Mill ndio
alikuwa kijana wakwanza kutoka kwa mzee Mgini. Ujana mwingi, hakuwahi kuutaka
uzee hata siku moja. Uvaaji wake na alivyo, ungesema ni kaka yao mkubwa.
Alilipenda jiji na starehe zake kama zilivyo. Hakuwahi kutongoza msichana
ilimradi awe msichana. Alisimamia vigezo vyake. Ni bora asilale na huyo
msichana kama kwanza si mweupe, halafu asi
we amebeba maumbile aliyoyataka yeye.
Swala la kuzaa
kila kona yeye kwake ilikuwa fahari. “Huwezi jua atakayekuja kukusitiri
baadaye. Hivi vitoto viwili mnazaa kwenye ndoa, mnanyang’any’ana na magonjwa,
kifo, na shetani. Ukipata mmoja jambazi mwingine mchoyo,
ujue ndio basi tena. Au kakigongwa kamoja na gari kakafa ndio
umebakiwa na jambazi au mchoyo. Sambaza mbegu.” Ndio ulikuwa
usemi wake baa na kwa kila mtu aliyemfahamu.
Kwa Kina Mgini.
Pam akapelekwa
nyumbani kwa Mgini. Mill hakumdanganya. Mzee alijijenga huyo! Jumba lilikuwa
kama hekalu mpaka akashangaa ni kwa nini Mill akajibane kwenye kijumba kidogo
vile hapo kwa Mike. Kulizungushwa uwa mkubwa na pia kulikuwa kama na nyumba nyingine
ndogo kama tatu, nazo nzuri haswa ndani ya ua hiyohiyo.
Ilikuwa mida ya
jioni. Giza halikuwa limeingia sawasawa. Alipendeza Pam. Alivaa moja ya gauni
alilokuwa ameletewa na Mill. Refu mpaka chini ila limemshika vizuri kwa
heshima.
Wakakaribishwa
ndani sebuleni. Akashangazwa na kundi la vijana kama wapo
uwanjani wanasubiria mpira. Akaanza kutetemeka. Ila akashangaa Mill anaanza
kucheka kwa masikitiko. “Mashabiki nyinyi!” “Ni baba huyo! Kasema
unaleta mchumba. Wote lazima tukae hapa. Tuone jinsi wewe ulivyo na
akili sio sisi mafala.” “Hajasema tu hivyo. Kasema tuje tuige mfano.”
“Kasisitiza lazima tuwepo na umesema hutaki ulevi.” “Hayo
nimemwambia yeye ninayemletea mkwe.” Mill akawajibu wadogo zake
waliokuwa wakishindania kumjibu kaka yao.
Pam akababaika,
hajui baba ni yupi! Wote wasafi, halafu wapo kama vijana! Nyumba safi halafu na
sebule yenyewe kubwa, kila kitu hapo ni cha thamani. “Shikamoo baba.”
Aliyeitika akajua ndio mwenyewe. Halafu asilimia kubwa wote walikuwa na
mwili mkubwa kama baba yao. Yaani warefu halafu wapana kama huyo Mill.
“Karibu mama.
Hapa ni nyumbani. Na hawa wote si wageni na wala sijaona muondokaji
hapa ila Mill tu. Wamejaa hapa, wanabadilisha miaka tu, hakuna anayetaka
kutafuta kwake.” Wote wakacheka.
Pam akasogea
kumsalimia na kumpa mkono. “Mbali na baba, anayempa mkono ni mama Kenny
tu. Hakuna kuanza habari zenu za kihuni kwa mwanamke
wangu.” “Sasa tutafahamianaje naye kwa karibu kama unamficha?”
“Unataka kumfahamu kwa karibu ili iweje?” Mill akamuuliza kwa ukali
kidogo.
“Sawa bro.
Lakini sisi wote hapa tupo kwa ajili ya kukutana na shemeji.” “Sijawaita.
Nimemleta kwa baba tu. Haya. Mshamuona, ondokeni bila ya…” “Mzuri aisee!
Huyu kweli haaribu ukoo wa mzee.” “Hana mdogo wake wa kike?” Mwingine akadakia.
“Mimi hata dada yake sina neno, bora awe amefanana naye hivyohivyo.” Pam
akazidi kuona aibu, tena alikuwa amesimama na Mill katikati ya sebule.
“Kama kafanana
na upande wa mama yake, hata mama yake mdogo mimi sina shida, naoa.”
“Kama kachukua upande wa baba, mimi hata shangazi yake!” Mwingine tena
akadakia. “Haya, ondokeni. Naona muda wenu wa kukaa hapa umeisha.” Wote
wakasimama wakicheka mpaka baba yao.
“Bro anataka
kuoa peke yake!” “Nyinyi si waoaji.” “Pam anipe mdogo wake halafu muone
kama mimi sitaoa. Tena naoa kabla yako.” “Haya ondokeni.” Mzee akaweka
msisitizo, wakaondoka wakilalamika.
“Karibu ukae
mama. Mama mwenye nyumba atakuja muda si mrefu na yeye umsalimie.” “Asante
baba.” Ndipo wakakaa. “Unaendeleaje? Mill aliniambia ulikuwa mgonjwa.” Pam
akauliza kwa kujali. “Ni yale maradhi ya kunyimana raha. Usile
hiki, usinywe kile, kama vile wanakukomoa!” “Unafuata mashariti
lakini baba?” “Hata kidogo.” Wakasikia sauti ya mwanamke ikijibu.
“Baba!” “Hivi
nilitaka kukutafuta ili uzungumze naye. Hanywi chai isiyo na sukari.
Vyakula vyote alivyokatazwa, baba yako anakula. Bia zake ni vilevile.
Hapo umemkuta sababu alijua ni wewe unakuja.” “Ndio umepata jukwaa, mama
Kenny?” Akaingia huyo mama hapo sebuleni.
“Basi vile vyote
alivyokatazwa hospitalini, ndivyo anavyovifanya. Na hapo ukitoa
tu mguu wako, jua yupo nyuma yako. Anaenda baa. Akikuomba chakula anachokitaka
yeye, ukampikia alichoshauriwa hospitalini, anakwambia ataenda kula baa.
Hali nyumbani, anakwenda kula huko wasikojua anamshariti. Ukimwambia
apime sukari kabla hajala, anakwambia ili iweje?” “Mnakaribia kunikera,
ili niondoke humu ndani.” Akajibu mzee Mgini.
“Kwa nini
unafanya hivyo baba?” Akalalamika Mill. “Nisikilize Mill. Huu ugonjwa hauna
tiba. Kweli wewe unataka nife kifo cha mateso? Yaani nijinyime sasahivi kama
ndio nitaishi milele?” “Lakini unaweza kuishi na huu ugonjwa kwa muda mrefu
baba, bila matatizo!” “Hivi unajua tokea waniambie nina kisukari ni watu
wangapi nishazika ambao walikuwa hawaumwi hata kidogo?” “Basi
ndio usemi wake huo?” Mama Kenny akadaikia.
“Wote tutakufa.
Hakuna atakayeishi hapa duniani milele. Mimi nimekataa kuishi kwa kujinyima.
Nikijinyima kwa hili halafu nikatoka hapa nikagongwa na gari, nikafa
kwa hiyo ajali je? Dawa unazonisisitiza kunywa kila wakati mpaka siwezi
kupumua, nameza. Shida ni nini?” “Haziwezi kufanya kazi kama hufuati
mashariti, baba! Kweli unataka uondoke uache vijana wako hawana muelekeo
kama hivi?!”
“Unamuona kuna
hata mmoja wao hapo mwenye muelekeo wa maisha? Yaani mimi nishindwe
kufurahia maisha kwa ajili ya wajinga hao? Ni wewe, Kenny na Sheila ndio naona
mna malengo ya baadaye, na ndio maana mnaona sizembei. Wengine
wote ni kama hivyo. Kweli eti nyinyi mnataka nikae hapa kama mfungwa kwa ajili
ya wapuuzi hao? Anayetaka kunitumia sasahivi, anitumie. Nikiondoka
shauri yao. Pam mama, wazazi wako wapi?”
Pam akagutuka
maana mzee alishaanza kugomba nyumba nzima. “Mama anaishi na wazazi wake huko Mlalo,
Lushoto.” “Huko milimani haswa! Lakini tutaenda tu. Lazima akirudi Mill
safari ingine, twende tukaone wazazi. Nijitambulishe na kulipa mahari
kabisa. Wasije niwahi wahuni wengine wa hapa mjini, wakalipia vijana
wao. Mill keshawahi, tunaenda kumalizana kabisa. Au unasemaje?”
Pam akacheka kwa wasiwasi akimwangalia Mill aliyekuwa amenyamaza baada ya swala
la ugonjwa.
“Eti Mill? Huyu
si umesema unaoa kabisa?” “Kama utakuwa hai baba! Unamipango
mingi wakati hutaki kuhakikisha inakukuta ukiwa hai!” “Kuwa na
imani wewe!” “Imani bila matendo itasaidai nini baba? Tafadhali
fuata mashariti.” “Sawa.” “Mmmh!” Mama Kenny akaguna.
“Naona muda wako
wakukaa hapa sebuleni umekuishia, mama Kenny. Unataka kunikera tu
bila sababu!” “Unamdanganya tu Mill. Akiondoka hapo, unarudia mambo yako kama
kawaida. Usimdanganye.” “Sasa, safari hii namuahidi mimi
mwenyewe. Acha kumtia wasiwasi usio na sababu! Umesikia Mill?” Mill
akamwangalia akionyesha hana imani kabisa.
“Ukirudi
tunakwenda wote Mlalo, kujitokeza na kutoa mahari kabisa.” “Naomba
badili maisha baba! Taratibu. Nimeshakuletea aina nyingine ya sukari.
Kwa nini hutumii?” “Anakula baa. Sukari zako zipo nyumbani. Atatumia saa
ngapi?” Mama Kenny akajibu. Wakaanza kubishana yeye na mkewe hapo, Pam mgeni
ametulia. Ila akagundua akizungumza Mill anamsikiliza.
“Kuna chakula
Mill. Njoo ule na mgeni.” “Hicho chakula chako cha jumuiya mama Kenny,
nakushukuru sana. Acha tukale mbele ya safari.” “Kweli unamleta mgeni hata maji
asinywe!” “Atakunywa siku nyingine. Leo ilikuwa salamu tu. Tusikuharibie
bajeti yako. Wewe kuwa na amani. Ikifika siku ya kula, tutakwambia. Leo tunapita
tu. Sijamuona Sheila. Yupo?” “Amehamia chuo. Fujo za hapa amesema anashindwa kujisomea.
Naona anataka kukuiga wewe.” Mill akacheka. “Bora achukue chake mapema.”
Akasimama akijibu hivyo.
“Fuata masharti
baba, tafadhali.” “Acha kumsikiliza mama Kenny! Ukirudi utanikuta.”
“Nikukute mzima.” “Mill anapenda mambo ya wasiwasi! Maisha ni
hayahaya, halafu bado unataka kuyaishi kwa kujifinyilia. Pam mama,
karibu kwenye ukoo. Naona wewe hutaniharibia ukoo. Hatutaki mbegu za ajabuajabu
sisi. Tunataka wazaliwe watoto wanao eleweka sio wakuwatetea kila
wakati. Mara umtetee ni wa kike! Mara umtetee kafanana na bibi mzaa babu yake! Hatutaki
fujo sisi! Mtoto kama ni wa kike, basi aonekanike ni wa kike na sura ya
kike sio kama jambazi aliyeponea kuteketezwa kwa moto.” Pam akacheka akimtizama
Mill.
“Nitakupigia
kukuaga baba.” “Hurudi tena?” “Kuna
nini?” “Tutazungumza kesho. Lakini nataka tupate muda wa kuzungumza mimi
na wewe kabla hujaondoka. Sio hapa.” “Na isiwe baa, tafadhali baba.” Akamuona
anacheka. “Ndiko ulikotaka tukutanie?!” “Hapana wewe! Ni mazungumzo ya muhimu.
Siwezi kuzungumzia baa. Vipi wewe?” “Basi tupange chakula cha mchana pamoja
kesho.” Wakapanga na baba yake na kuondoka.
~~~~~~~~~~~~~~
“Mbona umekataa
kula kwenu?” “Aaaah! Huwa namuhurumia sana mama Kenny. Yeye mwenyewe hana
utulivu pale ndani. Fujo kama ile unayoiona pale. Kikipikwa chakula pale ni
kama cha jumuia nzima. Sitaki kujiingiza kwenye mipango yake na kumtia
shuguli zisizo na maana.” “Inamaana wote wale wanaishi pale?” “Wote kama
unavyowaona vile. Na asilimia kubwa pale hawajasoma, au hawataki shule,
wana kazi za kuwasaidia kuingiza pesa ya starehe, kuvaa vizuri
kama vile ulivyowaona pale na kuendesha magari mazuri hapa mjini. Kula,
kulala kwa mama Kenny.” Pam akanyamaza.
~~~~~~~~~~~~~~
Mill aliondoka
nchini kwa shida sana. Pam ni wale wasichana waliaji kwa kuagana na
kumpokea mgeni. Alilia alipompokea Mill ikawa zaidi alipokuwa wakiagana.
Ilibidi Mill kucheck in mizigo kwanza kisha kutoka nje kukaa naye mpaka
mwisho. Yaani yeye alikuwa abiria wa mwisho kuingia kwenye ndege na
mlango wa ndege kufungwa.
Mina&Andy
Kipindi
hicho cha maandalizi ya harusi mama Ron akajitahidi kumficha Mina, kwa hiyo
kuonana kwa wapenzi hao ikawa hadimu. Alipomaliza tu mitihani yake, akatulia
ndani akiandaliwa mwezi mzima kwa harusi. Mama Ron hakutaka hata atoke nje.
Mina akawa mwali haswa.
Siku
mbili kabla ya harusi, Mina na ndugu baadhi walio chaguliwa na mama Ron, waliondoka
jijini kuelekea nchini Kenya tayari kwa harusi. Walikuta wamechukuliwa upande
mzima wa hoteli, nzuri tu. Wakapokea ukarimu kama waliotoa kwa wageni wa
Andy nchini Tanzania.
“Nina
hamu na Andy, mama! Acha nizungumze naye hata kidogo.” “Naomba tulia Mina. Una
siku mbili tu! Utakabidhiwa huyo Andy mpaka kifo.” Mina akanyamaza
lakini akiwa hajaridhika. Muda wote Ron ndiye aliyekuwa akiwasiliana na
Andy kwa mipango na taratibu zote za hapo kabla na baada ya harusi watakapokuwa
mapumzikoni. Mina aliandaliwa mwili kiswahili
haswa! Kwa mwezi huo mmoja, ungependa kumtizama. Aliteleza na kuiva vizuri haswa.
~~~~~~~~~~~~~~
Usiku
wa kuamkua siku ya harusi, Andy alimtumia ujumbe. ‘Ngumu kuamini kesho muda
kama huu, utakuwa mikononi kwangu mpaka kifo chetu! Nakupenda Mina na
nina kusubiri kwa hamu.’ Ilimgusa Mina, akabaki akirudia
kusoma ule ujumbe akiwa amelala na mama yake. Akamuonyesha mama yake.
“Huyu
kijana anakupenda Mina mwanangu. Naomba ukatulie mama. Tafadhali Mina.” “Nimebadilika mama.
Nimetulia.” Mina akajibu na machozi. “Nimekuona. Ninachoongelea ni usije
ukafika huko, ukazoelea huu upendo ukaanza kuhangaika.” Mina alipewa
chumba cha peke yake na mama yake.
“Nimebadilika mama. Nitatulia.”
Mina akasisitiza kwa kuumia akiona bado mama yake anawasiwasi naye. “Nakuombea
iwe hivyo tu. Maana huwa mambo yanabadilika ukifika kwenye ndoa. Sasa usije
ukafika huko, ukazoelea mambo ukamsahau huyu kijana. Hii yote ni pesa anamwaga
kwa ajili yako tu. Naomba usije lisahau hilo.” Mina akanyamaza lakini
akiumia moyoni akaona aondoke hapo, aende akatulie bafuni. Alikaa huko
mpaka akajua akirudi atakuwa ameshalala. Na kweli alirudi akamkuta amelala, na
yeye akapanda kitandani na kulala.
Siku Ya Harusi Ya Mina&Andy.
Mmoja
wa ndugu aliyekuja naye Mina alikuwa ndiye anayempamba bibi harusi na
wasimamizi. Waliamka mapema sana ili wasichelewe kanisani. Kufika saa nane
mchana, kila mtu alikuwa tayari. Wakamuacha Mina na mama yake hapo chumbani
wengine wakatoka kwenda kujimalizia huko vyumbani kwao tayari kwa kanisani.
Akaanza
tena kwa Mina aliyekuwa ametulia kimya kwenye kochi akiogopa hata kumuongelesha
tena mama yake asije akaanza tena na kumuharibia mudi ya siku
hiyo.
“Nia yangu ni nzuri Mina. Nataka ukawe makini
huko. Zile tabia zako za kuchanganya wanaume walio marafiki,
naomba ujichunge nazo Mina. Sio ufike huko akakutambulishe kwa
marafiki zake halafu ukaanza kuwachanganya.” Mina alilia sana.
Ikawa
kama siku huyo mama Ron amekumbuka mabaya yote ya Mina. Alihakikisha
anamkumbusha uchafu wote huku akimuonya asije akarudia.
Mina alishindwa hata kumjibu maana alionekana kama anajazba. Akanyanyuka kwenda
chooni huku mama yake akiendelea kuongea. Akamtumia ujumbe Ron, nakuomba afike
hapo.
Ron
akafika hapo chumbani kwao kwa haraka. “Mina yuko wapi?” Akamuuliza mama yake
aliyemfungulia mlango. “Ananidharau! Mimi namuhusia, ananiacha na kwenda
kujifungia chooni, ananiacha nikiwa nazungumza!” “Kwani kuna nini tena?!”
“Namwambia akatulie huko atakapoolewa. Ona hii pesa anayotumia Andy kwa
ajili yake! Sasa sitaki akaanze ile michezo yake. Akaingia kwenye ndoa
na kuanza kuchanganya hata na marafiki wa mwenzie. Akaanza kutuingiza
tena aibu kwa ndugu wote waliojua leo anaolewa. Nikabaki kicheko tena.”
Ron akaumia sana.
“Mama!
Kwa nini imani yako inakosa matendo mama yangu?! Huyu Mina
ametuonyesha kwa vitendo amebadilika. Ulitaka afanyaje?” “Mimi
namuonya tu Ron.” “Usiendelee kuzungumza naye kama Mina wa nyuma! Mina
uliyekuwa ukimuomba Mungu ambadilishe, Mungu ametujibu.”
“Amesema
mwenyewe, hatakumbuka dhambi
zake tena. Ameziweka mbali kama mashariki na magharibi ilivyo mbali! Amemuita Mina ni mbarikiwa. Sasa kwa nini unamzungumzia
Mina wa zamani kwa Mina huyu ambaye hata Andy ametuhakikishia
hata kwake amekuwa mgumu?”
“Kwa
nini hutaki kutunza muujiza
wako? Kwa nini unashindwa kuishi na Mina huyu aliyebadilika, na
wewe ukakubali muujiza wako? Ulitaka nini kitokee ili uamini tena? Mina AMEBADILIKA
mama. Na Andy ametuomba tuishi na Mina huyu si wa zamani!
Kweli wewe unataka ukampotezee mtoto wako kwa Andy! Kwamba akiondoka, asirudi
tena kwako?” Kimya.
“Nikuombe
kitu mama yangu. Tafadhali mwache atulie ili ile garama uliyosema Andy
amelipia kutufikisha hapa leo, ilete maana. Kama sisi tumeshindwa
kuishi na Mina huyu, basi acha tumsaidie kumfikisha kanisani kwa Andy,
akaishi naye. Tafadhali mama yangu. Naomba tuwaache wenyewe.”
“Mwache
Mina atulie, afike kwa mwenzie akiwa ametulia. Tusiharibu
siku ya leo.” Mama yake akatoka hapo chumbani kwa hasira. Wasiwasi
ukabaki kwa Ron kama harusi bado ipo kwa Mina au amegairi.
~~~~~~~~~~~~~~
Nabii Hana
heshima nyumbani kwao.
Mama alishang’atwa na nyoka, ngumu kuamini
kama majani yakitikisika ni upepo tu.
Walifanikiwa
kuwakwepa kina Ruhinda, safari hii ni mama mzazi.
Harusi ipo?
0 Comments:
Post a Comment