Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 27. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 27.

Mina akarudi. “Hujambo mama?” Mzee Ruhinda akamsalimia kwa kujali. Mina akashangaa wanamshangaa. “Kwema!?” Mina akauliza akiwatizama wote hapo sebuleni. Kimya. “Mbona mnanitisha! Kuna nini!?” “Acha woga wewe. Subirini chakula sasa hivi kitakuwa tayari.” Paulina akaongea wakati ananyanyuka kwenda jikoni. “Unataka msaada?” Mama Ruhinda akasimama na kumfuata nyuma. Raza naye akamfuata, Mina akakaa wala hakuwafuata jikoni.

“Unaendeleaje baba?” “Mimi mzima Mina mwanangu na wewe?” “Mimi hata sijui baba! Nimeanza kujisikia vibaya! Lakini siumwi kichwa wala sina homa!” Mina akaongea kwa kulalamika kidogo. “Umekwenda hospitalini?” Paul akauliza. “Sijaenda. Nimeanzwa kama siku tano sasa. Nikawa najiambia labda ni hali tu ya hewa! Kwa kuwa sina homa, lakini bado! Yaani hapa nimetoka nje kutapika.” Mina na moyo wake akaongea bila hila.

“Pole mama. Inabidi kwenda hospitalini.” Mina akabaki ameinama. “Pole sana.” Pius akaongeza. “Sina raha baba, na sijui ni nini!” Mina akaongeza kwa kulalamika, kina mama Ruhinda wanasikiliza jikoni. “Tukimaliza kula, mimi nitakusindikiza hospitalini Mina.” Akadakia Paulina. “Usiku huu!?” Mina akashangaa. “Sasa utaendelea hivyo mpaka lini.” “Na kweli! Andy wangu anarudi jumatatu. Sitaki anikute hivi  wakati anahamu na sisi kweli! Nimeshindwa hata kumwambia kama naumwa ili nisimkatishe tamaa yakurudi nyumbani. Lakini naona ni kweli niende hospitalini ili kama kunakutibiwa nitibiwe nipone.” Mina akaendelea kulalamika.

“Na kweli umedhoofu.” Mzee Ruhinda akaongeza. “Yaani baba, sili chochote! Na harufu ya chakula imenishinda kabisa! Sitaki hapo nyumbani kupikwe kitu! Ayan wangu anakunywa tu uji na hayo maziwa! Mamu ndio huwa namwambia akale nje, mpaka najisikia vibaya! Sijui nimepatwa na nini na sijawahi kupatwa na hii hali jamani!” Mina akaongea kila mtu akimsikiliza. “Pole Mina. Basi ni heri ukamuone daktari.” Paul akaongeza. “Nitafanya hivyo.” Mina akakubali bila shida akiwa bado ameinama.

Baada ya muda akasimama kuelekea jikoni walipokuwepo wanawake wengine. “Wifi, naomba chakula kidogo tu nimlishe sasa hivi Ayan kabla hajasinzia. Sijampa chakula kizito kama siku tano sasa.” Ile ameingia tu jikoni, wakamuona anatoka mbio kwenda chooni. Wakamsikia akitapika.

Mmethibitisha sasa?” Akadakia Mamu kimbea! “Wewe mtoto acha umbea wewe! Kwanza umetoka wapi wewe! Huna hofu!” Mama Ruhinda akamkemea kabisa. Mamu akapoa. Akatapika Mina, nyumba nzima akasikika yeye akitapika.

Akatoka. “Pole sana mama.” Mzee Ruhinda akampa hiyo pole. Mina macho mekundu. “Mimi naona nirudi tu nyumbani, nisiwaharibie usiku wa leo.” “Bila kula!” Akauliza mama Ruhinda. “Yaani mama, hivi ninavyotapika, ndio hivyo. Siku ya tano sasa mama yangu. Sina raha! Nakuwa kama mtu mwenye mimba changa, wakati hata nilivyokuwa na ujauzito wa Ayan, nashangaa sikuwa nikitapika hivi! Kwanza nilikuja kuambiwa na mama kama ni mjamzito wa Ayan. Hata sikuwa nikijijua kama nina mimba vile ambavyo mimba haikunisumbua!” Maskini Mina akaongea kwa huruma bila hila.

“Hapana. Wewe acha mtoto akilishwa hapa, mimi na wewe twende hospitalini mara moja. Upimwe, wakupe dawa. Si sawa uendelee kuteseka.” “Asante wifi yangu. Hata mimi naona niende tu. Nateseka, na naona namtesa na Ayan wangu. Anakunywa uji na maziwa tu! Hapana. Nilijua vitaisha, lakini wapi!” Mina akaendelea kulalamika, wakimsikiliza huku akienda kuchukua pochi yake, Paulina akaacha chakula nakuwaambia watarudi baada ya muda mfupi tu. Akatoka na Mina akiwa anamuendesha kwenye gari yake.

Marefu Yasiyo Na Ncha.

Akampeleka hospitali ya kulipia. Jumamosi hiyo hawakukuta hata wagonjwa wengi. Walipofika mapokezi wakakutana na daktari amesimama hapo mapokezi akizungumza na manesi. Paulina akaanza kutaniana naye. Yule daktari alionekana kufahamiana sana na Paulina. Kumbe alisoma na Paul. Anawafahamu kina Ruhinda wote.

“Huyu mke wa Andy.” “Nafikiri tumeshawahi kuonana.” Daktari akaongea akimgeukia Mina. Mina hata  hakuwa akikumbuka. Na ile hali aliyokuwa akijisikia pale hata hakumkumbuka.

“Kwema lakini?” Daktari akamuuliza Paulina. “Naona utatusaidia.” Paulina akaongeza. “Bila shaka. Twendeni ofisini.” Wakaongozana mpaka kwenye ofisi au chumba ambacho anaona wagonjwa. “Wifi yangu ndiye anayeumwa.” Paulina akamtaka Mina ndiye azungumze sasa. Mina naye akaeleza kila kitu. Vile anavyojisikia na kinachoendelea. Hata daktari akabaki akimshangaa.

Dalili zote alizokuwa akieleza ni za UJAUZITO, lakini yeye hana habari! “Hata sijui ni nini, ila sijapandisha homa kabisa!” Mina akamalizia. “Nashauri tupime na mkojo.” Daktari akaandika vipimo ambavyo ameshauri Mina afanyiwe, huku akijua kwa asilimia kubwa tu ni kama ameshajua kabisa kinachomsumbua Mina, ila kwa kuwa wapo pale na ni hospitalini, akaona athibitishe.

Wakatoka hapo kwenda maabara. Mina akaenda kutoa mkojo akiwa ameshatolewa damu kabisa. Huko chooni nako akasikika akitapika sana. Akatoka na kwenda kukaa alipokaa wifi yake wakisubiria majibu. Wakati wanasubiria majibu pia Mina akakimbilia chooni kama mara mbili tena. Harufu ya hapo hospitalini ikamshinda kabisa.

Wakaitwa tena yeye na wifi yake kwa daktari akaambiwa alale kwenye kitanda kilichokuwa pembeni hapohapo ofisini. Mina akiwa na mshangao akalala. “Siku zako umepata mara ya mwisho lini?” Akaulizwa na daktari, wifiye akisikiliza. Mina akafikiria.

“Mwezi uliopita tu. Yaani nasubiria mwezi huu.” Akajibu Mina kwa kujiamini. “Unakumbuka tarehe?” Daktari akamuuliza. Mina akavuta kumbukumbu. “Mmmh! Sikumbuki. Ila nina uhakika nilipata kabisa. Hivi hapa nategemea wakati wowote.” “Vipimo vinaonyesha ni mjamzito. Tena hii mimba ni ndogo kabisa. Upo sahihi, ni mwezi sasa.” Mina akashituka sana na kukaa.

Haiwezekani! Mimi mume wangu amesafiri na ana miezi minne sasa, na sijalala na mwanaume tokea aondoke, na miezi yote nimekuwa nikipata siku zangu!” Paulina akanyanyuka pale kama swala, akampiga vibao vya usoni viwili vya haraka. Mina akashituka sana. “Acha uongo wewe mtoto.” Akamvuta kutoka pale kitandani, dokta akawapisha. “Vaa twende, usiendelee kutuaibisha!” Daktari kimya ameduaa kwa alichofanya Paulina, na anachokisikia. Alipomaliza kuvaa na viatu vyake Paulina akamtoa hapo kwa kumsukuma kwa hasira.

Akamwambia amsubirie hapo pembeni ya mapokezi anakwenda kulipia. Mina wakati amesimama hapo, hali ya kutapika tena ikamjia. Akakimbilia tena chooni kutapika. Akatoka Paulina akimsubiria nje ya choo akiwa amejawa hasira kama yeye ndio Andy. Akamdaka kumvuta kutoka chooni akamvutia nje kwa nguvu mpaka Mina akaanguka na kujigonga vibaya sana kwenye kiti.

Wazi aliumia lakini na yeye Mina akawa kama amepatwa na kibumbuwazi. Alikuwa kwenye mshangao na mshituko juu, ila kichefuchefu hakikumpa nafasi yakufikiria. Akamuamuru warudi kwenye gari. Mina akiwa kwenye mshituko akafuata maelekezo.

Akashangaa gari inaendeshwa anarudishwa nyumbani kwake. Kimya. Akamfikisha na kumvuta mpaka juu. “Fungua.” Akaamuru Paulina. Mina akatoa funguo kwenye pochi. Paulina akampokonya. Akafungua na kumsukumia ndani kama mbwa. Akampokonya na simu na kibao cha usoni juu kama anayemchapa mtoto wake wakumzaa.

“Nachukua hii simu ili usiwasiliane na mabwana zako wakaja kukutorosha hapa, Andy akadaiwa. Malaya wewe! Umeshindwa kuvumilia, unalala hovyo hovyo na watu halafu unamtesa mtoto! Nyumbani kwao hakupikwi, sababu ya watoto wa watu wengine! Hapa ni kwa Ruhinda, na Ayan ni Ruhinda. Baba yake anahangaika ili mtoto wake aishi vizuri, wewe unamtesa! Sasa nakufungia humu. Usitoke mpaka Andy aje, ajue hatima yako.” Mina akabaki palepale aliporushwa kwenye kochi, ametoa macho ameshikilia uso alipochapwa kibao.

Paulina akatoka hapo na simu yake, na kuhakikisha amemfungia ndani kama mfungwa. Mina akakimbilia chumbani kutapika tena akiwa haelewi ni nini kinamtokea. Mimba hiyo ya Roho mtakatifu! Hofu ikaanza kumwingia mpaka kwenye mifupa.

Kwa Kina Ruhinda!

Paulina akarudi kwake na jazba kweli kweli. Anaongea kwa hasira. Akasimulia yote. “Hapa nimemfungia mpaka mumewe aje! Nimempokonya simu na funguo zote. Gari yake itabaki hapahapa. Nitaenda kumchukua Andy mimi mwenyewe huko uwanja wa ndege. Na Ayan harudi tena huko. Anamtesa mtoto bila sababu!” Pakazuka ukimya wa hali ya juu.

Mwishoe mzee Ruhinda akaaga bila ya kuongeza neno. Mkewe naye akafuata kimya kimya. Akaja Paul. “Usiku mwema jamani.” Akaondoka Paul mwenye maneno mengi lakini siku hiyo hakuongeza neno. Paulina akashangaa hapati uungwaji mkono! Devi akawaambia wanae waende chumbani. Pius na Raza nao wakaondoka na watoto wao. Ayan na Mamu wakabakia hapo.

Andy Arejea Nchini.

Shuka Limekumbukwa, kumeshakuchwa.

Siku ya jumatatu mchana Paulina akatoa kazi muhanga, akaenda uwanja wa ndege akiwa na Ayan kwenda kumpokea Andy, akitumia gari ya Mina. Walifika muda mwafaka, na Andy naye anatoka. Akamsalimia na uso wa mshangao. Akamchukua mtoto wake. Akambusu zaidi ya mara tatu. “Mama yuko wapi Ayan mlinzi wangu?” Andy akamuuliza huku akimbusu. “Naona huyo mlinzi kazi imemshinda.” Akadakia Paulina.

“Vipi tena?” Andy akauliza. Maana alizungumza na Mina asubuhi na mchana wa siku ya jumamosi. Alipojaribu kumpigia tena usiku wa jumamosi ya Tanzania, hakuwa akimpata tena kwenye simu, lakini akajua amekwenda kwa Paulina, ila akashangaa jumapili siku nzima na hiyo jumatatu asubuhi pia alipompigia kumtaarifu anaondoka nchini Uswiz simu haikuwa hewani.

Wakasaidiana mizigo ya Andy mpaka kwenye gari. “Mbona naona gari ya Mina na mtoto, yeye simuoni!?” “Panda kwenye gari twende huku tunaongea.” Andy akaanza kuingiwa na wasiwasi. Akadhani labda Mina amemkimbia na kutelekeza mtoto. Lakini alizungumza naye jumamosi asubuhi vizuri na akamwambia anamsubiria kwa hamu! Iweje leo hayupo uwanjani kumpokea kama alivyoahidi kumpa mabusu mengi pindi atakapofika. “Labda mgonjwa!” Akajifariji Andy wakati anamfunga mtoto wake kwenye kiti. Akaingia garini kiti cha mbele cha abiria, maana Paulina alikaa kiti cha dereva kuashiria yeye ndio ataendesha.

Paulina akaanza. “Sasa kuniona hapa, muda huu, siku ya kazi ujue mambo sio mazuri.” Ilikuwa saa tisa alasiri tayari. Andy akamgeukia kumsikiliza. “Msichana aliyepelekwa na mama kumsaidia Mina, alikuja pale nyumbani na kutuambia mambo yanayoendelea nyumbani kwako. Unajua muda wote Mina alikuwa akiishi yeye tu na mtoto, hakuna aliyekuwa akijua kinachoendelea. Sasa alipoumia mguu ndipo mama akamtafutia msichana wa kumsaidia kazi. Tena Raza ndiye aliyempa mama, alikuwa awe wake.” Andy kimya akimsikiliza dada yake kwa makini.

“Tena siku hiyo anatuambia huyo msichana, watu wote walikuwa nyumbani kwangu. Anasema kuna mida ni kama Mina anakuwa anataka amtoe pale nyumbani kwako, abakie peke yake. Anamwambia aende akanunue chips kuku na akalie hukohuko asirudi nyumbani na wala asiharakishe kurudi.” Andy kimya.

“Halafu hana muda wala wakumpikia mtoto. Dada akimwambia apike, anamwambia kusipikwe mle ndani, yeye atoke tu akapumzike huko na kula huko huko. Anachosema anachomuona akimpa mtoto ni uji tu na maziwa. Mtoto wa miaka mitatu eti anapewa uji tu!” Akamuona Andy kimya, anamsikiliza.

“Sasa alipokuja na yeye hapo nyumbani si akaanza kutapika! Anatapika mfululizo. Huyo msichana akatuambia ameanza kama siku tano zilizopita. Akaulizwa kama unaumwa! Akaficha wakati huyo msichana alishatuambia kama ameanza kutapika. Tena baba akamuuliza kama ameenda hospitalini. Akasema hapana, kwa kuwa hana homa. Mimi nikaona nimchukue kwa nguvu, nikajue kinachomfanya atapike hovyo. Maana hata hapo kwangu alitapika zaidi ya mara mbili!” Paulina akaendelea.

“Nikampeleka hospitalini, akapimwa. Kila kitu kipo sawa, ila mjamzito.” Paulina akamgeukia Andy kama kumuona hali yake. Akamuona bado Andy ametulia tu, kimya. Akaona kama mdogo wake hajaelewa vizuri. “Yaani Andy, mimba yenyewe ndio WASIWASI sasa. Ana mimba ya mwezi.” Andy akafunga macho. Hapo Paulina akafurahi, akajua ujumbe sasa umefika kichwani kwa Andy, mdogoe. Akaendelea sasa.

“Lakini mimi nilijua yule mtoto si sawa. Akili zake za kitoto na umalaya.” Paulina akaendelea kuharibu kwa muda wakutosha tu huku akiendesha. “Na nilichofanya ili asiendelee kumtesa mtoto, nikamchukua dada wa kazi na mtoto. Wanaishi pale kwangu ili angalau Ayan ale chakula cha maana. Maana anasema Mina hataki kabisa pale ndani kupikwe, mtoto anakunywa maziwa tu na uji. Yeye Mina nikamfungia pale kwako ili oandoke salama, asitoroke au kutoroshwa na hao mabwana zake.” Andy akamgeukia akiwa amekunja uso kama aliyeshituka kidogo.

Paulina akaona hapo anatakiwa AONGEZE nguvu kwa Andy ili kukamilisha adhima yake. “Kabisa Andy! Anaweza akawa amepata mwanaume mjanja, akamwambia muachane halafu achukue mali zako wakaanze kwengine. Ukajikuta juhudi zako zote zimepotea bure, anafaidi kijana mdogo na Mina. Nimemfungia mpaka utakapokwenda kumtoa wewe mwenyewe na ufuate taratibu sahihi. Maana nikasema asije akatoroka, mama yake akaja kukudai.”

“Maana yule mama yake mwenyewe anaonekana ni wale wakina mama waswahili waswahili, shule yake kichwani haieleweki. Asije akakushitaki, ukaishia jela bure! Ni heri ukamkabidhishe kwao kwa heshima, muachane kwa amani.” Paulina akasawazisha na hilo kwa haraka sana. Nakuendelea.

“Sasa ili asije kukudai baadaye kama mke, na kwenda kutapanya nguvu zako na vijana wengine, nikampigia simu Rwetatika. Si unajua ni mwanasheria wa mambo ya jamii? Akaniambia nikutane naye asubuhi ya leo. Nikaenda. Tukazungumza naye kwa makini, nikamwambia jinsi unavyohangaika kwa ajili ya familia yako, wakati mkeo anastarehe na wanaume wengine. Mbaya zaidi anaonekana hatumii kinga. Leo kakuletea mtoto wa nje, kesho ni nini kama si gonjwa la kufisha!” Paulina akaweka msisitizo.

“Amenishauri vizuri, na akanichapishia hizi karatasi. Amesema, tuhakikishe Mina anaziweka saini kabla hamjaachana ili zije KUKULINDA baadaye. Na ameshauri, kama nilivyokwambia. Hakikisha unafuata taratibu zote. Mrudishe mpaka kwa mama yake, na usije kukaa naye hata usiku mmoja. Anaweza akatumia ujanja, akakuzushia jambo. Kesho ukalala wewe jela, wakati mwenzio anatapanya mali zako na watoto wadogo, halafu Ayan anazidi kuteswa.” Andy kimya.

“Chukua kilo kabrasha hapo, pitia hizo karatasi. Nashauri uziweke saini kabisa ili na yeye akiweka saini umrudishie Rweta, kwa usalama wako Andy ili yasije kukupata kama yaliyompata Mgeni. Mwenzio ametendwa na mwanamke, ameachwa kama mwehu. Nasikia yule mwanamke kaondoka na mali ya mwenzie anaichezea, tena baada ya kumuharibia kweli! Ameuza nyumba na kuondoka na magari yote.” Andy akabaki analitazama lile kabrasha. Paulina akamuona anapata ugumu. Akajua anahitaji kuongeza USHAWISHI.

“Hawa wanawake wanaingia kwenye ndoa na malengo Andy. Wanakufanya uwapende, halafu wanakugeuka. Na inawezekana Mina alikuwa na huyo mwanaume muda mrefu tu. Amejua utarudi au unaweza kumuhamishia huko Dodoma, ukamnyima uhuru wake, akaona azae ili kukupa sababu ya wewe mwenyewe umuache, halafu umlipe. Asiondoke mtupu, akutoe mali yote. Wajanja sana. Utajikuta ndio wewe sasa na mwanao mnahangaika, yeye anakula starehe tu. Unaanza maisha ya kumangamanga na Ayan.” Paulina akazidi KUMSHAWISHI.

Siku hiyo kwa mara ya kwanza, Andy akakumbuka tabia za Mina alizomsimulia maisha aliyoishi zamani. Kina Omar, Mozee na wengine wengi. Akaanza kumsadiki dada yake aliyekuwa akiongea mambo mengi kwa wakati mmoja na kuzidi kumchanganya. Akajua Mina amerudia tabia zake. Akaumia sana kumuamini.”

Andy akavuta lile kambrasha. Akasoma kidogo karatasi ya kwanza ilionyesha Mina ameamua kuanza maisha mengine kwa hiari yake bila Andy kumfukuza. Iliandikwa vizuri sana, Andy akaona hiyo imekaa sawa. Akaweka saini upande wake. Akaacha kwa Mina. Nyingine ilikuwa HATI YA KUACHANA. Andy akafunga macho asiamini kinachomtokea na yeye. Walipanga mipango ya usiku huo waende mapumzikoni wao kama familia. Alijua usiku huo atakuwa kifuani kwa mkewe, anakutana na hati ya talaka! Andy akaumia sana, lakini akaona dada yake yupo sahihi. Wao ni wasomi, lazima kufanya mambo kisomi si kihisia. Akaweka saini upande wake. Akafunga lile kabrasha. 

“Sasa hiyo itakulinda Andy. Mjini watu wanaishi kwa akili! Unaona watu wamekimbia shule, lakini wamefanikiwa kuliko waliojitoa na kukaa darasani. Kumbe wanakula kwa kupitia juhudi za wenzao. Kutwa wapo mjini wamependeza na wanaishi maisha yakifahari, hawana lamaana wanalofanya.” Paulina akaendelea kuongea akijaribu kuamsha hasira kwa mdogo wake. Andy akakumbuka vile anavyoteseka kwa ajili ya Mina na mtoto, kumbe Mina anakula tu raha! Yeye hakuwa muhuni hata. Hakuwahi kumtamani mwanamke yeyote tokea amuoe Mina.

~~~~~~~~~~~~~~

Akakumbuka kutokupokea simu zake, akajua ndio alikuwa kwa wanaume zake. Hata kujirudi mwezi mmoja uliopita, akakubaliana na dada yake kuwa ilikuwa hila tu kumuweka sawa, ili aje amgeuke. Akazidi kuumia. Akakumbuka umalaya aliokuwa nao Mina, akadhani kwa kumuweka ndani na kumpa kila kitu, atabadilika. Akakumbuka machozi ya Mina akimuahidi atabadilika, leo anamfehehesha kiasi hicho! “Hakustahili kunilipa kwa namna hii.” Andy akawaza kwa kuumia.

Akakumbuka misaada aliyoruhusu iende kwao. Jinsi alivyobadilisha nyumbani kwao kwa jasho lake asijue na kaka yake ndio amewekaza hapo kwa asilimia kubwa zaidi yake! Andy akazidi kuumia akajua ni kweli Mina aliingia kwenye ndoa kwa malengo. “Kweli nilifanya haraka.” Akajilaumu Andy akikumbuka hata Ron alimuonya.

~~~~~~~~~~~~~~

“Tumefika Andy.” Paulina akamtoa mawazoni. Akaangalia vizuri, ilikuwa nyumbani kwake. “Na wala usijilaumu. Wewe sio wakwanza kulizwa mjini. Wako wengi tu. Huwezi kujua yupi ni yupi. Wewe unakuwa na nia nzuri yakuanzisha familia, kumbe wenzio akili kichwani.” Paulina akaendelea.

“Sasa acha mimi nimuwahishe mtoto nyumbani akale, wakati wewe unamalizana na Mina. Mimi naona niwape nafasi. Gari yako ilishaletwa hapa tokea asubuhi na funguo amesema atazificha juu ya tairi la nyuma.” “Asante.” Andy akashuka garini akiwa hajaongea chochote zaidi ya hiyo shukurani. “Usisahau ulinzi wako na mwanao huo.” Akimaanisha lile kabrasha. Andy akarudi, akalichukua hilo kabrasha na kuchukua funguo za nyumba na mizigo yake mingine akahamishia kwenye gari yake, akabaki na begi dogo, akapanda nalo juu.

Andy kwa Mina.

Aliingia ndani akasikia sauti ya mtu akitapika bafuni. Akajua ni Mina. Akaamua akae tu sebuleni kwanza. Baada ya muda, akasikia kimya. Na yeye akatulia. Ilishakuwa saa 10 jioni. Aliposikia ukimya wa muda, akasimama kuelekea bafuni. Akamkuta Mina amekaa chini kabisa sakafuni amejiinamia. Mina akashituka sana alipomuona Andy na kusimama, akabaki akimtizama. Andy naye akabaki akimtizama kwa muda.

“Naomba ujiandae nikurudishe kwa mama.” Mina akashituka sana. “Naomba kusanya kila kitu chako. Usisahau chochote kile. Utakachoacha hapa, nitaamini hukitaki tena, nitatupa.” Mina akabaki ameduaa, akajua maneno yameshamfikia. “Anza kuviweka kitandani, nakwenda kukununulia masanduku.” Andy akatoka. Mina akaanza kukusanya vitu vyake. Akajua ndio anaachwa.

Baada ya muda Andy akarudi na masanduku makubwa 10. Akayasogeza mpaka chumbani. Mina akaweka vitu vyake vyote kwenye hayo masanduku. Akaanza kuyatoa hapo sebuleni, Andy anayabeba mpaka kwenye gari. Akajitayarisha nakutoka.

Talaka ya Mina.

“Kabla hujaondoka, naomba weka saini yako hapa.” Mina akamwangalia na kupokea zile karatasi. Akazisoma kidogo, akamwangalia Andy. “Unaniacha Andy!?” Mina akauliza kwa upole kama asiyeamini. Andy akainama, kimya. Mina akachukua kalamu pale mezani, akaweka saini yake, akabeba pochi yake, akatoka nje kabisa.

Baada ya muda Andy akatoka, alipoona gari ya Andy inatoa mlio, akajua imefunguliwa wanaondoka na hiyo gari. Mina akafungua mlango wa nyuma akaka, kimya. Giza lilishaingia. Hakuna aliyemuongelesha mwenzie mpaka nyumbani kwao.

Kisicho Riziki.

Wakashuka, Andy akaanza kutoa mizigo ndani ya gari. Akashangaa na Ron anatoka. “Niwasaidie?” Akauliza Ron. “Tafadhali.” Mina kimya akiangalia. Ron na Andy wakisaidiana kuingiza mizigo yote ya Mina ndani. Mina kuingia, akamkuta mama yake amekaa na wasiwasi usoni. Na kadiri mizigo ilivyokuwa ikiingizwa ndivyo mama yake alizidi kuingiwa na wasiwasi. Hata hawakusemeshana.

“Naomba tuzungumze kidogo.” Akaanza Andy. “Karibu baba.” Mina na Andy wakakaa. “Samahani mama. Najua niusumbufu, lakini kwa kuwa hili jambo nililianzisha hapa nyumbani, nimeona nisiishie barabarani tu.” Kimya. Mina ameinama akisikiliza.

“Nakumbuka mwanzoni kabisa nilipokuja kumchumbia Mina, nilisema maisha ya nyuma ya Mina sitajali, itajalisha baada ya maagano yetu sisi. Pale tutakapoanza kuishi pamoja kama wapenzi. Na ndivyo nilivyomwambia hata Ron.” Ron akatingisha kichwa kukubali.

“Nafikiri wote mnajua kama nilisafikiri. Sikuwepo hapa nchini kwa muda wa miezi 4, lakini Mina ni mjamzito wa mimba ya mwezi!” “Mina!” Mama yake akashituka SANA. Mina kimya. “Binafsi nimetafsiri kuwa Mina ameniambia kuwa anataka kuendelea na maisha yake. Nilichofanya, nimeona nimrudishe kwenu hapa nilipomtoa, tena kwa utaratibu sahihi. Nimempa karatasi za za za..” Hapo Andy akasita, akanyamaza kabisa. Pakawa kimya.

“Andy baba, mimi naelewa kabisa. Hapana jinsi nyingine. Kama wewe umeshakamilisha taratibu zako za talaka, na ukaridhika, sawa. Sidhani kama kuna lililobaki tena. Binafsi nikushukuru baba. Umekuwa mkwe mzuri, umenitunza vizuri na ukarudisha heshima niliyokuwa nimepoteza kwenye jamii. Nashukuru kwa kunirudishia mwanangu hapa, kuliko ungemuacha tu mtaani. Asante baba. Mungu akubariki, nakutakia kila la kheri.” Ilikuwa ni saa mbili usiku. Mama Ron akahitimisha, hapakuwa na nyongeza, Andy akaacha simu ya Mina mezani, akatoka.

Mina Baada Ya Kurudishwa Nyumbani.

Wakamuona anakimbilia ndani. Akaanza kutapika. Akatapika tena na tena, mama yake na Ron wakisikiliza. Kukawa kimya. Hali ya kutapika ikaendelea usiku kucha na asubuhi. Hakuna aliyelala wala kuzungumza lolote tokea Andy aondoke pale. Mina aliogopa hata kurudi kulala na mama yake. Akalala chumba ambacho hata hakikuwa kikitumiwa. Hakina kitanda, kipo kama stoo tu. Akawa na kazi ya kutoka hapo kwenda kutapika chooni na kurudi. Wakawa na kazi ya kusikiliza mlango ukifunguliwa na kufungwa akikimbilia kutapika.

Palipo pambazuka Ron akatoka kuelekea kazini akiwa na usingizi haswa, maana ni kama walikesha tu. Habari mbaya za kuachika kwa Mina na kutapika kwake kusikoisha. Aliondoka lakini bado alikuwa na usingizi. Alichukua nafasi ya Andy, hata na yeye alikuwa na usafiri wake wakumpeleka kazini sio kuwahi tena daladala. Ungejua mambo yamebadilika. Msafi na afya nzuri. Alichofanya si kujenga kwengine ila kuboresha pale kwa mama yake. Akaongeza pikipiki na gari moja ya biashara akaendelea kuishi na mama yake.

Na Nyumbani Napo Moto.

Mina akiwa anapitiwa na kiusingizi cha asubuhi, akasikia mlango unafunguliwa. Akakaa kwa haraka. “Sasa hapa, naomba tuwekane sawa.” Akaanza mama yake. Mina alimuona vile alivyokasirika. “Maisha ya hapa, ni mimi na Ron kufanya kazi kwa bidii kwa masaa takribani 16, ndipo tupate masaa machache ya usingizi. Hali yako hiyo, hakuna atakaye lala hapa. Na kwa kuwa wewe umeamua kuendelea kuzaa watoto wa baba tofauti tofauti, pata nafasi.” Mina hakuamini.

“Mimi nilipokataa kumsikiliza mama yangu, nikaolewa na mwislamu, nikaachwa, sikutaka shida na mtu. Nikatafuta sehemu ya kuishi na wanangu, kimya. Sikumsumbua mtu. Nilipambana kwa hali yangu mpaka mmekua.” Akaendelea mama Ron. “Kuachika wewe si wa kwanza na wala hutakuwa wa mwisho. Na mimba si ugonjwa. Utazaa tu. Sasa na kwa kuwa mimi nakufahamu wewe, huwezi kuishi bila wanaume wawili au watatu kushika huo mwili wako, hii historia itajirudia tena na tena. Shuguli yako hapa hatutaiweza.”

“Huko kutapika kunakotulaza sisi macho, Mungu atasaidia kutaisha tu. Utaingia kwenye kusaka tena wanaume wakukuchezea tena huo mwili wako kama kawaida yako tutaanza upya, kwa kuwa wewe hujui maswala ya kinga. Ulijiachia kwa Omar, ukashika mimba, ikawa bahati mbaya. Kwa Andy napo umezaa, na bwana HUYU naye umembebea mtoto. Huyu utazaa. Huyo ATAKAYEFUATA baada ya huyu, naye utambembea mtoto.”

“Zitaanza tena fujo za vilio vya kichanga humu ndani mchana na usiku huku ukitapika tena kama hivi kwa mimba ijayo. Utapatwa tena na hamu za wanaume. Utaanza tena kazi za kichanga, wanaume, mimba tena. Hapatakuwa na mapumziko kwetu ila starehe kwako wewe uliyechagua hayo maisha.” Mama Ron alikuwa akiongea kwa hatua, ila alijawa na hasira akitetemeka.

“Sasa wewe katafute sehemu nzuri ya kuishi. Upate nafasi ya kuwabadilisha wanaume zako huko, huku ukilea wanao. Waarabu, wahindi, wajerumani, waislamu, wakristo, kila taifa na dini, unawakusanya kwenye hiyo sehemu yako. Humu ndani wanawake wawili na wote tuna watoto, hatutatosha. Tugawane. Nipishe mimi nilee huyo aliyebaki, Ron na wewe katafute kwengine ukaanzishe kambi yako.”

“Na ikiwa mapema ni vizuri ili wenzako tunaoishi kwa kufanya kazi za kuajiriwa, tupate hayo masaa machache ya usingizi, tulale, maisha yaendelee.” Mina akavuta pumzi, akasimama na kutoka pale asiamini kama mama aliyekuwa akimbembeleza, amembadilikia, ANAMFUKUZA!

Akaenda kuoga. Huko bafuni nako akawa na kazi ya kutapika tu. Akatoka na kuweka simu yake kwenye umeme, akakuta mama yake alishaondoka. Akapiga simu kuita usafiri. Akapandisha mizigo yake yote aliyokuwa amerudishwa nayo nyumbani. Mina akaondoka nyumbani kwao walikokuwa wakimuomba Mungu arudi.

~~~~~~~~~~~~~~

Paulina Amesaidia Vizuri Sana Kuhitimisha Ndoa Ya Mdogo Wake. Wamefanya Kisomi Kama Wanavyodai Wao Kina Ruhinda!

Talaka Kimaandishi. Mina, Mke wa Ndoa Takatifu, Kusainishwa Kijanja, Tena Kwa Haraka, Ili aachike Bila Kupata kitu.

Ndoa Ya Watu Wawili, Ya Love At First Sight, Imesaidiwa Kuvunjwa Na Watu Wa Pembeni Kutokana Na Msingi Waliojenga Andy&Mina. Kulipotingishwa Tu Msingi, Nyumba Imebomoka, Hatimaye Kumebakiwa Na Jengo Zuri Lililojengwa Kwa Pesa Nyingi Sana Huko Kigamboni, Na Apartment Ya Kisasa Katikati Ya Jiji BILA Wanandoa Hao Waliokuwa wakipambana mchana na usiku kusaka MAENDELEO.

Nani Muhanga wa anguko hilo?

Na ni Nani Atanufaika Kwa Anguko Lao?

Inaendelea…


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment