Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 24. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 24.

Bado Mill hakujua chakumwambia Pam mpaka aelewe. Kwanza hata hakuwa amejua kama alioa huko nchini Marekani. Ilibaki ni siri kubwa sana kati yake na kina Mike. Moja kwa moja akajua akimwambia yote hayo juu ya Kisha, Pam atajua fika ndio sababu alikataa ndoa ya kanisani nchini Tanzania.

  “Nitamwambia nini Pam!” Ndio likawa swali lililokosa jibu. “Kwamba niliombwa penzi kwa nguvu!” Yaani hata yeye Mill akaona itasikika ni sababu ya kijinga sana. Akabaki akijiuliza bila jibu.

Hata Pam alipokuwa akimpigia simu alishindwa kabisa kupokea. Mwishoe akaamua kumblock kabisa kila mahali. Na huo ndio ukawa MWISHO wa kuwasiliana na PAM.

Aliyafanya hayo yote akiwa na paniki, hukumu, akasahau historia nzima ya Pam, vile baba yao alivyowatelekeza wao na mama yao. Na alimuapisha mara kadhaa asije kuwa kama baba yake, na Mill akaapa kwa mbingu na nchi, haitakaa ikatokea. Lakini yote hayo yakafunikwa kwenye ubongo wa Mill, akijua wazi, kwa vile Pam alivyo mzuri, atamtafuta kidogo tu, atachoka na kuamua kuendelea na maisha yake. Akahakikisha Pam hampati hata kwa barua pepe. AKAFUNGA hata akaunti ya barua pepe aliyowahi kumuandikia Pam. Ikawa hakuna jinsi ya kumfikia kabisa.

Kupenda Kubaya!

          Asijue na huku kwa Pam nako aliacha msala mwingine. Kazi ya kumsaka Mill ikaanza. Wasiwasi ukamjaa akijua pengine yupo matatizoni. Labda ajali mbaya au ugonjwa umempata mupenzi. Wakumuuliza ni nani! Jerry hajazungumzia naye tena swala la Mill. Na Jerry alikuwa akimkwepa. Hakutaka aingie katikati yake na Sandra ambaye wazi alionyesha kumchukia Pam. Sifa zote alizokuwa akimpa Pam, zikageuka kuwa lawama, sababu maalumu hana. Wivu kama yeye ndio Lona!

          Mwezi wa kwanza ukapita na wapili nao ukayoyoma bila ya kumsikia Mill. Pam akawa kama amechanganyikiwa. Si kwamba alizitaka pesa za Mill, HAPANA. Yeye wasiwasi wake uzima wa Mill tu! Japo kumsikia ajue yupo mzima. Alikuwa akimpigia simu zaidi ya kawaida. Asubuhi, mchana, jioni, na usiku. Tena hata usiku wa manane akishituka kutoka usingizini, basi atampigia Mill.

Za Mwizi zimefika 40.

          Arobaini zake kwa kina Lona zikawa zimetimia. Akiwa kwenye ile hali ya kuchanganyikiwa wakajua huo ndio wakati muafaka, wa kumlipiza kisasi. Wakamtega na malipo hewa. Wakamsainisha kumpa malipo apeleke benki. Wakamshanganyia hundi na pesa taslimu. Akiwa na mawazo yaliyosambaa, bila ya kuhesabu, akaweka saini kuwa amepokea pesa kiasi ambacho SICHO. Yeye hana habari anakimbilia kwenda benki, ilimradi tu atoke hapo ofisini, apate uhuru huko njiani amtafute Mill kwa simu.

          Kuja kurudi, Sandra anapitia mahesabu yake na ile slip ya benki aliyorudisha, akagundua upungufu wa pesa. Kumuuliza Pam yule aliyekuwa akimsifia zamani kabla ya Mill, kuwa ni mwaminifu sana, haibi hata shilingi, Pam hajui hata anachozungumzia.

Huwezi muibia mwizi. Ndio Sandra. Pesa hiyo aliyoipata kwa wizi alikuwa akiilinda kama anavyomlinda Jerry na roho yake. Ikaonekana ni kama ameiba pesa pale ofisini.

Akifa Nyani, Miti Yote Huteleza.

Ndilo lililompata Pam. Sandra hakutaka maneno mengi, akampeleka polisi bila ya kufikiria mara mbili. Na yeye akapata nafasi ya kumlipiza Pam. Alishafika sehemu akawa ameshakuwa kero kwake. Ilikuwa ukifika hapo ofisini kwake, unaweza sema Pam ndiye mmiliki. Alijawa neema huyo Pam! Na alivyo mzuri, Mill alimthaminisha haswa!

Alikuwa na aina ya marashi, akiwa ofisini kwake hata ukiingia mapokezi mtajua kama Pam yupo. Ilitulia vizuri mno. Mwanaume mwenyewe aliyekuwa naye, huwezi mfananisha na Jerry wala Mike. Mill alijaliwa mvuto wa kuanzia sura mpaka mwili, halafu aliujualia mwili wake. Ukiwakuta na Pam, unaweza sema walichaguana. Hawana picha wakapiga usitake kutulia na kuiangalia tena na tena. Kila kitu cha Pam kililia mafanikio. Hicho kilimkera sana Sandra.

~~~~~~~~~~~~~~

Alipofikishwa kituo cha polisi, kama wahalifu wote wanaofikishwa hapo kwa kosa hilo la wizi, usemi wao ni mmoja, “Sijaiba.” Yakawa maneno hayohayo kutoka kwinywani kwa Pam. Hakuna jipya, akasekwa lupango. Sandra anataka pesa yake.

Japokuwa wote wanajua mdeni hafungwi, lakini Sandra alitaka tu kumkomoa. Akasema anaweka fundisho kwa wafanyakazi wake wote, mtu mwingine asije rudia mfanyia hivyo.

~~~~~~~~~~~~~~

Pam alikuwa hajui chakufanya, hana msaada.  Nyumbani kwa shangazi na mjomba alishaondoka. Leo hawezi kurudi kuomba msaada wa swala wizi. Akajua na kwa kaka yake pia asingeweza msaidia hata kidogo. Kwanza mkewe ndiye mshika pesa yote. Leo anamwambia watoe mamilioni ya pesa kumlipia yeye atoke jela! Akajua hizo ni ndoto za alinacha. Akatulia akifikiria chakufanya.

~~~~~~~~~~~~~~

Miezi mitatu ikapita akiwa jela, nyumbani kwao hawajui kinachoendelea na yeye hakutaka kusema. Mawazo yapo kwa Mill, hata hajiangalii hali yake. Wakati mwezi wa tatu unakaribia kuisha, kesi yake haitajwi wala hana anayemtembelea huko rumande, Sandra akaenda kumuona.

Akamwambia atafuta kesi ya uwizi endapo atamlipa pesa yake. “Naitoa wapi hiyo pesa mimi!?” “Uza gari.” Pam akacheka. “Kumbe ndio maana umenifunga! Yaani wewe unaumwa na gari ambalo halina hata nusu ya thamani ya gari unayoendesha!” “Sina muda wa kujitetea Pam. Unanipa pesa yangu au la! Jiangalie ulivyo na ulipo. Unataka uje uzalie jela!” Ndio akili ikamrudia Pam na kuanza kujifikiria. “Hayakuhusu.” Akamjibu hivyo Sandra kwa jeuri, akamcheka na kuondoka.

~~~~~~~~~~~~~~

Japokuwa alijaliwa katumbo kadogo sana kalichobebwa na hips pana na tako la duara lililokuwa likionekana kwenye kila kitu anachotupia hapo mwilini mwake, mwezi huo kwenda wa 7 tumbo lilishaonyesha kabisa, kubwa haswa kama anayekaribia kujifungua, ila ni yeye tu hakuwa akitilia maanani. Ukabaki mtihani, nani wa kumsaidia angalau kumtoa jela!

Tumbo likazidi kukua, ndipo akasalimu amri. Akampigia simu mjomba wake. Akamueleza akimtaka msaada.

Baada ya siku mbili alifika hapo na mkewe. “Nisikilize Pam. Tushakusaidia  vyakutosha. Ni wewe mwenyewe ndio umechezea maisha yako. Sikukuonya mimi utulie? Ona ulipo? Upo jela na tumbo lisilo na baba.” Gafla Pam aliyekuwa akijitunza na shangazi yake kujua, tena wakati mwingine kumtolea mfano hata kwa wanae kuwa ametulia, eti leo gafla akaonekana malaya!

“Sasa sisi hatuna msaada wa kukusaidia. Maisha magumu. Pesa yenyewe hakuna. Kama unataka uza vitu vyako.” Ushauri uleule aliokuwa ametoa Sandra. Akaona hamna jinsi. Walipoondoka tu hao, akampigia simu Sandra. Akamwambia amekubali ampe hilo gari, afute kesi.

Bila aibu, Sandra akakubali. Alimfuata huko lupango na waraka kabisa. Akamsainisha kuwa analipa deni kwa hilo gari. Pam kwa uchungu mkubwa, akasaini ndipo akamtoa jela. Akachukua funguo za gari. Nataka na kadi yake. “Nitakupa.” “Usinitanie Pam. Zikipita siku tatu sijapata kadi ya gari, nakurudisha jela.” Pam akakubali bila shida. “Na pale ofisini kwangu nisikuone tena. Kibarua ndio kimeisha hivyo. Sitaki wizi.” Pam akachukua pochi yake na kurudi kwake.

~~~~~~~~~~~~~~

Uzuri alilipia hapo kodi ya mwaka mzima. Alikuta hapajaguswa. Kwa haraka ili asije ishiwa tena, akalipia tena hapo kodi ya mwaka maana ilikuwa imebakia miezi miwili kodi iishe. Akajiambia atajifungulia hapohapo. Japokuwa ilikuwa ni chumba kimoja tu na sebule, lakini alipapenda. Wapangaji wenzie walikuwa wastaarabu. Hakuna fujo na mambo ya ajabuajabu.

Alilala siku moja tu kutoa uchovu, kazi ya kuanza kumsaka tena Mill ikaanza. Piga simu kama mwanzo bila mafanikio. Siku inayofuata akaenda kuanza kliniki. Sababu ya watu kuwa wengi, alikaa huko karibia siku nzima. Sababu ya wasiwasi, hofu alikuwa amekaukwa mdomo, amechoka, Pam akarudia maisha ya daladala, ila safari hii na ujauzito.

Kwa kina Kamila.

Alitoka mida ya saa nane mchana akiwa na kadi yake ya kliniki, hata hajala, akapanda daladala mpaka alipokuwa akiishi Mill, nyumbani kwa Mike na Kamila. Alifika getini akiwa anatokwa jasho karibia aanguke. Mapigo ya moyo yalikuwa yakienda kasi kama aliyekuwa akikimbia kumbe ni kutembea tu juani.

Hata hivyo mimba ilishakuwa kubwa. Halafu aliambiwa mtoto wake ni mrefu. Mkubwa zaidi ya miezi yake. Hakushangaa. Mill ni mkubwa sana kama baba yake. Akajua mwanae amechukua mwili wa kwao. Akafika kwenye kibanda cha mlinzi, bila kukaribishwa, akakaa chini kabisa mlangoni akijipepea.

“Pole mama. Karibu.” Mlinzi aliyemkuta akawa mstaarabu kweli. “Ndio nishakuwa mama!” Akawaza Pam akiwa anajipepea amepakata tumbo lake. Urembo wote uliisha, ukabakia uzuri wa asili.

“Namuulizia Mill. Anaishi kijumba cha pembeni humo ndani.” “Mmmh! Simfahamu. Na mimi mgeni. Lakini mke wa mwenye nyumba yupo. Acha nimuulizie.” Pam akashukuru Mungu. Akajua Kamila alivyokuwa akimpenda na kumkarimu, basi atamkaribisha hata ndani, aombe chakula. Maana alikuwa na njaa kali, na kiu.

Akamsikia mlinzi akipiga simu ya mezani. Ukasikika mlio kwa sauti ya juu tu maana ni simu ya mezani hapo getini. “Kuna mgeni hapa getini. Amesema anamuulizia..” Akamgeukia Pam. “Mwambie naitwa Pam, namuulizia Mill na naomba kuzungumza naye.” Kwa tumaini kubwa sana, akamwambia akisimama kabisa maana alijua jibu ni afunguliwe geti aingie ndani, kama zamani alivyokuwa akitetemekewa alipokuwa na Mill.

Lakini Pam HAKUAMINI masikio yake aliposikia, “Mwambie hatupo.” Mlinzi mwenyewe alishindwa kumgeukia Pam. “Anahali mbaya dada! Ungemuona tu. Amekaukiwa, halafu ni mjamzito yule wa tumbo kubwa kabisa! Jasho linamtoka kama amenyeshewa mvua. Anaweza anguka kabisa.” Mlinzi akamsihi. Safari hii kwa sauti ya chini akiwa amempa mgongo kabisa Pam, na ameinamia simu kama asisikie.

“Mwambie hapa Mill hayupo, hajarudi nchini. Ataondoka tu.” Simu ikakatwa Pam asiamini. Huyo Kamila ndiye aliyekuwa akiwaletea chakula hapo alipokuwa akiishi na Mill, kama wapo fungate! Alikuwa akiwaletea kuanzia cha asubuhi mpaka cha usiku, akionyesha kuwajali na kumpenda sana Pam MBELE ya Mill! Leo anaambiwa anahali mbaya, kweli ameshindwa hata kumfungulia mlango kwenye nyumba aliyokuwa akimbembelezea akiwa na Mill! Pam HAKUTEGEMEA. Ikabidi aondoke tu maana hata mlinzi alishindwa kurudisha jibu. Akaanza kutembea taratibu kurudi barabarani.

Kwa Mama Kenny.

“Ni nini kinaendelea?!” Akazidi kuchanganyikiwa. Kila alivyokumbuka mapenzi ya Mill kwake, kwamba amemuacha hivihivi, ilikuwa haiingii akilini kabisa. Wema wa Kamila alipokuwa akienda kwake, leo amgeuke hivihivi! “HAPANA.” Akahisi jambo baya limepata Mill, ameogopa kumwambia. Akamtetea Kamila moyoni mwake.

Akajiambia hata kama waliamua kumuacha mama Kenny, lakini ni lazima watakuwa wanajua habari za Mill, aliyeachwa hapo kama msimamizi wa familia. Akaonelea aende kwa mama Kenny akajue ukweli.

Akachukua daladala ingine, na kuunganisha mpaka kwa mama Kenny. Akazunguka hiyo nyumba mpaka akakutana na hilo geti jipya lililokuwa limetenganisha nyumba yake na vijana wa Mgini.

Hapo akagonga, msichana wa kazi akaenda kumfungulia. Ilishafika saa 12 jioni. “Nimemkuta mama Kenny?” “Yupo. Na yeye amerudi muda si mrefu. Karibu ndani.” Akaongozana naye akijivuta mpaka sebuleni. Akakaa, msichana wa kazi akaenda kumuita mama Kenny.

Hakuamini kama ni Pam. “Nimekufananisha au ni Pam mwenyewe?” “Ni mimi, shikamoo.” “Mbona umechoka hivyo!?” “Maisha tu mama yangu.” Akamuita msichana wa kazi na kumuagiza juisi. “Naomba na maji tafadhali. Nimekaukiwa!” Mama Kenny akakaa.

“Kwema? Mbona umejiachia hivyo?!” “Mill yuko wapi?” Mama Kenny akatulia kidogo. “Sijui kama mzima au mgonjwa! Sijui kama yupo hai au amekufa! Sijui chochote na kwenye simu simpati kabisa.” Mama Kenny akaguna.

 “Acha nikwambie ukweli Pam, binti yangu. Kwa asilimia 100, mimi nilijua ni Mill peke yake atakuwa tofauti na babu yake pamoja na baba yake. Lakini kumbe sivyo! Kwa hakika hawa watu wana laana inayofuatilia kizazi hadi kizazi. Mill alikuwa mfano wa kuigwa hata Kenny alikuwa anatamani awe kama yeye.”

“Nilipoona mambo ni yaleyale, sikudanganyi Pam. Nilimpeleka mwanangu kanisani kuombewa. Atokwe na laana ya kwao. Si bure!”  Akazidi kumchanganya Pam. “Kwani Mill amefanyaje?!” “Hakuna aliyeamini jinsi alivyokuwa amekuleta hapa, nikafikiria amechagua fungu la tofauti, atatulia! Tukashangaa yupo na mwanamke mwingine huko na yeye ni mjamzito!” Pam akahisi hajamsikia vizuri.

“Unamzungumzia Mill!?” “Huyuhuyo. Kaanza na wewe. Kila nikiuliza mbona ndoa ya kanisani kimya ni ile tu ya kimila, baba yake akawa anamtetea hapa, eti anataka akakuolee hukohuko Marekani. Kavuta weee. Alipoona tu baba yake kaondoka, kachukua mwanamke mwingine.” “Haiwezekani mama Kenny!” “Wala si siri. Mimi namfuatilia mwanamke wake. Anajiita Kisha Mgini. Mwanamke wake mjamzito hata tumbo si kubwa, lakini limejaa huko Instagram! Linapigwa picha kila siku, zinatumwa. Ngoja nikuonyeshe.” Kenny akadakia na kumsogelea kabisa.

“Kwamba Mill AMEOA huko?!” Bado hakuwa akiamini. “Pam binti yangu, umetapeliwa kama sisi wote. Mchezo aliokuwa akifanya baba yake, ndio huohuo anafanya na yeye. Sema naona yeye amekuja kivingine. Tapeli mstaarabu. Maana baba yake hajawahi oa yeyote, wala kulipia mtu mahari. Ila Mill naona amejiongeza. Kwako alilipa mahari na ile ndoa yenu ya kimila, mwenzio kamuolea mahamani! Mbona picha atakuonyesha Kenny!” Kenny akafungua simu yake. Akamuonyesha picha zote.

Kamila na Mike walikuwepo huko mahakamani akifunga ndoa. Ndio akajua ni kwa nini Kamila alishindwa hata kuzungumza naye. Pam akajiegemeza kwenye kochi kabisa haamini. “Mill!” “Ni WASHENZI hao kina Mgini! Hujapata ona. Wanajua kuzaa kama panya! Si uliona watoto wa Mgini hapa? Kafa, kaacha wanae wana mangamanga! Hawana mbele wala nyuma. Malaya kama baba yao. Hivi kama hilo tumbo ni lake, ukimtoa tu huyo mtoto, kimbiza kanisani. Lasivyo jua umezalia watoto wa wenzio tatizo.” Pam akabaki kimya.

Mwenzie, Kisha Mgini, alikuwa na tumbo, ila amependeza haswa! Kila mwezi alipiga picha na kuposti, lakini tumbo wazi kabisa akiwa amelishika kwa kuvutia haswa. Pozi tofauti tofauti. Akaangalia picha zote na kumrudishia Kenny simu yake. “Nashukuru. Angalau nimejua ukweli. Sasahivi nitatulia niangalie yangu. Nilikuwa na wasiwasi sana. Maana aliniacha na mipango mingi! Sikudhania kama…” Pam akasita na kupotelea mawazoni asiamini.

“Halafu wewe si umesema ulikuwa humpati kwenye simu?” Kenny akamtoa Pam mawazoni. Akamtizama. “Amezifungia namba zako zote, ndio maana humpati. Lakini bro yupo, na anajibu jumbe kama kawaida. Acha nikuonyeshe.” Pam kimya akijiangalizia.

Kenny akamtumia ujumbe kwa kupitia namba ileile ambayo Pam yeye hampati, ila kwa simu yake yeye Kenny. ‘Unaendeleaje huko Marekani, bro?’ Hapohapo akamjibu. ‘Mzima. Kwema huko?’ ‘Kwema. Nilikuwa nikikusalimia tu.’ ‘Nashukuru. Nisalimie mama na Sheila.’ Akawa akimuonyesha Pam majibizano yao. Pam hoi haamini kama Mill yupo na ni mzima.

“Kuna chakula mezani.” “Naomba nile mama Kenny. Nina njaa. Sijala. Mpaka nasikia kizunguzungu.” Akakaribishwa mezani. Akala mpaka wenyeji wake wakabaki wakimwangalia yeye. Akamaliza na kushukuru. “Unayo nauli sasa?” “Ninayo. Na hivi nimeshiba, nikifika nikulala.” Akaondoka zake hapo.

~~~~~~~~~~~~~~

Haikuwa hivyo. Pam alihangaika kitandani, usinginzi hauji. Alikuwa na mshituko nakushindwa kuamini kama kweli ndio ametapeliwa na Mill. “Hakika ndege mjanja nimenaswa kijinga sana.” Akajilaumu Pam, asiamini jinsi alivyokuwa akijitunza, ameishia kutapeliwa.

“Lakini hapana!” Hilo ndilo likabakia kichwani kwa Pam kila akimfikiria Mill na jinsi alivyomuonyesha mapenzi! “Hakika HAPANA.” Akashindwa kuamini kabisa.

Hakukaa sana, ule mshituko na kutoweza kulala kukaibua pressure kali sana. Kila wakati mapigo ya moyo yanakwenda kasi. Mikono inatetemeka kama aliyejawa hofu ya ajabu sana.

Huku Kwa Mina.

Uhusiano wa karibu sana kati ya Mina na Pius ukaendelea. Pius aliweza kupiga simu muda na wakati wowote, tena kwa stori tu zakawaida. Shemeji akanogewa na Mina. Asipomsikia, siku haiendi. Kwenda kumuona na kukaa na Mina wacheke kwa muda wakutosha tu, likawa jambo la kawaida. Hata katikati ya siku, ungemkuta Pius nyumbani kwa mdogo wake akicheka na shemejie, ambaye alikuwa tu kwake, na yeye anamajukumu mazito tu ya kiofisi.

Wakaanzisha taratibu zao wao ndani ya familia hiyo hiyo. Kama movie day, yaani siku yakuangalia sinema pamoja au siku ya kwenda kula ice cream nje ya nyumba na mengineyo. Siku hizo walizojiwekea wao wawili, Mina na shemejie, Pius atatoka kazini na kuja hapo nyumbani kama ni siku ya kuangalia sinema. Atakaa kwenye makochi hayo kwenye kijumba hicho kidogo kama punje ndogo ya jumba lake, akiwa na Mina pamoja na Ayan, wakitizama movie. Mtoto akilala, atalazwa chumbani kwake. Hapo atabaki Mina na shemejie.

Atamvuta miguu amuegemee. Basi Mina atakuwa amekaa, miguu imepakatwa na shemeji. Movie na stori vinaendelea. Ataminyaminya hiyo miguu ya Mina hapo huku akiipapasa taratibu macho kwenye luninga, mpaka muda uishe, ndipo ataondoka. Hata Mina hakujua anaagaje huko kwa mkewe Raza. Lakini yeye alimpata Pius muda na wakati wowote aliotaka na kumfurahia.

~~~~~~~~~~~~~~

Tofauti ya Andy na Pius ikawa jinsi ya kujali tu. Andy alibadilika. Akimshika ujue anataka penzi si kama Pius, alimshika kwa kumbembeleza bila kuomba penzi. Andy hakuwa mchoyo wa pesa kabisa, ila mpaka uombe. Na ukiomba, haulizi, atatuma kiasi kile kile ulichoomba bila hata kuongeza shilingi. Kwa hiyo maisha yao ikawa ni mpaka Mina amuombe ndipo atatuma bila hivyo Andy hakuwa akikumbuka kutuma pesa. Ikawa tofauti kubwa sana kati yake na Pius.

Pius akaingia kwenye maisha ya Mina akawa kinyume kabisa na mdogo wake. Akawa ameshamsoma Mina ameshajua nini anataka. Pius akawa kile anacholilia Mina. Kumjali yeye kama Mina. Alimpapasa na kumbembeleza tena bila hata kutaka penzi kitu ambacho hakikua shida kwa Pius. Ni asili yake, Pius mtoto wa mama, amekua na yeye kwa kubembelezwa akakutana na Raza hapendi mapenzi ya kushikwa shikwa. Kwanza anaona kero.

Sasa Pius mtoto wa mama anayependa kupendana. Hata ukimkuta amekaa na mama yake, ataanza kumminya mabegani akimtaka apumzike aondoe stress za hiyo siku. Haya, kabla hujalia shida kama ni mtu wake, anakusaidia. Kwa sili tu alijaliwa kujali. Sio mchoyo.

Sasa wakakutana na Mina, mtoto wa mwisho kwao, mtafuta kupendwa.  Akafurahia mikono ya Pius ambaye anataka wa kumbembeleza ila hana. Raza ambaye yeye bora apewe pesa na Pius, na Andy aliyetingwa na majukumu WAKAWASAIDIA kuwaweka karibu. Yao yakaanza kuwanogea. Ikawa Pius na Mina kama waliokusudiwa. Upendo mwingi ndani ya mioyo yao, wenza wamewaacha wapo busy na yao.

Wakati Raza akitapanya pesa ya mumewe na kutingwa na majukumu yake binafsi na ya kiofisi, HAJALI ya mumewe, mumewe akapata  nafasi na Mina. Simu za Raza kwa mumewe ni kuomba pesa. Alipenda pesa kama benki. Na Pius alimjua. Ili kumtuliza ni kumpa kila pesa anayoomba tena wakati mwingine alimpa kabla, ili asimkere.

Kwa kumuangalia Raza, ungejua anayo pesa. Mashoga zake wa mjini walikuwa hadhi yake. Kula starehe kwenda mbele. Kukutana kwenye sehemu za starehe na mashoga zake yakawa maisha ya Raza karibu kila siku. Alitapanya bila kujipunja. Na kwa kuwa watoto wao, wao hawakuwa wadogo, halafu wa mwisho alikuwa na ratiba za kisomi, za hadhi ya wazazi wao, alikuwa na dereva maalumu kuhakikisha anafuata ratiba za binti huyo bila kukosea.

Kumtoa nyumbani na kumpeleka shule. Kisha kumfuata shule na kumpeleka kwenye mafunzo ya kuogelea kama ni siku ya kuogelea. Maana alikuwa akiogelea sana. Au kupelekwa kucheza tennis. Kama ni siku ya mchezo huo, na baada ya hapo kurudishwa nyumbani akiwa anasubiriwa na mwalimu maalumu wakumsaidia kusoma na kufanya kazi za shule.

 Hivyohivyo kwa dada yake. Alikuwa mwaka wa kwanza chuoni kikuu cha Dar-es salaam. Anao usafiri wake. Anachagua pakulala. Kazi za chuo zikiwa nyingi, basi atalala chuoni au akigombana na mama yake, basi hatakuwepo nyumbani. Kwa ufupi Raza na Pius hawakuwa na watoto wadogo kama Ayan.

Kwa hiyo kila mmoja maisha yake yakaendelea vizuri bila kukanyagana hapo jijini. Andy akaendelea na yake, Raza naye yake yakaendelea bila kubugudhiwa na mumewe. Hata akirudi kutoka kwenye starehe zake na mashoga zake, hakuna wakumuuliza kwani na mumewe naye anakuwa kwa Mina ndio pengine na yeye anakuwa amerudi hapo nyumbani kwao. Wamepishana kidogo tu.

Kwa kina Ruhinda kukawa kuna utulivu. Mina ametulia nyumbani kwake na mtoto wake. Hakuna hekaheka ya kukaa na Ayan. Mzee Ruhinda na mkewe wakarudi kazini wakiwa na akili iliyotulia, wakiwa na amani. Na Mina naye alibaki kufika nyumbani kutembea tu. Mwanae msafi, yeye mwenyewe ametulia. Hana huzuni wala kulalamika juu ya mumewe. Maisha yakaendelea kwa utulivu wa aina yake, kwa kila mtu. Kumbe Pius ndiye aliyekuwa AMETULIZA hiyo ghasia.

~~~~~~~~~~~~~~

Mwezi ulishapita, Mina hapokei simu za mumewe kabisa. Kwanza alishatoa Whatsapp kabisa ambayo aligundua ndio njia rahisi ya mumewe kumpigia. Ikawa huwezi kumpata Mina kwa njia hiyo. Andy akawa anahangaika kupiga mchana na usiku akidhani anaweza kumpata, lakini wapi.

Ila ujumbe wa mwisho aliomtumia kabla hajatoa Whatsapp ndio alijua anamfanyia makusudi. ‘Nilisikia ulifika salama. Na sisi hatujambo, tunaendelea vizuri. Nakutakia kila la kheri kwa hilo unalo lihangaikia.’ Mina akatuma huo ujumbe. Basi, kuanzia hapo ikawa kimya, na wala hakusubiri majibu, akatoa Whatsapp kabisa.

~~~~~~~~~~~~~~

Siku zilikwenda, Mina akiwa amejawa furaha tele, hana wasiwasi. Maisha yake na shemeji yake yakaendelea kama kawaida. Mara nyingine Pius alifika hapo mchana, na kujilaza kwenye makochi kama yupo kwake tu. Ataweza kukaa hapo akizungumza na Mina hata masaa mawili ndipo anarudi kazini. Swala lakuitiwa chakula cha mchana nyumbani kwa Andy likawa la kawaida sana.

Mina akiivisha, Pius anajua, kwa kuwa mara nyingi wanakuwa wote kwenye simu. Mina anapika na kufanya ya nyumbani, Pius ofisini akifanya yake. Basi akiivisha tu, anajua. Utasikia akimwambia Mina, “Nakuja na mimi kula.” Basi Mina atacheka hapo, shemeji anakuja kula. Watacheka na kufurahi ndipo anarudi kazini.

Na Pius naye hakuwa akimpa pesa ndogo. Ukimuona Mina, ungejua pesa ipo. Pesa ya kutoka kwa mumewe kwa matumizi yote ya pale nyumbani bado alikuwa akipokea kutoka kwa Andy na bado Pius sasa asiyejua kutuma pesa ndogo ndogo!

Zawadi zake kwa Mina si za mchezo na wakati wote zakushitukiza. Utoaji wake pia Mina aliupenda. Alikuwa akicheka Mina, kama amepewa ulimwengu. Akajazwa dhahabu za kiutuuzima. Nguo sasa! Pius alikuwa mwanaume anayependa kuvaa sana kama asili ya kina Ruhinda. Kwa hiyo zawadi ya nguo kwa Mina, ilikuwa kawaida. Wala hakuhitaji kutoka nje ya nchi ili arudi na zawadi. Akiwa hapo hapo Dar, alikuwa akitokea kwa Mina na zawadi kemkem.

~~~~~~~~~~~~~~

Mwezi wa pili ukaisha. Bado Mina akawa HAJAWASILIANA na mumewe. Hapokei simu zake kabisa. Andy naye akazira. Kila akiulizia hali ya Mina na mtoto, anaambiwa ni wazima kabisa na wanaendelea vizuri. Akaona amuache kwa muda labda atajirudi kwa kuwa na hamu naye, kwani alimjua mkewe. Mwingi wa upendo kwake, asijue kaka yake amejaa nyumbani kwake, Mina hana muda wa kuwaza kingine isipokuwa upendo wa Pius.

Maisha yakaendelea kwa Pius na Mina kwa nafasi yote. Andy akiendelea kuzira nje ya nchi, Raza busy na pilikapilika za jiji. Pesa ya mumewe ipo, kilichobaki matumizi na mipango tu.

~~~~~~~~~~~~~~

Wakati Andy Anasema Cha Nini, Pius Anakililia. Na Wakati Raza keshakinahiwa, Akipambana Na Starehe Za Jiji, Mina Amempata Pius Kilaini, Na Baraka Za Wazazi Juu!

Analiwazwa na kubembelezwa huku akipewa matunzo ya hali ya juu.

Ni Nini Kitaendelea Kwa Wawili Hao Walioachwa Huru Kabisa Mbele Ya Macho Ya Kila Mtu?

Pam Naye Aliyeachiwa Tumbo, Mill Akilea Tumbo Jingine Huko Ugaibuni, tena na ndoa juu!?

Usikose Muendelezo.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment