![]() |
Akili na mawazo
yako kwa Pam. Akajikuta akimshukuru Mungu angalau amepata naye muda japo
kwa muda mfupi, lakini angalau wameanzia sehemu. Alitamani kumuomba namba, ila
akaonelea amuache tu mpaka mwenyewe aje amuombe. Alikusudia ajitofautishe
na wanaume wote kwake. Asijiuze kwa mali na asikimbilie kuomba namba tena mara
baada tu ya kumsaidia! Akaona juhudi zake zisiwe bure kwa kukimbilia kuomba
namba, itakuwa kama kujilipa.
~~~~~~~~~~~~~
Na Pam naye huku
akabaki amejishika shingoni alipopokea busu la Mill. Mawazo yakirudia
kila neno alilozungumza Mill. Akavuta pumzi akimfikiria Mill. Ukweli
alishavutiwa naye. Macho yake! Jinsi alivyokuwa akijisikia akimwangalia! Halafu
Mill ana mwili mzuri wa kiume wa kuvutia. Kwa asili ni mtu mkubwa kwa maumbile.
Mrefu halafu mpana. Akaonekana ni mtu wa mazoezi. “Sasa na yeye kwa nini
hata asiombe namba!” Akajilalamisha mawazoni mpaka analala usiku mawazo kwa
Mill.
Alikuwa na
wakati mgumu akitamani kujua kama alipata ndege! Kama alifanikiwa kuondoka! “Aliondokaje
amelowa vile!” Hayo yakawa maswali yaliyomsumbua Pam usiku kuchwa, lakini
hakuwa na wakumuuliza.
~~~~~~~~~~~~~~
Jerry ndiye
rafiki mkuu wa Mill lakini pia ni mume wa Sandra, mmiliki wa hiyo ofisi, na
yeye Jerry anasimamia sheria za pale. Ishajulikana Mill ni wa Lona. Leo anavunjaje
mwiko kwa kumuulizia Mill wa Lona!
Alifika ofisini
siku inayofuata akaendelea na kazi kama kawaida, lakini rohoni hana amani
kabisa, mpaka akajishangaa.
Alishinda hiyo
siku mawazo yapo kwa Mill mpaka anatoka jioni, kimya. Ila Lona kwa kujibaraguza
akawa anamsema vibaya Mill. Kwamba ni mwanaume suruali tu, hana kitu.
Kajaa shombo. Ikawa akimsema makusudi mbele ya Pam mwenyewe ilimradi tu
kumuonyesha Mill aliyemkataa mbele ya watu wote, akisema anamtaka Pam, si
kitu. Pam alinyamaza tu kimya akamuacha aendelee kubwatuka siku nzima mpaka
jioni wanatoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Kesho yake mida
ya jioni karibu wanatoka, Jerry akampigia simu ya mezani akimuita ofisini
kwake. Akaenda. Akamkabidhi kabrasha. “Ndani kuna ujumbe wako. Sasa akili
kichwani.” Akapokea akiwa hajaelewa vizuri. Ilikuwa kama barua ndani ya
bahasha. Akafungua palepale mbele yake, akakimbilia kusoma jina chini ya
ujumbe, akakuta imeandikwa ‘MM’ moyo ukajawa furaha, akajua ni Mill tu. Ilikuwa
ni email/barua pepe imeandikwa kwa Jerry kutoka kwa millm@hotmail.com.
“Asante Jerry.”
Jinsi alivyoshukuru akijua ameshajua mtumaji, Jerry akajua Mill ashajishindia
Pam. Ila akashangaa sana. Asijue mwenzie alibaki mvuani kuweka msingi.
Na huyo Pam hajawahi tongozwa na mwanaume anayejitangaza hana pesa hata
mara moja. Mill ndio mwanamme wa kwanza.
Kwake akawa
amekuwa watofauti, akamuona yeye mkweli kuliko wanao mtongoza na kujigamba
wanayo pesa nyingi wakijinadi ni nini watampa.
“Lakini si
unaelewa ni lazima kwa hapa uwe makini?” “Najua bosi wangu.” Akamshangaza
vile anavyokubali. “Kwamba hata huo ujumbe mimi sijakupa!” “Najua. Na
nakuahidi sitakutaja popote. Na sitamwambia mtu. Nilikuwa na
wasiwasi kutaka kujua kama alifika salama, lakini nikashindwa kukuuliza.
Nashukuru na nakuahidi nitakuwa makini.” Jerry hakuamini. Pam!
Kwamba kirahisi
hivyo yupo tayari na Mill aliyemwambia hana kitu na ofisi nzima ilisikia kejeli
za Lona siku nzima iliyopita na siku hiyo akimtusi Mill kwa waziwazi! “Kweli
kila shetani na mbuyu wake!” Akajiwazia Jerry wakati Pam akitoka hapo
ofisini akiwa na hilo kabrasha lenye ujumbe kutoka kwa Mill.
Akaenda nalo
chooni. Akaanza kusoma.
‘Pam, namshukuru Mungu tumefika salama.
Na namshukuru Mungu na wewe ulifika salama. Nilipofika Doha, nilihakikisha yule
mzee alikufikisha salama kwa kuzungumza naye. Nilimuomba namba yake ya simu
kabla sijamkodi akurudishe nyumbani. Na yeye akawa muungwana, alipokea simu
yangu na kunihakikishia alikushusha nje ya geti la nyumbani kwenu. Hiyo
imenituliza na kunipa amani kwamba upo salama. Nakutakia kila la kheri.
Ufanikiwe katika kila jambo.’ Ikaishia hapo asiamini kama
aliweza muomba namba mwenye taksii, ila si yeye!
Akabaki akiwaza
hapo chooni. Mwishoe akatoka akiwa ameweka ile barua kwenye sidiria kabisa,
isije anguka.
“Mbona hata asiniombe namba yangu!” Gafla mchoyo wa namba huyo, akajilalamisha. Pam asiyethubutu kutoa
namba yake kwa mtu, mkali, asiyetaka na namba yake ya simu, gafla anaumia
kutoombwa namba ya simu! “Wanaume hawa! Huwezi jua. Ukute huko ana mtu wake, hataki
mawasiliano ya huku.” Huo ukawa ukweli alioupokea, na kuamini. Ila
akajikuta kawivu kanaanza tena.
~~~~~~~~~~~~~~
Juma hilo
likaisha, kukawa kimya hajasikia kutoka kwa Mill ila angalau Lona akapata
mwanaume mwingine aliyekuwa akisifiwa hapo! Pam akajua anamfanyia makusudi kama
kushindana. Ukweli Pam alikuwa mzuri wakuvutia. Kwa hiyo wateja wao
wengi walimkimbilia yeye, ndio wakazidisha mtindo wakuwahi. Na
hata huko wanapokuwa na hao wanaume, bado walibakia kumuulizia Pam wakiwataka
haohao kina Lona wawasaidie kwa Pam. Wakawa wakiishia kumponda Pam,
wakimchafua kwa hao wanaume kwa hili na lile ilimradi tu wabakie nao hao
wanaume.
Pam alikuwa
akijua, lakini hakuwa akijali. Ni Mill peke yake ndiye aliyeonyesha
msimamo wa waziwazi kuwa yeye hatachua mrembo yeyote pale ila
Pam.
Majigambo ya
Lona yakaendelea ya muda tu pale ofisini kuwa amepata mwanaume mwenye pesa. Pam
kimya.
~~~~~~~~~~~~~~
Siku ya jumamosi
ambayo ni nusu siku Pam alikuwa akienda yeye benki kuweka hundi walizolipwa
kama kampuni kisha kuondoka moja kwa moja nyumbani. Akaenda ofisini kwa Jerry
akamkuta anamuandalia. “Nimewahi sana nini?” “Nimemfanyia kusudi Lona. Alitaka
yeye ndio aende ili asirudi tena ofisini. Nikamwambia leo ni zamu yako na hata
hivyo sija andaa. Ndio akaondoka.” Pam akakaa.
“Katika hizi
hundi, katikati kuna ujumbe wako.” Akamuona anafikiria. “Vipi? Hutaki,
nirudishe majibu?” “Hapana, nafikiria jinsi ya kuwasiliana naye!” Jerry
akacheka sana. “Pammmm!” “Sio kwa nia mbaya!” Jerry akazidi kucheka.
“Pam huyu ndio wakuomba
mawasiliano ya mtu, kweli?!” “Amekua mtu mzuri!” Jerry hana mbavu. “Mill huyo?”
“Acha bwana Jerry! Mkeo ataingia sasahivi.” “Nitakavyokubadilikia! Kama
sikujui.” Akacheka akisimama. Walimjua Sandra. Mkali kama pilipili. Aliwaweza
wote hapo.
“Kwa hiyo upo
sawa nikimpa namba yako?” Akamchokoza. Pam akacheka akitingisha kichwa
kukubali. “Sawa mama. Mjumbe mimi sina neno! Ila chonde mama! Ukikamatwa,
hakika sikujui.” “Nipo makini. Usihofu.” Akatoka akiwa na shauku akitaka kujua
safari hii Mill amemwambia nini!
Alipopanda tu
kwenye gari ya kazini, dereva alivyoondoa gari akafungua bahasha. Kukawa na
ujumbe mfupi sana. ‘Pam, upo mawazoni mwangu.’ Ukaishia hapo.
Akatamani angeandika zaidi. Akabaki akiwaza nakutamani Jerry ampe namba yake
kwa haraka, asihau.
~~~~~~~~~~~~~~
Macho kwenye
simu hata alipokuwa saluni. Muda wote akitizamia ujumbe kutoka kwa Mill. Akawa mtumwa wa hiyo simu mpaka
akajichukia! Watu husubiri namba yake ya simu wakiisaka kwa udi na uvumba!
Leo yeye ndio amegeuka wa kusubiria simu ya mwanaume! Akazidi kujishangaa
kilichompata! Masaa yakazidi kuwa marefu zaidi ya Mungu alivyoyaumba. Usiku
ukazidi kuwa mzito kwa kutosikia kutoka kwa Mill. Akaanza kujidharau
kumpa namba bila kuombwa.
Kila Mtu
Hupenda Kupendwa.
Wakiwa wanapitiwa na usingizi ujumbe ukaingia na
kumfanya Mina kuchukua simu yake na kusoma. ‘Upo Mina
wangu?’ Akafurahi mpaka akajikuta akicheka. Alishajutia kitendo
chakumwambia achukue muda afikirie kabla hawajaendelea kwenye mapenzi. Akajua
baada ya pale alifikiria na kujiona mjinga kumkataa Lora kumtaka yeye mchafu. Sasa jinsi alivyoandika huo ujumbe! Mina akafarijika
sana na kujibu kwa haraka.
‘Ndio nilikuwa napitiwa na usingizi. Umekuwa na jumapili
nzuri?’ Mina akauliza. ‘Ilitaka kuisha vibaya,
lakini nipo sawa. Nilienda kukimbia baharini, ndio narudi. Angalau akili
imetulia.’ ‘Itabidi siku nyingine ukimbie na mimi akili itulie.’ ‘Ninaweza
kukupigia?’ Mina akamwangalia mama yake. Akamkuta mama yake akimtizama,
wakacheka kwa pamoja. “Anataka kunipigia.” “Nenda kazungumze naye.”
“Nitamuamsha Ron!” “Kakae sebuleni upunguze sauti.” Mina akatoka huku akicheka.
‘Sasa hivi unaweza kunipigia.’ Akamtumia huo ujumbe, Andy akapiga. “Kwa nini akili ilikuwa haijatulia?” Mina akaanza. “Mambo ya familia tu. Lakini nimefurahi kusikia sauti yako.”
“Kweli!?” “Kweli, si ndio maana nimetaka tuzungumze!” Mina akacheka. “Kuna kitu nilikutana nacho jana. Nikafikiri kitakufaa.”
“Nini?” “Najua upo unasoma. Lakini hivi unajua kitu hicho hicho unachosomea
pale, unaweza kukisomea kwenye chuo kama IFM na ukapata cheti kizuri zaidi?
Ukapata certificate in Computing and Information technology.” “Najua Andy.” Mina akaongea taratibu.
“Sasa kwa nini usihamie hapo? Sidhani kama
utaanzia mwanzo kabisa. Wanahamishia masomo yako na mitihani uliokwisha fanya.”
“Najua Andy, lakini ada yake ni kubwa. Nishauliza. Na nilishachukua mpaka fomu
zao.” “Basi tukutane kesho mchana tuzipitie pamoja.” Hilo likamfurahisha Mina. Wakazungumza kidogo,
wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~~
Kesho yake alipomaliza tu darasa la mwisho, wakati
anatoka, akamkuta Andy anamsubiria nje. Akacheka. “Nimefurahi kukuona.” Andy
akacheka. “Na mimi nimefurahi kukuona. Umependeza.” Mina akakunja uso huku
akijiangalia. “Sema asante bwana!” “Haya, asante.” “Sasa twende tukale, halafu
tukakutane na mtu pale IFM, atatusaidia.” Wakatoka hapo.
Akapelekwa kula sehemu nzuri, ya hadhi ya kina Andy.
Tatizo akawa hajui kutumia kisu na uma. Hilo nalo ikawa tofauti
nyingine. Familia hiyo ya Ruhinda hawali kwa mkono. Anampelekaje kwao!
Akamuona amekosa raha. “Tumia tu uma.” Mina
akamwangalia. Andy hakuwa akishika chakula hata paja la kuku kwa mkono. Ni uma
na kisu kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Hata wali alikula na uma. “Siwezi Andy!
Nashindwa.” “Unataka kulaje?” Andy akamuuliza kwa upole. “Huwa nakula kwa
mkono.” Andy akabaki kama anayefikiria. “Hata hivyo mimi nimeshiba.” Mina
akasogeza sahani pembeni. “Hujala hata kidogo!” “Nitaenda kula kwa mama Ron.”
Andy akacheka.
“Nenda ukanawe mikono ‘bathroom’ ndipo uje ule.” “Kwani hapa hawanawishi watu
mikono!?” “Hapana Mina.” Mina akaanza kuishiwa nguvu. “Nenda.” Mina akaenda
maliwatoni kunawa mikono na kurudi kula. Mara nyingi alitumia mikono, Andy
akimwangalia. Lakini akala mpaka akamaliza chakula chote kwa kutumia tu mikono
yake.
IFM
Walifika IFM wakakutana na Dean of students, ambaye alikuwa rafiki wa Andy. Akamuhoji Mina
maswali mawili matatu, kiurafiki tu. Alipoelewa mengi kutoka kwa Mina, ndipo
akamshauri Andy, asubirie aanze na wengine muhula unaofuata kwa kuwa ni kama
aliyoyasoma Mina, ni ya chini sana. Hayaendani na ya pale. Wakaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~
“Kwa hiyo ni kama pale napoteza muda tu?” “Hapana Mina!
Naomba usivunjike moyo. Maliza pale kwa bidiii zote, halafu baada ya miezi
mitatu tu, unakuja hapa. Tena kwa kuwa utakuwa na certificate ya pale, huku utakuja kufanya diploma.” “Ndio miaka
mingapi!?” Akauliza kwa hofu kidogo. “Kwani wewe ulitaka kusoma mpaka lini ndio
iwe mwisho?” “Sijui Andy! Wewe unanishaurije?” Hilo likamfurahisha Andy. “Wewe
bado mdogo Mina. Huna sababu yakutojiendeleza. Kama ukipata nafasi, itumie.”
Mina akanyamaza.
“Au unaonaje?” “Nitajitahidi Andy. Japo naona kama
hayo mambo unayotaka nikasomee sio kama hichi ninachofanya. Naona yatazidi kuwa
magumu!” “Naomba usiogope. Usiweke hofu kwanza ila jipe muda. Hakuna
haraka. Fikiria, halafu amua. Ila nakuahidi kama ukichagua chochote kile, mimi
nitakusaidia. Hata kutafuta mwalimu wa ziada. Ni sawa?” “Sawa.” Wakakubaliana.
Mchana huo badala ya Andy kuwepo kazini, alikuwa akihangaika na Mina.
Alimrudisha mpaka karibu na kwao ndipo akarudi kazini.
Andy kwa Ron.
Aliporudi, akamuita Ron ofisini kwake. “Niambie
kiongozi.” “Naomba leo baada ya kazi tupate muda wa mazungumzo.” Ron akashangaa
kidogo. “Kwema!?” “Kwema kabisa. Ni mambo nje ya kazi.” “Oooh! Hamna shida.
Nilifikiri ndio kazi imeisha!” Wakacheka kidogo na kukubaliana baada ya kazi,
watoke pamoja.
Mara nyingi Ron ndio anakuwa wa mwisho akimalizia
kufunga kazi za wote ndipo anamtumia Andy, nakuondoka. Andy alibaki ofisini
kwake akimsubiria. Alipoona tu ripoti imeingia, akajua amemaliza. Akasikia simu
yake ya mezani inaita. “Mimi nipo tayari. Ukimaliza
utanikuta hapo nje.” Alikuwa Ron. “Okay.”
Akajibu na kukata.
Baada ya muda akatoka na kumkuta Ron anazungumza na
dada yake. Akamuona anacheka, “Acha uchokozi Mina!”
Akamsikia akisema hivyo na kukata.
“Ungependa kula wapi?” “Kiongozi leo unataka ukanipe dinner?” Andy akacheka. “Mazungumzo yasindikizwe na
chakula.” Wakaongozana mpaka Surrender Pub.
Wakaagiza nyama choma. Wakajikuta wote hawanywi pombe. Wakaagiza na maji ya
kunywa wakaanza mazungumzo ya kawaida tu. Ila Ron akawa na hamu yakujua
anachotaka kuambiwa na kiongozi wake. Alimuona amejawa na wasiwasi! Akashindwa
kumuelewa ni nini hicho kizito anachotaka kusema. “Kwema lakini?” Ikabidi Ron
ammrudishe kwenye lengo la kukutana hapo. Maana wao si marafiki, nini
chakuwaweka pamoja!
“Nilisomea Nairobi tokea shule ya msingi mpaka
sekondari. Ila chuo kikuu ndio nilisomea chuo kikuu cha Kampala, Uganda.” Ron
akatulia akitaka kujua mwisho wa yale mazungumzo ni nini! Akabaki
akimwangalia na kumuongezea wasiwasi Andy. “Kuna kipindi mpaka mimi mwenyewe
nilifikiria kuwa padri.” Ron akacheka kidogo. “Kabisa. Maana shule niliyosoma
ilikuwa ni ya mapadri na wakawa watu wa karibu yangu sana.” “Ungefaa Kiongozi.”
Andy akacheka. “Nafikiri haukuwa wito wangu.” Wakacheka tena. “Nilipofika
chuoni, nikapata msichana.” “Uliacha wito, Kiongozi?” Wakataniana kidogo,
akaendelea.
“Lakini nafikiri haukuwa mpango wa Mungu. Tuliachana. Anyways, akaja Lora.” “Kiongozi leo unatafuta kitubio nini?” Wakacheka sana kisha
akaendelea. “Sasa Lora ni binti ambaye tumekuwa tukifahamiana. Ni mdogo kwangu
karibu kidogo kulingana na mdogo wangu wa kiume ambaye ni daktari pale
Muhimbili. Sasa tukirudi kwa Lora, ni kama wazazi wetu wote walitamani tuoane.”
“Lakini Kiongozi sio wazo baya!” Ron akaongea kwa utani.
“Wazo sio baya, lakini nafikiri hatukukusudiwa.”
Ron akatulia kidogo. “Mbali na kile kilichokuwa kikionekana kwa nje, hatukufika
mbali. Tulikuwa tumechukua muda wa kusomana tu, lakini week iliyopita, tukakaa chini na kutafakari, wote
tukakubaliana kuacha tu.” “Kwamba mmevunja mahusiano!?” “Yeah! Kwanza hatukuwa
tumefika mbali kwa ukweli. Ila pia kulikuwa na sababu nyingine iliyonifanya
nisivute zaidi.” Ron akawa ametulia anamsikiliza.
Chakula kikaletwa. Kama kawaida yake, akaomba kisu na
uma, Ron akanawa mikono, nakuanza kula na mkono kabisa kama dada yake. Aliokota
ndizi na nyama kwa mkono. Akala kachumbari pia kwa mkono, bila hata wazo la
pili, Andy akimtizama.
“Ehe!” Ron akataka aendelee huku akila kwa furaha zote
bila kuona kuna alichopungukiwa, mambo ya kutumia kisu na uma.
“Japokuwa
mahusiano yangu na Lora hayakuwa ya muda mrefu, lakini niliyasitisha mapema kwa
kuwa nilijihakikishia kabisa, kuwa hawezi kuwa mke wangu.” “Naona Kiongozi
unataka kuoa si kuchezea.” Ron akatania.
“Nashukuru kama hilo umelielewa. Lengo nataka mke. Si
msichana tu wakuonekana naye mbele za watu na kuburudishana tu. Hapana. Sijui
kama unanielewa?” “Naona kama nakupata!” Ron akaafiki nakuendelea kula. “Basi
ndio maana ilibidi kukatisha mahusiano yangu na Lora, sababu ya kile ninachojisikia
kwa Mina.” Ron akashituka mpaka akapaliwa na maji aliyokuwa anakunywa.
Akaanza kukohoa. Alikohoa kama dakika hivi mpaka macho yakawa mekundu.
“Pole sana.” “Subiri kwanza Andy!” Hapo jina la Kiongozi likaisha. Ron akanywa tena
maji. “Umesema Mina, Mina dada yangu mimi!? Au sijakusikia vizuri?”
“Namzungumzia Mina, ndiyo.” Ron akabaki akimtizama. “Najua utakuwa huamini
lakini nampenda sana Mina. Kile ninachojisikia kwa Mina, sijasikia kwa
mwanamke mwingine yeyote na...” “Subiri kwanza Andy. Wewe unaongea kitu ambacho
hukijui. Humjui Mina hata kidogo!” “Kwa sasa namfahamu kwa asilimia 90. Nilimpenda
nikiwa namfahamu kwa asilimia kama 7 hivi, lakini sasa hivi nina mfahamu kwa
asilimia 90.” Ron akakunja uso.
“Andy! Wewe ni mtu unayejiheshimu sana. Na mimi
nakuheshimu, tafadhali naomba kabla hujafika mbali katika hili na tukashindwa
kufanya kazi mimi na wewe, naomba hicho unachokifikiria kinakuvutia kwa
Mina, acha kabisa. Tafadhali sana.” “Labda kuwe kuna cha tofauti na kile
alichoniambia Mina mwenyewe.” Ron akatulia kidogo akimtizama ila mwishoe akaona
aulize tu.
“Inamaana
umeshazungumza na Mina mwenyewe!?” “Ndiyo.” Ron akamkazia macho. “Wewe ndiye
uliyetoka naye siku ya jumamosi!?” “Kwa kuwa nilitaka kumuhakikishia
nataka kutulia na yeye tu. Na kwa kuwa alishaniona na Lora, nilitaka ahakikishe
yupo na mtu ambaye yupo salama. Na nilitaka kumuhakikishia mimi sina mpango wakumchezea.
Kwa hiyo nilitaka awe na mimi hospitalini wakati naangalia afya yangu kwanza.
Ahakikishe naanza na yeye nikiwa mzima kabisa, ndipo nikamchukua mpaka nyumbani
kwangu. Tukapata muda wa mazungumzo. Mrefu tu.” Ron alibaki ameduaa.
“Na kwa kuwa saikolojia ni moja ya somo nililosoma na
kulifanyia kazi kidogo wakati nikiishi na mapadri kule Nairobi, nina uhakika hajanidanganya.
Ameniambia ukweli.” Ron akajivuta vizuri. “Labda niulize, upande upi wa Mina
unaoujua wewe?” “Wote, na ndio maana nimekwambia namfahamu kwa asilimia 90.”
Ron akawa kama hajamuelewa.
“Subiri kwanza Andy, kwa hiyo wewe unajua kuwa Mina
aliishi na...” “Omar, aliyemtoa kwa wafanyakazi wake? Wakaishi Iringa, akampiga
mpaka akamtoa mimba?” Akamalizia na swali lililomfanya Ron abaki ametoa macho.
“Nafahamu Ron. Ameniambia.” Ron akaishiwa
maneno. Akarudi nyuma na kujiegemeza kwenye kiti. “Tumekubaliana tupeane muda
wa kuchunguzana. Na yeye aangalie kama mimi nitamfaa kuwa mume wake.” Ron
akabaki akimtizama.
“Kwa hiyo ndipo
tulipofikia hapo, nilitaka na wewe ujue. Na ninafanya hivyo makusudi kwa
heshima ya Mina mwenyewe, na yenu. Sitaki kujificha naye. Nataka
hata wewe ujue, ili niwe huru na Mina.” Ron akashindwa ajibu nini! Andy
akaelewa yupo kwenye mshituko, lakini akaendelea tu akitaka ujumbe wake ufike
siku hiyo.
“Kwa sasa nimemuomba anisubiri. Anipe muda
wakumfahamu vizuri yeye kama Mina. Na mimi anifahamu. Akiona sitamfaa,
aniambie, na mimi nitamwambia, ndipo atafute mtu mwingine. Ameniahidi kuwa
hatakubali mtu mwingine mpaka ahitimishe na mimi.” Andy akajieleza vizuri tu.
“Hivi unajua kama Mina aliishia kidato cha nne, yaani
kwa mara ya kwanza ndio amekubali kusoma? Ndio anarudi shule sasa hivi!
Unalijua hilo?” Ron akauliza. “Najua, ameniambia. Na ninajua hapendi
hesabu.” “Sio hesabu tu. Mina hapendi SHULE. Ndio maana alivyokubali tu
kusoma, nilihakikisha hasubiri na hakuna kinachomzuia asisome.” Ron akaweka
msisitizo.
“Nafahamu Ron. Na ninakuahidi sitamfanya asisome. Leo
nimetoka naye IFM. Niliona kwa haraka masomo ya certificate pale. Nikazungumza naye kutaka kujua kama angependa
kusoma pale kwenye chuo ambacho angalau kinaeleweka. Akakubali lakini akasema
tatizo ni pesa. Sasa kwa kuwa yule Dean wa pale nafahamiana naye, nikaenda naye
leo. Akamuhoji maswali, akatushauri tusubiri aje aanze mwanzo kabisa. Kwa hiyo
nimezungumza na Mina. Nimemtia moyo amalize hiki anachokisoma sasa hivi, halafu
aende pale akasomee mambo ya IT.” Ron akatoa macho. “Mina asome IT!?”
“Amekubali. Na nimemuahidi nitamsaidia kama akikutana na ugumu wowote ule.”
“Amesemaje?!” Ron akauliza kama ambaye haamini. “Anaonekana ameridhia.”
“Mina!?” “Ndiyo.” Ron akakunja uso.
“Anajua kama anatakiwa akae darasani si pungufu ya
mwaka lakini au hilo hujamwambia!?” “Ron, Mina amebadilika. Tafadhali
naomba na nyinyi mumpe nafasi.” “Huelewi Andy! Huelewi na ninahofia unataka
kujiingiza kwenye kitu ambacho kitakuja kutukosanisha sana sisi na
kutufanya tushindwe kufanya kazi.” Ron akajisogeza vizuri kwa Andy.
“Mama yetu hana mwanaume, isipokuwa mimi. Kazi
niliyonayo, imempunguzia mama majukumu mengi sana. Naomba Mungu mchana na
usiku, mama naye akinisaidia kuomba ili kusiharibike jambo pale kazini,
ndio maana unaniona nahangaika na kujituma sana, Andy.” “Nafahamu Ron.” “Basi
naomba punguza kasi kaka. Mina bado mdogo mno. Akili zake zipo kama vile
ulivyomuona siku ya kwanza ulipokuja nyumbani. Ni mtoto. Ila wanaume
wakimtizama kwa nje kwa haraka, wanachanganyikiwa. Mina ni mtoto ambaye
bado anahitaji kuongozwa.” Ron akawa kama anamsihi.
“Nimekaa na Lora, nimekaa na Mina. Nimekuwa na
mahusiano ya kimapenzi pia. Ya muda tu. Najua ni nini naongelea Ron, na ninajua
ni nini nakifanya.” Ron akajua Andy ameshaamua. “Tafadhali mpeni Mina
nafasi na mumuonyeshe mnamwamini.” “Kwani hayo unayotuambia ni mageni
kaka? Mina ashaaminiwa pale nyumbani zaidi ya nitakavyokwambia! Hizo nafasi
unazosema apewe, amepewa mpaka mama amemaliza.” Ron akajiweka sawa ili kujaribu
kumshawishi Andy, pengine atamuelewa aachane na Mina, mdogo wake.
“Alianza kwa ukali kwa Mina. Mpaka kumchapa. Nikisema
kuchapwa, Mina amechapwa yule mtoto, hakuna jinsi. Lakini kama unavyomjua Mina,
akili zake za kitoto, akawa akichapwa, analia halafu anataka mama huyo huyo eti
ndio ambembeleze.” Andy akacheka. “Sikutanii. Ikabidi mama abadili adhabu.
Akidhani atajifunza. Labda kumnyima hiki au kile anachokipenda. Lakini Mina
hajui kununa. Mama napo hapo akashindwa. Akaona ni kama haelewi. Akajirudi kuwa
rafiki. Tunahangaika na Mina, naona tokea yupo darasa la saba.” “Ameniambia.”
Ron akashindwa kumuelewa.
“Kama ni lile umbile
lake, Andy, Kiongozi wangu, mbona Lora ni mzuri tu kaka?” “Sio umbile Ron, nampenda Mina.” “Daah! Kwa maana
nyingine ni kwamba umeamua?”
“Nakutaarifu ili ujue simuibi dada
yako. Nia yangu ipo dhahiri, labda abadilike baada ya hapa lakini si kwa
alivyoishi zamani.” Ron akabaki kimya akimtizama.
“Na atasoma. Naomba tumchukulie hatua kwa hatu kama
ulivyofanya naye. Na mimi nitamchukulia kwa utaratibu kabisa. Sitamuwekea pressure
yeyote ile ila kumtia moyo. Na hata akimaliza hii na kukataa kuendelea, pia
nitamuacha na kuheshimu maamuzi yake.” Ron kimya.
“Ron?” “Daah! Mimi sina chakusema tena Andy. Naona
umefikia maamuzi. Na ninavyokujua kwa kukuona pale kazini, wewe si mtu wa kubadilika. Ila naomba unihakikishie Andy, na hili
nitakukumbusha.” “Nini?” “Yatakapokushinda
kwa Mina, tafadhali usilete kwenye kazi
yangu. Usije ukanichukia mimi kwa kuumizwa
na Mina.” “Haitakaa ikatokea.” “Basi ni hilo tu kaka. Maana mahusiano yako na
Mina yanaweza yakaharibika, ila mimi hata iweje, Mina ni mdogo wangu. Katika
lolote, nitakuwa upande wake.” “Hilo nalielewa. Na ninakuahidi sitaingiza mambo
yangu na Mina, pale kazini.” “Basi ni hilo tu.” Ron akaonekana ni kama
ameridhia. Akaendelea kula.
“Naomba nikaribie nyumbani. Angalau mama anifahamu,
ili nisiwe naishia njiani na Mina. Sidhani kama ni jambo la heshima.” Ron
akanyanyua macho akabaki akimtizama. “Sijasema nakuja kutoa mahari Ron! Nataka
mama anifahamu, ili Mina anapotoka, mjue yupo kwangu. Na utakapomuona Mina pale
ofisini, awe huru hata kuja ofisini kwangu na kunisalimia.” “Unataka na kazini
wamtambue kama mtu wako!?” Ron akashituka sana.
“Mambo yakienda vizuri nitamuoa Mina. Sina chakuficha kwa yeyote. Kwa nini iwe tatizo watu
kumtambua kama nipo naye kwenye mahusiano?” “Hivi Andy umefikiria vizuri lakini?” “Mimi si mkurupukaji Ron. Nafikiri kwa
sehemu utakuwa umelifahamu hilo.” Ron akabaki akimtizama.
“Nataka Mina akisema ‘Ndiyo’ kwangu, awe anajua
anaolewa na mtu wa namna gani. Anifahamu katika kila eneo la maisha yangu.” Ron
akainamia sahani yake akaendelea kula. “Kwa hiyo siku gani ni nzuri kuja
kumuona mama?” Andy akaendelea. Ron akamtizama. “Daah! Umekazana Andy!” Andy akacheka.
“Ikishafika saa 12 kamili jioni, mama anakuwa
ameshamaliza shuguli zake zote, yupo nyumbani. Siku za jumamosi mara nyingi
anakuwepo nyumbani. Ana biashara ya chapati. Kwa hiyo anazipika. Jioni ndio
mimi nakwenda kumsambazia. Yeye anakuwepo tu nyumbani anapumzika. Na jumapili
inategemea. Tukitoka kanisani, huwa mara nyingi tunasimama sehemu kula, ndipo
tunarudi nyumbani. Siku hiyo hafanyi kazi kabisa.” “Basi mpaka hapo naona
jumapili ndio niongozane na nyinyi.” Ron akabaki akimtizama.
“Nije asubuhi, twende wote kanisani, tukale, ndipo
turudi nyumbani. Ni sawa?” “Nitamwandaa.” “Nashukuru kwa kunielewa Ron.
Utaturahisishia sana mimi na Mina.” Ron akavuta pumzi kwa nguvu. “Sijui niseme
na mimi nashukuru kwa heshima uliyotupa! Maana ungeweza
kupotea naye baada yakujua ni binti mrahisi tu.” “Hapana Ron. Nafikiri
nyinyi bado mna Mina yuleyule wazamani. Mina niliyekutana naye mimi si mrahisi
kama unavyodhania. Hana malengo mazito, lakini anao msimamo katika kidogo
alicho nacho. Hata pale kazini wamemjaribu jaribu, lakini amewakataa.” “Kina nani!?” Andy akacheka.
“Acha kupaniki bwana! Mimi mwenyewe nilisikia tu
fununu. Nilimuuliza jumamosi, akakiri ni kweli na aliwakataa. Kwa hiyo mpe credit
Mina wangu bwana! Amebadilika. Sio
mrahisi hivyo.” “Daah! Itachukua muda, lakini hata sisi tunamuona. Tokea arudi,
jumamosi ndio ametoka kwa mara ya kwanza. Mama alishindwa kufanya kazi kwa
wasiwasi.” “Aliniambia.”
“Sasa ndio ujue jinsi hali ilivyo mbaya! Mimi mwenyewe nilishindwa kutoka ikabidi nikae na mama.
Alikuwa akilia anasema hadhani kama atakuja kumuona tena.” “Hii jumamosi!?”
Andy akashangaa sana. “Ndiyo! Hii jumamosi! Mina ni mpoteaji sana. Na kama unavyomuona. Akirudi mtajua yupo. Sio mbishi
wala mvivu. Atafanya kila kitu utakachomwambia. Atasaidia kila mtakachomtuma.
Atawachangamsha, gafla anapotea.
Anarudi anakaa kidogo, anapotea
tena. Kwa hiyo mama anakuwa na wasiwasi sana. Na hakuna mwanaume hata mmoja aliyekuja
pale nyumbani kama hivi unavyotaka kufanya wewe. Wote wanamchukua juu kwa juu.
Hawajulikani majumbani kwao na sisi tunakuwa hata hatuwajui. Kwa hiyo
akiondoka, mnakuwa hata hamjui mumtafutie wapi!” Andy akanyamaza. Wakamalizia
chakula.
“Nitakuja nyumbani jumapili asubuhi.” Ron akamtizama
kama asiyeamini. “Nitakuja.” “Sawa Kiongozi.” Wakaagana, akamshusha Ron kituo
cha daladala pale pale Palm Beach, yeye Andy akarudi kwake. Akiwa na utulivu
kuwa angalau amefanikiwa kumuweka sawa kaka mtu, akajua mama yao hatakuwa na
shida.
Ikabaki kwao sasa, kwa kina Ruhinda. Anampelekaje Mina
huko kwao! Ndio ukabaki mtihani mgumu kwa Andy. Ukweli Mina na familia yake, walikuwa hawaendani
kabisa na kwao. Akatamani ingekuwa tofauti, lakini hawezi badilisha chochote.
Moyo na akili vinamtaka Mina. Anafanyaje?!
~~~~~~~~~~~~~~
Inaendelea…
0 Comments:
Post a Comment