“Naamini kwa sasa unanifahamu kwa asilimia 100,
Andy. Hakuna nilichobakiza. Kuanzia wazazi, mimi mwenyewe, zamani
na sasa. Unanijua.” “Sijui baadaye.” Mina akamwangalia na kuinama kama
anayefikiria.
“Eti Mina?”
“Mimi mwenyewe sijui baadaye yangu Andy. Ila naomba nikuombe kitu.” “Karibu.”
Andy akajiweka sawa. “Leo ndio umenifahamu kwa undani sana. Na wewe
unaonekana sio mtu mbambaishaji au tapeli. Hiyo naongea kutokana
na ulivyoniambia juu ya Lora na sifa zako nilizozisikia pale ofisini.”
Andy akacheka akijua jinsi maneno yanavyojua kuzagaa pale ofisini kwao! Akajua
hapo Mina amejazwa maneno juu ya kila mtu.
Mina akaendelea. “Naomba kwa leo tuishie hapa, ili
wote tupate muda wakufikiria. Tusipeane ahadi yeyote. Hata kuniambia
utanipigia simu, tuache kabisa, muda uje ujibu kila kitu.” Andy akatulia
kwa muda. Kila akitaka kumruhusu aondoke, moyo unakataa. Hisia anazozipata
kwa huyo Mina! Hajiwezi! Gafla akaanza kumuelewa Omar. “Ngumu kuishi bila
huyu kiumbe aisee!” Akawaza na kumwangalia, akakuta akimsubiria.
“Labda nikuulize swali moja la mwisho.” Andy akaanza.
“Wewe binafsi, upo na malengo gani ya baadaye?” “Nisikudanganye Andy, ili
unione wa maana. Binafsi maisha yangu ndio kama yanaanza. Natembea kwa
hatua ndogo ndogo sana, tena kwa tahadhari, nikijua mama na Ron
wananiangalia kwa makini, na mimi ninajiona ninawajibika kwao. Sijui mshahara
wa Ron, lakini anamsaidia mama kunisomesha. Hiki ninachosomea sasa hivi, hata
sikujua kama ningesomea. Nimekuja kukutana nacho muda mfupi uliopita. Nikiwa na
maana hii, sina uelewa na mambo mengi kiasi chakuweka mipango ya kusikika
yamaana.”
“Hata hapa
nilipokaa sasa hivi, sijui ni kwa nini nipo hapa sasa hivi. Nahisi ni kama
nilivyokwambia. Pale
hospitalini, moyoni kwangu ulisikika ukiwa halisi sana kitu ambacho
sikuwahi kukisikia kwa matapeli wote niliokuwa nao.” Mina akaendelea
taratibu.
“Nikikwambia nilikusubiria, niamini nilikusubiri.
Nilijiambia mimi ni mchemshaji, na
nimeishi na matapeli. Lakini wewe nikakutetea nafsini mwangu, nikasema upo
ukweli niliousikia tokea rohoni, ile siku nikiumwa. Nikawa najiambia lazima
utarudi tu. Hata kwa kuchelewa, nikajihakikishia utarudi kuja kuniona tena.
Nilikusubiria mpaka jumatano natoka pale hospitalini.”
“Lakini Ron alikuwa ameniambia wewe ni bosi wake sio
rafiki. Nikakumbuka hiyo hali yako ilivyo. Na pale uliponikuta nimelazwa,
nikajifariji kuwa labda nilikuwa sahihi, hukudanganya ila mazingira yalikushinda
kurudi. Nikatamani hata kukusikia ukiniambia sababu yakutokurudi! Ukanionyesha
ni kama hukumbuki kabisa! Nikazidi kujidharau nakujiona ni mjinga
ambaye nimeshindwa kujifunza kutokana na makosa! Nakuwa naamini watu
hovyohovyo tu! Sasa kuja kumuona na Lora naye, ndio ikabidi niwe mpole kabisa.”
“Daah! Kumbe afadhali ningerudi hata kwa kuchelewa!”
Mina akacheka na kuinama. “Nimeharibu.” “Ninachotaka kusema, ni maisha yangu
ndio yanaanza. Nasikitika kuwa yanaanza nikiwa nimeshakuwa mkubwa.
Lakini ndio yanaanza. Sijui kesho itakuaje Andy. Kama nilivyokusimulia,
mimi sio mtu wakusubiriwa. Au kuacha mipango yako kwa ajili yangu.
Nashauri..” “Umesema leo tusiwekeane ahadi. Tujipe muda. Sasa mbona
unataka kuniamulia tena!?” Mina akanyamaza.
“Mimi ndiye niliyeomba nafasi yakuwa muamuzi wa hili.
Unakumbuka?” “Nakumbuka.” Mina akajibu taratibu tu.
“Naomba nikuulize tena.” Mina akamwangalia. “Kwa hivi
ulivyonifahamu. Nikaharibu kwako kwa kutoa ahadi ambayo sikutimiza.
Ingekuwa sijaharibu hivyo, tukakutana kwenye mazingira mazuri, au nikarudi siku
ile hospitalini, unafikiri kama ningeomba mahusiano na wewe, ungekubali?” Andy
akauliza kama anayeogopa tena kumpoteza!
“Niambie ukweli wako kutoka moyoni Mina. Unafikiri
ningefaa kuwa mwanaume wako ambaye ungekuwa na mimi tu mpaka kifo?” Mina
akawa hamuelewi! Na yote aliyo mwambia! Akatulia akitafakari, mwenzie akajua
ndio anamkataa.
“Ndio niliharibu kwa
kiasi hicho!?” Akauliza kinyonge. “Kwamba siwezi kusamehewa tena?!” Yeye ndio akawa mbembelezaji tena! “Hapana
Andy! Ni mimi mwenyewe nakosa ujasiri!” “Tafadhali naomba unijibu tu. Hii
inamaana kubwa sana kwangu. Nataka kujua.” “Nikujibu hivi hivi kwa yote
niliyokusimulia juu yangu!?” Mina
akauliza kwa kumshangaa zaidi ila kuvutiwa naye. Kwamba ni kama
anampenda alivyo!
“Vyooote. Wewe kama Mina na jumla yako yote. Nataka
kujua. Je, ningefaa?” “Kwanza
naomba nikuhakikishie kuwa nimebadilika Andy.” “Sawa.” Andy akakubali
bila tatizo. “Na ninakuhakikishia sitarudia ile tabia yakuwa na wanaume
hovyo. Au kuwa na wewe na wanaume wengine, au kufanya ngono hovyo. Nimebadilika.”
Andy akacheka taratibu na kuongeza. “Sawa Mina. Mimi bado nataka jibu langu.
Unafikiri ningekufaa?” “Ndiyo Andy.” Mina akajibu taratibu na kwa unyenyekevu.
Akamuona Andy anafunga macho na kuvuta pumzi kwa nguvu.
Akajirudisha nyuma kwenye kochi. Akajiegemeza kichwa, akiangalia dari kwa muda.
Kila hesabu aliyokuwa akipiga hapo kichwani mwake, jibu ni Mina. Upendo ukawa
na nguvu kuliko yote. Nafsi inamtaka Mina.
Baada ya muda akamwangalia. “Nilikwambia kuwa nakupenda,
si ndiyo?” Mina akabaki akimwangalia. “Unakumbuka?” “Uliniambia kabla
sijakwambia historia yangu! Au kabla hujanifahamu!” Mina akajibu taratibu. Andy
akaenda kupiga magoti mbele yake. “Nilitaka kukubusu wakati ule, ukasema nisubiri
kwanza mpaka unieleze wewe ni nani. Umenieleza na umeniambia, umeniambia
ukweli. Si ndiyo?” Mina akatingisha kichwa kukubali.
“Naomba nisikie sauti yako Mina!” Akamvuta mikono yake
yote akaishika vizuri akibembeleza. “Sijadanganya na hakuna nilichokuficha
Andy.” “Sawa. Naomba tujipe muda wa pamoja. Sio tukiwa mbali, halafu tuone
itakwendaje.” Mina akanyamaza.
“Umenielewa lakini?” “Hapana Andy! Ndio inakuaje?”
“Tuwe pamoja, wakati wewe ukinifahamu mimi na kuangalia kama nafaa kuwa mume
wako, na mimi hivyo hivyo. Itakapofika wakati tukaona ni sawa tunaweza kuishi
pamoja, tufanye taratibu, tufunge ndoa. Unafikiri ni wazo zuri.” Mina akabaki
amemkodolea macho kama hamuamini! Anawezaje!? Hata Mina akashindwa
kumuelewa.
“Lakini
haitakuwa yakujificha. Mama ameshaingiwa na hofu kwa maisha uliyoishi
nyuma, pamoja na Ron. Halafu Ron yupo chini yangu, sitataka kuharibu
mahusiano yangu na Ron. Ni mtu ninayemtegemea sana pale kazini.”
“Utafanyaje Andy na yeye anajua unaye Lora? Ron hawezi kukubali.” Hofu
ikamuingia.
“Nitazungumza naye, nimweleze ukweli na nia yangu.
Unafikiri ataelewa?” Ikawa kama kengele tena. Andy anafanya kweli, anaendelea!
Akaona kama mambo yanakwenda kwa kasi sana. “Mina?” “Sijui Andy! Sijui! Au
labda tusubiri kwanza.” “Tunasubiri nini?” Andy akauliza akijua
ameingiwa hofu. Mara Mina akasimama ghafla kama aliyekumbuka kitu.
Akamuacha Andy amepiga magoti pale.
“Ni nini tena?!” “Sijui Andy, kama nimeingiwa na hofu
ya mahusiano! Unajua Omar aliniambia ananijua na ananipenda kama
nilivyo! Akasema atanichukua, atanipenda, halafu akaishia kunipiga
kila wakati! Akawa haniamini tena.” Andy akasimama.
“Mina!” “Hapana Andy. Hii historia inajirudia.
Naomba pata muda wakufikiria zaidi. Unampendaje mtu mwenye historia
ngumu kama yangu!? Hapana Andy! Mimi nimepita hapo unapotaka tupite
sasahivi. Sio rahisi Andy. Nilimuona Omar. Alikuwa kama amechanganyikiwa!
Haniamini na yeyote, kwa chochote. Kila wakati alikuwa akiota anaibiwa.
Hapana.” Mina akajirudisha nyuma kabisa. Andy alikuwa amemsogelea. Akampisha
pembeni, akarudi pale alipokuwa ameacha pochi yake. Akaichukua.
“Mimi sio Omar, Mina!” “Basi naomba tujipe muda.
Tafadhali pata muda wakufikiria bila mimi nyuma yako au bila kuona unawajibika
kunijulia hali au la. Tafadhali Andy. Jipe muda wakutafakari mbali na hisia.”
Mina akataka kuondoka.
“Subiri kwanza Mina!” Mina akageuka. “Nimeelewa.
Nitafanya hivyo. Na wewe naomba unipe muda.” Mina akawa hajaelewa. “Njoo.” Akasogea,
Andy akamshika tena mikono yote miwili.
“Unamaanisha nini?” “Wewe umesema nipate muda
nifikirie kabla yakuchukua hatua nyingine. Si ndivyo?” “Mimi ndivyo
ninavyofikiria.” “Wazo zuri. Lakini naomba na wewe unisubiri mimi.
Namaanisha mimi tu, usije kumfungulia mtu mwingine mlango kabla hujahitimisha
na mimi.” Andy akajiweka sawa.
“Hapa leo tumeweka msingi. Naomba tusidharau
mwanzo wetu. Mimi kwangu nahesabu umeniamini na kuniheshimu kwa
kunieleza ukweli wote. Sichukulii kuwa ni maongezi tu. Na imeniongezea kukuamini.”
“Kweli Andy!?” “Kabisa Mina. Ungeweza kufunika mambo hayo ya nyuma, ukaja
kwangu na Mina huyu. Na mbona tungeendelea tu! Lakini kwa kuniambia ukweli bila
kunificha, naona tunaanza msingi mzuri.” Kidogo Mina akatulia.
“Nachukua muda kama ulivyonishauri, na wewe naomba unisubiri
mimi.” “Sitakubali mwanaume mwingine Andy. Kwanza hata sikuwa na mpango
huo.” “Nashukuru. Naomba tujipe muda. Wewe hunifahamu kabisa. Pata muda na wewe
wakunisoma ili ujue utakuwa ukiishi na mtu wa namna gani.” Mina akatingisha
kichwa kukubali. Akamuona Andy anavuta pumzi kama aliyepata aghueni.
“Bado unataka kuondoka?” “Ndiyo. Naomba nikupe muda.”
Andy akacheka. “Mimi naelewa ninachozungumzia Andy. Pata muda wakufikiria.”
“Sawa. Lakini naomba nikusogeze mpaka karibu na nyumbani.” Mina akacheka. “Nitashukuru.” Akachukua funguo za gari, akavaa viatu,
wakatoka wakiwa wametulia kila mtu akiwaza lake. Njiani Mina alitulia kimya,
Andy naye kimya. Wakaendesha mpaka Tegeta karibu na njia ya kwendea kwao.
“Naomba nikuchukulie usafiri wa kukufikisha nyumbani.”
Mina akacheka kama anayefikiria. “Ron anapikipiki anaifanyia biashara. Huwa
tukifika hapa, tunamuita huyo kijana, anakuja kutuchukua na kutufikisha
nyumbani.” Akamuona anatoa walet na kumtolea pesa. “Basi hii itakusaidia
kulipia.” Akamkabidhi.
“Nimefurahi umeitikia wito na kuniahidi
kunipa muda.” Mina akajua ndio anamkumbushia. “Nitakusubiria Andy.
Nakuahidi sitafanya chochote bila kukwambia.” “Na ninaomba Mungu
chochote kisitokee.” Mina akacheka taratibu kama ambaye na yeye anafikiria.
“Si hakuna chochote kitakachotokea?” “Ndiyo Andy.
Nitakusubiria wewe.” “Hapo sawa.” Wakacheka kidogo, wakabaki wametulia
pale ndani ya gari kwa muda. Ila ile hali ya utulivu pale, kila mtu aliipenda.
Wakajisahau. Mwishoe Mina akacheka na kumuaga. “Asante Andy.” “Karibu.”
Akashuka garini.
~~~~~~~~~~~~~~
Alirudi nyumbani akamkuta mama yake yupo jikoni.
“Nimerudi mama.” Mama yake akageuka. “Mbona umejawa cheko?” “Nimefurahi.”
“Haya, niambie kila kitu.” Mina akaanza kujiuliza aseme nini na nini aache!
“Tumepeana muda, mama. Nimemwambia apate muda wakufikiria. Tuchunguzane, ndipo
tutajua baada ya hapo.” Mama yake akageuka vizuri.
“Safari hii nikijana wakueleweka, mama. Anajiheshimu
na ananiheshimu. Anathamini maisha yangu na anachukua mambo kwa
heshima.” Akamuona mama yake yupo kimya. Akaumia sana.
“Anaonekana
ananipenda mama! Na si kwamba anataka kunichezea. Anaonekana anataka kunioa.” Mina akazidi kuumia baada ya kuona vile mama yake
anavyomwangalia. “Nimebadilika
mama. Safari hii nafanya tofauti na ndio maana sikufichi kitu. Naomba nipe nafasi
nyingine.” Mina aliendelea kumbembeleza mama yake.
“Mina mwanangu, hakuna mwanaume aliyekamilika,
akakuona wewe, asikutamani. Hilo nalirudia tokea upo shuleni.” Mama yake
akaanza.
“Umetoka hapa hata miezi mitatu haijaisha, tayari mtu
anasema anakupenda na anataka kukuoa! Mtu huyo wa kukwambia leo anataka kukuoa
wakati hakufahamu, anatokea wapi kama sio anataka kuyagusa anayoyaona
kwa nje! Utajifunza lini Mina, mwanangu wewe?” Mina akazidi kuumia.
“Unataka nini kitokee kwenye maisha yako ili ujifunze!?
Unakumbuka lililokupata kwa Omar?” Mina akashindwa hata kumjibu.
“Unataka tena?” “Safari hii ni
tofauti mama!” “Tofauti yake ni nini? Niambie.”
“Kwa kuwa nitakuwa na
wewe katika kila hatua. Sitakuficha chochote katika kila hatua ili unishauri.” Hapo
akamfunga mdomo mama yake. Akanyamaza na kugeuka akaendelea na alichokuwa akifanya,
Mina akaondoka.
Kwa Kina Andy.
Siku ya jumapili baada ya kutoka
kanisani wakiwa wanakula vikiwa vimejaa vicheko, mama yake akaanza kumuulizia
Lora. Hasira ikapanda ndani ya Andy, akaweka kisu na uma chini kwa nguvu. Kila
mtu akamgeukia. “Naomba niweke hili sawa.” Akaanza Andy. “Nilichukua ushauri
wako mama. Na wengine ambao mnaotaka Lora awe mke wangu. Nikajaribu
mahusiano lakini imeshindikana.” “Umeanza lini na umeshindwa lini?” Akauliza mama yake. “Tafadhali naomba
nimalize mama. Kwa kuwa unataka Lora awe mke wangu mimi, si ndivyo?”
“Ndiyo lakini pia ujue mahusiano sio rahisi hivyo. Kuna kuvumilia, na watu
wanatofautiana na...” “Mama!” Andy akamuita.
“Mimi naona umuache amalizie mama.” Akashauri dada
yake. “Thank you.” Akashukuru Andy.
“Narudia tena. Nilichukua hatua kama ulivyotamani mama, niwe na Mina.”
Akashituka, akaangalia kila mtu. “Mina ni nani?” “Nilitaka kusema Lora. Mimi na
Lora, imeshindikana. Na haitawezekana. Kama unataka awe mkwe
wako, Paul huyo hapo. Muunganishe na Paul.” “Haa! Hapana!” Paul akakataa
kabisa.
“Kwa nini unakataa sasa?” “Ninaye mpenzi wangu. Halafu
Lora mkubwa kwangu na anajidai anajua kila kitu.” Paul akaropoka. “Haaa! Kwa hiyo wewe ulitaka
mimi ndio nimuoe!?” “Mama ndiye anayetaka umuoe. Mimi ushanisikia
nikisema umuoe Lora? Hata mara moja. Kwa kuwa namjua Lora vizuri sana.” Paul
akajitetea.
“Ana nini na wewe? Kama sio kutaka kumkatisha
tamaa mwenzio?” “Kila mtu atajionea mwenyewe. Lakini mimi sina mpango na Lora.
Ila ujue tu, Lora anadharau. Na ndio maana unamuona mpaka leo na uzuri
wake ule, hana hata boyfriend.”
Akaongeza Paul.
“Si watu wanamuogopa sababu ya elimu na kazi
yake?” “Kwani wasomi wangapi hapa duniani wameolewa? Kwani Lora ndio amesoma
peke yake?” Akauliza Paul. “Hata mimi nimesoma jamani, msinisahau.” Akaongeza
Paulina. “Haya! Mfano ulio hai huo hapo. Kama hata Andy ameshindwa, basi
ujue wazi Lora sio muolewaji yule.” “Kwa nini na wewe?” Mama yake
akauliza tena kwa hasira.
“Utanichukia bure mama yangu. Ila ujue mimi na Lora ni
kama tumekuwa pamoja tu. Japokuwa amenipita mwaka mmoja, kumbuka nimesoma naye
darasa moja. Na tumekuwa naye karibu hapa mjini. Mimi ananidharau kwa
kuwa udaktari wangu nimesomea Tanzania.” Andy akashituka na kumwangalia.
“Unajishuku tu.” Mama yao akatetea. “Najishuku nini
wakati nina kazi na nina tibu watu!? Lakini si kwa Lora. Aliniambia hata akiwa
kwenye hali ya kufa, nisimguse. Sina hadhi yakumtibu kwa kuwa nilisomea
udaktari wangu chini ya mwembe.”
Pakazuka ukimya. “Sasa mimi nikajua kwa kuwa Andy mwenzangu amesomea nje ya
Tanzania ambako Lora anapaita chini ya mwembe,
labda mwenzangu atakubaliwa! Lakini Andy huyo naye amenyanyua mikono.” “Kila
mtu anamadhaifu yake. Inatakiwa mjifunze kuishi na watu.” Mama yake akaongeza
akizidi kutetea. Kila mtu akainamia sahani yake. Hakuna aliyetaka kujibu tena.
“Kwanza Mina ni nani?” Baada ya muda mama yake
akauliza kama aliyekumbuka. Kimya. Andy akaendelea kula. “Wewe Andy?” Andy
akavuta pumzi kwa nguvu nakuweka chini kila kitu, uma na kisu. Wote
wakamgeukia. “Mina ni msichana ambaye tumepeana muda wa kuchunguzana ili tuone
kama tunaweza kuwa kwenye mahusiano.” Kimya. Akainama na kuchukua vitu vyake.
Kisu na uma, akaanza kula tena. “Sasa kama kulikuwa na Mina, uliwezaje
kumchunguza Lora nakufikia mwafaka kuwa hafai?” “Mama, mimi sio mtoto
mdogo.” “Mapenzi huwa hayana mtu mzima. Na unaweza kufanya maamuzi
mabaya sababu ya hisia tu.” Andy akamgeukia shemeji yake.
“Mbona unaniangalia kama unanilaumu!? Sijaongea
chochote na yeyote. Kwa hiyo kama kuna mwingine ulimwambia, ujue ndiye
aliyesema.” “Unaongea nini na wewe?” Paulina akamuuliza mumewe aliyejishuku.
“Sitaki Andy afikiri mimi ndiye nimemwambia mama juu ya Mina.” Andy akaishiwa
nguvu kabisa, wote wakamgeukia mume wa Paulina, Devi.
“Kwa hiyo wewe unamfahamu Mina?” Akauliza Paulina, mkewe. “Kwa hiyo nyinyi mpo
hapa, mnatusanifu tu tunavyomuongelea Lora, kumbe mna Mina nyuma ya
pazia?” Akauliza mama yao kwa ukali. “Mimi Mina simfahamu jamani. Na wala sina
habari naye.” Akajihami Devi. “Wewe leo utayaongea yote!” Mkewe akamtisha. Andy
kimya. “Wewe Andy?” Mama yake akamuita kwa ukali. Andy akamwangalia. “Mina ni
nani?” “Narudia tena, Mina ni binti ambaye tupo kwenye kufahamiana.
Nitakapokuwa na chakusema zaidi, nitawajulisha.”
“Kwa hiyo
umeona umjulishe shemeji yako, sisi..” “Nyinyi msubiri mpaka
nitakapokuwa na chakuwaambia.” Akamalizia Andy huku akimtizama shemeji
yake. “Sijasema kitu.” Akanong’ona shemeji yake. “Leo utayasema yote. Wala
usihangaike hapo.” Paulina akamwambia mumewe.
“Wasiwasi wangu ni kuwa, huyu Mina sijui, ndiye
aliyekufanya ushindwe kupata muda wakutosha na Lora.” Akaanza tena mama yake.
“Jamani, tutaonana tena jumapili ijayo.” Andy akasimama na sahani yake.
“Unanidharau mimi wewe Andy?” Andy
akasimama. “Labda nizungumze na mimi kidogo, kama nitakuwa nimemuelewa Andy na
wewe mama.” Akaanza mzee Ruhinda. Andy akageuka. Na wengine wote wakatulia
kumsikiliza.
“Kama nilisikiliza vizuri tokea mwanzo kabisa, na
kukuelewa mama, ulitaka Andy ampe nafasi Lora. Amchunguze, aone kama wataweza
kuja kuona. Au sikuwa nimeelewa?” Akamuuliza mkewe kwa tahadhari sana.
“Ndiyo. Maana Lora ni mwanamke wakuendana na Andy na
hii familia. Ataleta mwanamke gani humu ndani atakayefanana na Lora?” Andy
akashangaa sana. “Subiri kwanza Andy. Mimi ndiye ninayezungumza.” Mzee
Ruhinda, baba aliyesoma na kuongoza wazee wasomi mjini akataka aweke sawa hilo
swala.
“Sasa kama nimemuelewa sawasawa na Andy, ndio
amerudisha majibu baada yakuchukua hatua ya kile ulichomshauri. Kuwa,
Lora hatamfaa yeye kama mkewe.” “Asante baba.” “Ruhinda!” “Subirini
kwanza niongee mimi, ni zamu yangu.” Ruhinda akamkatisha mkewe na Andy.
“Inavyoonekana Lora anaweza akafaa sana kuwa mtoto
mzuri wa humu ndani. Akawa rafiki wa kila mtu. Maana nimeona na Paulina
amemfurahia sana Lora. Lakini kwa kuwa Pius ameshaoa. Na ninaona ndoa yake
imetulia. Hana mpango wa kumuacha mkewe, Lora hawezi kuwa mkwe
humu ndani kwa kuwa waliobaki hawa wawili, Andy na Paul, wote wawili, wameshindwa
kuwa na Lora.” “Hiyo ni dharau unayoifanya kwangu Ruhinda. Tena mbele ya
watoto!” Akaanza mama Ruhinda.
“Jamani! Mimi naeleza wanachosema wanao. Nasaidia
kukuelewesha tu!” “Mimi unaniona ni mjinga sana, sielewi?” Ugomvi akatupiwa
baba yao.
“Hujawahi kuyaheshimu wawazo yangu na hutakaa
kuniheshimu mimi kama mkeo na mama wa watoto wako, utafikiri hawa watoto
umewaokota barabarani!” Akabadilika mama Ruhinda. “Naomba uniambie nilipokosea!
Au kwenye tatizo ni wapi hapa!? Maana naona unataka kwenda kinyume na wewe
mwenyewe. Sikumbuki ulipomwambia Andy kuwa nilazima amuoe Lora!
Nakumbuka ushawishi tu! Na yeye amekurudishia majibu kwa wazi kabisa.
Sasa kwa nini unakasirika mama, na muoaji ni Andy?” Akajieleza Ruhinda
taratibu tu.
“Wewe hushauriki kama watoto wako. Unanidharau
kwa kila kitu ndio maana unashindwa hata kufikiria. Wewe umesikia kuna Mina
sijui! Sasa huyo Lora alifikiriwa saa ngapi mpaka akaonekana hafai, Mina ndiye
anayefaaa?” “Habari za Mina, huna
mke wangu. Andy ameomba umpe muda, kukiwa na chakusema, atasema.
Sasa kwa nini unawasiwasi wa Mina, ambaye hata hujajua kama na yeye ataolewa?
Kwa nini unatengeneza hali ya wasiwasi wakat...” “Mimi kama mama ndiye
ninayejua kinachomfaa mtoto wangu.” Mama Ruhinda hakutaka kushindwa.
“Ninaposema Lora anafaa ni katika kila kitu. Huyu Andy
aliyesoma shule za mapadri atapata wapi mwanamke mzuri kama Lora!? Unakumbuka
yule mwanamke aliyemletaga hapa wakati ule yupo chuoni? Haeleweki kama ni
mwanaume au mwanamke! Sauti ipo kama imekauka!” “Lakini si ndiye aliyekuwa amemchagua
mwenyewe?” Akauliza Ruhinda.
“Kwa kuwa wewe umekusudia kwenye maisha yako
uwe kinyume na mimi, hata jambo la msingi hutaona. Unanidharau na
kunipinga hata kwa jambo ambalo ni la msingi kabisa.” “Labda mama
ungetulia kwanza na kumpa nafas...” “Unamtetea baba yako kwa kila kitu!”
Paulina na yeye akageuziwa kibao.
“Nilitaka kusema huyo Mina, mama. Sio baba. Unaweza
kukuta unamkataa mtu mzuri kwa Andy bila kumfahamu.” “Naona tuache mambo
ya Mina kwanza ili hapa ndani apite Lora. Sitaki mpenzi wangu aje hapa,
muanze kumlinganisha na Lora.” Kila mtu akamgeukia Andy.
“Unaona sasa!? Wewe Ruhinda uliyekuwa ukitetea ujinga?
Huyo Mina ameshakuwa ni mpenzi!” “Ninachotaka kusema mama, Lora na Mina ni watu
wawili tofauti. Na kwangu Lora sio
kipimo cha mke, ila ni kipimo chako
wewe. Kama alivyosema baba, yeyote nitakayemchagua, ni wangu mimi. Nataka mke
atakayenifanya mimi niwe na furaha, sio yeyote yule humu ndani. Anaweza akakosa
vigezo kwenu, lakini akawa anavigezo
vyote vya kuishi na mimi. Nataka niliweke hilo wazi na wote mliheshimu.”
“Mimi naliona hilo ndilo la msingi.” Akaongeza baba yao.
“Ruhinda unatafuta matatizo wewe leo!” “Nimefanya nini
mimi!? Au ni mimi mwenyewe ndiye niliyekuwa nikimsikiliza Andy? Naona
eti ni kama ameongea jambo la msingi sana! Au wewe Pius unasemaje? Maana
naona wewe huwa ukiongea mama yako huwa anakusikiliza na kukuelewa bila shida.”
Pius akanyamaza. “Huo ni unafiki Pius. Unajua nipo sahihi ndio maana unashindwa
kuongea ili usimuudhi mama.” Andy akakasirika kabisa.
“Mimi nashauri Mina apewe nafasi.
Akaribishwe nyumbani kama Lora tu na..” “Subiri kwanza Paulina. Simleti Mina
hapa ili mumpitishe. Au mumchunguze. Naomba niliweke hilo wazi
kwenu nyinyi wote. Mimi ndiye muoji.” “Kabisa.” Akaongeza baba yao.
“Asante baba. Na mimi ndiye nina vigezo vya mwanamke nitakayeishi naye.
Nyinyi wote hapa hamna vigezo vya mwanamke ninayetaka kumuoa.” “Pana
ukweli hapo japo ni mchungu!” Akaongeza Paul. Mama yao akanyanyuka kwa hasira
na kuondoka.
Kwa kina Mina.
Mina aliendelea na shuguli zake kama kawaida bila hata
kuzungumza na mama yake tena. Akawa ametulia, mpole hata ule utani ukaisha.
Siku ya jumapili kama kawaida, Ron aliita taksii hapo nyumbani, wote wakaenda
kwenye kanisa wanaloabudu kila jumapili. Usharika wa Mbezi. Mina alikuwa
ametulia kweli kumbe mawazo kwa Andy akijutia kumpa muda wa kumfikiria.
Usiku wakati wamelala na mama yake, akaanza.
“Nina wasiwasi mama!” Mama yake akamgeukia. “Nini?” “Hajanitafuta tena! Unafikiri nitakuwa nimemtisha?” Mama yake akamuhurumia.
“Kwa nini ufikiri ulimtisha?” “Ni mtu wa maana mama!
Na anaonekana nia ni kunioa kweli. Aliniambia alinipenda mara tu aliponiona.
Nikaogopa yale ya Omar yasije kujirudia. Akawa ananipenda kwa muonekano tu.
Lakini mama, alikuwa na msichana wake mzuri huyo! Tena msomi, mimi mwenyewe
nawajua. Walikuwa wakipendezana.” Mina akaendelea.
“Sasa anasema tokea aliponiona mimi akanipenda.
Na alivyojisikia kwangu sio kama kwa yule dada, ikabidi amwambie ukweli kuwa
anampenda mtu mwingine. Wameachana. Sasa nilipoona amefika umbali huo zaidi ya muonekano,
ikabidi niwe mkweli kwake. Nikamwambia asimuache msichana wake kwa ajili yangu.
Nikapaniki mama, ikabidi nimwelezee historia yangu yote.” Mama yake
akakaa haraka kwa mshituko.
“Mina!” “Ningefanyaje mama? Huyo msichana aliyekuwa
naye ni mzuri mno. Halafu nilisikia ana kazi nzuri sana. Nikaogopa tusije tukaanzana,
akaja kunijua, akaanza kunichukia kwa kumuacha mwanamke kama huyo kwa
ajili yangu. Sitaki tena mambo ya nusu nusu mama! Nishacheza vyakutosha.
Sasa hivi nataka nikiwa na mtu, nitulie moja kwa moja.” “Umemwambia kila
kitu!?” “Kila kitu mama, sijabakisha.”
Mama yake akabaki ametoa macho.
“Nisingemwambia?” “Nafikiri ungesubiri kidogo,
Mina, mwanangu! Angalau afahamu huo moyo wako, ndipo umwambie kidogo kidogo.
Tena sio yote! Mengine ungeyaacha tu yabakie nyuma. Kwa wakati mmoja!
Utakuwa umemtisha sana.” Yaani mpaka mama yake aliishiwa nguvu.
Akahisi labda hajaelewa vizuri. “Unauhakika ni
yoooote!” “Jamani mama!” “Nauliza tu Mina, mwanangu mzuri. Yote kama
yalivyo au ulitafuta hekima kidogo?” “Sasa hekima gani?” “Labda kuacha vijipande vingine.” “Kama vipi?” Akamuuliza mama yake.
“Labda kama mahusiano waliyokuwa nayo Mozee, Afidhi na
Omar.” “Ningesemaje?” “Ungemwacha Afidhi, ukapunguza. Ukamtaja tu Omar
na Mozee!” Mina akanyamaza. “Kwani na yale ya shuleni ulimwambia? Utakuwa
hujamwambia. Si eti Mina, mama?” “Nilimwambia mama.” Mama yake akatoa macho.
“Ni vibaya sana?” “Uuuu! Mina, mwanangu wewe ni muwazi
sana! Wenzako vingine wanamezea!”
“Sasa akija kusikia kwa wengine?” “Angalau anakuwa ameshakujua mwanangu! Mbali
na mambo mengine, wewe ni mtu mzuri Mina! Unaweza kuishi na watu
ukiamua. Una upendo, huna majibishano na mtu!” “Nimetoa na zile
tabia chafu mama. Leo sijafanya kitu chochote na yeye.” Mama yake akacheka.
“Najua umebadilika. Nakuombea Mina! Nakuombea sana mwanangu.
Sitaki watu wakuchezee.” Mina akatulia. “Wakikuona tu hivyo, wanataka
kukugusa.” “Sasa hivi
nimebadilika mama.” “Basi, kuwa mvumilivu. Kama ni wako, atarudi.
Kama sio wako, Mungu atakuletea wakufanana na wewe.” Hilo likamfanya Mina
kutulia.
~~~~~~~~~~~~~~
Inaendelea….
0 Comments:
Post a Comment