Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 40. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 40.

Akampigia Ezra, na Junior alikuwepo. “Aisee sikukosea.” “Imekuaje?” “Kama nilivyowaambia. Mimi mwenyewe ameshanibadilikia, na amenikatia simu. Hivi tunavyozungumza sasahivi, yupo njiani anamfuata Jelini.” “Kwamba ameshajua?!” James akacheka kwa masikitiko. “Wewe hutamuweza Colins! Ameshampata, na amesema mpaka akazungumze naye kwanza ndio atanitafuta.” Wote kimya.

“Nashauri mlale tu.” “Unafikiri hatakutafuta tena?” “Ngumu kumtabiri aisee. Lakini najua mimi nilazima atanitafuta. Iwe kwa heri au shari. Atanitafuta tu. Nitamsubiria. Ila kilichonishangaza, hajakuzungumza vibaya kabisa. Kwanza ni kama hajakuzungumza kabisa. Na kwa jinsi ninavyomjua Colins, sio kwa bahati mbaya.”

“Unamaanisha ni jambo zuri au baya?” “Ungekuwa umeshamkera kwa namna yeyoye ile, kwangu angeshasema. Aliposikia tu ni kutoelewana kati yenu, nilidhani angelipuka, ila akanyamaza kabisa. Inamaana wewe ameshakuchunguza, ameridhika na wewe. Huna ubaya naye. Naona mbaya wake ni mimi.”

“Sasa wewe anakulaumu kwa lipi?!” “Utamuweza Colins! Wakati wote mimi ndiye mnyonge wake. Ndiko anakomalizia hasira zake kwangu. Nishamzoea. Na lazima atanitafuta tu ila sijui ni saa ngapi. Nyinyi pumzikeni. Nikisikia chochote nitawaambia. Ila jua kwa vyovyote vile atampata tu, na kuhakikisha yupo salama.”

“Kwanza Jelini anayo pesa na anajipenda, na anampenda sana mwanae. Hawezi kuwepo sehemu mbaya hata kidogo.” “Nakushukuru James. Ila jua simu yangu itabakia kuwa hewani. Muda wowote ule ukinipigia, utanipata.” “Sawa.” Wakaagana.

~~~~~~~~~~~~~~~

Wakati kila mtu anahangaika huku, Jelini na mwanae walikuwa kwenye siku ndefu ya starehe. Hapo walipo walikuwa wamelala yeye na mwanae hawana habari kinachoendelea huko ulimwenguni. Walilala kwenye chumba cha nguvu, aina ya presedential suite, ndani ya hoteli ya kitalii huko Kigamboni, ufukweni. Walishinda na mwanae majini karibia siku nzima. Wakala kwa kusaza mpaka usiku ndio wakarudi chumbani wakaangalia movie mpaka wakapitiwa na usingizi, hawana habari.

Old Is Gold.

Colins mwenyewe alifika kwenye hayo mazingira, akayafananisha na Jelini mpenda vizuri. Hodi ya Colins ndiyo iliyomtoa kwenye usingizi mzito. Akiwa usingizini bila kufikiria akaamka, akajitupia rob nyeupe ya hoteli na kwenda kufungua mlango, akashituka na usingizi kupaa alipoiona sura ya Colins mlangoni, hotelini, tena Bagamoyo!

“Colins!? Au naota!” “Umefungua mlango bila kujua nani anagonga Jelini! Angekuwa mtu mbaya je?” Hapo ndio akili ikawa anamrudia. “Nilikuwa na usingizi mzito.” “Pole kukuamsha.” Akatulia kama anayejaribu kuelewa.

“Naomba kuingia ndani.” “Samahani.” Ndio akampisha kwa haraka kwani hakuwa hata amemkaribisha ndani. Walibaki wamesimama mlangoni. Akaingia.

“Unafanya nini huku!?” “Nimekufuata wewe.” Jelini akakunja uso. “Naomba tuzungumze hapo kwenye baraza, tusimuamshe mtoto.” Akakubali. “Jifunike vizuri hapo nje kutakuwa na baridi, upepo mkali wa baharini.

Mrembo huyo na pesa yake, mbali ya kwamba alichukua presidential suite kama chumba cha raisi fulani hivi au milionea, basi pia alilipia hicho chumba pesa ya ziada ili apate kinachoangalia baharini.

Akajifunika vizuri na kutoka kumfuata Colins, alishatoka kwenye balcon/barazani. Akaenda kukaa pembeni yake. Wakaangaliana, Jelini akakwepesha macho.

“Vipi?” “Safi tu!” Colins akabaki akimwangalia mpaka akainama. “Umefunga simu zako zote Jelini, na nyumbani unatafutwa.” “Nilitaka kutulia peke yangu.” “Kwa nini na wewe ni mtu wa watu?” “Nilikuwa nimekasirika.” Akajibu taratibu tu, Jelini wa deko.

“Nini kimekuudhi?” Akanyamaza. “Eti Jelini?” Akatulia kwa muda kisha akamwambia. “Hongera. Nimesikia umepata mchumba.” Colins akabaki akimwangalia. Akainama tena akijaribu kujifunika vizuri. Colins akamsaidia kumfunika kwa upendo, Jelini akamwangalia wakati akimfunika. “Unampenda?” “Ni msichana mzuri.” “Anaitwa nani?” Hapo anauliza na chozi shavuni. Colins akamuona. Wakati anataka kujifuta akamuwahi kumfuta yeye.

“Anaitwa Kamila. Alinikuta nikiwa mpweke sana. Nilikuwa nimejawa hasira za kukupoteza wewe Jelini. Nilikuwa siwezi kulala. Nafsi yangu ilikuwa imejaa uchungu, nikijua ndio nimekukosa moja kwa moja, na mwanaume mwingine ndio anafanikiwa kukuingiza wewe kanisani.”

“Lakini nikidhani namsaidia yeye, maana nilikutana naye akiwa na hali mbaya sana, nikajikuta najisaidia mwenyewe. Angalau nikatoa mawazo yangu kwangu nikaanza kumsaidia yeye.” Akamsimulia jinsi ilivyokuwa na Kamila kwa ufupi ila kifasaha.

    “Umeelewa?” “Nimeelewa Colins. Na nimefurahi umepata mtu mzuri. Unastahili kuwa nafuraha.” “Na wewe hivyohivyo Jelini. Unastahili kuwa na furaha. Kabla sijampata Kamila, nilikuwa na kazi ya kumchunguza na kumfuatilia kwa karibu sana.” “Ezra!?” Jelini akashangaa sana.

    Kabisa. Sikutaka uingie pabaya. Nilijua itanitesa sana. Halafu pia nia yangu ingine ilikuwa kumtafuta ubaya wake. Lakini Jelini, Ezra ni mtu mzuri.” “Ni mtu mzuri, lakini sidhani kama ananipenda kwa dhati, Colins.” “Mimi nafikiri anakupenda.” “Mtu anayekupenda, hataki kukupoteza. Erza anaonekana anaweza ishi bila mimi na akawa tu sawa. Mpaka nimefikiria mwanzo wetu, naanza kutilia mashaka.” Akaendelea kulalamika.

    "Na mimi Ezra alinikuta na hali inayofanana kama aliyokukuta nayo Kamila. Nilikuwa mpweke na nilikusubiri mpaka nikawa nimekukatia tamaa Colins. Nahisi nilimkubali kwa haraka nikikimbia upweke, bila kumchunguza kama kweli ananipenda kwa dhati.”

    “Nilimkubali kwa sifa nzuri tu nilizokuwa nikizisikia kwa watu kama hivyo wewe unavyomsema. Ila yeye kama yeye, kwangu, sidhani kama ananipenda mimi kama Jelini. Namuhisi mimi kwake ni kama moja ya mipango yake, aliyopanga kutimiza maishani.”

    “Inamaana kama sio mimi, ingekuwa mwanamke mwingine, angeoa, ikawa basi. Mimi hivyo sitaki Colins. Nataka kuishia na mtu ambaye ninaleta maana kwake, mimi kama Jelini, sio kama mwanamke yeyote yule wakuoa. Umenielewa? ”  “Nakuelewa. Niambie jana ilikuaje?” Akanyamaza.

    “Niambie, usinifiche.” Akamsimulia ila sababu ikawa kama ya mafumbo, asiseme ni wivu wakusikia anamchumbia Kamila. Akamfumba asijue kama James alishamwambia chanzo ni nini. Colins akabaki kusikiliza akijidai hajui sababu, ila akitaka kujua walipokuwa faragha Ezra alizungumza nini cha kumkera. Naye hakumficha. Akawa muwazi kwake.

    “Hudhani kama ni wivu na hasira?” “Kasa alikuwa na wivu na wewe kama mwehu! Alikuwa akianza kukulalamikia mpaka anabadilika rangi, lakini hakuwahi hata kuhisi tunaweza kuja kuachana. Shida yake ilikuwa akitaka nimuhakikishie anabakia yeye tu mwenyewe moyoni mwangu, wewe haupo.”

    “Ulivyomuhakikishia umeshanitoa moyoni, aliridhika?” Akachomekea kwa wivu tu. Wala halikuwa swali la msingi. “Ndicho ninachokwambia. Japokuwa sikuwahi kumuhakikishia alichokuwa akikitaka, lakini Kasa alibakia akinitaka tu. Lakini yeye Ezra anaonekana kama hana shida na mimi! Sasa hapo tutakuwa na ndoa ya namna gani?”

    “Cha kwanza nataka kukuhakikishia, Kasa si hata robo ya Ezra.” Jelini akamwangalia amekunja uso. “Ezra anakupenda Jelini, ndio maana unaona na mimi akili imetulia, nimeweza hata fikiria mwanamke mwingine.” “Unajuaje!?”     “Tafadhali niamini tu. Ila jua Ezra anakupenda SANA. Hilo sina wasiwasi nalo hata kidogo. Nafikiri wivu na hasira, vimemfanya kushindwa kuzungumza na wewe, na pia alifanya haraka. Bad timing. Aliwahi sana kuzungumza na wewe. Angejipa muda baada ya pale. Hata kesho yake, nakuhakikishia asingezungumza hivyo. Alizungumza akiwa na hasira. Na najua kwa hakika kwa hili amejifunza.” Jelini akanyamaza.

    “Kingine cha pili, Jelini wewe una upendo MWINGI wa kukutosha wewe na yeye.” Ikamgusa sana Jelini. “Kujibu swali lako la kuwa mtakuwa na ndoa ya namna gani. Sina wasiwasi ukiolewa na mtu kama Ezra, upendo wako tu wewe mwenyewe, unatosha kumsitiri na yeye.” Hapo akamgusa zaidi mpaka akanywea, hasira zikaanza kupungua.

    “Unakumbuka uliniambia tujifunze kutoka kwenye makosa tuliyofanya mimi na wewe, na kusabisha mpaka leo hatupo pamoja?” Hapo akapandisha miguu kabisa juu ya kiti walichokuwa wamekalia. Cha miti ila kimewekwa mito mizuri, muundo wa ufukweni.

    Akajikusanya hapo kitini, akiwa amejivuta mwisho kabisa, akajiinamia kwa majonzi. “Unakumbuka?” Hakujibu kabisa. “Leo hatupo pamoja. Tumepoteza penzi la dhati kati yetu sababu ya kukosea. Tafadhali usikosee tena. Nakuahidi binafsi nitabadilika, nitafanya vizuri, na wewe naomba niahidi utafanya vizuri zaidi kwa sababu umepata mwanaume sahihi, Jelini. Ingekuwa ni mjinga mwingine, hakika nisingekwambia hivi. Lakini kwa Ezra, umepatia.”

“Unafikiri hivyo?!” “Nina uhakika wa asilimia zote. Nakuhakikishia Jelini, kama ingekuwa ni mtu mwingine, hakika usingenisikia nikikushauri hivi. Wewe unanijua.” Jelini akacheka akikumbuka walivyosumbuana na Kasa.

    “Colins!” “Mimi sipendi ujinga na sitaki mtu akuonee. Ila kwa Ezra, mimi mwenyewe nina muheshimu. Ametulia sana. Hata mwanamke aweje, hashawishiki. Na hilo nina uhakika nalo.” “Colins!?” Akamshangaza sana. Maana aliongea kama ambaye ameshamjaribu, na Ezra akashinda.

    Nakuhakikishia tena. Si muhuni hata wa vifichoni asipokuwa na yule mwenzie Junior. Yaani yeye mwenyewe ni MWAMINIFU. Anakutambua na kukutambulisha hata sehemu ambazo hazina maana na wala hawakujui au haiitajiki kujitambulisha kama anamchumba. Lakini kwake yeye anataka ijulikane anaye mwanamke wake, ambaye anampenda sana, Jelini.” Ikamgusa Jelini.

    “Halafu cha mwisho, ANAKUHITAJI sana. Najua unajua kama ni yatima.” Jelini akazidi kushangazwa. “Colins! Kwamba ndio unamfahamu kwa undani hivyo!” “Nisinge mzungumzia hapa, kama sina uhakika naye. Ezra anakuhitaji Jelini. Kuna sehemu amekuzungumzia. Nimesoma. Ni kwenye e-diary yake, mpaka mimi nilishangaa asiee!” “Amesema nini?” Akataka kujua.

    “Naomba nisikwambie kwa undani, pengine ni surprise amekuandalia siku moja uje usome, lakini yule jamaa anakupenda Jelini. Japokuwa namuonea wivu kwamba yeye ndio anaishia na wewe, lakini najua anastahili.” “Kweli Colins!?” “Kabisa.” Akamuhakikishia kisha akaendelea.

    “Acha nikwambie kitu kikubwa kilichonigusa kwa Kamila, ila nataka ujifunze na wewe, sio kukuumiza.” “Unaniringishia!” “Hata kidogo. Yeye si wewe, na hatakaa kuwa wewe. Hilo analijua. Nakupenda Jelini. Mungu anajua ni kiasi gani nakupenda. Unayo sehemu ya pekee moyoni mwangu ndio maana nakutakia mema. Nataka uishie pazuri ndio furaha yangu itakamilika.”

“Na nina uhakika Ezra atakupa hata yale ambayo mimi nimeshindwa kukupa. Nina uhakika. Na hata Kamila nimemwambia.” “Huyo msichana wako!?” “Kamila anajua you are a love of my life, Jelini. Anajua nakupenda.” Ikamgusa huyo Jelini mpenda kupendwa! Hapo roho shwari. Akaanza kufurahia.

    “Nimemwambia Kamila, umepata mwanaume wa uhakika. Kwa Ezra, umepatia Jelini. Usijitilie shaka. Ulikuwa sahihi, na nakupongeza. Yule atatimiza haja zako zote, na kukufuta machozi yote sisi wanaume tuliyo kusababishia. Umepatia kwa Ezra.” “Nashukuru Colins. Umejifunza nini kwa Kamila wako?” Colins akacheka.

    Akamsimulia kwa kifupi mahusiano ya Kamila na Mike mpaka Jelini akashangaa na kuumia. “Mimi nilikukatia tamaa mapema Colins!” “Acha nikutetee, maana na mimi nililifikiria hilo. Tofauti yako na Kamila juu yangu na Mike ni hii. Kamila hakuwa akimuona Mike, na waliachana pazuri. Mimi nilikusumbua sana kwenye maswala yangu na Love, na wazazi wangu wakichangia, kisha ukathibitisha nikiishi na Love. Hata kuho kunisubiri kwa muda ule, inathibitisha ulinipenda kwa dhati.” “Nakupenda Colins!” Akalalamika alivyosema ‘ulinipenda’.

    “Najua Jelini na ndio maana unaniona sasahivi nipo hapa. Ingekuwa mtu mwingine, sasahivi, nisingemuacha Kamila amelala ndani na kukufata huku.” “Pole, na samahani.” “Usijali. Nataka uwe na furaha Jelini. Na kama ulivyoniambia mimi, hata kama ukifika sehemu hujisikii, fanya kwa ajili yangu.” Akainama.

“Mimi hilo limenisaidia sana. Japokuwa nilikuwa na Kamila, sikuchukua hatua mpaka uliponiambia hivyo. Ikawa kama umenipa ruhusa au nimepokea baraka zako za kuendelea, ndio nikajisikia huru. Nikaweza kuchukua hatua kwa Kamila. Na wewe naomba iwe hivyohivyo.”

    “Huo upendo mwingi ulio nao, tafadhali utumie hata kipindi ambacho hujisikii. Ukifanya hivyo ujue utanisaidia na mimi maisha yangu yatakuwa rahisi kwa sababu unajua sitakuwa mbali na wewe. Sawa?” Jelini akatulia.

    “Jelini?” “Nimekuelewa Coly, na asante kuzungumza na mimi. Nilikuwa nina hali mbaya. Mbaya sana, nikijilaumu. Lakini umenisaidia. Asante.” “Karibu.” Wakatulia kidogo kila mtu akiwaza lake. Maana hapo ndio kama wanaagana rasmi.

    “Najua Jeremy amelala. Huwezi kumuamsha. Lakini si sawa kuendelea kuishi huku hotelini. Kila mtu anawasiwasi.” “Kesho nitarudi. Ila naomba leo usiku nipumzike tu. Waache usiwaambie nilipo ili nipumzike vizuri. Hata hivyo nimekua busy, nimechoka. Nilihitaji haya mapumziko na mwanangu.”

    “Nimekuelewa. Basi nikuache upumzike, nakutakia kila la kheri Jelini. Unastahili, kwa sababu wewe ni mtu mzuri. Na usisahau, ukihisi tu upendo unapungua kati yenu, jua wewe peke yako, unao upendo mwingi sana wa kufunika ndoa yenu. Sina mashaka juu ya hilo.” Jelini akainama akifikiria.

    “Naomba nikukumbatie kwa mara ya mwisho nikikuaga. Nakuahidi nitakuwa na heshima kwa Ezra na Kamila.” Akajisogeza karibu yake. Kwa mara nyingine tena Jelini akarudi mikononi kwa Colins. Akajipanga kama kawaida yake. Na Colins akamkumbati vizuri kama anavyopendaga Jelini. Akaenea mikononi.

    Bwana hisia zilizokuwa zikitembea hapo! Ilihitajika tunda la kiasi na kiwango cha juu sana cha commitment, kuachiana. Wakatulia kwa muda, mwishoe wakaachiana kabla hawajapitiliza.

    Akamsindikiza mpaka mlangoni. “Tafadhali usifungue tena mlango bila kujua ni nani anagonga.” “Nitafanya hivyo Colins. Na wewe kila la kheri.” Wakabaki mlangoni kwa muda wote wamepotelea mawazoni.

    Jelini amebaki amesimama mlangoni ameinama akiwaza na Colins ameshikilia kitasa kwa nje na yeye amepotelea mawazoni. Walijua ndio kutengana rasmi, ila kama hawaamini! Wakatulia hapo, kimya.

    Akamuona Jelini anamvuta mkono wa kulia taratibu, asijue anataka kufanya nini. Taratibu akanyoosha kiganja chake, kama kukunjua vidole, Colins ametulia tu akimwangalia anachotaka kufanya na huo mkono wake. Kisha akaunyanyua ule mkono na kumuwekea kwenye moyo wake. Kwa sekunde kadhaa bado Colins hakuwa ameelewa mpaka alipoanza kusikia/kuhisi mapigo yake mwenyewe. Kadiri moyo wake ulivyozidi kudunda, ndivyo ahadi ya Jelini ikazidi kujirudia kana kwamba ndio ana muahidi hapo.

    Jelini alipomuona anabadilika sura, akajua amekumbuka. Akajirudisha nyuma kama aliyefanikiwa kufikisha ujumbe wake. Colins alishindwa kujiachia. Akajihisi simanzi ya namna yake, akikumbuka hiyo ahadi ambavyo haikuwahi kufa hata alipochanganywa na Love pamoja na Kemi. Ilibaki imeandikwa moyoni mwake, akimtafuta aliyempa huku hajitambui.

     Ila ikaleta furaha mpya, kuona japokuwa kuna Ezra, bado ahadi ipo vilevile! Akatulia akiyatafakari yale maneno ambayo ni ahadi aliyopewa, hapo mbele ya Jelini. “Kila unapoyasikia hayo mapigo yako ya moyo. Popote ulipo. Muda wowote, hata kama mimi hunioni, ujue yupo Jelini anayekupenda kwa moyo wake wote, mpaka niondoke hapa duniani. Hakuna ulimwengu utakaokuwepo wewe, nisikupende Colins. Ujue nitakupenda mpaka kifo chako.” Mpaka akajihisi machozi kumtoka mbele ya huyo mrembo. Ila akajikaza.

   “Unakumbuka na mimi ahadi yangu kwako?” Akamuuliza taratibu na kumshika mikono yote miwili. Jelini akajifuta machozi kwa mabega. Akitingisha kichwa taratibu kukubali. Sasa yeye akachukua mkono wa Jelini na kuuweka kifuani kwake.

    Jelini akaanza kusikia mapigo ya moyo ya Colins. Mwili mzima unasisimkwa. Akamwangalia. Akiwa amemshikilia mkono wake kifuani kwake, na yeye akasema, Maadamu hayo mapigo ya moyo yanaendelea kudunda kwenye huu mwili, ujue unayo nafasi yako hapo daima. Na itabaki hivyo mpaka uje uhakikishe hakuna unachosikia kwenye huu moyo wangu, ndio ujue umepoteza mtu anayekupenda sana hapa duniani. Usije sahau hilo. Sawa?” Japokuwa safari hii ahadi yake aliibadilisha kidogo, Jelini alielewa kwa sababu yupo Kamila tayari kwenye maisha yake, lakini akaridhika na kutingisha kichwa kukubali. Colins akaridhika, akambusu kichwani na kuondoka kwa haraka kabla hawajaharibu.

Majibu Kwa Ezra.

Alipofika tu kwenye gari lake akamtumia ujumbe Ezra. ‘Jelini anaasili ya unyenyekevu. Rahisi kumpuuza na kumchukulia kawaida akiwa kwenye maisha yako. Unaweza jisahau ukadhani atabakia kuwa wako daima. Lakini nakuhakikishia, hutaki kupita tuliko pita sisi, kupitia ile hali ya kuondoka kwake kwenye maisha yako. Ni ngumu kuliko nitakavyokwambia. Ni pengo ambalo ni yeye mwenyewe anaweza liziba. Ongeza umakini kwake. Na jua kwa hakika, sipo mbali na yeye. Nakuona.’ Ujumbe ukaishia hapo. Ezra alishituka kupata huo ujumbe! Alijua fika ni yeye tu. Wakajaribu kumpigia, lakini ni kama simu zao ziligonga mwamba. Hawakumpata.

Kwa James.

    Kisha akampigia James, naye akapokea kwa haraka sana. “Tafadhali ongeza umakini James. Tafadhali sana.” “Sawa Colins. Lakini kumbuka ninatingwa na majukumu mengi ndugu yangu. Inakuwa…” “Kwa hiyo unachotaka kuniambia, Jelini, mtu rahisi sana kuishi naye, wewe anakushinda kumuangalia?!” Akauliza kwa ukali.

    “Basi Colins. Nikuahidi nitaongeza umakini. Umekutaje huko?” “Atarudi. Usiku mwema.” “Colins! Colin! Usikate.” “Unanichanganya tu James.” “Sawa. Anarudi lini?” “Acha kuniuliza maswali kama ambaye unajali sana kumbe shida yako ni usambaze taarifa.” “Najali.”

    “Kama unajali, ungejua alipo.” “Unatafuta kunilaumu bure wakati unajua fika ulichofanya kwenye access za Jelini. Unataka lawama tu.” “Jelini yupo salama na mtoto. Atarudi. Mpeni nafasi.” “Nipe basi na mimi access zake ili …” Akasikia simu imekatwa. Akaanza kucheka. “Colins!” Akaishia kusema tu hivyo kwa masikitiko.

Atafutaye Asiyechoka.

    Asubuhi kabla ya ibada akampigia simu mama Jema. “Samahani kukusumbua mama yangu. Kwanza nataka kujua umeamkaje na kutaka kujua kama umemsikia Jelini.” “Mpaka sasa sijamsikia.” “Samahani sana mama yangu kwa matatizo niliyosababisha. Ila jua simdharau Jelini. Nampenda sana. Ila nilizungumza nikiwa na hasira. Sikuwa na nia mbaya.”

    “Naomba ongeza umakini Ezra. Tafadhali usimchanganye Jelini. Kama umeshamfikiria, ukaona hutamuweza, bora jiachie tu, mimi niendelee naye taratibu.  Na wala hatutakosana. Nitaelewa tu maana na mimi namfahamu Jelini na mapungufu yake. Ila tatizo, Jelini ameshika hatima ya Jeremy ambayo sitaki mtu amyumbishe. Katika hilo kila mtu ataniona mbaya. Sitatania. Vurugu yako ile ya jana tu, sijui Jeremy alipo. Sijui anarudishwa lini! Hapana kwakweli.” Ezra akabakia na makosa yote yeye!

    “Nimejifunza mama yangu. Na nakuahidi hiki kilichotokea jana, hakitarudia tena. Nitaongeza umakini.” “Uwe na siku njema.” Simu ikakatwa. Sasa sijui kondoo huyo siku hiyo ya jumapili atakwenda tena kanisani au ndio amezira na kanisa! Akawaza Ezra asijue anawaambia nini wazazi wake.

Mshika Mawili…

    Kwa sababu ya kubadilika kwa ratiba ya kazi ya baba yake siku ya jumamosi, na pia mtu aliyetaka awapambie sehemu atakayo propose kuwa na tenda nyingi siku ya hiyo wakakubaliana swala la kumchumbia Kamila iwe siku ya jumapili, wakitoka kanisani. Walikusudia kiwe kitu kidogo ila kizuri chakuvutia.

Jumapili.

    Sasa Colins sababu ya safari ya Bagamoyo, akarudi nyumbani kwa kuchelewa, kuja kupata usingizi karibia kuna pambazuka. Watu wote wakawa wako tayari, yeye hajatoka chumbani na si kawaida yake. Wakabaki wapo sebuleni wanamsubiria huku macho kwenye saa, muda wa kanisani unakaribia haswa. Ila Kamila bado hakuwa akijua kama siku hiyo anachumbiwa.

    Mzee akaona aende akamgongee. Akagonga, mwishoe akafungua mlango. Colins amelala nusu mfu, akamuita akiwa ameshikilia mlango kama mwenye haraka, hataki kuingia. “Wewe vipi?! Unakaribia kuharibu ratiba nzima leo!” Colins akajaribu kufikiria akiwa ndio anatoka usingizini. “Ratiba!?” “Colins! Tafadhali amka na ukumbuke leo ni jumapili.” Akakaa ndio akili ikamrudia.

    “Naombeni mtangulie, nitawafuata. Nimelala muda mbaya.” “Nilisikia mageti yakifunguliwa usiku usiku, ulikwenda wapi?” Mzee akauliza akiwa bado mlangoni. “Nilitoka. Nyinyi tangulieni, naoga mara moja nakuja na Kamila.” “Unaharibu Colins. Hivyo sivyo tulivyopanga.”

    “Baba! Nimekwambia naoga mara moja nakuja. Mbona kama unataka kuleta tatizo ambalo halipo?” “Kwani ulipata dharula ya hospitalini?” “Hapana.” “Sasa kwa nini uliingiza ratiba unayojua itaharibu mpango mzima wa leo!? Ulikwenda wapi?” Mzee akazidi kung’ang’ania.

    “Wewe ndio unazidi kunichelewesha. Maswali yote hayo ya nini?” “Kwa sababu unataka kuharibu ratiba nzima tuliyopanga kwa makubaliano sisi wote hapa! Nakuuliza ulikwenda wapi usiku usiku angali ukijua wazi leo tunamiahadi ya kuanzia asubuhi, halafu unashindwa kujibu.” “James alinipigia nikiwa nimelala, akaniomba msaada ndio nikaenda kumsaidia.”

    “James huyu ndiye yuleyule shemeji yake Jelini?!” Kamila huko sebuleni roho ikapasuka kusikia Jelini, tena Colins alitoka! Akaweka masikio vizuri. “Kwani wewe unajua nawajua kina James wangapi?” “James ninayemjua mimi ndiye aliyekuja hapa mara ya mwisho kutupiga marufuku, hawatutaki tena. Tusiwasogelee, lasivyo tutaona mji mchungu. Sisi tukajiweka mbali, iweje leo ndio aje kutuingilia?”

    “Kama utakumbuka sawasawa, alikuja hapa akiwa ametumwa na mama mkwe wake. Si maneno yake wala ya Jelini. Nyinyi wazazi ndio mnaharaka ya kusema kwa niaba yetu bila kujua kile sisi tunataka. Kazi yenu ni kurushiana maneno ya kuumizana, bila kujua ni nini sisi tunataka.” “Haya, wewe unataka nini?”

    “Baba, wewe ndiye unayetaka kuharibu siku ya leo. Mimi kuitwa na James sidhani kama ni tatizo. Sijagombana na James wala Jelini. Nyinyi wazazi ndio mnamatatizo yenu, na sitaweza kuwasaidia. Kwa hiyo kama hutajali, naomba nipishe nioge kwa haraka, nitawawahi kanisani.” Mzee akatoka kwa hasira. “Twendeni.” Walioweza mfuata, mkewe na Connie wakamfuata. Kamila akabaki amekaa kama amegongelewa misumari. Mwili umekufa ganzi.

~~~~~~~~~~~~~~~

Colins hakuchukua muda mrefu akaoga kwa haraka, alishajua kitu cha kuvaa siku hiyo. Kwa hiyo hakuchukua muda mrefu akatoka na kumkuta Kamila amejiinamia kochini.

Maji Yashatibuka.

    Akamsogelea. “Samahani nimechelewa. Twende.” Kamila akamwangalia. “Naomba ukae tuzungumze.” “Kwa nini tusizungumze njiani ili tuwahi kanisani?” “Tumeshachelewa, na naamini haitachukua muda mrefu. Vinginevyo tuzungumze mkirudi kutoka kanisani.” Colins akashituka. “Kwamba wewe huendi tena kanisani?” Akabaki akimwangalia, Colins akaona akae tu.

    “Ulitaka kuniuliza nini?” “Naomba usinifiche Colins. Niambie ukweli. Jana usiku ulikwenda wapi?” “Kamila!” “Sio kawaida yangu, ila sijui kwa nini moyoni nimepatwa wasiwasi, nataka kujua. Kama unadhania nina haki yakujua, tafadhali niambie. Kama unadhania sio lazima, basi. Nikuache uwahi tu kanisani.” “Huna haja ya kuwa na wasiwasi. Kila kitu kipo sawa.” Akamuona anachukua pochi yake, akasimama.

    “Unakwenda wapi sasa!?” “Naingia chumbani kwangu. Uwe na ibada njema.” Akaelekea chumbani kwake. Akafikiria hapo kochini kwa haraka, akaona amfuate huko chumbani.

    “Nisikilize Kamila. Mimi ni mtaalamu wa mambo ya kompyuta. Jelini ni kama aliondoka nyumbani kwao bila ya kuaga, ndio kila mtu akawa na wasiwasi, James akanipigia kuomba msaada wa kujua alipo.” Kamila kimya akimsikiliza kwa makini lakini mapigo ya moyo yalishaanza kwenda kasi.

    “Kwa hiyo ndio hivyo.” “Sijaelewa.” “Ilibidi kuwasaidia.” “Kujua alipo au uliamua kwenda kabisa kumfuata huko alipo, baada ya kujua alipo?” Kamila akauliza swali la moja kwa moja. “Nilipojua alipo, ilibidi kumfuata kujua ni kwa nini ameondoka bila ya kuaga.” “Kwa nini shemeji yake ashindwe kwenda yeye, ukaenda wewe?!” Akameza mate akijua amekamatwa.

    Ila akajikaza. Akafikiria kwa haraka akapata jibu. “Cha kwanza jua hapo ni kama nilivunja sheria. Ni kosa.” Akajitia ubaya kwa makusudi. “Ni kama nilivuka mipaka ya mtu ambaye ni Jelini. Nimemuingilia na kujua alipo bila idhini yake. Kisheria pekee ni kosa. Halafu pili, sikujua ni kwa nini alifunga simu, ili wasimfikie. Sikutaka iwe kama mimi ndio namuuza.” “Mmmh!” Kamila akaguna.

“Alikuwa kwenye shida Kamila, ikabidi kwenda kumsaidia.” “Wapi?” Kamila akauliza taratibu tu.  Sasa hapo anajibuje kwa mfano!? Akaona amzuge. “Inasaidia nini Kamila!?” Hakumjibu akaendelea kuvua viatu. Akajua amekusudia kujua, amemgomea kwa vitendo.

    “Alikuwa Bagamoyo.” Kamila akageuka kwa mshangao. “Kwamba ulijua yupo Bagamoyo, ukaondoka usiku huo, mpaka huko, kwenda kujua anaendeleaje!?” “Kila mtu nyumbani kwao alikuwa na wasiwasi! Na nakuhakikishia hakuna jambo baya lililotokea kati yetu huko nilikomfuata.” Kamila akakaa.

    “Mimi wala sikulaumu Colins. Ila nafikiria tu.” “Unafikiria nini?” “Ule uzito na umuhimu wa Jelini kwako. Sidhani kama kuna mtu atakuja kupata hata nusu yake, kutoka kwenye moyo wako.” “Kamila!” “Hakika tena. Fikiria mipango tuliyokuwa tumepanga mimi na wewe leo. Twende kanisani, tukale, wazazi wakiondoka, tupate muda wetu wa pamoja, niogelee, kisha usiku twende movie. Lakini hayo yote umeyatupilia mbali mara baada ya kusikia Jelini, aliye na mchumba wake, yupo matatizoni.” “Bado tunaweza kufanya yote tuliyopanga. Tafadhali usikasirike Kamila. Hakuna baya limetokea kati yetu.”

    “Mimi nakuamini Colins. Nafikiria tu, ule umuhimu wake kwako. Uliweza toka usiku mwingi hivyo, ukaniacha mimi hapa ndani, ukishindwa kumuamini hata mchumba wa Jelini mwenyewe na Jelini! Au hata shemeji yake, aliyekutafuta kukuomba msaada, umeshindwa kumwamini na Jelini!” Colins hoi.

    “Ndio namfikiria mkeo na watoto wako. Najiuliza, ndio iwe Jelini anakuhitaji, mkeo yupo ndani, pengine ni mgonjwa. Si utamuacha ndani, ukimbilie kwa Jelini!” “Hunitendei haki Kamila!” “Narudia tena Colins, sikulaumu. Kama Mike angekuwa yupo mahali ananihitaji, najihisi na mimi ningefanya hivyohivyo kama wewe. Nisingefikiria mara mbili. Ningeendesha usiku kuchwa kumfuata nikajue ni kwa nini amekasirika.” Colins akakaa kitandani, hoi.

    “Nafikiri upo sahihi Colins, bado haupo tayari na mtu mwingine maishani. Kuanzisha lolote na mwanamke yeyote yule, si sawa kwako na kwa huyo msichana mwingine. Ni kumchanganya tu bila sababu. Nyinyi watu mnapendana, na mnanafasi ya kuwa pamoja. Jelini hajaolewa.” “Anaolewa jumamosi, sipo kwenye maisha ya Jelini kabisa! Ilikuwa ni kumsaidia tu!”

“Colins, tafadhali tambua mimi ni mtu mzima. Najua umaana na uthamani wa mapenzi. Usizungumze na mimi kama mpita njia.” “Sifanyi hivyo Kamila!” “Ndicho unachokifanya. Unanipa majibu ya jumla jumla, na unazungumza na mimi kama mtu ambaye sijitambui!”

    “Kwani kupangwa siku ya harusi ndio kifo? Useme ni kama hivi Mike ameondoka hapa duniani, hatarudi tena? Popote Jelini alipo, unaweza mfikia kama ulivyofanya jana usiku! Na nyinyi wawili mnapendana. Niambie ukweli Colins, kinachokuzuia ni nini?” Alibaki kama bubu akishindwa hata kumdanganya kwamba, ‘ni wewe!’ Kamila akamtizama pale alipokuwa ameinama, kimya.

    Akapata jibu lake. Akabadili nguo hapohapo Colins ameinama, mawazo mbali. “Namtumia ujumbe mama na Mike. Wakitoka kanisani badala ya kwenda hotelini, warudi nyumbani. Naandaa chakula.” Akanyanyua kichwa na kushangaa amebadili kabisa. “Tafadhali twende wote kanisani.” “Mimi leo ibada yangu itakuwa jikoni. Wewe nenda, usichelewe.” Kamila akatoka na kumuacha hapo chumbani. Akajua kweli bahari imeshatibuka.

Njia Panda.

    Maneno ya Kamila yakaanza sasa kujirudia akilini kwa Colins na kuanza kupata nafasi nafsi kwake, kiasi cha kumuweka njia panda ambapo hakuwepo kabisa mwanzo.

    Ni kweli bado Jelini hajaolewa! “Kamila yupo sahihi kama Ezra! Hatujachelewa.” Wazo walilopanda kwa zilipendwa hao, safari hii likaanza kuchepua na kwa Colins kama uyoga.

     Mbaya zaidi bado alimkuta Jelini na hisia zote. “Amekiri bado ananipenda.” Akarudisha kumbukumbu kwenye hisia zile alizozipata alipokuwa mikononi mwake wakiagana. Harufu ya Jelini ikawa bayana kana kwamba ndio yupo hapo. Pumzi tulivu za Jelini shingoni kwake alipokuwa amemkumbatia akazisikia kana kwamba ndio yupo hapo. Jinsi alivyokuwa ametulia! Akajishika shingoni taratibu kama kusikilizia ile raha aliyopata wakati Jelini yupo mikononi mwake.

    Lakini akajisuta na ushauri aliompa juu ya Ezra. Akajihisi safari hii amejifungia mwenyewe mlango. Lakini kumbukumbu zikamrudisha tena, japokuwa alimshawishi arudi kwa Ezra lakini bado ilikuwa ngumu hata kwa Jelini kumuaga pale mlangoni.

    Jinsi alivyomkumbusha ile ahadi yao kwa kumshika moyoni. Na yeye hisia alizopata pale aliposhikwa na Jelini moyoni! Mpaka Colins akasisimkwa tena! “Haiwezekani watu wawili warudie jambo hilohilo! Pengine kweli hatujachelewa!” Akazidi kuwaza hapo chumbani kwa Kamila, peke yake.

~~~~~~~~~~~~~~~

Maneno hujenga! Kila unalotamka, aidha kwa hasira au kwa furaha jua ni UJENZI unaoanzisha kwa uliyemtamkia.

Kumbuka sisi ni miungu wadogo. Tunayo pumzi ya Mungu ndani yetu. Aliumba vyooote kwa kutamka tu.

Kuwa MAKINI sana na KILA neno unalotamka kwa yeyote yule, hata mtoto mdogo. Unajenga na kuumba kwenye kila kinachosikia.

Sasa Ni nini Kitaendelea?

Nani anaishia na nani?

Usipitwe….


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment