Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 33. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 33.

Alikaa Mina mpaka usiku, Andy hajarudi. Akaona afike jikoni aangalie chakula. Akamkuta kijana wa Andy ameshasafisha. Jiko safi. Akajua alimtuma yeye mwenyewe. Akamlisha mtoto, akampa maziwa na kumrudisha chumbani. Mina naye akaona aende tu kulala.

Asubuhi akamkuta jikoni anapika. “Nilizungumza na Kashinde. Nimemuomba kama anaweza kubadilisha muda wa kwenda kumchukua huyo msichana. Akaja mapema kidogo labda hata kesho ili angalau tumuonyeshe mazingira, tumuachie nyumba, ndio tuondoke.” “Nimegairi. Hakuna safari tena, leo naanza kwenda kazini.” Mina akasimama pale nyuma yake kwani hakuwa hata amemgeukia wakati akizungumza naye. Mwishoe Mina akaamua aondoke.

Andy alipika kifungua kinywa kwa wote, akajitayarisha. Akatoka bila hata kuaga. Mina alipoangalia muda akajua ndio ameondoka moja kwa moja. Akatoka. Mtoto wake hakuwa ameamka na wala yeye hakuwa ameletewa kifungua kinywa chumbani. Hakujali.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Alirudi jioni kama saa kumi na nusu hivi. Akasalimia, akamshika Ayan kidogo, Mina akamuona anaingia chumbani kwake kubadili nguo za mazoezi, akatoka. Mina alishakuwa amepika. Mpaka Ayan anakwenda kulala usiku, baba yake hakuwa amerudi kutoka mazoezini. Mina na yeye akaona akalale tu.

Mungu Hutumia Yeyote.

Kesho yake akafanya hivyo hivyo. Kutengeneza kifungua kinywa na kuondoka bila hata kuaga. Ilipofika saa saba mchana Kashinde akawa amerudi na huyo msichana wa kazi. Alionekana ni dada mtu mzima. Tena mkubwa hata kwa Mina. Lakini alionekana ni dada anayejielewa, anapenda watoto na si mshangaaji.

Akamuuliza kama alishafanya kazi mahali. “Wakati mdogo. Nilifanya Dar kwa mama mmoja kwa miaka 18, ndipo nikaondoka kwenda kuolewa. Nina watoto watatu, wa mwisho ndio ameanza darasa la kwanza. Maisha yamekuwa magumu ndio nimeona nitafute tena kazi ili ziwasaidie wanangu.” Akajieleza vizuri tu.

“Oooh, kwa hiyo unaye mume? Au niulize watoto umewaacha na nani?” “Wapo na mama, lakini mwanaume aliondoka. Akaniachia watoto. Nilishajaribu kumfuata kuomba hata matumizi, lakini alinikatalia. Nimebaki nikihudumia hao watoto peke yangu. Hivi ilikuwa nije tokea majuzi, mtoto wangu mkubwa alikuwa mgonjwa, ndio nikamuomba Kashinde aniombee mnisubiri.” “Anaendeleaje sasa hivi?” Mina akauliza kwa kujali. “Anaendelea vizuri. Alimaliza na dawa.” “Afadhali. Kwa hiyo ndio umekuja moja kwa moja?” “Kabisa dada. Ila mtoto wako mkimya! Au hajaweza kuongea?” Mina akacheka na kumwangalia Ayan. 

“Anaongea na kuelewa kila kitu. Ila ni mkimya sana. Ukitaka akupende, umpe maziwa. Hapo mtaelewana. Anakunywa maziwa kabla na baada ya kila mlo.” “Inamaana kuanzia asubuhi?” “Ewaa! Kabla hujampa uji wa asubuhi lazima umkabidhi chupa yake ya maziwa ndipo baada ya nusu saa atakunywa uji, na ukishamsaidia kumsafisha mdomo, mnaagana na chupa nyingine ya maziwa mdomoni. Hapo mtaelewana.” Wakacheka. “Kama mtoto wa ng’ombe?” “Hapana, yeye anasema kama mtoto wa Mina.”  Wakacheka sana.

Mina akamuonyesha kila kitu na chumba chake. Akamwambia baba yake Ayan anakwenda kazini, anatoka asubuhi anarudi jioni. “Ila Andy ni msafi sana. Hivi unavyoiona hii nyumba ilivyo, ndivyo hivyo inatakiwa iwe kuanzia asubuhi tunaamka mpaka usiku tunaenda kulala. Kusizagae hata kandambili. Au asikute hata tone la maji limemwagika sehemu. Kila kitu anataka kiwe sehemu yake, kila wakati.” Wakacheka. Akamueleza taratibu zote. Mina akafurahia aina ya maswali aliyokuwa akimuuliza. Akajua kweli anajielewa.

~~~~~~~~~~~~~~

Maisha yakaanza. Judy akawa msaada kweli kwa Mina. Anamjali yeye na mtoto wake. Andy bado akawa na hasira vilevile. Juma la kwanza Judy akiwa ameanza kazi likaisha, akiwasoma wenye nyumba yake. Akaona kuna utofauti kati ya Mina na Andy.

“Nikuulize kitu mama mwenye nyumba wangu?” Mina akacheka. Andy alikuwa ameshatoka kwenda kazini. Siku ya ijumaa. “Niulize tu.” Mina akamkubalia. “Mbona sijawaelewa wewe na baba Ayan! Kama mnapishana vile! Hamlali chumba kimoja! Kosa gani kafanya umeshindwa kusamehe? Maana mwanaume kama yule hapa kwenye hili jiji, watakuliza wenzako!” Mina akabaki akifikiria asijue ajibu nini.

“Sio lazima ukaniambia, lakini ninachotaka kukwambia, ukishikwa, shikamana. Wapo wanawake kazi zao ni waume za watu tu. Kama bado hujachelewa, funga hiyo mianya mdogo wangu. Usikubali ukajaribiwa bila sababu.” Ikabidi Mina amwelezee kwa ufupi, Judy akabaki ameshangaa.

“Sasa umemwambia mwenzio?!” “Namwambia nini wakati hata mimi mwenyewe bado sijaelewa?!” Judy akashangaa sana. “Wewe mama Ayan kwani una miaka mingapi?!” “Kwa nini?” “Mimi naona kama wewe bado una mambo ya kitoto, hujayajua maisha! Hasira hiyo ikiendelea akakwambia sasa hivi naomba unipishe ninaye Judy wakunisaidia, unafanyaje na mtoto usiyemjua baba yake?” “Sasa nifanyaje!?” “Wewe Mina! Samahani mpaka nimekuita jina lako kwa mshituko bosi wangu!” Mina akacheka.

“Wewe usiwe na wasiwasi niambie tu.” “Mbona mimi umenieleza hapa! Kinachokushinda kumueleza na yeye ni nini?” “Hawezi amini!” “Hiyo itakuwa juu yake yeye. Ila angalau utakuwa umempa heshima yake. Alikuwa mumeo, akakukuta mjamzito! Kweli mpaka leo umeshindwa kumwambia! Kwanza naona mimi wala asingeniacha. Siku ile ile hata njiani kwenda kwetu ningemwambia simama nikueleze. Na nikwambie kabisa, hasira hizo ni zakuona unazaa na mwanaume wako.”

Naogopa dada!” “Acha mimi nikuombee Mina. Ninaye Mungu anayetenda mambo kwa namna ya ajabu sana. Nilikwambia mume wangu aliniacha?” “Ndiyo.” “Nilimuomba Mungu anirudishie yule mwanaume mpaka nikachoka. Lakini hakuna siku watoto wangu na mama yangu wamelala njaa wala sijawahi kukosa pesa ya kuwatunza. Mungu ananijibu kwa namna ya ajabu mpaka nashangaa. Huyo Kashinde hapo, ananipenda anatamani kunioa hata leo!” Mina akacheka sana, akajua Andy alipatia.

“Sasa kwa nini hutaki akuoe?” “Mdogo kwangu, halafu nahisi nimeingiwa hofu. Akinigeuka na yeye! Maana hapa nina watoto watatu. Akinioa yeye, atataka watoto. Najiona umri umekwenda, na yeye bado kijana. Nimemwambia atafute mtu mwingine, lakini naona amekazana tu.” Mina akacheka sana.

“Muone hivyo hivyo Kashinde. Anamaneno huyo, hata mama anamjua. Ila ananijali sana. Alikuwa akinitumia pesa za matumizi, na alikuwa kila akija kule kijijini lazima aniletee zawadi. Watoto wangu wote wanamjua.” “Sasa si muoane tu. Kashinde ametulia.” “Na ametulia kweli, pale kijijini wanamjua. Ndio vijana wa mwanzoni kabisa pale kijijini kuokoka. Na alinipenda tokea zamani, mimi nikaona mdogo kwangu kama miaka miwili hivi au mmoja na miezi. Nikampuuza. Halafu nilikuwa nikiishi Dar yeye yuko huku! Nikampata huyo tapeli, amenizalisha na kunikimbia. Na wala usifikiri anaishi mbali. Yupo hapahapa Dodoma mjini.” Mina akabaki akicheka tu.

“Achana na mambo yangu na Kashinde, turudi kwako wewe ambaye mambo yako yanaeleweka. Nataka tuombe kisha akirudi jioni muombe akusikilize tu. Mwambie tu. Halafu mwache Mungu ashugulike naye. Fanya kwa upande wako, uone vile Mungu alivyo wa ajabu. Huwa unakwenda kanisani?” Hapo napo Mina akamwelezea kwa kifupi juu ya imani zao za dini.

“Kwa hiyo ndio maana unamuona kila jumapili anakwenda na Ayan kanisani.” “Sasa wewe achana na maombi yakuombewa kama maiti. Anza kumuita huyo Mungu wa mama yako na Ron kaka yako. Omba mwenyewe mdogo wangu. Ipo raha yake. Unamwambia Mungu kile unachokitaka wewe na unachojisikia. Ambacho hakuna mtu anakijua isipokuwa wewe. Omba kwa roho, achana na maombi hayo yaliyoandikwa na mtu mwingine. Roho Mtakatifu atakusaidia kuomba, ndipo utasikia raha.” Judy akamueleza Mina, mpaka akajisikia vizuri.

“Kwanza ulishawahi kumpa Yesu maisha yako Mina?” “Ndiyo. Zamani. Mama alinipeleka. Nikaombewa na nikaokoka. Ila nimejichanganya hapo katikati wala sitakudanganya.” “Mungu wetu ni warehema wala si kama sisi wanadamu tunavyo hukumiana. Yeye mwenyewe anaita wenye dhambi. Anasema atawapumzisha, na wala hatakumbuka dhambi zetu tena endapo utaungama kwa nia. Omba toba pale ulipomfungulia shetani mlango, uanze kukulia wokovu tena kwa upya. Soma bibilia na ujifunze neno.” Akazungumza naye, mwisho akamuombea huyo bosi wake. Mina akamwambia anajisikia vizuri.

Kwa Andy.

Andy alifanya kama kawaida. Alirudi nyumbani jioni. Akazungumza kidogo na mtoto wake chumbani kwake, akatoka kwenda mazoezini. Kila mtu alikwenda chumbani kwake, Mina akakaa chumbani kwake akimsubiria. Kwenye saa tatu usiku akamsikia amerudi. Akajua lazima aoge kwanza na kula kidogo. Akampa kama lisaa. Aliposikia mlango wa chumbani kwake unafungwa, akajua ameingia chumbani kwake. Akasubiri kidogo akijua lazima asafishe meno.

Alijua huwa siku za jumamosi haendi kazini, kwa hiyo ijumaa huchelewa kulala. Mara nyingine anakuwa tu chumbani kwake akijisomea vitabu au kuangalia movie. Akaenda kumgongea. “Ni Mina?” “Ndiyo, mimi Mina.” Akamkaribisha. Akamkuta amekaa kitandani. “Pole na kazi.” “Asante.” Akajibu huku akimtizama.

“Naomba kuzungumza na wewe.” “Karibu.” “Naweza kukaa hapo kwenye kochi?” “Karibu.” Akaenda kukaa. Akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha. Andy kimya akimtizama.

“Kuna kitu nataka kukwambia Andy. Najua kabisa hakileti maana au hakieleweki, na ni ngumu kuaminika. Sitashangaa kwa kuwa hata mimi bado nipo kwenye mshangao. Siamini! Lakini naona nawajibika kwako. Kilitokea nikiwa bado ni mke wako. Unayo haki yakujua ni nini kilitokea.” Akamuona Andy anakaa vizuri.

“Unakumbuka mawasiliano ya mwisho karibu unarudi nyumbani?” Andy kimya. “Maneno yote niliyokuwa nikikwambia?” Andy kimya. “Nakuhakikishia Andy, nilimaanisha. Sikukudanganya. Nilikuwa na hamu na wewe mpaka nilikuwa nasikia kuchanganyikiwa! Nilikuwa nikikusubiria kwa hamu uje uniguse, lakini siku kama 8 hivi kabla ya kurudi kwako, nikaanza kutapika sana. Yule msichana tuliyekuwa tukiishi naye,” “Mamu?” Andy akamuuliza.

“Ehe, Mamu. Akaniambia hiyo ni mimba. Sasa kwa kuwa Mamu ni muongeaji sana, wakati mwingine nilikuwa nikimpuuza tu. Lakini nikazidi kutapika mpaka siku ile niliyokwambia tunakwenda kwa Paulina, jumamosi, nilikwenda nikitapika. Nakumbuka mpaka nikamwambia baba, mzee Ruhinda. Wengine wakisikiliza. Nikamwambia baba, natapika kama mjamzito wakati hata mimba ya Ayan haikunisumbua! Baba akaniuliza, umekwenda hospitalini? Mbele ya watu, mimi najibu, sikuwa hata na wazo kama ni mimba. Nikamwambia nilifikiri ni ugonjwa, lakini nashangaa natapika tu ila sina homa. Paul akadakia kuwa, lazima kwenda hospitalini ili nikajue.” Mina akaendelea.

“Baba naye akanisisitiza nisizembee, nikamuone daktari. Nikakubaliana nao nikiwaambia basi nitafanya hivyo ili Andy wangu akija, anikute mzima. Sasa nikawa nimemuomba Paulina chakula ili nimlishe Ayan. Nikamwambia sijampikia Ayan muda mrefu, na pale nyumbani nimekataa kusipikwe sababu ya harufu inanishinda natapika. Nikamwambia...” “Hayo ni wewe ndio unamwambia Paulina?” Andy akauliza.

“Nilikuwa nikizungumza na baba pale sebuleni kwa Paulina, ila wote walikuwepo nafikiri waliweza kutusikia mazungumzo yetu na baba, na ndio maana wengine wakaweza kuniuliza na kunishauri kwenda hospitalini. Maana nilikuwa nimekaa sebuleni na baba, Paul, na Pius wengine jikoni na watoto upande wa kulia chakula. Tena nilifika tu, kisha nikatoka kwenda tena kutapika. Nikarudi moja kwa moja nikaenda kukaa mbele ya baba nikawa nimeinama huku nikizungumza naye au nao.”

“Maana nilikuwa nimechoka Andy, sina jinsi nikaeleza ukanielewa. Nilikuwa natapika, halafu sielewi na wala siamini kama ni mimba kwa kuwa wewe ndio mtu wa mwisho kufanya naye mapenzi! Na nilishapata siku zangu kama mara tatu hivi tokea uondoke. Kwa hiyo wazo la mimba sikuwa nalo kabisa.”

“Basi, wakati nimekaa pale ndio nikamuomba Paulina chakula nimpe Ayan. Nikamwambia namuhurumia Ayan wangu kwa kuwa kwa siku 5 mfululizo nimekuwa nikimpa uji na maziwa tu, sababu ya mimi kutapika na harufu zinanishinda sitaki nyumbani kupikwe kitu chochote.” “Subiri kwanza Mina. Hayo unazungumza mbele ya kila mtu!?” “Ndiyo Andy! Mimi sikujua kama ni mimba! Nikajua nimepatwa na tatizo baya. Halafu kwa kuwa Mamu alishanitisha kuwa kwa kina Raza ni washirikina sana na Raza hanipendi mimi na Ayan, Mamu aliniambia alishamsikia akisema huyu Ayan hataishi. Nikwambie ukweli Andy, mpaka nikahisi Raza ameniloga.” “Nini kilitokea?” Andy akataka aendelee.

“Basi. Nikawa sasa nasimama kufuata chakula jikoni wakati kina Paulina wanamalizia kupika vitu vingine, ili nimlishe Ayan, maana nilijua atakuwa anahamu tu na chakula. Ile nimeingia tu jikoni kwa Paulina, hali ya kichefuchefu ikanipata. Nusu nitapikie pale jikoni! Nikakimbilia bafuni. Nikatapika wee, ndio nikatoka nikakuta kila mtu ameduaa.”

“Lakini nikamkuta mama akinisubiri nje ya choo. Akanipa pole, mimi nikamwambia mama ni tatizo lililonipata. Nikamwaambia sina raha! Natapika kila wakati! Si ndio Paulina akasema anisindikize hospitalini? Nikakubali kwa haraka na kushukuru kuwa ananisindikiza hospitalini, nikiwa na uhakika baba yupo pale, Ayan wangu atakuwa salama. Maana nilikuwa naogopa kumuacha na Mamu tu. Sababu ya maneno yake na ukaribu wake na Raza, nikawa najiambia asije Raza akamtuma amdhuru mwanangu bure?”

“Ilifikia hapo!?” “Ni vile baba na mama hawataki ugomvi, lakini kila mtu anajua kama Paulina na Raza hawampendi Ayan. Hata Pius alikuwa akiniambia nisiwe nampeleka mtoto pale kwao labda yeye awepo. Na kuna kipindi baba akaacha kusafiri akawaambia wote, yeye ndio atakuwa akikaa na Ayan kama mimi ninadharula. Akasema hataki kumuona Ayan kwenye nyumba ya mtu yeyote. Popote alipo, apigiwe simu, atarudi kuwa na Ayan. Lakini sasa wewe unajua majukumu ya baba na mama, wakati mwingine walikuwa inabidi wasafiri.”

“Nikawa namuomba Ron. Ron ndio akawa kimbilio langu kubwa kama mzee Ruhinda na mama hawapo. Tena mzee Ruhinda alikuwa akimchukua na kuwa naye ofisini kwake kabisa. Ayan alikuwa ananiambia anaingia naye kwenye mikutano, anampa nafasi asalimie.” Andy akapoa, akijisuta yeye baba mtu alishindwa vipi!

“Basi, ndio Paulina akanisindikiza hospitalini. Baada ya vipimo ndio daktari akathibitisha ni mjamzito. Jamani Paulina alinipiga, pale ndipo nilijua dada yako ananichukia Andy. Kuna muda alinisukuma kwa nguvu mpaka nikaanguka sakafuni. Halafu mbele ya watu! Mara nyingine akanisukuma nikajigonga hapa.” Mina akamuonyesha. Andy akamsogelea na kuangalia. “Pole.” “Asante. Lakini nilikuwa na mshituko Andy, natetemeka kwa hofu sijui ni nini kinanitokea!”

“Kwani wewe ulikuwa ukienda kusoma na wenzio?” “Na mwanangu je? Nilikuja kushindwa. Sikuweza kwenda tena kwenye kusoma na wenzangu sababu ya mtoto! Unamuacha mahali, unaomba kwa masaa machache tu. Ilikuwa lazima niwe muungwana, niwahi kurudi kumchukua mtoto wangu. Sikutaka baba alemewe halafu amchoke japo siku za jumamosi wakati mwingine alikuwa akija kumchukua asubuhi ili nipate muda wakufanya mambo yangu mwenyewe, lakini Andy, nilikuwa siwezi kutoka sababu ya ubusy wa shule na kazi za pale.”

“Na unamjua Ayan nikiwa naye, anataka nilale naye kabisa. Aninuse mpaka aridhike yeye. Kwa hiyo ilikuwa ikitokea babu yake anakuja kumchukua, nilikuwa nasafisha nyumba sasa, au kukimbilia saluni au kufanya manunuzi. Marafiki walikuwa kwa simu tu. Lakini si kuonana.” Andy akanyamza.

“Najua hutanielewa Andy, lakini Mungu wangu atakuja kuyathibitisha haya siku moja. Sikukusaliti Andy. Ila sijui kilichotokea kwenye huu ujauzito! Hata baba wa huyu mtoto mimi simjui, Andy. Na Mungu wangu ni shahidi. Natamani ningekuwa na maelezo mengi yakueleweka, lakini sina Andy. Ndio hivyo tu.” Andy akabaki akifikiria.

“Unauhakika hakuna hata kijana uliyewahi kumfungulia mlango pale nyumbani?” “Najua hutaniamini Andy, kutokana na historia yangu ya nyuma ya uchafu. Lakini akili yangu ilijaa Ayan tu. Nilikuwa nikimuhurumia vile alivyokuwa akikataliwa na kunyanyaswa kwenye majumba ya watu. Nikakusudia kila wakati, kuwa naye mimi mwenyewe mpaka ilazimu sana. Sikuwa hata na wazo la mwanaume. Mbali na ndugu zako kuingia pale ndani, labda na Ron, hakuna mwanaume mwingine alikuwa akiingia.”

 “Namaanisha labda ulimkaribisha kwa wema tu, akakulevya hata kukuwekea kidonge kwenye maji! Akakufanyia ubaya, akaondoka wewe usijue.” “Hapana Andy! Mtu anifanye mapenzi, Ayan na Mamu wangekuwa wapi? Halafu wewe hujamjua Mamu. Hawezi kunyamazia jambo. Angeshasema kama nilishawahi kuingiza wanaume pale ndani.”

“Mbona amesema kuna siku ulikuwa ukimtuma mbali akale chakula na hutaki arudi nyumbani?” Mina akashangaa sana. “Andy wewe! Ndivyo alivyokwambia Mamu?” “Ndivyo alivyowaambia watu.” “Muongo. Naomba fikiria na mimi bila hasira.” Mina akakaa sawa.

“Mamu alikuja kuishi na sisi, muda wakulingana na ule ujauzito ulipogundulika. Nisikilize vizuri. Mimba inaanza kunisumbua, ina mwezi mmoja, sawa sawa na siku alizokaa Mamu. Nikaanza kutapika mwishoni nilipogundulika. Siku kama 5 kabla nikiwa naye nyumbani ndipo nikaanza kutapika nikawa sitaki kupika kabisa. Ndio nikawa namtuma akanunue chakula nje. Na sikutaka yeye ndio awe anapika kitu chochote mle ndani kuhofia asije akaniwekea mambo ya ajabu ya uchawi.”

“Kwa hiyo nikawa sitaki apike kabisa. Na sikuwa naweza harufu ya chakula chochote ndio maana nilikuwa nikimwambia akajinunulie chakula chake na ale huko huko. Hiyo yakumwambia akanunue chakula ilianza wakati nimeshaanza kutapika, yaani mimba ishakuwa na mwezi. Sasa huyo mwanaume nilikuwa nikimuingiza hapo akanipa mimba ipi na tayari nilishakuwa mjamzito?” Andy akaona ni kweli. Akabaki akifikiria.

“Halafu Andy, ukumbuke hapo na Ayan alikuwepo. Kweli unafikiri Andy mimi naweza kulala na mwanaume mwingine pale ndani, mwanangu akinisubiri sebuleni?” Hapo Andy na yeye akaona hapana.

“Kweli haieleweki!” “Sasa mimi nikadhani labda ndio Raza ameniloga, ili nidhaniwe nina mimba. Yaani hata huku kutapika na tumbo kuendelea kuwa kubwa nikawa nahisi ni uchawi tu, humu ndani hakuna mtoto. Sasa mtoto alipoanza kucheza ndipo nikaanza kuamini kidogo. Mwishoe nikaona ni heri nijiridhishe tu kuwa ni mtoto kweli aliyekuwepo tumboni si mazingaombwe.”

“Ndipo nikaomba nionyeshwe kabisa kwenye ultrasound. Mpaka yule mtu aliyekuwa akinifanyia Ultrasound alikuwa akinishangaa wakati akinifanyia hiyo ultrasound kwa maswali na kwamba anithibitishie kama huyu mtoto tumboni ni kama watoto wengine ambao anawaonaga kwenye matumbo ya kina mama wengine! Akanithibitishia huyu mtoto ni mtoto kabisa na ni mkamilifu, ndipo nikaanza kumnunulia vitu sasa.” “Umejua jinsia?” Andy akauliza.

“Hilo ndilo sikutaka kujua.” “Kwa nini?” “Sijui Andy! Labda ni vile kwenu au watu walionizunguka walivyokuwa na matatizo juu ya jinsia! Nimemzaa Ayan, mtoto wa kiume, badala kuwa ni baraka, wamegeuza kuwa tatizo! Nimeona hilo libaki kitendawili mpaka siku yakujifungua ndipo nitajua.” Andy kimya.

 “Ni hivyo tu Andy. Acha nikuache upumzike. Na pole, nimekwambia muda mbaya labda utashindwa kulala, lakini nimeona nikwambie tu.” “Leo umejibu mambo mengi sana. Kuna vitu niliambiwa, ndio leo kidogo vinajijibu.” “Sasa umejuaje kama katika hili sijakudanganya?!” “Kumbuka nimeishi na wewe kama mke wangu Mina. Nakufahamu sana. Na nimesoma saikolojia. Najua mtu anapoongea uongo. Na nimefurahi umeniambia. Nilikuwa nikiteseka, nakaribia kuchanganyikiwa.” “Pole Andy.” Andy akabaki akifikiria.

“Kuna kitu hakijakaa sawa Mina. Tafadhali pata muda wa kufikiria.” “Itabidi. Nilikuwa naogopa kufikiria sana kama alivyonishauri Pius ili nisijipe ugonjwa wa moyo.” “Sijaelewa.” “Hapana, si kitu. Ni Pius tu alinitia moyo kuwa katika kipindi hiki niangalie swala la mtoto tu, nisifikirie hayo mengine kama itakuaje hatima ya mtoto au imekuaje.” Andy akashangaa sana.

“Hayo Pius alikwambia lini!?” “Uliponifukuza kwako Andy.” Mina akajibu kwa wasiwasi kidogo. “Kwani uliendelea kuwasiliana na Pius?!” “Ndiyo. Alinisaidia hata kunichukua na kunipeleka hospitalini. Unakumbuka wewe ulinifukuza kwako, ukanirudisha kwa mama. Mama naye kesho yake asubuhi akanifukuza kwake, tena baada ya kuniambia maneno machungu kweli!”

“Nikawa sina pakwenda, natapika tu. Nikatafuta hoteli, ndipo Pius akanitafuta tena. Nikamwambia nipo hotelini, hali yangu sio nzuri. Wewe umeniacha na mama amenifukuza. Ndipo akaja pale hotelini, kweli akanikuta sina hata nguvu, nina hali mbaya! Akanisaidia na kunipeleka hospitalini. Pius amekuwa msaada sana kwangu na Ayan. Alikuwa hachoki! Hata wengine walipokuwa wamenitenga, alikuwa akinisaidia bila kuhesabu.” Mina akaendelea kumwaga sifa za shemeji yake, Andy akimsikiliza tu kwa makini sana.

Mina akaendelea asijue anaibua mengi ndani ya Andy. “Pius anajali Andy! Anajali sana. Katika ndugu zako wote, angalau Pius ndio hata baba alikuwa akimwamini akimtuma atupe msaada, atafanya kwa moyo na haraka.”

“Baada ya wewe kuniacha, ukanitoa kwako bila hata pesa ukawa umeniandikisha kuwa nimekubali kuondoka kwako na kuanza maisha yangu, nilijua kabisa ni njia ya kunibana ili nisipate kitu Andy. Nilielewa. Ila nikaondoka nikijiambia Mungu atanisaidia tu.”

“Sasa kipindi hicho sina kitu na sina watu, na hata wakati umenioa lakini upo busy na kazi, alinisaidia sana mimi na Ayan. Katika uzima na maradhi, bila kuchoka. Alikuwa akisikia Ayan anaumwa tu, au mimi, anaacha shuguli zake, anakuja kutusaidia. Mchana na usiku huku akinitia moyo. Alihangaika na mimi bila kuchoka. Nakiri kabisa, bila yeye, nisingekuwa hapa nilipo.” Andy kimya. Mina akaaga na kuondoka, Andy kimya.

Andy Asaka Ukweli.

Kwa Paul.

Alikaa hapo akifikiria. Akaangalia muda wa alipo Paul mdogo wake nchini India, akagundua kwao palisha pambazuka. Akampigia. Baada ya salamu, Andy akaenda moja kwa moja kwenye swali. “Uliponiambia niongeze umakini na nifungue macho, ulimaanisha nini?” “Mpaka leo bado hujatoka hapo Andy!” Paul akashangaa sana. “Kwa maana nyingine mambo ya familia yamekushinda kabisa Andy! Au nikuulize Andy, wewe umejiapia hizo juhudi zako ni za kazini tu, mengine unaachana nayo?” Paul akauliza kwa hasira na kushangaa sana mpaka Andy akawa anamsikia kwenye sauti yake.

Kwa kuwa alikuwa amekasirika, na alishapandisha jazba Andy akajua ataongea tu. “Wewe unamuacha mtoto kama Mina yule, pale jijini, anatunzwa na wengine! Mimi mwenyewe nilikuwa nikimtamani huyo mkeo ila tu kwa kuwa ni shemeji, nikaamua kukaa naye mbali. Hata alipokuwa akilia shida, ilikuwa ni afadhali nikamtoe mama kazini, niende naye nikamwangalie wakati mgonjwa ili nisije shawishika, nikashindwa kujizuia. Wewe uliamini vipi watu kwa mwanamke kama Mina?” Paul akamleta karibu.

“Yule mtoto ni mjamzito hata hajui! Yaani anamwambia baba yake mkwe dalili zote za mimba, yeye mwenyewe HAJUI kama ni mimba! Kila mtu akabaki ameduaa. Anajieleza hana habari! Lakini mimi nikajiuliza pale na baadaye, hata mama nikamwambia. Huyu Mina kama angekuwa amelala na mwanaume nje, angeficha. Ni kama na yeye ule ujauzito alikuwa haujui!”

“Nikamwambia mama, atulie, asiende kasi. Mama na baba ni watu wazima Andy. Ndio maana unaona linapokuja swala la Mina, wananyamaza kimya kabisa. Jiulize kwa nini ni kwa Mina tu, sio Raza au tuseme Devi?” Kimya. Akaona ajijibu mwenyewe. “Ni kwa kuwa wameishi na hao wakwe zao wote watatu, wanawajua. Linapofika swala la Mina, baba anapoa kabisa. Ameusoma moyo wa mkeo au aliyekuwa mkeo, wameshamjua.” Paul akaendelea.

“Siku ile Paulina aliporudi nakusema amemfungia Mina kwa kuwa amemkuta ni mjamzito, na vile baba anavyompenda Paulina na kumuunga mkono katika kila kitu, lakini siku ile baba hakuongea neno hata moja! Akasimama na kuondoka kabisa. Unafikiri ni kwa nini?” Kimya.

“Mkeo yule muwazi Andy! Anasomeka kama kitabu cha kiswahili kwa wazawa na akiongea jambo hafichi. Kama hujamjua, basi wenzako wote wanajua. Hata mama alishasema. Mina sio muongo na wala si mnafiki. Hajui kuficha jambo lolote. Natamani ungekuwepo siku akielezea jinsi anavyojisikia! Ungejua hata yeye hajui kitu. Tena anamweleza baba! Yaani baba yake mkwe, sisi tukimsikiliza.” Paul akaendelea kwa jazba.

“Wenzako wote pale wana watoto wa kike. Hilo moja. Unajua wazi Raza na Paulina hilo linawakera kuona Mina amefika tu na kuzaa mtoto wa kiume ambaye baba anamtambua kama Ruhinda wake, MRITHI! Mama alimlaumu sana baba, akamwambia anaanzisha chuki kati yao. Lakini baba akasema, hata asiposema, ni kweli. Ayan ndiye atabaki akibeba jina la Ruhinda miaka 50 ijayo ambapo wengi wetu hatutakuwepo. Hilo ni jingine.” Paul akaendelea.

“Wewe unajua kabisa Paulina ndiye kipenzi cha baba. Paulina hajui upendo mkubwa wa mtu mwingine isipokuwa wa baba. Leo unamuacha Mina anaingilia mapenzi yake! Baba amehamisha kujali kwa Paulina, anampenda Mina na mtoto wake! Baba, namaanisha mzee Ruhinda vile alivyo, niwakuacha mikutano nje ya nchi sababu yakukaa na Ayan! Hajawahi kumfanyia hivyo hata mtoto wake wa kumzaa mwenyewe, leo anakaa ofisini kwake na kuzunguka na Ayan! Anampiga picha Ayan amekaa kwenye kiti chake ofisini na kuitundika nyumbani kwake, sebuleni!”

“Fikiria Andy. Baba ndio anakwenda kuchapisha picha studio! Tena kwa mjukuu mmoja tu, aliyekuja juzi tu hapa wakati baba alishakuwa na wajukuu wengine wanne! Mzee Ruhinda anatangaza hataki kumuona Ayan kwenye nyumba ya mtu mwingine yeyote isipokuwa pale kwake Msasani! Anayemtaka Ayan, amfuate pale kwake! Hayo anawaambia watu, na yeye wakati mwingine anatoka kazini siku za kazi, anakuja kukaa naye pale nyumbani kwako ili mkeo aende shule! Kweli Andy?”

“Wewe unafikiri watu wengine, au wazazi wa watoto wengine, zaidi mama zao, vile unavyowajua wale wanawake wawili walivyo wakorofi, watakuwa na mahusiano gani na mkeo unayemuacha peke yake mchana na usiku?” Andy kimya.

“Sijui bwana Andy! Labda kwa kuwa mimi sijaoa sijui mambo ya ndoa, lakini acha nikwambie ukweli Andy, umecheza sana chini ya kiwango. Ni kama uliyemtupa mbuzi wako aliyenona, katikati ya simba. Unanunua alumasi, unakwenda kumvalisha nguruwe! Halafu unamkabidhi huyo nguruwe mwenye alumasi kwa mwenye bucha! Unafikiri watamfanyaje huyo nguruwe kama si kumchinja na kuficha hiyo alumasi?” Paul akazungumza naye kwa mafumbo, lakini Andy akawa ameelewa.

“Yaani wewe Andy, Paulina! Yaani Lina ndio anakupa muongozo WAKUMUACHA Mina, mwanamke ambaye hajawahi hata kumkubali kwenye ile familia! Yeye ndio unakubali akusaidie kumuacha mkeo! Kweli Andy?! Hata kama ni kuamini watu, Paulina! Yeye mwenyewe ndoa yake unaijua. Ni vile tu amepata mwanaume muungwana. Tokea lini yeye akawa anajua mambo ya ndoa? Kutwa yupo ofisini na safarini. Nyumba yake chafu. Tukienda kwake mama yake anatangulia kwenda kumsaidia kusafisha kwanza ili wageni ndio twende na kuweza hata kukaa, na hilo kila mtu analijua. Hajiwezi kwenye mambo ya nyumbani isipokuwa kazini tu. Leo ndio na wewe unamsikiliza! Au na wewe upo kama yeye! KAZI kwanza mambo ya familia baadaye?” Paul hakumuacha.

“Kuna kipindi mimi mpaka nikajiuliza ni kwa nini ulioa kama haupo tayari kutulia na familia, Andy?! Amebaki Pius anayejua ku balance mambo yake mengi na mazito, anazungukia nyumba zenu pia wakati nyinyi akili zenu mmeweka sehemu moja tu! Akiitwa Paulina shuleni kwa watoto wake, anampigia simu baba, baba anamtupa Pius. Mtu mkubwa na mzito mwenye madaraka mazito kuliko sisi wote! Eti ndio akaweke sawa mambo ya watoto wa Paulina shuleni, eti yeye Paulina anavikao vya muhimu!”

“Na mkeo naye akiumwa, au mtoto wako, Pius huyohuyo ndio aache majukumu yake, akahangaike na mkeo na mtoto wako kuwakimbiza hospitalini, kuwapa dawa na ahakikishe kuna chakula kwenye majumba yenu! Nyinyi mnahangaika na viofisi vinavyowalipa mshahara kama marupurupu ya Pius tu! Sasa wewe jiulize Pius anawezaje, halafu wewe na Paulina mnashindwa vipi!”

“Ushamsikia Raza akimlalamikia mumewe au anahangaika na familia yake? Maneno yote yale ya Raza na gubu lake, likifika swala la Pius anafunga mdomo kabisa, kwa jinsi Pius alivyoweza kuweka sawa nyumba yake! Watoto wa Pius wenyewe umeona jinsi wanavyompenda baba yao kuliko mama yao! Siku zote hutawasikia wakimlalamikia baba yao ila mama yao.”

“Mwanao mwenyewe ana mahusiano mazuri na Pius kuliko hata wewe baba mtu! Ndio ujue unakosea pakubwa sana Andy. Haya ninayokwambia hapa, si mama wala baba wanaweza kukwambia, ila mimi nakwambia, fungua MACHO, kama bado kujachelewa. Maana unaweza kukuta sasa hivi kuna amani usione mengi, kwa kuwa TATIZO lao, Mina, ameondoka. Amewapisha kwenye maisha yao. Sasa wewe si mtu mzima? Kaa chini na utafakari kwa makini sana. Jiulize na kuhesabu nani ANAYE NUFAIKA sasa hivi na kushindwa kwako kumtunza msichana kama Mina? Kushindwa kwako wewe, ujue kuna anayenufaika sasa hivi. Nani na kivipi? Akili kichwani kaka. Kwa heri. ” Paul akakata simu, akamuacha Andy usingizi umepaa.

~~~~~~~~~~~~~~

Kushindwa kwake Andy, kuna anayenufaika. Nani na kivipi? Swali ameachiwa na mdogo wake. Dr. Ruhinda.

Inaendelea….


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment