Mina alirudi kwake akiwa ameumia sana baada ya
Andy kumuhesabia kama na yeye ni jukumu zito sana linalomfanya ashindwe
kutulia nyumbani. Akajiandaa yeye na mtoto wake. Akakaa sebuleni akimsubiria
Andy. Mpaka saa 12:45 jioni inafika,
Andy hakuwa ametokea.
Simu ya shemeji yake Pius ikaingia. “Leo nimekuwa busy nimeshindwa kuwajulia hali. Nimepita pale
kwa mama, nimeambiwa leo hujatokea. Kwema?” “Kwema.” “Mbona kama huna raha,
unauhakika ni kwema?” “Kwema. Najiandaa na mtoto tunakuja ukumbini.” “Oooh!
Nishaelewa.” Mina akanyamaza.
“Kwa hiyo Andy hatakuwepo?” “Sijui Shem!
Mimi naona sijui tena.” Mina akaongea kwa
kulalamika. “Subiri hapo hapo nimpigie. Halafu
nitakupigia na wewe.” Mina akabaki amekaa na mwanae hapo kwenye kochi
akisubiria kujua mumewe yupo wapi. Mara simu ya shemeji Pius ikaingia tena. “Naona atashindwa kufika. Ameachwa na ndege.”
Mina akanyamaza na kufunga macho. Kwamba hata na treni amekosa!
“Nakuja kukuchukua wewe na mtoto. Usiendeshe
usiku huu.” “Mimi nipo sawa tu shem. Acha usisumbuke, sisi tutakuja tu.”
“Nilikwambia chochote ninachotaka kukufanyia, usihesabu kama ni usumbufu.”
“Asante.” Mina akaridhia.
Baada ya muda, shemeji yake akawa amewasili kumchukua
yeye na mtoto. Akamsaidia kumbeba mtoto mpaka kwenye gari. “Usikasirike bwana!”
“Hapana, nipo tu sawa. Pole na kazi.” “Asante. Tunafunga mwaka, ndio maana
nakuwa busy. Lakini siku chache tu tunamaliza.” Mina akanyamaza.
“Najua unachokifikiria. Lakini ujue mimi sipo
busy kama Andy. Andy ndio anaanza maisha ya kazi. Lazima apambane
ili kufikia ngazi fulani. Mimi huko nilishatoka. Ninapokwambia nipo busy, sio kiasi chakushindwa kuwa na familia. Ndio maana
sasa hivi nipo hapa na wewe, na nilishapita kwa wazazi na nishamuona Raza na
watoto. Tumeagana, wao wameelekea ukumbini, nikawaambia nakuja kwako ili
usijione peke yako.” Mina akazidi kuumia.
“Niangalie Mina.” Pius akamuita kwa upendo. Mina
akamwangalia. “Nilikwambia muda na wakati wowote ukiwa na shida yeyote.
Namaanisha yeyote ile, nipigie. Umenisikia?” Mina akatingisha
kichwa machozi yakimtoka na kutamani angeyasikia hayo kutoka kwa
Andy.
“Basi naomba usiwe na wasiwasi. Yote yatapita. Upo na
shida yeyote?” “Hapana shem. Asante.” “Una uhakika?” Mina akafikiria. “Sina
kwakweli. Huwa nikiwa nina shida, namuomba Andy anatuma.” Mina akajieleza
taratibu.
“Sasa hivi una kitu chochote unahitaji?” “Nimeandika,
nitakwenda kesho kununua. Huwa nakwenda siku za jumamosi nikiwa nimetumiwa pesa
na Andy. Ila leo nimekuwa busy halafu
nilidhani Andy angekuwepo nyumbani nimuachie mtoto niende au yeye ndio aende.
Huwa siku za jumamosi ndio zilikuwa siku zetu zakufanya manunuzi na ndio
alikuwa akituma pesa asubuhi au ijumaa usiku. Lakini naona mambo yamebadilika
kweli! Itabidi nianze kujipanga upya nikijua Andy anaweza asiwepo nyumbani.
Nijue sasa hivi nipo peke yangu. Shule na mtoto.” “Haupo peke yako bwana! Mimi nipo.”
Mina akanyamaza.
“Mina, mimi nipo.” “Acha kunitia moyo. Wewe upo na
familia yako shem. Halafu kazi, na majukumu mengine. Mpaka uje unifikie mimi na
Ayan ni saa ngapi? Nitajipanga tu.” Siku hiyo Mina kwa hasira akamlalamikia
yote shemeji yake bila kujijua. Akayatoa yote ya moyoni, akafarijiwa.
Mpaka wanafika ukumbini anacheka. Kazi ya Andy akaifanya kaka yake kwa
mkewe.
~~~~~~~~~~~~~~
Sherehe ikawa nzuri na ya kufana. Walikuja watu wa
muhimu watupu hapo kumpongeza mzee Ruhinda. Naye Mzee Ruhinda akawa amemshika
Ayan kila mahali. Akitangaza ni Ruhinda haswa, mrithi wa familia. Wivu ukawa ukimtesa sana Raza ambaye yeye,
kibinadamu, ndiye aliyetakiwa awe na huyo mrithi.
Kabla ya kuja Mina,
alipewa heshima kama mama Ruhinda
pia. Sasa hivi ni kama anasahaulika! Mina alishaingia kwenye picha, na kujazwa sifa haswa. Mzee Ruhinda ukumbini hapo
alikuwa akitangaza kuwa bila Ayan kufika hapo, shuguli isingeanza. Naye
Ayan aliposikia jina lake tu akaanza kupiga makofi akicheka kama aliyeelewa.
Wageni wote wakacheka na kupiga makofi.
Mjukuu huyo alishajua mapenzi ya babu yake, wala
hakusubiri kuitwa, akashuka kutoka pale alipopakatwa na mama yake, akamkimbilia
babu yake aliyekuwa amesimama mbele kabisa akizungumza kwenye kipaza sauti,
akataka ambebe. Mzee Ruhinda akiwa na kipaza sauti akamnyanyua na kumbusu
kwanza, akambeba vizuri, akaendelea kuzungumza na wageni wake.
~~~~~~~~~~~~~~
Sherehe ilipoisha, Pius tena akawarudisha tena
nyumbani. Safari hii vilijaa vicheko tu na ahadi ya kurudi kuja kumchukua mtoto
kesho yake ili Mina akafanye shopping
kama Andy hatatokea. “Naomba nipe akaunti namba yako niwe na mimi nakuwekea
pesa kidogo za matumizi sio kutegemea sehemu moja tu!” Kama aliyetumia akili fulani hivi, hakutaka kuwa akimrushia pesa kwenye
simu ila iwe benki kabisa.
“Hamna haja shem!” “Sasa unafanyaje kama Andy
akichelewa kutuma pesa kama hivi?” “Namuomba Ron. Halafu Andy akituma,
namlipa.” “Hayo sio maisha bwana! Wewe ulishatoka nyumbani. Mwishoe kina
Ruhinda wote tutaonekana hovyo.” Mina akacheka kwa masikitiko.
“Nitumie hiyo akaunti namba. Kwanza hayo maisha ya
kuomba omba sio mazuri. Unatakiwa uwe na pesa ya kujikimu kila wakati.
Sio kuombaomba.” Hilo nalo likamfariji sana Mina. Akatamani
kama Andy angelifikiria hilo.
Akamshukuru Pius mpaka akampa mkono, akitamani apige
goti. Kutoka kuhesabiwa na mumewe siku hiyohiyo, halafu shem anatoa ahadi
yakuwa akiweka pesa! Halafu shemeji mwenyewe ni Pius! Pesa ipo! Hilo
akajiambia wala hatajivunga. Akashukuru tena ndipo wakashuka garini.
Pius akamsaidia kumbemba mtoto mpaka juu nyumbani kwao. Yeye mwenyewe Pius
akambadilisha mtoto nguo na diaper, akamuweka kitandani na chupa yake ya
maziwa.
Ilimgusa sana Mina aliyekuwa akimwangalia nakutamani
kama angekuwa ni Andy anayafanya yote hayo. Maana hata akiwepo nyumbani
hakuwa na muda huo, wa mtoto. Busy. Shem akamgusa vilivyo. “Asante shem. Nakushukuru sana.” Pius
akamsogelea pale mlangoni, akamkumbatia kwa nguvu. Mina akatulia hapo akipumua
kama aliyepata faraja ya kweli.
~~~~~~~~~~~~~~
Pius akaondoka, akamuacha Mina akiwaza maisha yake na
Andy. Akakuta ujumbe kwenye simu aliyokuwa ameiacha hapo nyumbani kwa hasira,
Andy akimwambia kuwa amekosa ndege na treni, kwa hiyo weekend hiyo hatakuwepo nyumbani ila atajitahidi jumatano
kuwepo. Wala Mina hakujibu. Akazima simu na kulala.
~~~~~~~~~~~~~~
Maisha ya ubusy ya
Andy yakaendelea tena kwa kasi kubwa mpaka muhula wa mwisho wa masomo yake Mina,
huku bado akitaabika na swala la wasichana wa kazi. Lakini ukaribu na Pius
ukawa mkubwa sana kati yao, mpaka nyumbani kwa Andy kukawa kama kwa Pius. Na
Mina naye akazoea na nyumbani kwake Pius na Raza.
Kwa hiyo wakati mwingine alipokuwa na shuguli nyingi,
labda anapotaka kwenda shopping
zake, alikuwa akienda kumuacha Ayan kwa Raza, yeye anakwenda kufanya manunuzi
akimaliza anakwenda kumchukua mtoto wake wanarudi nyumbani.
Shida zake zote ni Pius ndiye aliyekuwa akijishugulisha
nazo pamoja na Ayan. Mina akiumwa, Pius ndio anakuwa mstari wa mbele. Kuna
kipindi Ayan aliugua, Mina alimwambia Pius tu kuwa wapo hospitalini, haraka
Pius akaenda. Akahangaika nao mpaka Ayan akamuona daktari akaambiwa hana
ugonjwa ni homa sababu ya jino lililokuwa likiota. Wakarudi nyumbani. Mina
alikaa nyumbani akiuguza, Pius akimuhudumia kwa chakula na kupita
kuwaona mpaka Ayan akapona na Mina akaweza kurudi shuleni. Andy yupo safarini
kikazi.
~~~~~~~~~~~~~~
Mina akapata msichana mwingine. Akaanza vizuri sana. Alichokosea
Mina wakati akimpongeza akamsimulia madhaifu ya wasichana wa kazi waliopita.
Akamwambia ule udhaifu wao wakumfungia mtoto ndani kisha kuondoka kwa
muda mrefu. Taratibu na yeye akaanza, anatoka masaa mawili, anarudi nakupika.
Anamkuta hapo nyumbani hajui kinachoendelea.
Sababu ya kuwa mwishoni mwa muhula, akajiunga na
wenzake kujisomea hapo chuoni baada ya madarasa. Msichana akawa anao muda
mwingi tu hapo nyumbani peke yake na mtoto. Akanogewa. Anatoka akiwa
amepika kabisa. Na kwa kuwa walikuwa wakiishi katikati ya jiji, basi wasichana
wa kazi hawakosi pakwenda. Mina akirudi nyumbani, anakuta nyumba safi, mtoto
msafi na kumepikwa.
Ila akaanza kuona tena mabadiliko kwa Ayan. Kwa
wema wa yule msichana na anavyojitahidi mbele ya macho ya Mina, akajua ni kukua
tu ndio maana anazidi kukonda, kumbe kula yake ni asubuhi anapolishwa na mama
yake, na jioni mama yake anapokaribia kurudi.
Maziwa mengi yanayoachwa kwa ajili ya huyo mtoto,
msichana wa kazi na yeye anakunywa kuondoa ushahidi. Mina hajui.
Hakukuta kosa kwa huyo msichana. Nyumba safi kila mahali, kila kitu anafanya
kama anavyomuachia maagizo. Na alikuwa mzuri sana kwenye mapishi. Akirudi nyumbani
chakula kinamsubiria.
Za Mwizi 40.
Siku hiyo nayo alirudi nyumbani mapema sababu yakuzidiwa
usingizi na kichwa kumuuma. Akashindwa kukaa mpaka kipindi cha mwisho. Akaamua
kurudi nyumbani, alale kidogo ndipo arudi akajisomee na wenzake. Sababu ya uaminifu
aliokuwa nao na huyo binti akawa habebi hata funguo za nyumba akijua anakuwepo
tu nyumbani.
Akapandisha mpaka juu nyumbani kwake. Akagonga bila
kufunguliwa ila akamsikia Ayan akilia sana ndani. Ayan si mlizi, akaingiwa
hofu. Mina akapaniki. Akasubiri nje ya mlango akidhani msichana atarudi, mtoto
akilia ndani, lakini yule msichana hakutokea.
Sababu ya kupaniki akampigia simu Andy. “Funguo nimeacha ndani na yeye amefunga mpaka hili geti
dogo!” “Subiri nizungumze na Pius.”
Baada ya lisaa pakawa pamejaa hapo nje ya
mlango wa Mina na Andy. Wakwe zake, Pius, Ron pia alifika hapo wakijaribu
kuvunja mlango. Ayan akawa amenyamaza. Wakajua labda amechoka kulia, amerudi
kulala. Walihangaika zaidi ya lisaa mbele ndipo ikabidi sasa kwenda kutafutwa
fundi wa vyuma ili aje na mashine yakukata hilo geti.
Juhudi zikaendelea mpaka wakafanikiwa kuvunja
geti, ukaja mlango. Hiyo ilikuwa baada ya masaa manne mbele tokea Mina afike
hapo. Wakaingia ndani wakamkuta Ayan amesimama kitandani, amejisaidia, diaper imejaa mkojo na kinyesi. Mina alikuwa akilia.
Mama Ruhinda ikabidi kwenda kumuogesha huyo mtoto.
Ndipo msichana wa kazi akaingia sasa. Alionekana wazi ameshituka sana. Hapo
hapo mzee Ruhinda akamwambia achukue mizigo yake yote, yeye mwenyewe
akamrudisha kwa ndugu zake na kumlipa bila kutaka ajieleze.
~~~~~~~~~~~~~~
Tatizo la
Mina likarudi pale pale. Hana msichana wa kazi na shule imefika ukingoni.
Akaanza kuhangaika. Mara Ron kaka yake amsaidie kukaa na mtoto.
Anampeleka ofisini kwa Ron ambako ndiko kulikokuwa ofisi ya Andy, baada ya Ron
kuchukua cheo cha Andy. Anamuacha hapo na begi lake na chupa kubwa ya maziwa.
Yeye anakwenda shule. Ron anakaa naye mpaka aje amchukue, ilimradi tu Mina amalize
hiyo shule.
Wakati mwingine ofisini kwa mzee Ruhinda, mara
nyumbani kwa mama Ruhinda. Kwa Raza, au Paulina. Hakuna ambaye hakusaidia
malezi ya huyo mtoto kipindi mama mtu yupo shule na dad kazini Dodoma akitengeneza pesa wawili hao
waishi vizuri mjini.
Huku Kwa Mill.
Akiwa mwaka wa
kwanza, alitokea mrembo mweusi wa Kimarekani, alijitambulisha kwa Mill
kwa jina la Kisha, akampenda sana Mill. Lakini Mill kwa kuwa alishawajua tabia
zao, hakutaka hata kumzungusha, akamkatalia. Hakuchoka kumganda Mill kwa
hili na lile ilimradi tu kuwa naye karibu. Yeye alikuwa akisomea mambo ya
maabara, Mill huo unesi. Kwa hiyo kuna masomo walisoma pamoja.
Hakuwa serious
sana na shule. Na shule yenyewe ya maabara haikuwa ya muda mrefu kama hiyo ya
unesi. Kuna kipindi aliahirisha muhula mzima. Akarudi kuendelea tena na
kumkuta yeye Mill bado akiendelea na chuo.
Akamjaribisha
tena Mill, ndio Pam akawa ameshaingia kwenye picha, Mill hasikii wala haambiwi.
Akamwambia kwa wazi kabisa kwamba yeye anamwanamke na huku nyumbani
anafahamika kama mkewe kabisa, anabaraka zote za wazazi na wameshafunga
ndoa ya kimila anasubiria afike hapo nchini Marekani, wafunge ndoa ili atambulike
hapo nchini kama mkewe kihalali. Kisha akajiweka pembeni.
~~~~~~~~~~~~~~
Sasa alipokwama
njia zote za kumleta Pam nchini na jinsi ya kuishi hapo nchini kiurahisi,
ndipo sasa ikabidi amfuate Kisha. Akajieleza ukweli wote. Kwamba amefiwa
na baba aliyekuwa akimsaidia, anaomba msaada wa ndoa,
akisharekebisha makaratasi yake, akimaanisha akisha adjust status
yake, kutoka kwenye status ya uanafunzi mpaka uraia basi atamtaliki
aendelee na maisha yake.
“Ndio
tunafanyaje endapo nitakubali?” “Ili kuaminisha watu wa Uhamiaji,
angalau tuwe na baadhi ya bills zenye majina yetu wote wawili.
Kama unaishi peke yako, unaweza hamia kwenye apartment yangu,
japo mimi siiishi sana hapo. Nakuwa huko ninakofanya kazi na kurudi hapo labda
kwa siku moja au mbili kwa juma. Upo huru kama upo na mahusiano, ila yasiwe
ya wazi mpaka watu wa Uhamiaji wakajua. Na naomba usimlete
mwanaume wako hapo kwangu endapo utahamia.”
“Cha msingi
ni usiri. Ikitokea tunatumia address moja kwamba tunaishi
pamoja, hiyo ndio wataamini kabisa. Na usiwe na wasiwasi. Kodi ya
pango nitalipa mimi mwenyewe na bills nyingine zote ni juu yangu.
Na pia nitakulipa. Utakapokubali tu, nitakulipa kiasi cha awamu ya
kwanza, kisha nakukamilishia yote tutakapo maliza process nzima.”
Kisha akaona MUUJIZA. Mungu ampe nini!
Analipwa! Halafu kuishi BURE! Simu analipiwa kila mwezi! Akajua na
chakula atapewa tu. Hakupindisha. Na hivi alishautamani
mwili wa Mill! Alitaka tu angalau amlale roho itulie. Akahamia kwa Mill haraka
sana wakati Mill mwenyewe anaishi huko anakofanya kazi za kulea wazee na
kurudi hapo mara chache chache. Hilo lilakaa sawa.
Lakini sasa akawa
ameongeza gharama zake, Kisha, na Pam nchini. Kisha lazima amlipe
na kumtunza. Halafu sasa, bado pesa ya Wizara ya Uhamiaji, ya kumuoa,
kisha kuanza hiyo proccess ya uraia, kisha kuja kuachana ambako
pia itagharimu pesa ili kukamilisha talaka nzima. Bado shule
ambayo ni lazima ikamilike maana imebeba ndoto zake kubwa. Ila garama
ya shule ingepungua endapo angemuoa Kisha. Status ingebadilika.
Kutoka kulipa ada ya International Student mpaka In-state fee.
Ambayo ni ndogo sana na rahisi kupata udhamini.
~~~~~~~~~~~~~~
Mchakato ukaanza
vizuri tu kati ya Mill na Kisha. Tena alipoona maisha yanambadilikia, akaacha
shule aliyokuwa akisoma chuo kimoja na Mill pamoja na kazi. Kama walivyo wengi
woa, Uvivu ila kujipenda. Mzigo kwa Mill ukaongezeka. Anaomba
pesa mchana na usiku. Naye Mill ili kuhakikisha hamuudhi, akawa anajitahidi.
Akiwa hapo
kwake, hawezi pokea simu za Pam, asije akamsikia Kisha, mwenye sauti ya
juu hata kwa jambo la kawaida. Ubusy ukaongezeka kwa Mill, simu za mara
kwa mara kwa Pam zikaanza kupungua. Jumbe zinachukua muda kujibiwa.
Na hivi Mill alishaanza kuhukumiwa kama anamsaliti Pam, basi hata
zungumza yake ikawa si ya uhuru. Ila kila wakati alikuwa akimkumbusha
Pam anahangaika kwa ajili yake ili waje kuishi pamoja.
~~~~~~~~~~~~~~
Ndani ya mwezi wa
kwanza karibu na mwisho wa Kisha kuhamia hapo, akarudi nyumbani kwake akamkuta Kisha.
Akamwambia ameshapata tarehe ya kwenda mahakamani kufunga ndoa,
ajiandae. Kama kawaida akamchomoa pesa, akitaka matayarisho ili apendeze
hata kama si harusi ya kweli.
Wakakaribisha watu wa chache kwa picha za kuaminisha Wizara ya Uhamiaji. Kisha
naye akakaribisha mashoga zake na watu wake wa karibu ila hakuwaambia
kama si ndoa ya kweli. Yeye alijisifu kwao kuwa amepata mwanaume anayemtunza
vizuri na anampenda sana. Wakati Mill yeye akijua si ndoa ya kweli, Kisha
alikusudia kumfunga abakie akimtunza daima.
Taka Cha
Mvunguni.
Siku moja kabla
ya kufunga ndoa, akawahi kurudi nyumbani akiwa ameshalipia mpaka sehemu
watayo jumuika wageni wao kama sherehe baada ya kufunga hiyo ndoa. Upande wa
Mill alikuwa amemualika Mike na Kamila kutokea Tanzania. Na watu
wachache sana aliokutana nao hapo nchini Marekani. Kisha na yeye alialika watu
wake wa karibu 10. Garama ikawa kubwa lakini Mill akahangaika mpaka
akapata hiyo pesa.
Alimkuta
sebuleni. Akamuuliza. “Upo tayari kwa kesho?” Akajibu, “Inategemea.” Sasa kwa
kuwa Mill alikuwa amechoka, amefanya kazi mfululizo kukusanya pesa, bado
shule! Hakutaka kuzunguza naye. Kisha ni muongeaji sana. Akapitiliza
chumbani kwake ili akaoge ndipo apate usingizi mfupi ajipumzishe ili asome.
Wakati ametoka
na taulo bafuni kwake. Maana ilikuwa ni apartment ya vyumba viwili, yeye
alichukua master bedroom, akamkuta Kisha yupo kitandani kwake na lingerie
nzuri sana. Mill akashituka sana. “Unafanya nini Kisha!?” “Wewe umeomba nikusaidie
ndoa ili utengeneze status yako, na mimi nakuomba penzi.
Nimekua nikukutamani kwa muda mrefu. Ila ulikataa kwa sababu ulisema una
mtu wako. Sasa sasahivi mimi nina hamu sana na penzi, naomba nisaidie.”
Mill akabaki ameduaa.
“Huwezi kuwa mbinafsi
Mill. Yaani wewe uwe wa kusaidiwa tu, huwezi saidia wenzio! Hiyo
itakuwa roho ya namna gani?!” “Nilikwambia kabisa nina mke!” “Kwani nimekwambia
naichukua moja kwa moja! Wewe vipi Mill!? Ni sex tu! Kama unaona
shida kunisaidia, basi. Na mimi SITAKI kukusaidia.” Akambadilikia.
“Wewe si mbinafsi? Hutaki
kunisaidia na mimi, BASI.” Akatoka hapo kitandani. “Na tafadhali usinitafute
tena. Yaani leo iwe mwisho.” Nusura Mill achanganyikiwe. Alishawekeza
pesa kwa huyo mwanamke, zaidi ya alivyopanga kumpa mwanzoni. Alishamlipa ile
pesa waliyokubaliana ya mwanzoni, lakini ikazidi. Walishapita hata nusu ya malipo yote. Kisha alimdai
akimwambia anashida nayo ya dharula. Anamgaramia hapo kama mkewe kabisa.
Halafu Mike na
Kamila walishatua nchini, wapo hotelini na ndio wametoka kuagana kuja
kukutana kesho yake mahakamani kwenye kufunga hiyo ndoa. Mbali na hayo
yote, ashalipia kila kitu mpaka mpiga picha, leo anamgeuka! Mill
hakuamini.
Akamtisha kabisa
kwamba anakusanya vitu vyake, anaondoka. Mill akambembeleza wee, lakini
Kisha akawa ameshika kwenye makali. Yeye ANATAKA penzi. Ndio akatoka kabisa
hapo ndani ya chumba, akimwambia anakwenda kufungasha aondoke.
Alimuacha Mill
amesimama na taulo lake, hapo chumbani kwake haamini kinachomtokea. Akahesabu faida
na hasara, akajikuta mizani inalemea upande mmoja. “Si ni sex tu!” Hapo
ndipo alipofikishwa na mawazo yake akiwa kwenye hali ya kupaniki.
Akamkimbilia
chumbani kwake, akasalimu amri. Usiku huo kabla ya ndoa yao wakafanya
mapenzi ya kutosha. Maana Kisha hakutaka mambo ya nusunusu. Akamfaidi
Mill wa Pam kwa kadiri atakavyo. Na hivi alishamvutia! Akajinoma
vilivyo.
~~~~~~~~~~~~~~
Kesho yake Kisha
aliamka na furaha huyo! Mambo akayapeleka kwa ufasaha na ushirikiano
wa hali ya juu sana, mpaka akamshangaza Mill. Kwa hakika
walitengeneza show ya aina yake. Kwa kuangalia tu picha na video, aina
ya harusi waliyo fanya, ungejua hao watu wanapendana na wamekusudiwa
kuwa pamoja. Yalikuwa maigizo ya hali ya juu. Ni wao wenyewe na kina
Mike tu ndio walijua ni maigizo. Ila kwa wageni wengine waalikwa na
ndugu wa karibu wa Kisha, walijua hao wawili wamependana kwa hakika.
Kulikuwa na kissing za nguvu na mengine mengi ilimradi tu, kufanikisha
shuguli nzima.
Tamu Yageuka
Shubiri.
Baada ya mwezi
maisha yakiwa yanaendelea akipambana, weekend hiyo akawa ameamua
kurudi nyumbani baada ya kuchapa kazi mfululizo bila ya kupumzika. Akawa
amemuahidi Pam atafika nyumbani, akioga tu, basi atampigia. Ile ameingia
tu nyumbani, akakuta ni kama anasubiriwa na Kisha, akiwa na mama yake.
Kidogo ikamtisha. “Kuna habari njema. Njoo ukae.” Mill akasita. “Ni kitu
kizuri, usitie shaka.” Kisha akazungumza na tabasamu kubwa mbele ya mama yake.
Sasa akijua
wazazi hawajui ukweli, ikabidi atii, aendeleze maigizo ya
mume. Akasogea walipokuwa wamekaa, ndipo akakabidhiwa kitu kama KIJITI, kilichobadili MAISHA ya Mill KABISA. Akidhania anatafuta njia fupi ya maisha, akajikuta
amejitia kitanzini yeye mwenyewe.
Kijiti kilibeba
majibu ya ujauzito. Alipoona tu alama ya msalaba kwenye kijiti
kile, na amekabidhiwa YEYE, karibia aanguke kwa mshituko.
Bila kutarajia,
yeye mtu anayesomea unesi, akajikuta akimuuliza mbele ya mama yake. “Inamaana
gani!?” Kisha akiwa amejawa tabasamu kubwa usoni, akamjibu “Tumejaliwa mtoto.”
“Lakini haya sio mapatano yetu!” Akatamani aseme hivyo, lakini akashindwa
maana mama yake Kisha alikuwa akimwangalia kwa makini sana. Alichofanya
ni kumrudishia na kuingia chumbani.
Alikuwa na hali
mbaya mpaka akakaukwa mdomo gafla. “Pam tena ndio basi!” Akajisemea
akiwa amesimama katikati ya chumba hajui akae au atoke.
~~~~~~~~~~~~~~
Kisha
akaingia. “Hata mimi sikupanga, mimba ilishika kwa bahati mbaya.” “Kwa
nini hukutumia kinga?” Akauliza swali la wanaume wa kiswahili, uzunguni
na kumfanya Kisha kumshangaa sana. “Hee! Kwani nini na wewe hukutumia
kinga!? Umechanganyikiwa nini?” Japokuwa alimjia juu, lakini akajua
alikuwa sahihi. ALIJUTA Mill, akawa hana wakumlaumu. Maji ndio
yashamwaGika, hayazoleki. Ngono alishafanya, majibu ya ile starehe ndio
amepewa! Nitamwambia nini Pam!” Ndio likawa swali lililokosa jibu.
~~~~~~~~~~~~~~
Inaendelea…
0 Comments:
Post a Comment