Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 19. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 19.

Mwaka wa mwisho wa shule hiyo ya unesi. Ikiwa imebakia mihula minne amalize, mzee wake akaanza kuuguwa zaidi kiasi cha kushindwa kwenda kazini na kufanya shuguli zake, na kuwepo tu ndani. Mill alishaanza kulemewa ada, akawa akifanya kazi kwa nguvu ila akiwasiliana na baba yake mara kwa mara. Hakutaka Mill aache shule na kazi arudi nyumbani. “Unataka kurudi huku halafu tuje tukwame wote? Huna utakalofanya. Tuliza mawazo shuleni na kazini.” Ndio ukawa usemi wa baba yake.

Alipopata simu za wadogo zake wakimtaka arudi nchini, akaamua kurudi kuja kuona linaloendelea. Pam alimpokea uwanja wa ndege, moja kwa moja akampeleka nyumbani kwa baba yake. Hakutaka hata kukaa, alichofanya Mill ni kumbeba na kumkimbiza hospitalini. Kwani alikuta kuanzia miguuni mpaka magotini amebadilika rangi kama ambaye damu imeacha kutembea chini. Mguu umeoza, na tumbo limeanza kujaa.

 Akalipia chumba cha binafsi ili baba yake alazwe hapo. Hakutoka huko hospitalini, mchana na usiku, alikuwa na baba yake. Kamila na Mike wakipeleka vyakula. Na Pam kwenda kushinda naye huko kuanzia asubuhi mpaka usiku akiwa amechukua likozo kama siku zote alivyomzoesha Mill. Akirudi nchini wanajifungia, fungate. Ila safari hii ikawa wanashinda wote hospitalini wakiuguza. Baada ya siku nne mbeleni, mzee akafariki. 

~~~~~~~~~~~~~~

Aliporudi kwao baada ya mwili wa baba yake kupelekwa chumba cha maiti, ambako marafiki zake wote, majirani na ndugu walikuwa wakikusanyika hapo kwa msiba wa mzee Mgini, akakuta hali ya fujo isiyo eleweka. Vijana wanataka mali ya mzee, lakini wakijua mzee aliacha maagizo yote kwa Mill, ambaye ndiye mtoto mkubwa. Yeye ndio agawe mali.

“Naombeni tumzike baba kwanza.” Mill akawatuliza. Wakafanya taratibu za mazishi, mama Kenny akiwa na wasiwasi sana, akijua wanae yeye wapo mwishoni kuzaliwa kwa baba yao. Watapunjwa na kaka zao. Mbali na  hiyo nyumba, na maduka ya vifaa vya magari ambako hakutaka kabisa mama Kenny ajihusishe nako, hakujua mzazi mwenzie ana mali gani nyingine maana aliishi naye kama hawara tu hata ndoa hakutaka kufunga na kila wakati alimruhusu kuondoka atakaposhindwa.

~~~~~~~~~~~~~~

Yaani wametoka tu makaburini, na Pam alikuwepo, wakakuta wote wamekusanyika sebuleni, wanamsubiria yeye. “Kwamba nyinyi hamuwezi kusubiri hata kesho?!” “Tuweke tu sawa, bro ili tujue moja. Maana kuna fununu zinasikika kuwa mama Kenny anataka tuondoke, huku Kenny mwenyewe anasema hapa ni kwao wao kwa sababu mama yao ndio amekuwa mwanamke wa mwisho kuwa na baba.” “Mzee alisema maagizo YOTE, wewe unayo. Akifa tu, tukusubiri wewe, utupe hatima yetu.” Mill alichoka kabisa.

“Mill, acha sisi tuwaache mmalizane kifamilia.” Mike akamuaga. “Nawashukuru aisee! Asante sana. Nitawaona baada ya muda mfupi.” Ndugu zake wote wakashangaa. “Sisi tulijua wewe ndio sasahivi utahamia hapa kama kiongozi! Nani sasa atasimamia mali za baba?!” “Maana hapa hakuna mtu atamsikiliza mtu mwingine ila wewe tu.” “Watu watatoana roho hapa bro, kama ukiondoka.” Mill akawatizama na kumgeukia Mike.

“Acha niwatoe.” “Hamna sababu. Au ulitaka tuondoke na Pam?” “Hapana. Huyu namtaka hapahapa nilipo. Ndio mambo ya familia haya. Lazima awepo.” Mike na Kamila wakaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~

“Naombeni mnisikilize kwa makini kwa sababu sitajirudia tena na tena. Na msiniingilie ninapo zungumza. Subirieni mpaka mwisho ndipo muulize maswali.” Wote kimya. Na mama Kenny na wanae pia walikuwepo.

“Najua baba hakuwa amemuoa mama Kenny. Lakini kisheria, mama Kenny ndiye MKEWE anayetambuliwa. Kwa sababu wameishi chini ya dari moja zaidi ya miaka miwili. Na ndiye aliyekuwa na baba mpaka kifo.” Kidogo mama Kenny akapumua kwa nguvu. Kama aliyepata aghueni.

“Ila ni kwa manyanyaso sana bro, ndio maana sisi tulikupigia simu uje.” Mmoja wao akaongea kwa jazba. “Alihama na chumba kabisa, msichana wake mwenyewe wa kazi anasema alikuwa akimnyanyasa sana mzee, anasema ananuka.” “Yaani msichana wa kazi ndiye aliyekuwa akimuhudumia baba kwa karibu, kuliko yeye, mama Kenny. Baba alipozidiwa zaidi, hawezi hata kutoka kitandani, akaanza ukorofi. Hataki kupikwe kama zamani, na akawa anafungia vyakula mpaka aliposikia wewe unakuja, upo njiani ndio akajidai mwema. Muulize, abishe. Tena yeye na mwanae Sheila.” “Unafiki tu kwa kaka Mill ili atuone sisi wabaya, atuchukie. Kwani wewe kilichokuwa kikikushinda kuwa na baba usiku ni nini?” “Haaah!” Wote wakahamaki kwa pamoja.

“Sio mama yenu huyo alitusemea kwa baba kwamba hataki kutuona nyumba kubwa, hatuna ustarabu labda iwe kufuata chakula tu? Tukaona isiwe shida, tukaacha kuingia humu ndani labda mpaka tuitwe na baba au chakula!” Mwingine akadakia. “Tena hata chakula chenyewe mlibadili utaratibu. Mlimwambia msichana wa kazi awe anatuwekea kule nje jikoni kama mbwa vile! Ilimradi tu, tusiingie ndani. Hatukulalamika. Mkaishia nyinyi wawili na mama yenu kuishi humo ndani? Sasa tungerudi vipi wakati nyinyi na mama yenu mlikuwa hamtutaki?” Wakaanza kubishana, Mill kimya.

“Acha tukwambie ukweli bro.” Mill akamtizama huyo mmoja wa wadogo zake. “Yaliyokuwa yakiendelea humo ndani sisi tulikuwa tukiambiwa na msichana wa kazi mpaka ikabidi tukutafute. Hawa watatu, WALIMSUSA baba. Sheila ndio hakuwa akitaka kurudi kabisa nyumbani, hataki kujihusisha kabisa na baba mpaka aliposikia umerudi nchini, umemchukua baba na kumkimbiza hospitalini, ndio akaja hospitalini akijidai alibanwa na shule kumbe alikuwa akikimbia hapa nyumbani. Nasikia alikuwa akisema nyumba inanuka donda la baba.” “Muongo, Kenton. Wananisingizia kaka Mill.” Sheila akaanza kulia.

Wote wakamdaka kumchangia kwamba anajiliza mbele ya Mill ila ni kweli. “Na Kenny ndio nasikia alikuwa hataki hata kuingia chumbani kwa baba. Wote hawa wakawa wanamlazimisha msichana wa kazi kwenda ndani kwake, mpaka yule msichana wa kazi akaja kutoroka. Huyo dada unayemuona hapo hana hata siku tano! Mgeni.” “Na wote tunahisi kilichomuua baba kwa haraka ni NJAA.” Wakaanza kushambuliana kwa maneno. Hawamalizi.

“Twende Pam. Tutarudi wakishamaliza.” Akamshika Pam mkono. Akasimama. Ikaanza kazi ya kumsihi Mill abaki wao wananyamaza. “Sijalala tokea nimefika hapa nchini, na muda wote nilipokuwa nikimuuguza baba hospitalini. Na huko nilikokuwepo sikuwa mapumzikoni. Nilikuwa shuleni na ninafanya kazi. Akili na mwili vyote vimechoka. Sitaki kelele.” “Tunanyamaza.” Wote wakajibu kwa pamoja.

~~~~~~~~~~~~~~

Mirathi aliyoacha baba kwangu, ipo na nitaituma kwenye kundi la familia. Mpaka mwisho nazungumza naye, hakunipa maagizo mengine ya tofauti ya mirathi kwamba anataka kubadilisha. Nilikuwa na baba mpaka dakika ya mwisho. Japokuwa alikuwa na hali mbaya, lakini alikuwa na akili zake timamu. Siku moja kabla ya kifo chake tulizungumza mengi, mpaka tukadhani amepata nafuu, anapona. Muulizeni Pam. Alizungumza sana na Pam kama ambaye hakuwa mgonjwa. Lakini hakugusia kabisa juu ya kubadili mirathi ya kwanza.” Mill akaendelea wote wakisikiliza kwa makini.

“Sasa iwe alinyanyaswa na mama Kenny au la, alikuwa mkewe na HAKUBADILI alichoniambia mwanzo, na mimi NAFUATA kauli ya baba bila kufuatisha HISIA zetu.” Kimya wakisikiliza kwa makini sana.

“Nyumba hii tuliyopo sasahivi hapa, alinikabidhi na hati yake pia, alisema HAPA, nimkabidhi yeye na watoto wake.” Hawakuamini.

Nakuhakikishia hayo si matakwa ya baba ya mwisho, bro.” “Hata kama. Mimi nasimamia tulichozungumza naye siku ya kwanza nimekuja kumtambulisha Pam kwa baba, akaniomba kikao. Na mama Kenny pamoja na Pam walikuwepo akinitaka tukutane naye siku inayofuata. Baba alikuwa ameshaandika mirathi yake, akaomba nimsaidie kuisimamia. Nilichomuomba mimi ni kunitoa kwenye mirathi yake.” Wote hawakuamini.

“Kwamba wewe bro, hutaki kitu kabisa!?” “Mimi nimeshachukua urithi wangu kwa baba. Na yeye nilimwambia kabisa, sihitaji kitu tena kutoka kwake. Mzee amenisomesha nje ya nchi kwa garama kubwa sana, bila kulalamika. Shule sijaimaliza, lakini palipobakia namuamini Mungu atasaidia.” Wote kimya.

“Sasa basi. Kwa kuwa undugu wenu na mama Kenny ulikuwa ukishikiliwa na baba, na kwa sasa hayupo, baba ametaka kujengwe ukuta hapo, kutenganisha nyumba ya mama Kenny pamoja na wanae, na hizo nyumba tatu za nje ambazo amesema zitabakia kwenu kama alivyowagawa yeye mwenyewe.”

“Hamtatumia geti moja na mama Kenny. Anataka yeye geti lake liangalie kwa ule upande mwingine, nyinyi mbakiwe na geti hilo la sasa. Eneo la Goba, alinipa mimi lakini litabaki la familia. Atakayetaka kuliendeleza, si kuuza, anitafute akiwa na mipango inayoeleweka, nitamkatia sehemu yake.” Kimya.

“Maduka yake yote matatu ya vifaa vya magari, alishauri myaendeleze ibakie kuwa ajira yenu nyinyi, bila Kenny wala Sheila, kwa kuwa mlikataa shule.” Wote kimya.

“Mnanielewa Sheila, Kenny na mama Kenny?” “Kwamba wanangu hawana kitu kwenye yale maduka!?” Akauliza kwa kulalamika. Wadogo zake wakataka kuanza kumchangia, Mill akawakatisha.

“Nisikilize mama Kenny. Narudia kufanya kile baba alichoniagiza. Kenny na Sheila kama wakikazana, wanauhakika wakumaliza chuo na kupata ajira ya kuwaingizia kipato.” “Wasipopata?” Akauliza tena mama Kenny. “Itakuwa bahati mbaya.” Mill akamjibu bila wasiwasi na kuongeza swali kwa ukali kidogo.

“Hivi unajua katika watoto wa baba wote, ni watoto wako tu ndio wamebahatika kupata eneo au nyumba kubwa kuliko wote?” “Afadhali umelitambua hilo bro! Tunashukuru.”

“Tafadhali kuwa muungwana mama Kenny. Wengine wote wanabakia kwenye nyumba ndogo, wakijibana. Watoto wako ni wawili tu, umebakishiwa jumba lote hili lenye vyumba kibao na wamesomeshwa! Ulitaka baba afanye nini zaidi?!” “Naomba tusikosane Mill. Yalikuwa ni maswali tu. Nimekuelewa na kukushukuru kusimamia haki. Maana ungeweza nipunja na wala nisijue. Mungu akubariki.” Akajirudi kwa haraka. Mill akamtizama na kuendelea.

“Swala la maduka naomba niweke msisitizo nikimalizia wosia wa baba. Ameshauri myaendeleze iwe ajira yenu nyinyi wote mkigawana majukumu kwa kuelewana mkisimamiwa na Kenton ambaye baba amesema anaufahamu wa yale maduka, anajua mambo mengi kwa kuwa alikuwa akifanya kazi chini yake kwa muda mrefu.” “Sio kwa kukukata bro, au kukupinga. Lakini wote tunajua Kenton ni cha pombe na hajiwezi kwa swala la wanawake. Akinywea pombe na kuhonga pesa yote ya mtaji.” Hapo wote wakachangia Kenton akibisha.

“Msijidai watakatifu mbele ya bro. Nani asiyekunywa kati yenu, na nani mwenye mwanamke mmoja kama bro! Baba mwenyewe alisema ni yeye peke yake kwenye ukoo mzima, amevunja rekodi. Mbona asiwataje nyinyi?” Kenton akawajia juu ila wote wakamkataa.

“Hapana bro! Katika hilo tunaomba utusaidie. SIO Kenton.” “Ndipo ninapotaka kumalizia wosia wa baba. Sio kwamba yeye ndio atasimamia peke yake, ila awasadie kuwapa muongozi. Lakini baba alisema, mkishindwa, mniambie, tuuze, mgawane pesa. Ndipo ninapokuja ushauri wangu mimi.”

“Jamani kuna uhalisia wa maisha mbele yenu. Wakuwalipia umeme na maji hayupo. Hizo nyumba hapo ni nzuri kama zilivyo kwa sababu baba alikuwa akizikarabati mara kwa mara. Naungana na baba. Biashara hizo, mjitahidi kwa kila namna, mziendeleze. Wekeni wawakilishi watatu kutoka kila nyumba, wawe karibu na Kenton, na muwe mna vikao kila mwezi, kupeana muendelezo. Kila mmoja wenu awe na uhuru wa kujua pesa inatumikaje. Na kusitolewe pesa benki bila makubaliano yenu WOTE. Kuwe na zaidi ya watu watatu wa kuweka saini benki ili kutoa pesa.”

“Hapo sawa bro. Ila ikitokea kuna kuzidiwa, utarudi kutusaidia kuuza na kugawana?” “Ndiyo. Lakini bado nasisitiza. Kuuza na kugawana pesa iwe jambo la mwisho kabisa. Mimi nawajua nyinyi. Haitachukua muda mrefu, pesa mtakayogawana yote itaishia kwa wanawake.” “Tutabadilika. Sasahivi tunakua.” “Basi endelezeni yale maduka. Kuliko kuuza, ni bora mkishindwana nyinyi wote, basi mgawane kwa nyumba. Kila nyumba iendeleze duka lake na kujipanua zaidi. Sio mkipata faida mnahonga! Panueni biashara, ndio urithi wenu wa MWISHO. Na wengi wenu mna mama zenu. Kueni kiakili, mtunze na mama zenu. Swali kabla sijaondoka?”

Mama Kenny akaonyoosha mkono. “Kuna pesa za mafao na salio benki. Hizo zinakuaje?” “Samahanini nilisahau. Pesa ya benki na mafao yake yote, aliniambia ameacha utaratibu nikachukue. Hapatakuwa na usiri. Nikishajua salio zima. Nitaweka kwenye kundi la familia. Tutajenga ukuta kutenganisha hizi nyumba. Zitakazo baki, baba ameomba niwagawie sawasawa.” “Hata mimi?!” Mama Kenny akashangaa sana.

“Kwamba wewe umefanyaje kwa mfano?!” Mmoja wao akauliza. “Mimi nilikuwa mke wa marehemu jamani! Kwamba mafao yake nilitakiwa nipewe mimi.” Wakaanza kumcheka. “Naombeni mnisikilize jamani! Baba amekufa hana furaha na maisha mnayoishi nyinyi.” Akawaonyeshea wadogo zake.

“Amesema kwa wazi kabisa. Maduka aliyowaachia, na mkipata hiyo pesa, acheni kuitumia kwenye pombe na wanawake. Ndio msaada wenu wa mwisho kutoka kwake. Ameomba MJIENDELEZE. Na naomba kuwakumbusha tena. Kuanzia kesho, hizi nyumba zinatengwa ramsi. Japokuwa hapatakuwa na uzio, lakini umeme na maji kila nyumba itajitegemea.”

Hakuna wakuwatunza tena kama watoto wadogo. Na mkumbuke inachukua muda kwa taratibu zote kukamilika kupata mafao ya baba. Anzeni kuchangamka. Kwahiyo mama Kenny, mafao ya mzee mtagawana na vijana wake.” Akaonekana kutoridhika.

“Twende Pam.” Wakasimama. “Nikitaka nianze ujenzi wa huo ukuta hata kesho?” “Tunza risiti, pesa ikitoka nitakurudishia.” “Ndio mwanzo wa kutengeneza risiti za uongo. Bro, hapo HAPANA. Sisi tunamjua mama Kenny.” Wakaanza kubishana. Mill akawa kama anayefikiria.

“Mimi nikitafuta fundi aanze huo ujenzi, nikaomba Kenny na watatu wenu kutoka kila nyumba msimamie, itakuwa sawa?” Ukaanza ubishi mwingine tena. Hata hao wanne hawaaminiani. Ila zaidi hawamtaki Kenny. Kenny akasema ni wivu tu. Wakabishana hapo. Mill akahitimisha. “Mimi nitasimamia huo ujenzi wa ukuta. Mnashida katika hilo?” “Labda mama Kenny na wanae. Sisi hatuna shida. Baba alishatuambia maagizo yote atakuachia wewe na utaendeleza hii familia. Sisi hatuna shida na wewe.” Wengine wote wakakubali kasoro mama Kenny na wanae wakanyamaza.

“Jamani, usiku mwema.” Akataka kuondoka akawa kama amekumbuka. “Kabla sijaondoka hapa, nataka kujua kama kati yenu nyinyi kuna aliyeacha kitu humu ndani kwa mama Kenny. Maana kuanzia leo, mtaingia humu ndani kwa kukaribishwa na mama Kenny na wanae. Kama una kitu chako, chukua, mtoke hapa kabla sijaondoka.”

“Kwamba tunaanza leoleo?!” “Chakula?!” Mwingine akauliza kwa kuhamaki. “Nyinyi si mmetaka kugawana leo kila mmoja apewe chake? Sasa nishawapa. Mnachosubiria hapa ni nini na nyinyi wote hampatani? Nataka kwenda kupumzika kabisa. Sio nafika huko zinaanza simu za nirudi kuamua ugomvi. Tushamzika baba. Wageni washaondoka. Waliobaki hapa ni ndugu wa karibu. Na wenyewe kesho au kesho kutwa nitafanya utaratibu waondoke. Msiba ushaisha. Haya na nyinyi naombeni muwapishe hapa.” Wakaanza kutoka mmoja baada ya mwingine mpaka mwisho.

“Nakushukuru sana Mill. Mungu atakulipa. Lakini jua wazi sikuwa nikimtesa baba yenu.” “Mimi sio mtoto mdogo mama Kenny. Usiku mwema.” Akamjibu hivyo kwa ukali kidogo na kuondoka na Pam wake.

~~~~~~~~~~~~~~

Mill aliondoka nchini akijua maisha ndio yamembadilikia, lazima afanye kitu cha ziada. Pam anamtaka na ndiye aliyeachiwa baraka zote za kusimama kama mama Mgini. Baba yake alizungumza sana na Pam akimtambua kama mwanamke wa kipekee katika ukoo wao kufikishwa alipofikishwa yeye na kina Mgini. Ile ndoa ya kijijini kwao kina Pam, mzee Mgini aliitambua kama ni ndoa KAMILIFU, kwani ya kanisani Mill alitaka wakafunge nchini Marekani ili watambulike kiserikali kama mke na mume iwe rahisi kumsaidia kuishi huko kwa urahisi.

Hapo mzee Mgini amekufa akijua ameshamuozesha kijana wake. Wanasema mahari huwa haimalizwi lakini mzee Mgini yeye alimaliza kwa kina Pam, akimwambia babu yake analipa yote ili ikumbukwe daima kuwa Pam ni Mgini na amefunga milango ya mwingine kuja kumlipia mahari huyo Pam. Kwamba wasije pokea mahari nyingine tena ya Pam, yeye ameshamaliza.

Akiwa mahututi hospitalini akamsihi asije mbadilikia kijana wake. Alimsifia sana Mill kwa Pam, akimuhakikishia Pam kuwa Mill amemaliza kwake, ni yeye tu kusimama kama mke zaidi wanapokuwa mbalimbali. Akamuomba amsaidie Mill kusimama na familia aliyoacha. Kwa hiyo Mill anaondoka nchini akiwa ameacha mke kabisa wala si mchumba.

Mbali na jinsi ya kumtoa Pam nchini, bado mzigo wa shule aliokuwa akimsaidia kubeba baba yake ndio umeshakuwa wake. Na Mill alikuwa akilipa ada kama international student, ada kubwa haswa.

Alihangaika kutengeneza njia ya kumfanya awe raia, IKASHINDIKANA. Ikabakia njia pekee ya kuoa mzawa wa Marekani ambaye angempa makaratasi/ kuja kuwa raia baadaye. Akajaribu kwa udi na uvumba kumtafuta mmarekani atakaye mlipa pesa ili amuoe kisheria, abadili status, lakini napo AKASHINDWA. Malengo makubwa, mazuri, lakini yakakumbana na UGUMU mkubwa sana.

~~~~~~~~~~~~~~

Safari ya mwisho kurudi Tanzania, Mill hakuwa na furaha kabisa. Wazi alijua cha kwanza atapotea nchini kwa kipindi chote anachoshugulikia kuwa raia huko nchini Marekani. Hawezi kutoka mpaka mambo yake yakamilike. Hata hivyo itamlazimu kuongeza juhudi ili kuhakikisha aharibu status yake ya kuwa mwanafunzi. Lazima ahakikishe anayo pesa yakutosha. Mchezo wa kurudi nchini kwa Pam, mara kwa mara lazima kupunguza.

Ikabidi awe mkweli kwa Pam, ila hakumwambia kama itabidi kuoa huko, ili yeye awe raia, kisha amkaribishe na yeye kiurahisi. Alimwambia itamchukua muda kurudi tena, inabidi akapambane. Kutengeneza pesa, yakuweza kuishi huko, alipe ada kama mwanafunzi wa Kimataifa kisha pesa ya kutosha kubadili uraia. Pam akaelewa akimuhurumia.

Kuagana Kwa Mara Ya Mwisho Kwa Pam & Mill.

Safari hii ni kama walikwenda fungate kabisa. Walijitenga na kila mtu, wakaenda kujifungia kwa majuma mawili mfululizo wakiliwazana, huku Mill hana raha! Anamuachia nani Pam wake? Je, atafanikiwa kuja kurudi kumchukua? Maana tokea uhai wa baba yake, walihangaika sana na baba yake kumtoa Pam nchini wakitumia benk statement ya mzee Mgini, lakini mara zote alishindwa kupata Visa.

Leo anaondoka bila tumaini, hajui anarudi lini! Na Pam naye alijua fika kazini analazimishia tu, lakini hawamtaki. Sandra mwenyewe alikuwa akimtafutia sababu kila wakati. Ikawa kuagana kwa uchungu, kila mmoja hajui hatima yake.

Baraka Za Ndoa Na Wajibu Wake.

Ndoa ya Mina na Andy ikaendelea kuonyesha matunda yakutamaniwa na wengi. Walishajaliwa mtoto huyo wa kiume ambaye ndio mjukuu pekee wa kiume kwa familia ya Ruhinda. Wakati Ayan akiendelea kukua vizuri, baba yake naye akapandishwa cheo kazini. Furaha ikazidi kuongezeka, ila ubusy nao UKAZIDI kuongezeka.

Kila baraka unayopewa, inakuja na jukumu lake. Basi ndio ikawa Andy na hicho cheo. Ile tabia yakurudi mchana nyumbani kwa chakula na penzi kwa Mina ikaanza kupungua kwa kasi kubwa. Maana wakati mwingine akirudi nyumbani Mina naye anashugulika na baraka nyingine, mtoto.

Alipokuwa akijitahidi kurudi nyumbani mida ya mchana anamkuta Mina naye anakuwa na kazi za mtoto. Na yeye Andy anakuwa na majukumu yanayomsubiria kazini, hawezi kukaa nyumbani muda mrefu. Matiti aliyozoea kuchezea atakavyo, yakageuka chakula chakutegemewa na mtoto. Penzi la harakaharaka alilokuwa akipewa mchana arudipo nyumbani, likawa likishindikana, Mina anakuwa na mtoto au kunakuwa na wageni wakumsaidia mtoto. Zaidi mama yake au mama mkwe.

Uhalisia wa maisha ukaanza kuchukua sura halisi. VINGI vilivyokuwa vikiwaweka karibu kama wapenzi, vikaanza kukosa nafasi. Kila arudipo nyumbani, habari ni ileile. Kama hataishia mikononi kwa mama yake, basi mama mkwe au Mina anabembeleza mtoto.

Baada ya muda Andy AKAACHA kurudi nyumbani kwa chakula cha mchana. Ikawa akitoka asubuhi ni mpaka jioni ndipo anaporudi. Ila mawasiliano hapo katikati ya siku yalikuwepo.

Andy alimnunulia Mina gari nzuri tu. Undugu na ukaribu na kina Ruhinda ukawa mkubwa. Mina kwenda na Ayan nyumbani kwa wakwe zake bila Andy likawa jambo la kawaida sasa. Anaweza kuanzia kwa wakwe zake Msasani. Atasalimia hapo akiwa na mtoto. Mzee Ruhinda acheze kidogo na mjuu, ndipo aende Tegeta kwa mama yake na Ron.

Mina akawa wa viwango. Anarudi nyumbani kutembea na mtoto, akiwa na usafiri safi pamoja na zawadi kemkem kwa mama yake. Mama yake akiwa na safari zake, basi Mina atakwenda kumchukua na kumsindikiza. Waliokuwa wakimsema Mina, wakafungwa midomo. Akaonekana amefanikiwa haswa, lakini majukumu yakiwatenga wanandoa hao.

~~~~~~~~~~~~~~

Maisha bila Andy yakaendelea. Uzazi ulishaisha muda mrefu tu, akabaki yeye tu na mtoto nyumbani bila Andy, na bila wakina mama wakumsaidia. Maana mtoto ashachangamka. Kina mama/bibi za Ayan wote waajiriwa. Na Andy lile pengo la kurudi mchana alishaziba na majukumu.

Upweke ukazidi kwa Mina. Wakati wengine wakiwapongeza kwa maendeleo ya kiuchumi, zaidi kupandishwa cheo mumewe na kuhamishwa makao makuu, kwa Mina ikawa tofauti. Akabaki na picha ile ya ndoa ya kabla ya kuzaliwa Ayan, na Andy yule ambaye hakuwa na majukumu mazito.

Kupishana hapo nyumbani likawa jambo la kawaida. Andy anaweza kurudi usiku tokea alipoondoka nyumbani alfajiri sana, Mina akiwa amelala. Tabia yakuchelewa kurudi nyumbani kutokea kazini ikawa kawaida sana.

Zile siku za jumamosi na jumapili ambazo Andy alikuwa akizitumia na familia, wakati mwingine hata hizo siku za jumamosi anakuwa anahitajika kazini, tena kwa muda mrefu tu. Ila jumapili Andy akawa akijitahidi kuwepo na familia. Kanisani, nyumbani kwa wazazi mpaka jioni. Wakirudi nyumbani wamechoka. Majukumu ya mtoto, tayari inakuwa imeshakuwa usiku. Muda wao, hao wawili kama wapenzi na wanandoa ukawa haupo au ni mfupi sana, pale usiku mmoja anapoomba penzi, basi.

~~~~~~~~~~~~~~

Mina ambaye amekuzwa kwenye kiasi, mali ya kutoshea siku moja, ila yupo na watu anao wapenda, hayo mafanikio makubwa akaanza kuona mzigo. Mpenda kupendwa. Mtaka mapenzi. Ashikwe. Anyonywe hapa na pale. Abembelezwe kama Omar alivyokuwa naye masaa mengi, akazidi kuteseka maana mwenzie anashinda kazini siku nzima mpaka usiku. Akirudi nyumbani, akili imechoka, anataka kupumzika tu. Wakati mwingine hata penzi anaona asamehe ili alale muda mfupi kesho awahi tena kazini. Yeye anashinda nyumbani na mtoto, hana awazalo ila familia tu.

~~~~~~~~~~~~~~

KILA MTU anaingia kwenye ndoa na MATARAJIO yake, na BADO jamii inayowazunguka INAWAPA matarajio yao.

Hutofautiana na si mara zote vinafanana.

Sasa mpaka kutimia matarajio ya WOTE, kwenye ndoa ya wawili hao na uhalisia wa MAISHA Ya ndoa hiyo, ndipo TALAKA nyingi hutokea, au kukiwa na rehema, basi, WAWILI hao hupitishwa kwenye SHULE inayowapa mtazamo halisi wa ndoa YAO, WAO wawili. Na wala SI ndoa kwa ujumla. Ndoa yao wao wawili, yenye msingi wao.

YAPI MAPITO ya hawa Love at First Sight?

Usikose kuwafuatilia.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment