Ndipo akagutuka. “Nimemkuta Ron?”
Ikabidi aulize tu kwani Mina alifunga mikono kifuani na kubaki
akimtizama na yeye. Alipomuulizia Ron, akamuona anacheka kisha akamwambia.
“Shiiiiii!” Akamshika mkono na kumvutia ndani huku yeye akinyata.
Andy asielewe. Mina akaendelea kucheka kwa kujitahidi kupunguza sauti, halafu
akawa kama aliyehamasika ghafla, huku amemshika Andy mkono akimuongoza njia
mpaka karibu na sebuleni.
Kisha akamvuta ili ainame, akaelewa anataka ampe
sikio. Andy akainama na kumpa sikio. “Usiongee chochote.” Akamnong’oneza
sikioni akicheka taratibu. Kisha akamvuta tena kwa kumsogeza mpaka karibu na
kochi. Akamuona Ron amelala huku anakoroma.
Mina akazidi kucheka huku ameshika mdomo wake.
Akanyata mpaka sehemu ya kulia chakula akachukua jagi la maji, Andy akawa
ameshaelewa ila akabaki akimtizama huku akitabasamu na kutaka kujua anachotaka
kufanya.
Akarudi pale sebuleni alipokuwa amelala Ron kwa
kunyata huku akimsihi Andy asiongee chochote kwa kuweka kidole chake kimoja juu
ya midomo yake, akammwagia maji kichwani, Ron aliruka mpaka akaanguka sakafuni kutoka kochini. Andy
akashangaa sana, hakutegemea!
“Hakika nitakuua Mina!” Ron aliongea akiwa chini
sakafuni, ameloa. Ile kuamka tu, Mina akaanza kukimbia huku akipiga kelele.
“Mama niokoe! Ron anataka kuniua mimi!” Andy akiwa ameduaa, akashangaa Ron
ananyanyuka kwa kasi na kuanza kumkimbiza Mina. Alikimbia mpaka nje alipokuwa
mama yake akaenda kusimama nyuma yake. “Leo lazima ulie Mina.” Ron aliongea
huku akimfuata nyuma kwa hasira. “Utaniangusha bwana Mina, ni nini?” Andy
akasikia sauti ya kimama ikiuliza.
“Leo mwanao lazima alie huyo. Ona alivyonilowesha nikiwa usingizini.” “Mimi nilikuwa
namuamsha. Alikuwa anakoroma
pale sebuleni, wakati mgeni wake amekuja, yeye hana habari! Ulitakiwa unishukuru sio kutaka kunipiga!” “Ona mama! Ona wewe
mwenyewe. Mtoe hapo nyuma.” Akamsikia yule mama akicheka.
“Usicheke mama bwana! Atakuja kuniua usingizini kwa mshituko!”
“Kwanza ulikuwa unanuka jasho. Hapo nimekusaidia kuoga. Unakwenda kujikausha tu
na kujipaka mafuta.” Mina aliongea nyuma ya mama yake. Ron akataka kumvuta,
Mina akapiga kelele kwa sauti. “Mwache bwana wee!” “Wewe unamuendekeza mama.
Huyo nikimbamiza mara mbili tatu, akili yake itakaa sawa.”
Ron akataka tena kumshika. “Bwana weeee! Nenda kwa
mgeni wako.” “Muongo huyo mama. Hakuna mgeni yeyote!” “Yupo, tena amekuona
unavyokoroma.” Ron akarudi ndani huku akilalamika, Mina na mama yake wakicheka.
“Wewe cheka tu, nikikukamata ndio utanijua.” “Utamkamata nani wewe! Unasaidiwa,
badala ushukuru, unaleta ubabe!
Na siku nyingine akija msichana wako namfungulia mlango akuone jinsi unavyokoromaga, uone kama hujaachwa.” Mama yake akaanza kucheka
tena. “Akija kukukamata huyo!” “Kwani mimi sina miguu! Hawezi.”
Ron alirudi ndani, kweli akamkuta mgeni wake amesimama pembeni ya sebule, akaanza
kucheka. “Karibu Mkuu hapo kwenye kochi kavu, nisubiri nikabadilishe. Huyu
mtoto mjinga tu.” Ron akapitiliza ndani chumbani kwake.
Baada ya muda akatoka akiwa amebadilisha. “Ngoja
nikutambulishe kwa mama kabla hatujatoka kwenda kwa kina Hatibu.” “Litakuwa
jambo zuri.” Mara mama yake akaingia. “Mama, huyu anaitwa Andy, tupo naye
kazini. Amehamishiwa kwenye tawi letu.” “Kwa hiyo mpo pamoja na Hatibu?” “Kwa
kitengo chetu, ndiyo, au kwa
kile tunachofanya, ila yeye ndio bosi
wetu wa kitengo chetu.” “Acha hizo bwana Ron! Si umwambie tu mama kuwa
tunafanya kazi pamoja!” Wakacheka, Andy akasimama na kumsalimia mama yake Ron
kwa heshima tu. Wakazungumza kidogo, wakatoka.
~~~~~~~~~~~~~
Walitoka pale bila yakumuaga Mina kwa kuwa hakuwepo, wakaelekea nyumbani kwa kina
Hatibu kumchukua ili waende mpirani uwanja wa Taifa. Wote walijikuta wapo ofisi
moja na wote watatu wakawa wapenzi wa timu inayofanana, halafu wafanyakazi
wengine waliopo nao kitengo kimoja, wapinzani
wao. Siku hiyo ya jumamosi timu yao walikuwa wakicheza mpira wa miguu na timu
ya kutoka nchini Nigeria. Walikubaliana wakutane,
kisha waongozane uwanja wa mpira.
~~~~~~~~~~~~~
Hatibu na Ron walianza kazi hapo kwenye hiyo kampuni
wakati mmoja, wakajikuta mambo mengi wanaendana ndipo ukaribu ukaongezeka,
wakaishia kuwa marafiki. Aliyekuwa kiongozi wao wa hicho kitengo alipata kazi
kwenye kampuni nyingine kwa mshahara mkubwa zaidi, akaacha hapo kazi na kuacha
nafasi hiyo wazi. Walifanya kazi kwa majuma kadhaa bila kiongozi, ndipo
wakaletewa Andy kama kiongozi wao wa hicho kitengo.
Watatu hao hawakupishana sana kiumri, lakini kwa muonekano tu, Andy alionekana analipwa
vizuri zaidi yao. Au ana hali ya maisha nzuri zaidi yao. Alikuwa na gari nzuri
sana. Na alikuwa akionekana nadhifu wakati wote. Hawakumsikia akilia shida kama
wao kukopana pesa mara kwa mara pale
ofisini.
~~~~~~~~~~~~~
Wakiwa ndani ya gari ya Andy mazungumzo ya hapa na pale yakaendelea mpaka walipofika uwanja wa Taifa,
Andy akiwa ametulia sana. Mpira ukaendelea, wakishangilia na kukatishwa tamaa
wakati timu yao ilipoanza kufungwa, Andy alikuwepo kama hayupo. Hatibu na Ron
wakawa busy kushangilia wala wasijue kinachoendelea kwa Andy, kwanza hakuna
aliyemjali mwenzake pale uwanjani. Kelele mpaka mpira ukaisha. Wote wakakutana
hawanywi pombe. Wakaamua kurudi tu nyumbani. Walimshusha Hatibu kwanza na ndipo
safari ya kurudi Tegeta Mwisho
kwa kina Ron ikaanza.
Foleni za barabarani na kuanzia muda waliotoka
uwanjani na fujo, giza liliwakuta njiani.
Andy akatafuta jinsi ya kuuliza tokea walipokuwa peke yao,
walipomshusha Hatibu, akashindwa, ndipo wazo likamjia. “Sikumkuta mzee
nyumbani!” Akaanza Andy. “Tunaishi na mama tu. Mzee alikuja kuoa mwanamke
mwingine.” “Kwa hiyo mlizaliwa wawili
tu?” Akatumia akili kwa haraka ili kumsogeza Mina kwenye mazungumzo.
“Kwa mama, ndiyo. Ni mimi na Mina tu. Lakini huko mzee alipo anayo familia
nyingine.” “Pole sana.” “Naona tumeshazoea hayo maisha. Hamna hata anaye
lalamika tena.” Akatafuta tena kuuliza,
lakini ikabidi azunguke.
“Kwa hiyo ni mama ndiye aliyekuwa akiwasomesha?” “Kwa
sehemu kubwa ni mama. Hata wakati mzee alipokuwepo, mama alikuwa akihangaika
mwenyewe. Ndio maana hata nafikiri hatukuona tofauti kubwa sana mzee
alipoondoka. Hata pale ni mama ndiye aliyejenga kwa mshahara wake huohuo wa
ualimu. Alikuwa akijenga huku tunasoma.” “Na Mina naye alisomea Dodoma?”
Akamsikia Ron akiguna.
“Vipi?” “Aaah! Mina na shule! Hataki kabisa kusoma.
Ameishia kidato cha nne, basi.” “Labda kuna kitu anapenda kufanya badala
ya shule.” “Kupika. Hicho ndio kitu anapenda kufanya kuanzia
asubuhi mpaka jioni na uchokozi.
Basi.” Wakacheka.
“Amegoma kukua, na wala hana analowaza la msingi. Vile
unavyomuona ndio kamaliza. Hajui kukasirika na hata ukimkasirikia...” Ron
akafikiria. “Kwanza huwezi kumkasirikia Mina kwa muda mrefu. Sijui ameumbwaje
yule mtoto!” Wakacheka.
Andy akatamani
kuendelea kusikia habari za Mina, lakini akajikuta ameishiwa maswali ya mitego ili kumfahamu zaidi Mina.
Walifika nyumbani kwa kina Ron, ni kweli ilikuwa Tegeta Mwisho haswa.
Walipokuwa wakiishi ilikuwa mbali na barabarani. Na barabara ya kufika kwao
ilikuwa ya udongo tena mbaya. Kama walionunua hicho kiwanja kwa bei ya chini
haswa. Lakini nyumba ilionekana ilijengwa na kukamilika kwa bati safi tu.
Safari hii Andy hakuwa na sababu ya kushuka garini.
Ron aliteremka kwenye gari na kumshukuru kwa lifti na kuwa pamoja siku hiyo ya
jumamosi. Hata hakumkaribisha ndani, akafunga mlango kwa ahadi ya kuonana siku
ya jumatatu kazini.
Huku Kwa Andy
Andy alirudi nyumbani kwake, akajiweka kochini,
akajikuta anacheka. Akamkumbuka Mina
na utundu wake, akacheka tena.
Akachukua rimoti ya tv na kuwasha ili aangalie kinachoendelea ulimwenguni.
Akajirudisha nyuma ya kochi.
Lakini akahisi sauti ya Mina masikioni kwake kama
anayemnong’oneza kitu kama vile alivyofanya nyumbani kwao. Andy akajishika
sikio. “Nachanganyikiwa nini!”
Akajicheka na kuamua kubadili alichokuwa amekiweka kwenye luninga akiwa hata
hajui ni nini kilikuwepo, akabadilisha kulia na kushoto, akakumbuka anatakiwa
kanisani siku inayofuata asubuhi. Akaona akajipumzishe mapema, asiendelee
kupoteza muda pale kochini.
Kwa Kina Ruhinda!
Siku za jumapili familia hiyo ya kina Andy huwa
wanakutana nyumbani kwa wazazi wao Msasani, kwa chakula cha mchana wakiwa na
familia zao. Dada yake Andy, Paulina, yaani mtoto wa pili kuzaliwa kwao, alikuwa
ameolewa na wana watoto wawili. Wakike.
Kaka yake mkubwa, Pius, naye alikuwa ameoa na watoto wawili, wakike. Mdogo wake wa kiume anayemfuata
Andy, yaani waane kuzaliwa, ambaye ndio kitinda mimba, alikuwa daktari katika
hospitali ya taifa Muhimbili. Yeye hakuwa ameoa.
Ilikuwa familia ya kisomi. Walio staarabika sana. Kila mtoto kwenye hiyo familia alisoma vizuri kama wazazi wao. Mzee Ruhinda
alikuwa Mkurugenzi kwenye taasisi ya fedha. Mama Ruhinda alishastaafu, lakini
alifanya kazi akiwa kiongozi wa ngazi ya juu tu katika bodi ya mambo ya
ukaguzi/Auditing kisha akajiingiza kwenye NGO ambayo bado alikuwa kwenye
ngazi ya juu tu akitumika huko.
Walikuwa na ndoa iliyoheshimika kwenye jamii. Wakalea
watoto wao vizuri bila shida. Ni Andy na mdogo wake anayemfuata, Paul ndio
hawakuwa wao wameanzisha familia.
Walikuwa ni wakristo wale wakwenda kanisani kila siku
ya jumapili ya bila kukosa.
Wakatoliki damu. Andy alihudumia
kanisani, altareni tokea mdogo
kabisa akiwa na mapadri akitumika katika kila misa, mpaka wakahisi atakuja kuwa
padri. Alisoma vizuri katika shule za mapadri nchini Kenya, Nairobi, kuanzia
darasa la tano mpaka sekondari. Ila chuo kikuu kwa shahada zote mbili
alimalizia Kampala nchini Uganda, ndipo akarudi nchini Tanzania na kupata ajira
bila shida. Akiwa ni mtoto ambaye hajakulia nyumbani kabisa.
Kwa kuwa walikuwa wakimlipa vizuri na hakuwa na
majukumu yeyote yale, alianza kuishi kwenye apartment za mtaa wa Zanaki.
Katikati ya jiji, zikiwa zimekamilika kila kitu ndani, pakamfaa haswa.
Kwani hakutaka hata kununua kitanda kwani bado alikuwa akijishauri kama anabaki
nchini Tanzania, au arudi alikokulia, nchini Kenya ambako ndio kama
nyumbani.
Maisha yakaendelea hapo akitumia vitu vya mle ndani
ila akanunua gari nzuri sana ya garama ili imsaidie usafiri wakumzungusha jijini.
Maisha nchini Tanzania yakaanza bila uhakika
sana wakuwepo hapo nchini kwa muda
mrefu, akisoma upepo, kama ambaye bado hakuwa na sababu ya kumbakiza sana
nchini japo alikuwa na hiyo kazi
nzuri ambayo alijua angeweza kuipata
hata huko nchini Kenya, na familia yake ambayo bado alijiona kama mtu wa nje
tu. Maana ndugu zake wote walisomea nchini wakiishi nyumbani kwao. Akawa kama
aliye mguu mmoja ndani mwingine nje.
Maisha yakawa ni kazini
na siku za jumapili kanisani kisha
kuwepo nyumbani kwao Msasani
akijaribu kujiunga na hiyo familia aliyokuwa akiiona wakati wa likizo tu. Sasa
akawa amerudi akijaribu kuwa mmoja wao.
Shemeji yake, mume wa Paulina, alimwambia kuna viwanja
vinauzwa Kigamboni, kujenga sio swala baya. Akaona hana chakupoteza. Pesa ipo.
Ndipo akamsadia mchakato mzima wa kukimiliki hicho kiwanja, akaanza kujenga
taratibu bila haraka wala shida kwani mshahara aliokuwa akilipwa, aliweza kulipia
apartment hiyo nzuri na ya kisasa alipokuwa akiishi, kuendesha gari ya
kifahari na kujenga bila kuhisi kupungukiwa. Pesa yake ni yake. Hana
wakushiriki naye kipato chake. Kila anayemzunguka ana maisha mazuri na
wanaingiza pesa nzuri tu.
Maisha yake yakaendelea yakiwa hayana makuu. Hanywi
pombe, haongi mwanamke, hana familia inayomtegemea isipokuwa akijisikia kwa
vitu vidogo vidogo kama zawadi kwa wazazi, watoto wa kaka yake na dada yake na
hao ndugu, basi.
~~~~~~~~~~~~~
Wote walikuwa wakienda kusali kanisa moja. Familia nzima.
Mpaka familia ya kaka yake na dada yake, walikuwa wakikutana kwenye misa ya
kwanza kabisa ya kingereza ndipo wanarudi nyumbani kwa wazazi wao, wote, kama hakuna mwenye udhuru.
Watapika na kula pamoja ndipo anayetaka kubaki au kuondoka, ruksa. Lakini
ilifanyika kama desturi yao kuwa
kila mlo wa mchana siku ya jumapili ni lazima
wawe pamoja.
Jumapili Baada Ya Kumuona
Mina.
Kutoka anapoishi Andy mpaka kanisa la St. Peter
hapakuwa mbali sana haswa siku za jumapili mida hiyo ya asubuhi ambapo hakuna
foleni. Dada yao wa pekee Paulina na familia yake waliishi Kinondoni, na
familia ya kaka yao mkubwa aliyewahi kushika wadhifa ya msaidizi wa Gavana wa
pesa, aliishi Mikocheni karibu na Kawe. Walikuwa na nyumba kubwa sana na ya
kifahari. Akiwa kwenye wadhifa huo, alinunua nyumba mbili maeneo ya karibu
kabisa na bahari, akabomoa na kujenga kwa muundo mzuri sana. Ukiingia hapo
ndani ya uzio utajua Pius anayo pesa.
Kama kawaida ya familia hiyo ya kisomi, wote
walijikuta wamefika kanisani dakika 15 kabla ya misa kuanza. Wakasalimiana wote
wakiwa nje ya kanisa hilo. Zaidi watoto wao ambao walikuwa wanne, wote wakike. Wamekuzwa kwa malezi ya kigeni na kisomi.
Shule ni kila kitu kwao, na watoto wakaelewa hilo. Lugha ni
moja tu, kingereza kwa familia nzima
kwa muda mwingi wanapokuwa peke yao. Wakubwa kwa wadogo. Wakasifiana kupendeza
kwa hili na lile, huku wakubwa wakipeana kwa ufupi habari za majukumu yao na
maendeleo ya nchi huku wakisubiria muda wakuingia kanisani ufike.
Baada ya Misa kuisha, marafiki wa karibu sana wa
familia hiyo ambayo waliendana kidini, maadili, uchumi pia, Machaki, ikawasogelea wakiwa na binti
yao ambaye hakupishana sana na Paul kijana wa mwisho wa familia hiyo ya
Ruhinda. Aliitwa Lora. Binti mzuri, nadhifu, msomi aliyekuzwa kwenye maadili
kabisa yanayofanana na kina Paulina, kasoro yeye alisomea shahada yake ya pili
nchini Uingereza. Vicheko vikaendelea mwishoe wakaagana.
Kaka yao mkubwa kina Andy, yaani Pius alishamshawishi
Andy kumchangamkia Lora. Na hilo likawa jambo lililopo kwa wazazi pia. Zaidi
mama Ruhinda, alimpenda sana Lora. Lakini kwa Andy aliweka uzito fulani hivi,
ndugu wakawa hamuelewi, isipokuwa
Paul mdogo wake. Yeye aliweza kuhisi ni kwa nini Andy anakuwa mzito kwa Lora.
Kama kawaida, walipofika nyumbani wanawake wote
waliingia jikoni wakisaidiana na msichana wa kazi kuandaa chakula cha mchana.
Misa ilikuwa ikiisha mapema tu. Kwa hiyo walikuwa na muda wa kutosha wakuongea
wakati wakisubiria chakula. Jikoni alikuwepo mama yao, Mama Ruhinda, wifi yao,
mke wa Pius, Raza, naye ni mama Ruhinda mdogo, Paulina na msichana wa kazi.
Sebuleni alikuwa Mzee Ruhinda, vijana wake hao watatu
na mkwewe, mume wa Paulina. Watoto walikuwa sebule ndogo, maalumu kwa ajili ya
wajukuu hao. Ilikuwa na kabati ndogo ya vitabu pembeni. Tv kubwa tu, na games
pembeni. Meza nzuri tu ambazo huchezea na kuandika kama wangetaka. Kwa hiyo
kila mtu alijua wapi pakukaa na nini chakufanya wanapofika kwenye nyumba hiyo.
Wapo wajukuu waliopenda kucheza games kila
wakifika hapo. Wapo waliokimbilia kusoma vitabu vya hadithi ambavyo mama
Ruhinda alijitahidi kuwabadilishia wajukuu zake mara kwa mara ili wakifika
hapo, wanaopenda kusoma, wasichoke kusoma vitabu. Yupo aliyependa kuchora. Basi
siku hiyo inakuwa siku ya furaha na mapumziko kwa wote. Na wajukuu hao
walipenda siku hiyo ya kukutana hapo nyumbani kwa bibi na babu yao.
~~~~~~~~~~~~~
“Wewe vipi? Mbona kila saa unashika sikio?” Shemeji
yake akamuuliza Andy. “Na mimi nimemuona tokea kanisani! Au lina infection
nini?” Pius akaongeza, Andy akajishitukia. “Nipo sawa tu.” Akajibu na
kujitahidi kutoshika. Wakamuona ametulia sana siku hiyo na tabasamu usoni
wakati wote.
“Umemuona Lora leo? Amependeza kweli!” “Umeanza mama.
Nimeshakwambia sina shida ya kuona.” Mama yake akakaa huku akicheka.
“Mbona swali dogo tu, lakini maelezo mengiii! Mama
ameuliza kama umemuona Lora, basi?” “Na mimi nilikuwepo kanisani mkubwa! Wote tumemuona.”
Andy akamjibu kaka yake, wote wakacheka. “Ndio uchangamke Andy! Vijana wa mjini
watamuwahi!” Pius akaweka msisitizo.
“Kwanza ni binti anayeheshimika sana kwenye kampuni
yao! Sifa zake zipo hata kwenye bodi ya wakurugenzi.” Akaongeza Mzee Ruhinda.
“Hata kwenye jamii. Ni binti mzuri kwa kweli. Ametulia. Msomi. Halafu hatakuwa
mzigo kwako. Inamaana mnasaidiana kwenye maisha. Halafu..” “Bila kukosea hizo
sifa zitakuwa ni za Lora tu!” Akaingia
Paulina hapo sebuleni na glasi ya juisi.
“Ulijuaje!?”
Wote wakacheka. “Namjua mama kwa Lora. Huwa sifa zake haziishi.
Akianza hapo, mpaka tunaondoka humu ndani. Mimi naona tuyamalize. Huyo Andy
kama ni muoaji, basi ataoa. Kama si muoaji, utamnadi huyo Lora mpaka utachoka.”
Dada mtu akaongeza. “Na mimi naona tubadili tu mazungumzo.” “Ulitaka
tuzungumzie nini na wewe! Utaishia kuoa watu wa ajabu ajabu!” “Hakuna mtu wa
ajabu mama. Kila kitu ni taratibu.” “Mpaka lini?” Mama yake akamuuliza Andy.
“Njaa inauma mama yangu!” Andy akabadili mazungumzo, wote wakacheka. Mama yao
akaguna.
“Maana Lora...” Akataka kuanza tena mama yao, wote
wakaanza kucheka. “Mama Ruhinda! Jambo haliishi?” Paulina akauliza huku
akicheka. “Wewe mwenyewe unampenda Lora!” Mama Ruhinda akamwambia Paulina.
“Nampenda haswa. Natamani hata aolewe leo na huyo Andy. Maana ni binti mzuri,
ametulia. Amesoma..” Andy akasimama. “Ngoja mimi nikacheze game na watoto. Naona
hapa kwenye vikao vya harusi, sitapaweza.” Andy akaondoka hapo wote wakicheka.
Walikula huku wakitaniana kwa hili na lile. Mwishoe
akaaga kaka mkubwa na familia yake, wakaondoka. Andy yeye hakuwa na haraka
yakuondoka hapo kwao. Mara nyingi alikuwa anakuwa wa mwisho kutoka hapo.
Akajikuta amebaki yeye na shemeji yake, Devi, kwenye baraza la nyuma ambapo na
kwenyewe kulikuwa na sehemu nzuri tu ya kukaa. Mama Ruhinda aliweka viti vizuri
ndani ya baraza hilo kubwa na kulizungushwa maua mazuri sana aliyokuwa akiweka
mbolea ya maganda ya kila kitu anachotumia jikoni kwake. Basi maua hayo ya
kwenye vyungu ambayo yalikuwa ndani na nje ya baraza hilo yalikuwa yakistawi
sana. Huwezi kukosa maua nyumba hiyo.
Asilimia 7.
“Wewe leo una nini? Tabasamu halikuishi!” Akacheka Andy kisha akamwangalia shemeji yake
kama anayetaka kumuuliza jambo kisha akasita. “Ni nini?” Akacheka tena mwishoe
akaamua amuulize tu. “Eti wewe unaamini kwenye ‘Love at first sight’? Yaani
unamuona tu mtu kwa mara ya kwanza. Humjui hata jina lake, unajikuta unampenda kiasi chakumfikiria wakati wote! Unaamini hiyo inawezekana?” Shemeji yake
akacheka kidogo huku akifikiria.
“Humfahamu kabisa?” Devi akamtega kutaka kujua kama ni
yeye mwenyewe Andy ndio amependa au la! Andy akamgundua. “Acha hizo bwana! Wewe
nijibu kama kuna kitu kama hicho?” “Sawa. Basi niulize hivi, inamaana huyo ‘aliyependwa’ hafahamiki
kabisa?” Andy akacheka taratibu kama anavuta hisia, Devi alimuona maana aliweza
kuzisoma hisia nzito usoni kwa Andy
mpaka akashangaa.
“Come on Andy! You are in Love Man!” “Shhhhh!
Usitake mama Ruhinda atoke. Wewe nijibu. Kitu kama hicho kinawezekana?” “Hafahamiki kabisaaa!” “Labda niseme kwa asilimia 7 tu. Vile vitu vya msingi.”
“Navyo vipoje? Vinaendana?” Andy akanyamaza kama anayefikiria.
“Kwa sababu Andy, zipo hisia na uhalisia wa
maisha. Je katika hizo asilimia 7,
ngapi zinaendana?” Andy kimya. Hata
katika zile 7, alizomfahamu Mina, hawakuendana
hata kidogo. Akasita. “Lakini sijawahi kujisikia hivyo kwa mwanamke mwingine
yeyote, Devi! Nakwambia ukweli ile ni ya kipekee.”
Akajitetea Andy akisikika ameshindwa kujibu swali.
“Asilimia ngapi, Andy?” Shemeji yake akasisitiza swali
lake. “Sijui.” “Come on Andy. You are smarter than that.” Akaongea
akimjua fika shemeji yake, si mjinga. “Sidhani kama inajalisha.” “Niamini mimi kuwa huwa inakuja kujalisha baadaye. Sana tu. Sasa kabla hujavuka zaidi ya hizo asilimia 7 unazomfahamu, nashauri weka kikomo. Back off.” Shemeji yake
akaweka msisitizo. Kimya.
“Unanielewa Andy? Mahusiano ambayo unafikiri
yatakupelekea ndoa, ni zaidi ya
hisia. Ndoa ina uhalisia wake ambao haupelekwi na hisia peke yake. Ndoa sio
kufanya mapenzi tu. Baada ya hapo kuna kula,
kulea watoto. Ikiwepo wavae vizuri,
wasome shule nzuri na waishi kwenye mazingira mazuri, ambayo inahitajika pesa nzuri. Sio hisia peke yake. Hisia hailipi ada ya shule wala
hainunui chakula. Sijui kama unanielewa?” “Nahisi nimeelewa. Na asante kwa
ushauri. Nafikiri upo sahihi.” Andy akaafikiana na shemeji yake.
~~~~~~~~~~~~~
Alitoka pale angalau ule muhemko juu ya Mina ukachukua sura nyingine. Maneno ya shemeji yake
yakaanza kumwingia. Mina hajasoma. Ameishia kidato cha 4 tu. Na kaka yake
ameshamwambia Mina hataki kusoma. “Haonekaniki
kama ni mtu mwenye uchu wa maendeleo. Angetafuta hata biashara akafanya!”
Akawaza Andy akijitia moyo katika ushauri wa shemejie.
Hata hivyo katika familia ile ya kila mtu anayeimba
usomi na maendeleo, Mina anaingiaje pale! Andy akaona ajitulize. Hata hivyo
hadhi ya maisha yao ni ya chini mno,
atamtambulisha vipi kwa wazazi! Akaona kweli asiongeze asilimia nyingine.
Zibakie zilezile 7 alizomfahamu na aachane naye. Akajituliza.
Jumatatu!
Andy alifika kazini akaanza kazi kama kawaida.
Waliingia kwenye kikao cha asubuhi ambapo kiongozi wao wote alikuwepo. Akatoa
muongozo wa juma zima, Andy na watu waliokuwa chini yake wao wakarudi idarani
kwao. Akagawa majukumu, kila mtu akaanza kazi. Alimtizama Ron kama amuulize
kitu, lakini akasita na kujionya. Akakumbuka ushauri wa shemeji
yake.
Akaondoka kabisa pale karibu na Ron na kuelekea kweye
ofisi yake iliyokuwepo pembeni ya chumba hicho kikubwa tu ambacho wapo kina
Ron, Hatibu na wafanyakazi wengine wanne ambao walipanga meza zao kuzunguka
hicho chumba.
Lora Avunja Ukimya.
Ujumbe ukaingia. ‘Karibu kwa
chakula cha mchana.’ Andy akasoma na kubaki akijishauri. ‘Ni lunch tu, acha woga Andy!’ Ujumbe mwingine
ukaingia baada ya dakika 10. Andy akacheka. ‘Nilikuwa
na kazi kidogo ndio mana nimechelewa kujibu. Samahani. Wapi na saa ngapi?’
Andy akarudisha ujumbe na kubaki akijishauri baada ya Lora kujibu. Hakika
alisikia uzito, lakini akaona ni kweli Lora ni binti ambaye anafaa, ajaribu tu.
Ulipofika muda wa chakula cha mchana, Andy akawaaga kuwa anatoka kwa chakula
cha mchana. “Leo kiongozi unakwenda kula kwa wakuu nini?” Akatania Hatibu. Andy akacheka tu na
kuondoka.
Alikuta Lora alishafika. “Nimechelewa nini?” Akauliza
Andy wakati akikaa. “Hapana, ila mimi sikutaka uje ndio unisubirie.” Wakacheka.
“Vipi kazi lakini?” “Kama kawaida tu. Siwezi kulalamika. Vipi na wewe?” “Na
mimi hivyo hivyo, siwezi kulalamika.” Akajibu Andy.
Muhudumu akaleta menu ya chakula na vinywaji.
Wakaagiza. “Kwa hiyo umeridhika na ulipo?” Akauliza Lora na tabasamu usoni.
Andy akacheka kidogo. “Niseme kwa sasa, ndiyo.” Lora akacheka. Jinsi
alivyocheka Andy hakuelewa. Akakunja uso kidogo. “Kwa nini umecheka?” “Aah! Nimefurahi tu.” “Nini kimekufurahisha?” Andy
akataka kujua zaidi maana kwa jinsi alivyolisoma lile cheko ni zaidi ya kuonyesha furaha. Maana Lora
alicheka baada yakumjibu.
“Nimefurahi ulivyosema umeridhika. Ndio mtu wa kwanza kumsikia anasema ameridhika na
alichonacho.” Akaanza Lora. Andy kimya akitaka kusikia mwisho wake.
“Haswa kwa msomi kama wewe. Sijui kama unanielewa?
Mwingine angesema anatamani kazi ya bosi wake. Au anataka kuhama kampuni ili
kutafuta nafasi ya juu zaidi.” Lora aliongea na tabasamu lakini ikamkera kidogo Andy. “Umejaliwa roho
ya kuridhika. Ni kitu kizuri.” Akamalizia kwa kurekebisha kama kujirudi baada ya kumuona Andy
hachangii ila kumsikiliza tu.
“Vipi mama Ruhinda lakini?” Akabadilisha mazungumzo.
“Yupo.” Akajibu Andy na tabasamu. “Alinikaribisha siku ya jumapili, lakini bado
hapajakuwa na utulivu. Nimemuahidi nitakuja.” “Karibu sana.” Akamalizia Andy.
Chakula kikaletwa. “Unaonekana ni mpenzi wa samaki!” Akachangia Lora na tabasamu kama kurekebisha
ile hali ya uzito pale. “Sana! Kukiwa na uchaguzi, lazima samaki atashinda tu.” Akajibu Andy huku
akitengeneza kitambaa kilichowekwa hapo mezani maalumu cha kujifutia au
kujifunika usijichafue wakati wakula. Akakitoa pale kilipokuwa kimepambwa
pembeni na kukitandika mapajani. Wakaanza kula kimya kimya. Visu na uma tu ndio
vilisikika.
“Vipi lakini na wewe kazini? Umeridhika? Maana nimesahau kukuuliza na wewe.” Ikabidi Andy awe
muungwana. Lora akacheka. Ni kweli alikuwa binti anayeoonekana anajielewa au anaelewa ni nini anazungumza. “Kwa kweli siwezi kulalamika.
Nimeanza kwenye nafasi nzuri, na mshahara mzuri. Nikijilinganisha na wengi
ambao nilisoma nao darasa moja na
nikawaacha hapa nchini wakiwa wameshaanza kazi hapa nchini kwenye makampuni
mengine, kulalamika ni kukufuru.”
Lora aliongea kiustarabu tu ila kwa kujigamba kidogo.
“Kwa maneno mengine umefikia ngazi ya juu kabisa!” Lora akacheka kidogo akitafuta
jinsi ya kuzungumza kama asiharibu, kisha akasema. “Sio kwa kiburi,
lakini ndiyo.” Wakacheka kidogo huku
Andy akimwangalia.
“Si unajua kabla ya kwenda chuo kusoma shahada ya pili
UK, nilifanya kazi inayofanana na hiyo?” Andy akabaki ametulia kidogo. “Kwa
hiyo niliondoka pia nikiwa kwenye nafasi nzuri, nilichofanya ni kuongeza ujuzi
tu. Halafu nikapata muda wa Internship,
mafunzo, huko huko nchini Uingereza kama mwaka hivi. Ikanisaidia kuongeza ujuzi
zaidi. Niliporudi hapa nchini, nikamkuta na mkurugenzi wetu naye anastaafu.
Nikaomba mimi ile nafasi, na kwa kuwa nilishafanya naye kazi. Na tukawa tukielewana, halafu nimesoma, kwa hiyo alinipopeleka jina
langu kwenye bodi ya wakurugenzi ambao ndio kina mzee Ruhinda.” Lora alicheka
kidogo.
“Basi, nikafanyiwa usahili, na Mungu akawa upande
wangu. Nikapata ile nafasi. Inanichukulia muda, lakini nafurahia sana.” “Hapo
ni kweli umefika ngazi ya mwisho
kabisa. Huna pakupanda tena.” Wakacheka kidogo na kuendelea kula.
~~~~~~~~~~~~~
Akamuona Andy anaangalia saa yake ya mkononi. “Vipi,
muda umeisha nini?” “Umejuaje?” Andy akacheka kidogo huku akiuliza na kutizama
saa yake ya mkononi tena. “Naona macho mkononi!” “Yeah! Ndio tumeanza juma,
kuna mambo yakuweka sawa kabla halijaharibika jambo. Lakini nashukuru sana kwa
chakula. Nimefurahia samaki.” Lora akacheka kiuungwana.
“Nimefurahi umekuja Andy. Naamini tutapata tena muda
kama huu.” “Naamini hivyo.” Akajibu Andy na tabasamu huku akimwita muhudumu.
“Mimi ndio nimekuita Andy. Naomba nilipe.” Andy akacheka. “Naomba kwa leo mimi
ndio nilipie, wewe utalipa wakati mwingine.” Akaomba Andy kiuugwana.
“Sikio linawasha?” “Kwa nini?” Akajishitukia Andy na kushusha mkono akiwa
anamsubiria muhudumu aliyemwita afike hapo. “Naona unalishika kila wakati!
Isijekuwa ni infection!” “Hapana. Lipo tu sawa.” Hata Andy hakujua kama anashika sikio kila wakati. Muhudumu
akaleta bili, Andy akasoma. Akafungua walet yake, akatoa pesa na kumkabidhi.
Akamshukuru muhudumu kwa huduma na kumgeukia Lora. “Asante.” “Karibu na kazi
njema.” Andy akatoa tabasamu na kusimama. “Na wewe uwe na wakati mzuri.”
“Asante.” Andy akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~
Aliingia kwenye gari yake akavuta pumzi kwa nguvu na
kubaki kama ameduaa. Kama asiyejua chakufanya tena. Alikaa pale mpaka
akashituliwa na Lora akiwa anagonga kioo cha dirisha lake la gari.
Akashusha. “Vipi, gari ina matatizo?” “Hapana. Vipi?”
Wote waliwekeana tabasamu. “Nimeuliza tu. Maana nimekukuta umekaa tu ndani ya
gari, nikajua umeshindwa kuondoka wakati uliaga ukiwa unawahi kazini!” Andy
akajua amekamatwa. Akaona haitaji kujieleza kwa Lora. “Uwe na wakati mzuri
Lora.” Akajibu hivyo Andy na tabasamu la kutotaka kuulizwa zaidi. Lora akarudi
nyuma, Andy akaondoa gari.
~~~~~~~~~~~~~
Andy aliingia ofisini kwake na kutulia mezani.
Akashangaa ni nini kibaya kilitokea kati yake na Lora! Lora hakuwa mgeni kwake.
Alimfahamu kwa muda mrefu tu, lakini siku ile ikawa ngumu kweli kati yao. Labda
kwa kuwa safari hii kulikuwa na agenda nyuma yake! Akajishangaa. Lora alikuwa
msichana sahihi kwa mazingira yake na wazazi wake. Hakuhitaji marekebisho
yeyote ili kuwa katika ulimwengu wake. Lakini!
“Ananiona
mimi sina malengo ya mbeleni!” Akawaza Andy. “Au ananiona mimi ni kama mtu ninayeridhika kirahisi tu!”
Akaendelea kutafakari mazungumzo yao yaliyoendelea kwenye chakula cha mchana. “Au pengine hapakuwa na jambo baya! Mimi
ndio nimeelewa vibaya1” Akajaribu kujituliza. “Labda tutoke tena.” Akajishauri Andy.
~~~~~~~~~~~~~
Ndio Kwanzaaa, tunaanza. Love
at First sight! Ni kweli ipo?
Andy atafuata ushauri wa Shemeji au atafuata
moyo?
Ni Mina asiyeendana na Familia,
au Lora anayeendana na familia?
Inaendelea…
0 Comments:
Post a Comment