Baada ya hapo
ilikuwa jioni tu, wakaamua kwenda kula Mlimani City. Wakati wakila, Lona
akampigia Sandra akimpa muendelezo wa mambo ya kazini, akagundua yupo hapo, na
yeye hakuwa mbali, akaamua kumfuata kumkabidhi baadhi ya karatasi ya hicho
walichokuwa wakizungumzia.
Akili ilimpaa
alipofika na kumkuta na Mill naye yupo! Alifurahia Lona, mpaka akakaa kabisa bila
hata ya kukaribishwa! Tena akavuta kiti karibu kabisa ya Mill. Akaanza
kuzungumza yeye, akitaka kumsikia Mill. Habari za huko na mengine mengi ilimradi
tu. Isitoshe akaomba na picha ya kumbukumbu siku hiyo. Wanao mjua
Mill walijua wazi hafurahii ila kuwa muungwana tu kwa Lona.
Alipoona hamalizi, amejaa hapo katikati yao, akichangia kila mazungumzo
kama aliyepagawa, Mill akaomba arudishwe nyumbani, amechoka na safari.
~~~~~~~~~~~~~
Kesho yake
asubuhi ofisini ikawa nongwa. Habari ikabadilika. Ikawa Mill amerudi
nchini, wametoka kwenda kula. Lona akajigamba kwa hili na lile
juu ya Mill, mpaka akamchefua Pam aliyeanza hata kumfikiria Mill. “Ni wale wale tu.” Akajuta hata
kumpitisha akilini mwake.
Alipotoka
hospitalini kumuona baba yake mchana, moja kwa moja ofisini kwa Jerry. “Pam
yupo?” “Acha nikutahadharishe, Mill. Ile picha aliyoomba jana Lona,
akisema kama ukumbusho, imezagaa hapa ofisini, imekua gumzo.” Mill akashangaa
sana. “Kwa nini tena!?” Akamueleza.
“Haiwezekani
Jerry!” “Nakwambia tena. Na hii ofisi ni ndogo na SHERIA yake kubwa
na ya kwanza ambayo wamekubaliana mpaka hata kwa Sandra ni kama
nilivyokwambia. Msichana ANAYEMUWAHI mwanaume
hapa, MWIKO kwa mwanamke mwingine hata kumtizama kwa jicho la pili.”
“Lakini Lona si mwanamke wangu!” “Maadamu amekuwahi, basi hapa inachukuliwa
tayari wewe ni wake. Na katika hilo hata Sandra ilibidi
kulisimamia ili kufanya hawa wanawake wanne, waweze kufanya kazi bila malumbano.
Maana walishapigana hapa. Lona huyohuyo na mwenzie. Safari ile hukumkuta,
alikuwa amejifungua. Sasahivi yupo. Ndio wakawekeana hiyo sheria mpaka kusainishana
kwa Sandra.” Mill akatamani kurukwa na akili.
“Haiwezekani
Jerry!” “Nenda kamuulize Sandra hapo ofisini kwake atakwambia.” “Nampenda
Pam, siwezi kukubali kirahisi! Japokuwa nimekuja kumuona baba, lakini nilikuwa
nikikusanya pesa, ili nije kukaa kidogo, nijaribu tena kwa Pam. Lona hawezi
akanifanya nikamkosa Pam.” “Nahisi katika hilo ushachelewa. Inamaana Pam
ameshajua kila kitu. Amejua upo nchini kwa ajili ya Lona.” “Sio kweli!” Mill
akapinga kwa uchungu kabisa.
“Lakini ndivyo
wote hapa wanavyojua, tena kutoka kwa Lona mwenyewe na ushahidi juu. Picha.
Utapinga vipi?” “Ninachojua ni lazima niwe na Pam.” Jerry akanyamaza. Asijue
safari hii anamshauri vipi tena. Ukimya wa muda, akaamua kuondoka.
Wakati anatoka
akakutana na Pam mapokezi. Mapigo ya moyo yakaanza kubadilika. “Mzima Pam?”
Ikawa kama hajamsikia kabisa, akachukua kabrasha hapo juu ya kaunta, akaondoka
kabisa kurudi ofisini kwao hata asimtizame wala kumjibu. Mill
akajua Jerry alikuwa sahihi na kwa Pam ndio amejifungia milango yote.
Akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Akapotea kabisa
hata Jerry hakutaka kumtafuta kwa muda wakutosha ili tu Lona akose
chakuzungumza. Baba yake alishatoka hospitalini, akawa yupo tu mtaani. Hana
afanyalo, anajipanga jinsi ya kurudi kwa Pam. Mike akawa akimwangalia tu
hana jinsi ya kumshauri. Kwa hakika alikuwa amenyongea. Gafla Mill aliyekuwa na
utulivu wake tu, hana shida, mapenzi yakamnyong’onyesha.
Akiwa amebakisha
siku chache aondoke bila jibu ya jinsi ya kumfikia Pam, akaamua kuyavulia
maji nguo. Akatoka kama mwehu mpaka ofisini kwa kina Jerry. Bahati
yake mbaya akawakuta wote mapokezi, wakiongea na kucheka na pochi zao begani,
akajua ndio wanaagana. Muda wa kazi umeisha. Sandra na Jerry nao pia
walikuwepo. Lona akaanza kumchangamkia, akamuona Pam anageukia mapokezi,
akainamia simu yake. Mill akashindwa kujizuia.
“Samahani
Lona. Ni kwa heshima kubwa sana, lakini nimekuja hapa kwa ajili ya Pam.”
Pakazuka ukimya. Pam alishituka na kugeuka. “Samahani sana. Lakini huo ndio ukweli
na siwezi kuendelea kujificha. Na sio kwamba nimekuja tu hapa kutokea
Tabata, hapana. Nimetoka mbali kwa ajili yake.” “Mimi nilishakuwahi.
Pam hawezi kutuingilia.” Bila woga Lona akaongea mbele yao bila kupepesa
macho.
“Najua mna
sheria mmejiwekea. Lakini nilitaka Pam anisikie mimi mwenyewe. Nimevumilia, nimeshindwa
na mimi naondoka nchini. Siwezi kuondoka nalo hili moyoni bila ya
kumwambia Pam mwenyewe. Aliyenirudisha hapa nchini ni Pam, na mzee wangu
ni mgonjwa. Ni hilo tu nataka Pam UNIELEWE.” Hapo akamwangalia Pam
kabisa mpaka akainama kama aliyekuwa hajui chakuzungumza.
“Basi haitawezekana
tena. Maana ndio sheria kubwa ya hapa, na hata Sandra mwenyewe anajua.
Tulikubaliana tokea zamani. Huyo Pam kama angekuwa anakutaka, angekuwahi
tokea mwanzo. Mimi nishakuwahi, hawezi hata kukusogelea tena.”
Mill akamtizama akiwa anaweka huo msisitizo wake, alipomaliza tu, akageuza
macho kwa Pam.
“Pam?” Akamuita,
kimya akiwa ameinamia simu yake. “Lona alitukuta Mlimani City akiwa amemfuata
bosi wenu. Hatukuwa na miahadi mimi na yeye. Na yeye ni shahidi yangu,
huyu hapa. Namuheshimu kwa sababu ni dada mzuri tu na anajali. Lakini wewe
ndio sababu ya kunirudisha hapa nchini. Sina uwezo wa kurudi huku kwa
mwaka mara tatu au nne. Nimelipa garama kwa ajili yako.”
“Nimetoka mbali
kwa ajili yako, wewe, Pam. Na ujue tu mimi si tajiri mwenye mapesa mengi
ninayezunguka tu kwenye ndege! Hapana.
Sina hata vigezo vya kuweza kukopeshwa kwenye kampuni kama hii yenu, hata kama
nikitaka kukopa nionekane na pesa kama wengine mliozoea kuwaona hapa, mimi
siwezi. Na huu ni ukweli.” “Mmmh! Huo tena msala! Wote mnakuwa
mnalia shida!” Akakejeli Lona na kucheka kwa sauti tu na kufanya wenzie
wawili pia wacheka.
Lakini Mill
akaendelea. “Kuniona hapa, jua ni juhudi tu. Nilikuwa nikifanya kazi kwa
nguvu zote. Mchana na usiku ili tu nipate nauli ya kurudi huku, nikuone wewe,
Pam.”
“Nasikitika muda
umeniishia, nimeshindwa kuzungumza na wewe. Na kesho naondoka. Ni hilo
tu nilitaka ulisikie kutoka kwangu mimi mwenyewe kabla sijaondoka.” Pam hata
hakumjibu wala kumwangalia. Akabaki ameinamia simu yake. Kimya.
Mill akaondoka.
Na Pam naye akaondoka hapo mapokezi kurudi ofisini kwao wakati walikuwa
wameshafunga hata kompyuta. Inamaana siku ya kazi ilisha isha. Lona na yeye
akatoka kwa haraka kama anayemuwahi Mill. Wengine wakaondoka kimyakimya.
Siku Aliyokuwa
Akiondoka Nchini.
Siku aliyokuwa
akiondoka Mill nchini alikuwa akiondoka na Mike pamoja na Kamila. Lakini
kulikuwa na mvua karibia siku nzima. Kamila alishakuwa amemuandalia vyakula
mbalimbali vya kubeba na kuondoka navyo nchini kama kawaida yake kumfungashia
Mill vyakula vya nyumbani na wao wakawa wameshajifungasha vya kwao tayari kwa
safari. Ndege ilikuwa ikiondoka saa nne na robo usiku. Kupitia uwanja wa ndege
Doha kisha moja kwa moja mpaka JFK nchini Marekani. Kisha wangechukua gari ya
kukodi hapo uwanja wa ndege JFK, mjini New York, yakuwapeleka mjini Maryland ambapo anaishi
Mill.
Mike alikuwa na
Kamila kwenye nyumba yao kubwa. Walimpa Mill nyumba ndogo ya uwani. Kwa hiyo
kila alipokuwa akifika nchini, anashukia hapo. Akawafuata nyumbani kwao kwenye
hiyo nyumba kubwa. Akaanza moja kwa moja. “Kuna mvua sana. Nina wasiwasi na
Pam.” Wawili hao wakabaki wakimwangalia. “Namaanisha jinsi atakavyorudi
nyumbani.” Kimya. Mike na Kamila wakabaki wamemkodolea macho.
“Mbona
mnaniangalia tu kama naongea kigiriki?!” “Sijui unataka nifanye nini Mill!
Foleni sasahivi ni mbaya. Jiji limefunga, na yamebaki masaa machache tuondoke
nchini. Hivi nilitaka kukupigia nikushauri tuwahi kuondoka, kupambana na foleni
ili tusichelewe ndege.” “Namaanisha hivi, sitaondoka hapa nchini bila ya
kujua kama Pam yupo salama na mvua hizi pamoja na radi.” Akaongea kwa
msisitizo.
“Labda tumpigie
simu Jerry, umuulizie wakati tukielekea uwanja wa ndege.” “Hapana.
Nataka kwenda mimi mwenyewe.” Mike akabaki akimtizama.
“Basi au mimi
nichukue usafiri mwingine, tukutane uwanjani.” “Kama umekusudia kwa kiasi
hicho, basi tuondokeni sasahivi.” “Una uhakika? Maana sitaki kuwavurugia
mipango yenu.” “Mpango tulionao na Kamila ni kuondoka na wewe. Na kwa
asilimia kubwa yupo tayari. Naomba tumpe kama dakika 20 ajiweke sawa ndio
tuondoke.” “Sawa.” Mike mtu wa watu. Anaweza kuchukuliana na yeyote.
Mill alimjua. Sio rahisi kumkwaza Mike. Hata hapo yeye aliongea kwa
amri, lakini Mike akiwa ametulia kabisa. Alipopata alichokitaka, akaondoka
kurudi kwake, nyumba ndogo.
Baada ya nusu
saa wakawa kwenye gari kuelekea ofisini kwa kina Jerry, wala si uwanja wa
ndege. Barabarani akawa ametulia, anatamani Mike aliyekuwa akiendesha, apaishe
gari kama anayewahi kuokoa kitu.
Wakafika mpaka
ofisini kwa Jerry. Wakakuta karibia wote wanatoka. Mmoja wao alipanda kwenye
gari lake ni kama akawapa lifti kina Lona na mwenzie. Wakatulia kidogo wamuona
Sandra, Jerry, vijana wake wawili na Pam wanatoka. Wale vijana wawili wakapanda
kwenye magari yao, Jerry akafunga milango ya ofisi, yeye na mkewe wakaondoka na
kumuacha Pam amesimama pale nje. Wakamuona anatoa simu kama anayeangalia
ujumbe. Kisha akabaki amesimama peke yake.
“Naomba usogeze
gari pale ujaribu kumpa lifti.” “Unauhakika Mill! Maana hujui anapoishi!
Hatujui itabidi tumpeleke umbali gani na sisi tuna safari! Tutachelewa ndege.”
“Nina uhakika Mike. Hakika siwezi kuondoka hapa nchini na
kumuacha amesimama pale. Sitaweza Mike. Sitaweza kufanya chochote
huko niendapo. Kwanza sitaweza kuondoka.” Mike aliposikia hivyo na
hapakuwa na mwanya uliowekwa wa kushauri akasogeza gari.
“Hujambo Pam?”
Pam akawaangalia wote ndani ya gari. “Sijambo. Habari?” “Nzuri tu. Tunaweza
kukusogeza kuliko ukae hapo peke yako.” Mike akawa muungwana yeye ndio
akazungumza naye. Mill kimya pembeni yake. Kamila kiti cha nyuma amejituliza.
“Mimi nipo sawa. Nashukuru.” “Mvua inanyesha na barabara zimefunga. Nina
uhakika hata daladala zitakuwa hazitembei tena mida hii. Unarudije nyumbani?”
Mike akashika kazi ya kumbembeleza ili watoke hapo.
“Mimi nipo sawa.
Namsubiria kaka. Alisema atakuja kunichukua ndio maana nimebakia hapa
nikimsubiria.” Mike akamgeukia Mill. “Hakika siwezi nikaondoka nikamuacha
hapo nje na walinzi.” “Utafanyaje Mill, na mwenyewe amekataa?
Anamsubiria kaka yake.” “Niache nisubirie naye. Nyinyi tangulieni na
mizigo yangu. Nitachukua taksi kuwafuata.” “Mill!?” “Hakika siondoki
bila kuhakikisha yupo salama.” “Kuna walinzi hapo. Kwa nini usiwaamini
naye?” “Ingekuwa ni Kamila, ungemuacha hapo?” Mike akakwama.
“Nawaachia kila
kitu changu. Check in mizigo yangu yote, niachie carry on yangu
tu. Mimi nakuja nikikimbia.” Akashuka bila kutaka kumsikiliza tena Mike.
Ikabidi kweli Mike na Kamila wawahi uwanja wa ndege na mizigo yake. Yeye
wakamuacha.
Kwa Mara ya
kwanza Mill&Pam peke yao.
Akamsogelea pale
ukutani alipokuwa amesimama. Macho yakagongana, kwa haraka sana Pam akakwepesha
ya kwake na kurudisha kwenye simu. “Pam!” Akamuita kwa upendo, akamwangalia.
“Nataka kuhakikisha upo salama. Nitasimama hapa ili nisikukere. Ukija
kuchukuliwa, na mimi nitaondoka.” “Mimi nitakuwa salama tu! Ungeondoka na
wenzio uwahi ndege!” “Hakika siwezi. Sitaweza hata kufikiria
nikijua nimekuacha hapa nje peke yako! Acha nikuache kwenye mikono salama ya
huyo kaka yako, ndio niondoke kwa amani.” Pam akatulia.
Mill akajivuta
pembeni kabisa. Lilikuwa baraza kubwa tu, juu limefunikwa na kumezungushiwa
ukuta mzuri tu. Upo nusu wa hilo baraza kisha ngazi nne tu. Akawa amesimama
kama mwisho, Pam mwanzo. Kimya akiangalia simu yake, yeye Mill ametulia tu.
Baada kama ya
dakika 5, akamuona anamsogelea. Akaenda kusimama pembeni yake. “Asante
kujali.” Akamsikia akiongea kwa sauti ya chini. “Karibu. Lakini naomba usiwe
unafanya hivi, Pam! Wanadamu ni wazuri kukiwa na mwanga. Kukishakuwa na giza,
wanageuka kuwa wanyama wa hatari waliojawa uchu
wakupitiliza. Si sawa. Tafadhali ongeza umakini.” “Kaka
aliniahidi tokea mchana kunipitia. Anafanya kazi benki.” Akamtajia. Hapakuwa
mbali sana na hapo.
“Ni Teller.
Nahisi pengine anafunga mahesabu ndio maana hata ameshindwa kunitafuta. Si
unajua ni mpaka wao waweke sawa mahesabu ndio watoke?” “Umejaribu kumpigia?”
“Simu yake siipati. Ila atanitafuta tu.” Mill akatulia. Pam anayezungumza naye
hapo, amepoa na sura ya kike. Si jeuri kama alivyozoeleka.
“Unaendeleaje
lakini?” “Vizuri.” Akamjibu kama anayepata shida kumtizama. “Vizuri hii
ni ya jibu la wote, au kweli unaendelea vizuri?” “Mimi naendelea vizuri
kabisa.” Akajibu vizuri kwa aibu zile za kike kabisa na kuzidi kumvutia Mill.
“Baba
anaendeleaje?” Ikabidi na yeye kuwa muungwana, akamuuliza. Mill akamtizama kama
ambaye hakutegemea. “Uliniambia ulirudi nchini kwa ajili yake pia!” Akajua jana
alimsikiliza ila alishindwa kujibu mbele ya wafanyakazi wenzie.
“Anaendelea vizuri. Alishatoka hospitalini. Asante kujali.” “Kwamba amepona
kabisa?” “Ugonjwa alionao si wakupona kabisa. Ni kisukari. Na yeye ni mnywaji
pombe asiyeweza acha. Ameathirika. Hivi wamemkata kidole gumba.
Kilikuwa na kidonda. Kimeoza. Hawakutaka isambae. Lakini naona anaendelea
vizuri.” “Afadhali.”
“Nilipokwambia
sikuwa na miahadi na Lona. Yaani kile kilichoonekana kwenye picha
aliyowasambazia si ilivyo, umeelewa?” “Ulisema jana.” “Nataka kujua kama umeniamini?”
“Nimeamini. Lakini hakuna jinsi ya kufanya. Ile sheria ya kuwahi pale
wanaisimamia mpaka Sandra mwenyewe amehakikisha wote ametusainisha na kutuapisha
kwamba hatuta kiuka. Lona amekuwahi, Mill. Hakuna mtu pale
anaweza badilisha hilo.” “Mimi sidhani kama mapenzi ya kweli yanazuiwa na sheria
kama hiyo!” Pam akainama.
“Upendo una nguvu,
Pam! Una nguvu ya ajabu SANA. Labda kusiwepo na penzi. Lakini penye
penzi la kweli, hapatakosekana njia.” Akamuona amekunja uso akiwa bado
ameinama. Mara simu yake ikaanza kuita.
~~~~~~~~~~~~~~
“Ni kaka!”
“Afadhali tujue amefikia wapi.” Akapokea kama aliyepata ruhusa. “Kaka?” Akamsikia akimuita. Akasikiliza kwa muda, akamuona anapoa. “Poleni. Basi
mimi nilikuwa nikikusubiria hapa nje kazini!” Akamuona
anasikiliza kisha akasema. “Hamna neno. Nitatafuta njia ingine.” Akakata akiwa anaonekana ameumia.
~~~~~~~~~~~~~~
Akamuona amepoa.
“Vipi?” “Anasema aliondoka huku mjini tokea mchana, mkewe alimpigia simu mtoto
wao alipandisha homa.” “Poleni.” “Nashauri wewe uende tu, mimi nitatafuta jinsi
yakufika nyumbani. Usichelewe ndege.” “Siwezi kukuacha hapa Pam. Hakika siwezi.
Bora nikose ndege, lakini nihakikishe wewe upo salama. Acha nitembee kidogo
niangalie taksii. Narudi sasahivi, sitachelewa.” Akaondoka kwa haraka.
Pam akamuona
anaingia kwenye mvua bila kujali. “Sasa atasafirije akiwa amelowa hivi!?”
Akajiuliza asiamini. Baada ya dakika kama 8 hivi, akamuona anarudi na magari
mawili. Akashuka.
~~~~~~~~~~~~~
“Huyu
nimezungumza naye, atakupeleka mpaka nyumbani. Kati ya madereva hawa wawili,
huyu anaonekana ni mtu mzima na akili zake ni za mzazi. Hawezi kukugeuka
njiani. Ila niahidi hutarudia kujiacha peke yako kwenye mazingira kama
haya Pam. Ni bora umwambie Jerry akusub..” Akakumbuka kuna Sandra ambaye hawezi
kuruhusu.
“Tafuta mapema
kujua jinsi ya kurudi nyumbani salama. Taratibu tutatafuta gari yako.”
“Nitaongeza umakini. Asante kujali. Uwe na safari njema.” “Na wewe ufike
salama. Acha niwahi.” Pam akampa mkono. Akacheka.
Akaopokea na
kumsogelea kisha kumbusu shingoni vizuri. Alimsisimua Pam na kushindwa kuelewa.
“Pole. Nimekulowesha kidogo.” “Nakuhurumia wewe utasafiri umeloa.” “Usijali.
Panda kwenye gari na mimi ndio niondoke.” Pam akaondoka na kupanda kwenye hiyo
taksii aliyomtafutia. Akampungia mkono, akaondoka na ndio Mill akaanza
kukimbilia uwanja wa ndege.
Mpenda Chongo,
Kaona Kengeza.
“Nilisikia, lakini si kutoka kwa Lea mwenyewe. Ila kwa
aliyeambiwa na Lea kuwa Gichiri alikuwa akikutaka.”
Mina hakutegemea! “Mliishia wapi na Gichiri?” Andy akauliza taratibu tu.
“Hakuniambia mimi moja kwa moja. Alimtuma Lea kwangu. Lea akaniambia. Lakini
nikagundua Lea mwenyewe kumbe anamtaka Gichiri. Lakini Gichiri ni kama alikuwa
akimuogopa Lea, akidhani ni mali ya bosi wenu. Ndio nikamwambia Lea, akamjibu
Gichiri kuwa simtaki. Lea akauliza
kutaka uhakika, akaniambia maana yeye anamtaka
Gichiri, kama kweli mimi simtaki,
yeye atazungumza naye. Basi, sikujua kilichoendelea. Ndio nikaacha ule mpango
wakuwa sekretari, nikaanza kusomea mambo mengine, nikaacha kukaa pale mbele.
Wakati mwingine nilikuwa nakwenda kukaa chini ya meza ya Ron, nafanya mambo
yangu kwenye laptop aliyoninunulia. Makusudi tu, ili ajue ada anayonilipia naithamini na nimebadilika.”
“Kwa nini leo ulikuja ukilia?” Mina akainama. “Eti
Mina?” “Tokea nirudi kutoka kwa Omar, sijawahi kutoka kama hivi. Kwa hiyo mama
akawa anawasiwasi kuwa nimerudia
tena. Kila nilivyokuwa nikimwambia kuwa ninakutana na mtu kwa mazungumzo tu,
alikuwa akiniomba nirudi nyumbani, kama haamini tena! Iliniuma Andy.
Niliharibu sana nyuma. Mama anahofu na mimi. Hivi hapa nilimuahidi
nitampigia ili kumuhakikishia nipo sehemu salama. Nimesau tu. Naomba nimpigie
nimtoe wasiwasi.” “Utafanya vizuri.” Andy akamruhusu.
~~~~~~~~~~~~~~
Akatoa simu na kumpigia mama yake. “Nipo salama mama. Tumeshatoka hospitalini. Nipo tunazungumza
tu.” Akasikia kama mama yake anamuuliza swali. Mina akacheka. “Kila kitu kilienda salama.” Akamuona anacheka na
kukata simu.
~~~~~~~~~~~~~~
“Angalau ameridhika.” Mina aliongea wakati anarudisha
simu kwenye pochi yake. “Kwani wanajua upo na mimi?” “Hapana! Ndio maana mama
aliingiwa na wasiwasi akitaka nimwambie nitakuwa na nani, nikashindwa.”
“Kwa nini?” Mina akamwangalia kidogo akainama.
“Eti Mina?” “Kwa kuwa hata mimi nilikuwa sijui
nakwenda wapi Andy! Halafu Ron alitusikia mimi na mama tukiongea. Akataka
angalau niwaambie nitakapokuwa, lakini nilishindwa!”
“Fikiria mwenyewe, kwa kule nilikotoka, maisha niliyoishi, halafu eti leo Ron ajue
nipo hapa na wewe, wakati wanajua unaye Lora, unafikiri
angenielewa?” Andy akabaki amenyamaza. Mina naye akabaki kimya akimuacha
atafakari. Alimwambia mazito ambayo yatamfanya abakiwe akimtafakari.
Ukimya wa muda ukapita. Kila mmoja kimya.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kwa jinsi alivyompenda
huyo Mina, wakati huo alikuwa anashindwa
kufikiria japo ameshamjua
huyo Mina ndani na nje! Ingekuwa msichana mwingine, angeshamtafutia sababu aondoke hapo
kwake. Ila kitendo chakushindwa kumfukuza mpaka hapo, akitamani aendelee KUWEPO naye tu hapo, akajiaminisha
ni kweli anampenda huyo Mina.
Ila sasa
atafanyaje na Mrembo huyo anayegombaniwa na wengi, katikati ya jiji hilo
la wajanja! Anabeba kama ilivyo
atajua mbele ya safari, AU ajiachie tu kuepusha dhoruba ya baadaye!
Akabaki
akipiga hesabu, gafla zikageuka kama anazochukia Mina,
zimejichanganya herufi na namba!
Algebra ya Mapenzi.
Andy
atafanyaje?
Inaendelea…
0 Comments:
Post a Comment