Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 5. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 5.

Andy alikaa hapo kwa muda akiwa ameduaa, asiamini kilichomtokea. Akajuta kumuudhi Mina kwa ajili ya Lora ambaye hana hata nidhamu! Akajichukia kupuuza hisia za siku ya kwanza tu pale Lora alipomcheka baada yakumwambia anaridhika na kazi yake. Akajuta na kuona anamkosa Mina sababu ya Lora ambaye ni bure kabisa! Akachukia kudhalilishwa na Lora ambaye ni kama mdogo wake tu! Akafikiria jinsi alivyosoma na kuheshimika na wengine, Lora anamwambia SIO KITU! Akashangaa sana nafsini mwake, akaona heri aende tu mazoezini. Maana ni kama kichwa kilikuwa kinataka kupasuka.

Alikwenda gym. Alifanya mazoezi siku hiyo zaidi ya siku zote alizokumbuka kukaa gym. Kila kiungo alikipatia zoezi zito, mpaka ile sauti ya Lora ikaanza kupungua masikioni kwake. Akakimbia kama lisaa lizima kwenye mashine kitu kisicho kawaida yake. Akasikia kifua kimefunguka. Ndipo akarudi nyumbani.

Mapenzi Ni kama uyoga, huota popote.

          Hakuchagua kumpenda Mina. Alijikuta tu moyo umependa. Alioga na kwenda kujitupa kwenye kochi, angalau akiwa ametulia lakini mawazo yakiwa kwa Mina. Ujumbe ukaingia. ‘Nimepata barua. Asante Andy.’ Moyo wa Andy ulijawa furaha, akacheka. Ulielewa? Na je, ujumbe ulileta maana?’ Akauliza Andy. Akaona amesoma.

‘Kwanza nilifurahi kuona umechukua muda wako kukaa chini na kuniandikia mimi! Najua una majukumu mengi, Andy. Lakini kitendo cha kuandika na kuniletea mpaka pale, nimeona umenithamini. Asante. Na samahani kama nilikuwa mkali sana kwako. Sijui kwa nini niliumia sana! Samahani.’ Mina akamrudishia ule ujumbe.

‘Hapana. Mimi nilikukosea. Samahani na pole.’ Andy akarudia tena kuomba msamaha. ‘Yameisha. Uwe na usiku mwema.’ ‘Kuna sehemu niliomba kuanza upya. Sijui ulisoma?’  Akarudisha huo ujumbe kwa haraka.

Mina akacheka. ‘Niliona, lakini sikuelewa Andy!’ ‘Ukinipa nafasi, nitakueleza vizuri.’ Mina akabaki akitafakari. Muda kidogo ukapita akisubiri. ‘Umeshalala?’ ‘Hapana. Nafikiria.’ ‘Tunaweza kukutana?’ Akamuuliza. ‘Sidhani. Maana nakuona upo na majukumu mengi Andy. Halafu una watu wanao kuhitaji. Sitaki tuwekeane tena ahadi ikashindikana tena.’ ‘Nipe nafasi ya pili, utaona mabadiliko.’ Akarudisha hayo majibu kwa haraka.

‘Labda uniambie wewe ungependa tukutane wapi! Mimi natoka darasani saa nane mchana. Jumatatu mpaka ijumaa. Jumamosi na jumapili baada ya ibada, nakuwa tu nyumbani.’ Mina akarudisha huo ujumbe.

‘Basi naomba jumamosi hii, mida ya saa nne asubuhi tukutane. Nakukaribisha nyumbani kwangu.’ ‘Nyumbani kwako!?’ Mina alishituka ndio maana akauliza hivyo. ‘Ndiyo. Sehemu ninayoishi.’ Mina akashindwa ajibu nini.

‘Mina?’ ‘Naogopa Andy!’ ‘Kwa nini? Au huna imani ya kuwa sisi peke yetu tu?’ ‘Hapana Andy. Wewe nakuamini. Lakini watu wanaotuzunguka, hawawezi kutuelewa! Zaidi wewe unajulikana kuwa ni mpenzi wa Lora. Naamini hata yeye hatafurahia kujua kama nipo kwako. Labda kama na yeye atakuwepo.’ Andy akausoma ule ujumbe. Akaishiwa nguvu kabisa.

‘Tunaweza kukutana sehemu ya nje tu, lakini sidhani kama nyumbani kwako ni sehemu sahihi. Naomba na wewe ufikirie Andy. Tafadhali. Nina maana nzuri tu kusema hivyo.’ Mina akaongeza ujumbe mwingine. ‘Nimeelewa Mina. Kuna sehemu nyingine ambayo wewe unafikiria tunaweza kupata wakati mtulivu na kuzungumza?’ Andy akauliza akimpa nafasi na yeye achague.

‘Kwa haraka sina sehemu ninayofikiria. Lakini leo ni jumatano. Naomba tupate muda wakufikiria. Halafu tutajulishana. Ni sawa?’ Kadiri alivyokuwa akisoma majibu ya Mina, moyo wa Andy uliendelea kufurahia. ‘Wazo zuri. Nashukuru Mina.’ ‘Asante Andy. Usiku mwema.’ ‘Na wewe.’ Angalau majibizano hayo yakamtuliza kabisa Andy.

~~~~~~~~~~~~~~

Lakini yale mazungumzo yakaibua wasiwasi mwingine kwa Andy. Lora anajulikana na wengi kama mpenzi. Tena kwa mabusu ya hadharani. Leo gafla anaonekana na Mina! Akakumbuka jinsi Ron anavyomchunga dada yake! Akajua Ron hatakaa akamuelewa.

Lea ambaye amekaa na Mina pale kazini na mara zote aliwakuta wakizungumza na kucheka, je? Halafu Lea alishakuwa akipokea maua na chocolate kutoka kwa Lora, akitaka amfikishie yeye Andy. Kwa muda mfupi sana tokea wawe na Lora, Lora alishakuja pale kazini, wakatoka pamoja, tena Lora akiwa amemshika mkono na kumuegemea kabisa, watu wote wakiona, na wakati mwingine Mina alikuwepo.

Muda mfupi Mina aliofanya kazi pale akielekezwa kazi na Lea, na kwa kuwa alikuwa mdogo wake Ron, alishajulikana na kila mtu pale kazini kwao. Na kwa utundu wa Mina, na vile anavyomchokoza kaka yake kila mara, wafanyakazi wote pale kwenye ofisi ya hapo Samora, walimfahamu Mina vizuri tu tena kwa kila wanapopita mapokezi na kumkuta amekaa hapo na Lea. Kwa hiyo Mina na Lora wote walikuwa wakijulikana vizuri sana hapo kazini kwao. Akapoa kidogo.

Na nyumbani kwao anawaambia nini? Kuwa Lora amemwambia hafai! Hana akili za maendeleo! Kwamba yeye sio mwanaume wa ndoto zake! Akaona nikujidhalilisha. Kwa kuwa alifanya mazoezi mengi, mwili ulichoka, akashindwa kufikiria matatizo. Akaenda kitandani. Akarudia tena jumbe za Mina. Akalala.

~~~~~~~~~~~~~~

Alhamisi ikawa ndefu kwa Andy, zaidi ya siku zote alizoishi duniani. Angalau Lora aliondoka kwenye picha, japo aliacha janga baya sana moyoni kwa Andy. Alimshusha hadhi kwa namna mbaya SANA. Ni kama alimtusi bila kumbakisha, akamdhalilisha na kumuacha. Alimvua uanaume wote na kumpunguzia ujasiri. Akabaki akijiuliza, na kujijibu huku akijitetea yeye mwenyewe, kisha kujifariji.

Akavuta simu yake na kutizama jumbe za usiku uliopita. Akatamani kumpigia Mina, akaona atulie. Akakumbuka ndiyo yaliyomponza. Akamtumia ujumbe mfupi, ‘Naamini siku yako inaendelea vizuri.’ Baada ya muda akarudishiwa ujumbe. ‘Nashukuru kwa kunijulia hali. Nipo darasani. Mwalimu ametupa muda wa kujifunza. Nakutakia siku njema.’ Ikawa kama ameaga tayari.

Andy akatamani kama wange chat kidogo. Lakini akaona awe mstaarabu. ‘Asante na wewe. Nimefurahi umejibu.’ Mina akarudisha emoji ya mtu akicheka na ujumbe. ‘Hata mimi nimefurahi.’ Andy akacheka na kubaki akiangalia zile jumbe. Ron akaingia na Hatibu.

“Kiongozi naona leo mambo mazuri. Tabasamu mchana huu!” Hatibu akamchokoza. Wakacheka. “Kiongozi anakula mema ya nchi! Kiti kikubwa! Upepo mzito! Shida ipo wapi!” Ron akaongeza, wakacheka. Walifika hapo kumtaarifu kuna sehemu wanakwenda ila watawahi kurudi.

~~~~~~~~~~~~~~

Usiku wakati analala, akiwa anajishauri kama atume ujumbe wa usiku mwema kwa Mina au la. Kijana huyo mtu mzima ambaye hakuwahi kupitia maisha hayo ya ujana ya mahusiano yakimapenzi kwa uzito huo, akawa hajui anatakiwa afanye nini. Ujumbe ukaingia akiwa anaitizama simu yake.

‘Nilitaka kukutakia usiku mwema tu. Naamini sijakosea.’ Andy akakaa kwa haraka. ‘Naona umeniwahi. Na mimi nilikuwa nimeshika simu ili kukutakia usiku mwema.’ Akajibu Andy kwa haraka. ‘Asante.’ Akajibu Mina. ‘Umeshapata sehemu ya kwenda jumamosi?’ ‘Bado.’ Mina akajibu kwa ufupi.

‘Au ulisahau? Mwenzio nasubiria kwa hamu!’ Akatuma huo ujumbe tena. Mina akacheka asimuelewe Andy. Kimya. ‘Umeshalala?’ ‘Bado, namsubiria mama na Ron.’ ‘Kwa hiyo naweza kupiga?’ ‘Ndiyo.’ Alipopata tu huo ujumbe, Andy akapiga. Mina akapokea kwa haraka.

“Pole na kazi.” “Asante, na wewe pole na shule.” Mina akacheka kidogo. “Asante. Sikutarajia kama naweza nikafurahia shule!” “Walimu walikufanya nini huko shuleni?” Akauliza Andy kwa utani. “Wala sio walimu. Ni mimi tu mwenyewe.” “Itabidi unisimulie zaidi siku ya jumamosi.” Mina akacheka.

“Vipi?” “Nina uhakika hutaki kujua historia yangu, Andy. Unaweza ukakinahiwa, ukashindwa hata kunitizama usoni. Ukaanza kunikimbia.” Andy akacheka. “Ndio mbaya kiasi hicho?” “Zaidi ya hivyo unavyofikiria. Nakutakia usiku mwema.” Akajua  anamkimbia. “Usinikimbie bwana Mina! Hatujamaliza swala la wapi tunakutana.” Mina akacheka taratibu bila yakujibu.

“Mina?” “Sijui Andy. Lakini..” Akasita. “Nini? Niambie tu.” “Labda hiyo siku ya jumamosi tuzungumze kwenye simu tu. Itapunguza usumbufu.” “Sikujua kama kwako unaona ni usumbufu! Samahani.” “Hata kidogo. Naomba usielewe vibaya, ni kwa ajili yako. Najua una mambo mengi na watu wa muhimu wakuwafikiria. Sitaki niongezeke kwenye mambo yatakayokusumbua, na yanayokufanya uyafikirie”

“Naomba hilo nije nilieleze kwa undani siku tutakayo kutana. Ila wewe sio usumbufu na ninaitamani hiyo jumamosi ingekuwa kesho.” “Kweli Andy!?” “Sina sababu ya kukudanganya Mina. Natamani muda na wewe.” Akamsikia Mina akicheka taratibu.

“Na naomba uwe na imani na mimi.” “Nakuamini Andy.” “Basi naomba ukaribie kwangu. Lakini nitataka kukuongezea imani yako kwangu.” “Kwa kufanyaje?” “Tuanzie hospitalini, nataka nipime UKWIMI nikiwa na wewe.” “Andy! Mbona unaniogopesha?” “Kwa kuwa namaanisha kile ninachotaka kukwambia.” Mina akanyamaza. “Ni sawa, Mina?” “Sawa, lakini nina maswali mengi!” “Naomba uyatunze mpaka jumamosi. Unaweza kukuta yakajijibu.” “Sawa.” Mina akajibu huku akivuta pumzi. “Sasa hivi naweza kulala vizuri nikijua tuna uhakika wa kukutana jumamosi.” Wote wakacheka. “Haya, usiku mwema Andy.” “Na wewe Mina.” Wakakata.

~~~~~~~~~~~~~~

Siku ya ijumaa kila mtu alijua Andy anafuraha. Aliimba kwa miluzi mfululizo.  Aliingia na kutoka ofisini kwake kama ambaye asiyeweza kutulia sehemu moja. Mina naye hakuonekana hapo ofisini kuanzia siku alipopata barua kutoka kwa Andy, hakurudi hapo tena.

Usiku tena akataka kupiga, Mina akamwambia yupo na mama yake. ‘Tunakutana wapi?’ Andy akauliza. ‘Naweza kukukuta hospitalini.’ ‘Wazo zuri. Au ulitaka nikufuate?’ ‘Hapana. Nitakuwa sawa tu. Asante kwa kujali lakini.’ ‘Karibu, ila ukikwama, unijulishe.’ Wakaagana.

Hayawi, Yamekua.

Mina alijitahidi kupendeza. Mama yake alibaki akimtizama. “Umesema unaenda wapi tena?” “Acha kunitega mama! Sijakwambia wapi ninapokwenda.” Mama yake akacheka kwa wasiwasi kidogo. “Na ninaomba usiniulize sana. Nimekuahidi kuto kukudanganya. Ila nakuahidi nikirudi nitakwambia kila kitu.” “Basi niambie hata unapokwenda.” Mina akasimama kama anayefikiria. Akasita.

“Mama bwana!” “Usiniambie mengi. Niambie tu unapokwenda Mina, mama. Niondoe wasiwasi.” “Nitarudi mama. Sitoroki tena. Kwani nilipokuwa nikikutoroka nilikuwa nakuaga au ulikuwa ukiniona nikiondoka?” Mama yake akanyamaza.

“Naomba niamini mama. Tafadhali. Nimekuahidi nimebadilika, nimebadilika.” “Naomba ibakie hivyo Mina, mama yangu mzazi. Tafadhali mama. Tumepumzika zaidi ya mwaka. Angalau akili zangu zimetulia.” Mina akakaa, nakuanza kulia.

“Usinielewe vibaya Mina mwanangu. Na wala sina nia ya kukutesa. Lakini wewe ni shahidi. Naingiwa na wasiwasi kila ninapokuona unatoka hapa nyumbani. Nakuwa sijui kama nitakuja kukuona tena au la!” “Nimebadilika mama. Safari hii nimebadilika. Nakwenda kuonana na mwanaume.” Mina akaongea akisihi. “Lakini huyu mwanaume sina maelezo naye mengi, ndio nakwenda kumsikiliza.” Mina akajifuta machozi.

“Una muda gani tokea umfahamu?” Mama yake akamuuliza. “Sio muda mrefu mama. Lakini ameniomba tukutane naye hospitalini kwanza ili apime afya yake. Amesema baada ya hapo ndipo tutapata muda wa mazungumzo. Anaonekana ni mtu mzuri. Sina uhakika na chochote ndio maana nilikuomba niende kwanza nikamsikilize, ndipo niwe na cha kukwambia.” Mama yake akanyamaza.

“Mama?” “Sijui Mina, mama! Sijui!” “Ni nini mama jamani!?” Mina akaongea kwa kulalamika. Ron akaingia. “Sikiliza Mina.” Akaanza Ron. “Umetupa muda mfupi mzuri sana. Ukatuonyesha upande wako mwingine ambao hatukuuona kwa muda mrefu sana labda tokea utoto wako. Umerudi shule. Ukasoma na mwalimu wako anakusifia.” Akaendelea Ron.

“Mama alikuwa na tumaini kubwa sana. Sasa hili unalotaka kulianzisha tena ndilo linalotutia mashaka.” Mina alilia sana. “Nimebadilika Ron! Nimekuomba uniamini. Naomba niamini. Nimebadilika kaka yangu. Najua umenigharimia. Najua namgharimu mama. Nimebadilika. Nafikiria zaidi sasa hivi kuliko zamani. Ndio maana sikuondoka hivi hivi, nimemuaga mama. Na nimeahidi nitarudi. Sitoroki tena.” Mina aliongea huku akilia.

“Sina maelezo mengi na huyo mtu, ndio maana nimemwambia mama anipe muda. Nimfahamu ili nijue ni nini chakuongea na yeye juu yake. Lakini nataka kuwaambia kwa haraka ni mtu mzima. Ametulia. Anamajukumu yake. Naamini atakuwa mtu mzuri ndio maana nimempa nafasi yakumsikiliza. Sina maelezo naye mengi.” Mina akajaribu kujieleza zaidi.

 “Naomba uniamini mama. Nitarudi na sitachelewa kurudi. Na nitakupigia baadaye ili tu ujue nipo na nitarudi nyumbani. Naomba uniamini mama yangu. Najua nimekuwa nikikwambia hivi halafu naharibu, lakini safari hii nimeamua mama yangu. Mwanaume nitakayemkubali, ujue atakuwa mume wangu. Na nitamwambia cha kwanza, lazima aje kwenu, mumfahamu kwanza.” “Kama ndio hivyo ni sawa.” Mama yake akakubali.

“Na wewe Ron?” Baada ya mama yake kukubali, Mina akataka kumsikia kaka yake pia. “Naomba ukumbuke ahadi ya safari hii Mina.” Mina akainama na kuendelea kulia. “Sisi tunakufikiria ndio maana tunakwambia hivyo.” “Najua.” Mina akajibu.

“Basi naomba LEO urudi Mina. Iwe leo tafadhali. Uje ulale hapa nyumbani isiwe vinginevyo.” “Nitarudi Ron! Nakuahidi nitarudi.” “Sawa.” Ron akatoka. “Nitarudi mama.” “Sawa Mina mwanangu. Na hiyo simu ya baadaye usisahau. Ujue naisubiria.” Mina akaumia sana. Akanyanyuka nakutoka hapo chumbani, akitamani kama asiende. Lakini akajua Andy anamsubiria, lazima aende. Alishamuamsha na ujumbe mzuri wa kumwambia ni kiasi gani anamsubiria kwa hamu.

Mina&Andy.

Alifika hospitalini sehemu ya kuegeshea magari akiwa anaonyesha wazi alikuwa akilia. Andy akamwangalia kwa makini. “Vipi? Nini kimekuudhi?” Akatingisha kichwa kukataa na machozi yakaanza kumtoka tena. Andy akamsogelea na kumvuta mkono aliokuwa akijifutia machozi, akaubusu. “Twende tukapime afya. Baada ya hapo tutapata muda wa maongezi.” Akambusu tena, akamshika mkono vizuri kwa upendo.

“Ungependa na mimi nipime au itakuwa gharama sana?” Akauliza Mina wakati wanaingia ndani. Andy akasimama na kumshika mikono yake yote miwili na kumtizama kwa karibu. “Juu ya gharama, hapana. Kuhusu kupenda kwangu haijalishi. Upime, usipime, kwangu ni sawa. Upo huru kufanya unachotaka. Ila mimi kupima inamaana kubwa sana, kwa kile ninachotaka kukwambia baada ya hapa.” “Basi na mimi naomba kupima, japo nilishapima miezi sita iliyopita.” “Sawa.” Andy akakubali bila shida.

Walitolewa damu, wakakaa nje wakisubiri. Andy akamvuta mkono na kuanza kuuchezea mkono wake taratibu. Mina akamuona kama anayefurahia japo mawazo yake yalikuwa mbali. Mara kadhaa alivishika vidole vyake na kujaribu kuvipanga hivi na vile. Mina akawa akifurahia haswa. Akacheka taratibu. “Una vidole vizuri!” Akamsifia. Mina akacheka huku akimwangalia kama asiye muelewa lakini akasema. “Asante.” Mina akataka kama kumuegemea lakini akajishitukia. Akacheka na kuinama akiwa amevuta mkono wake. Andy akambusu kichwani na kucheka taratibu. 

“Huu mkono ulikuwa kwangu Mina! Umeupokonya.” Akauvuta tena uleule mkono wa Mina aliokuwa ameushikilia, Mina akacheka. Andy akapishanisha vidole kama alivyomfanyia Lora na kuishia kumkera, lakini kwa Mina akafurahia na kumtizama machoni. Mina akacheka tena na kuinama.

Wakaitwa ndani kwa mshauri nasaa. Wakapewa ushauri mrefu tu kwa muda mrefu ndipo wakapewa majibu yao. Wote hawakukutwa na vijidudu vya UKIMWI. Andy hakushangaa, kwa kuwa alijijua. Alifanya vile kwa ajili ya Mina. Mina naye tokea alipopima akiwa na mama yake, hakukutana na mwanaume tena kwa hiyo na yeye alijua wazi hakuwa na vijidudu vyovyote vile.

~~~~~~~~~~~~~

“Mbona hukuonyesha kushangaa matokeo, japo kufurahia tu? Au ulijua nini?” Mina akacheka wakiwa wanaondoka hapo kuelekea nyumbani kwa Andy. “Mama alishanipeleka kupimwa hospitalini zaidi ya mara tatu, kwa hiyo nilijua kama sijaathirika.” Andy akamtizama. “Kwa nini mama alikupeleka kupimwa mara zote hizo!?” “Kwa kuwa hakuwa akiamini kama sijaathirika.” Mina akajibu. “Kwa nini hakuwa haamini?” Mina akanyamaza. “Mina?” “Kwa maisha niliyoishi, Andy!” Mina akajibu kwa unyonge. Andy akamwangalia. “Ndio maisha gani hayo?” Akauliza tena Andy. Taratibu tu.

“Naomba tuyaache Andy. Tafadhali.” “Kwa nini?” “Kwa kuwa sitaki na wewe uongezeke kwenye idadi ya watu ambao wananitilia mashaka! Naomba tuzungumzie kitu kingine. Tafadhali Andy.” Andy akamwangalia na kurudisha macho barabarani. Wakanyamaza mpaka walipofika nyumbani kwa Andy. “Naishi juu kabisa. Karibu.” “Asante.” Wakaongozana. Mina alifunguliwa mlango, kuingia pananukia.

“Nani anapika?” Akauliza Mina huku akicheka. “Nilipika ndio nikaondoka.” “Kumbe wewe ni mpishi mzuri!” Andy akacheka. “Vitu vichache sana. Vingine nilinunua. Nilitaka ukija kusiwe na mwingiliano. Muda utakao kuwa nao niutumie vizuri.” Mina akacheka na kumtizama vizuri kama ambaye anamchanganya.

“Njoo tule kwanza, ndipo tuzungumze.” “Asante. Ila nyumbani kwako ni pazuri Andy. Pasafi!” “Nikwambie ukweli?” Mina akatingisha kichwa huku akitabasamu. “Vingi unavyoviona hapa, nimevikuta humu humu ndani. Na ndio moja ya kitu kinachonifanya niishi hapa.” “Sikujua! Lakini pia hongera.” Andy akacheka na kuhamia sehemu ya kulia chakula. “Kaa hapa, nipashe chakula moto, nikilete.” “Si nikusaidie?” “Mgeni siku ya kwanza.” Mina akacheka na kukaa vizuri.

Andy akaandaa chakula na kukileta pale mezani, wakala kimya kimya, akimuona vile anavyotumia kisu na uma vizuri. Akawa mpole. “Unataka nikuongeze kitu chochote?” “Hapana. Nashukuru. Nimetosheka.” “Unaogopa kunenepa?” Mina akacheka. “Hata wazo la unene na wembamba halipo kichwani kwangu. Nakula mpaka nishibe. Hapa nimeshiba. Sijivungi.” “Kama hivyo sawa. Na baadaye ukisikia njaa, uniambie.” Mina akacheka na kushukuru. Akamsaidia kutoa vyombo na kuhamia sebuleni. Hapakuwa pakubwa sana. Unaona kila mahali.

“Nikuulize kitu Andy?” Andy akakaa kochi la pembeni yake. “Chochote kile, karibu.” “Kwa nini nipo hapa? Na kwa nini umetaka mimi nijue kama hujaathirika?” Andy akacheka kidogo kama anayefikiria. Kisha akamuuliza. “Umeshasikia Love at first sight?” Mina akacheka kidogo. “Yaani unamuona tu mtu, unampenda?” “Ewaaa! Bila kumfahamu hata kidogo.” Mina akacheka kidogo na yeye akawa kama anafikira, akamuona anakunja uso.

 “Hivi inawezekana kweli au inakuwa kama zile tabia za wanaume wale wanao kuwa na tamaa tu?” Andy akashituka kidogo. “Unamaanisha nini?” “Si unajua kuna wanaume wanavutiwa labda na rangi fulani ya mwanamke. Au labda unakuta umbile au sauti? Basi akiona hicho kitu tu kwa mwanamke, anamwambia unampenda. Na mbaya unakuta wanaanza mahusiano.” Mina akaendelea.

“Wakianza mahusiano, anagundua labda umbile peke yake halitoshi kwenye mahusiano. Anaanza kumnyanyasa mwenzake. Tena hata kumpiga. Unakuta anampiga kila wakati, tena bila kosa!” Akamuona Mina anatokwa na machozi.

“Halafu anaanza kumpiga hata kama hajamjibu kitu kibaya! Anampiga tu hata akimkuta mwenzie amelala, anaanza kumpiga bila sababu. Unakuta sasa huyo mwanaume anakuwa alianza mahusiano kwa kutamani tu.” Ikabidi Andy ahamie hapo. “Sizungumzii aina hiyo ya kupenda Mina!” Akamgeuzia upande wake na kumfuta machozi kabisa. “Nazungumzia kupenda kule ambako huwezi hata kupumua au kufikiria kwa ajili ya huyo mtu uliyemuona na kumpenda! Unatamani awe wako kwa garama yeyote ile. Yaani unakuwa umeshajumlisha madhaifu yote, ukajiambia nikimpata mimi huyo mtu, nitakuwa naye vile alivyo.” Mina akacheka taratibu.

“Hayo mapenzi ya kwenye movie za kizungu bwana!” Mina akaongea huku akijifuta machozi. “Kwa hiyo huamini katika mapenzi ya kweli?” Mina akafikiria kidogo, kikawa kama kitu kimepita kichwani. Akamwangalia Andy. “Kwani wewe unaamini!?” Mina akauliza kwa upole. “Lakini ni swali la kijinga hilo. Nimewaona wewe na Lora jinsi mnavyopendana. Lazima unaamini. Samahani.” Akajijibu Mina mwenyewe na kuendelea.

“Lakini Andy, mimi nilifika sehemu nikaacha kuamini kabisa. Inawezekana ipo, ila si kwangu. Naomba usichukulie jibu langu maanani.” Mina akajirudi.

“Kwa nini?” “Aaha! Nahisi sikubahatika tu. Samahani. Ulikuwa ukiongea wewe. Endelea.” Andy akajirudisha nyuma ya kochi akifikiria aanzie wapi tena. Akakumbuka Mina huwa anakwepa hapo. “Lakini nitataka kujua zaidi Mina!” “Hutakaa ukaniangalia jinsi unavyonitizama sasa hivi Andy. Hutakaa ukatamani hata kunisikia.”

Mill Kwa Pam

Kazi ya kumuweka kwenye mstari Pam, ikaanza. Mill akaanza kwa kwenda ofisini mida ya mchana. Anatoa ofa ya vinywaji. Anamtuma mesenja wa ofisi, apite kote aulizie wanataka vinywaji gani, kisha akanunue. Akafanya siku ya kwanza na ya pili. Anazunguka kila meza anawaambia ofa ni kutoka kwa Mill, waagize wanachotaka.

Lona akazidi kupagawa na Mill akijua anayo pesa. Piti anaporudisha jibu kwa Mill, anagundua Pam hajaagiza kinywaji chochote. Ikawa hivyo mpaka mara ya tatu. Mill akashangaa maana wengine walikuwa wakiagiza soda na maji pia. Kama kufuru tu.

“Kwamba hata maji hataki!?” “Dada Pam hana maneno mengi, kaka yangu. Ukimfikia na kumwambia ni vya bure yeye anasema, ‘asante’, yupo sawa. Sina jinsi ya kumlazimisha.” Akatoa pesa kwa walio agiza, akaondoka.

Siku inayofuata akawahi asubuhi na mapema. Akamuomba tena Piti aulize kitafunwa. Maana hapo ofisini walipata kahawa na chai ya bure. Piti akapita tena kila meza. Wengine wakaagiza kupitiliza. “Pam ameagiza nini?” Likawa swali la kwanza mara Piti aliporudi na kikaratasi kilichoandikwa oda za wafanyakazi wengine. “Amenishukuru tu na kuniambia yeye ameleta kitafunwa chake.” Mill hakukata tamaa.

Kesho yake akafanya hivyohivyo. Matokeo yakawa yaleyale. Akafanya kwa juma zima. Kama kuweka mazoea, ili Pam ajue kuna uhakika na vitafunwa vya bure asibebe, aje aagize pale, lakini ikawa hola.

~~~~~~~~~~~~~~

“Sasa hapa utaishiwa Mill, ukose hata nauli yakurudi Marekani.” “Nitauza kile kiwanja.” Jerry akawa anacheka, hana mbavu. “Nashauri uanze kuuza hiyo gari kwanza.” “Nakusaidia wewe, kukuhakikishia ule umbali nilio tayari kwenda kwa ajili yake.” “Mike unamsikia?” “Nishamwambia akiishiwa nitamsaidia nauli ya kurudi. Ndio maana unamuona hana neno kuliwa pesa yote.”

~~~~~~~~~~~~~~

Wakafikiri anatania. Alichofanya ni kubadili gia. Akahamia kwa chakula cha mchana. Lona akawa anazidi kufurahia akijua anahongwa yeye. Maana alikuwa kila akisikia Mill amefika, basi atapata sababu ya kumfuata hapo ofisini kwa Jerry, maneno mengi hamalizi!

“Pam ameagiza chakula gani?” “Amesema yeye huwa analeta chakula kutoka nyumbani.” “Basi ukiwa unawapelekea wengine chakula, tangaza kuwa na kesho chakula kitakuwepo. Wote wajiandae kwa chakula.” Piti si mbishi. Muungwana. Kazi yake kutumwa. Akakubali. Akafanya hivyo na kufanya wote kumpongeza Lona kwamba safari hii kapata mwanamme wa kuwafaa wote. Lona akajisifu kuwa ashaachana na wanaume wa bongo, kapata mmarekani, anatema dola.

Kesho yake na siku inayofuata ikawa hivyohivyo. Pam hakuagiza. Akaendelea kuhangaika bila mafanikio. “Nifanyaje Jerry?” Jinsi alivyomuuliza, haikuwa ya utani. Ikabidi Jerry awe rafiki. “Kama rafiki wa kweli na mtu ninayemfahamu Pam, nakushauri uache. Unajimaliza bure. Ila kama binadamu, nashauri pengine badili njia. Hii ya kuhonga ushaona haifai. Na hivi Lona anavyojisifia, sijui utafanyaje? Itamuina ngumu hata kwa Pam kukufikiria. Atajua ni mchezaji tu.” Mill akaondoka akiwa ameumia ila hajakata tamaa.

Anamkwepaje Lona bila kuleta matatizo kwa Pam? Na anampataje Pam asiyehongeka? Yakabaki maswali yasiyo na majibu. Akaangalia muda, ukawa hautoshei. Alikuwa amebakisha siku chache aondoke nchini huku hakuna dalili ya kumpata Pam.

~~~~~~~~~~~~~~

Akatulia kama siku tatu bila kutokea hapo ofisini kwa kina Jerry. Siku ya nne wakapita mida ya jioni akiwa na Mike. Hakutaka kuingia ndani, wakamuita Jerry nje. Wakawa wakizungumza. Mike ndani ya gari, Jerry na Mill nje. Ila Mill akawa ameegemea gari wanaongea na kucheka. Warembo wakatoka na pochi zao kwamba ndio wamemaliza siku ya kazi. Moyo ukapasuka paa! Kama kumeanguka chuma sakafuni baada ya kumuona Pam.

Kabla hajatupia salamu, Lona akamuwahi wakiwa wanaelekea walipo upande wa kufuata daladala. “Umepotea Mill! Nilijua umeondoka bila ya kuniaga.” “Nipo. Majukumu tu.” “Kama mnaondoka sasahivi tunaomba lifti.” Akaongea tena Lona. Wawili kati ya hao wasichana watatu akiwepo Pam wakachangamkia kuomba lifti. Pam hata hakuwatizama mara mbili. Akaungana na kijana mwingine ambaye anafanya kazi hapo, wakawa wanaendelea na safari yao.

“Pam, kuna nafasi ya kuwatosha wote nyinyi watatu.” Mill akajikaza na kumwambia kwa sauti ya kusikika kabisa. Akamgeukia. “Nashukuru, asante.” Hakujibu kwa jeuri, lakini akawa anaondoka. “Tunaweza kukusogeza na wewe. Itakupunguzia usumbufu wa daladala.” “Nashukuru. Lakini mimi nipo sawa. Asante. Muwe na jioni njema.” Akaondoka kabisa hapo. Ila hata vile alivyojibiwa, nakutakiwa jioni njema, akaridhika.

“Leo nakupeleka kwenye ile nyama choma, niliyokuahidi. Safari hii mimi ndio nakupa ofa Mill.” Lona akahakikisha anamtoa macho na mawazo kwa Pam. “Nashukuru sana. Ila naona itabidi tufanye wakati mwingine. Tupo na ratiba ngumu kidogo.” Jinsi alivyomjibu, sura ya kazi na sauti kakamavu, Jerry akajua Pam keshamchanganya. Akaaga na kurudi ndani. Wakaondoka na hao warembo.

~~~~~~~~~~~~~~

Siku zikaisha za kubaki nchini. Alikuwa akiondoka na ndege ya usiku, mida ya saa nne akaamua kwenda ofisini kwa Jerry, akitamani kumuona Pam kwa mara ya mwisho kabla hajaondoka na azungumze naye japo hata salamu tu. Akamkuta Jerry ofisini kwake na Sandra hivyohivyo. “Itakuwa sawa nikimfuata ofisini kwao?” “Utamwambia nini?” Jerry akamuuliza. “Nimuage tu.” “Mill!?” “Hakika siwezi ondoka bila ya kuzungumza naye hata kidogo!” “Utamwambia nini na Lona yupo palepale?” Mill akafikiria na kushindwa cha kujibu.

Mara mlango ukagongwa, akaingia Pam. Jerry na Mill wakaangaliana. “Naona niende sasahivi kabla hapajakuwa na foleni nikachelewa.” “Naondoka usiku, Pam. Nimekuja kukuaga.” Mshangao wa Pam uliweza kuonekana mpaka usoni. Na vile alivyozungumza Mill, Pam akabaki amekunja uso akimtizama kama ambaye hajamsikia sawasawa au hajamuelewa! Mill naye akabaki akimwangalia.

Mara Lona akaingia. “Harufu yako nimeipata tokea ofisini kwetu! Nikajua tu upo.” Hapohapo Pam akatoka bila ya kusubiri. Mill alitamani alie. Lona alijaa hapo kwa hili na lile mpaka Mill akaondoka nchini, hajapata nafasi na Pam.

~~~~~~~~~~~~~

Ni ipi hiyo historia ya Mina ya kutisha kwa kiasi cha kuogopa kusema au hata mama yake na Ron kushindwa kumuamini tena?

Japokuwa Mill amejaribu kutupia neno, lakini imekua kama amegonga mwamba. Lona yupo katikati ya Love At First Sight!

Endelea kufuatilia.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment