Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 3. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 3.

Masaa yalizidi kwenda, akashangaa hata Ron haagi kuwa anatoka kwenda hospitalini labda kupeleka chakula cha mchana! Andy akakosa hata sababu yakuuliza kinachoendelea huko hospitalini. Na hivi hakujua hata hospitali aliyolazwa, akajituliza. Kwa asili Ron alikuwa mchapa kazi sana. Alitulia mezani kwake siku nzima akifanya kazi mpaka ikafika saa 11 jioni muda wakutoka. Andy akaangalia saa, akaona haji kumuaga. Ikabidi yeye ndio atoke.

“Nilijua unawahi hospitalini!” Ron akanyanyua uso. “Nitawapitia. Nimezungumza na mama, anaonekana amepata nafuu. Alikuwa amelala karibu siku nzima, mama akapata nafasi hata yakurudi nyumbani na kupika. Anasema amerudi hospitalini, bado alikuwa amelala.” Akaongea Ron na kufikiria kidogo. “Sijui kwa nini! Nahisi labda yule niliyemkabidhi dawa za Mina hakuzifikisha sehemu husika au sijui wamecheza mchezo gani! Lakini nahisi hawakumpa dawa ya maumivu niliyokuwa nimeandikiwa na daktari, nikaenda kununua.” “Matapeli wale. Wanaweza kukufanyia mazingaombwe hapohapo na usielewe.” Akadakia Hatibu.

Ukazuka mjadala hapo. Kila mmoja akachangia lake, na kutoa malalamiko yake. “Sasa Hatibu?” Ron akauliza huku akisimama. “Kesho basi. Msalimie mama na Mina. Ningekuwa siendi Tandika, tungeongozana.” “Hamna neno. Kesho.” Akakusanya vitu vyake pale mezani, Andy akabaki kama amepigwa ganzi. “Kiongozi!” Akaita Ron akiwa anazima kompyuta. Andy akabaki anamwangalia. “Nishakutumia kila kitu. Naona mambo sio mabaya. Kama kuna jingine, tafadhali iwe kesho. Naomba mimi niwahi.” “Sawa.” Ron akaondoka hapo kwa kasi.

Kwa Mina.

Mina aliruhusiwa hospitalini baada ya siku mbili mbeleni. Akapewa dawa zakumeza mara moja tu kama kumalizia dozi yake akiwa nyumbani. Ila ukweli alikuwa na nafuu kubwa hata kichwa kikawa kimetulia.

~~~~~~~~~~~~~

Kuna mtu alikuwa akinunua chapati kama 25 hivi kila siku kutoka kwa mama yao na kwenda kuuza ofisini kwao kwa faida kidogo. Ikawa nayo ni moja ya biashara yao hapo nyumbani kuongeza kipato. Wakati mwingine ni Mina ndiye aliyekuwa akipika kama mama yake amezidiwa na majukumu mengine.

Siku hiyo asubuhi wakati Mina ameenda barabarani kwenda kumkabidhi hizo chapati kwa kuwa Ron aliwahi kuondoka, yule mama akamwambia Mina ana mtu anamfahamu anatafuta mtu wa kazi, hotelini. Mina na mapishi, akahamasika. “Ni kazi gani?” “Nafikiri ni uwe wazi kwa chochote atakachokupangia siku hiyo. Ni mgahawa mdogo tu, amepata katikati ya jiji. Anakuwa na wateja wengi, anahisi wafanyakazi wake wanalemewa, anataka kuongeza mfanyakazi.” “Basi mama atakupigia simu.” Wakaagana na kuondoka.

~~~~~~~~~~~~~

Akarudi nyumbani kwao na furaha zote. “Mwenzio nimepata kazi.” Mama yake akamwangalia na kuendelea na shuguli zake. “Usinidharau! Mpigie mama Pius umuulize. Amesema kuna kazi.” “Kazi gani?” “Ya mgahawani.” Akamwangalia tena, akaendelea na shuguli zake bila ya kumjibu. “Nitafanya mama!” “Wewe umetoka kuumwa juzi, hata juma hujamaliza, unataka kwenda kuanza kazi, kama si kutafuta kuongeza idadi ya sehemu utakazokuwa umeachishwa kazi ni nini!” Mina akanyamaza.

Akakumbuka alishatafutiwa kazi ya kuuza duka, baada ya siku tano tu akafukuzwa. Mama yake akamtafutia tena kazi sehemu ya kuuza duka la vipodozi, nako pia hakufikisha hata mwezi, akaachishwa.

“Nimebadilika mama. Sasa hivi nitatulia kazini.” “Kilichokubadilisha ni nini?” Mama yake akamuuliza. “Nimekua. Sasa hivi najua umuhimu wa kutulia.” “Basi rudi shule, Mina mwanangu. Soma kitu kidogo hata mapishi tu! Uwe na cheti.” Hapo akawa amemmaliza nguvu. Akamuona amenyamaza. “Yaani wewe unaona kwenda kuuza migahawa ya mtu ndio sawa badala ya kufikiria kuwa na chako?” “Taratibu mama. Nipe muda. Acha nianze na hii.” Mama yake akanyamaza.

“Si nikajaribu tu mama!” “Hayo ndio nisiyoyataka mimi. Unajaribisha kila mahali! Hutulii. Ukitafutiwa sehemu, unaanza vizuri, siku hazifiki hata tatu umeshatoa kasoro.” “Safari hii utaona mabadiliko.” Mama yake kimya.

“Mama?” “Hapana Mina. Wataishia kukuzalisha, nianze kuja kulea watoto humu ndani wasio julikana baba zao. Mimi nina mambo mengi sana sasa hivi yakufanya. Siwezi kuja kuanza ulezi humu ndani. Wewe tulia humu ndani. Ukitaka kutoka hapa iwe shule. Sio kwenda kuwahudumia wanaume huko mjini.” Mama yake akakataa kabisa. Nakuondoka.

~~~~~~~~~~~~~

Usiku Ron aliporudi Mina akazungumza naye. “Niombee kwa mama, Ron!” “Wewe simfanyaji kazi Mina. Utasumbua tu, na kuharibu mahusiano ya mama. Unakumbuka kule kwenye duka la madawa? Yule mama alikuja kumlalamikia mama hapa, mama akamlipa. Unaingiza hasara badala ya faida. Wewe tulia humu ndani.” “Nimebadilika Ron.” “Basi rudi shule.” Ron naye akaongea kama mama yake. Mina kimya.

“Wewe si umesema umebadilika? Rudi shule.” Kimya. “We Mina?” “Sasa nikasomee nini?” Akauliza kwa hasira. “Wewe unapenda nini?” “Kupika tu. Na sitaki nifundishwe hesabu, wala biology sijui au sayansi! Mimi sitaki kufundishwa vitu ambavyo hata sitavitumia maishani.” Ron akamfikiria dada yake, akabaki kimya. “Mkiniruhusu kwenda kufanya kazi, safari hii mtaona natulia, nafanya kazi.” “Sijui bwana! Ngoja nizungumze na mama kwanza.” “Nawasikia sana.” Mama yao alikuwa chumbani kwake, akajibu.

“Huyo atasumbua tu, Ron. Ataishia kutuingiza hasara humu ndani, tuanze kulipa tena huko watakapokuwa wamempa kazi. Hakuna faida, ila hasara itakuwa yangu. Akae hapahapa ndani.” “Siharibu tena mama. Safari hii natulia kazini.” “Mmmh!” Mama yao akaguna.

“Kazi yenyewe ni wapi?” Akauliza Ron. “Eti huko katikati ya jiji. Kulikojaa wanaume wenye njaa za kila namna! Halafu eti ndio na yeye anataka aende akawahudumie! Kama sio kutaka kutuletea mtoto humu ndani ni nini? Hebu njoo ulale.” Mama yake akakataa kabisa.

“Mimi sitalala na mtu tena. Mbona nimetulia tu.” “Si kwa kuwa upo humu ndani muda wote! Sasa unataka kufuata vishawishi kwa watoto walioshindikana kwa mama zao, na wake zao! Si watakuchezea uje uniachie mtoto humu ndani? We Ron nenda kalale, uwahi kazini kesho.” Mina akaanza kulia.

“Nimebadilika mama. Nitatulia kama Ron. Nitafanya kazi na wala hutasikia malalamiko. Mwambie mama Jumaa awe ananiulizia huko kazini. Akisikia tatizo hata dogo tu, akwambie.” “Bwana weee, njoo tulale.” Mama yake akakataa kabisa.

“Labda mama tumpe nafasi ya mwisho. Na kwa kuwa ni huko huko mjini, mimi nitakuwa nakwenda naye na kurudi naye.” “Ron, unatafuta balaa mwanangu wewe!” “Nitamwangalia mama. Mjaribishe.” “Utakuja kusema nilikwambia mimi. Haya! Wewe ona hayo machozi, ujirudi wakati ulianza naye vizuri sana.” Mama yao akatoka.

“Nimebadilika mama.” “Kama kweli umebadilika, kwa nini huendi shule? Alichokwambia Ron si ndicho nilichokwambia na mimi asubuhi?” Kimya. “Ron, baba, naomba huyu niachie mimi mwenyewe. Atatuzungusha hapa, wote tuishie kuumwa vichwa. Unakumbuka habari za yule mwarabu?” “Mbona sijakuwa na mwanaume mwingine tena, mama? Nilikwambia nitatulia, mbona niliacha mambo ya wanaume. Kwani nilirudia tena?” “Ukifika huko ukakutana na mwingine akakudanganya kama yule mwarabu aliyekutorosha hapa, mimi nikabaki hapa kama mwehu?” “Mbona nilitulia baada ya pale na nikaomba msamaha?” Mina akaendelea kuwakumbusha kwa kuwabembeleza huku akilia.

“Mnaondoka hapa wote wawili. Mnaniacha peke yangu, mbona siendi popote na wala sileti mwanaume humu ndani? Kwani mnafikiri mimi sitongozwi tena? Nilijifunza kutokana na makosa, halafu nilikuwa mdogo, mama. Sasa hivi nimekua mkubwa.” Mina akaendelea kubembeleza. Lakini ikawa kama anayempigia mbuzi gitaa kwa mama yake.

“Ukitaka nikuruhusu utoke humu ndani, iwe shule. Wewe chagua chochote unachotaka kusoma kisicho na hesabu wala biology,  mimi nitalipa, ukasome. Lakini si kazi. Unataka kuniua Ron, mwanangu!” Mama yao akawabadilikia.

“Hivyo alivyo huyo, eti uende ukamuweke katikati ya wanaume wenye uchu! Ili iweje kama sio kutaka kunichanganya mimi akili? Niambie huo mshahara wanaotaka kukulipa huko, mimi nikupe kila mwezi lakini sio kwenda kuuza mgahawa.” Akataka kurudi ndani, akageuka.

“Na ninaomba kitakachotoka hapo mdomoni kwako ni unaomba kwenda shule, Mina. Hapo tutaelewana. Sema shule yeyote ile, mimi nitauza hata viatu, usome. Lakini sio kwenda kuwahudumia wanaume huko mjini.” Mina akaishiwa nguvu.

“Wewe unaakili Mina. Na cheti chako cha kidato cha nne sio kibaya. Kwa nini hutaki kusoma na sisi tupo hapa kukusaidia?” Ron akamuuliza kwa kumjali dada yake. “Jinyime hata miaka miwili tu. Upate kitu chakueleweka. Umepoteza muda mwingi sana hapa nyumbani ukizunguka tu, au kulala. Soma.” “Mimi sitaki kusoma mambo magumu halafu hayana hata maana maishani!” “Basi somea hata mapishi. Mwenzio narudi tena kusoma masomo ya jioni ili nipate shahada ya pili.” “Ron!” Mina akamshangaa sana kaka yake. “Kweli Mina. Sina kinachonizuia.” Mina akatulia.

“Tuanze wote, Mina. Wewe chagua unachotaka kusoma, nitakutafutia shule hata ya jioni. Tunakuwa tunaenda wote.” “Hicho kitu kikiwa na mahesabu je? Maana huwa wanapenda kufanya mambo magumu bila sababu!” Mina akalalamika. “Mimi nitakusaidia au tutatafuta mwalimu waziada akusaidie.” Mina akabaki akifikiria.

Kisha akawa kama amepata wazo. “Basi nianze kusomea mambo ya usekretari. Kwani yana mahesabu?” Ron akacheka. “Nimekwambia usiogope. Mimi nitakufundisha. Na ili uwe sekretari mzuri, ongeza na kompyuta.” “Sasa wewe hapo unataka kumpoteza kabisa.” Akadakia mama yao.

“Ungebaki hapohapo kwenye usekretari. Unataka kuweka ugumu, mwenzio aache.” Akaongeza mama yao akiwa chumbani. “Eti Mina mdogo wangu? Itakusaidia kupata kazi haraka. Husomei mambo magumu. Ni vile vitu vya msingi tu. Angalau uijue kompyuta na jinsi yakutumia. Mimi nakuaminia.” Mina akacheka.

“Mmmh!” Wakamsikia mama yao anaguna ndani. “Nitaweza mama.” “Kwani hilo ni tatizo Mina mwanangu? Ni uweze na utulie mpaka umalize. Maana kumaliza tu hicho kidato cha nne, nilicheza ngoma zote!” “Sikusumbua sana mama jamani! Darasani nilikuwa nikiji...” “Usitake nitoke hapa kitandani.” “Lakini si nimesema nimebadilika?” Akamkatiza mama yake kama asikumbushie huku akitaka kuanza kulia.

“Mimi naona tuanzie leo. Kwa hiyo umekubali kusoma kompyuta?” Ron akauliza. “Maana pale karibu na ninapofanya kazi, kuna chuo kidogo tu, wanasomea mambo ya kompyuta. Kuchapisha. Microsoft word na Excel. Hivyo tu. Wala huhitaji mambo mengi.” “Sawa.” Kukazuka ukimya wa gafla kama ambao hawakutegemea.

“Tatizo lenu nyinyi hamniamini. Nimesema sawa, mnakuwa kama mnasita tena! Sasa mnataka nini kutoka kwangu?” “Mimi nakuamini Mina. Kesho nakwenda kuzungumza nao, nakujia na fomu zakujaza, nalipia kabisa, jumatatu uanze kama wananafasi.” “Sawa.” Akakubali bila shida.

“Mimi nina wazo.” Akatoka mama yao. “Hiyo ada usilipe yote Ron, mwanangu. Lipa kidogo ili akajaribu. Vikimshinda, usiwe umepoteza pesa yote.” Mina akaguna. Akasimama na kuondoka hapo kabisa. “Umenisikia Ron, baba? Tuna shida sana na pesa. Naomba tusitupe pesa kwa ajili ya Mina. Unamjua Mina, hatabiriki. Anaweza akazua jambo mahali, tukahitaji hizo pesa kwa ajili ya kwenda kulipa, ili asipelekwe polisi.” “Naomba tumpe nafasi nyingine mama.” “Sawa Ron. Mimi nipo hapa, na utakuja kuniambia. Wewe unasahau mimi ndio nimehangaika naye huyu, mpaka nikaona akae tu nyumbani?”

“Kila mahali anaanza vizuri tu. Kabla hata hajafunga juma, anaharibu vibaya sana mpaka ananiachia deni mimi, nabaki nikilipa ili wasimpeleke polisi. Unakumbuka aliporudi hapa baada ya kutoroka na yule mwanaume wake fundi sijui mfanyakazi wa mwarabu, nikamuomba asome hata certificate ya mambo ya stoo?” “Nakumbuka mama. Lakini ameahidi amebadilika.” “Kwa lipi Ron? Nililipa pesa yangu pale TIA, akasoma mwezi mmoja tu, akaanza sababu na kuacha chuo kabisa. Pesa yangu ikapotea hivihivi! Mina sio..” “Naomba tujaribu tena mama. Sasa unafikiri mwisho wake utakuwa nini? Tujaribu tu.” “Sawa baba. Mimi nakuhurumia wewe. Pesa yako unaihangaikia sana. Sitaki kuja kuona inapotea hivi hivi.”

“Wewe usiwe na wasiwasi.” “Au basi nipe mwezi huu nikupe mimi hiyo ada yake.” “Usiwe na wasiwasi mama. Mimi pesa ninayo.” “Na wewe chuo chako nani atakulipia ada? Naona heri wewe mwenye uhakika uanze, yeye tunayembembeleza asubiri mpaka nipate pesa. Ya kwangu ikipotea ni afadhali kwa kuwa Mina ni jukumu langu, sio wewe ambaye unaanza maisha.” “Wewe usijali mama. Naamini yote yatakwenda pamoja.” Ron akajaribu kumtuliza.

 “Haya. Ila nakuahidi mwisho wa mwezi nitakurudishia ili na wewe usome vizuri.” “Nikiishiwa nitakwambia. Usiwe na wasiwasi.” Mina akaumia sana huko chumbani alipokuwa amelala, lakini akanyamaza. Ni kweli alishaharibu sana hapo.

~~~~~~~~~~~~~

Ron akamalizia taratibu zote za shule ya Mina. Alitakiwa kuingia mchana wa saa nane na nusu kutoka saa kumi na nusu jioni. Ron akaipenda hiyo ratiba. Siku ya ijumaa usiku aliporudi nyumbani akamfuata Mina chumbani. Akarusha zile fomu kitandani. “Unatakiwa kuanza shule jumatatu. Ratiba zote ziko hapo, pata muda wakusoma.” Mina akakaa. “Nashukuru Ron. Nakuahidi nitatulia.” “Naomba iwe hivyo Mina. Mama anahangaika sana kwa ajili yetu. Jitahidi.” “Nitajitahidi. Si umesema nikikwama utanisaidia?” “Uliza tu.” “Nitatulia Ron. Nakuahidi safari hii nitatulia.” Ron akatoka.

Jumatatu.

Jumatatu wote walitoka, wakamuacha Mina nyumbani kwa makubaliano atakwenda shule mchana. Kila mtu aliomba Mungu asibadili mawazo. Ilipofika mchana kweli Mina akatoka na kuelekea mitaa ya Samora, karibu kabisa na ilipo ofisi ya kaka yake. Alipofika tu, akamtumia ujumbe Ron. ‘Nimefika, sijapotea.’ Ron akashukuru Mungu. ‘Haya. Ukitoka uje hapa moja kwa moja, tutarudi wote nyumbani.’ ‘Sawa.’  Akamjibu kaka yake.

Kwenye saa 11 kasoro ndipo Mina akawa amemaliza, akaanza kutembea taratibu kwenda ofisini kwa kaka yake ambako hakuwa hata amewahi kufika. Akafika mapokezi, akamkuta sekretari nadhifu sana. Mzuri, ofisi safi mpaka akababaika. “Mimi ni dada yake Ron. Namtaka Ron.” Yule msichana akacheka na kunyanyua simu. “Una mgeni wako hapa.” “Mwelekeze aje huku.” Akakata simu. “Amekwambia uende.” Mina akafikiria kidogo.

Kisha akaona aulize. “Kwani wewe kazi yako ni nini hapa?”  Akauliza bila aibu kama kawaida yake. “Mimi ni sekretari wa hapa.” “Ndio umesoma sana eeh!?” Yule dada akacheka. “Kiasi. Na wewe unataka kuwa sekretari?” Mina akacheka na kutingisha kichwa akikubali. “Ni ngumu?” Akamuuliza tena. “Ni umakinifu tu. Utaweza. Siku nyingine ukiwahi nitakuja kukuonyesha ninachofanya, sasa hivi nakaribia kutoka.” “Basi mwambie Ron. Ukimwambia wewe, ndio atanikubalia kukaa hapa. Hivi hivi atakataa.” Akacheka. “Nitamwambia.” “Asante. Akikubali nitakuwa nawahi kidogo halafu tunakaa wote ndio nakwenda shule.” “Unasomea nini?” Mina akamuelezea. “Umeanza pazuri sana.” Akamtia moyo.

Mara Ron akaja. “Nilikwambia nini wewe?” Akamuuliza Mina kwa ukali kidogo. “Ni yeye ndio ameniongelesha Ron! Muulize mwenyewe.” “Twende.” Akamshika mkono kabisa. “Sijafanya kitu Ron!” Mina akajitetea. “We Ron!”  Yule msichana akamuita wakati Ron akimvuta Mina. Akageuka. “Mwache bwana! Mimi ndio nilikuwa namuuliza maswali. Nimekaona karembo ndio nikamuuliza anafanya nini! Na nimemkaribisha kesho aje aone kazi zangu.” Ron akamgeukia Mina kwa ukali.

“Unapata dhambi bure Ron!” Mina akalalamika. “Sijafanya kitu chochote zaidi ya kukuulizia wewe.” “Hujaanza maswali yako pale?” Ron alimjua Mina. “Hajaanza bwana.! Muache.” Akamtetea kabla Mina mwenyewe hajajibu. Ron akamvuta mkono na kuondoka naye pale.

“Hii ofisi ipo kimya kama unavyoona. Ni kazi tu. Usiongee chochote. Umenisikia Mina?” Kimya huku wakiendelea kutembea na kaka yake akiongea sauti ya chini. “We Mina?”  Akamwita kwa ukali. “Si umesema nisiongee wewe? Unanianza mwenyewe!” “Na hapa mwenzio naheshimiwa, usianze uchokozi wako.” Mina akacheka. “Ukianza fujo hapa, nakuacha hapa hapa mjini, uone kama giza halijakukuta mtaani unahangaika.” “Utapambana na mama Ron.” Akajibu Mina huku akicheka.

Wakaingia ofisini. “Mbona unamvuta!?” Hatibu akauliza huku akicheka. Ron akavuta kiti pembeni yake, nyuma ya meza. “Ukae hapo na usifungue mdomo hata kwa neno moja, mpaka nimalize kazi ndio tuondoke.” Kimya. Hatibu akaanza kucheka. “Mina! Mina!” Hatibu akamuita. Mina akamwangalia kama acheke, akanyamaza. “Kumbe Mina mtoto mzuri? Ukiambiwa jambo unasikia!” Mina akacheka na kumwangalia Ron. Ron alionekana na kazi yakumalizia. Akaendelea na kazi zake.

Baada ya muda wakaanza kuaga mmoja baada ya mwingine. Akabakia Hatibu na wao. Ilipofika saa 11 kamili Hatibu akaaga. “Mina! Nitakuona lini tena mtoto mzuri?” Hatibu akauliza huku akicheka. Mina kimya. “Mina?” Kimya. Hatibu akazidi kucheka. Akaondoka.

Mara mlango wa ofisini kwa Andy ukafunguliwa. “Namalizia kiongozi. Naona itaisha mapema hata kabla ya 11 na nusu.” “Hamna shida. Mimi bado nipo.” Macho ya Andy yalitua kwa Mina. Mina akainama. Ron akarudisha macho kwenye kompyuta, Mina akaendelea kuangalia daftari. “Sikujua kama Mina upo!”  Kimya. Hakumjibu.

“Ameanza shule. Anatoka mida hii, ndio nimeona awe ananipitia ili anisubirie tuwe tunarudi naye nyumbani. Au kuna tatizo akiwa hapa?” Ron akauliza kwa wasiwasi kidogo akihisi amevuka mipaka. “Hamna shida. Anaruhusiwa kukaa popote pale.” “Nashukuru. Naamini hatasumbua.” Andy akacheka, Ron akamgeukia Mina, bado alikuwa ameinama vilevile, kimya. Ron akaendelea na kazi zake, Mina akafungua mkoba wake akaanza kutoa makaratasi fulani na kuanza kuyasoma. Hakuwa amemsalimia Andy na macho yalipogongana tu, akainamisha, hakurudia tena kumtizama. Andy akaondoka kurudi ofisini kwake.

~~~~~~~~~~~~~

Alikaa pale, vilevile bila hata kusogea au kuzungumza mpaka Ron alipomwambia waondoke. Akakusanya vitu vyake. “Vipi lakini? Umeonaje siku ya kwanza?” Ron akamuuliza wakati anakusanya na yeye vitu vyake. “Sio mbaya. Leo ilikuwa utangulizi tu. Hakuna hesabu.” Ron akacheka. “Umeuliza?” “Ndio lilikuwa swali la kwanza. Lakini anaonekana ni mwalimu mzuri.” Mina akamuelezea kaka yake huku wanatoka.

“Kwa hiyo utarudi tena kesho?” Ron akamuuliza kumjaribisha. “Nitasoma Ron. Ila naomba niruhusu niwe nakuja kukaa na huyu sekretari wenu hapa! Nakuahidi sitasumbua. Nitafanya kile atakachokuwa ananituma, basi.” “Sijui Mina! Sitaki Andy aone kama nafanya fujo au najichukulia madaraka!” Mina akapoa kidogo.

Kisha akauliza. “Kwani ndio bosi wenu peke yeke?” “Kwa kitengo chetu, ndiye kiongozi wetu japo anao viongozi wengine juu yake. Ila anao uwezo wa kusema hakuhitaji hapa kwenye kitengo chake, ukafukuzwa. Wanamtegemea sana. Na yeye sio kama yule kiongozi wetu aliyepita. Huyu anachapa sana kazi, hana maneno mengi au mambo ya uswahili swahili.” Mina akafikiria.

“Nitatulia Ron!” Akabembeleza. “Acha kesho nizungumze na Lea ili nijue anataka ufanye nini. Halafu nitakwambia kama uwahi au la.” Mina akafurahi sana. “Ukinifanikishia hilo, nitakuwa nakufulia nguo zako zote mpaka suruali.” Ron akacheka sana. “Acha hongo wewe!” “Ndio uende ukampange huyo Lea. Huwezi jua nitapata ujuzi, nikawa sekretari mzuri sana.” “Haya. Naona safari hii kweli umebadilika!” Wakaendelea kuzungumza wawili hao wakirudi kwao.

~~~~~~~~~~~~~

Siku inayofuata kama kawaida Ron aliondoka asubuhi na mapema na kumuacha Mina nyumbani. Ilipofika kama kwenye saa nne hivi, simu ya kaka yake ikaingia. Akapokea kwa haraka sana. “Lea amesema unaweza kuja wakati wowote umsaidie kazi.” Mina akafurahi sana. “Nakuja sasa hivi.” “Sasa uje umevaa kwa heshima Mina. Sio zile nguo zako zakubana.” Mina akanyamaza. “We Mina?” “Sasa mimi nitavaa nini Ron jamani!?” “Tutanunua nguo nyingine, lakini leo naomba ujitahidi uvae kwa heshima. Na si unajua hakuna kulipwa?” “Najua Ron. Si najifunza tu!” Ron akakata simu.

Saa tano na nusu Mina akawa amefika pale ofisini. Lea akaanza kucheka. “Sasa wewe sekratari wangu itabidi tuanze marekebisho. Sekretari ni kioo cha ofisi au kampuni nzima. Kabla mteja hajamuona au kuzungumza na meneja, anaanza na wewe. Kwa hiyo lazima upendeze. Acha kubana nywele kama mtoto wa shule ya msingi! Mina akacheka.

“Akikusikia Ron, atanikatalia mwenzio kuja hapa. Taratibu.” “Basi tuanze na nywele hizo. Toa hicho kibanio nyuma. Achia nywele. Mwenyewe una kasura kazuri na umbo zuri. Lazima upendeze.” Wakacheka taratibu. Lea akamtoa kile kibanio, akamchana nywele vizuri na kumpaka mafuta ya mdomo akampa na hereni alizokuwa nazo kwenye pochi yake.

“Jiangalie kwenye kioo uone jinsi ulivyopendeza.” Mina akacheka. “Haa! Nimebadilika mpaka sura! Asante.” Wakakaa chini wakicheka maana alikuwa akimtengeneza hapohapo mapokezi. Akaanza kumuonyesha anachofanya huku wanacheka.

Andy alifika pale na kuduaa. “Nimeongea na Reji, amesema ni sawa. Anaweza kukaa tu hapa.” Akawahi Lea akijitetea. Kila mtu alijua alishakuwa na mahusiano na Reji ambae ni bosi wake Andy.

Mina akageukia kompyuta. “Naamini hakuna shida. Si ndiyo?” Akaongeza Lea kijasiri kidogo. Maana alishatanguliza kuwa ameongea na bosi wao. “Hamna shida. Hujambo Mina?” “Sijambo. Shikamoo.” Akasalimia Mina akiwa ameinamia kompyuta bila hata ya kumwangalia. Mlango ukafunguliwa, alikuwa Lora. Wote wakageukia mlangoni.

“Si ndio muda wenyewe au nimewahi?” Akauliza Lora na tabasamu kubwa usoni. Andy akaangalia muda. “Naona ni sawa. Karibu.” Lora akafika pale mapokezi akawasalimia Lea na Mina, akambusu Andy. Ni kama Andy hakuwa ametarajia. Akapata busu la mdomoni na tabasamu zuri. Mina akarudisha macho kwenye kompyuta. Andy na Lora wakaondoka pale mapokezi wakielekea ofisini kwa Andy.

Alipojiridhisha wapo peke yao, Lea akamgeukia Mina. “Wewe Mina vipi!?” “Nini?” “Mjini watu hawasalimiani, ‘shikamoo’. Sasa utawapa wangapi ‘shikamoo’!?” Mina akacheka akifikiria. “Lakini Ron aliniambia ni bosi wake!” “Kwa hiyo!?” “Si mkubwa kwa Ron!” “Inahusu!?” Mina akaanza kucheka tena.

“Acha mambo ya ajabu bwana!” “Sasa nimsalimieje?” Wakaanza siku hiyo vizuri. Akampenda sana Lea. Mcheshi na akaonekana amemkubali Mina.  Muda wake wa kwenda shule ulipofika, Ron akamfuata. “Alishaondoka.” Lea akamwambia Ron. “Afadhali.” Hilo likamfurahisha sana Ron.

 ~~~~~~~~~~~~~

Walifanya hivyo hiyo siku ya jumanne mpaka ijumaa. Mina anafika hapo asubuhi ya saa nne. Ikifika saa nane na dakika 20 anakwenda shule, akitoka saa 10:30 jioni au 10:45 jioni anarudi kwa Lea. Wanamalizia kazi. Lea akiondoka, anakwenda kukaa ofisini kwa kina Ron.

Siku ya ijumaa akamuomba Lea wakati anaondoka amwachie kompyuta ili aendelee kujaribisha kuchapisha kama mazoezi. Akamkubalia. Ilipofika saa 10:50 jioni, akaondoka na kumuacha Mina kwenye kompyuta. Ron alijua.

Akiwa anahangaika na kuchapisha taratibu akashitukia Andy amesimama mbele yake. “Lea ameniruhusu.” Mina akaongea kwa kujihami akionekana wazi ameingiwa hofu. “Hamna shida. Vipi lakini, unaendeleaje?” “Vizuri.” Akajibu Mina na kurudi kwenye kompyuta. Kimya kikazuka.

“Ulipona kabisa?”  Andy akauliza. Mina akatulia kidogo kama anayejiuliza jambo, kisha akaendelea kuchapa. Mara Ron akaja. “Umefanya nini tena!?” “Sijafanya kitu Ron jamani! Na wala sijasimama hapa kwenda popote, kama ulivyoniambia.” Mina akajitetea.

“Nilikuwa natoka, nimesimama tu hapa kusalimia. Hamna alipokosea.” Andy alitetea huku akicheka. “Maana Mina bwana! Twende.” “Ndio ujue unanioneaga bure mimi!” Akakusanya vitu vyae. “Kesho tumeambiwa kama tunataka kufanya mazoezi ya kuchapisha ili kuongeza spidi twende hapo chuoni.” “Nimekwambia nyumbani kuna kompyuta.” “Lakini hauna zile games za ku type!” “Nimekwambia nitakuwekea. Twende, kabla hatujazidi kuchelewa.” Andy alibaki pale mapokezi ameinamia simu yake kama anayeitumia huku akiwasikiliza ndugu hao wawili.

“Kwa hiyo nimwambie mwalimu sitakwenda?” “Una nini wewe Mina!? Kwanza nani amekwambia uwe na namba yake? Nilikwambia nini wewe?” “Naomba usikasirike Ron! Sijafanya kitu chochote. Karatasi zile ulizonipa siku ya kwanza kabisa, ndio amesema zina namba zake za simu. Sio kwamba nina namba yake kibinafsi!” “Basi hakuna kumtumia ujumbe.” Ron akaongea kwa mkwara.

“Sasa unakasirika nini wakati wewe mwenyewe ulijaza namba yangu ya simu kwenye zile fomu? Na mwalimu yule amefungua kundi kwenye Whatsapps tupo humo wanafunzi wote. Mawasiliano yote yanaendelea humo ndani. Na alitaka kujua wangapi watataka kwenda ili ajue kama atafungua chumba cha kompyuta au la! Sio mimi peke yangu.” “Naomba twende nyumbani Mina. Utafanyia nyumbani.” “Sawa. Nisaidie sasa kubeba! Upoje Ron?” “Halafu wewe utabeba nini?” “Kwani wewe unabeba nini?” Mina akamuuliza.

“Mimi nabeba mkoba wangu na wewe beba wako.” “Wenzako wanabebea dada zao mifuko yao, wewe sijui ni likaka la namna gani!” “Haya kusanya basi twende!” “Kwa hiyo utabeba?” Mina akauliza huku akicheka. “Naomba nipe, twende Mina. Mama ataingiwa na wasiwasi.” Mina akacheka, nakumalizia kila kitu kuweka kwenye mkoba wake.

Ron akaubeba mkoba wa Mina ulioonekana ni wa kike kabisa. “Usiku mwema Kiongozi.” Akaaga Ron. “Na nyinyi.” “Unataka nikwambie leo tumejifunza nini?” Akamsikia Mina akimuuliza kaka yake huku akicheka. “Unafurahia lakini?” Andy akaendelea kumsikia Ron akimuuliza dada yake wakiwa wanaelekea mlango mkubwa ili watoke.

~~~~~~~~~~~~~

Siku ya jumatatu darasa la kina Mina liliahirishwa. Kwa hiyo akawa yupo tu pale ofisini karibu siku nzima akitumwa huku na kule na Lea. “Hizi ni za Andy. Mpelekee ofisini kwake, mwambie ni fax zake zimekuja na jina lake.” Mina akazipokea. Badala ya kwenda ofisini kwa Andy moja kwa moja akapitiliza mpaka ofisini kwa kaka yake.

“Unataka nini huku?” “Nimekuja kukusalimia Ron, jamani!” “Nenda katulie Mina!” Mina akaanza kucheka. “Ron muoga jamani! Sasa unafikiri hapa mimi nitaharibu nini?” “Hukawii hata kuangukia kompyuta wewe! Ondoka bwana.” Kila mtu akaanza kucheka, Mina akaondoka.

Akamuona anaelekea ofisini kwa Andy. “We Mina!?” Akashituka Ron mpaka akasimama. “Huko ni ofisini kwa bosi, wewe!” “Relax, Ron! Nimetumwa hizi karatasi.” “Tafadhali usiguse kitu humo ndani.” Mina akacheka. “Mina?” Ron akaita kwa kunong’ona ila kwa ukali. “Sigusi kitu. Namkabidhi tu karatasi zake halafu..” “Na usiulize swali lolote lile. Mkabidhi karatasi zake, kisha toka. Unanisikia Mina?” “Sawa.” Hatibu alikuwa akicheka sana.

“Mina hatulii bwana!” “Anaakili  zake timamu. Hawezi kufanya jambo la ajabu.” Akamtetea Hatibu. “Daah! Natamani kama ungemjua huyo. Aliuza duka la watu, mama akaishia kulipa hasara.” Wote wakaanza kucheka. “Kweli tena. Akiwa kazini huyo, mama yake anakusanya pesa yakuja kulipa hasara atakayoingiza.” Wote wakazidi kucheka.

Kwa Mara ya Kwanza, Mina Ofisini kwa Andy

Mina akagonga akasikia akikaribishwa. Akaingia. “Nimetumwa na Lea. Amesema nilete ni Fax, imetumwa kwako.” “Asante. Vipi lakini?” “Salama. Niweke wapi?” Akauliza maana aliambiwa na Ron asiguse kitu. “Nitazipokea. Asante.” Mina akasogea karibu. “Unaonaje kazi ya sekretari?” Akauliza tena Andy. “Bado najifunza.” “Lakini kwa mwanzoni? Shule?” “Naendelea vizuri.” Akajibu taratibu, akainama kama anayefikiria, kisha akaamua kuondoka.

“Mina!” Andy akamuita na kusimama. “Samahani siku ile nilishindwa kurudi hospitalini kukuona.” “Kwa nini?” Akauliza Mina kwa upole, Andy hakutegemea. “Nilipata wageni nikashindwa kuondoka.” “Sema wageni wa muhimu kuliko kuja kuniona mimi hospitalini nikiwa mgonjwa!”  Andy akababaika sana.

Ila akaishia kusema. “Walikuja kuondoka muda wa kuona wagonjwa ulikuwa umeshakwisha.” “Walikaa mpaka jumatano niliporuhisiwa kutoka hospitalini?”  Akauliza Mina kwa upole na uchungu kama anamdai huyo Andy. Andy akashindwa kujibu kabisa.

Usingeniahidi wakati ulijua wazi una watu wako wa muhimu. Ulinidanganya bila sababu, tena ulirudia zaidi ya mara moja! Nikakuamini. Usifanyie hivyo watu. Ni vibaya.” Mina akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~

Andy aliumia sana. Akabaki amesimama pale nakushindwa hata kurudi kukaa. Ni kweli Mina alilazwa, akatolewa hospitalini siku ya jumatano. Kama alishindwa siku ya jumapili, na jumatatu? Jumanne! Jumatano je! “Inamaana Mina alinisubiri!” Akajiuliza Andy.

“Asingeumia hivi!”  Akazidi kujichukia. Akamlaumu Lora na Devi, lakini mwishoe akajilaumu mwenyewe, akatamani kama amfuate pale mapokezi, lakini Lea alikuwepo. Na Lora alishajaa mle ndani, watu walishajua amepata msichana.

~~~~~~~~~~~~~

Siku inayofuata Ron alitakiwa makao makuu ya ofisi yao, Kinondoni. Wakati Mina yupo kwa Lea, karibia na muda wa darasani  kufika, Ron akamfuata na kumwambia anakwenda Makao Makuu, lakini lazima arudi pale ofisini kumfuata kabla ya saa 11 jioni, warudi wote nyumbani.

Akiwa darasani, yakaanza manyunyu. Akamtumia ujumbe Ron. ‘Umesharudi? Mvua inaanza, usije ukarudi nyumbani ukanisahau, Ron!’ ‘Acha woga wewe. Nitakuja kukufuata. Nisubirie palepale kwa Lea.’ Hapo Mina akavuta pumzi.

~~~~~~~~~~~~~

Saa kumi kamili mwalimu akawaruhusu na kuwaambia mvua itanyesha sana, wawahi kuondoka. Mina akakusanya vitu vyake, akakimbilia ofisini kwa kina Ron. Akamkuta Lea anaondoka. “Nawahi foleni.” Akamuacha hapo. Akaenda ofisini kwa kina Ron. Akamkuta amebaki Hatibu tu. “Ron hajarudi mpaka sasa!?” “Sidhani kama atarudi sasa hivi.” “Mpigie. Mimi siwezi kurudi nyumbani bila Ron.” Hatibu akacheka na kupiga simu alipokuwa Ron. Akamsikia akicheka. “Sawa.” Akajibu na kukata simu. “Wamekwambiaje?” Mina akauliza. “Wamesema Ron ametoka hapo muda sio mrefu anakimbilia kituoni.” Mina akatulia kwenye kiti cha Ron. Kimya.

“Mvua imeanza Mina. Mimi naondoka.” “Basi mimi nakwenda kumsubiria Ron hapo mapokezi. Sitaki kubaki hapa peke yangu.” Wakaongozana mpaka mapokezi. Hatibu akaondoka na kumuacha Mina amekaa hapo. Akaanza kuchapa. Hata spidi ilishaongezeka. Muda ulishapita akiwa shuleni. Alibakisha majuma machache tu amalize maswala ya kompyuta.

Wakati anachapa, Andy akatoka ofisini kwake nakumfuata pale. “Mvua inanyesha. Unataka lifti?” Mina akanyamaza. “Mina?” “Mimi namsubiria Ron.” Mina akajibu bila hata kumtizama.

“Ron amekwama kituoni. Hamna daladala zakuja maeneo haya. Kwa nini nisikusogeze mpaka alipo?” Mina akanyamaza. Andy naye akatulia kama anayesubiria jibu. Akamuona anaendelea kuchapa. “Mina?” “Mimi namsubiria Ron. Ameniambia atakuja kunichukua hapa. Najua atakuja. Ron huwa hanidanganyi. Kwa hiyo lazima atakuja. Hata kama kwa kuchelewa, lakini najua atakuja tu.” Andy akajua ni ujumbe wake huo.

“Kila mtu ameondoka hapa ofisini.” Akamuona anakusanya vitu vyake. “Unakwenda wapi sasa?” “Kumsubiria Ron hapo nje kwa mlinzi.” “Sijakufukuza!” Mina akamwangalia. “Kwani wewe huondoki sasa hivi? Si umesema watu wote wameondoka!” “Sina haraka. Nafikiri humu ndani ni sehemu sahihi yakusubiria. Hapo nje pako wazi tu mvua itakunyeshea.” Mina akarudi kukaa.

Akajaribu kumpigia simu Ron, simu ikawa imefungwa. “Ron alisema anaacha simu yake ofisini kwa ajili ya mvua. Isiloe.” Mina hakumjibu, akanyamaza na kurudisha macho kwenye kompyuta.

“Nataka kutengeneza chai. Nikutengenezee na wewe?” Mina akapandisha mabega juu kukataa. “Kahawa?” Akaendelea kuuliza kwa kumbembeleza. Akakataa. “Soda?” Akapandisha tena mabega juu, kukataa. Akamuona ananyanyuka anaelekea upande zilipo ofisi zao. Akamsindikiza kwa macho mpaka akapotelea. Akamfuata. Akaona amekwenda kwenye meza ya Ron anatafuta kitu.

“Unataka nini?” Andy akamuuliza. Kimya. “Labda ukiniambia naweza kukusaidia.” Kimya. Akamuona anajisugua pembeni ya mabega.

“Unasikia baridi?” Kimya. “Mina?” “Naomba uniache. Sitaki kuongea na wewe. Kama hujajua, basi ujue nimekukasirikia.” Andy akatamani kucheka vile alivyoongea kitoto, asijue mwenzie anamaanisha.

“Naomba unisamehe kwa kukuahidi kuja na kushindwa kuja.” “Kwa nini nikusamehe? Kwani ilikuwa bahati mbaya? Ulichagua mtu au watu wa muhimu kuliko mimi. Sasa kwa nini unaomba msamaha? Nimekwambia usinidanganye.” “Sikudanganyi Mina!” Andy akajaribu kujitetea.

“Mimi huwa najua mtu akinidanganya. Na huwa sipendi kudanganywa. Kwanza hata sidhani kama ulikumbuka kama nilikuwa hospitalini!” “Kumbuka mimi mwenyewe ndiye nilikuja kukuona Mina! Sikuwa na sababu ya kuja, isipokuwa kujali.” Mina akakunja uso. Kisha akaamua kuondoka.

“Mina?” “Naomba uniache. Sitaki kudanganywa zaidi. Wewe unajali kwa sekunde. Unatoa ahadi, halafu hata hukumbuki! Baada ya miezi ndio unakumbuka! Wewe ni mbaya Andy.” Mina aliendelea kutembea kurudi kwenye meza ya mapokezi. Andy akaingia ofisini kwake, akachukua koti akatoka.

Akamkuta ameinama kwenye meza yake anachapa. Akazunguka nyuma ya meza akamfunika lile koti. “Asante.” Akashukuru. “Unataka chai, Milo, cocoa au kahawa?” “Mimi sitaki kitu.” “Kwa kuwa umenikasirikia?” Akanyamaza. Andy akavuta kiti alichokuwa amekalia Mina, taratibu tu na kumgeuzia nyuma alipokuwa amesimama. Mina akamwangalia.

“Nikwambie ukweli utanisikiliza?” Mina akabaki kimya akimtizama. Akavuta kiti na kukaa mbele yake. “Unamjua yule msichana anakuja hapa kunitembelea?” “Yule mpenzi wako?” Andy akababaika kidogo. “Si yule anapenda kukubusu midomoni? Au unamzungumzia msichana gani mwingine?” Mina akaendelea kugongelea msumari.

“Anaitwa Lora. Tunafahamiana muda mrefu. Nafikiri tokea watoto, ila yeye ni mdogo kidogo kwangu, ni kama analingana na Paul mdogo wangu wa mwisho japo si marafiki wa karibu.” “Ila alikuwa rafiki yako wewe?”  Andy akacheka kidogo.

“Mimi nilisoma shule ya bweni tokea chekechea mpaka chuo. Nilirudi hapa kwa ajili ya hii kazi.” “Unaipenda?” Mina akauliza kwa upendo. “Yeah! Naipenda.” Andy akajibu huku akicheka. “Hongera.” Andy akacheka na kuendelea.

“Sasa, siku ile nilipokuja kukuona, nilipanga kurudi kwa hakika.” Andy akamweleza ukweli bila kumficha. Akamuona anacheka. “Ila ni mrembo huyo! Na yeye amesoma kama wewe?” Andy akacheka sana. “Ndiyo. Ila ana kazi kubwa zaidi yangu.” Mina akafikiria kidogo.

Kisha akamwangalia. “Sasa uliposikia kama nimehamishwa hospitali, kwa nini hukuuliza ili uje unione? Au hukuona umuhimu tena?” Akauliza kwa upole na unyonge.

`“Niliona umuhimu Mina. Ila kumbuka mimi ni bosi wake Ron. Sio rafiki. Leo namuuliziaje habari zako? Unafikiri atanielewaje?” Mina akanyamaza na kuinama.

“Ndio maswali yaliyonifanya nishindwe kujua hata ulipo na kuja kukuona.” Mina akanyamaza. “Huwezi amini nilitamani hata kuja nyumbani, pia nikaona sitaeleweka vizuri.” “Kwa nani? Ron au Lora?” Akauliza tena taratibu tu. “Ron! Wala sina wasiwasi na Lora. Ila Ron. Naona jinsi Ron anavyokuchunga. Najua asingeelewa kama ningekuulizia kwake.” Mina akavuta pumzi kwa nguvu, akanyamaza.

“Umenielewa?” Akauliza Andy na kujisahau akamvuta mkono na kuushika. “Haijalishi tena, Andy.” Akajibu taratibu. “Inajalisha kwangu, Mina.” “Sidhani. Tuache tu.” “Kwa nini!?” “Iwe ulikuja, au hukuja. Niwe nimekuamini au sijakuamini, itasaidia nini?” Mina akauliza taratibu tu.

“Kama kwako haijalishi, kwangu inajalisha Mina. Sitaki unione mimi muongo.” Mina akacheka taratibu na kuvuta mkono wake, akaukalia na kuinama. “Mina?” Na yeye akamuita kwa kubembeleza. Mina akanyanyua uso na kumtizama. “Umenielewa?”

“Kuwa ulikuwa na ugeni wa muhimu ndio maana ulishindwa kuja?” Mina akauliza kwa upole tu. Andy akazidi kuumia. “Nilikusubiri Andy. Kila wakati nilikuwa nikiangalia mlangoni nikidhani utatokea. Sijui ni kwa nini nilikuamini kuwa ulimaanisha! Na sijui kwa nini imeniuma! Sijui! Labda pengine ni vile ulivyoniahidi kwa kumaanisha! Au vile ulivyorudia! Sijui Andy!”

Lakini ujue wewe sio mtu wa kwanza kunidanganya. Nina uzoefu wa kudanganywa. Ila sijui kwa nini hii imeniumiza!” Mina akajifuta machozi.

“Pengine ndivyo jinsi ulivyo unakuwa hivyo unapozungumza na watu. Lakini kwangu ulisikika tofauti. Ulisika kama mtu ambaye unajali tofauti na wengine. Ulisikika kama mtu ambaye huwezi kuchezea hisia za mtu.” “Samahani Mina!” Andy akazidi kuumia.

“Hapana Andy. Sio kosa lako. Nafikiri ni tatizo langu mimi. Nilikuelewa tofauti na ulivyo.” “Mina, sikukusudia kudanganya. Ni kweli nilijali ndio maana...” “Ulibaki na Lora na si kuja kwangu uliyeniahidi.” Mina akamalizia na kujifuta machozi. “Samahani nilikusoma vibaya Andy. Sio kosa lako, na wala sikutakiwa kukulaumu. Kila mtu anatoa kipaumbele kwa watu wake wa muhimu.” Akavua lile koti, na kumuwekea mapajani kwake. Akaenda chooni.

~~~~~~~~~~~~~

Andy njia panda ya mahusiano, ndani ya Penzi zito. Atafanyaje?

Inaendelea…


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment