![]() |
“Nimeshazungumza na wazazi, wameelewa. Hakuna atakaye
msumbua tena. Hata mimi ninaondoka kabisa hapa nchini.” Ron akashangaa
sana. “Kwa nini!?” “Sitaki kumuharibia Mina. Amenieleza maisha yake, na jinsi
mama alivyonieleza, naona ni heri nimuache tu. Mimi nimesoma Ron. Naweza
kupata kazi popote kwa mshahara wowote. Nipo hapa nchini kwa ajili ya undugu
tu. Tanzania sio nyumbani kama ilivyo Nairobi.” Andy akaegemea meza, Ron akiwa
amesimama anamsikiliza.
“Nikirudi Nairobi nitaweza kupata kazi na kuishi
vizuri tu.” “Sasa unaacha kazi hapa, umeshapata kazi kule?” Ron akauliza
akisikika kujali. “Kule ni nyumbani Ron. Nina familia inayonielewa na inayoendana
na mimi, sio kama hawa kina Ruhinda. Wale Mapadri ndio wamenilea mimi tokea mdogo
sana. Katika uzima na maradhi, wamekuwa na mimi. Nina baba kule, zaidi
ya huyu mzee Ruhinda. Ni baba kweli kweli kama alivyo mama Ron kwako.”
Wakacheka.
“Kwa hiyo ninaposema ninarudi Nairobi, ujue narudi
nyumbani kwa watu tunaozungumza lugha moja na kuelewana.”
“Nafikiria kukupendekeza wewe kwenye hii
nafasi. Nafikiri utaweza Ron. Unafanya vizuri sana.” Ron akavuta kiti na kukaa.
“Mimi huwa napatwa na kigugumizi linapofika swala la mapenzi.” Akaanza Ron. “Kidogo kama lina nichanganya vile!
Sijui kwa kuwa nazungukwa na mifano ya ajabu ajabu ya watu wanaosema wanapenda au tulikuwa tukipenda!”
Andy akarudi kukaa.
“Unajua niliishi na baba na mama. Wale watu sio kwa
maneno. Hata kwa vitendo ungejua ni watu waliokuwa wakielewana.
Walikuwa wakianza kucheka kwenye mazungumzo yao ambayo hayakuwa yakiisha,
utajua ni watu wanao elewana. Stori za chuoni na kazini pia zilikuwa
haziishi. Maana wote walikuwa wakifundisha shule moja kama mama alivyokwambia.”
“Hapakuwa na ugomvi, labda kule kupishana kwa kawaida
tu. Sasa baba alivyoanza fujo zake za dini, hakika ungemuonea huruma,
Andy. Yaani yeye mwenyewe dini ilionekana kama imekuwa mzigo kwake! Ile furaha
ikamuisha kabisa. Ikawa fujo tu. Mara msikie ameoa huku. Haya, mkitulia
mwezi hauishi, mnamuona amerudi nyumbani kama mgonjwa. Baada ya muda
tena mnaona anakuja kufuatwa na dada yake. Anatolewa pale nyumbani, anakwenda kuozeshwa
kwengine! Kama mjinga vile!”
“Nakumbuka kwenye kikao cha mwisho cha ndugu zake
pamoja na mama. Mimi nilikuwepo. Mama alitaka Mina aende akasubirie kwa jirani.
Wakati huo tulikuwa hatuishi pale Tegeta.” Ron akaendelea kama anayezungumza kwa
kuvuta kumbukumbu.
“Nakumbuka kumwangalia baba na mama kwenye kile kikao.
Wazi baba alionekana hakubaliani na ndugu zake kwa kile wanachomwambia
mama. Lakini hakuongea sana zaidi yakusema watoto ni wa mama, aachiwe
kuamua kufanya kile anachotaka na sisi. Basi. Wakamtisha mama, wakondoka na
baba.”
“Siku baba anakuja kuomba talaka, nakumbuka
baba kuzungumza maneno kama yale aliyozungumza mama. Juu ya sijui nyota yake na mwanamke aliyeoa. Lakini
hakuwa hata na ujasiri na kile alichokuwa akikizungumza kwa mama! Na
chakushangaza, alilala pale nyumbani siku hiyo. Alilala kama aliyekuwa amechoka
haswa, alikuja kuamka saa nne asubuhi. Akasema hajalala usingizi wa namna hiyo
kwa muda mrefu sana. Akaja kuondoka tena jioni yake. Hakurudi
tena pale.”
“Sasa nakumbuka na wewe ulikuja pale nyumbani kwa staili hiyo hiyo. Ulizungumza na mimi. Ukajieleza kwa kina.
Nikakuhoji maswali. Sijui kama unakumbuka siku ile uliponiita pale Surrender?”
Andy kimya.
“Wasiwasi wangu juu yako na Mina ilikuwa ni sababu ya
vile ninavyokufahamu Andy. Nikakuuliza kama kweli unamaanisha kwa Mina?
Nikajaribu kukumbusha anapoishi Mina na watu tunao mzunguka. Maana nimeona hata
ongea yako. Kula yako. Tabia zako. Jinsi unavyojibeba. Nilijua wazi mnatoka
kwenye dunia mbili tofauti!”
“Ndio maana uliniona siku ile nikashangaa sana kuwa unawezaje kumuacha msichana kama Lora, kwa
ajili ya mtu kama Mina! Tena nikakuonya kabisa, usimuache Lora kwa ajili
ya Mina. Nikijua unafanya kosa. Lakini ukaeleza hoja zako kwa makini sana. Lakini lililokuwa kubwa ambalo mpaka
sasa linasikika masikioni kwangu ni mapenzi.”
“Kweli ni mapenzi.” Akaongeza Andy.
“Sasa hapo ndipo ninapochanganyikiwa Andy! Maana
unaongea kama mama. Hivyo hivyo. Kuwa yeye na baba walipendana sana. Si na wewe ulimsikia?” Andy kimya. “Changamoto alizokutana nazo
baba, ni kama hazitofautiani sana na wewe! Yeye aliondoka akionekana kabisa hana furaha, ameenda kuoa. Ukimuona,
huwezi kumlinganisha na sisi kabisa. Ni yule muislamu, ambaye huwezi kudhani
hata alishawahi kumtongoza mkristo! Ana mke wake na watoto. Lakini nilikaa naye
kwa muda mfupi tu, sikumuona yule baba niliyekuwa nikimfahamu mimi. Sijui kama
unanielewa?”
“Kimaendeleo anaonekana amepiga hatua kubwa sana
tofauti na vile alivyokuwa na sisi. Alikuja kuwa mwalimu mkuu wa shule ya
sekondari. Nafikiri alirudi chuo au sijui, lakini akahamishwa akawa Afisa elimu
hukohuko Mkuranga. Analo gari na ana nyumba yeye na mkewe. Wapo tu vizuri.
Lakini ukimwangalia, ni kama hayupo pale kwenye yale mafanikio.” Ron akajisogeza tena.
“Hivi ni muda gani umepita tokea ufike pale nyumbani
uzungumze juu ya upendo wako kwa
Mina?” Ron akamuuliza Andy bosi wake.
Andy Kimya. “Sidhani hata kama miezi mitatu imefika. Kwa hakika hata
hamjatimiza miwili. Au nimekosea?” Kimya. “Leo tumekaa mimi na wewe tena.
Nashuhudia ukifanya kama kile alichokifanya baba yangu! Unakimbia kama yeye!”
“Kwa uhakika kabisa, utapata kazi nzuri. Mshahara
mzuri. Unarudi nyumbani, huna tofauti na baba yangu! Alifanya kama wewe! Hatua kwa hatua, hivyo hivyo!
Mpaka natilia mashaka hata ile waliyosema walimloga
baba na Mina! Wewe unanifanya nitilie mashaka. Maana wewe huonekaniki kama wazazi wako na ndugu zako wamekuloga! Lakini unafanya kama baba yangu tu! Sasa najiuliza,
hivi haya mapenzi watu wanayosemaga
yapo, yanakuwepo kweli au nihisia tu za muda!” “Yapo Ron.” “Sasa
huwa mnashindwa wapi!?” Akauliza Ron
kwa kushangaa sana.
“Eti Andy? Huwa mnashindwa
wapi? Maana kama nikimwangalia baba yangu, mpaka niliacha kwenda kumsalimia.
Amezeeka kuliko mama na wakati nafikiri umri wanalingana na mama! Mama
anaonekana anaaghueni ya maisha kuliko hata baba ambaye ni Afisa elimu!
Mama anazidi kuwa kijana, na maisha yake yanaendelea, lakini yeye aliyekimbia,
haonekaniki kufurahia hata!”
“Nikikuonyesha
baba yangu, utasema alitakiwa kustaafu. Amechoka, utamuhurumia. Ukifika tu,
anataka kujua habari za mama, anavyo endelea! Kama anakula vizuri. Kama
anafuraha. Maisha yake yakoje, hana hata habari na sisi ila kutaka habari za
mama tu! Sasa mimi najiuliza, kama anampenda
kiasi hicho, ni kwa nini hakupambana
hata kidogo kutunza anachokipenda!”
“Dini yake yenyewe aliyokimbilia, haionekaniki hata
kumpa furaha. Anaswali swala tano. Lakini huwezi ona ni wapi anafuraha. Akienda
na kutoka kuswali yupo vilevile. Sasa unajiuliza, amekimbia nini na amepata
nini! Watoto ambao amepata, ambao anawaongoza kwa njia anazopenda yeye na ndugu
zake, ukiwaangalia, bora sisi.”
“Wakwanza kule kwa mke wake huyo wa dini yake, ni
wakike. Anavaa kama vile walivyotaka Mina avae. Lakini hata kabla hajamaliza
darasa la saba, alishazaa. Sidhani
hata kama walitofautiana sana tabia na Mina wa zamani. Tabia zao nilikuwa nikizilinganisha tu. Na yeye umbile ni
kama Mina. Wote wamefanana na huyo bibi wa Unguja, sema bibi amezeeka sana ndio
maana ni rahisi kuwafananisha na shangazi.”
“Haya, huyo wapili ambaye ni wakiume, walimpeleka
kwenye shule ile waliyotaka mimi nipelekwe, yule kijana alikataa shule
mapema sana, sidhani hata kama alikwenda sekondari. Yupo tu nyumbani. Halafu
ndio wana binti mwingine mdogo tu. Ukiangalia unajiuliza, hivi huyu baba mwenye
familia hizi mbili, ameshindwa wapi?
Huku hayupo na kule kwenyewe alipokimbilia
pia aliyokimbilia hayatoi matunda ya
maana!” Kimya.
“Sijui bwana! Ila nikushukuru kwa kunifikiria kwenye
hii nafasi. Asante sana. Na ninakuahidi nitafanya vizuri. Sitakuangusha.” Ron akatoka, nakumuacha Andy amepoa kimya. Andy
alirudi kukaa kwenye meza yake. Akafuta kabisa ile barua aliyokuwa ameandika kwenye
kompyuta yake, yakuacha kazi.
Akabaki akifikiria chakufanya.
Atafutaye Hachoki.
Ijumaa usiku wakiwa wamekaa tu nyumbani kwao, kama saa
mbili na nusu hivi, wakashangaa hodi mlangoni. Ron akasimama kufungua mlango.
Alikuwa Andy. Ron akashituka kidogo. “Karibu Kiongozi!” Mina na mama yake
wakakaa sawa pale ndani. “Asante.” “Karibu baba. Naona wewe si mkulima.”
Wakacheka. “Kwa nini mama? Au ndio mmemaliza kula nini?” “Muda si mrefu.” Andy
akakaa. “Hamna hata masalio?” Akauliza Andy huku akicheka. “Pole. Tumekaa
kihasara hapa, hakuna aliyepika. Na msomi wetu naye ametuambia amechoka,
alikuwa na mitihani leo. Imebidi kumaliza kiporo cha jana.” Andy akamwangalia
Mina.
“Pole na mitihani.” “Asante.” Mina akajibu. “Ulionaje?”
“Sio mbaya, uzuri mwalimu alitutolea mambo yale yale aliyotufundisha. Kwa hiyo
nimefanya.” “Mwambie juu ya ile website.” Mama yake akamwambia Mina.
Mina akainama. “Ni nini Mina?” Andy akauliza kwa kumbembeleza. “Sio kitu. Mama
naye!” Mina akajibu huku akicheka kwa
wasiwasi.
“Nataka kujua na mimi.” “Hata sio kitu cha maana Andy.
Tulipewa kazi yakutengeneza website ya mtu. Sisi wote pale darasani.
Mwalimu akasema atakayeitoa vizuri, itakuwa moja ya maksi za mtihani wa mwisho,
na pia huyo mtu akilipa hiyo hela ya website yake, mwanafunzi
atakayeshinda, atalipwa nusu ya hiyo pesa.” Mina akacheka kwa aibu.
“Kwa hiyo wewe umeshinda?” Andy akauliza, Mina
akacheka huku akitingisha kichwa kukubali. “Safi sana. Hongera. Nikirudi kutoka
safari nitakuletea zawadi.” Mina akakunja uso. “Unasafiri Andy?” “Naondoka na
ndege ya kesho asubuhi. Mambo yote yakienda sawa, nitarudi jumanne au
jumatano.” Mina akabadilika usoni. “Sasa mbona hujaniambia?” Akalalamika Mina,
kama sio yeye aliyesema aachwe.
“Ndio maana nipo hapa Mina. Nimekuja kukuaga.
Safari imekuwa ya ghafla. Sijui kama nilikwambia mama.” Akamgeukia mama Ron.
“Nililelewa na mapadri, huko Nairobi. Sasa mmoja wa
mlezi wangu. Ni kama baba yangu kabisa, anaishi huko. Miaka miwili iliyopita,
alipata uaskofu. Ndiye nakwenda kumuona. Nilipanga kwenda na Mina weekend
ile inayofuata. Ili akamuone. Alitamani sana kumuona Mina. Lakini ameitwa na
uongozi huko Italy. Weekend hiyo niliyopanga kwenda na Mina, hatakuwepo.
Sasa kwa kuwa anasafiri, na ni ghafla, nimeona niende tu nikazungumze naye
kabla yakuondoka.” Mina akainama.
“Sitakaa sana, nitarudi.” Akaongeza Andy, Ron akajua
ameamua kubaki. “Tunashukuru kwa kuja kutuaga Andy. Uwe na safari
njema.” “Asante mama.” Andy akabaki akimwangalia Mina, Mina na yeye
akamwangalia. “Kweli hujala?” Mina akauliza. “Sasa swali gani hilo? Wewe
mwambie asubirie chakula ukapike mara moja kwenye gesi.” Mina akacheka.
“Utasubiria?” Mina akauliza huku anacheka na kusimama. “Mara moja tu, utakula.”
“Basi twende nikusaidie hata kukata nyanya.’’ “Ila ujue ni ugali tu na
mchicha.” “Nitakula huo huo, twende.” Wakaongozana mpaka jiko la ndani.
~~~~~~~~~~~~~~
“Tokea lini kitu unachosoma umeanza kukiona sio chamaana?” Wakamsikia Andy akimuuliza.
Mina hakujibu. “Au tokea ukutane na kina Ruhinda?” Mina hakujibu. “Niangalie
mimi, Mina. Njoo kwanza.” Wakawa wanawasikia. “Najua familia ina nguvu, lakini si kwa Ruhinda kwangu au kwetu. Nina familia nyingine ambayo wamenilea mimi na wanaheshimu maamuzi yangu. Hiyo ndiyo
nitakupeleka kukutambulisha. Najua watakupenda na kukuheshimu.” “Unajuaje Andy?” Wakamsikia Mina akiuliza.
“Kwa kuwa ndio wamenilea hivi. Mtazamo nilio nao mimi ndio
wao. Hivi ninavyotazama mambo na
watu ndivyo wao walivyonifundisha.
Nimekuzwa hivi na wao. Huyo askofu ambaye ni kama baba yangu, nilimgusia tu juu
yako, akataka nikupeleke. Kwa hiyo najua ni nini ninashozungumzia.” Mina akanyamaza.
“Halafu Mina, kuhusu hii familia ya hapa, naweza kuwa
siku ile sikusema kitu lakini Mina, nakuhakikishia, haitakaa ikatokea tena. Nimeshazungumza nao na
nimeweka mipaka juu yetu.” “Juu yetu!? Unamaanisha nini?” Mina akauliza
taratibu.
“Nakuhakikishia hawatatuingilia tena. Kile
tunachofanya na kuamini, ni mimi na wewe tu. Cha msingi ni mimi
na wewe tupange na kuelewana. Hata ukiona lipo jambo ambalo hujalielewa
na kulipenda, tafadhali niulize, sawa?” “Siku ile nilichukia Andy, walinidhalilisha
na kunicheka waziwazi!” “Sio wewe tu! Kukudhalilisha wewe ndio mimi.
Hawakufanya vizuri, naomba unisamehe mpenzi wangu.” “Nimefurahi umerudi Andy.
Nilikuwa na hamu na wewe!” Andy akacheka.
“Mbona hukunitafuta sasa?” “Nilijua na wewe unanifikiria
kama ndugu zako! Au utaanza kunidharau.” “Nakupenda Mina. Na mimi
nilikwambia. Sipo kwenye maisha yako, kujaribu. Na ndio maana mimi
nakutambulisha kila mahali. Sina chakujificha, najivunia vile
ulivyo. Naamini mambo mengine kama wapi tunakwenda kuabudu siku ya jumapili,
hayo ni mambo yamakubaliano tu. Lakini hayawezi kutufanya tushindwe kuwa
pamoja.” “Wewe ni mtu mzuri Andy.” Mina akamwambia kwa upendo.
Kila
mtu akacheka. Mina akasikia. “Bwana mama! Sasa mnasikiliza nini?” Andy akaendelea kucheka. “Sasa mimi sikuwa na
njaa. Nilitaka tu kupata muda na wewe. Maadamu umenisamehe, acha
nikajiandae na safari.” Mina akacheka. “Kwa hiyo sasa hivi utanipigia?” Mina
akauliza kwa deko. “Nitakupigia kesho asubuhi kabla sijaondoka na...” “Ukifika.
Ili nijue kama ulifika salama. Halafu jumatatu urudi.” Andy akacheka. “Ukitaka
nirudi jumatatu nitajitahidi kurudi.” “Nataka.” Mina akaweka msisitizo.
“Basi nitarudi jumatatu. Mungu akipenda jioni nitakuja
kukuchukua shule.” “Week ijayo
ndio mwisho wa shule.” “Hongera sana.” “Asante. Sasa hivi tumeongea ndio
nimeona nimefanya jambo la maana.” “Sana. Na usikubali mtu akwambie
vinginevyo. Ingekuwa rahisi si kila mtu angejua unachofanya! Mimi mwenyewe
sijui kutengeneza website japo
nina shahada mbili! Hata ukinipa kompyuta na milioni tano ukaniambia
nitengeneze, sitaweza kwa kuwa sio kitu nilichosomea. Na watu wanaishi kwa hiyo
kazi tu. Ila sema kwa ajili ya ushindani au kujua zaidi, ndipo watu
wanajiendeleza zaidi kwenye mambo hayohayo. Zipo mpaka shahada zake! Na
nikwambie ukweli tu Mina, nchi nyingine kompyuta designing zinalipa sana. Na
ndio ajira ambazo watu wanalipwa pesa nyingi kulinganisha na hata hiki
ninachokifanya.”
“Kweli Andy?” “Kabisa. Mambo yanabadilika. Kila kitu
ni kwenye kompyuta. Sio mahospitalini sio kwenye mabenki. Kila mahali ni
kompyuta. Wewe utakuja kuona. Kazana tu kuongeza ujuzi. Ili uwepo kwenye nafasi
ya juu, utaona. Tutakuja kuzungumza na kupanga zaidi. Si bado unapapenda IFM?”
Mina akatingisha kichwa kukubali.
“Basi tutapanga
zaidi.” Wakatoka hapo jikoni kurudi Sebuleni. “Naomba niwaage.” “Naona
umeongeleshwa, hata maji ya kunywa hujapewa!” “Mama! Andy hana njaa! Alikuja tu
kuniona.” Mina aliongea na cheko, wakacheka.
“Haya baba. Uwe na safari njema.” “Asante. Ron!” Ron
akamwangalia. “Niambie kiongozi.” “Tutaonana.” “Asante. Karibu sana.” Andy
akatoka na Mina akiwa amemshika mkono.
Alichofanya nikufungua mlango wa dereva, Mina
akapanda, yakaanza mabusu. Andy akiwa amesimama nje ya gari katikati ya mapaja
ya Mina akiwa amekaa akiaangalia nje. Andy aliendelea kumkumbatia kwa nguvu
huku akimvutia kwake.
“Naomba kuachana iwe kitu cha mwisho kabisa
Mina. Iwe ni pale tutakapoona hakuna suluhi nyingine.” “Mimi mwenyewe sitaki tuachane
Andy. Wewe nakupenda kiukweli.” Andy alifurahi huyo, nakushukuru Mungu
kuzungumza na Ron. Angekimbia mapenzi matamu ya Mina. Akarudi haraka kwenye
midomo yake.
“Nakupenda Andy. Nilikuwa na hamu na wewe!” “Hata
mimi. Tutapata muda wakutosha nitakaporudi. Tulale pale kwenye kochi,
nikukumbatie vizuri wakati nikinyonya hiyo midomo yako.” Mina akacheka na
kufunika uso. Andy akajiweka uso kifuani kwa Mina. Katikati. Mina akamkumbatia
kichwani nakujilaza, Andy akapitisha mikono nyuma yake akamkumbatia vizuri.
Wakatulia kwa muda.
Alitulia Andy kapo katikati ya matiti hayo kama
aliyelala, Mina akiwa amemlalia kichwani huku vidole vyake vikimpapasa nyuma ya
shingo.
“Utanifanya nilale hapa kifuani kwako!” Mina akacheka.
Akambusu mara kadhaa hapo katikati ya kifua. Akasimama akihema huku akimwangalia
Mina. Akacheka na kuinama mbele ya Mina. “Acha mimi niondoke, kabla sijashindwa
kuondoka kabisa.” Mina akacheka taratibu na kushuka garini.
“Jumatatu umeniahidi utakuja kunichukua shule.” “Mbona
na kulala kifuani hukumbushii?” Mina akacheka sana. Akambusu tena. “Eti Mina?”
“Utalala mpaka uchoke.” “Nisipochoka?” Mina akazidi kucheka.
“Kesho sitakuwepo. Hii ni pesa ya kununua vyakula vya
hapa nyumbani na matumizi mpaka nikirudi.” “Huna haja yakufanya hivyo Andy.
Sisi tupo sawa tu.” Andy akakunja uso. “Ni wewe unaongea au ni kina Ruhinda
kupitia mdomo wako?” Mina akanyamaza.
“Eti Mina?” “Ni kwa sababu naona kuna kila kitu ndani!”
“Nimetoka kuzungumza nini na wewe pale jikoni?” “Kwamba ni mimi na wewe ndio tutapanga
mambo yetu.” “Na ndivyo tulivyokuwa mpaka nilipokupeleka kwa kina Ruhinda!
Ndipo umeanza kutilia mashaka mapenzi yangu, na kunitilia mashaka
mimi mwenyewe kwenye kila kitu kwako. Na sasa unaanza kubadili utaratibu
wetu.” Mina akanyamaza.
“Jumamosi ilikuwa siku yetu yakununua vyakula vya
nyumbani. Ni nini kimebadilika?” “Hamna Andy. Ila nimeona unasafiri. Utahitaji
pesa zaidi.” “Siwezi nikawa na amani kule kama huku sijakuacha vizuri.” “Mimi
nipo sawa Andy, usiwe na wasiwasi.” “Wewe unamtegemea Ron na mama. Unajuaje
walivyo kwa sasa kipesa? Yaani unajulikana upo na mimi, halafu hata pesa ya
vitu vidogo vidogo unataka umuombe mama! Sasa kuna kuwa na faida gani ya mimi
kuwepo kwenye maisha yako? Kama ningekuwa sina kazi, hapo sawa. Lakini nina
kazi na uwezo. Naomba wakati unaishi hapa nyumbani, mahitaji yako yawe juu
yangu mpaka tutakapoanza kuishi wote. Ni sawa?” Mina akajisikia vizuri.
“Asante Andy.” “Tafadhali usianze kuzungumza lugha za
watu wengine, na siku nyingine huna haja yakujieleza kwa yeyote yule
jinsi ya sisi tunavyoishi. Zaidi wanapokuuliza juu yetu. Haimuhusu
mtu, labda upende mwenyewe. Lakini si kama walivyokuwa wakikuhoji siku ile. Huwajibiki
kwa yeyote isipokuwa mimi. Sawa?” “Sawa.” Mina akakubali na tabasamu la aibu
usoni huku akipokea zile pesa. “Asante Andy.” “Karibu.” Andy akaondoka. Mina
akarudi ndani na cheko.
~~~~~~~~~~~~~~
“Muone! Si ulisema humtaki tena wewe!” Mama
yake akamtania. “Namtaka Andy lakini sio wale ndugu zake.” Wakacheka. “Na
maneno yote yale niliyompa siku ile, sikutegemea kama atakuja kurudi huyu
kijana! Anaonekana anakupenda.” “Mimi mwenyewe nampenda.” Wakacheka, Ron kimya.
Andy akiwa anaelekea uwanja wa ndege alimpigia simu
asubuhi kama alivyoahidi, wakazungumza wakikumbushana wanavyo pendana. “Urudi Andy, ujue nakusubiri.” Andy akalifurahia sana
hilo. Kutoka kujisikia familia yake haimuhitaji, leo mrembo Mina, toto zuri
anamwambia anamuhitaji! Ikamuongezea faraja ya ajabu. Kuwa na yeye
anahitajiaka!
“Nitarudi kwa ajili yako Mina.” Akamsikia Mina akicheka kwa furaha. “Nakupenda Mina. Nakupenda sana.” “Ukirudi nitakuonyesha
jinsi ninavyokupenda na kukuhitaji Andy.” Wakazungumza mpaka Andy
akafika uwanja wa ndege, akamsubiria mpaka akapanda ndege ndipo wakaagana.
Na alipotua tu uwanja wa ndege wa Nairobi akampigia
tena simu kumtaarifu kuwa amefika salama na amepokelewa. “Uwe na wakati mzuri, Andy.” “Asante na wewe Mina, wangu.”
Wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~~
Jumamosi usiku Ron akapata simu kutoka kwa Andy. “Najua itakuwa nimewataarifu muda mfupi, lakini alitaka kuja
kuwaona kabla hajasafiri.” “Sidhani kama kutakuwa na tatizo. Nitazungumza na
mama, kisha nitakutaarifu. Lini?” “Kesho ingekuwa nzuri, lakini ana misa mpaka
jioni. Naomba iwe jumatatu tafadhali.” “Basi nitazungumza na mama, kisha
nitakujulisha.” Ron akaonekana kutoa ushirikiano.
“Nashukuru sana Ron, asante kwa kila kitu.”
“Karibu. Mnategemea kuwa wangapi?” Andy
akakadiria. “Lakini Ron, tafadhali msihangaike sana.
Lengo kubwa ni kutaka kukutana na nyinyi na mfahamiane.” “Sawa.”
Wakapanga, wakaishia kukubaliana wao wawili, wakahitimisha kila kitu.
Ukisema Cha nini!
Mama Ron alijawa furaha hata hakujali udhia wa muda. Aliomba rafiki zake wakaribu wafike hapo
nyumbani siku ya jumatatu, wakamsaidia kupika na kuandaa hapo tayari kwa
wageni. Ilipofika saa 11 jioni Andy akawa anawasili na wageni wake wanne. Macho
yaliwatoka na kuongeza utisho wa namna yake pale walipoona ni mapadri
wenye sare za kipadri na askofu mwenye kofia ile ndogo siyo ya misa pamoja na
joho lake.
Heshima
ikaongezeka zaidi. Na hata mama Ron akajisikia vizuri mbele ya wenzie. Ni Mina.
Mtoto aliyesumba jamii. Anajulikana kama mtoto aliyeshindikana.
Leo ameleta watu wa heshima wa kiasi hicho! Angalau mama Ron akaanza kufutwa
machozi kwa namna yake.
Walikaribishwa ndani, yakaanza mazungumzo. Hali ya
hofu ikaanza kupungua kwani wakaanza kusikika ni watu wa kawaida, waliojaa unyenyekevu
wa kiutumishi. Walikarimiwa vizuri na kwa heshima. Wote wakaonekana kumfahamu vizuri
Andy.
“Andy ni mtoto niliyemlea mimi mwenyewe tokea mdogo
kabisa.” Akaanza huyo askofu. “Anao udhaifu ambao inabidi Mina uufahamu
ili uweze kumuelewa na kumchukulia.” Wote wakatulia kumsikiliza. “Akikasirika
au akiingiwa hofu, huwa hawezi kabisa kuongea.” Hapo hata
wale mapdri walianza kucheka na Andy mwenyewe kwa kuwa hawakuwa wakijua ni nini
askofu wao anataka kuzungumza.
“Wakati ni mdogo tu. Waliletwa kwangu kuwa wamevunja
kioo cha mlango wa kanisa dogo la mapadri. Nikawachapa wote na kuwapa adhabu.
Hiyo ikaisha. Siku nyingine kabisa alipokuwa akisafisha ofisini kwangu kwenye
mazungumzo yakawaida tu, ndipo akaniambia hakuwepo katika kundi la wale
watoto waliokuwa wakicheza na kuvunja kioo.”
“Nilishangaa lakini sikumwambia. Ndipo ikabidi sasa
kufuatilia kwa yule aliyekuwa amewaleta kwangu. Akaniambia yeye aliwakusanya tu
wote waliokuwa karibu na tukio siku ile, na kuwaleta kwangu. Ndipo ikabidi sasa
kuwa naye karibu na kumchunguza zaidi. Ndipo nilipo gundua huo udhaifu
kwake.”
“Unaweza kumchapa mpaka ukachoka, akiona umetulia
kabisa. Siku nyingine, ndipo anaweza hata kuzungumza na wewe akajieleza na
ukamuelewa. Kwa hiyo ni kitu nilitaka na nyinyi mkifahamu juu ya Andy.”
Wakapata jibu la kwa nini siku alipompeleka Mina kwa kina Ruhinda hakuzungumza.
Ikawa kama anamjibia Andy.
Akaendelea huyo aliyekuwa baba wa Andy. Askofu. “Kitu kingine
ambacho Mina awe na uhakika nacho, Andy anapoamua kufanya jambo. Au
anapokwambia ‘Ndiyo’ kwa jambo
fulani, ujue atalisimamia na kulilinda kwa gharama yeyote ile labda hilo jambo limfie, kwamba haliwezekaniki tena na yeyote.”
Akaendelea.
“Mimi ni mpenzi sana wa maua. Sasa nilipokuwa
nikisafiri, mtu niliyekuwa nikimwachia maua yangu ya ofisini. Ndani na nje,
alikuwa Andy. Kwa kuwa nilikuwa ninauhakika nitayakuta salama.
Mtu hupimwa kwa vitu vidogo. Katika hilo tu, nikajua nikisafiri
nani nimuache katika lipi, lakini Andy katika yale mambo yaliyohitaji umakinifu
na uendelevu bila kukosa.”
“Padri Antoni ni pacha wa nje wa Andy. Walijiita hivyo
tokea wapo wadogo, wamekua pamoja tokea siku ya kwanza wazazi wao wanawaacha
pale shuleni. Isipokuwa mwenzake aliamua kuingia kwenye upadri.
Anamfahamu Andy ndani na nje, na ndio maana na yeye alitamani kuja kuona
familia ya Mina. Tunashukuru sana kutupokea na kutukarimu.” Yule
askofu akashukuru kwa heshima wakapeana mikono.
“Sasa Andy ameniambia anataka kuoa karibuni ila
Mina anasoma.” Mina akacheka na kuinama. “Kwa heshima yako mama, tunaomba tu
baraka zako ili tulikamilishe hili na ninakuahidi Mina ataendelea
kusoma tu hata akisha kuolewa na Andy. Ukikubali hili, basi tutarudi
kutoa mahari baada yakujua taratibu zote.” Mama Ron hakutegemea swala la ndoa
kwa Mina tena kwa haraka vile! Asijue mwenzie huwa anaonjeshwa asali, ndio anataka kujenga mzinga kabisa! Ndio haraka zote hizo. Akababaika kidogo maana
wote walikuwa wakisubiria jibu, lakini mwalimu akachangamka. “Nashukuru kwa hiyo heshima, basi Ron
atamjulisha Andy.” Hilo likawa lipo sawa.
“Ombi la mwisho.” Askofu akaendelea, wakacheka.
“Hilo hata magoti nitapiga mama.” “Hamna sababu. Karibu tu.” “Asante.” Akatulia
kidogo yule askofu. Mapadri wengine wakimsikiliza kwa makini sana bila
kuingilia zaidi yakutingisha kichwa kuafiki kila anachokizungumza askofu
wao.
“Huyu Andy ni mtoto niliyelea mwenyewe kama
nilivyowaambia. Nakuomba mama, na Mina mwanangu, nifungishe hiyo ndoa
mimi mwenyewe kama nilivyofanya kwa mwenzie kumpa upadrisho. Hata Andy mwenyewe sikuwa nimemwaambia hilo. Lakini
ni ombi langu binafsi kwenu.” Mama Ron akacheka na kuinama kama
anayefikiria. Pakazuka ukimya.
“Inamaana hiyo harusi ikafungwe Roman?” Akauliza mama Ron. “Tafadhali mama.” Akasihi askofu
na kuendelea. “Lakini wapi wataabudu baada ya hapo, ni juu yao wenyewe.
Ila ile siku ya harusi, tafadhali naomba hiyo niisimamie mimi
mwenyewe.” “Naomba hilo nimuachie Mina mwenyewe. Ila binafsi, kwa heshima mliyotuonyesha, hakika imenigusa. Sidhani
kama Mina atakuja kupata heshima kama hii!” Wakamuona yule mama
anafuta machozi.
“Mungu awabariki. Binafsi ni wapi
wanaenda kuabudu baada ya hapo au sasa hivi, sijali. Maadamu dini
ni moja, hilo halina shida kabisa kwangu. Sitataka madhehebu yawazuie
Andy na Mina. Naamini watafikia tu mwafaka.”
Mina hakutegemea.
Maana alijua swala la dini ndilo liliharibu
ndoa ya wazazi wake, kusikia hivyo! Hata Andy akasimama. “Asante mama. Nashukuru.”
Akampa mkono kabisa. Vikaanza vicheko hapo, mwishoe wakaagana. Askofu na
mapadri walikuwa wakienda kulala kwenye nyumba za mapadri Kurasini. Andy
akawarudisha.
~~~~~~~~~~~~~~
Ndani ya mwezi, Mina akalipiwa mahari na mapadri hao.
Mama Ron siku hiyo alialika ndugu karibu wote walioweza kufika, majirani na
wafanyakazi waliokuwa wakifanya kazi na mama huyo na kumfahamu Mina kama mtoto asiyewezekanika.
Muhuni na hashikiki.
Watu walikula na kunywa, wakisherehekea mahari ya Mina BILA kina Ruhinda
wala upande wa baba yao Mina na Ron ambao waliwasusa.
~~~~~~~~~~~~~~
Andy hakurudi tena nyumbani kwao na wala hawakumuona
kanisani. Ila siku hiyo ya jumapili familia hiyo wakiwa kanisani wakasikia
tangazo la kwanza la ndoa kati ya Andrew Ruhinda na Aminata. Baba yake
akashituka na kumgeukia mkewe, wakabaki wameduaa.
Tangazo lilisema ndoa hiyo itafungwa jijini
Nairobi nchini Kenya katika kanisa kubwa la Cathedral Basilica of the Holy Family. Jambo zuri
kwa kijana wao, likageuka fedheha kwa familia nzima ya Ruhinda. Vile
wanavyofahamika na kuheshimika kwenye jamii. Halafu Andy anaoa bila wao
kuambiwa au hata kukaribishwa! Ikawa aibu
kubwa kwa familia ya Ruhinda haswa kwa watu wa karibu yao, wanao wafahamu
familia hiyo. Kila walipoulizwa juu ya harusi hiyo, hawakuwa na
majibu yakutosheleza.
~~~~~~~~~~~~~~
Andy amesimama
kiume mpaka amefanikiwa hatua ngumu na ya msingi. Anabaraka zote za baba mlezi
na mama Ron. Bado siku takatifu atakapokabidhiwa Mina kama mke.
Mill naye huko
kwa baba yake?
Inaendelea….
0 Comments:
Post a Comment