![]() |
“Ameshaharibu nini tena huko kazini kwako? Maana
nilikuonya Ron! Usimfikishe kazini kwako, atakuharibia lakini hukutaka kunis..”
“Mama! Mama! Hajafanya kitu kibaya bwana! Nimekwambia ametulia. Kwanza
huwezi amini.” Ron akacheka kidogo nakutingisha kichwa.
Akaangalia mlango wa chumbani kwa mama yake, ambako
analala na Mina. “Nini?!” “Huwezi amini leo amekwenda IFM kwenda kuulizia
chuo.” “Huyo Mina?!” Mama yake akashangaa sana. “Mimi mwenyewe sikuamini.”
“Labda mwanangu kakua jamani! Mungu wangu mkubwa!” Mama yake akaangalia
juu kabisa kama anayemshukuru mungu.
“Lakini kuna jingine.” Akapunguza kabisa sauti. “Wewe
umemjua aliyemfuata siku ya jumamosi?” “Amekataa kabisa kunitajia jina. Lakini
si unamjua Mina alivyo msiri kwenye hayo mambo yake? Mpaka yamuharibikie
ndio atarudi analia hapa, na majina atataja. Lakini si kabla.” Mama yake
aliongea kwa sauti ya chini, ya kunong’ona na yeye kama Ron.
“Wewe umemjua?” “Unamkumbuka yule bosi wangu alikuja
hapa kunichukua tukaenda kuangalia mpira?” “Subiri kwanza Ron. Yule kijana!?”
“Anaitwa Andrew Ruhinda, ila watu wamezoea kumuita Andy.” Mama yake akabaki
ameduaa. “Ndiye aliyenichelewesha. Anaonekana ana nia na Mina, mama.
Hivi ameomba kuja kukuona ili ajitambulishe kwako rasmi.” Mama yake akabaki
bado ametoa macho.
“Mama?” “Umesema ndiye aliyekuwa naye jumamosi?” Mama
yao akataka uhakika kwanza. Maana alimjua binti yake. “Amesema alianza naye
hospitalini.” “Basi kweli ameamua. Ujue Mina alikuwa anawasiwasi hatamtafuta
tena, kwa kuwa alimwambia ukweli wote juu yake!” “Ameniambia!”
“Mimi mpaka nikamlaumu Mina. Nikamwambia ameharakisha
sana.” “Mimi huwa sielewi mama. Sijui ni bahati Mungu amemjalia
Mina au sijui! Hivi unajua amemuacha mwanamke mzuri tu sababu ya Mina!?”
“Ameniambia Mina! Nahisi ni bahati. Maana mimi nilijua wanachanganywa na
huo muonekano wake wa nje, lakini kama na wewe unasema huyo mwanamke alikuwa
mzuri, basi ni bahati.” “Mzuri sana tu ila yeye anaonekana wa kileo zaidi na amesoma si kama Mina!” Wakabaki kimya kwa
muda.
“Sasa unasemaje?” Mama yake akavunja ukimya. “Kuhusu
nini?” “Kumkaribisha huyo kijana hapa nyumbani! Mimi binafsi sidhani kama ni
sawa Ron.” “Kwa nini?” “Wewe unamjua Mina. Akiharibu huko si atakuharibia
na wewe?” Mama yao akasita. “Mina anaonekana amebadilika mama. Hata pale
kazini nimesikia walikuwa wakimtongoza anakataa. Naomba tumpe nafasi nyingine.
Tena uzuri safari hii analeta mwanaume nyumbani! Huoni kama itakuwa nafuu?
Itakusaidia au itatusaidia kujua kinachoendelea kwenye maisha yake na
kumshauri.” “Mmmh!” Mama yake akaguna.
“Lakini ameonyesha mabadiliko makubwa kwa kweli.
Ametulia na shule.” “Hilo ndilo linanipa moyo mama. Pengine amekuwa sasa.”
“Labda.” Wakanyamaza kwa muda. “Amesema anakuja jumapili hii asubuhi, halafu
twende naye kanisani na kurudi hapa nyumbani.” Mama yake akacheka kama
aliyeridhika.
“Anaonekana amempenda Mina! Mungu amsaidie mwanangu
jamani. Atulie na huyu.” “Hilo ndilo la msingi. Maana amesema yeye hajali ya
nyuma, labda kuanzia hapa. Kwa maana nyingine inategemea na Mina mwenyewe.
Ameniomba nimuache Mina awe huru, hata akija kazini, aingie ofisini kwake, nisimkataze.”
“Kwamba anataka hata kazini wamtambue?” “Ndivyo alivyosema. Hana chakuficha
kwa yeyote. Anasema anamtaka Mina amfahamu bila kificho.”
“Mmmh! Labda hatimaye Mungu amenisikia jamani! Nilimlilia
Mungu na huyu mtoto! Mchana na usiku bila kuchoka.” “Nakumbuka mama.
Mara tuambiwe alishachukuliwa nafsi yake ndio maana hasikii!”
Wakaanza kucheka. Wakazungumza wakikumbushana shida walizopata na Mina mpaka
kufika hapo, kila mtu akaenda kulala.
Mina alikuwa amelala, hana habari. Mama yake
akamwangalia. Kisha akamfunika vizuri, na yeye akajilaza pembeni yake asiamini
na usiku huo yupo hapo.
Kipendacho Roho.
Jumapili asubuhi ya saa tatu kamili Andy alikuwa
akiegesha gari mbele ya nyumba ya kina Mina. Mama yake akamwangalia Mina wakiwa
chumbani. Akamuona anacheka na kuchungulia dirishani. “Amefika mama!” Mama yake
akacheka. “Nenda sasa kampokee.” Mina akatoka mbio.
“Karibu.” Wakamsikia ameshafika nje. “Naamini nimefika
muda sahihi.” “Mama anamalizia kujiandaa, anatoka sasa hivi. Umependeza Andy!”
Andy akacheka. “Na unanukia vizuri.” “Njoo kwenye gari nikupe zawadi yako.”
Akamvuta mkono.
“Umeniletea nini?” “Pafyumu. Nimekuona unapenda harufu
nzuri.” Akacheka. Akafungua mlango akamtolea kimkoba. “Angalia kama utapenda.”
“Asante.” Mina akaanza kuifungua kuitoa kwenye boksi. “Nzuri hata kwa kuitizama
kwa macho! Chupa nzuri. Inaonekana imekugharimu sana!” Akasifia. “Pulizia uone
kama utapenda harufu.” Akajipuliza. Akaipenda. “Asante. Nimependa. Naenda
kumpulizia na mama. Twende.” Na yeye akamshika mkono wakawa wanangia ndani.
“Mama! Andy amekuja.” Ron akatoka akamsalimia Andy kwa
kumshika mkono. Mina akaingia chumbani kwa mama yake akamwacha Andy na Ron.
“Ameniletea pafyumu.” “Naipata hiyo harufu.” “Jipulize na wewe mama yangu,
unukie.” “Siku nyingine bwana! Ameleta leo tu, halafu aone wote tunanukia kama
tulikuwa na...” Mina akampulizia mama yake kila mahali. “Mina!” “Na wewe unukie
mama yangu.” Wakaanza kucheka.
Baada ya muda wakatoka chumbani. “Karibu Andy
mwanangu.” Andy akasimama kusalimia. “Asante mama. Nashukuru kwa
kunikaribisha.” Akampa mkono na kumsalimia. “Na mimi nimeshukuru kwa hiyo
heshima yakutaka kufika nyumbani. Karibu.” Wakakaa. “Najua ibada inaanza saa
nne na nusu. Lakini niliomba kuwahi kidogo ili nizungumze na wewe pamoja na Ron
kabla hatujaenda kanisani.” “Karibu.” Mama yao akakaa vizuri.
Andy akaanza kusugua mikono kama anayetafuta
pakuanzia. Mina alikuwa amekaa tu pembeni ametulia. “Labda niseme tu kwa
kifupi, ili nisikuchoshe kwa habari ndefu mama yangu.” “Hata kidogo. Labda kama
unataka tukutayarishie kifungua kinywa ule wakati unaongea.” “Asante mama
yangu. Lakini nilimwambia Mina msisumbuke na kifungua kinywa kwa leo. Huwa nina
mtindo wa kuamka mapema sana. Nikishafanya mazoezi nakuwa na njaa, siwezi
kuvumilia. Inabidi nile tu. Kwa hiyo hapa nilishapata kifungua kinywa, labda
nyinyi. Naweza kusubiri.” “Hapa hakuna mfanya mazoezi baba. Lakini tunakula
mapemaa.” Wote wakacheka.
“Hapa tulishakula, tunasubiri cha mchana tu. Wewe
endelea.” “Asante.” Andy akatulia tena kidogo kama mwenye hofu. Pakazuka
ukimya. “Labda niseme, au labda nianzie tulivyokubaliana na na..” Akasita na kucheka kwa hofu. Wote walikuwa
kimya wakimtizama mpaka akawa anashindwa kuzungumza. “Sikujua kama itakuwa
ngumu hivi!” Andy akaongea huku akisugua mikono na kucheka kama kujituliza.
Wote wakacheka na kunyamaza tena.
“Labda nianzie mwanzo, lakini nitafupisha ili
nisiwachoshe.” Akaanza tena. “Mara ya kwanza kumuona Mina hapa nyumbani,
nilivutiwa naye sana. Nikadhani ni hisia tu. Nikajaribu kujituliza kwa hili na
lile. Wakati huo tayari kulikuwa na shindikizo la Lora, kutoka kwa wazazi.
Nikajaribu kupuuza juu ya Mina, nikaona nifanye hatua ya mbele zaidi kwa Lora,
ili angalau kumtoa Mina mawazoni. Ron na Mina wanamfahamu Lora. Ni binti
aliyekuzwa kwenye mazingira yanayofanana na kwetu, hata wazazi wetu walifikiri
ndiye angekuwa mke sahihi kwangu.”
“Lakini kila nilipokuwa nikijitahidi kwa Lora, haikuwa
kama ninavyojisikia kwa Mina. Nikaona sijitendei haki mimi mwenyewe na
Lora pia. Ikabidi kumwambia Lora kabla hatujafika mbali. Sikudanganya, japo
alikasirika sana. Nilimwambia kuna mtu nampenda sana. Na
ninahofia kwa kadiri ninavyopoteza muda, naweza kumpoteza.
Kufupisha stori, baada yakuona Lora ameshatoka kwenye picha, ndipo nikamwambia
Mina. Baada ya mazungumzo ya muda mrefu na Mina, akihofia kudanganywa,
tukakubaliana tupeane muda wakuchunguzana ili tuje kufikia muafaka. Yeye
achunguze kama mimi nitakuja kumfaa kama mume, na yeye kama mke. Hatukupeana
muda, ila nilimwambia atakapoona yupo tayari aniambie na mimi hivyo hivyo.”
“Tumekubaliana kwa kipindi hicho kusiwe na mtu
katikati yetu. Ni mimi na yeye tu, mpaka tuone hatutafaana. Tutaambizana,
na ndipo kila mtu ataendelea na maisha yake. Sasa kwa makubaliano hayo ndipo
nikaomba angalau na mimi mnitambue kama nipo na Mina. Sina kificho
kokote na kwa yeyote. Na nia yangu ni kutaka kuoa. Nampenda Mina.
Na naomba Mungu atusaidie, kusitokee chochote chakututenganisha. Tuweze
kurekebisha tofauti zetu ili tuweze kuwa pamoja. Ni hivyo tu mama
yangu.” Andy aliongea kwa heshima.
“Labda niulize Andy.” “Karibu mama.” Mama yao akakaa
vizuri. “Kama nimekusikia vizuri, Lora alikuwa chaguo la wazazi. Umesema
mnaendana. Kwa haraka haraka, wewe umetuona sisi. Maisha yetu. Unamfahamu Mina
kwa kiasi. Najua wazi ipo tofauti kubwa sana kielimu na kiuchumi.
Hata maadili, nikikuangalia, unaonekana umekuzwa kwa namna yakisomi.”
Mama Ron akaendelea.
“Swali la kwanza, wazazi wako wanajua juu ya
muafaka wako na Lora? Swali la pili, wanajua juu ya Mina? Namaanisha
wanajua vizuri juu ya Mina?” Mama Ron akauliza vizuri.
“Nilipomalizana na Lora, niliwaambia. Huwa tunakutana
kwa chakula cha mchana kila siku ya jumapili baada ya misa, nyumbani kwa wazazi,
Msasani. Jumatano nilihitimisha na Lora, jumamosi tukakubaliana na Mina,
jumapili nilipofika nyumbani nikawaambia hitimisho langu na Lora. Na
makubaliano yangu na Mina, japo sikuwa nimekwenda kwa undani kama hivi
nilivyojieleza kwako. Lakini Mina atakapokuwa tayari, nitampeleka
kumtambulisha.” Pakazuka ukimya.
Andy akawaangalia kwa zamu. Akamsogelea Mina na
kumshika mkono. “Labda niseme hivi, kama nilivyowaambia wazazi wangu.” Wote
wakamwangalia. “Mimi ndiye muoji. Najua ninataka mke wa namna gani.
Mimi ndiye nitakayeishi na mke wangu mpaka kifo. Nafikiri nina haki
zote zakuchagua mke mwenye vigezo vyangu mimi. Hata kama kwa wengine
itakuwa ngumu, lakini mimi muoaji niwe nimeridhika naye.” Andy
akaendelea.
“Sikuwa na wanawake wengi kabla. Nilisoma shule ya
bweni ya mapadri. Ila nilipata msichana wakati nipo chuoni. Nikaja kuwa na
Lora, niko na Mina. Nimesoma saikolojia. Nina uwezo wakumsoma mtu na kumuelewa
hata kama anazungumza kingine, nina uwezo wa kuujua ukweli.”
“Kwa uwazi
alionao Mina. Vile alivyoniamini na kujifungua kwangu bila
kunificha chochote! Vile ninavyojisikia nikiwa na Mina, ndivyo
ninavyotaka iwe hivyo kwa maisha yangu yote. Najua mnaweza kusema ni mapema
sana kusema hivyo, lakini Mina ana vigezo vingi vya mwanamke ninayemtaka
kwenye maisha yangu. Nampenda Mina.” Andy akawa kama amemaliza. Ron
akamgeukia mama yao.
Akajua ndio anasikilizwa yeye. “Mimi binafsi nirudie
tena kukushukuru kwa heshima uliyompa Mina. Asante. Na ninaahidi
kuwaombea. Ili iwe kama Mungu alivyokusudia. Hivi unavyotuona hapa ndio familia
imekamilika. Tunaishi sisi tu. Unakaribishwa muda na wakati wowote ule.”
Andy akaachia mkono wa Mina akasimama. Akamsogelea mama yao akampa mkono.
“Asante mama yangu. Nashukuru sana. Angalau itaturahisishia mimi na Mina.”
“Nitawaombea.” Mama Ron akaongeza.
~~~~~~~~~~~~~~
Kijana huyo aliyekuzwa na malezi ya kipadri, kwa mara
ya kwanza mapenzi yakamfikisha kanisa ya Kiluteri. Hapakuwa na maji
mlangoni ya kuweka ishara ya msalaba kama alivyozoea na kupiga magoti. Akawa
mpole akifuatisha anachofanya Mina mpaka mwisho.
Baada ya ibada, akasahau yupo na familia hiyo
inayoendeshwa na mwalimu wa shule ya sekondari. Aliyepambana kufikisha
wanae hapo walipo. Hapakuwa na muda wakuwafundisha kula kwa kisu na uma, ila kuhakikisha
chakula kipo mezani, kila wakati. Basi.
Akawapeleka kwenye hoteli inayolingana na kina
Ruhinda. Yenye napkins za
vitambaa safi vyeupe, kwenye meza zilizopagwa vizuri visu, umma na vijiko. Tena
vijiko vya size tofauti tofauti. Kwa supu, chakula na dessert kama wangechagua dessert ya kutumia kijiko. Wakabaki wakiangaliana.
~~~~~~~~~~~~~~
Mama Ron mwenyewe alihamia Dar kikazi. Alizaliwa
kijijini, akakulia kijijini. Akaja mjini akiwa binti tu. Maisha yakachanganya
na ubusy. Waliomzunguka na mwanaume aliyempata walikuwa watu wa kawaida sana. Kula kwa
mkono, suna! Hapakuwa na maswala ya
kula na kisu pamoja na uma. Kwenye sherehe alizokuwa akihudhuria yeye ni kula
pilau kwa mkono, wakijitahidi ukumbini basi kijiko. Leo wameketishwa kwenye
visu na uma! Wakabaki hawajui chakufanya na hivyo vifaa hapo mezani.
~~~~~~~~~~~~~~
Mpaka muhudumu anamaliza kutaja aina ya vinywaji
walivyo navyo, wote wamechanganyikiwa. Wakaishia kuagiza soda aina ya Sprite.
Nazo hizo soda zikaletwa na glasi za namna yeke na ice cubes/barafu kwenye birauli za aina yake.
Kila mmoja alipokabidhiwa menu ya vyakula, ikawa msala
mwingine. Hakuna kati yao aliyeelewa hata kimoja wapo. Kila kitu kimeandikwa
kwa lugha ya kigeni. Andy alishachagua chakula chake, akaendeleza mazungumzo
akiwa ametulia anasubiri muhudumu arudi amwambie anachotaka.
“Andy!” Mina akaita kwa upole, Andy akamgeukia. “Mimi
mwenzio sielewi hapa. Sioni hata wali na maharage!” Andy alicheka sana. “Mina!”
“Kweli bwana! Hata chips hamna!” Mina akalalamika huku akiendelea kusoma.
“Naona Mina na mimi hatutofautiani baba.” Akaongeza mama Ron. “Nimesoma mpaka
nimechanganyikiwa. Huku huwa hatuji baba!” Akaongea mama Ron kinyenyekevu
lakini wakacheka.
“Labda niulize, mnataka kula nini? Naweza kumuita
muhudumu akaja, mkamwambia mnachotaka kula.” “Kwani wewe unataka kuagiza nini?
Nionyeshe hapo kwenye menu.” Andy akamfungulia Menu yake akamuonyesha.
“Namba 17.” Mina akaanza kusoma. Akamwangalia usoni.
Andy akaanza kucheka. “Sasa ndio nini hivi!?” “Nimetaka tu kiazi kikubwa kimoja
kilichookwa, watakiweka cheese, watamwagia
vipande vidogo vya beacons,
nitaomba na sour cream
juu yake. Wataleta na mchanganyiko wa mboga mboga, ni aina ya kama kachumbari
lakini yenyewe ni kama inasukari sio chumvi, inaitwa slow, na kipande cha nyama ya ng’ombe ya kuchoma, lakini
upande wa mguu. Nitaomba medium rare,
kwamba nyama wasiikaushe sana.” Wote wakabaki wametoa macho.
“Kumbe ndio maana hatuelewi! Vyote hivyo!” Andy
akazidi kucheka. “Mavyakula mengi hivyo!” “Wewe unataka kula nini?” “Chips
kuku.” Mina akajibu haraka sana. “Hivyo tu!?” Akauliza Andy kama anayeona
anajipunja. “Kwani huwa wanakula na nini?” Andy akazidi kucheka. “Hutaki hata starter?” Mina akabaki ametoa macho. “Naona mimi niwe kama
Mina tu. Hizo starter
tuache.” Wakazidi kucheka. Ukaanza utani, mpaka chakula kikaja.
“Lakini hata mimi sifahamu vitu vyote. Wakati mwingine
unawaita, wanakuelekeza.” Wakamuona yeye Andy anatumia kisu na uma. Anakula
bila shida. Wakapoa. Hapakuwa na kunawishwa mikono. “Twende mama.” Mina akamtoa
mama yake pale.
“Kuzaa kuna kuona mengi!” Walipofika chooni wakaanza
kucheka. “Sasa pale tutakulaje?” “Ndio maana nimekuleta huku unawe, twende
ukale kwa kutumia mkono mama yangu.” “Aibu gani hii!” Wakazidi kucheka.
Walirudi mezani Ron alikuwa akila kwa mkono hana hata
habari. Kuku, chips vilikwenda mdomoni kwa kutumia mkono bila shida. Wala wazo la pili halikuwepo kutoka kwa Ron.
Walikula wakizungumza ndipo akawarudisha nyumbani.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakati huku ya Mina yakimuendea sawa, jumapili ya Pam
ilikuwa ikimuendea kombo. Mpaka siku
hiyo hakuwa amesikia chochote kutoka kwa Mill. Akakata tamaa akijua kama Jerry
hajasahau kumpa, basi Mill hakuitaka. “Hata hivyo hakuniomba. Sijui
kwa nini nimejidhalilisha kwa kiasi hiki!” Akaanza kujilaunu akiwa amekata
tamaa.
~~~~~~~~~~~~~~
Usiku wakati
akilala, akiwahi sababu ya kazi siku inayofuata, ujumbe kwa WhatsApp ukaingia. ‘Nashukuru kwa
namba Pam wangu. Ila nilipewa bila masharti. Sasa sijui mida hiini ni mibaya?’ Nusura aruke. Akajibu kwa haraka. ‘Ni sawa tu. Hakuna masharti.’ Akamuona amesoma na kujibu hapohapo. ‘Kwamba hata nikitaka kuisikia
sauti yako sasahivi ni ruksa?’ Pam akacheka na kujibu. ‘Hakuna
masharti.’ Akamjibu, ‘Nashukuru’. Kisha akaona anampigia.
“Mzima Pam?” “Mimi mzima lakini
nilikuwa na wasiwasi na wewe! Uliondoka umeloa na ulikuwa na safari ndefu!
Hujaugua?” “Nashukuru kujali. Lakini huwa nina mtindo wa kusafiri na nguo za
ziada. Nilibadilisha kwenye ndege. Nilikuwa sawa tu. Niambie hali yako.” “Naendelea
vizuri.” “Kama ingekuwa vibaya, ungeniambia?” Akamsikia akicheka taratibu.
“Eti Pam?” “Naendelea vizuri.” “Vizuri
hii ni ya wote. Sasa nipe yangu ya peke yangu. Ya ukweli.” “Nipo sawa Mill.
Asante kunijali mimi kama Pam.” Mill akacheka kama
anayefikiria. “Ni nini?” “Hata nikikwambia sasahivi, haitaleta maana. Ushazoea
kusikia ukiambiwa na wengi. Nina uhakika unaambiwa kila siku.” “Wengi wananidanganya.” Ikawa kama
analalamika.
“Katika hao wengi na mimi unahisi nitakuwa
mmoja wao?” “Sijui Mill! Mimi sikufahamu.” “Ila kwa muda mfupi niliokuwa na
wewe, umeshaniweka kwenye kundi lao?” “Nisinge kupa mawasiliano yangu.” Hapo akaridhika.
“Nashukuru kama unaniamini, na
nakuahidi sitakudanganya. Sawa?” “Nakusikiliza.” “Basi naomba vitendo
ndio viongee. Ila jua nimefurahi sana kukusikia.” “Kwa nini sasa wakati
hata hunijui?” “Naomba ulitunze hilo swali nitakuja kukujibu endapo Mungu
atajalia kuonana. Ila jua nimefurahi kukusia. SANA. Na nimefurahi kupata namba
yako.” “Ila hiyo namba niliomba upewe tokea jana!” Akajua alikuwa akisubiria simu yake tokea hiyo jana.
“Pole.” “Sio kwamba nalaumu!” Mill akacheka. “Silaumu bwana!” “Hamna shida, ila na mimi nimepewa sasahivi,
na kukupigia. Nisingeweza subiri. Muda mwingi simu ya Jerry inakuwa
mikononi kwa Sandra. Mawasiliano yeyote yanayokuhusu wewe inabidi
kutumia barua pepe, tena ya zamani sana, enzi ya tokea tupo shuleni na
Jerry, ambayo Sandra haifahamu. Kwa hiyo hata utumaji wake lazima uwe
nje ya alipo Sandra.”
“Kwa jinsi alivyonieleza Jerry ilimbidi
aage kwenda kunyoa nywele na huko ndiko alitafuta Café akanitumia email
yenye namba yako. Anasema alikuwa na Sandra tokea jana, asingeweza ku risk.
Umeelewa sasa?” “Mimi nilijua hujataka au na wewe Sandra wako huko amekubana.” Mill alicheka sana.
“Usicheke bwana!” “Huku hakuna Pam
mwingine! Upo peke yako.” “Mmmh!” “Kwamba huamini?” “Mimi sijui bwana! Sasa kwa
nini?” “Kwani wewe hujamsikia Lona? Mie choka mbaya.” Alishituka Pam! Maana ndio maneno aliyokuwa akiyasema ofisini,
akimkashifu Mill. Akajua Jerry amemwambia.
“Eti Pam? Maana hata wewe sikujua kama utanitafuta
tena.” “Amepatwa wivu tu. Hamaanishi. Mimi namfahamu Lona na nishamzoea.
Tafadhali asikuumize.” Akamsikia akicheka. Kisha
akaongeza.
“Hata kidogo. Na mimi nilimuelewa. Ila
sababu ya kutokuwa na Pam mwingine huku au huko ni utapeli mwingi.
Ukiacha mwanamke huko nyumbani jua utakuwa na kazi ya kumtunza
ila wanafaidi wengine. Huku nako hakuna mapenzi ya kweli kama
hivyo Mike na Kamila. Usanii mwingi. Na mimi sasahivi sina muda. Nina
malengo ambayo nataka yatimie mapema.”
“Bado nasoma. Nilimaliza shahada ya
pili huku, nikagundua kuna kitu kingine nikisoma kinaweza nisaidia zaidi.
Shahada ya pili nilisoma bila kufikiria. Nilitaka tu niwe huku. Lakini
sasahivi nina malengo. Nasomea ujuzi. Na baba ndiye anayenisaidia kwa
asilimia 60. Hiyo iliyobaki lazima nipambane mwenyewe.”
“Kwa hiyo nina shule ngumu na
nina kazi ninayofanya usiku na wakati mwingine nikipata nafasi naomba kufanya
kazi masaa ya mchana. Nipo busy mno. Kwa hiyo sina muda wa Pam
mwingine. Pam wangu mmoja tu.” Pam akacheka
sana.
“Piga simu muda wowote utakao ila jua
kuna muda naweza shindwa kupokea. Zaidi ninapokuwa na mgonjwa au mtu namuhudumia.
Nitakutumia ratiba yangu vizuri ili uwe unajua nilipo na ninachofanya wakati
wote. Sio ratiba ngumu maana haibadiliki. Na najitahidi isibadilike angalau kwa
muhula mzima wa shule ili isiathiri shule yangu. Umeelewa?” Akawa ameibua swali kwa Pam.
“Kwamba wewe ni daktari huko?” “Hapana.
Nipo nafanya kazi kwenye nyumba ya wazee huku nikisomea unesi.” Pam akashangaa sana. “Nina shahada ya uongozi, inayoendana na
mambo ya uhasibu. Nikafanya ya pili hukuhuku nikazama kwenye mambo ya uhasibu
zaidi lakini naona pesa yake haiwezi nitunzia Pam wangu na watoto
wetu.” Pam hakuamini.
“Hiki ninachofanya usiku, nina malengo
nacho. Naiba ujuzi. Ila sasa, ukifungua sehemu kama hii kwa kiwango hikihili,
lazima uwe na RN, ambaye lazima utamlipa mshahara mkubwa. Sasa kwa nini mimi
mwenyewe nisiwe huyo Registered Nurse na mmiliki?” “Unaakili!” Akacheka.
“Itanisaidia kusimamia biashara yangu
kwa urahisi. Nitaajiri watu wenye elimu ya chini yangu ambao nitawalipa pesa ya
kawaida. Na pia itanisaidia kupata kibali cha kuanzisha kampuni yangu kwa
haraka. Sasa malengo kama hayo hayahitaji watu kama kina Lona wa
huku. Sitatulia.” Pam alicheka sana.
“Wewe unamsema Lona wakati hunijui
mimi!” “Sasahivi nakufahamu kwa asilimia kubwa sana Pam. Nyingine najua
tutaendelea kufahamiana taratibu. Ila kwa nilipo, na ninapokwenda, najua wewe
ndio utaniwezea. Au utapawezea.” “Sijui Mill. Wewe upo mbali,
mimi nipo huku! Ndio inakuaje?” “Naandaa mazingira Pam wangu. Tutakuwa pamoja
tu. Usiwe na wasiwasi. Nipe muda mama. Na usinikatie tamaa. Hilo ndilo
ombi langu kwako. Umenielewa?” “Nakuelewa Mill.”
“Ewaaah! Mipango inaweza sikika
mizuri, lakini kufikia inaweza kutugarimu mno. Hapa nilipo penyewe si rahisi.
Lakini nimejiwekea malengo ambayo hayawezi timia bila mimi mwenyewe kuyasimamia.
Ndio maana unaona na wewe nimekushirikisha mapema. Ujue mwisho tokea mwanzo,
unisaidie kutembea. Ilitufikie mwisho mzuri.” Akazidi
kumgusa Pam.
“Sitaki tuishie kuwa ombaomba. Au
watoto wetu wahangaike. Nataka uzee wetu uwe wa heshima, sio wakudharauliwa
hata watoto wanaogopa kuwasiliana na sisi wanaogopa tutaomba pesa! Hapana.” Pam akacheka ila furaha!
~~~~~~~~~~~~~~
Hajawahi pata
mwanaume anayemuonyesha mwisho mzuri hivyo mpaka uzee! Wote aliokwisha
kutana nao, mwisho wao ni kitandani wakishamvua nguo. Leo Mill anazungumzia
mpaka watoto! Mipango yao ya pamoja mpaka uzeeni! Wala hakuhitaji
kutongoza. Mke alishajipatia. Hapo anamuuzia sera za maisha yao wala si yake huko ugaibuni!
Akaupata moyo wa Pam kwa asilimia ZOTE.
~~~~~~~~~~~~~~
“Uko Pam?” “Nipo.” “Basi nisikuchoshe.
Nikuache upumzike.” “Hunichoshi. Ila sema najua na wewe unahitaji kupumzika.
Tutazungumza wakati mwingine.” “Unaendaje kazini?” “Nawahi daladala. Asubuhi si
shida nikiwahi kutoka nyumbani. Jioni ndio kuna sumbua kidogo. Lakini
nimeshazoea.” Mill akafikiria kidogo.
“Ningemtuma dereva wa Mike akuletee
gari yangu. Maana inakaa tu pale kwake. Lakini najua Sandra anaifahamu. Anaipenda
sana. Ameniambia anakusanya pesa nimletee kama hiyo.” Pam akapigwa na butwaa.
“Au hapatakuwa na shida?” “Mmmh! Usijisumbue.
Mimi nitakuwa sawa tu.” “Wewe kupata usafiri ni muhimu kwangu wala si usumbufu.
Usalama wako ni muhimu sana Pam. Hiyo gari inakaa tu hapo mpaka mimi nirudi
nchini. Haina matumizi. Ingekufaa.” “Siwezi kuendesha gari nzuri zaidi
ya Sandra. Huwa hapendi kupitwa na yeyeote pale kati yetu. Tunamchukulia
kwa tahadhari sana. Aje aone naendesha gari anayoitamani na hana uwezo
nayo! Italeta shida sana. Halafu mimi mwenyewe naishi kwa watu. Wakiniona na
gari ya thamani hivyo!”
“Sikujua kama unaishi kwa watu!” “Sio
kwa watu baki. Ni kaka yake mama. Mjomba na familia yake. Alitusaidia mimi na
kaka. Kaka alipooa akaondoka, ndio nimebaki mimi na binti zake. Napo nahisi
muda wangu wa kukaa hapo umeshaisha, natakiwa kuondoka ila navuta
tu.” “Kwa nini hutafuti kwako?” Akanyamaza.
“Pam?” “Nina majukumu mengi. Kaka kabla
hajaoa ndiye aliyekuwa akimsaidia mama. Sasahivi ameoa, mkewe hataki
kabisa. Anasema hawawezi kusaidia tena mtu. Na wao wanajijenga.
Na ubaya au uzuri, kaka alimuoa yeye akiwa amejenga. Kwa hiyo ni kama kaka
amehamia kwake, hana usemi sana. Yeye ndio anaongoza mambo ya familia.”
“Kwa hiyo kila pesa ninayopata najibana
kumsaidia na mama anayetunzwa huko kwa bibi na babu.” Kidogo akaibua maswali kwa Mill. “Naona nikianza kupanga, hapa mjini
ambapo maisha ni magumu, nitamaliza kidogo ninachoingiza hapo
ninapofanya kazi kwa Sandra na Jerry! Na ndio imekuwa kisingizio changu
wakati wote kwa shangazi anapotaka nihame, nipishe chumba kwa binti zake.”
“Sasa nikianza kuonekana na gari hapa
kwa shangazi, itazua maswali. Atalalamika akisema nakataa kuhama kwake ili
nijitajirishe wakati naendelea kuwabana hapa. Zaidi binti zake ninao
tumia nao chumba. Sijui kama unanielewa?” “Nahisi nimekuelewa kwa sehemu.
Pole.” Akamsikia akicheka.
“Sio mbaya kwa kiasi hicho. Nipo sawa
ila na mimi nina malengo yangu. Sitaki kutoka hapa kwa shangazi kwa haraka
kabla sijajiandaa vizuri. Nitakuwa sawa tu juu ya usafiri. Usiwe na
wasiwasi.” “Basi jua nina wasiwasi. Acha nifikirie nijue chakufanya. Ila nina
swali juu ya mama.” Akamsikia amenyamaza.
Pam aliona historia yake ni ya aibu asije kudharaulika
na Mill ambaye ni mgeni kwake. Au asije akaiga na kumfanyia na yeye. Akaamua
ayafiche moyoni na kumshangaza Mill. Mill asijue ni makubwa na mapana
yaliyomfanya Pam kuchukia wanaume na kuwaona kama nyoka. Aliwachukia wanaume kupita
kiasi yaani huyo Mill alimgusa kwa tofauti ndio sababu aliweza hata
kuzungumza naye.
~~~~~~~~~~~~~~
Ipi nayo
historia ya Pam?
Inaendelea…
0 Comments:
Post a Comment