno.” “Ilitokea ajali tu!” Mill akawa anajitetea.
“Basi sivyo
alivyosema mwanao. Kasema mtoto wako kampiga na game kwa makusudi
akimsingizia WIZI. Na wewe ukaamini kama kaiba.” “Na Shema si
mwizi, wote tunamjua. Akiokota hela, haweki mfukoni mpaka
wenzie wanamcheka.” Mwingine akadakia. “Hata uangushe pesa hapa,
akiokota yeye jua utaipata pesa yako.” Akaongeza baba Batuli.
“Sio kwamba niliamini!
Ila nilikuwa najaribu kuwapatanisha.” “Sasa hapa uondoke, lasivyo
usiku huu utakuishia vibaya.” “Wameenda wapi?” “Kuna dispensari moja ipo kule
mbele ya CCM. Kuna daktari pale anampenda sana mama Shema. Atakuwa ndio
kaenda hukohuko.” Mill akaondoka kama akimbie.
“Sasa na wewe
mambo ya kupendwa yanamuhusu vipi?” “Ndio ajue tena hayupo peke yake.”
Wote wakacheka. Mill akasikia ila akanyamaza na kuongeza mwendo atoke hapo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akaendesha akitafuta hiyo dispensary
mpaka akapapata. Akajiandaa kuingia akijipanga, mpaka akapata ujasiri.
Palikuwa pametulia mlango umefungwa kwa nje. Akajua siku hiyo huwa
hapafunguliwi, inamaana kama kweli wapo ndani, huyo daktari yupo hapo kwa ajili
ya Pam.
Akagonga mpaka
mlango ukafunguliwa. Alikuwa Pam. Roho ikampasuka paa! Alikuwa mwekundu kama
apasuke. “Wewe ndio wa kumuita mwanangu mwizi?!” Likawa swali la kwanza.
“Umenikuta nikiishi uswahilini ukadhania nimekuza jambazi!”
“Nisikilize Pam.” “Kati yako na Shema, nitamsikiliza Shema, kwa sababu
yeye si muongo. Umeniumiza Mill, kuliko ulivyowahi kuniumiza.
Hivi ninavyozungumza na wewe, nisiwahi kukuona tena.” “Pam!” Pam akatoka
nje kabisa.
“Nina faida gani
na mtoto anaye vaa viatu vipya halafu mmempasua kichwa? Nina
faida gani na mtoto anayevaa nguo mpya huku ananyanyasika?” Pam alikuwa
anaongea mpaka anatetemeka. “Nimemfikisha hapo alipo, sitashindwa
kumuendeleza zaidi. Uliniacha nikiwa na mimba yake huyu, si amefika hapo alipo?
Hakika nisikuone Mill. Leo mwisho wako. Hutakaa ukamnyanyasa
mwanangu.”
“Nikija kukuona
kesho au kesho kutwa, itakua mbaya! Hutaamini na utajuta hata kunifahamu.
Nimempiga picha ushahidi wa kile ulichomfanya wewe na watoto wako. Huyu
daktari ni shahidi wa kumtibu leo. Wewe si unapesa, utataka kunichukulia
hatua, sasa NIANZE uone jinsi nitakavyo kumaliza. Hutakaa ukamuona huyu
mtoto mpaka aje kuwa mtu mzima, na tena pengine aje akutafute mwenyewe.”
“Siwezi kufanya
hivyo. Naheshimu kila unachokisema juu yake. Na samahani sana, Pam. Nia
yangu ilikuwa nzuri. Nahisi nimefanya haraka.” “Naomba uondoke, kabla hujaniumiza
zaidi. Na ukumbuke, USIRUDI tena. Si pale tunapoishi tu, hata kazini kwangu nisikuone
Mill. Nitazungumza na yule mama na nitamuonyesha picha kwa kile ulichomfanya
mwanangu.” “Nakusihi Pam, usifike huko. Tafadhali mpenzi.” “Basi usitufuate
nyuma tena. Kazae kwingine. Shema SAHAU.” Akaingia ndani na kumuacha
amesimama nje.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Inaendelea…
0 Comments:
Post a Comment