Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At Firs Sight - Sehemu ya 20. - Naomi Simulizi

Love At Firs Sight - Sehemu ya 20.

Kwa kuwa Mina aliacha kuendelea na shule sababu ya baraka ya ndoa, ikaja baraka ya mtoto, mtoto wake alipofikisha tu mwaka, akamkumbushia Andy swala la kurudi shule. “Naona na mimi nirudi shule.” Andy mwenyewe akashangaa. “Bado unataka kusoma!?” “Miaka miwili tu! Nitasoma Andy. Acha tu nisome. Mama ameniahidi kunisaidia mtoto siku za darasani wakati ananitafutia msichana wa kazi.” Bila shida, na kwa kuwa pesa ilikuwepo, Mina akaanza shule.

Mtoto huyo wa Mina na Andy, ungempenda. Hajui kukataa watu na pia hakuwa mlizi. Ilimradi umpe maziwa, basi atazunguka na chupa yake, akiwa na usingizi ukimuweka kitandani kwake bila shida, atalala. Hilo likawa na faida na hasara kwa huyo mtoto na sehemu wanayoishi, katikati ya jiji kwenye mengi.

Wasichana wa kazi wakawa wakimpuuza sana. Mina akitoka tu kwenda chuo, akiwaachia mtoto, na wao wanaondoka. Wanampa huyo mtoto maziwa, wanamuweka kitandani kwake, na wao wanaondoka na kumfungia ndani. Wakawa wakimpuuza huyo mtoto hawamjali. Afya yake ikazidi kudhorota Mina asijue sababu, maana akirudi anamkuta mtoto msafi na msichana wa kazi yupo.

~~~~~~~~~~~~~~

Siku moja darasa la mchana la Mina liliahirishwa. Akaingia vipindi vya asubuhi tu na kuamua kurudi nyumbani. Alifika akakuta nyumba imefungwa. Kwa kuwa alikuwa na funguo ya akiba, akafungua. Alimkuta mtoto wake anaongea kitandani. Msichana wa kazi hayupo.

Akamtoa na kumsafisha. Hapakuwa hata na chakula kilichopikwa. Akapika na kumlisha mwanae. Akamuogesha kabisa, bado msichana wa kazi akawa hajarudi. Akiwa amemlaza mtoto wake kitandani kwake yeye akijisomea, akasikia mlango unafunguliwa. Akaangalia saa. Akaona ni muda karibu na ule aliomwambia yule msichana atarudi siku hiyo. Akaumia sana.

Basi hata ajali, hakujali kwa kuwa hakujua kama Mina yupo ndani. Akaanza kuzungumza na simu yake bila hata kuingia na kumtizama mtoto. Akamsikia yupo jikoni, ndipo akahisi ameshituka baada ya kukuta chakula. Pakatulia.

Mina akajua ameshajua kama yupo ndani. Akatoka.  “Hivi ndivyo unavyofanya kila siku ninapokuachia mtoto wangu?” Mina akamuuliza taratibu tu. Akajaribu kujitetea uongo wa wazi kabisa, jioni ileile Mina akamuondoa.

Baraka & Jukumu Lake.

Na hivi kila baraka huja na majukumu yake. Kuitunza hiyo baraka ili idumu, basi ndicho kilichowapata wanandoa hao. Ila kwa swala la mtoto ikawa Mina ndio anahangaika mwenyewe. Baraka ya uchumi, Andy ambaye akili alishazamisha kazini, ili ya nyumbani yasiharibike, pesa isipungue ila kuendelea kuongezeka. Kwa hiyo yeye yake yakawa yakimuendea vizuri huko kazini. Hana kipingamizi. Akabakiwa na maisha yake, na kazi tu. Anadamka asubuhi, anawahi kazini mpaka usiku anaporudi nyumbani. Yanayoendelea hapa katikati nje ya ulimwengu wa kazi, hayakumuhusu moja kwa moja japo ni familia yake.

Shuguli ikabakia kwa mkewe. Shida za wasichana wa kazi kwa malezi ya mtoto wao, na shule inayo endelea. Mina akaendelea kupambana kwa juhudi zote ili chochote kisikwame. Msichana wa kazi akisumbua, mama Ron na mama Ruhinda ndio wanahusika na Ayan ili shule ya Mina isisimame na asilemewe. Na yeye akaweka juhudi na uaminifu. Mwaka wa kwanza wa Mina ukaisha, Ayan akiwa na miaka miwili tayari.

Jamii inayo wazunguka ikizidi kuona mafanikio kwao. Kwa upande wa kina Mina, kuona Mina ametulia kwenye ndoa yenye pesa na mume mwenye juhudi ya kazi, anamtoto na amerudi shule. Huo ukawa muujiza kwa mama Ron ambao hata malaika angeshuka kutoka mbinguni na kumwambia huko mbinguni hakuna Mungu, asingeamini. Na kwa upande wa kina Andy, ni kweli alifanya vizuri. Akafanania na kina Ruhinda kabisa. Na akawa ameleta faraja ya huyo mjukuu. Watizamaji jamii wakazidi kushangulia ndoa hiyo. Maisha yakaendelea

~~~~~~~~~~~~~~

Utendaji kazi wa Andy ukawa mzuri SANA. Andy muaminifu na mchapa kazi haswa. Sifa yake ni kama baba mlezi wake alivyosema. Hataki jambo limuharibikie mkononi. Jambo alilotabiri yule baba mlezi, ikawa tofauti. Si Mina, uaminifu akaweka kwenye KAZI. Usingemkuta Andy akizembea kazini. Alichapa kazi vilevile kama alivyokuwa mseja.

Hajui Mina anaendeleaje kibinafsi wala maswala ya mtoto hayakuingilia kazi yake kabisa. Alipomuona Mina ameshikilia ya familia, yeye akazidi kuzama kazini na kuwa mfano mzuri sana mpaka akachaguliwa kwenda kujaribisha kufungua tawi Dodoma ili akifikia idadi kadhaa ya wateja fulani, kampuni ifungue huko tawi jingine. Na yeye ndio akaahidiwa ikifanya vizuri, atapewa Zone/kanda ya kati.

Baraka Zikazidi Kumiminika.

Mina anafanya vizuri CHUONI, Andy naye anafanya vizuri sana  KAZINI na mshahara kuongezeka, huku mtoto wao akizidi kukua. Akiwa yupo mwaka wa pili chuoni, mumewe akaanza safari za Dodoma huko kuliko ongezeka baraka. Wanao wazunguka wakaendelea kufurahia mafanikio yao, wasijue kinachoendelea ndani ya hiyo ndoa.

Walishaanza kuishi kama WAPANGAJI waaminifu. Walianza kwa ahadi nzuri tu. “Usijali Mina. Nikifanikiwa huko, utasahau shida zote. Tutakuwa tunazungumzia mshahara wa mamilioni mengi mnoo.” “Naomba usinisahau Andy!” “Ni kwa muda tu.” Shida ya Mina ni watu kama alivyozoea kwa mama yake, maisha ya umoja si mapesa.

Lakini Andy yeye amelelewa kwenye mafanikio makubwa. Halafu Lora alishamuingia akilini, alitaka kuhakikisha alichomwambia Lora hakitimii kwake. Ayan anakua na kukutana na baba aliyefanikiwa  SANa kwenye maisha si kama alivyosema Lora.

Akaongeza juhudi kazini. Safari za Dodoma zikaanza huku akijitahidi kuwepo nyumbani siku za weekend. Mina akabakiwa na jukumu zito la mtoto asiye na msichana wa kazi na shule hiyo ya mwaka wa mwisho.

~~~~~~~~~~~~~~

Andy akawa na pesa nyingi sababu ya marupurupu mengi anayokuwa akilipwa kazini zikiwepo hizo safari, malazi ya kila siku huko aliko Dodoma, maana bado alikuwa ni mwajiriwa wa Dar. Kwa hiyo huko Dodoma ikawa ni kama anatumwa na kampuni, kikazi. Lazima kugharamiwa. Na mengine mengi. Kwa hiyo kweli PESA ilikuwepo. Akaona aendeleze nyumba yake ya Kigamboni.

Hiyo nayo ikaongezeka kuwa BARAKA ingine, iliyohitaji muda wake PIA. Kusimamia ujenzi. Siku za jumamosi anaporudi Dar kwa familia, karibu siku nzima yupo kwenye ujenzi wa nyumba yao, Kigamboni. Akirudi amechoka. Wakati mwingine Mina anaporudi na mtoto nyumbani wanamkuta amelala kwenye kochi, hoi.

Akiwa macho napo simu haziishi. Atapigiwa simu na wafanyakazi wa Dodoma kwenye hilo tawi jipya alilofungua. Wakiuliza maswali na yeye kufuatilia kwa karibu sana  kujua mambo yanavyoenda huko, ili KUSIHARIBIKE kitu. Huko Dodoma kukawa kukipewa kipaumbele cha hali ya juu. Iwe kwa uwepo wake au kwa simu awapo nyumbani. Halafu napo bado huku wakishindana na wajenzi wa nyumba yao huko Kigamboni, wakitaka hili na lile.

Mina akianzisha mazungumzo, akitaka kuzungumzia jambo na mumewe, simu itaingilia. Pakawa na fujo ya namna yake, ya maendeleo. Hakuna utulivu wakifamilia. Andy akaweka kipaumbele kwenye mambo yake na yao kama huo ujenzi wa nyumba YAO, kazi ambayo inasadia familia kiuchumi maana Mina hakuwa na kazi, yeye ndio breadwinner. Ikawa hekaheka ya maendeleo katikati yao akitaka jambo katika HAYO lisiharibike, Mina akimwangalia tu.

Akiwa Dar kwa familia, hajulikani kama yupo nyumbani au bado yupo Dodoma kazini. Yupo nyumbani kimwili lakini mawazo na muda wake wote vipo Dodoma kwa simu kama si Kigamboni.

~~~~~~~~~~~~~~

Wazungu wanausemi wa wapenzi wakiwa kwenye hali hiyo, ku grow apart. Ikawa dhahiri sasa, wapenzi hao wakawa wapangaji wenye jukumu la kuwalazimu kuishi nyumba moja wawapo mji mmoja. Na Andy naye ikawa kama anayejitahidi tu kuwepo nyumbani, lakini sio kwa wakati huo. Ikawa kama lipo jambo la msingi na muhimu sana, pengine angemaliza kwanza, ndio angetulia. Ikawa anakimbizana nayo. Busy kuanzia asubuhi mpaka usiku. Jumapili wakitoka kanisani, wanaenda kujumuika na wenzao kwa wazazi mpaka jioni. Usiku au jumatatu asubuhi anarudi Dodoma.

Mina akajaribu kuzungumza naye, nalo HILO halikufanikiwa kufikia mwisho, kwani simu ya kikazi ikaingia ambayo ilimlazimu Andy kutoka kwenda kuzungumza nao akitoa maelekezo.

~~~~~~~~~~~~~~

Siku hiyo ya birthday ya mzee Ruhinda, watoto wote walikuwepo na Andy akamuahidi Mina atarudi ili awe naye kwenye sherehe. Mina akaenda saluni, akatengenezwa vizuri. Akampigia simu Andy. “Naondoka na ndege ya mwisho ya huku.” “Utawahi?” Mina akauliza kwa wasiwasi. “Nimekwambia nitawahi Mina! Au unafikiri na mimi nafurahia haya maisha?” Andy akiwa amechoka, hajala siku nzima, halali vizuri, mambo mengi, akaanza kumfoka. Mina akanyamaza.

“Au wewe ndivyo ulivyokuwa ukifikiria kwamba nafurahia hivi?” Kimya. “Mimi nahangaika kwa ajili yetu wote! Nilipokwambia nakuja huku kikazi ulifikiri nipo huku kustarehe? Nina nyumba ambayo najenga ambayo inabidi kazi hii hii ndio nijitahidi nilipwe ili iweze kukamilika. Shule yako pia inahitajika pesa. Bado wewe mwenyewe na mtoto mnahitaji pesa. Hapo usisahau gharama za hapo nyumbani ili maisha yenu ya kila siku yaende vizuri. Chakula, maji, umeme, kodi na mambo mengine yote ni MIMI. Ulitaka nifanye nini?” “Mimi sikutaka unihesabie jinsi ninavyokugharimu Andy na wala sikukupigia ili nikuudhi. Lakini kumbuka hii ni week ya pili haupo nyumbani!” Mina akaongea taratibu tu.

“Ndio nakuuliza unafikiri mimi nafurahia haya maisha?” “Mimi naona tuagane Andy. Huko unakokwenda, unataka kuniumiza bila sababu. Hii ni birthday ya baba yako. Uje, usije ni juu yako.” “Kwa nini nikuumize sasa!? Mimi nimezungumzia uhalisia tu.” “Kazi njema Andy.” Mina akakata simu.

~~~~~~~~~~~~~~


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment