Alipokaribia mitihani ikabidi Mina kutafuta muda wa
mazungumzo rasmi na Andy. Alimtumia ujumbe kuwa anaomba atafute muda usio na mwingiliano,
ampigie kwa kuwa ana kitu cha muhimu sana anataka kuzungumza
naye. Usiku kabisa Andy akampigia. Akajua ndio muda aliopata. Mina akajiweka
sawa ili kuzungumza naye bila hasira. “Nina mitihani
ambayo sitaki chochote kiingilie Andy. Na nimechoka kumuhangaisha mtoto. Juzi
nimetoka kumchukua kwa Raza, sijafurahia jinsi alivyoniangalia na kunijibu.
Nimebakisha kidogo tu nimalize. Tafadhali naomba chukua likizo hata ya siku 10
tu, nifanye mitihani.” “Sawa.” Mpaka Mina akashangaa. Hakutegemea jibu
la kukubaliwa kwa haraka kiasi hicho.
“Weekend hii nitakuja, tutapanga vizuri.” Mpaka Mina akakosa jibu. “Mina?”
“Kama nitakuona Andy! Maana huwa unakuja na kuishia kwenye ujenzi Kigamboni.”
“Si nimetoka kukwambia kuwa nitakuona weekend hii? Unataka nini kutoka kwangu Mina?”
“Ungeniuliza mapema hilo swali, ningefurahi sana Andy. Ila pia kwa kuwa
umeuliza acha tu nikwambie.” Andy kimya.
“Upo Andy?” “Nakusikiliza maana sijui tena
chakufanya!” Andy akajibu. “Mimi nakutaka wewe Andy. Ukiniambia nichague, ni heri kuwa
na wewe kuliko hili gari na hiyo nyumba ya Kigamboni. Vyote vinakosa maana kama
vikiwepo hapa, halafu wewe haupo Andy.” “Lakini ni kwa muda tu
Mina!”
“Ulianza na Dodoma tu Andy! Sasa hivi
umekabidhiwa Morogoro na Iringa.” “Bado sijakabidhiwa. Nashika kwa muda tu.
Mambo yatapungua, nitarudi nyumbani na tutakuwa wote.” “Sawa Andy! Naomba usije
ukanogewa na kunisahau kabisa. Jua nipo nyumbani, nakusubiri.”
“Nitakuona weekend hii,
kwa hakika.” Wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~~
Weekend hiyo Andy alirudi nyumbani, hakugusa chochote,
akawepo tu nyumbani na Mina pamoja na Ayan. Mina akakatwa kiu zake zote. Andy alimtendea haki vilivyo. Mina alijawa
cheko kila wakati. “Nakupenda Andy.” Mina akarudia tena na tena kila
aliposhikwa na kukumbatiwa na Andy. “Nakupenda Mina. Nakuahidi mambo
yatabadilika.” “Kweli Andy?” “Kabisa. Na nitakuja kukaa na mtoto siku tatu
kabla yakuanza mitihani yako.” Hapo napo Mina akatoa penzi zito la shukurani.
Jumatatu Andy akaondoka na kurudi Dodoma.
~~~~~~~~~~~~~~
Andy akawa mwaminifu katika hilo. Siku 5 kabla ya
mitihani ya Mina, akarudi nyumbani. Akawa baba kweli kweli na kumshangaza
Mina. Akitoka lazima awe na mtoto wake. Kumlisha na kumfanyia yote bila hata
kuombwa na mkewe! Mina akapata muda wakutosha wa kujiandaa na mitihani.
Kukawa na amani na utulivu kwenye kila nyumba
na ofisi aliyokuwa akitembezwa huyo mtoto. Mina naye akatulia.
Akakazana akifanya mitihani yake vizuri na kwa amani hata mama yake hakuamini
kama ni Mina yule waliyekuwa wakimlazimisha kusoma, sasa amegeuka ndiye mwenye njaa haswa na shule!
Mama Ron akaona Mungu amemjibu kwa wakati
mmoja. Ron amepandishwa cheo, Mina ametulia nyumbani kwenye ndoa yake na
anasoma! Hakuna jinsi ungemwambia mama Ron Mungu hajibu maombi akaamini.
Imani yake kwa Mungu ikaongezeka maana hata yeye maisha yalimbadilikia.
Ron na Mina walikuwa wakimtunza sana huyo mama yao aliyekuwa ametengwa na ndugu
na kuachwa na mume.
Baraka Nyingine
Tena.
Wakati Mina anafurahia uwepo wa mumewe nyumbani,
familia imetulia, aibu ya kuombaomba kushikiwa mtoto imetulia,
asijue likizo hiyo aliyochukua mumewe ilikuwa na jambo nyuma yake.
~~~~~~~~~~~~~~
Mina alitoka kwenye mtihani wa mwisho akiwa na
furaha zote. Akakuta Andy na mtoto wanamsubiria nje ya chuo. Akacheka. “Vipi
mtihani?” “Mgumu Andy!” Akalalamika wakati anakaa sawa garini. “Pole na hongera
kumaliza.” “Asante. Nashukuru kuja kuwa hapa na sisi. Najua una mambo mengi.
Lakini kwa hili, nakushukuru.” Andy akacheka huku akiondoa gari.
“Nataka nikakupongeze.” Mina akacheka. “Nataka
twende tukajifungie Bagamoyo. Siku 4 tu. Sisi watatu tu.” Mina akafurahia sana
hilo asiamini. Wakati wanarudi nyumbani kujiandaa, njiani akampigia simu mama
yake kumuaga na kumpa habari za mitihani. Kisha akamtaarifu na mama Ruhinda
kuwa hatakuwepo weekend
hiyo, atakuwa mapumzikoni na mumewe pamoja na Ayan. Kisha akazima simu
kabisa.
Hakutaka muingiliano na yeyote yule! Andy wake yupo! Hataki kelele na mtu ila kumsikia tu Andy
na mwanae. Ungemuona Mina, ungedhani amepewa ulimwengu kumbe Andy amempa muda wake. Dhambi zote akasamehe. Akasahau yote na wote, akili
yote kwa mumewe.
~~~~~~~~~~~~~~~
Mina, Ayan na Andy walifika Bagamoyo wakiwa wamejawa
vicheko. Hata Andy alijua Mina anayo furaha. Akafanya na yeye ajisikie
vizuri. Hoteli tu waliyoshukia, ungejua pesa ipo. Waliagiza chakula chumbani,
Mina akiwa anamuogesha mtoto wao baada yakujimwagia maziwa. Andy akampokea
wakati wanatoka bafuni. Akamchokoza Ayan wakati mama yake anamwandalia nguo.
“Utafanya nini baada ya hapa?” Andy akamuuliza.
“Nimemuhangaisha sana mwanangu Andy. Nataka nitulie nyumbani. Tupendane
kwanza hata kwa mwezi. Ndio nitajua wapi pakutafuta kazi na mimi
nianze kuingiza pesa, angalau nikupunguzie majukumu labda utapata muda wakutulia
nyumbani na sisi.” Mina akaongea kwa upole.
“Siku ile nilikuwa nimechoka Mina! Si wewe wala Ayan ni mzigo kwangu. Nyinyi
ni jukumu ninaloyafanya kwa furaha kabisa. Ila ile kazi kule nafanya kwenye
mazingira magumu sana! Natumia muda na nguvu nyingi kuelekeza hiyo timu
mpya ya wafanyakazi, na wateja pia.” Mina akanyamaza. Hakumjibu. Andy akajua ile
siku aliumia .
~~~~~~~~~~~~~~
Akafikiria na kugundua ni kama Mina aliacha
kabisa kumuomba pesa zake yeye binafsi za matumizi. Akabaki akifikiria
nakuvuta kumbukumbu zaidi. Kila pesa aliyoomba baada ya yale mazungumzo,
haikuwa kwa ajili yake tena. Lakini Mina hakuonekana kama mwenye shida!
Alizidi kupendeza, tena sana. Hata akimwangalia akagundua ana hali nzuri
ya kitajiri. Kila kitu chake kilikuwa cha hali ya juu mno. Sio vya bei ya kawaida. Andy akamwangalia tena. Hata
hapo alikuwa nadhafu, amejaa dhahabu kila mahali!
Akataka kutafuta muda wakumuuliza anakidhi vipi tena mahitaji yake binafsi, mbona haombi tena
pesa, akaona asianzishe jambo jingine, wakati LAKE, lililomfanya awalete
hapo, Mina akidhani ni mapumziko ya yaliyojawa upendo na kujirudi, kumbe
anayo ajenda yake, bado hajazungumza naye. Akaona hilo la ukidhiji wake wa mahitaji, alinyamazie tu. Kumbe kaka
yake anamwaga mapesa kwenye akaunti ya Mina, wala si kumrushia kwenye
simu! Hapo Mina anapesa kama ameajiriwa kwenye kampuni kubwa na kulipwa
mshahara wa hali ya juu sana.
~~~~~~~~~~~~~~
Mina akamvalisha mtoto wake kimya kimya, akamlisha
kisha akamuweka kitandani na chupa ya maziwa. Mtoto huyo wa Mina, alikuwa
akinywa maziwa, kila wakati, kama maji ya kunywa. Na hajali. Yawe
moto, vuguvugu au yawe baridi, atakunywa tu. Na ni mara chache sana
ukimsikia akilia.
Mina akarudi kukaa karibu na chakula. “Vipi na wewe
huko? Ipo hata dalili yakurudi huku Dar au ndio umehamia huko
moja kwa moja?” Mina akauliza kwa wasiwasi. “Sasa hivi nataka tuishi
wote Mina. Popote nitakapokuwepo, nataka na nyinyi muwepo.” Hilo Mina
akalifurahia.
“Itakuwa afadhali Andy! Hivi tunavyoishi sidhani
kama ni sawa.” “Utakuwa tayari kuhama hapa Dar?” “Unafikiri hawatakurudisha
tena Dar?” “Sidhani. Labda niache kazi nitafute kwengine.” Mina kimya.
“Naomba niambie Mina.” “Sijui Andy! Lakini naona tumeachana
muda mrefu sana. Umekuwa ukifanya mipango yako bila hata kunishirikisha!
Sasa hivi umefika mbali! Ukiniomba ushauri leo, nashindwa hata
naanzia wapi!” Mina akalalamika.
“Tulianza vizuri Andy, ni nini kilitokea tena!?”
“Maisha tu Mina. Majukumu.” “Mmmh!” Mina akaguna nakuanza kula. “Mbona
unaguna?” “Nahisi tofauti Andy! Tulipoteza lengo. Tukaweka vitu
vingine mbele, tukasahauliana. Ulifika hatua yakunihesabia Andy!
Wakati mimi sijawahi kukuomba gari wala haya maisha. Wewe
mwenyewe ulifanya, nikashangaa ukageuka nakuanza kulalamika!”
“Sikukusudia mpenzi wangu. Siku ile nilikuwa nimechoka, nahisi nikakumalizia
wewe hasira. Naomba unisamehe.” “Nimekusamehe Andy.” Akakubali hapohapo bila
kubembelezwa.
“Naamini hatupo mbali sana Mina. Unafikiri tunaweza kuendelea?
Au umeshanichukia kabisa?” “Mimi nakupenda Andy. Naamini tunaweza
kurekebisha.” “Hapo umenipa moyo.” Mina akacheka. “Sasa je, utakuwa
tayari tukaishi Dodoma?” “Ndio itakuwa maisha yetu yote!?” Mina akauliza
akifikiria familia yake. “Tutaangalia watakachotulipa na upepo. Tukiona
hapatufai, hapa Dar tuna nyumba Kigamboni. Umesoma na mimi nimesoma, hatuwezi
kushindwa kupata kazi, lakini tusije kuishi tena mbali mbali.” Mina alifurahi
huyo! Hakuamini.
“Tutaongozana popote Andy. Na mimi nataka tuwe pamoja.
Sio hivi tunaishi mbalimbali halafu bila sababu! Sioni kama ni sawa.
Hata watu watakuwa wakitushangaa! Ingekuwa mimi nimefungwa na kazi huku siwezi
kuwa na wewe huko, hapo sawa. Lakini kutuacha tu nyumbani halafu wewe
unakua pengine! Mimi hivyo sipendi Andy. Nataka kuwa na wewe.” Andy
akacheka akimfikiria Mina na anachotaka kumwambia.
~~~~~~~~~~~~~~
“Njoo kwanza Mina wangu.” “Ukitulia unakuwa mtu
mzuri Andy!” Andy akacheka akitafuta njia ya kuzungumza naye ili kumuweka sawa.
“Nakuwa nimechoka! Njoo hapa.” Mina akahamia mapajani kwake kwa upendo. “Sasa
nikwambie kitu?” “Nakusikiliza.” “Nakuomba nipe miezi 4 mingine. Niende
safari ya kikazi, ni masomo mafupu.” Mina akaishiwa nguvu, silo alilotegemea.
“Minne tu. Nikirudi baada ya hapo, tunahamia Dodoma.
Tunaanza kuishi wote.” Mina akasimama. “Usiondoke Mina. Njoo tuzungumze.”
“Labda niulize Andy, hapa unaniaga au unaomba tushauriane?”
“Nimechaguliwa na ofisi kwenda kuongeza ujuzi kwa miezi minne tu, nchini Uswiz.
Nita..” Mina akaondoka kuelekea bafuni.
“Mina?” Andy akamuita. “Tupo hapa kunitaarifu
Andy. Umeshanitaarifu. Sitaki ugomvi na maneno. Naomba
tumalize hizo siku zilizobaki hapa hotelini kwa usalama. Na mimi nimechoka
kweli sababu ya mitihani. Tupumzike, tukitoka hapa, maisha yakaendelee vile ulivyochagua
wewe Andy.” “Mbona unafanya mambo kuwa magumu Mina!? Hizi nafasi
watu wanazililia!” “Andy, mwenzio nimechoka. Naomba nikaoge nilale.”
Mina akaelekea bafuni. Hata hakumalizia kula.
Akaoga, nakutoka kwenda kulala kitandani. Akajifunika,
kimya. “Acha hasira Mina.” Kimya. “Mina?” “Naomba kulala Andy. Naomba tutumie
hizi pesa ulizolipia hapa hotelini vizuri. Unafikiri tunaweza?” “Kwa nini
tusimalize hili?” “Kwani unataka kunisikia nikisema nini Andy? Mbona
kama nimekuachia uendeshe hii familia vile unavyopenda wewe? Mimi
sijakataa chochote. Tuendelee hivyo hivyo unavyofikiri ni sawa. Mimi
sina chakuongeza tena. Lakini kama unataka nisilale, nitakaa.” Akatoka
kabisa kwenye shuka. “Basi bwana!” Andy na yeye akaelekea bafuni, Mina akarudi
kulala.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakakaa hapo hizo siku 4 lakini kimya kimya. Mina
mchache wa maneno. Anajibu kila swali analoulizwa vizuri tu. Bila kiburi wala
kinyongo. Anakula vizuri. Anaweza kutoka na mtoto kwenda kucheza, wakati
mwingine Andy anawafuata, wakati mwingine Andy anabaki chumbani kupiga simu
zake. Wakati mwingine Mina akisikia simu yake inaita tu, anamchukua mtoto wake,
anatoka hapo chumbani anakwenda naye upande wa baharini kucheza mpira
mpaka Andy awafuate.
Siku zikaisha, wakaondoka hapo hotelini kimya kimya. Hawakugusana
hata kwa mapenzi. Walipofika Tegeta, Mina akaona Andy anaelekea nyumbani kwao.
Hakumuuliza. “Nataka kwenda kumuaga mama.” Hakumjibu. Tena safari hii akakaa
kiti cha nyuma na mtoto wake.
Kwa Mama Ron!
Walifika kwao wakamkuta mama yake na Ron. Mama yake
Mina aliposikia Andy anakwenda masomoni, tena Ulaya! Akafurahia SANA.
“Yaani ndoa yenu imekuja na baraka baba! Hongereni sana. Umeanza Dodoma,
wakakuongeza na hiyo mikoa miwili mingine, sasa hivi ndio wanaona ukaongeze
ujuzi! Mungu mkubwa.” Mina akamuona mama yake amefurahia sana. Ila Ron
alinyamaza kimya hata hakuchangia kitu.
“Naomba muendelee kumsaidia Mina kwa miezi hii 4 tu.
Nikirudi sitawaacha tena. Nahangaika mama kwa ajili ya familia yangu!”
“Na Mungu atakusaidia baba. Sisi tupo, wala usiwe na wasiwasi. Kwanza
mwanao huyo hana shida baba. Mpole kama wewe.” Andy akacheka.
“Kweli kabisa! Yeye umpe maziwa yake, hataongea wala
kulia. Kimya.” Mama Ron akatoa sifa nyingi wee. Akimpamba mkwewe na
mjukuu wake. Mina kimya akisikiliza. Mwishoe wakaaga na kuondoka.
Kwa Ruhinda.
Wakaelekea mpaka kwa Ruhinda. Akamkuta baba na mama
yake. Akawaambia vile vile kama kule kwa kina Mina. Ila hapo pakazuka ukimya
mkubwa tofauti na kwa mama Ron. Ikawa kama wazazi wake hawajui waseme
nini, mwishoe mzee Ruhinda akauliza. “Unaondoka lini?” “Kesho usiku.” Pakazuka
ukimya mwingine. Mpaka Mina akashangaa asiamini kama safari ndio ipo
tayari kwamba mpaka na tiketi! Akaumia sana. Lakini kama aliyejionya,
akanyamaza.
“Nilazima niende, lasivyo muda wote
niliohangaika Dodoma, Morogoro na Iringa utakuwa bure. Ni miezi minne tu
yakumalizia ili nipewe zone nzima ya kanda ya kati. Najua baada ya hapo nitatulia na familia.”
Ikabidi Andy ajitetee sababu ya ukimya, alipoona wote kimya.
“Huyu mume wangu hana neno. Hapa ni nyumbani. Mkeo
naye kama unavyomjua, hana makuu. Ni hivyo tu wakati huu na mimi nina
safari mbili tatu hivi. Nikirudi, nitatulia nao.” Akajibu mama Ruhinda akiwa
amempakata Ayan. Lakini ni kama na yeye alijitoa, akiaga kuwa atakuwa busy na safari za kikazi. Mzee Ruhinda kimya kwa muda kama
anayefikiria.
“Ruhinda?” Mkewe akamshitua. “Kuhusu hawa wawili usiwe
na wasiwasi. Nilimuona vile Mina anavyojituma na mambo ya familia. Amehangaika
hapa na mtoto naona mpaka amemaliza hiyo miaka miwili akiwa peke yake. Sidhani
kama atashindwa hiyo miezi minne tena. Na kama tulivyokwambia Mina, muda na
wakati wowote unapokuwa na shida, tupigie.” “Asante baba.” Mina akajibu,
macho ameelekezea chini akijikaza asilie. Wakaaga na kuondoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Walipofika nyumbani, Andy akamlaza mtoto. Akamkuta
Mina anakunja nguo chumbani. “Kuna kitu unataka nikusaidie kuandaa kabla ya
hiyo safari?” Mina akauliza. “Naona kila kitu kipo tayari. Nilishaandaa kipindi
upo kwenye mitihani. Asante.” Mina akanyamaza. “Nitarudi Mina. Na usifikiri
ndio nafurahia kuwaacha! Na mimi natamani tubaki wote.” “Sawa Andy.
Mungu akusaidie.” Akajibu tu hivyo Mina.
~~~~~~~~~~~~~~
Akaingia kuoga, akamuacha Andy anasoma vitu na kuweka
kwenye kibegi kidogo. Akatoka, Andy naye akaingia kuoga, kisha akawahi
kitandani. “Naomba uniage vizuri Mina.” Andy aliingia ndani ya shuka alilokuwa
amejifunika Mina. Bila kinyongo, Mina akachangamkia penzi. Akamzungusha Andy
hapo kitandani mpaka akamuona ameridhika. Akaenda kuoga tena, akarudi
kitandani.
Andy naye akatoka akaelekea bafuni akarudi akidhani
Mina amelala, akajilaza pembeni yake. Akasikia anamvuta mkono, akaubusu
na kuuvuta karibu yake, akaukumbatia kwa upendo. “Asante Mina.”
Andy akashukuru asiamini, lakini Mina hakujibu.
~~~~~~~~~~~~~~
Kesho yake akaamka akakuta Andy alishaandaa kifungua
kinywa, mtoto msafi. Hapakuwa na maongezi mengi. Baada ya chakula cha mchana
akamuomba Mina kama anaweza yeye na mtoto wakamsindikiza uwanja wa ndege. Mina
akakubali. Muda ulipofika, akamtaarisha mtoto wake vizuri, wakaondoka. Njiani
Andy akawa akimuaga Mina.
“Nitakuwa nikiwapigia simu mara kwa mara.” Mina
akabaki ametulia tu. “Nitakuwa nikikutumia pesa za matumizi kama kawaida. Sitasahau.
Halafu hii gari yangu unaweza kwenda kuiacha nyumbani kwa wazazi kwa ajili ya
usalama.” “Nitafanya hivyo nikitoka tu uwanja wa ndege.” Akaafiki Mina bila
ubishi.
“Nakupenda Mina. Nakupenda sana mpenzi wangu.
Nahangaika, lakini tukija kupumzika, tutapumzika pazuri. Tafadhali nipe hiyo
miezi minne ya mwisho. Nivumilie mpenzi wangu. Sijapoteza dira, ila inanilazimu
kuchukua au kufanya maamuzi magumu ili tu wewe na watoto mje muishi
vizuri zaidi. Tafadhali niage na kicheko angalau niondoke vizuri.” Mina alikuwa
ameshamfikisha uwanja wa ndege, Andy ametoa mabegi yake amerudi kusimama
dirishani, Mina hakutaka hata kushuka. Kimya.
Akarudi upande wa nyuma kwa mtoto wake, akambusu na
kumuaga. Kisha akarudi tena pale kwa Mina dirishani, akamkuta anafuta machozi.
“Nakupenda Mina. Nakupenda sana mpenzi wangu.” “Asante
Andy, uwe na maisha mema huko.” Mina akaaga na kuondoka.
Maisha Mapya bila Andy Nchini.
Alitoka uwanja wa ndege akaelekea Msasani. Wakati anaingia getini, Pius naye akawa
anaingia nyuma yake. Pius mtoto wa mama. Lazima amuone mama yake kila siku kama
yupo hapo jijini, na mawasiliano ya simu ni ya mara kwa mara. Na kwa asili Pius
alikuwa mtu wa kujali, mapenzi kwa mama yake yalikuwa dhahiri. Huwezi
kumsema Pius mbele ya mama Ruhinda, hapo nikutaka umuudhi huyo mama.
Alimpenda huyo mtoto mkubwa kuliko hata kiziwanda Paul. Hakuna kukosana kwa
wawili hao. Na jambo alilojua litamuuzi mama yake, hatalizungumza Pius, hata
iweje.
Mina akaenda kuegesha gari sehemu ya kuegeshea magari
lakini mwisho kabisa kwa kuwa alijua litakaa hapo kwa muda mrefu. Akashuka na
kuzunguka nyuma. Wakati anamfungua mtoto wake, Pius akamsogelea. “Vipi Mina?”
“Safi shem. Pole na kazi.” “Asante. Acha nikusaidie.” Pius akasogea pale
mlangoni. “Nashukuru. Ila nataka kutoa na hicho kiti.” Akamsaidia kufungua kiti
kizima cha mtoto, akamtoa mtoto na kiti chake. “Anasinzia huyu.” Pius aliongea
wakati anamkabidhi mtoto. “Asante. Sitakaa sana. Naingia kumsalimia baba, naona
gari yake ipo hapa nje, niondoke niwahi nyumbani ale ndio alale.” “Mtarudije
nyumbani?” Pius akauliza kwa kujali kama kawaida yake. “Hata sijui shem!
Nahisi nitachukua taksi hapo nje. Acha nisalimie ndani kwanza mengine nitajua
baadaye.” Mina akataka kuondoka.
“Mina.” Mina akasimama. “Mimi nitawarudisha nyumbani.”
Mina akainama nakuanza kulia. Giza lilishaanza kuingia. “Kila kitu kitakuwa
sawa. Usiwe na wasiwasi. Nimekuahidi mimi nitakuwa na wewe,
wakati wote. Unakumbuka?” Mina akatingisha kichwa kukubali.
“Basi naomba tuwe tunazungumza. Chochote kile, usisite
kuniambia. Hata ukitaka mtu wa kuzungumza naye, nipigie simu. Sawa?”
Mina akatingisha kichwa kukubali. “Basi naomba unyamze. Tukamsalimie mzee,
twende.” Akajifuta machozi.
Walimkuta mzee Ruhinda anasoma kitabu kama kawaida
yake akiwa peke yake, anasoma. Ni msomaji sana. Wakamsalimia. “Vipi mwenzako
ameondoka salama?” “Nilimshusha uwanja wa ndege. Ameomba niache hapa gari yake
mpaka atakapo rudi. Funguo hizi.” Mina akaweka mezani. “Hamna shida. Sasa
mtarudije nyumbani?” “Nitawarudisha mara moja.” Akadakia Pius. “Afadhali ili
asihangaike na mtoto.” Mzee Ruhinda akalifurahia hilo.
“Acha niwahi baba, Ayan anasinzia.” “Naona na chakula
humu bado, dada ndio anapika. Na mama yenu leo atachelewa.” “Nitarudi jumamosi
mcheze mpira na Ayan.” Akaongeza Mina akimchungulia Ayan kule alipojiegemeza na
chupa yake ya maziwa. “Ewaah! Hayo ndio maneno. Naona leo hataki hata kushuka!”
“Si unamjua huyu na maziwa? Hapo nimemfunga mdomo.” Mina na Pius
wakaondoka.
Inaendelea…
0 Comments:
Post a Comment