“Kusanya vitu wakati mimi naenda ofisini kwetu
kumpigia kwanza mama simu kumtoa
wasiwasi.” “Na mimi nilitamani kumpigia, lakini sina hela kwenye simu Ron! Jana
ulisema leo ndio utaniwekea!” “Nilisahau.” Ron akajibu kirahisi tu huku
akielekea ofinisi kwao.
Andy naye akarudi ofisini kwake. Mina akakusanya vitu
vyake na kumfuata Ron. Akamsikia akizungumza na mama yake. “Nipo naye hapa. Yupo sawa tu.” Kisha akaongeza. “Basi acha tujaribishe tuone kama tutapata daladala. Usiwe na
wasiwasi mama. Tutafika tu, japo sijui ni saa ngapi.” Wakaagana.
“Haya twende. Lakini usibebe simu wala huo mkoba.
Vitaloa na kuharibika.” “Nitaacha wapi sasa?” “Lete nikuwekee hapa kwenye meza
yangu mpaka kesho.” Wakati wanataka kutoka, Andy naye akatoka.
“Naweza kuwasaidia usafiri mpaka nyumbani.” Ron
akageuka. “Kweli Kiongozi!? Maana najua kwako ni hapo mlango wa pili tu. Kwetu
ni parefu mnoo!” “Hamna shida. Twendeni.” Ron akamshika mkono Mina. “Twende.”
Akawa anatembea akimvuta kutoka nje, Andy akiwatizama kwa kujiiba bila kuongeza
neno mpaka lilipokuwa gari la Andy ambapo wao viongozi hupata sehemu maalumu ya
kuegesha magari yao nje ya ofisi tu, sio mbali.
Walipofika kwenye gari yake akawakaribisha. Ron akakaa
kiti cha mbele, Mina akakaa nyuma. Kile kitendo cha kutoka tu ofisini kuingia
garini ambako ni sehemu ya nje tu, wakaloa. Andy alikuwa na mwamvuli. Hakuwa
ameloa. “Unasikia njaa? Maana nilisahau kukuachia hela, nilijua nitawahi.” Mina
akajua kaka yake anamuuliza yeye. “Lea alininunulia chakula mchana. Halafu
wananidai shule.” “Si ndio malipo ya mwisho?” “Bila hivyo sifanyi mtihani.”
“Ulivyojitahidi hivyo!” Mina akacheka.
“Si nilikwambia nitamaliza? Na mpaka safari hii
nifanye mtihani.” Ron akacheka. “Lazima utafanya tu. Nitalipa mwisho wa mwezi
kabla ya muda wa mtihani kufika. Wewe kazana kusoma ili ufaulu vizuri.”
Akamsikia anacheka.
Ron akageuka. “Nini?” “Nimenogewa mwenzio.” “Na nini?”
Ron na mdogo wake waliendelea kuzungumza pale garini kama Andy hakuwepo. Na
yeye Andy kimya akisikiliza huku akiendesha. “Ungekuwa na hela, au kama
ungekuwa na wewe hurudi chuo, mimi ningeendelea, Ron.” Ron akashituka mpaka
akageuka kabisa.
“Kwamba ungesoma tena baada ya hapa!?” “Pale pale
chuoni wana masomo ya kompyuta ngazi ya juu kidogo, halafu yule mwalimu
uliyesema nisimpigie.” Wote
wakacheka.
“Na usimpigie.” “Basi yupo na yeye kwenye lile kundi
letu. Kwa hiyo anayo namba yangu na wala hajanipigia na wala sijampigia.” Ron
akacheka. “Ehe!” “Basi alisema pale pia wanafundisha mambo ya kompyuta kama
yale, ila wanafundisha kwa ndani kidogo. Wanafundisha jinsi ya kutengeneza website
mbalimbali. Kutengeneza logo za makampuni. Kalenda. Lebo. Vitu vingi.” “Kwa
hiyo unataka na wewe ujifunze?” Ron akataka uhakika.
“Nimekwambia nimebadilika Ron! Nitasoma. Sasa hivi nimetulia. Kama ungekuwa na hela,
ningesoma.” “Nitalipa Mina.” Mina hakutegemea. “Na wewe chuo?!” “Wewe usijali
juu ya hela. Hata hivyo mama hajashindwa kukusomesha Mina. Kwanza atafurahi
sana ukimwambia unataka kuendelea. Na hivi ulivyojitahidi mpaka sasa!”
“Na umwambie mama kuwa nimekaa hapo ofisini kwenu,
sijavunja hata kikombe!” Ron akacheka. “Usicheke Ron! Mwambie mama ili aamini
kuwa nimebadilika. Sasa hivi mimi ni mtu wakuaminika.”
“Anajua Mina. Mama anakufuatilia au anatufuatilia kwa makini sana. Wewe kazana
upande wako, mengine yatajijibu yenyewe.” “Asante Ron. Nimefurahi umeniamini. Na nakuahidi nitafanya vizuri mpaka utafurahi.” Ron akacheka taratibu na kugeukia mbele.
~~~~~~~~~~~~~
Maswali mengi yakaibuliwa ndani ya Andy aliyekuwa
akiwasikiliza hapo wakati anaendesha. Wakatulia kwa muda. Ron alipogeuka nyuma,
akamuona amelala kabisa. “Mina! Mina!” Ron akamuita lakini hakuamka. “Nataka
alale kabisa kwenye kiti. Hapo ataumia shingo. Amekaa vibaya.” Andy akaona vile
unavyomjali. “Unataka tusimame?” “Naona tutakuchelewesha tu. Ngoja nimvute.”
“Hata hivyo magari hayaendi. Unaweza kufungua mkanda na kugeuka nyuma.
Sitaondoa gari mpaka umalize.” Ron akaona ni wazo zuri.
Akaruka kabisa nyuma, akamtoa mkanda na kumvuta.
“Bwana Ron!” “Nakuweka vizuri, acha ubishi.” “Nasikia baridi.” Akamsikia Mina akimlalamikia
kaka yake. “Itabidi ujikaze tu. Hamna kitu chakujifunika. Mimi mwenyewe
nimeloa. Sogea juu kidogo, shingo itakuuma.” Mina akasogea. Akamfunga tena
mkanda akiwa amelala vilevile. “Usianze sasa kukoroma na kumwaga mate kwenye
gari ya watu.” Akamsikia Mina akicheka taratibu. “Achana na mimi, Ron.” Ron
akacheka na kurudi kukaa kiti cha mbele.
~~~~~~~~~~~~~
Mpaka anawafikisha nyumbani, ilishakuwa saa 4 usiku.
Mama yao akatoka na mwamvuli mpaka pale garini. “Wote tumeloa mama. Huo
mwamvuli jifunike tu wewe.” “Si atakohoa huyu! Mbona hata hujamfunika bwana!”
“Sikuwa na kitu chakumfunika mama. Wote tumeloa, mizigo yote nimeacha ofisini.”
Andy kimya.
“Mina! Mina mama!” “Mtingishe huyo mama. Hivyo
unavyomuita hawezi kuamka. Au rudi
ndani mimi nitamuamsha.” “Sasa sio kwa nguvu na wewe mpaka umuue kwa ugonjwa wa moyo!” Ron akacheka.
“Huu ndio muda wakumlipiza
huyu.” Akamsikia mama yao anacheka. “Ujanja wote umemuisha. Muone. Mina!” Akamuita
tena. “Na kweli mwanangu safari hii amejitahidi.
Sijui ndio amekuwa kweli!” “Naona akili zimeanza kuongezeka. We Mina! Mina.”
Ron akamtingisha, akakaa. “Tumefika nyumbani. Shuka ili mwenyewe Andy arudi
kwake na yeye akapumzike.” Mina akabaki amekaa. “Mina!” Mama yake akaita.
“Mama!” “Twende ukabadili nguo ulale.” Ron akamgeukia Andy na kumshukuru kwa
kuwaleta nyumbani kisha akashuka.
“Asante baba. Mungu akubariki.” Akashukuru mama yao
pia. “Amina mama.” Andy akajibu na kugeuka. Akamwangalia Mina. “Asante kwa
lifti. Urudi salama.” Mina aliongea na sauti ya usingizi. “Karibu.” Andy
akajibu na tabasamu. Mina akashuka.
~~~~~~~~~~~~~
Baada ya mama yake kumwambia atamsomesha, akabadilisha mawazo juu ya kuwa
sekretari. Akakazana na mambo ya kompyuta. Akaacha kwenda kukaa pale mbele kwa
Lea, sehemu ya mapokezi. Akitoka shule akawa anakwenda kukaa mezani kwa kaka
yake. Anafanya kazi zake za shule au anasinzia hapo mpaka waondoke. Andy akamuwinda, mpaka akachoka. Wakawa
wakiangaliana kwa mbali tu. Na Mina naye akajitahidi hata wasipishane koridoni
hapo ofisini.
Alipomaliza mitihani ya awamu ya kwanza akaunganisha.
Safari hii ikawa anaingia shule asubuhi kutoka mchana. Hakuwa na sababu
yakumsubiri tena Ron, na wakati mwingine alitafuta sehemu yakujisomea. Anakaa
hapo anasoma kidogo. Au anakwenda kwa Ron kumsalimia, ndipo anarudi nyumbani.
Akaweka bidii, Ron akampa zawadi ya laptop. Mina
akaweka muda mwingi wa kufanya kazi kwenye hiyo kompyuta.
~~~~~~~~~~~~~
Siku hiyo alitoka shule akaenda ofisini kwa Ron moja
kwa moja kwenye meza yake. “Njaa inauma Ron!” Ron akanyanyua uso. “Kwa nini
hujala?” “Sina hela!” Ron akamtizama kama asiyemwamini. “Mina!” “Mama alinipa,
lakini kuna kitu nilinunua.” Akatoa walet yake akampa. “Hiyo na ya kesho. Sasa kesho
nisiione sura yako hapa ukiomba hela.” Mina akacheka.
“Mina!” Hatibu akamuita. “Nataka unitengenezee website.”
“Sitaki uchokozi wako Hatibu.” “Sasa wewe msomi gani hutaki kazi?” “Ndio
nimeanza tu jamani!” “Kazana sasa. Mimi mteja wako wa kwanza.” “Kwa hiyo
utanilipa?” “Pesa nyingi sana.” Mina akacheka. Wakati anageuka, akamuona Andy,
kumbe alikuwepo hapo lakini upande wa mwisho kwenye meza ya mwenzao mwingine
kina Ron.
Mina akataka kutoka, Ron akamuwahi. “We Mina?
Unakwenda kula wapi sasa?” “Mgahawa wenye AC na pazuri, ili nisome kidogo.”
“Nimekwambia hiyo pesa na ya kesho Mina! Usirudi tena hapa kesho na shida ya
pesa yakula!” “Wewe usiwe na wasiwasi.” Mina akaondoka huku akicheka na wengine
wakicheka.
Moyo Hauchagui Yupi Wakupenda.
Na kweli alikwenda kutafuta mgahawa mzuri, akakaa hapo na kutoa laptop
yake. Baada kama ya nusu saa tu, akashitukia Andy amekaa mbele yake. Akabaki
ameduaa. “Naomba nikuagizie chakula.” Mina akabaki akimtizama bila ya kujibu.
“Nilikuahidi siku ile hospitalini.” “Siku ile uliniahidi mengi na hukufanya
Andy, kwa nini unataka iwe leo? Au kwa kuwa watu wako wa muhimu leo
hawapo mimi ndio nakuja nyuma?” Mina
akauliza taratibu tu.
“Nilikuomba msamaha Mina! Mbona unashindwa
kunisamehe?” “Kwa kuwa halikuwa kosa Andy. Ulichofanya ni kugawa muda wako kwa
mtu wako wa muhimu. Hukukosea.
Ulikuwa radhi kuniacha mimi
hospitalini, nikiwa nalia kichwa
kinaniuma, ukabaki na mpenzi wako ukifurahia. Tafadhali usizungumzie uliyosema
siku ile hospitalini, kwa kuwa unaniumiza
bila sababu!” Mina akakusanya vitu vyake pale, akaondoka kabisa, nakurudi
nyumbani.
~~~~~~~~~~~~~
Siku inayofuata akiwa darasani, mwalimu akaingia na
kuweka bahasha kwenye meza yake. “Iliachwa hapo ofisini kwangu.” Ilikuwa
bahasha iliyofungwa, juu imeandikwa ‘Mina.’ Mina
akafungua huku akihisi itakuwa imetoka tu kwa Andy. Ilikuwa imeandikwa kwa
mkono. Akaanza kusoma palepale.
Mina!
Upo sahihi. Nilikosea sana. Hakuna namna rahisi yakueleza hili na
ukanielewa kile nilichokuwa nikijisikia
kila wakati nilipokuwa nikiangalia saa yangu nakujua muda wakukuona unazidi
kuisha. Kile ulichosikia na kukihisi wakati nikikupa ahadi ya
kurudi kuja kukuona, ilikuwa ni sahihi.
Sikukudanganya. Nilimaanisha kwa
ukweli, ila nilishindwa kutimiza ahadi yangu. Si kwa kutoona umuhimu wako, ila
mazingira yalikataa.
Nakuandikia kukuahidi haitakaa ikatokea tena. Nimejifunza kutokana
na hilo pia. Ukinipa nafasi nyingine, utakuja kuona mabadiliko. Tafadhali Mina.
Naomba unisamehe na unipe nafasi nianze upya. Utagundua mimi sio tapeli. Tafadhali Mina. Hiyo ni
namba yangu ya simu. Nasubiria majibu yangu.
Andy!
~~~~~~~~~~~~~
Andy aliiandika hiyo barua kwa mkono kusudi tu,
kumuonyesha Mina amechukua muda wake, akamwandikia na kuipeleka yeye mwenyewe. Na ni kweli ilimgusa Mina. Akabaki darasani
akimfikiria Andy lakini asimuelewe. Akawa na maswali mengi yasiyo na majibu.
Andy naye akawa na wasiwasi kila wakati macho kwenye simu wakati wote. Mpaka
anatoka saa 11 jioni, Mina akawa hajamwandikia chochote. Akajua bado amemkasirikia.
Tatizo ni kile anachojisikia Andy kwa Mina, alijua
ni ngumu kwa mtu mwingine anayemfahamu yeye kibinafsi na familia
aliyotoka, kumuelewa. Alimpenda kupita alivyowahi mpenda
mwanadamu mwingine yeyote. Na hakujua ni kwa nini kwa Mina imekuwa hivyo!
Alimfanya mapigo ya moyo yaende kasi
nakushindwa kujisaidia. Alimfikiria kuliko anavyojifikiria mwenyewe. Na
Andy anajipenda haswa. Kwa kumtizama tu, utajua ni mtu anayejijali. Kuanzia
mwili mpaka anachowaza, utajua ni mtu anayejielewa.
Lakini kila muda mdogo anaokuwa naye na kuzungumza
naye hata jambo dogo tu, moyoni kwa Andy ni tukio la kukumbuka na
kumfanya abaki akiwaza. Atabakia akifikiria midomo yake. Jinsi alivyozungumza.
Alivyosimama na mengine mengi ilimradi alimpeleka kasi japo hawakuendana
kabisa.
Kisicho Riziki, Hakiliki.
Andy alijawa wasiwasi, asijue kingine chakufanya.
Lakini ile hali ikamfanya athibitishe
penzi lake kwa Mina. Alishakuwa na msichana, lakini hakuwahi kujisikia vile.
Kila sekunde iliyokuwa ikienda, hajamsikia Mina, alizidi kuvurugwa. “Mungu wangu
nisaidie!” Andy akajisalimisha kwa Mungu wake.
Kazi zilikuwa haziendi, macho kwenye simu muda wote.
Akajiambia labda Mina atamjibu baada ya nusu saa, ikaja saa, mwishoe akajiambia
labda anataka muda wakutosha. Kwa hiyo itakuwa baada ya kutoka darasani.
Ilipofika kwenye saa 10, akaamua kumtafuta Lora. ‘Tunaweza kuonana leo kwa juisi?’ Akamtajia na sehemu na muda. Lora akajibu, ‘I would love that.’ Andy akashukuru vile
alivyojibu kuwa angependelea.
Muda ulipokaribia, Andy ambaye hakuwa amefanya kazi
karibia siku nzima, akaamua kusogea tu kwenye miahadi yake. Akafika hapo,
akatafuta sehemu ya kukaa, akakaa hapo kama dakika kumi mbele ndipo Lora
akatokea.
“Samahani, nilikuwa na majukumu, hivi hapa nimeacha
ili tuje tuzungumze.” Andy alisimama wakati amefika. Akamvutia kiti, akakaa.
“Asante.” Lora akashukuru wakati anajiweka sawa kitini.
Akamwangalia vizuri. Akampa tabasamu. “Mbona kama
umejawa na wasiwasi hivyo?” Lora akamuuliza. Andy akacheka kidogo kama
anayetafakari kitu. “Vipi?” Lora akauliza tena. “Hapana. Hii hali haihusiani
moja kwa moja na hili ninalotaka kukwambia, japo inahusu.” Lora akajiweka sawa.
“Tuagize vinywaji kwanza?” “Ninahamu ya kujua unachotaka
kuzungumzia zaidi kuliko hata hiyo
juisi.” Andy akacheka kidogo na kufikiria tena kama anayetafuta pakuanzia.
Muhudumu akaja, Andy akaomba waagize tu juisi maadamu wapo pale eneo la
biashara, basi waagize hata hiyo juisi.
Yeye akaomba aletewe juisi ya embe, Lora akaagiza ya
nanasi. Muhudumu alipoondoka tu, Lora akamgeukia Andy. “Niambie chochote
unachofikiria Andy. Nakusikiliza” Andy akavuta pumzi kwa nguvu. Akamtizama
Lora.
“Naomba niwe mkweli kwako Lora. Tafadhali usinielewe
vibaya.” “Mbona unanitisha tena?” Lora akauliza na tabasamu usoni. “Yuko binti nampenda sana. Nimejitahidi kupuuzia hisia zangu, lakini nahisi nimeshindwa. Yeye sijamwambia. Lakini
naona na nimejithibitishia kuwa nampenda na ninamuhitaji kwenye maisha yangu.”
“Sasa kadiri muda unavyozidi kwenda bila kumwambia, na
hivi tunavyoendelea na wewe, naona
ipo hatari yakumpoteza kabisa.” Andy
akaendelea kwa tahadhari sana. Kama anayetoa plasta kwenye kidonda kibichi.
“Sasa nimeona nikwambie ukweli ili nisiwe kama tapeli kwako wakati sisi tumefahamiana kwa
muda mrefu sana. Sitaki tuje tuwe maadui. Ninajua wewe ni muelewa, hata hili
najua utalibeba vizuri na utaelewa tu.” Ile tabasamu alilokuja nalo Lora liliisha. Akabadilika kabisa usoni mpaka akamuogopesha Andy.
Lora Ambadilikia Andy
Vibaya Sana.
“Nilijua tu Andy!” Akaanza Lora taratibu. “Mimi sio
mtoto mdogo. Unakumbuka nilikushika mkono kanisani? Niliingiza mkono wangu
katikati ya mkono wako. Baada ya muda mfupi sana ukauachia. Ilikuwa kama kule kusimama, ndiko kuliko kuokoa.” Andy
akajisikia vibaya hakujua kama Lora alilijua hilo.
“Nilihisi,
lakini nikajiambia nilazima nihakikishe. Mara kadhaa nikataka nafasi ya
kukushika, ukawa kama unanikwepa
mpaka usiku tulipoondoka. Nilikuwa pale na familia yangu, lakini nilikuona wazi
mawazo yako hayakuwepo pale. Mara
zote uliweka macho kwenye saa.” Lora akaendelea.
“Nilijua.
Na nikakuona hata jinsi unavyoniangalia, ni kama unanikwepa. Ndio maana kuna kipindi nilikwambia, inabidi
niwasubirie baba na mama kwa kuwa wamelewa.
Sijui kama ulielewa?” Andy kimya.
“Ile kitu ikanifanya nilipofika nyumbani nifikirie
zaidi. Nikaanza kuvuta taswira ya mabusu yote tuliyopata mimi na wewe. Nikaona
ni kama mimi mara zote ndio naanza kukubusu. Na nikajiambia inakubidi kwa
sababu ya busu la kwanza tulilopata nyumbani kwako!” Lora akaendelea ila kwa
jazba kidogo.
“Ndio maana umeona ni kama na mimi niliamua kukuacha
Andy. Niliona kuna uzito fulani
kwako. Lakini na mimi naomba niwe mkweli
tu, Andy. Unisamehe.” “Hamna shida.” Lora akapata jukwaa.
“Tuwe tu wawazi, ipo pressure pia ya wazazi
nyuma yetu. Sijui wewe, lakini mimi nyumbani umekuwa ukiimbwa sana. Mama
anatamani sana kuona tunaoana.” Andy
akacheka kidogo. “Kweli Andy! Lakini ukweli mimi na wewe hatuendani kwa mambo ambayo sidhani kama wazazi hata tukiwaambia, wataelewa. Usinifikirie vibaya, lakini
Andy, mimi napenda niolewe au niwe kwenye mahusiano na mtu ALIYENIPITA.” Andy
akatoa tabasamu. Akamkumbusha mwanzoni kabisa.
“Sitaki
kujutia baadaye, ndio maana umenikuta bado nipo peke yangu. Nina wanaume wengi
tu wanao nizunguka na kunigombania, lakini bado sijampata mtu sahihi kwangu.” Hapo akajisifia kwa waziwazi. Ila
Lora analipa.
“Kwako nilijaribu
sababu ya historia ya wazazi. Na nikajua pengine naweza kuja kukubadilisha
mawazo na mtizamo.” Andy akakunja uso kidogo. “Nilikuomba usinielewe vibaya
Andy! Na nikaomba ruhusa ya kuwa muwazi kwako.” “Ni sawa kabisa.” “Sasa mbona
unakunja uso?” Lora akauliza kwa ukali kama mwalimu kwa mwanafunzi darasani.
Akiwa amejitoa vazi la wema kabisa.
“Ni kwa kuwa bado sijakuelewa
unamaanisha nini! Nilikuwa najaribu kutuliza mawazo, ila sina nia nyingine.”
Andy akajaribu kumtuliza.
“Nakubali muonekano wewe ni mzuri tu. Ndio maana kila
tunapokuwa mimi na wewe, watu wanatusifia kwa nje. Lakini maisha ni zaidi ya muonekano. Sijui kama unanielewa?”
“Bado.” Andy akawa mkweli.
“Ndoa ni ya mpaka kifo kwa sisi wakatoliki. Haya, tunaingia kwenye ndoa, wewe ukiwa na haiba yako hiyo hiyo yakuridhika kwa ulichonacho wakati mimi
naona bado unanafasi kubwa sana ya kukua katika maisha! Unaweza kupambana na ukasonga mbele au ukapata zaidi.” Andy alitulia
akimwangalia Lora, asimmalize.
“Naomba unielewe
na ukubaliane na mimi tu Andy. Umekuja nchini una zaidi ya miaka mitatu. Mpaka leo unaishi kwenye apartment
za gharama sana. Huna majukumu,
hutegemewi na watu. Kinachokushinda
kujenga mpaka sasa ukaishi kwako ni nini kama si kuridhika na kuona ni sawa hiyo pesa unayotupa kwenye ile apartment ya gharama vile!” Lora
akaendelea.
“Haya. Labda hilo tukalifumbia
macho. Tukaoana. Unafikiri tukija kupata watoto, tutawaleaje? Tutawafundisha
nini watoto kwa msimamo na mtizamo kama wako?
Au kwa jinsi tunavyo tofautiana! Mimi
nitawaambia kazaneni, wewe utakuwa ukiwaambia inatosha, mmefanya vizuri sana! Sasa
tutakuwa tukijenga familia ya namna gani?” Lora aliongea kwa kujiamini bila
hata kung’ata maneno. Kama anayehutubia kwenye vikao vya kazini kwake.
Mrembo huyo msomi alikuwa akizungumza kana kwamba
anaongea na wafanyakazi waliopo chini yake. Andy alibaki kimya akimsikiliza.
Muhudumu alishaleta juisi, lakini hakuna ambaye aligusa ya kwake.
“Ni kweli tusingefika
mbali. Hata mimi nakuunga mkono. Kama kuna mtu umempata, yeye akaridhika na wewe hivyo ulivyo! Nashauri
umchangamkie tu kabla hujapoteza hiyo bahati. Ila binafsi naona hapana.” Akaweka msisitizo Lora kana
kwamba yeye ndiye aliyekuwa amemuita hapo Andy.
Andy akatoa tabasamu. “Hayo yote ulipanga kuja kuniambia lini? Maana ni jana usiku tu umetoka
kunitumia ujumbe na kuniambia unanipenda
sana.” Andy akauliza taratibu tu.
Hapo Lora akapaniki. “Unajua ni kama vile wewe ulivyokuwa ukipokea busu langu. Unajiambia moyoni pengine kuna kitu cha
tofauti utakuja kujisikia baadaye!
Ndivyo hivyo hivyo na mimi. Nilikuwa najiambia labda baadaye utakuja kupata ile hali ya muamko wa maendeleo. KUTAMANI zaidi. Hutabaki kuridhika na vidogo.” Andy
akacheka taratibu huku akimtizama akiwa ametulia tu.
“Kweli Andy! Hata mama nilimwambia. Natamani kuolewa
na mtu ambaye ananipita kimasomo, mshahara na cheo. Yaani
mwanaume ambaye ukisema ni KICHWA ndani ya nyumba, anakuwa kichwa katika kila eneo.
Sio kwenye neno la Mungu tu, halafu kwengine anapelea! Yaani inabidi mama ndio awe anapambana! HAPANA kwakweli.” Lora akawa kama amemvua nguo
Andy. Alijitahidi kumdhalilisha kisomi. Ilimradi tu kuachwa kule
kusimuache yeye ameshindwa.
“Halafu hata hivyo sasa hivi nipo kwenye kipindi
ambacho nahitajika sana kazini. Sina muda wa ‘drama’. Hata hapa nimekuja
ili kujua una shida gani! Nikahisi
ni kama ulitaka kuja kuniomba kunioa,
nilipanga kukwambia HAPANA kwakweli!” Andy akacheka na kuinama kama
anayefikiria.
“Kama huna la nyongeza, naomba niwahi kwenye
majukumu yangu ya msingi.” “Ni hilo tu. Hakuna lanyongeza.” Lora
akasimama akafungua pochi yake, akatoa pesa. Akaiweka hapo mezani. “Naamini
itatosha kwa vinywaji vyote na tip ya muhudumu.” Akaongeza Lora na
kuondoka kwa kujiamini. Andy alibaki
ameduaa.
Mill&Pam.
Wakati
Mike amejitosa kwenye kampuni kubwa ya urithi akifanya kazi kwa bidii na
kuingizia kampuni hiyo faida bila wizi, akiishi na Kamila, yeye Mill alikusudia
maisha yawe nchini Marekani. Kupambana kufa na kupona mpaka afanikiwa
huko. Na Jerry mmoja wa rafiki yao wa muda mrefu tokea sekondari, yeye alioa
mapema tu. Sandra alihakikisha hachezewi.
Alimbana Jerry mpaka akamuoa.
Na Sandra mwenyewe alikuwa akilipa.
Alijaliwa uzuri wa kike. Na ni wale ambao huwa wanasifa ya, ‘beuty with the
brain.’ Alikuwa mzuri wa sura na umbile, lakini pia alijaliwa akili
nzuri ya kufikiria pamoja na utendaji.
Pesa ya wizi waliyopata yeye na wenzie
waliokuwa wakifanya kazi pamoja yeye hakuichezea, akaizalisha na
kumfanya afanikiwe mapema sana.
Alitokea kwenye familia yenye uwezo na
inayofahamika. Alipomaliza tu chuo cha uhasibu IFM, akatafutiwa kazi kwenye
benki kwenye kitengo cha mikopo, wanalipwa kwa commision, yaani malipo
kwa vile walivyokopesha wateja na mshahara kidogo.
Sasa kwa kuwa malipo makubwa ya kipato chao
ilikuwa ikitegemeana na ukopeshaji aliungana na vijana wengine watatu hapo, wakatafuta
njia ingine mbadala ya kujinufaisha.
Wanne hao wakawa wakitoka kwenda
kwenye maofisi ya watu, mashuleni na sehemu zenye mkusanyiko wa wafanyakazi
wengi, basi wanauza mikopo ya benki yao lakini haikujalisha. Wakope au
wasikope, maadamu waliandikisha majina ya wahudhuriaji, basi wakirudi
ofisini kwa majina yaleyale, wanayatengenezea taarifa ya kutosha,
kisha wanawapa mkopo hewa. Ile pesa inaingia mifukoni mwao.
Kazi ikaendelea kwa wanne hao. Kupiga
pesa ya kampuni kwenda mbele. Ila Sandra akili kichwani. Pesa akawa anaiweka
kwa jina la Jerry ili wasimkamate. Lengo ni kuja kufungua kituo
chake/chao cha kukopesha.
Basi Jerry akaanza mchakato wa kujenga kampuni
yao, Sandra ameajiriwa, anaendelea kuiba kwa akili. Mafanikio ya haraka.
Hakubweteka kama wenzie. Pesa ya kuanzisha tu cha kwao ilipotimia na Jerry
kukamilisha utaratibu wote, hakufanya kama wenzie. Starehe za kupitiliza,
wakitapanya, akajitoa mapema hata kabla hawajakamatwa maana
dalili zote, walikokuwa wakielekea ni kukamatwa, wenzie walizidisha tamaa na
starehe za ujana.
Yeye na Jerry wakakazana kwenye lao
kwa juhudi zote. Na hivi Sandra alishakuwa na uzoefu, haikuchukua muda kufanya
vizuri, akitumia madhaifu ya kule alikokuwa ameajiriwa na kuiba hiyo
pesa, kubana wafanyakazi wake na kujinufaisha zaidi.
Hakutaka kuajiri waliosoma sana ili asilipe
mshahara mkubwa na pia awaendeshe vile atakavyo. Aliajiri warembo wa
nguvu kwenye kampuni yake. “Huhitaji wasomi kukopesha watu. Tutatumia
udhaifu wao, kufanya biashara yetu.” Ikawa ndio falisafa ya Sandra.
Akaajiri warembo na vijana wawili tu. Yeye na
Jerry ndio wakawa wanashikilia pesa yote. Hakuna mwanya wakuiba. Walibana kila
kona, huwezi muibia mwizi. Sandra akaweka juhudi, maisha yakaendelea na Mungu
akawajalia watoto wawili. Sandra akahakikisha hakuna kosa la mimba ya bahati
mbaya. Watoto wawili tu. Wote wakiume. Basi.
~~~~~~~~~~~~~~
Sasa Mike mtu wa watu, japokuwa Sandra alikuwa akimbana sana Jerry mpaka
kukera, lakini hakumpoteza kama rafiki. Na Jerry naye akawa Mike ndio mtu
wake wa kutolea dukuduku lake la ndoa. Yakimzidia kwenye ndoa yake
basi Mike akawa ndio jalala lake. Atamtupia kila kitu. Na Mike naye
alijaliwa hekima ya ajabu. Alijua kumshauri na kumtuliza mpaka akabakia
kwenye hiyo ndoa yake na Sandra japokuwa yeye mwenyewe Mike hakuwa na ndoa
takatifu ila alikuwa akiishi tu na Kamila kama mke mpaka ikazoeleka kama ni
mkewe kihalali.
Mill
yeye hakuwa akiwepo nchini mara kwa mara, kwa hiyo ukaribu ulikuwa zaidi kwa
Mike lakini alikuwa akirudi basi kukutana ni mara chache sana, tena
sehemu za kula. Na mara nyingi Sandra alikuwepo kama mlinzi. Hawakujali
hilo. Ukaribu na kwa Sandra ikabidi pia kuongezeka. Maana ilikuwa ukimtaka
Jerry ni lazima upitie kwa Sandra.
~~~~~~~~~~~~~
Kuna
kitu Jerry alimuagiza Mill amletee kutoka nchini Marekani. Kwa hiyo alipofika
nchini siku inayofuata ilikuwa ya kazi, ikabidi wamfuate ofisini kwake. Mike
alimsindikiza. Walipofika mapokezi Jerry naye akatoka wakawa wanazungumza hapo
mapokezi kama ambao hawataki kukaa sana hapo. Wakabidhiane, waondoke kisha kuja
kukutana jioni kwenye nyama choma.
Wakati
wakizungumza hapo wakiwa wamesimama tu, na Pam naye akiwa na mwenzie
wakawa wanatoka kuelekea benki. Kwa hakika Mill alichanganywa. Alipatwa
hali ambayo haijawahi mpata kwa mwanamke. Mwenzie Pam akamchangamkia haswa
kama aliyeona alumasi mchangani.
“Bosi, huyo
mteja mpya nimemuwahi mimi. Nitamuhudumia mimi mwenyewe.” “Lona kwa
kuwahi! Huyu sio mteja, ni rafiki yangu.” “Sasa uwaambie bosi wangu. Nishawahi
mimi.” Bado Mike na Mill walikuwa hawajaelewa ule MSISITIZO. Mill yeye
hakuwa hata akimtilia maanani huyo Lona, mawazo yalikuwa nje alikotoka
Pam.
Lona akaendelea
kung’ang’ania. “Sio tena na mwingine…” “Lona, huyu ni rafiki yangu.”
“Nimekusikia lakini…” “Haishi hapa nchini.” Ikabidi Jerry amkatishe maana
alizidi kung’ang’ania.
“Hivi
unavyomuona, anapita tu. Anaondoka. Ni mkazi wa Marekani.” “Kwani
Marekani mbinguni Jerry bosi wangu! Au kutaka kunibania tu?” “Basi
mama.” “Maana naona unamsemea!” Lona akaendelea kulalamika. Jerry akanyanyua
mikono juu akicheka. “Basi Lona. Najiweka pembeni.” “Na wengine uwaambie.
Uwe shahidi yangu. Sio kuja kunikana baadaye wakati umenisikia kabisa,
NIMEWAHI.” “Sawa mama. Mill huyo!” Mill ndio akarudisha akili pale.
“Kwema?” Akawa
anawauliza akiwaangalia sasa, Jerry na Lona. “Nakukaribisha mjini. Na baada ya
kazi mimi nipo free, naweza kukuzungusha mjini.” “Unafikiri basi mimi
mgeni? Najua kila kona. Nilikuwa machinga kabla sijaondoka.” “Machinga
uwe wewe!” “Muonekano unaweza kukudanganya. Ila asante. Sasa Jerry?” Akawa kama
anamtoa kwake. Akataka aendelee na Jerry.
“Sasa hapa kuna
viwanja vipya. Sehemu mbalimbali za kula. Najua huko mnalishwa mavyakula
yakizungu. Hapa nitakupeleka kwenye kuku wa kienyeji. Kuku wa kweli. Halafu ofa
yangu. Wala usijali.” “Basi hilo nitalikumbuka.” “Na…” “Lona! Unachelewa benki
na utagombana na Sandra.” Ikabidi Jerry kuingilia maana alizidi kumbana Mill.
Ndio akili ikamrudia, akaondoka huku akiomba Jerry ampe Mill namba yake.
Jerry akacheka
akitingisha kichwa. “Nikupe namba yake?” “Nataka ya yule mwenzie. Anaitwa nani
tena?” “Pam.” “Ewaah!” “Sasa kama unataka mwanamke, ni afadhali ujichukulie
Lona. Pam hutamuweza.” “Kwa nini?!” “Nakwambia humuwezi Pam.
Kwanza si umemuona jinsi alivyotupita hapa? Hata salamu hajawapa. ndivyo
alivyo Pam. Wewe kama unahamu na waswahili, Lona huyo!” “Wewe vipi Jerry! Mbona
unaning’ang’anizia nisikotaka? Nimekwambia namtaka Pam.”
“Usifikiri haja hiyo unayo wewe peke yako! Ni msururu. Wanakuja
kukopa hapa, hata wasio na shida na pesa, ilimradi tu kumpata Pam na
bado wanagonga mwamba. Achana naye. Vipi Mike?” Akawa anamkwepa Mill kwa
kurudisha mawazo kwa Mike, Mike akacheka.
“Naona upo
kimya!” “Mimi yangu macho kaka.” “Naomba namba ya Pam.” “Mill!” “Hakika namtaka
yule mtoto.” “Humpati. Nakuhakikishia humpati. Mimi nawajua wote hawa
wasichana. Achana na Pam. Nikupe ya Lona?” “Wewe vipi Jerry?! Mwanamke wako
nini?” Jerry akashituka sana.
“Naona
unanibania!” “Sasa kama unafikiri mimi nakubania, jioni tukikutana, mwambie
Sandra unataka namba ya Pam. Nakuhakikishia mimi sitamwambia chochote Sandra.
Halafu utamsikia atakachokwambia juu ya Pam. Mimi nitanyamaza kimya.” “Sawa.”
Wakaondoka.
~~~~~~~~~~~~~
Jioni
wakakutana. Mike na Kamila, Jerry na Sandra, na huyo Mill. Katikati ya vicheko
Mill akachomekea mpaka akamshangaza Jerry. “Mzee! Bado unalo tu!?”
“Kwani wewe ni Sandra!?” “Kwa Pam wala usijichoshe. Jiachie tu. Kuna
warembo pale kibao.” “Mimi namtaka Pam.” “Humpati. Kama ni shida ya
mwanamke, wewe endelea na Lona. Kwanza nasikia ameshakuwahi.” “Mbona nina
uhakika nazungumza kiswahili lakini ni kama hamnielewi! Ninayemtaka mimi,
Mill, ni Pam. Na si kwamba nina shida na mwanamke, nina shida na Pam.”
“Wala haupo peke
yako. Kuna msururu pale! Tuna kazi ya kujiangalizia na kujipatia pesa.”
“Sikukwambia mimi?” Jerry akamuuliza. “Wanakuja kukopa pale hata wasio na shida
na pesa! Ilimradi tu wakutane na Pam. Na nikikwambia msururu, basi jua
ni mrefu. Walio nazo na wasio nazo, wote wapo
wamejipanga, wakiamini siku moja watapata ‘ndiyo’ ya Pam.” Sandra
akaongeza kumuweka sawa, aelewe. Lakini wapi! “Na mimi najiunga.” Mill
akafanya wacheke wasiamini.
“Hakika ninamtaka
Pam. Mimi sijapata mwanamke mwenye vigezo vyangu vyote. Ndio kwa mara ya kwanza
nakutana naye. Pam! Hakika nitapambana.” “Sasa wewe unajuaje kama anavyo
vigezo vyako vyote?” Mike akamuuliza.
“Ya ndani ndio
nitataka msaada. Lakini mpaka sasa, kwa tabia yake, kwa jinsi
nilivyowasikiliza hawa wanae fanya nae kazi, ambao wanamjua, nisharidhishwa
naye. Si malaya. Kwamba hata nikimuacha hapa nchini, nitakuwa na
amani kuwa hatanisaliti. Na ndicho kilichokuwa kikinisumbua, hata Mike
nilimwambia. Natamani kuoa nyumbani, lakini wengi niliokutana nao, mambo
mengi, hawajatulia. Ndio nimekutana na Pam. Sasa nikipata nafasi ya
kumfahamu zaidi, naoa!” “Acha masihara Mill! Kwamba unataka wa kufunga
pingu kabisa!” “Sasa upate mtoto kama Pam, halafu unamuachia nani kama si
ukichaa huo? Wewe vipi Jerry!?”
“Kwanza wala
usiende mbali, hiyo ya kumfahamu Pam kwa kupitia mwenyewe, sahau. Pam ananyodo,
wote pale wanamjua. Kupata salamu yake mwenyewe shida!” “Yeye mwenyewe shahidi.
Alitupita pale bila hata kutuangalia! Na si kwa bahati mbaya! Ndio
mtindo wake. Hasimami kusalimia mtu.” “Basi huyo ndio namtaka
mimi.” Mike akabaki akimwangalia tu.
“Kaka mbona
hutii neno?” “Acha mimi niwe mtizamani tu.” Mike akajibu akicheka.
“Naombeni namba yake ya simu.” “Huo ndio mwiko wake. Na pale
nishawaonya. Atakayemtoa Pam pale, ajue anamfuata. Namfukuza kazi mchana
kweupe. Maana alisema mtu asigawe namba yake hata akija kaka yake yeye mwenyewe
Pam, akauliza namba yake, asipewe. Lasivyo tutaonana wabaya.” “Na
anavyokwambia hivyo Sadra, hataki mtu ambugudhi Pam. Na wote wanamjua,
Pam kipenzi cha Sandra. si mwizi.” Jerry akaongeza.
“Na kwambia
hivi, hata umpe milioni 10 apeleke benki. Kule akaambiwa katika hiyo milioni
10, kumezidi elfu kumi, Pam atarudisha. Na ni yeye peke yake ndio mwaminifu
pale. Nikiwa na dili zangu za maana, kama mimi na Jerry hatupo, basi namuachia
Pam, japo yeye peke yake ndio hajasoma pale. Hana elemu kubwa, lakini ni
bora pesa yangu aishike yeye, ndio napata amani popote pale nilipo lakini si
wale wengine. Kwa hiyo kama unataka namba ya Pam, uipate kwa Pam mwenyewe.”
Mill akatulia akifikiria.
“Upo kaka?”
“Mpaka hapa mnachofanya ni kunipa sababu ya kupambana mpaka nimpate.
Naona sifa zake zinazidi tu. Hakika mimi ndiye nitamuoa Pam.”
Akaapa Mill wengine wanao mfahamu Pam wakicheka. “Walioapa kama wewe ni wengi
Mill! Wengi sana.” “Wanaapa kwa mke wa mtu! Pam mke wangu mimi na Mungu
alikuwa akinitunzia mimi.”
“Wewe kijukuu
cha mtume?” “Wala si kijukuu cha mtume, mimi mwana wa Mungu, na nilishaomba
kwa Mungu mwanamke kama Pam. Ni muda tu. Atakuja kukutana na mumewe.”
Wakaendelea kumtania kwa hili na lile, wakazungumza mengi Mill akijipanga na
kuomba ushirikiano wao. Zaidi kutoka kwa Jerry na Sandra. “Wala usiwe na
wasiwasi na sisi. Sisi tupo kama alivyosema Mike, watizamaji. Ilimradi
tu, usimkere kiasi chakushindwa kufanya kazi. Hapo tutagombana.” Sandra akaweka
msisitizo.
~~~~~~~~~~~~~~
Je, Andy amekosa bara na pwani? Lora amemuacha kwa fedheha kubwa sana, huku akiwa hana tumaini na Mina
ambaye hata hajafahamu lengo lake ila kujua mahusiano kati yake na Lora. Kile anajisikia kwa Mina,
tokea siku ya kwanza anamuona, hawezi jisaidia japo vigezo vingi hawaendani.
Ila moyo umependa tokea siku ya kwanza anamtia machoni. Love at First sight.
Mill ameapa kumpata Pam mwenye vigezo vyake vyote alivyoona siku ya
kwanza kumtia machoni. Love at first sight.
Amekubali kuunga msafara kama wengine.
0 Comments:
Post a Comment