“Subiri kwanza Mina.” Akamkimbilia. “Mwenzio mjamzito
Andy!” “Haiwezekani!” Andy akaanza kucheka kwa furaha. “Andy!” Mina akashangaa
asimuelewe na malengo waliyokuwa nayo juu yake. Akamnyanyua na kumrushia
kitandani. Akaanza kumbusu tumboni, Mina akasikia nguo ya ndani ikishushwa,
akaanza kucheka taratibu akijua mchezo unaofuata sio wakitoto.
Andy alifurahia Mina alijua kwa ufanywaji wake
mapenzi siku hiyo, mpaka akashangaa. Andy alichangamkia mapenzi tena na tena
akimpongeza Mina kwa maneno na vitendo, alipomaliza, akarudi
tumboni. Akambusu tena na tena.
Akakumbuka kisa cha Omar jinsi alivyotafuta mtoto na huyo
Mina, leo bila kutoa jasho ila starehe tu, Mina anambebea mtoto!
Hakuamini. “Nimefurahi Mina! Nimefurahi sana. Na kuhusu shule, vyote
vitaenda tu, wala usiogope.” Wakaweka mipango hapo kitandani Mina
akicheka na kuanza kufurahia mimba sasa.
~~~~~~~~~~~~~~
Mambo yakabadilika, Andy ndio akawa anaamka kuandaa
kifungua kinywa akimtaka Mina apumzike tu. Atapewa penzi zito asubuhi hiyo.
Watakwenda kuoga, Mina atarudi kitandani. Andy anamwandalia kifungua
kinywa kizuri akidai ni chake na mtoto, atampelekea kitandani yeye anawahi
kazini. Kazi ya Mina ikawa kula kulala. Akaanza kupanuka na kuzidi kuiva.
Hana anapokwenda, analelewa kama mgonjwa. Akitoka hapo
yupo na Andy. Kliniki, kanisani na sokoni. Akipata kitu kizuri, basi
atamnunulia na mama yake na kutaka ampelekee kabla hawajarudi nyumbani. Basi
watapita kwa mama yake, watacheka kidogo, yeye na mumewe wanarudi
nyumbani.
Maisha yakawa ya amani na furaha. Akili na macho ya
Andy vyote vipo kwa Mina kitu alichokuwa akikifurahia sana Mina.
Wakitembea mkono wa Mina upo kwapani kwa Andy. Mina akajawa deko lakupitiliza. Hajaongea,
Andy ametenda. Penzi zito likanoga.
Kina Ruhinda.
Mmoja wa mfanyakazi mwenzake Andy alikuwa akibatiza
mtoto kwenye kanisa lile lile ambalo walikuwa wakienda kina Ruhinda. Na wao
wakaalikwa kuhudhuria. Andy akaona kwa kuwa na wao ni wa RC basi na wao waanzie
kanisani kabla ya tafrija. Mina alikuwa
amependeza na kigauni chake na tumbo la mimba ya miezi 8 akiwa amejazia haswa.
Cheko, mkono kwapani kwa Andy wakisogelea jengo hilo
kubwa ambalo ndio kanisa ambalo kina Ruhinda huudhuria wakati wote. Na
wao wakawa wapo kwenye ibada hiyo wakiwa na wao wamehudhuria moja ya ubatizo wa
mjukuu wa rafiki yao.
Kwa kuwa haikuwa ni misa wanayokwenda kina Ruhinda,
Andy hakuwa na wasiwasi wa kukutana nao. Lakini ikawa sivyo.
Wakiwa wanasogelea jengo la kanisa, ana kwa ana
na familia hiyo ya Ruhinda. Tena wote. Wakaduaa. Mina akajirudisha nyuma ya
Andy taratibu kama anayejificha. Pakabaki kushangaana. Andy bila
kupoteza muda. “Shikamooni.” Wazazi wakaitika.
“Hongereni Andy na Mina.” Akaongeza mama Ruhinda. Mina
hakujibu, ila Andy akaitika kwa mshangao kidogo. “Asante! Japo sijui ni kwa
nini!” Bila kusubiri jibu Andy akaendelea. “Anyway niwatakie misa njema.” Akamvuta Mina.
“Karibuni nyumbani Mina.” Mina na Andy wakamgeukia
mama Ruhinda kisha Mina akamtizama Andy. “Asante. Lakini tupo hapa kwa ajili ya
ubatizo wa mtoto wa rafiki yangu. Kwa hiyo tuna mipango tayari.” “Hata wakati
mwingine Andy mwanangu. Karibuni nyumbani. Milango ipo wazi. Umesikia Mina
mama? Karibu sana.” “Asante.” Mina akajibu kwa kifupi tu. Andy akakunja uso
kidogo kama mwenye swali, lakini akashindwa kuliuliza, akaona
waondoke tu. Ndugu zake wengine kimya wakishangaa. Hata baba yake hakuongea
kitu zaidi ya kuitika salamu. Wakaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakati wanatoka, mama Ruhinda akawawahi tena. “Andy!”
Mina na Andy wakasimama na kugeuka. “Tuna chakula chakumshukuru Mungu kwa ajili
ya kaka yako kutimiza miaka 45, jumapili ijayo. Naomba na nyinyi mfike
nyumbani.” Akaongea mama Ruhinda kwa kujihami. “Asante.” Akajibu jibu la jumla
Andy nakutaka kuondoka na mkewe.
“Mina mama, utakuja? Najua tulianza vibaya na
ninaomba unisamehe. Najua sikufanya vizuri na ndio maana nilikuja
kukuona shuleni kukuomba msamaha.” “Mimi nimesamehe mama. Yameisha.” “Asante Mina
mwanangu. Basi nawaombea kila la kheri na nina amini nitawaona nyumbani wewe na
Andy.” Mina akamwangalia Andy, Andy naye akabaki akimwangalia. “Naamini
tutakuja mama.” Mina akajibu huku akicheka kidogo akimtizama Andy. Andy kimya.
“Basi nitawasubiri.” Akajibu mama Ruhinda na tabasamu na kuondoka.
Kwa Kina
Ruhinda Tena.
Jumapili inayofuata Mina na Andy walikwenda kanisani
kwao Mwenge, sio pale walipokuwa wakienda kina Ruhinda. Kisha wakaenda nyumbani
kwa kina Ruhinda. Walikuta watu wengi na kumeandaliwa vizuri tu. Marafiki
wakaribu wa hao kina Ruhinda hapo ndio waliokuwepo hapo. Vikajaa vicheko.
Alipoingia tu Mina na Andy, mama Ruhinda akamuwahi.
Akamfuata na kumshika mkono kabisa. Akamtambulisha kwa
kila mtu akijivuna. Andy kimya akiwatizama. Mina alijawa cheko, Andy
akimwangalia tu. Pongezi zikaendelea kwa Andy kwa mke mzuri na mtoto wanaye
mtarajia siku za karibuni. Gafla Mina akawa ndio jina hapo kwenye hiyo tafrija.
Upendo alioonyeshwa, na kujaliwa, yeye Mina akasahau ubaya
wote.
“Ungependa tufanye babyshower?” Mama Ruhinda akauliza kwa kujihami ila kwa upendo
sana kwa Mina. Mina akamwangalia Andy, akakuta akimtizama. Walikuwa wamebaki
ndugu tu hapo, watoto wakisinzia. “Kama mtaona sawa, tunaweza kuifanya hapahapa
ili kupata zawadi za mtoto.” “Tulishanunua kila kitu cha mtoto. Andy
ameshafunga hata kitanda kabisa. Chumba chake kipo tayari.” Mina akaongea kwa
upole na cheko akimwangalia Andy.
“Hata diaper na baby wipes tu!” Mama Ruhinda akaweka msisitizo. “Tena
mama, tunaweza kuwaambia watu iwe ni zawadi ya diapers na baby wipes
tu. Mnaweza mkapata nyingi wala msinunue mpaka mtoto anafika mwaka.” Akadakia
Paulina kwa mama yake kama kuweka msisitizo. “Kwani umebakiza muda gani
ujifungue?” Akauliza Raza naye akionekana akiwa amehamasika. Mina
akamwangalia tena Andy huku akicheka kama ambaye ameshalemewa.
“Kwani mmeshajua hata mtoto mwenyewe ni jinsia gani?”
Akadakia Devi mme wa Paulina. Wao walikuwa wamekaa sehemu ya sebuleni, wanawake
na hiyo mipango sehemu yakulia chakula. Andy kimya akiwa amekaa sehemu ambayo
wanaonana na Mina vizuri tu. Pakazuka ukimya. Wakisubiri jibu.
“Andy?” Mina akamuita taratibu kama akimtaka yeye ndio
ajibu. “Tunategemea mtoto wa kiume baada ya majuma matatu kuanzia sasa, anaitwa
Ayan. Kama ilivyo maana ya jina lake, ni zawadi
yetu kutoka kwa Mungu. Naomba kwa sasa Mina akapumzike. Amekuwa na siku ndefu
sana. Asanteni kutukaribisha.” Andy akasimama.
Mina akajua ndio wanaondoka. “Asanteni kwa kila kitu.
Nitakwenda kuzungumza na Andy, kisha nitawajulisha.” Mina akaongezea huku
akisimama. Andy akamsogelea. “Pochi na viatu vipo wapi?” Andy akamuuliza huku
akimsaidia kusimama na kumuweka nguo vizuri kama mtoto mdogo! “Viatu nilivua
pale nje kabisa na pochi...” Mina akajaribu kukumbuka. Mama Ruhinda akasimama
haraka kwenda kumtafutia.
“Hongereni sana Andy na Mina. Mungu akujalie Mina
ujifungue salama. Utuletee huyo
Ruhinda hapa. Na sisi tunamsubiria kwa hamu.” Akaongeza mzee Ruhinda. “Asante
baba.” Akaitika Mina na cheko la heshima kidogo. Ndio kila mmoja akatoa tena
pongezi kwa mjukuu huyo wa KWANZA wa kiume kwenye familia hiyo, maana ni
kama palizuka ukimya kwa ndugu wa Andy baada ya kujua ni mtoto wa
kiume.
“Kama mtaafikiana na mwenzio juu ya hiyo babyshower anayotaka kuwafanyia mama yenu hapa, itakuwa njia
nzuri pia ya mama yako kushirikiana na mama hapa, wakafahamiana
zaidi. Na huyo mzee mwenzangu akakaribishwa ramsi nyumbani.
Azaliwe akijua mji wake.” Akaongeza mzee
Ruhinda kwa furaha ya waziwazi baada yakujua mjukuu ni wa kiume, kila mtu
akamuona alivyobadilika ghafla. Maana alikuwa kimya muda wote, gafla akawa
amechangamka!
Mina akamwangalia Andy, Andy akaanza kutafuta pochi ya
mkewe. “Basi nitazungumza na Andy, akikubali nitamwambia na mama, halafu Andy
atawajulisha. Asanteni.” Mina akajibu kwa heshima, mumewe akaipata pochi
pembeni ya kochi alilokuwa amekalia yeye mwenyewe muda wote. “Twende Mina.
Usiku mwema.” Andy akaaga akimshika mkewe mkono kwamba waondoke. “Na nyinyi.”
Wakatoka mpaka mlangoni mama na baba Ruhinda wakisindikiza.
“Nishike mgongoni wakati nakuvalisha viatu.”
Wakamsikia Andy akimwambia mkewe. “Mguu wa kushoto umevimba zaidi Andy! Kiatu
hakiwezi kuenea sasa hivi. Acha nikanyagie tu.” “Ulikumbuka kunywa maji leo?”
Wakamsikia Andy akiuliza taratibu kwa kumjali mkewe. “Nilikunywa. Lakini
sidhani kama yalitosha.” “Itabidi kesho turudi kwa daktari.” “Mpaka kesho
nitakuwa sawa Andy. Usiwe na wasiwasi. Nikifika nyumbani nitainyoosha. Asubuhi
utaona. Itakuwa imerudi kuwa sawa.” Wakabaki wakiwasikiliza.
Andy amebeba pochi ya Mina, anamvalisha viatu
mlango. “Kazana maji Mina mwanangu. Na hivyo ulivyosema ndio muhimu.
Usiining’inize sana.” “Nitajitahidi mama. Usiku mwema.” Mina akaitika na kuaga
tena, wakaondoka.
Babyshower ya
Mina.
Kina Ruhinda wakachangamkia hiyo babyshower mpaka wakawashangaza Andy na Mina! Ikawa tena kama
sherehe kubwa! Walikuwa wanaume na wanawake! Andy na Mina kimya wakijiangalizia
hekaheka. Mzee Ruhinda alitangaza wazi kuwa Mungu amempa mrithi wa kwanza, kitu ambacho
hata Andy mwenyewe hakufurahia. Akaona si sawa kwa kaka yake ambaye
alikuwa na watoto wa kike watupu. Lakini Pius hakuonekana kujali sana. Na yeye
alikuwepo hapo akifanikisha.
Mama Ron, Ron na ndugu wa karibu pamoja na marafiki wa
mama Ron baadhi nao walikuwepo hapo kwenye hiyo sherehe. Mama Ron akijivuna haswa! Mina
aliyekuwa gumzo kwa jamii, ameolewa
pazuri!
Ila hakuwa na imani nao sana. Alimwambia Mina ale kabisa nyumbani ashibe, na akifika pale na kinywaji chake kwenye
chupa. Akamuonya kwenye sherehe nzima asije kula wala kunywa isipokuwa kitu
alichofika nacho hapo. Naye Mina akafuata kama mama yake. Jambo la furaha
likageuka, kujihami.
Andy alikuwa mtulivu na makini katika kila
analolizungumza na kusikia, akimwangalia Mina wakati wote. Marafiki wa karibu
ndio waliokuwepo hapo na pakapambwa vizuri. Ni kweli kulifana na walipata
zawadi zaidi ya walivyotegemea. Zawadi nyingi waliacha hapo, Mina na Andy
walisema hawana nafasi yakuweka na vingi walishanunua. Basi, shuguli ilipoisha
Andy akamchukulia taksii mama yake Mina, wakarudi nyumbani na Ron, wao wakarudi
kwao. Mina alikuwa amechoka.
Mungu Humpa Amtakaye, Na Hakuna Wakumuuliza Kwa
Nini.
Katika wote ambao pengine wangestaili kushika
mimba hiyo ya mtoto wa kiume pengine angekuwa Raza, kama si Paulina. Raza alimtafuta
huyo mtoto wa kiume kwa garama kubwa mno mpaka akasalimu
amri. Alitaka sana kumzalia
Pius mtoto wa kiume, ambaye ni kijana wa kwanza wa Ruhinda. Yeye na mumewe walimsaka
mtoto wa kiume kwa wazi kabisa bila kuficha, wakiomba msaada mpaka wa kitaalumu,
wakiwa tayari kutumia pesa aina yeyote ile ili tu Raza azae mtoto wa kiume.
Raza amesoma na anakazi nzuri tu. Mumewe ndio hivyo. Wakati
akitafuta huyo mtoto wa kiume ndio alikuwa ameingia kuwa miongoni mwa watu
watatu wa msaidizi wa Gavana wa pesa wa Tanzania. Pesa ilikuwepo ya
kumpeleka Raza kwa daktari yeyote yule, popote kule duniani kusaidia
kupata mtoto huyo wa kiume, lakini akaishia mtoto wa pili tena ndio na
kizazi kikatolewa kabisa akiwa anaponea kifo. Habari ya mtoto wa kiume ikaishia hapo, hawakuzungumzia
tena. Pius akaridhika na watoto wake wawili wakike.
Ikawa hivyohivyo kwa Paulina, msomi wa kike wa Ruhinda.
Yeye alishapanga kuingia leba ni mara mbili tu. Akapanga mtoto wa kwanza
wa kiume, na wa pili wakike, BASI. Na mimba zake hazikuwa za kushika
hovyohovyo. Yeye na mumewe walishapanga muda. Wakati wakiwa tayari kwa mtoto wa kwanza, walikwenda kwa daktari.
Wakazungumza naye ili kupata ushauri wa kushika mimba ya mtoto wa kiume. Walifuata
mashariti yote lakini akaishia wakike.
Wapili naye hawakukata tamaa wakijua ndio wa mwisho.
Safari hii wakaongozwa na daktari kabisa. Devi mumewe akiwa mstari wa mbele, LAKINI
akaishia mtoto wa kike na yeye akapatwa na matatizo ya uzazi. Hata
walipotaka kujaribu mtoto wa tatu, ikashindikana. Wakaishia hapo. Na wao
wawili, wakike.
Mzee Ruhinda akapenda wajukuu zake hao wakike, ila
moyoni akijua ndio jina litakufa endapo hao watoto wawili waliobaki, Andy na
Paul wasipopata hao watoto wa kiume. Sasa alipokuja Mina ambaye kwanza walimdharau.
Hakutoka kwenye hali kama zao, halafu kubeba mtoto wa kiume! Akainua FURAHA
ya ajabu kwa Ruhinda mwenyewe, na mkewe pia.
Mina ambaye kwanza hata hakuwa akijua umuhimu
wa huyo mtoto wa kiume. Mumewe wala hakuwahi kuzungumzia anataka mtoto
gani! Kwanza hata hawakuwa wakizungumzia kuanzisha familia ila tu
kufurahia mapenzi. Eti leo anabarikiwa mtoto wa kiume bila hangaika yeyote!
Japokuwa Raza na Paulina hawakusema, lakini mioyoni walijiambia Mungu
ana upendeleo.
~~~~~~~~~~~~~~
Zilikuwa zimebaki siku kama 7 Mina kujifungua huyo
mtoto aliyekuwa akisubiriwa kwa hamu na baba yake lakini pia na bibi na babu
yake. Siku hiyo akiwa amelala na mumewe akaanza kulalamika. “Nasikia maumivu
Andy! Kiuno, tumbo na vichomi. Unafikiri ni sababu ya kukaa sana wakati wa
kusuka?” Andy akakaa na kuwasha taa. “Pole. Kudhani kama ndio uchungu?” Mina
akafikiria. “Bado week nzima,
ndio maana nimesuka hizi nywele ili nikae nazo muda mrefu.” “Basi subiri nikupe
dawa ya maumivu, halafu nikubembeleze ulale. Maumivu yakiendelea hivyo mpaka
asubuhi, nakupeleka hospitalini.” Mina akakubali.
Andy akawa na kazi ya kumsugua kiuno na kumpapasa
kuzunguka tumbo zima. Mina analala kama dakika 20, Andy akisinzia, anamsikia akilia.
“Inauma Andy! Naomba nimpigie simu mama nimuulize.”
“Sasa hivi ni saa 9 usiku, Mina! Mama amelala. Heri twende tu hospitalini.”
Wakakubaliana hivyo.
Akamletea nguo hapohapo kitandani, akamvalisha. Ile
Mina anasimama tu kutoka kitandani, chupa ikapasuka. Wakaangaliana, ndio
wakajua ni kweli ulikuwa uchungu.
Uzuri hawakuwa mbali na hospitalini. Akambemba mpaka kwenye gari, njiani
akampigia simu Ron na mama yake. Wakakubaliana watawafuata hospitalini.
Akaendesha mpaka hospitalini, akambemba Mina mpaka
mapokezi, wakampokea na kumkimbiza leba akiwa
na Andy. “Usiniache Andy!” “Siwezi. Nipo na
wewe. Usilie na wala usiogope. Sawa?” “Sawa, ila vinauma!”
“Najua mpenzi wangu. Pole.” Mina akawa anasukumwa kwenye kigari akipelekwa leba, Andy amemshika mkono.
~~~~~~~~~~~~~~
Bado mapenzi yalikuwa mazito yakutokea uchumba, ndoa, na fungate
yao haikuwahi isha. Wawili hao wakajuliana na kupendana
haswa. Kwa hakika Andy akapata alichokuwa akitamani maishani na kuzidi.
Mina akawa mke wa zaidi ya ndoto zake. Akianza kumpa penzi, basi mtoto wa
mapadri atabaki akimfikiria mpaka
kazini nakumfanya arudi tena mchana.
Usingekuta wakipishana kwa neno. Kwa haiba Mina alijua
kuishi na watu. Hakuwa na makuu na kujishusha kwake haikuwa tatizo.
Halafu hakuwa mgomvi kabisa. Akampatia vilivyo
Andy. Akajifunza kwa haraka sana kuishi naye. Usafi na akamjulia ukimya wake.
Nini anapenda na wapi asivuke mipaka. Kwa ufupi akampatia vilivyo. Ndio ikaja baraka ya mimba, tena mtoto wa
kiume, mali hadimu
kwenye familia ya Ruhinda, tena hata hakutarajia! Mungu awape nini!
~~~~~~~~~~~~~~
Wakaingizwa
chumba chakujifungulia, Andy akapewa kiti pembeni ya Mina, akawa amemshika
mkono akitetemeka huku amefunga miguu. Kila nesi akimuongelesha, alibaki
amefunga macho akilia tu, mpaka nesi akaishiwa maneno. Uzuri alikuwa
hospitali ya wenye pesa zao. Amelipiwa kuzaa first class, chumba kizima peke yake anasubiriwa na wauguzi
wakutosha na daktari yupo tayari kuitwa muda wowote atakao hitajika ili kuja
kusaidia. Ilimradi tu jambo lisiharibike kwa mjukuu huyo wa kwanza wa kiume kwa kina Ruhinda. Kwa hiyo hata wauguzi wanazungumza
naye kitajiri sio kukaripa.
Alikuwa
akizaa kwa kawaida na hakutaka sindano za kupunguza maumivu
wakati wa kujifungua, “Epidural”. Alishaogopeshwa na watu kuwa aina hizo
za sindano zina madhara makubwa. Anaweza kupooza endapo atatumia sindano hiyo.
Kwa hiyo akawa akiyapata maumivu yote kama yalivyo.
~~~~~~~~~~~~~~
Ikabidi mumewe asaidie maana wauguzi wote waliishiwa
lugha ya kuzungumza naye. Mina anatetemeka haijulikani kama ni baridi au hofu,
na muda wa kusukuma ulishafika. “Unasikia baridi?” “Nahisi
hofu ya ajabu na maumivu makali sana, Andy.” “Niangalie Mina.” Alikuwa
akilia sana, anatetemeka mpaka midomo inacheza. Kamasi na machozi vimejaa uso
mzima. Kumbe akili ilimrudisha siku mimba ilivyotoka na kusafishwa akiwa Iringa
kwa Omar bila ganzi, tena akiwa na kipigo kikali.
Andy
akasimama na kumbusu mara kadhaa, huku akimsafisha uso, wauguzi wakijiangalizia
tu mpaka akaanza kutulia. “Najua unaumia, lakini naomba usiogope, jipe
moyo ukijua unafanya jambo lakijasiri. Maisha ya Ayan yanakutegemea wewe
sasa hivi. Fuata unachoambia na hawa manesi. Fungua miguu, ili akusaidie.
Sawa?” “Sawa.” Akapewa denda la mwisho, mpaka akafungua miguu.
“Mtoto anatoka!” Akapiga kelele aliyekuwa anataka kumpima
tena njia na kuishia kukutana na kichwa cha Ayan. “Akifunga tu miguu, ataua
mtoto wake.” Akaongeza kwa paniki. Wala Andy hakupaniki. Akambusu mkewe na
kumwambia. “Usiwe na wasiwasi Mina, karibu sana unamaliza upumzike. Naomba
utulie.” “Sawa Andy.” Mina akatulia na
kuanza kufuata maelezo, Andy akimbusu na kumfuta machozi.
Akaanza kufuata maelekezo jasho likimtoka na mashozi
kama anayenyeshewa mvua. Baada ya hangaika ya muda akisukuma, yule nesi
akamwambia asukume kwa nguvu kwa mara ya mwisho, ila iwe ya nguvu sana.
Mina akaminya mkono wa Andy kwa nguvu
huku ameng’ata meno. Akasukuma Mina kwa uchungu, maumivu makali,
mpaka akafanikiwa kumtoa Ayan.
Huyo mtoto ametoka tu, Mina na Andy wakasikia analia
hapo hapo. “Hili dume linaonekana akili yake itakuwa juu sana.” Mmoja akaongea
akicheka sababu ya huyo mtoto kulia kwa haraka.
“Hongereni sana na pole mama.” Mina akawekewa mtoto
kifuani huku akitokwa na machozi na kucheka. “Ayan!” Mina akamgusa. Na Andy
akambusu akiwa vilevile bado hata hajasafishwa vizuri. “Ayan!” Andy naye akamuita
taratibu huku haamini kama ni mtoto wake. Ungejua wawili hao wamebarikiwa
hiyo zawadi ya Ayan. Walijawa furaha macho kwa mtoto hawaamini kama ni wao.
~~~~~~~~~~~~~~
Simu ya Andy ikaanza kuita mfululizo. “Mama huyo!
Ngoja nipokee.” Andy akasogea pembeni wakati Mina akiendelea kusafishwa na
kushonwa. “Mina amejifungua salama. Yeye na Ayan wote
wapo salama.” Mina akamsikia mama yake akifurahia. Akacheka. “Tupo tu hapa nje tunawasubiria.” Wakaagana na kukata.
Alirudishwa chumbani akalazwa na mtoto wake. Wote
hawakuwa na tatizo. “Pole mama yangu mzazi. Pole sana na hongera.” Mama yake
Mina akawa akimbembeleza Mina lakini akijivunia. “Nimeshonwa
pakubwa mama! Inauma. Mtoto alikuwa mrefu na mkubwa sana.”
“Nimezungumza nao pale ndani, wanakuja kukuchoma sindano ya maumivu ili
upumzike. Pole.” Andy akaingilia. “Kweli huyu mtoto ni mkubwa sana, lazima
kuchanika. Pole mama.” “Asante. Ila nimefurahi!” Wakacheka.
~~~~~~~~~~~~~~
Andy hakuwa anamuweka mtoto chini. Kila mama yake Mina
alipombadili na kutaka alale, Andy alimnyanyua. “Naona Kiongozi umeokota
alumasi!” Ron akamtania. Bado ilikuwa alfajiri tu, hakuwa hata amerudi nyumbani
kujiandaa kwenda kazini. Mina alipitiwa na usingizi baada ya sindano.
“Daah! Siamini kama ni wangu, aisee! Nilikuwa
nikimsubiri kwa hamu! Chumba chake nilianza kukiandaa naona akiwa hata
hajatimiza miezi minne!” Wakacheka. “Watoto watamu! Hisia yake ya upendo
ni ya tofauti!” “Huwa hakuna anayeelewa hilo Andy mwanangu, mpaka upate wako.”
Ron akacheka. “Mimi sasa hivi hapo nakuelewa mama. Ni hisia za ajabu na kipekee
mno.” Muda wote huo wanazungumza, Andy macho kwa mtoto wake.
~~~~~~~~~~~~~~
Mina aliamka aliposikia tu mtoto wake ananung’unika.
“Dume hilo! Hakuna kulala! Uzazi ndio umeanza.” “Nilikuwa nimepitiwa na
usingizi mzito! Unafikiri ni njaa?” Mina akauliza wakati akikaa kwa shida.
“Nakwambia kama ulifikiri mimba ilikuwa kazi, basi ujue ndio umeanza.”
Wakacheka.
Mama yake akamchukua mtoto kutoka kwa Andy, akamuwekea
Mina. “Toka Ron.” “Naona umeanza kupona, na ujeuri umeanza upya!” Ron
akasimama akijua dada yake anataka kunyonyesha. “Sasa Kiongozi?” “Nisaidie kwa
leo. Nenda kaangalie mambo yasiharibike pale ofisini. Mimi..” Andy na Ron
wakawa wanatoka huku wakiongea.
“Andy!” Mina akaita. “Nakuja sasa hivi, nampa maagizo
Ron.” “Naomba usisahau kumwambia mama yako tafadhali. Amekuwa akiniulizia hali
yangu na mtoto kila siku!” “Halafu kweli! Nitawapigia. Asante
kunikumbusha.” Ndipo akatoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Ilipofika saa nne asubuhi chumba cha Mina kilikuwa
kimejaa maua, kadi na baluni nzuri za rangi ya bluu. Kina Ruhinda walijaa humo kumpongeza
Andy na Mina. Ila mama Ruhinda yeye tokea afike asubuhi, hakutoka.
Alikuwa na kazi yakuagiza tu. Mzee Ruhinda, Pius, Paul, Raza, Dave na Paulina
ni kama walifika wakati mmoja alfajiri na mapema kabla ya kwenda maofisini kwao.
Mzee Ruhinda alijawa furaha, ungejua bila
kuuliza. Alikaa hapo kwa muda ila ikabidi kuondoka baada ya kuchukua picha
zakutosha, akasema anakwenda mkutanoni, ukiisha tu, anarudi tena.
Ikawa hivyohivyo kwa wengine muda wa ofisini ulipofika
wakaondoka kwa ahadi ya kuja kurudi baadaye. Ilikuwa siku ya kazi. Wote hao wananyadhifa
za juu kwenye maofisi yao. Lazima kuwepo ofisini siku ya kazi inapoanza. Ila Paulina
baada ya kama masaa mawili akarudi tena akawa hapo na mama yake, pamoja na wengine.
~~~~~~~~~~~~~~
Mina alijazwa sifa, akikohoa tu, kila mtu
anauliza kama yupo sawa. Dume la nguvu, mjukuu wa kwanza wa kiume, Mina
amewaletea bila shida! Mzuri, amekomaa na anaonekana ni Ruhinda kwelikweli.
Muda wa asubuhi wakati wanaume hao wakina Ruhinda
wakiwa wamejaa kwenye hicho chumba, walikuwa wakitaniana kuwa wao wanadamu kali
sana. Mtoto amewafanana haswa.
Wanaume hao wote walikuwa warefu, walionyooka wima. Weusi waliokolea, kasoro
Pius kidogo alichukua rangi kidogo ya mama yake. Akatoka kama maji ya kunde.
Halafu wasafi kwa kuwatizama hata ngozi. Huna muda ukawakuta ni wachafu, yaani
usafi wa mwili wao na mavazi ni kama asili. Na wote walichukua mwili wa
baba yao, sio mkubwa. Hata Paulina mwili ulikuwa kama baba yake.
Kila mmoja alibashiri chake juu ya Ayan. Mama Ruhinda
alikuwa akicheka mpaka ungejua mama huyo amefurahi. Mama Ron hakuwa
akiamini kama Mina amemketisha na WAKUU!
~~~~~~~~~~~~~~
Maana Pius, kaka mkubwa wa familia hiyo, ndio huyo miongoni
mwa watu watatu wa msaidizi wa Gavana wa pesa wa Tanzania. Na ametumika kwenye
hiyo ofisi kwa miaka mingi sana mpaka akaizoea kama kiganja cha mkono wake. Kwa
kumuangalia tu, ungejua anayo pesa na utisho wa mamlaka.
Mzee Ruhinda mwenyewe alikuwa mkuu wa boardies za pesa za wakurugenzi za taasisi zaidi ya 6 hapo
nchini. Kwa umri huo, bado alikuwa akiongoza! Kijana mdogo, wa Ruhinda, Paul,
ndio huyo dokta wa hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hospitali ya Hindu mandal.
Kijana mdogo tu, lakini jina zuri pia.
Paulina ndio huyo naye yupo ngazi ya juu sana kwenye board ya Auditing nchini,
kama kazi aliyoifanya mama yake kwa miaka mingi sana. Paulina alipoingia hapo
akafanya vizuri akiongozwa na mama yake.
~~~~~~~~~~~~~~
Kwa hiyo hicho chumba kilijaa neema ya madaraka tupu na Mina ambaye hakuwa kitu, Mungu akampa cha
tofauti na wao wote. Kuzaa mtoto wa kiume wa kwanza kati yao. Uthamani wake ukapandishwa
hakuna aliyekumbuka hata shule yake kichwani.
Pesa kila mtu hapo anayo, kasoro mtoto wa
kiume. Mina akaiunuliwa gafla. Akaleta sababu ya kina Ruhinda hao, mida
hiyo ya asubuhi, kukutana kabla ya majukumu yao mazito ya kazi. Vilijaa
vicheko, kila mmoja akizungumza lake mpaka walipotawanyika kuwahi maofisini.
~~~~~~~~~~~~~~
“Baada ya hapa mmepanga nini?” Mama Ruhinda akauliza
kwa upole. Andy alikuwa na yeye ametoka. Mina akacheka lile swali. “Vipi?”
“Andy! Yaani wakati nipo mjamzito, nilimuomba nikijifungua, nikakae kwa
mama mpaka angalau mtoto achangamke. Akakubali vizuri tu. Hapa mlipomuona anazungumza
na mimi, alikuwa akiniambia anakwenda kuchukua likizo yake kazini,
tukiruhusiwa, arudi na sisi nyumbani.” Wakacheka.
“Kumbe safari sio ya Tegeta tena?!” Mama Ron akauliza akishangaa.
“Amebadili mawazo, anasema hawezi kulala nyumbani wakati sisi tupo
Tegeta, labda tuhame naye!” Wakazidi kucheka. “Tokea mtoto ameletwa
hapa, hataki awekwe chini. Ukimchukua tu kutoka kwake pengine umbadilishe,
anasubiria kama sekunde hivi, ukimaliza tu, anamchukua mwanae, anakaa naye
pale, anabaki akimwangalia, mnamuona anacheka taratibu.” “Na mabusu
hayaishi!” Akaongeza Paulina kwa mama
yake Mina. Wakacheka. “Kumbe na wewe umemuona?” Mama Ruhinda akauliza.
“Nilikuwa namwangalia tu.” Wakacheka.
“Kwa hiyo hapa naona safari ni yakurudi tu nyumbani.
Itabidi mama ndio awe anakuja nyumbani kunisaidia.” “Nilishajaza fomu zangu za
likizo. Nikawaambia Mina akijifungua tu, naanza likizo. Kwa hiyo wala usijali.
Nitakuwa nakuja asubuhi, jioni Ron akitoka kazini ananipitia, tunarudi
nyumbani.” “Asante mama.” Mina akafurahi.
“Basi naona mimi niwe mpole tu. Nilitaka niombe
angalau siku hizi za mwanzoni tukakae wote pale nyumbani ili tukusaidie mtoto
mpaka upone kabisa, lakini naona heri nimuache tu Andy afurahie mwanae.”
Akamalizia mama Ruhinda.
“Lakini asante mama. Nashukuru kwa moyo wa
utayari wa kutaka kutusaidia.” “Karibu Mina mwanangu. Sasa muda huu
wakati huyu kaka amelala, na wewe lala. Kina Ruhinda usiwaone wembamba hivyo,
wanakula hao! Utanikumbuka.” Wakacheka.
“Sikutanii Mina mwanangu. Mimi nilikuwa nikinyonyesha,
mpaka napitiwa na usingizi bado wamo tu.
Ndio baba yao akawa anasema tuwaanzishie na maziwa mengine. Lakini nikawa
nakazana hivyo hivyo. Nilikuwa nakonda kama kijiti kwa kunyonyesha. Labda kwa Paulina kidogo.” Akamwangalia Paulina.
“Wanao walaji mpaka sasa hivi mama.” Paulina akaongeza, wakacheka. “Lala Mina.
Angalau upumzike. Kazi yakuzaa sio ndogo.” Mama yake akaweka msisitizo. Mina
akacheka na kulala.
~~~~~~~~~~~~~~
Nyumbani kwa Andy kukawa kituo cha kina Ruhinda.
Walikuwa wakipokezana na kupishana hapo mchana kutwa, usiku ndipo walibaki Andy
na Mina wakilea wenyewe. Ila saa 12 alfajiri, mama Ron anakuwa ameshawasili
hapo nyumbani. Atawasaidia kazi hapo na mtoto, huku akimtaka Mina ajilaze
mgongo, apone uzazi. Mina akawa wakudekezwa na kulelewa.
~~~~~~~~~~~~~~
Bado Ndoa
Ya Mina Ipo Fungate, Haijaanza Kupitishwa MOTONI Kama Nyingine.
Mungu Ameweka
Mkono Wake Hapo, Kila Kitu Kinakwenda Kirahisiii!
Nini Kitaendelea
Kwao!
Mill&Pam
Je?
Inaendelea…
0 Comments:
Post a Comment