Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 39. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 39.

Junior akamuona amepotelea kabisa mawazoni. “Ezra?” Ikabidi amrudishe pale kimawazo. “Ninachojua, siwezi ishi bila Jelini. Nampenda.” “Utafanyaje?” “Kingine nilicho na uhakika nacho, alinichagua mimi dhidi ya Colins. Kama atakubali yaishe tuendelee, nitajifunza kuishi na hiyo hali.”

“Unauhakika!?” “Acha nikwambie ukweli Junior. Jinsi ninavyokuwa na Jelini, hutahisi hata kama anamjua Colins. Hutamsikia hata akiropoka juu yake. Sijawahi kuta jumbe zake tena. Na nimeshakwambia Jelini hajui kuficha simu zake. Namba zake za siri zote ninazo. Akibadili ananiambia bila shida, na hajawahi kunizuia simu zake hata mara moja.”

“Nina uhuru na simu zake kama zangu. Sijawahi kuta jumbe yeyote ya ajabu yakumtilia mashaka. Zaidi ya ile simu yake ya biashara ndio utakuta kuna wanao mtongoza tu. Lakini hajawahi nitia wasiwasi wa kumshuku. Nafikiri ndio maana jana nilipaniki. Sikutegemea. Nilijua mambo ya Colins yaliisha kabisa.”

“Kwa hiyo kwa kujibu swali lako, nina uhakika. Jelini kama Jelini kwangu ni kweli ananipenda na kuniheshimu sana. Hatuna shida, na wala huyo Colins hajamfanya kwangu akawa tishio. Wakati wote tukiwa pamoja, tunakuwa na wakati mzuri. Sijawahi kuwa na aina ya utulivu pamoja na furaha maishani kama ninapokuwa na Jelini. Aisee nampenda Jelini.”

“Na acha nikwambie ukweli mwingine. Tulikuwa tukitizamia fungate yetu kwa hamu sana. SANA. Wote tulikuwa tukiutizamia muda wetu tutakaoupata wa faragha wa pamoja. Usiku wa kutoagana. Kuamka pembeni ya kila mmoja wetu.”

“Sijui kama nitakuja shika mwanamke tena, nikaridhika kama nilivyomshika Jelini, Junior. Anautulivu fulani hivi mkononi! Acha kaka. Nitachanganyikiwa nisipomuoa Jelini, jumamosi. Siwezi kuja anza na mwanamke mwingine. Hatakua Jelini, hataweza kuwa Jelini.” “Basi tuombe kisha tuanze kumsaka. Usiku huuhuu mpaka kieleweke. Tujue moja.” Wawili hao wakaanza kuomba. Safari hii hata Erza mwenyewe aliweza kuomba. Wakamuombea ulinzi huko alipo na mtoto, kisha amani.

“Tutampatia wapi na simu zote kafunga?” “James anaweza tusaidia. Tumpigie yeye tumuombe atusaidie kuangalia kwenye hiyo mitandao yao, atusaidie kujua alipo.” Wazo la Junior likawa sahihi, wakampigia James.

Kwa James.

“Kwanza niombe msamaha kwa nililoanzisha. Sikukusudia kuleta vurugu ya namna hii.” “Hapana James. Sio kosa lako. Mimi ndio nimekosea. Lakini naomba msaada wako. Kujua alipo ili nikazungumze naye. Usiku huu usipite hivihivi sijazungumza naye.” “Tumetoka sasahivi kuzungumza na mama. Anawasiwasi sana juu ya Jelini kuondoka na mtoto. Lakini tumemtuliza, nashauri na wewe mpe muda, atarudi tu. Hawezi kukaa muda mrefu na mtoto wa bibi.”

“Siwezi nikamuacha aendelee kuwa kwenye hali hiyo, James! Tafadhali nisaidie.” Akamsikia kama anacheka kwa masikitiko. “Acha nikwambie ukweli. Hilo unaloniomba, nimeshalifanya. Nimekata tu simu ya mama, nikaamua kujua alipo ili angalau kupunguza wasiwasi. Lakini nimekuta restriction hizo!” “Unamaanisha nini? Mbona kama kuna jambo unashindwa kuniambia?”

Akatulia kidogo kama anayefikiria jinsi ya kuzungumza. “Nisaidie James ndugu yangu.” “Sitaki kuharibu zaidi.” “Si kwangu. Nimejifunza kutokana na makosa. Na naahidi mimi mwenyewe nitatafuta nafasi yangu ndani ya moyo wa Jelini, hata kama kumejaa Colins. Naahidi nitatafuta bila kumuumiza.”

“Na hicho ndicho pia nilitaka kukwambia Ezra. Colins na Jelini ni penzi ambalo walikuwa wakilitizamia kwa muda mrefu sana, wakiamini wao wawili wakifanikiwa kuja kuwa pamoja, furaha yao itakamilika. Walishapanga mpaka watoto watakao kuja zaa pamoja. Na Colins ndio mwanaume wa kwanza kufanikiwa kuingia moyoni kwa Jelini. Ni nini nataka kusema?”

“Baada ya Colins, au katikati yao alishapita Kasa. Nafikiri unamfahamu.” “Namkumbuka.” “Basi Kasa ni ndoto ya mwanamke yeyote atakayefanikiwa kumpata na Kasa akimpenda. Na alimpenda Jelini karibia kurukwa na akili. Kwanza tunahisi alirukwa na akili kwa ajili ya Jelini. Hata angemuomba damu yake, nahisi kwa Jelini angempa bila maswali.”

“Lakini katika yote, Colins hakuwahi toka moyoni kwa Jelini. Na haikuwa siri. Kasa alipolijua hilo, kuwa japokuwa Jelini anakila kitu, na angempa chochote anachotaka, maana Kasa anapesa chafu isiyo na matumizi. Mimi mchaga nikikwambia anayo pesa, niamini anayo pesa, maana anamiliki mpaka migodi.” “Kweli anayo pesa.” Mpaka Junior akaafiki.

“Ewaaah! Hapo unapoishia kuelewa, ndio anzia pesa ya Kasa. Akajaribu kuwa akimpa mahela Jelini ili kujishindia moyo wake. Lakini akaja kugundua moyo wa Jelini haufurahishwi na pesa ila kumjali. Basi yule mzee alibadili maisha yake kiasi cha kukera familia yake na watu wake wa karibu. Maana ana vijana wakubwa tu. Lakini yote hayo ilikuwa kwa ajili ya Jelini.”

“Ninachotaka kusema ni, yeye aligundua siri na kujibadilisha yeye. Akatafuta nafasi yake katikati ya hao wawili, akafanikiwa kumtuliza Jelini japo Colins hakuwa mbali.” “Unamaanisha nini?” Ezra akauliza.

“Huna utakapomuweka Jelini, macho ya Colins yasimuone. Walisumbuana na Kasa mpaka kutishiana risasi kwa ajili ya Jelini, lakini Jelini ni mtu wa maneno yake. Japokuwa anampenda sana Colins, ila kwa kuwa alikuwa na Kasa, hakuwahi kumsaliti. Ndivyo alivyo na wote hao wanamjua. Si mtu wakujipinga, na si mtu wa kuwa na wanaume wawili.”

“Colins hajawahi kumtoka moyoni, na kwa jinsi ilivyo mpaka sasa inamaana Jelini hajatoka moyoni kwake pia japo anataka kuchumbia mwanamke mwingine.” “Unamaanisha nini?!” James akatulia.

“James?!” “Sitaki kutibua hii hali Ezra. Nashauri uache, Jelini atarudi tu, mtazungumza.” “Nakuahidi sitarudia nilichofanya. Tafadhali nisaidie tu kwa namna yeyote ile.” “Kwa kifupi, hakuna anayeweza kujua Jelini alipo, isipokuwa Colins tu.” “Kwamba hata ukiingia kwenye mitandao yenu hiyo huwezi?!” “Nilishafanya hivyo ndio maana nilicheka mwanzo.”

“Nilipovuta namba zote za Jelini, au chochote kinachomuhusu alipo, nimekuta kumewekwa security restrictions hizo! Sikuamini. Nikatafuta kichwa kingine, ninachokiamini cha mambo ya cyber security. Bila ya kumwambia ni namba za nani na wapi nimekwama, yeye mwenyewe moja kwa moja akaniambi ni kichwa kimoja tu, anachojua kinaweza kufungua zile restrictions. Guru.”

“Guru?!” Wote wakajikuta wanauliza kwa pamoja. “Jina analojulikana nalo Colins huko kwenye ulimwengu wetu. Anapofika kwenye hizo anga, hanaga mpinzani. Alijaliwa kipaji cha ajabu sana. Pale tulipokuwa tukifanya naye kazi, kila mtu. Nikimaanisha wote, wazawa na wageni waliokuwa wakija pale kwenye ile kampuni, walikuwa wakisalimu amri kwake, na kubakia kumuita ni mungu wa mitandao. Kwamba anaweza amuru chochote kitokee kwenye kompyuta kikatokea.”

“Kwanza huyo jamaa mwenyewe alipofungua tu namba ya Jelini, akitaka kujua alipo, huo ukinzani wake tu, alishituka sana mpaka akaniuliza, ni namba za raisi wa wapi, nisije mtia matatizoni.” “Kwa jinsi zilivyo fungwa?!” Junior akauliza. “Ewaaah! Naona sasa mnanielewa. Na najua amefanya makusudi.”

“Naona kabla ya kuuliza kwa nini, naomba kupata ushauri wako, jinsi yakufanya kuanzia hapa.” “Hakuna jinsi. Ni aidha msubiri Jelini mpaka arudi mwenyewe, kitu ambacho mimi nashauri hivyo ili kuyafanya haya mambo yasiende mbali.” “Chaguzi ya pili ambayo unasita kusema ni kumtafuta Colins?” Esra akauliza.

“Ewaah! Ambapo, kwa jinsi ninavyokijua kichwa cha Colins, huwezi kumuamsha sasahivi na kumwambia nifungulie access za Jelini, akafungua. Hata iweje hatafanya hivyo kwa sababu amefunga kwa makusudi. Inamaana atataka kujua ni kwa nini tunataka kujua Jelini alipo, tena usiku huu! Na huna jinsi ya kumdanganya Colins. Lazima ajue ukweli wote.”

“Na akijua ukweli, ndio atasumbua sana, akiona kila mtu hamjali Jelini. Atajihusisha na hilo jambo, mpaka atawakera! Kasa anamjua, Jema na mama yake pia wanamjua. Na huna jinsi yakumkataza akakubali. Walikuwa wakitishana na Kasa mchana na usiku mpaka kwa risasi.”

“Nikuulize kitu James?” “Karibu Junior.” “Kwa jinsi unavyowajua, na kwa hali ilivyo, unafikiri Jelini hatamtafuta Colins kweli?” “Hathubutu hata iweje. Ndio mwiko wake na wote wanamjua. Huko ameenda kutulia tu, atarudi. Kichwa cha Jelini hakitaki kupata moto. Kikishapata moto tu, lazima akakitulize. Hatakagi kelele kichwani mwake ndio maana hajui kugomba na hataki kumuudhi mtu. Akitulia, atarudi tu. Msiwe na wasiwasi.”

 “Hakika nina wasiwasi James. Lazima nimpate Jelini usiku huu.” “Basi jua lazima, namaanisha ni LAZIMA Colins ahusishwe. Sasa mimi na wewe hapa tulipo, hatujui kichwa chake kilipo usiku huu, vile atakavyoamua sasahivi baada ya kusikia haya.”

“Kama kwa hakika yeye ndio mtu wa mwisho kunisaidia,” “Kama atakusaidia.” Akamkatisha kwa haraka. “Unamaanisha nini tena!?” “Kwa jinsi ninavyowajua hawa wawili, na Colins anapokuwa linapokuja swala la Jelini, kwanza hashauriki, pili akijua ukweli, wewe utakuwa mtu wa mwisho kabisa kutaka hata kusikia jina lako, labda baadaye Jelini aje akuzungumze vizuri.”

“Kasa amegeuka kuwa adui yake, hataki hata kumuhisi. Na wangefika mbali sana, ila Kasa alisaidwa na kijana wake ambaye tulifanya kazi pamoja na Colins. Kwa hiyo anamfahamu Colins na kile anachoweza fanya. Anasema ilibidi azungumze na baba yake kwa kituoa maana Kasa ni mkorofi. Mkorofi haswa na mbishi. Akamuonya kuwa pale alipoharibu kwa Jelini, iwe hivyohivyo, akiongeza kingine, hamtaki Colins amfuatilie nyuma. Maana atamlipa kisasi vibaya sana. Na hataweza kumkamata.”

“Sasa nahisi kuanzia hapo, ndipo alipomficha Jelini mtandaoni. Kwamba japokuwa Kasa anayo pesa, hata akimtafuta mtu wa namna gani, hawezi kujua Jelini alipo, labda Jelini mwenyewe amwambie. Lakini si vinginevyo. Mimi nahisi hivyo. Kama ana sababu ingine, hatasema. Kwa hiyo kwa kifupi, ni kwamba…” “Kama tunamtaka Jelini usiku huu, ni kumtumia Colins.” “Ewaa! Napo, narudia tena, inategemeana na Colins. Anaweza asiwe msaada kwetu ila kwa Jelini.”

“Kwamba atamtafuta yeye mwenyewe!?” “Hiyo ni LAZIMA. Atamtafuta yeye mwenyewe mpaka ampate ndipo ataamua kama atujulishe amempata au la. Zaidi wewe Ezra. Inamaana itategemeana na atakachosikia kutoka kwa Jelini juu yako. Uwamuzi ni wako. Mama yake nimezungumza naye naona ameridhia kumuacha mpaka arudi, japo sijamwambia hayo niliyowaambia nyinyi juu ya Colins na mengineyo.” Kimya, Ezra akifikiria. Junior naye kimya akimpa nafasi yakufikiria.

James naye kimya. “Sitajisamehe endapo chochote kibaya kitampata Jelini nikiwa mimi ndio nimesababisha. Acha tu amtafute. Hata kama ni yeye, amtafute tu ampate na ahakikishe yupo salama. Hilo ndilo la muhimu. Mengine tutajua mbele ya safari.” “Sawa. Ila nashauri kama mpo barabarani. Mrudi tu nyumbani, sehemu mtakayo pumzika. Colins hatabiriki. Anaweza akanibadilikia mimi mwenyewe, usiku huu, na mimi nikawa ni adui asiyetaka kunisikia mpaka atakapompata Jelini.” “Sawa James. Wewe tujulishe itakavyokwenda.” “Sawa.” Ndipo wakaagana.

Kwa Colins.

James akaitizama ile simu akifikiria mazungumzo yake na Colins jinsi yanavyoweza kuisha vibaya, bila kupata jinsi ya kuzungumza naye akamuelewa. Mwishoe akaona anazidi kupoteza muda, akampigia.

Ikaita mara kadhaa ila akapokea akisikika alikuwa usingizini. “Kwema James?!” “Samahani kukuamsha. Nilitaka msaada wako.” “Karibu.” Akaanza kwa ustaarabu kweli ila James akijua baada ya hapo, haitakuwa shwari tena.

“Tunaomba msaada wako kujua Jelini alipo.” Pakazuka ukimya wa muda mfupi, kumbe anaangalia saa. “Kwamba wewe na hao mnaotaka kujua Jelini alipo, mpaka sasa, usiku mwingi hivi, kati yenu hakuna anayejua Jelini alipo!?” “Acha kupaniki Colins ni…” “Unazungumza nini James wewe?! Unajua sasahivi ni saa ngapi? Yaani mpaka sasahivi nyinyi watu wazima na akili zenu, hamjui Jelini, mtu rahisi hivyo, alipo!?”

“Si ndio anaendelea kutafutwa! Naom…” “Subiri kwanza. Ni nani ambaye anamtafuta? Kwamba hata huyo mchumba wake hajui alipo?” “Hajui.” “Kwa nini?!” “Colins. Wewe usitake kufanya haya mambo kuwa makubwa.” “Kwamba mpaka sasa wewe huoni kama haya mambo ni makubwa!? Angekuwa haonekaniki Jema, bado ungetulia kama hivyo!?” Akambadilikia.

“Nakuuliza James? Unaniambia nisiyafanye mambo kuwa makubwa, wewe huoni kama tayari haya mambo ni makubwa sana!?” “Nafikiri nimekosea tu kuzungumza.” “Huko ni kutokujali. Na sikutegemea kwa mtu kama wewe unaweza fanya hivyo! Unaaminiwa na familia ya mama Jema. Halafu unashindwa kutimiza majukumu madogo tu! Na hapo una mtoto mmoja tu!” “Jema ni mjamzito.” “Acha kunichanganya  zaidi James.”

“Umekasirika Colins. Utashindwa kumpata Jelini.” “Sio mimi. Hapa namfuata.” “Tafadhali Colins, naomba nijulishe.” “Unanitania wewe James!?” “Nimekuomba Colins?” “Yaani yeye na akili zake awafungie nyinyi simu, halafu mimi nivunje uwaminifu wake kwangu?! Kwa nini nifanye hivyo?” “Ili kutengeneza.” James akasikia gari linafunguliwa. Kwamba ameshajua alipo, na kweli anamfuata.

“Nisikilize Colins. Huyo Jelini anatafutwa na mchumba wake, hapa tunapozungumza anasubiria jibu.” “Kwa nini yeye asijue Jelini alipo kama kweli ni mwanaume anayejua kuwajibika?” “Kulitokea kutoelewana ndio Jelini akaondoka.” “Acha kunipotezea muda kwa habari nusunusu James. Wewe unanijua. Mimi si mjinga. Kama unataka niendelee kukusikiliza, zungumza kitu kinachoeleweka au na mimi nakufungua simu, nitaenda kujua ukweli kutoka kwa Jelini mwenyewe. Usizidi kuniudhi!”

“Wewe nilikuomba rasmi kumlinda Jelini. Nikiwa nakuamini. Leo anapotea, unanyamaza mpaka usiku huu ndio unanitafuta!” “Jana uliponipigia ukiniambia umepata mchumba, unachumbia, Jelini alikuwepo akasikia na kushituka kiasi ya kwamba kila mtu akajua. Tulikuwa nyumbani kwa wakwe zake na mchumba wake alikuwepo.” Hapo Colins akapoa.

“Jelini amechumbiwa na mwanadamu Colins. Kama mimi na wewe, lazima kupatwa wivu. Wakatoka nje kuzungumza juu ya hilo, nafikiri kuna maneno yalizungumzwa…” “Tafadhali James.” Akawa akama anamuonya, James akaelewa.

“Basi niseme kuna maneno alizungumza huyo mchumba wake ndio yakamtibua Jelini. Na kabla hujataka kujua ni maneno gani, mimi sijui alichozungumza mpaka kumtibua Jelini.” Kimya. “Colins?” “Nitakutafuta baadaye.” “Kwa nini usiniambie alipo ili…” Simu ikakatwa. Na hakumpata tena. Alitegemea.

~~~~~~~~~~~~~~~

Haya Tena, Wakiwa Wameshapata Wachumba Wakueleweka, Na Siku Chache Zimebakia Aolewe,

Jelini Na Colins Maisha Yawapa Faragha Nyingine Tena.

Nini Kitaendelea Kwa Wawili Hao Huko Hotelini!

Usipitwe….



CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment