![]() |
“Kwanza
haitakuwa sawa kwa Jelini mwenyewe na Ezra.”
Akatamani kama angekuta kosa kwa Ezra, akajipatia sababu, lakini akajikuta Ezra
hana hatia ya kumpokonya Jelini. Akajirudi na kuona maamuzi aliyokuwa
nayo tokea mwanzo yalikuwa sahihi. “Siwezi kuyumbishwa na maneno yaliyojaa
wivu na hasira.” Akasimama kabisa ili kutojipa nafasi ya kuendelea kufikiria
zaidi.
Akasimamia maamuzi
yake ya tokea mwanzo anamfuata Jelini hotelini na kumuacha.
Akatoka kabisa hapo chumbani kumfuata Kamila akikusudia kutengeneza kwake.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akamkuta jikoni ameanza
kuwa busy na msichana wa kazi
akimsaidia kuandaa aanze kupika. “Nakupenda Kamila. Nakupenda na hata Jelini
anajua kama yupo Kamila kwenye maisha yangu na mimi ndio nimebahatika.” Akaanza
kumpata. Akamwangalia. “Na ujue nimekusifia sana kwa Jelini.” Akaendelea
akimjua Kamila, moyo mwepesi.
“Nimejisifia jana,
utafikiri niliulizwa!” “Unanipamba tu.” “Sasa kwa nini nikudanganye? Na James
mwenyewe anajua kama Kamila ni Mungu kunifuta
machozi. Nimewaambia Kamila wangu hana
makuu. Hata kama mimi walikuwa wananiona ni mbaya, basi kwa Kamila mimi sina hatia. Kamila wangu ananisitiri. Upendo wake unafunika mapungufu yangu YOTE. Nimejisifu kweli!” “Unanipamba
tu.” “Nimpigie simu James nimtege halafu umsikie akisema sifa za Kamila wangu?”
Akapandisha mabega akikataa, ila akatoa kilichomkera.
“Sasa wewe kwa nini unaniacha humu ndani unamkimbilia Jelini?” “Na nimezungumza
naye sana jana. Tulikutana mimi na yeye wote tunamapungufu. Ila nikamsihi
ajaribu kubadilika, nikamwambia mimi nimejifunza sana kutoka kwako. Nikampa mifano yako na Mike
mpaka akatulia. Nimemshauri arudi kwa mchumba wake.” “Kwamba wewe humtaki tena huyo Jelini?!” “Sasa mimi
si nishapewa Kamila wangu!” Hapo dhambi zote akasamehewa. Cheko Kamila, hana makuu. Akiwekwa sawa kidogo tu,
bila nguvu nyingi, keshalainika.
“Nakupenda Kamila. Na jana sikukuaga
kwa sababu kwanza nilijua utakua umeshalala. Maana mimi mwenyewe aliniamsha
kwenye usingizi mzito, nyumba nzima ilikuwa imepoa, hata sikujua kama baba
angesikia! Nilitoka kwa kunyata ili nisisumbue yeyote yule. Sikutaka wote
tukeshe.” Akamuona amenyamaza.
“Umenisamehe?” “Kwa
kumkimbilia Jelini?” Colins akaanza kucheka. “Usicheke bwana!” “Mimi nahisi
hata mbinguni nitavikwa taji. Wakati watu wote wamelala, mpaka malaika, mimi
nilienda kuokoa ndoa. Ulitakiwa
unipongeze.” “Sasa siku nyingine wewe usiwe na wasiwasi. Kule kumtafuta kwenye
kompyuta yako hapo chumbani, nakumpata, kisha kumpa shemeji yake pia utavikwa taji.” “Hilo nimeelewa. Kama wewe
ukisema nivunje uaminifu wake kwangu, kwa kutoa siri ya alipo, basi nitafanya
hivyo.”
“Kwanza ulimfuata wapi?”
Colins akaanza kucheka akimwangalia. Kamila akakunja uso na kugeuka kabisa.
“Usiniambie ni hotelini Colins, bwana!” “Nakwambia hakuna kilichotokea. Na
nilimwambia kabisa, kwa heshima yako na Ezra mchumba wake.” Akatulia
akitafakari.
“Kwa hiyo Jelini anajua
kama sasahivi una mchumba anaitwa Kamila?” “Sio hivyo tu, na sifa zako kibao anazo. Wewe acha kupika, twende zetu tukamalizie ibada,
twende tukale na familia. Ratiba yetu ya leo iendelee kama tulivyo panga.”
Akakubali kwa roho moja, akatoka hapo jikoni kwenda kubadili.
Raha Ya Mpatano Baada Ya Ugomvi Wa Wapenzi.
Colins akamfuata wakati
anatoa nguo ndio akawa anaingia. Akamkumbatia akiwa na chupi na sidiria tu.
“Sitakusaliti Kamila.” “Hata na Jelini?” “Hata na Jelini.” Zikaanza kissing, wakajisahau, akamtoa chupi.
“Nina hamu na wewe Colins!” Akajilalamisha. Akavuta godoro na kulitupia
sakafuni, mchezo ukaanza hapo wakiwa wamekumbatiana kama wasianguke.
Na hivi Kamila ashajua kama
Jelini anajua kama yeye ndio mmiliki wa Colins, akajawa sifa huyo! Hisia
zikawa juu haswa. Akishikwa kidogo, anapiga bao. Akamng’ang’ania mwenzie
kwa uchu, wakikataka kiu vilivyo. Kuja kumaliza, na ibada kule inakaribia
kuisha.
Wawili hao mara ya mwisho
ya penzi, waliachana wakijua wangerudi Kigamboni kwenda kuishi wote. Kwa hiyo walikatishwa. Penzi lililofanywa hapo
kwanza la wizi wakijua wanaweza wasije pata tena nafasi kama hiyo tena,
pili wasijue ni lini tena watapata nafasi kama hiyo. Basi wakakomezea mpaka
kupitiliza.
Huku Kuliko Ungua Mpini, Kukabaki Shoka.
Wakati yupo kanisani.
Ameshindwa hata kupiga kinanda siku hiyo, wala gitaa hakuweza, akiwa amekaa kwenye
kiti ameinamisha kichwa chini, waumini wengine wakiendelea kumsifu Mungu wao
wakiimba na kucheza. Asilimia 99 ya kanisa walikuwa wamesimama wakicheza kwa
shangwe, yeye alibaki tu amekaa, ameinamisha kichwa, mikono ameifungamanisha
mbele kama anayeomba kumbe anashindwa hata kuzungumza na Mungu wake!
Akahisi mikono laini
inajipenyeza katikati ya viganja vyake. Ezra hakuamini! Maana alijua kwa
hakika atakuwa Jelini tu, hakuna msichana mwingine angethubutu kumshika
hivyo. Akafungua macho kuangalia, Jelini alikuwa amekaa kiti cha pembeni yake,
karibu yake kabisa.
Akajikuta anapiga magoti
mbele yake na kumlalia. Kichwa ameegemeza magotini kwake amefunga macho. Wawili
hao wakajisahau, Jelini akaanza kupitisha kucha pembezoni mwa sikio,
mkono mwingine anampapasa mgongoni. Uzuri watu walikuwa wamesimama, wao wamekaa
kiti cha mwisho kabisa, wachache sana waliona. Wakakaa hivyo kwa muda, kisha
akarudi kukaa. Akamwangalia.
Jelini akamwangalia na
kuinama. “Samahani kukuumiza.”
Akanong’ona karibu kabisa ya sikio lake, japokuwa mziki ulikuwa
ukitumbuiza kwa nguvu, aliweza kumsikia. Kisha akaongeza. “Na asante kwa kurudi.”
Jelini akamshika tu kiganja cha mkono uliokuwa karibu yake. Akapishanisha
vidole na kutulia wengine wakiendelea kumsifu Mungu.
Wakatulia, baada ya muda
akamuaga kwa kumnong’oneza sikioni. “Inabidi nirudi nyumbani sasahivi.” “Hatukai
mpaka mwisho?” Akamwambia atoke nje wazungumze.
Wakatoka lakini akampitia
mtoto wake kwa Jema na familia yake walipokuwa wamekaa. Akatoka naye nje.
Akampandisha garini na kumuwashia gari kabisa ili apate hewa kwa kuwa
alipandisha vioo, ndio akatoka kuzungumza na Ezra.
“Lazima nirudi nyumbani
sasahivi kwa ajili ya kumrudisha Jeremy kwa mama. Jema ameniambia anawasiwasi hajalala vizuri. Na bibi anaingia muda
si mrefu. Nataka anikute ndani.” Alitamani kuuliza mengi. Zaidi kama bado ndoa
ipo. Ila akashindwa. Akabaki amesimama mbele yake, kimya.
Mwishoe Jelini mwenyewe akavunja
ukimya. “Mimi sijasoma, lakini
nafanyaga maamuzi yangu mimi mwenyewe.”
“Najua Jelini. Na naomba unisamehe kwa kukuumiza. Nakiri ni wivu ndio
umenifanya nizungumze hivyo, lakini sikudharau.”
“Halafu mimi sio mtu wa kuendeshwa na mama. Tena nahisi
nakusikiliza wewe zaidi kuliko hata mama.
Sikutaka kuolewa na wewe eti kwa sababu mama ametaka! Niliamua mimi mwenyewe.” Akaendelea. “Na mimi swala la ndoa kwangu
ni muhimu kama wewe. Nataka kuolewa
na mtu anaye nihitaji Ezra! Mtu ambaye nimeleta maana kwake sio niwe nimeingia katika moja ya mipango ya
mtu, ambaye anataka kuoa. Ndio Jelini nikatokea kama mwanamke. Hivyo hapana.”
“Nakupenda Jelini.” “Lakini
mimi nataka kuolewa na mtu ambaye ananihitaji Ezra, sio mtu ambaye hana
shida na mimi kama Jelini, ila mwanamke. Kuniambia unanipenda halafu upo tayari
tuachane siku chache kabla ya ndoa!
Mimi hiyo imenitisha. Tena
unaniambia sijachelewa!” “Nimekosea Jelini. Nimekosa mpenzi wangu, sijui
niliingiliwa na nini!”
“Ila jua nakupenda na nakuhitaji SANA. Sitaki hata kuhisi maisha bila wewe. Inawezekana
niliongea kwa kiburi tu nikiwa na hasira, lakini sikuoi wewe kwamba bora naoa
mwanamke! Hapana. Kama ingekuwa hivyo, ningekuwa nimeshaoa muda mrefu sana.
Wanawake ni wengi. Tena warembo tu, lakini mimi nakutaka wewe Jelini. Nimekosa,
na nimejifunza kutokana na makosa.
Naahidi haitarudia tena.” Jelini kimya.
“Umenisamehe?” “Yameisha
Ezra. Ila inabidi mimi niondoke sasahivi.” “Naomba nikupigie baadaye
tuzungumze.” “Labda usiku wakati wa kulala. Kutakuwa na fujo nyumbani,
hapatakuwa na kusikilizana.” Ezra akajua amembadilikia. Jelini si
wakutotaka kuzungumza naye eti mpaka usiku! “Uwe na siku njema Ezra.” Akamuaga
akitaka kurudi garini.
~~~~~~~~~~~~~~~
Mara Junior akatoka.
“Jelini! Jelini!” Akageuka maana alishafungua mlango wa gari. Akafunga na kurudi.
“Vipi? Upo mzima na mtoto?” “Sisi wazima, ndio tunarudi nyumbani.” “Pole kwa
matatizo.” “Nimeshapoa.” Wakanyamaza kama hawajui wazungumze nini tena!
Akamwangalia Ezra, akamuona kama hayupo sawa.
“Nikuulize kitu Jelini?”
“Niulize tu.” “Kwa hili lililotokea. Unafikiri bado harusi ipo?” “Mimi
sijui!” “Jelini!” “Kwani tokea mimi umenifahamu Junior, ushawahi hata nihisi
nina sitasita kwenye mahusiano yangu
na Ezra?” Akamuuliza na kuongeza.
“Au ushaona hata mara moja
nipo na nyinyi kama nipo mguu mmoja ndani mwingine nje?” “Hapana
Jelini.” “Sasa kwa nini leo ndio mnaniuliza!? Mimi sina akili za kushikiwa.
Nina akili zangu binafsi. Na nina uwezo wa kufikiria na kufanya maamuzi yangu
mwenyewe.” “Najua Jelini!”
“Na mimi si mbambaishaji.
Nikiamua kufanya jambo, nafanya vizuri, tena kifasaha. Sijawahi kuwapa sababu
hata mara moja kama mimi moyo wangu haupo na Ezra. Wakati wote nimesimama
na nyinyi na kuonyesha mwenzenu nawahitaji. Lakini mnaniumiza jinsi mnavyonitilia
mashaka! Sijui natakiwa kufanya nini ili mniamini!”
“Basi Jelini. Basi mama. Nakupenda
ndio maana sitaki kukupoteza. Nakujali ndio maana unaona nakuuliza. Na hatukudharau
hata kidogo. Tafadhali usiumie.” “Nimeumia Junior.” “Pole. Unataka tukuletee
nini nyumbani?” “Mimi sitaki kitu. Kwanza kutakuwa na wageni. Na wageni wa mama
Jema ni komba. Kutajaa pombe hapo, hapatakuwa na pakupita.” Wakakwama.
“Acha mimi nimuwahi mama, nimtulize
kabla dada zake hawajaja. Nilikuja hapa mara moja tu, kumuona Ezra. Nishamuona,
acha niwahi nyumbani, nimrudishie mama, Jeremy. Atulie maana nasikia hajalala.”
Akarudi garini na kuondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Mbona huna raha tena!?”
“Sijui Junior! Sijui kama ndoa ipo au la! Nimeshindwa
kuuliza, nimeshindwa kupata jibu la moja kwa moja. Sijui kama nimesamehewa
kabisa! Sijui kama tutarudi kuwa kama zamani! Jelini si wakuondoka bila hata
kunishika! Hajui kama tutawasiliana au la! Sijui Junior.”
“Sijui nawaambia nini
wazazi! Nahisi nimechanganyikiwa. Natamani kusogeza hii harusi mbele ili
niwekane naye sawa, nimrudishe pale tulipokuwa kabla ya hili tukio.” Akawaza na
kuongeza.
“Jelini alikuwa akinipenda
sana. Napenda vile alivyokuwa akionyesha ananihitaji. Alivyokuwa akifurahia
nikimshika na kutaka kunisikia kila wakati. Sijawahi pata upendo kama wake.
Nahisi navurugukiwa kabisa.”
“Sikiliza Ezra. Tumia
huohuo udhaifu wake kumrudisha
kwako. Sasa hivi amekasirika. Mbembeleze
kabisa ukimuonyesha unamjali na kumuhitaji. Yeye mwenyewe
alikuwa amepania safari ya fungate
na ndiye ametuhamasisha sisi wote
mpaka tumeandaa masanduku ya huko, akiwa mstari wa mbele kundaa sanduku
la Emelda pia, na kuhakikisha masanduku yote yapo kwetu tayari kwa safari.”
“Na akahangaikia hati yake
na ya Emelda mpaka Visa zote zikawa tayari.” “Kumbe unakumbuka?” “Nakumbua. Ni yeye
mwenyewe Jelini.” Ezra akajibu.
“Sasa ndio ujue Jelini alikuwa
yupo tayari na harusi ya jumamosi, ila amekasirika tu. Na japokuwa mama alisema
tuwaache wapumzike mpaka siku ya harusi, tunaweza jiiba hata jumatatu mchana wazazi
wakiwa kazini, tukaenda mpaka kwao, kujipanga naye upya. Sawa?” Akamtuliza
mpaka tumaini likamrudia ndio wakarudi kanisani.
~~~~~~~~~~~~~~~
Alirudi kwao akamkuta mama
yake yupo kitandani kama mgonjwa. “Mimi nimemrudisha huyo Jeremy. Na muulize
kama kuna jambo baya nimefanya.” Kimya. “Na nimewahi kurudi ili bibi anikute
ndani. Kwa hiyo usinilaumu. Mimi
naenda zangu kunywa dawa ya usingizi. Nalala. Sitaki usumbufu.” “Nashukuru kwa
kuwahi kurudi.” “Mimi sio mtoto mbaya.” Mama yake akakaa.
“Najua. Kwa hiyo harusi ipo
au bibi yako akija nimwambie nini?” Akanyamaza. “Eti Jelini, mama yangu mzazi,
nikupendaye? Na Mode anakuja kukufunda.”
“Nishamwambia mimi ndio nitamfunda.” Angalau mama Jema akacheka.
“Anakuja sasahivi.” “Mimi
nataka kulala mama.” “Basi nitawaambia taratibu. Ila ujue na Jema akitoka
kanisani anakuja na familia yake.” “Mimi nalala.” “Hata Jema humtaki?” “Sasa
hivi nimekukasirikia wewe.” “Sasa
mimi nimefanyaje?!” “Huniamini na Jeremy wakati nishakuonyesha mara kibao mimi nimebadilika, lakini huniamini. Muulize huyo Jeremy kama
mimi nimefanya jambo baya.”
“Basi mama yangu mzazi.
Akifunga shule, wewe mchukue popote unapotaka kwenda, ilimradi kila usiku
nizungumze naye. Hapo hatutakuwa na neno. Lakini si katikati ya shule, halafu
ukiwa umekasirishwa, unakuwa kama unakimbia watu! Sijui alipo! Sijui
anapokwenda kulala! Sijui nani atamsogelea, nani atamgusa! Hapo utaniua na pressure.” Akaondoka bila ya kujibu.
~~~~~~~~~~~~~~~
Alivyo Jelini, akaingia
chumbani kwake na kufunga mlango kabisa. Akaoga tena na kuvaa nguo za kulalia
kabisa, akanywa kweli dawa za usingizi. Tena akajiongezea dozi. Akawasha mziki
kwa sauti ya kuenea chumba ili kelele za nje zisimkere. Akafunga madirisha
yote. Giza. Akajiwashia A/C. Jelini mpenda kitanda, akazima kama mshumaa.
Love Comes To Those Who Belive It
Familia ya Komba walishaandaa mazingira maalumu ya
kuchumbiwa kwa Kamila siku hiyo. Wawili hao baada ya penzi zito la mpatano, walijua
ibadani wameshachelewa. Wakaoga na kuelekea hotelini ili kukutana na familia
huko wakitoka ibadani.
Wakaenda kwenye
hoteli ileile iliyokuwa imeacha historia mbaya kwa Colins. Love na Kemi wakiwa wamegongelea
msumari wa mwisho wa mapenzi kwa Jelini.
Walishaweka reservation
kwa familia nzima. Kwa hiyo wakaenda sehemu na kwenye meza waliyokuwa
wameandaliwa. Wakakaa hapo na kuagiza vivywaji wakisubiria waliofanikiwa kwenda
kanisani wafike hapo wajumuike nao.
Kukawa na hali ya
utulivu iliyomuhakikishia Colins hata kama angeomba ndoa, angekubaliwa tu. Kamila
alikuwa ametulia, anaonekana anafuraha. Na mchezo aliotoka kupewa, alikuwa mwepesiii.
Alipopata ujumbe kutoka kwa Connie kwamba
wamefika akamwambia wakatembee kidogo baharini. “Bwana Colins! Mwenzio nimevaa
kiatu cha juu, siwezi tembea mchangani!” “Vua mimi nitakusafisha miguu
tukirudi.” Akacheka mwenyewe kwa deko! Akavua viatu ndipo wakatoka hapo kuelekea ufukweni.
Sasa kadiri walivyokuwa wakitembea, akagundua Colins
anapunguza maneno. Na yeye akatulia wakawa wanatembea kimya kimya. Mbele akaona
kitu kilichomvutia macho.
“Ona Colins! Pale pamepambwa vizuri mpaka nataka tujiibe
tukapige picha!” Colins akacheka sana kwa furaha akijua aliyemlipa atengeneze
hivyo, ametimiza lengo. Mlengwa amefurahia.
“Twende.” “Ndio umepapenda kiasi hicho!?” “Sasa wewe
huoni jinsi kulivyotengenezwa kwa unadhifu! Tena hakuna mtu. Twende tujiibe
tukapige picha.” “Unauhakika? Tusije..” “Acha woga bwana! Twende.” “Sawa!
Tukikimbizwa ujue umejitakia.” Kamila akaanza kucheka mbavu hana, ila
akawa amekusudia kwenda.
Wakasogea mpaka pale. Ndipo akagundua lile shada kubwa
sana lililotengenezwa kwa maua meupe kwa muundo wa moyo, katikati kuna
maneno. Ushabiki, akasogelea karibu asome. ‘Will you Marry
me, Kamila?’ Kamila alishituka sana na kumgeukia Colins,
akakuta amepiga goti.
“Colins!?” Akamsogelea pale alipopiga goti.
“Namaanisha nikikwambia siwezi tena kuishi bila wewe Kamila. Na
kama sijakwambia vyakutosha, amini nakupenda. Nakupenda Kamila, na nakuhitaji.”
“Lakini hujanijibu, Colins! Iweje Jelini aje arudi na sisi tumeshafika mbali!
Sio sawa.” “Nimefunga milango yote yakutoka na kuingia kwa yeyote yule.”
“Hata Jelini!?” “Hata Jelini. Na jana nilikutambulisha kwake ramsi.
Anakufahamu na ametutakia kila la kheri. Ameniambia nakustahili. Sasahivi ni
mimi na wewe, tutengeneze chetu.” Kamila alifuhi huyo!
“Kwa hiyo ndio umekubali?” “Nimefurahi! Nimefurahi sana.”
Colins akaanza kucheka. “Sema sasa ‘ndiyo!’ ndio uendelee kufurahia.”
“Mwenzio nakupenda Colins. Na nilikuwa natamani tubaki sisi tu. Sasa
ulivyoshindwa kunijibu juu ya Jelini, nikaingiwa na wasiwasi. Nikajua tupo
pamoja kwa muda, pengine ni mpaka Jelini aolewe ndio uhakika wangu
kwako. Halafu ulipomfuata jana usiku ndio nikakata tamaa kabisa.
Nikajua mimi tena basi!”
“Na ndio maana nimeamua kufanya sasahivi kukuhakikishia
kama ninakupenda wewe, na nimekuchagua wewe hata kama bado Jelini
hajaolewa. Nakuhakikishia sasahivi ni mimi na wewe tu. Na kukubali kwako ndio kunisaidia
kufunga milango yote hata ya mimi kufikiria mwingine. Ndio nitakuwa nimejifunga
kwako tu.” Akazidi kufurahi huyo Kamila, haamini.
“Goti limechoka Kamila! Si ukubali uvae pete, mengine
baadaye.” Akaanza kucheka, mbavu hana mwenzie amebakia gotini.
“Anakukomoa?” Wakamsikia Mill. Kamila hakuamini. Akazidi
kuruka ruka alipoona wanamsogelea. “Leo kaka utakoma!” James naye akaongeza.
“Na kwambia na kesi zangu zote zinaendeshwa hapahapa, hivihivi!”
Wote wakazidi kucheka. Kamila anafurahia.
“Sasa Kamila mwanangu, hiyo furaha ungeendelea ukiwa na
pete mkononi.” Ndio akarudi kwa Colins. “Nimefurahi Colins! Kwa hiyo utanioa
kabisa ile ya kanisani!?” Watu wote wakazidi kucheka.
“Leo mzee siku yako mchangani.” James akazidi
kuwachekesha. “Nivalishe halafu unijibu! Nimechanganyikiwa! Sikuwa nimetegemea
kabisa! Nimefurahi sana.” Ungeweza ona furaha ya Kamila waziwazi. Hakujificha
kama anapenda ndoa.
Hatimaye Colins akamvalisha, wakaanza kupiga makofi na
kushangilia. Colins akasimama na kupata kiss, ila Kamila akalifanya fupi
na kumnong’oneza. “Sasa hapa na baba yupo!” Colins akashangaa sana. “Kamila!?”
“Kweli tena. Mimi naona aibu. Siwezi tena.” Wakawapongeza hapo na picha
kuendelea.
~~~~~~~~~~~~~~
Na hivi mzee ndio alikuwa kijana wake wa pekee anaoa,
akataka kumbukumbu ya kueleweka. Kulikuwa na mchukua video na picha pia.
Aliyewaandalia hapo kwa kupapamba baada ya kuona wanamalizia kufurahia akasogea
hapo. Wakamshukuru kwa kazi nzuri. “Naona Kamila mwenyewe amepafurahia sana.
Nashukuru.” “Nilikwambia kazi zangu sibabaishi.” “Nashukuru.”
Ndipo wakaondoka eneo la baharini na kurudi kwenye sehemu
waliyokuwa wameandaliwa meza chache zilizounganishwa pamoja kwa ajili ya mlo rasmi
wa pamoja. Full course meal, ndiyo waliyo kuwa wakihudumiwa siku hiyo.
Maalumu kwa ajili ya kuchumbia kwa Colins. Wakala siku hiyo kama tafrija
kabisa.
Walikuwa na wakati mzuri sana! Walikuwa watu wa karibu tu
na Colins, Mill na watoto wake. Wazazi na Connie akiwa na yeye na mchumba wake,
japo bado hawakuwa wamevishana pete, ila alifahamika mpaka nyumbani. Na huyo James
ambaye bado alikuwa haamini kama Colins anachumbia mtu mwingine na si Jelini! Ila
akakubali Colins amepata msichana mzuri.
Yeye alikuwa peke yake. Alitokea kanisani akamuacha Jema
akienda kwao na mtoto pamoja na msichana wa kazi, yeye ndio akakimbilia huko
kwenye shuguli. Kisha akawepo Colins mwenyewe na Kamila. Ungejua yapo mapenzi
kati yao. Kila wakati kuangaliana, na kupeana kiss fupi.
“Nimependa pete yangu! Nzuri sana. Asante.” Akamwambia
Colins. “Na imekupendeza sana. Una vidole vizuri sana Kamila.” “Asante! Ila
bado siamini kama na mimi nitaingia kanisani kuolewa! Nilikuwa natamani!
Nimefurahi sana.” Akaendelea kufurahia.
~~~~~~~~~~~~~~
Karibu na mwishoni, akahamisha kiti karibu na baba
Colins. “Nimefurahi baba! Nimefurahi sana.” “Hongera Kamila binti yangu.” “Wewe
ndio nikushukuru zaidi. Mimi sikuwa hata najua kama nitakuja kuolewa! Ila wewe
baba yangu, umehakikisha na mimi naolewa. Asante sana.”
“Unastahili Kamila binti yangu. Ni haki yako na hilo nitalisimamia mpaka
kanisani.” Alijawa furaha huyo! Cheko muda wote.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Sasa, na mimi zamu yangu watu wanilipe pesa yangu yote
niliyokuwa nikiwachangia kwenye shuguli zao. Jumamosi ijayo, kikao cha kwanza.
Zege hailali.” Baba Colins akasikika akiwa amehamasika haswa. “Hutaki mchezo
mzee wangu!” “Kabisa. Nimekua na kazi ya kuozesha watoto wa watu, kwangu
kulikuwa kimyaa! Kama sikujaliwa watoto wakati Mungu alinipa watoto wazuri kama
mke wangu!” Watu wakazidi kucheka. Ila kikawa kipindi kizuri haswa.
~~~~~~~~~~~~~~
“Jamani, naomba ni propose a toast to James and
Jema. Wamebarikiwa mtoto wa pili. Jema ni mjamzito.” James hakuamini.
“Kwamba wewe jana ulinisikia ila ukanipuuza!?” “Unaharibu James.” James
akatingisha kichwa akiwa haamini. “To James, Jema and family.”
Wote wakanyanyua glasi juu na kugonga kwa pamoja wakirudia, “To James, Jema
and Family.” Wakanywa kwa pamoja na kumpongeza huyo James. Na kuendelea
kufurahia baraka juu ya baraka.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakati wao wanasherehekea, kina Simba wapo msibani. Ni
kama wao walipoteza mtoto mmoja rasmi. Love hatakaa akatoka jela.
Shitaka la mauaji lilikuwa likimuhusu. Ulikuwa wakati wa kuvuna walichopanda
kwa shangwe na wivu.
Kasa alijiweka pembeni kabisa kwenye shitaka la
Kemi. “Nilishamuonya, tena kwa kurudiarudia. Aachane na Jelini, aangalie
maisha yake, lakini hakunisikiliza. Akahangaika na Jelini kama amepagawa. Akahakikisha
amemtoa kwenye maisha yangu kabisa. Napo pia hakutulia akaendelea
kumfuatilia mtu asiye muhusu.”
“Sasa wote tumeishia kupoteza kwa namna moja au
nyingine. Amenipokonya mapenzi ya kweli, yeye mwenyewe amepoteza uhuru
wake, wanae watakua bila mama, bila familia nzuri kama mwanzo. Maana
mumewe hataki hata kumsikia, na anaoa siku za karibuni. Wote tutajifunza
kuishi na matokeo ya mapando ya Kemi.” Kasa alikuwa akimwambia
kila aliyekuwa akimuuliza wakitaka kujua atamsaidiaje Kemi.
~~~~~~~~~~~~~~
Mama yake alipotaka kuingilia, Kelvin akamuonya. “Jihusishe
kwa mbali sana mama. Hapa nchini utapaona pachungu na huko pia unaweza
ukashindwa kuishi. Hii kesi inaangaliwa na macho makali yaliyokusudia kumuona
Kemi analipa uovu wake aliorudia tena na tena kuutenda.”
“Na Kemi nilimuonya
kama hivi ninavyozungumza na wewe. Tena kwa kurudiarudia, asijiingize kwenye vita
ambayo nilimuhakikishia kabisa, hataweza kushinda. Hakunisikiliza mpaka
alipojibana mwenyewe na hakuna jinsi ya kujitoa. Sasa na wewe nakuonya mama.”
“Watanifanya
nini!?” Akauliza kwa jeuri. “Nashauri uache
sasahivi, kabla hujapata majibu ya maswali yako, ukiwa majutoni, ambako
hutaweza kujitoa tena. Kwa sababu nakuhakikishia mama, utajuta na hutatoka.
Jiweke pembeni kama baba. Muombee Kemi, kama ni muujiza, basi Mungu mwenyewe atende.
Ni hilo tu mama yangu. Lasivyo, chochote kibaya ulichowahi kukitenda sirini
hapa duniani, utashangaa kinachimbuliwa na kuja kuwekwa mwanangi
kama alivyofanyiwa Kemi. Hakuna nchi itampokea tena Kemi. Ubaya wake
wote upo kwenye kila ulinzi wa kila nchi hapa duniani. Sasa na wewe
usijiingize.” Kelvin akamuonya.
~~~~~~~~~~~~~~
Colins amefanikiwa kushinda nafsi na kusimamia msimamo
wake, amejifunga kwa Kamila.
Kwa Jelini nako Je?
Usipitwe…
x
0 Comments:
Post a Comment