Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 42. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 42.

Hodi ya mlangoni ya taratibu isiyoisha ikamtoa usingizini. Akaenda kufungua. Alikuwa Jema. “Nimekusubiria mpaka nimechoka. Nataka kurudi kwangu.” “Nilikuwa nimelala. Mimi sitaki kusumbuliwa.” Akajilalamisha hapo mlangoni. Jema akamwangalia na kuingia akimpita, akaenda kukaa kitandani kwake. “Njoo ukae hapa.” Akarudi kulala akimwangalia dada yake.

“Unaendeleaje?” “Naendelea vizuri.” Jema akabaki akimwangalia. “Nini sasa?” “Nataka kukwambia kitu, unaweza usiamini. Lakini siku ile James aliponivalisha pete ya uchumba, kwa surprise ya kipekee kule kazini. Nikawapigia simu wewe na mama nikirukaruka, huwezi amini. Siku ileile, mchana wake, hivi unajua nusura tuachane?” Jelini akashituka mpaka akakaa.

“Nyinyi! Mnavyopendana hivyo! Kwa nini!?” Jema akacheka. “Maana James anakupenda Jema! Tena na kukutetemekea. Mpaka sisi tunashangaa!” “Kuna vitu nilikuja kugundua juu yake. Kwa hakika nikataka tuachane. Sikutaka tena hata ndoa. Nikaona bora nimrudishie pete yake, maisha yaendelee.” “Sasa nini kikakufanya usimuache?” “James mwenyewe na mimi mwenyewe kujifikiria.”

“Acha nikwambie ukweli Jelini. Sisi tumezungukwa na kina mama ambao hawana ndoa. Kuanzia bibi mpaka mamdogo Mode. Ona walivyofanikiwa. Ukiwaangalia hapo nje, wanafuraha hutaona kuna upungufu kwenye maisha yao. Wapo huru. Wana kaumoja kao hivi. Wote wamejaliwa watoto. Mamdogo Mode ndio huyo anasema alitaka mmoja tu wa kiume, akampata na kufunga kizazi. Ni kama kila kitu chao kipo sawa. Kelele unazozisikia hapo nje ni furaha tupu.”

“Mimi sasa hivi nawaaga kuwa lazima niwahi kurudi nyumbani ili kumuwahi James, wote ni kama hawanielewi na kuona ni kama najipunja, niendelee tu kukaa nao hapo tuendelee kufurahia. Sasa, usipoangalia, hiyo hali kuna jinsi ya kuizoelea. Ukitingishwa kidogo tu huko nje, unaona bora urudi huku ambako kupo salama, kuna furaha na uhuru, kama mama zetu. Ndio maana mpaka leo watoto wa mama mkubwa hawajaoa japo ni wakubwa kwetu, na hawataki kuoa. Kila siku wanasababu mbaya juu ya wanawake. Ushajiuliza ni kwa nini?” Jelini kimya.

“Ni huu uhuru tunaopata hapa kwa mama zetu. Hata ukibadili wanaume au wakibadili wanawake, hakuna wakukuuliza wala kukukataza. Kwa mama zetu ni sawa tu.” Jema mwenyewe akajibu.

“Haya maisha hapa ni mazuri sana, na yanaleta uhuru wa namna yake, mpaka uwe unajua kwa hakika ni nini unataka.”

“Japokuwa James ananipenda sana, na tunaonekana kama tupo sawa, lakini na sisi tuna changamoto zetu, Jelini. Ilibidi kutengeneza msingi wetu kama wengine. Na si kazi ndogo na si ya siku moja. Ni kazi ya kila siku, bila kuzembea bila ya kuchoka, tukibebana. Leo anakosea yeye, kesho mimi. Au hata yeye mara nyingi ila na mimi huwa nakosea, tunabebana. Si kazi ya mtu mmoja wala, siku moja.”

“Na ukishaanza tu kuhesabu makosa ya mwenzio, jua ni kama unajiongezea mzigo kwenye furushi unalobeba. Maana wewe ndio unahatima ya jinsi ya kubeba mahusiano yenu. Kiurahisi au kwa uzito. Ukianza kuhesabu na kuweka moyoni, jua unajiongezea mzigo wa kubeba. Mkizungumza na kusamehe. Sahau. Endelea. Siku akikosea tena, unaanza kwa lile kosa la siku ile, sio kuleta mpaka ya nyuma mliyokwisha zungumza na pengine ulisamehe.”

“Namaanisha unaanzia kwa hilo. Ukianza kukumbushia ya zamani, jua ulilibeba. Hilo tukio la siku hiyo ndio limefunua la sirini. Utalemewa.” Jema akendelea taratibu tu.

“Usilemazwe na maisha ya hawa mama zetu. Ndoa ina raha yake, japo changamoto zipo. Lakini upendo…” “Husitiri wingi wa dhambi.” “Kumbe unajua!?” “Najua Jema. Tulifundishwa. Ila kutembea kwenye vitendo ni ngumu!” “Sasa jua hivi, kwenye mahusiano, unaposamehe, jua ni kama umeweka deni kwake. Kesho utakapokosea na wewe. Maana lazima tu utakosea Jelini. Utakapokosea, jua na yeye atajisuta, itabidi asamehe.”

“Na wala sitakudanganya. Hiki kilichotokea kati yenu, inaweza isiwe mwisho. Vitabadilika tu sura na majina. Acha kukimbia.” “Mimi sikukimbia kwa hili. Ezra alinionyesha hana shida na mimi, Jema! Ningefanyaje?” “Wewe ulichangia Jelini. Na wewe umemuumiza Ezra. Tafadhali jiweke kwenye nafasi yake, ufikirie.”

“Wewe ungejisikiaje, atajwe EX, wake. Tena uliyejua alikuwa akimpenda sana, apaniki kama wewe vile ulivyofanya?” Jelini akanyamaza na kurudi kujilaza.

“Mimi nakwambia kwa sababu unajua nakutakia mema Jelini. Na lazima tutoke kwenye maisha haya ya kina mama zetu. Si sawa Jelini. Sisi wawili kwenye huu ukoo wetu, lazima kuleta mabadiliko kwetu na kwa watoto wetu.”

“Au wewe unapenda Jeremy aje aishi maisha kama wanayoishi wajomba zake, watoto wa mama zetu? Kuwa na wanawake kila kona na hawataki kuoa kama mama zetu?” Jelini akapandisha mabega kukataa.

“Sasa hilo haliwezi kutokea mpaka sisi tulipe garama. Tutengeneze mfano wa kuiga watoto wetu, ili wafuate nyayo zetu huku tukiwaombea. Sitegemei JJ aje awe tofauti na kile anachokiona baba yake na mimi tukiishi. Chochote tunachokifanya pale kwetu, ni shule ya baadaye kwa JJ na ndugu zake. Na nimekusudia kwa garama yeyote ile, kumsaidia yeye JJ na wadogo zake, waje kuwa na maisha tofauti na tulivyokuzwa sisi. Kwa kuishi kwa mfano. Na huwa namkumbusha James kila wakati.”

“Japokuwa JJ bado ni mdogo, lakini hatupandishiani sauti sisi mbele yake. Joshua na Naya nao wanafanya hivyohivyo na kina Geb na Nanaa kumbe nao wanafanya hivyohivyo. Ni kitu tunakumbushana. Na Joshua haachi kutusisitiza kuwa ndoa zetu na jinsi tunavyoishi nyumbani ndio shule ya KWANZA na msingi wa maisha ya watoto wetu baadaye.”

“Japokuwa sisi hatukubahatika kwenye familia zenye ndoa na mifano ya kuiga, lakini Yesu ametukomboa Jelini. Roho mtakatifu ndio mwalimu wetu. Uzuri wake, atatufundisha hata yale mama ameshindwa kutufundisha au ambayo pengine tungekuwa na baba, angetufundisha.”

“Ezra anakupenda kwa dhati Jelini. Hutapata mwanaume kama Ezra.” “Na Colins ameniambia.” Jema hakuamini. “Colins!?” “Hakika mimi mwenyewe amenishangaza. Anasema kwa Ezra nimepatia. Amemchunguza, anasema hana hatia, na yeye peke yake ndiye ataweza kunipa yale yote niliyokuwa nikitamani.” Akamsimulia alichoambiwa na Colins, na kumshangaza sana Jema.

“Na ujue kwa Colins hadanganyi maana na yeye anakupenda kama mwehu! Atakuwa kweli amemchunguza.” Jelini akatulia. “Sasa ndio nilikwambia, jiweke kwenye nafasi ya Ezra, halafu upite pale ulipo mpitisha siku ile. Lazima ungeumia Jelini. Ulionyesha hisia zako waziwazi kwa Colins.” Akapoa.

“Halafu eti katika yote bado anataka muendelee, yupo tayari kukuoa akijua moyo wako upo kwa mwanamme mwingine! Kweli Jelini? Utampata wapi mwaaume kama huyo?” “Nampenda Ezra.” “Basi huo upendo, sasa hivi anauhitaji sana. Ana hali mbaya. Nimetoka kuzungumza na Junior. Alinitafuta kuzungumza na mimi, nikamuhurumia Ezra, ikabidi nimpigie ndio nikamtuliza na kumwambia umelala. Yule kijana atachanganyikiwa au hata kufa kwa ajili yako Jelini!” “Sasa mbona mimi nilishamwambia yameisha!”

“Mimi sijui Jelini. Lakini nakwambia ukweli kabisa. Haya maisha hapa, kama mama zetu, unaweza dhania ni mazuri. Ila kuna mazuri zaidi upande mwingine wa ndoa. Zaidi ukipata mwanaume anayekupenda kama Ezra. Nakuhakikishia hutajuta.”

“Uzuri nyinyi wote wawili mnaomba. Msingi wenu ni Yesu. Na Ezra ana HOFU ya Mungu ya kweli si kama hawa walokole wa siku hizi wasanii. Kukuumiza wewe kwa makusudi itakuwa jambo la mwisho kabisa akijua, Mungu anamwangalia. Ezra ni kama kina Joshua. Wanamjua Mungu na kujitahidi kuishi vile inavyompendeza.”

“Chukua nafasi yako. Tengeneza chako Jelini. Haya ni maisha ya mama. Si yako. Na kama ulivyo sema, hutaki Jeremy aishie hivi. Basi lazima akuone kwa vitendo wewe umebadilika. Unaishi unachotaka aje aishi. Umeelewa?” Akatulia kama anayejifikiria.

“We Jelini?” “Mimi nimeelewa.” “Haya, anza kwa kukubali katika lililotokea kati yenu, na wewe umechangia.” “Najihisi mimi ndio nimekosea Jema. Kwanza kama Ezra ndio angekuwa amefanya kama mimi, nahisi ndio ingekuwa basi. Mimi ndio nimekosa Jema, sio yeye. Mimi ndio nimemuumiza Ezra. Lakini sikukusudia.” “Usilie sasa. Ezra anakupenda na unanafasi ya kutengeneza. Mtakua na ndoa nzuri sana. Usiogope.” Akamfanya atulie.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Sasa ushajiandaa na fungate? Maana mamdogo Mode alikuwa anasema anamuhurumia kijana wa watu wa kanisani. Utambemenda.” Akamchokoza na kumfanya acheke sana.

“Mchozi tu. Kila saa ananipigia simu eti ananikumbusha eti Ezra ni mtoto mdogo sana, nimchukulie taratibu nisimpe ya walio kubuhu wa mjini.” Wawili hao wakazidi kucheka.

~~~~~~~~~~~~~~~

Mama yao akasikia nje. “Na Jema ndiye anayemuwezea huyo. Hapo kashatulia.” Mama yao akanong’ona, Mode akakimbilia ndani. “Nipe staili za mtoto wa kanisani. Utamfanyaje?” “Dozi yake ileile. Hakuna kupunguziwa.” Mode akaanza ushabiki kelele.

“Kutwa mara tatu?” Mode akaendelea kuuliza kishabiki. “Na kwambia dozi yake ileile kama ya walio kuhubu. Mpaka nimfanye kama nilichomfanya Kasa, ananiota wakati hajalala. Kila saa anahisi anaibiwa tu.” Hawana mbavu.

“Unamkoleza kama mwehu?” “Kama mjinga.” Jelini akazidi kujibu na kumfanya mama yake mdogo azidi kushabikia.

Wengine wakaingia mpaka bibi yake. Akaruka kwenda kumsalimia bibi yake. Akamchangamkia kama sio yeye. “Mwenzio naolewa, kama Jema, bibi.” Akajisifia. “Kwa hiyo umempata wa kukubembeleza?” Wote wakacheka maana alishamwambia bibi yake akimpata wa kumbembeleza ndio ataolewa.

“Tena huyu sana, bibi. Halafu anajua kuniweka mkononi. Naolewa.” Mama yake akahema kama aliyetua mzigo, wengine wakazidi kucheka. “Hongera. Na wewe nimekuletea zawadi nzuri kama Jema.” Stori zikaanza hapo chumbani kwa Jelini akiwa na nguo zake za kulalia. Maneno mengi. Mode akaanza kutoa mautundu, wakishindana na Jelini.

“Ni shapata ya usiku huu, acha nimuwahi James kabla hajalala.” Walicheka, mbavu hawana. “Ipi Jema?” Hawakuamini alivyoirudia mbele yao. “Jema umekubuhu wewe mtoto!” Mode akazidi kuhamaki. “Unafikiri ningepata mimba ya pili hivihivi!” Akajibu akibeba vitu vyake. Hawana mbavu. “Mama Jema, kwa heri.” Akamuaga mama yake. Akatoka naye kusindikiza mwanae na mjukuu.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Asante kwa kuzungumza naye, Jema. Nakushukuru mama. Na wewe Mungu akusaidie kwa watoto wako.” “Amina mama. Lakini unamjua Jelini akikutana na mamdogo Mode. Atajisahau, wakati kijana wa watu huko anahangaika. Hakikisha unamtoa pale akazungumze naye.” “Wewe ndio unamuweza. Rudi umkumbushe.” “Na kweli. Au na wewe wafukuze dada zako. Waambie bibi anataka kupumzika.” “Unamuona bibi yako alivyochangamka vile! Ashalewa, hapo ni kukesha.” “Basi acha nimtoe Jelini, akazungumze naye waendelee na fujo zao.” Jema akarudi ndani.

“Jelini, Ezra anakutafuta tokea asubuhi. Tafadhali mpigie sasahivi. Haya, kina mamdogo ondokeni azungumze na bwana harusi.” Wakatoka cheko limewajaa, Jelini amerudia hali yake.

 Better Late Than Never.

Akachuku simu ili ampigie, ndipo akakutana na jumbe za Ezra. ‘Tafadhali usinichukie mpenzi. Nahisi nitakufa.’ Jelini akashituka. Huo ulikuwa ujumbe wa kwanza. ‘Nihurumie, unisamehe mpenzi. Jua nilikosea, lakini sikuwa na nia ya kukuumiza kwa namna yeyote ile. Nina hali mbaya kupita hivyo ulivyoumia wewe. Ni kama nimejiumiza mwenyewe. Sikujua kama yale maneno yalibeba maana mbaya ya kiasi hicho! Nihurumie, nisamehe.’ Ukawa ujumbe wa pili.

‘Najua itachukua muda kurudia hali yetu ya zamani, lakini naomba usininyime mawasiliano.’ Ikabidi kuangalia kama kulikuwa na missed call. Akakuta alimpigia mara mbili. Mara baada ya ibada na masaa mawili yaliyopita. Akajua hapo ndipo Junior alipomtafuta Jema baada ya kumkosa kwa mara ya pili.

Akarudi kwenye jumbe tena. ‘Kutokukusikia au kunisikia, si kawaida yetu Jelini. Wakati wote sisi tunazungumza. Nimeshazoea kukusikia mpenzi wangu. Kuninyima mawasiliano ni adhabu ngumu sana kwangu, tafadhali nichagulie ingine, sio hiyo.’ Jelini akamuhurumia.

‘Nifikirie ukijua sina mtu mwingine maishani, ila wewe. Nakuhitaji Jelini.’ Ikabidi kuacha kusoma na kumpigia.

Ikawa kama aliyekuwa na simu mkononi. Akapokea ilipoita tu. “Pole Ezra, nilirudi nyumbani nikaamua kulala kabisa, yaani ndio naamka. Sio kwamba nimekunyamazia. Nilishasema yameisha.” “Bado unanipenda Jelini? Niambie tu ukweli. Au ndio nimekukera kabisa?” “Nakupenda Ezra.” “Na bado unataka nikuoe au umenikatia tamaa?” Akatulia kama anayefikiria na kumuumiza Ezra.

“Nakupenda Jelini na nakuhitaji sana. Tafadhali usibadilike kwa makosa yangu.” “Hapana Ezra. Mimi ndio natakiwa kukuomba msamaha.” Ezra akatulia akihisi hajamsikia vizuri. “Mimi ndio nili…” Akakwama kama ambaye hakujua aseme nini. Na Ezra naye akatulia kabisa kusikiliza.

“Ninachotaka kusema, ulikuwa na haki ya kukasirika. Unanipenda sana Ezra. Kitu kilichonipata siku ile usiku mbele yenu, sikutegemea. Nilishituka bila kupanga hata mimi nilishangaa. Ni kitendo nilichofanya kama kupepesa macho. Najua nilikuumiza na kukukasirisha kwa sababu umeona jinsi ulivyojitoa moyo wako kwangu halafu mimi ni kama nipo kwa mtu mwingine.”

“Lakini Ezra, jua nakupenda mpenzi wangu. Zile ni hisia ambazo zipo ndani nafikiria zinakuja kuibuka katika matukio kama yale, lakini usifikiri nakuwa na wewe nusunusu. Hapana. Nakutaka wewe, na nakuhakikishia sitakusaliti hata na Colins. Mimi ndio nimekosa Ezra. Sio wewe. Naomba msamaha.” Ezra hakutegemea.

“Nina hali mbaya Jelini, nahisi kuvurugikiwa kabisa.” “Nikikushika itasaidia?” Akabembeleza. “Nahisi nitatulia kabisa. Nikukumbatie, unikiss, halafu uniambie kama unanipenda, na jumamosi usiku utalala kifuani kwangu.” “Na huo utakuwa mwanzo wa siku nyingi za sisi kuwa pamoja. Nitakupenda Ezra mpaka kifo chetu.”

“Nakuahidi sitakusaliti. Na sitarudia tena kufanya nilichofanya juzi. Nita omba msamaha na kwa Junior. Sio sawa kwako, ni kama nilikudhalilisha mpenzi wangu. Nisamehe.” “Acha nikuone kwanza Jelini. Hapa nishachukua funguo za gari, nakuja kwenu. Nikifika utoke nje, tukishapata muda wetu ndio nitaingia ndani kusalimia.” “Wala huna haja ya kuingia. Sasahivi wote wamelewa. Hakuna mtakachoelewana. Kwanza nataka muda wetu wa peke yetu.” Hapo akazidi kumpagawisha Ezra. Akamuaga kama apae kuwahi huko kwa kina Jelini.

Akakimbilia bafuni kusafisha kinywa akijua kiss za mpatano zinafuata. Akaweka pipi nzuri mdomoni kutoa ladha ya dawa ya mswaki, akaanza kumuandalia uji wa haraka haraka.

~~~~~~~~~~~~~~~

Inaendelea…


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment