Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 6. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 6.

  Bado Andy akabaki hamuelewi. “Nakuhakikishia Andy, hutaki kujua.” “Naomba mimi ndio niwe muamuzi wa nini chakufanya baada ya kukusikiliza, Mina.” Mina akanyamaza. “Tafadhali. Nataka kukufahamu zaidi. Na ninataka kukufahamu kupitia wewe mwenyewe.” “Kwa nini Andy!?” “Kwa sababu nakupenda na nimekuchagua wewe. Nataka wewe ndio uwe mpenzi wangu.” Mina akabaki ameduaa.

Andy aliongea maneno machache lakini mazito kwa Mina. Akarudi nyuma kabisa pale alipokuwa amekaa kama anayemkimbia Andy. Akabaki akimtizama. Andy naye akanyamaza, wakabaki wakiangaliana. Akajifuta machozi vizuri. Akasimama. “Unaenda wapi sasa?!” “Narudi nyumbani kwa mama Ron, Andy.” “Hatujazungumza!” “Hapana. Uliniambia kuna kitu unataka kuniambia. Sasa umeshaniambia, naona mimi niondoke. Naweza kutumia choo kabla sijaondoka?” Andy akasimama kwenda kumuonyesha.

Mina akakaa chooni, akajiosha uso. Ndipo akatoka. “Asante kwa chakula, Andy. Nashukuru.” “Naomba tuzungumze, Mina. Usiondoke tafadhali.” “Naomba nikwambie ukweli Andy.” “Nakusikiliza. Lakini naomba tukae.” “Hapana Andy.” Mina akakataa mpaka akatingisha kichwa.

“Mimi sipo hivyo kama unavyonifikiria nipo. Kama umemuacha Lora kwa ajili yangu, nakuhakikishia umekosea kabisa. Na kama mimi ndiye uliyekuwa ukizungumzia ‘Love at first sight’, ujue kuna mwenzio alijaribu kama wewe, haikuishia vizuri. Naomba mimi niondoke Andy.” Andy akamsogelea.

          Akamshika mikono yote miwili na kumvutia sebuleni. “Nataka kujua iliishiaje?” “Akaanza kunipiga! Mpaka mama akaja kunitoa huko.” Andy hakuwa akielewa. “Ulikuwa umeolewa?” Mina akanyamaza. “Mina?” Kimya. “Tafadhali naomba uwe na imani na mimi! Hata hivyo huna chakupoteza. Hata nikijua, hunipendi, pengine hatutaonana tena, na mimi nakuahidi sitamwambia mtu.” Mina akacheka.

“Kwa hiyo huna chakupoteza. Niambie tu.” “Sijasema sikupendi bwana, ila naona kama tumekuwa na mahusiano au niseme mawasiliano mazuri. Sitaki tupoteze. Mwenzio nafurahia.” “Nakuahidi hatuwezi kupoteza. Ila kutusogeza karibu zaidi.” Andy akamsogeza karibu.

“Nataka kukufahamu Mina. Nilikupenda siku ya kwanza unanifungulia mlango nyumbani kwenu.” Mina akacheka na kujifunika uso na kuendelea kucheka. “Nilivyomchoza Ron?” Mina akauliza huku akicheka. “Kila kitu. Nataka kukufahamu kwa kuwa nakupenda wewe. Hata Lora nimemwambia kuwa siwezi kuendelea naye kwa kuwa hisia zangu zipo kwa mtu mwingine.” “Usingefanya hivyo kwa haraka Andy! Angalau ungezungumza na mimi kwanza, unifahamu kabla hujamuacha Lora, msichana mzuri!”

“Hapana. Wewe umenisaidia kutoingia kwenye ndoa ambayo ingevunjika baada ya muda mfupi sana. Hisia zangu kwako na kuwa mkweli kwake kumenisaidia kumjua Lora wa kweli ambaye alikuwa nyuma ya Lora yule uliyekuwa ukimuona akinibusu mbele yenu. Akileta maua na chocolate. Ni watu wawili tofauti.” Andy aliongea kwa kumfikiria Lora.

“Sijui ingekuaje kama tungeoana!” “Kwa hiyo Andy wewe unatafuta mwanamke wa kuoa kabisa!” “Kwa sasa sitafuti tena. Na ndiyo! Nasubiri nini tena?” Mina akacheka na kuinama kama anayefikiria. “Nikwambie ukweli Mina?” Mina akamwangalia. “Jinsi ninavyojisikia nikiwa na wewe, au nikikushika au ukinishika, sijawahi kujisikia hivyo kabla. Nafikiri ni zaidi ya mtazamo wako wa nje. Huwa nakaa hapa nakumbuka jinsi ulivyonishika na jinsi nilivyojisikia kwa wakati ule.” Andy akaendelea taratibu huku akivuta hisia.

“Ungenihurumia siku ile ya jumapili ambayo nilikuahidi nitarudi kukuona! Kumbe hata Lora alinigundua! Nilikuwa sijatulia, natamani waondoke nije.” “Kweli?” Mina akauliza huku akicheka taratibu. “Na kwa taarifa yako nilikuwa nakuja kwa ajili yangu zaidi.” “Andy!” Akampiga kidogo. “Kwani wewe hata ulijua kama nitakuja kukuona? Kwanza sidhani hata kama jina ulikuwa ukilijua.” Mina akakubaliana na hilo huku akicheka.

“Sasa je! Mimi ndio nilitaka kuja kukuona Mina, ile ahadi ilikuwa kwa ajili yangu. Nashangaa ni kwa nini wewe ndiye uliyeumia!” “Ni jinsi ulivyoniahidi Andy. Ulinifanya nikusubirie siku nzima. Nilikuwa nalia maumivu ya kichwa huku naangalia mlangoni nikijiambia labda utakuja.” Andy akamsogelea karibu. Akaweka mkono pembeni ya shingo huku akimtizama Mina, Mina akajilaza kwenye ule mkono kidogo. “Pole na samahani.” Mina akacheka. Wakati Andy anataka kuinama kumbusu, Mina akakwepa.

“Hapana Andy. Naomba unisikilize kwanza, ndipo uamue.” Mina akajisogeza pembeni kabisa. “Nisikilize kwanza Andy. Ili unijue kwanza. Nimekuwa nikifanya makosa kama haya. Nimeishia kumuumiza mama na Ron. Nimewaahidi kubadilika.” “Okay.” Andy akajirudisha nyuma.

Juu Ya Mina.

Mina akaanza. “Mwanaume wa mwisho niliyekuwa naye, alisema ananipenda hivyo hivyo. Akataka niache kila kitu nikaishi naye.” “Inamaana alikuoa?” Mina akanyamaza kidogo, kisha akaona ajibu tu. “Nilitoroka naye, nikaenda kuishi naye Iringa.” “Kwa nini hukuaga?” “Kwa nani sasa? Mama au rafiki yake?” Hapo Andy akawa ameshachanganywa. Ila akauliza.

 “Kwa nini umuage rafiki yake!” “Ndiye aliyekuwa mwanaume niliyekuwa naye kwa wakati huo, baada ya kuachana na rafiki yao.” Andy akajikaza, na kutulia. Ila akauliza akihisi pengine hajaelewa vizuri. “Kwa hiyo walikuwa marafiki watatu?” Mina akarudi kukaa, Andy naye ikabidi arudi kukaa alipokuwa amekaa tokea mwanzo.

           “Nilianzana na Afidhi, nikiwa kidato cha pili. Tukawa naye kwa muda, lakini kila mtu akasema haniongozi vizuri.” “Kivipi?” Andy akauliza haraka kabla hajaendelea. “Alinitorosha wakati nipo kidato cha pili. Akanifungia kwenye chumba chake kule  Magomeni Mapipa. Nikakaa hapo kama miezi miwili. Ndio rafiki yake, Afidhi, yaani Mozee, akaniambia lazima nirudi nyumbani. Mama atakuwa na wasiwasi.” “Muda wote huo wakati upo na Afidhi hukuwa ukiwasiliana na mama?” Mina akainama na kupandisha mabega kukataa.

“Ehe?” “Sasa ndio Mozee akanilazimisha niondoke. Kila siku Afidhi alipokuwa akienda kazini, yeye akawa anarudi nyuma ananiambia lazima niondoke.” “Alikuwa akifanya kazi?” Andy akauliza taratibu. “Afidhi na Mozee walikuwa wakifanya kazi kwenye magari ya baba yake Omar. Omar alikuwa mwarabu aliyezaliwa hapa Dar, lakini mama yake na baba yake walikuja kurudi Arabuni ndio Omar na kaka zake wakaachiwa mali zote. Lakini Omar ndiye aliyekuwa karibu na kina Afidhi, kama mmiliki wa karibu anayewasimamia kwenye kazi. Wakawa kama wameunga urafiki na Omar. Au nisema Omar aliweza kujishusha akawa kama rafiki yao.” Mina akaendelea.

“Sasa kumbe walipokuwa wakikutana wao watatu, Afidhi akawa anawasimulia mambo yetu.” “Unamaanisha nini?” Andy akauliza taratibu. “Mambo ya mapenzi!” Mina akajibu huku ameinama. “Ehe!” “Sasa ndio akasababisha tamaa kwa wenzake. Alipokuwa akiondoka ananiacha nyumbani, Mozee akawa anakuja ananishawishi nirudi nyumbani, akasema Afidhi haniongozi vizuri. Akaniambia hata hivyo ananidanganya, ameoa.” “Ilikuwa kweli?” Andy akauliza.

“Mozee alikuwa muongo tu. Alikuwa anatafuta njia ya mimi na Afidhi tuachane ili anichukue yeye. Siku hiyo akaja na taksii, akanichukua na kunirudisha nyumbani. Hapo ikawa nilipotea kama miezi miwili hivi.” Andy alikuwa akimtizama Mina kwa utulivu, Mina alikuwa anaongea ameinama.

“Si ndio nikaanzana na Mozee sasa! Hapo nikawa namkwepa Afidhi, na yeye akaniambia Afidhi ananitafuta kama amechanganyikiwa! Inabidi nimkwepe. Tukawa kwenye mahusiano na Mozee, mpaka nikaja kugundua na yeye alinidanganya juu ya Afidhi. Nilipomuuliza, akaniambia alifanya hivyo kwa kuwa ananipenda sana, anaona kama Afidhi hakuwa akinipenda kweli kama eti yeye! Lakini sasa kuanzia hapo nikawa simwamini tena. Nikaanza kumkwepa na yeye.”

“Akaanza kuwa kama amechanganyikiwa. Ananifuata mpaka shule! Nikitoka namkuta ananisubiria nje. Mara aje mpaka nyumbani, ikawa fujo tupu.” “Anataka nini sasa?” Andy akauliza. “Ananitaka mimi!” Mina akasikika kitoto. “Akawa ananililia turudiane. Mimi nikamwambia siwezi kwa kuwa yeye ni muongo! Akawa hasikii wala haniachi. Ananivizia kila mahali.” “Ulimwambia mama?” Mina akatingisha kichwa kukataa.

“Kwa nini sasa hukumwambia mama?” “Ningemwambia kipi niache kipi Andy? Nilikuwa na majanga mengi, matatizo kila mahali. Mama alikuwa akihangaika na kesi zangu mchana na usiku. Kipindi hicho mimi nahangaika na Mozee, mama naye alikuwa akiomba kwa kusihi mpaka kulia kila siku kwa uongozi wa shule nisifukuzwe shule.” “Kwa nini?” Mina akavuta pumzi kwa nguvu, akanyamaza.

“Mina?” Akamuona anajifuta machozi akiwa ameinama vilevile.  “Niambie tu.” Akambembeleza. “Mwalimu mkuu alinifumania kwenye vyoo vyakiume. Wakataka kunifukuza shule, kwa kuwa pia nilikuwa wakati mwingine siingii darasani.” Mina akanyanyua uso na kumtizama Andy. Akakuta ametulia akimtizama. “Nilikwambia inatisha, Andy!” “Nini kilitokea Mina?” Mina akarudisha uso chini. Na kujifuta machozi.

“Basi, ndio mama akawa ananifungia ndani. Anatoka na mimi asubuhi kwenda shule, nakurudi naye jioni. Ukumbuke hizo fujo zote hizo nipo kidato cha nne sasa. Ron alikuwa chuo tayari, huko Dodoma, akarudi, akaniomba nitulie angalau nimalize kidato cha nne. Tukazungumza nikamwambia mimi sipendi kukaa darasani.” “Kwa nini Mina?” “Nilikuwa naona wanatufundisha vitu ambavyo hata sitakuja kuvitumia maishani! Nikaona napoteza muda.” Andy akacheka.

“Kwa mfano nini?” “Mahesabu yale wanayochanganya namba na herufi!” Andy alicheka sana. “Usinicheke bwana Andy! Kwani wewe pale kazini kwenu mnatumia hayo mahesabu?” “Algebra?” “Ehe! Ona jina lenyewe jamani!” Andy akacheka tena na tena. “Kwa hiyo ndio maana ulikuwa hutaki shule?” “Nilikuwa naona napoteza muda. Hata hivyo acha tu niwe mkweli. Akili yangu haikuwa imetulia Andy. Mimi mwenyewe nikikaa na kukumbuka mambo niliyofanya! Najishangaa.” Andy akampa tabasamu akiwa amerudi kutulia tena.

“Ikawaje sasa?” “Kuhusu nini tena?” “Mozee na shule.” Mina akacheka na kuinama. “Usiniache njia panda. Tafadhali nimalizie. Nataka kujua.” Mina akamtizama kama ambaye anamshangaa kutaka kujua uchafu wote huo! Alipomuona ametulia, akaamua kuendelea. “Kabla mama hajanifungia, nilikwenda nikawafuata wote. Mozee na Afidhi. Hapo Omar alikuwepo. Nikawaambia siwataki wote. Na akiendelea kunifuata kila mahali, mama amesema atawapeleka polisi. Nikawadanganya kuwa nimempa mama picha zao. Waniache. Hapo nikawa nimeenda na kijana mwingine hivi. Akawatisha akiwaambia yeye ndio Ron. Basi. Wakaacha kunifuata. Sasa kumbe na Omar akawa ananitaka na yeye.” “Omar bosi wao kina Afidhi!?” Mina akakubali macho chini.

“Ikawaje?” “Mimi sijui alipata wapi namba yangu ya simu, na yeye akaanza kuwasiliana na mimi kwa simu. Akaanza kawaida tu. Ananihusia nitulie niachane na watu wote, nijitahidi nimalize shule kama mama alivyoniambia.”

“Akawa mwema kweli! Ushauri hauishi! Na simu kila wakati. Lakini nilikuja kugundua ni wivu tu. Jamani Omar ana wivu, ule wakupindukia. Hataki hata kuhisi kuna mtu ananiongelesha! Alikuwa akinikuta naongea na mtu yeyote, hata mfanyakazi aliyemuweka yeye mwenyewe, ananipiga.” Andy akakunja uso. “Umevuka mbele, umeniacha nyuma kabisa. Uliishia akikuhusia umfuatilishe mama.” “Ule ulikuwa uongo wakunitenga na kila mtu, na kunifanya nikae ndani. Nilipomaliza tu mitihani ya kidato cha nne, mama akajisahau kidogo tu, na yeye akapata mwanya.” Mina akamwangalia Andy.

“Nakusikiliza Mina.” “Aliniambia ananipenda, anataka anitunze. Niwe mpenzi wake yeye. Akanipanga na mipango mingii. Akaniambia ana nyumba Iringa, niende nikaishi naye. Yeye hatakuwa kama kina Afidhi. Atanitunza vizuri. Basi. Siku hiyo mama alipoondoka tu nyumbani, nikamuandikia ujumbe kuwa nimeamua kuondoka, kwenda kuolewa. Asinitafute wala kuchanganyikiwa kama mara ya kwanza nilipoondoka. Nikamuachia huo ujumbe, nikaondoka na Omar. Lakini Andy, nilijuta.” “Kwa nini?” Andy akauliza taratibu tu.

“Alinitoa hapa, na kwenda kunifungia nyumbani kwake Iringa mjini. Alikuwa na nyumba nzuri kweli. Akaniwekea wafanyakazi wawili. Kila kitu alikuwa akinunua yeye, hataki nitoke nje. Alikuwa kama amepagawa! Hana amani popote anapokwenda, wakati amenifungia ndani! Siruhusiwi kutoka hata nje!”

 “Kwanza tulianza vizuri. Furaha na utulivu. Siku moja wakaja rafiki zake mle ndani, na ndugu zake. Ni wale waarabu kabisa. Sasa mmoja wa rafiki zake akamtania tu. Akamwambia akifa yeye, ataomba anirithi. Atanioa mke wa pili. Na atahakikisha anachangamka kunizalisha kwa haraka ili nisije kumkimbia. Wote tukacheka. Wakawa wanatania hivi na vile, kumbe Omar amekasirika anakaribia kupasuka!”

“Walipoondoka wageni, alinipiga kama anayetaka kuniua. Akaanza kuongea mambo mengi, ndipo nikajua hata sifa alizokuwa akinisifia juu ya umbile na mengineyo ilikuwa ni tamaa tu. Kina Afidhi walimfanya anitamani tu.” “Kivipi?” Andy akauliza tena. “Nikikwambia Mozee alichanganyikiwa, ni alichanganyikiwa kweli kweli. Akawa kama mwehu, anasema yeye hawezi kuishi bila mimi. Akawa ananitafuta kama mwehu. Si ndio Afidhi akajua kuwa kumbe rafiki yake alimzunguka! Wakaanza kugombana kazini na kupigana. Omar akawa anawasikia na kuwaamulia wanavyogombana.” “Kukugombania?” Mina akanyamaza na kuinama.

“Kwa hiyo na yeye ndio akakutamani?” Andy akauliza. “Nilikuja kujua hilo nilipoanza kuishi naye. Bila kosa ananipiga. Mtu unayempenda kweli huwezi kumpiga vile. Alikuwa akinipiga Andy, mpaka napoteza fahamu.” “Sasa kwa nini hukurudi nyumbani?” Andy akauliza. “Alikuwa akinifungia Andy! Sikuwa nikiruhusiwa kutoka wala kuzungumza na mtu. Mpaka wasichana wa kazi wa ndani hakutaka niwe nao karibu. Wafanyakazi wanabadilishwa kila kukicha. Akiona tu nazungumza na msichana wa kazi, ujue anampiga na kumfukuza. Walinzi nao wakawa wanaambiwa walinde nje. Hawaruhusiwi hata kukaribia mlango wakuingia ndani. Ikawa fujo. Akanijengea hofu, nilikuwa siwezi hata kutoka chumbani.” “Kwa nini!?”

“Aliniwekea kamera kila mahali! Akitoka hapo, ujue macho yake yananiona kwenye simu. Halafu alikuwa na pesa nyingi za kuhonga popote. Akawa ananitishia eti hata mama yangu mzazi hawezi kuja kunitoa pale. Mimi ni wake mpaka kifo. Ikawa fujo, yeye mwenyewe hana amani, mimi nikilio kila wakati. Kazi zinamshinda kwa kuwa hana anayemuamini na mimi. Hawezi kusafiri tena kurudi huku kwenye biashara zao. Amebaki na mimi kifungoni.”

 “Basi tukahangaishana wee, ndio kama baada ya mwaka na miezi hivi nikashika mimba. Tena mtoto mwenyewe alikuwa akimtafuta, sina raha! Kila wakati ananiuliza kama sijashika mimba. Sina raha, anataka mtoto, mimi nikawa sitaki kuzaa naye.”

“Uzuri alikuwa hataki nipate shida. Ananinunulia kila kitu, na hakutaka nifanye kazi. Lakini wivu ulikuwa ukimfanya hata tusitulie. Lakini nilimuelewa ni kwa kuwa nilitembea na Mozee, baada ya Afidhi. Na wote walikuwa marafiki sana.” “Halafu ukaja kumkubali na yeye.” Andy akaongezea kugongelea msumari. Mina akainama.

“Lakini nilimuhakikishia kuwa sitamsaliti.” Akaongea kwa aibu bila hata kumtizama. “Ikawaje baada yakushika mimba.” “Jamani Omar alifurahi! Sitasahau! Akawa ananipenda. Akajirudi na kuwa mpole. Lakini akawa ananifungia vilevile.”

“Ila sasa mimi nikawa simtaki hata kumuona. Alishakuwa amenipiga mara nyingi mno. Halafu alikuwa akishanipiga hivyo, anaomba msamaha mpaka analia! Ataapa hapo kuwa hatarudia tena, lakini anakuja kurudia. Kwa hiyo nilijua ni ngumu kuja kubadilika. Ni mtu mwenye mkono wakupiga tu. Basi. Nikiwa na ujauzito wa miezi mitatu, siku hiyo tukawa tupo sebuleni. Yeye ni msafi sana. Yaani ni wale wanaume wanaooga kwa kujisafisha kama wanawake. Huwezi kumkuta na harufu popote, muda wowote. Msafi na harufu safi wakati wote. Anaweza oga hata mara tatu kwa siku. Na hapo ni Iringa, na kuna baridi. Nyumba imezungushiwa vigae, gari anaegesha nje ya mlango. Hachafuki, lakini lazima aoge kila wakati.”

“Kipindi hicho tukawa hatuna msichana wa kazi. Alikuwa na bibi anamleta pale atufanyie kazi. Naye akawa anakuwa mgonjwa mgonjwa. Kwa hiyo Omar ndio akawa anafanya kazi za mle ndani kwa asilimia kubwa, ananiambia mimi nikae tu. Basi. Tulipokuwa hapo sebuleni, akataka mapenzi baada yakumaliza shuguli zake huko jikoni. Baadaye akaamua kwenda kuoga, mimi nikiwa nimejilaza kwenye kochi. Alitaka sana nikaoge naye. Sasa mimi nikamwambia nimechoka, nataka kupumzika. Lakini ukweli alikuwa ameshanikinahi, nasikia shida akinishika. Nikajua nikienda naye bafuni, atanigusa tena. Nikamdanganya kuwa nimepatwa vichomi, nataka nipumzike, ndio nikaoge.”

“Yeye akatangulia bafuni. Omar alikuwa hawezi kukaa na jasho hata tone. Na ilikuwa akiingia kuoga, unaweza kumsahau. Atajisugua kama ametoka shamba! Aliponiacha pale kwenye kochi, nikapitiwa na usingizi. Nafikiri nililala kama dakika 15 hivi. Nikashituka, akawa bado hajarudi. Nikajiambia niwashe tv kwa kuwa Omar aliizima wakati mimi nilikuwa nikiangalia mchezo.”

“Omar akiwa kwenye mapenzi hataki kelele ya kitu chochote kile. Si redio, sio tv au simu. Alikuwa akiniambia anataka utulivu kabisa. Anisikie mimi tu bila mwingiliano wa chochote. Yaani anisikie mpaka pumzi yangu.” Andy akapandisha nyusi moja juu, Mina akainama.

“Alipotaka tufanye mapenzi, alinikuta mimi naangalia mchezo, nikamwambia asubiri kwanza. Akasema mchezo ndio usubiri, akanizimia tv. Basi nilipotoka usingizini wakati yupo bafuni, mimi nikapapasa nikaokota rimoti aliitupa chini, kwenye kapeti. Ile nimeinyanyua tu, na yeye akawa anatoka chumbani anarudi pale sebuleni.” Mina akanyamaza kidogo.

“Nini kilitokea?” Mina akaguna akiwa ameinama kisha akamwangalia Andy. “Nilikwambia hakuwa akitaka niwasiliane na yeyote yule. Kwa hiyo alikuwa akitembea na simu zake kila mahali. Sasa wakati yupo jikoni, nafikiri kuna mtu alimpigia. Akazungumza naye na kuiacha hiyo simu huko huko jikoni. Alipotoka na kuniona nimeshika kitu cheusi, yeye akajua ni simu yake. Maana simu yake ilikuwa na cover jeusi.”

 “Sitakaa nikasahau ile siku. Jamani Omar alinivamia kwa kunirukia. Ile rimoti ikaruka nakuingia chini ya makochi. Akaanza kunipiga kuwa nimetumia simu yake. Nilikataa kwenda kuoga naye ili huku nyuma niibe simu. Nilikuwa siwezi kuongea Andy, jinsi alivyokuwa akinipiga kama mwehu.”

“Yeye mwenyewe analia huku akinipiga, mimi nalia.” “Sasa yeye analia nini?” “Analia anasema nataka kumkimbia. Yeye amejitahidi kunipa kila kitu, lakini mimi siridhiki. Amejishusha amekuwa kama mtumwa wangu, lakini bado siridhiki. Akanihesabia hapo. Analia kuwa nimebadilika hata jinsi ninavyofanya naye mapenzi, sio kama mwanzo. Namuonea kinyaa. Sitaki tena aniguse. Yaani ni shutuma nyingi akilia kama mwehu huku akinipiga. Akasema eti napanga mipango nimkimbie na mtoto wake.”

“Uzuri nyumba yake ilikuwa na kapeti nyeupe. Akawa amenitoa pale kwenye kochi, ananipiga chini. Si nikaanza kutokwa damu, ndio akili zikamrudia sasa. Akajua ameshaua mtoto. Akanibeba na kunikimbiza hospitalini. Mpaka kuja kuonana na daktari, nakufanyiwa vipimo, tukaambiwa mimba imetoka. Jamani Omar alilia, karibu kuchanganyikiwa. Akatolewa pale, akaambiwa inabidi mimi nilazwe. Akaitiwa taksi, ikamrudisha nyumbani. Simu hana, akakumbuka iliingia chini ya makochi. Kufuata, akagundua kama ilikuwa rimoti, simu aliiacha jikoni. Alilia Omar, akarudi hospitalini usiku kama saa nane analia, anaomba msamaha.”

“Yaani Omar anakuwa kama anapagawa na pepo! Anakasirika, likishuka, utamuonea huruma. Lakini nilikuwa nimeshachoka Andy. Mwili ulishachoka na vipigo. Nikawa nimeshakata tamaa hata yakuja kujiokoa tena mikononi mwake. Basi, nakumbuka manesi wakamfukuza na kumwambia arudi nyumbani. Aniache nipumzike mpaka kesho yake asubuhi. Alipoondoka tu, nikamuomba nesi aliyekuwepo hapo anipe simu.” Mina akajifuta machozi.

Nikatamani kumpigia simu mama ili nizungumze naye tu, lakini hofu yakurudi nyumbani ikawa imeniingia. Naona aibu kurudi. Ule muda wote nilioishi na Omar ukanifanya nikae chini nijifikirie, nikaona ni heri nife tu, mama yangu apumzike. Na hapo ukumbuke mama alitulea mimi na Ron, tena yeye peke yake bila msaada.” “Baba yuko wapi?” Akajifuta machozi.

“Alioa mwanamke mwingine wa dini yao baada ya mama kukataa kubadilisha dini kuwa mwislamu. Tena hapo sisi tulishakuwa wakubwa tu ndio anataka eti na mama abadili dini halafu yeye mwenyewe baba hakuwa hata anajali mambo ya nyumbani! Alikuwa yupo kama hayupo tu. Nafikiri alioa wakati mimi sijui nipo darasa la tano, nafikiri.” “Huwa anakuja kuwatembelea?” Mina akafikiria.

“Mmmmh! Sikumbuki. Hata hatukuwa na mahusiano naye mazuri. Kwanza hata hatujali mimi na Ron. Mama alitubadilisha majina mapema sana. Alipoondoka tu, mama akabadilisha majina yetu kabisa. Mimi nilikuwa naitwa Amina, ndio akaniita Aminata. Ron alikuwa Ramadhani, jina la baba yake baba. Mama akaenda kutoa hilo jina. Ndipo akampa jina la Ron. Akatoa kabisa ubini wa baba, akatupa wake. Nafikiri hicho ndio kikamuudhi baba zaidi, akasema hatutaki tena.” “Pole Mina.”

 “Asante, lakini hata sijali. Ni mwislamu yule haswa. Ukimuona huwezi kujua hata alioa mkristo. Amerudia dini yake, na anaishika kwelikweli. Ni yule wa swala 5 mpaka ana alama hapa kwenye kipanda uso. Ana mke na watoto wake wale wakuvaa hijabu. Hawajiachi wazi kama hivi mimi. Hana hata shida na sisi! Kwanza hatuendani kabisa. Tuache hayo.”

“Basi, nikapewa simu, lakini nakumbuka nikashindwa kabisa kumpigia mama. Nilikuwa nahamu nao! Ron na mama. Nilikuwa nina majuto, nikajiambia ni heri nimuombe mama msamaha kabla sijafa pale au Omar akaja kuniua. Nikamrikodia mama ujumbe kwa kutumia Whatsapp. Nikamuomba msamaha. Nikamwambia nipo mahali ambapo sijui kama nitatoka, au kama nitakuja kumuona tena. Nikamkumbusha mabaya yote niliyoyatenda. Nikamuomba msamaha na kumshukuru kwa kutonikatia tamaa tokea nafikiri darasa la saba nilikuwa namsumbua mama. Basi. Nikamtumia ule ujumbe. Haukufika, nikasubiri baada ya muda, nikajaribu kufuta, nikaona inakubali kufuta kwenye ile simu ya yule nesi tu, lakini sio kwa mama. Nikajua akija kuwasha simu hata kama ni siku nyingine, atakutana na ujumbe wangu.”

 “Ulimwambia ulipo?” “Hapana Andy! Sikutaka aje anikute vile. Nipo nimepigwa! Halafu mpaka mimba ikatolewa! Nilikuwa naogopa. Siju ni aibu! Sijui Omar alishanitisha sana mpaka nikawa sina tumaini, sijui! Ila nilichotaka ilikuwa kuomba msamaha na kumshukuru, basi.”

“Kesho yake asubuhi Omar akaja na kuanza fujo tena, anataka waniruhusu nirudi naye nyumbani. Manesi wakamkatalia na kumwambia wanamwitia polisi. Lazima nitibiwe nipone. Sasa mimi nikashangaa. Maana Omar alikuwa anafahamika na kila mtu, na walikuwa wanamuogopa sana pale mjini. Nikashangaa ni kwa nini siku hiyo wale manesi wanamkatalia, hawafanyi kama anavyowaamuru! Basi, wakaja askari, wakamfukuza. Wakamuogopesha kuwa usiku nilizidiwa karibu ya kufa, kwa hiyo akinitoa pale vilevile, nitamfia njiani. Ndio akakubali kuondoka. Nikashinda pale, mchana akarudi, akawa ananiomba msamaha.” Mina akacheka na kuguna.

“Omar akiomba msamaha, utamuhurumia! Nakwambia alikuwa pale wodini amepiga magoti analia. Sasa kwa kuwa mimi namjua, nikawa nipo kimya tu, watu wengine wakaanza kumbembelezea. Moyoni nikawa nasema ni vile hawamfahamu. Hapo alikuwa analia msiba wa mtoto ambaye hata hakuwa anacheza bado huko tumbonj! Akalia hapo wee, mimi nikapitiwa na usingizi.” Akatulia kidogo, akamuona anafuta machozi akiwa ameinama.

“Nikaja kuamshwa na kilio cha mama. Sikuamini Andy! Kumbe usiku ule kabla hapajapambazuka, ule ujumbe ulipoingia kwa mama, ndio akampigia simu yule nesi na kumuulizia. Yule nesi akamwambia kwamba pale ni hospitalini, nimelazwa. Na mume wangu ndiye aliyenileta akiwa amenipiga mpaka akanitoa mimba. Ndio mama akamwambia mimi bado ni mdogo, na Omar alinitorosha tu nyumbani. Akamuomba yule nesi asiniambie chochote, mpaka atakapokuja yeye mwenyewe. Ndio yule nesi akamuhurumia mama, akawaambia manesi wengine. Wakakubaliana wamdanganye Omar.”

“Mama alikuja na Ron, pamoja na polisi kutoka huku Dar ambapo hakuna anayemfahamu Omar. Yule polisi alikuwa kama ndugu wa mama. Akamtisha Omar, ndio Omar akamuomba mama msamaha, akasema atajirekebisha, yupo tayari alipe mahari, anioe kihalali. Mama akakataa katakata. Akasema mimi bado mdogo, hataki niolewe. Akamwambia akija kusikia hata amenitafuta, safari hiyo watamfunga jela. Alilia Omar, lakini akakubali kuniachia. Akataka kutoa gari iturudishe Dar, mama na Ron wakamkatalia. Wakamwambia hawataki hata kumuona pale hospitalini karibu na mimi.”

 “Basi. Mama na Ron wakakaa na mimi pale hospitalini Iringa kama siku tatu hivi, nikaruhusiwa, ndio nikarudi nyumbani. Lakini Andy, nilirudi nikiwa nimejifunza, sikuwa na hamu. Sikuwa natoka, labda mama anitume dukani, narudi nyumbani haraka.”

“Kwanza aibu, hata kwa ndugu huwezi kwenda! Wenzangu nilikuta wapo mbali kielimu. Mimi nikakuta majibu nimepata daraja la tatu kwenda nne.” “Lakini bado ulijitahidi.” “Nilikuwa namasomo yangu hayo, nilikuwa sifeli. Na ndio yaliniokoa.” Andy akacheka.

“Masomo gani?” “Kiswahili, English, nilichukua na mapishi, na historia. Hayo nilikuwa nasoma na kuzingatia kidogo.” Wakacheka kidogo, kisha wakatulia.

“Ehe!” “Ndio basi nimemaliza. Lakini mama na Ron wanawasiwasi sana na mimi. Kila ninapotoka asubuhi, mama alikuwa akiniambia leo mpaka analia, eti anakuwa na wasiwasi hajui kama nitarudi nyumbani. Vile ulivyokuwa ukiniona nakuja kukaa pale ofisini kwenu, nilikuwa nikifanya makusudi ili kuwathibitishia nimebadilika. Sitoroki tena na wala hakuna mambo ya wanaume. Ndio maana nilikuwa nikitoka tu shule, nakimbilia pale kwa Ron.” “Kumbe!” Andy akacheka kama anayefikiria. “Nini?” Mina akamuuliza. “Umejibu mambo mengi sana.” Mina akainama. Pakazuka ukimya. Mina akajua ashakinahiwa na uchafu wake, anatafuta jinsi ya kujitoa. Wote kimya.

~~~~~~~~~~~~~

Pale Penzi/hisia Zinapokutana na uhalisia WENYEWE.

Ndipo Penzi hupitishwa kwenye moto. Hapo ndipo hung’aa au huteketea kabisa.

Andy ametambulishwa kwa Mina mwenyewe.

Uwamuzi ni wake.

Kusuka au kunyoa!

Inaendelea…


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment