Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 31. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 31.

Wakati anapata usingizi usiku wa saa nne baada yakufanya kazi zake  kwenye kompyuta yake, akasikia hodi mlangoni. Mina akashituka. Alikuwa akilala kinyumba cha nje tu. Kila ilipokuwa ikifika saa kumi na mbili jioni alikuwa akifunga milango yote mpaka kigeti cha hapo nje mbele ya mlango wa kuingilia. Akachungulia dirishani. Akamuona Andy amembeba mtoto, wanatetemeka baridi.

“Ayan!” Akaanza kufungua mlango wa ndani kwa haraka. “Poleni.” Akatoka ili afungue geti dogo. Ayan akamwangalia. “Pole baba. Pole sana.” Mina akamwambia mwanae. Akafungua geti, akataka kumpokea, Andy akamkatalia. “Labda ukae naye. Usimbebe.” “Basi niwekee hapo kitandani nimfunike na mablangeti.” Andy akamuweka kitandani. Mina akamuona anatoka. Kumbe alikwenda kushusha mizigo kwenye taksii.

Akashusha masanduku makubwa mawili na dogo kidogo. Akafunga mlango. Mina hakujua kama anabaki au anaondoka. Akaona anyamaze. “Huyu ameingia baridi. Nimembandikia maji ya moto aoge, kisha nimpe maziwa.” “Naona na chakula pia. Hatujala.” “Sawa.” Mina alikuwa akichemsha maji kwa mashine. Kwa haraka yakachemka. Akamuogesha mtoto haraka, akampa maziwa wakati anapasha chakula moto.

Hakuwa hata na meza. “Unataka kuoga kwanza au kula kwanza?” “Utakuwa na nafasi ya mimi kulala usiku huu?” Mina hakuwa na vitanda viwili wala kochi. Akafikiria kwa haraka. “Hiki kitanda ni kikubwa Andy. Tulaleni wote kwa usiku huu, kesho tujipange upya. Kuna baridi sana huko nje, na ni usiku sana sasa. Jikaze tu tubanane.” “Asante.” Andy akashukuru na kusogea sehemu ya kuchemshia maji.

Mina anatayarisha chakula, Andy anajitayarishia maji ya kuoga. Akamuona amekuwa mwenyeji. Akajiwekea maji. Akamuomba taulo. Akampa safi kabisa. Akaelekea bafuni na begi lake. Baada ya muda akatoka, Mina akimlisha Ayan. “Anasinzia huyu!” “Tumekuwa na siku ndefu. Anahaki ya kuchoka.” Akajibu akisogea pale.

“Chakula kipo hapo.” Akajiwekea, akaanza kula, huku Mina akimlisha Ayan. “Jikaze ule Ayan. Ukishiba utalala vizuri.” Mina akaendelea kumbembeleza, mwishoe akaona ni heri ampe tu maziwa mengine. Akamuwekea chupa nyingine ya maziwa mdomoni, akamfunika. “Nitakuja Ayan. Lala.” Akamuona amefunga macho huku anakunywa hayo maziwa.

“Pole. Naona umeshika sahani. Sina meza, ila nitanunua.” “Nipo sawa tu. Nimeshamaliza. Asante.” “Basi nikupokee, na wewe ulale.” Andy akamkabidhi sahani, akarudi bafuni kusafisha meno, akarudi na kupanda kitandani. Akakuta Mina amemuwekea blangeti jingine.

“Nimefurahi Andy! Asante.” Mina akamuwahi na sauti yake ya kitoto, kabla hajalala. Andy hakujibu, lakini akajua amemsikia. Akaweka mambo sawa, akazima taa, akapanda kitandani na wageni wake, wakalala.

~~~~~~~~~~~~~~

Asubuhi baada ya kupata kifungua kinywa Andy akamwambia Mina aandike kila kitu anachohitaji hapo, pamoja na kitanda cha Ayan, akanunue. “Nitajitahidi kuwahi kuvileta mapema. Nina ondoka na ndege ya mchana.” Akajua ndio anaambiwa asimuhesabu hata kwa chakula cha mchana.

Kwa kuwa Mina anajua aina ya maisha yao watatu, akajua ni nini mtoto wake atahitaji. Akamwandikia kila kitu, akamkabidhi. Andy akatoka. Alirudi kwenye saa tano na kila kitu alichotumwa na Mina, akamsaidia kuweka sawa pale ndani. Akapanga vitu vya mtoto hapo hapo ndani. Akakaa.

 “Ukiwa na shida yeyote, naomba unitaarifu Mina. Nitarudi kwa haraka tu nikusaidie.” “Asante Andy. Nashukuru sana. Naamini tutakuwa sawa. Si eti Ayan?” Ayan akakubali. Andy akamuita amsogelee pale alipokuwa amekaa. Akamsogelea. Akamkumbatia na kumbusu. “Usimsumbue mama, Ayan. Chochote anachokwambia, usikilize. Sawa?” “Sawa.” Ayan akakubali. Andy akambusu tena kijana wake, akabaki kama anayefikiria, mwishoe akasimama.

“Hii pesa itakusaidia kwa matumizi ya hapa. Dawa zake zakumpaka huko kwenye mapele zipo kwenye sanduku lake pale, nilishampaka asubuhi.” “Sawa.” Akamkabidhi Mina ile pesa, akashukuru. Nakuondoka.

~~~~~~~~~~~~~~

Maisha ya Mina yakarudi kuwa na furaha haswa. Hiyo siku alijawa furaha kama amekabidhiwa ulimwengu. Yupo na mtoto wake! Hakuwa akiamini. Walishinda wakicheza magari, huku akimwangalia anavyopanga vitofali vyake wakicheka. Kwa asili Ayan alikuwa mtulivu sana, ila mama yake alijua jinsi yakumfanya acheke. Mpaka nyumba kubwa walijua Mina ana mgeni. Kwake kulijaa vicheko na fujo ndogo ndogo.

Usiku Andy akapiga simu, Mina akampa mtoto simu. Andy akashangaa Ayan ndio anapokea. Akamsalimia, na kuzungumza naye kidogo. “Dad amesema alifika salama.” Ayan akamwambia mama yake. Akajua ndio ujumbe wake yeye.

~~~~~~~~~~~~~~

Maisha yakaendelea. Baada ya siku 7, Andy akarudi na gari yake kubwa. Alifika hapo asubuhi kama kwenye saa mbili. Mina na mtoto wake walikuwa wamelala. Hakuwa amemwambia kama atafika, kama kumfumania vile! Lakini uzuri Mina alijituliza kulea mwanae. Akaamka kwenda kumfungulia. Akamkaribisha ndani. “Ayan bado amelala.” Akaongea kwa kunong’ona. Andy akamsogelea pale kitandani. Akabaki akimwangalia vile alivyo lala. Akamfunika tena vizuri. Mina akaanza kujitayarisha.

Anatoka bafuni kuoga, akamkuta Andy amelala kwenye kiti. “Andy!” Akamuita taratibu. “Panda kitandani ulale kidogo.” Bila hata kubisha, Andy na nguo zake akapanda kitandani. Akamfunika mablangeti mawili, hata dakika haikupita akamsikia akihema kama aliyelala.

Hakujua kama ndio aliendesha usiku kuchwa ndio anafika au alikuwa hotelini. Akaanza kuandaa kifungua kinywa. Saa nne na nusu mtoto akaamka. Akamlisha, mpaka akamaliza na kumuogesha, Andy amelala. Akapika chakula cha mchana, akamlisha mtoto, Andy bado amelala. Wakaamua na wao wapate usingizi wa mchana. Ayan akalala kitandani kwake. Wapi Mina alale! Akabaki akifikiria, mwishoe akaamua ajilaze pembeni kabisa hapo hapo kitandani. Wote wakalala.

Baada ya masaa mawili akaamka na kumkuta Andy akimwangalia. Mina akaona aibu. “Nilikuwa nakoroma?” Andy akacheka. “Pole. Nalala vibaya siku hizi!” “Hujakoroma bwana! Acha hujihami.” Mina akacheka na kujiweka sawa. “Unakula vizuri?” “Hivyo hivyo.” Mina akajibu pakawa kimya.

“Unafikiri utaweza kuendelea kuishi na Ayan kwa muda gani? Nikimaanisha kabla hujajifungua.” Mina akashituka sana. “Nilipata ile nafasi ya kazi Dodoma. Sasa hivi ninauhakika wa kutulia Dodoma tu. Nilinunua na nyumba kabisa. Muda huu nilipokuwa nimemuacha hapa Ayan, nilikuwa nikimalizia kununua vifaa vya ndani. Nimeridhika kuwa imekamilika. Niliulizia shule pale, naona wanazo nzuri tu. Ndio maana nauliza ili nijipange. Sitataka Ayan akaishi kwa mtu mwingine tena. Kama sio wewe, ni mimi.” Mina akabaki kimya kwa muda.

“Ukinipa mimi, nitatafuta mfanyakazi wakutusaidia kazi, na nitamuanzisha shule. Ni kweli anauelewa mzuri tu. Anafaa aanze shule.” Mina akajifuta machozi. “Natamani ingekuwa hapa Iringa Andy!” “Kwanza ni kwa nini ulichagua kuishi huku? Mbali sana na nyumbani!” “Mama alinifukuza pia. Halafu sikuwa na pesa yakutosha. Nilijua pale Dar nisingepaweza. Nyumba zakupanga ni gharama Andy, sikuwa najua!” Andy akacheka kidogo kama anayefikiria. Mina akajifuta machozi.

“Kweli! Si unajua pale kwa mama tulianza kuishi nikiwa mdogo sana? Kwa hiyo nilikuwa sijui maswala ya kodi. Nilipoanza kutafuta sehemu ya kuishi ndipo heshima ya lile jiji ikaongezeka. Nikajua sitapaweza.” “Hapa unalipa kiasi gani?” Andy akauliza. Akamtajia.

“Lakini kwa kuwa ni kama nilipamalizia ujenzi, sidaiwi kwa muda mrefu. Nafikiri hata miezi 7 ijayo. Nitapiga naye mahesabu, maana kila nikinunua kitu, tunaandikishana.” Kimya. “Ndio maana nasema ingekuwa Dodoma ni karibu na hapa, ningekuomba mimi hiyo nafasi ya kazi hapo nyumbani kwenu.” Andy akamwangalia.

Ningeweza Andy! Kumbuka mimi nawafahamu. Hutahitaji kunielekeza chochote. Najua nini unapenda, nini hupendi. Kwenye chakula hivyo hivyo. Na bado Ayan angepata nafasi ya kuwa karibu na sisi wote. Lakini ni Dodoma!” Mina akafikiria kidogo.

“Nikuombe kitu Andy?” “Nini?” “Namuona kama sasa hivi anakula vizuri. Ameanza kuchangamka na madonda yamekauka. Naomba niachie kwa muda mpaka kodi ya hapa iishe. Nitajaribu kuangalia sehemu ya kuishi Dodoma. Nikipata sehemu nafuu, nitahamia huko. Ili tuwe karibu.” Andy akafikiria.

“Tukichukulia miezi 7 tu ijayo kama ndio kodi yako inaisha hapa, inamaana ndani ya huo muda utakuwa umejifungua. Utakuwa na mtoto mdogo Mina. Utawezaje na watoto wawili wote wanakulilia wewe peke yako?” “Mimi ni mama yao Andy. Sihitaji kufundishwa nimpende yupi kwanza aje yupi. Sihitaji kukumbushwa Ayan anahitaji kula au kuoga. Nitajipanga vizuri tu, naomba usiwe na wasiwasi juu ya hilo na uwe na hakika katika hilo Andy. Ayan hatateseka sababu ya mdogo wake.” Andy akanyamaza.

“Naomba usiwe hata na shaka juu ya hilo Andy. Nakuhakikishia. Hakuna atakayemtunza Ayan vizuri kama mimi. Nimeishi na watu, nimeona. Na ubaya au uzuri Ayan ni mpole au mrahisi sana kuishi naye, kiasi ya kwamba nirahisi kumsahau au kumpuuza. Lakini hicho hakiwezi kutokea akiwa na mimi, Andy.” “Najua Mina. Hilo sina wasiwasi nalo. Ila wewe mwenyewe. Hutalemewa?” “Hata kidogo.” Mina akakaa kabisa ili kumshawishi.

“Naamini nitaweza Andy. Labda kwa siku zile nikiwa nakaribia kujifungua na baada. Ili nipone vizuri. Hapo nitakuomba msaada. Lakini wakati mwingine, naomba uwe na amani. Na nitajitahidi kutafuta makazi karibu na wewe ili uwe na uwezo wa kuja kumtembelea wakati wowote.” Andy akanyamaza.

“Andy?” “Nafikiria Mina!”  Akamuona anafunga macho kama anayesikilizia maumivu, Mina akaelewa. “Sikukusudia kukuharibia taratibu ya maisha Andy. Sikukusudia kukufedhehesha.” Akamuona anafuta machozi. Mina akajisikia vibaya sana. “Nilikuwa nahangaika Mina. Nilihangaika sana ili siku kama hii itukute pamoja, wote tupumzike. Naona juhudi zangu zimegonga mwamba!” Mina akaanza kulia na yeye. Alilia sana Mina.

Mpaka akatoka pale kitandani na kwenda maliwatoni. Kwa mara ya kwanza akatamani kama angekuwa na maelezo ya kumpa Andy, siku hiyo amueleze lakini hakuwa nayo. Ni mjamzito asiyejua ilikuwaje. Na alijua hakuna ambaye angemuamini. Ni Mina! Akaendelea kulia. Akasikia mlango unafunguliwa na kufungwa. Akajua anakwenda kukimbia kama kawaida yake mpaka atulie. Mina akatoka, akawa amekaa akifikiria. Ayan aliamka, akahamia kulala kitandani kwa mama yake. Akawa amemlalia huku anakunywa maziwa.

Andy akarudi anatokwa jasho kama amelowa mvua. Akajitayarishia maji, akaenda kuoga, akatoka. “Kuna kitu cha kula?” Mina akasimama kumuwekea kwenye sahani. Akampangia vizuri kwenye stuli aliyonunua mara baada ya Ayan kuhamia hapo, akamkaribisha na kurudi kukaa mbele, kitandani alipokuwa amemuacha Ayan.

Ayan akajirudisha kwa mama yake, akamlalia. “Umeshiba au unataka uji?” “Nataka uji.” Ayan akajibu. “Sema naomba bwana Ayan, vipi wewe!” Andy akaingilia. “Njoo basi ukae hapa na dad ule, au unataka nikulishe?” Akamuona Ayan anacheka. Akajua anamuogopa baba yake. “Njoo nikwambie mama.” Mina akacheka. Akaweka uji kwenye bakuli akarudi pale alipokuwa amejilaza Ayan.

“Nini?” Mina akamuuliza mwanae huku akicheka. “Mikono imechoka.” Ayan akamnong’oneza mama yake masikioni Mina akacheka sana. “Ayan wewe! Kunywa maziwa tu ndio mikono huwa haichoki, kingine chochote mikono inachoka! Aibu zako.” Ayan akacheka.

“Njoo ukae hapa ule Ayan. Mama amepika, sisi tunakula. Njoo ukae hapa.” Ayan akamwangalia mama yake, akarudisha macho kwa baba yake. Wakamuona anatoka kitandani taratibu kama anayesubiria mama yake amuokoe. “Njoo ukae hapa.” Baba yake akamuwekea msisitizo. Akaenda kukaa, Mina akampoozeshea uji akampa kwenye bakuli. “Usijimwagie.” Akamwambia kwa upendo akitamani amlishe tu. Akaanza kunywa taratibu huku akimwangalia mama yake. Pakawa kimya.

~~~~~~~~~~~~~~

“Nimepata wazo Andy, naamini itaturahisishia.” Andy akamwangalia. “Kwa sasa si upo likizo ya kuhama?” Andy kimya akimsikiliza. “Na kama nimekuelewa vizuri ni kama ulishahama. Basi kwa siku hizo zilizobaki za likizo, unaweza kumchukua Ayan, mimi nianze kuhangaikia makazi huko huko Dodoma. Ikitokea napata kabla hujaanza kazi, nitahamia. Ikitokea nakosa, umrudishe Ayan hapa ili uweze kutulia kazini. Au unaonaje?”  Andy akanyamaza.

“Nataka kukaa na mama.” Ayan akawafanya wote wamgeukie. Alikuwa ametulia, hawakujua kama anasikiliza. Kwa mara ya kwanza huyo mtoto akaongea juu ya aishi wapi. “Ni kwa muda tu Ayan. Na mimi nikiweka mambo sawa kama dad, tutakuwa wote.” “Au tuwe wote wakati ukiweka mambo sawa, mama.” Akaongeza Ayan na kushangaza sana wazazi wake, wote wakanyamaza. Andy akala mpaka akamaliza.

Hatimaye!

Kesho yake asubuhi akiwa anampimia mteja maziwa, akahisi mtu mwingine ameongezeka kaunta. Ilikuwa mida ya saa tano. Huwa mida hiyo wanakuwa hawana wateja wengi. Alipomuangalia, akakuta Mill amesimama pembeni kabisa. Pam alishituka mpaka akamwaga maziwa ndoo nzima. Bosi wake akaona kupitia dirisha la ofisini kwake. Ilikuwa mbaya sana.

Alimfoka Pam kama mtoto mdogo na kumwambia atamkata mshahara, mwezi huo asitegemee kitu, kama hataki aondoke. Alimsema mbele yao, asijue Pam alikuwa kwenye mshituko hawezi hata kumsikia. Alibaki akiyaangalia yale maziwa pale sakafuni bila ya kusogea wala kupepesa macho. “Samahani.” Mill akasema hivyo na kuondoka kabisa hapo.

Pam alikuwa amefunga nywele na kuvaa kofia ya wavu kwa afya, ili nywele zisiingie kwenye maziwa, na apron nyeupe. Akaanza kusafisha hapo, bosi wake akiendelea kufoka huku akimuhudumia mteja aliyekuwa pale. Kisha akaondoka hapo kurudi ofisini kwake huku akiendelea kuongea.

Pam akabaki amesimama kaunta akisubiria wateja ila mwili mzima ukitetemeka. Baada ya kama lisaa, akamuona Mill upande mwingine anaenda ofisini kwa bosi wake. Hata hakuendelea kumuangalia tena, na hakujua ameenda kuzungumza nini ila alihisi.

Baada ya kama dakika 10 akatoka bosi wake, yaani mama Chali, akiwa na tabasamu kubwa. “Kumbe unamgeni hujaniambia! Nenda kazungumze naye, nitakushikia mimi mwenyewe.” Akajua amepewa tu hela na Mill. “Hamna haja. Mambo ya nyumbani nitamaliza nyumbani. Naomba niendelee na kazi mpaka muda wangu wa kwenda kula.” Vile alivyomjibu bila tabasamu, akaondoka.

Baada ya muda akamuona Mill anatoka bila ya kurudi pale kaunta alipo. Akatulia kimya. Akaendelea na kazi mpaka muda wake wa chakula ulipofika, mtu wa kumpokea akaja, akatoka mpaka hapo mgahawani wanapokula.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Akatafuta sehemu akakaa. Isah akamfuata. “Nikupe nini dada yangu? Mtori bado upo.” “Usimuendekeze huyo, mpe chakula.” Pam akaanza kucheka. “Hamu yakula haijarudi dada Tuma! Nihurumie.” “Basi utazidi kunyongea. Ugonjwa hauishi!” “Nikiendelea kula mtori na limao jingi jua ndio napata nguvu, kesho nakuletea chapati tani yako.” “Mmmh!” Akamsikia Tuma akiguna. “Nakuletea dada Pam, wala usijali.” Pam akacheka na kutulia.

Akashangaa Mill anakaa mezani kwake. Alishituka ila akajikaza. “Ulikuwa ukiumwa nini?” Pam hakumjibu wala kumwangalia, kama hayupo. “Shema anaendeleaje na mkono?” Ikawa kama anazungumza na upepo.

“Najua umenichukia. Na najua umefanya kazi nzuri sana kumlea Shema, lakini tafadhali ongeza umakini Pam.” Pam akamwangalia amekunja sura huyo! “Unamuacha mtoto anacheza mpira barabarani! Akigongwa?” “Acha kunifundisha jinsi ya kulea mtoto wangu.” “Naomba kukurekebisha. Ni mtoto WETU. Na katika hili naomba tuweke tofauti zetu pembeni, lizingatie tafadhali. Kosa dogo tu, tunaweza kumpoteza, halafu tukaishia kuambiwa ‘samahani, ilikuwa bahati mbaya’. Ambayo haitasaidia.” Pam akasimama na kuondoka hapo kabisa.

“Pam!” Mill akamfuata. “Naomba unisikilize. Nimekuja kuzungumza na wewe.”

Wala hakugeuka. Akarudi kazini kwake na kufunga mlango kwa nyuma na kupitiliza nyuma kabisa na kukaa huko kwa sababu muda wake wa kula ulikuwa haujaisha. Akatulia huko.

Baada ya muda kidogo akasikia sauti ya Isah akimuilizia. Akamfuata. “Nimekuletea chakula. Na mumeo amesema nikuletee na sambusa pamoja na Fanta pineapple. Amesema ujikaze ule.” “Mume wangu!?” Akashangaa Pam. “Yule uliyekuwa umekaa naye pale. Alirudi akajitambulisha na kuomba uletewe ulichokuwa umeagiza. Ila uongezewe na hivi.”

Pam akabaki amesimama akiangalia kile chakula, akitamani kama akimwage kwa hasira lakini Fanta Pineapple huwa inamchanganya hawezi kujizuia. Na alijua Mill alimfanyia makusudi akijua hiyo soda ni udhaifu wake. Halafu harufu ya sambusa ikaanza kumuita. “Achana naye.” “Ashalipia kabisa. Acha nikuwekee hapa niwahi kumsaidia Tuma.” Akaweka na kuondoka akamuacha amekodolea macho hivyo vitu.

Bosi wake akamfuata tena, ila akashangaa anajichekesha wakati si kawaida yake. Mkali kwao kwelikweli. Akiwepo hapo, hata maji hayanywewi. Na alishamgombesha mbele ya watu mpaka wateja! Pam akajifanya kama hajamuona. Si ni muda wake wa chakula! Akatulia tu.

“Sambusa zinanukia vizuri! Naomba moja ya kuonja.” “Chukua tu.” Akachukua na kuvuta kiti kabisa, akashangaa anakaa. “Kumbe una mume! Mbona hatuambizani!” Akamuuliza kishoga wakati wala si marafiki! Pam alimtizama tu na kurudisha macho kwenye chakula chake.

Ni siku iliyopita tu, alitoka kumuomba ampe nusu ya mshahara wake amlipie mwanae michango ya shule, ni darasa la nne, lazima alipe ndipo aweze kufanya mitihani, na kumnunulia viatu, akamkatalia akimwambia amezidi. Leo anataka habari zake za nini! Alipomuona amemtizama vile, akanyanyuka na kuondoka. Jeuri ya Pam si ya kufundishwa. Na hivi alishatendwa, alijawa chuki usingemkuta akicheka kama zamani.

Akataka kususia chakula, ila akashindwa. Akala chote na kusukumia na soda ndipo akarudi kazini.

~~~~~~~~~~~~~~

Mill alishajua mida anayotoka. Akarudi tena hapo saa nane kamili. Kwenye saa 8:15 mchana akamuona Pam na mtoto wake wanatoka. Ila Shema amevaa sare za shule. Akashindwa kuelewa mida hiyo ni kwa nini atokee kazini kwa mama yake na nguo za shule! Akawakimbilia mpaka akawafikia. Pam alipogeuka akamuona ni yeye, akaendelea na safari. “Twende Shema.” Akamshika mwanae mkono akawa kama anamvuta.

“Badala ya kupanda daladala naweza kuwapeleka nyumbani.” Pam wala hakumjibu. Akaendelea kumvuta mtoto, haelewi. “Kwani huyu ni nani?” Kimya. “Mama?” “Twende, acha maswali mengi.” Wakafika kituoni, basi likaja, wakapanda na kuondoka. Walifika wanakoishi, akasalimia wapangaji wenzie hapo, wakaingia ndani kwake.

~~~~~~~~~~~~~~

Mwanae aliingia tu ndani akaanza kubadili nguo akawa anataka kutoka. “Kwani ni lazima na leo uende Shema mwanangu wewe? Si utulie tu ndani? Hilo gozi limekuwa chafu halifai! Tulia kidogo.” “Yaani nikae tu hapa ndani, nisikilize taarabu?” Hapo akakwama.

“Sasa sio upotee kabisa mpaka giza likukute hukohuko. Nikitoka kukutafuta tena! Kesho hutoki.” “Siendi mbali mama. Napiga danadana tu hapo nje.” “Shema!” “Basi nitakuwa narudi kukuangalia kila wakati. Siendi mbali.” “Sasa ole wako ujisahau huko na mpira, usirudi kama ulivyoahidi.” Akawa anamsaidia kuvua nguo.

~~~~~~~~~~~~~~

Mara akasikia sauti ya Mill akisalimia nje. Hakika hakuamini. “Mimi naitwa Mill, mume wake Pam, mama yake Shema. Sijui nimemkuta?” Pam alishangaa mpaka akakaa kitandani. Mwanae akamwangalia kama hajaelewa. Ukiwa chumbani kwao kila kinacho zungumzwa uwani, na kila anayepita nje mtaani na kutukana basi wanasikia yeye na mwanae.

 “Umesema wewe mume wa mama Shema!?” “Ndiyo. Mume wa Pam.” Wote wakatoka kumuangalia, tena kwa kuitana, Mill akiwaangalia. “Mama Batuli njoo muone mume wa mama Shema!” “Kwani mama Shema ana mume na wewe, kama si uongo huo?” “Huyu hapa.” Wakazidi kutoka, Mill amebaki amesimama hata hajakaribishwa.

“Lakini sura si ngeni! Unafanana sana na Shema!” “Kasoro rangi ya mama yake. Shema mweupee.” Shema akamwangalia mama yake. “Ila sura ya Shema na urefu ule, ni wewe mtupu!” Kila mmoja akasema lake, Mill amesimama tu juani. “Na kama ungekataa mimba, ungeumbuka.” Wakacheka kama mazuri.

Mmoja akauliza swali. “Mbona hatujawahi kukuona miaka yote wamehamia hapa?!” “Nilikuwa nje ya nchi. Nikapatwa na matatizo yaliyonifanya kushindwa kurudi huku nyumbani. Sijui wapo?” “Wameingia ndani na mwanae muda si mrefu. Walikuwa hapa wakisalimia. Umembahatisha.” Wakamuonyesha chumba.

Akaenda kugonga. Kimya. Akagonga tena, Shema akaenda kufungua akiwa ameshika mpira wake mkononi. “Shikamoo.” Akasalimia. “Marahaba. Unaendeleaje?” “Vizuri.” Ila safari hii jinsi alivyomsalimia na kumuangalia, ilikuwa tofauti kabisa.

“Unaenda kucheza?” “Mama ameniruhusu.” Mill akacheka kama kuweka hali ya utulivu kati yao. “Unakwenda wapi? Nataka na mimi nije tucheze wote.” Hapo akampata. Akaanza kutabasamu. “Na mimi nilikuwa nikicheza sana mpira nilipokuwa na umri kama wako mpaka sekondari.” “Kumbe unajua!” “Ni wakati huo nikiwa kijana! Sijacheza miaka mingi sana. Acha nizungumze na mama yako, halafu nitatoka tucheze kidogo.” “Basi nitakuwa hapo nje.” Shema akatoka amechangamka kwelikweli. Mpira tena! Akawa amempata kirahisi.

~~~~~~~~~~~~~~~~

          Hata hakumwangalia wakati akiingia. Akavua viatu na kwenda kukaa. Ni chumba kilichokuwa na kochi kubwa moja, kitanda kikubwa kimoja. Kisha kukawekwa kabati kubwa la nguo na vyombo kiasi. Kwa ufupi sebule, chumba, sehemu ya kulia chakula, na jiko dogo la mafuta, vyote vilikuwa sehemu moja.

“Pam mpenzi! Nimerudi mama, japo kwa kuchelewa.” Kimya. “Unakumbuka nilikwambia ninakwenda kuandaa mazingira, mimi nipate uraia wa kule, kisha nikuombee wewe Green Card?” Kimya. “Nilikwama njia zote, nikaishia kuoa. Uraia umekuja na watoto wawili! Ile ndoa niliihitimisha kwa shida sana. Ila nilifanikiwa kutoka, nimerudi hapa nchini na watoto wawili.”

“Naona umejiongeza kutoka kwa baba yako na babu yako. Wao walikuwa wakizaa hovyo, naona wewe umeamua kuboresha. Unaoa na kuacha huku ukitapeli wengine. Na kwa umri huo, ukiendelea hivyo au ukakazana kidogo tu, ukija kufika umri wa baba yako, utakuwa umemfikia, kama si kumpita idadi ya watoto.” “Pam, umekasirika.”

“Hapana. Ila kitakachoniudhi, na ukaniona mbaya, si utapeli ulionifanyia mimi ila kumuingiza Shema kwenye maisha machafu mliyokuwa mkiishi kwenu. Shema hatakuwa muhanga wa laana na maisha uliyochagua kuishi wewe. Hutamfanya mwanangu kama moja ya nazi unazokusanya shambani na kuweka kwenye kapu moja na wanao ulioanza kukusanya kila kona ya dunia kama baba yako.” “Pam!”

“Kwa chochote utakachofanya, usimuhusishe Shema na maisha yako. Hakika nakuonya. Huyu mtoto nimemuombea kama alivyonishauri mama Kenny.” Mill akashangaa sana. “Nimemtenga na roho chafu za kwenu, kama mama Kenny alivyowaombea watoto wake. Sitaki Shema aje awe kama wewe, au baba yako. Hakika sitaki. Na nakuomba na wewe uliheshimu hilo.”

“Wewe una nguvu, na pesa unayo. Endelea kuoa na kuzaa huko, kusanya watoto kila kona kama baba yako, lakini si Shema. Huyu mtoto ni mzuri sana. Uliza hapo nje. Kila mtu anampenda hapa mtaani. Anapenda shule. Si kama wale ndugu zako. Mtulivu. Anaheshima kwa kila mtu. Mwanangu si mwizi. Hajui ugomvi na mtu. Sasa wewe unataka umtoee kwenye haya maisha anayoona wanaume hapo nje wametulia na wake zao. Unataka kumuingiza kwenye maisha yako ya useja?” Mill ALIUMIA sana.

“Japokuwa sina uwezo, lakini hii nyumba nimeipenda na nimechagua kuishi hapa na Shema. Aone wanaume ambao pengine hawajasoma au hawana makazi kama hayo yenu, lakini wametulia na wake zao na watoto wao majumbani kwao. Si matajiri hao. Lakini Shema mwanangu anakitu cha kujifunza kwao. Japokuwa yeye hajajaliwa familia kama hizi, ila ANAJIFUNZA kuwa, kuna wanaume WAAMINIFU. Kwenye shida na raha, WAPO na wake zao na watoto.”

“Sasa unataka umtoe hapa, ukamuingize kwenye maisha yako hayo na ndugu zako, yasiyo na maana ila uharibifu tu? HAPANA.” “Nisikilize Pam. Najua nimekuumiza. Ila Shema ni mtoto wangu, na umezaa na mimi. Kama Mungu aliniona sifai mimi kuwa baba yake, angekupa na mwanaume mwingine. Ila amenipa mimi. Na KUKUKUMBUSHA kama ni wangu, amempa kila kitu changu. Sina mtoto ninayefanana naye kama Shema.”

“Na mimi nilirudi nikiwa nakutafuta wewe.” “Ili unifanye mimi mama Kenny?” “Pam, nimekosa. Najua sasahivi hata nikisema hutanielewa. Ila jua nimerudi kukutafuta WEWE kama Pam, sio kama mama Kenny. Sijawahi kukuona hivyo na wala sina mpango wa kukufanya hivyo. Imetokea nina watoto nikiwa nimeshapata baraka zote za wazazi wetu na Mungu, tukafanyiwa harusi ya kimila kule kwenu baada ya mahari, kitu ambacho baba hakufanya kwa mama Kenny. Mimi nimefanya kwako.” “Basi sitaki.”

“Nahisi umeshachelewa. Wazee wako walishapokea mahari yangu na tumeombewa baraka zote na marehemu baba yangu na kwenu walinikabidhi wewe rasmi.” “N…” “Hapana Pam. Usiongee tena, umekasirika. Utazungumza jambo ambalo utakuja juta. Nisikilize msimamo wangu, kwa sababu kuanzia sasa nitasimamia hapo.” Akanyamaza.

“Shema ni mwanangu. Sitamtelekeza eti kwa kuogopa nitaharibu. Nakusudia nisiharibu kwake ila kumtengenezea na kumsaidia pale nilipoharibu mimi, basi yeye asiharibu. Shema ni mzaliwa wangu wa KWANZA, nitawekeza kwake nikijua ni kiongozi wa wadogo zake.”

“Na kwa taarifa yako tu. Damu ya Shema ni Mgini kwa asilimia 100. Nikiwa nimekata tamaa ya kukupata maana kila nilikokwenda walinipa habari zako mbaya, lakini damu ya mwanangu ILINITAFUTA mpaka akanipata. Bila Shema, nisingekuwa hapa leo. Na SITAMUACHA. Na kwenda kucheza naye mpira kidogo, ndipo nitaondoka.” Akasimama nakutoka. Akakuta watu wanasikiliza madirishani. Akashangaa sana asielewe ndio maisha ya uswahilini, kila habari ni ya wote! Wakaanza kukimbia alipotoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Akaenda akamkuta Shema anacheza na wenzie. Akabaki amesimama tu pembeni akimwangalia. Alipomuona baba yake akamfuata. “Unataka kucheza?” “Endelea na wenzio. Nitakuja kukuchukua, twende tukacheze uwanjani.” “Kwenye uwanja kabisa!?” “Unaogopa nitakufunga?” Akacheka sana.

“Hapana, ila sema mimi sina viatu. Alivyoninunulia mama vyakuchezea, vilipasuka. Akaenda kunishonea mara mbili, vikafaa ila mara ya tatu nilivyopasuka wakati naumia huu mkono, alipovirudisha tena kwa fundi amemwambia havifai tena. Amesema nitumie vya shule mpaka atakapo ninunulia vingine. Lakini nahofia kuchezea mpira visije haribika nikakosa vyakuvaa shuleni, maana najua hawezi ninunulia viatu vingine kwa haraka. Kwa hiyo nikiwa nacheza tu hapa, nacheza bila viatu. Huko uwanjani si watataka viatu?” Mill akaumia sana.

“Nione miguu yako.” Akacheka na kumuonyesha miguu hiyo isiyo na viatu. “Mimi nina miguu mikubwa sana.” “Kweli una miguu mikubwa kama yangu! Viatu ulivyokuwa umetoka navyo ndani vipo wapi?” “Nimemuomba mama yake Abuu anishikie wakati tunacheza.” “Basi utaenda kuniletea niviangalie.”

“Nikuulize swali jingine?” “Juu ya nini?” “Mbona na leo hukwenda shule?” “Nilikwenda shule kama kawaida lakini wakaja kunitoa tena darasani. Mama alipata hela kidogo. Akaona asisubirie mpaka apate zote, leo niende tu na hiyo hela ndogo ili nisome na wenzangu tukijiandaa na mitihani ya darasa la nne. Lakini wamekataa. Wanasema ana deni kubwa, huwa halipagi hata michango mingine midogomidogo, angalau alipe nusu. Ndio nasubiria.” Mill akazidi kuumia.

“Sasa ukirudi shule unafanyaje kufikia wenzio darasani?” Akamuona anacheka. “Hutafeli?” “Siwezi. Muulize mama. Darasani najitahidi. Alikuwa akinilipia tution. Nikawa nafundishwa. Yule mwalimu akamwambia mama naelewa, yeye ataendelea kunifundisha tu bila kufuata silabasi. Nimekuja kugundua nimemaliza hesabu zote za darasa letu mpaka za mbele.” Akaendelea Mili akimsikiliza kwa makini.

“Mimi nilianza shule nikiwa mdogo sana kiumri, ila mrefu tu. Halafu nikawa najua mambo mengi. Mwanzoni kabisa bibi alipokuwa akinilea, akawa ananifundisha kusoma na kuhesabu. Bibi yangu mimi ni mlemavu. Kwa hiyo mama alipokuwa akienda kazini, anatuacha ndani tu. Ndio nikaanza kuongea na uelewa wa kusoma na kuhesabu.” Mill akawa akimsikiliza mwanae huku akipata majibu ya maswali mengi sana aliyokuwa hajui hata ayaulizaje.

“Sasa baadaye nilipobakia na mama tu, ndio akawa akiniacha kwa mwalimu wakati anaenda kazini. Akawa ananifundisha na watoto wakubwa. Ndio akaniombea shuleni nianze na miaka 5. Ila wao wakawa hawaamini kama nina miaka mitano. Wakanipa hesabu nikaweza. Ndio nikaanza darasa la kwanza . Huwezi amini sasahivi nipo darasa la nne, nasoma na watoto wakubwa kwa umri ila mimi mrefu.” Mill akacheka.

“Kweli tena! Na nawasaidia darasa la tano hesabu.” Mill akacheka kwa furaha. Maana watoto aliotoka nao huko Marekani, ni mzigo. “Kweli! Muulize mama.” “Nakuamini Shema. Sema nimefurahi sana. Hongera. Kaniletee viatu nione.” Akaenda kuleta. Mill akatafuta kuona namba ya kiatu, akashindwa. Maana kilionekana kilitumiwa zaidi ya uwezo wake. Vilishonwa tena na tena.”

Mwishoe akamtuka kalamu na karatasi. Akamchora mguu, na kuondoka akiwa amemwachia maagizo. “Mwambie mama asipike, nitaleta chakula cha usiku.” Pam alivyosikia hivyo, akafyonza rohoni na kupika. “Anataka kunifanya mimi mjinga kila siku! Asiporudi, anilazie mtoto njaa!” Shema akashangaa mama yake anaendelea kupika. Akamuacha tu.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Aliwafuata Pam na mwanae tokea kazini mpaka hapo kwao. Alipoona ni uswahilini akahofia wahuni wasije ng’oa vioo vya gari yake ya thamani. Akaamua kutafuta sehemu salama. Akaacha gari hapo na kutembea kurudi mpaka hapo kwa Pam. Ndio maana ilikuwa rahisi kuwafuata mpaka nyumbani.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Kwenye majira ya saa 12:45 jioni akarudi tena kama aliyekuwa akikimbia. Alikuwa na mifuko huyo, Shema alisharudi nyumbani, akaoga, akawa anasubiria msosi alioahidiwa na baba yake. Alipomuona anaingia na mifuko kwenye mlango wa hapo uwani akasimama kwa haraka. Akampokea baadhi ya mifuko na mkono mmoja. Pam akawa kama hajamuona!

Yeye na mwanae wakahangaika kubebelezea mizigo mpaka akamaliza. Akamsogelea pale alipokuwa akipika na wenzie. Wote kimya. “Naomba tuzungumze hapo nje.” Kimya. “Pam? Au unataka nizungumze mambo yote hapahapa?”  Ikabidi Pam akubali. “Naomba niangalizie.” Akamwambia mwenzie, na kuongoza njia akitaka kuingia ndani. “Naomba iwe nje, tafadhali.” Akamsikia, akabadili njia kutoka.

“Ni sawa tukizungumzia ndani ya gari?” “Sitaki.” Mill akamwangalia kwa muda na kumuomba wasogee mbali kidogo na watu. “Nilimwambia Shema akwambie usipike!” “Mimi si mjinga kama ulivyonifikiria. Na wala si toi lako la kubonyeza kila unapojisikia. Tafadhali usinipotezee muda.” Mill alimtizama, akajua kweli amembadilikia.

“Vitu viwili. Nimeleta baadhi ya matumizi ya Shema. Tafadhali angalia na unijulishe kinachopungua.” Akaona amenyamaza, akajua kweli amelemewa. “Pili, nakushukuru kunibebea mzigo wa malezi mpaka hapa. Umefanya vizuri Pam. Inaweza isilete maana kwa sababu ni mimi nazungumza, lakini kutoka ndani ya moyo wangu, nakupongeza. Shema ni mtoto mzuri sana. Japokuwa sijakaa naye muda mrefu, lakini kwa muda mfupi niliozungumza naye, ni mtoto mzuri sana na anakipaji ambacho nahisi kikiendelezwa vizuri, atafika mbali.” Akamuona ametulia.

“Nakuja na pendekezo la pili sasa, kwa kusema hivyo, naomba nimuhamishe shule. Nimpeleke kwenye shule itakayomuendeleza zaidi.” “Wewe unataka kumchanganya mtoto, Mill. Unataka kumpeleka kwenye mashule yenu hayo yanayozungumza lugha zenu, wakati huku alipo anafanya vizuri sana. Shema anaakili ya mtoto kama wa darasa la saba!” “Kama wanalitambua hilo mbona hawampeleki huko darasa la 7, wana kazi ya kumfukuza tu shule?”

“Nilipungukiwa pesa kidogo. Na jumatatu nikipokea mshahara wangu nakwenda kumalizia. Kwanza wala si pesa nyingi. Mwache atulie pale alipopazoea.” “Hapana Pam. Mimi nipo na nina uwezo. Tafadhali acha nimsaidie mwanangu kukuza kile Mungu amemuwekea ndani yake, kutokana na pesa yangu si mazoea. Na najua wewe ukiafikiana na hili, na yeye atakubali tu.”

“Hiyo shule ni shule gani?” “Ni nzuri sana. Ndiko wanakosoma hao watoto wangu wengine.” “Sasa nakuonya wewe na hao watoto wako, msije ninyanyasia mwanangu kwa sababu mnamuona hajaendelea kama nyinyi. Nikikuhisi tu, na nikisikia wanao wanamnyanyasa mwanangu huko kwenye mazingira unayotaka kumpeleka wakati hapa ametulia, utaniona mbaya zaidi ya mwanzo. Nitamchukua mwanangu na nisiione sura yako hapa.” Mill akacheka kwa masikitiko.

“Cheka udhani nakutania. Pam uliyekutana naye safari hii ni mama Shema, uliza hapa mtaani kama kuna anayegusa mwanangu hata kwa bahati mbaya.” “Sawa. Nitakuwa makini.” “Hakika katika hilo Mungu akusaidie. Hutampelekesha mwanangu utakavyo kwa madai unamsaidia. Kwanza mwenyewe alivyo vile wala hataki msaada. Halafu anafikaje huko shuleni wakati sisi tunakaa huku au kutaka kuongeza shuguli zisizo na sababu?” “Ndio linakuja ombi la msingi. Na naomba ulifikirie kabla hujakataa.” Pam akabaki akimtizama. Mill akameza mate.

“Uhamie…” “Uishie hapohapo na usije rudia tena. Nimekwambia mimi si mjinga kama unavyofikiria. Usinifanye mimi toi lako.” “Sivyo…” “Nakuonya. Hakika nakuonya. Mara ya kwanza ulikuja na maneno yako yaliyojaa hekima, nikakuamini, kumbe ni tapeli, mstaarabu.” “Pam!” Mill alikuwa anashindwa hata kujitetea.

Ulinitoa katikati ya maisha yangu. Nikiwa nimezungukwa na ndugu, jamaa na marafiki. Nikiwa nasita, na kukupa madhara yake mpaka kazini kwangu, ukanishawishi kwa maneno ya ulaghai, mpaka ukanitoa katikati ya ulinzi wa watu, ukanitenga na kunitelekeza kikatili bila huruma, ukaenda kuzaa huko na mjinga mwingine kama mimi na yeye ukamuacha kama mimi tu.”

“Nimepata shida kufika hapa nilipo. Kwako panaweza kuonekana duni, lakini pale ndani tunaishi kama ndugu. Shema akiwa na shida pale, mimi sipo, atasaidiwa kama mimi nipo. Kwa ugonjwa na uzima, tunasaidiana kwa uwezo wetu, ndio maana umeweza kumkuta Shema yupo vile. Mtaani kote yule mtoto anasifiwa na kupendwa mpaka na watoto wadogo.”

“Mwanzoni ulinitapeli mimi, ikawa sawa. Sasahivi unataka unitoe hapa nikiwa na mtoto, ukanitende unyama kama ulionitenda mwanzo! Acha kunifanya mimi mjinga. Hapa sitoki. Ongea jingine kama huna, nenda zako katafute watoto kwengine. Nguvu ya kuzaa unayo. Maneno ya utapeli unayo, nenda katafute malaya wengine, sio mimi.” Pam akataka kuondoka.

“Sijamaliza Pam!” “Nahisi mimi nimeshamaliza.” “Naomba namba yako ya simu ili tuwe tunawasiliana kwa mambo ya msingi.” Pam akarudi pale aliposimama. “Unaomba nini?!” “Namba ya simu.” “Hukuwa na namba yangu ya simu wewe?” Mill akanyamaza na kukumbuka jinsi alivyomblock kila mahali ili asije hata kosea akapokea.

Alipomuona amenyamaza, akaanza kuondoka. “Wewe hujanijua vizuri wewe.” Akamsikia akiongea huku akiwa anarudi ndani.

“Pam! Pam!” “Unanipotezea muda.” “Basi nimnunulie yeye simu. Awe…” “Usithubutu. Unataka kumgeuza mwanangu kama yale makuku ya kizungu yakufugwa ndani? Awe mjinga kama matoto yenu hayo mnayoyafungia kwenye mageti! Unafikiri mimi ndio masikini sana, sina uwezo wa kumnunulia simu? Usimuone mtaani anacheza yule, ukafikiri mimi sijui mamichezo yenu hayo ya kwenye simu yanayo pumbaza akili! Akifika umri wa simu, nitajua, halafu mimi, ndio nitampa simu. Usitake kunichanganya sasahivi.” Mill akakwama. Alidhania Kisha ni mkorofi, sasa akakutana na mbogo, aliyejeruhiwa. Moyo umejaa uchungu, hawezi jisaidia. Mill akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Inaendelea….


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment