![]() |
“Jelini, umevaa kitu ndani wewe mtoto?” “Nimevaa mama
jamani! Siendi kumtega! Mwenyewe namgeuza geuza samaki wangu mpaka
jumamosi. Nikimuanzia leo, hataondoka hapa.” Mode alicheka, hana mbavu. “Dozi
yake?” Akaendelea kumchokoza. “Ileile kama ya makurubembe ya mjini! Hapunguziwi
mtu kitu.” Na yeye akaendelea kujibu akitoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Akatoka nje ya geti, akamkuta anamsubiria nje ya gari.
Akamdaka na kumkumbatia kwa nguvu zote. “Pole Ezra, na samahani mpenzi.”
Akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu akiwa bado amemkumbatia.
“Niambie kama umenisamehe.”
Akajivuta pembeni kidogo na kapu lake dogo mkononi, akibembeleza kama
siye yeye! Ulimi laini, wa kuyeyusha hasira. “Yameisha Jelini. Yameisha
mpenzi. Niahidi kama tutabaki salama.” “Tutakuwa salama Ezra. Tena mimi na wewe
tu. Njoo ndani ya gari unywe uji, upunguze njaa.” Kama kawaida, wakakaa kwenye
uwanja wao wanapofanya mengi. Kiti cha nyuma.
Akashusha cup holder/kitu cha kuegemea au kuwekea chupa
au vikombe au glass, cha katikati
ya kiti cha nyuma, akamminia uji na kuanza kumpoozeshea kama mtoto, Ezra
akimwangalia asiamini kama huo usiku
unaishia hivyo, maana alijua ndio basi tena.
“Huu utafaa.” Akabaki amejiegemeza. “Ezra? Unasinzia?”
“Hapana. Nahisi nimechoka tu. Sijapumzika, sijala, sijanywa, nilikuwa na hofu!
Sijawahi ogopa hivi Jelini! Sijawahi. Halafu nikawa sijui jinsi ya
kutengeneza.” Jelini akamuhurumia na kuzudi kuhukumiwa.
“Pole Ezra. Na samahani sana. Nikikuahidi sitarudia
tena nilichofanya itasaidia?” “Naweza kukosea tena Jelini!” “Sasahivi najua
unanihitaji na unanipenda Ezra. Mwanzoni uliponiambia sijachelewa,
ukweli ulinitisha. Nikajua hunihitaji mimi kama Jelini. Lakini sasahivi
nina uhakika wa mapenzi yako ya dhati kwangu. Mengine najua ni mapungufu
ambayo tutajifunza kuishi nayo kwa kadiri itakavyokuwa ikitokea.”
“Nakuahidi chochote kitakachotokea kuanzia sasa nitajua ni
hasira tu lakini si kwamba hunitaki. Nitajifunza kuishi na wewe, sitaondoka tena. Tafadhali naomba
yaishe. Nakuahidi haitatokea tena.” Akajibembelezesha
kwa mengi akimtuliza. Na hivi Ezra mwenyewe alishakuwa akitaka yaishe na kujiapia ataishi naye hivyohivyo akijua anayependwa ni Colins, hakutaka mengi.
“Yameisha Jelini. Na nimefurahi bado mipango yetu itaendelea. Au unasemaje?” “Na mimi
nataka iendelee. Najua unaweza ukachoka
au ukazoea, lakini mwenzio nakupenda
na nakutaka wewe Ezra. Ninakusubiria wewe.” Akataka kumkiss.
“Utaungua na uji. Kula kwanza. Mimi mwenyewe nina hamu na
wewe.” “Naomba uweke hapo mbele angalau nikushike kidogo. Pengine nitatulia.
Nilikuwa na hali mbaya! Kidogo tu.” Uji ukahamishwa kiti cha mbele. Akarudisha
ule mkono wa katikati ya kiti cha nyuma, akajisogeza mpaka kifuani, akajiweka
kama wanavyopendaga wengi walio bahatika kumkumbatia kimwana huyo.
Zile pumzi nzuri shingoni kwa Ezra, na harufu murua,
akainama kupata kiss. Jelini akamdaka midomo, mikono laini na kucha
vikaanza kubarizi shingoni, masikioni mpaka kwenye nywele. Ezra alipewa romance
hiyo, mpaka akalemewa akitamani amalize kila kitu.
“Natamani jumamosi ndio ingekuwa leo.” “Unakumbuka
mafundisho ya mchungaji?” Ezra akacheka na kumuachia. “Naona bora basi ninywe
tu uji.” Jelini akampa bakuli la uji wakicheka.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Maana waliambiwa kadiri siku zinapokaribia za
kufunga ndoa, ndio hatari inapoongezeka. Kujimilikisha siku chache
kabla ya ndoa na tamaa kuzidi. Aliawaambia kama hawatakuwa makini
wanaweza kujikuta wanakula ng’ombe mzima na kubakisha
mkia.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati anakunywa uji akamuona Jelini anatoa simu kama
anayetaka kuitumia. “Nakuhitaji tuwe wote hapa garini Jelini! Nani tena huyo!?”
“Junior. Nilikuta jumbe zake, sijasoma wala sijamjibu, nikakupigia wewe kwanza.
Acha nizungumze naye kwa ufupi tu wakati unakula. Nimtulize. Anawasiwasi
sana.” Hapo akakubali akijua na yeye atapata majibu mengi ya wasiwasi
wake maana alimjua Junior, kuna upande yeye alimuwezea Jelini.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akampigia hapohapo akapokea. “Jelini?”
“Samahani Junior. Nilirudi nyumbani, nikalala kabisa. Jema ndiye aliyeniamsha.
Isingekuwa yeye, pengine mpaka sasahivi ningekuwa nimelala.” “Hamna shida.
Nilitaka kukujualia hali.” “Nashukuru kujali Junior. Ila…” Akasita na kumwangalia Ezra aliyekuwa akisikiliza ila
macho kwenye uji aliopikiwa. Ulikuwa ukinukia karanga. Mzuri.
“Ni nini
tena?!” “Mimi nampenda Ezra. Na si kwamba nipo naye nusu nusu. Kwamba nipo naye
lakini akili zipo kwa Colins.” Junior kimya akisikiliza. “Unanisikiliza?”
“Nakusikiliza Jelini.” “Nampenda
mpenzi wangu na nina muheshimu.
Najua kile kilichotokea juzi kinaweza onekana vibaya, lakini sio kwamba kuna
kitu kinaendelea kati yangu na Colins.”
Akaendelea.
“Ila naomba
unielewe Junior. Huyu Colins alikuwa kwenye maisha yangu, tena ya karibu sana.
Tukapita naye kwingi. Tukapanga mpaka idadi ya watoto. Kulikuwa na mahusiano ya
ndani sana. Lakini tulishakubali kama hatutaweza kuwa pamoja. Na mimi sio
muhuni.” “Nazidi kukuelewa Jelini.” “Basi jua mimi sio msaliti.” Akaendelea wakimsikiliza kwa makini sana kutaja kujua
moyo wake zaidi.
“Ninachotaka
kusema, si kwa kujitetea, najua nawajibika kutoa maelezo kwenu na kuomba
msamaha. Ni kama nimemdhalilisha
Ezra wangu. Lakini sikukusudia. Ni jambo lilitokea kama vile kazi ya macho ya kawaida. Huwazi wala
kupanga wakati gani unafunga na kufungua. Ilinitokea kwa kunishitukiza. Na mimi nilijisikia vibaya, ndio maana niliondoka
pale. Nilijua nimeharibu.”
“Sasa Ezra
alipokuja na kuzungumza na mimi vile, nikajua hanitaki tena! Ananioa kama msichana mwingine tu. Sio mimi kama Jelini. Na mimi nia yangu nataka
kuolewa na mtu ambaye ananipenda na nimeleta maana kwake.” “Ezra anakupenda
sana Jelini. Sana, mpaka namuhurumia!”
“Ndio nimejua kama ile ilikuwa ni hasira tu, kwa sababu nilimuumiza. Lakini na mimi nampenda
mpenzi wangu. Sipo naye kwa bahati mbaya.”
“Nimeamua
kuwa na Ezra, kwa sababu najua ni majibu ya maombi yangu. Hata Colins mwenyewe
amekiri hivyo. Na nakuahidi nitajifunza kuishi na majibu ya maombi yangu.
Hapa nilipompitisha Ezra siku mbili hizi, sitarudia
tena, nikijua ananipenda.” Anaendelea kuzungumza,
asijue alivyo washitua. Wao walibakia kwa Colins! Mpaka Ezra akashindwa kunywa
huo uji.
“Unasema Colins
amekiri nini?” Jelini aliropoka. Akajua amekamatwa tena.
Akatulia. “Jelini?” “Nipo.” “Tunazungumza tu. Nataka kujua yeye Colins alisema
nini?” “Sio muhimu na sisemi hivyo kwa sababu yeye amesema. Mimi mwenyewe
nampenda Ezra. Na sitamsaliti hata na Colins.” “Hilo umethibitisha. Na
nakushukuru kwa uaminifu wako. Ila
nilitaka kujua kwa upande wa Colins.” Kimya.
“Tafadhali
Jelini. Najua nyinyi wawili mnahistoria nzito.
Na nasikia sifa ya Colins, hakubali
kushindwa, zaidi linapofika swala lako.” “Safari hii amekubali kushindwa na
Ezra. Anamsifia sana!” Wakashangaa wasiamini.
“Kwamba
anamfahamu Ezra?!” “Na wewe. Anawafahamu vizuri sana, tena kwa undani. Alikuwa
anatamani kama angemkuta Ezra na mapungufu ili ampatie sababu. Lakini anamfahamu
Ezra kwa undani, naona kuzidi ninavyo mfahamu mimi! Kwa kweli amemsifia. Na
nina uhakika amemtega Ezra na
mwanamke, akagundua Ezra si malaya.”
Walishituka wawili hao, mpaka Ezra akapaliwa na uji. Ikabidi Jelini ampigepige
mgongoni na kumpa maji. “Pole.” Jelini akaendelea kumtuliza akimpapasa
mgongoni.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Hawakutegemea wala hakuwa akikumbuka kama kuna tukio
lolote la tofauti la mwanamke kumtongoza.
Ni kama alishazoea hayo. Wanawake wa jiji hilo!
Wakutane na mwanaume mwenye pesa
kama za Ezra! Halafu anausafiri kama wake! Mjumba wa nguvu vile! Sura inalipa! Hao
wawili walishazoea kutongozwa mpaka kwa hila.
~~~~~~~~~~~~~~~~
“Daah!
Nahisi Ezra yupo kama mimi. Sijategemea!” Junior
akasikika upande wa pili, akitaka Jelini arudi kwenye simu. “Colins
anamuheshimu Ezra. Sana. Kwa hiyo usiwe na wasiwasi juu ya Colins. Na yeye
anataka nifanikiwe. Hatatusumbua na Ezra. Usiwe na wasiwasi.” “Nashukuru
kusikia hivyo mama. Kwa hiyo harusi bado ipo?” “Mimi bado nataka kuolewa na
Ezra.” “Yesss!” Junior akasikika. Jelini akacheka taratibu.
“Tunakupenda
Jelini. Na hili sitachoka kukwambia. Tunakupenda na kukuhitaji sana. Wewe ni kiungo muhimu kwetu sisi wanne. Bila wewe, ujue kila kitu kina simama.
Mipango yetu yote tuliyopanga kufanya weekend
hii sisi wanne kabla ya harusi, jua ilisimama kwa sababu wewe haukuwepo.”
“Samahani Junior.”
“Ndio ujue
ulivyo wa muhimu kwetu. Ezra hajala
tokea tulipofungua ile ijumaa. Hata maji ameshindwa kuweka mdomoni. Ndio ujue hatukudharau. Maana tungekuwa
tunakudharau, au wewe ni kama mwanamke tu mwingine, maisha yetu yasingesimama
wewe unapoondoka. Ndio uelewe umuhimu wako, hata kama tusipo kwambia.”
“Na mimi
nawahitaji Junior, ndio maana niliumia
nilipodhani mnanichukulia poa. Na nakuahidi sitarudia tena. Sasahivi nakuahidi mabadiliko. Sisemi hapatakuwa na
matatizo, lakini si kwa namna hii. Nitakabiliana nayo nikijua Ezra ananipenda
na ananihitaji.” “Nashukuru Jelini.”
“Kwa hiyo
na wewe umenisamehe kwa kumdhalilisha Ezra?” “Yameisha mama. Sisi tunataka
amani kati yetu. Tutabebana hivyohivyo katika madhaifu yetu. Usikimbie tu. Ila
nina ombi.” “Ombi gani?”
“Naomba uwe
unatufichia aibu yetu.” Jelini akaelewa na kuumia sana mpaka
akajikuta machozi yakimtoka. “Tafadhali, nakusihi. Ikitokea tunakukosea, kama
ni Ezra, zungumza na mimi. Nakuahidi sitamtetea. Na kama ni mimi au Emelda,
zungumza na Ezra. Tubebe tafadhali.
Itatusaidia kuwa imara kuliko umoja wetu uongozwe na watu wa nje.” “Nimekosa
Junior.”
“Hapana. Si
kwa kukutuhumu. Ninaomba huu ndio
uwe msingi wetu kuanzia sasa. Najua bado hujatuamini kama mama, Jema pengine na
Colins. Lakini nakuhakikishia na
sisi tunahitaji kuwa katika moja ya watu unao waamini unapokuwa umeumia. Na sisi tuwe kimbilio lako.
Binafsi nakuahidi kuwa na wewe pale hisia zako zinapokuwa zimeumia au upo na shida. Na sina tabia ya kumchoka mtu au
kumuhesabia mtu. Hilo ndilo ombi langu kwako. Tubebe, tusitiri maana najua sisi
sio wakamilifu.” Akapoa huyo Jelini, akashindwa cha kujibu.
“Umenielewa?”
“Nimeelewa
Junior. Na sitarudia tena. Nakuhidi nilichofanya juzi, kusambaza mambo ya
ndani, huko nje, hakitarudia tena. Utaona kwa vitendo. Nampenda Ezra. Sitaki
kumdhalilisha.” “Nakushukuru. Basi nikuache
upumzike. Nilitamani tutoke sisi wanne kesho, lakini mama amekataa. Anasema alishatuambia mwisho ni jumamosi. Kuanzia leo
mnatakiwa mpumzike ndani.”
“Hata hivyo
kuanzia kesho kuna ratiba zinaendelea pale nyumbani kwa mchungaji. Wakina mama
wanakuja kuanzia saa nne, kuzungumza na mimi pamoja na Emelda. Mama mchungaji
ameweka hiyo ratiba mpaka siku ya kitchen party. Na amemsisitiza na mama
pia. Hapatakuwa na mwanya. Tuvumilie tu. Kuanzia jumapili ijayo tutakuwa huru.”
“Hayo ndio nilitaka kukusikia ukisema. Asante Jelini. Usiku mwema.” “Na wewe
Junior. Nitakuona jumamosi.” “Daah! Asante mama.”
Wakacheka na kuagana.
~~~~~~~~~~~~~~~
Inaendelea…
0 Comments:
Post a Comment