![]() |
“Yapo mengi. Wananiletea kutokana na ninavyohitaji.
Tena wakati mwingine akikosa wateja, ananipunguzia bei ili nichukue mengi. Kwa
hiyo nagandisha kwenye friji, nakuwa nampashia tu huyu. Kwa hiyo maziwa yapo.”
Mina akamuwekea mtoto wake maziwa, akachukua ile chupa na kwenda kujilaza
kitandani kwa mama yake.
“Njoo mama.” Ayan akamuita mama yake. Mina akaenda,
akajilaza kwenye mto ili mwanae aweze kumnusa huku anakunywa hayo
maziwa. Na kweli akamsogelea mama yake akaanza kumnusa huku anavuta maziwa
yake. Andy na Mina wakacheka. “Ujue umekuwa mkubwa wewe Ayan!” Ayan akacheka na
chupa mdomoni. Akatulia.
~~~~~~~~~~~~~~
“Ile nyumba ni kubwa kama ile tuliyokuwa tukijenga
Kigamboni.” “Hivi ulimaliza? Maana nakumbuka ilibaki kidogo tu kuisha.” “Ni
kama imeisha. Bado kidogo sana. Nilihamisha nguvu kwenye hii ya Dodoma. Kuna
vitu sikuvipenda nilipo inunua. Nikabomoa na kurekebisha. Ilivyo sasa
hivi ni afadhali kwa kuwa haikuwa ramani yangu, sio mbaya.” “Hongera Andy, unajitahidi
sana.” Andy akatulia kidogo.
Kisha akaendelea. “Nilichotaka kusema ni hivi, pale
unaweza kabisa kupata sehemu ya kuishi.” Mina akawa kama amepigwa na butwaa.
“Hata kama tutakuwa na msichana wa kazi, bado utapata nafasi yako tulivu bila
shida.” Mina kimya akishindwa ajibu nini.
“Kama unahofia
uhuru wako, pia hakuna atakayekubana, ila nisingependa kumuona mwenzio pale. Hilo sitaruhusu. Ila kama ni wewe tu,
haitakuwa na shida.” Andy akaweka msisitizo kwa jazba kidogo baada ya kuona
Mina hajibu, akijua anamkatalia.
“Au unaweza kupaacha hapa ikawa ni sehemu yenu yakukutania.
Ukitaka, unaweza kuishi kule na sisi, na ukawa ukirudi hapa.” Mina akaumia
sana. “Sina maisha mengine ninayoishi zaidi ya haya Andy. Hivi unavyoniona
ninaishi hapa na Ayan ndio hivyo hivyo. Hakuna mwanaume anayeingia
hapa mchana wala usiku. Ni wewe tu ndiye mwanaume pekee unayeingia hapa
nakulala. Na sikudanganyi. Hakuna anayepajua hapa isipokuwa wewe na
Ayan. Hata Ron pia hajui nilipo.” “Basi kama kinachokuweka hapa ni unafuu
wa maisha, twende ukaishi na sisi Dodoma.” Mina akatulia tena.
“Au mpaka ushauriane na mwenzio?” Andy akaanza
tena. “Hakuna mwenzangu
Andy! Nipo kama hivi. Lakini nafikiria sasa hivi nipo peke yangu. Baada ya muda
nitajifungua, itakuaje na mtoto?” “Mimi na wewe tulikuwa na mipango
ya miaka na miaka. Nilikupigia simu siku ile jumamosi asubuhi, tulikuwa na
mipango ya kwenda mapumzikoni mara nitakaporudi nchini. Ilifanikiwa?”
Mina kimya.
“Sidhani kama sisi mipango ya baadaye
imetusaidia sana. Kinachowezekana sasa hivi, naona tukifanye tu.
Baadaye itakuja na itajijibu.” “Sawa.” Mina akakubali akijua Andy anakaribia
kupandisha hasira. “Kwa hiyo umekubali kuhamia Dodoma na sisi?”
“Ndiyo, lakini nafikiri nitawafuata baadaye.” “Mpaka uage kwanza?!” Andy
akauliza kwa hasira.
“Sina mtu ninayewasiliana naye isipokuwa wewe
Andy! Ila nina kliniki siku ya jumatano ijayo. Kuna jinsi najisikia, nataka
nikienda kliniki nimuulize daktari.” “Nani amekwambia Dodoma hakuna
madaktari na huwezi kuanza kliniki huko?” Andy akauliza tena.
“Unakumbuka ulinifukuza kwako nikiwa natapika
sana? Sasa huyu daktari nilianza naye muda mrefu, naona kama ananipatia
Andy! Ananisaidia sana. Nilikonda kupita kiasi, wakasema sio vizuri
mimba inakuwa, halafu mimi napunguza uzito na si kuongezeka. Ndio
akanipa dawa na ushauri ambao nimeona unanisaidia. Nataka niende
angalau nizungumze naye na nimwambie hivi ninavyojisikia. Wanipime, anishauri
dawa na ndipo nimwambie kuwa ninahama, halafu nimuombe kama anaweza
kunihamishia kwa daktari mwingine mzuri kama yeye huko Dodoma.” Kimya.
“Umenielewa Andy?” Mina akauliza taratibu. “Sasa kama
unaumwa sasa hivi, kwa nini tusiende kwa daktari tukajua kama kuna tatizo
au la! Kuliko kusubiri mpaka jumatano ijayo!?” “Nahisi pia inaweza ikawa sio
tatizo kubwa labda mabadiliko tu ya mwili.” “Wewe acha daktari akatuambie huko
huko.” “Na kliniki?” Andy akasimama kwa hasira. “Mbona kama unaweka vipingamizi
tu!?” Akagomba, Ayan akashituka. Akatoa shingo kwa mama yake akamwangalia baba
yake.
“Naomba ukae Andy, usikasirike.” “Naona kama huoni
ushauri wangu ni wa maana! Huoni kama upo umuhimu wa wazo langu! Unang’ang’ania
daktari mmoja tu! Kwani ndiye huyo huyo aliyekuzalisha Ayan? Mbona Ayan
alizaliwa vizuri tu na daktari hakuwa huyo? Au kuna kitu kingine ambacho mimi sikifahamu?”
“Unataka tuondoke hapa lini?” Mina akaona ayafanye yaishe.
“Hata leo.” Mina akashangaa. “Usiku huu!” “Ndio
maana nimekuuliza unataka kumuaga nani?” “Naomba ukae Andy. Najua unahasira,
na mimi sikulaumu. Lakini naomba utulie tuzungumze.” Andy akabaki amesimama
kwa muda, kisha akarudi kukaa.
“Kwa kuwa nitakuwa Dodoma kwa muda. Pengine mpaka muda
wa kujifungua ukifika ndipo nitakapo rudi huku kuja kujifungua, na pengine nitakaa
kidogo mpaka mtoto aelewe muda wake wa kulala. Ili usiku asijekuwa usumbufu
kwa wengine. Kwa hiyo nilazima hapa niache mazingira mazuri yakueleweka.”
Mina akaendelea.
“Naomba tufanye hivi. Nipe siku ya kesho ya kumuweka
sawa huyu mama, nimwambie nitakuwa nikirudi hapa, asije akaingiwa tamaa,
akapakodisha kwa mtu mwingine ili ajipatie pesa. Halafu nimtafute na
daktari wangu. Nizungumze naye kuwa nitaondoka, lakini karibu na kujifungua nitarudi
kwake. Kisha niwafuate Dodoma baada ya kuweka mambo yangu sawa. Na sitachelewa.”
“Na kingine, naomba usiwe unasafiri usiku Andy!
Humo barabarani unakutana na madereva wengine usiku wamelewa au kuchoka.
Wanaweza kukusababishia ajali. Kama unafanya safari zakuendesha
mwenyewe, naomba iwe mchana Andy. Ni sawa?” Kimya. Mina akajua anataka
kufikiria. Akaona anyamaze.
“Mama! Njoo nikwambie.” Ayan akamuita taratibu, Andy
akimsikia. Mina akamgeukia. “Mwambie dad wewe unataka kukaa na mimi tu. Tubaki wote, asinichukue.” Mina akamuhurumia. “Hata hivyo mimi nataka niwe na wewe
Ayan. Ila lazima nitibiwe mwanangu, halafu nitakufuata.” “Kwa nini usitibiwe
hapa na mimi? Mimi nitakuwa nakupa maji ya kunywa.” Mina akamuhurumia
sana Ayan mpaka akaanza kulia. Akajua anaogopa labda baba yake atakwenda
kumuacha kwa ndugu.
“Naomba twende hospitalini sasa hivi Mina. Najua
hospitali nzuri tu hapa. Twende ukapimwe kila kitu kwanza, tujue unatatizo
gani.” Mina hakubisha. “Nashukuru Andy. Asante.”
“Karibu.” Akajibu ila safari hii akisikika ametulia sio kwa hasira tena.
“Unaenda na mimi, mama?” “Nakwenda kuvaa, nakuja sasa hivi Ayan. Nisubiri.”
“Nakusubiria mama. Usiniache. Twende wote.” “Mama anakuja Ayan. Njoo
nikubadilishe uvae nguo nzito kidogo. Kuna baridi nje.” Ayan akashuka kitandani
kwenda kwa baba yake, na Mina akaenda kujiandaa.
~~~~~~~~~~~~~~
Walifika hospitalini, wakaingia wote kwa daktari. Kwa
kuwa alikuwa daktari mgeni, ikabidi Mina ajieleze na aina ya dawa alizopewa
atumie na vile anavyojisikia kwa wakati ule. Akaandikiwa vipimo, wakatoka.
Alipokuwa anakwenda kutolewa damu, akafanya makusudi kumpa Andy simu
yake amshikie. Haikuwa na namba ya siri, kwa hiyo alijua Andy ataweza
kuingia popote na kujiridhisha kuwa hana mwanaume mwingine.
Akaondoka nakumuacha Andy na Ayan wakimsubiria. Bila
kupoteza muda Andy akaanza kupekuwa
simu ya Mina. Akaingia kulia na kushoto. Juu chini, akakuta namba za watu wote
na wengine anao wafahamu hata yeye, lakini akakuta jumbe zake tu. Hilo likamtuliza
kidogo.
Huwezi ukaishi na Mina kama mpenzi ukamkinahi huyoo
mtoto! Hapendi ugomvi, amejawa upendo na kujali kwa aina yake.
Andy alishakuwa na hamu naye, ila wivu wa mume mwenzie ndio
ulikuwa ukimsumbua akidhani mwenzie anafaidi kuliko yeye. Akaona ambane
mpaka arudi naye Dodoma.
“Pole.” Mina alitoka amejishikilia damu isitoke sehemu
aliyotolewa damu. “Pole mama.” Ayan naye akaiga na kusimama akimfuata mama
yake. “Asante. Wamenitoa damu nyingi!” Mina akakaa na mwanae akamuegemea. “Ndio
vizuri tujue tatizo ni nini.” Ayan akambusu mama yake kama kumkumbushia
na yeye yupo. Mina akamwangalia na kumshika vizuri.
“Nimekuta namba ya daktari wako humu kwenye simu yako,
nimejaribu kuwapigia, inaonekana hata kesho anakuwa na kliniki sehemu nyingine.
Tunaweza kwenda huko ukazungumze naye kabla hatujaondoka.” “Sawa.” Mina
akakubali bila swali lakini akacheka moyoni akajua Andy amepekua simu yake vilivyo.
Vipimo vilionyesha hana ugonjwa wowote. Akashauriwa
apate muda wa mapumziko tu na anywe maji yakutosha. Andy akalipia hapo,
wakaondoka kurudi nyumbani kwa Mina. Njiani Mina akaona ashukuru. “Nashukuru
Andy. Asante. Angalau sasa hivi nitakuwa sina hofu ya ugonjwa.”
“Karibu. Naomba jaribu kuwasiliana na mwenye nyumba wako. Bado nimapema. Kama
bado hajalala, ukazungumze naye.” Mina akabaki akijifikiria.
Andy akamgeukia. Akajua ataanza kugomba tena.
“Kwani kesho unataka tuondoke saa ngapi?” Ikabidi tu aulize. “Mapema tu.
Tukitoka kwenda kukutana na huyo daktari wako, haturudi tena hapa, tunaelekea
Dodoma, ili nisiwe naendesha usiku.” Mina akacheka na kuinama, maana Andy aliongea
akimnukuu yeye.
“Au kuna mtu mwingine nilazima umuage?”
“Hapana. Naomba simu nimpigie huyo mama.” Andy akamtolea simu yake mfukoni, maana
alibaki nayo tokea alipomuachia kule hospitalini, akamkabidhi. Mina akazungumza
na huyo mama, akamkaribisha nyumbani kwake.
Andy alimshusha nyumba ya mbele, akaingia kwenda
kuzungumza na huyo mama. Alikuwa muungwana, wala hakuhitaji maelezo
mengi akawa amemuelewa kabisa. Hapakuwa na shida. Ila Mina alimwambia
atakuwa akirudi mara kwa mara mpaka muda wa kujifungua ufike. Wakakubaliana
na akamruhusu aondoke na funguo zake ila akamuomba amuachie moja ili
kukitokea chochote cha hatari humo ndani kwake akiwa hayupo, basi aweze kuingia
na kusaidia. Hilo halikuwa na tatizo, akamuahidi kumpa kabla hajaondoka.
Andy arudi na Mina Dodoma.
Mina aliweka kila kitu sawa ndipo safari ya kuelekea
Dodoma ikaanza. Alishangaa vile Andy alivyomtaka abebe vitu vyake vyote hasa
nguo. Kila Mina alipomwambia labda abakishe hata baadhi ya vitu, zaidi vya
mtoto mchanga ambavyo alikuwa amemnunulia tayari akijiandaa ili
akijifungua asipate shida, lakini alikuwa akilazimishia kwa ukali
kuwa abebe vyote, kila kitu, kwa nini anakataa anakuwa ni mtu ambaye
kama hana uhakika na maamuzi yake. Kama anayekwenda kujaribisha
ili vikishindikana akimbie. Baada ya ubishi wa muda, Mina akaona
akusanye kila kitu kasoro vifaa. Wakajaza hilo gari. Vitu vya Mina na wanae, ndipo
wakondoka.
Hata safari ya kwenda kumuona daktari wake wa kliniki nayo
ikaonekana ni tatizo. Andy akawa mkali kuwa ni kama Mina anataka kwenda kuonana
naye tu. Hana tatizo lolote lile. Akitaka ampigie simu amuage wakiwa
njiani. Sio lazima kwenda kuiona sura yake huyo daktari. “Wapo mamilioni
ya wakina mama hapa duniani. Wanazaa bila shida yeyote ile na
hawazalishwi na huyo daktari wako.” “Basi Andy. Naona hiyo siku ya
kujifungua ikifika nitajua chakufanya.” Mina akaona yaishe. Andy hakumjibu
akaendelea kukanyaga mafuta wakiondoka mkoani Iringa.
Andy alikuwa akiendesha mwendo wa kawaida tu. Mwangalifu
barabarani mpaka abiria wake wakalala. Mina aliomba wasimame mara mbili tu
njiani ili ajisaidie. Baada ya kama masaa manne na nusu wakawa wameshawasili
Dodoma. Mina akakaa sawa. “Hapa ndio Dodoma, Andy?” “Tumeianza kama dakika 10
zilizopita.” Macho yakawa nje akiangalia jiji kuu la Tanzania. Hakuwahi
kufika.
Andy akaendesha mpaka nyumbani kwake. Mina akashangaa
nyumba inafanana kama ya wazazi wake. “Ulichukua ramani ya kwa wazazi?”
“Kidogo. Napenda pale nje kwao palivyo. Hata huko nyuma utapaona, panafanana
kasoro hii sio gorofa.” “Ila pazuri Andy. Hongera.” “Asante.” Andy
akamshusha Ayan.
“Nisubirini nichukue baadhi ya mizigo tufungue mlango.”
“Unaishi peke yako?” “Yupo kijana anaishi nje, aliniahidi ataniletea msichana
wa kazi nikiwa tayari. Ila nahisi ni mkewe, ila anaogopa kuniambia!”
Mina akacheka wakawa wanamfuata kwa nyuma.
Ndani palikuwa pasafi sana. Hakushangaa, Andy ni msafi
na anapenda kila kitu kikae sehemu yake. Mina na mwanae wakakaa hapo
sebuleni kama wageni. Andy akaanza kuingiza mizigo. Wakamuona anaingiza ndani
kabisa. Akafanya hivyo mizigo yote mpaka akamaliza. “Njooni huku niwaonyeshe
vyumba vyenu.” Wakaanza cha Ayan. Kikawa kweli cha mtoto wa kiume kama kile
alichokuwa amekitengeneza kule cha Kigamboni. Wakamuacha Ayan chumbani kwake akiangalia na
kupanga michezo yake, aliyokuja nayo na aliyoikuta hapo.
Ndipo akampeleka Mina kwenye chumba chake. Hapakuwa
mbali na hapo kwa Ayan. Kilikuwa kikubwa na kitanda kizuri tu kama palipokuwa
pameandaliwa maalumu au kama kuna mtu anaishi hapo. “Nani alikuwa anatumia hiki
chumba?” “Hakuna! Kwani vipi?” “Kimekaa kama vile kilikuwa kikitumiwa na
mtu!” “Sijawahi kuingiza mwanamke humu ndani Mina, kama huo ndio wasiwasi
wako.” Mina hakujibu, akaelekea upande mwingine wa hicho chumba.
“Muulize huyo kijana hapo nje kama ameshawahi ona
msichana anaingia humu ndani. Hata mara moja. Na Mungu wangu ni shahidi.”
“Nashukuru kunikaribisha hapa Andy. Asante.” Mina akafungua masanduku yake
nakuanza kutoa vitu vyake akiweka kitandani.
“Unataka nikusaidie ili upumzike?” “Hapana, nipo tu
sawa.” Andy akabaki amesimama. “Sasa unafikiri huyo msichana tumuagize lini?
Maana nilimwambia huyu kijana tutazungumza tukirudi. Na nimeona
ameshasogea mlangoni. Aliniambia huyo msichana ni mzuri sana, hatasumbua.
Na nikiangalia, na ushauri wa jana wa daktari, ni kweli unahitaji kupumzika. Tutahitaji
msaada.” Kutokana na alivyoongea, Mina
akajua ujio wa Andy Iringa, ilikuwa ni kwenda kuwachukua aje aishi nao.
Haikuwa matembezi. “Mimi nakusikiliza wewe Andy.” “Basi nitamwambia
akamlete tu.” “Asante. Nashukuru Andy.” “Karibu.” Akatoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Maisha yakaanza hapo ndani, Mina asijue sasa kama
amekwenda hapo kulea au ndio kulelewa! Andy akawa busy akiwasaidia yeye na mtoto. Anaamka asubuhi, anapika.
Mina kabla hajatoka kitandani na yeye anapelekewa uji kama ujauzito wa Ayan.
Akimaliza akitaka kutoka, anakuta Ayan alishaogeshwa, msafi na ameshalishwa.
Akitaka kufanya chochote, anakataliwa. “Mimi
nipo likizo. Nikianza kazi utafanya tu. Sasa hivi pumzika.” Mina
akakumbuka alipokuwa Uswiz alimwambia akirudi atarudia yale maisha ya
mwanzoni. Andy akawa anajituma mpaka Mina akawa anamuonea huruma. Maisha
yakaendelea mpaka Mina akaanza kunenepa kwa kula na kulala tu.
Moyo Uliojeruhiwa!
“Nimebakisha siku kama tano likizo iishe. Nafikiria
kumpeleka Ayan mahali nilipaona wakati fulani nikiwa nafanya kazi hapa Dodoma.
Pazuri sana. Naamini Ayan atafurahia.” “Sawa.” Mina akaafiki. “Kwa hiyo na wewe
utaongozana na sisi?” Andy akauliza. “Yule msichana wa kazi anakuja
jumamosi hii. Labda wewe uende na mtoto, mimi nibaki nimsubirie ili
awepo hapa nyumbani mtu wa kumpokea na kumuelekeza mambo ya humu
ndani.” Mina akajibu vizuri tu akidhani ni wazo ambalo lingefurahiwa,
lakini ALIJUTA.
Andy akageuka akawa kama simba mpaka Mina akajiuliza
hiyo safari ilikuwa yake au ni ya mtoto! Andy alikuwa akigomba
akiingia na kutoka bila kutulia. “Sijajua natakiwa kufanya nini hapa duniani!
Najiona ni kama nimefanya kila kitu na bado haionekaniki kama
nimefanya! Nimejishusha na kufanya ambayo ninauhakika mwengine asingeweza,
lakini ni kama bado naonekana sina ninachokifanya!” Akaelekea jikoni,
Mina akasikia vyombo vinavunja. Na glasi zinapigizwa chini.
Akamchukua mtoto wake akaenda kumfungia chumbani.
“Hata kama ni dharau au hunioni mimi ni bora kuliko wanaume
wengine, lakini sio lazima kunifanyia hivyo kwa waziwazi. Unanivunjia heshima
kwa kiasi kikubwa sana. Umekubali kubeba mtoto wa mwanaume
mwingine ndani ya ndoa yetu!”
“Nimekubali tuishi pamoja tulee mtoto, napo
unaona shida kuongozana na mimi! Nina ubaya gani
unaoshindwa kuvumilia kwa siku chache tu kuonekana na mimi hadharani?”
Andy alitoka hapo akaendelea kugomba.
Alipoondoka tena kwa mara nyingine, Mina akakimbilia
chumbani kwake akaanza kuhema. Hakuwahi kuonana na Andy huyo simba. Andy ni mkimya, hakujua kama ni mkali wa kiasi kile.
Mlango ukafunguliwa. “Na ninajua tokea mwanzo nakuomba uje uishi
na mimi hapa Dodoma ulikuwa unatafuta sababu ya kuondoka humu
ndani ili ukawe huru huko. Sasa leo umeipata, ondoka tu.” Akafunga
mlango na kuondoka.
Mina alijua haitakuwa rahisi kuendelea kumuona na
tumbo kubwa akizunguka mle ndani na mtoto asiye wake. Akajua ni mengi
yanaendelea ndani mwake, asijue chakufanya. Bado ana hasira na ni
ngumu kukubaliana na hali ya kuwa yeye amebeba mimba si yake. Mina
akabaki ametulia chumbani kwake. Akasikia gari likitoka. Akajua ni yeye.
Kwa Pam&Mill
Alipoingia tu
ndani baada ya majibizano na Mill nje, Shema akamuwahi. “Naomba kufungua mifuko
mama. Ameniambia ameninunulia viatu. Halafu kuna chakula kinanukia hicho!”
Akambembeleza mama yake. “Hiyo nyama choma inanukia mpaka huku nje, mama Shema!
Tuonje.” Akacheka na kuingia ndani chumbani kwake na mwanae. Akakuta ameleta
kuku mzima wakuchoma, na nyama ya mbuzi nyingi haswa. Chips, ndizi za kukaanga
na fanta pineaple nne. Akawapakulia wenzie, akawapelekea akarudi ndani.
“Haya kula halafu ujaribishe.” Wakakaa na mama yake wakala.
Kuja kufungua
hiyo mizigo, Pam mwenyewe akapoa. Alimnunulia Shema viatu vizuri na japokuwa
Pam wa safari hii amechoka ila alijua ni vya bei. Alinunua 5 pairs.
Vyakuchezea mpira viwili, kanisani kimoja na shule viwili. Akamnunulia
jezi zakuchezea mpira tano. Nzuri sana. T-sheti na chupi zakutosha na
singilendi. Mfuko mwingine alimnunulia mwanae deodorant, mpaka akamshangaza
Pam. “Kamsikia mwanangu ananuka kwapa nini!” Akacheka moyoni ila kwa
shukurani. Maana asingeweza nunua vyote hivyo. Akaweka na lotion nzuri,
inanukia karibu na yeye. Hapo Pam akapotelea mawazoni mwanae akijaribu.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Siku ya jumamosi
hiyo alikuwa akifanya kazi nusu siku. Akatoka kwenda kazini akamuacha Shema
amelala. Kwenye majira ya saa tano akamuona amemsimamia kaunta kama mteja.
Alipohakikisha amemuona, akasogea pembeni kabisa. Akahudumia wateja, walikuwa
wengi akashindwa kutoka.
Akamuona anaenda
ofisini kwa bosi wake. Akakaa huko mpaka saa 6 mchana alipokuwa anamaliza na
kutoka. Akaenda kutoa epron yake na nyavu kichwani akabakiwa na kitambaa
alichokuwa amefunga. Akaenda kumuaga bosi wake, Mill akiwepo hapo. Akamchangamkia
kwelikweli. Lakini Pam hakutaka unafiki, akaondoka zake.
Mill
akamkimbilia. “Pam! Pam! Simama basi.” Hakusimama. Akamkimbilia mpaka akamfikia
na kwenda kusimama mbele yake. Ndio akasimama. “Mmeamka salama?” “Unanipotezea
muda. Ongea shida yako.” Mill akatingisha kichwa kwa masikitiko.
“Naondoka.” “Sawa Pam. Leo nimemuahidi Shema nitakuja kumchukua, twende
tukacheze mpira. Ni sawa?” “Isizidi saa 12 kamili jioni. Lasivyo utanisikia
kwenye vyombo vya habari.” “Pam!” “Hakika sikutanii.” “Kesho huyu mtoto
haendi shule. Nataka kumpeleka kwa kinyozi, kisha..” “12 kamili awe amerudi.
Usiniletee mchezo. Kama hutaki basi.” Akabaki akimwangalia.
“Wewe
unahangaika nini na mwanangu mmoja tu, wakati unao watoto kibao na bado utazaa!
Fujo zote hizi kwa Shema ni nini lakini?” “Ndiye mtoto peke yake ninaye
fanana naye hivi.” “Umekutana na tapeli mwenzio nini? Akakubambikizia
watoto wa tapeli mwenzenu!” Akamkejeli lakini Mill akaendelea.
“Halafu Shema
ndio mzaliwa wangu wa kwanza. Lazima niwekeze kwake.” Pam akampita na kuendelea
na safari yake.
“Viatu
vimemuenea vizuri?” Hapo akasimama. “Nakushukuru sana. Sana. Asante kwa
kila kitu ulichomnunulia. Shema anakua kama uyoga! Miguu na yenyewe
inakua kwa haraka, halafu mpira ndio kila kitu kwake. Nimepitia kipindi
kigumu hapo katikati. Nimejikuta nimeshindwa kumnunulia viatu kwa
haraka. Ila ni uhitaji aliokuwa nao kwa muda mrefu sana, ila sema
amejaliwa si mtoto mlalamishi. Ukimwambia asubiri,
atasubiri bila kukughasi. Kwa hiyo umeleta kwa wakati muafaka. Nakushukuru
sana.” Alizungumza kwa kutulia na unyenyekevu kama sio yeye, mpaka Mill akabaki
amepigwa na butwaa.
“Na nashukuru
kwa pesa pia. Jumatatu nitaenda kumalizia michango yote ninayodaiwa huko
shuleni kwao.” “Si tumesema anahama shule? Zile pesa ni zako wewe na mahitaji
yako binafsi!” “Lazima nimalizie deni, na awepo darasani wakati
ukihangaikia uhamisho.” “Uhamisho si wakuhangaikia, Pam. Wanataka pesa tu. Na
pesa ipo.” “Upande mmoja wa nafsi yangu una wasiwasi sana, lakini
upande mwingine naogopa nisije mnyima mwanangu nafasi nzuri. Lakini
ingekuwa vinginevyo, asingehama.” Akawa kama anayefikiria.
“Niambie
wasiwasi wako.” “Jana nimezidi kufikiria hilo swala. Shema hajasoma hizo
shule zenu za lugha zenu hizo. English anaiona kwenye somo tu.
Naona kama mtamchanganya huko! Anafanya vizuri sana shuleni. Leo
anakwenda kuanza upya wakati yupo darasa la nne! Hakika sina
amani. Au kwa nini asianze huko
sekondari?”
“Hapana Pam.
Mimi nipo nita…” “Sasa hivi ukiwa umesimama hapa ndio upo. Wazimu
wako ukikupanda, na tamaa zako zikikuwaka, utaondoka hapa,
umuache mwanangu njia panda. Huko sitaweza mlipia, na huku hawezi
kurudi. Asiee HAPANA. Nimekumbuka.” Hapo hasira zikarudi.
“Pam! Tafadhali
nisikilize.” “Hatahama shule ambayo mimi sina uwezo wa kumlipia.
Atasoma shule ya uwezo wangu, sio uwezo wako wewe tapeli.
Acha kutaka kumchanganya mwanangu. Kwanza ni katikati ya muhula. Unataka
kumchanganya tu.” “Mimi sitaondoka tena nchini. Na sidanga..” “Usinitanie
kabisa! Wewe maneno yako ni kama upepo. Hayana maana
kabisa. Acha kunipotezea muda.” Mill akaumia sana.
Akaondoka kurudi
kituoni. “Acha nikupe lifti mpaka nyumbani.” “Sina shida.” “Sasa si tunakwenda
nyumba moja?!” “Kwa sababu tofautitofauti. Wewe achana na mimi. Utamkuta Shema
yupo tayari. Kwanza alilala na viatu, nimemvua alivyopitiwa na usingizi. Nikimaanisha
anakusubiria. Sasa usimtapeli mwanangu kama ulivyozoea kutapeli
wengine.”
“Pam, nimekosa
mama. Nisamehe.” “Acha kunifanya mimi mtoto mdogo. Umekosa kwani ilikuwa bahati
mbaya? Wewe ni TAPELI tu Mill. Na mama Kenny anasema akikuona atakushauri.
Ukapige magoti kanisani, uombewe. Walikuwa wakikuheshimu sana
pale. Kenny alikuwa anakufuatilia mtandaoni, anasema alikuwa haamini
kama ni wewe! Wote wakaniambia upo kama baba yako. Huna huruma. Roho
zenu za kinyama. Hamjui kumfikiria mtu yeyote linapofika swala lenu.
Ni nyinyi tu. Kwanza sikuamini kama UMENITELEKEZA!”
“Maana
nilihangaika na tumbo langu! Shema ni mkubwa, ananilemea. Lakini nilikuwa sijali
wala sijikumbuki mimi, nakuhurumia wewe, kwa vile nilivyokuamini!
Sikujua kama wewe ni tapeli katili wa kiasi hicho! Nimefungwa jela, sina
hata wazo kama nimewekwa rumande, hofu yamgu kwako! Najiambia masikini
Mill atakua yupo matatizoni, baba hana, mama hana. Hakuna
atakayeona uzito wa kumtafuta huko, kujua kinachoendelea.”
“Yaani Sandra
anakuja kunipokonya gari kule rumande, mimi nashukuru Mungu. Maana yeye ndio
kama aliyenikumbusha kama ni mjamzito. Akili ilikuwa haipo kabisa, nipo jela,
ila akili ipo kwako tu, muda wote nakuhurumia. Wala pia sikuwa
nikijua kwa nini Sandra amenifunga! Sijifikirii mimi, hofu ipo kwako
muda wote!”
“Sasa
aliponiambia nimpe gari ndio atanitoa rumande na kufuta kesi, lasivyo nitazalia
jela, ndio nikagutuka sasa, kumbe mimi mjamzito! Na ndipo akili ikanijia
kumbe hapa shida ni wivu tu, kunirudisha chini! Aliniambia nikimpa gari
ndio atanitoa, sikutaka mengi, shida nitoke, nihamasishe watu wakutafute
huko, wajue kulikoni! Usaidiwe!”
“Nimetoka tu,
bila kupumzika akili ipo kwako nakuhurumia. Nina njaa, jua
kali, natafuta mtu anayeelewa mambo ya huko, basi usaidiwe. Simu yako, hapatikaniki
si mchana si usiku. Na mimi nilivyokuwa mjinga, eti nakupigia kila saa!
Sasa vile NILIVYOKUAMINI na yale maneno yako yaliyokuwa yamejaa hekima,
nisijue kama wewe ni TAPELI tu, ushamalizana na mimi, umehamia
kwa fala mwingine kama mimi, eti mimi nikazidi kuchanganyikiwa,
najihakikishia upo matatizoni kabisa.”
“Zunguka!
Zunguka! Zunguka na wewe. Kunywa hata maji naona najichelewesha, nawahi
kukuokoa. Hangaika! Hangaika na wewe, ndio nikasema japokuwa mama Kenny, hataki
undugu na nyinyi, labda yeye atanifungulia mlango maana wote uliowafundisha
kunikimbia, bwana walinitenda! Huko sitakwenda.”
“Basi, ndio
nikafika kwa mama Kenny. Namuelezea wasiwasi wangu juu yako kwamba kuna kitu
hakipo sawa, upo matatizoni, naomba msaada utafutwe, mama Kenny akanihurumia
sana yule mama. Akaniambia, Pam binti yangu, umetapeliwa. Mimi tena hee!
SIAMINI!”
“Akashika kazi
ya kunisimulia. Akaniambia yeye amekuza wanae pale ndani, akiona binti wadogo
kama mimi, wakifika pale na matumbo yao kwa baba yenu. Akasema
yaani vilevile kama mimi. Na mzee Mgini alikuwa akiwaambia, kama wanauhakika
ni wake, wakishusha mzigo, wawalete pale. Alikuwa akiwaambia hakatai
damu yake. Anasema nyumba ile ilijaa vilio vya wanawake, wa idadi
ya wale watoto.”
“Akaniambia mimi
si wa kwanza na wala nisidhani nitakua wa mwisho. Alisema na babu
yenu ni wale waliokuwa wameshika pesa nyingi kipindi cha nyuma wengine
hawana pesa. Pesa ilikuwepo mfukoni kwake, basi akaniambia alikuwa malaya
kama baba yenu na wale ndugu zako pale. Ndio akasema ilibidi yeye kufunga
na kuomba, na kupeleka wanae wakaombewe kabisa, kuwatenga na roho
za KWENU. Kwani bado nilikuwa namuamini! Mill anidanganye mimi!
HAIWEZEKANI. Wanamsingizia Mill.”
“Kumbe Kenny
ananiangalia tu, anajua siamini. Ndio akanisaidia. Akaniambia wewe ni mzima.
Huna tatizo. Na una mwanamke ana mimba ila yake ipo Instagram.
Akaniambia yupo huko anapost kila siku maendeleo ya mtoto na bwana wewe
upo. Mimi bado siamini. Mill si muongo jamani! Ndio
kuonyeshwa picha sasa.”
“Nikidhania mimi
nimebeba malaika, kumbe Marekani kuna uliyembebesha mungu mtu!
Bwana mwanamke alikuwa amependeza na tumbo lake! Tena analipiga picha tuputupu,
uchi halijafunikwa hata na nguo, na wewe bwana unaonekana upo tu!
Kwengine umelishika tumbo kabisa! Mimi tena hee!”
“Mama Kenny
akaniambia ila wewe umejiongeza. Pengine ulitaka kumuonyesha baba yako
wewe ni watofauti, ili uendelee kuchota mapesa yake. Ukamtapeli
utaoa. Ndio kumpeleka baba yako mpaka mlimali, kwenda kulipa mahari.
Akasema umeona mchezo mtamu, ndio umeendelea kujiongeza utapeli
wako wa kudanganya kama kuna ndoa. Ndio picha zenu sasa za harusi
na yule mwanamke wako, nikaonyeshwa. Baba ulipendeza wewe! Suti
ya nguvu, nyeusi imekukaa kitajiri kwelikweli! Na mashoga zako wakike na
wakiume walikuwepo!”
“Basi mimi pale
ndio akili ikanijia. Ndio maana na wenyewe wananifukuza makwao, na siwapati
kwenye simu! Kenny akanicheka, hana mbavu. Akaniambia sio kwamba siwapati
kwenye simu, ni kwamba umenifungia simu zangu. Nikawa kama mjinga
zaidi, SIELEWI. Mama Kenny akasema, nyinyi kina Mgini mkiondoka kwa
mwanamke, mnakua mmemalizana kabisa. Ashaona kwa wengi.”
“Ndio Kenny
akanisaidia kunihakikishia. Akachukua namba ileile niliyokuwa nayo
nikiwasiliana na wewe, sikupati. Akaniambia nikupigie na kukutumia
ujumbe palepale. Nikawaonyesha kuwa sikupati na jumbe zangu zote tiki
moja. Kenny hana mbavu. Akasema niangalie sasa simu yake.”
“Akakutumia
ujumbe, ‘vipi bro, upo mzima na familia huko?’ Palepale zikatokea tiki mbili. Gafla zikageuka za rangi ya bluu.
Akaniambia ushapokea na umesoma. Mimi tena hee! Bwana ulivyokuwa wewe! Palepale
ukamjibu, ‘huku kwema kabisa. Vipi na nyinyi?’ Pale
ndipo nikajirudisha kwenye kochi. Na kuhema.”
“Mama Kenny
akaniambia, nikatulie, nijilelee tu mtoto wangu. Habari yangu ilishakwisha
muda mrefu sana. Ile mahari waliyolipwa bibi na babu, ndio zawadi yangu.
Yule mama akanikarimu chakula, na maji, kisha kunitakia safari njema kwenye
maisha. Ndio hofu sasa!”
“Tumbo kubwa
zaidi ya urefu wangu na umri wake. Hospitalini wananiambia mtoto yupo kama wa
miezi tisa huko tumboni. Nazaaje? Sina kazi, sina familia, Mill aliyenitelekeza,
alishanitoa muda mrefu sana huko kwenye familia, na kila anayenifahamu.
Mama yangu alizaa, akapooza. Akaachwa. Uzuri wake yeye, alikuwa na
pakurudia. Mimi narudi kwa nani!? Hofu, silali.”
“Pressure.
Ndugu hawanitaki, sina pakwenda wala wakunisaidia. Ndio
nikamuomba mama yangu aje mjini haraka, nipo matatuzoni. Mama yangu yule mlemavu,
akaomba aletwe huku mjini vilevile. Nakwenda kituoni kumpokea, ndio anakutana
na tumbo lisilo na baba. Baba yupo Instagram na tumbo JINGINE.
Nikamueleza ukweli wote na kumuonyesha na picha zenu sasa.”
“Nikamwambia kwa
mara ya kwanza maishani, naogopa. Silali kwa hofu, nisije kufa
wakati wa kujifungua, mwanangu akatupwa tu kama mzigo au nikapatwa matatizo,
nitafanyaje nipo peke yangu! Basi, siku ya kwanza mama amefika hapa jijini, na
kulala na mimi, akaniwekea mkono usiku, kama kunikumbatia nilale ndio nikaweza
kufunga macho, na kunywa dawa, nikaweza kulala.”
“Ule ukweli
ukawa unaniingia taratibu. Kila nafsi ikitaka kukutetea, basi na mimi
nikawa follower wa Kisha Mgini huko Istagram. Bwana
mlikuwa mnawapambe nyinyi! Mashabiki kibao mpaka wa hukohuko kweni wana LIKE
na ku comment kwenye kila post za Kisha Mgini. Starehe
zenu na kina Mike na Kamila nchi tofauti tofauti! Mpo wenyewe na Kisha! Mimi
ninakazi ya kufuatilia tu ili kujikumbusha, na kukubali ukweli
kwamba, wewe upo MZIMAA, ila mimi ni gazeti ushamaliza kulisoma, umetupa
kama uchafu! Nikabakia kujiangalizia tu maisha yako na mwanamke
wako mtandaoni! Kumbe nazidi kujimaliza mwenyewe, pressure
haishuki.”
“Mwishoe yangu yakanishinda,
mwili ukalemewa, Shema nikazaa kabla ya siku zake. Mrembo Kisha yeye akawa
anazidi kushamiri na tumbo lake, na bwana wewe, upo nyuma yake
kila wakati! Picha za mtoto wenu huko tumboni nazo zikawa zinatumwa na
Kisha kila mkitoka kliniki! Mimi tena hee! Kumbe kuna wanaume wanapelekaga
wanawake zao kliniki! Kama kwenye movie! Halafu na yeye mtoto wa kiume! Mapenzi
mazito! Hakika siamini kama na YULE, naye ulimuacha!” Mill alikuwa
amebadilika sura, kama aliyekuwa amelemewa na mzigo hapo aliposimama. Kuushusha
hawezi! Kukaa hawezi! Na Pam naye alionekana lazima
amuweke sawa hapohapo kwenye jua kali.
“Sasa nisikilize
Mill. Baba yako aliwakusanya pale kama anayevundika maembe, akaacha
watoto wake hawana mbele wala nyuma. Wanakazi ya kupigana mchana
na usiku, nasikia wameuza mpaka madirisha kwenye zile nyumba alizowaachia.”
Mill akashituka sana.
“Sasa wewe
ukaona usirithi mali, urithi umalaya. Sasa Shema hatakuwa moja ya
watoto unaofikiria kuwakusanya halafu uje uwaache kama
alivyowafanyia baba yenu. Nitakuwa makini sana na wewe. Sasa
nikuone unakosea hata stepu moja. Hakika utaniona mchungu, kuliko
shubiri. Sikutanii juu ya Shema.”
“Na leo, saa 12 isipomkuta
pale ndani, jua ndio mwisho wa kumchukua, na nisije kukuona tena
pale. Kama unafikiri nakutania, au ni Pam yule wa wakati ule wakumlaghai,
basi nisimuone Shema saa 12 jioni. Huwezi kufuata mashariti yangu, muache.”
Pam akaondoka kabisa, Mill akabaki miguu imekufa ganzi. Bado amelemewa.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Ni Nini Kitaendelea
Kwenye Mioyo Hiyo Iliyojeruhiwa Kwa Wapenzi Hao Wa Love At First
Sight?
Inaendelea…
0 Comments:
Post a Comment