Alifika
hapo kwa mzee Ruhinda mida ya saa tano asubuhi, akafunguliwa geti. Hakutaka
kuingia na taksii ndani, ilimshusha nje ya geti. Akaanza kutembea taratibu
mpaka ndani. Akagonga kengele, Ayan akamfungulia. Mpaka Mina akalia baada ya
kumuona. Ayan alikuwa amebadilika sana, lakini akafurahi kumuona.
“Mama!” “Ayan!”
Mina akapiga magoti akamkumbatia mtoto wake. “Mama!” Ayan akamuita tena wakati akimnusa mama yake shingo, kama kawaida yake. Mina akacheka.
“Muone! Hujakuwa tu Ayan jamani? Bado unanusa tu!” Akajigaragaza huyo
mtoto shingoni kwa mama yake huku amefunga macho. Mina alikuwa akijisikia
vizuri.
“Unazidi kurefuka Ayan! Unataka kumpita mama?” Mina
akaendelea kuzungumza na mtoto wake hapohapo mlangoni kwa nje. Amepiga magoti
ameegemea visigino, mwanae amemkalia amemkumbatia na kujizungusha shingoni
akimnusa.
“Mbona unanyonya kidole bwana? Umeanza lini? Eti Ayan?
Niangalie basi.” Ayan akabaki amemkumbatia mama yake akimnusa mpaka masikioni.
Mina akaona amuache tu hapo. Akawa ametulia kimya.
“Na mimi nina hamu na wewe Ayan.” Mina
akamwambia kwa upendo huku akimsugua mgongoni. Alipoona hajibu, akaona akae
chini kabisa sakafuni, Ayan akamkalia. Wakatulia hapo. Ilikuwa ndani ya baraza
lililofunikwa, ndipo unaingia ndani kabisa.
“Umeanza kula mwenyewe vizuri?” Mina akamuuliza tena
mwanae. “Eti Ayan? Bado unakunywa maziwa na chakula?” “Unafikiri ananyimwa
chakula huyo mtoto? Kupungua hivyo ni kukua usifikiri anateswa! Anapewa
sana chakula.” Akadakia Paulina akiwa
ndani, akatoka pale nje. Mina akanyamaza.
“Unakuja hapa, unaanza chokochoko! Ungekuwa
unamtaka huyo mtoto, ungeacha umalaya.” “Paulina jiangalie wewe! Mungu
amekupa watoto wakike, mabaya yote unayonifanyia na kunipangia
kunifanyia, Mungu atakulipiza! Shauri yako! Wewe ona mimi nimenyamaza,
ukadhani mimi ni mjinga. Nimemuachia Mungu wangu.” Mina akaongea kwa
upole tu.
“Nimekufanya nini chakulaaniwa? Uache kulaaniwa
wewe tapeli wa ndoa, nilaaniwe mimi!” “Mimi si tapeli. Muulize Andy.
Kuna kipindi alinipa mpaka kadi zake za benki. Zote nilikuwa nikishika mimi
mpaka ya akiba. Sikuwahi kuchukua hata shilingi bila ruhusa yake.
Ilikuwa kama sijampata Andy kwenye simu ni heri nimuombe pesa mama yangu au
Ron, kuliko kujichukulia tu. Hata nisipompata kwa simu hata siku tatu,
ilikuwa ni heri nibakie na shida yangu kuliko kujichukulia pesa.
Andy mwenyewe ni shahidi. Muulize mdogo wako. Sijui kuiba mimi, na si muongo.
Na wala sikujaliwa kuwa na tamaa za hovyo.”
“Andy ameniacha kama mwanamke aliyeniokota
tu barabarani. Ameniacha na mabegi yangu tu, sijalalamika wala kushitaki
popote. Nimemtafuta kwa ajili ya mwanangu tu.” “Si kwa kuwa tulikuwahi kwa
mahesabu! Ulifikiri sisi wajinga tukuache umfilisi Andy. Tulikuwahi.”
Akaongea Paulina.
“Mimi sijui mlichofanya na sijali. Yote
nimemuachia Mungu wangu. Ananilipa kwa namna yake, sijawahi kuishiwa
hata siku moja. Sitaki maneno Paulina. Nipo hapa kwa kuomba ruhusa.
Sijaja tu.” “Sasa nani anataka maneno?” Akauliza Paulina.
“Wewe na mwenzio Raza. Usinione nimenyamaza
ukafikiri mimi ni mjinga mtu wa kumchezea hovyo! Tafadhali tuheshimiane.
Kunyamaza kwangu usifikiri sizifahamu haki zangu, ni kwakuwa nimeamua kunyamaza,
kuwe na amani.” Mina akaendelea.
“Ulinipiga sana siku ile hospitalini. Ukanidhalilisha
mbele za watu kwa kunipiga makofi mpaka ya usoni, na kunisukuma.
Ulinisukuma kwa nguvu pale hospitalini nikajigonga kwenye ukuta na
ukanisukuma tena mpaka nikaanguka sakafuni nikajigonga kwenye kiti.
Mkono wangu mpaka sasa unauma. Kama haikutosha, ukanipiga tena uliponiacha
pale kwa Andy na kunipokonya vitu vyangu. Sikukurudishia wala kukushitaki
sehemu sababu ya heshima ambayo hustahili Paulina. Wewe ni mbaya
Paulina. Omba Mungu akusamehe.” “Aanze na wewe.” Paulina akajibu.
“Mimi sizungumzi mabaya juu ya watu na wala sipangi
mabaya juu ya watu. Nikija kwenu nazungumza yanayonihusu mimi tu. Napenda
watoto wenu, sina shida na mtu. Lakini Paulina wewe na Raza mnanichukia
bila sababu! Nilikusikia ukinisema kwa Raza, naringa kama nimezaa ulimwengu.
Msichana wa Raza, Mamu aliniambia mipango yenu na hila zenu za kunitoa
kwenye hii familia.”
“Mkasema najidai kwa kuwa nimezaa mtoto wa kiume.
Sina akili, ndio maana pesa ya Andy yote namalizia kwa mwanangu.
Sina akili ya maendeleo. Namwendekeza mtoto wangu, na mtahakikisha nawapisha
hapa. Mkaanza kumnyanyasa mwanangu. Mnamsema na mnakataa
asipewe maziwa. Mnamlalamikia mwanangu eti anawamalizia maziwa majumbani
kwenu! Mamu aliniambia na ndio maana sikutaka ugomvi na mtu, nikawa nikiwa na
kitu cha lazima, naenda kumuacha mwanangu ofisini kwa babu yake. Maana hata
huyu msichana wa hapa mlimpandia chuki dhidi ya mwanangu. Mamu aliniambia
maneno yote aliyokusikia ukiyasema Paulina.” “Muongo huyo Mamu.” Paulina
akakataa kama ameishiwa nguvu.
“Kubali ukatae, utajijua wewe na Mungu wako.
Sikukuuliza wewe wala Raza kwa kuwa nawaheshimu na mimi si mgomvi.
Hunidai chochote kile Paulina. Nimeondoka kwa mdogo wako sijachukua kitu
chochote kile. Kila kitu Andy alininyang’anya na TALAKA alinipa.”
“Huna undugu na mimi. Naomba uniheshimu.
Ukishindwa, nifanye kama mpita njia tu. Huna haja hata yakunisalimia. Hamnidai
chochote, nipo hapa kwa ajili ya Ayan tu. Na ndio maana sikutaka kumkera
yeyote, nimebaki hapa nje.” “Hata kuwepo hapa unatukera.” Akajibu
Paulina.
“Ondoka! Kwani hapa ni nyumbani kwako?! Hapa ni kwa
wazazi, unapo kwako. Nimekaribishwa, sikuja tu. Na nipo hapa kwa
heshima, sitaki ugomvi na wewe. Naomba niongee na mwanangu, niondoke.
Lakini pia kama huwezi, unataka ugomvi na mimi, mimi naondoka,
nitamtafuta mwanangu wakati mwingine. Mimi maneno siwezi.”
“Na nikishindwa kumuona mwanangu, vyombo
husika vitanisaidia. Naweza nikawa nimeshindwa kuwa mke, lakini si
mama kwa mwanangu. Nyinyi wote ni mashahidi. Ayan
hakuwa hivi wakati nipo naye. Amezeeka mwanangu wakati ni mtoto mdogo!”
“Umeanza dharau? Kwa hiyo anateswa?” “Paulina naomba unyamaze. Tafadhali.” Andy
akatoka.
“Huyu Mina ana...” “Please. Acha. Acha kabisa. Nimezungumza na baba na mama, wakaniruhusu
Mina aje aone mtoto. Hakutaka ugomvi na mtu ndio maana aliomba iwe
asubuhi, na ninafikiri ndio maana yupo hapo nje. Ingia ndani ili apate muda na
mtoto. Tafadhali naomba uwapishe.” “Yaani mimi ndio wakumpisha huyo!
Kwa lipi! Kwa fedheha yote hiyo bado hana aibu ya kuleta sura
yake hapa!” Paulina akajibu kwa jazba.
“Sitakuruhusu uongee vibaya na Mina mbele ya
Ayan. Huyo ni mama yake hata iweje. Na hukupaswa kumpiga Mina. Huko ni kunivunjia
heshima kwa hali ya juu sana. Na sitakusamehe Paulina.” Mina akashangaa
Andy amemtetea. Jua lilishaanza kuwa kali. “Kwa lipi mno!?” Paulina
akauliza kwa ukali na ushari. Mina akasimama na mtoto wake. “Jamani mimi
nimekuja kuona mwanangu. Sitaki ugomvi na matusi.” Mina akatoka na mtoto
wake.
Akaenda kukaa na mtoto wake nje kabisa nyuma ya
nyumba. Akahisi kama ananjaa. Akamtumia ujumbe Andy. ‘Tafadhali
naomba maziwa yake huyu kama yapo. Kama hamna basi. Ila ana njaa.’
Akamtumia ujumbe. Baada ya kama dakika 10 akamuona Andy anakuja na chupa imejaa
maziwa.
“Sema asante bwana. Wewe vipi Ayan!” Mina akambusu.
Akamuweka sawa. Lakini Ayan akarudi shingoni na chupa yake. Anamnusa mama yake
huku anakunywa hayo maziwa. “Kaa vizuri bwana Ayan!” Andy akataka kumtoa.
“Mwache tu.” Mina akamkataza. “Hatakuumiza hivyo?” “Hapana. Mwache tu.” Mina
akaendelea kumsugua mgongoni. Andy akamwangalia kwa muda, akaondoka kama
kuwapisha.
Ayan akahangaika hapo, mpaka akasinzia. Mina
akaanza kulia. Alimkumbusha mbali. Mtoto amelea kwa shida mpaka kumfikisha
hapo, halafu anatengwa naye! Ni kweli Ayan alikuwa amekonda
haswa. Alilia Mina, akashindwa kujizuia. Akampakata vizuri akawa
anamwangalia nakuzidi kulia.
Upande wa chupi alijawa mapele kama yenye
usaha. Ayan alivuta hayo maziwa mpaka akamaliza yote ndipo akapotelea
usingizini kabisa. Mina alikaa naye hapo kwa muda akiendelea kumwangalia mwanae
huku akilia.
Mwishoe akaona aondoke tu. Akamtumia ujumbe Andy kuwa
aje amchukue, amelala. Kwa haraka, Andy akaja. “Naona amelala. Asante kwa
kuniruhusu kuja.” “Karibu.” Andy akamchukua. “Nimeshindwa hata kumpa zawadi
zake. Hakutaka hata tuzungumze. Naomba akiamka, umkabidhi hizi zawadi.” Mina
akafungua pochi kubwa aliyokuwa amekuja nayo.
“Hii nimemfungia kabisa. Atakuja kufungua mwenyewe.
Ila huu mfuko una nguo zake za kulalia nimekuwa nikimnunulia, na boxer zake.” Akaweka pembeni yake maana Andy alikuwa
amesimama na mtoto. “Nilikuwa nikimnunulia boxer mbali mbali, za cartoons kumvutia ili tuachane na diaper. Sijui
amefikia wapi! Naona yupo na diaper bado. Ila ukimvalisha huwa anapenda.” Mina
akaongea hivyo na kusimama. “Muwe na wakati mzuri.” Kimya. Mina akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Alitoka hapo akashindwa hata kutulia. Alikumbuka vile
Ayan alivyokuwa akimng’ang’ania. Jinsi alivyobadilika kiafya. Mapele
aliyoyaona! Mina alilia njia nzima kurudi hotelini. Akaingia na kujitupa
kitandani akilia. Taswira ya Ayan ikaendelea kumjia vile alivyobaki
kijiti. Hana hata nyama! Akaendelea kulia akijua maneno ya Paulina na Raza yametimia,
sasa hivi wapo huru kumtesa mtoto wake vile watakavyo.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Akashangaa usiku unaingia na kuendelea, Pius hapigi
wala hakutokea. Mina akazidi kuumia. Akajiambia ndio yupo na Raza, mkewe.
Mtu chake. Akajua Raza amemshikilia mumewe, ndio maana alishindwa
kurudi au hata kumtafuta tena.
~~~~~~~~~~~~~~
Ule muda wa
peke yake pale hotelini, ukampa nafasi ya kujitafakari kwa upya. Aliwaza Mina
na kuwazua. Mwishoe akaona ameshajichanganya tena. Na amesharudia
historia. Anatembea mlemle waliko mtabiria watu. Kurudia
maisha ya zamani. “Mimi ndiye nimeshika hatima ya wanangu na nawajibika
kwenye maisha yangu.” Akawaza Mina na kuamua kufanya mapinduzi makali ya maisha yake.
~~~~~~~~~~~~~~
Akawahi kuamka mapema sana. Nia ni Pius asije kumkuta
tena pale. Alishaamua aachane naye kabisa. Alijua Pius anampenda sana,
na angempa chochote anachotaka, lakini akajua kuwa naye ni kujiweka njia
panda. Atabaki akiiba penzi huku watoto wakimsubiria na yeye. “Bora
nishike moja.” Kwa mara ya kwanza akaadhimia kukana nafsi yake.
Akazima kabisa simu yake. Akatoka hapo saa kumi na nusu alfajiri kuelekea kituo
cha mabasi yatakayomtoa kwenye hilo jiji. Akaondoka na basi la kwanza kabisa
kurudi Iringa.
Mama ni Mama tu.
Alifika kwake, hajala tokea alipopata kifungua kinywa
jana yake wakati anakwenda kukutana na mwanae. Akalia hapo wee, akaona
asipoteze muda. Amtafute tena Andy. ‘Naomba usikilize
huo ujumbe wa sauti, tafadhali Andy.’ Akatuma huo ujumbe na
kuanza kurikodi. “Andy, najua mimi ni mtu wa mwisho
kabisa unayetaka kumsikia kwa sasa. Lakini Andy, mimi ni mama yake Ayan.
Naweza nikawa nimeshindwa kabisa kuwa mke mzuri, lakini Andy, wewe nishahidi,
hata ndugu zako watanitetea katika hili, sijawahi kushindwa kuwa
mama. Hata kama hutaki kukumbuka nyuma,
lakini naomba kumbuka afya ya Ayan tafadhali.” Mina akasikika akilia.
“Mimi nilikuwa na huyo mtoto katika
ugonjwa na uzima wangu, Andy. Sikuwahi kulalamika kama ni mzigo.
Japokuwa hukuwa na muda na sisi, nafikiri unakumbuka afya ya Ayan
ilivyokuwa na sasa. Kama umepata nafasi yakumuosha, utagundua ana mapele
yenye usaha kabisa. Mimi sijui ni nini, lakini nina uhakika
yatakuwa yanamletea homa, hakuna anayejua kwa kuwa Ayan ni mkimya sana.
Nakuomba Andy, nipe Ayan nimlee mimi.” Akasikika akilia kidogo, akatulia na kuendelea.
“Ninapo sehemu ya kuishi, na utakaribishwa muda na wakati
wowote kuja kumuona. Huhitaji hata kuomba ruhusa, ya kuja kwangu. Unakaribishwa
muda na wakati wowote utakapotaka kumuona mtoto, milango ipo wazi. Mimi
ni mama yake Ayan. Tafadhali naomba fikiria hilo kabla hujanikatalia.
Asante.” Mina akatuma huo ujumbe mrefu wa
sauti.
Baada ya kama lisaa akaona Andy yupo online. Akafungua jumbe zake. Mina akakaa. Akajua anasoma na
kusikiliza. Akasubiri kwa muda akaona anajibu. ‘Unauhakika?’
Akauliza Andy. ‘Kabisa Andy. Ayan hajawahi kuwa
mzigo kwangu, na nitamlea bila shida.’ Akajibu kwa haraka. Alimjua Andy
na kazi. Akajua anaweza kukubali. ‘Unataka iwe lini?’
Akauliza. ‘Nimeshaondoka Dar. Lakini naweza kurudi
hata kesho kuja kumchukua. Nitarudi sababu ya Ayan.’ Kimya
kwa muda.
Mina akaona amuwahi kabla hajampoteza. ‘Huhitaji kunigaramia
chochote. Nina nauli yangu na ya Ayan. Niruhusu tu nije kumchukua.’
Wasiwasi ukamzidia akijua anakaribia kukataa asijue mshituko wa Andy ni
kushangaa kumbe Mina hayupo jijini Dar! ‘Unaishi wapi
kwa sasa?’ Andy akatuma hilo swali.
‘Iringa. Lakini Andy nina sehemu nzuri tu.
Tutatoshea na mtoto. Unaweza hata kuja kupaangalia kwanza, ujiridhishe. Ayan
hatapata shida.’ Mina akaendelea kumshawishi.
Akaona Andy anapiga. Nusura aruke.
“Andy!” “Iringa unaishi maeneo gani?” Akakumbuka Andy ni mwenyeji Iringa. Huwa anakwenda
sana kikazi. “Gangilonga.” Akamuelekeza. Andy
akaonekana kuridhika na maelekezo. “Muda gani ni mzuri
kwako?” “Muda na wakati wowote Andy. Hata saa sita za usiku, karibuni. Na huwa sitoki
mara kwa mara. Muda mwingi nakuwepo nyumbani.” “Sawa.” Mina alitamani
aulize atamleta lini mwanae, akaona asiharibu. Akatulia, simu ikakatwa.
~~~~~~~~~~~~~~
Hakutaka kitu kiharibike. Akaamua kusoma jumbe zote
alizokuwa amemtumia Pius. Akakuta anamtafuta kama aliye changanyikiwa. Alishaonjeshwa
asali ya Mina, anataka kujenga mzinga.
Shilingi imepinduka. ‘Pius, kilichotokea kati yetu si sawa.
Tumekosea. Tulikuwa na mahusiano mazuri sana, lakini tumeyaharibu
kwa kuchanganya na mapenzi. Si sawa na tumevuka mpaka. Naomba
nikupe nafasi na familia yako. Na mimi hivyo hivyo. Nahitaji kutulia kwa ajili
ya wanangu. Mahusiano yeyote yale ya kimapenzi kwa sasa nitakuwa nikijiweka njia
panda, nakujichanganya
kabisa. Asante kwa kila kitu, tafadhali naomba uheshimu maamuzi yangu
na usinitafute tena. Kwa heri.’ Akatuma
huo ujumbe na kufuta jumbe zote alizokuwa akiwasiliana na shemeji ‘P’.
~~~~~~~~~~~~~~
Kesho yake akaenda kununua namba nyingine. Akamtumia
ujumbe Andy. ‘Ikitokea unanitafuta na hunipati kwa ile
namba ingine, tafadhali wasiliana nami kwa kupitia namba hii pia. Mina, mama
Ayan.’ Akaweka na msisitizo, kisha akamtumia Andy tu. Alihamisha hapo
namba za watu wote. Lakini aliyemtaarifu juu ya namba hiyo mpya ni Andy tu.
Ndipo akatulia.
Kwa Colins.
Baada ya
kuzungumza na Jerry, alibaki kwenye gari zaidi ya masaa mawili, hawezi
kuondoa gari, hajui anachowaza. Baadaye akiwa kwenye hiyo sintofahamu,
wazo jingine likamjia, akaamua kwenda kwa Colins. “Kwema Mill? Mbona upo
hivyo?” “Najua unaweza usinielewe Colins. Tafadhali nisaidie kujua jina
la yule kijana uliyemuona hapa, ukasema anafanana sana na mimi.”
Colins akakunja uso. “Najua haitaleta maana kwako, lakini naomba msaada
wako.”
“Mill! Hivi
unajua ni wagonjwa wangapi wanakuja hapa kila siku?” “Anza kwa kukumbuka siku, tarehe,
kisha angalau muda. Hilo tu.” Colins akatulia. Akijaribu kufikiria siku alipomuona
huyo mtoto, kwa kufikiria sababu iliyokuwa umempeleka mapokezi.
“Muda naweza
kukumbuka, ilikuwa mchana maana tulitoka kula na Kamila.” “Tafadhali naomba
uandike kabisa.” Colins akakunja uso na kufikiria tena. Akaandika muda kati ya
saa 7 mchana mpaka saa 8.
“Tafadhali
kumbuka siku ili itusaidie ku..” “Subiri kwanza nijaribu kwa majina.”
Akasogelea kompyuta. “Unahisi anaweza kutumia jina gani la mwisho?”
“Anaweza hata kuwa ni mtoto wa wadogo zangu! Jaribu kumtafuta kwa jina la Mgini.”
Colins akaweka hilo jina la Mgini kwa mwezi huo na kubonyeza, search.
Mill akazunguka nyuma ya meza ya Colins ili kuona kompyuta kabisa. Baada ya
mtandao kufanya kazi yake ya kutafuta, ikarudisha jibu 0. Kwamba hakuna
Mgini yeyote aliyekwisha kutibiwa hapo kwa huo mwezi. Mapigo ya Mill yakazidi
kwenda kasi.
“Naomba
jaribisha kwa jina la Shelukindo.” Colins akakunja uso na kumtizama Mill. “Nina
maana yangu Colins. Tafadhali nisaidie tu.” Colins akaandika hilo
Shelukindo. Wakasubiria kuona majibu, ikarudisha 1. Akamwangalia Mill.
“Fungua
tafadhali.” Akamsihi huku mapigo ya moyo yakienda kasi zaidi. Wakafungua
wakakuta jina limeandikwa, Shema Shelukindo. Mill akameza mate. “Umri?”
Colins akafungua. Akakuta miaka 9. Miguu ya Mill ikaanza kutetemeka.
“Basi anamwili mkubwa zaidi ya umri wake. Ukimuona, ni mrefu
kama…” Ndio taarifa zikafika kichwani kwa Colins.
Akasogea na kiti
chake nyuma kabisa akiwa na mshituko. “Kwamba ulimuacha Pam akiwa mjamzito!?”
“Sikujua Colins! Mungu wangu ni shahidi, SIKUJUA.” Colins akafikiria
tena akaona amuulize tu. “Nikuulize kitu Mill? Ila usinielewe vibaya,
nikutaka kuelewa zaidi. Mliachana na Pam kwa makubaliano gani?”
Kimya. Akamuona amebadilika kabisa, mpaka macho yakawa mekundu.
Colins naye
akanyamaza na kurudi kwenye kompyuta. “Huwa mnaandika taarifa kamili za
mgonjwa? Kama taarifa za wazazi wa mgonjwa endapo mgonjwa ana umri mdogo? Na
ugonjwa aliokuwa nao?” “Kutokana na maelezo ninayosoma hapa, anaonekana
alivunjika mkono. Ni kama alifanyiwa tu vipimo na kuondoka. Inawezekana kabisa
walichotaka ni kipimo tu, na kwenda kuhudumiwa kwenye bei nafuu. Acha
niangalie taarifa zake zaidi.”
Colins kusoma mtu aliyemleta hapo, akakutana
na jina la Isah Hamidu. Na namba ya simu. Mill akaichukua. “Nashukuru
sana Colins. Ila kujibu swali lako, wala sina haja ya kukuficha, nilimtelekeza
kabisa Pam.” Colins akakunja uso.
“Kwamba ulipotea
tu?!” Alishindwa kujibu mpaka akamuumiza Colins. “Natamani kukuuliza swali,
lakini naona haitasaidia. Ila acha nikuulize la pili yake. Kama ungejua
kama Pam ni mjamzito, unafikiri ungefanya tofauti?” “Nikikujibu
kitu chochote sasahivi, nitakuwa nikijitetea tu, Colins. Naomba tuache
tu. Ila jua nilikosea kupita hivyo unavyofikiria hata sasa. Nimeharibu
maisha ya Pam kupita nitakavyokueleza. Sina jinsi nikajitetea. Na
Jerry yupo sahihi. Kabla sijatafuta aliyemuua Mike, natakiwa kujiangalia
mimi mwenyewe. Nimeua au kuangamiza maisha ya Pam. Nashukuru
Colins.” Akatoka.
Kwa Isah Hamidu.
Akaingia garini
na kumpigia simu huyo Isah Hamidu aliyekuwa amempeleka Shema hospitalini.
Akajifanya kama ni muhusika wa ile hospitali.
Isa akapokea. “Habari za mchana Isah?” “Nzuri. Nani mwenzangu?” Akamtajia jina la hiyo hospitali. Akamkumbusha alimpeleka mtoto hapo. “Napiga
kufuatilia maendelea ya mtoto.” “Mama yake aliona hapo kwenu pesa nyingi,
akaenda kumfunga POP kwenye hospitali ya Temeke, huku karibu na kazini. Mtoto
mwenyewe michezo mingi, hatulii. Kutwa mpira! Namwambia atamfilisi mama
yake! Hasikii. Pesa yenyewe ngumu.”
“Kwa hiyo unafanya kazi na mama yake?”
“Mimi nafanya kwenye mgahawa wa hapa karibu na kazini kwa dada Pam. Huwa
anatuletea hapa chapati. Ndio siku hiyo akaniomba nimpelekee mtoto wake
hospitali, yeye alinyimwa ruhusa.” “Umesema anafanya kazi wapi?” “Ni Depo
ya maziwa. Wanauza maziwa hapa Chang’ombe.” Akamuelekeza. “Ila umesema
mtoto alipatiwa matibabu, sisi huku tufunge faili lake?” “Huko dada Pam harudi
tena. Mnagarama sana aisee! Funga tu.” “Asante sana.” Akakata simu.
Chang’ombe.
Akafikiria
kidogo na kuamua kwenda angalau akapaone kwanza. Akampigia simu mfanyakazi wa
nyumbani, anayekuwepo hapo kusaidia watoto wake wakitoka shule. Akamuomba
asiondoke siku hiyo mpaka atakaporudi.
Safari ya
Chang’ombe ikaanza. Foleni. Mpaka anafika pale kumefungwa ila akajua ni penyewe
kabisa. Jina linafanana. Akaegesha gari na kubaki garini anawaza. Mwishoe
akaona anapoteza muda, aondoke tu.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Kesho yake mida
ya saa nne asubuhi akawa amewasili hapo. Akaegesha gari ng’ambo ya pili ya
barabara akawa anaangalia. Wateja hawakuwa wengi sana. Akabaki akichungulia.
Mara akamuona mtoto kama alivyoelezwa na Colins. Moyo ulipasuka! Alikuwa
mzuri huyo mtoto! Na alijua ni mwenyewe kwakuwa alikuwa na POP ameshikilia
mkono ila bado anacheza mpira nje ya hiyo sehemu.
Akashituka maana
wakati mwingine mpira ulikuwa ukikimbilia barabarani, magari yanapita.
Akajua Pam yupo kazini, hamuoni. Alishituka Mill mpaka akashuka garini
na kumfuata taratibu asimuogopeshe.
Mill kwa Mwanae
Shema akasimama
alipomsogelea. Akasalimia kwa heshima. Mill alikuwa amepigwa na butwaa
akivutiwa na uzuri wa huyo mtoto. Hakufanana na Pam hata kidogo ila rangi tu.
Yaani kama ingekuwa amekana mimba, kweli angeumbuka.
“Hujambo Shema?”
Shema akamwangalia kwa makini alipomtaja mpaka jina kama anayemfahamu kabisa!
“Sijambo, shikamoo.” Akasalimia kwa uso mdadisi, akijaribu kukumbuka au kama na
yeye anayemfananisha. Kabla hajaitika hiyo salamu, Shema akamwambia. “Sura yako
sio ngeni! Ila sijui nimekuona wapi!” “Pengine kwenye kioo. Mbona
una nguo za shule na haupo shuleni? Unaumwa?” “Wamenipa barua, wamesema nimletee
mama. Akinipa hela ndio nirudi. Ila mama amesema nisubiri,
nitarudi tu shule.” Mill akaumia sana.
“Ila hapo unapocheza ni hatari. Nimeona
mpira unakwenda mpaka barabarani. Si salama kwako. Wanaweza kukugonga. Hakuna
sehemu nyingine yakucheza mbali na hapa?” “Nitaenda kucheza nyuma.” Akaenda
kuokota mpira wake.
Mill na yeye akarudi
kwenye gari akiwa hajielewi. “Ni mwanangu kabisa huyu, hakuna ubishi!
Nitamwambia nini Pam!?” Akafikiria na kushindwa kupata jibu ila hofu
huku maneno ya Jerry yakijirudia. Akajua wote wanamsingizia tu Pam,
hawajui ukweli ulivyo. Akamuona mwanae anarudi ndani taratibu huku akiangalia
nje. Kwa hofu, akaondoka kabisa hapo.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Mama yake
akamaliza wateja na kumfuata. “Vipi mkono?” “Hauumi.” “Mbona umekuja huku
nyuma? Mama Chali amekufukuza kule mbele?” “Kuna baba mmoja ameniambia nisicheze
kule mbele, mpira unaenda barabarani, nitagongwa na magari.” Pam akakunja
uso.
“Ni nani?!”
“Mimi simjui ila sura sio ngeni. Nikamuuliza akasema niangalie kwenye
kioo.” Pam akashangaa sana. Akatoka kabisa mpaka nje, hakumuona mtu.
Akarudi ndani lakini akiwa na maswali.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Damu Nzito Kuliko Maji.
Akiwa Amekata Tamaa Kabisa, Damu Ya Mwanae Imemtafuta Mill Mpaka Amempata Baba Yake Bila
Kutarajia.
Mina Naye Analilia Mtoto Wake.
Ni Nini Kitaendelea kwa Wapenzi Hawa Wa Love At First Sight?
Kwa Mara Nyingine Tena, WOTE WANNE,
MAISHA Yamewakutanisha Wakiwa wameshaonja joto ya jiwe
ya UHALISIA WA MAISHA & Mapenzi?
Bado
Penzi Lipo?
Je, Itakuwa Rahisi Kama Mwanzoni?
Inaendelea….
0 Comments:
Post a Comment