![]() |
Maisha Mapya baada ya Talaka na kufukuzwa
nyumbani.
Mina alikuwa
amechoka, hana hata akili yakufikiria. Alichofanya ni kutafuta nyumba ya kulala
wageni yenye choo humo humo ndani, akaingia humo na kuanza kutapika.
Asingethubutu kwenda kwa ndugu yeyote, kuogopa kumfedhehesha mama yake
zaidi. Alijua jina baya alilonalo kwa ndugu.
Kwanza akajua watafurahi ameachika na utabiri
wao umetimia kuwa Mina, hatawahi kutulia kwa mwanaume mmoja. Akaona
atulie tu hapo hotelini. Akaendelea kutapika na kurudi kitandani. Akakuta Pius
amemtumia pesa nyingi, na ujumbe kuwa ahadi yake ipo pale pale. Akiwa na shida yeyote amtafute.
Akaanza kulia.
Pius!
Akalia hapo asiamini kama bado Pius anaweza kuendelea
kumjali, tena baada yakumpuuza takribani mwezi sasa! Akajisikia vibaya
kuona alimtupa Pius na kumpuuza vibaya vile! Aliacha kupokea simu
zake kabisa ila kuwa akimtumia ujumbe kuwa yupo kwenye simu na Andy. Baada ya
muda akajua ujumbe umemfikia, kwani aliacha kumpigia simu za mara kwa mara.
Ikawa jumbe moja moja akimuulizia kama yeye na mtoto wapo salama. Napo akawa akimjibu
kama anayemsumbua tu. Mina akajisikia vibaya sana. Akajuta.
Akaamua kumrudishia ujumbe, ‘Asante
na samahani.’ Akamwandikia hivyo tu akautuma ule ujumbe. Akaona simu
yake inaita. Pius! Mina akapokea. “Asante kwa pesa.” “Ulipata
dawa ya kuzuia kutapika?” “Hapana. Bado
natapika sana.” “Uko wapi?” Mina akaanza
kulia tena. Akalia hapo, Pius akimtuliza. “Lazima
kwenda hospitalini. Huwezi kuendelea kutapika hivyo. Nakuja kukuchukua.”
Akamuelekeza alipo.
Baada ya dakika 45, Pius akawa ameshawasili.
Ilibidi kumsubiria atapike tena ndipo watoke. Alimshika mbavu wakati
akitapika, angalau Mina akapata nafuu mbavuni. Kwani zilikuwa zikimuuma
sana kila alipokuwa akitapika. Akamfuta vizuri na kumrudishia nywele zake
vizuri.
“Pole sana Mina.” “Asante.”
Akashukuru kutoka moyoni asiamini kama Pius yuko naye tena. Alikuwa na
kizunguzungu, mpaka kuona giza kwa kutapika siku nyingi bila ya kula. Wakatoka
moja kwa moja mpaka hospitalini, Pius akiwa amembeba mpaka garini. Alimpeleka
kwenye hospitali nzuri tu. Mina akapata huduma ya kwanza tena kwa haraka.
Wakamchoma sindano yakuzuia kutapika na kumuwekea dripu ya maji kwa kuwa
alikuwa amekaukiwa haswa.
Sindano aliyochomwa ilimpa usingizi pia mbali ya
kumsaidia kuzuia kutapika. Alilala mpaka Pius alipomuamsha kuwa wameruhusiwa.
Akaandikiwa na dawa. Pius akanunua hapo hapo hospitalini, akamrudisha hotelini.
Akasogeza gari karibu kabisa ya mlango. “Naweza kukubeba Mina.” Mina akaanza
kulia tena, lakini akakataa nakumwambia safari hiyo anaweza kutembea.
“Nikuletee chakula gani, kabla hujarudi tena kulala?”
Pius akauliza kwa upendo. “Leo naomba nisile
kabisa. Harufu ya chakula inanitesa sana. Labda nipumzike tu.” Wakarudi
ndani kwenye chumba alichokodi.
Alikwenda chooni kujisaidia, asiamini hajatapika.
Akapanda kitandani bila hata kubadili nguo. Pius akamsogelea, akamfunika vizuri
na kukaa hapohapo kitandani akaanza kumsugua mbavuni taratibu. Akamuona
anasinzia. “Asante.” Akaongea wakati
anapotelea usingizini. Akakaa hapo mpaka alipohakikisha amelala kabisa. Ndipo
akaondoka. Alichukua funguo moja, moja akamuachia na kufunga kwa nje.
~~~~~~~~~~~~~~
Mina alilala mpaka akasikia Pius akimuamsha tena.
Tayari ilikuwa asubuhi ya siku inayofuata. “Nilikuwa nimechoka!” Mina
akalalamika. “Nenda kaoge, uje ule.” Bila swali, akaenda kuoga, na kusafisha
kinywa, akarudi. “Nimekuletea mtori. Kuna limao hapo. Jaribu uone kama utaweza
kula.” Mina akajifuta machozi wakati akikaa. Akajimiminia mtori. Akala mtori
wote uliokuwa kwenye bakuli akabakisha mwingine. Akamwambia Pius atakula tena
mchana.
“Kunywa na hizo dawa, ndipo urudi kulala. Nitakuona
baadaye.” “Asante.” Akashukuru. Alikuwa amemletea na chupa za maji. Akasubiri
mpaka akanywa dawa, ndipo akaondoka. Akarudi kulala.
~~~~~~~~~~~~~~
Alilala mpaka kama kwenye saa saba mchana, akaamka
sasa akiwa na nguvu. Akapata nafasi sasa na kuwaza maisha yake na nini
kinamtokea. Aliwaza Mina, bila kupata majibu yakueleweka. Akaumia kuona
amefukuzwa nyumbani kwao. Akamkumbuka Ayan. Mina akaanza kulia.
Alilia Mina bila kunyamaza mpaka akapitiwa na usingizi.
Pius alirudi mida ya jioni. Akamkuta amejilaza tu
kitandani. “Umeshindaje?” Mina akakaa. “Sijatapika tena. Nilikula kile chakula
chote na nimeweza kulala. Uchovu umeisha. Njoo ukae hapa.” Akamtaka Pius akae
kitandani. Pius akakaa.
Ahadi Mpya kati ya Mina na Shemeji{Pius}
Mina akakaa kimya kwa muda, kisha akaanza. “Naomba
nikushukuru kwa kuwa na mimi muda wote. Zaidi kipindi nilichohitaji faraja
na msaada. Umekuwa faraja na msaada ambao sikutegemea. Maisha
yangu yamebadilika ghafla bila kutarajia na sina majibu. Lakini
najua ni mjamzito, baada ya miezi nane nitakuwa na mtoto. Lazima maisha
yaendelee. Wapi, kivipi, nafanya
nini, hayo yote nimejiambia yatajijibu taratibu kadiri siku zinavyo kwenda.
Lakini naona nilazima nichangamke.”
Mina akaendelea akiwa ametulia.
“Nashukuru sana kwa kujali na kuja kunipeleka
hospitali. Angalau sasa hivi naweza hata kufanya kitu au kufikiria. Asante
sana.” “Karibu.” Pius akaitika. “Kesho nitatoka hapa, nikatafute sehemu ya
kuishi mimi na mtoto, kama Mungu atanijalia nikija kujifungua salama.
Nikishatulia, ndipo nitafute kazi sasa yakuja kumsaidia mtoto au yakututunza
mimi na mtoto.”
“Unafikiria kuishi maeneo yapi?” “Sijawahi hata
kulifikiria hilo! Ndio inabidi kuanza sasa. Nitakapopapata ndio hapo hapo.”
“Unataka nikusaidie kutafuta.” “Hapana shem. Nitakutegemea mpaka lini?
Mwisho tutajikuta wote tunakwama kwenye moja. Umeacha kazi na familia
yako ili uwe na mimi hapa, kuniuguza. Najua hii haitaendelea daima. Acha
na mimi nihangaike mpaka niweze. Naamini nitapata sehemu nzuri tu
yakuishi na kazi. Maisha yataendelea tu.” Pius akabaki kama anayefikiria.
“Nina ombi moja na la mwisho kwako.” Pius akamtizama. “Najua nimeondolewa kwenye maisha ya mtoto wangu na
unajua mazingira yanayo mzunguka. Tafadhali shem, kila utakapoweza naomba ukamtizame.
Ayan ni mtoto mrahisi sana, kwa hiyo ni rahisi pia kumsahau.” “Nitajitahidi
Mina.” “Asante.” Mina akawa kama amemaliza,
akajifuta machozi.
“Na mimi nikuombe kitu.” “Karibu.”
Mina akajiweka sawa. “Usikate mawasiliano na mimi. Kwa lolote na
chochote, naomba tuwasiliane kama zamani. Hata ukibadili namba, naomba
na mimi niwe wa kwanza kujua.” Mina akainama. Akakumbuka
alivyokuwa akimpuuza siku chache
zilizopita. Akabaki ameinama akimfikiria kaka huyo. ‘Ni upendo wa namna gani huu!’ Mina akajiuliza.
Pius sio mchovu mchovu. Ni mtu mwenye nyadhifa ya juu
sana na familia yake. Kaka mzuri wa kupata mwanamke yeyote yule anayemtaka
mbali na Raza. Lakini bado amemng’ang’ania! Mina akashindwa kumuelewa.
“Kingine.” Mina akanyanyua uso kumuangalia. “Pesa
isiwahi kuwa tatizo. Nitajitahidi kuwa nikiweka pesa kila wakati. Ni
rahisi na salama. Hapatakuwa na maswali.” “Labda kwako, lakini si kwangu. Najua
nimewashangaza wengi shem, lakini naomba uniamini shemeji yangu,
sija.....” Mina akasita kisha akaendelea.
“Najua ni ngumu kueleweka kwa sasa. Na sitaaminika.
Ila nakuomba, kwa imani tu. Niamini shem. Sina mahusiano ya nje
ya ndoa yangu. Vile ulivyokuwa ukinikuta nipo nyumbani kwangu wakati wote,
ndivyo ilivyokuwa. Hakuna kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia.
Hata marafiki walinishinda sababu ya Ayan. Ilikuwa lazima niwepo alipo
kwa kuwa niliona ni kama kwenye nyumba za wengi hatakiwi. Ndio maana
nilikuwa nikijitahidi sana kupunguza safari za mbali na mtoto wangu, ili
niweze kuwa naye. Na nilikuwa nikitoka, endapo ikinilazimu tu. Tafadhali naomba
uniamini.” “Naomba nikushauri kitu
Mina.” Mina akakubali.
“Narudia tena. Kitendo cha wewe wakati wote kujua ni nini
chakufanya, ni hatua ya kwanza na kubwa ya msingi. Kama
nimekuelewa, utamtunza mtoto. Si ndiyo? Au utakuja kumtoa?” Mina akashituka
sana. “Hapana shemeji! Sitathubutu na Mungu anisaidie. Nitahangaika
naye hivyo hivyo. Ila sitaua kiumbe kisicho na hatia!” “Na mimi sitakuacha uhangaike
naye.” Mina alikuwa hamuelewi Pius. “Anawezaje!” Akajiuliza bila jibu.
“Nitakusaidia kwa kadiri niwezavyo, labda
usiniambie. Kwa hiyo kama nilivyokuwa nikisema, weka akili na mawazo yako
kwenye hilo. Jiangalie kwa makini sana afya yako. Hilo liwe la kwanza
na la muhimu. Utulivu ili usianze magonjwa ya moyo. Tafuta faraja
katika hilo, ukijua baada ya muda utakuwa na mtoto wako. Acha kwa sasa kuhangaika
kuaminisha watu kwa hili linalokupata. Haimuhusu tena mtu.
Halafu limeshatokea, huna chakufanya. Watu huamini kile
watakacho. Achana na watu kabisa kujieleza ili wakuamini. Kutafuta ni nini chakujitetea,
iwe sio kipaumbele, na usifanye hivyo. Sawa?” Mina akatingisha kichwa kukubali.
“Halafu tunza ujauzito wako vizuri. Hakikisha
unakula vizuri na kulala vizuri. Achana na mawazo yakuhangaika kutafuta
kazi kwa sasa mpaka ujifungue na mtoto akue kidogo. Mimi nitakuwa
nikikuwekea pesa kila mwisho wa mwezi. Hesabu ndio mshahara wako,
kazi ni kulea huyo mtoto tu.” Mina akajifuta machozi.
“Na ili usipoteze ujuzi. Fanya kama ulivyokuwa
ukifanya nyumbani. Sijui kama uliondoka na laptop yako.” “Ninayo.” “Basi endelea kufanya mazoezi. Ukiona
upo tayari anza kutengenezea watu website. Na
mimi nikipata kazi au mtu anataka afanyiwe kazi zake nitamtuma kwako. Tengeneza
hizo logo, website, kadi za harusi na mialiko mbali mbali. Tena unaweza hata
kununua mashine ukawa ukifanyia tu nyumbani, unawatumia ili tu usiboreke.” Mina akalifurahia sana hilo wazo.
“Tafuta mashine ya kuprint, ndogo na nzuri, ya kisasa,
utakayoweza kuiweka ndani. Niambie bei yake. Nitakununulia. Na mimi
nikiiona kabla yako, nitainunua. Au nikipata mtu anayesafiri
nitamwagiza.” Kidogo Mina akatulia. Akaanza kuona mambo yatafanyika tu.
“Nakusihi utulie kabisa Mina.” Wivu wa kuishi
mbali na Mina ukaanza kumsumbua Pius. Akaingiwa na wasiwasi wakuwa naye mbali, akaanzisha
mahusiano mengine.
“Tulia, weka mawazo yako kwako na kwa mtoto, basi.”
Mina akamuelewa. “Nitatulia. Nakuahidi nitatulia. Siwezi kujichanganya
tena kwa sasa. Nitatulia shem.” “Basi. Tuwasiliane tu. Swali lolote
lile, tuwasiliane. Ukikwama popote pale, nitafute, tutashauriana.”
“Asante. Na nitafanya hivyo. Ila usiponisikia kwa muda, ujue ni kwa kuwa
nimepumzika pengine nahitaji muda wakujiweka sawa. Nikitulia kabisa, nitakutafuta.”
“Hiyo naichukua kama ahadi ambayo hutaivunja
Mina. Nitakusubiri. Naomba usichukue muda mrefu kunitafuta.” Mina
akamsogelea. Akambusu shavuni na kumkumbatia. Alilia Mina. Akalia huku
amemkumbatia shemeji yake. Pius akawa akimbembeleza tu. “Kila kitu kitakuwa
sawa, na utashangaa.” Akambusu tena shavuni na kukaa pembeni. Akaona aende
akaoshe uso, akarudi.
“Kesho nitatoka mapema sana kuanza kutafuta pakuishi.
Kwa hiyo huna haja yakuja.” “Basi na mimi nitakwenda kuweka pesa ili ikusaidie
upate nyumba nzuri na vifaa vyakuanzia maisha.” Mina hakuamini kinachomtokea.
Alijua atapata shida, lakini akajikuta
mambo ni mazuri ni kama maisha mengine yalikuwa yakimsubiria NJE ya
ndoa yake. Wakaagana, Pius akatoka.
Mina na Makazi Mapya.
Ujasiri
ukaongezeka kwa Mina. Anaanza maisha na pesa! Mungu ampe nini! Ilikuwa
bado ni mapema tu pale Pius alipomuacha. Akaanza kupigia simu watu aliosoma
nao, waliomfahamu akiwa Mina mke wa Andy Ruhinda. Akaanza kuulizia kama
wamesikia sehemu kunakodishwa nyumba ndogo. Iwe chumba kimoja, au
viwili. Iwe inajitegemea. Mina
alihangaika usiku huo kwa simu, akitaka kujua hata kama kuna mtu anafahamu
dalali, lakini mpaka saa tano usiku, hakuwa amepata jibu la kueleweka. Akabaki
akiwaza.
Na kote alipokuwa akiwapigia, alijaribu kuulizia kodi
walizokuwa wanalipa wao na familia zao. Akagundua maisha ya Dar ni magumu.
Wengi wakamshauri labda akakae nje kidogo ya mji ndio itakuwa nafuu. Akabaki
akiwaza. Akajiambia ahadi za shemeji, zitabaki kuwa ahadi mpaka ziwe zikitimia.
Chochote chaweza kutokea, akabadili mawazo. Akaona wazo la marafiki zake ni
jema. Heri akaanze maisha mbali na jiji la Dar.
“Nisije
kutapanya pesa ndogo niliyonayo, nikitegemea ahadi.” Akawaza Mina. “Wapi
niende?” Swali likafuata. Mina mtoto wa jiji la Dar kama si kwa mama yake
basi kwa wanaume. Hakuwahi kuwaza anakula nini wala analala wapi. Mama yake na
hao wanaume waliokuwa wakimtorosha kwao ndio waliokuwa wakihangaika
naye. Akaja na Andy ndio akamuhamishia kwenye apartment wala asijue analipa kiasi gani.
Sasa yupo mtaani na mimba asiyojua ameipataje! Ameachika,
nyumbani amefukuzwa. Lakini maisha lazima yaendelee. Hajui maisha
mengine isopokuwa hapo jijini Dar na... Mina akakaa. “Iringa!” Akaongea kwa
sauti. Akakumbuka alishaishi Iringa na Omar. Akapapenda japo alikuwa akifungiwa
ndani. Alipenda hali yake ya hewa, moyo ukajawa furaha. Akaona huko kutamfaa.
Akapanga mipango yake akakubaliana nayo ndipo akalala.
~~~~~~~~~~~~~~
Aliamka asubuhi na mapema kabisa. Akapiga simu
mapokezi kuomba aitiwe usafiri. Ilipokuja, akapandisha mizigo yake yote, safari
ya kutafuta kituo cha mabasi yaendayo mikoani ikaanza. Akafurahia maamuzi yake,
akakumbuka shemeji yake alimwambia kitendo chakujua nini chakufanya wakati wote ndio njia ya mafanikio, hata kama
si sahihi, ni heri ajaribu akosee, kuliko kubaki njia panda hajui chakufanya.
Alifika kituo cha mabasi, akapata tiketi yake,
wakampandishia mizigo yake yote, mabegi ambayo alikuwa ameshayaandika jina lake
na namba ili yasipotee au kuibiwa hata moja. Akamuonyesha kondakta ambaye
angekuwepo kwenye hilo basi. Andy alimnunulia masanduku mazuri sana. Akajiambia
ndio kiinua
mgongo chake alichotoka nacho kwa
Andy. Akajicheka. Akataka kufikiria hilo, akakumbuka alivyohusiwa na Pius.
Atafute faraja, asiwaze vitu vitakavyomnyima raha. Akatoa mawazo huko.
Akapanda basi na kutulia kwenye kiti na kumtumia ujumbe Pius akimtaarifu
maamuzi yake kuwa anahamia mjini Iringa.
~~~~~~~~~~~~~~
Hakuwa amekumbuka swala la baridi ya mkoa huo wa
Iringa. Basi lilifika mida ya jioni, Mina anatetemeka baridi. Akachukua tena
taksii mpaka hotelini na kwenda kujifungia. Kwa hofu ya kuishiwa na hakuwa
akitapika, alichukua hoteli ya kawaida sana, tena mtaani kwani hakujua atakuwa
hapo kwa muda gani.
Kesho yake akaenda mapokezi kuzungumza na muhudumu wa
hapo. Akamueleza uhitaji wake wa sehemu ya kuishi. Akamwambia shemeji
yake yupo anamalizia nyumba ndogo ya chumba kimoja cha nje, alimsikia akitaka
kukifanyia biashara. “Naomba namba yake ya simu.” “Lakini bado hakijaisha
vizuri. Nafikiri amekwama pesa.” Yule kijana, muhudumu akamtahadharisha. “Wewe
nipe namba yake.” Yule kijana akamtajia, hapo hapo Mina akapiga.
Huyo mama akapokea, akamwambia ni kweli anayo sehemu.
Alianza kujenga. Lakini ameishiwa pesa. “Nimeshafunika
juu na inayo madirisha na mlango tayari. Mpaka umeme upo, sema sijavuta maji na
choo cha ndani hakijakamilika.” “Naweza kuja kupaona?” “Nipo nyumbani. Karibu.
Kama unachukua taksii mwambie akulete mtaa wa Gangilonga. Aje mpaka mwisho
kabisa. Mwambie jiweni kwenye nyumba za Kotazi. Nyumba yangu ipo mwisho kabisa.
Juu, upande wa kushoto kama unatokea mjini, na ina nyumba ndogo nje, lakini
nyuma.” Wakakubaliana, Mina akarudi ndani akajiandaa na kutoka.
Akachukua taksii aliyoipata hapo nje tu ya hiyo hoteli.
Yule kijana muhudumu wa pale akamsaidia kumuelewesha
dereva taksii, kwa kuwa yeye anapafahamu na ni mwenyeji. Kwa urahisi sana yule
dereva akawa ameelewa. Wakaondoka mpaka kwenye hiyo nyumba. Akamkuta huyo mama.
Akachukua funguo na kwenda kumuonyesha.
“Mpaka kigeti cha nje nilishaweka.” “Mbona hii ipo tayari
kabisa!” Mina akashangaa. Mina akaingia
upande wa choo. Akashangaa. “Hii ni kazi ya siku moja au mbili tu mama yangu.
Wewe kama unaye fundi mpigie. Tuandikishane mkataba, mimi nikupe hela,
animalizie, kesho au kesho kutwa nihamie.” “Kama pesa ipo, mume wangu ndio
mjenzi. Atatengeneza kwa haraka tu.” Hilo likamfurahisha Mina.
Wakaingia ndani ya nyumba ya huyo mama, wakaandikishana
kuwa amemkabidhi pesa kwa ajili ya ujenzi hapo, utakapoisha yeye Mina ndiye
atakayehamia na pesa aliyompa ndio itakuwa kodi. Wakawekeana saini, Mina
akamrushia pesa hapo hapo bila tatizo, akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya siku tatu, Mina akahamia hapo akiwa
amesaidiwa na kijana wa huyo mama ambaye alikuwa na gari. Akaenda naye kununua
kitanda cha kawaida tu, godoro, meza, kabati na vyombo. Kila alipokuwa
akikumbuka kitu, alimuomba waongozane kwenye manunuzi. Mpaka anamaliza week, nyumba ya Mina ikawa inavitu vichache, vyakawaida
sana, lakini panakalika. Ndipo akapumzika. Kwa mara ya kwanza akawa na kwake.
~~~~~~~~~~~~~~
Siku kumi na nne tokea apelekwe na Pius kwa daktari,
Mina akaishiwa zile dawa za kuzuia kutapika. Na zenyewe alikuwa akila kama pipi. Kila akisikia kichefu chefu anameza. Akaishiwa. Siku
ya tatu yake, kazi ya kutapika ikarudi vile vile. Akawa hawezi kulala wala
kufikiria. Nikutapika tu. Yule mama pale akajua, akamfariji kuwa baada
ya miezi mitatu, atakuwa tu sawa. Akawa na kazi ya kuhesabu siku akisubiri hiyo
miezi mitatu ya mwanzo wa ujauzito iishe, apumzike kutapika.
Kwa Andy.
Huku kwa Andy yeye, siku aliyomrudisha Mina
kwao, alitoka hapo akiwa amejawa na hasira, na aibu juu.
Akikumbuka jinsi alivyoonywa na mama yake asimuoe Mina, akakimbia
naye mpaka Kenya na kwenda kumuoa huko! Alikuwa akiendesha huku akifikiria hili
na lile, roho ikimuuma sana. Akakumbuka hili na lile nakuzidi kuumia. “Yaani mimi nahangaika huko, Mina anafanya
umalaya, tena bila kinga!” Andy akazidi kukasirika huku maneno aliyojazwa
na dada yake yakijirudia kichwani.
Akaendesha mpaka kwa dada yake ambako yupo mtoto wake.
Akafika hapo ilikuwa inakaribia saa nne usiku. Kila mtu amelala kasoro Paulina.
Akamwambia Ayan alishakwenda kulala. Akaomba mchukue hivyo hivyo. Paulina
akamuamsha na msichana wa kazi, Andy akashukuru na kuondoka nao wote
wawili.
Alirudi nyumbani asiamini kama Mina hayupo
pale. Lakini akajifariji angalau yeye na mtoto wake watalala pazuri bila
kelele ya kutapika. Alishamsikia Mina akitapika, akajua uwepo wake pale
ndio ungemkera zaidi. Heri alivyomtoa usiku uleule.
Akaenda kumlaza mtoto wake chumbani, akamkuta yule
msichana kwenye makochi. Akashindwa kuelewa. “Kwani wewe ulikuwa ukilala wapi?”
“Hapa kwenye makochi japo dada aliniruhusu niwe nalala chumbani kwa mtoto.
Alisema hamna neno, lakini mimi napenda kuangalia tv. Nikiamka hata
usiku au asubuhi, nawasha, mwenyewe naangalia. Hapa nilikuwa nasubiri patulie,
nirudi kulala hapa kwenye makochi. Na..” Andy akaondoka kama ambaye ametosheka
na hayo maelezo. Mamu alikuwa muongeaji
haswa.
Andy akatoa mizigo yake yote kwenye gari akawa
anapandisha juu. Yule msichana ametulia kimya akimtizama tu. Hakumsaidia hata
kwa kujisogeza. Andy akaingia chumbani kwake na kufunga mlango. Mamu akajua
ndio amekwenda kulala, akawasha tv mida hiyo kwenye nyumba hiyo ya vyumba
viwili tena ndogo tu.
Andy akaenda kuoga, akatoka wakati anavaa nguo za
kulalia, akagundua hiyo tv kweli imewashwa usiku huo. Akanyamaza. Akasema labda
itazimwa, atoe nguo kwenye masanduku aliyotoka nayo safari apange
kabatini mpaka Mamu alale.
Andy akakutana na zawadi nyingi alizokuwa
amemletea Mina. Akaumia sana. Akaanza kazi ya kuzirudisha ndani ya begi.
Zote za Mina akaweka kwenye hilo begi na kusukumia uvunguni mwa kitanda.
Alitumia pesa nyingi sana kwa ajili ya zawadi za Mina. Ilikuwa ni kama kumshukuru
na kumpa pole ya upweke.
Mpaka saa saba usiku tv ilikuwa inatoa
tu sauti. Akatoka, akamkuta Mamu ametulia kimya anaangalia kama ndio pamepambazuka.
“Siwezi kulala na kelele za tv.” “Naweza kupunguza sauti.” Mamu akamjibu bila
hata shaka. Akachukua rimoti, akapunguza Andy akimwangalia. “Hiyo sauti hapo pia itakukera!? Maana ni kama
nimebakisha tano tu! Au nayo unataka nipunguze?!” Mamu akamuuliza Andy yaani
kama anayemuingilia kwenye maisha yake, Andy akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Asubuhi Andy akaamshwa na sauti ya mtoto wake
anaongea kitandani. Akajua amemka. Akawa anasubiria kuona kama
Mamu atamtoa hapo. Ayan akaongea hapo weee akiendesha magari yake hapo
kitandani, kisha akabadilika akaanza kumuita mama yake. Andy akaona atoke tu.
Akamkuta Mamu amelala kwenye kochi, kavua shati, amejifunika kanga, hana habari
utafikiri ndio usiku wa giza nene!
Akapitiliza chumbani kwa Ayan akamkuta amesimama.
Akajua njaa ndio inayomfanya asimame mpaka atake kuruka kitandani. Tayari
ilikuwa saa nne asubuhi. Kitanda chake kilizungushiwa mbao za urembo kama
kulinda asianguke. Akamtoa kitandani kwake.
Akaelekea jikoni. Akafungua friji. Akakuta uji. Akajua
ni wa siku zilizopita. Ulifanana na mapishi ya Mina. Akajua ni Mina ndiye aliyepika,
ulipobaki akauhifadhi humo. Ayan alionekana na njaa, hawezi kusubiri.
Akampashia moto huo uji, akamwambia akae kwenye meza, akaanza kumlisha
mpaka akamaliza. Lakini Ayan akawa akimwangalia kama hamuelewi vizuri au
anayemfananisha. Andy akajua.
~~~~~~~~~~~~~~
Hawakuwa wameonana kwa muda wa miezi 4 na hata
alipokuwepo hapo hawakuwa karibu kihivyo. Hata kipindi cha mwisho alipokuwa
naye, wakati Mina anafanya mitihani, Mina alikuwa akimlisha mtoto wake
na kumfanyia kila kitu ndipo anamuacha na baba yake anakimbilia kufanya
mitihani akimaliza anarudi haraka nyumbani.
Wakajikuta wote ni wakimya. Ayan anakuwa kimya, na baba yake anakuwa na shuguli
zake. Kama hayupo kwenye simu basi ana mambo yake kwenye kompyuta. Ayan akiona
baba yake yupo busy,
anaelekea chumbani kwake kuchezea magari mpaka amuite au mama yake arudi kutoka
shule. Kwa hiyo hawakuwa karibu kihivyo.
~~~~~~~~~~~~~~
Ayan akabaki kimya hapo mezani akila, akimtizama kama anayemfikiria.
Alipomaliza tu uji, akamuomba baba yake maziwa. Ndivyo alivyozoea huyo mtoto.
Kila chakula, lazima amalizie na maziwa. Hapakuwa na maziwa. “Hamna
maziwa.” Ayan akamtizama baba yake kwa muda, akamuona anashuka kwenye kiti.
Akaelekea kwenye friji. Andy akasimama. “Huko kwenye friji pia hamna,
Ayan. Twende tukanunue.” Andy akamsafisha, wakatoka hapo. Mamu amelala
hata hajageuka!
Wanarudi, ilishakuwa saa sita mchana. Mamu bado
amelala. Ikabidi amuamshe. “Kwani sasa hivi saa ngapi?” Akamuuliza Andy. Andy hakumjibu,
akaendelea na shuguli zake. Kumuogesha Ayan huku akifikiria pengine Mamu
ataanza kupika chakula cha mchana. Na yeye akaoga wakati Ayan amekaa chumbani
kwake, akichezea magari yake.
Andy akatoka, Mamu amekaa kochini. Akamdaka. “Nilikuwa nakusubiria unipe pesa ya chakula, nikale.”
Andy akabaki akimtizama. “Mwenzio dada alikuwa akinipa hela nikale huko huko
kwa kuwa humu ndani alibadilisha utaratibu, akaacha kupika. Akawa
hataki kupikwe tena. Kwa hiyo nikawa naenda kula chips.” “Kwani wewe
kazi yako humu ndani ni nini?” Andy akamuuliza.
“Si kazi za ndani! Lakini dada alikuwa akipika
mwenyewe, na mwanae ana muhudumia mwenyewe. Nikajua ndio utaratibu wake. Kila nyumba ina utaratibu wake, inategemea na
huyo tajiri. Sasa dada wa hapa yeye nili..” “Subiri kwanza.
Unaongea sana unanifanya nashindwa kufikiria.” “Mbona nilikuwa
nakujibu tu! Labda kama hupendi...”
“Nimekuomba unyamaze kidogo tu. Haya, kwa
kifupi sana, nani amekuleta hapa. Taja tu jina bila maelezo.”
“Unamjua yule Raza?” “Kwa hiyo umeletwa hapa na Raza?” Andy akauliza akitaka
kufupisha habari.
“Hapana! Yaani Raza, ni kama ndiye ninayefahamiana
naye mimi. Ndio akaniambia kuna mama anataka mfanyakazi, kwa kuwa mfanyakazi
wake ame..” Andy akafunga macho. “Nani amekuleta hapa?” “Si ndio
nakujibu sasa?!” “Tafadhali nipe tu jina.” “Ndio hivyo! Raza akanipeleka kwa
mama yake mkwe, ndio mama yake mkwe akasema hapa pana uhitaji kuliko
yeye, ndio akanileta hapa. Tena wakati huo mkeo alikuwa kavunjika mguu.
Hana ile hali yake..” “Wazazi wako au ndugu zako wako hapa karibu?” “Unamjua
mama yake wa kufikia Raza?” Andy akaondoka.
Akatoka kabisa pale akaenda kumpigia simu mama yake. “Shikamoo mama.” “Marahaba. Vipi safari?” “Ilikuwa nzuri tu.
Naomba nikushukuru kwa msaada mliokuwa mkimpa Mina zaidi kumlea Ayan.” “Mkeo
alikuwa akihangaika naye huyo Ayan yeye mwenyewe, Andy. Msaada ni kidogo
tu.” Andy akatulia kidogo kama tena anachanganywa.
Ila akaendelea. “Nilikuta
msichana wa kazi hapa. Lakini nafikiri hapa ni padogo sana na mimi nipo
mwenyewe. Sidhani kama ni sawa kuishi hapa na msichana kama huyu. Si sawa.”
“Umewaza vizuri. Unaweza kumleta tu hapa, nitamrudisha kwa Raza.” “Asante.” Andy
akaaga na kurudi ndani.
“Una mizigo yeyote hapa?” “Kijibegi tu hapo chumbani
kwa mwanao.” “Ulishakaa humu ndani siku ngapi?” Akaanza kuwaza. “Mmmh!” Akaguna
Mamu. “Wala si muda sana. Ni kipindi kileee...” “Umeshamaliza mwezi?” Andy
akauliza tena akitaka kufupisha habari. “Nahisi. Kwani vipi?” “Nataka kukulipa,
nakurudisha kwa mama. Kwa sasa hivi mimi sihitaji msaada wowote humu
ndani.” “Sawa.” Mamu akanyanyuka bila shida akaenda kuchukua kibegi chake.
“Sasa unanirudisha na njaa!? Maana sijala.”
“Naamini kwa mama kutakuwa na chakula.” Andy akamuita Ayan, akamwambia
wanakwenda kwa babu. Wakatoka. “Si ungenipitisha hapo nikanunue hata chips yai!
Au unaona nitakuchelewesha?” Mamu akamuuliza. Andy kimya. Akafungua gari.
Akamfunga mtoto wake mkanda, akamwambia apande. Hakumjibu mpaka walipofika kwa wazazi
wake ndipo akamwambia ashuke.
Hakumkuta mama yake mida hiyo ya mchana. Akampigia
simu kumwambia amemuacha hapo, na kama kuna malipo yeyote yale, amalizane naye,
yeye atamrudishia. Hakutaka hata kuzungumza na Mamu tena. Akaondoka na
mwanae baada yakumchukulia maziwa hapo. Uzuri wa Ayan awe na maziwa mdomoni.
Hutamsikia akiongea. Andy akaenda kununua vitu vya kupika hapo ndani na
mahitaji mengine. Alikuwa na likizo ya siku 15, akaona azitumie na mtoto wake
wakati akijipanga upya. Maisha yakaanza.
~~~~~~~~~~~~~~
Mwezi wa kwanza ukawa wa hasira sana akimlaumu
Mina kumuharibia mipango yake. Kumpotezea muda. Kujilaumu
kwa nini aliamini yeye ndio ataweza kumtuliza Mina, mwanamke
aliyezoea kuwa na wanaume zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja. Akamlaumu
wee huku maisha yakiendelea mpaka likizo ilipoisha. Ukweli mambo ya kazini
kwake bado hayakuwa yamekaa sawa kama alivyokuwa amemuhidi Mina,
kuwa akirudi atatulia sehemu moja na familia.
~~~~~~~~~~~~~~
Ikabidi kurudi kuzungumza na wazazi wake, akawaomba
Ayan akae hapo kwa muda mfupi tu, wakati anakwenda Dodoma kuweka mambo sawa.
Wazazi wakakubali kwa makubaliano ya kumuongeza msichana wao wa kazi mshahara
ili angalau Ayan aangaliwe na msichana wa kazi wakati Andy yupo Dodoma.
Mwezi wa kwanza ukaisha, na wa pili pia. Andy anakuja
kila weekend. Anamchukua mtoto wake, anakwenda kukaa nae kwao,
jumatatu anamrudisha tena kwa wazazi wake, anarudi zake Dodoma.
Wazazi wakaona siku zinazidi kwenda, hachukui
mtoto wake. Hawakumuuliza mbona makubaliano yalikuwa ya mwezi tu. Kimya, wakijiangalizia.
Mzee Ruhinda na mkewe ni watu wazima wenye majukumu mazito. Hawashindi
nyumbani. Na swala la kusafiri ni kitu cha kawaida sana kwao.
Katikati ya mwezi wa pili wa kuishi hapo, wazee hao
wakawa na safari wote wawili. Kwa kuwa afya ya Ayan
ilishaanza kuyumba, kwa kukosa matunzo, wakamshauri Andy mtoto ahamie
kwa dada yake, wakati anajiweka sawa. Paulina naye akamwambia hamna shida
kabisa, msichana wake anapenda watoto, Ayan ahamie hapo.
Ayan akahamia kwa shangazi yake. Mara akakae na
baba yake siku za weekend, endapo
weekend hiyo atarudi jijini kama hatazidiwa na kazi, jumatatu
anarudishwa tena kwa Paulina. Mara apelekwe kwa mzee Ruhinda
akakae na msichana wao wa kazi, msichana wa Paulina akiwa anaumwa au
Paulina akisema anampa msichana wake mapumziko. Ikawa FUJO tu, huyo
mtoto hajulikani ataamkia nyumba ipi.
~~~~~~~~~~~~~~
Andy akaanza kumkumbuka Mina. “Aliwezaje kusoma na huyu mtoto!” Akajiuliza Andy. “Hata huo uhuni alifanya saa ngapi na
kumlea huyu mtoto muda gani!” Hapo Andy akajiuliza na kumpongeza Mina. Ayan
aliyekuwa na mama yake sio huyu! Alikuwa amekonda haswa. Ungejua
wazi HANA matunzo.
~~~~~~~~~~~~~~
Siku hiyo Pius alipita kwa waazazi wake kuangalia
nyumba, akamkuta Ayan na msichana wa kazi. Kwanza akashangaa. Ayan alikuwa amebadilika,
amekonda, ametulia peke yake kwenye kochi. Msichana wa kazi naye
na shuguli zake. Pius akaumia sana. Akamkumbuka Mina na kile alichomuomba
rasmi. Akampigia simu Andy kumtaarifu atamchukua Ayan kwenda kuishi naye kwa
muda mpaka wazazi warudi hapo. Andy akamshukuru na kumruhusu.
Raza ni mkali haswa. Hataki ujinga kwa
mtoto wala mkubwa. Ukizingatia ni Ayan, mtoto wa kiume ambaye yeye hakujaliwa,
chuki yake ikawa waziwazi. Pius akawa anajitahidi kumuhudumia yeye
mwenyewe kwa kadiri anavyoweza. Napo akashindwa. Nyumba
mwanamke! Raza akazidi kumlalamikia
kuwa lazima Ayan aondoke pale, kabla msichana wao hajaondoka kwa kulemewa na malezi ya ziada
ya huyo mtoto ambaye hakuwa kwenye makubaliano naye tokea mwanzo. Raza akasema
watoto wake yeye, au wao ndio wataishia kulipa gharama ya umalaya wa
Mina. Raza akaweka mguu chini, hamtaki
huyo mtoto hapo kwake. Pius akasalimu amri.
Kwa shingo upande
akijua uvivu wa Paulina, maana hata watoto wake yeye mwenyewe wanalelewa na
mumewe Devi, ikabidi kumrudisha tena kwake. Ayan akawa mtoto wa kumangamanga.
Leo yupo Msasani kwa babu na bibi yake akilelewa na mfanyakazi, kesho Kinondoni
kwa shangazi yake, kidogo anarudishwa Mikocheni kwa Raza, Pius akijua atawahi
kurudi nyumbani anaenda anampitia popote alipo Ayan, anakwenda naye kwake. Dad
wake akifanikiwa kurudi jijini Dar, anamfuata huyo mtoto alipo. Anakaa
naye siku mbili, anahamishwa nyumba nyingine, dad anarudi kazini Dodoma. Maisha
yanaendelea.
~~~~~~~~~~~~~~
“Mwenzio mama alikuwa akimchapaga Ayan. Usimuone mdogo
hivyo, mama anasema anachapika sana.” Mtoto mdogo wa Raza akamwambia
babu yake alipomkuta amekaa na Ayan. Babu yake akanyamaza akishangaa moyoni
vile huyo Ayan alivyo mkimya, unawezaje kumchapa! “Halafu kama hivyo unavyompa
maziwa hivyo, mama alikuwa anasema dada amchanganyie na maji. Asinywe
maziwa peke yake, ni gharama.” Akaongeza huyo mtoto.
“Babu! Si na
wewe unajua maziwa ni gharama sana? Hata mama mwenyewe hanywi chai ya
maziwa vizuri sababu ya ugumu
wa pesa.” Mzee Ruhinda akajua hayo ni maneno ya mama yake sio yule mtoto. Mzee
Ruhinda akamtuma maji ya kunywa ili kumtoa kwenye hayo mazungumzo.
Mzee Ruhinda akaumia sana lakini asijue
atamsaidiaje huyo mtoto. Baba yake haonekaniki kuwa na dalili ya kutulia
na mwanae. Ayan afya yake inazidi kubadilika na yeye majukumu yake yanazidi
kumsonga. Yeye na mkewe wakajiambia labda kwa kumpeleka Andy shule za bweni
huko Nairobi kumemuathiri. Haoni shida kumuacha mtoto wake kwa watu.
Wakashangaa hata hiyo afya yake haimshitui! Ila wakaamua kunyamaza.
~~~~~~~~~~~~~~
Tembo
Wakigombana, Manyasi Ndio Huumia.
Inaendelea…..
0 Comments:
Post a Comment