Kuna usemi unasema Timing is everything. Mina
akabaki ametulia kiti cha mbele, kimya. “Niambie habari za mapumzikoni?” Pius
akamchokoza. Mina akainama, kimya. “Maana uliondoka bila hata kuaga!
Nikasikia tu Mina na familia yake wamekimbilia baharini! Nikasema hatuagani!” Mina hakujibu. “Eti Mina?” “Hata mimi
nilikuwa siijui hiyo safari, shem. Nilikuja kuchukuliwa mara baada ya mtihani
wa mwisho, tukaondoka.” “Hata simu?” “Niliacha simu nyumbani. Sikuwa na simu
wakati wote.” “Hapo sawa. Nikajua tunasahauliana.” “Hapana. Samahani.”
Mina akaomba msamaha kwa upole. Pius akacheka kidogo.
“It’s ok. Bora mmerudi salama.” Mina akanyamaza.
Alimfikisha nyumbani, hakuishia kwenye gari.
Akamsaidia kutoa kiti cha mtoto kwenye gari yake na kukifunga kabisa kwenye
gari ya Mina, ndipo akamchukua mtoto kutoka kwa Mina, akambemba,
kupandisha ngazi mpaka juu kwenye apartment
yao. Mina akafungua mlango, Pius akamwambia aingie yeye kwanza, ndipo wakaingia
yeye akiwa amebeba mtoto.
“Najua umechoka shem. Naomba muweke tu hapo kwenye
kochi ili nimuandalie chakula. Nakushukuru kwa msaada.” “Usijali. Wewe andaa
tu, ngoja nikae naye kuliko kumuweka chini awe peke yake! Mkishatulia, ndio
nitaondoka.” “Asante shem.” Mina akakimbilia jikoni. Alishapika mchana,
alichofanya ni kumpashia moto tu.
“Njoo baba.” Pius akabaki akimwangalia Mina na mwanae.
“Ukimaliza kula tu, sikusumbui tena. Nakuogesha, harakaharaka nakuacha ulale.
Umesikia?” Mina akaendelea kumlisha mtoto wake huku akizungumza naye.
“Shem, nikuwekee chakula au utakwenda kula nyumbani?”
“Nitakwenda kula nyumbani. Asante. Unahitaji lolote?” Pius akauliza kwa kujali.
“Hapana shem. Nashukuru kwa pesa unayonipa. Nimefanya mengi kwa hiyo
pesa! Umenifanya nitulie. Nakushukuru sana.” Mina akajibu kwa
unyenyekevu sana. “Usijali. Na kama ukiwa na kitu kingine, niambie
tuzungumze tujue chakufanya.” Akajibu kwa kujiamini. Pesa ipo, na
mkewe anafanya kazi nzuri tu. Pesa haikuwa tatizo. “Usiwe na shida yeyote ile ukanyamaza.
Nishirikishe.” Ile ikamgusa zaidi Mina. Pius akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Mina akaanza kulia asiweze kujizuia. Alilia. Akalia.
Akalia. Alikuwa akimuogesha mtoto huku analia. Anamvalisha, huku analia.
Akamuweka mtoto wake kitandani chumbani huku analia. Alipoingia chumbani
alishindwa kulala. Alilia karibu usiku kucha, moyo ukimuuma vile jinsi Andy
alivyombadilikia. Mkali, hana muda tena na yeye ila majukumu ya
kazi tu. Hali ya upweke ikaongezeka moyoni, akabakia hana jinsi ila kusubiri
akijua hapatakuwa na mwisho.
~~~~~~~~~~~~~~
Aliingia kwenye ndoa na Andy akijua ataanzisha familia
ambayo ni ya baba na mama. Sio kama vile alivyokuzwa yeye na Ron.
Akazidi kushuhudia historia ya mama yake ikijirudia kwake. Ni kama Ayan anakuwa
bila baba yake. Tokea anamaliza mwaka mmoja, Andy akaanza ahadi
zisizo isha. Ilianza taratibu na baraka za Mina. Kuchelewa kazini,
Mina akawa anaelewa kwa kuwa angalau kulikuwa na MAWASILIANO kati yao.
Mambo yakaanza kubadilika. Ila hali ya ufamilia
ikaisha. Hakuna tena kuzungumza
au kupanga PAMOJA kama ilivyokuwa mwanzoni. Ikawa ni yeye akitoa
muongozo wa nini anafanya. Yeye TU, bila
maswala ya mkewe wala mtoto. Akamuacha Mina jijini na mtoto kama ambaye hajaolewa.
Ukali na ubabe
akieleza nini anafanya tena kwa faida ya Mina ambaye hakuwa na makuu
kama Lora. Mina hakuwahi kuhitaji makuu, yeye ndiye aliyempa
makuu na kumuacha akihangaika kwenye maisha ambayo hata hakuwahi
kufikiria.
Ukweli hata Mina alijua anachokifanya ni kitu kizuri
kwa ajili ya familia. Lakini hapakuwa na MAWASILIANO kati yao, wao
kama wanandoa. Hilo ndilo
likawa TATIZO kubwa kati yao. Andy ambaye hakuwa akilala vizuri
sababu ya kazi, akaishia kuwa mkali kwa Mina ambaye yeye alijua watalea
wote mtoto hata kwa kupeana tu mawazo.
~~~~~~~~~~~~~~
Bila wao wenyewe kujua tatizo lao
lilipo, Andy akidhani Mina analalamika bila yakuelewa uthamani wa
kile anachokifanya kwa familia, na Mina akiumia akiona Andy
amembadilikia, bila kujua kuna majira ya kila jambo. TATIZO ikawa ni MAWASILIANO
kati yao.
Mipango MIZURI ilikuwa ikipangwa na kila
mmoja wao ndani ya ndoa, na kila mmoja akipambana kivyake kuendesha hiyo mipango ndani ya familia
bila kupambana kwa PAMOJA kama wanandoa. Siku zikaenda. Andy anafanikisha
kivyake, na Mina hivyohivyo wasijue wanakumbatia BOMU hatari sana kwa
ndoa yao.
~~~~~~~~~~~~~~
Mina akaanza kumfikiria Andy, akajua hatakuja kubadilika
kamwe. Ni mtu anayependa kazi, na yale maisha kwake ni sahihi.
Akakumbuka maneno ya askofu wake juu ya Andy, kuwa Andy hapendi kitu kimuharibikie
mkononi. Akajua yeye na mtoto ndio watalipa hiyo garama ya
uaminifu na uchapakazi wa mumewe. Aliibeba hiyo kazi kama yake! Mchana
na usiku bila kuchoka.
Akaanza kuvuta kumbukumbu ni wapi anguko la ndoa yao
lilipoanzia. Akakumbuka alianza akiwa hata bado hajaamishwa hapo jijini Dar.
Ayan akiwa na miezi kadhaa. Akawa busy kazini,
simu hapokei kwa wakati. Akaanza vizuri kwa kumrudishia hizo simu
na msamaha akitoa sababu za kueleweka tu. Pengine alikuwa mkutanoni au alikuwa akizungumza
na simu ya kikazi wakati Mina akipiga. Hapo hapakuwa na shida, mkewe akawa
akielewa na kumpa pole. Mina akaendelea kuvuta kumbukumbu ni kama
akaanza kuacha kupokea simu zake nyingi na kutorudisha mpaka
anaporudi nyumbani basi kuzitolea maelezo ni kwa nini hakuzijibu na
kurudisha.
Akakumbuka jinsi na Dodoma napo kulivyoanza. Alianza
kwa kumtaarifu safari ya Dodoma kama ni safari ya kikazi. Mina akazidi kuwaza. “Inawezekana
tokea mwanzo Andy alijua atahamishiwa Dodoma ila alisita kuniambia. Na hajawahi
kuzungumza na mimi juu ya safari zake zaidi ya kuniaga usiku mmoja kabla
hajaondoka asubuhi yake!” Mina akakumbuka kwa uchungu sana.
Akakumbuka hata hilo akawa kama amelichukulia sawa na kumtia moyo akijua ni kwa
muda tu.
Mwanzoni alimrudishia majibu Mina kuwa huko
anafanya vizuri mpaka akawatia tamaa wenye kampuni. Wakamwambia aanzishe tawi
jingine na Iringa. Mina akakumbuka hapo ndipo ukorofi na ubabe
ukazidi. Harudi nyumbani na kumpata kwa simu ni shida.
Hajui uzima wake wala wa Ayan. Hata akipiga simu inakuwa kama anajambo la muhimu
linalo msubiri huko kuliko kuzungumza naye kwenye simu.
Iringa nako akapata mwitikio mkubwa. Wenye kampuni
wakamtuma tena akajaribu na Morogoro. Andy ambaye hakuwa na wegazi wa mke wala mtoto, ni yeye tu, huko Morogoro akafanikisha
kwa kiwango cha juu sana. Mina na Ayan wakisubiria nyumbani
wakati yeye akihangaika mkoa mmoja hadi mwingine.
Mina akakumbuka kuahirisha kwake kwa safari za kurudi
nyumbani kwenda kuwaona. Kukaanza kwa kuomba msamaha akimwambia
anaumia kutowaona. Akaja hatua yakutolea tu maelezo ya kawaida
kama kitu tu cha kawaida kuwa hataweza kufika weekend hiyo na inayofuata. Ikaja sababu ya kukosa
ndege na treni. Ndipo ukaja UBABE na UKALI sasa. Kuja nyumbani ni kwa shida,
na mkali kwake japo anakuwa ni yeye mwenyewe ndiye aliyemuahidi atarudi
kuwaona.
Haya, napo akifanikiwa kufika nyumbani nako ujenzi wa
nyumba yao unakuwa unamchukulia nafasi, na kazi za huko alikotoka, zinahamia
kwenye simu. Simu yake inakua busy
akipigiwa na wafanyakazi walioko chini yake kuuliza hili na lile. Andy anakuwa
nyumbani kama hayupo au kama aliyelazimishwa kutimiza jukumu fulani.
Maisha ya ndoa ni kama yaliwekwa pembeni kabisa.
Akaonekana ni kama anatimiza jukumu zito sana la kulazimishwa.
Akawa MGENI kwenye ndoa yake mwenyewe, hajui kinachoendelea anapokuwa hayupo
na wala anapokuwa nyumbani hana muda wakutaka kujua yaliyompita. Mwingi
wa majukumu ambayo ni kweli yalikuwa MUHIMU kwao wote wawili kama wanandoa, ILA hapakuwa na MAWASILIANO&MAKUBALIANO
kama wanandoa na kuweza kujipanga na kukubaliana kupambana kwa kugawana.
~~~~~~~~~~~~~~
Mina akaumia akikumbuka uzuri aliosema yule askofu ambao Andy anao, kwake umekuwa udhaifu na mwiba wa kumchoma yeye. Jukumu alilochagua Andy lisimfie au kumuharibikia ni kazi wala si yeye na mtoto! Akalia hapo asiwe nawakumbembeleza. Mina tokea
mtoto alipenda kupendwa na mtu wa kumfuatisha ndio maana japo
alikuwa mzuri sana, hakuwahi kutafuta mwanaume mwenye pesa ila KUMJALI, ndio
maana alikuwa akilala na kila mwanaume anayeonyesha ana muda naye.
Hata kama ni konda wa daladala, hakuwa na shida kuhamia uswahilini ilimradi tu aonekane ana
muda naye. Ila si pesa utakayomuhonga. Wewe muweke mkononi, mpapase,
basi ameridhika. Hakuwa na shida. Sasa leo kujaziwa mipesa benki, gari
zuri na kumfungia hapo gorofani, silo fungu lake hata kidogo. Sicho angechagua.
Bora vile
alivyokuwa akikimbizana na Ron nyumbani kwao KULIKO hayo maisha
hapo. Akajiambia angalau huyo Andy angekuwa akirudi nyumbani hizo siku mbili
kama alivyoahidi na kumuonyesha anamtaka yeye. Kwamba ana muda naye!
Lakini Andy alikuwa akirudi nyumbani na mipango mingi mno wala yeye
hakuonekana ni kipaumbele!
Ukweli hata yeye Mina aliona jinsi mumewe anavyoingiza
pesa. Ujenzi wa nyumba ya Kigamboni uliendelea kwa kasi tena kwa thamani
za hali ya juu. Na yeye Mina alikuwa na pesa nyingi! Maisha kwake na mama yake yakabadilika
kabisa.
Kila
alipokuwa akinunua kitu kizuri alimfikiria na mama yake. Mina na mama
Ron wa miaka mitatu iliyopita, sio hawa. Waliosheka vizuri na vitu vya thamani. Kwa pesa ya Pius
na ya ziada ya mumewe wakasaidiana na Ron, wakamaliza kujenga kwao. Tena ndani
na nje. Alimshirikisha Pius juu ya tatizo la maji nyumbani kwao, akamsaidia
mpaka mama yake akapata maji mpaka ndani.
Pius alimpa pesa akanunua matanki makubwa yakuhifadhia
maji kwao. Usingekosa maji nyumbani kwa mama Ron. Mama yake akawa mwenye furaha
KULIKO hata Mina mwenyewe, akifurahia mafanikio ya Andy, ASIJUE na
pesa nyingine, tena NYINGI zinatoka kwa shemeji Pius.
Sasa hivi Andy yupo nje ya nchi kwa ahadi kuwa
akirudi atatulia. Lakini Mina anamjua Andy wa baada ya ndoa. Hajui mahusiano ya mume na mke, ila mwadilifu wa kazi. Tena mwadilifu haswa, familia yake changa ndio iliyokuwa ikilipa garama. Mina ndio akawa muendesha familia hiyo. Uzima na
ugonjwa wa huyo Ayan ilikuwa Mina bila Andy kupata muda wakujua
maendeleo yao.
~~~~~~~~~~~~~~
Sio kuwa kina Ruhinda hawakuliona hilo. Zaidi baba
yake lilimuogopesha sana. Mina alikuwa binti mdogo, tena mzuri SANA.
Hakuna anakopita usigeuke. Hata kama hukumuona, basi cheka yake nzuri
itakufanya utake kumuona mchekaji. Leo anamuona binti huyo anaachwa
akizunguka tu hapo jijini, kwa uhuru wote!
Hamna mtu anayejua anaingia saa ngapi na kutoka saa
ngapi! Akaangalia Mzee huyo, akashindwa kumwambia mwanae kwa kuogopa
kumuudhi. Yeye Mina ndio alijua anaingia na kutoka saa ngapi hapo nyumbani.
Nini afanye na mtoto huyo. Akawa ni kama binti ambaye hajaolewa.
Akizunguka nyumba hii na ile kuomba msaada wa kushikiwa mtoto ili aende huku na
kule.
Kilichokuwa kikiwatia moyo, ni ile hali yakumuona Mina
anawakimbilia wao zaidi. Hatasita kumpigia simu mama Ruhinda na nyadhifa
zake zote, atoke kazini aende akakae nyumbani kwake kwa masaa machache aende
kwenye mtihani, au kwenda kumuacha kwa wakweze akisema anawahi kwenye mtihani,
atarudi. Nidhamu kwa wakweze na kwenda kushinda huko hata siku
nzima akalifanya jambo la kawaida kwake. Wakausoma moyo wake, wakamuona na yeye
ni kama mtoto anayetafuta kwa kiu mahusiano. Mina sio
mgomvi, mvumilivu na anapenda watu.
Ila kuachwa mwenyewe vile! Mpaka lini?
Hilo likawa swali linalomtia wasiwasi sana mzee Ruhinda, lakini
akajiambia anyamaze tu. Kila Andy alipokuwa akitoa UDHURU wakutokuwepo
nyumbani kwake na akajua, alikuwa akishituka sana moyoni. “Unawezaje kuacha familia changa kama hiyo
kwa muda mrefu hivi?” Akawa mtu wakujiuliza mzee Ruhinda na kubaki akitizama
tu kwa macho.
~~~~~~~~~~~~~~
Swala kama Andy ni muhuni au ameanzisha
mahusiano mengine ya kimapenzi huko nje, hakuna aliyewahi kumtilia mashaka.
Hata kwa kumtizama tu, ungejua ni kijana mwadilifu. Anajiheshimu.
Ila majukumu yake ya kazini, aliyaweka mbele, akijiambia na kuwaambia
watu, itakuja kubadilika. Hakuna aliyeliona hilo, mpaka hapo Ayan ana miaka
mitatu, baba yake anahangaika na majukumu ya kazi.
~~~~~~~~~~~~~~
Kesho
yake Andy alipiga simu kutaka kumtaarifu Mina kuwa alifika salama, lakini Mina hakupokea.
Ikaita na kuita, Mina akaona azime kabisa. Alipomkosa Mina akapiga simu kwa
mama yake, mama Ruhinda. “Naona mambo yake na mtoto tu
yatakuwa yamemtinga, lakini yupo salama. Jana nilirudi nyumbani, baba yenu
akaniambia alipita hapo kuacha gari yako. Ilikuwa usiku, na hana usafiri
wakumrudisha nyumbani yeye na mtoto. Lakini uzuri Pius naye alikuwa amepita pale
nyumbani, ndio akawarudisha nyumbani kwenu. Nilimsikia baba yenu
akimuuliza leo asubuhi kwa simu, nikamsikia Pius akisema aliwafikisha salama.”
Andy akanyamaza. Akajua Mina bado amemkasirikia.
“Basi nitawajaribisha tena baadaye.” “Vipi lakini huko?
Unapaonaje?” Akauliza mama yake. “Mapokezi sio
mabaya. Nashukuru.” “Afadhali.” Mama Ruhinda akaishia hivyo tu kama aliyejionya
asiwe anaongea mengi na mtoto huyo asije akaharibu tena. Andy akaaga.
~~~~~~~~~~~~~~
Jioni Pius tena akapita kuwaona. Lakini alishazungumza
na Mina asubuhi kuwajulia hali yeye na mtoto. Mchana tena alipiga,
lakini ndipo Mina akawa amezima simu ili mumewe asimpate. Ndipo akapitia
sasa kujua kulikoni.
“Kwema? Mbona hupatikaniki kwa simu?!” “Kwema.
Nimekuwa na mambo mengi tu. Lakini tupo salama.” Mina akajibu wakati
anamfungulia mlango shemeji yake. Macho mekunduu, na yamevimba. Pius akaingia
kabisa na kukaa.
Mina akaenda kukaa pembeni yake, Pius akabaki
akimwangalia. “Sijapika leo. Ni chakula cha mtoto tu, labda nikupe juisi au
ungependelea soda?” Mina akavunja ukimya. “Na wine hatuna. Tokea mmalizie siku ile na mama, sikununua tena.” “Basi
nitakuja nazo kesho. Usijali. Lakini kwa nini hujapika? Utakula nini?” “Nasikia
kushiba leo. Sijisikii vizuri.” Mina akaongea kwa upole, macho chini.
“Unaumwa?” “Hapana. Nafikiri ni mawazo tu shem. Lakini
nipo sawa. Usiwe na wasiwasi. Hata kutonipata kwa simu, nikutaka muda wakufikiria.”
“Juu ya nini?” Mina akanyamaza. “Nilikwambia unaweza kuzungumza na mimi,
chochote Mina.” Mina akanyamaza.
“Niambie unafikiria nini?” Pius akauliza kwa
kubembeleza. Kaka hao walifanana, ungejua ni ndugu tu. Kasoro Pius hakukolea
rangi kama wenzie, yeye alikuwa maji ya kunde,
na alionekana ameshiba madaraka na pesa. Hapo alipokaa, harufu ya
neema ilienea hapo sebuleni. Msafi kama ndio anakwenda kazini, kumbe ni
jioni anatoka.
Akamsogelea Mina na kumshika mkono. “Mina?” Mina
akamwangalia. “Nini kinakusumbua?” Shemeji akabembeleza. “Nafikiria
maisha yangu shem. Mimi kama mimi na hatima ya mtoto wangu. Hiki anachopitia
Ayan, kukuzwa na mama tu, hamna tofauti na kaka yangu Ron alivyokuzwa
na mama peke yake, wakati baba alikuwepo.” “Lakini Andy atarudi
baada ya miezi minne!” Mina akamwangalia Pius kama kumsuta.
Pius akacheka. “Haya, tuseme akijiweka sawa, atatulia
nyumbani.” “Ambayo hiyo ni lini, shem?” Mina
akauliza taratibu tu. Akajifuta machozi. “Andy
anapenda kazi kuliko kitu chochote kile. Akirudi, kitakachobadilika ni jina tu
la mahali atakapotakiwa kuwepo. Tena akionyesha ni muhimu sana, na hawezi
kusubiri. Kwa hiyo yatakuwa ni yale yale.” Mina akaendelea taratibu kwa
kuumia.
“Mimi nisingeweza kufanya anachofanya
Andy. Unawezaje kuishi, tena sio kwa muda. Kuishi mbali na watu unaowapenda?
Mbona hapa Dar kazi zipo tu shem? Au hata kwa nini asituchukue tukaishi
naye huko? Ni nini chakusumbua familia kwa kiasi hiki! Ona mwanangu!
Anakuwa bila baba! Wanaume anao waona ni babu yake, na nyinyi anko zake tu.
Hana tofauti na sisi.” Mina akaendelea.
“Andy hajui uzima wangu wala ugonjwa.
Kila kitu nilazima umuombe. Sio kama wewe hivyo unavyofanya kuniwekea pesa. Na
pia hata hajiulizi ninaishije kwa matumizi yangu binafsi!
Inamaana hapati hata muda wakunifikiria sababu ya majukumu! Maana
ingekuwa mwanaume mwingine, angejiuliza. Hivi nilivyo, natunzwa na nani!
Lakini hilo halipo kwa Andy sababu ya majukumu. Naishi hapa kama
mtu niliyezalishwa tu na mwanaume, tena kama mume wa mtu ambaye anaishi
na familia yake huko Dodoma. Sasa ndio najiuliza, hiyo itaendelea mpaka lini?” Pius akanyamaza kama aliyefungwa mdomo maana ilikuwa
kweli.
Akaona abadili mazungumzo. “Unataka kula nini niende
nikakuletee?” Mina akanyamaza. “Lazima kula Mina. Upo na mtoto. Naamini hivyo
sivyo unavyotaka Ayan awe anakuona kila siku. Hutaki mtoto wako akue kwenye
mazingira ya simanzi. Sikatai kuwa unatakiwa ufikirie, lakini
nataka kukukumbusha upo na jukumu la mtoto pia. Anakutizama wewe
zaidi na ndio mfano mkubwa wa maisha atakayokuwa nao. Ninauhakika unataka akue
awe mtoto mwenye furaha, mtulivu na msikivu. Si ndiyo
hivyo?” Mina akakubali.
“Basi, chakwanza nilazima wewe uchukue hatua na
usimame kwenye nafasi yako kama mama. Na ukiweza, fanya yale ambayo
unajua Andy alitakiwa kufanya kama baba kwake. Nimekuona ulikuwa ukifanya
vizuri sana. Umetulia na mtoto. Sasa usipoteze dira. Kulia siku nzima na yeye
akikuangalia, unamdhoofisha. Mtakuwa wote hamna furaha. Nashauri katika
mazingira hayahaya uliyonayo sasa hivi. Hivi hivi ilivyo, tafuta jinsi
yakuishi kwa furaha wewe na Ayan. Huku ukifikiria unachofikiria.” Pius
akaendelea.
“Nimekwambia pesa isiwahi kuwa tatizo.
Mimi nipo. Ukiwa na shida yeyote ile tafadhali usisite. Na
nitajitahidi niwe nakuwekea pesa za matumizi ya hapa nyumbani, na kila mwisho
wa mwezi nitakuwekea benki. Bado wazo la kuanza kazi unataka lisubiri?”
“Nahofia kumuacha Ayan, shem. Huyu mtoto atakuzwa na watu baki mpaka lini, wakati mimi na baba yake wote tukihangaikia
pesa! Nimejaribu wasichana wa kazi, imeshindikana. Nahisi hapa tunapoishi pia
panachangia kuwashawishi wanapokuwepo tu hapa nyumbani wakiwa hawana
chakufanya. Wanaishia kumtesa tu mwanangu! Maadamu bado upo uwezo, acha
nimsogeze angalau afikishe miaka 4 yakuanza shule ndipo na mimi nitafute kazi.”
Mina akajieleza akiwa ametulia.
“Safi kabisa. Si umeona sasa? Kule kujua ni
nini chakufanya kwa sasa tu, inatosha Mina. Tuliza mawazo katika hilo na
tumia nafasi vizuri. Mjenge mtoto wako vizuri. Kwa furaha na mapenzi yote.
Hakikisha hapo hapabadiliki, ndipo mengine yafuate. Si unaona ni sawa?”
“Nashukuru kunisaidia shem. Naona nitafanya hivyo. Acha nitulie na mtoto.”
Kidogo Mina akatulia. Hata usoni akaonekana amepata nafuu.
~~~~~~~~~~~~~~
“Basi subiri nikakuletee chakula.” “Asante.” Pius
akatoka, Mina akaenda kuoga kabisa. Akavaa vizuri. Pius anarudi, akakutana na
Mina wa tofauti. Mrembo na cheko. “Umependeza Mina! Mpaka natamani nikutoe!”
Mina akacheka sana. “Nimeanza kufanyia kazi maneno yako.” “Safi sana. Usiwe
unashinda ukilia. Ukijisikia kulia, ingia chumbani, nipigie simu ulie na
mimi lakini sio mbele ya mtoto.” Ikamgusa sana Mina. “Asante shem.” Akampa shemeji yake busu la
shavuni lililomsisimua Pius vilivyo. Akamuachia chakula nakuondoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Mapenzi kwa
binti huyo mdogo haswa, karibu kuweza kumzaa, mke wa mdogo wake, na yeye yalishamuanza
muda mrefu sana. Pius alimpenda Mina, akawa akitaka kumuona kila wakati
na kumsikia kwenye simu mara kwa mara. Akikaa naye karibu ikawa ndio burudani
moyoni kwa Pius. Andy ndiye aliyemsaidia kumsogeza kwake zaidi. Ubusy wake Andy, na kwa kuwa na yeye ni kaka
wafamilia, ndio ikawa zawadi
yake. Anatumwa na kina Ruhinda kumtizama mke wa mdogo wake, lakini kumbe
ndio ilikuwa furaha yake.
Alipoona Mina anaachwa huru na mumewe hapo
jijini, na yeye wasiwasi ukamwingia kama baba yake. Na yeye akaamua
kunyamaza kimya, lakini akachukua hatua yakujimilikisha Mina. Akamvuta
karibu yake zaidi. Wivu ukaanza kwa Mina, utafikiri yeye ndio Andy! Anahofia
walimwengu wasije kumteka. Mtoto akiumwa, au hata yeye mwenyewe Mina
asilalamike kuumwa kidogo tu, Pius yupo. Tena yupo kwa hali na mali. Pesa yakutosha akawa akimpa Mina kiasi chakumshangaza
hata Mina mwenyewe.
Akiwa na tatizo lolote lile, Pius akawa kimbilio
la Mina. Akamsogeza mpaka nyumbani kwake, ili tu azoeane na Raza na awe huru
kufika kwake. Lakini Mina akagundua Raza amembadilikia, hampendi kabisa.
Dada huyo msomi, mwenye pesa akawa na mambo ya kulalamika kama mswahili ambaye
hakwenda shule, anayeshinda kibarazani tu kuzungumza ya watu, siku nzima.
Chuki yake kwa Mina akashindwa kuificha. Na
wala hakuweza kuwa mnafiki kwa Mina. Mina hakujua ni kwa nini,
lakini hakuweka mazingira rafiki
nyumbani kwake, si kwa Mina tu hata mwanae pia.
Wakati mwingine Mina akifika nyumbani kwake na mwanae,
anaweza kumuonyesha na yeye ndio anataka kutoka, na Mina aondoke.
Tena kwa waziwazi. Na swala la kuacha mtoto wake kwake, alishalalamika
kuwa msichana wa kazi aliye naye ni mmoja tu. Kumuacha Ayan pale ni kumuongezea
majukumu msichana wake wa kazi, anaweza kukimbia kwa hofu ya kuongezewa
majukumu.
Kwa hiyo Ayan alipokelewa hapo siku ambazo Raza
mwenyewe anakubali kuwa atakuwepo naye pale, tena akiwa ameombwa na mama
Ruhinda, au Pius akiwepo hapo nyumbani. Vinginevyo aliachwa kwa mzee Ruhinda.
Msichana wa kazi anakaa naye ndipo mzee au mama Ruhinda anarudi kukaa naye kama
mama Ron yupo na majukumu mengine.
Paulina yeye alijulikana. Hata watoto wake
mwenyewe hakuwa na muda nao, labda Devi akisaidiana na wasichana wake wa kazi.
Kwanza mvivu na hapendi majukumu ya nyumbani kabisa. Na
wakati wote kwake kunakuwa na wasichana wawili wa kazi pamoja na kijana wa nje.
Dada huyo msomi mwenye PHD, ukimtizama tu, utaona aibu yakumuomba akukalie
na mtoto wako, labda umpe kalamu. Mpenda kazi, kama Andy. Majukumu ya
ofisini ndio kipaumbele, nyumbani ni mumewe.
Paul naye mara chache. Tena akiachiwa mtoto hatakataa,
ila baada ya nusu saa ukimpigia simu, utamsikia yupo na mtoto hospitalini.
Alipata dharula, anamgonjwa huko. Anamtibu na Ayan akimsaidia hapohapo
alipo. Hatamuacha mtoto popote, ila ujue atazunguka naye kila mahali mpaka
mawodini kwa wagonjwa wake. Ndipo mzee Ruhinda akamkataa Paul kuwa hafai
kuwa na mtoto. “Jamani, mkikwama kabisa msisite kuniambia.” Paul alikuwa
akiwachokoza. “Wewe hapana bwana! Utamtia maradhi mjukuu wangu bure!”
Mzee Ruhinda akawa akimkataa kabisa.
Swala la kupigiwa simu Pius na kusema yupo kwa Andy,
wala si kwa Mina tu, likawa likisikika la kawada na la kujali
japo si kwa Raza ambaye alishakiri kwa mumewe kuwa hao kina Ruhinda wana mtetemekea
Mina. Akikohoa tu, kila mtu kwenye familia hiyo anamkimbilia. Akatoa
mengi ya kukashifu akiona Mina ndio anatetemekewa kama mungu mtu! Akawa yeye anamkwepa Mina na
mwanae.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakati Andy Akipambana Na Maisha Ya Kazi, Ili Kuleta Maendeleo Kwenye Familia Aliyoiacha Katikati Ya Jiji La Dar, Kaka Yake Ameona Aingilie
Kati KUMSAIDIA Kumtenga Mkewe Na Vishawishi.
Yale Yote Ya
Andy Aliyoyaacha Kwenye Familia Yake, Amekusudia Kuyabeba Ili Kuziba Pengo la Andy, Ili Mina Asione Upungufu, Na Kushawishika Na Wanaume Wa Nje.
Ni Nini
Kitaendelea?
Usikose
Muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment