Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 38. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA - PART 4 - SEHEMU YA 38.

Ile hali aliyoondoka nayo Jelini na majibu yake ya mwisho, vikamuacha Ezra kwenye wasiwasi, asijue hali ni mbaya huko kwa Jelini kuliko alivyodhania. Akasubiria muda wakutosha akivizia ampigie shuguli zikiwa zimepungua asijue kwa hasira Jelini alikunywa dawa za usingizi. Tena zakumtosha kuzima kabisa, akalala hajitambui wala hakuwa na kazi.

Aliporidhia kuwa huo ndio muda muafaka, pengine wamesharudi nyumbani, akampigia. Simu ikawa inaita, hamna majibu. Wawili hao walishazoeshana kupigiana simu wakiwa kitandani wakilala. Kwamba sauti zao ndio za mwisho masikioni mwao kwa siku. Ila usiku huo hata hakutakiwa usiku mwema!

Usingizi ukampaa. Akabakiwa na kazi ya kupiga simu, kumbe mwenzie simu kaacha kwenye pochi, kalala, hana habari na kinachoendelea huku duniani.

~~~~~~~~~~~~~~~

Asubuhi akaamka. Akaona hizo missed call zaidi ya 20. Akafyoza. “Yeye si hataki kubabaishwa? Sasa asubiri. Mimi sitingishi kiberiti. Changu kimejaa. Sina shida.” Akaazimia Jelini. “Kwani lazima ndoa! Ebo! Mtu asinichanganye mimi.” Akazidi kujipandisha mukari akisahau mipango yote ya ndoa.

Ni Ezra huyohuyo alimshawishi aache ubahili, aajiri vijana wakutosha kwamba siku za jumamosi awe na msaada wa kutosha. Kwa hiyo hapo alikuwa na kazi ndogo tu, anamaliza siku nzito ya kazi kirahisi, na pesa nzuri bado inaingia.

Akawahi kutoka kabla ya muda wake. Akaenda kufanya shuguli zake, mapema sana akamaliza. Akarudi nyumbani. Akaoga na kufungasha mizigo yake na mwanae. Akamchukua Jeremy akimwambia wanakwenda kupumzika sehemu nzuri. Jeremy akafurahi huyo!

Akampigia simu mama yake kumtaarifu. “Jelini! Jelini wewe! Hizo hasira zitakupeleka sipo!” “Acha niende nazo kokote zitakaponipeleka. Maisha ni yangu. Nikijuta ni mimi mwenyewe nitajuta. Haimuhusu mtu.” “Sawa. Ila ninachokuomba ni uwe mwangalifu mama mzazi. Rudi ukiwa mzima. Utaniua mama yako endapo chochote kitatokea. Umesikia mama?” Akanyamaza. Kisha akaongeza.

“Nimeondoka na Jeremy.” Hapo akamvuruga mama yake. “Unarudi lini?” “Sitaki kuulizwa.” “Hakika utanijibu Jelini. Bora ungeondoka peke yako na si na Jeremy. Huyo mtoto siku ya jumatatu anatakiwa shule. Umenisikia Jelini? Hapo sitaki unitanie.” “Kwani nimekwambia sirudi?” “Lini?” “Nimesema nitarudi, na Jeremy ataenda shule.” “Nasisitiza kuwa jumatatu, asubuhi, huyo mtoto awe amekaa darasani kwake. Usinitanie.” Hakumjibu.

“Tena awe amekaa darasani akiwa hana usingizi, yupo tayari kujifunza. Unanisikia Jelini.” Akaona simu imekatwa. Hapo akamchanganya mama Jema. Akampigia mara ya kwanza, hajapokea. Akarudia tena. Akajua amepaniki, akapokea. “Jeremy atarudi.” “Jelini nakuonya wewe mtoto!” “Sasa mimi nimefanyaje?!” “Nilikwambia nini juu ya maisha yako na wanaume zako?” Kimya.

“Sikukuonya na kukusisitiza mambo yako na wanaume zako havimuhusu Jeremy?” “Mimi nimetoka na mwanangu. Sasa kosa lipo wapi?” “Toka naye kwa utaratibu unao eleweka. Sio kwa sababu wewe umechanganywa, ndio umchanganye na Jeremy. Sitakuruhusu Jelini.” “Mimi simchanganyi mwanangu. Nimemchukua kwenda kupumzika naye tu.”

“Sasa, hakikisha kwenye hayo mapumziko hutii pombe hata tone kinywani mwako.” “Mimi nimeacha pombe.” “Nakuonya Jelini wewe! Maana mimi na wewe tunafahamiana. Usije kukutana na kina Doro wengine, ukanywa. Ukajisahau, ukamuacha Jeremy huko nisikokujua mimi, halafu hana ulinzi, wewe hujitambui.” Mama Jema akaendelea kukazia hukumu.

“Usiku wa leo, anipigie simu, nihakikishe yupo mzima na yupo kitandani kwake.” “Mimi sitaki kuingiliwa.” “Basi mrudishe nyumbani. Lasivyo, nitakusaka hapa mjini hata na jeshi la polisi, mpaka nikupate, nimchukue Jeremy. Sasa usinijaribu, maana unanijua.” Na kweli alimjua mama yake. Kwa Jeremy huwa hazembei.

“Sinywi pombe na Jeremy atakupigia wakati analala. Sitaki fujo, nataka kupumzika.” “Na jumatatu, kipindi cha kwanza, kimkute amekaa kwenye dawati lake. Ameshiba, na hana usingizi. Umenielewa Jelini?” Kimya.

“Jelini?” “Mimi nilitaka kukaa mpaka jumanne.” “Sio na Jeremy. Mwache nyumbani, wewe nenda kokote unakotaka. Kwa muda wowote utakao. Akifunga shule, wewe mchukue, sitakuwa na neno endapo utakuwa ukitimiza masharti yangu huko ulipo. Lakini huyo mtoto hatakosa shule si kwa starehe zako, wala si kwa hasira zako. Usitake kunichanganya. Au lasivyo, nafunga biashara zote sasahivi, naanza kukusaka mpaka nikupate.”

“Huyo Jeremy atakupigia simu usiku, na jumatatu atakuwa shule.” “Na usinywe pombe.” “Nishasema sinywi pombe.” “Na hilo ulikumbuke. Sasa nisimsikie Jeremy mida yake ya kulala.” “Hata lala saa mbili mama, kama siku za shule. Leo nataka kukaa naye muda mrefu.” “Basi nisilale bila kumsikia.” “Mnanifanya mimi mjinga. Sina akili.” Akaanza.

Akalalamika hapo akilia, analaumu hili na lile, hamalizi. “Sasa unaendeshaje na hicho kilio Jelini, kama si kunitafutia balaa mimi! Ukipata ajali?” Akaendelea kulia. “Wewe nenda kapate muda wa kutulia na mtoto. Usinywe pombe, hata kwa kushawishika. Jeremy anipigie simu. Jumatatu awepo shule. Hapo hatutakosana? Kwanza mimi na wewe huwa hatukosani.” Akampamba hapo huku akimbembeleza mpaka akatulia. Kama kawaida yake kupenda kubembelezwa ndio udhaifu wake na mama yake alimjulia. Akatulia kabisa ndio wakaagana.

Bora Aibu Kuliko Fedheha!

Alipoona Ezra anaendelea kupiga. Akamtumia ujumbe. ‘Nimesafiri. Sipo mjini.’ Akautuma huo ujumbe na kuzima simu kabisa.

Jelini pesa anayo, kazi ni matumizi. Alikuwa aende Zanzibar, lakini alipoona mama yake anamkazania Jeremy, akaamua kwenda Bagamoyo. Akatafuta hoteli nzuri ufukweni, starehe yeye na mwanae zikaanza. Wamekutana wapenda kuongea. Maneno mengi! Stori haziishi. Kucheka kwa kila jambo na wote wapenda kula.

Kula, kuogelea na kucheka wakati wote. Wamependeza, ukimuona Jelini utasema nili milionea fulani hivi. Akawa amejiwakilisha kwa vazi la ufukweni, mahiri sana. Nadhifu. Na vile alivyopendelewa umbile, kila mtu alikuwa akimwangalia yeye na mwanae. Asijue hali ya Ezra huko alipomuacha.

~~~~~~~~~~~~~~~

Akahangaika wee, Jelini hapatikaniki kwa simu. Safari za nyumbani kwa mama Jema zikaanza. Kila akienda, geti limefungwa. Akawa anahofia kumfuata kazini, au kumpigia simu. Mama Jema mtu wa kazi, siku ya jumamosi ndio siku yupo busy kupitiliza. Simu za wanae tu. Jeremy, Jema na Jelini ndio huwa anapokea simu zao. Jumbe ndio hasomi kabisa hata wanae wanamjua. Tenda zake zote za siku hiyo, anapokea mwisho ijumaa. Jumamosi ni utekelezaji tu. Ukitaka mfuate kituoni kwake.

~~~~~~~~~~~~~~~

(Yakobo 3:5-9) Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivunia matendo makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana. Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfululizo wa maumbile, nao huwashwa moto na Jehanamu. Maana kila aina ya wanyama, na ya ndege, na ya vitambaavyo, na ya vitu vilivyomo baharini, vinafugika, navyo vimekwisha kufugwa na wanadamu. Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti. Kwa huo tunamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo unawawalaani wanadamu walioumbwa kwa mfano wa Mungu.

Kwa Mama Jema.

Kwenye majira ya saa tano usiku kuelekea saa 6 ndio akawa anarejea nyumbani. Akakuta gari la Ezra nje. Akajua tayari. Kwa kuwa alikuwa amechoka na hasira za kuchukuliwa Jeremy, hakutaka usumbufu wa kukaribishana ndani. Akashuka garini.

Ezra na Junior nao wakashuka garini. Wakasalimiana. “Pole na majukumu mama.” “Nashukuru. Mnaendeleaje?” “Sisi wazima. Ila nimekuwa nikimtafuta Jelini bila mafanikio.” “Sio wewe umemwambia hajachelewa?!” Mama Jema akaanza.

Jinsi alivyomuuliza, mpaka Ezra akashindwa kujibu, Junior akakunja uso na kumtizama Ezra. “Eti Ezra? Hujamshauri Jelini na kumwambia hajachelewa? Na asikubali kuolewa na mtu eti kwa sababu ametambulishwa kila mahali mpaka kanisani na kwa wazazi? Tena ukamwambia asiogope kukuumiza au kukuingiza aibu. Ukamwambia ni bora aibu, kuliko fedheha. Hukusema hivyo wewe, au Jelini amedanganya?” Junior akawa kama anaota.

“Sikuwa na maana hiyo mama yangu!” “Ila hayo ndiyo maneno uliyomwambia si ndio?” Kimya. “Ezra! Mimi nimechoka, nataka kupumzika. Sijakaa tokea asubuhi. Kukaa kwangu ni hapo ndani ya gari, nikiwa narudi hapa kwangu. Tafadhali tusipoteze muda.”

“Lakini sikuwa namaanisha hivyo inavyosikika!” “Wewe hujamjua Jelini na kichwa chake. Na nahisi unataka kumuoa mtu usiyemjua kabisa. Sifa yake ya kwanza, hataki kuchosha akili yake kufikiria chochote kitakachompotezea muda. Hanaga mawazo mazito kwa sababu hataki kujichosha kufikiria. Kile unachozungumza mdomoni, anakipokea kama kilivyo na kukitendea kazi.” Hapo Ezra ndio akakosa nguvu kabisa karibia aegemee magoti.

“Kingine. Jelini uliyekuwa naye wewe, hakuna mtu anayeamini kama ni Jelini niliyezaa mimi. Mimi mwenyewe hata malaika angeshuka na kuniambia Jelini angeweza kuishi maisha aliyoishi na wewe, nisingemsadiki. Amebadilika sana kwa ajili yako wala si mimi. Kichwa chake yule akiamua jambo, si wakumrudisha nyuma, hata mimi simuwezi mpaka ulipokuja wewe.”

“Na sijui kama alikwambia, sisi na milango ya kanisa tumeanzia pale kwenu. Tena kwa kulazimishwa na Jema, kelele isiyoisha. Kutufuata hapa mchana na usiku na simu zisizo koma. Mpaka tukakubali yaishe. Tukaanza kwenda kanisani.”

“Sasa kumuona anaungana na nyinyi mpaka siku za katikati ya juma, Jelini yupo kanisani! Tena anafanya juhudi mwenyewe, kwa furaha! Jelini!” Mama Jema akawa anashangaa kabisa. “Kwa hakina hakuna aliyetegemea.”

“Sasa eti na wewe unaona mwenzio anajitoa vyote hivyo, tena kwa ajili yako, mpaka kufunga na nyinyi! Jelini mpenda mlo, asiyejua kupitwa na mlo hata mmoja! Leo anafunga na nyinyi bila kulalamika, halafu unamwambia anafanya kwa ajili ya mama yake!” “Haiwezekani! Labda hakuelewa.” “Si umuulize Ezra huyo hapo kama hajasema hivyo?” Akamwangalia Erza.

“Junior! Inasikika vibaya, kuliko nilivyo maanisha. Unajua nampenda Jelini.” “Kwa vyovyote utakavyosema sasahivi, lakini hayo ndio maneno yako wewe mwenyewe, kwake. Kanusha tu hapa nijue Jelini amedanganya.” Kimya, wote wakimwangalia. Junior akapata jibu lake.

“Sasa! Wewe unamjua Jelini au unamsikia? Unampa Jelini njia rahisi ya kutoka! Jelini asiyependa shida! Haya!” “Sasa atakua amekwenda wapi?!” “Sijui. Amechukua mwanae, ameniambia wanasafiri. Sasa sijui! Ila nataka kukwambia jambo la mwisho kabla sijawaaga.” Mama Jema akaendelea, ila walijua ana hasira. Si sura waliyomzoea.

Wakabaki kama wanafunzi wa shule ya msingi, mbele ya mwalimu mkuu. “Hapo mliposimama nyinyi, au mlipoegesha gari lenu, mkimsubiria Jelini, nyinyi sio wa kwanza.” “Naelewa mama.” “Hapana Ezra. Huelewi.” Akaweka msisitizo.

“Mida hii kusubiria getini wewe si wa kwanza, na usifikiri ndio utakuwa wa mwisho. Na hapa mmejikuta peke yenu ni kwa sababu Jelini, yeye mwenyewe, amekomesha hiyo misafara ya hapa. Yanakuja kusimama magari hapa! Utashangaa na kujiuliza anayefuatwa ni nani! Weza fikiri ni raisi au mtu wa maana sana, kumbe ni Jelini asiye na shule kichwani.” “Mimi simdharau Jelini!” “Sivyo anavyofikiria sasahivi baada ya mazungumzo yenu.”

“Mama Jema!” “Kwa nini nikudanganye Ezra?! Wewe mtu mzima na akili zako anapoambiwa unafanya jambokwa ajili ya mama yako’. Unakuwa umeambiwa nini kama si kwamba wewe huna maamuzi yako binafsi, wala huna akili ya kufikiria, ila unaendeshwa na mama yako? Eti Junior?” Junior akabaki amepigwa na butwaa.

“Hakika imesikika vibaya! Sikumaanisha hivyo hata kidogo.” “Ila ulimaanisha hutaki kubabaishwa! Kwamba upo sawa bila yeye! Mbaya zaidi unamwambia Jelini aliyezoea kubembelezwa tokea analetwa hapa duniani! Jelini! Wewe hujamjua Jelini. Mimi nilikuwa nambemba mgongoni, nafanya naye kazi siku nzima. Utainama unapiga deki, na yeye yupo mgongoni, ndio tulia yake. Ukimuweka chini, ni kilio kama amekatwa mahali. Hawezi maisha bila mkono.”

“Hataki maisha ambayo yeye habembelezwi. Huna mali utamuhonga Jelini, ukamridhisha kama kumuweka mkononi, na kumuonyesha unamuhitaji. Kwanza hana shida ya pesa ya mtu. Hajajaliwa tamaa ya pesa. Nina uhakika huko alipo, na hivi mimi wa kumkemea juu ya matumizi sipo, atakuwa anachafua pesa yeye na mwanae, tena pesa yake mwenyewe hajahongwa na mtu.”

“Shida yake. Udhaifu wake, ndio huo. Umuweke mkononi, umbembeleze. Tena kwako wewe naona amejitahidi SANA. Eti alikufuata mpaka nyumbani, tena usiku, anakwambia usimuache! Jelini! Halafu eti hataki umvue pete! Jelini!” Mama Jema akacheka kwa masikitiko.

“Jelini ang’ang’anie pete! Pete ambayo nina uhakika ameshaacha hapo ndani na jumatatu atakuwa na pete kama hiyo uliyomvalisha, tena kubwa zaidi maana hajui hujibana. Mpenda mazuri na makubwa.” “Mama!” Ezra akashituka sana.

“Nakwambia wewe hujamjua mtu uliyetaka kumuoa. Kwanza alikuwa hataki ndoa kabisa! Anasema ndoa ni mateso. Na kunyanyasana kihisia. Akasimamia hapo mpaka alipoona ndoa ya Jema. Vile James anavyomuenzi mkewe. Ndio akapata moyo. Lakini si vinginevyo. Hapo umemrudisha kulekule alikokuwa. Hataki tena.” “Haiwezekani!”

“Wala usipate shida. Pata nafasi na Jema atakwambia akili ya Jelini. Hajuagi kufikiria. Hataki kujichosha na mipango ya kesho. Kama hivi kaondoka na mwanae anayemrudishaga hapa, basi ujue huko ni starehe kwenda mbele, akili ya kesho haipo kabisa.”

“Yaani alale, aamke ajikute na mwanae! Shida zake zote zimeisha. Sasa hivi huko alipo hana analowaza isipokuwa kile anachokiona pale. Mwanae ambaye ndio roho yake.”

“Ungekuwa unauwezo wa kumuona sasahivi huko, unaweza usiamini hata kama alikuwa na mpango wa kuolewa jumamosi ijayo, kitchen party alhamisi na nina uhakika hata hakumbuki kama bibi yake anakuja mjini kesho kwa ajili yake. Hivi leo nimezuia dada zangu wasije hapa. Maana walikuwa waje wakeshe washerehekee naye, kabla ya harusi. Nikawaambia wasije, maana hakuna harusi tena.” “Usingefanya hivyo mama.” Akamtibua.

“Unazungumza nini Ezra? Mimi ni mama yake Jelini. Namfahamu kwa kulea mwenyewe bila hata kusaidiwa na jirani. Nazijua akili zake na vile anavyofanya. Hatajichosha kufikiria lolote. Si la kesho na madhara yake. Yeye anafanya ya leo. Yakienda sawa ni sawa. Yakienda vibaya, anabadili gia. Sasahivi anastarehe na mwanae, mengine atakuja kukutana nayo hapa, akirudi. Sasa unataka nikusanye watu hapa kusherehekea kuolewa kwa nani?” Hapo hasira zikampanda zaidi.

“Hivi unajua madhara ya maneno uliyomwambia Jelini kwa kiburi au bado unajiona upo kwenye nafasi ya kunilaumu mimi?” “Hapana mama yangu. Sikuwa na nia hiyo.” “Nakwambia mama yangu hatoki migombani mpaka jambo la msingi. Nakwambia anakuja kesho kwa harusi ambayo haipo. Unafikiri mimi nipo kwenye wakati gani kama si kujidhalilisha hapa mjini?” Akawaka.

“Sasa kabla hujakosana na mimi zaidi. Maana ukimchanganya tu Jelini, ujue umekosana na mimi kabisa. Tena utakosana na mimi vibaya sana. Hutanipenda.” “Sina nia yakumchanganya mama yangu.” “Basi umemtingishia kiberiti mpaka amechoka.” “Haikuwa nia yangu.” “Ulitegemea nini kwa mtu kama Jelini!? Kwamba atakutetemekea daima!? Kwa nini!?” Akawa ameshalipuka.

“Ndio shida yenu nyinyi. Mtu akijishusha tu kidogo, mnataka mpaka kumkanyaga! Badala uenzi kama wenzio, wewe ndio unapandisha mabega na kuvimba kichwa!? Wewe hujaona wenzio wanavyohangaika na Jelini mpaka leo japo hawapo kwenye maisha yake? Wakisikia tu Jelini ana shida, wote wanakimbia. Sasa wewe unafikiri ni kwa nini?” Kimya.

“Washazunguka, wamehangaika, wakagundua hawatapata mtu kama Jelini. Mwanangu hana makuu! Hana tamaa! Sasa kaamua kitulia na wewe, na wewe unamringia tena! Jelini! Sawa. Tutakuja kukuona.” “Nampenda Jelini mama yangu na sikukusudia kumuumiza.”

“Kama kweli, basi usingemwambia uliyomwambia.” “Nakiri nilipaniki baada ya kumuona anapaniki juu ya Colins. Nikaingiwa wivu.” “Wewe hukujua kama Colins alikuwa mpenzi wake kabla yako?” “Nilijua.” “Hukujua kama alikaa muda wote akimsubiria yeye?” “Nilijua.” “Sasa wewe unachofikiri kwa penzi alilokuwa nalo kwa Colins, kwamba litakufa gafla tu kwa sababu unamuoa wewe!?” Yaani akafanya kumshangaa kabisa. Hapo ashakasirika kupindukia. Kwanza alikuwa amechoka. Halafu hugusi mtoto wa mama Jema akakuona au kukusikia. Anakuwa simba.

“Wewe umeanzana na Jelini ukijua wazi mwanaume aliyewahi mpenda hapa duniani ni Colins. Amerudi Colins, bado amekuchagua wewe! Sasa badala uangalie yako, ujenge msingi wenu nyinyi imara, wakumfanya aendelee kubaki kwako na asijutie maamuzi ya kumuacha mwanaume anayempenda, eti na wewe unamuonyesha hujali! Kweli!? Jelini!?”

“Nimekosea mama yangu.” “Na wala si mara moja, na mwenyewe anajua.  Ameyatunza, akiyavumilia, mpaka yamemfika kooni ndio ameamua kukuachia maisha yako yaendelee bila yeye anayefanya kwa ajili ya mama yake.” “Nitazungumza naye, nimuombe msamaha.”

“Nakuonya Ezra, usimchanganye Jelini. Nakuonya kabisa. Jelini amebeba hatima yake na Jeremy. Usiku huu Jeremy angekuwa amelala hapa ndani, ila wewe umesababisha hayupo, na sijui alipo.” “Nitarekebisha mama yangu. Naahidi nitarekebisha makosa yangu.” Akajishusha kabisa japo ametupiwa lawama zote nzito.

“Kaa chini. Jitafakari. Jua ni nini unataka kabla hujamtafuta tena. Umenielewa Ezra?” Hapo mama Jema kichaa chake kishapanda. Wanae agombeshe mwenyewe si mtu mwingine awafanyie jambo.

“Wewe si umesema ni bora aibu kuliko fedheha?” Kimya. “Sasa, kabla hujapoteza ubora wa hata hiyo aibu, tulia, jua ni nini unataka kabla hujamtafuta Jelini. Nishakupa madhaifu yake yote. Tafakari ndio urudi hapa, au umtafute tena. Kama ni mahari yenu, nitawalipa. Kwani shilingi ngapi bwana!?” Akaondoka na kuingia ndani na kuwaacha wamesimama hapo. Aliwabadilikia vibaya sana. Hawakuamini.

Marafiki Wa Katika Kila Hali.

Wakarudi garini, Junior akamuona alivyo na hali mbaya ila akashindwa chakuzungumza. Kimya kwa muda hata gari hawakuondoa. “Nimeharibu Junior! Sidhani kama safari hii, katika hili kama nitaweza tengeneza.” Junior akafikiria bila kupata jibu, na bila kujua chakuzungumza.

Alimsindikiza hapo, asijue kile alizungumza na Jelini, na vile kilivyopokelewa masikioni mwake na kutafarisiwa akili kwa Jelini, mpaka kupokelewa kwa namna ile kwenye moyo wa mama yake.

Maji yalikuwa yametibuka vibaya sana. Akashindwa chakumwambia ila akaona wajisalimishe tu kwa Mungu wao. “Acha tuombe Ezra. We will never go wrong with prayer.” “Siwezi hata kuomba! Ila nataka ujue sikukusudia kumuumiza Jelini.” Junior akamgeukia vizuri.

“Naomba kukuuliza.” Ezra akamwangalia. “Katika yote. Tukiwa tumebakia mimi na wewe tu hapa. Bila mtu mwingine anayetusikiliza. Je, kwa kujua moyo wa Jelini, bado Colins hajamtoka, wewe binafsi, utaweza ishi naye hivyo alivyo?” Kabla hajajibu akaongeza.

“Na kabla hujajibu, kumbuka reaction yako ya leo baada ya kumuona anashituka kusikia tu jina lake, na vile alivyokuwa pale alipojua amepata mwanamke mwingine. Je, utaweza ishi naye hivyo?” Ezra akatulia akifikiria. Junior naye akampa muda wa kutafakari. Kimya hapo garini, upepo wa a/c ukifukuza joto na mbu.

Kisha akaongeza. “Kama alivyokwambia mama Jema. Na mimi naunga mkono. Fikiria kabla hatujaendelea. Fikiria ukiwa umeweka mbali kabisa maswala ya harusi na garama zote tulizowekeza. Nataka ufikirie na unipe jibu ukiwa unayaona maisha yenu, baada ya harusi.” Kisha akawa kama amepata wazo.

“Hebu fikiria Ezra. Yaani baada ya kufunga na kuomba jana kwa mara ya mwisho kabla ya harusi. Tukiombea hii ndoa, ndio yote haya yanatokea! Inaweza sikika ni ajali mbaya sana. LAKINI kumbe Mungu anataka kukutambulisha kwa mwanamke unayetaka kumuoa.” Hapo Ezra akamgeukia vizuri.

“Ninaweza nisiwe sahihi Ezra. Lakini Mungu huwa anatumia upumbavu wetu sisi wenyewe, kufanya mambo yake. Tulifunga na kuomba kwa hakika, tukimlilia Mungu kwa ajili ya wanawake tutakao kuja oa. Sasa, leo umemjua Jelini halisi kabisa. Huyo ndio Jelini mwenyewe, na yote umeyasikia kutoka kwa mama yake mzazi. Mungu amekufungulia Jelini mkamilifu. Je, utaweza ishi naye hivyo?”

~~~~~~~~~~~~~~~~

JINSI MANENO YALIVYO NA NGUVU. NENO MOJA LINAWEZA IBUA MAMBO MENGI.  

Zikiwa zibebakia takribani siku 7, ndoa ifungwe, Jelini ameondoka hana mawasiliano na mchumba. Mama yake yupo tayari kurudisha mahari.

Je, Ezra naye ana kifua cha kuyavulia maji nguo na kuyaoga?

Ni Nini Kitaendelea?

Usipitwe.





CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment