![]() |
Akamchukua na
kumrudisha nyumbani. Uzuri Mill alimletea mama yake vifaa mbalimbali vya kutumia.
Haikuwa shida tena kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Anaweza kujisaidia
mwenyewe kwa vitu mbalimbali. Na ni mpishi mzuri sana.
Pam akamsimulia
juu ya Mill. Hata mama Eric hakuamini. “Haiwezekani Pam! Mill!?” Ikabidi
na yeye amfungulie Instagram, amuonyeshe mama yake ndipo akaamini.
“Alinifungia
simu zangu. Nikajua amepatwa na tatizo pengine simu ikapotea.
Sikujua kama ndio amenifungia kunikwepa! Kumbe yupo mzima, na
anawasiliana na watu wengine kama kawaida. Ni mimi tu. Silali mama! Nina pressure
haishuki.” Akamuelezea mama yake kila kitu.
Ikabidi sasa
mama Eric yeye kujikaza ili awe msaada hapo. Wakaanza kulala pamoja.
Usiku walalapo, na kumshika kama kumfariji, angalau Pam akaanza kulala na
kutulia. Kazi hana, anatumia akiba.
Mama yake
akamwambia akiwa hapo nyumbani waanze kupika chapati na maandazi waanze kuuza.
“Mama!” “Nilikuwa nikifanya hivyo wakati nyinyi wadogo. Si haba. Unapata
pesa.” Wazo likamjia Pam, kwenda kutafuta na kwenye mabaa wanayouza kifungua
kiywa. Akajua wanywa supu na mtori watapenda. Akazunguka sehemu kadhaa,
akabahatika kwenye baa moja. Wao
wakataka chapati tu.
Mama Eric
akaanza kazi ya kupika hizo chapati, kisha Pam anapeleka au wao wenyewe
wanakuja kufuata. Wakati mwingine walitaka zaidi. Ikasaidia pesa ya chakula.
Maisha na mama yake hapo jijini yakaendelea.
Siku Nazo
Hazigandi.
Kufikisha miezi
nane na siku chache, mwili wa Pam ukalemewa na kushindwa
kuendelea kubeba huyo mtoto mwenye mwili mkubwa kama baba yake. Akajifungua
salama tu ila kwa kuchanika haswa. Mtoto alikuwa mkubwa sana na Pam
alikuwa akisikia njaa hata baada ya kula. Basi alikuwa na kazi ya kula kama
mchwa! Akampa jina la babu yake. Shemaghembe ila yeye akamfupisha na kumuita
Shema.
Baada ya siku
mbili tu, mtoto aliyekuwa amezaliwa kabla ya siku kutimia akaonekana hana
tatizo, Pam na mwanae wakaruhusiwa kurudi nyumbani, mama yake akashika kazi ya
ulezi.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Ukawa mchana,
ukawa usiku. Mtoto anakua kama uyoga! Alifanana na Mill mpaka macho yao na
masikio madogo yaliyojikunja kidogo kwa juu. Ilikuwa kama kopi yake
kuanzia utosi mpaka unyayo kasoro tu rangi ilikuwa ya mama yake. Pam
alikuwa akimwangalia mwanae na kupotelea mawazoni asiamini kama kuna
wanaume matapeli kwa kiasi kikubwa kama hivyo Mill, au ni yeye tu
na ukoo wao!
Pam hakuwa
amesoma shule ndefu sana. Elimu ya kidato cha nne, tena kijijini na pia
alifeli. Kazi gani aombe! Akazunguka mpaka akajikuta anaomba kazi kwenye Depot
ndogo tu ya familia moja wanayouza maziwa wanayoingiza kutoka kwenye kiwanda
cha maziwa huko Tanga.
Wanauza maziwa
ya kupima na ya paketi. Mtindi na fresh. Akaanza hapo kazi. Ni maeneo ya
Ch’angombe unashukia Veta. Sio mbali na kituoni. Anafanya kazi jumatatu mpaka
jumamosi mchana. Saa moja na nusu anatakiwa kufika kazini. Mbili kamili
wanafungua milango, anafanya mpaka saa nane, anapokelewa na msichana mwingine.
Kijana aliyekuwa hapo ni mmoja wa ndugu wa mwenye hiyo depot, alikuwa
hapo muda mwingi. Kama kuwasimamia na kusaidia kuuza kama wakizidiwa. Zaidi
mida ya asubuhi na jioni watu wanapotoka makazini.
Angalau akaanza kuingiza
pesa. Japokuwa haikuwa nyingi, lakini ilikuwa nafuu kuliko kukosa
kabisa. Mama yake akawa anabakia na mtoto nyumbani. Akitoka kazini wanasaidiana
na mama yake kupika hivyo vitafunywa. Watu wa kwenye baa wanakuja kuchukua au
Pam anawapelekea asubuhi akiwa anaenda kazini. Na karibu na kazini napo pia
palikuwa na kimgahawa. Nako akapata tenda. Angalau maisha yakawa
yanaenda.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Mpaka mtoto ana
miaka mitatu, hakuwahi kumsikia wala kukutana na Mill au Mike
hata kwa bahati mbaya barabarani. “Kweli Dar kubwa!” Alikuwa akijisemea
Pam. Pam alijidharau kupita kiasi. Ule ujasiri wa zamani uliisha
kabisa. Alijawa hasira na uchungu wa kusalitiwa. Usingemkuta akicheka
kwa furaha.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati maisha
yanaendelea, wakisaidiana na mama yake, babu akaugua, ikabidi mama Eric arudi
kijijini ila ikabidi ondoke na Shema kwa muda ili mama yake afanye kazi.
Lakini Pam
akashindwa. “Siwezi kulala bila mwanangu, mama.” “Utafanyaje kazi na mtoto
utamuachia nani?” Hilo likawa swali la msingi. Ikabidi aanze
kutafuta shule ya chekechea karibu na pale. Akahangaika lakini mitaa hiyo bei
kubwa. Hata hivyo kodi ilishaanza kumlemea.
Akahama hapo na
kupata chumba mitaa ya Tandika. Basi moja tu mpaka kazini kwake na si mbali
kama alikokuwa akiishi mwanzo. Lakini nyumba ikawa tofauti na alikotoka! Kwanza
ilikuwa uswahilini haswa. Wapangaji walikuwa familia tatu na yeye
angekuwa wanne. Na chumba alichopata ni cha uwani wanakopikia wote.
Watu wakianza
kupika nje, ndani mnasikia kila kitu au ukiwa ndani wa nje wanasikia
japo kukawa kama na ukuta uliozunguka chumba chake na sebule ukafunga huo uzio.
Kwamba mlango wa kuingilia chumbani kwake na sebule upo ndani. Unaingia hapo
uwani kwa kigeti kidogo kizuri tu, ndipo utakutana na kwa Pam, au unaingilia
mlango wa mbele kwa mwenye nyumba. Madirisha yake mawili yapo nje kabisa
wanakopita watu huko mtaani, halafu dirisha moja lipo uwani. Taarabu ikipigwa
kwa jirani, unazima redio yako, wote mnasikiliza mpaka atosheke ndio na wewe
uwashe yako.
Lakini alichokifurahia
Pam, waliishi hapo kama ndugu wakipatana sana. Aliona jinsi
wanavyolea watoto wao, akajua kwa hakika hapo patamfaa. Kila mtoto wa
hapo ndani ni wa kila mzazi. Japokuwa walikuwa na hali za chini kiuchumi,
lakini walisaidiana sana. Kama binadamu wengine kulikuwa na kupishana
ila na walijua kupatana. Na kwenye ugonjwa wote walibebana na kuuguzana.
Hilo akamshukuru Mungu kwa yeye aliyekuwa hana mtu hapo mjini.
Akaenda kijijini
kumchukua mwanae, akamuanzisha shule ya chekechea karibu na
anakoishi. Basi muda ukifika wakutoka, yeye mwenyewe kama amechelewa, anamuomba
mama yeyote hapo anaenda kumchukua mwanae, wanakaa naye mpaka mwenyewe anarudi.
Angalau hapo uswahili na huo umoja wao, ukamfaa sana Pam na mwanae. Kazi
ikawa inafanyika na mwanae anaendelea kukua.
Muendelezo Wa
Mill Kutokea
( MAPENZI
& PESA - PART 4 - SEHEMU YA 30.)
Sasa aliporudi
nchini na watoto wawili, maisha ya ugaibuni yakiwa yamemshinda. Uraia
aliokuwa akiuhangaikia, aliupata na mafanikio ya hali ya juu. Ukweli
Mill alifanikiwa kipesa, kasoro ndoa tu. Malengo mazuri aliyokuwa
nayo, ikakosekana njia sahihi ya kuyafikia. Mpaka Kisha alipofanikisha
kumpa uraia wa nchini Marekani kwa kupitia ndoa.
Biashara ya
nyumba ya kulelea wazee alifungua mjini Maryland zaidi ya tatu.
Kisha akawa anaajiri watu kwenda kusaidia wazee aliokuwa akipata, majumbani
kwao. Kwa hiyo akawa anaingiza pesa kotekote, tena si kwa kubabaisha kwa
kuwa alikuwa akilipwa na serikali upande wa afya kwa wazee hao.
Ndani ya muda
mfupi sana, alinunua si nyumba, ila hekali la hali ya juu hukohuko mjini
Maryland. Aina ya magari aliyokuwa akiendesha yeye na mkewe, hata wa kazi wa
huko walijua weusi hao, WAMEFANIKIWA.
Uzuri alijenga
mpaka nyumbani. Alinunua kiwanja, alipoona hakitoshi, akamuhamisha jirani yake
hapo na kumlipa zaidi ili anunue na kiwanja chake. Napo akapata kiwanja kikubwa
sana, eneo alilopenda yeye, akajenga nyumba muundo uleule kama wa nyumba
aliyokuwa akiishi mjini Maryland nchini Marekani. Alichimba kisima cha maji na kuingiza
pump za mamilion ya pesa kuvuta maji. Nyumbani kwa Mill hapo Dar hapakuwa na
mgao.
Na kwa sababu ya
shida ya umeme, akaleta mtaalamu kutoka nchini Marekani. Akaangalia mazingira
na nchi nzima. Akaingiza mitambo yake mwenyewe, kimyakimya, nyumba ikawekwa Solar
Power. Yaani wakati nyinyi mnaungua na jua. Mnalalamikia jua
kali nje, ndio furaha ya Mill. Nyumba yake inatengeneza umeme, kwa jua
hilohilo.
Ukifika kwa Mill
unaweza sema ni kama hapo kwake kupo mbingu nyingine. Kijani kibichi
kuanzia getini mpaka nyuma. Maji yapo masaa 24, mashine zinamwagilia asubuhi na
usiku. Umeme wa kumwaga. Na asivyopenda matatizo, akafunga generetor
za umeme za nguvu. Hutakatikiwa umeme nyumbani kwa Mill. Akafunga central
A/c. Yaani kiyoyozi kinapuliza baridi masaa yote, nyumba nzima.
Akiwa nchini
Marekani alikuwa akiagiza thamani nzuri sana za ndani kwake huku Tanzania.
Yaani anarudi kuishi na wanae nchini Tanzania, hawaoni utofauti na
maisha ya kwao, kasoro tu lugha na mazingira wakitoka kwao.
Maisha ya Mill
Nchini Tz.
Kama alivyokuwa
amekusudia kumtafuta aliyemuaa Mike. Hakuacha. Kifo cha Mike kilikuwa kikimuuma
sana. Maisha yakazidi kukosa furaha bila Mike mtu wake wa karibu sana.
Alitafuta watu
wake wa karibu waliokuwa wakimfahamu Mike, pamoja na ndugu zake. “Najua Mike
amefariki. Kwenu ni muda mrefu, lakini kwangu na Kamila kwa sababu hatukumzika,
tutafanya misa, na tutakusanyika sehemu kama kumuenzi.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Akatafuta kabisa
sehemu ya kukodi kwa sababu ni kama mali ya Mike ilirudi kwa ndugu. Hakuacha
mtoto wala Kamila hakuwa mke, kwa hiyo ndugu walipopokonya kila kitu, hapakuwa
na nyumba yakufanyia hiyo kumbukumbu yake, ndio Mill akakodi ukumbi. Pakapambwa
vizuri lakini kimsiba.
Akatengeneza
picha za Mike, na video zake. Wakachanganya na clips mbalimbali
alizokuwepo yeye na watu wake wakaribu kwenye matukio tofauti tofauti. Zikawa
zikirushwa hapo ukumbini. Kwengine ni yeye mwenyewe Mike akiongea. Ukawa wakati
wa furaha na majonzi wakilia.
Kamila na Colins
pamoja na familia yake pia walikuwepo. Marafiki wa tokea sekondari
waliokuwa wakisoma pamoja nao pia walikuwepo. Jerry alikuwepo bila
Sandra. Na hao ndugu wa Mike wenyewe
ambao walishapoteza mali zote pia na wenyewe walihudhuria kwa wingi tu.
Kukawa na kula na kunywa kwa kusaza.
Karibu ya mwisho
Mill akatoa TANGAZO lililochanganya wengi. “Mike amekufa lakini bado anaishi
moyoni kwangu.” Akaendelea. “Kifo chake kilikuwa cha mateso MAKALI
sababu alipewa sumu. Mwili wake kwa ndani uliharibika sana,
hakuweza hata kusubirishwa sababu ya kuharibiwa na sumu.”
“Moyo wangu unaniuma,
kila nikifikiria mateso aliyopitia kabla ya kifo chake, mtu kama Mike.
Mike! Kiumbe kisicho na hatia na mtu, hakika nataka haki
itendeke. Nyinyi wote nilio waita hapa ni watu wakaribu na Mike. Na wengine
mlikuwa naye siku ya mwisho ya uhai wake.” Akatulia.
“Sasa basi,
yeyote atakayeniletea fununu za kweli. Namaanisha taarifa
yenye ushahidi juu ya aliyempa sumu Mike. Nitamlipa pesa.”
Alipotaja hayo mamilioni ya pesa atakayotoa kwa atakaye muweka
muuwaji mwangani, wote walishangaa mpaka Kamila. Hakutegemea kama Mill
alikuwa na utayari huo.
Akazua gumzo
hapo ndani. “Acha niweke sawa. Hiyo pesa haitakuwa na maswali. Nitakukabidhi
bila shida. Ila na mimi nitataka ushahidi, na uwe tayari kwenda mpaka
mahakamani kushuhudia hili.” Hapo pakatulia kidogo. Watu WANAFIKI! Wanaweza
semana nyuma ya mgongo, lakini si uso kwa uso. Mill akawagundua. Akaona
aweke msisitizo. “Namaanisha hivi, iwe na kwa msaada wenu au la,
NITAMPATA aliyemuua Mike. Na nitahakikisha ANALIPA. Na Mungu anisaidie.” Akataja namba
ya simu yake na nyingine.
“Nimeshafungua
kesi.” Watu wakashangaa sana. “Kabisa. Sitatulia mpaka nimpate aliyemuua
Mike. Namba ya pili niliyotoa ni ya mpelelezi niliyempata na kukubali
kufanya kazi na mimi kwenye hili swala. Vipimo vya hospitalini
ameshavichukua. Amehakikisha kweli kilichomuua ni sumu aliyonyweshwa.
Ameshaanza upelelezi wake. TUTAMKAMATA tu. Asanteni.” Akawashukuru kwa
kuhudhuria hapo, na kuruhusu wanaotaka kuondoka wawe huru, wanao pendelea
kubaki kula na kunywa, ruksa.
~~~~~~~~~~~~~~
Colins na yeye
siku hiyo akapata bahati ya kukutana na Mike. Video alizokuwa
ametengeneza Mill, utafikiri Mike mwenyewe yupo hai hapo! Alionyesha
nyakati tofauti tofauti za furaha walizokuwa pamoja, nchi mbalimbali
akipewo hata huyo mrembo Kamila, yeye Mill, watoto na Kisha. Nyingine wao tu
wawili. Mike na Mill. Walionekana ni watu waliokuwa wameshibana sana. Na
hata kwenye hizo picha tu Mike alionekana ni mtu aliyekuwa akipenda
amani.
~~~~~~~~~~~~~~
Wao walikuwa
watu wa mwisho kuondoka hapo. Kamila akapata nafasi ya kumshukuru Mill
na kumuomba azungumze naye pembeni. “Ni nini?” “Unakumbuka nilikwambia nitamtafuta
yule binti mkubwa wa dada yao kina Luca?” “Ulisema upo naye karibu. Kwema?
Maana leo hajatokea!” “Amesafiri kikazi. Lakini Mill, kuna mambo mimi ameniambia
jana, tena nilikuwa na mama, ikabidi kuweka spika, na kumuomba mama asikilize.”
“Amesema nini?!”
“Ameniambia mke
wa Luca ndio mbaya wangu, nisikae nae karibu au nijiepushe
naye sana. Niache kabisa kula chochote anachonipa.” “Kwa nini?! Yeye ndiye amemuua
Mike!?” “Na mimi nilimuuliza. Akasema alicho na uhakika nacho ni kuua
watoto wangu.” Mill akashituka sana.
“Anasema yeye
ndiye anayempandikizia hasira mumewe kwamba yeye ndio mtoto wa kiume wa
kwanza, kwa nini Mike ndio achukue MALI za baba yao. Nasikia akawa analalamika
sana na kusema mwishoe Mike naye atazaa mtoto wa kiume, atamrithisha
mali hizohizo, mwisho kabisa mali zote za Luca zitapotelea mikononi kwa
Mike na wanae.”
“Zulfa nasema anauhakika
kwa asilimia zote, kwa sababu aliyekwenda naye kwa mganga kunifunga
kizazi amemwambia.” “Kamila!?” “Mama Colins ni shahidi yangu. Na
ninahisi kabisa atakayekuwa amemsindikiza ni mama yake Zulfa mwenyewe,
ndio maana Zulfa ameshindwa kumtaja mama yake. Maana yule wifi pia
hakuwa amefurahia Mike kusimamia mali ZAO. Anasema anauhakika
na akaniambia mganga alimpa dawa, anipe. Kuwa kila mimba nitakayokuwa
nikishika mtoto anakufa. Sasa mimi sijui Mill.” Roho ilimuuma
sana Mill.
“Una jinsi ya
kumuuliza kama ndiye aliyempa Mike sumu?” “Mbona nilimuuliza! Akasema katika
hilo hana uhakika, lakini akaniambia mimi nitumie tu akili. Mara
ya mwisho sisi tulikuwa nyumbani kwake mama Luca aliyetayarisha
chakula, na Mike kuugua mpaka kifo. Akaniambia, mtu anayeweza kuua
watoto wa Mike ili wasije kurithi, anashindwa vipi kumuua
Mike mwenyewe ambaye amerithi?” “Kamila?!”
“Nakwambia
hivyohivyo na mama Colins ni shahidi yangu. Anasema yeye anahisi amesubiria
kuona Mike anakufa kwa njia zake nyingine, ila akawa hafi. Anasema
anahisi atakuwa pengine pia amejaribu kumuua kwa uchawi
akashindwa, ndio akaona bora ammalize kabisa kwa sumu. Tena
akasema hivi, huoni walivyoishiwa kwa haraka?” “Unamaanisha nini?”
“Si nilikwambia walinipokonya
kila kitu mpaka gari?” “Nakumbuka.” “Sasa Zulfa anasema wameishiwa mpaka
wanapikia na kuni hapa katikati ya jiji. Anasema gari walilonipokonya
na kumpa mtoto wao yule mkubwa wakiume, unaambiwa nusura limuue.
Zulfa anasema eti alishawaambia babu yao, yaani baba yao kina Luca, amekasirika
wao kuchukua mali, ndio maana amewapokonya kwa haraka.
Unaambiwa ni kama wamepatwa na laana! Ile nyumba waliyonipokonya mimi,
Zera anasema imekua kama gofu, mpaka imeoza, hapafai. Mpaka geti hamna.”
Mill alishabadilika sura.
“Unafikiri Luca anahusika?”
“Na hilo nilimuuliza. Ila yeye anavyomjua mjomba wake alisema anauhakika hausiki.
Anasema yeye ni hasira tu, lakini si mtu mwenye roho ya kuua. Na
mimi nahisi ni kweli. Maana Luca alidhania eti mimi ndio nimemuua
Mike. Akataka kuniwajibisha kama hivyo wewe unavyotaka kufanya.” “Na
mimi aliniambia hivyohivyo. Kwa hiyo ni kweli. Hausiki. Lakini Kamila,
kama ni mkewe, hakika nitamkamata tu na atalipa kwa yote. Kumnyima
Mike watoto na kumuua yeye mwenyewe. Nitapeleleza tu, na nitahakikisha
na yeye anapewa kipaumbele kwenye upelelezi wa kipolisi. Usilie, wewe
nenda kapumzike. Nitakujulisha.” Kamila alikuwa akilizwa na mengi.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Siri ya kuwa Pam
alifika kwake na alikuwa mjamzito, hakumwambia hata Mike. Alilificha
hilo, asiseme. Hapo anajilaumu kwa mengi, lakini hawezi kusema
tena. Alishahisi pengine Mungu anamlipiza KISASI kwa
alichomfanyia Pam, kwamba Mungu ndiye aliyekuwa akimuulia kila kiumbe
aliyebeba yeye.
Akamfanya Mungu
ni mdogo, eti kumuadhibu kwa kosa la kuficha kama Pam anamtoto aliyejua
wazi atakuwa ni wa Mill. Akahukumiwa kumficha Mill aliyekuwa nao yeye na
Mike katika shida na raha bila kuwachoka. Mpaka sasa hata Mike hayupo bado anamjali.
Akajisikia kuhukumiwa lakini hapakuwa na jinsi ya kujirudi. Akanyamazia
tu akijua kwa hakika hawezi kuja kumpata Pam. Kwanza miaka mingi
ilishapita. Akajua kwa wakati huo Pam atakuwa na maisha yake, hana habari
naye.
~~~~~~~~~~~~~~~~
“Umefikia wapi
kumtafuta Pam?” Akaona aulize tu. Mill
akijua ana nia njema kumbe analake, anataka kuepusha kikombe.
“Aisee sijampata! Nilikwenda alipokuwa akiishi zamani. Hawajui hata
namzungumzia nani! Nimekuta wapangaji wengine kabisa na wenyewe hawana hata
mwaka hapo.” “Kwao?” “Huko Lushoto!?” “Namaanisha hapa Dar.” Kamila akaendelea
kudodosa.
“Ni kama nilichangia
kuharibika kwa mahusiano yake na mke wa mjomba wake kabisa.
Alikasirika sana kitendo cha sisi kwenda kulipa mahari kijijini aliko
mama yake Pam, wakati anasema ni kama Pam nilimtoa kwake na malalamishi
mengi. Nimeshindwa kwenda.” “Jerry anasemaje?” “Anasema hana taarifa zake
zozote. Alikutana naye mara moja tu kama alivyosema, tena zamani sana. Mbali ya salamu anasema hawakuzungumza
na hajamuona tena. Ila bado sijakata tamaa.” Akaongea Mill akifikiria.
Hapo akamtia hofu Kamila. Alijua angekata tamaa, ila bado anania ya kumsaka!
Akaona aondoke.
Cha Mtu Mavi!
Mina aliuguza huo mguu akiwa na msichana wa kazi
akimsaidia. Aliletewa na mama Ruhinda. Akawa kitandani tu akimtuma hiki na
kile. Pius akakosa sababu ya kufika hapo mara kwa mara, uhuru wa
kuwa hapo kwa Mina, hakuna tena sababu ya huyo msichana wa kazi, na mama
Ruhinda kupita hapo mara kwa mara.
Siku ya tano yake akamkumbuka sana Andy.
Akatamani kama angekuwepo pale. Akalia kuanzia anaamka asubuhi mpaka mchana,
akaamua kumpigia kwa video akiwa amejilaza na mtoto wake kitandani.
Haikuita hata
mara mbili Andy akaipokea kwa haraka. Mpaka akamuona Andy anafuta machozi
wakati anawaangalia. Mina akamuhurumia. Alishindwa hata kuzungumza. “Andy!” Mina akaita kwa upendo. Andy akabaki akifuta
machozi. “Niliumia mguu mwenzio!” Mina akaongea
kwa kulalamika.
Andy akafuta tena machozi. “Pole.
Nini tena?” “Niliutengua kwa bahati mbaya.” Akamuona anafunga macho. “Lakini sasa hivi naendelea vizuri.” “Sasa nani anakusaidia
wewe na mtoto?” Andy akauliza kwa kuumia sana. “Mama
Ruhinda alinitafutia msichana wa kazi. Sasa hivi ndio naishi naye hapa.” “Pole
Mina. Pole sana mpenzi wangu.” “Asante, unamuona Ayan?” “Mbona na yeye amelala
au mgonjwa?” “Mzima kabisa. Atakuwa amesinzia tu. Babu yake alipita asubuhi,
amemnywesha uji vizuri tu, ndipo akaenda kazini.” Andy akanyamaza
kidogo.
“Kwa heri. Nilitaka kukusalimia tu.”
“Nashukuru Mina. Nilikuwa na wakati mbaya, hivi nilikuwa nataka kurudi
nyumbani.” Mina akawa hajamuelewa. “Shule imeisha mapema?” “Hapana Mina! Nimeona siwezi
kuendelea na haya maisha. Vitu vyote vinakosa maana bila wewe, Mina.
Niamini kuwa nahangaika kwa ajili yetu wote. Sasa itanisaidia nini nipate
yote haya halafu nakukosa wewe?” Mina akanyamaza.
“Na ninakusikiliza sasa hivi. Ukitaka
nirudi, narudi mama. Nimetoka kuangalia tiketi, nimeona naweza kupata ya kurudi
huko hata kesho kutwa. Lakini ukiniambia utakuwa na mimi kwa muda huu uliobaki,
nitamaliza.” “Umebadilika Andy! Hata naona sikuelewi tena.”
“Nitajirekebisha. Nakuahidi.
Tutarudia maisha yetu yale ya mwanzo kabisa mpenzi wangu. Sawa?” “Kwa hiyo nikusubiri kwa
hamu, safari hii hudanganyi?” “Tafadhali Mina.
Usinikatie tamaa mpenzi.” Mina akajifuta machozi.
“Niambie kama bado unanipenda Mina.”
“Nakupenda Andy na ndio maana nimetulia kwako tu.” “Nakushukuru kwa
hilo. Umekua mke ambaye sikutarajia! Umenivumilia hata pale niliposhindwa
kuwa mume mzuri. Umeshika nafasi ya baba ambayo nilipelea sana. Nakushukuru
Mina wangu.” Andy akampamba mkewe, mpaka
Mina akajisikia vizuri na kujipongeza kushinda nafsi na
kumsubiria mumewe.
“Ninahamu na wewe Andy! Nataka unikumbatie
tena na kunibusu.” Andy akacheka kwa
furaha. “Na mimi ninahamu ya kukukumbatia, kunyonya
hiyo midomo yako huku nikifanya mapenzi na wewe.” Mina akacheka sana. “Mtoto anakusikia Andy!” “Acha hizo bwana! Si amelala?”
Mina akamuhamishia mtoto kamera. “Amelala bwana! Ila
ujue ni kweli. Nilikuwa nataka kurudi.” “Maliza tu Andy. Lasivyo gharama yote
tuliyolipa mimi na Ayan itakuwa bure kabisa.” “Unauhakika Mina?” “Ndiyo Andy, nitasubiri.
Si bado siku..” “40 mama. 40 tu.” Andy akamalizia. “Basi hizo nitasubiria Andy. Mungu akusaidie urudi
salama.” Andy alifurahi sana. Wakazungumza kidogo wakaagana wote wakiwa
wametulia. Shida ya Mina ni kumsikia Andy bado anampenda na kumuhitaji.
Sasa ashamsikia, Mina roho kwatu.
Dhambi zote ameshasamehe.
~~~~~~~~~~~~~~
Nyumbani kwa Mina kukawa na msichana wa kazi, anaitwa
Mamu, ambaye anafahamiana kwa karibu sana na mpaka ndugu wa Raza, mke wa
Pius. Alitakiwa awe mfanyakazi wa mama Ruhinda, Raza alimtafutia, lakini mama
Ruhinda akampa Mina. Alimuita Pius shemeji, na alimfahamu kwa kumuona
Pius ukweni.
Kwa hiyo uhuru wakufika pale ukapungua,
ikawa kwa simu ndio mara nyingi lakini napo mambo yakabadilika kwa kuwa
Andy akarudi
pichani kwa NGUVU. Simu kwa mkewe
asubuhi akiamka, mchana akila, na usiku akienda kulala. Na lazima awaone.
Azungumze na mkewe na mtoto, ndipo wanaagana. Kwa hiyo Mina akawa amerudisha
mapenzi kwa mumewe. Pius akipiga simu habari anazopewa ni za Uswiz,
alipo Andy. Atamsimulia hili na lile juu ya Andy wake. Hata Pius akajua Mina amerudisha
furaha.
Akiwa na shida yeyote ile hapigi tena simu kwa mtu
mwingine, ni Andy, mumewe ambaye sasahivi ana muda naye, na simu zake hazisubiri.
Anapokea kwa wakati na anamsikiliza mkewe. Andy atambembeleza hapo na kumshauri
kwa hili na lile. Mina akapunguza mawasiliano na Pius. Akipiga simu,
Mina anaweza asipokee, anamrudishia tu ujumbe. ‘Nitakupigia
shem.’ Hapo anaweza kumrudishia hiyo simu siku hiyo au hata kesho yake.
Hilo likaanza kumnyima raha Pius. Akaanza kumkumbuka
Mina aliyeonja penzi kwa usiku moja tu. Kila akikaa, anakumbuka jinsi
alivyomfaidi mtoto huyo mdogooo, mke wa mdogo wake, lakini Mina mwenyewe hana
taarifa hata. Akawa ameshapona, anaendelea na maisha kama kawaida.
Mawasiliano na Andy yakawa ni ya kila mara. Mina akawa
akimsubiria kwa hamu mumewe, akiahidiwa hili na lile atakachofanyiwa siku ya
kurudi kwake. Siku nazo zikawa zikienda bila shida. Mina anamsubiria mumewe kwa
hamu, hana jingine analofanya wala kuwaza. Yeye mawazo yapo kwa Andy.
Yasirini Yaja Mwangani.
Siku moja asubuhi Mina aliamshwa na kichefuchefu
kikali, akashangaa sana. Hata alipokuwa mjamzito, hakuwa akitapika. Akakaa.
Ghafla kitu kikapanda, akakimbilia chooni. Mina alitapika mpaka akamuamsha
Mamu, msichana wake wa kazi. “Dada! Upo salama?” “Hata sijui ni nini!?” Mina
akatoka bafuni na kwenda kupika uji wa mtoto wake.
Huko jikoni akapatwa tena na kichefu chefu. Akarudi
bafuni kutapika. Kuanzia hapo, Mina akawa na kazi ya kutapika hana
anachoweka mdomoni kikapita na harufu nayo ikawa shida. Hataki tena yule
msichana wa kazi apike chochote pale ndani. Akawa anampa pesa ya kwenda kununua
chips. Tena akale huko huko asije nazo ndani. Mwanae ni uji tu. Hapo Andy
alikuwa amebakisha siku kama 8 tu arudi nchini.
Lakini akashangaa hana homa, wala haumwi na kichwa ila
kutapika kama mgonjwa haswa. Akajiambia ni hali tu, itaisha. Hata hakwenda hospitalini. Akaendelea na hayo maisha ya
shida yakushindwa kula chochote ila kutapika tu.
~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya siku chache jumamosi ambayo jumatatu yake
mumewe alikuwa akirudi, ilikuwa wakutane nyumbani kwa Paulina, aliwakaribisha
kina Ruhinda wote kwa chakula cha usiku. Ilikuwa lazima Mina naye ahudhurie na
Ayan ambaye babu yake alishapiga simu kuzungumza naye na kumwambia Mina
anamsubiria kumuona jioni nyumbani kwa Paulina.
Mina akajiandaa bila hata kupaka pafyumu, na mtoto
pamoja na msichana wa kazi, wakatoka mpaka nyumbani kwa Paulina Kinondoni B,
karibu kabisa na makaburini. Msichana wa Mina akataka kumbemba mtoto, Mina
akamwambia anataka yeye abebe begi la mtoto, yeye atamshika tu mkono atembee,
asibebwe.
“Eti kaka mkubwa! Unataka kubembwa.” Ayan akamwangalia
mama yake na chupa ya maziwa mdomoni, akacheka tu. “Tembea bwana!” Mina
akamlazimisha atembee. Wakaingia ndani. Ule mchanganyiko wa harufu za
vyakula pale, Mina akawa amechafukwa haswa. Akawasalimia na kuwaambia
atarudi baada ya muda mfupi sana. akakimbilia nje, bila kutaka kuwatia hofu.
“Hapo mwenzenu anaenda kutapika tena, huyo!”
Msichana wake wa kazi akaongea kwa kusengenya. Wote wakamgeukia. Mama
Ruhinda akamtizama kwa mshangao. Kama anayemuuliza ‘huna hofu!’ Nyumba ilijaa watu wa maana watupu! Kina Ruhinda na
watoto wake. Wote wasafi, halafu wakubwa kuliko huyo msichana aliyeongea kama umbea.
“Kwani anaumwa?” Akauliza Paulina. “Ile itakuwa mimba
tu! Japo mwenyewe anakataa. Kabla ya kuja huku pia katapika wee,
ndio tukaja. Kila siku asubuhi anatapika. Nyumbani hakupikwi,
hataki harufu. Ananipa pesa nikale chips, tena gengeni. Nisirudi nazo
hapo nyumbani. Hataki harufu. Ana kazi yakumnywesha mtoto wake
uji na maziwa kila saa, hataki kupikwe. Mimi nishazaa, najua tapika ya
mimba.” Mamu akaongeza bila kumumunya maneno. Pakazuka ukimya wa ghafla.
~~~~~~~~~~~~~~
Maji Yashamwagika…
0 Comments:
Post a Comment