![]() |
“Naomba nitoe angalizo.” Akaingilia Devi. “Sasa na
wewe usianze.” “Hata! Naomba tu niseme jambo pengine mtaelewa. Maana
msipoangalia, mtampoteza Andy, kabla hajarudi kwenye maisha yenu.
Kumbukeni Andy hajakuwa kama nyinyi. Maisha ya Andy amekuwa akiwa mbali
na nyinyi, tokea mtoto.” Hapo wote wakanyamaza.
“Andy hayajui haya maisha na nyinyi wote. Ni
kama mtoto wa kambo kabisa.” Mama yake akashituka kidogo. “Naomba
niwe wazi mama. Kwa heshima tu. Maana watoto wako wote umewakuza hapa nchini, ukiwaongoza
na upo karibu nao. Ni Andy peke yake ndiye aliye watofauti.” Akaendelea Devi na
kuwanyamazisha wote.
“Huyu Andy ni mtoto wenu, lakini amekuzwa mbali
na tofauti na wengine wote. Sijui kama mnamfahamu msimamo wake juu ya
watu wengine ukoje!? Eti jamani?” Kimya.
“Maana ni rahisi Paulina na Paul au hata Pius, kutizama
mambo kwa jicho lako wewe mama, tofauti na Andy ambaye anatizama macho yake
kama Padri.” Devi akawatizama
machoni. Ndio ni kama wanaanza kufunguka.
“Mtazamo wake na wenu katika mambo au wetu sisi
wote ni tofauti kabisa. Mimi najua ninachokiongelea, kwa kuwa nipo
karibu sana na Andy, na nyinyi pia. Niwaambie ukweli kabisa. Jinsi anavyotizama
mambo Andy, ni tofauti sana na nyinyi wote, na ndio maana akiwa na
swali, hatampigia simu kaka yake Pius, atanipigia mimi.” Wote
wakashangaa.
“Na alivyo na akili, atahakikisha anapiga muda anaojua
sipo na dada yake. Atapiga kwenye simu ya mezani ya ofisini kwangu. Na
atahakikisha anaweka wazi kabisa kuwa swali lake ni kwa sikio langu tu.
Hatasema moja kwa moja, lakini utajua ndivyo anavyomaanisha.” Wakapoa.
“Chakuwahakikishia ni hivi, huyo mtoto, amemuingia
Andy, kuliko atakavyosema. Ni Love
at first sight. Anampenda Mina
kuliko nitakavyowaambia, mkaelewa! Na mimi nilishajaribu kuzungumza naye mara
ya kwanza tu alipomuona na kumfanya ashindwe kulala. Nikazungumza naye
na kumuonya kwa muda mrefu sana, ndipo ikabidi amtafute Lora kwa
mara ya kwanza kabisa, ili kumsahau Mina.” Wakashangaa sana.
“Kabisa! Lora alimtafuta ili asaidie kumtoa Mina
kwenye mawazo. Lakini Andy alishindwa kabisa. Tulikuwa tukimuita asilimia 7.” “Nani?” Akauliza Paul. “Huyu Mina. Kwa vile
alivyokuwa amechanganywa na huyu mtoto, akiwa hamjui, akawa anasema
anamfahamu kwa asilimia 7
tu, lakini yupo tayari kuwa naye hata kama hizo 93 ni mbovu, atajifunza
kuishi nazo.” Wakaangaliana.
“Kuna kipindi alisikia huyu mtoto anaumwa amelazwa,
Lora akiwa kwenye picha, akanipigia kuniuliza chakufanya, nikamshauri aachane
naye asimtafute kabisa ili asiendelee kuchanganywa. Atulize akili kwa
Lora. Kweli akafuata ushauri wangu. Lakini hilo ni kosa ananilaumu nalo
mpaka juzi nilipompigia simu kumjulia hali baada ya kupotea hapa. Na akakataa
kabisa kumzungumzia Mina na mimi. Ni kama ananilaumu nilimshauri amtelekeze
Mina akiwa mgonjwa tena amelazwa hospitalini.” Wote kimya.
“Ninachojaribu kukwambia mama yangu, na kukuomba.
Najua unawapenda sana watoto wako na unawatakia mema, lakini nashauri
labda kwa ajili ya kumpata Andy, angalau msizidi kumsukumia mbali
na nyinyi, akaona mnamdharau au hamumuheshimu. Nyinyi woote,
nashauri mjikaze tu, mjifunze, na mumuonyeshe mnaheshimu
maamuzi yake.”
“Ila mkiendelea kutoa kasoro kila mwanamke anayemleta
kwenu kwa heshima, kama yule Mganda sijui au Mkenya, mtampoteza Andy
kabisa.” “Na kweli! Si mliona aliacha kuja hapa karibia mwezi sasa?” “Sawa sawa
Pius. Na msifikiri kwa Andy inamsumbua. Hana anachokosa na kupoteza
kwenu. Anaona nyinyi mpo timu moja, yeye yupo timu pinzani.” “Halafu
yuko peke yake!” Akamalizia mzee Ruhinda.
“Kumkosoa, kumcheka na kumbeza
mbele ya msichana wake, sidhani kama ni sawa jamani!” Wote wakamgeukia
Paul. “Mbona mimi nampenda tu Mina! Pale kanisani mbona mimi ndiye
niliyemsalimia wakati nyinyi mlimchunia!
Sema mimi nilikuwa nacheka ule utaratibu na
vigezo vya hapa nyumbani na vile yule mtoto alivyo.” Paul
akajitetea.
“Ni wewe Paulina ndio ulikazana kumuuliza maswali Mina
kama mnataka kumuajiri!” Paul akamrushia mpira dada yake kujitoa lawamani. “Mimi
nilitaka kumfahamu zaidi.” Na Paulina naye akajitetea. “Mmmh! Si kwa jinsi ile
bwana! Tulisikia sana wakati mnamfukuza jikoni.” Akaongeza Paul akitoa
lawama kwake zaidi. “Na mlimkatalia kwa kejeli mbele ya Andy mwenyewe!
Tena baada ya yule mtoto kujinyenyekeza! Mngempa hata mchele aoshe
jamani!” Devi aliendelea kulaumu.
Kama kitu kikamwingia mama Ruhinda. Alipoa kama
sio yeye. Kila mtu akajisuta. “Ila wenyewe wanaonekana wanapatana na kuelewana.
Si mmemsikia Mina?” Kwa mara ya kwanza
Raza akaongea kwenye mjadala wa Mina hapo mezani. “Anaonekana anamshauri
vizuri, japo ni mdogo kwake. Hakutaka Andy aondoke hapa. Ingekuwa mtu mwingine angemshawishi
Andy waondoke naye.” Akaongeza Raza.
“Na nafikiri hilo ndilo la msingi jamani! Ndoa ina
mambo mengi sana mbali na uchumi.” Akaongeza mzee Ruhinda kwa tahadhari.
Wakaendelea kula kimya kimya.
Kwa Andy & Mina.
Andy alimtoa hapo akataka apande kwenye gari yake,
Mina akakataa. “Mimi nataka kwenda kwa mama yangu, Andy.” “Twende tukazungumze
kwanza.” “Mimi sioni chakuzungumza.” Mina
akaanza kulia tena. “Niangalie Andy. Mimi na nyinyi
tuko tofauti kwa kila kitu! Hakuna popote tutakapoenda mimi na wewe. Siwezi
kuishi maisha ya kujitetea, Andy. Sitaweza.” “Hutaishi na
wao, utaishi na mimi.”
“Hata uniambie vipi, wale ni ndugu zako
Andy, hawatakaa wakaondoka maishani kwako. Watakuwepo tu. Na mimi bado
nitabakia kuwa mtu wa nje.” Andy akataka
kumshika, Mina akarudi nyuma.
“Mimi naondoka Andy. Hata hivyo mimi na
wewe tunatofautiana. Wewe una dini yako na mimi nina dini yangu.
Kanisani kwenu mnafanya mambo mengi sana, mimi siwezi. Halafu
wewe umezaliwa kwenye familia ya watu wanao dharau watu. Wanataka watu wanaofanana
na nyinyi. Hiyo hatuwezi kubadilisha. Na kama hunifahamu bado, mimi watu
kama ndugu zako siwezi kuishi nao Andy. Wanadharau watu wengine.
Mimi nimezoea maisha kama ya pale kwetu. Tunakuwa na amani na tunaheshimu kila
mtu. Siwezi Andy.” Andy alibaki
kimya anamsikiliza.
“Wewe endelea na maisha yako. Tafadhali
naomba uniache kabisa. Mimi ndio nimetulia, nataka kutulia nyumbani. Mambo kama
haya sitaweza Andy. Wewe tafuta mwanamke anayefanana na watu wa
kwenu. Mimi naondoka, naenda zangu kwa mama yangu na Ron.” Hapo hapo Mina akaondoka. Akakimbilia kituoni,
akapata daladala, akaondoka. Na kumuacha Andy na hali mbaya na ahadi
za yote atakayofanyiwa baada ya kutoka kwao. Alishaona siku yake ikiisha akiwa amejawa
na penzi la Mina, sio KUACHANA.
~~~~~~~~~~~~~~
Mina alipopanda tu kwenye daladala akampigia simu kaka
yake kumuomba amfuate kituoni alijua watakuwa wameshatoka kanisani. “Kwema
huko?” Akauliza mama Ron baada ya Ron kukata simu. “Sidhani. Kwa nini mimi
nimfuate, asiletwe na Andy? Halafu kama analia!” “Basi huko atakuwa ameshawatoroka.”
Wakacheka.
“Ngoja nimpigie, maana anaweza kuwa analia kweli.
Mpaka aje afike hapa kichwa kitakuwa kinamuuma, kesho tena patakuwa hamna
shule.” Mama yake akampigia. “Vipi mwanangu mzuri?
Mambo yameenda vizuri huko?” Akaanza mama yake. “Mama,
wale watu wabaya.” Mina akamuelezea mama yake kuanzia mwanzo mpaka
mwisho. Mama yake akaumia sana. “Pole. Njoo
mama. Tena tulikuwa tupo tu hapa Mbezi kwa Mangi tunakula. Shukia hapo kituoni
utatukuta hapa.” Akamtuliza, Mina akatulia.
~~~~~~~~~~~~~~
Hapohapo Andy akarudi nyumbani kwao, hata ndani
hakuingia tena, akachukua gari yake akaondoka kuelekea nyumbani kwa kina Mina. Alikuwa
na hali mbaya, kuachana na Mina haikuwa chaguzi. Kwamba haipo hata
mezani. Alimtaka huyo Mina kwa hali na mali.
Alishalemazwa na penzi la kuonjeshwa na Mina! Hapo alikuwa akisubiria
kwa hamu siku atakuja mvua nguo amfaidi kwa undani. Leo wanampokonya
tonge mdomoni! Hakukubali. Akakanyaga
mafuta mpaka Tegeta, lakini akakuta nyumba imefungwa. Akataka kumpigia simu
Ron, akaona awe muungwana. Asubiri tu.
Mungu Humpa Amtakaye.
Alikaa hapo mpaka ikafika saa 11 jioni ndipo akaona
wanakuja, tena kwa kutembea tu. Wote watatu. Andy akashuka garini. Ron
akasalimiana na Andy, Mina akaenda kufungua mlango, akapitiliza mpaka chumbani.
Mama Ron akamkaribisha ndani. “Karibu baba.” “Asante.” Moja kwa moja kwenye
makochi. Andy, mama Ron na Ron.
“Samahani mama yangu, najua Mina amekwambia.” “Wala
huna haja yakuomba msamaha Andy mwanangu. Haya matabaka kwenye maisha ni
Mungu mwenyewe ndiye ameyaweka. Hujalia watu kwa kadiri apendavyo yeye.
Na ni ngumu sana matabaka haya kuendana, PENGINE kuwepo mkono wa
Mungu mwenyewe, yaani Mungu aruhusu, lakini si vinginevyo.” Andy aliumia
sana kusikia hivyo.
“Lakini Mina atakuwa na mimi, mama! Ataishi na mimi.”
Akamuona mama yake anacheka taratibu kisha akaona aongee tu. “Mimi nitakuwa mkweli
kwako Andy. Sitakuficha. Hayo ni maneno ya mwanzoni kabisa watu
huyasema, kabla uhalisia wa ndoa haujaingia. Ni wachache sana wanaweza
kusimamia hapo.” Mama Ron akaendelea.
“Huyu Ron huyu, ni mtoto wangu. Hata aoe mzungu au
mswahili kama mimi mama yake, bado mimi ni mama yake tu. Ipo nguvu kubwa
sana ya mama kwa mtoto. Wewe utakuwa shahidi yangu kwa lililotokea leo.”
Mama Ron akaendelea. Taratibu tu.
“Mina aliponisimulia mkasa mzima. Jinsi mambo yote
yalivyoenda. Mwishoni nilimuuliza swali moja tu. Katika yoote hayo, wewe
ulisema nini? Sikusikia jibu lakueleweka kuwa katika yote hayo wewe ulisimamia
upande gani au kwenye yale mahojiano, ulizungumza nini.” Andy akashituka
kidogo.
“Niliambiwa karibu kila mtu alizungumza,
kasoro wewe. Sikumwambia kitu Mina, lakini mimi mwenyewe nikafikiria.
Kama leo ulikuja kumchukua hapa mwanangu, ukampeleka kwenu, mbele
ya ndugu zako wanamsodoa, kesho akiwa mke wako mmeshazaa watoto wawili
watatu, umeshamzoea, si watampiga, wewe ukiangalia na kumtoa tu
kwenye ugomvi?” Andy akainama.
“Silaumu, lakini kwa haraka haraka, nasema inatokana
na malezi na makuzi ya kwenu. Kile kilichoongelewa pale hakikuwa kosa.
Kinaendana na nyinyi. Ndipo tunaporudi kwenye matabaka. Yapo Andy baba,
na wala hatuwezi kuyaepuka. Mlipo nyinyi na sisi ni tofauti
kabisa.” Akaendelea mama simba, akilinda mwanae. Ila kwa utaratibu tu bila
ugomvi.
“Na sikwambii kwa hili lililotokea leo, hapana.
Ni kwa uzoefu wangu wa haya mambo. Hawa watoto wawili, sikuzaa na muhuni
wa mtaani. Alikuwa mume kabisa. Ila sababu ya utofauti wa DINI tulifunga
ndoa ya serikalini. Tulikutana chuo cha ualimu, mapenzi yakawa mazito
kuliko utofauti wetu wa dini. Wazazi pande zote walituonya na kutukatalia.
Lakini wakati ule hapakuwa na jinsi tukaweza kuishi mbalimbali.
Tukajikaza, sisi wenyewe, tukafunga ndoa. Maisha yakaanza.”
“Mwaka uleule akapatikana Ron. Wale ndugu waliosema wametususa
sababu ya mimi kuolewa na mwislamu, na yeye kuoa mkristo,
wakaanza kurudi kwenye picha taratibu. Na huwezi kumkataza mama yake asifike
nyumbani au dada zake kuja kuona mtoto ambaye ni damu yao.”
“Kwao ni watu wa Pemba, Unguja kabisa. Wana uarabu,
rangi kama hivyo Mina au huyu Ron, na nywele hawa watoto wamechukua kwao sema
Mina amechanga kidogo na zangu ndio maana unaziona hivyo. Lakini ni kama hivi
Ron akiacha kunyoa mpaka chini kabisa. Ni waislamu wa swala tano.
Alfajiri swala ni ya msikitini. Mwanamke lazima kujisitiri. Ramadhani
lazima kupikwe futari, ila na mwanamke wa dini yao. Mimi mkristo.”
“Wakwe wakija nyumbani, alfajiri wanaondoka na baba
Ron kwenda msikitini, mimi nimelala ndani. Chakula ninachopika mimi hakiliwi
kwa kuwa ni mkristo hawaamini nyama niliyopika kama imechinjwa na
mwislamu na chakula ninachopika mimi hakiwezi kuliwa futari kwenye mwezi
mtukufu!”
“Taratibu uhalisia wa mambo ukaanza kujidhihirisha.
Mwenzangu akakazana kwa hili na lile ili tu kunusuru ndoa yetu ambayo
pia haikuwa sawa kwa utaratibu wa kwao. Si ya msikitini. Tukakazana wee,
LAKINI ukweli ukabaki pale pale. Mama ni mama. Ndugu zake ni ndugu zake.”
“Na uislamu wa mwenzangu au aliyekuwa
mwenzangu, hakuukuta ukubwani. Ni yule wakuzaliwa nao. Hana ukweli wa Mungu
mwingine isipokuwa aliofundishwa tokea mtoto. Na mimi hivyo hivyo. Fujo
zikaanza. Ndugu wanamkumbusha hili na lile kwa makuzi ya kwao.
Ikawa sasa mwezi wa ramadhani hakuna anayekuja kwetu, na yeye sasa inabidi
kwenda kufuturu kwa dada yake, Mwananyamala! Ikawa fujo. Siku za
sikukuu, mume yupo kwao, Unguja.”
“Haya, dada yake akaachika, na yeye akarudi kwao
Unguja. Sasa kizazaa
mwezi mtukufu. Baba yao hawa anakwenda kufuturu wapi kipindi hicho! Ikawa sasa fujo
zaidi. Mara usikie kaoa mke wa daku, sijui wapi, mara usikie kamuacha. Ikawa sasa haonekaniki
nyumbani. Hekaheka isiyoeleweka. Mimi na watoto wangu tukawa sasa makafiri. Hawatutaki tena.”
“Mwishoe nikaja kusikia amekwenda kupewa mke, huko kwao
Unguja. Ndipo akaoa sasa, na ndio mwanamke ambaye akawa anatambulika
nyumbani kwao na kuheshimika. Tulikuwa tukifanya kazi pamoja.
Tukifundisha shule moja. Fujo zakuoa zilipoanza, nafikiri kwa heshima
yangu, akaomba uhamisho. Akahamia Mkuranga.”
“Sikumuona yeye wala ndugu zake tena wakija hapa kwa la kheri
wala la shari. Uzuri tulikuwa
tumeshapanunua hapa, tumeanza msingi. Alipoanza hekaheka zakuoa, ndipo
mambo yakaanza kuwa magumu sasa, ndipo nikaanza jukumu la wanangu mimi peke
yangu bila msaada hata wa ndugu zangu, sababu walinikataza kuolewa naye,
sababu ya dini, nikamngang’ania. Sasa kule kuachwa na watoto wawili, na
yeye kuoa mwanamke mwingine wa dini yao nikageuka mimi kicheko
kwa familia.”
“Hakuna anayetaka nimkaribie hata kwa kuomba
chumvi. Wakanisusa mimi na hawa watoto wangu. Wakinicheka mimi na
wanangu. Nikikwambia nipo mimi na wanangu, sio kwamba sina ndugu hapa mjini,
lakini ni vile walivyotugeuza sisi kichekesho na kuonekana sisi ni watu tulioshindwa.”
“Na bahati yake ilivyokuwa nzuri, mwenzangu alivyoniacha
tu nakuoa, huko Mkuranga akapandishwa na cheo, akawa mwalimu mkuu, wa
shule ya sekondari Mkuranga. Ndugu zake wakazidi kufurahi na kumthibitishia
mimi ndiye niliyekuwa na mkosi kwenye maisha yake. Namuwekea nuksi, mkewe mpya ndio nyota yake safi. Nyota zao sijui zinaendana, sasa hivi mambo yake
yanaenda vizuri.”
“Hayo naambiwa na Kasimu mwenyewe, wala si
ndugu zake. Yeye mwenyewe aliniambia mara ya mwisho alipokuja hapa kwangu,
kunipa talaka yangu. Kwamba anataka huyo mke wake mpya, ndiye
atambulike hata serikalini, anataka atoe jina langu.” “Watoto!?” Akauliza Andy kwa mshangao.
“Hao watoto alishawatoa zamani sana kwenye
maisha yake. Yaani hao alikuwa hata azungumzii tena baada yakumkatalia Ron
asianze madrasa, na bibi yao alipokuja hapa, akataka Mina awe anavalishwa
hijabu na mambo yao mengi. Nikakataa. Nikasema huyu mtoto mdogo hivi
avaliswe hijabu na baibui, atachezaje! Wakasema maumbile
yake hayafai kuachwa wazi, Mina ni mpana chini kama shangazi zake lazima
asitiriwe kwa baibui na hijabu. Nikawaambia huyu mtoto hajachagua
kuzaliwa hivyo, hawawezi kumnyima raha mwanangu, wamwache. Hapo
Mina alikuwa darasa la 5 anakwenda la sita ndipo bibi yake alipokuja na hiyo
hoja. Kuwa apelekwe shule ya kiislamu na mwili wake usitiriwe, ninavyomvalisha
mimi si sawa.”
“Halikuwa jambo dogo hata kidogo! Na mimi kwa kuwa
mtoto wao alishaanza kumanga manga huko nje. Hajali nyumbani, nikawa
nina nguvu na watoto wangu. Kasimu akawa anaona hata aibu kulazimisha.
Maana alikuwa anaonekana nyumbani mara chache. Na mara zote anazokuwa akirudi
anakuwa kama aliyekimbia huko. Yaani anakuja kupumzika tu. Na haji
na chochote.”
“Akila vizuri mfululizo labda wiki moja au mbili,
akapata usingizi mzuri hapa, utasikia anaitwa tena kwao, Unguja. Kwa
hiyo hata yeye alijua mimi ndio nahangaika na watoto. Hawezi
kunilazimishia matakwa ya kwao. Basi nikawakatalia wazazi wake,
nikakataa watoto wangu kuhama shule, na nikawaambia Mina havai hijabu wala
baibui.”
“Wakanitisha hapa wee, wakaniambi maneno yavitisho,
na Kasimu, baba yao akisikia. Maana walikuja wazazi wake wote wawili, kaka zake
na dada yake mkubwa. Mkorofi kweli kweli. Tena kafanana na Mina kuanzia
kichwani mpaka unyayo utafikiri alimzaa yeye! Kasoro roho zao tu, naona
hapo Mungu alinihurumia.”
“Wakanitisha na wanangu. Wakaniambia kama
Kasimu hatawapata hawa watoto, na mimi pia sitawapata. Wakasema
mengi, Kasimu akabaki kimya hapa. Wakaondoka na mtoto wao, na mimi
nikabaki na wangu, ndio mpaka leo sijawaona hata kupotea njia.”
“Lakini ukiniambia kama Kasimu hakuwa akinipenda,
sikubali. Kasimu alinipenda sana, ila kulikuwa na pressure kubwa sana kutoka kwa ndugu zake na dini.
Yeye kama binadamu alishindwa chakufanya.” “Pole mama.” Andy akasikika
kama aliyeingiwa na huruma.
“Asante Andy mwanangu. Lakini ninachotaka kukwambia,
huyu Mina unayemuona hapa, ni kwa maombi. Nimehangaika kwa kufunga na
kuomba ili arudi na awe kwenye hali
hiyo. Muulize Ron atakwambia.” Ron kimya.
“Tulikuwa tukipiga magoti hapa usiku
kuchwa tukimsihi Mungu aturudishie Mina. Siku aliponitafuta kwa ujumbe
akiwa Iringa amelazwa, sikupata ujumbe wake kwa wakati kwa kuwa nilikuwa kwenye
mkesha wa maombi na huyu Ron. Akatuma ujumbe usiku, nikaja kuona ujumbe saa 12
alfajiri baada ya maombi. Ndipo nikapiga simu na kumpata nesi aliyemwazima
simu. Hiyo ni baada ya kama miaka miwili ya kupotea kwake. Ninachotaka
kukwambia mwanangu, huyu Mina ni muujiza wangu. Kwa wengine anaweza kuwa
kituko au asiye na mbele wala nyuma. Lakini hapo alipo huyo, ni muujiza niliohangaika nao kwa
mateso makali kwa miaka kama 8 hivi.”
“Natunza kama yai mpaka nione mwisho
wake. Sitaki aje achanganywe hapo katikati kwa maneno yakumvunja moyo. Hajapita kama walipopita wengine. Hilo hata
yeye anajua. Anachosoma kwa wengine si kitu, lakini kwangu au kwetu ni muujiza
mkubwa mno. Ile tu kuona anakaa chini na kujifunza kitu, na kukizingatia!”
“Na akarudi nyumbani.” Ron akaongeza. “Ewa! Kama alivyosema Ron. Ni muujiza
ambao hakuna anayetuelewa. Hata Mina mwenyewe haelewi ila mimi na
Ron tunajua ni nini Mungu ametutendea.”
“Kwa hiyo nikuombe kitu Andy mwanangu, naomba tumpe
nafasi tu. Acha sisi tukokotane
naye kidogo kidogo, hivyohivyo. Kama ni mpango wa Mungu akasogea na kufikia
hivyo viwango vya juu, mkaja kukutana tena, basi. Ila kama sio
bahati yake, Mungu akusaidie upate unayefanana naye. Lakini huyu Mina
nakuomba atulie baba. Tafadhali sana. Mwache tu tuvutane hivyo
hivyo kwa daraja letu sisi. Ila sidhani kwa sasa kama yupo tayari kukutana
na watu wa madaraja yenu hayo. Mtamchanganya na kumfanya
atilie mashaka hata kile anachokifanya sasa. Sijui kama
umenielewa?” Andy akanyamaza.
Akajua ndio amenyang’anywa mke. Ndio anafukuzwa
ukweni. Andy akabaki kimya kwa muda akiwa ameinama. Wakamuona anasugua mikono.
Kama anayetaka kuzungumza jambo, anashindwa. Akavuta pumzi kwa nguvu
akiwa vile vile ameinama. Pakawa kimya kabisa.
Mwishoe akaona azungumze tu. “Naomba radhi mama, kwa kushindwa
kusimama na Mina.” Akaanza Andy macho mekundu. “Naomba mnisamehe sana.
Samahani.” Kimya. “Naomba niwaache mpumzike. Muwe na usiku mwema.” “Na wewe
pia.” Akasimama Andy. Akasogea mpaka mlangoni akageuka.
“Nampenda sana Mina. Sana. Sikuwa naye kwa majaribio.
Nilitaka awe mke wangu. Nilimpeleka nyumbani nikifikiria na wao wataona kile
nilichoona mimi kwa Mina, mbali na vigezo vingine. Lakini nasikitika
imekuwa tofauti na imenigharimu kumkosa Mina. Usiku mwema.” Andy akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Mina ni kama akajionya hata hakutuma ujumbe wa bahati
mbaya kwa Andy akiuliza kama alifika nyumbani salama au la. Andy naye akatulia
kabisa. Hapakuwa na mawasiliano hata ya ujumbe kati yao. Jumapili hiyo ikaisha
pakiwa kimya na ahadi zote za huba kuzikwa na kina Ruhinda na wenyewe
kushindwa kuzitetea..
Mtafutaji
Asiyechoka!
Wakati huku
mahusiano ya Andy na Mina yameingia msukosuko wazazi nao wakiwa
wameingilia kati, huku kwa Pam na Mill mahusiano yao yakaanza kwa kasi.
Mill yupo na Pam kama mke kabisa. Anamuwazia kuanzia asubuhi
mpaka usiku anakwenda kulala. Swala la kuhama na usafiri ikawa kero yake
yeye Mill. Kila wakati anawaza hilo tu. Shida ikawa yake kuliko Pam mwenyewe. “Sitaki
mtu amnyanyase Pam wangu.” Akakusudia moyoni.
Akamuomba aanze
kutafuta pakuishi. “Nasita kutoka kwa shangazi Mill! Najiona kama najitenga
na kujiweka peke yangu!” “Umekua Pam. Hata yeye mwenyewe atakupongeza.” “Tatizo
likinipata huko?” “Pam mpenzi! Naomba tutembee kwa imani. Naweza nisiwe
na majibu yote sasahivi, lakini naomba weka imani.” Kama kawaida yake. Mill
alijaliwaga hekina ya maneno. Alijua kuzungumza kiasi cha kumuweka sawa
Pam kila wakati.
Wakati
akiendelea na juhudi ya kutafuta chumba sehemu karibu na Kinandoni zilipokuwepo
ofisi za Sandra, karibu sana na Ubalozi wa Ufaransa, Pam akaanza kupokea mahela
kutoka kwa Mill. Ya kodi na ya kununua gari. “Huna haja ya kuagiza. Tembelea
kwenye yard. Nunua tu hapohapo nchini.” “Au ninunue kwa Sandra? Huwa
anakuaga na magari anauza kwa wanaokopa na kushindwa kulipa. Yanakuwa na
bei nzuri.” “Hapana Pam. Hayo magari yamebeba vilio vya watu. Yanauzwa
si kwa hiari ya wa miliki. Iweje uje upokonywe kwa nguvu huko barabarani? Ni
bora tugaramie, uwe salama.” Hilo nalo likakaa sawa.
Pam akafanikiwa
kupata chumba Mkwajuni. Chumba kimoja na sebule. Hakuchukua muda, akakijaza
vitu muhimu. Wakati akifanya yote hayo ni Mill peke yake aliyekuwa akijua mbali
na mama yake mzazi ambaye ndio msiri wake. Walifanya mambo yao kimya kimya. Na
yeye hakubadilisha maisha hata kuanza kujinunulia nguo mpya au kununua vyakula
kazini. Pesa akawa anabania. Hata waliokuwa karibu naye hawakuona chochote cha
tofauti.
Jerry hakujua
kinachoendelea tena kwani wawili hao walibaki kuwasiliana wenyewe. Na yeye Pam
kazini hakusema chochote. Simu za Mill anapokea na kuzungumza faragha.
Hakuna aliyejua kinachoendelea kumbe Pam ndio ameishia kujazwa madola.
~~~~~~~~~~~~~~
Alipokamilisha
chumba chake ndipo akaaga sasa kwa shangazi yake na mjomba. Na akawapa na
zawadi ya shukurani, akahama. Uhuru ukaongezeka. Ndipo akanunua gari
sasa, tena hapohapo mjini. Akabahatika gari nzuri sana. Pam akawa wa usafiri binafsi
sio wakudandia daladala. Ndipo minong’ono ikaanza sasa ofisini, ila hakuna
mwenye jibu juu ya mabadiliko yake.
~~~~~~~~~~~~~~
Alipoona
amejiweka sawa, ndipo akamkaribisha mama yake amtembelee mjini. “Njoo mama
yangu uoshe macho mjini.” Mama Eric akafurahi huyo! Uzazi
mzuri. Na yeye ndio msiri wa bintiye. Yupo kijijini, lakini kila
linaloendelea anamuhusisha mama yake kijijini.
Ikabidi amuombe
mama yake, yaani bibi Shelukindo ambaye ni kama miguu yake, amsindikize mjini.
Wawili hao wakatoka milimani, wakatua jijini kwa Pam. Wanawake watatu wa kisambaa
ndani ya chumba kimoja. Vicheko wakati wote.
Mill akipiga
simu basi atampa mama na bibi awasalimie pia. Akazoeleka huyo Mill hata kabla
hajaonana nao. Penzi likanoga. Pam si malaya japo ni dawa ya maradhi
ya wengi wenye gonjwa na maumbile ya kibantu. Akajaliwa juu mpaka
chini. Akajaliwa na rangi ya mama yake, basi shida mjini. Lakini yeye kimya.
Akili, moyo vyote kwa Mill wake.
Bibi Shelukindo
vya mjini vikamchosha, akamkumbuka mumewe, wakamua kurudi na mwanae
kijijini, ambaye ni mama Eric na Pam, lakini bado Pam akiwatunza kwa ukaribu
tu.
Hatimaye Mill
Arudi Jijini. Safari hii kwa ajili ya Pam.
Pam akatunza
siku zake za likizo akimsubiria Mill. Mapenzi ya kwenye simu yakawanogea,
Mill akazidiwa. Mwili unamtaka tu Pam. Shule zilipofungwa tu, kimya
kimya akarudi jijini. Hata Jerry hakujua. Ila Mike na Kamila walijua
kama anarudi mjini. Hakutaka mtu ampokee uwanja wa ndege ila Pam tu.
Pam akawahi
uwanja wa ndege akimsubiria, peke yake. Alipendeza huyo Pam, kwa hakika alivutia.
Ungejua matunzo anayopewa, anastahili. Hatimaye muda ukawadia. Ndege
iliyokuwa imembeba Mill ikatua kwenye viwanja vya ndege vya Mwalimu Nyerere.
Pam alikuwa miongoni mwa wengi waliokuwa wamesimama nje ya mlango kumsubiria
Mill.
Wakaendelea
kutoka abiria tofauti tofauti wa mataifa mbali mbali kutokea Doha, ambapo Mill
aliunganisha ndege yake kutokea nchini Marekani. Yaani karibu na mwisho, akiwa
anakaribia kukata tamaa, ndio anamuona Mill anatoka na masanduku mengi
aliyokuwa ameyapanga kwenye kigari.
Moyo wa Pam ulijaa furaha ya ajabu kumuona Mill. Akashindwa kujizuia.
Akamkimbilia na kumrukia, akajikuta machozi yakimtoka. Mwili wa Mill ni
mkubwa, hakushindwa kumdaka, na kumkumbatia. Pam alikuwa haamini kama ameshikwa
na Mill! Mwanaume aliyefanikiwa kuuteka
moyo wake vilivyo na kuyabadili maisha yake kwa hadhi ya namna yake.
Akambembeleza
hapo, akaanza na busu la shingoni karibu na shavu. Ndevu zilizozunguka midomo
ya Mill na kuungana na ndevu za chini ya kidevu, zikachongwa kwa umaridani
mpaka kukutana na nywele za kichwa pembezoni mwa masikio zikamsisimua
Pam vilivyo.
Ndipo akamkiss
chavuni kidogo, akaja midomoni. Akanyonya midomo yake akiwa amemkumbatia. Kisha
akahamia sikioni. “Na mimi nimefurahi kukuona Pam.” Akamnong’oneza sikioni na
kumbusu na kukumsisimua zaidi.
~~~~~~~~~~~~~~
Huyo Pam
hakuwahi ona mwanamme wa kumpa mwili wake mpaka Mill. Hapo alikuwa tayari na
penzi la Mill bila kuombwa, angempa. Alikuwa akimtamani huyo Mill asijue
mwenzie alikuwa anamuandaa muda wote. Hakuacha kumwambia jinsi
anavyompenda na kumuhitaji. Aliamsha hisia za Pam, hapo walikuwa
wamejiandaa kujifungia kwenye kijinyumba anachoishi Mill na alisha mwambia Pam.
Hapo Pam ameenda
kumpokea, lakini na yeye anasanduku la kuhamia hapo mpaka Mill aondoke nchini.
Alijifungasha vitu vyake vya msingi alivyojua angehitaji anapokuwa na Mill,
akafunga chumba chake na kwenda huko uwanja wa ndege kama anayesafiri.
~~~~~~~~~~~~~~
Atafutaye hachoki, akichoka keshapata!
Hangaika ya Mill hatimaye imezaa matunda. Pam mikononi mwake, na
yupo tayari na fungate ya kabla ya ndoa.
Yapi yataendelea kwa wote?
Mina&Andy je?
0 Comments:
Post a Comment