![]() |
“Pam?” “Naomba tusizungumzie huko.” Akamsikia hata sauti imebadilika. “Mimi mumeo, Pam. Na huu ndio mwanzo wa
kufahamiana.” “Mume tena!” Akawaza Pam. “Nitakufahamu vipi kama kuna mambo unanificha?” “Mambo mengine ni fedheha.
Tuyaache tu.” “Kwangu si fedheha maana mimi ndio wewe, na wewe
ndio mimi. Aibu yangu ni yako na yako ni yangu. Hatuwezi kukwepana tena.
Au unataka mahusiano yetu yawe na vificho?” Akazidi kumuweka
sawa akimbembeleza. “Hapana. Lakini naona…” Akasita.
“Labda niulize. Baba yeye yupo wapi?”
“Wakati Eric yupo darasa la sita, mimi latatu, mama alishika ujauzito wa
mapacha. Wakati huo tulikuwa tukiishi na baba huko Ruvuma. Kipindi hicho au
sijui uwezo, mama hakuwa na uangalizi wa kitaalamu wa hospitalini. Watoto
walifia tumboni, yeye hakujua. Siku za kujifungua zikafika na kupita ikabidi
kuanzishiwa uchungu. Sasa inavyoonekana kwenye kujifungua ndiko kulitokea
makosa. Walivuta wale watoto lakini mama akaathirika vibaya. Akapooza
kuanzia kiuno kuja chini. Na penyewe ni kama aliponea kufa.” Akaendelea.
“Baba alipoona mama amekuwa mzigo. Mtu
wa kuhitaji msaada wakati wote. Hawezi kutembea. Hajui haja
inatoka wakati gani, ni mtu wa kujisaidai hapohapo akatuchukua mimi na Eric pamoja
na mama yetu, na kuturudisha kwa bibi na babu. Inavyosemekana alisema angerudi,
lakini mpaka hivi tunavyozungumza, hakuna anayejua alipo. Hatujui kama yupo hai
au la.”
“Mjomba huyo ninayeishi naye sasahivi,
au aliyetuchukua ukubwani kutusaidia mimi na Eric alisema alishakwenda
kumtafuta huko Ruvuma tulipokuwa tukiishi mwanzo, inavyosemekana alihama,
hakuna anayejua alipo. Ndio hivyo. Tukaishia kuishi kwa bibi na babu.”
“Eric alipomaliza kidato cha nne,
akafaulu shule za bweni. Akafanya vizuri mpaka chuo cha uhasibu. Akawa akiishi
kwa mjomba huku akisoma. Akamaliza na kupata kazi benki, ndipo akafahamiana na
Sandra. Akamuomba anipe kazi. Wakati huo mimi nilikuwa kijijini. Nilimaliza
kidato cha nne, nikafeli. Kwa hiyo nikawa nipo tu hapo, tukisaidiana na bibi
kumsaidia mama, maisha yakawa yakiendelea.”
“Bibi yangu ana roho nzuri sana.
Anaupendo sana na wanae. Alimuomba mjomba amsaidie kudadisi kama kuna
chochote kinaweza fanyika kwa mama. Wakati mimi bado nipo kule kijijini nasoma,
mjomba alikuja kumchukua mama. Akasema kuna madaktari wamefika nchini, wanatibu
wakina mama wenye kistula. Unajua aina hiyo ya ugonjwa?” “Hapana. Labda jina
ndio limenichanganya.”
“Wale kina mama wanapata tatizo la
kujisaidia baada ya kujifungua. Basi akasema atampeleka waone watamsaidia vipi.
Nakumbuka bibi alikuja naye huku mjini. Alikuwa hataki mtu mwingine amuhudumie
asije mnyanyasa mwanae. Kufupisha habari, mama alifanyiwa. Ikasaidia kwa
kiasi. Anaweza kujisikia haja. Ila hana uwezo wa kushikilia kwa muda mrefu. Sio
mgonjwa. Akikaa hivi, unaweza usijue kama ni mlemavu. Mambo mengi anafanya
akiwa amekaa. Na bibi naye anajitahidi naye sana kufanya awe msafi. Kwa hiyo
ukimkuta amekaa, ni mpaka akwambie.”
“Kwa hiyo hiyo ndio historia yetu.
Mimi, Eric na mama. Nahisi hata nikija kukutana na baba yangu naweza
nisimkumbuke. Ni muda mrefu. Na nafikiri na yeye aliweka juhudi za makusudi
tusiwe na mahusiano naye. Maana anapajua kwa kina mama, ila amechagua kutorudi.”
“Pole sana Pam.” Akasikia kuumia.
“Huwezi amini, Mill. Eti inaniuma
sana. Nimeshindwa kuelewa kabisa, mpaka leo! Najiuliza ni baba wa namna gani
anayeweza telekeza mke na watoto wawili, tena baada ya mwenzie kupata
matatizo ambayo na yeye alichangia! Hakika inaniuma sana kiasi ya kwamba
imenijengea chuki kwa wanaume. Naona wote ni matapeli tu.
Wanakutaka kwa kukutumia tu. Unakuwa kama bidhaa tu. Yakutumia, wakishamalizana
na wewe, wanakutupa.” Ndipo Mill akamuelewa
kukwepa kwake wanaume.
“Wamejaa utapeli na usaliti.”
Akaongea kwa uchungu na hasira. “Si wote Pam.”
“Basi mimi sijabahatika kukutana na hao wazuri. Maana wote hao wanaolala na
kina Lona. Au hao wanao wahiwa na kina Lona na wenyewe kukubali,
wote ni waume za watu. Wanawahonga mahela ya aibu mpaka uchungu.” Akaendelea kwa hasira.
“Poliny amezaa na mume wa mtu. Na
alimshikia mimba makusudi kwa sababu anayo pesa. Sasahivi amenunuliwa gari na
anatunzwa na huyo mtoto. Sasa jiulize, huo uaminifu uko wapi? Kama hawa
wanaume wangetulia, hiyo pesa wanayotumia kwa hao wanawake wa
nje, si wangewekeza kwa wake zao na kujenga familia zao? Najiambia
pengine ndicho anachokifanya na baba yangu huko alipo. Kupata starehe ya
wanawake tofauti tofauti kwa garama anayolipa mama yangu na mimi.” “Pole Pam.
Pole sana mpenzi wangu.” Akamtuliza maana aliweza sikia hasira moyoni
mwake.
Mill Naye Na Ya Familia Yake.
“Na mimi nina historia inayofanana na
hiyo ila tofauti kidogo. Imenifanya niwe makini sana na maamuzi yangu juu ya
mapenzi, nikihofia nisije rudia kosa la baba yangu.” Mill akaendelea.
“Ninachoshukuru yeye hakuwa akitelekeza
watoto. Alikuwa akizaa na kututunza. Mimi nililelewa na mama, lakini kwa pesa
ya mzee. Japo mama alikuja kuolewa kwengine, lakini swala la kunitunza
halikuwa likisumbua, kwa kadiri ya uwezo wake. Nilipofika kidato cha nne, mama
mzazi alifariki.” “Pole Mill.” “Asante.” “Pole sana.” “Nashukuru.”
“Akatuacha watatu sasa. Mimi na wadogo
zangu. Baba wa kambo naye akaoa. Ndipo akanitaka niondoke.” “Hee!” Mill akacheka. “Ukifikiria, ni haki yake Pam! Undugu wetu ulikuwa kwa mama. Mama hayupo.
Kinachonibakiza kwake ni nini?” “Na wadogo zako!?” “Wao hawakutaka kusoma.
Waliacha shule mapema sana na kuingia mtaani kujitegemea wakiwa wadogo tu. Wote
wawili ni wakiume. Kwa hiyo kubakia pale ndani na mke mpya, akaona shida.”
“Haya, nikamtafuta baba. Hakuwa na
neno. Kuja kwenda kwake! Huku Dar sasa. Kumbe sikuwa peke yangu. Kuna watoto
wengine nao wanatunzwa kwa huyo mwanamke, napo hapo hana ndoa. Ni mwanamke
aliyezaa naye watoto wawili. Wakike na wakiume. Huyu mwanamke akaonekana amemuweza.
Akambana na kufanikiwa kuishi naye hapo kwenye hiyo nyumba kubwa niliyowakuta
wakiishi. Ndio sasa na yeye anakaribisha watoto wake hapo, kitu kilichokuwa kikimkera
huyu mwanamke.”
“Kumbuka sikuwa peke yangu. Kila mtoto
anatabia zake. Na yeye huyu mwanamke ni wale wanawake walio jiendeleza, anamsimamo
wake jinsi ya kulea watoto wake. Sasa kuchanganyiwa na watoto waliolelewa na
wakina mama tofauti tofauti! Wengine tumekutana hapo ukubwani, hawataki
shule wala kazi. Wengine wazurulaji. Wengine walevi na bangi za ujanani. Ni
fujo kwa yule mama, na yeye hawezi ondoka pale, maana tayari anao watoto wawili
na mzee. Maendeleo mengi ya mzee aliyapata na yeye akiwepo. Anajiaminisha kama
ndio mke halali.”
“Ila hakuwa na mapenzi hata kidogo na
huyo mwanamke. Kila wakati anamwambia akichoka, au akiona watoto wake ni
mzigo, aondoke amuachie watoto pale, atatafuta mwanamke mwingine atakayeweza
ishi na vijana wake.” “Mill!” Pam akashangaa sana.
“Acha mama. Mazingira ya ujabu
na udhalilishaji wa hali ya juu, mimi sikuwahi ona. Maana kule kwa mama
yangu mzazi, kulikuwa na kuheshimiana, japo hapakuwa na uaminifu.
Lakini mzee wa kule alikuwa akifanya mambo yake kwa wizi, mama asijue.” Mill akaendelea.
“Sasa kuja kuishi na baba mzazi! Na
kwenye mazingira ya mama anayewalalamikia kila wakati! Kwanza mzee mwenyewe
alikuwa hashindi nyumbani. Watoto wake wenyewe utajua kabisa hajasingiziwa.
Ni wake. Umbile ni kama hivi unavyoniona mimi. Tulizaliwa wote wakubwa kama
baba. Mbali na muonekano, wengine tabia ni kama za mzee. Walevi
na wahuni kama mzee mwenyewe.” “Jamani!” Pam
akazidi kushangazwa.
“Acha mama. Nakwambia nilitoka kwenye
familia, nikahamishiwa kwenye aina hiyo ya fujo, halafu aliyenikaribisha
mwenyewe hayupo hapo. Kumuona mara chache chache. Akirudi ni usiku, amelewa.
Ukimtaka ni udamke naye kabla hajatoka kwenda kazini.”
“Mchana yupo kazini, na biashara zake,
baada ya hapo, jioni anakuwa baa na wanawake wengine. Mimi nikakazana
kusoma. Hakuwa na shida na si mchoyo na pesa yake, nafikiri ndio maana
wasichana walikuwa wakimpenda. Alinisomesha bila shida. Na mpaka sasa ananisaidia
japo naona anakaribia kushindwa.” “Sababu ya ugonjwa?” Pam akauliza.
“Ugonjwa umemnyong’onyesha. Halafu
imekuwa zile mbio za sakafuni. Amefika ukingoni. Kwa asilimia fulani
inabidi ajirudi sasa kwa huyu mama, ambaye amemuumiza kwa miaka yote. Anajirudi
akiwa mgonjwa, anaanza kuoza! Huyu mwanamke kama binadamu hana
furaha naye. Maana uzima wake alikula na wanawake wengine, sasahivi ndio
anajirudi! Kwa asilimia kubwa utaona jinsi anavyo mnyanyapaa.
Ndio maana nikisikia amezidiwa, narudi kumuuguza.” “Na ndugu zako
wengine?” Akamsikia Mill akicheka kwa masikitiko.
“Wewe tuombee watoto wetu tu.
Uzazi si kila kitu, mama. Yaani wale watoto wapo kunufaika tu. Na
nina uhakika sasahivi mzee anamajuto, hawezi sema. Maana hata
watoto wa huyu mama anayeishi naye sasahivi, walimuona jinsi mzee anavyoishi na
mama yao, basi na wenyewe ni kama wamemzira mzee. Hakuna anayemjali
sana, ndio maana inabidi mimi kuingilia kati. Nikiwepo mimi ndio angalau
mambo yanaenda. Nikiondoka tu, kila mtu anampuuza. Na mwenyewe
anajua ndio maana hataki kukaa tu nyumbani. Na kwa kuwa ni kazi ya
serikali, basi anakwenda hivyohivyo.” “Pole Mill. Pole sana.”
“Asante. Kwa hiyo kwa kukua nikiona
hizo fujo kotekote, kwenye familia ya baba na mama, kumeniongezea umakini
sana. Maana nasikia na babu naye alikuwa hivyohivyo kama baba. Na
vijana wa baba wapo hivyohivyo. Najionya kwa kujikumbusha kila
wakati kuwa makini. Nikishajiingiza sehemu nikaona hakuna muelekeo, siwekezi
muda wangu wala mapenzi. Najitoa mapema sana.” “Na huko nako kuna mapenzi ya
kitapeli? Maana kwenye movie mnaonekana tofauti!” Alicheka Mill. Alicheka sana.
“Usicheke hivyo bwana! Inamaana wewe hujabahatika
hata mzungu?” Alizidi kucheka Mill mpaka kupaliwa. “Bwana Mill!”
“Mimi naona sina bahati. Sijapata mzungu.” “Mmmh! Kwa nini sasa? Hutaki watoto
wakishombeshombe?” Alimfanya azidi kucheka. “Mimi nahisi
wewe haupo serious.” “Huku michezo michezo ya kijinga utajikuta unanasa
wewe mwenyewe.” Akawa hajaelewa.
“Kuna ambao wanaweza jitegesha
makusudi, wapate mimba uanze kuwatunza. Zaidi weusi wa huku. Na mimi hilo nimekataa.
Si nishakwambia nataka nirekebishe makosa ya kuanzia babu yangu?” “Nakumbuka.”
“Basi mtindo wa kuonja onja visivyo vyangu, sina. Nikikwambia naiapisha
nafsi, jua nafanya kwa makusudi kabisa. Sitaki kujiingiza matatizoni kwa tamaa
za muda mfupi. Nipo makini huko na huku. Nikikwambia upo peke yako huko
na huku wala si kwa kukupamba.” “Lakini hunifahamu Mill wewe! Kama na
mimi tapeli je?” Akawa kama anamuonya.
“Usidhani nazungumza na wewe hapa nachoma
muda wangu bure! Nishakuchunguza, nishajiridhisha. Labda tu
uniambie kama hunitaki.” Kimya. “Pam?” Kimya. “Unanikana mama watoto wangu?” Akamsikia Pam
anaanza kucheka. “Naona unataka kunikana mapema kweupee! Au maneno ya Lona
yamekuingia?” “Hata kidogo. Ila wewe ndiye umemkasirisha. Ulikuwa unawanunulia
vyakula, gafla unawaambia huna hela!” Alicheka Mill.
Akacheka sana.
“Mwenzio alikuwa anajivunia kama nini!
Kwamba amepata mmarekani ” “Lona si mwenzangu. Mwenzangu ni Pam. Na
honga yote ile wala si kwa ajili yake. Nia yangu ilikuwa WEWE.” Alicheka Pam. Alicheka sana. “Acha masihara Mill!” “Mimi nimlishe
Lona na wenzie kwa kipi mno!?” Akamfanya Pam azidi
kucheka.
“Hakika mimi sikuwa na habari!
Mwenzio mimi nabania pesa. Sikosei kuja kazini bila chakula. Shangazi
analalamikaga, lakini sijali. Kikipikwa usiku, nakula nusu, nusu naweka cha
mchana nile kazini. Na kitafunwa najitahidi pia kubeba. Si thubutu kumwaga pesa
yangu mjini kwenye migahawa.” “Ndio maana kila nilipokuwa nikiuliza umeagiza
nini, naambiwa hujaagiza. Lakini ndio hata maji ya kunywa ulikuwa hutaki Pam
wangu au kunitesa tu!” Pam akazidi kucheka.
“Mimi nakunywa maji ya bure ya palepale
kazini!” “Mmmh! Ulinifanyia kusudi tu bwana!” “Halafu sikutaka fujo na
Lona. Ni muongeaji sana.” “Na ndiye anayeninyima raha. Maana najua akijua kama
tunawasiliana, atakuingiza matatizoni.” Akatulia.
“Pam?” “Inabidi kuwa makini. Ila sijui
mpaka lini!” “Muda utajibu. Usiwe na wasiwasi. Ninachotaka ni kukutoa
barabarani usiku. Hilo sitaweza kufikiria mpaka nifanikiwe.” Akajua anazungumzia gari.
“Usiwe na wasiwasi. Mimi nipo salama.” “Siwezi kutokuwa
na wasiwasi, Pam. Hapana. Nipe tu muda mpenzi. Tutarekebisha kote. Kwa shangazi
na usafiri. Tutaangalia kipi kianze.” Pam akatulia akimfikiria Mill. Alikuja na gia kubwa
huyo! Mpaka akamfunga akili Pam. Simu ya kwanza tu, wanazungumza na kupanga
kama wanandoa!
“Naomba nikuombe jambo moja muhimu sana
kwangu, Pam.” “Ni nini?” Pam akamuuliza taratibu akimfikiria huyo
Mill anataka kuomba nini! “Naomba tukubaliane jambo. Ndio uwe msingi wa
mahusiano yetu, ambao tutausimamia mpaka mwisho.” Pam
akashangaa.
“Upo au nishakutisha.” “Nakusikiliza
Mill.” “Nashukuru. Naomba tubakie wawili tu.” Pam
akamuelewa. “Mimi si muhuni Mill!” “Hapana. Sijamaliza.” Ikabidi atulie. “Kuachana kwetu iwe ni mpaka tuzungumze kama hivi. Isitokee maneno
ya kusikia yakakufanya ukaniacha, ni mpaka uhakikishe kutoka kwangu mimi
mwenyewe. Tuzungumze, ndio tukubaliane. Na mimi hivyohivyo. Kama hujanisikia
mimi mwenyewe kukwambia tuhitimishe, makubaliano yetu yanabakia ni mimi
na wewe tu.” “Mill wewe!” Pam akashangaa sana.
“Wewe upo huko. Mimi nipo huku. Ukipata
mwanamke huko, ukaamua kuachana na mimi?” “Bila mimi mwenyewe kukwambia,
chochote utakachosikia ni batili. Nisubirie mimi mwenyewe nikwambie. Na
nakuahidi sitakusaliti. Sitakutelekeza. Kilichotokea kwa baba
yako, naomba usinifananishe na mimi.”
“Nakusudia kufanya tofauti na baba
yangu. Na naomba uwe na mimi. Tujenge familia yetu. Tuwape watoto wetu kile
sisi tumekosa. Au unaona ni ngumu sana?” Kimya. “Au unaona
nimeharakisha sana? Kwamba ningevuta muda kwanza. Na maneno mengi ndipo baadaye
nikwambie?” Kimya.
“Mwenzio najua ninachotaka. Na maadamu
nimekupata wewe, sitaki kuvuta. Nakupenda Pam. Nakupenda sana. Ninapokwambia
upo mawazoni mwangu, amini umefanikiwa kuingia moyoni mwangu siwezi kujisaidia.
Ndio maana unaona nimejisalimisha kwako mapemaaa!” Kimya.
“Unanitisha Pam wangu! Ndio
unanikataa?” “Hapana Mill! Ila sikuwa nimejiandaa. Nipo kama nimepatwa na
mshituko.” “Pole. Nikuulize swali?” “Niulize tu.” “Nitangulie kuomba radhi
pengine ndio lilitakiwa swali la kwanza. Upo kwenye mahusiano yeyote?” “Nisingeomba
mawasiliano na wewe, Mill. Wala nisingekuwa na wewe kwenye simu muda wote huu.”
“Nashukuru. Basi kama hakuna mtu, naomba mimi niwe kwenye kuchunguzwa.
Ukiridhika na mimi, uniambie. Sawa?”
“Sawa. Na samahani Mill. Kwenye swala
la mahusiano naomba niwe mkweli. Nimetishwa sana na wanaume. Na kwa
kadiri ninavyoona wanaume wengine wanavyofanya hata pale ofisini kwetu na
wanawake! Imezidi kunitia woga. Unajiuliza mwanaume huyuhuyu yupo na mke
nyumbani, bado yupo na wanawake wengine nje! Anamwaga pesa nyingi kwa mwanamke
wa nje, anabakisha nini kwa mkewe? Inawezekana alianza hivyohivyo kwa mkewe.
Akihonga mapesa. Alipomuoa na kumuweka ndani ndio akageuka kama baba yangu! Inaniuma!
Inaniuma sana na kunitisha.”
“Pole Pam.” “Hivi unavyoniona mimi, ni
kama mama alijizaa. Inamaana thamani yake iliisha pale tu alipopatwa na matatizo!
Kweli jamani?” “Nisikilize Pam na acha kulia. Mimi si
baba yako. Na nimekusudia kuwa na wewe. Utakaposema ‘ndiyo’ kwangu, na
ukatulia na mimi, jua mimi ndiye nitakuzika au wewe ndio
utanizika. Katika shida na raha, jua hutanikwepa. Nitasimama na wewe
bila kuchoka. Unanielewa? Na sina sababu ya kukudanganya. Kwanza kwa nini
nikwambie yote haya? Si ningeishia salamu tu na maongezi ya kawaida kawaida
tu?” “Lakini kweli!” Akawaza kwa sauti.
“Kulikuwa na faida gani au haraka gani
ya kukwambia yote haya na nisha kupata kwenye simu? Si nisingeyaleta yote haya!
Nayaleta kwa sababu mimi mwenzio nishaona mpaka uzee wetu. Pam aliye
bibi si mrembo kama sasahivi.” Akamfanya Pam acheke.
“Kabisa.” “Basi Mill. Nimekuelewa. Mimi
nitatulia na wewe.” “Na hakuna kuhitimisha hewani. Kama tulivyoanza kwa
mazungumzo, tutahitimisha mimi na wewe kwa mazungumzo.” “Sawa.” “Kwa
hiyo nijihakikishie Pam ni wangu?” Pam akacheka
sana.
“Mill ulivyo na haraka!” “Sitaki
michezo ya barabarani. Mwenzio najitunza Pam. Sitaki kuchezewa.” “Hutaki
hata tufahamiane kwanza!?” “Nataka, lakini tukiwa sisi tu. Tusichanganye watu
hapo katikati. Iwe mimi na wewe tu. Tujuane mapungufu yetu na lengo iwe kusaidiana
ili tuendelee, sio tufahamiane halafu tukimbiane.” Mill alikuwa mtu wa kuzungumza vitu sahihi vya kumvutia Pam,
mpaka akamuweka sawa. Yaani mpaka wanaagana, wawili hao wanazungumzia maisha ya
pamoja si kutengana kama wanao anza, ila wanao endelea.
~~~~~~~~~~~~~~
Pam akalala usingizi mzuri. Na alishavutiwa na
Mill. Kwanza muonekano tu wenyewe analipa. Halafu mwanaume anayezungumzia uzee
wake! Mkweli kwake! Hajaanza kama wengine kumtongoza kwa majigambo! Pam
akajiaminisha amepata.
Asijue furaha
aliyoweka kwa Mill. Huko alikuwa akishangilia mpaka Mike akajua usiku huohuo
kama Mill safari hii amepata. Alijawa mipango mpaka Mike akamuhurumia na
kumuomba atulie kwanza.
“Taratibu Mill! Tafadhali
tulia, mchukulie taratibu sana, asije kuja kukufanya kichaa pindi
akikusaliti. Tulia kaka.” “Hakika situlii mpaka mimi ndio niwe wa kwanza
kumfikisha kanisani. Nikishamuoa. Nikafanikiwa kupata naye watoto.
Hapo ndio nitatulia.” Akafikiria akajipinga. “Hapana. Kwa Pam sitatulia
aisee! Labda kaburini.” Akaongea akiwa amejawa tabasamu. Akikumbuka sauti ya
Pam na uzuri wake! Akatamani angekuwa karibu. Lakini ndio amerudi nchini. Akapoa.
Akivuta subira.
Jumatatu.
Mahusiano yakaanza rasmi kati yao. Ila hata Mina
alijua Andy anampenda. Alimchukulia taratibu, vile alivyo. Siku ya
jumatatu alipotoka shule, akaenda ofisini kwa kaka yake. Akakaa nyuma ya meza
yake kama kawaida. Chini kabisa, akaanza kufanya kazi zake.
“Kiongozi huna kazi zako unataka kufanyiwa mtandaoni?”
Hatibu akamchokoza Andy alipoingia hapo ofisini kwao. Andy akawa hajaelewa.
“Tuna kampuni yetu tumefungua mimi na Mina. Mimi meneja masoko. Natafuta
wateja, halafu nampelekea bosi wangu Mina.” Andy akamsikia Mina anacheka nyuma
ya meza. Watu wengine wakaanza kucheka.
“Bosi wako anafanya kazi kwenye mazingira magumu
kweli!” Mwenzao akadakia. “Mwanzo mgumu. Au unasemaje bosi wangu?” Hatibu
akadakia. Mina akaanza kulalamika. “Ron mnyanyasaji! Ananifukuza mezani kwake, anasema
nitamuangushia vitu vyake, wakati mimi nimetulia.” “Wewe hutulii bwana!
Unanifanya nashindwa kufikiria. Kaa tu hapohapo.” Ron akamjibu huku akiendelea
na kazi.
Andy akaenda kumchungulia pale chini alipokaa. Akaanza
kucheka. “Sasa hapo haumii?” “Nitafanyaje? Ron amenifukuza mezani.” Mina
akalalamika. “Njoo ofisini kwangu.” Mina akaanza kucheka huku anaziba mdomo.
Ron hata hakunyanyua kichwa kuwatizama, akaendelea na kazi zake.
“Twende.” Akazunguka kule nyuma alipokuwa amekaa Mina,
akamkusanyia vitu vyake vyote. “Andy!” Mina akanong’ona kama anayesita. Andy
akamshika mkono na kumnyanyua pale. Pakazuka ukimya kila mtu akiwa kama anashangaa,
hawaelewi. Andy ni kiongozi wao, na wanajua yupo na Lora! Iweje leo Mina
anakaribishwa ofisini kwake kwa staili ile! Utani wote ukaisha. Andy aliweza
jua hali ya pale imebadilika gafla kwa alichofanya. Akaondoka na Mina, akamuingiza
ofisini kwake.
Penzi Kikohozi!
Kisha akatoka. “Naombeni niweke jambo moja wazi. Kwa
kuwa sina ninachoficha.” Kila mtu akamgeukia Andy. “Nilitaka kuliweka
wazi hili ili mjue na kuelewa tu. Nipo kwenye mahusiano na Mina. Nimeona
niliweke wazi kwenu kama wenzangu hapa kazini na kwa kuwa mlishakuwa mkimuona
Lora akifika hapa. Lora ametambua uwepo wa Mina kwenye maisha
yangu, na yeye Lora kama binti tuliyekuwa naye tokea watoto, ameelewa na
ameheshimu hilo.”
“Na sisi tutaliheshimu hilo Kiongozi.” Akadakia
mfanyakazi mwingine ambaye yupo hapo na kina Ron. “Nafikiri tunatakiwa kusema
hongera.” Ukaanza utani kidogo, angalau ile hali ya wasiwasi ikatulia pale, Ron
hakuchangia lolote akawa anaendelea na kazi. Andy akarudi ofisini alipokuwa
amemuacha Mina.
Mina alifurahi sana. Akamkuta akicheka. “Unacheka
nini?” “Nimefurahi. Nilikuwa naogopa!” Andy akacheka. “Nilikwambia sina kitu
chakuficha.” “Sasa hivi nimeamini.” “Kwa hiyo ukiwa unakuja, unakuja kujisomea
hapa.” Mina akafikiria kidogo.
~~~~~~~~~~~~~~
“Nini?”
“Tunatofautiana sana Andy.” “Kivipi?” Andy akauliza lakini alijua wazi ni
kweli. “Upo na ustaarabu fulani hivi! Ambao mimi sina!” “Usiogope.
Taratibu utajikuta tunaanza kufanana. Kikubwa ni mimi na wewe tuelewane.
Mengine nitajifunza kutoka kwako na wewe utajifunza kutoka kwangu. Kile
unachokiona kinatakiwa marekebisho, niambie ili tuzungumze.” Hapo Mina
akaridhika.
“Basi naomba nifundishe kula kama wewe.” Andy
akacheka. “Unapenda?” “Sio mbaya nikijua, ili tukifika kwenye migahawa kama ile
uliyotupeleka jana, na mimi nijue jinsi ya kutumia vile vitu vyote.” Hilo likamfurahisha
sana Andy.
“Basi nitaandaa
chakula kesho jioni, halafu nitakufundisha jinsi yakutumia vifaa vyakulia
chakula, si ngumu.” Mina akafurahi na kubaki akitizamia siku ya kesho, ajifunze.
Akakaa hapo na Andy mpaka jioni, wakatoka pamoja.
Jumanne.
Siku inayofuata, jumanne, Mina alitoka
shule, alipoingia tu ofisini kwa kina Ron, Lea akamuita kwa kumkonyeza. Mina
akaanza kucheka. “Mtoto mbaya wewe!” “Nimefanyaje dada yangu?” Mina akauliza
huku akicheka. “Umekaa hapa, unakataa dagaa kumbe unaye sato wako
unambanika taratibu!” Mina alicheka mpaka akakaa.
“Hongera mwaya Mina mdogo wangu! Andy ametulia na
anajiheshimu.” “Asante.” Mina akajibu kwa aibu. “Na utulie hivyo hivyo ili
usimpoteze. Lakini nakuaminia mdogo wangu. Wewe umetulia.” Mina akacheka,
akijua Lea hamfahamu hata nusu.
Mlango wa Andy ukafunguliwa. Akatoka. “Nilijua
umepotea!” “Nilikuwa namsalimia dada Lea.” Mina akasimama na kumsogelea. “Vipi
mtihani?” “Tumefanya kwenye kompyuta, tukapewa majibu yetu hapohapo. Nikisema,
utafikiri najisifia. Heri ujionee mwenyewe.” Andy akacheka huku
wakiingia ofisini kwake.
Baada ya muda wakatoka wawili hao. Andy akaaga kuwa
wataonana kesho, wakaondoka. Ilikuwa saa 11 kasoro. Mina akampigia simu mama
yake na kumwambia anakwenda nyumbani kwa Andy. Mama yake akajibu tu, ‘sawa’.
Nyumbani kwa Andy Tena Ila Kwa Sura mpya.
Walikwenda mpaka nyumbani kwa Andy. “Nilishatoa nyama
yenye mfupa na kuilainisha. Nikupika tu kidogo kwa muda mfupi. Unataka
kujifunza kuandaa meza?” “Hapo nitakuwa nimejifunza vitu viwili kwa wakati
mmoja.” Andy akacheka. Akamvuta karibu. “Unanifurahisha Mina! Una moyo mnyenyekevu
na kupenda kujifunza.” Mina akacheka taratibu.
“Asante.” Andy akamwangalia kama apate busu, akaona
awe mpole. Akamwachia. “Naenda kubadili nguo, nakuja. Kama unataka kuzunguka
kupaona humu ndani, karibu.” “Niambie nikuandalie nini jikoni.” “Hapana.
Mapishi yenyewe ni rahisi sana. Sipiki kitu kigumu. Nakuja sasa hivi.”
Akamuacha pale.
Akatoka na sweatpants ya kijivu na t-shirt nyeupee.
“Andy wewe ni msafi!” “Nimeishi na mapadri. Hapakuwa na jinsi yakutokuwa msafi.
Kila kitu kilitakiwa kiwe sehemu yake. Sasa hiyo ni kwa miaka yote nimekua nao
tokea mtoto mpaka mtumzima! Sina jinsi nyingine ninayojua inatakiwa iwe,
isipokuwa hivyo. Maana hapakuwa na uchaguzi. Hata kama hutaki ilikuwa lazima
uwe kama wao.” Mina akamfuata nyuma.
Akaanza kumuelekeza jinsi ya kupanga meza na vijiko.
Kipi kikae upande upi. Mpaka Mina akamaliza wakati Andy anaendelea kupika.
Akamtolea vitambaa vya napkins. “Njoo navyo hapa jikoni nikufundishe vile
wanavyovikunja kama hotelini kwa muundo tofauti tofauti.” Mina akaanza
kujifunza taratibu.
Hatua kwa hatua, mpaka akaweza. “Unaakili sana, Mina!”
Mina akacheka sana. “Kweli! Sidhani kama kuna kitu utataka kujifunza
ukashindwa.” “Asante Andy. Na wewe ni mwalimu mzuri.”
Wakahamia mezani. Akaanza kumfundisha jinsi yakushika
kisu na uma. Sehemu gani yakuweka napkin ili asijichafue na pia kutumia
kujifutia wakati wakula. Mina akajitahidi kufuata maelekezo.
Kutumia uma na kisu kula nyama yenye mfupa, ikawa
ngumu, akamuhurumia. “Basi nenda kanawe mikono uje ushike kwa mkono.”
“Sasa nitajifunzaje? Acha nihangaike tu mpaka niweze.” Mara
kadhaa nyama ilianguka nje ya sahani kabisa. Anaokota na kuirudisha kwenye
sahani.
Akamuona ameanza kukata tamaa. “Niangalie Mina.”
Akamwangalia. “Ili hiyo nyama isianguke, lazima uishikilie vizuri kwa uma.
Kandamiza uma vizuri kwenye sehemu yenye mnofu. Ukishaona umeishikilia vizuri,
ndio ukate sasa.” Akajaribu. Akamuona anacheka. Akajua anaanza kuelewa.
Kidogo ile hali ya wasiwasi ikapungua usoni. Japokuwa
hakuweza kuacha mfupa mtupu bila nyama kama Andy kwa kutumia hizo nyenzo,
lakini akafurahia kuona na yeye angalau ameweza kukata na kula kwa kisu na uma.
Walimaliza kula, wakaongea kidogo wakicheka.
“Nifundishe na hivyo unavyoshika glasi.” Andy alicheka mpaka akapaliwa. “Mina!”
“Kweli bwana! Nataka na mimi niwe wamaana.” “Wewe ni wamaana hata kama
hutakula kwa kisu na uma. Bado wewe ni wa maana. Hii ni njia tu ya kula.” Mina
akajisikia vizuri. Akasimama na kwenda kumbusu shavuni.
“Asante Andy.” Andy akacheka na kumvuta, akamuweka
mapajani. Mina akawa amemkalia mapajani. Akamvuta mkono na kuubusu mara kadhaa
huku akimtizama. “Nakupenda Mina. Nafurahia kuwa na wewe kila wakati.” Mina
akacheka taratibu. “Asante Andy.”
Akambusu shavuni na kusimama.
“Mimi ndio nakuoshea vyombo. Umepika, naosha vyombo.”
Andy akacheka tu. Wakasaidiana kutoa vyombo, wakipeleka jikoni. Mina akaanza
kuosha wakati Andy anasafisha meza, alivyomaliza akamfuata jikoni.
Akabaki akimwangalia anavyoosha vyombo pale kwenye
sinki. Mina akageuka. “Unawaza nini? Mbona kimya?” Mina akamuuliza na kuendelea
na kuosha vyombo. Kimya.
“Andy?” Akamuita na kugeuka kabisa baada ya kumuona
yupo mbali kimawazo. “Usiwe mbali bwana
wakati mimi nipo hapa!” Mina akalalamika nakumfanya Andy acheke. “Sasa
unawaza nini?” “Nakufikiria wewe!” Mina
akakausha mikono akamsogelea.
“Nini tena?” Mina akauliza kwa upole na kuongeza swali
jingine. “Kuna kitu nimekuudhi au nimekosea?” Mina akauliza kwa
wasiwasi. “Hapana. Lakini sidhani kama unajisikia ninachojisikia mimi,
Mina!” Mina akashangaa kidogo. “Kivipi tena!?” “Ahhaaa! Sijui.” Andy akatoka
nakurudi sebuleni, Mina akamfuata na kwenda kukaa pembeni yake.
“Kwa nini unasema hivyo Andy!?” Mina alikaa pembeni
akisugua mikono yake kwa hofu, akajua ameshaharibu. “Unajua nilishakuwa
na Lora nikiwa nimeshakuwa na wewe. Vile nilivyokuwa nikijisikia wakati
nakushika wewe, ni tofauti nilivyokuwa nikimshika Lora. Ikaanza kuwa shida hata
kumgusa! Na alikuwa akinigusa nilikuwa nikijitahidi kumkwepa kama
hivi wewe unavyonikwepa mimi.” “Sikukwepi Andy!” Andy akabaki
akimtizama.
“Kweli Andy!”
“Ila ni nini? Hivi unajua ni mara ngapi nimekuwa nikijaribu kukubusu na
kukumbatia na wewe kunikwepa?” “Andy!” Mina akaishiwa nguvu. Akamsogelea
na kumshika. “Sitaki ufanye kwa kuwa nimelalamika Mina.” “Hujui ni kiasi
gani nafurahia ukinigusa Andy! Napenda unavyonishika na kila kitu, lakini...”
Mina akasita.
“Nini?” “Nakosa ujasiri Andy!” “Kwa nini!?”
Andy akashangaa. “Andy!” Mina akamshangaa kama vile asichoelewa ni nini!
“Tafadhali niambie. Sielewi tatizo ni nini!”
~~~~~~~~~~~~~~
Love At first
Sight.
Bado tofali zinapangwa. Kutoka kuona, kupenda, mpaka kuweza kuja kuishi pamoja, ni safari
ndefu inayotakiwa kujuana, na kuvumiliana mbali na hisia.
Inaendelea…
0 Comments:
Post a Comment