Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 2. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 2.

Juma hilo likaenda taratibu Andy akifikiria juu ya maisha yake. Ni kweli alitakiwa kuoa. Hana kisingizio chochote. Na mama yake alishakazania hilo swala, hapakuwa na maongezi mengine kati yao ila ndoa. Na akizungumzia ndoa, Lora ndio mke.

Ijumaa jioni akaamua kumtumia ujumbe Lora akiwa hana uhakika kama atajibiwa baada ya kuachana kwa staili ile siku ya jumatatu. Lora hakuwa binti wa hovyo. Mwanaume yeyote angefurahia kumpata. Kwa uzuri alijaliwa. Binti wa kisasa na hata kwakumwangalia tu, alionekana ana mipango.

‘Week yako inaishaje?’ Akatuma huo ujumbe. Akasubiria karibu masaa mawili, hajajibiwa. Andy alijua anajifanya aghali tu, lakini alijua na yeye analipa. “Atapata wapi mwanaume kama mimi!” Akajisifia Andy kwa kiburi kidogo. Baada ya masaa mawili na nusu, Lora akajibu. ‘Nani mwenzangu?’  Andy akacheka sana. ‘Samahani nilikosea namba.’ Na yeye Andy akaweka nguvu, akatuma huo ujumbe na kusogeza simu mbali kwa hasira.

Jioni wakati anakaribia kutoka ofisini, akaona simu ya Lora ikiingia. Akaiangalia na kuamua kuipuuza. Alishamkera. Akarudisha simu mfukoni, akaenda kuwaaga kina Ron. “Tutaonana jumatatu jamani.” “Mapumziko mema Kiongozi.” Akajibu Hatibu na wengine kasoro Ron aliyekuwa ameinamia kompyuta yake kama amezama kwenye anachofanya.

Ikabidi Andy ajisogeze. “Sasa vipi kesho?”  Akauliza Andy akitaka uitikiwaji kutoka kwa Ron zaidi. “Mimi nipo tu, Mkuu.” Akawahi Hatibu. “Tupe muongozo. Au unasemaje Ron?” Ron akanyanyua kichwa na kumtizama Hatibu akiwa amekunja uso kidogo kama ambaye hakuwa akijua ni nini Hatibu anazungumza.

 “Vipi kesho yako? Kiongozi anauliza.” Hatibu akamuweka sawa. “Kwani kesho kuna mpira tena!?” Ron akauliza kwa mshangao kidogo. “Kwani lazima mpira tu, wewe vipi bwana?” “Hapana. Nilijua nimepitwa na ratiba ya soka.” “Kwa hiyo?” Hatibu akauliza huku Andy akiwaangalia. “Tunaweza kukutana kwangu tukaangalia ligi ya Uingereza kesho jioni. Au mnasemaje?” Akaongeza Andy, lakini nia yake zaidi ni Ron. Ukweli Andy hakuwa na marafiki wengi mjini. Tokea mtoto alikuwa akiishi Nairobi shule za bweni.

“Mimi nitatokea Kiongozi. Mpira wa wengi unanoga.” Akaongezeka na mwingine na mwingine, wakajikuta wamefika wanne, lakini Ron akawa hajatoa jibu la moja kwa moja. Simu ya Lora ikaingia tena. Akataka kuipuuza, akaona aipokee maana kila mtu alitulia kwa muda wakimtizama yeye na simu aliyokuwa ameitoa mfukoni, akabaki akiitizama ikiita. “Basi nitawaona kesho jioni.” Akaaga Andy huku akipokea simu.

“Hellow!” “Andy?” Akauliza Lora. “Ulikuwa ukimpigia nani?” Andy akauliza taratibu tu. “Samahani. Tokea asubuhi nilikuwa na vikao vya hapa na pale, mambo yalikuwa mengi. Nilisoma ujumbe bila kusoma jina.” Andy akajua anadanganywa. “Okay.” Akajibu Andy. “Kwa hiyo ndio sikuwa nimejua kama ndio wewe, nikakuuliza ni nani!” “Utakuwa hukusoma ujumbe uliofuata. Niliomba msamaha kuwa nilikosea namba.” Akamsikia Lora anacheka.

“Nani huyo mwenye bahati yakuuliziwa week yake inaishaje?” “Mwenye namba yangu sahihi.” Akajibu Andy huku akitoka hapo ofisini. “Haya bwana! Na mimi nataka kujua week yako iliendaje?” “Acha kuiga sasa!” “Siigi! Kweli nataka kujua.” Lora akaongea huku akicheka. “Ilikuwa nzuri.” “Nimefurahi kusikia hivyo.” “Yaani umefurahi kusikia week yangu imeenda vizuri!?” Andy akauliza kama hasadiki. “Kabisa.” “Sawa.” Wakatulia kidogo.

“Kesho tunaweza kukutana kwa kifungua kinywa?” Akauliza Lora. “Ila mimi huwa siku za jumamosi natumia muda mwingi mazoezini, gym.” “Naweza kuja huko nikaungana na wewe?” “Unamaanisha uje ufanye mazoezi!?”  Akauliza Andy kama ambaye hajamuelewa vizuri wakati amemsikia vizuri tu. “Ndiyo. Au hamruhusiwi wageni? Maana mimi huwa nakimbia kila siku asubuhi. Sasa naweza kuja kukimbia huko na wewe.” Andy akatulia kidogo, akaona atoe nafasi nyingine.

“Sawa. Hiyo itakuwa nzuri tu. Sikujua kama unapenda mazoezi!” “Ni kukimbia tu. Huwa siwezi kuanza siku bila kukimbia. Labda niwe mgonjwa.” Hilo nalo likamfurahisha Andy. Angalau akaanza kucheka na kuendeleza mazungumzo baada yakuona na hilo wanaendana. Waliendelea kuongelea mambo mengi juu ya umuhimu wa mazoezi huku wakicheka. Waliambiana hili na lile, safari hii na yeye Lora akawa kama amejionya. Akajiwinda maneno.

Andy & Lora.

 Siku ya jumamosi saa moja kasoro asubuhi wote wakajikuta wanaegesha magari yao sehemu moja. Wakacheka. “Mimi nilikuwa nakuwahi wewe ili nisikucheleweshe.” “Na mimi nilikuwa nakuwahi, sikutaka unisubirie kama siku ile.” Andy akaongeza wakati anamsogelea. Akataka kumpa mkono, Lora akajidai kama hajauona, akamsogelea na kumbusu shavuni na kurudi kumwangalia machoni na tabasamu zuri usoni. Andy akacheka kidogo.

Wote walikuwa wamevaa nguo za mazoezi. Lora alipendeza na mwili wake, ungependa kumtizama. Wakaingia ndani moja kwa moja wote wakaelekea kwenye traid mill, mashine ya kukimbilia au kutembea. Wakaanza kukimbia. Kweli Lora alionekana ni mkimbiaji. Alikimbia mpaka Andy mwenyewe akasalimu amri. “Mimi naona nihamie kwenye kunyanyua vyuma.” Lora akacheka huku akiendelea kukimbia. “Nitakufuata. Acha mimi nimalizie hizi dakika tano.” “Sawa.” Andy akaondoka na kumuacha akikimbia.

Wakati anaendelea na mazoezi ya kifua, Lora akawa anakuja akiwa anatokwa jasho, anajikausha na taulo dogo. “Ndio unafanya nini?” Akauliza. “Pumzika kidogo, nikuonyeshe.” Akasimama pembeni huku akimwangalia akiendelea. Baadaye akajiunga naye. Akawa anamwelekeza na kufanya pamoja. Kukawa na kucheka na mazungumzo kidogo juu ya kile wanachokifanya.

Wakawasogelea warembo wawili. “Rafiki yangu amependa couple yenu!” Mmoja wa wale warembo wakawaambia Lora na Andy. Wakacheka. “Asante.” Akajibu Lora huku akimwangalia Andy. Wale warembo wakaondoka. Wakabaki wakicheka tu bila kuzungumzia hilo tena. Andy alikuwa amevaa na yeye kata mikono nyeupe na pensi nyeusi na mistari mweupe pembeni. Raba nzuri ya Nike, na soksi hizo hizo za Nike nyeupe. Safi.

~~~~~~~~~~~~~

Andy alimwambia baada ya mazoezi waende nyumbani kwake atamtengenezea kifungua kinywa kizuri. Mrembo Lora akahamasika kujaliwa na pia akakubali akitaka pia akapaone nyumbani kwake kujua jinsi alivyojijenga kama ni mume wa kuoa au la! Maana hata yeye Lora alikuwa na mume wa ndoto zake. Hakutaka mwanaume aliyechini yake kiuwezo na kimawazo. Angalau walingane na awe na akili za maendeleo sio mzubavu.

Kwa umri wake na urembo wake hakuwa amekosa wanaume au mume wa kumuoa, ila alichagua sana. Hakupata mwenye vigezo vyake vyote. Kila mwanaume alikuwa na kasoro alizoshindwa kuzifumbia macho na kukubali ndoa.

Kwa Andy.

Wakaongozana mpaka kwa Andy akamkaribisha sebuleni. Akawa muungwana akajituliza kochini akisubiria mwenyeji wake afanye mambo yake kama alivyoahidi. Andy aliingia jikoni akaanza kwa kutengeneza smothie nzuri yenye virutubisho muhimu kwa mwili. Lora akaipenda. Wakati wakinywa hiyo smothie, akarudi tena jikoni kutengeneza omlet nzuri sana aliyochanganya na uyoga. Ikaleta ladha zuri kwa zile mboga mboga alizochanganyia kwa kiasi na viungo kwenye yai. Hapo napo Lora akasifia. Wakakaa na kula na maongezi ya hapa na pale wakijaribu kufahamiana.

Hapakuwa na ubishi kuwa wawili hao waliendana. Muda mwingi walijikuta wakicheka mpaka mapungufu mengi aliyoyaona kwa Andy akakubali kuyafungia macho. Angalau Andy akapitishwa japo hakuwa asilimia 100 kwake. Akajiambia akitangaza ndoa, wakishaoana, kwa kuwa amesoma na ana kazi tayari atamrekebisha tu. Kwa wakati huo afunike kombe, mwanaharamu apite.

“Sasa kabla muda wa chakula cha mchana haujanikuta hapa, acha mimi niende. Nikaoge, niende salon.” Andy akacheka na kusimama ili atoe vyombo. “Nashukuru kwa kuja. Uwe na siku njema.” Akaelekea jikoni.

Wakati anageuka akiwa jikoni, Lora alikuwa nyuma yake. Andy alijua anachotaka. Akajisogeza karibu zaidi. “Nimefurahia kila kitu.” Lora aliongea kwa  sauti tulivu na ya chini. “Hata mimi nimekuwa na wakati mzuri. Naamini tutapata wakati..” Lora akawahi midomo ya Andy. Akambusu mara mbili mfululizo. Andy akamshika kiunoni na kumvutia kwake na mkono mwingine akamshika shingoni ili kupata busu zuri zaidi.

Wakabadilishana ndimi, Lora akitoa  pumzi nzuri  za kimahaba. Mwishoe  Andy akamwachia na  kumwangalia, Lora akacheka akilamba midomo ya nje taratibu kama aliyefurahia walichokuwa wamefanya, huku Andy akiwa bado amemkumbatia. Akambusu kichwani. Lora akamwangalia.

“Nitakuona wakati mwingine. Asante.” Lora akajitoa mikononi huku akicheka taratibu. Akaondoka wote wakihema maana walifikia sehemu ambayo ni vile Lora alikumbuka amelowa jasho kwa mazoezi na atakuwa akinuka huko chini zaidi. Asingethubutu kujitoa kwake kwa mara ya kwanza akiwa na harufu ya jasho, lasivyo angechangamkia penzi. Lakini alifurahia sana.

Jioni Ya Jumamosi.

Ilipofika jioni kina Hatibu na wafanyakazi wengine wakaanza kuingia mmoja baada ya mwingine. Andy akajua Ron alishindwa kufika, akatulia tu. Alishapata busu zito asubuhi kutoka kwa Lora, nafsi ikatulia. Akawahudumia vinywaji wageni wake huku maongezi na vicheko vikiendelea lakini upande mwingine wa nafsi ya Andy ulitaka kujua ni kwa nini Ron hajafika. Akapingana na hilo wazo lakini akashindwa.

Hatibu alipokuwa anafuata maji jikoni, Andy naye akamfuata akijidai anataka kumsaidia. “Naona Ron ameshindwa kufika!” Akatupia hilo neno wakiwa jikoni akimpa maji mgeni wake. “Nilikuwa naye hospitalini karibia jioni nzima hii. Tulikuwa tukisubiria dada yake apewe kitanda.” Moyo wa Andy ukashituka sana.

“Hospitali tena!?” “Yeah. Nilimpigia mchana kumwangalia, na kumuuliza kama ataweza kuungana nasi, ndio akaniambia wapo pale tokea asubuhi, amemsindikiza mama yake,  dada yake alikuwa akipandisha homa tokea jana asubuhi. Asubuhi hii akaanza kutapika ndio ikabidi wampeleke hospitalini.” Hatibu akawa amemaliza.

“Sasa walimkuta na nini?” Andy akauliza tena. “Wamempima vitu vingi, lakini si unajua mambo ya hospitali kama zile! Ugonjwa ni mmoja tu. Malaria. Wamemuanzishia dripu. Naona watamlaza hapo kwa siku chache. Ameshindwa kumeza dawa, anatapika sana. Ila mpaka mimi naondoka, alikuwa amelala.” “Kwa hiyo wamemuacha na mama yake?” “Hapana. Pale hakuna nafasi ya kulala na muuguzaji! Wodi yenyewe ilikuwa imejaa. Ilibidi kusubiria kweli. Wamekaa pale tokea asubuhi!”  Andy akajisikia kuumia sana mpaka akajishangaa!

“Umesema ni hospitali ya wapi?” Hatibu akamuelekeza mpaka wodi. “Lakini si unajua pale mida yake? Labda kumpigia tu Ron nakuulizia hali yake. Ila nafikiri Ron atakuwa kazini jumatatu. Hawezi kuacha kuja kazini sababu ya hilo.” Hatibu akaongea hivyo asijue tatizo wala sio kazi. Zile habari zikamuumiza sana Andy na kumpokonya raha nzima ya mpira. Na bahati mbaya na timu yake ikawa imefungwa. Usiku huo ukawa mbaya zaidi kwake hata asikumbuke tena busu la Lora.

Jumapili. Mina!

Alishindwa kujizuia kabisa. Asubuhi na mapema Andy alielekea hospitalini kumuona Mina kana kwamba anamfahamu. Akaulizia ilipo wodi aliyoambiwa na Hatibu, akaonyeshwa. Alimkuta Mina amelala. Akamgusa. “Mina!” Akamgusa tena kidogo. Akaamka. Mina akamwangalia akacheka. “Rafiki yake Ron?” Akauliza na tabasamu la usingizi. “Ulikuja nyumbani.” Akaongeza Mina kama anayejaribu kumkumbuka na cheko la kichovu. Andy akacheka huku akitingisha kichwa kukubali.

“Wewe mbaya!” Akalalamika Mina taratibu. “Kwa nini unasema hivyo, Mina?” “Uliondoka bila kuniaga wakati mimi ndiye niliyekufungulia mlango, wakati rafiki yako akiwa anakoroma!” Wakacheka taratibu, Mina akafunga macho. “Samahani.” Andy akamfanya Mina afungue macho. Akacheka taratibu. “Nakuchokoza tu. Hata hivyo sikuwepo nyumbani. Mama alinituma, kurudi nikaambiwa mlishaondoka.” “Afadhali sina kosa.” Wakacheka tena kidogo.

“Unajisikiaje?” Akamuuliza. “Nimeacha kutapika. Ila kichwa bado kinauma sana.” Machozi yakatoka pembeni ya macho ya Mina, akataka kujifuta. Andy akayawahi. Mina akacheka taratibu. “Asante. Lakini mama amesema labda dripu ya tatu itakuwa nafuu.” “Labda. Pole sana.” Akamfuta tena machozi. “Ila bado kichwa kina moto!” Andy akampapasa kichwani kwa upendo, taratibu. “Walinipa dawa ya kushusha homa. Sidhani kama masaa nane yamepita. Wanakuja kuichoma hapa.” Akamuonyeshea pale palipounganishwa dripu. 

“Unajua hata wanakupa dawa gani?” “Walimwandikia Ron, jana. Akaenda kununua. Ni nyingi, ila najua ipo yakuzuia kutapika na kushusha homa.” “Pole sana. Basi ni kweli kuzipa hizo dawa muda, utapona tu.” “Naamini hivyo.” Mina akajibu taratibu. Wakatulia kidogo.

Kisha Mina akamwangalia. “Umependeza na unanukia vizuri.” Andy akacheka. “Nikitoka hapa, nakwenda kanisani.” “Basi uniombee nipone.” “Nitakuombea.” Wakacheka tena taratibu. “Sijakuletea kitu. Unatamani kula nini?” “Hamna shida. Nashukuru hata kwa kuja kuniona.” Mina akanyoosha mkono wake wa kushoto kule alipokuwa amesimama Andy, Andy akaupokea na kuuminya kidogo. Mina akacheka taratibu kama aliyeridhika.

“Nitakuona baadaye.” “Kwani utarudi tena?” Mina akauliza. “Ndio maana nimeuliza una hamu ya kula nini!” Mina akacheka na kung’ata midomo. “Niambie chochote kile.” Akamwambia kwa kumbembeleza. “Natamani bahati hiyo ningeipata wakati mwingine.” Wakacheka.

“Wakati mwingine unakuja, niambie leo.” “Tokea juzi sina hamu kabisa ya kula. Ila mama alisema ataleta uji wa limao, nijaribu kunywa leo kwa kuwa sijala kama siku tatu hivi, natapika tu!” “Pole sana.” “Asante. Kwa hiyo usilete kitu chochote kile.” Bado Andy alikuwa amemshika mkono. 

Mwisho akajishitukia na kumwachia. “Sawa. Basi nitakuona baadaye.” “Haya. Asante.” Mina akafunga macho, Andy akimtizama. Akamfunika vizuri. Akabaki akimtizama. Mina akafungua macho, akamkuta bado amesimama akimwangalia.

Akatoa tabasamu. “Nilifikiri umeshaondoka! Nafunga macho kupunguza maumivu ya kichwa. Eti naona kama huu mwanga wa taa unanizidishia maumivu ya kichwa!” Andy akamgusa tena kwenye kipanda uso taratibu. “Pole. Wewe pumzika tu, mimi nitaondoka.” Hapo hapo Mina akafunga tena macho. Akatamani kama ainame na kumbusu, akaona aondoke tu kabla hajafanya jambo lakuja kumfanya ajute baadaye.

Akamtengenezea shuka tena. “Asante.” Mina akashukuru akiwa amefunga macho. Andy alitamani kama asiondoke, lakini pia hakuwa na majibu yakutosheleza kwa Ron endapo atamkuta hapo, na kwa familia yake endapo atakosa kufika kanisani kama ilivyo ada kwao. “Nitakuona baadaye Mina.” Kama aliyekuwa akiahidi. Mina akafungua macho na kutingisha kichwa kukubali. Andy alimtizama kidogo, akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~

Alifika kanisani akiwa amewahi kidogo. Akabaki akifikiria garini. Akapotea kabisa mpaka akasikia kioo cha gari kikigongwa tena taratibu. “Lora!” Akashusha kioo. “Nimeshajua kwenye gari ndio maeneo yako yakupata muda wakutafakari mambo yako.” Wakacheka, Lora akajisogeza na kumbusu midomoni. Lakini safari hii Andy hakurudisha busu. Lora akashangaa nafsini kwake. Akashuka. “Umependeza sana Lora!” “Asante. Hata wewe.” “Asante.” “Naona muda umefika.” “Kina mama Ruhinda wapo kule mbele, naona wote wamefika, nilikuja kukuangalia wewe.” “Oooh! Niliwahi kidogo, nikaamua kutulia hapa. Vipi lakini?” Andy akauliza huku wakitembea kuelekea jengo la kanisa.

“Safi. Jana nililala vizuri.” Wakacheka, Andy akijua anachomaanisha. “Siku nyingine huwa hulali vizuri?” Andy akauliza na kumtizama na tabasamu. “Jana zaidi.” Wakacheka, ukimya ukazuka. Andy akapotelea mawazoni huku wakitembea.

Waliwakuta wazazi wao hapo nje wakiongea na kucheka pamoja na ndugu zao. Andy akasalimia wote. “Leo umechelewa wapi?” Akauliza mama yake. “Imekuwa kinyume. Niliwahi zaidi nikaamua kubaki kwenye gari.” Maongezi yakaendelea kidogo, wakaingia kanisani. Wakajikuta wamekaa pamoja. Lora na Andy. Andy akatoa tabasamu.

“Leo naona ndio siku ya kutimiza ahadi yangu kwa mama Ruhinda.” Lora akanong’ona. “Oooh! Leo ratiba imeruhusu?” Andy akauliza na tabasamu, Lora akacheka na kutingisha kichwa kukubali. “Karibu sana.” “Asante.” Walikuwa wakinong’ona. Misa ilipoanza tu, wakanyamaza.

Kwa Mina.

Wakati amelala, akamsikia mama yake anaongea na Ron. Akafungua macho. “Vipi?” Ron akamuuliza. “Kichwa bado kinauma sana.” “Usilie sasa. Wamekupa dawa?” "Hata sijui!” “Pole mama yangu mzazi. Utapona.” Mina akafunga macho. “Hakipoi mama! Kinauma sana.” Mina akalalamika huku akilia. “Naenda kumuuliza yule nesi pale kama wamempa dawa ya kupunguza maumivu. Kichwa gani hakitulii jamani!” Mama yao akaondoka pale.

“Halafu rafiki yako alikuja.” Mina akamwambia Ron huku akifuta machozi. “Hatibu?” Akauliza Ron kwa uhakika. “Hapana bwana na wewe! Yule aliyekuja nyumbani akakukuta unakoroma.” Ron akacheka. “Yule sio rafiki yangu wewe, bosi wetu! Alikuja muda gani?” “Asubuhi hii.” Mina akajibu. “Labda Hatibu atakuwa alimwambia jana alipoona sijakwenda nyumbani kwake na Hatibu. Alitukaribisha kwake jana jioni tukaangalie mpira.” Mina akanyamaza kama anayefikiria.

Mara wakamsikia mama yao akijibiwa vibaya sana mpaka wagonjwa wengine wakamgeukia. Yule nesi alikuwa ana mjibu lakini kama anayemgombesha! Na alionekana mdogo hata kwa mama yao.

Ron aliumia sana. “Samahani mama. Nimeuliza tu. Sikuwa na nia mbaya.” Wakamsikia mama yao akiongea kwa unyenyekevu. “Hapana bwana! Maana nyinyi mmeshazoea kusema manesi wa hapa hatufanyi kazi yetu vizuri, tunaiba dawa za wagonjwa wenu, tunawauzia wengine. Kwa hiyo kila tunalowafanyia mnaona halifai!” Mama Ron akaona aondoke tu arudi alipokuwa amewaacha wanae.

Kwa Andy.

Misa iliendelea, akili na mawazo ya Andy vilikuwa hospitalini, kwa Mina. Akasugua mikono taratibu huku akikumbuka kuminya mikono ya Mina, nakuona tabasamu usoni mwake. Akavuta pumzi kwa nguvu, akatamani kama angeendelea kubaki naye pale akimfariji wakati mgonjwa. “Huu ndio wakati ambao pengine angenihitaji zaidi!” Akajutia Andy kutokuwepo pale na Mina. “Lakini hata hivyo walisema huwezi kukaa pale muda mrefu.” Akajifariji huku misa ikiendelea.

Kijana huyo aliyetumikia altareni hakuhitaji kuwepo pale kimawazo ili kujua ni wakati gani wakupiga magoti, wakusimama na kukaa. Alifuatisha kila kitu bila kukosea, japo mawazo hayakuwepo pale kabisa.

Akashitukia mkono wa Lora katikati ya mikono yake. Akashituka kidogo na kumtizama. Akapokelewa na tabasamu zito kutoka kwa Lora. Naye akarudisha. “God! Natamani Lora ndiye angekuwa Mina.” Akawaza Andy huku akitamani atoe ule mkono wa Lora pale katikati ya viganja vyake. Lakini isingekuwa rahisi. Lora alishapenyeza kabisa na vidole vyake katikati ya vidole vya Andy. Akafungamanisha kabisa. Hakupata kile alichokipata wakati alipomshika Mina na kushindwa kumwachia. Andy akashangaa.

 Akahisi labda hakuwa amemshika vizuri Lora. Akaminya kidogo kama alivyomfanya Mina, Lora akacheka kwa sauti ya chini kwa furaha, akajiegemeza kidogo begani, lakini haikuwa kama kwa Mina. Akaangalia ile mikono yao pale ilivyokuwa. Akaona hakuna jinsi nyingine angeushika ule mkono wa Lora, akajisikia alichojisikia kwa Mina ambaye hata hawakupishanisha vidole! Akasogeza kulia na kushoto. Haikuwa kama Mina, akatulia. Mungu akasaidia ikafika muda wakusimama. Ikabidi kuachiana mikono. Hilo likamfurahisha Andy.

Misa iliisha, wakakusanyika nje. Kila mtu akatafuta sababu ya kucheka, lakini walijua hatimaye Andy amemfurahisha mama Ruhinda, maana alikuwa na furaha yakupita kiasi. Alichangamka akajikuta anaalika nyumbani kwake familia yakina Lora, wote. Wazazi na ndugu zake. Paulina na Raza, wakakonyezana. Andy akawaona na yeye akacheka taratibu. Baada ya mazungumzo, wakakubaliana familia zote waelekee nyumbani kwa Ruhinda kwa ajili ya chakula na ilikuwa siku ya mchezo. Game day.

~~~~~~~~~~~~~

Kama ilivyo desturi yao wanawake walielekea jikoni ila wakamwambia mama yake Lora na Lora, wao wakae tu sebuleni. Wakiwa jikoni Lora naye akaingia humo ndani. Zikaanza stori huku kila mmoja akiandaa chakwake kwani waligawana. Baada ya muda na yeye mama Lora akaingia humo jikoni. Vicheko vilitawala kwenye hiyo nyumba ungejua wazi ni watu ambao wanaelewana katika kila eneo. Chakula kiliwekwa mezani, kikasindikizwa na mazungumzo mazuri na vicheko vingi tu, wasijue kile kinachoendelea ndani ya cheko la Andy. Alitamani familia hiyo ya kina Lora waage ili na yeye atoke. Lakini haikuwa hivyo. Ni kama hawakuwa na haraka kabisa! Baada ya chakula wao wakaunga kwenye game. Mashindano na vicheko vikakolea.

Muda wa mchana wa kuona wagonjwa ukafika na kupita. Bado ugeni upo. “Hata hivyo sasa hivi ni kwa wanao peleka chakula tu.” Akajifariji Andy wakati akiangalia saa yake. Lakini haikuwa hivyo. Wakaendelea kuwepo tu mpaka jioni.

 Ilipofika saa 12 na nusu jioni ndio watu wakaanza kutawanyika. Alianza kuondoka dada yao na watoto. Walisema wanawahi kurudi nyumbani kesho watoto wao wanamitihani shuleni wanataka siku hiyo wawahi kulala. Maana waliunganisha na mpira, ligi hiyo hiyo ya Uingereza. Zikaletwa bia hapo. Jumapili ikazidi kupendeza ndipo Paulina na Devi wakaona waage. Vilijaa vicheko vya kilevi huku wakishangilia mpira. Wakati wote Lora alikuwa karibu na Andy kitu kilichozidi kumfurahisha mama yake.

Saa moja kamili, ndipo Lora akaondoka na wazazi wake. Maana wadogo zake wawili walishaondoka mapema na gari yao. Walikuja pale wakiwa wanaendesha magari mawili tofauti. Walipowaacha hapo, ikabidi Lora ndiye awe dereva kwani wazazi wake walikuwa wamekunywa. Andy aliangalia muda na kuumia sana moyoni.

Akabaki akisaidia kusafisha pale, kwani alianza kuondoka dada yake, akaacha bado watu wakinywa na kula kidogo kidogo. Paul naye aliga baada ya muda mfupi tu, akasema ameitwa kazini. Akaja wifi yake na kaka yake, sababu ikawa kama ya dada yao. Kurudisha watoto nyumbani sababu ya shule kesho yake. Akajikuta amebaki na wazazi wake wakiwa wamekunywa na wao, hakuna jinsi mama yake angeweza kumsaidia msichana wa kazi. Andy akasaidia kusafisha pale ndipo akarudi kwake, ilishakuwa saa tatu na nusu usiku. Akajichukia kupita maelezo. Kutoa ahadi mara mbili mbili na kushindwa kutimiza! Hilo likamuumiza mwenyewe hata kabla hajalaumiwa na mtu.

Jumatatu.

Jumatatu siku ya kazi, foleni. Hakuna jinsi angeenda hospitalini asubuhi hiyo na kuwahi kazini kwenye kikao cha asubuhi. Akaazimia kuanza ofisini kwanza, ndipo mchana anunue chochote aende akamuone Mina hospitalini. Alifika kazini, akapata ujumbe kutoka kwa Ron akimuomba au kumtaarifu kuwa atachelewa kidogo. ‘Bila shaka.’ Akamjibu kwa haraka, akielewa kabisa kuwa nilazima anapitia kwanza hospitalini kumuona dada yake.

Ilipofika kama kwenye saa tatu hivi, Ron akawa anaingia kazini. Moja kwa moja akaelekea ofisini kwa Andy. “Samahani sana nimechelewa.” “Hamna neno. Vipi hali yake lakini?” “Imebidi nimuhamishe asubuhi hii. Bado analalamika kichwa. Tumefika asubuhi ya leo, tumemkuta analia, anaonekana hajalala, nikaona...” Mara mlango ukagongwa mara moja. Wote wakageukia mlangoni. Ron alikuwa amekaa mbele ya meza ya Andy.

Akaingia Lora natabasamu zuri. “Leo siku nzima nitakuwa hapo kwenye hiyo hoteli jirani yenu. Tuna kikao hapo.” Akamsogelea Andy na kumbusu midomoni. Alikuwa ameshikilia kimfuko, wazi kilionekana kimebeba vitafunwa. “Nimekuletea sambusa za chai.” Akaongeza Lora. “Mimi naomba niwaache Kiongozi.”  Akasimama Ron. “Hapana, mimi sikai, nimepita tu kumletea kitafunwa. Nyinyi endeleeni tu na kazi.” “Hamna neno. Sisi tupo tu, tutazungumza hata baadaye. Hapakuwa na mazungumzo ya maana.” Akaaga Ron, nakutoka.

Lora alijawa tabasamu zuri, akapendeza. Ungependa kumtizama binti huyo ambaye hakuonyesha hata na hila usoni mwake isijue kinachoendelea moyoni kwa Andy. Na kweli hakukaa muda mrefu. Akaacha zile sambusa, na kumwambia anarudi kwenye kikao, walikuwa na mapumziko mafupi, wakapewa hizo sambusa, akamwambia alipozipenda yeye, akaona amletee na yeye. Lora alifanya jambo zuri sana lakini lilimnyima raha Andy, alishindwa hata kusimama na kumsindikiza. Miguu ilimwisha nguvu, akabaki ameduaa.

Anarudije tena kuuliza kwa kaka yake Mina aliyeshuhudia akidakwa midomo asubuhi hiyo na mrembo aliyeacha kikao na kuleta sambusa, habari za Mina aliyemuahidi jana angerudi kumuona halafu asiende, huku nyuma akazidiwa mpaka kuhamishwa hospitali! Anaulizaje tena! Anaanzia wapi! Heri ingekuwa Hatibu, lakini ni Ron ndiye aliyeshuhudia! Andy akabaki ameduaa pale mezani.

Akajua maji yameshavuka magoti. Yanapanda juu. Akamuhurumia Mina, asijue chakufanya. “Heri ningefuata ushauri wa Devi.” Akajilaumu Andy kujipeleka yeye mwenyewe hospitalini na kutoa ahadi ambazo hata hakuulizwa.

Akakumbuka jinsi alivyolia Mina akimwambia kichwa kinamuuma na kushindwa kumsaidia kwa chochote, na wala hakurudi! “Heri kaka yake amemuhamisha hospitali nyingine.” Akajifariji lakini bado moyo ulimuuma, dhamira ikazidi kumsumbua kwa msichana mgeni kabisa kwake!

Akakumbuka vile Mina alivyomshukuru kwa dhati kwa kumfuta tu machozi na kumshukuru kwa kwenda! Akakumbuka jinsi alivyomshika mkono. Akavuta pumzi kwa nguvu, Andy akabaki hajui chakufanya. “Daah!” Tayari Andy akajikuta yupo kwenye wakati mgumu, tena njia panda.

Kwa Shemeji.

Andy akanyanyua simu na kumpigia simu shemeji yake. “Kwema?” Akauliza Devi. “Kwa mfano ile asilimia 7 ipo matatizoni, unafanyaje?” Moja kwa moja akatupa swali bila hata salamu. “Nilikwambia Andy, BACK OFF!” “Nilifuata ushauri wako.” Akajitetea kitoto. “Sasa umejuaje kama yupo matatizoni?” Andy akanyamaza. “Unajiingiza pabaya Andy! Toka mapema kabla hujaingia nakushindwa kujitoa kabisa.” “Nitajuaje sasa kama nimeshaingia kabisa?” “Kwani unashindwa kujitoa?” Akauliza. Kimya. Hakupata jibu.

“Andy?” “Nafikiri naweza.” Akaongea kama asiye na uhakika, Devi akajua. “Andy!” “Naweza.” Akamuhakikishia. “Hapana Andy. Tunazungumza hivi ni kwa kuwa umeshajua huwezi kujitoa tena. Lakini mimi nakuhakikishia UNAWEZA Andy. Hesabu hasara na faida. Andika hata chini hapohapo ulipokaa. Ona wapi kunalemea. Kisha chukua hatua tafadhali.” Devi akashauri. Kimya.

“Nikwambie ukweli mwingine, Andy?” Akauliza kwa tahadhari. “Nakusikiliza.” “Nahisi ukiendelea kutafuta asilimia nyingine zaidi, unavingi vyakupoteza kuliko faida. Niliwaona jana na Lora. Nyinyi watu kwa kuwaangalia tu, mnaonekana mlikusudiwa kuwa pamoja. Mama hajakosea. Hata Paulina alisema wakati tunarudi nyumbani. Nashauri rudisha macho yako sehemu sahihi. Utapunguza migongano na misuguano isiyo na sababu.” Kimya.

“Unanisikia Andy?” “Nipo.” Shemeji yake akacheka kwa kusikitika. “Najua upo, lakini nataka kujua kama unanisikia!” “Nimesikia.” “Kweli Andy? Maana kile nilichokiona jana kati yenu, si chakukiachia.” “Wakati mwingine muonekana wa nje huwa unaficha uhalisia wa ndani.” Ule usemi ukamfanya shemeji yake atulie kabisa. Akajua lipo zito linaloendelea kwa Andy.

“Labda niulize tena. Ni kwa asilimia ngapi, umempenda Asilimia 7?” “Kwa asilimia 120.” Akajibu Andy kwa haraka bila hata kuchelewa. Shemeji yake akabaki kimya kwa muda akajua mambo yamebadilika.

“Kwa asilimia ngapi unajisikia kumpenda Lora?” “Naam!” Andy akauliza kwa mshituko kidogo akajidai kama hajasikia swali. “Andy!?” Devi akamuita kwa kumshangaa. “Umesema nini? Naomba urudie swali.” “No. Never mind.” Devi akajua anapoteza muda tu. Hakutaka kurudia tena swali.

Kuanzia mwanzo mpaka mwisho Andy alikuwa akisikia neno hadi neno. Ghafla hajasikia swali la msingi hivyo! Akaona amwache tu. “Basi tutaongea baadaye.” Andy akaaga kwa haraka kama ambaye aliyeshukuru kutoulizwa tena hilo swali. Bila kusubiri jibu, akakata simu.

~~~~~~~~~~~~~

Kwa Asilimia 7, zimeshazidi asilimia 120, wakati Lora, kipenzi cha familia, ameshindwa kujibu na kusema wakati mwingine muonekano hudanganya! Kipi kitaendelea kwenye hizo asilimia 120 wakati hata hospitalini alishindwa kutokea!

Inaendelea….


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment